Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Amb Dr. Diodorus Buberwa Kamala (11 total)

MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo ahadi ya kulipa fidia wananchi waliotoa maeneo yao kupisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Omukajunguti:-
(a) Je, ni lini wananchi wanaohusika watalipwa fidia walizoahidiwa?
(b) Je, ujenzi wa uwanja huo utaanza lini?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ina mpango wa kujenga kiwanja kipya cha ndege katika Mkoa wa Kagera katika eneo la Omukajunguti kitakachokuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa kama Airbus 320 au Boeing 737 zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 100 mpaka 200 kwa wakati mmoja. Eneo hilo lina ukubwa wa hekta zipatazo 2,400 linalojumuisha Vitongoji vya Mushasha, Bulembo na Bogorora. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa uthamini wa mali za wakazi wa eneo hilo uliofanyika mwaka 2010 ulibainisha fidia ya shilingi bilioni 12.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kuwa kutokana na fidia hizo kutolipwa kwa wakati italazimika kufanya marejeo ya uthamini wa awali kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi husika. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya kuanza kulipa fidia kwa wananchi wa eneo hilo. Mara taratibu za marejeo ya uthamini zitakapokamilika zoezi la ulipaji fidia litaanza.
(b) Mheshimiwa Spika, ujenzi wa kiwanja cha ndege kipya katika eneo hilo upo katika mpango wa maendeleo wa muda mrefu. Ujenzi wake utategemea kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri wa anga na kufikia ukomo wa uwezo wa kiwanga cha sasa cha Bukoba. Serikali itaendelea na maandalizi ya awali kwa ajili ya kiwanja cha ndege kipya yaani kwa kukamilisha ulipaji wa fidia, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali ili kubaini makadirio ya gharama za uwekezaji katika kiwanja kipya.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Tulipoanza kutekeleza Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki, kuna bidhaa kutoka Kenya ziliwekwa kwenye kundi „B‟ ambazo zilikuwa zinatozwa kodi iliyokuwa ikipungua taratibu hadi ilifikia kiwango cha asilimia sifuri mwaka 2010.
(a) Je, bidhaa hizo ziliongezeka kwa kiasi gani kuingia Tanzania kuanzia mwaka 2005 – 2015?
(b) Je, viwanda vya Tanzania vinavyozalisha bidhaa za kundi „B‟ vilikabiliwa na changamoto zipi kutokana na kuondolewa kwa kodi iliyokuwa ikipungua taratibu hadi kufikia asilimia sifuri mwaka 2010?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye vipengele (a) na (b), naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, lengo kuu la Umoja wa Forodha ni kukuza biashara ya bidhaa baina ya nchi wanachama na kuongeza uwekezaji na uzalishaji ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Katika utekelezaji wa Umoja wa Forodha, nchi wanachama zilikubaliana kuwa na kipindi cha mpito cha miaka mitano kuanzia Januari, 2005 hadi Disemba, 2009 ambapo baadhi ya bidhaa kutoka Kenya kuingia nchi za Uganda na Tanzania ziliendelea kutozwa Ushuru wa Forodha uliokuwa unapungua taratibu na kufikia kiwango cha sifuri Disemba 2009. Bidhaa za Kenya ambazo hazikuondolewa ushuru moja kwa moja wakati wa kuanza kutekeleza Umoja wa Forodha ziliwekwa katika kundi „B‟ ambazo ni zile zilizosindikwa kwa kiwango cha kati (semi finished goods) na zile zilizokamilika (finished goods).
Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo mafupi, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye vipengele (a) na (b).
(a) Mheshimiwa Spika, thamani ya bidhaa zilizonunuliwa kutoka Kenya mwaka 2005 ilikuwa ni shilingi bilioni 64.837 ikilinganishwa na hela za Kitanzania shilingi bilioni 174.396 mwaka 2010. Aidha, mwaka 2015, thamani ya bidhaa hizo ilifikia hela za Kitanzania shilingi bilioni 267.881 ambapo manunuzi yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 14.9 katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015. Bidhaa ambazo Tanzania imekuwa ikinunua kwa wingi kutoka Kenya ni pamoja na dawa baridi, mafuta ya kula, saruji, sabuni, vipuli vya kuendeshea mitambo, dawa za mifugo, madaftari, bidhaa za plastiki na vifungashio vya bidhaa ambavyo vingi vinatumiwa na wajasiriamali wadogo wadogo na viwanda vidogo vidogo.
(b) Mheshimiwa Spika, viwanda vya Tanzania vilikabiliwa na changamoto ya ongezeko la bidhaa za kundi „B‟ kutoka Kenya hali ambayo iliongeza ushindani ukizingatia sekta ya viwanda nchini Kenya ni shindani, kuongezeka kwa vikwazo visivyo vya kiforodha kwa bidhaa kundi tajwa zinapoingia nchini Kenya kama vile vinywaji vikali vinavyozalishwa na viwanda vya Tanzania na utamaduni wa Watanzania kupenda bidhaa za kutoka nje zaidi.
Katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya kudhibiti na kusimamia uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha, kuboresha mazingira ya uendeshaji wa biashara kwa kuwa na miundombinu iliyo mizuri kama ya barabara, bandari, viwanja vya ndege pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika na bei rahisi na kuhamasisha wafanyabiashara kuzalisha bidhaa zenye ubora na viwango vya Kimataifa ili kuleta ushindani katika Soko la Afrika Mashariki.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA Aliuliza:-
Jumuiya ya Ulaya inatekeleza Mkakati wa Ajenda ya Mabadiliko.
Je, Tanzania imejipangaje kukubaliana na changamoto zinazotokana na Ajenda hiyo ya Mabadiliko ya Jumuiya ya Ulaya?
NAIBU WAZIRI, MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA
AFRIKA MASHARIKI Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, agenda ya Mabadiliko ya Umoja wa Ulaya ilipitishwa mwaka 2011 ikiwa na lengo la kuongeza ufanisi wa Sera ya Maendeleo ya Umoja huo. Mabadiliko haya yanahusisha kanuni mbalimbali za kutoa misaada ya maendeleo. Kanuni hizo ni pamoja na utofautishaji wa kiwango cha maendeleo kilichofikiwa na kila nchi inayotarajiwa kupatiwa msaada.
Katika kutekeleza hili, Umoja wa Ulaya unalenga kutoa misaada kwa nchi zenye uhitaji zaidi na mkazo ukiwa katika kusaidia kupunguza umaskini katika nchi hizo. Kanuni nyingine ni kuelekeza misaada yake katika sera za kipaumbele ambazo zimebainishwa katika Mkakati wa Kimataifa wa Maendeleo Endelevu wa 2030. Mkakati wa Ajenda ya Mabadiliko umeainisha maeneo yatakayopewa kipaumbele katika utekelezaji wake ikiwemo masuala ya haki za binadamu na utawala bora, usawa wa jinsia, vyama vya kiraia na Serikali za Mitaa, rushwa, sera, usimamizi wa kodi na usimamizi wa sekta ya umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maelezo hayo, napenda kuliarifu na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali imechukua hatua mahsusi zifuatazo katika kukubaliana na changamoto zitokanazo na Agenda ya Mabadiliko ya Umoja wa Ulaya:-
(i) Serikali imeimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha tunapunguza utegemezi kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo;
(ii) Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kuzingatia Sera ya Ubia baina ya Serikali na Sekta binafsi ya mwaka 2009 na Sheria ya Ubia baina ya Serikali na Sekta Binafsi ya mwaka 2010. Mkakati huu unasaidia kuongeza wigo wa vyanzo vya fedha za kugharamia miradi ya maendeleo na kupunguza utegemezi kwa wahisani;
(iii) Serikali inaendelea kuwashawishi wawekezaji kutoka nchi mbalimbali kuja kuwekeza zaidi hapa nchini. Jitihada hizi zinaenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kufanyia biashara nchini na kupunguza gharama za kufanya biashara na uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi kuwekeza hapa nchini; na
(iv) Wizara yangu imeanzisha idara maalum ya kuratibu masuala ya diaspora kwa lengo la kuratibu uhamasishaji wa Watanzania waishio ughaibuni kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi yetu, ikiwa ni pamoja kuwekeza hapa nyumbani.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Msitu wa Hifadhi ya Taifa Minziro una vivutio vingi vya utalii.
(a) Je, ni watalii wangapi wametembelea msitu huo ndani ya kipindi cha miaka 20 hadi sasa?
(b) Je, wananchi wanaoishi karibu na msitu huo wananufaikaje?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya mwaka 2015, Msitu wa Hifadhi wa Minziro haukuwa miongoni mwa maeneo yaliyohifadhiwa na kusimamiwa kwa ajili ya shughuli za utalii. Hata hivyo, kwa sasa hifadhi hiyo ipo katika hatua za awali za maandalizi ya mpango endelevu wa kuendesha utalii wa ikolojia katika msitu huo.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015 Serikali ilianzisha mradi wa kuboresha uhifadhi wa bionuwai katika hifadhi 12 za misitu ya mazingira asilia zilizopo nchini. Hifadhi hizo zikiwa ni pamoja na Mlima Rungwe kule Mbeya, Udzungwa na Kilombero zinazopakana na Iringa na Morogoro, Uluguru na Mkingu zinazopakana na Morogoro, Amani, Nilo na Magamba zilizopo ndani ya Mkoa wa Tanga, Chome kule Kilimanjaro, Rondo – Lindi na Mlima Hanang Mkoa wa Manyara, chini ya mradi unaofadhiliwa na Mfuko wa Mazingira na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP). Aidha, kutokana na kuwepo kwa mipango ya awali ya kuanzisha utalii wa ikolojia katika hifadhi hiyo, katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2015 jumla ya watalii 11 walitembelea hifadhi hiyo ambapo tisa ni raia wa kigeni na wawili ni Watanzania.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanaoishi jirani na Msitu wa Minziro kwa kutunza, kuhifadhi na kulinda msitu huu kwa sasa wananufaika kwa kupata vyanzo bora vya maji, hali ya hewa iliyo bora na ardhi yenye rutuba na sifa nyinginezo muhimu kwa kilimo na maisha ya wananchi kwa ujumla. Aidha, katika siku zijazo baada ya kukamilika kwa mpango unaoandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu, wananchi hao watanufaika kwa kupata gawio la asilimia 26 ya mapato yatakayotokana na utalii wa ikolojia ambao hufanyika kwa njia shirikishi na wananchi katika kusimamia hifadhi na kuendesha utalii huo.
MHE.BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Kupitia vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwaka 2015 Serikali ya Kenya iliruhusiwa na Jumuiya hiyo kuuza ndani ya nchi hiyo bila kutozwa kodi bidhaa za ngozi na nguo zinazozalishwa nchini humo kwenye maeneo huru ya uwekezaji (Export Processing Zones [EPZ]).
Je, ni sababu zipi za msingi zilizotumika kufanya uamuzi huo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Afrika Mashariki ibara ya 25 inahusu kanuni zinazosimamia uzalishaji kwenye maeneo huru ya uwekezaji kutoka nje, teknolojia na kutengeneza ajira. Ibara ya 26 inaeleza kuwa viwanda vilivyopo kwenye maeneo haya havipaswi kulipa kodi hata kidogo…

…havipaswi kulipa kodi hata kidogo wanapoingiza malighafi kwa ajili ya uzalishaji. Aidha, viwanda hivi vinaanzishwa kwa ajili ya kuongeza mauzo nje na kupata fedha za kigeni na wanaweza kuuza kwenye soko la ndani asilimia 20 ya kiwango kinachozalishwa kwa mwaka huska na kulipa kodi kiasi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia Mkutano wa 17 wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ulizungumzia suala la mitumba ya na viatu, Serikali ya Kenya iliwasilisha ombi la kuuza asilimia 20 ya bidhaa zinazozalishwa katika maeneo huru ya uwekezaji yaani EPZ bila kulipa kodi. Sababu ya msingi iliyowasilishwa na Kenya na kukubaliwa na nchi wanachama ni kuwa kwa kuuza bidhaa hiyo bila ushuru wananchi wangenunua bidhaaa mpya kutoka maeneo huru ya uwekezaji badala ya mitumba. Pamoja na kukubali ombi hilo iliamuliwa kuwa bidhaa kutoka maeneo huru ya uwekezaji yaani EPZ ikiingia katika nchi za jumuia itatozwa kodi zote pamoja na ushuru wa forodha.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
(a) Je, lini mradi wa maji ya kutoka Mto Kagera utaanza kuhudumia wananchi wa Kyaka na Bunazi?
(b) Je, mradi huo utagharimu kiasi gani cha fedha?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa kutoa maji Mto Kagera kwenda kwenye Miji ya Kyaka na Bunazi. Kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa makabrasha ya zabuni za ujenzi inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi za utekelezaji wa mradi huo zitajulikana ifikapo mwezi Septemba, 2018 baada ya kukamilika kwa usanifu unaoendelea.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Serikali iliunda Bodi ya Kusajili Wakandarasi (CRB) ambayo ina jukumu la kusajili, kuratibu na kusimamia mwenendo wa makandarasi nchini.
• Je, tangu kuanzishwa kwa CRB ni wakandarasi wangapi Watanzania wamesajiliwa na taasisi hiyo?
• Je, Serikali Kuu na Halmashauri za Wilaya zinatumia vigezo gani kutoa kazi kwa wakandarasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ka niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Bodi ya Usajili wa Makandarasi tangu ilipoanzishwa mwaka 1997 imesajili jumla ya makandarasi wa Kitanzania 13,523. Kati ya makandarasi hao, makandarasi 8,935 usajili wao uko hai na makandarasi 4,578 wamefutiwa usajili kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kushindwa kulipia ada ya mwaka na kukiuka taratibu nyingine zinazoongoza shughuli za ukandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumiwa na Serikali katika utoaji wa zabuni kwa makandarasi vinazaingatia matakwa ya Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2011 na Kanuni zake za mwaka 2013. Vigezo hivyo ni pamoja na kampuni kusajiliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi, ukomo wa ukubwa wa kazi kulingana na daraja la usajili, mahitaji maalum ya mradi husika, wataalam, vitendea kazi, uzoefu wa utekelezaji wa miradi ya aina hiyo na uwezo wa ampuni kifedha wa kutekeleza mradi husika. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Chuo cha Maendeleo ya Wananchi - Gera ni muhimu katika kuchochea maendeleo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha utendaji wa chuo hicho?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vilihamishwa kutoka iliyokuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika mwaka wa fedha 2016/2017 kuja Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kufuatia uhamishio huo Wizara ilitoa kandarasi kwa vyuo vitatu ambavyo ni Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kina wa hali halisi ya miundombinu na vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika Vyuo vyetu vya Maendeleo ya Wananchi kabla ya kuanza taratibu za kuvifanyia ukarabati ikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera. Vilevile Wizara inaendelea kufanya tathmini ya rasilimali watu kwa vyuo vyote kwa lengo la kujua hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini kuhusu hali ya vyuo hivyo, Wizara itabaini mahitaji ya wafanyakazi, miundombinu, vitendea kazi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuvipatia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa vyuo hivyo kikiwemo Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Gera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji utakaofanyika utalenga kuimarisha utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi kwa fani zilizopo kwa sasa. Aidha, fani na stadi nyinigne mpya tofauti na za sasa zitaanza kutolewa katika vyuo hivyo kulingana na mahitaji ya soko la ajira na mahitaji ya jamii husika.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Je, Kiwanda cha Sukari Kagera tangu kimepata mwekezaji mpya baada ya kile cha mwanzo kushindwa kuendelea na uzalishaji kimetoa mchango gani kwa Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Kiwanda cha Sukari cha Kagera kibinafsishwe, faida na michango mbalimbali imepatikana kama ifuatavyo:-
a) Uzalishaji wa sukari umeongezeka kutoka tani 15,362 mwaka 2004/2005 hadi tani 75,568 mwaka 2017/2018, uzalishaji huu umesaidia kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza bidhaa hii toka nje ya Nchi.
b) Pia kiwanda kina utaratibu wa kuwatumia Wakulima wa nje (outgrowers) katika kulima Miwa inayotumika kuzalisha sukari. Mpaka sasa kuna wakulima 500 wanaolima eneo la ekari 5,019 za miwa. Kwa mwaka 2017/2018 tu wakulima hao waliweza kuzalisha tani 60,000 za miwa ambazo ziliwapatia kipato cha shilingi bilioni tatu.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwaka 2018 kiwanda kimetoa ajira 6000 ikilinganishwa na ajira 124 zilizokuwepo mwaka 2006. Aidha, kiwanda kimejenga Hospitali yenye vitanda 78 vyenye uwezo wa kufanya operation kwa kutumia Madaktari Bingwa. Hospitali hiyo sasa ndiyo ya Rufaa kwa zahanati 11 katika eneo hilo.
d) Katika juhudi za kuchangia elimu, kiwanda kimechangia vifaa vya ujenzi, ujenzi wa madarasa, kuchimba visima vya maji, kujenga vyoo, kujenga nyumba za walimu, kuchangia madawati, kujenga maabara na kuchangia vifaa vya kufundishia kwa shule 23 katika Wilaya ya Misenyi.
e) Aidha, katika juhudi za kuhifadhi mazingira, jumla ya miti 20,000 imepandwa katika eneo la kiwanda, pia kiwanda kimejenga mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,250 kwa kiwango cha changarawe ambazo pamoja na kutumika kwa shughuli za kiwanda hutumiwa pia na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitatu iliyopita kuanzia 2015/2016, 2016/2017 mpaka 2017/2018 Kiwanda cha Kagera Sugar kimelipa jumla ya shilingi 44,461,815,798 kama kodi Serikalini.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
(a) Je, Ranchi ya Missenyi ina ng’ombe wangapi kwa sasa?
(b) Je, wananchi wanaoizunguka ranchi hiyo wananufaikaje kutokana na uwepo wake?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI aliuliza:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ranchi ya Missenyi iliyopo Wilayani Missenyi, Mkoani Kagera ni miongoni mwa ranchi sita za mfano zinazoendeshwa na Kampuni ya Taifa ya Ranchi (NARCO). Ranchi hii kwa sasa ina ng’ombe 1,670, mbuzi 212 na kondoo 120. NARCO inaendelea kuiboresha na kuiongezea mifugo zaidi ili iweze kwenda sambamba na eneo lake ambalo ni hekta 23,998.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ranchi ya Missenyi hutumika kama shamba darasa kwa jamii ya wafugaji na inatoa elimu ya nadharia na vitendo kwa wafugaji kuhusu ufugaji wenye tija. Vilevile ranchi hii hutoa fursa ya upatikanaji wa mifugo bora kwa ajili ya nyama na uzalishaji mitamba chotara kwa ajili ya wafugaji wa ng’ombe wa maziwa. Katika kipindi cha mwaka 2017/2018 jumla ya mitamba 12 iliuzwa kwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kata ya Mabale na mbuzi sita walitolewa na ranchi kwa wafugaji wa Kitongoji cha Rwengiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2018/2019 NARCO imepanga kutenga vitalu kwenye baadhi ya ranchi zake ikiwemo Ranchi ya Missenyi kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji wa maeneo ya jirani kupata maeneo ya malisho na maji wakati wa kiangazi.
MHE. BALOZI. DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-

Mto Kagera ni chanzo muhimu kinachoweza kusaidia upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wanaopakana nao:-

Je, kwanini Serikali isifanye utaratibu wa kuvuta maji hayo ili yawasaidie wakazi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeshaanza mipango ya kutumia Mto Kagera kama chanzo cha maji katika maeneo mbalimbali yanayopakana na Mto huo. Kwa sasa Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba (BUWASA) imepanga kuutumia Mto Kagera kama chanzo cha maji kwa Miji ya Kyaka na Bunazi pamoja na vijiji mbalimbali vinavyozungukwa na mto huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa mradi kwenda Miji ya Kyaka na Bunazi kwa kutumia chanzo cha mto huo, BUWASA imemwajiri mtaalam mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni na matarajio ya usanifu huo utakamilika mwezi Septemba, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matarajio ya ujenzi wa mradi huo utaanza katika mwaka wa fedha 2020/2021.