Supplementary Questions from Hon. Tecla Mohamedi Ungele (22 total)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali pia napongeza kazi inayofanywa na Sekretarieti ya Mkoa wa Lindi na Halmashauri zake katika kutatua migogoro hii.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ni lini itajenga mabwawa kwa ajili ya kunywesha mifugo hiyo? Hapa tumeona katika jibu la msingi shida kubwa ni kugombania maji pamoja na malisho.
Mheshimiwa Spika, pili, tunaomba kazi hii ya kutatua migogoro katika Mkoa wa Lindi iharakishwe maana Sekretarieti ya Mkoa imeelemewa na migogoro hiyo. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na suala hili?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tecla, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kutambua umuhimu na katika mkakati wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan wa kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 tumetenga jumla ya shilingi milioni 900 kwa ajili ya kujenga mabwawa katika Mkoa wa Lindi. Bwawa moja litajengwa katika Wilaya ya Liwale na lingine katika Wilaya ya Nachingwea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Lindi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejipanga vyema kwa kutumia Kamati inayoshughulikia migogoro ya ufugaji na wakulima kwenda kuweka kambi kuzungumza nao na kushirikiana katika kutafuta mbinu za kusuluhisha migogoro hii, ikiwa ni pamoja na kutatua lile tatizo la nyanda za malisho.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi kubwa ya Wizara ya Serikali kufanya ukarabati wa chuo hiki cha Ualimu Nachingwea, lakini kuna uhaba mkubwa wa samani, yani viti, meza, kwa ajili ya wanafunzi hao, lakini pia chuo hakina uzio. Je, Serikali ipo tayari kupanga bajeti kukamilisha mahitaji hayo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na jitihada kubwa ya vijana wa Mkoa wa Lindi kuwa na ufaulu mzuri katika kidato cha sita kwa miaka mitatu mfululizo inaonesha kabisa vijana hawa wako tayari kwa ajili ya elimu ya juu.
Je, ni lini Serikali itajenga chuo kikuu Mkoa wa Lindi kwa ajili ya kuchochea maendeleo kielimu, kiuchumi, kiutamaduni na kijamii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya swali la msingi kwamba, Serikali imeendelea kukarabati vyuo hivi kwa kuhakikisha kwamba, tunakwenda kuimarisha, lakini tunakwenda kuongeza nguvu ili kuongeza udahili kutokana na uhitaji mkubwa sana wa walimu. Nikaeleza katika swali lile la msingi kwamba, Serikali bado inakihitaji chuo hiki ili kiweze kutoa taaluma hiyo ya astashahada na stashahada ili kuongeza idadi hiyo ya walimu.
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile katika swali lake ambalo linauliza suala la miundombinu ya samani, kwa takwimu tulizokuwanazo chuo chetu cha Nachingwea kina jumla ya viti 400 mpaka hivi sasa, kwa rekodi tulizonazo, lakini wanafunzi waliopo ni 295. Katika muktadha huo haioneshi kwamba, kuna uhaba wa samani kama viti na meza, lakini sambamba na hivyo tuna computer 30 ambazo zinawezesha vitengo vyetu vile vya kutumia computer kupata mafunzo kwa kutumia computer, lakini tuna projector tano ambazo zimenunuliwa hivi sasa na computer mbili ambazo zilikuwa za zamani.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali imeendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba, tunatengeneza mazingira mazuri ya kupata walimu wa kutosha. Na katika kipindi kilichopita Serikali imeweza kutumia jumla ya shilingi bilioni 84.1 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba, tunatengeneza miundombinu, lakini vilevile samani zinapatikana.
Mheshimiwa Spika, suala la uzio; Serikali bado inaendelea na mkakati wa kuhakikisha tunaboresha mazingira haya. Na hili sasa tunaliingiza kwenye bajeti kuhakikisha maeneo haya yanapata uzio ili kuweza kutengeneza usalama wa mali pamoja na samani za vyuo.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kuhusiana na suala la chuo kikuu:-
Mheshimiwa Spika, nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa hivi sasa bado vyuo vyetu vilivyopo hapa nchini, vyuo vikuu, vina nafasi za kutosha. Na tunawashauri tu wananchi wa Lindi waweze kuvitumia vyuo ambavyo vipo kwasababu, vyuo havijengwi kwa kufuata mikoa wala kanda, bali vyuo hivi vinakuwa ni vya kitaifa, basi wanafunzi hawa wanaweza kwenda katika vyuo vingine ambavyo pale Mtwara tuna chuo kile cha St. Marius wanaweza kupata taaluma yao pale, lakini tuna matawi ya vyuo vikuu huria karibu katika mikoa yote ikiwemo na Mkoa huu wa Lindi.
Mheshimiwa Spika, lakini katika Chuo chetu cha Dodoma walihitajika kudahiliwa wanafunzi au kuna nafasi 40,000 lakini mpaka hivi sasa wanafunzi waliodahiliwa ni 29,595 kwa hiyo, tuna nafasi za kutosha katika vyuo hivi ambavyo vinatosheleza ku-absorb wanafunzi wote. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kadhia inayowapata wananchi wa Karatu ndiyo hiyo inayowapata wananchi wa Mkoa wa Lindi Wilaya ya Kilwa, Liwale, Lindi Vijijini, Nachingwea. Hata hivi juzi tu Wilaya ya Liwale, Kata ya Mbaya kuna mwananchi kule ameuawa na tembo. Pia wanaharibu mashamba ya vyakula na mazao kiasi kwamba wananchi wanaendelea…
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa.
MHE. TECLA M. UNGELE: Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili la wanyama kule Nachingwea, Liwale na Kilwa ili wananchi wa huko nao wawe na maisha mazuri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Lindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekwishakuelezea kwenye jibu langu la msingi nimetoa rai kwa wananchi kupanda mazao ambayo yanaweza yakaepusha hawa wanyama. Hata hivyo, tukumbuke kwamba tunaishi kwenye maeneo ambayo yalikuwa ni njia za wanyama na tukumbuke kwamba hawa wanyama walikuwepo kabla hata ya sisi kuwepo.
Kwa hiyo, wanyama siku zote wanaenda kwenye maeneo yao ya siku zote ambayo sisi ndiyo tumefanya mashamba. Niwaombe wananchi tena kwamba waendelee kupanda mazao haya ambayo tunahamasisha, lakini ikishindikana basi wasilime kwenye maeneo ambayo yako kandokando ya hifadhi. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi katika Mkoa wa Lindi na hii inaleta ufaulu hafifu kwa wanafunzi katika masomo hayo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupatikana walimu wa sayansi kwa haraka iwezekanavyo kunusuru shida hiyo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia naona kwenye majibu kuna upatikanaji/kibali cha kuajiri walimu 10,000. Katika hilo naomba sana Serikali watupe kipaumbele Mkoa wa Lindi, kwa sababu tuna changamoto kubwa ya walimu. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tecla Mohamedi Ungele Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na upungufu wa walimu wa sayansi katika shule zetu za sekondari nchini kote na tumefanya tathmini, kubaini mahitaji ya walimu wa sayansi angalau kuwezesha shule zetu kuwa na walimu wanaoweza kutosheleza mahitaji ya wanafunzi. Ndio maana katika ajira zilizopita asilimia 75.5 ya walimu wote walioajiriwa walikuwa ni walimu, wa masomo ya sayansi na utaratibu wa kuendelea kutoa kipaumbele kwa walimu wa sayansi katika ajira zinazofuata utaendelea.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la kibali cha walimu katika halmashauri hiyo kupewa kipaumbele katika walimu 10,000, tutawapa kipaumbele na kazi iliyofanyika tumeainisha Mikoa yote yenye upungufu mkubwa zaidi wa walimu na watumishi wengine. Mikoa hiyo na Halmashauri hizo zitapewa kipaumbele wakati wa kuajiri watumishi hao. Ahsante. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu hayo ya Serikali. Swali la kwanza; kwa kuwa magonjwa yasiyoambukiza ni tatizo kubwa katika Mkoa wa Lindi. Je, ni lini sasa watapeleka specialist hao wa internal medicine? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ni lini Waziri atakwenda Mkoa wa Lindi pale Hospitali ya Sokoine kwenda kuona hali halisi ya ukosefu wa Madaktari hao na kadhia wanayopata wananchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ni lini Serikali sasa itapeleka Daktari huyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge tukae naye pamoja tuwasiliane na Afisa Utumishi na Wizara ya Utumishi tuone ni lini watakamilisha mchakato huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ameniuliza kwamba ni lini tutakwenda Lindi ili kwenda kuona matatizo yanayoendelea pale. Namuahidi Mheshimiwa Mbunge mara tu tukimaliza Bunge, tutashirikiana na yeye na Mbunge mwingine wa Mkoa wa Lindi twende huko. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, maeneo mengi Mkoa wa Lindi yana changamoto ya usalama hasa katika migogoro ya wakulima na wafugaji hata wakati wa msimu wa korosho na ufuta usalama wa wananchi unakuwa mgumu. Maeneo mengi yapo mbali na Makao Makuu ya Wilaya, mfano Kilimarondo ipo kilometa 120, Nambiranje Wilaya ya Ruangwa napo ni mbali, pia Nangaru Wilaya ya Lindi.
Je, Serikali itajenga lini Vituo vya Polisi maeneo hayo ili kuwahakikisha usalama wa wananchi. Ahsante? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na changamoto hiyo ama uhitaji huo wa vituo vya Polisi katika Mkoa wa Lindi, lakini kuna kazi ambayo tayari tumeshaanza kuifanya. Kwa mfano, katika bajeti hii ambayo tunaendelea nayo kuna maeneo ambayo Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo vya Polisi na hata bajeti inayokuja tumezingatia hilo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo hatuwezi kutatua changamoto hii kwa wakati mmoja kwa maeneo yote, lakini nitakapokuja kwenye ziara kuitembelea Kilwa Kaskazini nitamuomba Mheshimiwa Mbunge nae tuwe pamoja ili tuangalie namna gani tunaweza kuharakisha utatuzi wa changamoto hii. (Makofi)
MHE. DKT. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa umbali kutoka Nachingwea – Liwale ni zaidi ya Kilometa 130 na Kilwa – Liwale ni zaidi ya kilometa 260.
Je, ni lini Serikali itajenga vituo vya polisi pale Kibutuka Wilaya ya Liwale na Njinjo kule Wilaya ya Kilwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Ungele kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa umbali alioutaja Mheshimiwa Mbunge kwamba kutoka eneo moja hadi kituo cha Polisi ni zaidi ya kilometa 100 ina-justify kabisa umuhimu wa uwepo wa kituo cha Polisi. Nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tutaelekeza Kamanda wa Polisi Mkoa na Jeshi la Polisi kwa ujumla wake kufanya tathimini ya uhitaji wa kituo cha Polisi maeneo hayo uliyoyarejea ili mpango wa ujenzi wa vituo hivyo uweze kutekelezwa. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni lini Barabara ya Masasi – Nachingwea - Liwale itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tecla Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja sasa hivi zinafanyiwa evaluation, ndiyo moja ya barabara ambazo ziko kwenye EPC+F. Ahsante. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi Vijiji vyake havijapata umeme. Wakandarasi wale kasi yao siyo nzuri hasa maeneo ya Vijji vya Nachingwea na Kilwa Kisiwani.
Je, ni lini Serikali itakamilisha usambazaji wa umeme Vijiji vya Mkoa wa Lindi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tecla Mbunge kutoka Lindi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji takribani vijiji vyote vilivyobakia ambavyo havijapata umeme vimeingizwa katika program ya kupata umeme ya round hii ya awamu ya tatu mzunguko wa pili. Kama nilivyoeleza na changamoto zile zilizojitokeza za kupanda kwa bei ya vifaa vya umeme inashughulikiwa na imani yetu ni kwamba lengo la Serikalii la kukamilisha upelekaji wa umeme katika vijiji vyote vilivyobakia litatimia Desemba, 2022.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa maeneo mengi Mikoa ya Lindi na Mtwara yalihusika katika harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika hasa Kusini mwa Bara la Afrika.
Je, Serikali ina mpango gani kuharakisha maendeleo katika maeneo hayo ambayo yaliathirika? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mama yangu Tecla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza kabisa mchango wa wapigania uhuru kwa ajili ya nchi yetu kupata Uhuru kutoka kwa Mkoloni fidia yake haipimiki. Kwa sababu mashujaa hawa walijitoa kwa ajili ya nchi yetu kupata uhuru na tunajifunza kutoka kwao kwamba uzalendo huu lazima tuuendeleze na tuwe tayari kupigania nchi yetu bila kutegemea fidia, lakini vile vile nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mama yangu, Mheshimiwa Tecla, Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kutekeleza Ilani inapeleka maendeleo kote nchini ikiwemo maeneo ya Mikoa ya Kusini. Kwa hiyo ningependa kumwondoa wasiwasi Mipango ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi iko makini katika kuhakikisha maendeleo tunayapeleka kote ikiwemo maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu ya Serikali. Nina maswali mawili ya nyongeza.
a) Je, ni lini malambo ya kunyweshea maji mifugo hiyo yatajengwa maeneo ya Ngunichile, Kibutuka na Njilinji ili kuondoa migogoro hiyo?
b) Je, ni lini utengaji wa ardhi utafanyika katika maeneo ambayo kunatokea vifo na migogoro hiyo hususani Kibutuka na Njilinji, Ngunichile Natekwe na kwingineko?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la kwanza Mheshimiwa Ungele tutashirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuweza kuona ni namna gani tutajenga kwa haraka sana haya malambo ya maji Mtekwe na Kimambi kuhakikisha kwamba mifugo iliyokuwepo kule inaweza kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, kuhusu upangaji wa ardhi, sheria zipo wazi, kuna Sheria Namba Tano ya Ardhi ya mwaka 1999 Toleo la 2002 juu ya matumizi bora ya ardhi ambapo inatoa mamlaka kwa vijiji kupanga matumizi bora ya ardhi ambapo wanatakiwa kutenga malisho, maeneo ya masoko, mashamba na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nichukue nafasi hii kwenye Bunge lako tukufu kuwaomba na kuwaasa viongozi katika halmashauri zetu nchini ikiwemo Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha wanasimamia sheria hii kwa kupanga matumizi bora ya ardhi ili kuepuka mogogoro ya ardhi na hasa ile ya wakulima na wafugaji.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa maeneo mengi katika Mkoa wa Lindi yana maji ya chumvi. Je, ni lini Serikali itawapatia maji safi na salama wananchi wa Kata za Ngunichile, Tarafa ya Kilimarondo na Namapwia kwenye Wilaya ya Nachingwea, Lihimalyao, Kibata na Kandawale kule Wilaya ya Kilwa? ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tecla kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yote aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge ni kweli yana shida ya maji ya chumvi, Mheshimiwa Mbunge unafahamu mradi wetu mkubwa ambao tayari tumeongea, hata juzi tulikuwa pamoja na tayari tunautengea fedha ule mradi ili sasa tuweze kupata maji ya uhakika yakiwa safi na salama na kuondokana na visima hivi vinavyotuletea maji ya chumvi.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa juhudi kubwa za Serikali kwenda kutujengea Mahakama ya Wilaya kule Nachingwea. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kuna upungufu mkubwa wa Watumishi katika Idara ya Mahakama Wilaya ya Nachingwea; je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa kazi? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Hakimu mmoja anahangaika kuhudumia Mahakama ya Mwanzo zaidi ya tano, lakini fedha za kuhudumia shughuli za Mahakama hazitoshi; je, Serikali ina mkakati gani kuongeza fedha kila mwezi kwa ajili ya shughuli za Mahakama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru. naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ungele kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ninakiri ni kweli tuna upungufu wa watumishi katika Muhimili wetu wa Mahakama kama ambavyo upungufu huu upo katika Serikali kwa maeneo mbalimbali. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa akituongezea watumishi katika Muhimili wetu wa Mahakama, na ninyi ni mashahidi ndugu zangu ni majuzi tu ametuteulia Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na kadhalika, tunaendelea kuomba kupeleka vibali kwa ajili ya nyongeza ya watumishi.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Nachingwea ni kweli wana upungufu wa watumishi. Primary Court (PC) ambazo zina Mahakimu ni tatu, Primary Court ambazo zinahudumiwa na hao Mahakimu watatu ni watano. Mheshimiwa Mbunge nikuhaidi kwamba tutaendelea kuwasiliana ndani ya Serikali kuongeza Mahakimu katika Mahakama hizo ili huduma iweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anazunguzia suala la nyongeza ya fedha, kwamba hawa watumishi wanapokuwa wanatoka maeneo hayo kuhudumia Mahakama zile ambazo inabidi waende, kwa kuwa Mahakimu hawajafika wanahitaji fedha kwa ajili ya kuhudimia.
Mheshimiwa Spika, nishukuru Bunge lako Tukufu, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwamba mhimili wa Mahakama umekuwa ukiongezewa fedha. Mwaka huu ambao bajeti hii tunayoendelea nayo OC ya Mahakama ilipanda kutoka bilioni 60 mpaka bilioni 70, maana yake tunayo nyongeza ya zaidi ya bilioni 11. Kwa hiyo, tuwashukuru kwamba mmetuongezea na sisi tutaendelea kupeleka hizo fedha za OC ili Mahakimu hawa waweze kuhudumia maeneo ambako wanakwenda kuhudumia. Ahsante.(Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi. Shule nyingi za Msingi za Mkoa wa Lindi ni za zamani, zimejengwa mwaka 1947 na zingine kabla ya hapo, ikiwepo ya Lionja, Ngunichile, Kivinje, Ntua na kwingineko. Je, Serikali ina mkakati gani katika shule hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tecla, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Lindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu katika mpango ambao tathmini inafanyika ni pamoja na hizo shule ambazo ameziainisha katika Mkoa wa Lindi na tathmini yetu itakapokamilika tutaainisha maeneo yote kila mmoja ni wakati gani utatekelezeka. Kwa hiyo nimwondoe shaka kwenye hilo. Ahsante sana.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, nina swali la nyongeza. Kwa kuwa uzio ni muhimu katika mazingira ya magereza. Je, nini kauli ya Serikali kujenga uzio ulioko imara kwa Gereza la Liwale na Nachingea kwa sababu kwa sasa iko kwa kiasi cha miti imejengwa kwa miti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele Mbunge wa Viti Maalum Lindi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyokwishasema uzio ni kitu muhimu katika magereza yetu na kwa vile ukarabati unaendelea nitumie nafasi hii kumtaka Mkuu wa Gereza la Liwale aendelee katika mipango yake kuweka kipaumbele katika uzio ili anapomaliza ukarabati wa majengo hayo basi uzio pia uweze kuendelezwa.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante, stand ya Lindi Manispaa bado haiko vizuri, mabasi yote yanayotoka Mtwara, Songea na mkoa mzima kwa ujumla yanapitia pale.
Je, Serikali ina mkakati gani kujenga stand ile kuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tecla Ungele, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ungele amekuwa ni miongoni mwa Waheshimiwa Wabunge ambao wanawasemea sana wananchi kwa Watanzania kwa ujumla na wananchi wa Mkoa Lindi, naifahamu sana stand ya Manispaa ya Lindi kwa sababu nimekuwa kule kwa miaka kadhaa, ninafahamu kwamba tunahitaji kuijenga, tuotoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, kutambua hii ni kipaumbele cha Halmashauri kufanya tathamini ya gharama na kuona kama inaweza ikajengwa kwa mapato ya ndani au wawasilishe kama mradi wa kimkakati. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Spika, ahsante, Lindi na Mtwara tunashukuru kwa jitihada za Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuletea maendeleo na ndiyo maana akaridhia kusaini kwa Mkataba huo wa EPC + F hapo Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Spika, kusaini mkataba ni jambo moja na kuanza ujenzi ni jambo lingine; je, ni lini sasa Mkandarasi ataanza kazi ya Ujenzi Masasi – Nachingwea – Liwale? (Makofi)
Swali la pili; je, ni lini sasa barabara ya Nachingwea kwenda Kilimarondo itajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Tecla Ungele, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale kilometa 175 kama nilivyosema katika jibu la msingi inatekelezwa kwa utaratibu wa EPC + F na iko kwenye hatua kama ambavyo barabara zote zipo.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi Waziri alitolea maelezo wako wanapitia usanifu wale Wakandarasi ambao wamepewa hizo barabara na tunategemea Januari wakandarasi watakuwa wako site baada ya kukamilisha zile taratibu zao za kupitia ule usanifu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hilo linaendelea na barabara hizo zitaanza kujengwa. Kinachoendelea tu hapa ni kwamba ni utaratibu ambao ni mpya kwetu sisi lakini wanatakiwa wale ambao wamepewa hizo kazi nao lazima wapitie usanifu na wajiridhishe.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu barabara aliyoitaja hiyo kwenda Kilimarondo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, barabara hiyo baada ya kufanyiwa usanifu bajeti ikiruhusu basi tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami, kwa sababu lengo la Serikali ni kuzijenga barabara hizi kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali. Naomba kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Lindi una maeneo mengi sana yaliyoko mbali na hospitali za Wilaya yakiwepo Kilimarondo kule Nachingwea, Nanjilinji Kilwa, Milola kule Mchinga; je, Serikali itatupa kipaumbele kutupatia magari hayo yaliyoongezwa katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Tecla Mohamed Ungele, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, magari haya yatakayoletwa kuna halmashauri zitapata magari zaidi ya moja. Sababu ya halmashauri hizo kupata magari zaidi ya moja itakuwa ni kukidhi vigezo vya kitaalamu, ikiwemo umbali kutoka kituo hicho kwenda kituo kingine cha jirani, lakini pia population ya eneo hilo pamoja na mazingira ya kijiografia. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Ungele kwamba, tutafanya tathmini kwa Halmashauri hizo alizozitaja ili kuona kama zinakidhi vigezo hivyo. Ahsante.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa jitihada kubwa za Serikali za kupeleka maji kule Matekwe na kule Lihimalya. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ni shahidi alivyopita Ngunichile, aliona maji wanayokunywa wananchi wa Ngunichile, alishuhudia mwenyewe maji ya kuokota chini. Je, hizi fedha zilizoombwa milioni 670 ili kukamilisha ule mradi wa kupeleka majisafi na salama Ngunichile, lini fedha hizo zitapelekwa? (Makofi)
Swali la pili, Kata ya Kandawale, Kilwa Kaskazini ni sehemu yenye mwinuko na ni changamoto kubwa ya majisafi na salama. Je, ni lini Serikali mtapeleka maji safi na salama Kata ya Kibata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tecla Ungele, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Tecla, kwa kweli alinipa ushirikiano sana kwenye ziara yangu, nilipokwenda kule. Eneo hili la Ngunichile kweli tumefika na kazi zimeanza, kadri fedha zitakapoendelea kupatikana Mheshimiwa Tecla Ungele, tutaendelea kupeleka fedha kwa awamu hakika Ngunichile wanakwenda kunufaika kwa maji safi na salama kwa ufuatiliaji wako mahiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Eneo la kule Kilwa hii Kata uliyoitaja Mheshimiwa ipo katika mpango wa kuhakikisha tunakwenda kupeleka maji kwa kuchimba kisima kirefu na kusambaza vichotea maji maeneo ya karibu na makazi ya wananchi. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu ya Serikali nina swali la nyongeza.
Kwa kuwa jamii yetu bado elimu hii ya uibuaji miradi yenye tija haijaeleweka vizuri. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka elimu hii kwa jamii na elimu hiyo iwe endelevu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na jambo la elimu kwamba haijaenea vizuri kwa wananchi, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako kwamba, katika utaratibu wa mikutano ile mikuu ya Vijiji, Kata au Shehia ambayo inakwenda kuibua miradi, hatua ya kwanza wanayofanya wataalam wetu ni kuendelea kuelimisha kwanza wananchi kabla hawajaibua miradi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida kubwa ambayo inatokea ni kwamba wananchi wanakuwa na vipaumbele vyao dhidi ya ile mipango ambayo Serikali inaileta, kwa hiyo, hapo ndipo pamekuwa na tatizo na mgongano wa mara kwa mara. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi wetu ili kuhakikisha kwamba wanafika sehemu wanaibua miradi ambayo inaendana moja kwa moja na changamoto zilizopo katika maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji.
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ujenzi wa jengo la Chuo cha Uuguzi Nachingwea ulioanza mwaka 2022 ulitarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022 lakini hadi leo bado haijakamilika, je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa chuo kile ili kuongeza idadi ya wauguzi na kupunguza shortage ama upungufu wa wauguzi nchini Tanzania? Ahsante.
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia taarifa zangu kama Nachingwea ipo, kwa kweli Mheshimiwa Tecla amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa ujenzi wa Chuo cha Afya Nachingwea, lakini kwa sababu na yeye ni mwanataaluma wa kada ya wauguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kukiri ni kweli ujenzi umechelewa, lakini tumepata fedha hizi za Benki ya Dunia na tumeweka katika orodha yetu Nachingwea moja ya majengo ya kumaliza. Kwa hiyo, naomba nikuhakikishie na mimi tukimaliza Bunge nitafanya ziara Nachingwea kufuatilia ujenzi wa jengo hili ambalo lilikwama kwa muda mrefu. (Makofi)
MHE. TECLA M. UNGELE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali la kwanza; je, Serikali itapeleka lini x-ray kwa sababu Kituo hiki cha Afya Kitomanga hakina huduma ya x-ray kwa muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Serikali ina mpango gani wa kujenga uzio Kituo cha Afya Kitomanga ili kuleta usalama kwa wagonjwa, lakini pia kwa watoa huduma za afya katika kituo kile? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishatoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaatiba. Katika Halmashauri zote 184 katika mwaka huu wa fedha pekeyake kila Halmashauri imepata kati ya shilingi milioni 700 na zaidi hadi shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Kwa hivyo kipaumbele mojawapo katika vifaatiba ni kununua digital x-rays. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumechukua hoja ya Kitomanga tutafanya ufuatiliaji na kuona uwezekano wa kupata digital x-rays kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na uzio, tunafahamu tunahitaji kuwa na usalama katika maeneo ya vituo vyetu ni jambo la msingi, lakini safari ni hatua. Tunakamilisha kwanza miundombinu ile muhimu ya kutoa huduma, lakini pia Manispaa ya Lindi nitoe maelekezo haya waanze kutenga fedha kwa awamu angalau kuanza ujenzi wa uzio wakati Serikali inaendelea kukamilisha miundombinu mingine. Ahsante sana.