Supplementary Questions from Hon. Dr. Thea Medard Ntara (36 total)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo yamenikatisha tamaa, nimechanganyikiwa, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Serikali ilianzisha Kitengo cha SUA huko Tunduru, Waziri anijibu, je, ni lini tawi hilo litaanza kufanya kazi kama Chuo Kikuu Kishiriki au Centre na twende wote huko tukaone?
Swali la pili, Vyuo Vikuu Vishiriki vya Taasisi ya Dini vilivyopo Kusini kama hicho alichokitaja, Stella Maris na kile kingine kipo pale Songea kinaitwa AJUCO, vimeendelea kuzorota na vingine vimefungwa. Serikali ndio inatakiwa kusimamia hivyo vyuo ili viweze kusimama kwenye sehemu yake. Mheshimiwa Waziri ataniambia wanasaidiaje hivi vyuo ambavyo watoto wanaosoma ni Serikali hii hii ili viweze kusimama na kufanya kazi yake kikamilifu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Thea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Chuo chetu cha SUA kilikabidhiwa eneo katika majengo ambayo yalikuwa ya camp ya waliokuwa wanajenga barabara. Serikali imefanya yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli udahili katika chuo hiki cha Tunduru bado haujaanza na kinachokwamisha kuanza udahili pale ilikuwa bado kuna miundombinu ambayo siyo toshelezi. Bado hakuna mabweni pamoja na maabara katika eneo hili. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Chuo chetu cha SUA kimepanga kuanza kutoa kozi fupi fupi pale katika eneo letu la Tunduru kwa wakulima wetu kwa lengo la kuongeza mnyororo wa thamani kwenye mazao ya korosho, mihogo pamoja na ufuta.
Mheshimiwa Spika, halikadhalika majengo yale yaliyopo kwa hivi sasa yanatumika kwa ajili ya kufanya mafunzo kwa wanafunzi wetu wanaosoma Shahada ya Wanyamapori na Utalii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Chuo chetu cha SUA kinaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutosheleza au kujenga miundombinu ili tuweze kuanza kutoa huduma pale mara tu majengo hayo yatakapokuwa yamekamilika.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, amezungumzia juu ya vyuo binafsi ambavyo vipo katika Kanda hiyo ya Kusini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imekuwa inafanya juhudi tofauti tofauti kuhakikisha vyuo hivi vinaendelea kutoa huduma. Serikali imekuwa ikifanya yafuatayo kupitia Tume ya Vyuo Vikuu:-
Mheshimiwa Spika, tumeendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha kama vyuo hivi vinatoa huduma sawasawa na elimu Bora; Tume yetu imeendelea kutoa ushauri wa kitaalam; na Tumeendelea kutoa mafunzo kwa viongozi pamoja na Wahadhiri wa vyuo hivi. Katika mwaka huu fedha, TCU imeendesha mafunzo ya Wahadhiri pamoja na wamiliki zaidi ya 218 kuhakikisha kwamba vyuo hivi vinasimama sawasawa. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibuyake, lakini niseme tu kwamba mpaka sasa vyuo vikuu vina shida sana ya wahadhili na mfumo huo unachukua muda mrefu mno, yaani mtu anaomba kibali inachukua miezi sita na zaidi.
Ni lini watarekebisha na kuona kwamba huo mfumo unakuwa mwepesi ili tupate wahadhili wa kutosha katika vyuo vikuu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Dkt. Thea Ntara ni mwakilishi wa vyuo vikuu hapa ndani ya Bunge na kwa kweli anaitendea haki sana nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tulitambua kwamba mifumo ambayo tulikuwa nayo nyuma ndiyo iliyokuwa ikileta matatizo na kusababisha ucheleweshaji mkubwa sana wa upataji wa vibali vya wageni. Mfumo ambao ninauzungumza ambao upo kwenye piloting kwa sasa ni mfumo mpya na tulipoanza kufanya majaribio kibali kina uwezo wa kutoka ndani ya siku moja ama siku mbili.
Naomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na amani, tutausimamia vizuri mfumo hu una kuondoa tatizo la upatikanaji wa vibali kwa maprofesa, wahadhili, lakini na wageni wote wanaotaka kupata vibali hapa nchini. (Makofi)
MHE. DKT THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri, kwa mara ya kwanza mimi naona amelitendea haki sana swali hilo, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; ili kuendelea kupunguza uhaba wa wahadhiri;
Je, Serikali haiwezi kurudisha utaratibu wa kuwafanya wahadhiri hao wafundishe hata baada ya miaka 65 kama nchi nyingine za Marekani na Ujerumani?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wahadhiri wetu kufundisha zaidi ya miaka 65 ni suala la kiutumishi kwenye kanuni zetu za kiutumishi. Nimuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tunalichukua suala hili, tutakwenda kukaa na wenzetu wa Wizara ya Utumishi ili tuweze kuangalia namna gani ya kurekebisha sheria zetu zile ili ziendane sasa na mahitaji haya muhimu ya soko letu la wahadhiri nchini. Ahsante sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, je, Serikali haioni wakati umefika wa kushirikisha sekta binafsi na taasisi za fedha katika kuwezesha wahitimu wa kilimo kujiajiri kwa uratibu na usimamizi wa Serikali?
Swali la pili; kwa kuwa Benki ya CRDB imeonesha njia ya kushusha riba mpaka asilimia Tisa; je, Serikali haioni kuwa ipo haja sasa kuratibu punguzo hilo la riba, kuweka mpango wa kuwezesha vijana kufaidika na mikopo hiyo kwa ajili ya kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwanza sekta binafsi na taasisi za fedha ambazo zinaweza zikasaidia vijana pengine kuweza kupata nafasi na kuziratibu kwa ajili ya kuwapa nafasi na fursa, hili tunalichukua kama wazo ambalo tunaweza tukawasiliana na Mheshimiwa Mbunge baadae na kuona namna nzuri ya kuliratibu suala hili ili vijana wetu waweze kupata ajira lakini pia kupata fursa mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo ameliulizia kwa mpango mzuri ambao umeanzishwa na Benki ya CRDB wa kushusha riba kwa asilimia Tisa. Nieleze tu kwamba pia katika ofisi ya Waziri Mkuu tayari tumekwishaanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwa kuanzia zile fedha zinazotolewa katika ngazi ya Halmashauri asilimia Nne kwa vijana pia fedha ambazo zimekuwa zikitolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana sambamba na hilo na Mabenki mengine ambayo yamekuwa yakitoa riba mbalimbali tunaendelea kuratibu na tayari mazungumzo yamekwishaanza lakini tutamshirikisha Mbunge ilia one hatua hizo na pengine atakuwa na mawazo ya ziada ambayo yatatusaidia zaidi katika kufikia azma njema ya kuwasaidia vijana wetu. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, kwanini Serikali isiridhie sehemu ya mkataba huo ambayo haina matatizo wala ukakasi ili kuwasaidia wafanyakazi wa majumbani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Serikali inawasaidaje wafanyakazi wa private sectors wakiwemo wa mahoteli na kwenye baa waweze kujiunga na vyama vya wafanyakazi ili kulinda maslahi yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mambo ambayo hayana madhara yanayoendana na mila, tamaduni na desturi ya nchi yetu, tayari sheria yetu ya ajira na mahusiano kazini ya sura namba 366 imeshayazingatia hayo na tumeyafanyia domestication kwa maana ya kuchukua na kuyaweka kwenye sheria zetu za ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika eneo hilo, siyo mikataba yote ya Kimataifa ambayo tunairidhia kwa ujumla wake. Tuna haki kwa mujibu wa Sheria za Kimataifa ya kusaini tu, lakini kuna process nyingine ya kufanya ratification na baada ya hapo unaweza ukawa unafanya reservation. Kwa hiyo, tuna reservation kwenye baadhi ya vifungu vya Mkataba huu wa Kimataifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hilo, nimhakikishie Mheshimiwa tayari Serikali ina utaratibu mzuri wa kuhusiana na Mikataba ya Kimataifa kwenye masuala ya haki za wafanyakazi kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani (International Labour Organization). Sambamba na hilo, tunaendelea kuratibu hata wale wafanyakazi wa majumbani walio nje nchi, kwa mfano, kwa nchi za Mashariki ya Kati, kule Oman, wako zaidi ya wafanyakazi 14,000 ambao walikuwa wanafanya kazi kule na 55 wako kwenye kada nyingine tofauti na ufanyakazi wa majumbani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, umejibu vizuri hilo swali, tuendelee.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili la kuhusiana na wafanyakazi wa hotelini kuingia kwenye vyama vya wafanyakazi, tunayo pia sheria inayohusiana na masuala ya Trade Unions ambayo ni sheria inayoratibu uwepo wa Trade Unions. Vyama hivi vya wafanyakazi wana haki ya kukusanya wanachama katika maeneo mbalimbali yaliyosajiliwa. Kwa hiyo, tayari utaratibu huo unafanyika na tumeshaanza kutembelea baadhi ya hoteli na maeneo mengine kuhakikisha wafanyakazi hawa wanapewa mikataba na kulinda haki zao za msingi. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana Mheshimiwa Spika, nauliza ni lini Zahanati ya Mdunduwaro – Songea Vijijini itamalizika ili wananchi wale wapate huduma, toka 2014?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ntara, amekuwa akifuatilia sana suala la Zahanati ya Mdunduwaro nami nimekwisha wasiliana na Watendaji mara kadhaa tukiwa nae na ujenzi unaendelea vizuri hatua za ukamlisha. Tulishakubaliana, ifikapo Septemba, mwisho mwaka huu Zahanati ya Mdunduwaro itaanza kutoa huduma. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, kuhakikisha kwamba zahanati hii inakamilika mwisho mwa mwezi Septemba, ianze kutoa huduma kwa wananchi. Ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo ya Waziri, naomba kufahamu kuhusu wale Maprofesa na Madaktari 203 ambao walistaafu kwa sasa wako wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, sehemu ambayo nguvu zinaisha haziwezi kufanya kazi ni sehemu ya ubongo. Kwa hiyo ina maana kwamba mtu anaweza akafanya kazi hata akiwa na miaka 70 mpaka 75 kama tunavyoona baadhi ya maprofesa humu ndani. Sasa ni lini Serikali kama Waziri alivyoahidi mwaka jana, ni lini Serikali sasa itaruhusu hawa watumishi wanaostaafu kwa miaka 65 waendelee kubaki chuoni mpaka miaka 75?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Ntara kwa kufuatilia kwa karibu sana maendeleo pamoja na upatikanaji wa watumishi hasa Wahadhiri katika vyuo vyetu. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kweli kulingana na miongozo ya Utumishi wa Umma, wenzetu katika vyuo vikuu, Wahadhiri wale pamoja na Maprofesa huwa wanastaafu wakifikia umri wa miaka 65, tofauti na maeneo mengine ya Utumishi wa Umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika kipindi cha miaka mitatu watumishi zaidi ya 203 walistaafu kwenye maeneo mbalimbali ya vyuo vyetu hapa nchini. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Ntara kwamba miongoni hawa watumishi 203 ambao wamestaafu basi watumishi karibu 103 walikuwa wamebakishwa vyuoni kwa mikataba maalum. Miongoni mwao walikuwa ni watumishi 98 ambao walikuwa ni Maprofesa na watumishi karibu watano walikuwa ni Senior Lectures.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Licha ya juhudi kubwa anazofanya Mbunge wa Jimbo la Peramiho, je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi pale Peramiho?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Thea Ntara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hitaji la kuwepo Kituo cha Polisi katika eneo la Peramiho ni kubwa kutokana na kukua kwa kasi ya shughuli za kibinadamu kwenye eneo hilo la Peramiho. Namwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Ruvuma, tutaona uwezekano wa kuingiza eneo la Peramiho katika mpango wa ujenzi wa kituo cha polisi. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Ahsante kwa majibu yako Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa Mkataba Na. 189 umefikia wapi ili kuboresha mishahara ya wafanyakazi wa majumbani?
Swali langu la pili, suala la kuboresha mishahara ya Wakuu wa Vyuo Vikuu limefikia wapi mpaka sasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tayari kuhusiana na Mkataba wa Kimataifa Na. 189 tunafahamu kwamba Serikali yetu tayari ilikwisha kuanza kufanyiakazi kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kulikuwa kuna vipengele ambavyo bado tulikuwa tunaendelea kuvifanyia kazi kwa maana ya kwamba, vipo ambavyo vinavyoendana na hali yetu ya kiuchumi na uhalisia wa kimazingira pamoja na tamaduni zetu, lakini kuna vifungu vingine ambavyo vilionekana na katika msingi wa Sheria za Kimataifa kuna kusaini Mkataba wa Kimataifa, unaweza uka - ratify lakini pia ukawa una- reservation kwenye baadhi ya maeneo. Kwa hiyo, hizo hatua zote Serikali inaendelea kuzichukua kwa haraka, nina imani ndani ya kipindi cha mwaka huu wa fedha hayo yote tutakuwa tumekwisha kuyaangalia hasa kuhusiana na haki na stahiki za mikataba ya wafanyakazi wa ndani.
Mheshimiwa Spika, katika hilo tumeanza awali kupitia Kamishna wa Kazi kuweza kuona namna gani ambavyo tunaweza kutengeneza standard ambazo zinaendana na nchi yetu za kuangalia maslahi kwenye kundi hili ambalo kimsingi maeneo mengi wanakuwa na uonevu na manyanyaso mengi. Kwa hiyo, tunaliangalia sana kama Serikali.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Medard Ntara ni kuhusu maboresho ya mishahara katika Vyuo Vikuu. Hili tayari limeanza kufanyiwa kazi na Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ni mratibu na Wizara ya Elimu ambayo pia ndiyo yenye dhamana hii katika kuangalia. Tunazidi kuangalia viwango kulingana na hali ya kiuchumi, pia uhalisia wa kidunia kwa sasa. Kwa hiyo, hivi karibuni Mheshimiwa Ntara nitamueleza hatua ambazo tumekwisha kuzifikia. Kwa hatua ya sasa siyo vema sana kuzitaja hapa hadharani. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hili wimbi kubwa la ukatili na tabia zote mbaya katika jamii: Je, Serikali haioni sasa iko haja ya kuimarisha Polisi Jamii kwenye vijiji ili angalau huo ukatili uweze kutambulika kwa haraka zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba swali hili linakaribiana sana na swali lililoulizwa na muuliza swali la msingi. Ni kweli, sasa hivi tumeweka hawa Wakaguzi wa Polisi kama viongozi kwenye ngazi hizo za kijamii, lakini pia wapo Polisi wa kawaida wenye vyeo vya chini ili kushirikiana na hawa Polisi Kata. Kwa hiyo, ushauri alioutoa Mheshimiwa tunauzingatia na ndiyo maana tutaendelea kuimarisha eneo la Polisi Kata kweye kata zetu zote ili waweze kutimiza wajibu wao huu wa msingi, ahsante sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista kwa kazi nzuri anayoifanya katika kile kijiji kwenye zahanati.
Je, ni lini sasa Serikali mtapeleka vifaa tiba kwenye Zahanati ya Mdunduwaro ili ianze kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika,
ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ntara lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa namna ambavyo wameendelea kusimamia ujenzi wa Zahanati ya Mdunduwaro na ni kweli kwamba Mheshimiwa Jenista Mhagama amekuwa akilifuatilia na Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara amekuwa akilifuatilia.
Nimhakikishie kwamba tulishakubaliana kwamba kwanza Zahanati ile ikamilike kabla ya tarehe 30 Machi, isajiliwe, lakini tumeshakubaliana vifaa tiba vitapatikana ndani ya halmashauri kwa sababu tayari wana vifaa ambavyo havitumiki katika vituo vingine, lakini na Serikali itaongezea kuhakikisha kwamba kinaanza kutoa huduma, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; niulize hivi, je, Serikali haioni haja sasa ya kutoa tamko la kuondoa udhalilishaji wa watoto wa kike wanaoolewa chini ya miaka 18 badala ya kusubiri maoni ya wadau kwa kitu ambacho kiko wazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, napenda kutoa jibu kwa Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ina taratibu zake na mtoto wa kike anaruhusiwa kuwa na umiliki wa kitu cha peke yake kuanzia miaka 18. Kwa hiyo, ushauri huo tunaomba tuendelee na kuwapa Serikali majukumu haya ili kuhakikisha nini tunakifanya katika nchi yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nauliza je ni lini barabara ya kuunganisha kutoka Mbambay hadi Ludewa itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFRY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara inayotokea Mbambay Wilaya ya Nyasa kuja Litui na kuvuka daraja la Luhuu tayari tumeshakamilisha daraja na usanifu umeshakamilika kati ya Mbambay hadi Litui, fedha inatafutwa ili sasa tuanze kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTALA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nami napenda kuuliza Lake Nyasa ina maji ya kutosha sana. Serikali ina mpango gani wa kutumia yale maji angalau vijiji vile karibu na lake vipate maji ya kutosha? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na pia nikubaliane nae. Sisi kama nchi hapa palipofikia hatuna sababu tena ya kulalamika juu ya changamoto ya maji, lazima tukubali tutumie rasilimali toshelevu tulizonazo ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia katika kuhakikisha tunawekeza miradi mikubwa na kutatua matatizo ya maji.
Mheshimiwa Spika, tumeona jitihada za Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan juu ya uwekezaji wa miradi mikubwa tunataka kuyatoa maji ya Ziwa Victoria kuyaleta Dodoma. Pia mpango wetu ni kuhakikisha maji ya Ziwa Tanganyika yanaenda kuwanufaisha wananchi katika eneo hilo la Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Barabara inayotoka Dodoma kwenda Iringa ina mashimo, yaani haipitiki, ni shida tupu.
Je, Serikali haioni iko haja sasa ya kwenda kufukia tu yale mashimo badala ya kusubiri muda eti ya kuikwangua barabara yote kiasi ambacho itachukuwa muda mrefu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ntara, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba barabara ya Dodoma – Iringa ina mashimo lakini atakubaliana nami kwamba jitihada zimekuwa zikifanyika sana za kuhakikisha kwamba yale maeneo ambayo ni korofi yanazibwa na yanaendelea kuzibwa. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi zina madaraja. Kwanza, ukiangalia madaraja yapo mengi, sasa wakati tunajenga hiyo barabara traffic haikuwa imetegemewa kama ilivyo sasa. Kwa hiyo sasa hivi bado tunaendelea kufanya economic design kuona namna ya kuboresha hiyo barabara kwa sababu sasa imeoneka ni barabara ambayo inapitisha traffic nyingi lakini pia kuna magari mengi makubwa na mazito ambayo yanapita kwenye hiyo barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Suala hili limekuwa lina muda mrefu sana, na watoto wanazidi kunyanyasika kwa kuolewa na umri mdogo; je, Serikali imejiwekea muda gani wa kufanya marekebisho hayo ya sheria?
Mheshimiwa Spika, swali labgu la pili; hivi hamwoni kwamba ipo haja ya kusitisha suala la maoni ya wadau, kwa sababu suala hilo ni wazi halafu hao wadau wengi ni hao hao wanaopenda kuoa watoto wadogo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa majibu kwa swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, baada ya Mahakama ya Rufani kutoa maamuzi kwamba Serikali ibadilishe umri wa chini wa mtoto kuweza kuoa au kuolewa, Serikali ilileta mapendekezo hapa Bungeni. Bunge lako tukufu ndilo liliagiza Serikali ikachukue maoni zaidi kutoka kwa wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, maelekezo hayo tumeyatekeleza, tumekamilisha na tuko tayari sasa kuja mbele ya Bunge ku-share maoni hayo pamoja na mapendekezo yaliyowekwa Mezani. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa, hapa Bungeni nyie mnapaswa kuleta Muswada. Ndiyo unamaanisha mko tayari kuleta Muswada? Kwa sababu maoni na mapendekezo, maana yake unayaleta kule ofisini, siyo hapa ndani. Sasa nataka nielewe vizuri, mnaleta Muswada au mnaleta hayo maoni na mapendekezo? Kwa maana maoni na mapendekezo hayawezi kuja hapa Bunge, hapa Bungeni tunasubiri Muswada.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, tuko tayari kuleta Muswada. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ubakaji na ulawiti kwa watoto ni zaidi ya uuaji. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuondoa dhamana kwa wale wanaume wanaolawiti na kubaka watoto? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dhamana ni haki ya mtuhumiwa na inaweza ikaondolewa tu pale ambapo inaonekana ni muhimu na mazingira yanalazimisha lazima iondelewe. Katika kesi nyingine zote hizi discretion ya kuondoa dhamana inabakia kwa Mahakama, endapo Mahakama itaridhika kwenye mazingira haya, huyu mtu asipate dhamana, basi hatapata dhamana hata kesi hizo za ulawiti na ubakaji kama ambavyo Mheshimiwa ameuliza. (Makofi)
MHE. DKT. TEYA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika Daraja la Kijazi ile flyover ukipita inavutia na imenyooka, sasa ukiendelea kule mbele ukapita kwenye ile flyover pale VETA yaani sisi tunaoangalia inaonekana pale juu ukingo ule umepinda. Mheshimiwa Waziri, anasemaje kuhusu ile? Inaleta picha mbaya.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama Serikali tuchukue na tuliangalie kama limepinda ama ni design, halafu tutakuja kulitolea majawabu kama tatizo lilikuwa ni usanifu ama tatizo lilikuwa ni Mkandarasi kama anachosema Mheshimiwa Mbunge kitaonekana kwamba kina mapungufu, ahsante.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri nikupongeze yaani kwa hilo kwa leo nikupongeze, lakini nina swali moja tu la nyongeza. Chuo cha Dodoma ambacho ni kikubwa Afrika Mashariki, na ni kikubwa kweli, kina pia hizo kozi; na kwa hiyo katika kuendelea kufata hizi Sera za Kimataifa, je, Serikali ni lini itaanza kujenga sasa maana yake mmesema vyuo vingine vitajengwa lakini kwa Chuo hiki cha UDOM ni lini chuo hicho mtaanza kujenga teaching hospital?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKINOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa pongezi alizotoa Mheshimiwa Mbunge na pongezi hizi moja kwa moja ziende kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sababu yeye ndiye ambaye amewezesha mambo haya yote kuweza kutokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya msingi, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma wale ambao wanasoma fani au kozi hizi za tiba, wanafanya mafunzo yao kwa vitendo katika hospitali yetu ya Benjamin Mkapa, ambayo iko karibu kabisa na Chuo hiki cha Dodoma. Lakini vilevile wanafanya mafunzo yao katika Hospitali yetu ya Milembe hapa Dodoma. Pia wanafanya mafunzo yao kwa vitendo kwenye hospitali za mikoa ya Dodoma, Singida Pamoja na Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu, na nilithibitishie hapa kwamba Serikali inaendelea na jitihada za kuona vyuo hivi vinakuwa na hospitali zake zenyewe za kufundishia ikiwemo na chuo hiki cha Dodoma. Kwa hiyo tutaendelea kutafuta fedha ili takwa hili la kimafunzo liweze kufikiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri na ya kuleta tumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza;
a) Je, ni lini sasa mtaanza mchakato wa kuwashirikisha wadau kuhusu ujenzi huo?
b) Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari sasa kuambatana na Mheshimiwa Manyanya na Mheshimiwa Agnes Hokororo, ili kwenda kufanya mikutano kwenye maeneo haya mawili ili wananchi waelewe kabisa kwamba, huo mradi sasa ni kweli utaenda kuanza?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, suala la mchakato wa kwanza katika ujenzi huu wa standard gauge kupitia mfumo huu wa Public Private Partnership kwa njia ya ubia, tayari tumeitisha kikao tarehe 15 ya mwezi wa sita, mwezi huu, ambapo kitashirikisha Wizara yetu ya Ujenzi na Uchukuzi, pamoja na Wizara ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara na Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake zote pamoja na wadau wote ambao wanashiriki katika uchimbaji wa makaa ya mawe. Na kwa hivyo basi, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge wa Mikoa hii ya Ruvuma pamoja na Mtwara kushiriki katika mkutano huu pamoja na Lindi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, kuhusu kuambatana kwenda site; niko tayari kuambatana na Waheshimiwa aliowatamka, Mheshimiwa Angelina Manyanya pamoja na Agnes Hokororo na yeye mwenyewe Mheshimiwa Dkt. Ntara, ili tukapate kutoa elimu na kuwaelimisha wananchi katika maeneo hayo kuhusu uwepo na ujio wa mradi huu muhimu katika Mtwara Corridor.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri kwa majibu yake. Sasa swali la kwanza, sehemu kubwa ya bonde la Kilombero imechukuliwa kama hifadhi, maeneo ambayo wakulima walikuwa ndio wanalima kupata chakula.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka miradi ya umwagiliaji ya kutosha ili chakula kisipungue?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kuwa na ghala moja la chakula naona kama ni risk.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza ghala jingine la chakula hasa kuliweka katika mikoa ile inayozalisha sana ikiwemo Mkoa wa Ruvuma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Katika swali lake la kwanza, katika kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Mkoa wa Morogoro kupitia bajeti yetu tulitangaza hapa ndani Bungeni kwenye kiambatisho namba tano cha bajeti yetu. Tumelezea vizuri kabisa kwamba Serikali inakwenda kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa mabonde ya kimkakati 22, na mabonde matatu yatatoka ndani ya Mkoa wa Morogoro, yaani kwa maana ya bonde la Kilombero ambalo lina hekta 53,340. Tuna bonde la Usangule ambalo linakwenda kuhudumia mpaka Malinyi ambalo lina hekta 2,500 na tuna bonde la Ifakara - Idete ambalo linagusa Wilaya yote ya Kilombero.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo katika eneo lake la Malinyi tunao mradi ambao unaendelea mradi wa Itete wa scheme ya umwagiliaji ambao pia utasaidia kutatua changamoto hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, Serikali inayo dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha ile mikoa mitano ambayo ndio Ghala la Taifa la Chakula kuendelea kuimarisha huduma mbalimbali, hasa katika upatikanaji wa huduma za ugani lakini vile vile na upataikanaji wa pembejeo za mbolea ili wakulima wetu waweze kulima na kuongeza tija, ikiwemo Mkoa wa Ruvuma ambao ni kati ya Mkoa unaofanya vizuri sana kwenye kilimo cha mazao ya chakula.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana; sasa licha ya Serikali kutoa namba ya kuwaripoti matapeli wa mitandaoni, je, Serikali ina mpango gani wa kuona sasa waathirika wanapata mrejesho badala ya kutegemea majibu ya automatic yale mifumo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ntara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze kwa swali zuri ambalo linatarajia kutoa elimu kwa watu wote. Kwanza kabisa, tuna namba 15040 ambapo ukikutanaa na namba za kitapeli basi unaweza ukatuma ujumbe na ujumbe huu utafika TCRA, baada ya hapo TCRA wataendelea kuufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipokee ushauri wa Mheshimiwa Mbunge wa kuona ni namna gani baada ya tatizo kufanyiwa kazi basi mtoa malalamiko aweze kupatiwa mrejesho.
Mheshimiwa Spika, tutalifanyia kazi, lakini vilevile napenda kuwaomba watanzania pale ambapo wanapigiwa simu na mtu akajitambulisha kwamba natoka Vodacom, Tigo na kadhalika basi naomba sana wapokee namba ambayo ni huduma kwa wateja ambayo ni namba 100. Tofauti na namba hiyo basi tuelewe kwamba hao sio watumishi wa Vodacom, Tigo wala kampuni yoyote ya mawasiliano, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na hayo majibu yanayoridhisha kiasi, nina swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hawa wanafunzi wanaokwenda kusoma katika Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, naomba Mheshimiwa Waziri atuhakikishie kwa sababu hawa wa maendeleo ya jamii wanaegemea kwenye upande wa afya na elimu; je, wako katika kundi la kupata mikopo au ni wale wa VETA na vyuo vingine vya afya tu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya swali la msingi, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba inatoa mikopo kwa wanafunzi wote wa elimu ya juu pamoja na wale wa elimu ya kati. Lakini naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatarajia kuanza kutoa mikopo kwa wanafunzi hawa wa elimu ya kati kama ilivyosomwa katika bajeti ya Serikali ya mwaka ujao wa 2023/2024 Serikali inatarajia kuanza kutoa mikopo kwa wananfunzi wa elimu ya kati katika kada za ualimu, afya pamoja na sayansi.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kupanua wigo wa kutoa mikopo hii katika kada nyingine kwa kadri ya upatikanaji wa fedha na uwepo wa bajeti, nakushukuru.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Je, Serikali haioni haja sasa ya kufanya utafiti kujua watoto wangapi waliopo Bwenini wanafanyiwa ukatili wa kijinsia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Mheshimiwa Mbunge anaomba Serikali iweze kufanya utafiti, nimwondoe hofu Serikali iko tayari kuchukua ushauri wake tuweze kufanya utafiti wa kuweza kujua athari zinazotokea katika unyanyasaji wa watoto wetu katika maeneo aliyoyataja.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; je, Serikali ina mpango gani wa kuwatumia vijana waliohitimu masomo ya environmental science katika kusaidia kueneza elimu hii ya kupunguza hii hewa ya ukaa?
WAZIRI WA NCHI. OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu, Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara kutoka Mkoa ule wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli sasa hivi tuna vijana wengi sana wamehitimu environmental science katika vyuo mbalimbali ikiwepo Dar es Salaam, SUA pamoja na University of Dodoma na vyuo vingine.
Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana katika ajenga hiyo kikubwa zaidi tunachokifanya ni kwamba si rahisi Serikali ikaajiri watu wote, lakini tumeweka suala zima la kuleta hamasa katika makundi mbalimbali hasa kutumia vijana hawa na hasa wakati fulani nilipokuwa katika mkutano pale Dar es Salaam, mkutano unaohusiana na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi tulitoa maelekezo katika NGOs mbalimbali sasa zifungue milango kwa vijana waliosoma environment science. Hata kuwapa internship au mikataba ya muda mfupi kwa lengo kubwa vijana hawa waweze kutumia kiupana zaidi kwa ajili ya Taifa letu hili.
Mheshimiwa Spika, imani yangu maelekezo yale tuliyoyatoa katika taasisi mbalimbali wenzetu wataenda kuyazingatia kwa lengo kubwa vijana hawa waweze kutumika kwa mustakabali wa nchi yetu katika utunzaji wa mazingira.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la ujenzi wa kiwanja hicho umechukua miaka saba, kama kuna hilo tatizo, sijui mgogoro inanishangaza.
Je, Serikali sasa ina mpango gani wa ku-review mkataba huo ili kuhakikisha ujenzi huo unakamilika na kiwanja kinatumika mara moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa karibu wa suala hili. Kabla hajaliuliza hapa bahati nzuri aliwahi kufika ofisini na tulilijadili kwa kina.
Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge katika kikao hiki cha tarehe 4 Machi, 2021 pamoja na mambo mengine kilijadili vilevile kufanya review ya mkataba lakini vilevile kufanya review ya design ya viwanja vile. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi, review imeshafanyika na mchakato sasa mwingine unaendelea katika kuhakikisha kwamba tunafanya review ya thamani au gharama za ujenzi ili kazi hii iweze kukamilika kwa haraka. Nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Waziri kwa ushirikiano katika eneo hilo nimekuwa nikisaidia sana. Lakini swali langu la kwanza swala la wadau kutoa maoni pamoja na elimu limefanyika kwa muda mrefu sana.
Je, Serikali kupitia comissionar wa kazi haioni iko haja sasa ya kuharakisha kuridhia mkataba huo angalau wawe parcial ili wafanyakazi hao wawe rasmi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, baada ya Serikali kupitia VETA na CVM kuzindua mitaala ya wafanyakazi wa majumbani, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza udahili wa wanafunzi hao kwa sababu sasa hivi hata wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu na Vyuo vingine wanaajiriwa kufanya kazi majumbani. Ni mpango gani sasa Serikali inafanya ili wanafunzi wawe wengi katika hivyo Vyuo vya VETA? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI) Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Thea Medard Ntara kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mkataba huu wa kimataifa tayari Serikali ilikwisha kuanza kuchukua hatua toka mwaka 2021 lakini kwa sehemu kubwa kama Mheshimiwa Mbunge anavyoelewa na nampongeza sana amekuwa akipambana sana amekuwa akipambana sana kuhusiana na swala hili. Katika mikataba ya kimataifa ina hatua za msingi tatu, hatua ya kwanza ni ya ku-sign pale ambapo wanachama wa umoja huo wanapokutana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya pili ni reservation na ya tatu ni lactification. Kwenye reservation ni pale ambapo nchi inaruhusiwa kutokukubaliana na baadhi ya matakwa ambayo yameelezwa lakini, katika ratification ni pale ambapo tayari mme-sign na badae mnaingia kwenye ratification kwamba mnaamua kuzi-domesticate hizo sheria ziweze kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufanya hivyo pamoja na uchambuzi ambao umeeleza na wadau ambapo tuliwashirikisha tulibaini kwamba sisi tulikuwa mbele kidogo ya mkataba huu wa kimataifa wa mwaka 2011 kwenye masuala ya kazi, Sheria tayari sisi tunazo nchini ambazo zinaeleza utaratibu wa kazi lakini pia masuala ya mkataba na hatua nyingine maswala ya mishahara lakini pia masuala ya afya na usalama mahali pa kazi na masuala ya ifadhi ya jamii. Haya yote yapo yameelezwa kwenye mkataba lakini sisi tulikuwa tumekisha kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaenda kuangalia sasa yale ambayo yatakuwa yanautofauti na ambayo yatakuwa na tija kwa upande wetu. Kwa kweli kundi hili ni muhumu na tunaendelea kulihudumia.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili la kuhusu mtaala wa wafanyakazi. Ni kweli Serikali ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliona umuhimu wa wafanyakazi wa ndani kuwa wananyanyasika sana na kwa Sheria tuliyonayo katika Kifungu cha tano cha Sheria ya Ajira na mahusuano kazini, Kifungu cha sita, cha saba lakini pia kifungu cha 11, vyote hivi vinaeleza kuhusu haki na wajibu wa wafanyakazi hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa sababu tumeanzisha hiyo program kwenye Vyuo vya VETA wewe mwenyewe utakuwa shahidi na Waheshimiwa Wabunge kwamba wafanyakazi wa ndani wananyanyasika sana kwenye maeneo mengi. Sasa tumeona kuanzisha utaratibu huo wa taaluma na kutangaza zaidi ili udahili uongezeke lakini pia kuhakikisha wanafanya kazi kimikataba na watambue na hata sisi kama wawakilishi…
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na mimi niulize ni lini Vijiji vya Mdundwalo, Maposeni, Malamala na Kimbango Nyasa vitapatiwa hivyo visima vya maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Ntara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo haya aliyoyataja Mheshimiwa Dkt. Ntara tayari usanifu unafanyika, gari la kuchimba visima liko kule tumeishachimba kisima kikatoka maji machache sana kiasi kwamba hayawezi hata kupanda kwenye kichotea maji hata kimoja. Niwapongeze sana Regional Manager (RM) Ruvuma niliwaagiza, kwa sababu Dkt. Ntara hili swali ameishaniuliza mara nyingi tukiwa kwenye kiti. Tumeishafanyia kazi na wananchi wametoa ushirikiano kuna mto unaitwa Mpulanginga, huu mto umeonekana una maji ya kutosha kwa maeneo ya Mdundwalo na Maposeni. Lakini vilevile maeneo haya mengine ya Nyasa vilevile baada ya gari kumaliza hapa tunarajia liende huko likaweze kuchimba visima ili wananchi wapate maji safi na salama. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru kwa majibu. Swali langu la kwanza; kwa nini, Serikali isitoe fedha kwa haraka kukamilisha hayo mabima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, bado kuna upungufu mwingi wa madarasa, je, Serikali inachukua mkakati gani wa kudumu kuhakikisha hali hii haijitokezi tena? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara. La kwanza, kwa nini Serikali isitoe fedha hizi kwa haraka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe ya kwamba, katika Sera ya Ugatuaji wa Madaraka (D-by-D) jukumu la kujenga miundombinu yoyote ya maendeleo katika halmashauri zetu nchini ni jukumu la Halmashauri yenyewe. Serikali Kuu inafanya usimamizi na ku-complement jitihada za wao wenyewe katika zile halmashauri kule. Hivyo basi, ni jukumu la Mkurugenzi kuweza kufanya tathmnini katika eneo lake na kutenga fedha katika fedha za maendeleo kuweza kumalizia nguvu za wananchi zilipokwenda kama kwenye zahanati, vituo vya afya na madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha inayotafutwa Serikali Kuu ni kwenda kuongeza tu nguvu na kasi katika eneo husika. Hivyo, basi, Serikali Kuu inaendelea kutafuta fedha hizo kama ilivyotafuta fedha za kuweza kumalizia maboma na kuongeza madarasa katika miaka mingine kama ambavyo kila Mbunge humu ndani na halmashauri yake walipata shule mpya kupitia Mradi wa SEQUIP na Mradi wa BOOST.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikkienda kwenye swali lake la pili; hali hii itaendelea kuwa hivi kwa sababu, elimu ya awali ni bure, kwa Sera ya Serikali yetu hii. Elimu ya msingi ni bure, elimu ya sekondari ni bure kwa hiyo, idadi huongezeka kadiri mwaka unavyokwenda na huwa mahitaji nayo yanaendana na wale wanaotoka huku nyuma, wanaotoka awali kwenda darasa la kwanza, wanaotoka darasa la saba kwenda Form One. Kwa hiyo, kila mwaka Serikali inaendelea kufanya tathmini na maoteo ya wale ambao wanamaliza na kuona ni namna gani ambavyo fedha inaweza ikapatikana kwa ajili ya kuondoa upungufu huu wa madarasa.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na kazi nzuri iliyoanza pale katika Mlima Nyang’oro niombe kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri;
Je, Serikali ina mpango wa kuweka miundombinu ya taa pamoja na mawasiliano kwenye eneo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwa upande wa taa kuna kitu tunakifanya katika Mlima wa Kitoga; na limekuwa ni ombi actually la Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu ya kona nyingi tuweze kuweka taa ili watu waweze kuonana na hasa kunapotokea changamoto upande wa usiku. Tumelipokea na tunalifanyia kazi, ahsante.
SPIKA: Wizara ya Mawasiliano, Waziri, Naibu Waziri. Waziri wa Nchi kuna swali hapa linalohusu Mawasiliano. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, sahamani maana Mawaziri wa Nchi tupo kadhaa lakini ngoja nilibebe tunalichukua na…
SPIKA: Ngoja, ngoja, ngoja kwa sababu swali linahusu mawasiliano na hapa ndani hakuna Waziri wala Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, sasa wewe ndiye Waziri wa Nchi unayeshughulika humu ndani. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni suala linalohusu sekta maalum kwa hiyo tunalichukua na tutalifikisha kwenye sekta ili sekta iweze kutayarisha majibu na kumjibu Mheshimiwa Bunge ipasavyo. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na mpango huo mzuri wa urasimishaji na umiliki wa ardhi hizo, je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa nyumba zote za tope kwenye ardhi hizo? Ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Ntara, hebu rudia swali lako.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, pamoja na mpango wa urasimishaji na umiliki wa ardhi hizo, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba nyumba zote za tope zinaondoka kwenye ardhi hizo kabla hata hawajafanya huo urasimishaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ujenzi wa nyumba hizi unategemea hali halisi ya wananchi wa eneo lile. Katika namna yoyote ile, kuondoa nyumba za tope maana yake ni kuongeza uhamasishaji kwa jamii kuitumia mifumo mbalimbali ya kujipatia fedha zinazoweza zikawahamisha kutoka kwenye nyumba za tope kwenda kwenye nyumba za kisasa.
Mheshimiwa Spika, nawaomba tu Waheshimiwa Wabunge muwe sehemu ya wahamasishaji ili maeneo ambayo nyumba za tope zipo, basi tushirikiane katika kuwahamasisha wananchi wa eneo lile kutumia uchumi walionao katika maeneo hayo kuboresha makazi yao, ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri yanayoonesha angalau matumaini, nina swali moja la nyongeza. Je, atatuhakikishia kwamba ukarabati utaendana sambamba na kuweka vifaa vya ufundishaji katika vyuo vyote ikiwemo vyuo vya kati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza kwenye jibu la msingi kwamba, tumepata mkopo wa zaidi ya dollar milioni 425, matumizi makubwa ya mkopo huu ni kuhakikisha tunakwenda kuviongezea miundombinu vyuo vyetu hivi vikuu, lakini vilevile tunakwenda kuboresha mitaala na kuanzisha mitaala mipya na vilevile tunakwenda kusomesha Walimu/Wahadhiri kwa ajili ya vyuo hivi. Sambamba na hivyo tunakwenda kununua vifaa kwa ajili ya vyuo vikuu vyote vya umma nchini. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi hili eneo la vifaa nalo vilevile limezingatiwa. Kwa vile amezungumzia vilevile vyuo vya kati, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge vyuo vya kati navyo tumevitengenezea mkakati wake maalum kabisa.
Mheshimiwa Spika, kwanza tuna mradi wetu wa EASTRIP ambao zaidi ya Dollar za Kimarekani milioni 75 tumeweza kusaini kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivyo lakini vilevile kwa ajili ya ununuzi wa vifaa. Kwa hiyo, sambamba na huu mradi wetu wa HEET ambao utashughulikia vyuo vikuu, lakini tuna miradi mingine midogo midogo ambayo itashughulikia vyuo hivi vya kati kwa kuhakikisha kunakuwa na wahadhiri wa kutosha na vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwenye vyuo vyetu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri, baada ya kumpata Mkuu wa Chuo Dar es Salaam ambaye ameanza kutangaza habari za chuo hicho, Chuo chetu cha Utalii - Dar es Salaam kinajiandaa kuwa kituo cha umahiri. Je, Serikali imefikia hatua gani katika mipango yake ili kuona kabisa kwamba watoto wanaotoka pale wanakuwa mahiri kweli kweli?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kumekuwa na malalamiko mengi sana kuhusu wahudumu wetu, yaani wanaita Wazungu Customer Care, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kwamba vijana wetu wote wanaomaliza Vyuo vya Utalii vya Binafsi na vya Serikali wanapata mafunzo kazini ili watoe huduma bora katika mahoteli yetu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ntara, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo chetu cha Utalii kilichopo Dar es Salaam na matawi yake kule Arusha na Mwanza, kimefanya maboresho katika mitaala ya mafunzo ili kuongeza umahiri wa wahitimu wetu katika sekta ya utalii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kuimarisha mitaala hii, tunayo imani kubwa sasa kwamba mafunzo yatakayotolewa na umahiri wa wahitimu wetu utakuwa wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwenye eneo la customer care, ni kweli imekuwepo changamoto ya wahudumu wetu kulalamikiwa mara kwa mara. Nataka nimhakikishie kwamba jambo hili linafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na kama anafuatilia kwa ukaribu huduma sasa hivi za watu wetu zimeanza kuimarika kwa kiasi kikubwa.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ili utekelezaji mahiri uonekane kiuhalisia Serikali inaonaje sasa kuvielekeza vyuo kuwa na jiji au halmashauri za kuzilea kama wafanyavyo wenzetu kule Japan, China na Indonesia.?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wanafunzi wanapata shida sana unapokuja wakati wa kwenda field kupokelewa katika taasisi au idara mbalimbali. Je, Serikali ina mpango gani sasa kutoa mwongozo kwa idara na taasisi hasa za Serikali kupokea wanafunzi wa kufanya tafiti zao freely bila vikwazo vyovyote? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Dkt. Thea Ntara, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hakuna utaratibu wa vyuo vikuu kulea halmashauri au majiji katika nchi yetu. Utaratibu uliopo ni kwamba halmashauri hizi ziko huru kupata huduma katika vyuo vikuu au vyuo vikuu vishiriki kwa kadiri ya chuo kikuu kilivyokuwa na wabobezi katika eneo fulani. Sasa kwa vile Mheshimiwa Mbunge ametoa ushauri hapa tuweze kuangalia jambo hili, basi ushauri wake tumeupokea na tunaenda kuufanyia tathmini kuweza kuangalia namna gani vyuo vyetu vinaweza vikashirikiana na halmashauri hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la pili kuhusiana na suala la mwongozo, tunaomba nalo tulipokee. Tutakwenda kukaa na halmashauri zetu pamoja na taasisi nyingine ili kuweza kuona namna bora ya wanafunzi wetu wanapokwenda kufanya tafiti zao katika maeneo mbalimbali ya taasisi hizi nchini wasiweze kupata usumbufu wa aina yoyote, nakushukuru sana.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka huduma za theatre, x-ray na vitanda vya kuzalisha katika Kituo cha Afya cha Mkwawa University?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali imeshapeleka fedha nyingi katika halmashauri zetu. Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda katika mwaka huu wa fedha karibu kila halmashauri imepata si chini ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kununua vifaa tiba vya majengo ya upasuaji lakini pia x-ray zimepelekwa za zaidi ya shilingi bilioni 93. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili ni endelevu na tutahakikisha kituo cha afya hicho pia kinapata vifaa tiba.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo: -
Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa mradi wa Bonde la Mto Msimbazi (Dar es Salaam Metropolitan Development Project Phase Two)?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali imejipangaje kuwalipa fidia wananchi wanaoishi katika eneo la mradi wa ujenzi wa Daraja la Jangwani kuanzia Magomeni, Jangwani hadi Fire? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ujenzi wa Daraja la Jangwani tunafanya kazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa maana ya ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi pamoja na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Suala la fidia linaenda sambamba na jitihada hizi za ujenzi kupitia Mradi wa DMDP.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, Serikali tumejipanga, Wizara ya Ujenzi wakati tunajenga Daraja. Pia Ofisi ya Rais, TAMISEMI kupitia mradi wa DMDP tutashirikiana kuhakikisha ujenzi unaenda sambamba na fidia kwa wananchi, ahsante sana.