Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Neema Gerald Mwandabila (25 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kipekee kuweza kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa kibali kuingia mahali hapa, hakika nimeona ni kwa namna gani jinsi Bungeni kulivyo pazuri kiasi kwamba kweli ukiwa umeingia humu kutoka lazima utamani kutoa roho ya mtu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikishukuru Chama Cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli Rais wetu kipenzi kwa kuweza kuhakikisha uchaguzi huu unakuwa wa haki, lakini pia kusimamia wanyonge wote wa nchi hii waweze pia kushiriki katika maamuzi ya kutunga sheria katika nchi hii. Niweze kushukuru familia, wadau, rafiki, jamaa, viongozi wa dini na marafiki zangu wote wana maombi wote walioweza kunisaidia kuweza kufika mahali hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho lakini si kwa umuhimu nishukuru Wanasongwe, niwashukuru wanawake wa mkoa wa Songwe kwa kuweza kuwa wazalendo na kunipa nafasi ya kuweza kuingia mahali hapa, bila kura zao haikuwa rahisi, lakini waliweza kusimama imara na kunipa kura na leo niko ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujielekeza katika hotuba hotuba ya Mheshimiwa Rais. Kipekee niseme hii ni hotuba ambayo imejaa matumaini mengi kwa Watanzania. Watanzania tunayo imani kubwa na Mheshimiwa Rais kulingana na namna ambavyo ameweza kufanya kazi kubwa ndani ya miaka mitano iliyopita, aliyofanya ni mengi kila mtanzania anajua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite katika kipembele cha elimu ya ufundi, nikirejea vyuo vya VETA na DIT ambavyo viko katika Mkoa wangu wa Songwe. Serikali imeweka pesa nyingi sana katika hivi vyuo vya VETA na DIT, ni vizuri vinavutia na vina mazingira mazuri sana kwa watoto wetu kuweza kupata mafunzo ya ufundi pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyopo ni kwamba, hivi vyuo havitumiki ipasavyo, havitumiki kwa kiwango kinachostahili. Ukienda katika maeneo yale idadi ya wanafunzi waliopo katika vyuo ni wachache. Kama Serikali imeweka pesa basi tutafute namna ambayo itakuwa nyepesi kwa vyuo hivi kuweza kupata wanafunzi na mchango wangu kwa Serikali, ningependa kushauri mambo yafuatayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kungekuwa na direct enrolment ambayo wale wanafunzi ambao wanakuwa hawajapata nafasi ya kuingia Sekondari, wapewe nafasi, wachaguliwe kama wanavyochaguliwa wale walioenda sekondari, waweze kupangiwa vyuo vya ufundi. Hii itasaidia wale wazazi wa wale watoto waone kama watoto wao nao pia wamepata opportunity na wakawajibika kuwapeleka watoto katika hivyo vyuo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe kwa halmashauri kwa sababu tayari tunayo 10% ambayo tunatoa kama mkopo, tungetumia pesa hii kuweza kusababisha mafunzo kwa vile vikundi ambavyo vimekuwa vimeanzishwa. Kumekuwa na changamoto ya utoaji wa pesa nyingi kwa vikundi lakini wanavikundi wanashindwa kubuni miradi yenye tija, wanaishia kubuni pikipiki, wanaishia kubuni bajaji, lakini pia wanaishia kubuni kubuni miradi ya ufugaji kuku, kitu ambacho kinasababisha washindwe kufanya marejesho mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea na kumalizia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda umeshaisha Mheshimiwa, kengele imeshagonga.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Mpango huu wa Mwaka Mmoja, lakini pia wa Miaka Mitano inayokuja. Kipekee kabisa nikupongeze kwa namna unavyoendesha Bunge hili, kikao hiki. Hakika unatutendea haki kama Wabunge na tunafurahia uendeshaji wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu dakika tano ni chache, lakini namuomba Mungu aniongoze ili niweze kuongea vyema kwenye suala la TANESCO, suala la nishati kwa ujumla, lakini pia, suala la TRA. Hakuna changamoto kubwa ninayoipata katika Mkoa wangu wa Songwe kama kusikia umeme umekatika, umeme hauna nguvu, umeme hautoshi, hakika wanavyokuwa wanaelezea wananchi kule huwa inasikitisha sana. Unakuta mwananchi ana ofisi, ofisi yake inategemea umeme. Analipa pango, analipa gharama nyingine zote, lakini mwisho wa siku anachokipata anakuta ni kichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika kusema hayo nasema gharama za uendeshaji wa umeme katika nchi yetu bado ni za juu. Ukiangalia kwa upande wa TANESCO, ni base katika suala la domestic electricity, gharama inayolipwa kwa kila watt below 75 ni shilingi 100. Gharama inayoenda kulipwa above 75 kilowatts ni 350, hapa sijazungumzia suala la industrial electricity. Tunapoongelea ushindani wa soko na Mheshimiwa wetu Rais amejitanabahisha kuwa sera yake kubwa ni kuifanya nchi ya Tanzania iwe nchi ya viwanda na tunajua viwanda haviwezi kuendelea pasipokuwa na umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia kwa namna gharama hizi za umeme zinavyokuwa na nikiangalia soko la bidhaa zetu tunakotaka kuzipeleka, unakuta wakati mwingine tunawapa wakati mgumu wajasiriamali wetu na wawekezaji kwenye ushindani wa soko katika mataifa mengine. Nitarejea katika mfano mdogo tu wa sukari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niseme kwetu sisi Tunduma hatuna shida sana na sukari kwa sababu, tuko mpakani tunatumia sukari ya Zambia. Wakati mwingine nawaza kwamba, inakuwaje nchi ndogo kama Zambia inatushinda sisi Tanzania kwenye uwekezaji wa sukari mpaka inaanza inafanya supply kwetu katika kanda zetu za mpakani kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sukari Zambia inauzwa Sh.2,000 ukija huku kwetu sukari inaenda hadi Sh.3,000. Sasa unapoongelea shilingi 3,000 na sidhani kama kuna Mtanzania yeyote humu ndani asiyependa kitu cha bei rahisi, hata kama tunasema ni uzalendo hauwezi ukaenda kwa style hiyo kwamba, nafanya uzalendo huku naumia. Kwa hiyo, niombe, niiombe kwanza Bodi ya Sukari itafute namna ya kuifanya biashara ya sukari kama fursa ya kuipatia Serikali pesa. Kama watawekeza vizuri na kama pia watu wa nishati watatuonea huruma kupunguza ghrama za uendeshaji wa viwanda naamini nchi yetu inakoenda itakuwa ni nchi ambayo ina mafanikio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani Zambia nchi ambayo ni ndogo walipe umeme kwa gharama za shilingi 77 kwa domestic, lakini pia kwa business wanalipa shilingi
108.99 wakati hapa Tanzania domestic tu ni shilingi 100 na tena ni shilingi 350 yani kwa wale ambao wanatumia above 75 kilowatts. Kwa hiyo, niiombe Serikali iangalie na itathmini vizuri kwenye suala la nishati ili viwanda vyetu viweze kukua, lakini pia iweze kufanya tathmini vizuri kwa kutafuta mazao ambayo yataweza kupunguza adha kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nirudi kwenye suala la TRA ambalo pia yamekuwa ni malalamiko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba niishie hapo. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika nashukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kidogo katika huu Mpango wa Miaka Mitano. Kwanza kabisa kabla sijaendelea, napenda niunge mkono hoja Mpango huu. Pia napenda kuwapongeza Wizara ya Fedha kwa Mpango huu, tunaamini miaka mitano hii, haya mambo yote yaliyoandikwa humu yakitekelezwa tutakuwa tuko sehemu nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mchango wangu napenda kujielekeza katika mambo mawili. Katika hayo mambo mawili, napenda kuongelea mambo ya uzalishaji wa bidhaa muhimu za ndani; mfano sukari, chumvi, mafuta ya kula ambayo iko katika page ya tano na ya sita kwenye mambo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kuongelea kwenye ukuzaji wa soko la ndani. katika kukuza uchumi wa nchi, tunajua kabisa nchi yetu na Mataifa mengine yameathiriwa sana na suala la Corona. Tukisema kwamba tunaweza kuongeza fedha kutoka nje, siyo jambo jepesi, lakini lazima tujitathmini. Soko la ndani tulilonalo kwa bidhaa zile za msingi ambazo kila Mtanzania lazima atatumia, tumejidhatiti vipi?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika kuchangia hayo, nilitaka nirudi kule kwetu Songwe, Wilaya ya Momba katika Kata ya Ivuna ambapo tuna mradi wa chumvi. Huu mradi upo na tafiti zilishafanyika na ikaonekana kabisa chumvi iliyopo pale ni ya kiwango kikubwa sana ambacho hakiishi leo, lakini siioni ile dhamira ya Serikali kuwekeza pale pesa ya kutosha ili chumvi ile iweze kuhudumia angalau Kanda ya Chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapoongelea chumvi, ni kitu ambacho mtu anaweza asitumie sukari, lakini chumvi akaitumia. Kwa hiyo, katika Wizara hii nilitamani tuongezee kipengele cha chumvi, kwa sababu mpaka sasa hivi sielewi kama chumvi iko Wizara ya Madini au iko sehemu gani? Kwa sababu kwenye Madini haijawekwa na sioni popote chumvi ambapo inasoma katika Mpango huu.

Mheshimiwa Spika, katika Mradi huu wa Chumvi, tunaishukuru Serikali, ilitenga shilingi milioni 535, lakini ikaweza kutupatia shilingi milioni 120, si haba, lakini kiwango cha pesa kinachohitajika ili uzalishaji uwe mkubwa ni karibu shilingi bilioni nane. Kwa Serikali hii ya Tanzania ambayo ni Tajiri, siamini kama inashindwa kweli kujikita kuweka fedha kiasi cha shilingi bilioni nane izalishe chumvi ambayo ni lazima itauzika na ikizidi tunaweza tuka-export nje.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka nijikite hapo. Otherwise ningependa pia kuchangia kwenye kipengele cha mafuta kidogo. Tunaamini kabisa kwamba Watanzania wengi ni wakuliwa na wangeweza kupata fedha kupitia hii fursa ambayo ipo kwenye mafuta kwa kujielekeza kuzalisha mbegu za alizeti, chikichi na hata kuzalisha ufuta wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme kwamba kama kweli tuna dhamira ya kukuza uchumi, lazima tuwatazame hawa watu ambao wanaitwa wakulima; watu wa chini kabisa ambao ndio wanatufanya wote tuwe na amani hapa, maana bila chakula tunaamini kabisa hakuna mtu ambaye angekuwa yupo comfortable kukaa hapa kama chakula kisingekuwepo. Kwa hiyo, kabla haujatokea mgomo wa wakulima, napenda kuona kabisa wakulima wanapewa kipaumbele, kwa mambo yao yale ya msingi mfano hiyo fursa ambayo ipo ya kuzalisha mafuta, mahindi na kadhalika, yangekuwa yanachukuliwa kwa uzito. Kama ni viwanda vya uchakachuaji wa hizo bidhaa, viwekwe vile ambavyo vina ubora vitafanya finishing nzuri na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nisiseme mengi sana, naomba niishie hapo. Otherwise naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia. Awali ya yote, napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa moyo mkunjufu kabisa kwa viongozi wa Wizara hii, Mawaziri, Makatibu kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanya jitihada kubwa kuhakikisha tunapata maji katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijachangia kile ambacho kinaugusa moyo wangu sana nilitaka nitoe kama taarifa kwa Wizara hii kwamba ile miradi ya maji waliyoiweka kule Tunduma maji hatupati na kisingizio ni kwamba fedha za kununua LUKU hakuna. Naambiwa kwa wiki fedha inayotakiwa ni karibu shilingi 700,000 hadi shilingi 1,000,000. Kitu ambacho siamini kabisa kwamba Wizara mpaka sasa imeshindwa kukaa na watu wale kule chini kuweza kuweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha tunapata maji. Hata hivyo, tunawashukuru sana kwa ile miradi ya maji, tunaamini kama mambo haya madogo madogo atayazingatia tutaweza kupata maji kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Wizara iweze kukaa na wale watu wahakikishe Mji kama Mpemba unaokua kwa kasi uweze kupata maji. Ni mji unaokuwa kwa kasi lakini mpaka saa hizi maji hakuna na wanategemea mradi wa kutoka Ileje kuja Tunduma kitu ambacho najua mradi huo hautakamilika leo. Niikumbushe Wizara kwa kuiomba kwamba ule Mradi wa Maji kutoka Ileje kuja Tunduma ambao ni karibu shilingi bilioni 17 tu, mtusaidie tuweze kufanya kazi haraka kulingana na mahitaji ya Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilitaka kuiomba Wizara kuhusiana na maji Wilaya ya Ileje. Maji yanayotoka ni machafu, yana takataka kitu ambacho siamini kama Wizara inashindwa kutoa chujio la kuchuja maji katika Kata ya Itumba ili tuweze kupata maji masafi. Hata sisi tungependa kuonekana tuna nguo safi, nadhifu na hata yale mashuka kwenye hospitali kule ya wilaya yawe basi yana mvuto kwa sababu maji yale yanapelekea hata mashuka kwenye hospitali ile yanakuwa machafu. Alikuja Mheshimiwa Mollel, Naibu Waziri wa Afya aliona hali halisi na namna mashuka yanavyoharibika katika hospitali ile ya wilaya kutokana tu na kwamba maji ni machafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, napenda sasa kujielekeza kwenye hoja ambayo kwa kweli inaniumiza na inatia uchungu sana ninapokuwa nikiifikiria. Katika shule zetu nyingi maji hakuna. Tarehe 8 Machi, nilipata nafasi ya kwenda kwenye shule mbili ya Chikanamlilo na Mpakani Sekondari, Chikanamlilo ipo Wilaya ya Momba, tulikuta watoto wanaugua matumbo kwa sababu hakuna maji. Nimshukuru Mheshimiwa Condester aliweza kuwapatia zile taulo za kike zenye dawa ili wale Watoto zaidi ya mia moja waweze kupona ule ugonjwa uliokuwa unawasumbua wa matumbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilipopewa hii changamoto pale kwamba maji hakuna nilijaribu kufuatilia, uzuri wake tulikuwa na Mheshimiwa DAS pale. Maji katika Kata ya Ndalambo yapo shida ikaonekana ni kwamba shule haiwezi kuvuta yale maji kwa sababu gharama za kulipia yale maji ni kubwa na shule kwa kulingana na pesa inayopata haiwezi kugharamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikaona sasa hii ni changamoto ya sisi kama viongozi kuichukua na kuweza kuisemea kwamba Wizara ya Maji na hizi taasisi nyingine mfano hii Wizara ya Elimu waweze kukaa, wajadiliane, waangalie kwanza ni kwa namna gani hizi shule ziwe na uhakika wa maji? Nilitamani kama viongozi tuje na sheria ya kwamba maji kwenye shule iwe kigezo kimojawapo cha kuhakikisha shule inasajiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imagine tangu asubuhi mtoto anaenda shuleni, hanawi mikono, atatamani ale kitu, atalamba mikono; penseli zenyewe wanalamba, watoto wataacha kuugua? Kwa hiyo, niseme kwamba kwa hili ningependa kabisa Wizara ya Maji ichukue kama changamoto ya msingi na ikiwezekana kwenye miradi yake ya msingi, waongeze mradi ambao utakuwa mahususi kwa ajili ya taasisi ambazo zinahudumia watu wengi ambazo ni shule, vituo vya afya, mahospitali na vitu kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa sababu Sheria ya Maji imetaja wazi kabisa kwamba maji ni haki ya kila mwananchi, maji ni huduma ya msingi, usafi wa mazingira ni huduma ya msingi ya wananchi, watuangazie katika eneo hili. Kwa sababu, kutibu maradhi yatokanayo na uchafu ni gharama kubwa sana, pia kitendo cha kutokuwa na uhakika wa maji kinasababisha watoto washindwe kusoma vizuri. Hii ni kwa sababu sehemu wanazoenda kutafuta maji ili waje wamwagilie tu kwanza maeneo yao pale ni shida; na maji ya kuja kusafishia tu madarasa yao inakuwa ni shida. Kwa hiyo unakuta mtoto anachoka kuchota maji. Badala ya kukaa atulie kusoma, anawaza tu dumu lake la maji atunze vipi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya kusema hayo, naomba niseme nashukuru. Mchango wangu unaishia hapo kwa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika Wizara hii muhimu katika ustawi wa Taifa letu. Awali kabisa kwanza ningependa kutoa pongezi kwa Wilaya ya Kigamboni kwa shughuli waliyoifanya ya kuweza kumbaini mwizi wa mafuta kwa kweli nilipoisikiliza ile clip nilijisia vibaya sana nikaona kwamba kumbe wafanyabiashara wetu wanahujumiwa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Sara Msafiri Pamoja na uongozi wake wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na kwa miaka hii miwili niseme kwamba bado wamechelewa wanatakiwa wajidhatiti kuhakikisha maeneo yale ya Kigamboni yanakuwa salama kwa ajili ya kuhakikisha mafuta hayaibiwi tena. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningependa kuipongeza Wizara hii kwa sababu Waziri wa Wizara hii na viongozi wake wamekuwa ni watu wanaotusikiliza vyema na pia wamekuwa wakitoa ushirikiano kwetu mkubwa tunapokuwa na changamoto katika maeneo yetu tunawashukuru sana viongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitapenda kujielekeza moja kwa moja kwenye changamoto za wananchi bajeti kweli ni nzuri inatia matumaini lakini kama ilivyo ada hatuwezi tukaacha kuongelea changamoto za wananchi wetu ambazo wanakuwa wanatupasia ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto ambazo tunakabiliana nazo ni Pamoja na usambazaji wa umeme ambao unaenda kwa kulega lega na tunapokuwa taunafuatilia tunaambiwa kwamba bajeti inayotoka katika Wizara kwenda katika maeneo yetu kwa ajili ya usambazaji wa umeme inakuwa ni ndogo sana kiasi kwamba mwisho wa siku mameneja wetu katika mikoa na wilaya zetu wanapata changamoto ya kuonekana kama hawafanyikazi kumbe bajeti wanayopewa kwa ajili ya kuhakikisha umeme unawafikia wananchi inakuwa ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, nilitamani kuiomba Wizara itengeneze mkakati mzuri ambao utahakikisha umeme unasambazwa kwa ukubwa kwa maana ya kwamba wanapokuwa wanaweka bajeti ndogo ile tija ya usambazaji wa umeme inakuwa haionekaniki na wananchi watakuwa wanaendelea kuona kwamba watu wa TANESCO ni watu wanaokula rushwa sana kitu ambacho wakati mwingine unakuta hata wale mameneja hizo rushwa hawali ila tu ni mazingira ya usambazaji umeme yanakuwa yako duni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia nilipenda kuongelea suala la umeme wa REA kwa maeneo ya mjini. Siyo miji yote kwamba ina mitaa katika miji mingine mfano mimi kwangu kule Tunduma tuna maeneo mengine ambayo ni vijiji ndani ya mji mfano Chiwezi, Mpande ni maeneo ambayo kwa kweli ni magumu kwa usambazaji wa bajeti hii inayopelekwa kuweza kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano nikitolea eneo la Chiwezi bajeti tu ya kupeleka umeme kule ili iweze kufika ni takriban bilioni mbili wakati huo huo meneja wetu wa wilaya anapewa bajeti ya milioni 260. Kwa hiyo, unakuta mazingira kama hayo maeneo kama ya Chiwezi yanaweza yakawa hayapati umeme kwa wakati na mwisho wa siku nilitamani sana kuiomba Wizara ichukue hii kama special mission ya kuweza kuhakikisha maeneo haya yanapata umeme kwa bajeti ambayo ni nje ya ile wanayokuwa wametoa kwenye wilaya.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kumekuwepo na changamoto ya umeme kukosa nguvu na kitendo cha umeme kukosa nguvu mara nyingi huwa kinatokea pale ambapo transformer inakuwa imezidiwa uwezo wa kufanyakazi na tukiangalia transformer nyingi zinazokuwa zimewekwa vijijini yaani ni zile zenye uwezo mdogo unakuta ndani ya muda mfupi zile transformer zinakuwa zinazidiwa kiasi kwamba umeme unakuwa hauna nguvu. Nilitamani sasa kama Wizara waje na mpango mbadala badala ya kupeleka hizo transformer zenye uwezo mdogo maeneo yote wajaribu maeneo mengine kwa assessment zao wapeleke zile transformer ambazo zitakuwa ni kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umeme unapokuwa unakosa nguvu ina maana kwamba kazi nyingi zinashindwa kufanyika vizuri na hata kama watu wamejiajiri kupitia umeme unakuta wanashindwa kufanya kazi zao ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ningependa kuongelea suala la bei za umeme tunapoongelea Wizara hii ya Nishati kwenye kipengele cha umeme hii ndiyo sehemu watanzania wengi wanaweza kujiajiri. Kaatika kujiajiri huku gharama za umeme zinapokuwa ziko juu ina maana uendeshaji wa hizo projects zao unakuwa uko juu na ndiyo tunarudi palepale kwamba ushindani wa soko wazalishaji wa bidhaa watashindwa kuendana na gharama za soko kwa maana ya kwamba ushindani utakuwa ni mkubwa Zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najaribu ku-imagine mfano watu maeneo kama ya institution kama shule, labda hospitali, hoteli hawa watu wanapata wakati mgumu wa ku-run haya maeneo kulingana na kwamba gharama zinakuwa zinapanda na kile kipengele cha kusema sijui kuna tariff one, tariff two kwa matumizi ambayo ni ya kawaida tulitamani Wizara iweze kuliangazia na kuliondoa kwa sababu haiwezekaniki mtu anayetumia umeme eti kisa anatumia umeme mwingi ndiyo apewe gharama kubwa wakati yule anayetumia umeme kidogo anapewa gharama kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika principle ya soko maeneo yote anayetumia kikubwa ndiye anayeongezewa. Kwa hiyo, nilitamani Wizara katika hili waweze kujitafakari na kuangalia namna gani wanatusaidia watanzania tuwe wateja wao wazuri ili tuweze kufanya mambo ambayo yataleta maendeleo kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kupitia hotuba ya Waziri nimefurahi sana kuona mradi wa kusafirisha umeme kutoka Iringa, Mbeya, Tunduma hadi Sumbawanga kwangu nimeona ni faraja kwa sababu hali ya umeme kwenye eneo letu la Mkoa wa Songwe limekuwa ni jambo ambalo wananchi wanalalamika sana. Umeme haupo, umeme unakatika katika mara kwa mara na inapofika Jumamosi wananchi wameshajiandaa…

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge na hasa kuna wengine wananigeuzia na viti kabisa nitafikia mahali nitaanza kutaja makundi ya wazozaji humu ndani itakuwa ni aibu maana yake nawaona nina kioo hapa ambacho kinanionyesha na kutaka kuangalia.

Sasa nikikutaja ni aibu kwa wapiga kura wako lakini pia kanuni hairuhusu kugeuza kiti ukampa mgongo Spika. Kwa hiyo, angalieni huku huku tumuangalie anayechangia. Mheshimiwa Neema Mwandabila endelea. (Makofi)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante nadhani utanilindia muda wangu huo mchache.

Mheshimiwa Spika, nimefarijika kuona huu mradi wa usafirishaji wa umeme unaotoka Iringa kuelekea Sumbawanga ambapo kwa upande wa Tunduma kutakuwa na kituo cha kupozea umeme. Kwangu naiona faraja kwa sababu wananchi ni kitu wanachokisubiria kwa hamu umeme umekuwa ni wa shida sana, na kumekuwa na changamoto ya umeme kukatika kila inapofika Jumamosi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama umeme utakuwa unapozewa Tunduma naamini kabisa zile changamoto zingine zinazokuwa zinatokea zinapelekea umeme kukatika katika zitaweza kupungua, na gharama ya mradi huu ni trilioni 1.4 na nikiangalia kuanzia pesa iliyotengwa hii bilioni moja kwa namna fulani inatupunguza matumaini kwamba utaenda kwa kasi hii japo naamini kabisa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii Pamoja na Katibu Mkuu wako vizuri kuweza kutusaidia, kwa hiyo, nilitamani bajeti iwe angalau inasoma vizuri ili kuweza kututia matumaini kwamba mradi huu utaenda kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sitajitendea haki kama nitashindwa kuongelea suala la joto ardhi sisi kwetu kule Songwe tumebahatika kuwa na eneo ambalo linakiashiria cha joto ardhi eneo la Nanyala Mbozi. Mheshimiwa Waziri aliweza kutembelea eneo lile akaangalia lakini kwenye hii hotuba sijaona akizungumza neno katika eneo hili nilitamani kwa niaba ya wananchi wa Songwe tungependa kusikia kwamba baada ya yeye kutembea pale amekuja na mkakati gani wa kutusaidia kama wana Songwe ile fursa ya kuweza kupata umeme iweze kuwa revealed kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia sisi Songwe pia tuna utajiri wa makaa ya mawe sijaona katika hotuba wakiongelea kitu hiki hata kidogo na tunajua makaa ya mawe ni nishati sasa nashindwa kuelewa kwamba haya makaa ya mawe yanachukuliwa kwa namna gani. Kwa hiyo nilitamani kuona kwamba Wizara kama Wizara imejipangaje kutumia haya makaa ya mawe yaliyopo kwetu kule Ileje katika namna ambayo itakuwa na tija katika uzalishaji wa umeme na nishati zingine.

SPIKA: Ahsante Neema Gerald Mwandabila.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante niseme tu naunga mkono hoja na niwatakie viongozi utekelezaji mwema. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia bajeti hii iliyopo mbele yetu ambayo imewasilishwa ili tuweze kuijadili na kuendelea kuweka mapendekezo yetu ambayo tungependa kuona Serikali inayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa namna ambavyo ina watu makini. Naamini haya tunayoyaongea watayachukulia kwa uzito wake na kwenda kuyafanyia kazi. Kipekee pia niungane na wenzangu kumpongeza Mama yetu, Mheshimiwa Samia. Mimi ni mmoja kati ya watu wanaoamini kwamba mama hajawahi kufeli. Kwa hiyo, nina matumaini makubwa kwamba mama atatuletea mambo mazuri ambayo yataenda kuleta mabadiliko katika Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najivunia kutoka katika Mkoa wa Songwe, mkoa ambao ndiyo unaoongoza kwa ukusanyaji kodi kwa ile mikoa ya ukusanyaji kodi wa kati, Mkoa wa Songwe ndiyo unaongoza. Kwa hiyo, nilitaka nitunze hiyo kumbukumbu vizuri. Kwa hiyo, ninapokuwa nachangia haya nataka kuonyesha kwamba Mkoa wa Songwe ni katika maeneo ambayo Serikali inaweza ikapata fedha nyingi kama wataamua kuufanya mkoa wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya yote, nilitaka kuongea kwamba ujenzi wa dry port kwa Mkoa wa Songwe eneo la Mpemba pale Tunduma ni kitu kisichoepukika. Tunayasema haya tukiwa tunaamini kabisa Kariakoo na Bandari ya Dar es Salaam kumeshakuwa busy sana. Kama Reli ya TAZARA itatumika ipasavyo, ikawezeshwa na dry port ikajengwa Mpemba, niwaambie kabisa, Kariakoo nyingine itaenda kuota pale Tunduma. Pale itakuwa chanzo cha kuweza kutengeneza free market katika eneo la Tunduma. Kwa maana hiyo, uchumi unaoendelea Kariakoo utakuwa umehamia Tunduma. Kwa hiyo, tutakuwa tumeongeza maeneo ambayo yanaipatia Taifa letu kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo la dry port pale Tunduma, napenda pia kuongelea suala la kupunguza msongamano wa magari pale Tunduma. Ni kweli kuna mkakati wa ujenzi wa barabara, lakini ipo haja ya kufanya haraka kuhakikisha barabara ile ya pale Tunduma inayoingia mpakani inatanuliwa ili magari yasipate msongamano wa kuelekea Zambia. Kwa sababu kwa kitendo cha magari kukaa njiani muda mrefu pale, kwa namna moja au nyingine yanaiingizia hasara Taifa kwa maana ya kwamba magari hayavuki mengi kwa wakati ipasavyo; na pia hakuna barabara ya mchepuko endapo barabara ile itapata breakage, hakuna barabara ya kutoa magari yapite njia mbadala yaweze kwenda kuingia boda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo mambo pia naomba kama Wizara yayachukulie kwa u-serious wake na kuyafanyia kazi haraka. Uchumi wa Taifa hili kwa upande wa Tunduma kama kweli patapewa kipaumbele, naamini kabisa Taifa litapata mapato mengi kutoka eneo la Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze kwenye suala la VAT. Sheria ya Ongezeko la Thamani inasema kwamba ili mtu aweze kusajiliwa kuwa Wakala wa kukusanya VAT, awe na mzunguko wa shilingi milioni 100. Ukijaribu kulitazama kwa kina hili jambo linakuwa ni kama ni gumu katika utekelezaji wake kwa wale Maafisa Mapato wanaokuwa wamepewa hii kazi. Unapoongelea mzunguko wa shilingi milioni 100 ni kitu cha kawaida kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kupata mzunguko wa shilingi milioni 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unaposema hiyo shilingi milioni 100, ina maana unawalenga wale watu wanaofanyabiashara ya rejareja. Unaposema ongezeko la thamani, hatuna maana kwamba bidhaa hiyo moja iweze kuongezeka thamani kila inapoenda kwa muuzaji mwingine.

Ushauri wangu ulikuwa ni kwamba, tungependa kuiona Serikali inafanya mabadiliko katika eneo hili. Kutoka shilingi milioni 100, basi iende kufanya kuwe na shilingi milioni 300. Unapomwongelea mfanyabiashara mwenye mzunguko wa shilingi milioni 300, huyu ni stable person ambaye yeye kwa shilingi milioni 300 yake hiyo anakuwa ni supplier wa bidhaa na siyo yule mfanyabiashara wa rejareja. Kwa hiyo, kama kweli Serikali ikiweza kuliona hili na kulifanyia kazi. Ina maana kwamba kwa namna moja Serikali itapunguza mgogoro na wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu kule mpakani tuna mgogoro mkubwa sana kati ya TRA na wafanyabiashara. Wafanyabiashara wengi hao wenye mzunguko wa shilingi milioni 100 wamekuwa wanalazimika kufunga biashara zao kwa sababu tu hawawezi kulipa hilo ongezeko la thamani. Kwa kitendo cha kuwaingiza wao kwenye ongezeko la thamani, ina maana kwamba unawafanya washindwe ku- compete kibiashara katika lile eneo la Tunduma, kwa sababu wapo ni registered wapo ambao ni un-registered. Wale wanaokuwa registered ina maana kwamba sasa wanashindwa kuuza bidhaa zao kwa ile bei ambayo ipo sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo la kuongeza kutoka shilingi milioni 100 hadi kwenda shilingi milioni 300, kinachofanyika ni kwamba, wafanyabiashara wengi pia wanafilisika, kwa sababu kinachokuja kutokea yale malimbikizo inakuwa kama wanapokwa zile fedha zao kiasi kwamba wanakuwa hawezi tena kuendesha biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea suala la ushuru wa forodha wa vitenge. Kuwepo kwetu mpakani tunaendelea kujifunza mengi. Kwa wastani kontena karibu milioni 500 zinapita kuelekea Zambia na Kongo pale katika mpaka wa Tunduma. Mwisho wa siku nikuhakikishie, pakifanyika uchunguzi zile kontena 500 sidhani kama zote zinatumika kwa Zambia au kwa Kongo, zinarudi tena Tanzania. Changamoto iliyopo ni kwamba kodi ya vitenge kwa Tanzania ni asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote ni mashahidi kwamba vitenge vinavyotengenezwa nchini havina quality hiyo ambayo tunataka kuvilinda. Vingekuwa ni vitenge vizuri, ambavyo vina mvuto, naamini kabisa ingekuwa sawa kweli kuweka hiyo kodi ambayo ipo. Mwisho wa siku ukienda Zambia unakuta wao wana kodi ya asilimia 20, ukienda Kongo ni asilimia 25. Unapopitisha kontena la fourty fits kwa Tanzania unalipa zaidi ya shilingi milioni 100, lakini kwa Zambia na Kongo inakuwa ni chini ya shilingi milioni 30. Katika hali ya kawaida gap ya shilingi milioni 70 siyo ya kitoto, ni fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa siku, pale mpakani tuna watumishi 12 tu ambao wana-deal na mpaka Maafisa Kodi, hawawezi kukimbizana na kontena 500 zote hizi kwa mwezi.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mzungumzaji anayezungumza sasa kwamba kupitia hilo ni kweli kabisa na jambo hilo limesababisha wafanyabiashara ambao walikuwa wanafanya biashara Kariakoo ambao walikuwa ni majirani zetu; Zambia, Malawi, Rwanda na Burundi ambao walikuwa wanajaa pale Kariakoo kununua bidhaa hii ya kitenge, sasa hivi hawaji na wafanyabiashara hawa wamehama, wanaenda kwenye nchi hizo hizo kwenda kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ni kweli kabisa hata Kariakoo wamekimbia, kontena moja shilingi milioni 300. (Makofi)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Niseme tu, taarifa yake naipokea na hali halisi ndiyo ilivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema heri nusu shari kuliko shari kamili. Kitendo cha kwamba tunapoteza fedha nyingi kisa tu, kuhakikisha tunalinda viwanda vyetu vya ndani ambavyo havifanyi vizuri, tunakuwa hatujitendei haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niseme, sisi wenyewe ndiyo tunahamasisha magendo; na kwa…

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa. Niko hapa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa kweli niungane na hawa waliopita kuhusiana na masuala ya vitenge. Kweli kuna jambo inabidi tuliangalie vizuri sana. Nasema hivyo kwa sababu hata mimi nililifuatilia na nikalishughulikia suala hilo kwa muda mrefu. Kuna changamoto kubwa na wale akina mama wamekuwa wakilipa kodi ya kutosha. Tunalinda viwanda vya ndani ambavyo na vyenyewe ukivichunguza wanadai kwamba wanaenda kununua huko huko nje, halafu wanarudi wanasema wametengeneza ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliangalie hilo suala kwa umakini kwa faida ya nchi yetu. (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo, Mheshimiwa Neema.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Manyanya. Tunachohitaji ni pesa za kuendesha Taifa letu. Tuangalie namna zote ambazo zinazuia tusipate pesa. Suala la vitenge nimeona kwenye hotuba inasema kwamba wanamwachia Kamishna. Tuwe wakweli, kumwachia Kamishna wa TRA ni kuongeza urasimu na kutengeneza mianya ya rushwa. Kwa maana hiyo, nilitamani hili wakalitafakari na waje na percent, ile asilimia ambayo kweli kama Taifa tutakuwa tunajua hiki tutapata na hiki kitatuongezea kitu kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niseme kabisa magendo kwa nchi hii tusiendelee kuhamasisha kwa kuweka kodi zisizolipika; na pale mpakani nimeshasema watumishi ni 12, sidhani kama wata-deal na sukari, wata-deal na magendo yote yanayopita pale, hawataweza. Otherwise iongezeke timu ya kufanya kazi katika mpaka ule. Ule mpaka ni wa faida, ule mpaka una pesa, ule mpaka unaweza ukalisadia Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nirudi kusema kwamba nina maombi mengine maalum kwa Wizara. Songwe tungependa kuona kilimo cha Alizeti na Ufuta kinapewa kipaumbele. Nimeona wameitaja mikoa mitatu. Taifa hili tunahitaji mafuta, tunahitaji mbegu za mafuta zilimwe kila sehemu. Songwe tumekuwa tunalima mahindi, ndiyo yenyewe hayauziki. Hatuna kilimo ambacho tunaweza tukajivunia kwamba hiki ni kilimo cha biashara. Naomba watuzingatie watu wa Mkoa wa Songwe kwa kuhakikisha zao la alizeti na ufuta linapewa kipaumbele na wananchi wanahamasishwa ili tuweze kuchangia uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuongelea suala la TFS. TFS kuna changamoto kubwa. Wanatoa vibali kwa wananchi vya uvunaji wa mkaa, mvunaji wa mkaa anapata nafasi ya kuweka watu wake wa kumvunia mkaa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia kidogo, samahani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuvuna mkaa vibali vya kutoa mzigo porini watu wautoe kwa wakati havitolewi kitu ambacho wafanyabiashara wengi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, unaweza ukamwandikia Waziri wa Fedha kwa sababu wengine watakosa nafasi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni hii katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka 2023/2024. Niseme tu, kabla sijaendelea nilitamani nitumie nafasi hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuweka ruzuku katika mbolea. Ambako tunaona wakulima wengi sasa hivi wana amani. Pia, niweze kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Waziri Kindamba kwa namna ambavyo amekuwa akiendelea kupambana na wahujumu mbolea ya Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kuona kwenye mitandao kwamba kule Mkoani Songwe kulikuwa na wahujumu uchumi kupitia mbolea, waliokuwa wanatoa mbolea Tanzania kwenda Malawi. Kwa hiyo sasa hivi imebadilika, kwamba mbolea badala ya kutoka Malawi kuja Tanzania sasa hivi inatoka Tanzania Kwenda Malawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nilitaka nijielekeza kwenye kuchangia katika mapendekezo haya ya huu mpango. Kimsingi nitajikita katika maeneo matatu ambayo ni vipaumbele vya mpango huu. Eneo la kwanza, nitaanzia kwenye kuchochea uchumi shindani na shirikishi, ambapo hapa kuna masuala ya usafirishaji, umeme na TEHAMA. Tunafahamu kwamba barabara ya TANZAM imekuwa ni barabara muhimu sana, na barabara hii ndiyo inayosafirisha mizigo mingi kuelekea Nchi za Ukanda wa SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikiongea hapa mara nyingi, lakini kwa awamu hii ninatamani kuomba Wizara ya Fedha iweze kuweka kipaumbele ujenzi wa barabara hususan kwenye eneo la Mlowo-Tunduma. Kama vile walivyotia kipaumbele kwa eneo la Mbeya waweke kwa Tunduma kwa sababu barabara ile inapata jam kubwa sana. Mawaziri ni mashahidi, wamepita kule na wameona, kwamba hali ya pale si nzuri, mizigo mingi inashindwa kufika kwa wakati katika destiny pale mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, nilishaongelea kwamba barabara ile kutoka Mlo kwenda Tunduma hakuna barabara ya mchepuko ambayo kama barabara hii ikapata tatizo lolote kutakuwa na njia mbadala ya kuweza kufika mpakani. Kwa hiyo, niombe kupitia bajeti hii, waweze kuitazama barabara hii kama ilivyo muhimu. Kama wanavyowekeza kwa upande wa Dar es Salaam wangewekeza Tunduma nadhani tungepunguza changamoto nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuongelea na kuipongeza Kamati ambao wameweza kuona umuhimu wa kuendelea na mchakato wa hii Sheria ya TAZARA. Nilikuwa natamani kusisitiza pia wafanye haraka iwezekanavyo ili kuboresha hii sheria ili uwekezaji katika TAZARA uendelee na hivyo uweze kuleta tija katika usafirishaji wa mizigo inayoenda huu Ukanda wa SADC. Kwa hiyo, kwa hili niombe pia kwenye bajeti ijayo waipe kipaumbele TAZARA ili iweze kufanya kazi yake kama ambavyo ilikuwa imetarajiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu ambacho kimekuwepo, na sijajua ni kwa namna gani huu Mpaka wa Tunduma haujapewa kipaumbele. Kama uwekezaji unavyofanyika Dar es Salaam wangeweza kufanya uwekezaji huu Tunduma mimi nina uhakika nchi hii ingeongeza mapato kwa kiwango kikubwa sana. Tunafahamu mizigo mingi inayotoka Dar es Salaam kwa asilimia 70 inapita kuelekea Ukanda wa SADC. Kama tungepajenga Tunduma tukaweka masoko ya Kimataifa pale, tukajenga dry port pale tunaamini kabisa mapato ya nchi hii yangeongezeka; na hata kwenye nchi hizo za Ukanda wa SADC wale wenye mitaji midogo wangeweza kulifikia Soko la Tanzania na kwa namna hiyo tungeweza kupata mapato kutoka kwenye hizo nchi za upande wa SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwaombe Wizara kupitia bajeti hii tunayoielekea, huu mpango wa kuelekea bajeti hii inayokuja, wafanye, ikiwezekana, utafiti kwa Mji wa Tunduma, waangalie ni fursa gani zipo ambazo wanaweza wakazifanya kuhakikisha tunatengeneza fursa za kimapato kwa nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunafahamu pia huu Mpaka wa Tunduma ndio Mpaka wenye changamoto za magendo mengi sana. Magendo mengi yanaenda, bidhaa zinakuwa kama zinaenda Zambia, kama zinaenda Kongo lakini zinapiga u-turn, zikifika Tunduma zikaenda Zambia zinarudi tena Tanzania. Na huu udhibiti wa magendo katika ule mpaka ni kitu ambacho Wizara inatakiwa ikichukulie kwa namna ya kipekee sana. Pale pia kuna deficit ya watumishi, lakini pia mikakati madhubiti ya kuhakikisha kwamba mazingira ya udhibiti wa magendo yanawekwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi si mtaalam wa mambo ya kodi na wala si mtaalamu wa mambo ya udhibiti wa magendo; lakini magendo nayaona yakitoka Zambia yakirudi Tanzania. Kwa hiyo tunafahamu kabisa nchi zile tunazopakana nazo wao wana mazingira ambayo yanawashawishi wafanyabiashara wa Tanzania wakawekeze na kusajiri kampuni kule ili wanapokuwa wanapeleka mizigo kule, inapiga u-turn ionekana kama ilikuwa imeenda Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, niombe sana watumishi pale mpakani waongezwe. Nadhani hii kwenye upande wa mapato ya nchi tutakuwa tunaisaidia nchi kuweza kupata fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nilitamani kuongelea kwa upande wa Tunduma; ni kwamba tumekuwa tunaona kabisa kuna masoko mbali mbali ambayo yanaendelea kujengwa. Kuna Soko la Kakozi ambalo unaona kabisa ni soko la Kimatifa na ni soko zuri. Hata hivyo bado halijakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme tu, Wizara ije na mkakati kabambe au maalum kwa ajili ya ile zone ya Tunduma na Momba kwa ujumla. Nadhani kuna kitu ambacho tutafanya additional katika mapato ya nchi hii. Nitakuwa sijajitendea haki kama sintoongelea hiki kipengele cha kuchochea maendeleo ya watu, kumarisha afya, maji, elimu, upimaji wa ardhi na kuimarisha huduma za maendeleo ya jamii na makundi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuongelea hiki kipengele kwa sababu ni kipengele ambacho huwa kinanigusa sana, hususan ukiangalia na changamoto ambazo zimekuwa zikiendelea. Kama vile ongezeko la magonjwa ya afya ya akili, vifo vya watu kujiua au kuua. Nilitamani kwamba kwenye hiki kipaumbele ambacho kimeandikwa kuchochea maendeleo ya watu kuimarisha afya, maji nakadhalika, hapa kwenye maendeleo ya jamii na makundi maalum, hii makundi maalum ingetamka ustawi wa jamii. Kwa sababu tunafahamu hii Wizara ina kada mbili tu, ina maendeleo ya jamii ina ustawi wa jamii. Ustawi wa jamii ndicho kitu kinachobeba makundi yote haya maalum mengine. Kama kweli nchi inataka kupiga hatua kwenye maendeleo ya watu tuanatakiwa ku-invest kwenye eneo la ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ni nyingi, kada hii ina wataalamu wengi wazuri. Nitumie forum hii pia kumshukuru Rais ameajiri Maafisa Ustawi wa Jamii 139. Tunafahamu mahitaji halisi kwa mwaka uliopita kwenye bajeti iliyopita tulikuwa tunaona ni asilimia 97 ya upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii kwenye maeneo yetu. Hawa ndio watu ambao wanaweza waka-stabilize hali halisi ya kisaikolojia ya wananchi wetu ili waweze kufanya vizuri kwenye uchumi, katika mambo mengine ya kielimu na masuala mengine ya kijamii. Hata kupambana na hivyo vikundi vya mikopo na nini, huwezi ukapambana na kuchukua fedha huku akili yako kisaikolojia haiku vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninaomba Wizara hapa, wanaposema maendeleo ya jamii na makundi maalum, ile makundi maalum iondoke na badala yake waweke ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kitu kingine pia nilitamani kuomba kwenye mpango wa bajeti unaokuja suala la maji, kama walivyotuahidi kwa mji wa Tunduma, tunajua changamoto ya mji wa Tunduma. Ninaitaja sana Tunduma kwa sababu ni mji ambao ni mpakani na ndiyo wageni wengi wa nchi zingine wanapokuja wanafikia Tunduma kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna maji pale na kuna mradi ambao tumeahidiwa wa almost bilioni 17 basi watusaidie uweze kuisha haraka ili hata watu wanapokuja kuwekeza Tunduma wawe na uhakika wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia; na niseme tu ninayofuraha kubwa sana kuanza kuchangia kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kuwa champion namba moja wa masuala ya lishe katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe tu ni wiki mbili zimepita tumeona Mheshimiwa Rais ameenda kuzindua jukwaa la mfumo wa chakula Barani Afrika, Dar es salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu leo utajikita sana kwenye suala la lishe kwa sababu ni kitu ambacho kama taifa tunapitia changamoto kubwa sana. Na kama tunavyoona, hali ya udumavu kwa nchi yetu tuna asilimia 30, kitu ambacho kama taifa tunatakiwa kujitathmini na kuangalia ni jitihada gani za msingi tunazoziweka ili kuhakikisha hali ya lishe nchini inaimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimeongelea suala tu la udumavu kwamba ni asilimia 30, lakini tuna kitu kinaitwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo hayo yanaenda kwa asilimia 45. Kwa hiyo unaweza ukajumlisha asilimia 30 na asilimia 45 unaweza ukaona kwamba ni kwa kiwango gani nchi yetu ina hali mbaya ya lishe. Kwa hiyo naomba tu niweke msisitizo kwamba kama Taifa ipo jitihada ya kufanya kuhakikisha suala la lishe linapewa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea suala la lishe tunaona mikoa inayozalisha chakula ndiyo mikoa ambayo inateseka na hali ya lishe duni. Ukiangalia Mikoa kama ya Iringa, Njombe, Rukwa na mikoa mingine kama Songwe, Morogoro, Mbeya unaona bado hali hali duni ya lishe iko juu. Tunapoongelea udumavu kwenye mikoa yote hii iko juu ya ile cut-off point ya hali ya udumavu kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninazidi kusisitiza tu kwamba kama taifa tuone umuhimu wa kupambana na suala la lishe ili tuweze kuondoa hizo changamoto za utapiamlo. Tunapoongela lishe ndicho kitu kinachogusa kuanzia wakati wa mimba mpaka mtu anakuja anazeeka. Katika suala la lishe tunaangalia kuanzia chakula kinapozalishwa, kinapovunwa shambani, kinavyochakatwa mpaka kinavyokuja kwenye utumiaji ule wa mwisho; lakini pia bila kusahau zile hatua za uchakataji wa hiki chakula ili kiweze kuhifadhika kwa matumizi ya baadaye. Kwa hiyo kuna mambo mengi ambayo kama taifa tunatakiwa tuzingatie kwenye suala la lishe ili tuweze kuwa na Taifa ambalo litakuwa na afya nzuri na litakuwa na tija kwenye mchakato mzima wa maendeleo ya kiuchumi wa taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo langu kubwa katika kuongea haya yote ninayoyaongea ni kwamba mpaka saa hizi Sera ya Lishe ya Taifa inayotumika ni ya mwaka 1992. Ni miaka 30 nyuma tangu hiyo sera ianzishwe mpaka leo sioni jitihada ya Ofisi ya Waziri Mkuu kuja na Sera ya Taifa ya Lishe ambayo itaenda kusaidia kupunguza changamoto zote za masuala ya lishe yanayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona taifa limekuwa linapitia hatua mbalimbali za masuala ya lishe, tunaona kwamba kama Taifa wameweza kuajiri maafisa lishe, walau angalau sasa kila halmashauri ina afisa lishe mmoja, ambao nao si toshelevu. Lakini tunaona kumekuwa na uanzishwaji wa kamati za lishe kwenye halmashauri zetu, na ni kuanzia ngazi ya taifa tumekuwa na nutritiol steering committee pamoja na ngazi ya mkoa na wilaya, na wamekuwa na harakati za kuhakikisha zinaenda mpaka kwenye ngazi ya kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaona kabisa kumekuwa na utengenezaji wa mikakati ya lishe. Tumeona mkakati wa MNAP1, MNAP2 lakini mambo hayo yote yanafanyika kindi ambacho hatuna sera ambayo inaweza ikasimamia haya mambo yote; yaani sera inayoenda na wakati ya kuweza kuyasimamia haya mambo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumeona kabisa Mheshimiwa Rais aliweza kusaini mikataba ya lishe na wakuu wa mikoa; na hii mikataba ya lishe imeenda mpaka ngazi ya chini kabisa kwenye kata, watu wamesaini mikataba ya lishe; lakini inasainiwa kutoka kwenye msimamo upi wa kisera?

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapokuwa nayaona hayo ninazidi kuona umuhimu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuona umuhimu wa kufanya uwepo wa sera ambayo inaenda na wakati ya masuala ya lishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa sera ya lishe ulikuwepo na umeanza tangu 2017 ni miaka mitano zaidi saizi mpaka saizi hatuoni matokeo ya sera ya lishe. Ninapokuwa nayajadili haya natamani kuona Waziri Mkuu atapokuwa ana-wind-up mwishoni atuambie ni wapi ambapo hii sera ya masuala ya lishe imeweza kukwama? Kwa sababu tumeona kumekuwa na uzalishaji wa vyakula saizi tuna vitu vinaitwa GMO.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vitu ambavyo vina-impact kwenye chakula na afya za Watanzania, lakini tunaona kabisa kumekuwa na kemikali mbalimbali ambazo zinaingizwa nchini kwa ajili ya processing za vyakula mbalimbali. Kuna udhibiti gani, lakini tumeona athari ambazo zimetokea pale ambapo TFDA iliweza kuvunjwa ikapelekwa ikapelekwa TBS. Tumeona ni wapi ambapo tumekuwa tukifeli kama Taifa. Kwa hiyo kuna mambo mengi katika masuala ya chakula ambayo yamekuwa yakiendelea ambayo yanahatarisha usalama wa chakula chetu, kitu ambacho kingekuwa na sera nzuri inayoenda na wakati ingekuwa rahisi kwa wasimamizi au waratibu wetu wa masuala ya lishe kuweza kuzingatia vigezo ambavyo viko kwenye hiyo sera. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea suala la chakula ni suala la Kitaifa, lakini ni la Kimataifa na ndio maana utakuta wakati mwingine hata bidhaa zetu zinazuiliwa kwenda Mataifa mengine. Mfano mzuri ni lile suala la mahindi yale yalikuwa yanaenda Kenya, masuala ya sumu kuvu, unaona kabisa usimamizi wa namna ya utunzaji wa vyakula vyetu ina maana hauko smart mpaka mahindi yanazuiliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama tutakuja na sera nzuri, sera ambayo inaenda na wakati, ina maana hata wajasiriamali wetu, wakulima wetu wataweza kuzalisha vyakula vitakavyokuwa na ubora na mwisho wa siku sisi kama Taifa tutakuwa tuna uhakika wa chakula kilichobora, lakini pia sisi kama Taifa tutakuwa na uwezo wa ku-supply vyakula vyenye viwango vya Kimataifa. (Makofi)

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MBUNGE FULANI: Endelea ni kengele ya kwanza.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilifikiri muda umekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu, Ofisi ya Waziri Mkuu ije na kauli ya kusema ni wapi mchakato wa masuala ya Sera ya Lishe umekwamia. Kwa sababu haiwezekani jambo moja miaka mitano linaendelea kutokutekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho ningependa kukiongelea, na-declare interest kwamba mimi ni mkazi wa Mji wa Tunduma na Mji wa Tunduma kama Taifa huwa siku zote naendelea kusisitiza kwamba ni mji wenye tija na ni mji ambao kama Taifa kweli litaamua kuwekeza ni kitu ambacho wanaweza wakapata fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na mipango mingi ambayo inatekelezwa upande wa Dar es Salaam bila kuzingatia destination ya ile mizigo au shughuli zile zinazofanyika Dar es Salaam kwamba zina impact ipi kwa Mji wa Tunduma. Natamani kuona kwamba mipango yao Ofisi ya Waziri Mkuu, sera zao wanazoziunda katika kuhakikisha wanakuza uchumi wa nchi hii, wawe wanafanya kwa kuzingatia na Mji wa Tunduma au Mkoa wa Songwe kwa ujumla; la si hivyo tutakuwa tunawekeza sehemu moja, tunaboresha eneo la Dar es Salaam pekee yake, lakini eneo ambalo mizigo hii inaenda kama Tunduma unakuta halipewi kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu hali ya Tunduma kwa maana kwamba kwa kuweza kusaidia mchakato mzima wa ukuaji wa maendeleo ya nchi hii kwa kulinganisha na Dar es Salaam, haina mazingira mazuri. Naamini kabisa kama kweli asilimia 70, kwa sababu takwimu zilizopo ni asilimia 70 ya mizigo inayotoka Dar es Salaam inapita custom ya Tunduma. Waone jitihada ya kuwekeza kule, nakumbuka ni juzi tu hapa Mheshimiwa Stella alikuwa anauliza suala la dry port, yakajibiwa majibu kirahisirahisi tu. Majibu ambayo hayakuonesha kwamba Serikali inayo dhamira ya kuhakikisha kwamba kwanza inalinda barabara zetu ambazo zinajengwa kwa gharama kubwa, lakini pia kuona umuhimu wa kuongeza soko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kukiwa na dry port Tunduma, wafanyabiashara wa nchi zingine za SADC wanaweza kuona wepesi wa kuja kuchukua mizigo yao pale au kuagiza kupitia bandari yetu kwa sababu huduma inakuwa imesogezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu na niombe kwamba Wizara hii ya masuala ya mipango izingatie pia Mji wa Tunduma katika mipango yake, ahsante. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kuweza kupata nafasi hii jioni hii kuweza kuchangia katika Muswada huu wa Bima ya Afya kwa watu Wote. Kabla sijaenda mbali zaidi natamani kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali ya Dkt. Samia kwa kuona umuhimu wa jambo hili na kuona kulifanya haraka kabla ya uchaguzi wa 2025 haujafika, tuwe tumeweza kuwaangalia watu wetu katika eneo la suala la bima ya afya hii kwa watu wote. Pia, nitumie nafasi hii kukipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa sababu, wakati tunajadili wakati huu wao waliweza kuliona tangu hapo, hata wakaweza kuliweka kwenye ilani yetu pendwa ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli bima hii ya afya ilikuwa na changamoto hata tukawa tunaweza kuirudisha mara nyingi. Ilikuwa iingie tangu mwezi Februari, lakini tunaona Wizara kwa kushirikiana na timu yake wakaenda kupambana kuhakikisha wanafanya marekebisho ya kutosha kulingana na ushauri wa Kamati, lakini na Wabunge wote kadiri ambavyo walikuwa wameshauriwa. Kwa hiyo, tunampongeza Mheshimiwa Ummy na timu yake yote kwa kuweza kufanya jitihada ya makusudi kubadilisha maeneo yote ambayo tulikuwa tunaona yana changamoto hadi kuleta Muswada huu ambao una matumaini kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, mimi kama Mbunge ambaye niko kwenye Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii niseme tu ninayo furaha kubwa sana kuweza kushiriki katika kujadili mjadala huu kwani naona wale watu ambao ni makundi maalum wameweza kupewa kipaumbele na kuangaliwa kwa namna gani watasaidiwa, ili waweze kuwa na uhakika wa kuhudumiwa katika afya zao, hasa pale wanapokuwa wamepata changamoto. Kila mtu anahitaji kuwa na afya njema na tunajua kabisa Taifa lolote linategemea nguvukazi ambayo iko vizuri kiafya. Kwa hiyo, kwa hili naendelea kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kuweza kuyaona makundi haya maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu bima ya afya imekuwepo, kumekuwa na skimu mbalimbali za bima ya afya. Nataka nijikite kwenye ile bima ya afya ya watu ambao tulikuwa tumewalenga watu wengi (ICHF) ambayo ni bima iliyoboreshwa. Tunafahamu bima hii ilikuwa ni nzuri na nia yake ilikuwa ni njema kwa wananchi. Wananchi walipewa dhamana ya kuchangia Sh.30,000 tu lakini tunatambua kwamba, kulikuwa na changamoto kubwa katika kuhakikisha wananchi wanaingia kwenye Mfuko huu wa Bima ya Afya.

Mheshimiwa Spika, kufeli kwa jambo lolote huwa hakutokei hivihivi, nina imani kwamba, Waziri na timu yake wamefanya utafiti wa kutosha kujua ni kwa nini hii bima iliyoboreshwa ilikuwa inawafanya wananchi washindwe kujiunga. Kwa hiyo, zile changamoto ambazo zilikuwepo wataenda kupambana kuhakikisha wananchi wengi wanajiunga, kwa sababu unapoongelea suala la afya, ukiwa mzima huwezi ukaona shida yake, lakini pale ambapo utaumwa, ambapo huwezi kwenda sehemu yoyote kutafuta chochote, ndipo ambapo unaanza kuona umuhimu wa bima ya afya. Kwa hiyo, nimwombe Waziri kwenye hili aweze kuwa na tafiti ya kutosha kuangalia ni namna gani bima ya afya ile nyingine ambayo ilikuwa imelenga kundi kubwa la watu ya CHF ni kwa nini ilikuwa inafeli.

Mheshimiwa Spika, na kiukweli naamini bima hii ya afya kwa watu wote itaenda hata kunusuru ule mgogoro ambao ulikuwepo kati ya watu wa TASAF na Maafisa wetu Maendeleo ya Jamii kwa sababu, walikuwa wanalazimishwa kuingia kwenye bima ya afya kwa kilekile kipato kidogo wanachopewa cha kujikimu maisha yao. Kwa hiyo, naamini kile kiwango cha TASAF wataendelea kukipata, lakini pia watasaidiwa kwa namna nyingine kuweza kupata bima ya afya. Kwa hiyo, hili pia linanipa faraja kuona kwamba, sasa Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii watakuwa katika hali nzuri ya kufanya kazi zao.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu inakuja hapa, Serikali inahitaji fedha kwa ajili ya kuendesha Mfuko huu wa Bima ya Afya kwa watu Wote. Katika kuendesha mfuko huu mimi natamani kabla ya kum-term mtu kwamba, ni maskini, iangalie kila mtu kwa kiwango chake anaweza kuchangia shilingi ngapi kwenye Mfuko huu. Najaribu kusema hivi kwa sababu, natambua makundi ya watu wanapishana; kuna mtu anaweza asiwe na uwezo wa shilingi 10,000 lakini uwezo wa shilingi 5,000 anao, lakini mwingine anaweza asiwe na uwezo wa shilingi 10,000 lakini shilingi 50,000 anayo. Kwa hiyo, natamani kabla ya kumpeleka mtu kwenye hali ya kimaskini waangalie je, huyu mtu anaweza kupata angalau hata shilingi 5,000 hata shilingi 10,000 ili tu awe sehemu ya kuchangia Mfuko wetu wa Bima ya Afya. Niseme tu kwa kufanya hivyo itakuwa chanzo cha mapato cha Mfuko huu kimeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe angalizo moja kwa maana ya kwamba, lengo la bima ya afya sio kumwongezea mzigo mwananchi. Yeyote anayechangia si kwa maana yeye anakuwa na fedha nyingi kiasi kwamba, hana majukumu mengine. Nataka kuongelea kundi la watumishi na wale wote ambao watakuwa wamepewa dhamana ya kuchangia ambao wako kwenye mifumo isiyo rasmi wana uwezo wa kuchangia. wanapokuwa na watoto ambao wako shuleni, tumeona hapa umri ambao umetajwa ni miaka 21, lakini uhalisia ni kwamba, kuna watoto wa vyuo vikuu ambao ni wa wazazi ambao ni watumishi, wanaenda chuoni zaidi ya umri huo, unakuta mtu anamaliza chuo ana miaka 25.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kwenye hii bima iweze kueleza au watakapotunga kanuni zao waweze kueleza wazi kwamba, mtoto yeyote ambaye anaendelea kuwa kwenye mahitaji au ulezi wa mzazi wake asiweze kuingizwa kwenye kundi la kujilipia bima ya afya. Nasema hivi kwa sababu, tunaona watoto wanaenda vyuoni, kunakuwa na hela ambayo inachangiwa kama bima chuoni, wakati huo huo mzazi huku anaendelea kulipa na ile hela haitatoka kwenye mfuko mwingine zaidi ya mzazi yuleyule. Kwa hiyo, unakuta huku mzazi amejiandikisha yeye labda na mume wake tu, lakini anaenda kutoa fedha nyingine kwenda kuchangia kwenye Mfuko wa Bima ya Afya kwa ajili ya watoto wake ambao bado wanamtegemea ambao wako chuoni.

Mheshimiwa Spika, kwa hili wakiweza kutuangalia kwa namna moja au nyingine, watakuwa wamepunguza machungu ya Watanzania ambao wana mzigo mkubwa wa kuendesha maisha na kimsingi maisha kwa sasa hivi yamekuwa ni magumu sana na kila mmoja wetu hapa analifahamu hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ambacho ningependa kuongelea katika Muswada huu, kumekuwa na mpango wa kuwahudumia wazee, ambao ndio lile lile kundi la wenye uhitaji, kiukweli huduma kwa wazee hazikuwa nzuri kwa kiwango hicho. Hazikuwa nzuri kwa kiwango hicho kwa sababu, kwanza hata maeneo waliyokuwa wanapewa huduma kulikuwa na hali fulani ya unyanyapaa.

Mheshimiwa Spika, sasa basi tunajua bima zinazoenda kutengenezwa zitakuwa na kiwango fulani cha huduma. Magonjwa makubwa yanapokuja, mfano magonjwa ambayo mtu labda anatakiwa kwenda hospitali kubwa kama Muhimbili, huko Mloganzila, sijui Jakaya Heart Institute kwa hiyo, unakuta kwamba, wazee wengi hawatakuwa na uwezo wa kwenda huko na ni wazee wetu tunawapenda, tungependa waendelee kuishi na hawana uwezo. Nafahamu sio wazee wote ambao hawana uwezo, lakini wapo ambao specifically ni kweli hawana uwezo, wangeangaliwa au wangetengewa namna ya kuweza kusaidiwa mpaka huduma ya mwisho kabisa kwa sababu, tunapoongelea huduma ya bima ya afya kwa watu wote lengo ni kuweza kum-cover mtu katika hali zote.

Mheshimiwa Spika, najua kwamba, wana utaratibu mzuri wa kuweza ku-screen watu kutenganisha kwamba, huyu anaweza akahudumiwa kwenye level gani, huyu level gani na vitu kama hivyo. Kwa hiyo, kama wataweza kujiongeza na kufanya katika maeneo hayo, kweli, Watanzania wengi wataweza kupona na afya zao zitakuwa nzuri.

Mheshimiwa Spika, pia hata wale wote watakaokuwa wamepewa zile bima za bure; sidhani kwamba, lengo lao ni kwamba, wakiumwa kichwa au wakaumwa tumbo ndio waweze kuhudumiwa, lakini watakapoumwa yale magonjwa magumu ambayo mtu hana chochote basi waangalie namna ya kuweza kuwasaidia. Natambua kumekuwa na utaratibu wa kutoa misamaha kupitia ofisi mbalimbali za Maafisa Ustawi wa Jamii, lakini kumpa Afisa Ustawi wa Jamii uwezo wa kutoa misamaha, wakati mwingine wamekuwa wakitoa misamaha fake, kitu ambacho kinakuwa kinaendelea kuipa Wizara mzigo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama watakuwa wanatengeneza kanuni zao, waangalie namna ya mambo yote haya watayawekaje ili kuweza kulisaidia Taifa letu. tunajisikia vibaya kuona kwamba, mfuko wetu huu wa bima ya afya ya Taifa unatumia fedha nyingi wakati mwingine kwa hali za kisanii tu, inakuwa sio sawa. Kwa hiyo, kama watatengeneza udhibiti mzuri, naamini mambo mengi yataenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, niweze kusema nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kidogo katika wizara hii nyeti, lakini pia niseme kwamba nina imani na wizara hii kwa sababu ina viongozi makini ambao wamekuwa wakiendelea kufanya kazi vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo machache ambayo ningependa kuongelea kupitia wizara hiikwa maana ya kukjenga ili tuweze kuona tunaelekea wapi katika kuboresha kilimo nchi hii, nilikuwa napitia taarifa tuliyopewa hotuba ya Waziri kuna mambo baadhi niliweza kuyaona yakanipa shaka kwamba hivi tunakoenda tutafanikiwa kweli au tataendelea kupiga mark time.

Mheshimiwa Spika, niliona suala la takwimu wakakiri wazi kwamba hakuna takwimu zinazoonyesha mahitaji ya mbegu nchini, wakulima wapo tunawafahamu na tunajua kabisa maeneo gani wanalima nini na maeneo gani wanalima kilimo gani, watusaidie kupata hizi takwimu ili wanapokuja kama ni suala la mbolea tujea wanatuletea mbolea kiasi gani ambazo zinahitajika na watanzania. Lakini kama ni suala la mbegu wajue kwamba ni kiasi gani cha mbegu kinachohitajika Tanzania ili tuweze kuwa na uhakika wa hizo mbegu.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujikita kwenye suala la uzalishaji wa mbegu nchini hapa Tanzania tunamekuwa na baadhi ya makampuni private ambayo yamekuwa yakiendelea kuzalisha mbegu, lakini tuna shirika pia la kiserikali ambalo limekuwa likiendelea kuzalisha mbegu. Hatujapata takwimu kujua kwamba ni makampuni mangapi Tanzania mpaka sasa yanazalisha mbegu.

Mheshimiwa Spika, naamini kama wizara itajikita kwenye kuwawezesha wazalishaji wa mbegu, hizi tunazohitaji nchini nchi yetu itaweza kufanya vizuri, ndipo ambapo tunaweza kuona kwamba kilimo kinageuka kuwa ni fursa ya kiuchumi kwa maana kwamba tutaweza kuzalisha mbegu nyingi na tutaweza kuuza nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa niliyo nayo mpaka sasa Tanzania tuna kampuni moja tu ambayo inauza mbegu nje ya nchi na nimesikia kwamba uwa wanauza Rwanda. Lakini changamoto ambayo wanayo haya makampuni ya mbegu mojawapo imekuwa ni kwamba hawajapata support ya kutosha kutoka Serikalini na wao kama wao wangependa kuona kwamba Serikali inaitambua hii sekta na kuipa kipaumbele hili waweze kufanya vizuri katika uzalishaji wa mbegu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kiufupi ni kwamba tume- experience kwa nyakati tofauti kumekuwa na uhaba wa mbegu mfano kwetu sisi Songwe tumekuwa tukiona kabisa wazi mbegu wakulima wanachukuwa Zambia wanakuja kupanda Tanzania kwa upande fulani inakuwa ni Illegal business lakini ndio inayowasaidia kama Tanzania tukijipanga vizuri kwenye mbegu naamini tutaweza kufanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, makampuni haya yanatamani kungekuwa na uwezeshaji kwa namna ya kwamba kuwe angalau na grants hizi ruzuku lakini pia kufanyike uwezekano kwa mabenki ambayo yanatoa mkopo kwa riba nafuu ili yaweze kuijenga vizuri. Kwa mwaka 2014/2015/2016 tunafahamu sote, haya makampuni ya mbegu yalipewa kazi ya kugawa mbegu kwa mawakala kwa njia ya ruzuku na tunachofahamu mpaka sasa makampuni haya mengi hayajalipwa pesa zao.

Mheshimiwa Spika, na kwa maana hii kwa kutokulipa pesa hizi kwa wakati Serikali kwa makampuni haya yanashusha uwezo wamakampuni haya kuweza kujiendesha na mengine yamefilisika yamekufa. Kwa hiyo, nilitamani sana kusikia kauli ya Serikali kuona kuwa watalipa lini fedha zao ili makampuni haya kama yanakosa ruzuku kama wanakosa mikopo basi pesa zao wapewe ili waweze kuzalisha kwa upana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kusema hayo pia nimepitia eneo la uzalishaji wa mbolea nikaona kwamba mahitaji ya mbolea Serikalini tumeweza kufanikisha kuyafikia kwa asilimia 94.4, ni kiwango kizuri wizara imejitahidi lakini katika eneo hili kuna baadhi ya mambo niliweza kuona kama ni changamoto.

Kwanza niliambiwa kwamba mbolea ambayo inazalishwa nchini ni tani 32239 nikajaribu kutafuta percent kwa kujua mbolea iliyopo nchi iliyozalishwa ndani ni ngapi nikapata ni asilimia 4.75 kitu ambacho nikaona kama uzalishaji wa ndani ni mdogo hivi mbona ni shida.

Mheshimiwa Spika, na sisi tunakiwanda chetu cha Mijingu…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Neema.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niungane na wenzangu kukupongeza, kwa mara ya kwanza unatuongoza vema. Tunaamini tumepata Mwenyekiti sahihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhaba wa muda nitaweza kuongelea mambo machache ambayo naamini Wizara ikiyafanyia kazi watakuwa wametunusuru sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe, hususan Wilaya ya Songwe yenyewe.

Mimi napenda kusema kwamba nilitamani sana niwapongeze watendaji wa Wizara hii kwamba wanafanya kazi vizuri, lakini nikikumbuka machungu ambayo tunayapata na watendaji wao wa chini kule, roho inakuwa inaniuma kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hii ndiyo Wizara pekee ambayo haina mahusiano mema nasi wananchi. Kimsingi tumekuwa tunalianao kila eneo. Tunaona kabisa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri ni watu wema, tunawaza ni kwa nini watu wao kule chini wanakuwa na roho za kiukatili namna hii kiasi kwamba inakuwa kama wao Kanisani hawakujui? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea suala la wavuvi ambao wanavua katika Ziwa Rukwa. Tunajua uvuvi ni kazi kama kazi nyingine na wale wavuvi wanafanya kazi zile kuweza kujipatia kipato ku-sustain maisha yao na watoto wao na ndugu zao wa karibu; lakini mambo yanayotendeka katika Hifadhi ya Katavi ni mambo magumu ambayo yanasikitisha. Wavuvi wananyanyaswa sana. Sidhani kama taarifa hizi zingekuwa zinafika kwao viongozi wetu; Waziri na Naibu Waziri kama haya mambo yangekuwa yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa kutoka kwa wavuvi ambao wanapatikana katika kambi za Kichangani, Malangali, Kasimanyenze, Kambang’ombe na nyinginezo, kule kuna kambi nyingi, wavuvi wale wanalalamika kwamba, ma-game, sasa sijaelewa ma-game na uvuvi kwa nini wanawaingilia wavuvi kwenye kazi zao eti kisa tu hifadhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ma-game wanaolinda hifadhi ya Katavi wamejitengenezea mazingira ya kujipatia kipato kisicho halali. Wamekuwa ni watu ambao wanawatishia wavuvi kwamba wakiwakuta kando kando ya ziwa wanaendelea na shughuli zao, wanawatishia na kuweza kuwapora mali zao. Pia wamejitengenezea utaratibu wa kupata rushwa. Watu hawa wamejitengenezea utaratibu wa kupata shilingi 300,000 kila wiki kwa kigezo tu kwamba, wavuvi wanaofanya kazi kule, hawatakiwi kukanyaga ardhi ya hifadhi. Mwisho wa siku tunajiuliza kwamba, ile hifadhi imewekwa kwa ajili ya kututesa au imewekwa kwa ajili ya kutusaidia kama Taifa tuweze kupata kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kisichoweza kuongeleka. imi naamini kabisa Wizara inaweza ikatafuta namna ya ku-compromise na wavuvi ili mwisho wa siku Serikali ipate pesa yake. Badala ya hizi shilingi 300,000 kuendelea kuingia mifukoni mwa watu. Serikali ingeweza kutoa vibali halali, kama inavyotoa vya watu kuwinda na kadhalika; wavuvi wanapovua samaki wao waweze kuwaanika kandokando ya ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wavuvi wamekuwa wakiendelea kupata tabu hii. Pale wanapoonekana hawana pesa ya kuwapa, wanachomewa vitu vyao; wavuvi wanachomewa mitumbwi, wavuvi haohao wanachomewa ngalawa, lakini chumvi zao zinaloanishwa. Pia hata samaki wale ambao wameshakauka wanachomwa moto. Sasa hebu jiulize, mtu kawekeza pesa yake, ni mtaji, ndio inamfanya afanye maisha, vinachomwa halafu anaishije? Anaenda kuanza vipi maisha upya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mambo haya ambayo yanakuwa yanaendelea, kwa sisi wanawake tunajua kabisa, imeshaelezwa hapa, ndio wanaofanya mazoezi ya kubaka wanawake. Sasa najiuliza kwamba, kuwa mwanamke ni kosa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba, kwa kweli sina amani na askari hawa. Napenda kuona kwamba Serikali inakuja na tamko au na neno ambalo kwa kweli litatufariji kuona kwamba wako kwa ajili yetu na siyo kwa ajili ya wanyama tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuunga mkono.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika Azimio la Bunge kuridhia Itifaki ya Bunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba hili jambo ni jema kwa maslahi ya Taifa letu na tunaamini sisi kama Watanzania tunakwenda kunufaika. Niwapongeze Wizara kwa kuliona hili na kulileta kwetu ili tuweze kulijadili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa niongelee sana kwenye Sera ya Chakula na Lishe. Unapoongelea chakula na lishe, ndipo ambapo utaona kwamba mimea, wanyama na usalama wa chakula unapoenda kuangukia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Chakula tunayoitumia mpaka sasa ni ya mwaka 1992. Kiuhalisia tunaona ni Sera ambayo imepitwa na wakati na inahitajika kufanyiwa marekebisho ili kuendana na wakati na mahitaji ya leo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuhakikisha hali ya lishe ya Watanzania inaendelea kuwa vizuri. TFNC walianza zoezi la mapitioa ya Sera ya Lishe mwaka 2015/2016 na kimsingi mwaka 2017 waliweza kutoa Waraka ambao waliuwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri ambao sekretarieti na Bunge zilipitia zikaona ipo haja ya kuwa na Sera ya Chakula na Lishe. Mpaka sasa hivi Sera ya Chakula na Lishe bado haijapitishwa kwa marekebisho ambayo yalikuwa yamefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, na tunachofahamu mpaka sasa hivi kama Taifa tunazo Kamati za Lishe ambazo zimekuwa zikiendelea kufanya kazi na Kamati ya Lishe hii ni mtambuka. Hapa najaribu kuonesha ni kwa nini tunahitaji Sera ya Chakula na Lishe. Unapoongelea lishe ni kitu mtambuka kinagusa idara nyingi. Kitu ambacho huwezi ukaongelea usalama wa chakula peke yake bila kuiweka kwenye Sera ya Chakula na Lishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilitamani tunapokuwa tunaenda kukimbizana na hili Azimio tukumbuke kwamba katika nchi yetu kuna baadhi ya mambo ambayo hayajakaa vizuri ikiwamo na Sera ya Chakula na Lishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi, tunafahamu kwamba usalama wa chakula umekuwa ukiathiri lishe za wananchi wetu na masuala ya usalama wa chakula yanagusa mambo ya kuanzia ngazi ya uzalishaji kwenye kilimo kwa maana unapolima lakini pale unapoenda kwenye usindikaji wa hivi vyakula lakini pia utakuta wakati wa transportation, usafirishaji wa haya mazao na hawa wanyama na pia katika eneo la matumizi yaani uhifadhi wa hivi vyakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninapokuwa nasema haya, nilitamani wasizingatie suala moja tu la sumu kuvu, wakumbuke kwamba kuna maeneo mengine ambayo mfano kuna maeneo ambayo yanakuwa na heavy metals mfano maeneo yenye zebaki. Kwa hiyo, tunapokuwa tunatengeneza maabara zetu zizingatie vitu vyote ambavyo vitakuwa na athari ya vyakula vinavyoingia nchini mwetu lakini hata vyakula ambavyo sisi tunatakiwa tuvitoe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu waliosema ipo haja ya kuwa na maabara za kisasa kwa maana ya kwamba wananchi wetu wasipate hasara ya kusafirisha mizigo ambayo inaenda kukataliwa baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu ninaiomba Serikali kupitia kikao hiki iweze kuona haja ya kuanzisha chakula na hata wanapoileta hiyo Sera ya Chakula, kwa miaka hii ambayo imekaa naona ipo bado haja ya kufanya amendment tena kwa sababu kuna mabadiliko ambayo yametokea hapa kati ndani ya miaka mitatu/minne hii ambayo yatakuwa hayamo mle kwenye ile sera. Kwa hiyo, badala ya kuendelea pale walipokuwa wameishia, wairudishe nyuma kidogo, hivi vitu vidogo vidogo viweze kuwa amended ili iendelee na mchakato, ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Nitajikita kwenye mambo mawili, sana sana katika suala la ustawi wa jamii na suala la pili litakuwa kuhusu dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa huu mwezi wa kwanza tumekuwa tukishuhudia matukio mbalimbali ya watu kufanya mauaji kwa watoto wadogo, wanandoa na watu mbalimbali katika familia. Tunafahamu chanzo cha mauaji hayo na kwa taarifa zilizopo mengi yametokana na masuala ya mahusiano, migogoro ya ndoa, uchawi pamoja na mirathi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukianza kuangalia masuala haya kwa jicho la kawaida unaweza ukalichukulia hili kama ni suala dogo sana, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo wimbi hili litakavyokuwa linaendelea kuongezeka kukua kwa watu tofauti fofauti na mikoa tofauti tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini, najaribu kuonesha role ya watu wa ustawi wa jamii ilivyo muhimu kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii ambayo ameitofautisha na Wizara ya Afya. Hapa nadhani ndipo roles za hawa watu wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii zitakavyoanza kutofautishwa kwa uzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wa ustawi wa jamii ni watu muhimu sana katika kufanya counselling kwa ajili ya ku-restore psychological status ya watu katika jamii zetu. Hata hivyo, unakuta watu hawa katika jamii hawatambuliki na hawapewi kipaumbele na hata bajeti yao ipo chini. Kwa hiyo kupitia taarifa hii ya Kamati ya Huduma ya Jamii nilitamani walichukue hili na kuweza kulifanyia utafiti vizuri au kulipa kipaumbele kwa namna tofauti ili watu hawa ajira zao ziongezwe, hata ikiwezekana wafikie angalau kwenye level ya kata ili wawe na uwezo wa kubainisha haya mambo yanayoendelea kwenye jamii haraka kabla mauaji hayajatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuongelea suala la dawa za kulevya. Kama tulivyosikia kwenye taarifa, kwamba changamoto ya dawa za kulevya katika nchi yetu bado ni kubwa na hususan kwa watu wanaotoka mipakani suala hili limekuwa ni gumu zaidi kwa sababu vijana wengi wanaathirika na dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kuwa kuna ongezeko, japokuwa taarifa hazijawa bayana katika taarifa ya Kamati, lakini niseme tu kuwa ongezeko la dawa za kulevya ni kubwa na warahibu hawa wana athari nyingi kwenye jamii. Tumeanzisha clinic mbalimbali katika maeneo mbalimbali ambapo warahibu hawa wamekuwa wakiendelea kupewa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja, unakuta mrahibu yuko kwenye methadone clinic lakini unakuta askari bado wanaendelea kumbughudhi na wakati huo huo wakimkamata na wakimpeleka Central Police wanamkatisha hii dozi ya methadone. Kwa hiyo natamani kwamba hili liweze kupewa kipaumbele, kwamba mrahibu anapokamatwa apewe fursa ya kwenda kupata huduma hii ya methadone kwenye zile clinic ili asiweze kukatisha ile dose yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi methadone clinics hakuna huduma za lishe. Tunafahamu kabisa kuwa mtu ambaye anatumia dawa za kulevya anakuwa katika mazingira hatarishi ya kuwa na lishe duni. Anaweza akawa na overweight au akawa na underweight, kitu ambacho tunajua kabisa, kwamba uwezo na ufanisi wake wa recovery mwilini unakuwa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natamani kuona kwamba katika vituo hivi suala la lishe linapewa kipaumbele ili hawa wanapoendelea na matibabu wapone haraka, kama lishe itakuwa vizuri wataweza kupona haraka.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba dakika moja tu.

MWENYEKITI: Haya, nakuongezea dakika moja Mheshimiwa Neema, malizia.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hawa watu wakishapewa matibabu wanashindwa kurudi kwenye jamii kwa sababu wanakuwa hawana kazi.

Kwa hiyo kama tunaweza kutenga asilimia mbili za mikopo kwa walemavu, asilimia kwa vijana na wanawake, basi kungekuwa na hili kundi pia lipewe kipaumbele kwenye jamii kama sehemu ya kukopeshwa fedha ili waweze kuingia kwenye jamii wakiwa na kipato. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu. Niipongeze Ofisi ya Waziri Mkuu na wataalam wake wote na mawaziri wote na viongozi wote ambao wako katika Wizara hii ambayo imekuwa ikiendelea kufanya kazi pamoja na Waziri Mkuu. Na niseme tu tunafarijika na namna wanavyokuwa wakiendelea kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kutoa hoja ambayo nimedhamiria sana kuna mambo ambayo nilitamani niyabainishe, ambayo ningetamani Ofisi hii ya Waziri Mkuu waweze kuona na kuyapa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kuhusu masuala ya utekelezaji wa miradi. Kumekuwa na uibuaji wa miradi mingi ambayo imekuwa ikiendelea kutelezeka, lakini mingi unakuta miradi imedolola na imekaa muda mrefu bila kumalizika. Nitatoa mfano wa mradi mmoja ambao tulipitia, Mradi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbalali ambao ulianza tangu 2011 na mpaka leo haujaisha. Nilitamani Ofisi ya Waziri Mkuu wawe na mkakati wa kuwa na timeframe kwa kila mradi unaoanzishwa, kwamba ndani ya muda fulani mradi huu unakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kitu kingine ambacho nimekiona na ningetamani kukichangia hapa ni katika masuala ya ardhi. Kumekuwa na tabia ya watu kubadilisha matumizi ya ardhi bila utaratibu, na unakuta Serikali inapoteza mapato mengi katika maeneo haya. Unakuta mtu aliomba kibali cha kupata eneo kama makazi badaye anakwenda kufanya biashara na wakati huo huo yeye anakuwa anaingiza pesa nyingi Serikali aipati chochote. Kwa hiyo, nilitamani pia Ofisi ya Waziri Mkuu iliangalie hili pia na kufanyia mkakati maalumu, badala ya kuendelea kutenga maeneo na kupima mapya kila siku na kugawa kuwe na uhakiki wa maeneo yalishatolewa na sisi kama taifa tuweze kunufaika kwa ubadilishaji wa maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu maeneo mengi ya miji yamechangamka lakini ukienda kuhakiki unaweza ukakuta either pale mjini hawana hati na yale maeneo hayajapimwa; lakini unakuta wao wanaendelea kufaidika na Serikali haipati kitu chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nilitamani kuongelea ni suala la TAZARA. Tunafahamu upo ukakasi katika suala la TAZARA, lakini tufahamu kabisa TAZARA ni uchumi wa Nyanda za Juu Kusini. Watusaidie hiyo sheria ambayo haifanyiwi marekebisho kwa kushirikiana na wenzetu wa upande wa Zambia walichukuwe kwa haraka. Katika hotuba hii sijaona kitu chochote kinachozungumziwa kuhusu TAZARA. TAZARA ni muhimu, TAZARA bado iko vizuri, lakini inachakaa na miundombinu inachakaa kwa sababu tu hakuna uangalizi mzuri kutokana na hiyo sheria wanayosema ina ukakasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirudi kwenye hoja halisi ambayo nilitamani kuizungumzia leo. Tunafahamu kabisa nchini hapa kuna janga la madawa ya kulevya. Tunapoongelea madawa ya kulevya mimi awali nilikuwa naona ni kitu cha kawaida sana; lakini kuna siku wabobezi wenyewe wa masuala ya madawa ya kulevya walinifafanulia, na hivyo niliona ipo haja kama taifa kuingia kwenye mapambano dhabiti ya kuahakikisha madawa ya kulevya kwetu inakuwa ni kitu cha kusimuliwa, kwamba yasiwepo kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapoongelea madawa ya kulevya unaongelea kuhusu nguvu kazi ya taifa ambapo vijana wengi wanaharibika na wanakuwa hawawezi kufanya kazi yoyote ya kulijenga taifa kwa kujipatia kipato chao wenyewe. Lakini pia tunaliongelea maadili ya taifa. Tunafahamu vijana wengi wanaotumia madawa ya kulevya ni watu ambao hawajali lolote na maadiliyao yanakuwa mabovu, wanakuwa vibaka, wengine ndiyo wanajiuza wengine unakuta ndio hao wanaoingia kwenye vitendo vya ushoga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa upande wa Serikali tunakuwa tunapoteza pesa nyingi kwa kununua hizi dawa, na taifa linapoteza fedha kwa biashara hii haramu. Sasa, kiuchumi hili linasababisha tunaendelea kushuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kusema nini; tunajua kabisa program mbalimbali za dawa za kulevya zimekuwa zikiendelea chini ya Kamishna Jenerali wetu Kusaya na wataalamu wake. Hata hivyo, bado ziko changamoto za msingi ambazo kama taifa tunatakiwa tuwape support Ofisi ya Mamlaka Dawa za Kulevya ili iweze kufanya kazi vizuri. Tunafahamu kabisa pesa inayotolewa ni ndogo, lakini pia kuna kitu ambacho kimesahaulika. Wanabainika watu wa dawa za kulevya lakini hakuna linkage na TAMISEMI ambao ndiyo iliyo karibu sana na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninataka kusema nini, kuna kundi la watu wa ustawi wa jamii ambao ndio wanao-deal na watu wote wenye changamoto za kijamii ikiwa ni pamoja na hawa wa dawa za kulevya. Kule chini hatuna watu ambao wanasimamia. Yaani katika TAMISEMI ukienda kufuata structure ile huwezi ukamkuta mtu ambaye yuko maalum kwa ajili ya kusimamia masuala ya kulevya katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii sasa inavyokuwa hapa unaona kwamba, mamlaka inapambana kwa namna yake lakini TAMISEMI yenye watu haina habari na hiki kitu. Kwa hiyo niseme tu mimi kwamba, ofisi hii ya mamlaka itengenezewe utaratibu wa kuwa linked na TAMISEMI ili waweze kuwahudumia na kuwabaini hawa watu kwa wepesi kuanzia kwenye ngazi za vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kutoa hizo pesa kwa ajili ya upambanaji wa uingizaji na matumizi na kupunguza madhara ya dawa za kulevya kuna kitu ambacho kimesahaulika. Kwamba, tukumbuke wale watu wanaotumia dawa za kulevya jamii imeshawatenga; ni watu wasiokubalika katika jamii. tunafanya nini kama Serikali kuwaaminisha hawa watu tumewatibu katika vituo vyetu vya matibabu ya dawa za kulevya ili waweze kurudi kwenye jamii na kupokelewa na kuweza kushiriki katika shughuli za maendeleo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme, kwamba ipo haja kupitia Ofisi ya Kamishna kutenga fungu maalum la fedha ambalo litasaidia katika kuwajengea uwezo au kuwapa mitaji hawa vijana. Na itengenezeke sera ambayo itaonesha kwamba hawa vijana, sasa baada ya kuacha madawa ya kulevya waingine katika utendaji kazi, hata wakawa wanarudishwa mmoja mmoja kwenye ofisi, kwa wale ambao wamesoma. Hii itasaidia kuepukana na changamoto hii. La sivyo tutakuwa tunawatibu lakini wanaendelea kurudi kwenye matumizi ya dawa kwa sababu watakuwa wanakosa support ya kijamii, kiserikali katika kuacha kabisa haya masuala ya dawa za kulevya. Tutakuwa tunafanya kazi ya kuwatibu, wanarudia, kitu ambacho siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuweza kunipa nafasi ya kuchangia juu ya taarifa hizi ambazo zimewasilishwa hapa hususani katika huduma za jamii, pamoja na maendeleo ya jamii.

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais na Wizara ya Afya, lakini pamoja na Wizara ya Elimu kwa namna ambavyo wameweza kujenga miundombinu mingi sana katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu karibu katika kila jimbo kuna majengo ya zahanati, vituo vya afya pamoja na madarasa mengi ambayo mpaka sasa hizi mengine yanakuwa yanakosa watoto. Kwa hiyo kwa hili nampongeza Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia Mheshimiwa Rais ameendelea kupambana na haya masuala ya vitendo vya ukatili kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii. Tunaona ni kwa namna gani ambavyo Mheshimiwa Waziri wetu Gwajima amekuwa akiendelea kupambana kupitia hii SMAUJATA na nini kuhakikisha zile kesi za watoto na akina mama wanaofanyiwa kule kama wale watu wa maeneo husika wanashindwa kuzingatia utaratibu wa kuzifikisha kesi mahakamni, yeye mwenyewe amekuwa akiingilia kati. Kwa hiyo, mimi niseme tu nawapongeza kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mjadala wangu leo mimi ninapenda nijielekeze kwenye hali ya ufaulu nchini. Tunafahamu kabisa mwaka huu hali ya ufaulu nchini imekuwa ya kusikitisha sana na kimsingi ni hali ambayo kama Taifa tunatakiwa tujitafakari na tuone ni nini kinatakiwa kufanyika kuona Watoto wetu wa Kitanzania wanapata elimu iliyo bora, elimu ambayo itakuwa na tija na kubadilisha maisha ya Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kauli ambayo ipo inasema collapse of education is a collapse of the nation (anguko la elimu ni anguko la Taifa). Natamani tulichukue hili katika hali ya uhalisia kabisa kwamba elimu hii isipopewa kipaumbele katika nchi yetu tutaendelea kuwa na taifa ambalo lina watu wasiokuwa na weledi wa kutosha kukabiliana na changamoto za maisha ambazo zinakuwa zinatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuaona masomo ya sayansi watoto wetu wame-fail sana na masomo ya sayansi ndiyo masomo mengi yanayoweza kumwezesha mtoto kuweza kujiajiri katika sekta mbalimbali. Mtu aliyesoma maabara ni rahisi kwenda kufungua kituo chake cha maabara na kufanya ile tasnia yake pale kwa kuwasaidia Watanzania na tasnia zinginezo.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni nini? Ninatamani kuona Serikali yetu hii ya Chama cha Mapinduzi inachukua hatua kubwa sana kuhakikisha kuwa lililotokea mwaka huu, mwakani halitokei.

Mheshimiwa Spika, ninaumia sana kwa sababu nina uzoefu wa namna ambavyo watoto mbalimbali au wazazi mbalimbali wamekuwa wakifanya jitihada ya kuhakikisha watoto wao waweze kufanya vizuri kwenye masomo. Kuna watoto ambao wanasoma katika private schools (shule za binafsi), watoto hawa mimi niseme tu kwa nafsi yangu naamini ndio waliotubeba kwenye matokeo haya ya mwaka huu. Wengi ndio walikuwa na nafasi ya kuweza kufundishwa na walimu kwa kutosha, lakini pia kwa kuwa na walimu wenye uangalizi na msisitizo wa ukaribu wa kuhakikisha wafanye vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninawapongeza sekta binafsi hii ya elimu kwa namna ambavyo wametubeba angalau kwa hizi asilimia ambazo tunakuwa tunaona kwamba tuna watoto waliofaulu kama Taifa wanatusaidia.

Mheshimiwa Spika, mimi nina-grade kwa namna nyingine kwamba wapo watoto ambao walikuwa wanasoma kwenye shule za Serikali ambao wazazi wao walijitoa kwa kuwatafutia walimu binafsi na tuition, ndio ambao wameweza kutubeba na kutufikisha Taifa kama hapo. Kwa hiyo pia niwapongeze wazazi ambao wamekuwa na wito wa kusimamia elimu ya watoto wao bila kuwaachia walimu peke yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuja kulitazama kundi la tatu la wale Watanzania ambao hawana wazazi wenye kipato kikubwa cha kwenda private, lakini hawana wazazi wa kuwatafutia walimu wa kuwafundisha tuition. Hawa ndio watoto wa Watanzania wengi, ndio wame-fail sana na kiukweli kwa kuliona hili ndipo ninaona gap la aliyenacho na asiyenacho linazidi kuongezeka katika Taifa letu. Kama Taifa nadhani kumekuwa na harakati nyingi za kupambana kupunguza gap la walionacho na wasiokuwa nacho. Lakini kwa kuendelea na mfumo huu wa elimu ambao watu ambao wanakuwa na fedha wanaweza kuwapeleka watoto kwenye shule nzuri na wakapata elimu nzuri na wengine wakabaki wakapata elimu yetu hii bure halafu wakakosa usimamizi mzuri, naiona hatari ya kuwa na Taifa ambalo watu wengi ni dhaifu na hawana ufikiri mzuri.

Mheshimiwa Spika, niseme tu ninaiomba Wizara hii watafute namna bora ya kuhakikisha watoto wetu wale wa Kitanzania, wale halisi wa mkulima, mfugaji, wavuvi wale watu wa chini kabisa wajasiriamali wadogo wadogo wanasaidiwa kupata elimu iliyo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaongea nikiwa na uchungu mkubwa sana, moyo wangu unaumia kwa sababu mimi ni kati ya wale watoto ambao tumesoma hizo shule lakini kwakweli bila ya yale mapambano binafsi ya mtoto kuhakikisha unajituma na nini, mazingira yalikuwa supportive, yanakusaidia kuweza kujituma ukawa na access ya hivyo vitabu, unakuta katika ripoti ya CAG unaona kabisa kuna vitabu havijapelekwa kwenye maeneo ya shule yetu, lakini unaona morale ya wazazi kuwahamasisha watoto kwenda shule imeshuka.

Mheshimiwa Spika, taarifa hizi tunaziona kwenye mabango yanayoendelea kutolewa na Mikoa mbalimbali kwamba wanafunzi idadi fulani hawajaripoti shuleni, wanafunzi kiasi fulani hawajaripoti shuleni, kwa hivyo, morali ya wazazi kusomesha watoto imeshuka, hii ni kutokana na kwamba watoto wengi ambao wamesoma wanaonekana ni mizigo wanaporudi nyumbani kwa sababu kwanza wanakuwa tayari wameshakuwa ni wavivu, hawataki kujituma na kazi zile za kawaida za kijamii zinazowazunguka hawataki kushiriki. Waliosoma wengi hata walioishia Form Four tu hawataki kushika majembe, hawataki kushiriki kwenye vikundi, wanajiona kama they are extra-ordinary, wanakuwa wako tofauti na wenzao wale ambao waliwaacha kabla hawajaenda kwenye hizo elimu zao, kwa hiyo wazazi pia morali imeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaona pia hata Walimu wetu, mimi naona morali ya Watumishi hususani Walimu pia imeshuka. Mwalimu badala ya kupambana kumsaidia mwanafunzi anapambana kupata extra money ya kujikimu yeye na familia yake, kwa sababu mwalimu mwenyewe angependa kuona mtoto wake anasoma katika shule hizo za private nzuri, kipato chenyewe ndiyo kama hiki ambacho tunakiona, wote tunafahamu kwamba kima cha chini cha mishahara bado siyo toshelevu kulingana na mfumko wa bei wa bidhaa mbalimbali na maisha kwa ujumla yanakuwa yamepanda gharama.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amekuwa akiendelea kuunda Tume mbalimbali, tumeona ameunda Tume ya Mambo ya Haki Jinai, lengo ni kuboresha haki ya Watanzania waweze kupata haki lakini hata elimu ni haki! Kwa hiyo, ninatamani kuona Mheshimiwa Rais atuangalizie au atuundie Tume nyingine ya kuchunguza huu Mfumo wa Elimu utaendelea kumkandamiza au kumuumiza mtoto wa kipato cha chini mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, katika suala la ufaulu nisiseme mengi niishie hapo, ufanyike utafiti wa kina wa kuhakikisha watoto wa chini wanasaidiwaje ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.

Mheshimiwa Spika, pia niendelee kuomba ukarabati wa shule…

SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha kengere ya pili imeshagonga.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru naamini majengo yote ya shule za zamani yatafanyiwa ukarabati. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika taarifa hizi ambazo zimewasilishwa; Taarifa ya Kamati ya Ukimwi na taarifa ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba ninayo furaha kubwa kuipongeza Hospitali ya Muhimbili kwa kuanzisha huduma ya Puto. Nadhani niwahamasishe wale watu waliozidi uzito ule uliokithiri, waende wakaweke. Kimsingi tumeona ushahidi kwa Peter Msechu, ndani ya wiki tu amepunguza kilo saba. Kwa hiyo, nawahamasisha sana Watanzania wenzangu, Wabunge wenzagu kutumia hii huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nirejee kwenye hoja zangu za msingi kuhusiana na Kamati ya UKIMWI na udhibiti wa dawa za kulevya. Ninarejea kwamba katika Mji wangu wa Tunduma, Mbozi na kanda nzima hii ya barabara ya Tanzam, ni moja ya maeneo yanayoathirika sana na masuala ya UKIMWI. Maeneo yote ambayo yana vituo vya ulazaji wa malori, watoto wa maeneo yale wengi wamekuwa wanatumika ndivyo sivyo, wanaharibiwa sana. Sijajua ni kwa nini madereva hawa na makonda wao wamekuwa ni watu wasio na huruma au watu wasiokuwa wa kujali kuangalia kwamba watoto wanaowaharibu ni kizazi kijacho. Kwani wanaweza wakawa wanawaharibu wale, lakini kwa sababu tunachangamana, kwa hiyo, wanapowaharibu wasidhani kwamba watoto wao wanakuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu, TACAIDS waje na mkakati maalumu wa ku-control hawa madereva wanaoharibu watoto wetu kwenye hivi vituo ambako malori yanalala. Kwa sababu kanuni na sheria ndogo ndogo zipo na zinatungwa. Kitendo cha kusababisha uharibifu wa Watoto na kuwasababishia maradhi, ni kosa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe tu watu wa TACAIDS kwenye hili watutazame. Watoto wetu wanaharibika sana, wanaacha shule kisa, Shilingi mia mbili mia mbili wanazokuwa wanapewa. Kwa hiyo, kwa hili naomba pia waweze kuliangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naona miradi mingi imelenga kuwasaidia wale wanaojiuza, wale ambao wanafanya ushoga na vitu kama hivyo, lakini kuwatazama wale watoto wanaotoroka shuleni na kwenda kuwakimbilia wale wa malori wapate chochote kwa sababu aidha ya njaa na nini miradi mingi katika maeneo hii haijazingatia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niendelee kuipongeza Mamlaka ya Kudhibiti Madawa ya Kulevya kwa namna ambavyo imekuwa ikiendelea kupamba na tumekuwa tukiona Kamishna wa madawa ya kulevya ambavyo amekuwa akiendelea kutoa taarifa mbalimbali kwamba wamekamata dawa kwa kiwango gani na ni watu gani wanahusika, japo wengine wamekuwa wanakasirika wakitajwa lakini ukweli ni kwamba madawa ya kulevya ni kitu ambacho kama nchi tumeendelea kukipinga na hatukitaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninataka kusema nini kwenye upande wa madawa ya kulevya kwamba waraibu ni watu ambao kwa namna moja au nyingine tuna wa-term kama ni waathirika, ni watu ambao wameshakuwa dhaifu hawawezi kujitegema kiuchumi bila kuwa-supported, sasa mpaka saa hizi hatujaona mkakati ambao upo wa kuhakikisha kwamba katika kila Halmashauri kumekuwa na mratibu wa masuala ya madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Halmashauri ndiyo kiungo cha Serikali Kuu na kule wananchi chini, kwa hiyo watusaidie kuweza kupata Waratibu kwenye Halmashauri zetu ambao wao watakuwa wanaendelea kusimamia haya masuala ya vilevi na madawa ya kulevya ili kupunguza vijana wetu na watoto wetu kuona kwamba masuala ya vilevi kama fasheni. Kwa sababu wakati mwingine masuala ya uvutaji bangi, masuala ya unywaji wa pombe uliokithiri au matumizi ya madawa ya kulevya yamekuwa yakiambatana na tabia hizi wanazoita tabia za kisasa za kuona kwamba haya mambo ni fasheni. Kwa hiyo, kama tutakuwa na waratibu kule ina maana kwamba watakuwa na programu zao kupitia Halmashauri za kufanya unasihi pia kuweza kufanya hamasa kwenye jamii ya kuzuia matumizi ya madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niseme tu kwamba nitakuwa sijajitendea haki kama nitashindwa kuongelea kuhusu Wilaya ya Songwe na mradi huu wa Peak Resources wa kuzalisha madini adimu ya magnet ambayo Tanzania nzima yamepatikana katika Kata ya Ngwala Wilayani Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaliongea hili na kwa uchungu mkubwa nikiiomba Serikali yangu wawape Peak Resources leseni, ni miaka minne tangu utafiti umekamilika. Ni kitu gani kinawafanya wao washindwe kutoa leseni kwa Peak Resources. Wamekuwa wanafanya majadiliano, makubaliano ni miaka minne ni majadiliano gani hayo yasiyoisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Songwe tunaamini kabisa kama ule mradi ukianza kufanya kazi wanawake wetu wa Mkoa wa Songwe kipato kitainuka. Wataweza kuuza hata mayai, wataweza kuuza hata kuku. Watusaidie kampuni hii ya Peak Resources iweze kupata leseni, maana tumekuwa tunafuatilia amekaa hapa Mheshimiwa Mbunge wa Songwe Mheshimiwa Phillipo Mulugo kila siku analia na hicho kitu, kuna wakati amejibeba toka Songwe kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kupokea hiyo leseni, lakini bado hiyo leseni hawakuweza kupata, sasa you can imagine kwamba ni kwa namna gani alifurahi siku hiyo na ni kwa namna gani siku aliweza kupata huzuni ya kukosa hiyo leseni.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini hakuna mjadala unaoweza kwenda zaidi ya miaka mitano mnajadiliana tu namna ya kufanikisha hilo suala, wakati ni kitu ambacho kina maslahi kwa Taifa! Imagine magnet Tanzania nzima inapatikana Songwe, mbona madini mengine wanapewa haraka haraka dhahabu na mengineyo. Hapa nimeona kwamba wanaenda kutoa leseni za helium why not katika huu mradi wa Peak Resources?

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie forum hii kuwaomba Serikali watupe leseni kwenye hiyo kampuni ya Peak Resources ili madini yaanze kuvunwa. Nitaendelea kuwahamasisha wanawake wa Jimbo langu waione hiyo fursa itakayopatikana kule kulingana na uwepo wa hii kampuni kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikiendelea kufanya kazi zake. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu. Napenda kuwapongeza Viongozi wa Wizara hii wote kwa namna ambavyo wamekuwa wakipambana kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama.

Mheshimiwa Spika, kabla sijajikita kwenye hoja ya msingi, nilitamani kuomba kwa Wizara suala la mpaka wa Tunduma waliangalie kwa karibu na ikiwezekana tunaomba watupe Wilaya Maalum ya Kipolisi katika Mkoa wa Songwe kulingana na mahitaji ambayo yapo na kiwango cha uhalifu ambacho kimekuwa kikiendelea kuongezeka kadri siku zinavyokwenda. Pia Kituo cha Polisi cha pale ni chakavu, kidogo na hakina hadhi ya kuwepo mpakani. Nalo hilo naomba waweze kutupa kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia napenda kumwomba Waziri atusaidie magari ya Zimamoto na gari la Utawala wa Zimamoto kwa Mkoa wa Songwe. Kwa sababu tunafahamu barabara ya Tanzam ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania. Hivi karibuni tumekuwa tukiona moto ukiendelea kuwaka barabarani na mwisho wa siku usafirishaji katika ile barabara haupo kwa sababu hakuna hata njia za mchepuko katika ile barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, napenda nirudi kwenye hoja ya msingi ya Jeshi la Magereza. Tumeona wamewasilisha taarifa nzuri, lakini sijaona sehemu ambayo wamewaongelea wafungwa kwa namna ambavyo wanastahili huduma za kibinadamu katika maeneo wanapokuwa pale Gerezani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kabisa moja ya haki za msingi za binadamu ni haki ya kuishi na pia kuhifadhiwa utu wake. Tumekuwa tunafanya ziara mbalimbali katika Magereza, hali ya magodoro Magerezani siyoo nzuri. Kwa mtu yeyote ambaye amefika Gerezani, ameingia akafanikiwa kuona hali halisi kule ndani, hali ya magodoro siyo nzuri. Nami ninarejea kwenye haki ya kuishi, kwamba mtu anastahili kupata chakula kupata matibabu lakini pia kulindwa afya yake iendelee kuwa imara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunawafahamu kabisa wanaoishi Magerezani ni ndugu zetu, ni sehemu ya jamii hii yetu na mwisho wa siku wanapotoka wanarudi kwetu. Wanapokwenda ndani kule wanalala kwenye magodoro ambayo ni chakavu yamechoka hatujui wamelalia watu wangapi ni risk kwa afya ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia bajeti hii nilitamani kuomba jambo moja, kama hawawezi kuwanunulia magodoro, wawaruhusu wanunue magodoro waingie nayo. Ninarudia kuliongea hili kwa uchungu kwa sababu hali ya malazi ya wenzetu kule ndani siyo nzuri. Sisi leo hii hatujijui, wengine tulishafika tukaingia mpaka Central, lakini hatujui kama siku moja mtu unaweza ukaingia ukalala mle. Hali ya malazi siyo nzuri, ni machafu, hayafai kwa afya ya binadamu. Wanapotoka kule watarudi na maradhi, watatuambukiza sisi pia huku kwenye jamii. Mwisho wa siku tutakuwa na jamii ambayo inaendelea kuwa na maradhi, inapambana na magonjwa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninataka kusema nini? Tuna wafungwa karibu 32,000 ambao Serikali kama kweli ikiamua kujitoa kuwahudumia kwa upande wa malazi, kama ambavyo inaweza kuruhusu wakanunua chakula…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo inaweza ikaruhusu wakatibiwa na watu wao wa nyumbani…

SPIKA: Mheshimiwa Neema Mwandabila, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nilikuwa nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Neema Mwandabila, maana yake sisi wengine ni wahanga, Gerezani tumekaa zaidi ya miezi minne, mitano. Unakuta hakuna magodoro, watu wanalala kwenye viroba na wengine wanalala chini kwenye cement hadi wanapata michubuko ya sehemu za mwili wao. Kwa hiyo, nampa tu taarifa kwamba asiombee aishie tu Central asije akaenda Magereza. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Neema Mwandabila, unaipokea taarifa hii?

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa yake na ninamwomba Mwenyezi Mungu aninusuru katika hili.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini? Serikali kama kweli inatambua kwamba jamii ile iliyopo kule ni ndugu zetu, kwa kiwango cha Shilingi 50,000/= kumgharamia mfungwa malazi ambao kwa ujumla wake inakuja kama Shilingi 1,600,000,000/= wanaweza kufanya. Kwa sababu ya majukumu ambavyo yamekuwa ni mengi na sasa hivi tuna janga hili la mafuta, tuwaombe wabadilishe au watengeneze utaratibu wa hawa wafungwa na mahabusu.

Mheshimiwa Spika, tunajua mahabusu sio mfungwa, hana hatia mpaka pale Mahakama itakapo-prove kwamba huyu ana hatia, ndiyo ataanza kutumikia kifungo. Imagine umekosa, haijajulikana kama umekosa, umekamatwa, umepelekwa kule, unakwenda kupitia hali ile; kwanza unapata msongo wa mawazo, lakini ndiyo hivyo afya inaharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu, kwa kuyaangalia hayo kwa namna ambayo ni ya kipekee, waone namna ya kutengeneza utaratibu kama walivyotengeneza kwenye chakula na kwenye mavazi ya mahabusu. Pia katika hili waone kwamba ipo haja ya kutengeneza utaratibu wa wafungwa, kama hana uwezo wa kununua, atatumia yale yale atakayoyakuta, lakini kama ana uwezo, utengenezwe utaratibu ambao ni wa kiusalama.

Mheshimiwa Spika, niliuliza hapa kipindi fulani ika-trend ikaonekana kama ni kitu cha ajabu, nikasema hawa hawajui hali iliyopo kule. Laiti wangejua hali iliyopo Magereza, suala la kwenda Magereza kama wadau namba moja wa kusaidia changamoto ya magodoro Magerezani ingeweza kusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, nisiseme mengi, pia naomba katika suala la mavazi, wale watu mavazi wanayovaa ni chakavu... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi jioni hii ili niweze kuchangia katika Wizara yetu hii muhimu sana ya Afya. Nitumie nafasi hii pia kuipongeza Serikali yangu, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali inayoongozwa na mama yetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, chini ya dada yetu Ummy pamoja na Mheshimiwa Mollel. Mimi binafsi niseme nina imani kubwa na hawa mawaziri wetu kwa namna ambavyo wamekuwa wakiendelea kutupa ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba nawapongeza kwa namna ambavyo nimeweza kuona wameelezea suala la lishe vizuri kwenye taarifa yao. Hii inaonesha kwamba Wizara kama hii wanaona umuhimu wa suala la lishe kwa nchi hii na kuangalia ni namna gani wanakwenda kuisaidia nchi kuweza kuondokana na changamoto za matatizo ya lishe yanayokuwa yanaendelea nchini. Kwa hiyo ninampongeza Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake kwa kuiona lishe kama ni kitu cha msingi. Nimependa zaidi sana pale walipoweza kuelezea kwamba wataanzisha viwanda vya utengenezaji wa vyakula dawa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ilikuwa ni ajabu lakini iliyokweli kuona kwamba Tanzania tunaozalisha karanga, tuna maziwa mengi ya kutosha eti tunaenda kuagiza plant peanut, maziwa F100 na F75 kuitoka Ufaransa; kweli ilikuwa ni ajabu; lakini naona wameliona hilo na wanakwenda kulifanyia kazi. Na ninaamini hili litaweza kuleta ajira kwa wananchi wetu wa Tanzania kwa sababu karanga ni zetu na maziwa ni ya kwetu. Ninashukuru sana kwa hilo kwa Mheshimiwa Waziri kuweza kuliona.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nilikuwa na mambo machache, ninadhani yanaweza kuleta tija kwenye Serikali yetu. Wameendelea kutujengea miundombinu mingi sana. Sisi kama Watanzania hususani kutoka Mkoa wa Songwe tunawashukuru na tunajivunia sana yale majengo mazuri ambayo mmeweza kutujengea katika nchi yetu. Tunawashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia wameendela kutoa vifaa tiba vya kisasa vizuri na vingi sana. Kwa hiyo, na hili tunawapongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu inakuja wapi? Hoja yangu inakuja, ni kwamba majengo na wataalamu waliopo kwenye majengo unakuta haviendani. Haviendani kwa ubora na wala haviendani kwa idadi ya watumishi wanaotakiwa kwenye yale majengo. Kwa hiyo nilikuwa natamani Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku wind-up mwishoni atusaidie kutueleza kwamba, ana mpango gani angalau wa kufanya reshuffling ya kupeleka wataalamu waliobora kutoka kwenye hospitali zile kongwe ambazo zina wataalamu wazuri Kwenda kwenye hizo hospitali za rufaa mpya ambazo zimeanzishwa, ili majengo na wataalamu watoe huduma iliyobora?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kitu kingine ni kwamba wametusaidia sana kuleta vifaa vingi sana; na nimshukuru Naibu Waziri Mheshimiwa Mollel, mwaka jana mwezi wa pili alitupatia x-ray katika Wilaya ya Ileje. Lakini nitoe tu masikitiko yangu leo hii hapa kwamba x-ray ile katika Wilaya ya Ileje mpaka leo haifanyi kazi. Nashindwa kuelewa kwamba Serikali kweli Serikali hii inayopambana kutoa fedha nyingi kwa ajili ya vifaa tiba inashindwa kufanya ufuatiliaji na kuhakikisha mitambo hii iweze kufanya kazi kwa wakati? Ile dhamira ya mimi kupambana kuomba x-ray mashine katika Wilaya ya Ileje haijaweza kufanikiwa kwa mwaka mzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo unaweza ukaona kwamba kuna wataalamu kule chini ambao wapo na wanafanya kazi na supervision wanafanya, na hiyo supervision wanazozifanya ipo haja ya wale wataalamu huko chini waangalie kwamba supervision zao zinakuwa zina tija gani? Kwa sababu kama x-ray imekuja mwaka jana mwezi wa pili mpaka leo haifanyi kazi; yaani unashindwa kupata picha kwamba wale wataalamu walioko kule chini ina maana hawaoni shida yetu sisi kama Watanzania kwenye eneo lile kwamba tunahitaji x-ray? Na kila siku wanakwenda wanachukua posho za hizo supervision na x-ray bado haifanyi kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo si kwa Ileje tu, Ileje is just a sample, lakini nchi nzima yaani kuna maeneo mbalimbali ambayo vifaa vizuri vinapelekwa vya kisasa lakini havifanyi kazi kwa wakati. Lakini pia vifaa hivi vinavyokuwa vinaletwa wataalamu wale wahandisi wa vifaa tiba tunao wanagapi wa kutosha kuweza kutengeneza? Je, hawa wataalamu wa kuweza ku–operate hivi vifaa kama nchi tumetengeneza mkakakti gani wa kuwa na wataalamu ambao wataweza ku–operate hivi vifaa?

Mheshimiwa Naibu Spika,unashangaa x-ray imeletwa unaambiwa mtu wa radiology hayupo. Kifaa kimeletwa unaambiwa mtu wa anesthesia hayupo. Sasa you can imagine; mipango ya ununuzi wa vifaa unaokuwa unaendelea nchini na utengenezaji wa wataalamu ambao wataenda kusaidia vifaa hivyo kufanya kazi hauendi sambamba. Kwa hiyo nimuombe Mheshimiwa Waziri kupitia bajeti hii aje na mkakati ambao utaonesha uwiano wa ununuzi wa vifaa vya kisasa unaoendelea lakini na wale operators, wataalamu ambao wameandaliwa kwa ajili ya ununuzi wa hivyo vifaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kitu kingine, nilitamani kuongelea suala la misamaha. Tumeona hapa, alikuwa naelezea Mheshimiwa Alice kwamba kuna burden kubwa ya utoaji wa misamaha kwenye nchi yetu. Kiukweli ukienda kufanya assessment, critical assessment misamaha mingi unaweza ukakuta ni fake. Yaani watu wanajitengenezea utaratibu wao wa kujipatia kipato ambacho wanaikosesha Serikali mapato, anapata yeye mfukoni kidogo anaandika misamaha isiyokuwa na tija. Kwa hiyo mimi niombe tu Mheshimiwa Waziri awe na uataratibu wa kufanya analysis nzuri ya misamaha iliyotolewa, ukiacha ile ambayo wana mpango wa kuitoa ili tuende sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu sawa tunatoa huduma za afya na watanzania wengi wazee wanakosa huduma kule kisa tu waliopewa misamaha mikubwa ni wengi. Kwa hiyo mimi niombe tu Mheshimiwa Waziri kwenye hili tusaidie, tusaidie sana Dada yetu Ummy kuhakikisha misamaha iwe ile ya kweli, kwa sababu tunaona burden iko kwenye NHIF, bima yetu ya afya inaelemewa lakini ukienda kufanya assessment unakuta na kwenyewe kuna utaratiubu ambao si mzuri ambao unafanyika wa watu kuwahudumia watu ambao hata hawako registered na bima, mtu anajipatia chochote kwenye mfuko wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimuombe tu Mheshimiwa Waziri, sisi tunapenda kazi yake anayioifanya, lakini suala la bima ni lazima atusaidie, suala la misamaha ni lazima atusaidie, kwa sababu haiwezekaniki bima mpaka leo eti tunakuwa tunaongelea bima kushindwa kuwahudumia wateja kwamba inaweza ika-collapse au ikafanya nini, wakati tuna uhakika waliojiandikisha na bima si wengi kiwango hicho.

Mheshimiwa Naibu spika, baada ya kusema hayo, I am sorry. Kuna suala la Tuduma. Tunduma iko mpakani, mpaka ule you can imagine tunapokea tu simu kila siku eti X-Ray hawana, Tunduma Mpakani, tena ni Halmashauri ya Mji ambayo sasa hivi mmetujengea Hospital nzuri haina X-Ray mpaka sasa hivi. Kwa hiyo nikuombe Waziri suala la Tunduma lichukulie kama emergency na ukatusaidie tuweze kupata X- Ray eneo lile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Baada ya kusea hayo naunga mkono hoja, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi leo hii asubuhi na mimi niweze kuchangia katika Wizara yetu hii ya msingi kabisa na ya muhimu.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kabisa Wizara hii ni Wizara kwa kweli ambayo imebeba dhamana kubwa ya Taifa letu katika kuhakikisha usalama wa nchi yetu kimaadili, kiuchumi na kuweza kusaidia mambo mbalimbali ya Taifa hili yaweze kwenda mbele.

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu ninampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuwa-support Wizara hii, na amekuwa akiendela kuwapa support; nadhani ni vile kwa sababu na yeye ni mtaalamu wa maendeleo ya jamii; kiukweli angalau tunaona Wizara hii inaendelea kuonekana machoni pa Watanzania. Na pia Mheshimiwa Waziri Gwajima na Naibu wake na timu nzima yake ya uendeshaji wamekuwa wakiendela kupambana kuhakikisha angalau afua za maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii zinakuwa zinajulikana katika makundi mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mimi nitaongelea nitapenda nijikite sana kwenye masual ala NGO; na niseme tu, uwepo wa NGO katika nchi yetu umetusaidia katika meneo mbalimbali. Niseme, kwamba tunafahamu kama Taifa tunakabiliwa na changamoto mbalimbali hususani za kimaadili. Tunaona kiwamba kuna masuala ya ushoga ambayo sasa hivi ndio yana-hit, na yamekuwa yakitupa stress Watanzania wengi, kuona kwamba jambo hili ni kitu kisichokubalika, ni kitu ambacho kinatweza utu wetu na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeona kuna changamoto ya dawa za kulevya, kitu ambacho kipo. Kiko underground lakini ukiweza kufuatilia wataalamu wanaoshughulika na masuala ya dawa za kulevya utagundua kwamba ni kitu kiko kikubwa lakini bado watanzania kama Watanzania hatujakipa kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna biashara ya ngono. Ni kitu ambacho kimendelea kushamiri; na biashara yoyote haiwezi kushamiri kama hakuna wateja. Lakini pia kuna suala la ubakaji na ualawiti ambalo limekuwa likiendelea katika jamii yetu.Hili suala limeenda mbali, kwenye shule zetu tumekuwa tukipata tarifa mbalimbali ambazo wataalamu wa ustawi wa jamii wamekuwa wakiendelea kufuatilia na kubaini kwamba zipo shule ambazo watoto wengi wameweza kuharibiwa na wameweza kushirikishwa katika matendo haya ya ngono ambayo ni ukatili wa kijinsia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi niseme tu, na nitoe masikitikop yangu hapa, niliweza kupata taarifa kutoka kwenye shule moja inaitwa Haloli Mbozi, kwamba watoto 30 kati ya watoto wa darasa la tatu na la nne walibainika kuwa wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono; wengine wamelawitiwa na wengine wamebakwa. Na wale wanaobainika wamefanya matendo haya mpaka leo sijasikia kauli wamefanyiwa nini?

Mheshimiwa Spika, niseme tu, kulingana na changamoto hizi tumekuwa na NGO ambazo zinafanya kazi nzuri na zinahitaji kupongezwa. Wamekuwa wakiendelea kuwabaini na kuwatambua waathirika wa matendo haya yote ya ukatili au matendo haya ya hovyo ambayo yamekuwa yakiendelea. Wametengeneza afua ambazo wanaendelea kuwabadili kitabia na kuwasaidia kiuchumi, na hawa watu wanakuwa wanafanya wanabadilika kitabia na kuweza kusimama binafsi na kuachana na matendo ambayo yanakuwa hayana maadili mema kwa nchi yetu. Kwa taasisi hizi nazipongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kumekuwepo na NGO ambazo Mheshimiwa Mwakyembe aliweza kuongea kwa huzuni sana. Alisema kwamba tuna NGO nyingi ambazo zimeeendelea kuwafundisha Watanzania ushiriki wa ngono za jinsia moja. Sasa, ninapata hofu kwamba kama Taifa tunakuwa na NGO ambazo zimeingia mpaka zimefika site zimefanya kazi, zimewafundisha watu ushoga na kama Taifa hatuna habari; mpaka wanakuja wanaharakati ndio wanaenda kuibua. Ninapata shaka na usalama wa nchi yetu kwamba kama hii ni ushoga tu taasisi nyingi zimeshapewa fedha na zimeshafanya kazi nzito na hakuna kilichokuwa kinaeleweka mpaka wanaharakati, ninapata hofu kubwa.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kama huu ni ushoga umefanya hivi, je, mambo mengine yanayohatarisha hali ya usalama wa nchi yetu hali ikoje? Na hii inaonesha kuna ulegevu wa ufatiliaji wa NGO hizi. Kwa hiyo nilitamani Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja atuambie, baada ya kauli zile nzito za Mheshimiwa Mwakyembe kwenye lile kongamano na yule mwanaharakati ambaye alikuwepo pale, Catherine Kahabi, wamefanya nini kuhakikisha kwamba kauli zile kama zina uhalisia au hazina uhalisia, au ijoke? Kwa hiyo kwenye hili nitamtaka Mheshimiwa Waziri aje na kauli atuambie ilikuwaje na imekuwaje mpaka leo tunakuwa na miongozo ambayo inaelekeza namna ya watu kuwasiliana wanaume wa jinsia moja, yaani jinsi ya kufanya mapenzi na practical zao? kwa sababu zile tuhuma ni nzito sana kwa nchi yetu. Kwa hiyo nilitamani Mheshimia Waziri aje atuambie.

Mheshimiwa Spika, lakini kitu kingine ambacho nataka nikiongelee nataka niongelee dhamana ya maadili ya Taifa letu. Kwamba tunataka kuiacha dhamana ya maadili kwa watu ambao si watu wa Taifa letu. Yaani imagine NGO’s kutoka mataifa mengine ndio wanakuja kuanza kubadili tabia za watu wetu ama kuzitengeneza tabia za watu wetu. Kwa hiyo ninatamani kada ya ustawi wa jamii ipewe kipaumbele. Ni kada ambayo inasahaulika sana. Yaani unakuta unapoongelea maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii, Wizara imejikita kwenye masuala ya maendeleo ya jamii tu. Ustawi wa jamii hausemwi. Ukiangalia ukienda ufuatilia bajeti ya ustawi wa jamii ndani ya Wizara hii unaweza ukakuta ceiling ni ndogo sana; na nilitamani Waziri atakapokuwa anakuja mwishoni kuhitimisha atuambie kwenye ajira hizi 800 za maendeleo ya jamii zilizotangazwa ndani yake ustawi wa jamii ni ngapi?

Mheshimiwa Spika, haiwezekaniki ajira 800 kutoka Wizara moja ziwe za kada moja watu wa ustawi wa jamiii hawapewi hizo nafasi. Asilimia 95.3 ni upungufu. Yaani katika hali ya kawaida utaona kabisa kama nchi hatuna uelekeo kwenye suala la kulinda zile values za nchi yetu. Kwa hiyo kwenye hilo Waziri pia nitamtaka mwishoni atuambie ana mkakakti gani wa kuhakikisha ajira za ustawi wa jamii zinaongezwa? na ikiwezekana kama kunakuwa na sintofahamu kwenye wizara kati ya ustawi wa jamii na maendeleo ya jamii ustawi wa jamii ipewe iwe institution, yaani inayojitegemea. Ikiwa idara maalumu inayojitegemea tunaamini itakuwa na uongozi wake na hata management ya masuala ya ustawi wa jamii kwa nchi hii yataenda vizuri. Tunafahamu ni kada mtambuka ustawi wa jamiii inagusa Wizara nyingi, lakini itakapokuwa kwenye idara moja ambayo inajitegemea tunaamini management yake itakuwa ni rahisi.

Mheshimiwa Spika, imagine wengine wako Wizara ya ndani, wengine wako sijui wako TAMISEMI, wengine sijui wako kwa Waziri Mkuu. Kwa hiyo niseme tu kwenye hili nitatamani kumsikia Waziri anatuambia nini kuhusu kuisimamisha kada ya ustawi wa jamii ili iweze kufanya kazi yake vizuri na kuwa na bajeti ya kutosha ili iweze…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Kengele ya pili ilishagonjwa Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niseme ninashukuru sana kwa nafasi na naunga hoja. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya msingi katika nchi yetu. Natamani nitumie nafasi hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Rais kikamilifu kwa namna ambavyo kwa Mkoa wangu wa Songwe wameweza kutujengea barabara ya kutoka Mpemba – Isongole. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze vile vile kwa kutujengea kile Kituo cha Forodha pale Mpemba ambacho ni kituo cha mpakani Tunduma ambacho kina heshima kubwa kuliko kile kituo cha upande wa Zambia, kiasi kwamba hata Wazambia wakati mwingine huwa wanakuja kupiga picha huku kwetu kwa namna ambavyo kimeboreshwa na kimekuwa cha kisasa sana.

Mheshimiwa Spika, pia niweze kuishukuru Wizara hii, kwa kweli wamekuwa ni watu wa msaada na ni watu wasikivu ambao mara nyingi tukiwafuata wamekuwa wakisikiliza changamoto zetu na kuzifanyia kazi. Pia niweze kuishukuru Wizara kwa kuona umuhimu wa kujenga hii barabara ya Igawa – Songwe mpaka Tunduma. Kipekee kwa kweli kwa Mji wa Mbeya wameutendea haki kwa kiwango cha pesa walichotenga kwa ajili ya barabara kutoka Uyole kwenda Ifigi. Nadhani hii pia itaweza kukupa heshima kwa Jiji la Mbeya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika barabara hii nilitamani kuwashawishi Wizara waone umuhimu au udharura wa kuijenga barabara hii kwa upande wa Tunduma pia. Ni kweli wataboresha Mbeya, lakini tujue kabisa Tunduma pia hali ni mbaya tunaona namna ambavyo foleni imekuwa ikizidi kila siku zinavyozidi kwenda na Mheshimiwa George alivyochangia jana alionyesha masikitiko yake ni kwa namna gani Tunduma kulingana na umuhimu wake katika uchumi wa nchi hii haijapewa kipaumbele, kwa hiyo niwaombe wizara kwa namna ya kipekee kabisa suala la kupanua hii barabara kutoka Mlowo kwenda Tunduma waone kama kipaumbele cha msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kupitia bajeti hii nitatamani nimsikie Waziri akieleza ni nini mkakati wake wa kidharura kuhakikisha barabara hii upande wa Tunduma inapanuliwa, hata kama watashindwa kuanzia Mlowo basi waseme neno kuanzia eneo la Chimbuya kwenda Tunduma hali ni mbaya hali sio nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unafahamu barabara yetu hii haina sehemu ya mchepuko, kama ikitokea ajali, moto au changamoto nyingine yeyote barabarani hakuna namna ambavyo magari yanaweza yakafika Tunduma, na tunafahamu kabisa magari mengi yanayoenda Tunduma ni magari yanayotakiwa yavuke nchi ya Zambia, Congo na nchi za SADC kwa ujumla, lakini wananchi wa Tunduma inakuwa ni adha tunafahamu kabisa Mbeya na Tunduma ni watu wanaoingiliana sana, kama kukatokea jam ina maana watu wa Mbeya hawawezi kuja kufanya kazi Tunduma, kitu ambacho katika hali ya uchumi kwa upande wa nchi tunakuwa tunazidi kuyumba.

Mheshimiwa Spika, kwanini ninasisitiza kuhusu barabara ya mchepuko, ni kulingana na hali ya mambo ambayo yametokea katika kipindi hiki cha kuanzia mwezi wa 12 mpaka sasa hivi. Kumekuwa na ajali nyingi sana katika barabara hii na kiukweli wananchi wameteseka sana kama alivyokuwa ameongea Mheshimiwa Stella pale jana.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuongelea suala la barabara hiyo ya kutoka Igawa kwenda Tunduma ningependa niweze kuongelea suala la barabara ya Mbalizi - Galula - Mkwajuni na Makongolosi. Tunafahamu Wilaya ya Songwe ina rasilimali za msingi, tunafahamu kabisa kule madini ya dhahabu ambayo yanashimbwa ile inaingiza pesa katika nchi hii, kule tunatarajia tupate madini ambayo ni ya msingi kabisa rare earth ambayo hayapatikaniki sehemu nyingine lakini mazingira ukiangalia ya barabara hii ni magumu. Mheshimiwa Mlugo amekuwa akilia kila siku lakini mpaka sasa hivi sioni uelekeo au utaratibu ambao Wizara imetenga kuhakikisha inaanza ujenzi wa barabara ya lami katika hili eneo.

Mheshimiwa Spika, niseme tu ukweli Songwe kama kweli ikafunguliwa Wilaya ya Songwe ni potential kwa nchi hii kwa maana ya kuweza kusaidia kipato cha nchi kiongezeke. Kwa hiyo mimi ninaomba Wizara itakapokuja kwenye hili waweze kusema neno, na kwenye hili nitashika Shilingi kwa sababu Songwe inakuwa sahaulika sana na ni Wilaya pekee ambayo kwa upande wa Mkoa wa Songwe tunaitegemea kwa mapato makubwa ukiacha Tunduma, kwa hiyo kwenye hili Waziri nitaomba mje na maelezo ya kutosha kueleza ni lini barabara hii itaanza kujengwa.

Mheshimiwa Spika, pia ninatamani kuongelea kwenye suala la TAZARA tunajua Mkoa wa Songwe na Mbeya hauwezi kuutenganisha na kwa namna hiyo ina maana tunategemeana sana na tunafahamu kabisa suala la TAZARA ni letu wote.

SPIKA: Sekunde moja.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naomba Wizara iweze kuweka mkakati maalum wa kuhakikisha TAZARA inaanza kufanya kazi ili pale Mpemba watakapojenga hiyo dry port ambayo tumeitengea eneo mambo yaweze kwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante.(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kupata nafasi hii ya kuweza kuchangia katika Wizara muhimu hii ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi yanayoendelea katika Wizara hii ambayo kwa kweli nisiposema ninakuwa kama sijitendei haki. Nimpongeze Mheshimiwa Gwajima na timu yake wamekuwa wakiendelea kupambana sana kwa kuwafikia wananchi hadi ngazi ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijachangia nilipenda nitumie forum hii kuwashukuru vijana wawili katika Mkoa wa Songwe; Mshomari na Sam Midadi ambao kiupekee wamenitungia wimbo maalum nikiwa kama dada yao ambao imewapendeza wao kwa jitihada zao na bidii yao na fedha kuona wamuimbe dada Neema. Kwa hiyo ninawashukuru sana popote walipo wapokee shukrani zangu za dhati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijielekeze katika kuchangia katika wizara hii na ningependa nianze na kipengele cha Ustawi wa Jamii; tunaona katika takwimu tulizoletewa tuna upungufu wa asilimia 97 ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika nchi yetu na kimsingi uhitaji au umuhimu wa hawa Maafisa Ustawi wa Jamii unaonekana kutokana na ongezeko la vitendo vya ubakaji, ulawiti, mauaji na pia utelekezaji wa familia ambao umekuwa ukiendelea kwenye jamii yetu. Hivi ni viashiria vya msingi vya kuonesha kabisa kwamba watu hawapo salama afya ya akili ya vijana wengi, wazee wengi na akina baba wengi huko kwetu na wanawake wengi kwa ujumla yaani jamii kwa ujumla haipo salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitamani sana kusema neno hili si kwa maana ya kwamba labda nina maana mbaya ila naona kwamba kitendo cha kutokuwa na Maafisa Ustawi wa Jamii inaonesha Serikali kwa namna moja au nyingine imeamua kuhalalisha vitendo hivi vya ubakaji, ulawiti na mauaji na utelekezaji wa familia kwa kutokuwa na mkakati maalumu wa kuhakikisha Maafisa Ustawi wa Jamii tunakuwa nao wengi wa kutosha. [Maneno Haya Siyo Sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge]

Mheshimiwa Spika, na…

SPIKA: Mheshimiwa Neema ngoja ngoja kidogo. Hiyo sehemu ya maneno uliyoyasema hapo kwanza yafute halafu uchangie upya hiyo sehemu maana siwezi hata kuyarejea. Kwa hiyo, yaondoe hayo maneno wewe mwenyewe halafu anza kuchangia upya ili pengine ukitumia lugha nyingine tutaelewa vizuri.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, naomba niyaondoe maneno kama ulivyoniambia ila ninataka niseme nini? Nataka niione dhamira ya Serikali kuhakikisha inatoa ajira kwa Maafisa Ustawi wa Jamii kwa wingi zaidi ili changamoto hizi za ubakaji, ulawiti, mauaji na utelekezaji wa familia zinazoendelea katika jamii yetu viweze kupungua. Tunaamini kabisa na tunafahamu kwamba Maafisa Ustawi wa Jamii ndiyo watu wenye elimu ya kuweza kufanya counselling kwa watu wetu na ndiyo watu wanaoweza kusaidia kubadili mwenendo na tabia ya jamii yetu na kufuatilia kwa ukaribu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninataka kuiomba Serikali kupitia forum hii kwamba wahahakishe Maafisa Ustawi wa Jamii wanaajiriwa wanakuwa wengi na mimi sidhani au sielewi ni kwanini Serikali haiipi kipaumbele kada hii kwa sababu hata ukiangalia mara leo wapo Afya, mara leo wapo Maendeleo ya Jamii, sijui kesho watakuwa wapi. Kwa hiyo ninatamani kwamba kada hii ya Ustawi wa Jamii ipewe kipaumbele na ikiwezekana itengenezewe sheria maalumu ya kuilinda taaluma hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niseme tu hata kiwango cha bajeti kinachotengwa kwa Wizara hii kinaonesha kabisa dhamira ya Serikali kupambana na vitendo hivi bado haijawa wazi sana. Ninatamani kuona kwamba katika Wizara ambayo ingekuwa inapewa kipaumbele ni pamoja na hii kwa kutengewa fedha ya kutosha.

Mheshimiwa Spika, ninapenda pia kwenda kwenye eneo la maendeleo ya jamii hususani kwenye hii ya mikopo inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Tunaona ni pesa nyingi inatengwa na tunaona kabisa ubunifu wa miradi unaoendelea kwenye halmashauri si toshelevu, si mzuri kwa maana gani naongea maneno haya tungekuwa na watu wa ku-design miradi wazuri tusingekuwa tunaona ya kwamba projects zinazoendelea ununuzi wa pikipiki tu, bajaji tu kila siku tunatamani kuona kwamba Wizara hii ya Maendeleo ya Jamii wanakuja na mkakati wa kuajiri wataalamu wa ku-design miradi watakaowafundisha jamii yetu wanawake, vijana na hao watu wenye ulemavu ili kuepuka miradi ya aina moja kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajua kabisa uelekeo wa nchi yetu ulikuwa ni viwanda na hatutajua miradi hii kupitia mifuko ya wanawake yaani kuna miradi gani ambayo mpaka sasa hivi wameweza kuifanya ambayo inaonyesha kabisa uelekeo wetu niwaviwanda. Vikundi vipewe fedha ya kutosha, lakini pia uelekeo ungeendana na hii Sera ya Viwanda ingependeza zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna kitu kingine ambacho nilitamani kukiongelea kuna kundi ambao lipo kwenye jamii, hawa mabinti wengine ambao walibakwa wengine ambao walilaghaiwa kwa namna moja au nyingine unakuta wamepata watoto, malezi ya watoto hawa mara nyingi yanakuwa yanayumbayumba. Ninatamani katika eneo hili la maendeleo ya jamii wangekuja na mkakati maalumu wa kuangalia namna ya kuwajengea uwezo hawa mabinti ili wawe na uchumi ambao ni stable, lakini mbali zaidi tunaamini kwamba wakijengewa uwezo hata utapiamlo kwa watoto wetu utakuwa haupo, hawa watu wote watakuwa wana uhakika wa chakula lakini na uhakika wa huduma zingine kama mavazi, malazi na matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nimekiona katika eneo hili la mikopo hii mpaka sasa hivi ni muda mrefu tumekuwa tukiendelea kutoa mikopo, lakini impact assessment ya mikopo hii haipo na ukiangalia mpaka sasa hivi ukiwauliza ni wanawake wangapi wamejikomboa kutoka kipato kipi kwenda kipato kipi au ni vijana wangapi walikuwa na uchumi huu saa hizi wapo uchumi huu taarifa hizi hazionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kupitia forum hii, Bunge hili tukufu nilitamani kuiomba Wizara wakafanye assessment tuweze kujua tulipokuwa na tunapoelekea ili hata unaposema tunatoa pesa nyingi iwe kweli ni pesa nyingi lakini zenye tija kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho nilitamani kukiongelea zaidi ni katika hili suala la ulinzi wa mtoto; tumekuwa tunaona ni kwa namna mbalimbali ambazo kila mwananchi, kila mtanzania anapambana kulea mtoto wake anavyojua yeye naniwapongeze kwa forum ambayo wameianzisha yakuwa na vituo vya malezi ya watoto katika kila kijiji na ninasikitika tu kwamba vituo vya mfano vyote vipo Dar es Salaam na vingine vinaletwa Dodoma. Mimi nadhani kama mfano ungeanzia kwa kila angalau yaani hata kwa angalau kila kanda kukawa na kituo kimoja ingependeza zaidi kwa sababu tungekuwa tunaendelea kuinua Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu, kwa hili nawapongeza na ninaamini kupitia Bunge hili tukufu hiki tutakiona na kukipa kipaumbele na kuhakikisha kila kijiji Tanzania inakuwa na hizi centers za kulelelea watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nashukuru sana kwa nafasi ya kunipa kuweza kuongea. (Makofi/Kicheko)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii iliyoletwa mbele yetu na Waziri wa Fedha. Kipekee napenda kuwashukuru viongozi wa Wizara hii, Waziri, Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Hamad Chande kwa namna ambavyo wamekuwa wakiendelea kufanya kazi vizuri. Pia nawapongeza Katibu Mkuu wa Wizara hii na Manaibu wote kwa namna ambavyo pia wamekuwa wakitekeleza majikumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee zaidi namshukuru Mheshimiwa Rais wetu kwa namna ambavyo amekuwa akifanya mambo mzuri, nami kama mwakilishi wa Mkoa wa Songwe, ninayo mengi mazuri ambayo najivunia ambao Mheshimiwa Rais ameweza kufanya kwa ajili yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitapenda kuongelea masuala machache ambapo suala moja kubwa ni kuhusu mkataba huu ambao umesainiwa wa uuzaji wa makaa ya mawe, ambapo nchi yetu ya Tanzania itaenda kuiuzia makaa ya mawe nchi ya Switzerland, na tumesaini mkataba wa kuuza tani 60,000 za makaa ya mawe kwa hiyo nchi ya Switzerland. Kwa sisi watu wa Mkoa wa Songwe hususan Wilaya ya Ileje, ni fursa nzuri sana ambayo kwa kweli tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutusaidia kuweza kuipata hii fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Wilaya ya Ileje ni moja ya wilaya ambazo zinamakaa ya mawe mengi sana katika nchi hii. Kwa taarifa ambazo zipo na zilizofanyiwa utafiti zinaonesha kuna reserve ya tani milioni 100 ya makaa ya mawe katika eneo hili kitu ambacho kwa kupitia huu mkataba uliosainiwa, tani 60,000 tutauza kwa 4.4 billion inaonesha kwamba kama tutafanikiwa kuuza haya makaa yote ya mawe ambayo ni tani milioni 100, kwa nchi yetu tunaweza tukaingiza kiwango cha Shilingi bilioni 6,900. Nadhani ni pesa nyingi sana ambapo kama nchi tunaihitaji kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba huu uliosainiwa utekelezaji wake unaenda kuanza ndani ya mwezi huu. Kwa namna hiyo, kupitia huu mkataba ambao ni wa miaka mitano, ina maana ya kwamba tutaweza kuvuna tani milioni 3.6 tu, kitu ambacho tunaona kwamba bado tunayo fursa ya kutafuta mikataba mingine mingi zaidi ili haya makaa ya mawe yaweze kutumika na kuliletea Taifa letu kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Kweli tumepata mkataba, lakini tunafahamu kwamba haya makaa ya mawe yaliko bado miundombinu haijakaa vizuri hususan kwenye barabara. Nilitamani kuiomba Wizara hii iweze kuweka kipaumbele cha ujenzi wa barabara hii ya kilometa saba ambayo fedha yake imetengwa kupita TARURA, badala utekelezaji uende kufanyika kupitia TARURA, tulitamani kwamba utekelezaji huu ufanywe na TANROAD ili iweze kufanyika kwa haraka sana kulingana na umuhimu wake ambao upo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama barabara haitakaa vizuri ina maana uzalishaji na usafirishaji wa haya makaa ya mawe itakuwa ni changamoto kubwa. Kwa hiyo, kwa maana ya ujenzi wa kiwango cha lami kupitia TANROAD utafanyika kwa haraka kitu ambacho tutakuwa tumeisaidia nchi yetu kurahisisha uuzaji wa haya makaa ya mawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Mpaka sasa hivi hii barabara ya kilometa saba imekuwa haitumiki. Kwa hiyo, wanatumia barabara nyingine mbadala ambayo ina kilometa 36 ambapo kwenda na kurudi unakuta kilometa 72, kitu ambacho kinaongeza gharama za usafirishaji wa yale makaa mpaka ile selling point ya haya makaa ya mawe. Ukiacha hivyo, pia ule mzunguko wa usafirishaji wa makaa ya mawe unachukua muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, najaribu ku-justify kwamba ujenzi wa hii barabara kwa kilometa saba kwa Serikali itaweza kuipunguzia gharama zisizokuwa za lazima. Kwa hiyo, nawaomba kwamba ile fedha iliyotengwa TARURA ihamishiwe TANROADS ili zoezi liweze kufanyika kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha hilo suala la barabara, pia tunafahamu kabisa kwamba pale Kyela kuna Ziwa Nyasa ambapo tumekuwa na mkakati wa ujenzi wa meli na meli zilizojengwa mpaka sasa hivi kwa usafirishaji wa mizigo hii zinaonekana ni ndogo, kama kweli Serikali ikiamua kuwekeza kwenye ujenzi wa meli nyingine mpya kubwa ya mizigo, itarahisisha usafirishaji wa haya makaa ya mawe kuelekea Mtwara.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kabisa kupita Ziwa Nyasa kwenda Mtwara ndiyo inakuwa njia nyepesi ya usafirishaji wa mizigo kuliko kusafirisha haya makaa ya mawe kupitia barabara ya kutoka Kyela, Mbeya, Makambako mpaka Songea kuelekea Mtwara. Kwa hiyo, naishauri Wizara ione umuhimu wa kuwekeza katika Ziwa Nyasa, kujenga meli nyingine mpya kubwa ya mizigo ili tuweze kusafirisha kwa urahisi na kwa namna hiyo tutakuwa tunazilinda barabara zetu ambazo tunazijenga kwa gharama kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuliongea hilo, natamani kuongelea katika kipengele cha TAZARA. Ninaongelea TAZARA kwa uchungu mkubwa kwa namna ambavyo imeharibika, imechakaa. Kitu ambacho tunajua, kama tuliweza kukaa awali, tukatengeneza hiyo sheria ambayo ipo na tukawa tunaitekeleza na sasa inaonekana kwamba hiyo sheria inakuwa kama haitupi fursa ya uwekezaji sisi kama Watanzania, tuone namna ya kuweza kupitia hii sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, natamani kuona Serikali inachukua hatua kwenye kufuatilia utekelezaji wa hiyo sheria ambayo inaifanya Tanzania ishindwe kuendelea kuwekeza katika TAZARA. Kwa namna hiyo, kama sheria ikibadilishwa tunaamini tutanunua mabehewa lakini pia tutawekeza kwenye repair ya hii reli ya TAZARA. Hivyo, Serikali iione TAZARA kwa jicho la kipekee. Kwa sababu tunaamini kabisa lengo la ujenzi wa TAZARA ilikuwa ni kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kuelekea nchi za SADC. Kwa namna hiyo na tunafahamu kabisa asilimia 70 ya mizigo inayoingia bandarini inaelekea nchi ya Malawi, Zambia na Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Serikali ilichukue hili kwa kipekee iweze kupitia hiyo sheria na kupitia kama tutaweza kuboresha utendaji kazi wa TAZARA. Tuweze kufikiria ni kwa namna gani tutengeneze bandari kavu katika eneo la Mpemba pale Tunduma. Tunajua kabisa bidhaa nyingi wanaonunua ni watu wa hizi nchi za SADC, kwa nini tusione umuhimu wa kujenga hii bandari kavu pale? Kwa sababu tutakuwa tumerahisisha mambo mengi, kwa sababu barabara zetu hazitaharibika lakini mizigo itafika kwa wakati. Uratibu wa mizigo utakuwa ni kwa haraka kwa sababu itakuwa ipo specifically kwa eneo la watu wa SADC. Kwa hiyo, ipo haja ya kuona Serikali inachukua hatua kwenye ujenzi wa dry port Tunduma pia kwenye utengenezaji wa hiyo meli, hii itachangiza uanzishwaji wa free market katika eneo la Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi pia kuweza kushiriki kuchangia katika mpango huu. Natamani leo nitumie nafasi yangu vizuri kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amefanya kazi nzuri sana ya kuleta fedha nyingi kwenye mikoa yote na hususan kwenye Mkoa wangu wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona ambavyo madarasa mengi yamejengwa, vituo vya afya vingi vimejengwa. Kiukweli ukiangalia unaona kabisa ile ni nguvu ya ziada ambayo Mheshimiwa Rais anastahili pongezi, lakini pia katika barabara tumeona ametoa fedha nyingi kwa majimbo yote ambazo ni fedha nyingi kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kama ni kufanya kazi Mheshimiwa Rais Mama yetu Dkt. Samia anajitahidi sana. Pia, amshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuweza kuanzisha dry port katika Mji wetu wa Tunduma, Mkoa wa Songwe. Tumeona kuna hatua ambazo zinaendelea. Kwa hiyo nisipotumia nafasi hii kumshukuru nitakuwa simtendei haki yeye pamoja na timu yake nzima ambayo wanaratibu suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kama dry port ikijengwa pale Mpemba tutaongeza wateja wengi wanaotumia bandari yetu ya Dar es Salaam lakini pia barabara zetu hazitaharibika. Pia, ajali zinazotokea katika ukanda huu wa barabara ya Tanzam zitapungua sana. Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha ujenzi wa barabara nne katika Mji wa Vwawa, Tunduma ambapo mkandarasi yupo na wanaendelea na utaratibu. Kwa hiyo, hili pia natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natumia nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais, sitaacha kumshukuru kwa ruzuku aliyoweka kwenye mbolea. Bado tuna-appreciate kwamba alitusaidia sisi kama wakulima. Mkoa wa Songwe una wakulima wengi sana. Natumia forum hii pia kumwomba kaka yangu Bashe atusaidie kwenye suala la pembejeo za mbegu na viuatilifu pamoja na viua magugu na viua wadudu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ilikuwa ni kubwa sana na tuliweza mbegu feki nyingi kiasi kwamba katika mikoa hii ambayo inazalisha mahindi wananchi wengi waliingia hasara. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Bashe aangalie ni namna gani ambavyo atafanya kuhakikisha wananchi mwaka huu hawatumii mbegu ambayo ni feki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza kusema kwamba Serikali yetu imekuwa ikiendelea kufanya kazi nzuri, tunafurahi, lakini kumekuwepo na maboma mengi ambayo wananchi wanajitolea kufanya kazi; wanafanya wanayajenga yanachukua muda mrefu kumaliziwa. Nawaomba Mawaziri wetu wenye dhamana ya afya, hususan TAMISEMI watusaidie kuhakikisha maboma haya yanaisha. Yamekuwa ni kero na wananchi wanapoteza ile morale ya kujitolea kujenga maboma mapya katika maeneo mengine. Kwa hiyo, hilo pia namwomba Mheshimiwa kaka yangu Mchengerwa aweze kuliangalia na kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa sijajitendea haki nisipozungumza suala la maadili, shule zetu nyingi hazina walimu wanawake. Nimefanya ziara kwenye Kata 30 katika Mkoa wangu, changamoto niliyoikuta ni shule nyingi za msingi na sekondari walimu hawapo. Mfano mzuri niliukuta katika Shule ya Kanga katika Wilaya ya Songwe. Walimu wapo 22 halafu walimu wanawake wapo wawili na ile shule takwimu inaonyesha mabinti ni wengi kuliko watoto wa kiume. Kwa hiyo, kwa hili pia namuomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Kaka yangu Mchengerwa waangalie namna ya kuwa na distribution nzuri ya walimu wanawake, kama hawapo basi ufanyike mkakati maalum wa kuajiri walimu wanawake ili waweze kusaidia ku-maintain maadili katika shule zetu ambazo zina watoto wa kike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine kabla sijachangia mchango wangu namuomba Dada yangu Ummy, Waziri wa Afya, alinipa miezi sita ya Sera ya Lishe na katika mpango huu niliposoma sijaona sehemu inayoeleza suala la lishe. Namuomba anisaidie suala la lishe liweze kukamilika, Sera ya Lishe ni muhimu kwa Taifa hili kwa sababu hali ya utapiamlo katika nchi hii haijakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi katika mchango wangu ambao nilidhamiria siku ya leo, niongelee masuala yanayohusu fedha zinazoletwa katika maeneo yetu. Tunajua Serikali inajitahidi kutenga fedha nyingi na inajitahidi kutoa maelekezo ya fedha nyingi iende kwenye miradi ya maendeleo. Wanatenga hizo fedha na wao wanaleta hizo fedha kwenye maeneo yetu, tunawashukuru sana. Kwa hili kwa kweli Wizara ya Fedha wamekuwa waaminifu kuleta fedha kwenye maeneo yetu. Nampongeza Mheshimiwa Mwigulu kwa hili wanatutendea haki sisi kama Wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja kujitokeza katika maeneo yetu ni kwamba kumekuwa na usimamizi duni wa hizi fedha kwenye maeneo yetu. Ninarejea kwenye kipengele cha udhibiti wa matumizi ya fedha katika huu mpango ambao Mheshimiwa Waziri ametupatia. Anasema fedha zote kutumika kwa wakati, kumekuwa na miradi ambayo inavuka mwaka wa kwanza, mwaka wa pili, mwaka wa tatu tunamuomba Mheshimiwa Waziri na timu yake waangalie namna njema ya kufanya hii miradi isiweze kuvuka muda mrefu na wawe wanaibainisha tuwe tunaiona ili tujue kwamba ni miradi gani imekuwa sugu haitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachokuja kusikitisha ni kutoa fedha sawa katika maeneo tofauti lakini maeneo mengine miradi inaisha na maeneo mengine miradi haiishi. Maeneo mengine wanaongeza fedha nyingi juu yake wakati maeneo mengine unakuta hawajaongeza hata fedha kidogo. Natamani iwe hivi, kwenye kudhibiti fedha zetu hata ongozeko linaloongezeka liwe na uwiano. Haiwezekani uniambie wewe Halmashauri yako Engineer alikosea estimation kwa kiwango hicho mpaka wewe uwe na ongezeko kubwa namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona nilivyopita kwenye miradi mbalimbali katika ziara yangu. Unakuta shule inajengwa kunakuwa na ongezeko la zaidi ya shilingi milioni 150, sasa unajiuliza hivi hiyo shilingi milioni 150 ina maana kweli Engineer alikosea kwa kiwango hiki? Kwa hiyo na hili namuomba Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ombi maalum kwa hawa Wakaguzi wa Ndani (Internal Auditor), hawa watu wanahitaji kujengewa uwezo wa kina, kwanza ni wachache. Mimi nashauri katika maeneo yetu, Halmashauri zetu, Wakaguzi wa Ndani waongezeke. Mbali ya hivyo watengewe fedha ya kutosha kuweza kuzunguka kwenye hiyo miradi zaidi wapatiwe vifaa vya usafiri ikiwa ni pamoja na magari ili waweze kufika maeneo hayo ya ukaguzi na kuweza kujua value for money ya hela zetu inakuwa ikoje.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia nasema hivi, force account imekuwa ni kichaka cha uharibifu wa fedha zetu. Miradi mingi iliyotekelezwa kwa force account ni dhaifu na fedha nyingi inaharibika.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia asubuhi hii, nina yangu machache ambayo ni ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, natamani kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko, Mheshimiwa Judith Kapinga ambaye ni Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara hii ya Nishati kwa kufanikisha kupata umeme huu wa megawati 235, sisi kama Taifa kwetu ni faraja. Kumekuwa na stabilization ya umeme kwenye Taifa, zile kelele za umeme zimepungua, kwa hiyo, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri. Kwa asilimia 96 ambayo bwawa limefika ni kwamba, zoezi la mgao wa umeme katika nchi hii litaisha kabisa ndani ya muda mfupi, kutakuwa hakuna mgao wa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia natumia nafasi hii kuendelea kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutupatia Chuo cha VETA pamoja na Chuo cha Watu Wenye Ulemavu katika Mkoa wa Songwe, ni faraja kwetu. Tunaomba wadau wote wa vyuo na vyuo vikuu waje kuwekeza katika Mkoa wetu wa Songwe kwani tunahitaji kuendelea kielimu. Kwa hiyo, natumia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais pamoja na Wizara ambayo iliona kwamba, upo umuhimu wa kupeleka vyuo hivi katika Mkoa wa Songwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti ya mwaka jana ya Ofisi ya Waziri Mkuu niliuliza kuhusu suala la Sera ya Lishe, nikaambiwa ndani ya miezi sita tutapata matokeo ya kinachoendelea. Mpaka ninapoongea hivi sasa sijasikia, sijapata ufafanuzi na wala sijaona taarifa yoyote inayoonesha sera hiyo imefikia hatua gani, hata kwenye taarifa hii ambayo imetolewa na Waziri Mkuu haimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kuwa kimya kwenye hii Taarifa ya Waziri Mkuu iliyotolewa hapa Bungeni inaonesha kwamba, katika suala la Sera ya Lishe hakuna kinachoendelea. Kwa hiyo, naomba kupitia Bunge hili, Waziri atakapokuwa ana-wind up aje na majibu ni kwa nini haijaonekana kwenye taarifa hii? Je, inafanyiwa kazi au haifanyiwi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, natamani kutumia nafasi hii pia kuongelea suala la kikokotoo. Tunapoongelea kikokotoo kumekuwa na kelele nyingi sana kwenye jamii, hususani kutoka kwa watumishi. Wengi wame-develop hofu ambayo inawafanya wanapoelekea kustaafu wahisi kama Serikali inawadhulumu. Mimi pia kabla sijapewa mafunzo nilikuwa kama hao wananchi, lakini kwa mafunzo ambayo nimepatiwa kuhusu kikokotoo nimewaza ni wapi, kama Taifa, tunashidwa kuwaelimisha wananchi hususani watumishi kwamba, kikokotoo hiki ni kizuri, kina tija na kinamweka mstaafu katika hali nzuri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilichokiona ni kwamba, Wizara haijawafikia watumishi na kuwaelimisha vizuri kuhusiana na kikokotoo kwa sababu, kwanza fedha ya mkupuo ambayo wanapewa ni ya kutosha. Sasa wanapewa asilimia 33 kutoka asilimia 25 waliyokuwa wanapewa awali, kwangu naona kuna ongezeko la asilimia nane ambayo huenda wananchi hawana ufahamu mzuri wa tofauti ya walichokuwa wanakipata awali na sasa imekaaje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na nilivyoelekezwa, nilivyofundishwa, kwenye mafunzo maalum inaonesha kwamba, mwisho wa mwezi mtumishi huyu ambaye amestaafu anaendelea kupokea kipato ambacho ni karibu na mshahara wake aliokuwa anaupata awali. Kitu ambacho kinawasaidia wastaafu ambao walikuwa wanachoka sana baada ya kustaafu na wengi wanasema walikuwa wanakufa. Kwangu mimi naona kama hali ipo hivi kelele zinatoka wapi? Pia bado kuna fungu la mkupuo kwa familia endapo mstaafu huyu atafariki. Kwa hiyo, kwa hili natamani Wizara iende kutoa elimu hii kwa wananchi, kwa watumishi, ili wajiandae na kustaafu ilhali wakijua baada ya kustaafu watapata faida zipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia kwenye Mifuko ya Hifadhi ambayo ni NSSF na PSSSF bila kuusahau Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi. Kimsingi wanafanya kazi nzuri, wanajitahidi na wanapambana kuhakikisha wanalinda thamani ya fedha kwa kuanzisha miradi ambayo inaendelea kuipatia kipato Mifuko hii, lakini kuna changamoto ndogo ambayo Wizara haina budi kuifanyia kazi. Kwanza ni kuondokana au kuepuka miradi ambayo marejesho yake ya fedha yatachelewa zaidi ya miaka 10. Nasema hivi kwa sababu miradi mingine inayoibuliwa inachukua muda mrefu kurudisha gharama na kuanza kupata faida. Kwa hiyo, namwomba Waziri asaidie, ili miradi isichukue muda mrefu wa marejesho ya thamani ya fedha ambayo inakuwa imewekezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu Kamishna wa Kazi na Mkurugenzi wa OSHA, watu hawa wanafanya kazi nzuri. Ombi langu kwa Waziri ni awasaidie kuongeza ofisi katika mikoa mingine. Tunatambua mahali pa kazi ni sehemu inayopaswa kuwa salama, kazi zipo katika mikoa yote, haiwezekani mkurugenzi akawa anateseka kutoka mkoa mmoja hadi mwingine kuhakikisha kazi inafanyika wakati Serikali ingeweza kutengeneza mazingira rahisi ya ufanyaji kazi. Vivyo hivyo Kamishna wa Kazi naye atengenezewe ofisi katika mikoa mingine na pia apewe vitendea kazi vya kutosha pamoja na watumishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja kuhusu kupeleka fedha kwenye maeneo ambayo Serikali inakuwa imedhamiria. Upo mfano hai, kuna fedha ambayo ilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule fulani katika Mji wetu wa Tunduma, shule ile ina madarasa 36 ambayo yapo na yanahitaji ukarabati. Madarasa 18 yapo yanatumika, lakini Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya kujenga madarasa mengine 10 wakati kuna vyumba vingine 18 vya madarasa ambavyo havitumiki. Sasa nawaza na kujihoji kwamba, hivi Serikali inapopeleka fedha kwenye maeneo yetu, inakuwa imefanya tathmini ya kina ya mahitaji ya watu katika maeneo husika?

Mheshimiwa Naibu Spika, nazungumza hivi kwa sababu, Mheshimiwa Waziri Mkuu katika ziara zake amekuwa mkali sana juu ya matumizi mabaya ya fedha, hata kitendo cha kupeleka fedha ambazo ni kinyume na mahitaji ya eneo husika pia ni matumizi mabaya ya fedha. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie, wanaposambaza fedha kwenye maeneo yetu wazingatie vipaumbele, kama kipaumbele chetu ni ukarabati basi watupatie fedha za ukarabati, kama mahitaji ni madarasa basi watupatie fedha za madarasa, lakini jambo hili la kusambaza hela kienyeji siyo zuri. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu tunategemea usimamizi utaenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia nataka niongelee kuhusu ukatili wa kijinsia. Kwanza natumia nafasi hii kuwapa pole wananchi na wakazi wa Mji wa Tunduma ambao kwa namna moja au nyingine wameathiriwa na vitendo vya ubakaji na ulawiti ambavyo watoto wao wamekuwa wakifanyiwa. Vitendo hivi vimekithiri sana, kiasi kwamba, sisi Wanatunduma, sisi Wanamomba, hatujisikii vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara, Sheria ya Ukatili wa Kijinsia, hususani juu ya ubakaji na ulawiti, ifanyiwe marekebisho ili hawa watu wakose dhamana.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema, ahsante kwa mchango mzuri.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba watu hawa wasipate dhamana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa muda niweze kuchangia. Nitumie nafasi hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwa namna ambavyo anapambana kuweza kuhakikisha analeta fursa mbalimbali katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu na mimi nina yangu machache katika Wizara hii. Jambo kubwa kabla sijaenda kuchangia haya mengine ambayo nimedhamiria, kwanza natamani kuiona Wizara hii inautazama Mkoa wa Songwe kwa namna ya tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Songwe ni Mkoa wa kibiashara, ni Mkoa wa viwanda, ni Mkoa wa uzalishaji na ni Mkoa ambao unazalisha vyakula kwa wingi. Tunazalisha kahawa na madini mbalimbali. Kwa hiyo, natamani kama Wizara wauone kwamba Mkoa wa Songwe ni Mkoa wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niongelee kwa maana ya Mji wa Tunduma kwamba Wizara naona haijafanya kitu kwa Mji wa Tunduma. Nimekuwa naongea hapa mara nyingi kukumbusha namna ambavyo Wizara hii ya Viwanda na Biashara, iweze kuona Mji wa Tunduma kama ni Mji ambao wanaweza kutengeneza wafanyabiashara wakubwa wengi. Pia, wanaweza kutengeneza viwanda vingi kwa sababu ndiyo mji ambao upo kwenye lango la SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri kwa namna ya tofauti na timu yake waende wakafanye research pale. Ni kwa namna gani Mji wa Tunduma unaweza ukawanufaisha kwa kuanzisha viwanda vikubwa? Pia, kwa kuweza kuanzisha biashara kubwa ambazo zinaweza zikahudumia Ukanda wa SADC. Kwa hiyo, ni namna ambayo wao kama Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Wizara ya Mipango, wanaweza wakajipanga kufanya kitu kwa ajili ya Mkoa wa Songwe na hususan kwa Mji wa Tunduma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niungane na wenzangu ambao wameongea kwamba, kama nchi tumeona kumekuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa dola. Tunapoongelea dola, ni kitu ambacho kama Taifa inaweza ikawa ni fursa kwa kuwa na reserve ya kutosha ya hela za kigeni kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mheshimiwa Mbunge ambaye sio mtaalamu sana wa masuala ya kiuchumi kwa maono yangu tu ya kawaida baada ya kusoma taarifa hii nimeona kwamba Wizara kama Wizara hawana malengo au mkakati maalum wa kulinda fedha za kigeni kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini? Hii ndiyo Wizara ambayo inaweza kutusaidia kutunza fedha zetu za ndani kwanza zisiondoke nje. Nilikuwa nasoma mahali hapa katika maandiko mbalimbali ambayo yameandikwa nikaona kwamba, kuna kiwango cha samaki ambacho kinaingizwa nchini. Niliwaza tu hiyo ni sample ya product ambayo nimeiona kwamba ni kitu ambacho kama Watanzania hatupaswi kuagiza. Minofu ya samaki imeingizwa yenye thamani ya dola bilioni 6.24 wanaagiza inaingizwa humu nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo fedha tungetumia minofu iliyomo humu humu nchini. Tuna Maziwa ya kutosha tungeweza kuhifadhi hii fedha na tusiwe na uhaba huo wa fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naenda kwa mazao ya kilimo ambayo yanaingizwa nchini kama vile ngano. Tunawezaje kuagiza ngano wakati hii ni fursa kwa wananchi wetu kuweza kulima na ku-supply kwa viwanda vyetu ambavyo vipo nchini ambavyo vinaagiza hizo ngano? Kwa hiyo, nataka kusema kwamba hii ndiyo Wizara pekee ambayo inaweza kutusaidia kama nchi kuhifadhi fedha za kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kusoma taarifa yao, sijaona wao kwamba wana malengo gani ya ku-balance uwiano wa import na export. Nilikuwa najaribu kuangalia kwa biashara waliyofanya kwa hizi Jumuiya za Ulaya, sisi kama Taifa tuliweza ku-import vitu vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.05, lakini export ikaenda kwenye shilingi bilioni 3,835. Sasa nawaza, inakuwaje tunaweza tuka-exceed; kwamba sisi tu-import zaidi kuliko ku-export?

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara wanafanya mkakati gani wa kuhakikisha kwamba tunakuwa na export nyingi? Kwa sababu tunatengeneza wafanyabiashara, tunatengeneza wajasiriamali wengi na tunatengeneza viwanda. Kama Wizara imejiwekea mkakati wa kutengeneza bidhaa ngapi ambazo ziingie kwenye masoko ya kimataifa? Kwa hiyo, hili nalo sijaliona huku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Wizara watengeneze mpango kazi ambao utaonesha kwamba wana-balance vipi import na export? Pia wanatengeneza wafanyabiashara wangapi ambao wataweza kuingia soko la Kimataifa kwa ku-export product zao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwa Viwanda vya SIDO. Hii Taasisi ya SIDO ni Taasisi ambayo kama Watanzania tunaitegemea. Nilikuwa nasoma katika taarifa hapa, wananiambia eti nchi nzima SIDO wamekuza wajasiriamali watano tu. Sasa nawaza Mkoa wa Mbeya, Songwe, Morogoro na mikoa yote Tanzania nzima, wakatuambia wamekuza wafanyabiashara watano? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naona ni kitu ambacho kama Taifa Wizara haina mkakati maalum wa kuhakikisha wanatengeneza wajasiriamali wengi zaidi ambao watahakikisha wanakua. Mimi nisiseme mengi, ninashukuru kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)