Primary Questions from Hon. Bahati Keneth Ndingo (10 total)
MHE. BAHATI K. NDINGO Aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha uanzishwaji wa hati fungani za Serikali za Mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, wakati wa kuwasilisha hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2021/22 Waziri wa Fedha na Mipango aliwasilisha kuhusu kuanzisha hati fungani za Halmashauri. Kifungu cha 92 ya hotuba yake ilieleza, katika jitihada za kupanua wigo wa vyanzo vya mapato rasilimali fedha Serikali itaangalia uwezekano wa kutumia hati fungani zitakazotolewa na Halmashauri za Manispaa na Majiji kama njia mbadala ya kupata rasilimali fedha kwa ajili ya miradi ya kimkakati.
Mheshimiwa Spika, hatua hii itapunguza mzigo kwenye mfuko mkuu wa Hazina ya Serikali hasa kwa Halmashauri zenye miradi ambayo imefanyiwa upembuzi yakinifu na kuwa na uhakika wa uwezo wa miradi hii kurejesha kwa faida kwa maana ya bankable projects.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (United Nations Capital Development Fund – UNCDF) na Mamlaka ya Usimamizi wa Masoko ya Mitaji (Capital Markets and Securities Authority- CMSA) imeanza mchakato wa kupitia miradi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuhakikisha Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji yatakayokidhi vigezo na masharti ya matumizi ya hati fungani yanaanza kutumia utaratibu huu katika mwaka huu wa fedha 2021/2022. Ahsante sana.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Vituo Vya Wazee nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu. Pia namshukuru Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kuwa nitafanya kazi kwa uwezo wangu wote na kwa kudra za Mwenyezi Mungu, nitatekeleza majukumu yangu ipasavyo katika kuleta maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha utoaji wa huduma, Serikali imeendelea kuboresha majengo na miundombinu ya makazi ya wazee kwa awamu ambapo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na mwaka wa fedha 2020/2021 ukarabati umefanyika katika makazi saba ya wazee ikiwemo; Nunge (Dar es Salaam), Kolandoto (Shinyanga), Njoro (Kilimanjaro), Magugu (Manyara), Kiilima (Kagera), Fungafunga (Morogoro) na Sukamahela (Singida). Aidha, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Makazi ya Wazee Wasiojiweza nchini kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha zitapopatikana. Ahsante. (Makofi)
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaweka mfumo utakaoruhusu wafungwa kupata haki ya faragha na wenza wao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutoa haki mbalimbali kwa wafungwa walioko magerezani kwa mujibu wa sheria. Haki ya faragha kwa wafungwa na wenza wao itaanza kutolewa pale ambapo mifumo ya kisheria, na miundo mbinu ya magereza itakapokidhi kutolewa kwa haki hiyo. Masuala mengine yatakayozingatiwa ni usalama, mila na desturi za Watanzania, kwani haki hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa faragha.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwajengea uwezo Wahitimu wa Vyuo nchini ili waweze kushindana katika soko la ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi ujulikanao kama, Higher Education for Economic Transformation (HEET), inaendelea na maandalizi ya uboreshaji wa mitaala iliyopo na uandaaji wa mitaala mipya zaidi ya 290 katika programu za kipaumbele cha Taifa ili kuwajengea uwezo wahitimu kuhimili ushidani wa soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua inayoendelea ni ukusanyaji wa maoni (tracer study and needs assessment) kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mahitaji halisi. Mitaala hiyo iliyoboreshwa inatarajiwa kuanza kutumika katika mwaka wa masomo 2023/2024, nakushukuru.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha jamii inarudi katika maadili mema kutokana na ongezeko la mmomonyoko wa maadili?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako hili Tukufu kujibu swali kama Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba dakika moja niweze kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa zawadi hii kwa uhai na kila kinachotokea kwenye maisha yangu likiwemo na hili. (Makofi)
Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais Mama yangu Daktari Samia Suluhu Hassan kwa imani hii kubwa aliyonipa na nimuahidi ya kwamba nitatekeleza majukumu yangu kwa weledi tuwatendee haki wananchi tunao wahudumia. (Makofi)
Niwashukuru sana wananchi wa Muheza kwa kuendelea kuniunga mkono na ushirikiano mkubwa wanaonipa na niwahakikishie Muheza bado Mbunge mnaye na nitahakikisha nawaheshimisha. (Makofi)
Nikushukuru wewe Spika na Wabunge wa Bunge hili la Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania kwa miongozo na maelekezo ya kila mara, hili ni darasa kubwa na ninaendela kujifunza. Mwisho niishukuru familia yangu mke na watoto wangu kwa mapenzi mengi yanayofanya kichwa changu kiendelee kutulia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, nijibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inachukua hatua zifuatazo ili kukabiliana na hali hiyo: -
(i) Wizara imeaandaa mwongozo wa maadili na utamaduni wa Mtanzania uliozinduliwa Tarehe 02 Julai, 2022 ambao unaendelea kusambazwa;
(ii) Kutoa elimu ya maadili na kufanya uhamasishaji wa mabadiliko ya fikra na vitendo kwa jamii kupitia Vyombo vya Habari. Mathalani, katika kipindi cha Januari – Aprili, 2023 Wizara imefanya vipindi 11. Pia Maafisa Utamaduni kutoka Halmashauri 16 kati ya Halmashauri 184 nchini wamefanya vipindi 21 kupitia vyombo vya Habari;
(iii) Kutoa elimu ya maadili kwa wadau wa malezi na makuzi ikiwemo Viongozi wa Dini, wamiliki wa vituo vya malezi na shule za awali na Wasanii. Aidha Wizara inameandaa mdahalo na semina maalum kwa Wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakati wa Tamasha la Pili la Kitaifa la Utamaduni litakalofanyika Mkoani Njombe tarehe 19-21 Mei, 2023;
(iv) Wizara inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Viongozi wa Dini, Machifu na Viongozi wa Kimila pamoja na Wizara zenye dhamana ya malezi na makuzi ya watoto na vijana pamoja na usimamizi wa maadili nchini katika kuandaa na kutekeleza mikakati ya pamoja, ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza: -
Je, lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi zilizopo Mbarali ambazo zipo katika hali mbaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge Wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya na ukarabati wa madarasa chakavu. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 na 2023/2024, Serikali imetumia shilingi milioni 360 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa 18 mapya katika Shule Kongwe za Chimala, Igalako, Ujewa na Isitu.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za Ipwani, Ibumila na Mbuyuni. Aidha, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe kote nchini. Ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza:-
Je, lini Serikali itakarabati shule kongwe za msingi zilizopo Mbarali ambazo zipo katika hali mbaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Keneth Ndingo, Mbunge Wa Jimbo la Mbarali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa mapya na ukarabati wa madarasa chakavu. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 na 2023/2024, Serikali imetumia shilingi milioni 360 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa madarasa 18 mapya katika Shule Kongwe za Chimala, Igalako, Ujewa na Isitu.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Serikali imetenga shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za Ipwani, Ibumila na Mbuyuni. Aidha, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe kote nchini. Ahsante.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza:-
Je, lini Serikali itawalipa mafao wastaafu wa Shamba la Kapunga Wilayani Mbarali lililokuwa linamilikiwa na NAFCO?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Ndingo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa ubinafsishaji kati ya mwaka 2003 na 2004, Serikali ililipa mafao ya wastaafu wote wa Shamba la Kapunga isipokuwa mafao ya mkataba wa hali bora ambayo hujumuisha mishahara miwili baada ya notisi, gunia tatu za mpunga kwa kila mwaka waliofanyia kazi au fedha taslimu kwa bei ya wakati huo ilipofungwa mikataba na mwisho walipwe mishahara ya miezi minne kila mmoja kwa kila mwaka waliofanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa madai hayo ni ya muda mrefu takriban miaka 19 iliyopita na baadhi ya wanaodai taarifa zao hazijahakikiwa. Ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikali inaendelea na uhakiki wa madai hayo ili kupata ufumbuzi kulingana na sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.
MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupanga matumizi bora ya ardhi kutokana na kasi ya ongezeko la watu nchini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kujibu swali hili naomba kwanza niombe radhi, kwamba Mheshimiwa aliyeuliza swali ni Mbunge wa Mbarali na si Mbunge wa Viti Maalum. Naomba hiyo iingie kwenye Hansard.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa, jumla ya vijiji 4,024 kati ya vijiji 12,318 vilivyopo nchini vimeandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha kuwa vijiji vyote nchini vinaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi. Miongoni mwa mikakati inayoendelea kutekelezwa ni pamoja na kuzihimiza mamlaka za upangaji kutenga fedha kwa ajili ya uandaaji mipango ya matumizi ya ardhi ya vijiji, kuendelea kutenga bajeti kwa Tume ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, kuandaa, kuwezesha na kusimamia upangaji wa matumizi ya ardhi, kuhamasisha wadau kuchangia upangaji wa matumizi ya ardhi na kubuni miradi ambayo inawezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ilibuni na kutekeleza Mradi wa Uboreshaji wa Usalama wa Milki (LTIP), ambao umelenga kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi ya ardhi miradi 1,667 katika kipindi cha miaka mitano. Aidha, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi imetenga jumla ya shilingi 5,041,232,000 kwa ajili ya kuiwezesha Tume kuendelea kupanga matumizi ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Mbarali na maeneo mengine ya nchi kuwa azma ya Serikali ni kupanga miji na vijiji vyote ili kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya ardhi linalochangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu. Niendelee kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge, kuhakikisha kwamba halmashauri zao zinaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kupanga miji na kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. BAHATI K. NDINGO aliuliza:-
Je, upi mkakati wa Serikali kuhakikisha miradi ya maji katika Jimbo la Mbarali inakamilika kwa wakati ili kuondoa changamoto ya maji iliyopo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama Wilayani Mbarali umeongezeka kutoka wastani wa 54% mwaka 2023 na kufikia 58.4% mwaka 2024. Hali hiyo imechagizwa kutokana na kukamilika kwa utekelezaji wa miradi ya maji Kibaoni, Matebete, Luduga - Mawindi, Mkunywa Awamu ya Kwanza, Miyombweni na Utengule - Usangu. Kukamilika kwa miradi hiyo kumesaidia wananchi wapatao 70,582 waishio kwenye maeneo hayo kupata huduma ya majisafi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji Chimala, Ruiwa na Igurusi Awamu ya Kwanza ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024 na kunufaisha wananchi 79,653 wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali itaanza utekelezaji wa Miradi ya Maji ya Ilongo Group Awamu ya Kwanza, Mbuyuni Awamu ya Kwanza, Itamboleo Awamu ya Pili, Iwalanje, Warumba, Vikaye, Isunura - Ikanutwa na Igunda - Muungano wilayani Mbarali.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati mahususi wa Serikali ni kuhakikisha inapeleka fedha zinazohitajika kwa wakati sambamba na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maji kote nchini ikiwemo Wilaya ya Mbarali ili miradi hiyo iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi.