Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Tecla Mohamedi Ungele (19 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii kwa ajili ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia nafasi hii ya Bunge ni nafasi adimu, mimi ninaisema ni kwa neema yake Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Pia nakishukuru Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Lindi na kutokana na juhudi na kazi zilizoonekana za Dkt. John Pombe Magufuli zimetia imani kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi hata mwaka jana tumepata majimbo yote kwa Chama cha Mapinduzi ukilinganisha na mwaka 2015. Pia nashukuru familia yangu na rafiki zetu wote kwa support walionipatia kwa muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika napenda kuchangia kwa muda mchache huu hotuba ya Mheshimiwa Rais kwenye ukurasa wa 32, 33 na 34 kwa maeneo ya sekta ya afya, maji na elimu. Napongeza kwa kazi zote alizofanya na ndiyo maana zimeandikiwa kwenye taarifa hii na pia hata kwenye Ilani ya Uchaguzi kwamba nini tutaenda kufanya kwa miaka hii mitano mpaka mwaka 2025.

Mheshimiwa Spika, sekta ya afya kwa mafanikio ni makubwa, mimi mwenyewe nina uzoefu mkubwa kwenye sekta ya afya ndio nilipokulia mpaka sasa hivi, kwa sababu zaidi ya miaka 30 nimeendelea kuudumu huko kama mwalimu muuguzi, na mkunga kwa hiyo, ninauzoefu mkubwa sana na maendeleo yaliyotokea na mafanikio yaliyotokea kwakweli ni makubwa sana huwa ninamwangalia Dkt. Johh Pombe Magufuli huyu ni daktari, huyu ni muuguzi ama yaani ana kila kila sifa, lakini nikiangalia kumbe ni sababu wa utegemezi wake kwa Mungu aliye hai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini napenda kuchangia kwa machache tu katika huduma za afya, pamoja na mafanikio yote hayo lakini kuongezwe ajira za wafanyakazi wa Wizara ya Afya ama idara hiyo ya afya ili tupate skilled personnel.

Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu ukiwa na wafanyakazi wa kutosha hata huyu mama nikitolea mfano mama mjamzito au mama anayekuja kujifungua au mtoto anayekuja kupata huduma pale watakuwa na muda mfupi wa kukaa pale kwa huduma kama ni huduma za kutwa ama hata za kulazwa hospitali lakini kutakuwa na muda mzuri wa hudumu hawa kuwaudumia hawa wagonjwa na pia hata stress za wafanyakazi zitapungua, kwa sababu wafanyakazi wako wengi na hata huduma atakayopata yule mgonjwa ama mama yeyote basi itakuwa ni nzuri.

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika eneo hilo hilo afya mimi kama Mbunge kwenye mkoa wangu au popote nitakaopita na utaalamu wangu nitaendelea kuwahamasisha akinamama wajawazito na watoto hata na jamii kwa ujumla waende kupata huduma za hospitali.

Mheshimiwa Spika, lakini pia napenda kuchangia kwenye sekta ya afya mafanikio mengi yamepatikana lakini tumeona changamoto hata Mheshimiwa Rais aliiona wakati wa kampeni kwamba maji bado vijijini. Kwa hiyo hata vijiji mbalimbali vya Mkoa wa Lindi vile vijiji vingine bado havijapata maji, nikiangalia yule mama mjamzito bado anaenda kuhangaika kutafuta maji bado anaangaika ili na lile kuangalia familia hivyo basi ni tatizo tunaomba maji, mwanamke huyu tumtue maji angalau hata anapokuwa mjamzito asihangaike kutafuta maji, akihangaika huku na kule bado hata uzazi wake hautakuwa salama.

Mheshimiwa Spika, pia nachangia kwenye sekta ya elimu kwa haraka haraka, nashukuru kwa elimu bila malipo hata mwanafunzi hata mtoto wa Mkoa wa Lindi anapata elimu na hata Tanzania nzima kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne. Lakini katika hili ninashukuru pia kwa kuzingatia masomo ya sayansi. Kwa uzoefu wangu wa vyuo vya afya mara nyingi tunakosa wanafunzi wazuri kwa sababu hawakufaulu sayansi kwa hiyo hilo nalo nalipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika elimu tunaomba elimu ya juu kwa Mkoa wa Lindi hakuna Chuo Kikuu kwa hiyo naomba kuwe na compass ya Chuo Kikuu Mkoa wa Lindi ili nako tupate elimu ya hali ya juu ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kutupatia uhai na hata sasa tunaendelea kuhudumu katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake ya bajeti iliyosheheni matumaini makubwa katika mwaka 2021/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia kwenye maeneo mawili; la kwanza kuhusu watumishi wa Idara ya Afya; kwa uzoefu na observations nyingi za Mkoa wa Lindi, vituo vingi vya afya vinahudumiwa na wahudumu wa afya yaani Medical Attendants. Sasa hii inaathiri utoaji wa huduma ya dharura ya uzazi yaani CEmONC na hiyo itaashiri kufikia malengo ya kupunguza vifo vya akinamama wakati wa ujauzito na kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mifano michache tu, najua wilaya zote zina shida hizo, lakini mfano Kituo cha Afya cha Nanjilinji, kimepata huduma nzuri za majengo na tunashukuru Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, lakini watoa huduma ambao wana ujuzi hawapo. Kunapotokea dharura ya uzazi, mzazi huyo anakimbizwa kwenye Hospitali ya Wilaya jirani ambayo ni Ruangwa ambapo kuna kilomita 44 kutoka Nanjilinji, tofauti na kutoka Nanjilinji kwenda Hospitali ya Wilaya Kinyoga kule Kilwa ambayo kuna kilomita 174.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara inayotoka Nanjilinji kwenda Ruangwa nayo sio nzuri, ni barabara ya vumbi lakini pia inapita kwenye Mto Nakiu ambao hauna daraja, sasa masika kama haya ukijaa, hebu ona sasa hapo, mgonjwa yule ni mama anayehitaji kujifungua, anayehitaji operation ya kujifungua, lakini anashindwa kuvuka pale na ambulance unayo lakini kuna shida. Mkoa wa Lindi una shida sana una changamoto za huduma za afya, majengo tumepata tunashukuru na vifaa sehemu nyingine vipo, lakini watoa huduma ni wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuchangia kwenye miundombinu, Mkoa wa Lindi kuna sehemu chache sana ile barabara kutoka Kibiti – Lindi – Masasi – Tunduru – Songea; ni hiyo tu ndiyo ya lami, lakini tunaomba ile barabara ya kutoka Masasi – Nachingwea; Nanganga – Ruangwa; Ruangwa - Nachingwea, Nachingwea – Liwale; na Nangurukuru -Liwale, tunaomba ijengwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna changamoto ya barabara za vijijini; natolea mfano kwa sasa ni masika, barabara zingine hazipitiki, mfano barabara ya kutoka Mipingo kwenda Mnyangara mpaka kule Namapwia ambako anatoka yule mjusi unayemsikia, sasa hivi hakupitiki kabisa. Pia kuna barabara ya kutoka Hoteli Tatu kwenda Pande na Lihimalyao kwenyewe ni changamoto kubwa. Pia kuna barabara inayotoka Somanga kwenda mpaka Kibata, nako ni changamoto; kwa ujumla barabara za vijijini Mkoa wa Lindi kuna changamoto kubwa. Jamani, tafadhali tunaomba mkoa ule uangaliwe kwa jicho la pekee ili kuwanusuru wananchi wale, ili nao angalau na wenyewe wachangie kwenye maendeleo ya nchi hii na wajisikie kwamba kwenye nchi yao ya kufaidi matunda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi. Awali ya yote, napenda kushukuru Wizara hii, kwa ajili ya ujenzi unaoendelea, sasa hivi mkandarasi yupo pale kwenye barabara ya Nanganga
kwenda Ruangwa. Ila ombi langu naomba ujenzi uende na viwango, lakini pia uende kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Nachingwea kwenda Liwale, kilometa 130; Nangurukuru – Liwale, kilometa 230; na Kiranjeranje - Namichiga – Ruangwa, kilometa 120. Hizi zote zipo kwenye hatua za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ufikie wakati zijengwe kwa lami. Kwa nini naomba hivyo? Barabara hizi kuwa katika kiwango cha lami ni muhimu sana kwa sababu usafirishaji wa watu, lakini usafirishaji pia kwa wagonjwa, lakini usafirishaji wa mazao ya korosho na ufuta ambayo ni mazao ya biashara kwenye Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaposhindwa kusafirisha mazao haya Maisha ya watu kule Mkoa wa Lindi yanakuwa duni. Naamini kabisa siku moja ukipata bahati kwenda Liwale utaona kabisa huku ulipo ni kugumu sana, lakini kule kunapatikana korosho na ufuta kiasi kwamba unaweza kukwamua wananchi wa kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ni mfanyabiashara gani atakayehangaika kwenda kununua korosho kule, badala ya kwenda kununua kwenye maeneo ambayo yanapitika. Naomba ufike wakati kuwepo na barabara ya lami kwenda Liwale na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea pia habari ya Uwanja wa Ndege wa Nachingwea. Nimeona kwenye Randama kunataka kuwekwa lami, naomba hilo lifanyike kwa umuhimu wake sana. Uwanja wa Ndege wa Nachingwea una umuhimu sana kwa sababu pale ni center mtu wa Liwale, Ruangwa, Masasi anaweza kusafiri kupitia Nachingwea kuliko kwenda Mtwara kilometa 200 kutoka Masasi. Pia itarahisisha wawekezaji, kule kwetu sasa hivi kuna madini, kuna madini Nditi, kuna madini Ruangwa, ni rahisi kwa wafanyabiashara wawekezaji kupitia kuanzia Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia na-share tu experience niliyoipata wakati wa mazishi ya Mzee Mkapa. Ndege nyingi, viongozi wengi walitua katika Uwanja wa Ndege wa Nachingwea, lakini uwanja ule kwa sababu ni wa vumbi adha iliyopatikana wanaifahamu mmojawapo akiwa Mheshimiwa Spika mwenyewe wa Bunge letu, Mheshimiwa Ndugai, anapafahamu Nachingwea. (Makofi)

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ungele kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Hamida Abdallah.

T A A R I F A

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayezungumza hivi sasa kwamba Uwanja wa Ndege wa Wilaya ya Nachingwea, atambue kwamba tumerithi kutoka kwa wakoloni kikiwemo pia Kiwanja cha Lindi Mjini. Kuna umuhimu mkubwa sasa Serikali kuona namna bora ya kuboresha uwanja ule, tena kwa haraka zaidi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, napokea kwa mikono miwili taarifa hiyo. Uwanja ule pia ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama. Nachingwea tuna vikosi vya jeshi, kwa hiyo kunavyokuwa hali yoyote ya kuhitajika usalama ndege pale zitatua na mambo mengine yataendelea. Ufikie wakati Wizara iiangalie Nachingwea na Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa ujumla. Ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ili nami nichangie hoja hii iliyotolewa na Kamati ya Masuala ya UKIMWI, dawa za kulevya, kifua kikuu na magonjwa yasiyoambukiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote tunamshukuru na tunampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza na kuongeza ujenzi wa madarasa katika shule zetu ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika madarasa hayo. Msongamano huo ndio uliokuwa unaleta magonjwa ya maambukizi ikiwa ni pamoja na kifua kikuu na mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitauelekeza kwenye kifua kikuu na ukoma. Kifua kikuu ni ugonjwa mkubwa na ni tatizo kubwa nchini Tanzania. Tunaona Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 ulimwenguni zenye maambukizi makubwa ya kifua kikuu; mwaka 2019 kulikuwa na wagonjwa 137,000. Kikubwa zaidi, kwa kifua kikuu kama mgonjwa hakugundulika mapema na hakupata matibabu mapema basi kuna hatari ya kwenda kwenye kifua kikuu sugu na hatimaye kusababisha kifo. Mgonjwa wa kifua kikuu asipopata matibabu anaambukiza watu wengine 10 mpaka 20 kwa siku. Hilo ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitachangia kuhusu ugonjwa wa ukoma. Bado ukoma ni tatizo kwenye nchi yetu; na ukoma nao unaambukiza kwa njia ya hewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zinaonesha mwaka 2019 kulikuwa na wagonjwa 1,600 nchini, lakini pia hata kihistoria ugonjwa wa ukoma una asili fulani ya unyanyapaa. Kwa hiyo kuna hatari wagonjwa hawajitokeza. Sasa, ushauri wangu ni kwamba, kuimarisha elimu ya afya katika jamii, lakini pia kutumia kikamilifu kada ya community health workers nchini kwetu. Tumeona sasa hivi wanaajiriwa kama medical attendance, lakini kada hii ilikuwa specifically kwa ajili ya kwenda kwenye jamii na ndiko watakakoshughulika na magonjwa haya sugu, kugundua wagonjwa wa kifua kikuu na maambukizi mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri kuwe na mafunzo maalum, iwe short courses ama course za muda mrefu kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ambukizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja kwenye Wizara hii muhimu sana Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii. Mheshimiwa Waziri Dkt. Dorothy Gwajima na timu yake yote, Katibu Mkuu na timu yote mpaka kule kwenye vituo vya afya na zahanati wanafanya kazi kubwa sana kuokoa maisha ya watoto, akina mama na wananchi wote kwa ujumla. Pia naipongeza Serikali nzima kwa ujumla kwa kazi kubwa inayofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia muda, naomba nijikite kwenye mambo makuu mawili. La kwanza, upungufu wa watoa huduma katika sekta ya afya lakini la pili, uhaba wa vitendea ikiwepo ambulance na vifaa vingine katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kwa ufupi hii suala la ambulance. Tunaona maeneo mengi yako mbali na hospitali za wilaya na huko kwenye maeneo hayo ya vijijini na kwenye kata kunatoa huduma mbalimbali lakini hakuna huduma ya ambulance. Nikitolea mfano kuna sehemu ambayo kuna zaidi ya kilomita 70 lakini inapotokea tatizo hakuna ambulance, mfano Nachingwea tuna ambulance moja ambayo ni mpya kwenye Kituo cha Afya Kilimarondo lakini zile ambulance zilizoko katika Hospitali ya Wilaya ni chakavu, hapa na hapa zinapata breakdown kiasi kwamba hata mgonjwa mwenyewe anaweza akafia njiani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye upungufu wa watumishi kwenye sekta ya afya, tumeona hapa Kitaifa kuna upungufu zaidi ya asilimia 53, hicho ni kiasi kikubwa sana. Nikienda kwenye Mkoa wa Lindi nikitolea mfano Wilaya kadhaa, Wilaya ya Ruangwa tulipaswa tuwe na watoa huduma 840 lakini waliopo ni 257 sawasawa na asilimia 31, upungufu ni asilimia 69. Nachingwea mahitaji ni 1,077 waliopo sasa hivi ni 305 tu upungufu ni 772. Wilaya ya Liwale wafanyakazi wa sekta ya afya ni 510 lakini waliopo ni 221 tu, upungufu ni 289. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama nilivyokuwa nimesema siku moja nilivyochangia mchango wangu hapa kwamba zahanati nyingi zinahudumiwa na medical attendants. Nasema hivi pamoja na upungufu huo, kwa mfano Wilaya ya Liwale mpaka kufika Hospitali ya Wilaya zahanati na vituo vya afya vingine viko mbali sana na ndipo pale tunapokuja kutoa mchango kwa kusema kwamba kuna tembo huko na kadhalika. Kwa hiyo, anapokuwepo mtoa huduma mmoja kwenye health facility fulani anapokuja kupata mshahara na kupeleka taarifa mbalimbali kwenye Hospitali ya Wilaya, humo njiani anakabiliana na mambo mbalimbali ikiwepo na wanyama wakali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma ya afya kunapokuwa na upungufu wa rasilimali watu matokeo yake ni kutokutoa huduma nzuri au huduma hafifu matokeo yake yanatokea pale pale, haisubiri baadaye. Labda ni mtu kutokuhudumiwa jambo fulani ni pale pale. Naamini kabisa kuna sekta zingine kama leo kukitokea kupata huduma hafifu matokeo au madhara yake yanatokea baadaye lakini kwenye sekta ya afya kama hakuna huduma nzuri matokeo yake yanatokea pale pale. Kama ni vifo vitatokea pale, kama ni mtu ana changamoto gani ni pale pale haisubiri baadaye. Kwa hiyo, jambo hili la kuwa na rasilimali watu wa kutosha kwenye health facilities ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nimeona baada ya kutoa changamoto hiyo niseme nini kifanyike? Ya kwanza nimeona, Waziri wa TAMISEMI ametangaza hapa ajira kama zaidi ya elfu mbili kwenye sekta ya afya. Naona jambo hili likitekelezwa kwangu ni faraja kubwa kweli na naamini kabisa Waziri wa TAMISEMI akiungana na Waziri wa Afya watasaidia kuangalia Mikoa ya Lindi na Mtwara na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suluhisho lingine ni mikataba ya ajira. Miaka iliyopita Wizara ya Afya iliungana na sekta binafsi kama vile bima na HITECH kupata ajira ya mkataba kwa ajili ya maeneo ya pembezoni, ile ilisaidia sana sijui ile program inaendelea au namna gani? Naomba Wizara ya Afya wajipange kutafuta kama ni wadau wengine kunusuru tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine naomba Wizara husika itoe vibali kwa halmashauri zetu ziajiri kwa mkataba lakini pia kutumia own source kwa ajili ya kuwa-retain wale wafanyakazi. Mara nyingi vijana wanaajiriwa kwenye maeneo yetu lakini kutokana na mazingira fulani baada ya miaka miwili au mitatu wanaomba kuhama. Kwa hiyo, naomba jambo hili la retention liangaliwe sana. (Makofi)

Sisi tulifanya research kuangalia ni jinsi gani itasaidia kuwa na retention mechanism Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kutumia vyuo vyetu vya afya na halmashauri husika na hili jambo liliwezekana. Naomba jambo hilo liwezekane Wizara husika ya Utumishi itoe vibali vya kutumia own source kwa ajili ya retention mechanism. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na awali ya yote naipongeza Wizara hii ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzungumzia kuhusu jinsi Tanzania tulivyoshiriki ukombozi wa Bara la Afrika hasa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, waasisi wetu Mwalimu Nyerere na wenzake waliamini kabisa kwamba uhuru wetu Tanzania hautakuwa na maana kama nchi za Kusini mwa Bara la Afrika hazitakuwa huru na ndiyo maana ilikuwa ni ajenda kubwa ya wakati ule. Hivyo basi, kwa nchi hii ya Tanzania tulivyoshiriki kwa kiasi kikubwa na wakati ule hasa kwenye Mikoa ya Kusini ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikawa ndiyo base kubwa ya wapigania uhuru wa nchi ya Msumbiji, Angola, Namibia, Afrika Kusini na Zimbabwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi imekuwa kama historia, lakini nakumbusha kwamba maeneo ya Lindi ikiwepo Nachingwea kulikuwa na maeneo ya Matekwe, Kwamsevumtini na kule Mtwara maeneo ya Samora na Lindi Vijijini, Lutamba, Ruvuma maeneo ya Namtumbo yale sehemu ya Seka Maganga na kwingineko ili kuwa ndiyo base na ma-camp ya wapigania uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yale pamoja na kuwa base tu lakini bado jamii husika ilikuwa nayo iko katika harakati zile, wanaotoka maeneo yale wanafahamu sana. Hivyo basi, wakati ule sasa, wakati wote wa harakati wa kupigania uhuru mikoa ile ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ilikuwa ni vigumu kwa wawekezaji kwenda kuwekeza kule kwa sababu wakati wowote Mreno anaweza akaja akaleta vurugu kule na wengine, kwa hiyo, hakukuwa salama. Hivyo tukaja kujikuta kwamba maeneo yale kwa namna fulani yakawa nyuma kimaendeleo, huo ni ukweli usiopingika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya harakati zile kwisha maeneo yale sasa Halmashauri husika zikaendeleza maeneo yale, wakaanzisha Sekondari zile za Matekwe na kwingineko, lakini ni juhudi za Halmashauri husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa baada ya kufanya hivyo nini ushauri wangu. Nashauri hivi tunaomba kwa Wizara hii ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa wizara hii naamini kabisa inaongozwa na Mheshimiwa Mama Mulamula na Naibu Waziri na timu yote ya Wizara ya Mambo ya Nje naamini kabisa wanavyofika wakuu wa nchi hizi za Kusini mwa Bara la Afrika tulizopambana kwa kiasi kikubwa kuwakomboa tunaomba muwaambie na muwalete maeneo ya Nachingwea na kule Ruvuma ili waje waone yale makambi, waje waone jitihada zile tulizozifanya sisi wenyewe ndani ya halmashauri husika bado hazitoshi tunaomba mchango wao, tunaomba waje waweke wafanye jambo fulani kama ni la maendeleo ili tuone kumbukumbu kubwa ifanyike kama inavyofanyika sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumzia hii kwa uchungu kweli, tumeachwa hivyo na ndiyo hiyo naona kama vile historia inajiendeleza vile kwamba kila kitu tuko hivyo tuko nyuma tu…

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Zuberi Kuchauka.

T A A R I F A

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe Taarifa mama yangu anachokizungumza ni kweli kabisa na ndiyo maana Mikoa ya Lindi na Mtwara miaka ya nyuma ilikuwa mikoa ya adhabu kwamba mtu akifanya makosa anapelekwa mikoa hiyo na mikoa hiyo haikuendelezwa ni kwa sababu tu ya hayo makambi ya hiyo vita za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla Ungele, malizia mchango wako.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napokea hiyo taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili siyo jambo geni kwa watu uliowafanyia hisani wakashukuru na kama mtu hashukuru basi kama kunauwezekano wa kumkumbusha. (Makofi)

M imi naamini kabisa watakapoletwa wale viongozi kule wakaona wakasema hapa ndiyo ilipokuwa camp fulani, hapa ndiyo ANC walikuwa hapa, watakuwa na uchungu fulani wa kuweka jambo fulani vinginevyo wala hawafahamu kwa sababu wako kwenye neema sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ndiyo ombi langu na hii imeshatokea na kwingine na kwingine, siyo ajabu hili ninalolizungumza, wakipelekwa kule wakaja kuona hali halisi ninaomba, ninaomba, ninaamini kabisa Mheshimiwa Mulamula ninakuaminia, ni mama, una uchungu wa nchi hii, ninaomba hilo uliweke katika priority naomba utuangalie kwa kila hali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali yayote namshukuru Mwenyezi Mungu kuturuzuku uhai na afya njema. Pia napongeza kazi nzuri inayofanyika na Wizara hii muhimu na naona viongozi wake wapo mahiri; na hata kazi hiyo imejionyesha hasa wanaposimamia miundombinu. Sisi kama kamati tulitembelea maeneo mbalimbali kwa ajili ya miradi ya ujenzi tumeona kule Arusha Technical, kule MUST Mbeya na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri ambaye tulikuwa naye kwenye ziara; kwa kweli ni mahiri yeye kweli ni quantity surveyor mzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo kazi ya mitaala inayofanyika na Wizara hii. Mitaala hii nasisitiza ilenge kuandaa vijana wetu kwenye ufundi stadi pamoja na kilimo, biashara na vinginevyo ambavyo vitawawezesha vijana hawa kumudu maisha badala ya kuendelea kutegemea kusubiri ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa najikita Mkoa wa Lindi; Mkoa wa Lindi vijana wale wanahitaji elimu ya fani mbalimbali. Pale Lindi Manispaa tuna Chuo cha VETA pale Mitwero, lakini chuo kile kinakabiliwa na uhaba wa wakufunzi kiasi kwamba hata malengo yanayotakiwa kufundishwa pale vijana wanakosa. Hivyo basi, tunaomba Wizara ifike muda mwafaka wawapatie wakufunzi pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo kule Nachingwea kwenye kambi ya Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa tuna chuo kidogo cha ufundi. Chuo kile kinawezesha vijana wanachingwea, Liwale, Ruangwa na kwingineko kote Mikoa ya Lindi na Mtwara kupata ujuzi wa ufundi stadi. Hata hivyo, chuo kile ni kidogo. Hivyo tunaomba Wizara ya Elimu ishirikiane na Wizara ya Ulinzi kukipanua chuo kile ili kitoe mafunzo kwa watu wengi na kwa stadi mbali mbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana wakati wa Bunge la Bajeti niliuliza swali kuhusu uzio wa Chuo cha Ualimu Nachingwea, na nikapata jibu zuri tu, kwamba fedha zimetengwa. Lakini hadi leo ninavyozungumza bado fedha hazijaenda na bado kazi haijafanyika. Sasa imefikia muda sasa naomba fedha hizo zipelekwe pale kwa ajili ya ujenzi wa uzio ili kuhakikisha usalama wa vijana wetu wanaosoma chuo cha uwalimu Nachingwea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mpango wa Chuo Kikuu Dar es salaam kujenga tawi kule Mkoa wa Lindi, pale Lindi Mjini; lakini hadi sasa hivi kasi yenyewe inavyokwenda bado si nzuri. Naomba kwa Wizara hii, chonde chonde, shughuli ile iharakishwe ili vijana wa Mkoa wa Lindi na kwingineko wapate elimu ya fani mbalimbali ili nao waweze kujiajiri kwaajili ya kumudu maisha na kuondoa umaskini unaokithiri katika maeneo yale. Ninaomba sana, sana katika Wizara hii waangalie elimu kwa eneo la pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami nichangie. Napongeza juhudi kubwa za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza miundombinu katika afya, elimu na sekta nyingine, hilo tunashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu unajikita kwenye Wizara ya Elimu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Taarifa ya Kamati imeainisha kabisa upungufu wa walimu kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nafuatilia hata taarifa ya leo, kwa mfano Wilaya ya Kilwa kule Mkoa wa Lindi, mahitaji ni walimu 1,406 wa Shule ya Msingi lakini waliopo ni 774, upungufu ni walimu 632. Hili ni tatizo kubwa. Nini maana yake? Upungufu wa walimu unaleta kuzorota kwa elimu na mwisho wa siku matokeo mabovu kwenye ufaulu wa wanafunzi. Kwa mfano, mwaka 2022 Wilaya ya Kilwa ni asilimia 75 ya wanafunzi walifaulu Darasa la Saba na ndiyo ilikuwa ya mwisho kwa Mkoa wa Lindi. Hii inasikitisha sana. Kama wengine walivyoendelea kusema kwamba ni changamoto, kukiwa na walimu wachache, kazi inakuwa kubwa.

Mheshimiwa Spika, kingine inasabisha utoro wa wanafunzi. Mwanafunzi anakuja, lakini hapewi kazi ya kushughulika. Kama tunavyofahamu, mwanafunzi huwa anashughulishwa. Wale walioko kwenye sekta ya elimu wanafahamu na wale walimu kwamba mwanafunzi lazima ashughulishwe. Ila kunapokuwa na uhaba wa walimu, mwanafunzi anakuwa wakati fulani hana chochote cha kufanya, basi anaona kesho yake wala kesho kutwa, wala mwezi ujao, asiende shuleni, maana anapoteza muda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini matokeo ya upungufu wa walimu shuleni? Kunakuwa na utovu wa nidhamu kwa wanafunzi. Kama tunavyofahamu, walimu hawa ndio washauri wa watoto hawa, lakini kunapokuwa na uhaba wa walimu, inaleta utovu wa nidhamu kwa watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia upungufu wa walimu unaongeza uzito wa kazi, yaani kunakuwa na increased workload. Hii ndiyo inaleta msongo wa mawazo kwa walimu hawa. Hata kimwili mwalimu yule anachoka kwa kazi nyingi. Hata Wabunge wengine kwenye michango yao walisema kwamba hata maandalizi ya masomo pia, siyo tu suala la kusimama darasani ukafundisha, lakini kuna maandalizi ya masomo, pia kuna kusahihisha, kuna kumpa ushauri yule mwanafunzi baada ya kusahihisha. Hili yote tunawapa kazi walimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho wa siku unaweza ukakuta hata vitendo vingine vya walimu, behavior nyingine wanazokuwa nazo walimu shuleni, na hata wakaleta mazingira fulani ya kuwafanyia ukatili fulani watoto hawa tunaowapeleka, ni kwa sababu ya upungufu wa walimu, pia msongo wa mawazo na ndiyo hiyo inaathiri hata afya ya akili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili tusipoliangalia huko tunakokwenda walimu watakuwa na changamoto ya afya ya akili, watoto watakuwa na changamoto ya afya ya akili, hata wazazi na jamii pia. Kama tunavyoona viashiria vinavyoendelea sasa hivi. Sasa tusifike huko. Naamini kabisa tunaweza tukanusuru jambo hili. Ni wakati umeshafika kwa Wizara yetu ya Elimu pia na Wizara husika ya kuajiri, hebu tuangalie tuweke mkakati, kama siyo ajira zile permanent, basi hata za mkataba ili angalau siku hadi siku inaendelea kupunguza tatizo hili la stress, na kadhalika, hata matokeo ya wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni hayo tu nilikuwa nayo katika sekta hii ya elimu na ninashukuru sana. Ninaamini mamlaka husika imesikia, itafanya maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichagie hoja ya hotuba ya Waziri Mkuu ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2023/2024 na namshukuru Mungu kwa zawadi ya uzima na afya njema.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo Watanzania, miaka miwili ya uongozi wake tumeshuhudia ubora wa miundombinu madarasa na vituo vya afya.

Mheshimiwa Spika, napongeza kazi nzuri inayofanywa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango. Pia nampongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa umahiri wa kazi kubwa anayofanya kumsaidia Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, mkoa wa Lindi haujaunganishwa na mkoa wa Mtwara au mkoa wowote kwa barabara kwa kiwango cha Lami. Tunaomba barabara inayotoka Masasi kupitia Nachingwea hadi Liwale ijengwe kwa kiwango cha lami mwaka huu 2023/2024, tafadhali tafadhali tumeahidiwa mara kadhaa haifanyiki.

Mheshimiwa Spika, tunaomba pia kupata maji safi na salama katika Kata za Ngunichile, Lionja, Mbondo kule Wilaya Nachingwea, hali mbaya bado akinamama wanahangaika kutafuta maji, wanakesha kutafuta maji hii ni hatari kwa usalama.

Mheshimiwa Spika, tunaomba ujenzi wa viwanja vya ndege Nachingwea na Lindi vijengwe kwa kiwango cha lami. Hii ni kwa sababu ya usalama, pia kinatumika na Mheshimiwa Waziri Mkuu anapoenda jimboni kwake Ruangwa, lakini pia kuna machimbo ya madini pale Nachingwea na Ruangwa, hii itavutia wawekezaji ndani na nje ya kupata usafiri wa uhakika, lakini pia Nachingwea kuna vikosi vya majeshi ya Jeshi la Wananchi Tanzania pia ni kwa sababu za kiusalama na utendaji kazi wao.

Mheshimiwa Spika, lakini pia Lindi kuna mradi mkubwa wa LNG hivyo kuhitaji usafiri wa ndege kwa saa 24 na wenye kiwango cha lami kwa mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kujali afya za Watanzania, na wote tunashuhudia miundombinu mbalimbali imejengwa sehemu zote nchini Tanzania kwa ajili ya huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, pia hata bajeti naona inaendelea kuongezeka kidogo kidogo kwenye Fungu Na. 52, lakini naamini Mheshimiwa Rais kwa sababu anajali afya ya Watanzania, ataendelea kuongeza siku hadi siku.

Mheshimiwa Spika, pia napongeza Wizara ya Afya; Mheshimiwa Ummy Mwalimu na timu yake yote mpaka kule vijijini kwenye ngazi ya kaya, watoa huduma za afya wanaendelea kutoa huduma na ushauri nyumba kwa nyumba.

Mheshimiwa Spika, najikita kwenye magonjwa yasiyoambukiza. Magonjwa yasiyoambukizwa ni tatizo kubwa na ni kilio kikubwa nchini Tanzania, pia ni gharama kwenye matibabu na athari yake ni kubwa sana. Wote tunashuhudia, miaka iliyopita hakukuwa na tatizo kubwa la shinikizo la damu, wala moyo wala sukari, lakini sasa hivi kila familia, na kama siyo kila familia hiyo, basi hata jirani yako anakumbwa na tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sababu za magonjwa yasiyoambukiza, machache ni mtindo wa maisha tunayoishi, vyakula vyetu, kutokufanya mazoezi, utumiaji wa tumbaku, matumizi makubwa ya sukari na kadhalika. Vitu hivi vinaweza vikazulika. Ukubwa wa tatizo, tunaona wakati wa janga la UVIKO lilivyoshamiri wagonjwa katika hospitali moja kule Dar es Salaam ilitoa taarifa kwamba asilimia 86 ya vifo ilitokana na wagonjwa ambao tayari walikuwa na kisukari, lakini asilimia 65 ya vifo vile vya UVIKO 19 tayari wagonjwa wale walishakuwa na shinikizo la damu na asilimia 45 tayari walishakuwa na pumu. Hivyo unaona magonjwa yasiyoambukiza ukiwa nayo, ukipata ugonjwa mwingine hali inakuwa ngumu zaidi.

Mheshimiwa Spika, tunaona pia hata mfuko wetu wa Bima ya Afya unalemewa kutokana na magonjwa yasiyoambukiza. Hata Mkoa wa Lindi kwenye Wilaya ya Nachingwea kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wenye magonjwa yasiyoambukiza kama presha na kisukari.

Mheshimiwa Spika, sasa nini kifanyike? Ni ushauri wangu kuwa imefikia wakati sasa naomba tume maalum ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza ianzishwe, kama vile tulivyoanzisha TACAIDS. Kwa nini nasema hivyo? Tunaona sababu zinazoleta magonjwa yasiyoambukiza nyingi ni za kijamii; mtindo wa maisha, kutokufanya mazoezi, consumption ya tumbaku; pia tunaona sababu nyingi ni za kiuchumi. Sehemu nyingi katika nchi yetu, tumbaku ndiyo uchumi, miwa ndiyo uchumi, na pombe ndiyo uchumi. Sasa tunafanye kujikwamua? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiachia suala la magonjwa yasiyoambukiza kwenye afya peke yake itakuwa ngumu kama ilivyotuumiza kwenye UKIMWI. Hivyo basi, tuliache jambo hili, afya waendelee kushughulikia matibabu, lakini pia kijamii tuendelee kuwa na mkakati maalum wa kuendelea kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza. Tunaona hata wakati wa masuala ya UKIMWI, sasa hivi tayari wenye maambukizi ya virusi vya UKIMWI wana uwezo kabisa wa kutambua kwamba hapa nifanye jitihada za kuzuia ili nisipate maambukizi mapya. Pia wale hawajapata kabisa, jamii inaelewa kwamba tusipate maambukizi mapya.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi, naomba hata kwenye magonjwa yasiyoambukiza, suala hili tuliache kwenye jamii, kwa sababu ni suala mtambuka, kila sekta ina husika kwenye masuala haya katika kuhamasisha kuzuia magonjwa yasiyoambukiza. Vinginevyo tutaendelea kugharamika bajeti itaendelea kuwa kubwa na kila familia itaendelea na simanzi kwa sababu ya athari ya magonjwa yasiyoambukiza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami nichangie hoja ya Wizara ya Afya. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kunipatia uhai hata sasa hivi niko naendelea na shughuli hii hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawapongeza Mheshimiwa Ummy Mwalimu Waziri wa Afya na Naibu wake Dkt. Molel na timu yote ya Wizara ya Afya hakika mnafanyakazi na tunawaombeeni usiku na mchana Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii ya Wizara ya Afya inawezeshwa na Jemedali mwenyewe Mkuu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kipaumbele kwa huduma ya afya kwenye nchi yetu hata amewezesha kujenga vituo vya afya, zahanati, hospitali kuanzia ngazi ile kule ya kaya, ngazi ya msingi hadi ya taifa kwa kweli tuna mshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa zahanati hizi na utoaji wa vifaa tiba kwenye zahanati hizi na hospitali hizi zimefanyika nchi nzima hata sisi watu wa Mkoa wa Lindi tumefaidika ni wanufaika wakubwa wa huduma hizi tunashukuru sana. Hata kule Nachingwea kumejengwa ICU nzuri na vifaa tiba vimekwenda na watalam wamekwenda ingawaje bado hawatoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huduma za ICU na huduma za emergency ni muhimu sana zinavyojengwa kwenye hizi Hospitali zetu za Wilaya kwa sababu jambo hili la kubadilika afya zetu inaweza ikabadilika hata wakati unatembea vizuri hivi lakini hali yako inaweza ikabadilika muda wowote lakini kunavyokuwa na hizi huduma za emegency na huduma za ICU unaweza maisha yakanusurika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan tunamshukuru sana. Lakini pia kuna huduma bobezi tumeziona kwenye wasilisho la Mheshimiwa Waziri, huduma bobezi hizi zinaboresha na zinatufanya Tanzania tuwe kitovu cha huduma hizi muhimu na pia kufanya nchi yetu iwe tuwe katika eneo lakuwa na medical tourism. Ukienda pale Ocean Road, ukienda pale Muhimbili, ukienda pale MOI, ukienda pale JKCI hakika mambo ni mazito yanayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nijikite kwenye mafunzo, eneo hili la mafunzo naweza niaeleza sana lakini muda hautanitosha kwa sababu ni eneo ambalo limelifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 30. Mafunzo ya Afya, mafunzo haya ya afya kwa vyuo vya kati tunaomba mafunzo hayo yaboreswe kwa sababu wahitimu hawa tunaowapata kwenye eneo hili la huduma za afya za kati, mafunzo ya afya ya kati hao ndiyo wanaenda kutumika kwenye zahanati, kwenye vitu vya afya na ndiko kule kuna mapungufu na ndiyo watu wetu wengi wako kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba katika hili miundombinu ya maeneo yale hasa kwenye vyuo vya Serikali naomba viboreshwe. Kwa mfano kuna jengo pale Nachingwea limeanzishwa lakuendelea kuboresha kile chuo ambacho mafunzo yake yalisitishwa na NACTE wakati ule ambayo sasa hivi ni NACTVET tunaomba na chuo kile kikamilishwe na jengo lile likamilishwe maana hata sasa wananchi wale wa Nachingwea na Lindi kwa ujumla tunategemea chuo kile ndiyo cha uuguzi pekee cha Serikali kwa Mkoa wa Lindi. Lakini jengo lile limesitishwa, hatujui kinachoendelea kwa kweli wananchi wale wana sintofahamu nini kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika hii huduma ninafurahishwa sana leo nilivyosikia yale mafunzo ya integrated and comminated community heathy worker. Nimefurahi sana Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu alivyosema yale mafunzo yanakuja tena ni program ambayo anaileta tena ile itakuwa ni tija kubwa katika jamii yetu kwa sababu wale watakuwa kwenye ngazi ya jamii kule. Wale watashughulika hasa kwenye kutoa ushauri na huduma mbalimbali kuhusu magonjwa yasiyo ambukiza na mambo mengine ambayo yangefanya yawe makubwa zaidi mpaka yakahitajika huduma kubwa zaidi. Hili napongeza wizara, nawapongeza sana Mheshimiwa Ummy Mwalimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna huduma za mama na mtoto, huduma hizi za mama na mtoto naomba ziboreshwe mtoto wa chini ya miaka mitano, mama mjamzito bado kuna maeneo mengine Mheshimiwa Waziri bado wamama wale wanahitajika kununua vifaa kwenda kujifungua tafadhali, tafadhali ninaomba suala hili liangaliwe. Kuna maeneo mengine Tanzania kuna shida mtu anakosa hata shilingi 500 sasa mtu huyu atakapoambiwa anunue vifaa hivi, kifaa hiki, kifaa hiki ili akajifungue hiyo tena itakuwa ni shida na tutazidi kuongezea ule uzito wa tatizo la vifo vya wazazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, yote kwa yote ninawapongeza sana Mawaziri hawa na Serikali yote ya Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi wanayofanya kuboresha afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii nami nichangie. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Naibu wake, Katibu Mkuu na timu yote ya Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii na wote kutoka kule ngazi ya Mikoa na Halmashauri kwa kazi kubwa wanayoifanya usiku na mchana. Hakika wanafanya kazi nzuri, inabidi kuwapongeza.

Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee nazipeleka pia kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya kujali jamii ya Tanzania na makundi maalum hasa wamachinga, ambao tunaona kabisa hata kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameeleza kabisa kwamba Mheshimiwa Rais ametoa hizo shilingi bilioni 22.9 hivyo, ombi langu ni fedha hizi zitolewe kwa wakati sasa hivi ili zifanye kazi inayopaswa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najikita kwenye eneo la ustawi wa jamii. Kazi ya ustawi wa jamii ni kubwa kwenye Wizara hii na tumeona kuanzia ngazi ya Taifa hadi kule kwenye Halmashauri. Kazi yake kubwa ni kuimarisha jamii zetu. Tumeona hata taarifa ya Kitaifa, imesema wimbi kubwa la watoto wa mitaani limepungua kwa asilimia 38. Pia hata migogoro ya ndoa imepungua kwa asilimia 27 hii ni jitihada kubwa kweli kwa Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata pia kwa Mkoa wa Lindi tunaona pamoja na maafisa ustawi wa jamii wachache, wako 19 tu lakini bado kumefanyika kazi kubwa na wamebaini ukatili wa kijinsia umepungua kwa kiasi kikubwa sana. Mashauri kama 1,105 yamefanyika kufuatilia changamoto ya ukatili wa kijinsia. Pia wamesimamia msamaha wa matibabu kwa walengwa zaidi ya 33,000 kwa Mkoa wa Lindi na mengine yote hayo ni mafanikio. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeona mmomonyoko mkubwa kweli wa maadili na maadili haya yanaanzia ndani ya familia, familia ni kila kitu, naamini kabisa wote tulioko hapa tumetoka kwenye familia na tunazihudumia familia. Kwa hiyo, kila kitu katika maisha kinaanzia kwenye familia; maendeleo yoyote, familia, sasa tunaona familia zetu zimeendelea kuathirika na mmomonyoko wa maadili, hili jambo ni hatari sana. Tumeendelea kuhangaika na elimu, tumeendelea kuhangaika na afya, tumeendelea kuhangaika na REA hii ya umeme vijijini, vyote hivyo ni kwa ajili ya maendeleo lakini bado kama hatutazingatia maadili ndani ya familia zetu itakuwa ni bure kabisa, itakuwa ni shida kabisa, mwisho wa siku tutakuja kupata kizazi ambacho wala hata hiyo elimu yenyewe haitaonekana, wala hata afya yenyewe haitaonekana. Mimi naomba haya mambo yote yaendane sambamba, tuendelee kuyaboresha maadili ndani ya familia na miradi mingine tuendelee kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunavyoona taarifa ya utafiti wa Serikali na UNICEF, walibainisha kwamba asilimia 60 ya watoto walioathirika katika ukatili wa kijinsia imetokea majumbani, pia asilimia 40 imetokea shuleni, kwa hiyo bado naendelea kusisitiza katika mchango wangu huu, nakumbuka hata mwaka jana nilichangia, bado mtoto huyu hayuko salama, kila eneo analokwenda. Hata mchangiaji mwingine alisema, hata kwenye vyombo vya habari, hata kwenye makanisa, hata kwenye misikiti, bado huko kuna unyanyasaji wa kijinsia, mtoto huyu hayuko salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunaona Wizara imekuja na mpango mkubwa huu wa malezi na makuzi ya mtoto huyu. Mimi naomba kwa kuwa vitendo hivi vya mmomonyoko wa maadili vimekithiri na mtoto huyu hana usalama wowote kila aendapo, ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa ninaomba na Wabunge wenzangu tusaidiane, tuungane mkono katika hili kwa sababu vita hivi ni vyetu sote. Kuwepo kabisa na mkakati wa Kitaifa vituo hivi vijengwe kimkakati kabisa, viwe vituo vya kielelezo kwa nchi nzima. Vituo hivi ndivyo vile tulivyosikia hata Mheshimiwa Waziri alivyosema, kwamba vituo hivi ndiyo vitamlinda mtoto kiakili, kimwili, kiafya ili angalau kumlinda asogezesogeze umri ambao ataweza kujitetea mwenyewe. Kwa sababu tayari akiwa mdogo hana utetezi wowote, akiwa wapi hana utetezi wowote, wazazi wake wanakwenda kazini wanamwacha mtoto hana utetezi wowote. Tunaomba tafadhali jambo hili lizingatiwe ili angalau mtoto huyu afikie umri ambao ataweza kujitetea mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba wote tuungane katika vita hii ya kupingana na jambo hili ili angalau kwenye jamii yetu lipungue kwa namna fulani ili tuwe na Taifa lililo na maadili mazuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mungu kwa nafasi hii na pumzi ya uhai. Natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi anayofanya ya ujenzi na huduma zingine katika jamii yetu na hasa Mkoa wa Lindi. Pongezi nyingi pia zimuendee Mheshimiwa Wizara, Mheshimiwa Naibu Mawaziri na watendaji wote wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kazi kubwa wanazofanya nzuri kona zote za nchi hii ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na sisi Wanalindi tunapongeza na tunamshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi inayofanyika ya ujenzi wa barabara kutoka Nanganga kwenda Ruangwa na hatimaye itaenda mpaka Nachingwea; kwa kweli tunashukuru sana. Tunaona sasa hivi nuru ipo ya Mkoa wa Lindi kuunganisha kwenda Mkoa wa Mtwara kwa lami, tunashukuru sana, ilikuwa adha ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na tunaona ukurasa wa 11 katika Hotuba ya Mheshimiwa Waziri tunaona kuna huu utaratibu wa EPC + Financing, tumeona utaratibu wa Barabara ya Masasi – Nachingwea kwenda Liwale unaenda kufanyika, zile kilometa 175 tunaenda kuziona kwa kutumia lami. Ahsante sana tunashukuru sana Wananachingwea, Wanaruangwa, Wanaliwale, Wanamasasi na Mkoa wa Lindi kwa ujumla. Barabara hii ilikuwa kweye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 ukurasa wa 75. Sasa Wanalindi wanashukuru inaenda kutekelezwa, ushauri wangu katika ujenzi wa barabara hii, wakandarasi watakapofika kwa utayari wa kujenga barabara ile, ninaomba, kwa kuwa Nachingwea ni katikati, ni center, basi watakapokuja na mitambo yao waielekeze mingine ielekee barabara ya kwenda Masasi. Ifanye kazi kuelekea Masasi na mitambo mingine ielekee Liwale, ifanye kazi kuelekea Liwale ili kazi hii ifanyike kwa wakati mmoja. Watafurahi sana watu wale, wananchi wa Nachingwea na kwingineko kote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo pia kwa habari ya viwanja vya ndege. Tunaona Uwanja wa Ndege Nachingwea na Uwanja wa Ndege wa Lindi, imeelekezwa sana, tunaendelea kuomba sana, tunaomba viwanja vile viwekwe lami ili viwanja vile vitumike wakati wote wa masika na wakati wa kiangazi. Kwa sababu sasa hivi Lindi kunakuja LNG, lakini pia Nachingwea viwanja vile vinatumika pia kusafirisha hata viongozi wa kitaifa. Tukiacha hata uchumi unaoenda kuongezeka kwenye maeneo yetu, tunaomba Waziri muangalie sana Viwanja wa Nachingwea na Lindi kwa upande wa lami. Lakini pia Mbunge wa Nachingwea alishasema wale waliopisha maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa viwanja vile basi walipwe fidia yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbushia Barabara ya Kibiti – Lindi ina lami tayari lakini kuna maeneo Mheshimiwa Waziri korofi. Kwa mfano kuna mahali panaitwa Muhoro, wameweka pale viraka viraka ambavyo ni shida, ajali zinatokea mara kwa mara, lakini kuna maeneo kutoka Somanga kuja Nangurukuru napo kuna changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona kuna eneo linaitwa Kiranjeranje, lakini pia kuna eneo kuanzia pale Kirangara kwenda karibu na Mchinga kwenye ile njia panda ya kwenda Moka, nako pale barabara imeonyesha kuzama kuzama na kuinuka, kuzama na kuinuka. Kama driver akiwa ni mgeni maeneo yale au ameenda kwa speed pale kuna kutokea ajali mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusingependa wananchi wapate ajali, tusingependa watu wawe navilema vya kudumu na tusingependa vifo vitokee. Tunaomba marekebisho hayo yafanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutuangalia Wananachingwea, kutuangalia Wanalindi, sasa hivi tunaenda kufunguka kuwa na mawasiliano na mikoa mingine kupitia lami. Hicho ni kilio cha muda mrefu, kulikuwa na vumbi, kulikuwa na hofu, kulikuwa na mahangaiko. Ukishafika Masasi ukiwa kwenye basi utasikia wanasema, enhee, sasa tunaenda Tanganyika, tunaenda kutanganyika sasa. Kwani hakuna viongozi? Haya nayasema kwa sababu anayesifia mvua imemnyeshea. Nimeshasafiri kwenye mabasi hayo mara kwa mara, nafahamu hali ilivyokuwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli sasa hivi sisi Wanalindi tunasema tuna imani na barabara hizi kwamba zinaenda kujengwa. Tuna imani kabisa kwa sababu hata vitabu vinasema kwenye Waebrania 11:1: “Imani ni kuwa na uhakika wa mambo yatarajiwayo, bayana ya mambo yasiyoonekana.”

Mheshimiwa Spika, sisi Wanalindi tuna imani sasa hivi kama ile barabara ya lami kutoka Masasi - Nachingwea – Liwale tumeipokea hivi tayari ni kama vile tunapita. Tunaamini hilo Mheshimiwa Waziri ataenda kutekeleza, barabara itajengwa na Wanalindi watafarijika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipa nafasi hii nami nichangie kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. Napongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na juhudi aliyoifanya kwenye ile shughuli ya Royal Tour ambayo ameendelea kuitangaza Tanzania katika uso wa dunia, lakini pia kuongeza mapato ya Taifa, kuongeza idadi ya utalii wa ndani na nje ya nchi, tunamshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napongeza juhudi za Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutatua migogoro na kushirikiana na wizara hii kwa ajili ya kuweka hali iwe ya usalama katika Nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona amepambana na amejitahidi sana kwa shughuli ile kwa kazi ile na kadhia ile iliyokuwa ya Ngorongoro lakini pia na nchi nzima kona zote wanashuhudia utendaji wake wa kazi wa uweledi na ufanisi mkubwa, tunamshukuru sana. Alikuja hata maeneo ya huko Lindi, maeneo ya Nachingwea akaenda kuona na kuwapa pole wananchi waliotajwa na kadhia ya Tembo mwaka jana lakini pia akawapatia chakula na kuwapa pole wale walioathirika kwa kuuliwa na ndugu zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kwa kazi ya Wizara hii, Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii ya Maliasili na utalii hata kwenye ngazi ya mikoa kule na wilaya mbalimbali kwa kweli tunashukuru utendaji wao wa kazi tunauona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wizara hii ndio inatunza ule uhalisia wa siri ambao Mwenyezi Mungu alitupatia. Tuendelee kuitunza ardhi na miti na kila kitu ili itupatie usalama na afya kwa ujumla kwa kweli tunawapongeza sana. Sisi Wanalindi tunaahidi kabisa kutunza vyanzo vile vya maji na misitu na tuona kwa kiasi kikubwa Mkoa wa Lindi unachangia maji na uhalisia na uasili wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ili kuhakikisha kabisa sustainability ya ile bwawa na tumeona matokeo yake na mafanikio yake tutayaona kama waziri wa jana aliyekuwa amemalizia ku-present jana katika ile Wizara ya Nishati. Tunaona kazi ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza pia kwa kazi ya Wizara hii ambayo inaendelea kutunza Utalii. Hata sisi Lindi pia tuna vivutio vingi vya utalii. Tunaona kule Kilwa Kisiwani, Tendaguru, tunaona kule pia kwenye Bwawa ambalo lina viboko ambao wana rangi ya pink ambao ni nadra sana katika dunia hii kuwaona. Kuna vivutio vingi, karibuni sana Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi ni mojawapo ya mikoa iliyoathirika sana katika kadhia ya tembo. Hali kule siyo shwari, ni tete. Tumeona mwaka 2022 Wizara hii ilijitahidi, katika mikakati yake mojawapo ni kupeleka ndege kule. Walipeleka ndege ya kuswaga wale tembo kuwapeleka kwenye hifadhi na jambo lile lilifanikiwa na wananchi walifurahia sana wakaendelea na kilimo na maendeleo kwa ujumla. Tuliwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanyama wale wamerudi tena. Wamerudi tena kwa kasi kubwa, wako makundi kwa makundi, wameendelea kuharibu mazao, wameua watu na wanaendelea kuua kila kuchapo. Wilaya zile za Nachingwea, Liwale, Milola, Kilwa na maeneo yote yale kule yameathirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali siyo shwari. Hivi sasa ninapozungumza, maeneo yale kuna njaa kali. Wananchi wale hawana chakula, watoto hawaendi shuleni kwa sababu ya tembo. Tembo wanazagaa kama vile unavyoona ng’ombe walivyozagaa. Kwa kweli hali siyo shwari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua pia mchango mkubwa…

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

TAARIFA

MWENYEKITI: Mheshimiwa taarifa.

MHE. HAMIDA M. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Tecla Ungele kwamba hali kweli siyo shwari, kuna tembo wengi ambao wanazagaa katika maeneo ambayo ameyataja, lakini kwa nyongeza sasa kuna fisi ambao wanasumbua wananchi nawanakula wananchi. Wananchi wameathirika sana na wanyama hawa, ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ungele, unapokea taarifa?

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua pia mchango mkubwa anaofanya Mkuu wa Mkoa wetu wa Lindi Mama Zainab Telack na Wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Lindi na viongozi wengine, na pia hata Jeshi la Uhifadhi Kanda ya Kusini wanafanya kazi kubwa kweli. Wakiitwa mahali wanakwenda. Ninachosema ni kwamba, wahifadhi wale wamezidiwa na idadi ya tembo. Nakumbuka Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, Mbunge wa Mchinga alishukuru kwa kujengewa kituo pale Milola na kupatiwa Askari na gari jipya, tukafurahi sana, lakini bado Askari wale wamezidiwa. Namomba wapewe chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi tumezawadiwa na Mwenyezi Mungu kuwa na eneo kubwa lakini lenye rutuba na wananchi wa Mkoa wa Lindi ni wakulima wanaopenda kulima chakula, wakala chakula chao na mazao ya kilimo na mazao ya biashara. Sisi kwa desturi yetu tusingependa kupewa chakula. Mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi, anafanya kazi akapata chakula, kwa sababu tunaamini chakula cha kuletewa hakiwezi kukidhi mahitaji ya familia, lakini pia kwetu sisi ni fedheha kuletewa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi hali ilivyo, kuna ulazima kabisa Serikali ipeleke chakula. Wananchi hawana chakula, watoto wa shule hawana chakula, na pia hii kadhia ya tembo hii inaathiri hata utendaji wa Wizara nyingine, Wizara ya Kilimo watu hawalimi vizuri; Wizara ya Elimu, watoto hawasomi. Kwa hiyo, naona miaka ijayo 10, 20 au 50 kule tutaendelea kuwa masikini kwa sababu mojawapo ya kumkomboa mwananchi ni elimu. Sasa kama leo mtoto haendi shuleni kwa sababu ya kadhia ya tembo, unategemea tutaendelea kuwa na maisha gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini kifanyike? Nasema hili kwa maumivu na uchungu na unyenyekevu mkubwa. Tunaomba huo mkakati wa kurekebisha sheria na sera za uhifadhi ufanyike haraka iwezekanavyo. Tumesikia Kamati wame-suggest hicho kitu, lakini pia tunaomba fidia. Kuna watu walioathirika wale, tunaona kimya tu, hakuna kinachoendelea. Kuna watu wamekufa pale Nungunichile, Namikango, Iyonja, kule Barikiwa na maeneo mengi tu kule Liwale vifo vinaendelea siku kwa siku. Tunaomba fidia zao zifanyike angalau ndugu zao wafute machozi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kufanyike utafiti wa kina kwenye Wizara hii, kwa nini bado kunaendelea? Tulisema kwamba shoroba unapita mahali fulani lakini mbona sasa hivi ng’ombe ndiyo wamehamia kwenye vijiji vyetu kabisa na vijiji vile vilikuwepo miaka yote? Kwa nini sasa hivi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaomba ufanyike mkakati mkubwa wa kuondoa wale wanyama.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri afike kule Nachingwea, Liwale, Kilwa na Milola aje aone hali halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kunipatia uhai.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nakupongeza kwa kazi kubwa unayofanya kuongoza Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuona umuhumu wa kuwa na Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum. Amewateua Mawaziri Dkt. Dorothy Gwajima na msaidizi wake Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis na Katibu Mkuu Dkt. Zainabu Chaula na timu yao ingine yote mpaka kule kwenye halmashauri wanaendelea vizuri kufanya kazi kubwa, kwa kweli ni wapambanaji timu yetu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kujikita kwenye maeneo mawili na kama si matatu; la kwanza matukio kadhaa ya unyanyasaji wa watoto yameendelea kutolewa taarifa siku hadi siku, kila siku kunavyokucha mikoa yote, pembe zote za nchi hii, yanatisha sana na hii ni changamoto kubwa sana wakati mwingine najiuliza hapa ni nini? Ni changamoto ya afya ya akili ama ni kitu gani au ni mazingira magumu ya hali ya uchumi ni kitu gani. Hivyo takwimu mbalimbali zimetolewa kila mikoa na zinajulikana, lakini mimi nakuja na jambo la ushauri kwa Wizara hii. Kwenye miaka ya 1980s mpaka 1990s tulikuwa na changamoto kubwa kweli ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI na ilionekana kwamba suala hili ni la kiafya tu, na kwa kweli tulihangaika sana ilivyoonekana ni health sector peke yake washughulikie masuala ya UKIMWI, lakini pale ilipokuja kujulikana kwamba suala hili ni cross cutting, ni mtambuka ikaja ikarudishwa kwenye jamii na zikaanzishwa Kamati mbalimbali za kudhibiti UKIMWI kuanzia ngazi ya Taifa mpaka ngazi ya vijiji, tukaona kumbe suala la maambukizi ya virusi vya UKIMWI si matibabu peke yake lakini pia hata maambukizi yake yanaenda kwenye social culture issues. Kwa hiyo, inahitajika jamii ihusike mpaka kule kwenye ngazi. (Makofi)

Kwa hiyo, hata hapa naona kuna mazingira fulani yanayoendelea na hili suala la mambo ya unyanyasaji wa kijinsia, yakionekana ya ubakaji na mengineyo yanayofanana na hayo. Suala hili inabidi sasa muda umefika tuangalie jinsi ya kulitatua, tulirudishe kwenye jamii na wanaohusika sana kwenye jamii yetu ni wale wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wanahusika, wanakubalika sana kwenye ngazi ya jamii. Tulirudishe suala hili kwenye ngazi ya jamii ili uhusike na itakavyoendelea hivyo, basi elimu itolewe kwa kila jamii kuanzia ngazi ya kaya, familia na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa kufanya hivyo itaonekana huu ukimya tunaouona hata humu ndani tumeendelea kupiga debe hii ni sisi wakina mama tu ndani tangu imeanza kuchangiwa, sijaona akina baba kuna nini hapa? Kwa hiyo hapa tayari kuna tatizo social culture issues, mambo ya kijamii, mambo ya tamaduni zetu, kuna nini katika suala hili la ubakaji na mengineyo yanayofanana na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niendelee kwenye makazi ya wazee; tumeona kuna makazi 14 ya wazee nchi nzima na bado kuna wazee 271 tu wako maeneo hayo. Lakini mimi nilikuwa naangalia angalizo kama haya makazi tunasikia huduma zao bado siyo nzuri, hazitoshelezi na kweli Serikali haiwezi ikakidhi huduma zote za wazee. Sasa nini kifanyike, mimi nilikuwa nashauri kwamba huko tunakoenda ni vizuri kabisa huduma hizi za wazee ikapewa sekta binafsi na iruhusiwe kama kuna watu binafsi wanaweza wakaanzisha makazi ya wazee iruhusiwe ili wenye uwezo basi watalipia, kama wafanyakazi wanaweza wakatunza pensheni zao ikatunzwa kule baadaye wanapokuja kumaliza kazi wakiwa na umri mkubwa zaidi wanahamia kwenye makazi yale na huduma zao na fedha zao zinakuwa zimetunzwa kule, ni jambo linawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine nilikuona naona bajeti ya Wizara hii. Tumeenda kwenye taasisi mbalimbali ya Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii kwa mfano kule Rungemba kunahitajika miundombinu ile irekebishwe. Kwa hiyo, tunaomba bajeti katika item ya maendeleo iendelee kupewa kipaumbele, ipewe fedha kubwa ili marekebisho mbalimbali ya vyuo yawezekane ili kwenye vyuo vile kuwe mahali pazuri pa kujifunza na kufundisha walimu wetu na hata vijana wetu wanaotoka mahala pale. Kwa kufanya hivyo jamii yetu itakuwa na hali nzuri tukiboresha maendeleo ya jamii na kila jambo litawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya mimi kuchangia bajeti kuu. Awali ya yote ninampongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuweka kipaumbele kuridhia mradi wa LNG kule Lindi kwa hiyo sisi wana Lindi na Mtwara na Taifa kwa ujumla tunashukuru. Hili ninajua kabisa ni kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu. Ninampongeza pia Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na timu yake yote kwa kuja na bajeti kuu hii nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nitajikita kwenye Mkakati wa Taifa wa Kupambana na Kukabiliana na Ukatili katika Jamii. Nakuja na takwimu chache tu angalau, Mpango Mkakati wa Kutokomeza Ukatili kwa Wanawake na Watoto (MTAKUWA) mwaka 2017/2018 hadi 2021/2022 ulidhamiria kupunguza ukatili katika jamii yetu kwa asilimia 50. Ukatili huu ni wa kimwili, kisaikolojia, kingono na hata kiuchumi. Pia kuna taarifa, walifanya hawa MTAKUWA, kwamba kati ya wanawake watano basi mmoja ame-experience ukatili wa kingono. Lakini pia kati ya wasichana watatu mmoja amepitia ukatili wa kingono. Kati ya wavulana saba mmoja amepitia ukatili wa kingono katika maisha yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tafiti za Serikali na UNICEF zimetoa taarifa kwamba ukatili huu kwa asilimia 60 unatokea nyumbani na kwa asilimia 40 unatokea shuleni. Hii ni hatari sana. Mtoto huyu atapona namna gani? Kama akinusurika ukatili pale nyumbani basi akienda shuleni atapata ukatili wa kingono na aina nyingine. Hili ni janga kubwa, tusilifumbie macho, hali siyo shwari. Madhara yake ni nini kwa ukatili huu; vijana wetu na wanawake wanaathirika kimwili, hata viungo vya uzazi vinaathirika lakini kikubwa zaidi afya ya akili inaathirika sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanapotendewa tendo hili la ukatili uwe wakingono iwe wa kiuchumi iwe wa kinini basi kijana huyu au mtoto huyu ana weka kumbukumbu zile kwenye sub conscious mind. Kinachotokea jinsi anavyoendelea kukua analeta ile event ama seen, inakuja usoni inakuwa kama screen inaendelea kum-disturb. Kwa maana hiyo sasa nini kinatokea; anakuwa na hofu hana ujasiri ni mwenye mashaka hata akienda shuleni hana mchango mzuri ndio wale unakuta hawana maendeleo mazuri kimasomo. Hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika Serikali yetu sasa, ninaona kwenye bajeti kuu hapa kuna rasilimali zimetengwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii imetengewa milioni 43; lakini pia afua maalum za kupambana na ukatili ni bilioni 2.65 kwa Mikoa yote. Ina maana katika Mkoa milioni 14 kwa mwaka. kwa wastani ni milioni moja kwa kila Halmashauri kwa mwezi. Hii ni hatari sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukatili huu ni vita kubwa. Sasa vita kubwa hii tunaenda na silaha kidogo sana. Ninaomba kabisa, bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii naomba iwe revised na iongezewe. Lakini pia kuna watendaji wetu kule, maafisa maendeleo ya jamii na maafisa ustawi wa jamii, hawa kazi yao kubwa ni kuhamasisha uchumi katika kaya na kuhakikisha kutokomeza mila na desturi potofu zinazosababisha ukatili pamoja na kuimarisha mahusiano katika familia pamoja na. hata hivyo, watu hawa kwanza ni wachache, tumeona katika taarifa, maafisa maendeleo ya jamii wapo asilimia 43 lakini maafisa ustawi wa jamii wako asilimia 97 tu nchi nzima. Sasa vita yoyote…

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa

T A A R I F A

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ustawi wa jamii upungufu ndio asilimia 97, sio kama alivyoongeza ndugu Mbunge. Ahsante sana.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tecla.

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, afisa maendeleo ya jamii kuna upungufu huo kama nilivyousema na afisa ustawi wa jamii pia upungufu wa asilimia 97.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwakuwa sababu mojawapo ya ukatili katika jamii yetu ni kutokana na changamoto ya uchumi, hivyo basi ile asilimia 10 iliyokuwa imepangwa kwa ajili ya kuhudumia jamii yetu; wanawake asilimia nne vijana asilimia nne, na wenye makundi maalum (walemavu) asilimia mbili ninaomba ibaki vile vile. Hata hivyo tulikuwa tunaomba hata iongezwe ifikie asilimia tisa kwa wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni hatari sana, kwa sababu hata kwenye halmashauri zetu ile tu iliyokuwa nne nne mbili (4:4:2) haitoshi. Bado kuna mlundikano wa maombi ya jamii yetu kuomba misaada hiyo ama mikopo hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tafani ninaomba tuiangalie jamii hii, tuangalie kuwakwamua hawa wananchi, hususani wanawake katika jamii yetu. Bila kufanya hivyo ukatili huu utaendelea na matokeo yake huko miaka 50 ijayo miaka 20 ijayo miaka 30 ijayo sijui tutakuwa na Taifa gani la Tanzania lisilojiamini na lisilokuwa na ubunifu kwa sababu tayari wameathirika na ukatili wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami nichangie hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipatia zawadi hii ya uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuleta ustawi na maendeleo ya jamii ya Watanzania. Nampongeza pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa ya kusimamia kazi za Serikali na pia kwa wasilisho zuri la bajeti na hotuba ya bajeti ya Wizara yake. Hotuba hiyo imesheheni mambo mengi ya sekta mbalimbali nchini zikiendelea kuleta maendeleo na kuchochea maendeleo. Pia nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zote zilizoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wanafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nauelekeza kwenye maeneo kadhaa. Hotuba ya Waziri Mkuu ina mambo mengi, lakini kutokana na muda, nitachangia maeneo machache tu. Kwanza, ni usafiri na usafirishaji. Tumeshuhudia miundombinu ikiboreshwa; barabara za mijini na vijijini na Watanzania wote ni mashahidi, lakini miundombinu hiyo imeharibiwa na mvua kubwa ya El-Nino. Tumeshuhudia maeneo mengine mawasiliano yalikatika. Kwa mfano kule Liwale, Barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale na Barabara ya Masasi - Nachingwea kwenda Liwale, Barabara ya kutoka Nanganga kwenda Ruangwa, zote zilikatika na maeneo hayo yalikuwa hayana mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni muhimu sana katika ustawi wa jamii, kusafirisha mazao, kusafirisha watu na kadhalika na maendeleo yote tu yanategemea usafiri. Ombi langu, barabara hizi zijengwe kwa umakini mkubwa kweli na kwa kiwango cha lami; vile vile Masasi – Nachingwea – Liwale, Nangurukuru kwenda Liwale na Daraja lile la Nanganga ambayo inaunganisha Wilaya ya Masasi na kule Ruangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia madaraja yajengwe kwa uimara mkubwa. Maeneo tuliyokuwa tumetegemea yawekwe makalvati, ndiyo hayo mvua hizi kubwa zimefika zikayavunja yale makalvati na kuyazoa kabisa, sasa hivi kumebaki wazi kabisa. Kwa hiyo, yatengenezwe madaraja makubwa na imara ya kupitisha maji katika maeneo mapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nachangia liko Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kuna program hii ya kukuza ujuzi kwa vijana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, vijana wamepata nafasi kwenda kusoma vyuo hivyo, tumeenda kule Rwazari kule Tabora Manispaa na kule St. Antony Manispaa ya Musoma na kwingineko, wanapata ujuzi wa ushonaji, useremala na mambo ya umeme na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, kwanza idadi ya vijana iongezeke na ichukue maeneo mengi ya Tanzania, kwa sababu maeneo mengi yana vijana ambao hawana ujuzi, lakini pia kuna vijana ambao wako kwenye makundi maalum, nao wanahitaji ujuzi, kwani nao wana umuhimu na wana vipaji vikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu lingine, vijana hawa wapatiwe vifaa vya kufanyia kazi wakishamaliza masomo. Tunawafundisha ujuzi pale, wanapata ujuzi vizuri sana na wenyewe wanafurahi sana, tumewaona tulipokuwa tumeenda wakati wa ziara za Kamati. Wanafurahi sana kupata ile nafasi na wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweke bajeti maalum ya kununua vifaa ili vijana wale wakishatoka kwenye mafunzo, wakisharudi majumbani kwao, basi kuwepo na mwendelezo wa kazi zile, wakajiajiri wenyewe na wakaendelee kufanya kazi ya kujipatia riziki, badala ya kutoka pale na ujuzi wao ambao hautakuwa na maana, kwa sababu wengine hawana uwezo wa kumudu kununua vifaa vya kufanyia shughuli zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia…

NAIBU SPIKA: Unaweza ukasogea mbele ukitaka kuchangia comfortably.

(Hapa Mhe. Tecla M. Ungele alisogea kwenye kipaza sauti kilichokuwepo mbele yake)

MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii ili nami nichangie hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunipatia zawadi hii ya uzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuleta ustawi na maendeleo ya jamii ya Watanzania. Nampongeza pia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi kubwa ya kusimamia kazi za Serikali na pia kwa wasilisho zuri la bajeti na hotuba ya bajeti ya Wizara yake. Hotuba hiyo imesheheni mambo mengi ya sekta mbalimbali nchini zikiendelea kuleta maendeleo na kuchochea maendeleo. Pia nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Mawaziri wote katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zote zilizoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wanafanya kazi nzuri kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu nauelekeza kwenye maeneo kadhaa. Hotuba ya Waziri Mkuu ina mambo mengi, lakini kutokana na muda, nitachangia maeneo machache tu. Kwanza, ni usafiri na usafirishaji. Tumeshuhudia miundombinu ikiboreshwa; barabara za mijini na vijijini na Watanzania wote ni mashahidi, lakini miundombinu hiyo imeharibiwa na mvua kubwa ya El-Nino. Tumeshuhudia maeneo mengine mawasiliano yalikatika. Kwa mfano kule Liwale, Barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale na Barabara ya Masasi - Nachingwea kwenda Liwale, Barabara ya kutoka Nanganga kwenda Ruangwa, zote zilikatika na maeneo hayo yalikuwa hayana mawasiliano.

Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ni muhimu sana katika ustawi wa jamii, kusafirisha mazao, kusafirisha watu na kadhalika na maendeleo yote tu yanategemea usafiri. Ombi langu, barabara hizi zijengwe kwa umakini mkubwa kweli na kwa kiwango cha lami; vile vile Masasi – Nachingwea – Liwale, Nangurukuru kwenda Liwale na Daraja lile la Nanganga ambayo inaunganisha Wilaya ya Masasi na kule Ruangwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia madaraja yajengwe kwa uimara mkubwa. Maeneo tuliyokuwa tumetegemea yawekwe makalvati, ndiyo hayo mvua hizi kubwa zimefika zikayavunja yale makalvati na kuyazoa kabisa, sasa hivi kumebaki wazi kabisa. Kwa hiyo, yatengenezwe madaraja makubwa na imara ya kupitisha maji katika maeneo mapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nachangia liko Wizara ya Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kuna program hii ya kukuza ujuzi kwa vijana, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, vijana wamepata nafasi kwenda kusoma vyuo hivyo, tumeenda kule Rwazari kule Tabora Manispaa na kule St. Antony Manispaa ya Musoma na kwingineko, wanapata ujuzi wa ushonaji, useremala na mambo ya umeme na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu, kwanza idadi ya vijana iongezeke na ichukue maeneo mengi ya Tanzania, kwa sababu maeneo mengi yana vijana ambao hawana ujuzi, lakini pia kuna vijana ambao wako kwenye makundi maalum, nao wanahitaji ujuzi, kwani nao wana umuhimu na wana vipaji vikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu lingine, vijana hawa wapatiwe vifaa vya kufanyia kazi wakishamaliza masomo. Tunawafundisha ujuzi pale, wanapata ujuzi vizuri sana na wenyewe wanafurahi sana, tumewaona tulipokuwa tumeenda wakati wa ziara za Kamati. Wanafurahi sana kupata ile nafasi na wanamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali iweke bajeti maalum ya kununua vifaa ili vijana wale wakishatoka kwenye mafunzo, wakisharudi majumbani kwao, basi kuwepo na mwendelezo wa kazi zile, wakajiajiri wenyewe na wakaendelee kufanya kazi ya kujipatia riziki, badala ya kutoka pale na ujuzi wao ambao hautakuwa na maana, kwa sababu wengine hawana uwezo wa kumudu kununua vifaa vya kufanyia shughuli zile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kupata nafasi hii na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uzima. Napenda kutoa pole kwa ndugu zangu na jamii yangu ya Mkoa wa Lindi kwa athari za Kimbuga kile cha Hidaya lakini Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa vijana wake wanafanya kazi usiku na mchana na mawasiliano yanaenda kurejea muda si mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya dhati kwa ajili ya kumtua mama ndoo kichwani, tunashukuru sana. Pia, nampongeza Mheshimiwa Waziri Aweso, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Watendaji wote wa Wizara hii ya Maji na Mameneja wa RUWASA, Meneja wa RUWASA wa Mkoa wa Lindi na mameneja wote wa Wilaya zote za Mkoa wa Lindi, wanafanya kazi nzuri sana kwa ajili ya kuwaletea Wananchi wa Mkoa wa Lindi maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wana-Lindi tunashukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ametupatia miradi ya maji mikubwa. Mradi wa kutoa maji kutoa Nyangao kupeleka Ruangwa – Nachingwea bilioni 119.5, si jambo rahisi ni jambo kubwa sana tunashukuru sana, vijiji 54 vinaenda kupata maji. Pia kuna mradi wa maji kutoka Ngapa kwenda Mchinga na sasa hivi tayari pale Mchinga wanapata maji ya bomba, maji safi na salama haijawahi kutokea na mradi ule unaenda mpaka Kilola Mbwani mpaka Kijiweni kwa kweli tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso tunakushukuru sana kwa kutekeleza adhima ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia kuna maji ya kutoka Mto Mavuji bilioni 44 maji yanaenda kupelekwa Nangurukuru, Kivinje, Kilwa Masoko haijapata kutokea, huyo ndiye Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tumepokea milioni 400 pale Liwale kwa ajili ya kutoa maji kutoka chanzo cha Turuki kuja Liwale Mjini pamoja na vijiji vyake nalo hilo halijawahi kutokea ndiyo tunayaona sasa hivi kwa Serikali ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikienda kule Nachingwea naona kuna Mradi kule Naipanga wa bilioni 1.6 na ule pia nawahakikisha ndugu zangu wa Nachingwea kule Naipanga wanaenda kupata maji muda si mrefu, hata Juni, hii haitafika. Sisi Wana-Lindi tunafurahi sana tunashukuru sana kupata maji safi na salama. Naamini kabisa kwa bajeti hii mimi naiunga mkono kabisa ipite kwa asilimia zote ili kuhakikisha Nachingwea na Mkoa wa Lindi kwa ujumla tunapata. Mheshimiwa Aweso anakwenda kumalizia ile miradi ambayo ilikuwa bado haijaisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa kupeleka maji Nachingwea, Meneja wa RUWASA ameomba shilingi milioni 670 ili Wananchi wa Ngunichile wapate maji safi ambayo wao tangu misingi ya ulimwengu iumbwe wao wanakunywa maji ya kuokota okota. Tunaenda kushuhudia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaenda kulimaliza hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia maji kutoka kwenye ardhi ya Mkoa wa Lindi hayana ubora ndiyo maana meneja wetu ameomba miradi ya mkakati ya kutoa maji kutoka Rufiji ili kuleta maji Kilwa, Lindi na Ruangwa na kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kuleta Nachingwea, Ruangwa pamoja na Liwale. Tunaomba mikakati ya mradi huo Mheshimiwa Aweso itekelezeke kwa kipindi hiki tunachopoitsha bajeti hii, vinginevyo Wana-Lindi wale wataendelea kunywa maji yenye chumvi. Zaidi ya hayo wananchi wale wa Mkoa wa Lindi wanashukuru kwa miradi kama hii ambayo haijawahi kutokea hata kwa wakati mmoja kupata maji safi na salama ambapo mradi mwingine utaenda kulisha kule Kitomanga na Kilangala ambapo sasa hivi tanki kubwa linajengwa pale maeneo ya Mkwajuni. Hizi zote ni juhudi za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakushukuru sana Mheshimiwa Aweso na timu yako yote, tunaomba mtuangalie bajeti hii tunaipitisha kwa asilimia zote ili miradi ile ikaendelee kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na Wana-Lindi wanaahidi kura zote kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, nashukuru ahsante sana. (Makofi)