Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Minza Simon Mjika (16 total)

MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, ni lini Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria utapelekwa katika Mkoa wa Simiyu hususani katika Wilaya ya Meatu kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Shirika la KfW la Serikali ya Ujerumani imekamilisha taratibu za kupatikana kwa wataalam washauri ambao watasimamia utekelezaji wa mradi huu mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Mkoa wa Simiyu. Mradi huu unahusisha ujenzi wa bomba kuu kilometa 195, matenki nane yenye ujazo wa lita milioni 11.9 na mabomba ya usambazaji kilometa 49.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi unatarajia kuanza mwezi Agosti, 2021 na miji mikuu ya Wilaya itakayonufaika ni Busega, Bariadi, Itilima, Maswa, Meatu na vijiji vya vilivyoko pembezoni mwa bomba kuu umbali wa kilometa 12 kila upande. Mradi umepangwa kutekelezwa kwa miaka minne. (Makofi)
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, ni lini barabara kutoka Kolandoto hadi Meatu itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge Viti Maalum, Simiyu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kolandoto hadi Meatu ni sehemu ya barabara ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti hadi Oldeani Junction yenye urefu wa kilometa 328. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hii ulishakamilika na ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza kulingana na upatikanaji wa fedha.

Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 5,000 zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Kolandoto – Mwanhuzi yenye urefu wa kilometa 62.5 na kipande cha Lalago – Ng’oboko – Mwanhuzi yenye urefu wa kilometa 74.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa Daraja la Mto Sibiti pamoja na barabara unganishi kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 25 mpakani mwa Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu na Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida ni hatua za awali za ujenzi wa barabara hiyo ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itachimba visima vya maji katika Kata ya Mwamanyili Kijiji cha Milambi Wilayani Busega ili kuwapunguzia adha ya maji akina mama wa Kijiji hicho?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama. Serikali itafanya upanuzi wa mradi wa maji wa Mwamanyili ambao chanzo chake ni Ziwa Victoria kwenda katika Vijiji vya Mwamanyili, Mwanangi, Milambi na maeneo ya Nassa Ginery. Upanuzi huo utahusisha ukarabati wa chanzo cha maji, ulazaji wa bomba la urefu wa kilometa 13.6 na ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 15. Kukamilika kwa utekelezaji wa mpango huo kutaboresha huduma ya maji hadi kufikia asilimia 54. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali imepanga kutekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Miji ya Busega, Bariadi na Itilima Mkoani Simiyu. Mradi huo utanufaisha zaidi ya vijiji 200 vya Miji hiyo.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Njika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kujenga Vyuo vya VETA katika Mikoa na Wilaya mbalimbali kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha kwa lengo la kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini. Kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 25 na Mikoa 4 ukiwemo Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu na maeneo mengine, wananchi wa Meatu wanashauriwa kutumia Vyuo vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo jirani kwa ajili ya kupata elimu na mafunzo ya ufundi. Nakushukuru.
MHE. ESTHER L. MIDIMU K.n.y. MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA Wilayani Busega?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inayo azma ya kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo, kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Spika, Busega ni miongoni mwa Wilaya 63 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa vyuo vya ufundi stadi katika mwaka huu wa fedha. Nakushukuru sana.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa fidia kwa Wananchi wa Simiyu wanaopakana na Hifadhi za Wanyamapori na kuathiriwa na wanyama hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto hiyo, Wizara imeendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kusimamia Utatuzi wa Migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori wa mwaka 2020/2021 mpaka 2025 kwa kufanya yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nikufanya doria za mara kwa mara kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu. Aidha, Mheshimiwa Rais alielekeza vijengwe vituo vya askari katika maeneo ya Busega na Meatu. Mchakato wa ujenzi umeanza ambapo vituo viwili vitajengwa katika maeneo tajwa mwezi Aprili, 2022. Sambamba na hilo, maombi ya vibali vya kuajiri askari 600 yameshawasilishwa kwenye mamlaka husika.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni kutoa mafunzo ya mbinu za kujilinda na kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu. Jumla ya Halmashauri 17 zimepatiwa mafunzo hayo. Aidha, Wizara ina namba maalum za simu kwenye kila kanda za kiutendaji ili kuwezesha wananchi kutoa taarifa za matukio ya wanyamapori bila malipo.

Mheshimiwa Spika, malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya Sh.790,721,500 imetolewa kwa wananchi 3,598. Aidha, Wizara imepokea maombi ya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi kutoka wilaya mbalimbali zikiwemo Wilaya za Mkoa wa Simuyu. Kwa sasa Wizara inafanya uhakiki wa maombi kabla ya malipo kufanyika. Ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaongeza Watumishi wa Afya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu mwaka 2018 ilikuwa na watumishi 130. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 Wizara iliwapanga watumishi 70 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu na kuhamisha wengine 18 hivyo kufanya jumla ya watumishi kuwa 218.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuwapanga watumishi katika mikoa hii ya pembezoni mwa nchi ili kufikia malengo kwa kadri tutakapokuwa tunapata vibali vya kuajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, lini Daraja la Lyusa na Itembe na kalavati la Nkoma, Lyusa na Mwanjolo vitajengwa ili Daraja la Sibiti lipitike mwaka mzima?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Lyusa na makalavati ya Nkoma, Lyusa na Mwanjolo yamejumuishwa katika mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti River – Lalago – Maswa yenye urefu wa kilometa 389 ambapo Mkandarasi ameshapatikana na mkataba wa ujenzi unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa daraja la Itembe lenye urefu wa mita 150 lililopo katika Mkoa wa Simiyu, kazi za ujenzi zinaendelea na zimepangwa kukamilika mwezi Oktoba, 2023; ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itaongeza watumishi wa afya katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali iliajiri watumishi 7, 736 wa Afya na Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ilipangiwa watumishi 104 na watumishi saba walipangwa Hospitali ya Halmashuri ya Wilaya ya Meatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2022/2223, Serikali itaajiri watumishi wa kada ya afya 8,070. Aidha, baada ya taratibu za ajira kukamilika watumishi hao watapangwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Meatu.
MHE MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani kwa kutengeneza barabara zote mbovu katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutengeneza barabara zenye hali mbaya katika Mkoa wa Simiyu kila mwaka kutokana na bajeti inayotengwa. Barabara zenye hali mbaya zimeendelea kupungua kutoka kilometa 1,512.71 sawa na asilimia 36.32 mwaka 2020/2021 hadi kilometa 1,126.38 sawa na asilimia 27.05 mwaka 2022/2023. Hii ni baada ya ongezeko la bajeti kutoka shilingi bilioni 5.13 mwaka 2020/2021 hadi shilingi bilioni 18.38 kwa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 17.78 kwa ajili ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini katika Mkoa wa Simiyu kufanya ujenzi na matengenezo ya barabara za jumla ya kilometa 995.21 ambazo zitapunguza barabara zilizo na hali mbaya kutoka asilimia 27.05 hadi asilimia 19 ya mtandao unaohudumiwa na TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuzihudumia barabara za Mkoa wa Simiyu kwa kutenga bajeti kwa ajili wa ujenzi na matengenezo ya barabara hizo kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka mtaalam wa X–Ray katika Hospitali ya Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 inaajiri watumishi 7,612 wa kada mbalimbali za afya, wakiwemo wataalam wa X-Ray. Hivyo, Hospitali ya Wilaya ya Meatu itapatiwa mtaalam wa X-ray baada ya taratibu za ajira kukamilika, ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga Zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mwongozo wa Ujenzi wa Zahanati katika Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa mwaka 2007 wananchi wanatakiwa kuanza ujenzi wa boma mpaka hatua ya lenta.

Mheshimiwa Spika, baada ya kufikia hatua ya lenta Serikali hupeleka fedha kwa ajili ya umaliziaji wa jengo. Hivyo wananchi wa Kata ya Binza wanashauriwa kuanza kwa utaratibu huo, ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, kuna mkakati gani wa kujenga vituo vya afya kwenye kata za pembezoni mwa Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miaka mitatu ya fedha 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 Serikali imejenga jumla ya vituo vya afya 466 vilivyogharimu shilingi bilioni 718.1 katika maeneo ya kimkakati kote nchini. Katika Mkoa wa Simiyu jumla ya vituo vya afya nane vimejengwa katika kata za kimkakati kwa gharama ya shilingi bilioni nne.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya katika kata za kimkakati kote nchini zikiwemo kata katika Halmashauri za Mkoa wa Simiyu.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Bukumbi – Meatu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Minza Simon Mjika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kata ya Bukundi ina Kituo cha Polisi ambacho kiko kwenye jengo lililoazimwa kutoka Idara ya Mifugo, Halmashauri ya Wilaya ya Meatu. Ofisi ya Mkurugenzi wa Wilaya ya Meatu imetoa eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 1,011.5 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi Kata. Ujenzi wa kituo hicho utazingatiwa katika mpango wa ujenzi wa Vituo vya Polisi Kata uliondaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI vitakavyoanza kujengwa nchi nzima kuanzia mwaka wa fedha 2024/2025.

Mheshimiwa Spika, katika awamu ya kwanza ya ujenzi wa Vituo hivi vya Polisi na Bukundi itakuwemo. (Makofi)
Ujenzi wa Shule ya Watoto Wenye Mahitaji Maalum – Simiyu

MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga shule ya watoto wenye mahitaji maalumu katika Mkoa wa Simiyu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi 2021-2026 kadiri iwezekanavyo watoto wenye mahitaji maalumu wanatakiwa kusoma katika shule jumuishi au vitengo. Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu ya shule ili ziwe jumuishi ikiwa ni pamoja na kupeleka vifaa visaidizi, walimu wa elimu maalumu na fedha ya chakula kwa ajili ya watoto wote wenye mahitaji maalumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Simiyu una jumla ya vitengo 15 katika Halmashauri za Bariadi Mji ina vitengo vinne, Itilima ina vitengo viwili, Bariadi Vijijini ina vitengo vitatu, Busega ina vitengo viwili, Meatu ina vitengo viwili na Maswa ina vitengo viwili.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kutolea elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu, kununua vifaa visaidizi, kupeleka fedha ya chakula na kuajiri walimu wataalamu wa elimu maalumu.
MHE. MINZA S. MJIKA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga zahanati katika Kata ya Binza – Maswa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Kata ya Binza wameanza ujenzi wa zahanati katika Kijiji cha Matarambuli. Aidha, halmashauri inaendelea kuhamasisha wananchi wa Kata ya Binza kuendelea na ujenzi mpaka hatua ya boma na Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati hiyo. Ahsante.