Primary Questions from Hon. Tecla Mohamedi Ungele (11 total)
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatafuta mkakati wa kudumu wa kutatua tatizo la migogoro ya wakulima na wafugaji katika maeneo ya Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Lindi kumekuwa na ongezeko la migogoro ya wakulima na wafugaji, hususan katika Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale. Migogoro hii imetokana na ongezeko la mifugo ambapo kumeongeza uhitaji wa nyanda za malisho na maji.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi pamoja na Halmashauri ya Wilaya za Kilwa, Nachingwea na Liwale imefanya uhakiki na kubaini jumla ya migogoro 19, ambapo jumla ya migogoro 12 imetatuliwa na migogoro saba iko katika hatua mbalimbali za utatuzi.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sekretariati ya Mkoa wa Lindi imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji 81, na kuunda kamati ya utatuzi wa migogoro kwa kila halmashauri ili kuwahamasisha wafugaji kufuga kibiashara kwa kuendeleza ranch ndogondogo, na kila halmashauri kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi kwenye vijiji vitano kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Halmashuri za Mkoa wa Lindi na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kutumia kiasi cha shilingi milioni 279.22 kwa ajili ya kuandaa mipango ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 15, ikiwa ni hatua za utatuzi wa migogoro hiyo. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja kukipandisha hadhi Chuo cha Ualimu Nachingwea kuwa Chuo Kikuu cha Ualimu kutokana na mahitaji ya Walimu kuwa makubwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha vyuo vya ualimu hapa nchini, kikiwemo Chuo cha Ualimu Nachingwea, ni kuhakikisha kuwepo kwa walimu mahiri na wanaotosheleza mahitaji ya walimu katika ngazi ya elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya watu wazima. Vilevile, Vyuo hivi vina jukumu kubwa la kuwezesha mafunzo ya walimu kazini ambapo walimu walio karibu na vyuo hivyo hupata nyenzo mbalimbali za kitaalamu ili kuboresha ujifunzaji na ufundishaji shuleni.
Mheshimiwa Spika, ongezeko kubwa la wanafunzi na shule katika ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari kutokana na Sera ya Elimu Bila Malipo, limesababisha kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa walimu katika ngazi hizo. Ili kukidhi mahitaji ya walimu katika ngazi hizo, Serikali inaendelea na ujenzi na ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vyuo vya ualimu, uwekaji wa samani pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Chuo cha Ualimu Nachingwea ni miongoni mwa vyuo vilivyofanyiwa ukarabati na ujenzi kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mahitaji ya walimu, hususan katika ngazi ya elimu ya awali na msingi ni makubwa kutokana na ongezeko kubwa la shule na wanafunzi katika ngazi hiyo, Chuo cha Ualimu Nachingwea bado kinahitajika katika kuandaa walimu wa stashahada na astashahada.
Mheshimiwa Spika, hivyo, wanafunzi wa shahada wanaweza kuendelea kudahiliwa na vyuo vikuu vilivyopo nchini kwa kuwa, bado vina uwezo wa kufanya hivyo. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza uhaba wa watumishi katika Idara ya Elimu katika Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Rais -TAMISEMI ilifanya tathmini ya mahitaji ya walimu katika shule za msingi na sekondari nchi nzima na kubaini kuwa Mkoa wa Lindi unauhitajii jumla ya walimu wa shule za msingi 4,760 na waliopo ni 3,544 ikiwa ni upungufu wa walimu 1,216 sawa na asilimia 25.5 ya mahitaji. Kwa upande wa shule za sekondari, Mkoa wa Lindi unahitaji walimu 4,580 na waliopo ni 1,682 na upungufu ni walimu 2,898 sawa na asilimia 63.3 ya mahitaji.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo nchini kote Serikali imetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini kuhakikisha wanafanya msawazo wa walimu katika maeneo yao.
Pili, Serikali inakamilisha muongozo wa walimu wa kujitolea, utakaotumika kuwapata walimu wanaojitolea katika shule zenye uhitaji mkubwa. Walimu hao wanaojitolea watatambulika rasmi kupitia mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya kupata chanzo sahihi cha kurejea utendaji kazi wao.
Tatu, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeomba kibali cha kuajiri walimu 10,000 katika shule za msingi na sekondari nchini ikiwemo Mkoa wa Lindi. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Mifupa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Lindi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Hospitali ya Rufaa ya Lindi ina jumla ya Madaktari Bingwa watano ambao ni Daktari Bingwa wa Upasuaji mmoja, Madaktari Bingwa wa Afya ya Uzazi na Mtoto wawili, Daktari Bingwa wa Mionzi mmoja na Daktari Bingwa wa Dawa za Usingizi mmoja.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza idadi ya Madaktari Bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Wizara imepeleka kusoma jumla ya Madaktari saba, ambao Madaktari wawili wanasomea Udaktari Bingwa wa Watoto, Madaktari wawili Ubingwa wa Upasuaji, Daktari mmoja Ubingwa wa Mionzi, Daktari mmoja Ubingwa wa Mifupa na Daktari Bingwa wa Afya ya Uzazi na Watoto mmoja.
Mheshimiwa Spika, kuhusu Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Serikali inakamilisha taratibu za uhamisho ili kumpeleka Hospitali ya Lindi. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kukomesha vifo na upotevu wa mali kutokana na migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya ya Kilwa, Nachingwea na Liwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoani Lindi ni miongoni mwa Mikoa ambayo imekuwa na ongezeko kubwa la wafugaji wanaohamia na mifugo yao ikiwemo ng’ombe na mbuzi katika kipindi miaka ya karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Lindi umekumbwa na migogoro ya wakulima na wafugaji katika Wilaya za Kilwa, Liwale na Nachingwea. Migogoro hii imesababishwa na ongezeko la mifugo iliyopelekea kuongezeka kwa mahitaji ya malisho na maji, ukosefu wa mipango ya matumizi ya ardhi, uuzaji holela wa ardhi na wakulima kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imechukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaondoa changamoto ya migogoro ya aridhi kwa kutekeleza yafuatayo: - kutenga maeneo kwa ajili ya mifugo, ujenzi wa miundombinu ya mifugo, kuwezesha upatikanaji wa malisho, uanzishwaji wa ranchi ndogo ndogo, kuweka utaratibu wa uingizwaji wa mifugo katika Mkoa wa Lindi, kuunda kamati za usuluhishi wa migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatoa kwa viongozi ngazi ya Mkoa na Halmashauri kote nchini kuhakikisha wanatatua migogoro kwa wakati, hii ikiwa pamoja na kuweka utaratibu mzuri wa matumizi ya ardhi.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-
Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Mahakama ya Wilaya Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali ili kuboresha mazingira ya utoaji haki. Katika mpango huo Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea imepangwa kujengwa katika mwaka huu wa fedha 2023/2024. Mshauri Elekezi ameshakamilisha usanifu na maandalizi ya gharama za mradi na taratibu za kupata Mkandarasi wa ujenzi zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, jengo linatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2024.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha miundombinu ya Gereza la Liwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele Mbunge wa Viti Maalum Lindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Magereza imeanza kuboresha miundombinu ya Gereza Liwale kwa kutumia fedha za vyanzo vya ndani. Jeshi la Magereza limejenga jengo jipya la Utawala na nyumba saba za watumishi kwa ajili ya kuishi askari. Majengo hayo yamekamilika na yamezinduliwa na Mwenge wa Uhuru tarehe 29 Aprili, 2022. Ili kukamilisha uboreshaji wa miundombinu iliyobakia, Shilingi 225,000,000.00 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023. Aidha, nawashukuru na kuwapongeza Mhe. Mbunge wa Jimbo la Liwale, Mheshimiwa Kuchauka, na Mkuu wa Wilaya ya Liwale kwa kuchangia mifuko ya saruji iliyosaidia ujenzi wa majengo ya utawala na selo moja ya Wanawake.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-
Je, nini mkakati wa Serikali kuboresha miundombinu ya barabara na kuinua maendeleo mikoa ya Lindi na Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifautavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa Mkoa wa Mtwara, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Mtwara – Nanyamba – Tandahimba – Newala – Masasi yenye urefu wa kilometa 210, ambapo sehemu ya Mtwara – Mnivata kilometa 50 ujenzi umekamilika na sehemu iliyobaki ya Mnivata – Newala – Masasi kilometa 160 pamoja na Daraja la Mwiti ujenzi umeanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2026. Aidha, Serikali imepanga kuifanyia ukarabati barabara ya Mtwara – Mingoyo – Masasi kilometa 200 ambapo maandalizi ya kutangaza zabuni za ukarabati wa barabara hii yako katika hatua za mwisho.
Mheshimwia Spika, kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara ya Nanganga – Ruangwa kilometa 53.2 ambapo umefikia asilimia 74 na ujenzi wa barabara ya Nachingwea – Ruangwa kilometa 52.8 upo hatua za mwisho za manunuzi. Aidha, ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale kilometa 175 utatekelezwa kwa utaratibu wa EPC + F na tayari mkataba wa ujenzi umesainiwa, ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzipatia magari ya wagonjwa Hospitali za Wilaya za Liwale, Nachingwea na Kilwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatapelekwa kwenye halmashauri 184 nchini kote zikiwemo Halmashauri za Wilaya za Liwale, Nachingwea na Kilwa. Asante.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza: -
Je, ni lini Wananchi wa Kata za Nachingwea, Kiegei, Matekwe na Namapwia – Nachingwea, Lihimalya na Kandawale - Kilwa watapatiwa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika kuboresha huduma ya maji kwenye Kata za Matekwe, Kiegei na Namapwia, Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 inaendelea na zoezi la uchimbaji wa visima vinne ambapo kisima kimoja tayari kimechimbwa katika Kijiji cha Kilimarondo na uchimbaji wa visima vitatu unaendelea na unatarajiwa kukamilika Mwezi Juni, 2024.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kata ya Nachingwea, Serikali inaendelea na kazi ya usanifu wa mradi pacha toka vyanzo vya Mbwinji na unatarajia kukamilika mwezi Juni, 2024, ambapo utekelezaji wa mradi utaanza katika Mwaka wa Fedha 2024/2025. Aidha, Kwa upande wa Kata ya Kandawale yenye jumla ya Vijiji Vinne, Vijiji viwili vya Kandawale na Mtumbei vinapata huduma ya majisafi na salama kupitia miradi iliyojengwa yenye jumla ya vituo 13. Pia, Vijiji vya Ngarambi na Matewa vinatarajiwa kuchimbiwa visima katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Kata ya Lihimalya, Serikali katika Mwaka wa Fedha 2024/2025 itafanya upanuzi wa Mradi wa Maji wa Pande kwa ajili ya kufikisha huduma ya maji kwenye vijiji vya kata hiyo.
MHE. TECLA M. UNGELE aliuliza:-
Je, lini Serikali itaboresha Kituo cha Afya cha kimkakati cha Kitomanga Mchinga kuwa Hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Kitomanga kipo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi umbali wa takribani kilometa 55 kutoka Makao Makuu ya Manispaa. Kituo hicho kinatoa huduma zote muhimu ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, upasuaji na kulaza wagonjwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mwongozo wa uanzishwaji wa hospitali nchini uliotolewa na Wizara ya Afya mwaka 2015, kila Halmashauri inapaswa kuwa na Hospitali moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/2022 hadi 2023/2024, Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni 1.8 katika Manispaa ya Lindi kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Kwa kuwa Kituo cha Afya cha Kitomanga ni cha kimkakati, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu yake kadri itakavyohitajika ili kiendelee kutoa huduma kwa ufanisi zaidi. Ahsante.