Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Furaha Ntengo Matondo (36 total)

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali.

Kwa kuwa mazingira ya jiografia ya Wilaya ya Ukerewe yanaathiri sana ufaulu wa Watoto wa kike, kwa nini sasa Serikali isione umuhimu wa kujenga shule maalum ya bweni katika Wilaya ya Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nipende kujibu swali la Mheshimiwa Furaha kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna changamoto za watoto wa kike sio tu kwa upande wa Ukerewe bali kwa maeneo mengi ya nchi yetu. Nipende kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba tuna programu mbalimbali ambazo zitawezesha sasa kwenye maeneo mengi ambapo tuna changamoto ya vijana wetu kutembea umbali mrefu kuweza kupata shule za bweni katika maeneo hayo.

Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge Serikali iko mbioni sasa katika mpango wake wa P4R kuhakikisha tunaweza kwenda kujenga shule kwenye maeneo ambayo yana changamoto kama hizi ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi.

Je, ni lini barabara ya Airport kwenda Nyanguge yenye urefu wa kilometa 46 kupita Kayenze itawekewa lami kwa kuwa barabara hiyo ipo kwenye Ilani ya Uuchaguzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya Airport – Nyanguge ni kama by pass kwa upande wa magari yanayokwenda njia ya Musoma na ni kweli ipo kwenye mpango na Serikali inatafuta fedha. Tumewasiliana sana na Mheshimiwa Angelina Mabula ambaye ni Mbunge mwenyewe akiwa anaifuatilia hii barabara.

Mheshimiwa Spika, ninataka nimhakikishie kwamba bado ipo kwenye mpango na itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Mkuyuni kupita Maina mpaka Mwatex yenye Km 11 tayari usanifu wake umekamilika.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga barabara hiyo kwa lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K.
MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Furaha, Mbunge wa Viti Maalum – Mwanza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii ya Mkuyuni hadi Maina imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, Wizara ya Ujenzi kwa kusaidiana na TAMISEMI tunatafuta fedha ili kuijenga barabara hii muhimu ambayo pia itakuwa kama bypass ya kuingia Mjini Mwanza. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zinaendelea, kutafuta fedha kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza msitu wa Rubya umetoa milioni 50 kwa ajili ya kujenga Kituo cha Polisi, pale Rubya.

Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea fedha ili kituo hicho kiweze kukamilika pamoja na nyumba za maaskari?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli fedha hizo zimetolewa, lakini mpaka sasa taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba kazi hizi zinaendelea vizuri na hakujaonekana dalili za kushindwa kukamilika wala wafadhili hawajaonesha dalili ya kushindwa kuendelea kukamilisha kituo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba tuwape muda wakamilishe tuone watafikia wapi, kama kutatokea changamoto baadaye, basi tutaangalia namna gani ya kuweza kulikabili.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Wilaya ya Ilemela hakuna Chuo cha VETA, lakini wameshaandaa eneo lenye ekari 70.

Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Ilemela ili kuondoa changamoto kwa vijana wetu ya kukosa ajira? (Makofi)
NAIBUWAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge anachosema kwamba Wilaya ya Ilemela haina Chuo cha VETA na ni kweli eneo tayari limeshatengwa na tayari tulishakabidhiwa eneo hilo rasmi sisi kama Wizara kupitia wenzetu wa Mamlaka ya VETA. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wilaya hii ni miongoni mwa zile Wilaya 63 ambazo zitapata mgao huu wa fedha hizi awamu ya kwanza kwa ajili ya kuanza ujenzi katika eneo hilo la Ilemela. (Makofi)

Mhesimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jiji la Mwanza hususan Manispaa ya Ilemela inakabiliwa na tatizo la maji. Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua visima virefu vya maji ambavyo havifanyi kazi kwa muda mrefu; mfano, Nsumba Kata ya Kiseke, Mtongo Kata ya Kayenze, Lugeye Kata ya Sangabuye na Kisami Kata ya Bugogwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge Viti Maalum Mwanza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli maeneo haya aliyoyataja hususani eneo hili la Jimbo la Ilemela kwa Mheshimiwa dada yangu Angelina Mabula tayari tumeanza kazi ya ufufuaji wa visima. Tayari visima viwili vimeweza kufufuliwa na kazi zinaendelea kuhakikisha visima vyote ambavyo bado vina maji ya kutosha tunakwenda kuvifufua.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mwanza tumekuwa na shida sana na kero ya maji, na hasa miradi ambayo haitekelezeki, na ukizingatia Mwanza tumezungukwa na ziwa.

Je, ni lini Serikali itatekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mwanza tukaondokana na kero ambayo inatukumba mpaka muda huu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri katika Jiji la Mwanza pamoja na mradi tuliokuwa nao lakini ongezeko la watu limesababisha uhitaji mkubwa wa maji. Tuna mradi sasa hivi tunaongeza chanzo katika eneo la Butimba ili kuongeza uzalishaji na wananchi hawa waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Tumepata fedha zaidi ya shilingi bilioni 65 katika kuhakikisha kazi ile inaanza na mkandarasi yuko site.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa sisi kama Wizara ya Maji tutausimamia na kuufuatilia mradi ule ukakamilike kwa wakati ili uweze kuongeza uzalishaji na wananchi wa Jiji la Mwanza kwa maana ya Ilemela pamoja na Nyamagana kuweza kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hospitali ya Wilaya ya Ilemela imejengwa lakini mpaka leo hatuna vifaa tiba.

Je, ni lini Serikali itapeleka vifaa tiba katika Hospitali ya Wilaya ya Ilemela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba hospitali zetu zote za halmashauri mpya ambazo zimekamilika ujenzi wake zinanunuliwa vifaa tiba ili zianze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa. Na katika bajetii ya mwaka huu ambao tunamaliza Juni 30, Serikali ilitenga shilingi bilioni 33.5, na fedha zote Mheshimiwa Rais amezipeleka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) na tayari taratibu za manunuzi zinaendelea kwa ajili ya vifaa tiba.

Mheshimiwa Spika, pia katika mwaka ujao wa fedha, fedha zimetengwa bilioni 69.95 kwa ajili ya vifaa tiba. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba Hospitali ya Wilaya ya Ilemela ni kipaumbele.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji katika Mji wa Kisesa, Bujora, Bukandwe na Bujashe katika Wilaya ya Magu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Matondo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote na yeye nimpongeze kwa sababu ni mfuatiliaji mzuri katika masuala ya huduma ya maji. Maeneo ya Kisesa, Bujora na kote alikokutaja Mheshimiwa Mbunge tunatarajia kuendelea kupeleka huduma ya maji safi na salama.
MHE. FURAHA MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lengo la Serikali ni kusogeza huduma kwa wananchi. Je, ni lini Serikali itaongeza idadi ya tarafa katika Wilaya ya Nyamagana na Ilemela kwa kuwa zina kata zaidi ya kumi na tano na zina tarafa moja moja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuongeza maeneo ya utawala ni moja ya jukumu la Serikali ambalo tumekuwa tukilifana mahali ambapo pana vigezo vyote. Kwa hiyo, kama kunakuwa na eneo halina vigezo maana yake tunakuwa hatuna hiyo fursa ya kuongeza. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Furaha Matondo kwamba endapo maeneo hayo yaliyoainishwa yakifuata taratibu zote na zikafika katika Serikali Kuu, basi Serikali itazingatia kulinga na vigezo vilivyowekwa kikatiba. Ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Wananchi wa Kata ya Nyasaka Mtaa wa Kiloleli B wamenunua kiwanja kwa ajili ya kujenga zahanati. Je, ni lini Serikali itawajengea zahanati katika kiwanja hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Kijiji hiki kwa kununua eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati lakini nimwelekeze Mkurugenzi kuanza kutenga fedha kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hii.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa kila Wilaya imeandikiwa kupata chuo cha VETA. Je, ni lini Serikali itaboresha chuo cha VETA Buhongwa ili kiwe na hadhi ya chuo cha VETA katika Wilaya ya Nyamagana?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwanza tunakwenda kujenga kwenye maeneo ambayo hayana huduma au hayana vyuo hivyo, lakini kwenye maeneo ambayo vyuo tayari vipo ni azma vilevile ya Serikali kuhakikisha kwamba, vyuo vile tunakwenda kuviboresha kwa maana ya kufanya ukarabati lakini vilevile kuongeza miundombinu. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, kwamba Serikali inaandaa bajeti kila mwaka ile ya kufanya maendelezo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo na chuo hiki ambacho amekitaja Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina changamoto kubwa sana ya watumishi kada ya elimu na afya;

Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili kuondoa changamoto iliyopo hasa ukizingatia Ukerewe ni kisiwa ambacho kimejitenga na wananchi wake wanapata shida sana?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali zuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, si tu suala la watumishi kwenye Kisiwa cha Ukerewe, tumeamua kama Wizara ya Afya tuchukulie Ukerewe kama kanda maalum; na ndiyo maana Hospitali ya Wilaya ya Ukerewe sasa inaenda kupewa hadhi kama hospitali ya mkoa. Maana yake ni kwamba sasa yenyewe haitaenda kupata watumishi na vilevile vifaa tiba na mambo mengine kama hospitali ya wilaya bali inaenda kupata kama hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunajua kwamba kuna visiwa mbalimbali; ukisema umemaliza kijiji kimoja kumbe kijiji hicho kina visiwa mbalimbali. Maana yake ni kwamba ukizungumzia zahanati hutaenda kufikiria Ukerewe ukasema kijiji ukadhani umemaliza. Tunatamani kila kisiwa kiwe na zahanati yake kwa ajili ya logistic zilizopo kule. Kwa hiyo tunachukua tutashirikiana na wewe Mbunge na Mbunge wa Jimbo tuhakikishe tumefikia azma yenu ambayo mnaitamani.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya lami kutoka Airport kwenda Nyanguge yenye kilometa 47? Kwa sababu, upembuzi yakinifu umeshafanyika na barabara hii ni Bypass ya kupita Serengeti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Mwanza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ni moja ya barabara ya Bypass katika Mkoa wa Mwanza, Airport – Igombe – Kayenze hadi Nyanguge. Namwomba Mheshimiwa Mbunge awe na Subira, tuone bajeti hii tutakuwa tumepanga nini? Ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Mwanango kupita Kahama inayounganisha Mkoa wa Shinyanga ili kukuza uchumi na ipo kwenye ilani ya uchaguzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tulishakamilisha usanifu wa kina na tumeanza kuijenga kwa hatua na hasa maeneo ambayo ni ya mijini, ikiwa ni mpango wa Serikali kutafuta fedha kuijenga barabara ya Mwanangwa-Solwa hadi Kahama kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, nashukuru majibu mazuri ya Serikali lakini niombe tu kwa kuwa maeneo ya kanda ya ziwa yamezungukwa na madini ya kila aina.

Je, hamuoni haja ya kujenga chuo cha madini katika Wilaya ya Sengerema ili kuwapatia wananchi wetu wapate ujuzi lakini waweze kuchimba kitaalamu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa, kuwa sasa uvuvi umekuwa ni wa kisasa;

Je, hamuoni haja ya kujenga chuo cha uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema ili wavuvi wetu waweze kuvua kitaalam tuendane na kasi ya Uganda nan chi nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo umesema hapa haya masuala ambayo ni yako chini ya Wizara ya Madini. Sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Madini. Swali lake la pili ni la Wizara ya Uvuvi, kuona mipango waliyonayo juu ya kuweka vyuo hivi katika kanda ya ziwa.

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Bugando ni Hospitali ya Kanda, kutokuwa na watumishi wa kutosha kunaathiri utendaji kazi na hivyo kusababisha vifo vingi sana; na kwa kuwa Bugando inahudumia mikoa ya Kanda ya Kati, mikoa ya Kanda ya Magharibi na mikoa ya Kanda ya Ziwa: Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kulipa umuhimu suala hili ili kuweza kupata watumishi wa kutosha na kuweza kuondokana na tatizo lililopo la vifo vingi vya wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tunapokea maombi yake, na tutaenda kuyachakata kwa sababu Hospitali ya Bugando kwa siku inapata wagonjwa 1,200 mpaka 1,500 na unaona idadi ya watumishi hapa ni 1,930. Sasa tutaenda kuchakata tuone tutakachoweza kufanya, lakini mwaka 2022 walipewa watumishi 367. Kwa hiyo, tutaendelea. Kwa kuimarisha Hospitali ya Kanda ya Chato na kuimarisha hospitali yetu ya mkoa iliyopo pale na hospitali za wilaya, foleni itapungua kwenye eneo la Bugando na itawezekana sasa kumaliza hili tatizo la watumishi na msongamano uliopo pale.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Katika kupunguza adha ya maji hususan Manispaa ya Ilemela, Serikali iliahidi kufufua visima vyote ambavyo havifanyi kazi. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kufufua visima hivyo ili kuondokana na changamoto ya maji katika Manispaa ya Ilemela? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu visima kufufuliwa Ilemela, tayari tumeshaagiza na katika mwaka ujao wa fedha tutahakikisha visima hivi vyote ambavyo vimechimbwa na bado vina maji mazuri tutavitumia kuhakikisha vinaongeza huduma ya maji katika maeneo yote ya Ilemela. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Ukerewe limekuwa likipata wakati mgumu sana wa kupata Wakandarasi na Wakandarasi kushindwa kuja Ukerewe kwa sababu ya gharama kubwa ya kusafirisha vifaa vyao. Nini mkakati wa Serikali wa kuichukulia Ukerewe kama eneo maalum la kibajeti kwa ajili ya barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tayari kuna timu ambayo inafanya tathmini kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuangalia jiografia ya nchi yetu, kuona bajeti inayopelekwa kwa ajili ya barabara na kama kuna uwiano ambao ni sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, timu ile tayari ilikuwa imemaliza kazi yake na sasa imepelekwa kwa independent consultants kuweza kuiangalia vilevile taarifa ile na kisha mapendekezo yale yakirudi basi formula ya kutoa fedha iweze kubadilika kadri ya mapendekezo ambavyo yatakuja kwa ajili ya utengenezaji wa barabara. Hivyo, basi nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge kwamba, naamini katika maeneo yenye jiografia ngumu ya ufikaji kama ya Ukerewe na yenyewe timu hii itakuwa imeangalia hayo matatizo ambayo yapo. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Bukonyo – Bukongo – Masonga yenye kilometa 32 kwa sababu upembuzi yakinifu ulikwisha fanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Ntengo Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge itajengwa baada ya kufanya usanifu wa kina wa mwisho ambapo ile barabara bado hatujafanya usanifu. Kwa hiyo tukishafanya usanifu tutajua gharama na ndipo Serikali sasa itatafuta fedha kujenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wavuvi wadogowadogo hasa Wilaya ya Ukerewe tayari wameshaunda vikundi na taratibu zote za mikopo wameshafata. Je, ni lini Serikali itawapatia mikopo ili waweze kununua nyavu na kuvua kwa halali na kuachana na uvuvi haramu?( Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge Dada yangu Mheshimiwa Furaha Matondo kwamba sehemu ya mikopo ya awamu ya kwanza ambayo tulitoa karibu asilimia 80 ya mikopo ilienda Kanda ya Ziwa kwa maana ya Ziwa Victoria, ni kwa sababu tu waombaji ni wengi na kiwango cha mikopo kilikuwa kidogo. Kwa hiyo sisi tutaendelea kuwazingatia kwa kadri ambavyo tunakuwa tukipokea fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo jambo hilo lipo katika mapango wa Serikali. Ahsante sana.(Makofi)
MHE. FURAHA M. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ukerewe ni kisiwa na kwenye bajeti ya mwaka huu Serikali imetenga fedha ya kujenga barabara hiyo ya kutoka Kisorya kwenda Nansio. Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli dhamira ya Serikali ni kuijenga barabara yote kwa kiwango cha lami na Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba tayari tumeshajenga sehemu kubwa ya hiyo barabara. Hela iliyotengwa ilikuwa kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa daraja ambalo lina kilometa takribani moja, lakini kwa maombi ya wana Ukerewe na Mheshimiwa Mbunge wa Ukerewe, wameomba badala ya kuanza daraja kwa kuwa tunavyo vivuko viwili vikubwa ambavyo vitaendela kufanya kazi na hasa baada ya kuongeza kivuko kipya ni bora tukajenga barabara ya lami kuanzia Lugenzi hadi Nansio na wakati Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi anawasilisha bajeti alitoa commitment kwamba tutaanza kujenga mwaka ujao wa fedha barabara hii kwa kiwango cha lami kuanzia Nansio kuja Lugezi. Ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilitangaza mabadiliko ya bei za umeme kwa wananchi wanaoishi mjini. Wananchi wanaoishi pembezoni mwa mji mfano Kishiri, Sangabuye, Buhongwa na Kayenze na tayari walishalipia umeme wa shilingi 27,000.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawekea umeme? Walishalipa kabla ya tangazo la Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa majibu kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba kusema maneno machache yenye uhalisia na ukweli; wale wote waliokuwa wamelipa shilingi 27,000 kabla ya mabadiliko ya bei wataunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, agizo hili liko kwa Mameneja wote wa Mikoa na wa Wilaya na wanajua, na tulikubaliana kuwa wale wenzetu waliokuwa wametangulia kulipa wapewe kipaumbele kwa kufanya first in first out. Kwa hiyo wale ambao bado hawajaunganishiwa na walishalipa shilingi 27,000 wasiwe na wasiwasi gharama italipwa na wale ambao wanaona wamechukua muda mrefu naomba tuwasiliane ili tuweze kuona tatizo na changamoto iko wapi ili tuweze kuondokana na tatizo hili.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela Kata ya Sangabuye Kituo cha Afya hakuna mawasiliano. Kata ya Kayenze Kisiwa cha Bezi hakuna mawasiliano. Ni zaidi ya miaka minne sasa Serikali iliahidi kupeleka minara katika kata hizo. Je, ni lini Serikali itapeleka minara katika kata hizo ili wananchi wa kata hizo waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Furaha Mbunge wa Viti Maalum Kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Sangabuye ni eneo ambalo liko pembezoni mwa Ziwa Victoria ambapo mwaka huu mwezi wa pili nilifanya ziara na nikajionea hali halisi. Na Serikali ilichukua juhudi mahususi za kuhakikisha kwamba tunatafuta mtoa huduma akajenge mnara. Na tayari mkandarasi wa kwenda kujenga mnara katika eneo la Sangabuye tayari ameshapatikana. Hivyo tunasubiri tu muda wa utekelezaji ukamilike na wananchi wa Kata ya Sangabuye na Kituo cha Afya kilichopo pale waendelee kupata mawasiliano na vilevile wakinamama ambao wanatakiwa kulipa kwa kutumia M-pesa na Tigo-pesa basi haya mambo yote yaweze kwenda bila kuwa na shida yoyote, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ina changamoto kubwa sana ya watumishi hasa kada ya afya na elimu: Je, ni lini Serikali itapeleka walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe ili kukabiliana na changamoto kubwa sana ya watoto wetu kukosa elimu na elimu kushuka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Furaha Matondo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ajira ziko katika hatua za mwisho na hizi ajira ni pamoja na kada ya afya na elimu, kwa hiyo, katika ule mgawanyo Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe vilevile tumeizingatia na itapata katika ule mgawanyo wa walimu pamoja na kada ya afya, ahsante.

MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Jinbo la Buchosa lina watu wanaozidi laki nne, lakini hawana Chuo cha VETA; je, ni lini Serikali itajenga chuo cha VETA katika Halmashauri ya Buchosa ili wananchi wale waweze kupata elimu, lakini pia waweze kujiajiri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Furaha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu ya elimu na hata katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi inazungumza ujenzi wa Chuo cha VETA katika kila Wilaya nchini. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tumeanza. Tulianza na Wilaya 25, lakini Wilaya nne nazo vilevile zilikuwa tayari zimeshajengewa katika mwaka ule uliopita wa fedha na sasa hivi Serikali tuko mbioni katika utafutaji wa fedha, ili basi Wilaya zilizobaki karibu Wilaya 70 tuweze kukamilisha ujenzi huu wa vyuo vya VETA katika Wilaya zote nchini. Nakushukuru sana.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itajenga chanja za kuanika dagaa Kanda ya Ziwa ili wafanyabiashara hasa akinamama walioko kule waweze kupata masoko lakini pia waweze kupata faida katika biashara zao wanazozifanya? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana mwaka wa fedha ujao unaoanza tarehe 1 Julai, Wizara na Serikali kwa ujumla tumekubaliana na Benki ya Wakulima – TADB kutoa mikopo kwa wavuvi na kwa wafugaji. Kwa hiyo, ninaamini Mheshimiwa Furaha atahamasisha wananchi na hasa wanawake katika Mji wa Mwanza ili waweze kujitokeza na kupata fursa hii ambayo wavuvi wote wanayo katika nchi yetu, lakini pia wavuvi ambao watakuwa wako kwenye vikundi na wale wavuvi ambao watakuwa wanaweza kufanya shughuli hii binafsi binafsi. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Ilemela, Kata ya Buswelu walijenga hospitali. Baada ya ukaguzi ikaonekana maeneo yale ni madogo ikahamishiwa Kata ya Sangabuya kwa ahadi kwamba maeneo yale yatakuja kupewa kituo cha afya. Lakini leo ni zaidi ya miaka minne hayajawa kituo cha afya.

Je, ni lini Serikali itaweka kituo cha afya katika majengo yale yaliyoko Kata ya Buswelu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwezi uliopita nilitembelea eneo hili la Kata ya Ilemela eneo la Buswelu na kuona yale majengo ambayo yamejengwa na Wizara ya Afya, lakini na jengo moja ambalo lilijengwa kwa ajili ya kituo cha afya, na nilitoa maelekezo majengo yale ifikapo mwisho wa mwaka ujao wa fedha yaanze kutoa huduma kama kituo cha afya badala ya kubaki bila kutoa huduma. Kwa hiyo, tumeshalifanyia kazi hilo na nimwakikishie kwamba litakwenda kukamilika, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza naipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri. Napenda kujua, katika utekelezaji wa Bima ya Afya, nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia akinamama wajane ambao hawatakuwa na uwezo wa kulipa Bima ya Afya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; maeneo ya miji mikubwa kama Mkoa wa Mwanza kuna wimbi kubwa la watoto yatima na watoto wa mitaani. Nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia watoto hao kuweza kupata Bima ya Afya ili waweze kupata tiba bora?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Moja, anazungumzia kwamba ni nini Serikali itafanya kwa akinamama wajane ambao hawana uwezo, kwa sababu inategemeana, kuna mjane, lakini ana uwezo na kuna wale ambao hawana uwezo. Ninyi Wabunge mnakumbuka hapa mlisisitiza utaratibu wa kuwasaidia wasio na uwezo na utaratibu huo huo utatumika kulisaidia hilo kundi ambalo amelitaja.

Mheshimiwa Spika, pia, amezungumzia watoto wa mtaani, nao vile vile wanaangukia kwenye eneo lile lile, lakini wote kwa pamoja suala la watoto wa mtaani tusione kama ni kundi maalum, tuone ni kundi la sisi kuhamasishana kuliondoa mtaani na kuhakikisha liko nyumbani, liwe na utaratibu mzuri. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la mawasiliano katika Wilaya ya Ukerewe, Kata ya Bukiko ambayo inatumia Mnara wa Halotel 2G na mawasiliano ni ya kusua sua sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Furaha, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilianza kupandisha hadhi minara ambayo inatoa huduma ya 2G kwenda kwenye 3G mpaka 4G. Tayari Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali tumepandisha hadhi minara 304. Hivyo tunaamini kwamba itakapokamilika tutaangalia baadhi ya meaeneo ambayo bado yana uhitaji huo. Kwa Kata ya Lukiko ambayo ipo katika Jimbo la Ukerewe tumeiingiza kwenye utekelezaji kwa kuhakikisha kwamba tunakwenda kupeleka mnara pale, nakushukuru. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Kwanza naipongeza Serikali kwa majibu yake mazuri. Napenda kujua, katika utekelezaji wa Bima ya Afya, nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia akinamama wajane ambao hawatakuwa na uwezo wa kulipa Bima ya Afya? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; maeneo ya miji mikubwa kama Mkoa wa Mwanza kuna wimbi kubwa la watoto yatima na watoto wa mitaani. Nini mkakati wa Serikali wa kuwasaidia watoto hao kuweza kupata Bima ya Afya ili waweze kupata tiba bora?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Moja, anazungumzia kwamba ni nini Serikali itafanya kwa akinamama wajane ambao hawana uwezo, kwa sababu inategemeana, kuna mjane, lakini ana uwezo na kuna wale ambao hawana uwezo. Ninyi Wabunge mnakumbuka hapa mlisisitiza utaratibu wa kuwasaidia wasio na uwezo na utaratibu huo huo utatumika kulisaidia hilo kundi ambalo amelitaja.

Mheshimiwa Spika, pia, amezungumzia watoto wa mtaani, nao vile vile wanaangukia kwenye eneo lile lile, lakini wote kwa pamoja suala la watoto wa mtaani tusione kama ni kundi maalum, tuone ni kundi la sisi kuhamasishana kuliondoa mtaani na kuhakikisha liko nyumbani, liwe na utaratibu mzuri. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Je, ni lini Serikali itatoa mafunzo kwa vikundi vya BMU (Beach Management Unit) kwa ajili ya kuwa na nguvu ya kuzuia uvuvi haramu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeshaanza kutoa mafunzo kwenye vikundi vya BMU. Kama Mheshimiwa Mbunge ana kikundi ambacho pengine kinahitaji mafunzo hayo, tuko tayari kwenda kumfundisha, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ni lini Serikali itakamilisha miundombinu ya Kituo cha Afya Nakatunguru katika Wilaya ya Ukerewe ili kiweze kuwa na hadhi, kwa sababu mpaka sasa hivi hakina wodi ya wanawake, wodi ya watoto, wodi ya wazazi na miundombinu siyo rafiki sana? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna vituo vya afya ambavyo vina upungufu wa miundombinu hususani wodi za wanaume, wodi za wanawake na wodi za watoto. Tumeshaanza utaratibu wa ujenzi wa majengo ya awali kwa awamu ya kwanza na baadaye tutakwenda awamu ya pili kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo hayo ambayo yanapungua. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, kituo hicho tutakipa fedha zikipatikana kwa ajili ya kukamilisha majengo ambayo yanapungua. (Makofi)
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Rex Energy inafanya kazi ya kusambaza umeme katika visiwa vidogo vidogo saba katika Jimbo la Ukerewe, lakini mpaka sasa mradi huu unasuasua kwa sababu mkandarasi hajalipwa ruzuku. Nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, Mkandarasi Rex Energy ni mkandarasi binafsi na amepewa leseni na halmashauri kwa ajili ya kufikisha umeme kwenye maeneo hayo. Utoaji wa ruzuku una vigezo na moja ya kigezo ni uwezo mzuri wa mwekezaji katika kutoa huduma. Tutajiridhisha juu ya vigezo hivi na kama mwekezaji huyu ana vigezo basi tutampatia ruzuku kwa vigezo ambavyo tunavyo, lakini kama hatakidhi vigezo tunataka tuwahakikishie kwamba tutatafuta mkandarasi mwingine ambaye ana uwezo wa kufikisha umeme katika maeneo haya, ahsante.
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa line kubwa ya umeme kutoka Bunda kupita Nansio, Wilaya ya Ukerewe ambao unachelewa kwa sababu ya wananchi kutokulipwa fidia. Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wale ili mradi ule uweze kuendelea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunafahamu juu ya umuhimu wa mradi huu wa kujenga njia kubwa ya kusafirisha umeme kutoka Bunda, Nansio kwenda Ukerewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili tuweze kulipa fidia kwa wananchi katika maeneo haya na ili mradi huu uweze kuendelea. Kadri ambavyo mradi unaendelea, tunaendelea kuwasiliana na ku-engage na wananchi ili tuweze kukubaliana ili mradi uweze kuendelea taratibu taratibu huku tunasubiri fidia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge suala hili linafanyiwa kazi na wananchi hawa watalipwa fidia yao kuanzia mwaka huu wa fedha. Ahsante
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, je, ni lini Serikali itamlipa mkandarasi ili aweze kukamilisha Mradi wa Maji wa Vijiji Nane, Ukara katika Jimbo la Ukerewe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu - Wizara ya Maji, ameshawaelekeza Regional Managers, Wakurugenzi wa Mamlaka ambao wote wana madai ya wakandarasi kuyawasilisha Wizarani ili yaweze kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa malipo, ili waendelee na miradi ikamilike kwa wakati, ahsante sana. (Makofi)