Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Suma Ikenda Fyandomo (11 total)

MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Igawa hadi Tunduma kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Igawa hadi Tunduma yenye urefu wa kilometa 218 ikiwa ni maandalizi ya kufanyia ukarabati kwa kiwango cha lami. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ilikamilika mwezi Agosti, 2021. Aidha, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina umejumuisha barabara ya mchepuo katika Jiji la Mbeya kipande cha Uyole – Songwe Bypass yenye urefu wa kilometa 48.9.

Mheshimiwa Spika, Serikali itafanya ukarabati na upanuzi wa Barabara ya Igawa hadi Tunduma kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza itahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili kuwa njia nne kwa sehemu ya Uyole – Ifisi yenye urefu wa kilometa 29 ili kupunguza msongamano katika Jiji la Mbeya. Taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata Mkandarasi zinaendelea na inatarajiwa kazi itaanza mapema katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ukarabati wa sehemu iliyobaki pamoja na kujenga Barabara ya Mchepuo ya Uyole – Songwe bypass. Ahsante. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Kiwira ili uanze kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha mapitio ya usanifu kwa ajili ya mradi utakaotumia chanzo cha Mto Kiwira kupeleka maji katika Jiji la Mbeya na Mji wa Mbalizi. Hatua inayoendelea sasa ni manunuzi ya Mkandarasi na katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi 4,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa chanzo na utekelezaji wa mradi utafanyika kwa awamu.
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: -

Je, Serikali inawasaidiaje wajane ili kuondoa mila na desturi potofu zinazomkandamiza Mwanamke kwenye suala la mirathi?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo Mbunge wa viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa wajane na katika kulinda haki zao kwa kutunga Sheria mbalimbali na Kanuni za kulinda haki za Wanawake wajane katika uuala zima la mirathi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mila na desturi potofu ni eneo ambalo Serikali imeanzisha mchakato wa mapitio ya sheria za kimila ili kuondoa aina yoyote ya ukandamizaji kwa wajane katika suala la mirathi. Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu Sheria ya Mirathi hususani umuhimu wa kuandika wosia ili kuondoa changamoto zinazotokana na mila na desturi potofu.
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kukamilisha Ujenzi wa Mradi wa maji Tukuyu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Maji Tukuyu Mjini ni wa miaka miwili na ulianza mwezi Agosti, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2023. Hadi sasa utekelezaji unaendelea na umefikia asilimia 82. Kazi zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa banio katika chanzo, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu Kilomita 9.5, ujenzi tanki moja lenye ujanzo wa lita milioni 1.5 na ulazaji wa mtandao wa bomba wa umbali kilomita 20.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Wilaya ya Rungwe?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niamba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za ajira zinaendelea kuchakatwa ili kupata Wenyeviti 57 watakaoweza kukamilisha uhitaji wa Wenyeviti 139 ambayo ni idadi ya Wilaya zote hapa nchini. Kwa sasa tuna Wenyeviti 82 tu ambao wanalazimika kuhudumia Wilaya zisizo na Mabaraza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wilaya ya Rungwe inahudumiwa na Mwenyekiti kutoka Wilaya ya Kyela.
MHE. PROF. SHUKRANI E. MANYA K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itapeleka vifaa kwenye Jengo Jipya la Mama na Mtoto katika Hospitali ya META Mkoani Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba kwa ajili ya jengo la huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Meta, Mkoa wa Mbeya. Aidha, vifaatiba hivyo vimeshaanza kupelekwa na kufungwa katika jengo la Mama na Mtoto kupitia Bohari Dawa (MSD).

Mheshimiwa Naibu Spika, jengo hili limeanza kutumika na ufungaji wa vifaatiba katika vitengo mbalimbali unaendelea na utakamilika mapema mwezi Julai, 2023. Naomba kuwasilisha.
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami kilometa 2.8 za barabara ambazo ni mchepuko kwenye barabara ya Pipeline?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa 2.8 za barabara za mchepuo eneo la Inyala. Kazi za ujenzi zilikamilika tarehe 24 Juni, 2023, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Wilaya ya Rungwe italetewa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suma Ikenda Fyandomo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuajiri Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi ili kuongeza kasi ya kusikiliza na kuamua mashauri ya ardhi. Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Rungwe ameteuliwa na kupangiwa kituo tarehe 18 Septemba, 2023 na tayari ameanza kazi. Nakushukuru.
MHE. SUMA I. FYANDOMO K.n.y. MHE. ANTON A. MWANTONA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaweka transformer kwenye Vijiji vya Mpindo, Kata ya Bulyaga na Isumba, Kata ya Kinyara ili wananchi wanufaike na Mradi wa REA III Awamu ya II?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unalenga kupeleka umeme katika vijiji 31 katika Jimbo la Rungwe. Hadi sasa, jumla ya vijiji 30 vimeunganishwa na umeme na kijiji kimoja kilichobaki ambacho kinaitwa Kyobo Juu kilichopo Kata ya Ikuti kazi inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Mpindo na Isumba vilivyopo Kata ya Bulyaga na Kinyara tayari vimeunganishiwa umeme na tayari transformer imefungwa tangu mwezi Mei, 2024. Kwa sasa kazi inayoendelea ni kuunganisha wateja wa awali katika vijiji hivyo ambapo jumla ya wateja 43 kati ya 44 tayari wameunganishiwa umeme, ahsante.
MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Igawa hadi Tunduma utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Barabara ya Igawa – Tunduma kwa njia nne inajengwa kwa awamu, ambapo sehemu ya kuanzia Uyole eneo la Nsalaga – Ifisi, kilometa 29, ujenzi wake unaendelea na hadi sasa umefikia 15.5%. Kazi za ujenzi zimepangwa kukamilika tarehe 13 Aprili, 2025. Kwa sehemu iliyobaki ya Igawa – Uyole, eneo la Nsalaga na Ifisi – Tunduma zitajengwa kwa utaratibu wa EPC+ F. Ahsante. (Makofi)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE K.n.y. MHE. SUMA I. FYANDOMO aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga nyumba za Askari Polisi pamoja na kukarabati zilizopo mkoani Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mbeya una mahitaji ya nyumba za makazi ya kuishi Askari Polisi 1,045 na nyumba zilizopo ni 186 na ni chakavu. Tathmini kwa ajili ya kubaini uchakavu na kuzifanyia ukarabati nyumba hizo zilizopo imefanyika na kiasi cha fedha shilingi 3,523,078,000 kinahitajika. Aidha, kiasi cha fedha shilingi 51,760,000,000 zinahitajika kujengea nyumba za makazi ya Askari ili kukidhi mahitaji ya mkoa. Serikali itaanza kutenga fedha kiasi kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026, ahsante.