Primary Questions from Hon. Mariam Madalu Nyoka (9 total)
MHE. MARIAM M. NYOKA Aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia ukarabati mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa ni ya muda mrefu na majengo yake yamechakaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariamu Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo chakavu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kubomoa majengo chakavu manne; jengo la Masjala ya zamani, choo cha nje cha wagonjwa, jengo la viungo bandia na jengo la zamani la huduma za kifua kikuu, kwa ajili ya kujenga jengo la kisasa la wagonjwa wa dharura ambalo limefikia asilimia 95. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi 630,340,507.00, ambapo hadi sasa fedha hiyo imetolewa yote. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2021. Ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha jengo la hosteli ya madaktari watarajali katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma lililoanza kujengwa mwaka 2014/2015?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja katika mwaka wa fedha 2022/2023 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la hosteli ya madaktari watarajali (interns) katika Hospitali ya Mkoa Ruvuma.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa hosteli hii utaendelea mara tu fedha hizi zitakapokuwa zimetolewa na tunatarajia ujenzi huu utakamilika ifikapo Juni, 2023.
MHE. JONAS W. MBUNDA K.n.y. MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Songea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariamu Madalu Nyoka Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka wa fedha 2019/2020 hadi 2021/2022 Halmashauri ya Wilaya ya Songea imepokea Shilingi bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Jumla ya majengo 14 yamejengwa kwenye Hospitali hiyo ambapo majengo saba yamekamilika na majengo mengine saba ujenzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -
Je, Serikali haioni umuhimu wa kununua gari la utawala na gari la Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mhehsimiwa Spika, Serikali imenunua magari 727 kwa ajili ya kubebea wagonjwa na magari 146 kwa shughuli za kiutawala. Hadi sasa magari 20 yamepokelewa na magari 117 yapo njiani kutoka kwa mtengenezaji.
Mheshimiwa Spika, magari yote yanatarajiwa kuwasili nchini na kukabidhiwa katika vituo vya kutolea huduma kabla ya mwezi Juni 2023. Aidha, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa Hospitali zitakazopata mgao wa magari hayo.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kujenga Barabara ya Mletele - Msamala – Mkuzo hadi Namanditi kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Mariam Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Barabara ya Mletele – Msamala – Mkuzo hadi Namanditi (Songea Bypass) yenye urefu wa kilometa 14 umejumuishwa katika mradi wa ujenzi wa Barabara ya Makambako hadi Songea yenye urefu wa kilometa 280. Sehemu ya kutoka Songea – Rutikira (km 97) ambao unagharamiwa kwa fedha za mkopo kutoka Benki ya Dunia chini ya mradi wa Tanzania Transport Integration Project (TanTIP). Maandalizi kwa ajili ya kutangaza zabuni za kumpata mkandarasi wa ujenzi yanaendelea, ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Kituo cha Afya cha Mjimwema hasa Wodi ya Akina mama, Wanaume na OPD kwani kimechakaa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya Mjimwema kilichopo katika Manispaa ya Songea kilijengwa mwaka 1982. Kituo hiki ni miongoni mwa vituo vya afya 202 vilivyofanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati mkubwa na kuongeza miundombinu ili kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za Afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2022/2023 na 2023/2024, Kituo cha Afya cha Mjimwema kilipelekewa shilingi milioni 35 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na wadau wa huduma rafiki kwa vijana kwa ajili ya ukarabati, ambapo majengo yaliyokarabatiwa ni wodi ya wanawake na watoto, jengo la huduma ya uzazi na mtoto (RCH), wodi ya wanaume na jengo la huduma za wagonjwa wa nje - OPD.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, kituo kimetenga shilingi milioni 28 kwa ajili ya kukamilisha ukarabati wa jengo la huduma za wagonjwa wa nje na wodi ya wanaume. Ahsante.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza:-
Je, wavuvi wameshirikishwaje katika mpango wa Serikali wa ununuzi wa Boti za uvuvi?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mradi huu, wavuvi walishirikishwa katika hatua mbalimbali ikiwemo kubainisha mahitaji, kufahamishwa kuomba mkopo wa boti pamoja na kuhamasishwa na kupewa elimu kuhusu fursa zilizopo kwenye mradi, ambapo, timu ya wataalam kutoka Wizarani walitekeleza jukumu la kuwatembelea wavuvi katika maeneo yao hapa nchini ili kupata maoni na mapendekezo yao kuhusu ukubwa wa boti na vifaa vyake pamoja na kutoa matangazo kwa njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari. Aidha, kupitia mchakato huo, jumla ya boti 160 zenye thamani ya shilingi bilioni 11.5 zimetolewa kwa wanufaika 3,163 ikijumuisha wanawake 1,008 na wanaume 2,155 katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kujenga kwa kiwango cha lami Barabara ya Frank Weston Tuwemacho – Namasakata hadi Misechela – Tunduru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kujenga barabara kwa kiwango cha lami kwani barabara za lami zinadumu kwa muda mrefu na zinahitaji matengenezo yasiyo na gharama kubwa. Aidha, TARURA inasimamia mtandao wenye jumla ya kilometa 144,429.77 ambapo barabara zenye kiwango cha lami ni kilometa 3,224.12 sawa na 2.23%; kiwango cha changarawe ni kilometa 41,107.52 sawa na 28.46% na kiasi kinachobaki cha urefu wa kilometa 100,098.13 sawa na 69.31% ni barabara za udongo. Kutokana na hali ya fedha iliyopo, kipaumbele cha Serikali ni kujenga barabara zenye mifereji kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Frank Weston Tuwemacho – Namasakata hadi Misechela ina urefu wa kilometa 62.9 ambapo kati ya hizo kilometa 41.9 zimejengwa kwa kiwango cha changarawe na kilometa 21 bado ni za udongo. Mwaka 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi milioni 104 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo ambapo kilomita 15 zilichongwa kati ya hizo kilomita tano ziliwekewa changarawe na kalvati mbili zilijengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwaka huu wa Fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 225 kwa ajili ya matengenezo ya barabara hiyo ambapo kilomita 21 zimechongwa. Kati ya hizo kilomita nane zimewekewa changarawe. Aidha, Serikali itaendelea kuihudumia barabara hii kwa kutenga bajeti kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MARIAM M. NYOKA aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kukarabati Kituo cha Afya cha Mkongo Gulioni pamoja na ujenzi wa Jengo la Mama na Mtoto na la Upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya cha Mkongo ni moja ya vituo vya afya 202 vilivyofanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati mkubwa ili viendane na mahitaji ya sasa ya utoaji wa huduma za afya.
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kutafuta na kutenga bajeti kwa awamu ili kuwezesha uboreshaji wa miundombinu kwenye Kituo cha Afya Mkongo Gulioni, ahsante.