Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Neema Gerald Mwandabila (32 total)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo imeweza kunijibu, lakini kiupekee kabisa nataka nitoe angalizo kwa Serikali kwamba Kituo cha Afya Tunduma asikichukulie kama vituo vingine ambavyo viko nje ya mpaka wa Tunduma kwa maana mahitaji yake yanakuwa ni makubwa zaidi, kwa hiyo anaposema kwamba ataweza kupunguza watumishi Tunduma tena awapeleke kwenye hospitali hiyo inayojengwa naona kama bado changamoto itakuwa kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ninapenda niulize maswali yangu mawili ya nyongeza; ni lini hasa Serikali itaweza kuanzisha huduma katika hii hospitali inayojengwa ambayo ameweza kutuonesha kwamba asilimia 82 ya ujenzi imeshafanikishwa. Kwa hiyo, ninatamani kujua ni lini hasa huduma zitaanza kutolewa pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ninapenda kufahamu mahitaji ya kituo cha afya kulinga na na nature ya watu wa pale tunahitaji madaktari, na madaktari aliyosema nina uhakika ni hao madaktari wawili ambao wanasubiria Hospitali ya Wilaya ianze kufaya kazi.

Sasa basi ninatamani kujua ni lini hasa Serikali itpeleka madaktari na wauguzi wakunga, siyo wahudumu wa afya kama walivyoweza kuanisha kwenye majibu yao, mahitaji yetu ni madaktari na wauguzi wakunga, specifically hapo ninapenda kupata majibu. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumhakikishia Mheshimiwa Mwandabila kwamba Serikali inakichukulia kwa umuhimu wa hali ya juu sana Kituo cha Afya cha Tunduma kwa sababu ya idadi ya wananchi wanaohudumiwa katika kituo kile na ndiyo maana katika maelezo yangu ya msingi nimeeleza namna ambavyo Serikali imepeleka watumishi wengi sana, watumishi 22 wa ziada ukilinganisha na ikama ya mahitaji ya kituo cha afya, na hiyo ni dalili kwamba Serikali inajali na kuthamini sana huduma za Kituo cha Afya cha Tunduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba kwa sababu tunaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Mji wa Tunduma, kwa vyovyote vile, idadi ya wagonjwa watakaotibiwa katika kituo cha afya itapungua na wengine watakwenda kutubiwa katika Hospitali ya Mji wa Tunduma itakapokamilika. Kwa hiyo, ile idadi ya wagonjwa ambayo itaondoka Kituo cha Afya cha Tunduma itakwenda kuhudumiwa katika hospitali ya mji na watumishi hawa waliopo. Lakini pia Serikali itakwenda kuajiri watumishi wengine kama ambavyo mpangio upo katika mwaka wa fedha ujao ili tuweze kuongeza watumishi katika hospitali ile ya mji lakini pia katika Kituo cha Afya cha Tundma.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Hospitali hii ya Mji wa Tunduma inayojengwa inatarajia kuanza huduma za awali za OPD ifikapo tarehe 27 Aprili, 2021 ili wananchi wetu waanze kupata huduma za awali za OPD wakati shughuli za umaliziaji na ujenzi wa miundombinu mingine inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza japo majibu walionipa angalau yanaridisha.

Swali la kwanza, natamani kufahamu; kwa kuwa magereza wao wamekiri bado uwezo wa kulisha mahabusu na wafungwa ni mgumu, upo kwa asilimia 54. Je, hawaoni sasa ipo haja ya hawa mahabusu kuweza kushirikishwa kuzalisha chakula chao tu kwa sababu maandiko yanasema kila mtu atakula kwa jasho lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili natamani kufahamu; tunafahamu kabisa Magereza changamoto ya magodoro ni kubwa sana. Katika changamoto hiyo, Serikali inawajibika kuhakikisha magodoro yanakuwepo kule, lakini hali bado ni ngumu; na tunafahamu kuna taasisi nyingi sana zinazokuwa zinahitaji magodoro kama shule na Serikali haiwapatii:-

Je, Serikali haioni iko haja sasa ya mahabusu au wafungwa wote wanaokuwa wanafungwa wakawa na kigezo cha kwenda na magodoro yao ili kuweza kupunguza changamoto ile kwa sababu sio wote wanashindwa kuwa na godoro hilo kuliko kuiongezea Serikali mzigo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kanuni au Sheria, hakuna eneo ambalo linakataza kwamba watu kuingia na vitu wanavyovitaka katika Magereza, lakini sasa sababu mbili ndizo ambazo zinatufanya mpaka tufike hatua ya kusema kwamba haiwezekani kila mtu aingie na kitu chake Gerezani. Sababu ya kwanza, moja ni busara ya Jeshi la Magereza kama Jeshi la Magereza. La pili, ni sababu za kiusalama.

Mheshimiwa Spika, unapochukua kitu ukakiingiza kwenye Magereza, maana yake kinaweza kikachomekwa kitu kingine ndani yake ambacho kinaweza kikaja kuwadhuru wengine. Ndiyo maana hata ukifika wakati ukitaka kuleta chakula au dawa au kitu kingine, lazima tukithibitishe tukihakikishe na tujue kwamba hiki kina usalama kwako, kwetu tunaokipokea na kwa yule ambaye anakwenda kukitumia. Kwa hiyo, suala la kila mtu aingie na godoro lake, pazito kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine tunaweza tukajikuta tunatengeza tabaka kwamba kuna mtu anaweza kuingia na godoro lake na mwingine akashindwa. Kwa nini sasa na mahabusu nao wasishiriki katika shughuli za uzalishaji? Mahabusu na wafungwa wote ni binadamu, lakini hata akiitwa mfungwa, maana yake kesi yake imeshakuwa held, kwa maana ya kwamba imeshahukumiwa aende jela miaka mingapi? Kwa hiyo, yule tunayo sababu ya kumwambia sasa nenda kalime, nenda kazalishe kwa ajili ya kutengeneza mazingira ya gereza. Sasa huyu mahabusu bado kesi yake haijahukumiwa kwa hiyo, yupo pale. Kusema tumchukue tukamfanyishe kazi, tukamlimishe bado kidogo busara hiyo hatujafikia. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona ili niweze kuuliza swali langu la nyongeza. Tunafahamu kabisa mradi wa STAMICO ni mradi ambao una maslahi kwa wananchi wa Kyela, Rungwe na Ileje. Ileje iko Mkoa wa Songwe. Ningependa kuona mradi huu unafanya kazi mapema sana.

Swali langu liko hapa, majengo yaliyojengwa eneo lile ni majengo mazuri ambayo ni kwa ajili ya ofisi na makazi ya watumishi. Makazi yale, siku hadi siku yameendelea kuharibika. Sasa natamani kujua, je, ni nini dhamira ya Serikali katika kuendeleza haya majengo yasiendelee kuharibika na kufanyika magofu huku wakati tukiendelea kusubiri huo mradi kufanya kazi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge, kuhusu ukarabati wa majengo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema STAMICO imeanza ukarabati wa mgodi wa chini kama sehemu ya maandalizi na ili tuweze kuanza mgodi ni pamoja na maandalizi ya nyumba za staff. Kwa hiyo, nipende kumhakikishia Mbunge tu kwamba jambo hili pia la ukarabati wa nyumba kama maandalizi ya mahali ambapo staff watakaoingia katika mgodi pia litakwenda kutekelezwa na tutawaagiza STAMICO kwamba wafanye mambo haya kwa pamoja ili pia tusiendelee kupata hasara ya nyumba ambazo hatimaye tunaweza tukahitaji kujenga nyumba mpya kumbe tungeweza kuzihifadhi hizi kwa ajili ya mkakati wa baadaye.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduma ni sehemu mojawapo ambayo tunapata changamoto sana ya kuwa na idadi kubwa ya watoto waliotelekezwa na mara nyingi watoto hawa waliotelekezwa huwa wanakimbilia Ofisi ya Ustawi wa Jamii. Wanapofikiwa kule, Afisa wa Ustawi wa Jamii anapaswa kuwahudumia kwa huduma zote yule mtoto anazokuwa anahitaji mpaka atakapopata kituo cha kumpeleka. Lakini changamoto wanayoipata ni kwamba hawana fedha za kuwahudumia watoto hawa.

Je, ni lini Serikali itakuja na fungu maalum kwa ajili ya Maafisa wa Ustawi wa Jamii kuweza kuwahudumia watoto wao. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila; ni kweli, Serikali inatambua kwamba bado hatujawekeza vya kutosha kwenye eneo hilo kuwawezesha Maafisa Ustawi wa Jamii wetu waweze kufanya kazi hizi. Naomba niahidi kwamba tutafanya tathmini tuone ili kwenye kipindi kijacho cha bajeti tuweze kuanzisha namna gani ya kuwawezesha hawa Maafisa Ustawi wa Jamii. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsate kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Wilaya yetu ya Momba ina Halmashauri mbili. Halmashauri ya Mji wa Tunduma na Halmashauri ya Wilaya Momba. Makao Makuu yapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba sehemu ambayo ni mbali kutoka Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Katika hali ya usalama Tunduma ina hali hatarishi zaidi kuliko Wilaya ya Momba nilitamani kufahamu ni lini Serikali itaweka Wilaya mbili za kipolisi katika Wilaya ya Momba yaani Mji wa Tunduma pamoja na Halmashauri ya Momba. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu kwa kifupi sana swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, suala la uwekaji wa Vituo vya Polisi au uwekaji wa huduma hizi za ulinzi na usalama zinategemea mambo mengi sana, ukiwemo utaratibu wa kuangalia kwanza mahitaji ya eneo hilo, kwa sababu inawezekana kuna mahali vituo vipo karibu na huduma zipo karibu, lakini kikubwa ni kwamba nimwambie tutakwenda tukakague ili tuone kama tutaona kuna haja ya kufanya hivyo basi tutaweka. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kama ilivyoelezwa hapo awali kwamba, kumekuwa na ongezeko la matatizo ya akili na tunafahamu ongezeko la matatizo ya akili ni pamoja na kukosekana kwa watu wa ushauri na unasihi. Je, ni nini mkakati wa Serikali katika kuhakikisha inaongeza Maafisa Ustawi wa Jamii mpaka ngazi ya kata? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge alivyosema. Tunachukua hilo wazo, lakini katika sehemu nyingi kuna Maafisa Ustawi wa Jamii, bahati mbaya tu tukienda kwenye wilaya zetu wamepewa kufanya kazi nyingine, unakuta wengine ni Watendaji wa Vijiji au wengine wanafanya shughuli nyingine ambazo sio za ustawi wa jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kikubwa kwanza tutaenda kusimamia waliopo kwanza wafanye kazi ambayo walitakiwa kuifanya na wawezeshwe kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa sababu tumefika kwenye level ya mkoa kupeleka wataalam hawa wanaoshughulikia masuala ya akili, basi tutashusha kwenye wilaya ikiwezekana kwenye vituo vya afya jinsi bajeti itakavyoruhusu. Ahsante sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa swali la nyongeza. Ni wazi Wizara hii imekuwa ikifanya kazi kubwa kuhakikisha huduma ya maji inafika katika maeneo mengi. Katika maeneo ya Majiji, Manispaa na Miji kumekuwa na changamoto ya milipuko ya moto. Ambapo ukiuliza unaambiwa visima vya maji ambavyo vitajaza kwenye magari maji kwa wepesi havipo. Swali langu nilitamani kufahamu ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha katika project, kila mradi unaokuwa unaandaliwa kunakuwa na setting ya visima au matanki ambayo yatajaza maji kwa haraka katika magari ya zimamoto? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila, kutoka Songwe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili swali aliloliuliza ni utekelezaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani na hawa wenzetu wa Zimamoto wanaufahamu wajibu wao. Taasisi zote za Serikali ambazo zinahitaji huduma ya maji wanafahamu wanapaswa kufika katika ofisi zetu kwenye mikoa yao. Ili waweze kuongea na wataalam wetu na kuona njia njema ya kutumia ili waweze kupata huduma ya maji katika ofisi zao. Taasisi zote za Umma zinapeleka maji kwa gharama zao na pale inapobidi kupata huduma ya kiupendeleo basi huwa wanafika na kuweza kueleza tatizo husika. Hivyo, wenzetu wa Zimamoto wanafahamu wapi wafike ili waweze kufanya vyema. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Nitakuwa na maswali mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoelekea, elimu ya Vyuo na Vyuo Vikuu inakuwa ni hitaji la msingi kwa wananchi na tunafahamu kabisa Mikoa ya pembezoni imekuwa inapata changamoto hiyo ya kupata huduma ya Vyuo na Vyuo Vikuu. Tunachofahamu Watanzania wengi ni masikini, hawawezi kwenda maeneo hayo wote na kupata hiyo, lakini tuna watumishi wetu wengi ambao wanahitaji kuendeleza ujuzi wao:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, ni kwa namna gani Serikali isione umuhimu wa kuwa na mgawanyo sawa (equal distribution) wa vyuo kwa maeneo yote? Kwa Mikoa yetu kumekuwa na changamoto ya kwanza vyuo vyote vinaenda katika Makao Makuu ya Kanda, lakini kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi, Serikali inao uwezo wa kugawanya kwamba chuo hiki kijengwe sehemu fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nakiona, ni lini Serikali itaweza kuendeleza Chuo cha Miyunga (DIT) kiweze kutoa Shahada katika eneo lile? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mwandabila kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika jibu la msingi ni kwamba Vyuo vyetu Vikuu vinaanzishwa au kupelekwa kwenye maeneo kulingana na uhitaji. Nimkahikishie Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba ipo miongozo ambayo imewekwa na Serikali na inatekelezwa na wenzetu wa TCU kwa niaba ya Wizara ya Elimu pindi wahitaji au taasisi zinapohitaji kufungua vyuo kwenye maeneo mbalimbali kuonesha maeneo yapi yenye uhitaji wa namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hili, kabla ya maeneo haya havijafunguliwa vyuo hivi, mara nyingi sana tunafanya assessment ambayo inaitwa need assessment ya kuhakikisha kwamba kweli tukipeleka chuo kwenye maeneo hayo, uhitaji huo utapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili, amezungumzia tawi letu la Miyunga kutoa Shahada. Chuo hiki cha Miyunga au Campus hii ya Miyunga ya DIT ilianzishwa mwaka 2017 ikiwa na malengo mahsusi. Malengo yake makuu ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunapata mafundi stadi na mafundi sanifu katika eneo la Uhandisi pamoja na eneo la uchimbaji wa madini. Masomo yanayotolewa hapa ni yale ya ufundi pamoja na ufundi stadi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anazungumzia kutoa Shahada, lakini tunafahamu kwamba Taifa letu bado lina uhitaji mkubwa sana wa kada hizi za kati za ufundi pamoja ufundi sanifu. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba dhamira ya Serikali ni kuondoa changamoto ya mafundi sanifu pamoja na mafundi stadi wa kawaida. Kwa hiyo, kwa sasa kwa mwelekeo wetu na dhamira yetu ya Chuo kile ni kuhakikisha kwamba inakwenda kutoa kada hizo na kada ya Shahada bado tutategemea vyuo vingine vilivyopo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kata ya Mlowo ni moja kati ya kata kubwa sana katika Mkoa wetu wa Songwe: Ni hatua zipi Serikali imefikia katika mchakato wa kuigawa kata hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Kata ya Mlowo ni moja ya kata kubwa, lakini utaratibu ni kwamba, endeleeni na taratibu za kuwasilisha maombi kwa mujibu wa taratibu za ugawaji wa maeneo ya utawala. Hata hivyo kipaumbele kwa sasa ni kuhakikisha tunaboresha miundombinu kwenye kata zilizopo kabla hatujakwenda kugawa kata hizi nyingine. Ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa mchakato uliopo unapoteza haki ya watu wengi kwa kutokupata haki zao kwa wakati, lakini wakati mwingine kwa watu wengine kushindwa kurudi Mahakamani kwa hofu na woga: Je, ni lini Serikali itakuja na sheria ambayo inatoa haki kwa wakati huo huo wa hukumu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia swali la pili; kumekuwa na utaratibu kwa watu kufunguliwa kesi baadaye kesi hizo zinafutwa, anafunguliwa kesi nyingine mbadala; je, ni vigezo gani vinatumika kumbadilishia mtu kesi kutoka ile kesi ya awali kuja kesi ya pili? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kufanya marekebisho madogo ya sheria kwenye eneo hili tunalichukua na tunakwenda kulifanyia mchakato ili tuone kama kuna sababu zozote za kufanya hivyo na Bunge lako Tukufu litajulishwa.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mabadiliko ya kesi wakati umeshitakiwa kwa kosa hili na baadaye unapelekwa kwenye kosa lingine, hilo linategemea sana mwenendo wa upelelezi ambao unaweza ukabaini uhusiano wa tukio lile na tukio lingine ambalo linakupeleka kwenye mashtaka mapya. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wanawake ni kundi maalum ambalo linatakiwa kuwezeshwa na kutambuliwa kisheria katika sheria zetu mbalimbali, je, ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha wanawake wanaingia kisheria kwenye hii Sheria ya Madini.

Mheshimiwa Spika, pili, Songwe pia ni moja ya mikoa maarufu sana kwa uzalishaji wa madini; je, ni lini Serikali itakuja kuwapatia wanawake wa Mkoa wa Songwe mafunzo juu ya uchimbaji wa madini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la kwanza, Serikali inawatambua wanawake kipekee kabisa, siyo kama kundi maalum bali kama wadau muhimu katika sekta hii ya uchimbaji madini, na ndiyo maana tumeendelea kuwashirikisha wanawake katika mafunzo mbalimbali. Wizara imeendelea kuwafundisha faida za kushiriki katika uchimbaji wa madini, na imewahamasisha wajiunge kwenye vikundi ambavyo mpaka sasa hivi Tanzania tuna zaidi ya vikundi 20 vya wachimbaji wanawake na hata kule Songwe pia tumeendelea kuhamasisha na wapo wachimbaji wanawake wasiopungua 15.

Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili, Wizara ina mkakati maalum wa kutoa mafunzo nchi nzima na baada ya Bunge hili taasisi zetu za GST, Tume ya Madini na STAMICO, wamepanga kwenda kutoa mafunzo katika Mkoa wa Songwe.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, Neema Mwandabila.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mji wa Tunduma upo mpakani na kituo kilichopo pale hakina hadhi ya kuweza kuhudumia katika eneo lile; wahalifu ni wengi kiasi kwamba kinalemewa.

Ni lini Serikali itaona umuhimu wa kujenga kituo cha chenye hadhi ya Wilaya katika eneo la Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu hivi majuzi kwamba Wilaya zote ambazo hazina vituo vya polisi ni mpango wa wizara kuanza ujenzi kwenye maeneo hayo. Kwa hiyo, eneo analolitaja hili ni moja ya maeneo ambayo yatazingatiwa katika ujenzi wa vituo vya polisi.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongea.

Mheshimiwa Spika, tunafahamu Mkoa wa Songwe ni Mkoa Mchanga na una uhitaji wa stendi kuu ya mkoa. Serikali imefikia hatua gani katika kuhakikisha ujenzi wa stendi hii unakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilikwishatoa maelekezo na utaratibu wa mikoa yote na halmashauri zote ambazo zina uhitaji wa miundombinu ya stendi kuandaa maandiko pamoja na kufanya tathmini ili kuziwasilisha Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya kuwasilisha Wizara ya Fedha na Mipango ili kuona kama inakidhi vigezo vya kuwa miradi ya kimkakati yatafutiwe fedha lakini kama hayakidhi basi kupitia vyanzo vingine vituo hivyo viweze kujengwa. Kwa hiyo naomba nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalifanyia kazi suala la stendi ya Mkoa wa Songwe na utekelezaji utafanyika, ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, barabara ya Tanzam ni muhimu sana na imekuwa magari ya mafuta yanawaka moto na Mkoa wa Songwe hatuna gari la zimamoto. Ni lini Serikali italeta gari ya zimamoto katika Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itapatia Songwe; tumeweka kwenye bajeti katika magari 12 yatakayonunuliwa mwaka huu mikoa isiyokuwa na magari kabisa ikiwemo Songwe itapata gari hilo, ahsante.
NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kwamba kuna uzalishaji holela wa miche hii ya maparachichi na katika mikoa inayolima parachichi, Songwe pia ni mkoa mmoja kati ya mikoa inayolima parachichi: Ni nini mkakati wa utoaji elimu kwa wananchi na wakulima ili waweze kuepukana na hawa matapeli, wazalishaji wa hizi mbegu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kupitia mwongozo ambao tutautoa, utatoa mfumo mzima wa upatikanaji wa miche bora na yenye kuleta tija kwa wakulima wa parachichi na hivyo itaondoa changamoto iliyopo hivi sasa ambapo katika baadhi ya maeneo kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, kuna chongomoto ya upatikana wa miche bora ya parachichi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kupitia mwongozo huu wa TOSCI, maana yake utakuwa ndiyo mwongozo utakaomfanya mkulima yeyote wa Tanzania ambaye anataka kulima parachichi ataufuata na itakuwa ni sehemu salama kwake kwa sababu ni taasisi ya Serikali ambayo itafanya kazi hii ya kuhakikisha kwamba wakulima wote wanapata miche bora.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Wilaya ya Ileje hivi karibuni tumeona namna gani maafa yamekuwa yakitokea kutokana na maporomoko yanayotokea katika barabara ya Ikuti, Sange, Katengele, Kafule mpaka Ikinga. Nilitamani kufahamu ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha barabara hizi zinajengwa kwa kiwango cha lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara alizozitaja za kuanzia Isongole, Ibungu, Katengele hadi Kimo ambayo inaunganisha Ileje na Wilaya ya Rungwe; lakini pia barabara za Isongole, Ibungu, Malangali, Ikinga hadi Kasumulu zinazounganisha Wilaya ya Ileje na Kyela ni barabara ambazo zinapita kwenye miinuko na ni kweli kulitokea maporomoko makubwa sasa mimi mwenyewe nilienda kwasababu zilikuwa zimefunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kinachoendelea sasa hivi ni kwamba ni kuzifanyia usanifu wa kina barabara ya Isongole, Ibungu, Malangali, Ikinga hadi Kasumulu ili kufanya maandalizi kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Lakini hatua ambazo zimechukuliwa kwa sasa ni kuondoa vile vifusi ili barabara ziweze kufunguka maana yake zilikuwa zimefungwa na nisema tu katika haya maporomoko tulipoteza watu watano baada ya kutokea land slide kwa hiyo unaweza ukaona lakini barabara ya kutoka Ibungu kwenda Tukuyu tutaainisha maeneo korofi ili yaweze kufanyiwa matengenezo maalum na barabara hiyo iweze kupitika kwa kipindi chote cha mwaka, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka kufahamu ni lini Serikali itaipatia Kampuni ya Peak Resources leseni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba utaratibu wa kupata leseni za madini uko katika mfumo wa kieletroniki na mfumo huo unafikika kwa njia ya kimtandao. Baada ya mtu kuingia kwenye mtandao na akaomba leseni utaratibu mzima wa jinsi ya kujaza fomu, ada zinazohitajika unalipiwa kimtandao na kwa kawaida kama mifumo iko sawa na hakuna break down kwenye system ndani ya wiki, mbili leseni huwa zinatoka, lakini kama kuna changamoto kwenye leseni yoyote, Ofisi yetu ya Madini iko wazi saa zote na tuko tayari kutoa ushirikiano ili leseni anayoisemea iweze kupata.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninashukuru kwa majibu mazuri lakini kuna changamoto ambayo ipo.

Mheshimiwa Spika, hii barabara tunayoiongelea hapa ni barabara ambayo ni ahadi ya Hayati Mheshimiwa Rais Magufuli na pia kumekuwa na barabara nyingine ya Chapwa, Chindi, Msangano ambayo hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja Songwe tarehe 06 Julai, 2020. Ninataka kufahamu kwa nini ahadi za Viongozi hazitekelezeki kwa wakati?

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto nyingine ambayo ipo ya ujenzi hafifu wa barabara za lami kwa TARURA. Ninataka kufahamu ni kwa nini barabara zao haziwi na ubora, mfano mzuri uko katika Jiji lako la Mbeya utaona barabara ya Kabwe – Isanga, barabara ya Mafiati - Airport, barabara ile ya kutoka njiapanda ya Ilonda kwenda Isyesye ni barabara zinazoharibika kabla ya muda.

Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu ni kwa nini barabara zao zinakuwa hazina ubora? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi zote za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji wake na Serikali imekuwa ikitekeleza ahadi za viongozi kwa awamu kwa sababu ziko nyingi, kwa hiyo kadri ya fedha zinavyopatikana ahadi zile zinatekelezwa. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba ahadi hii ya Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu ni kipaumbele na Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji. Ndiyo maana katika bajeti ijayo itatenga Bilioni Moja na Milioni Mia Tano kwa ajili ya kuanza utekelezaji huo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu barabara za lami za TARURA barabara zetu za lami za kipindi cha nyuma kabla ya 2022 zilikuwa zinajengwa kwa maana ya kubeba uzito wa chini ya tani 10 hadi 15, baada ya kuona siyo rahisi ku-control magari yenye uzito mkubwa Serikali kupitia TARURA tumeborsha sasa tunakwenda tani 30 na kuendelea. Kwa hiyo sababu ya kuonekana barabara zile zilikuwa ni dhaifu ni kwa sababu zilikuwa zinajengwa kwa kiwango cha tani 10 lakini magari mazito zaidi yaliweza kupita, tunaamini sasa hatutakuwa na changamoto hiyo kwa sababu tumeboresha mfumo huo. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi ya maswali ya nyongeza. Nitakuwa na maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali haina utaratibu maalum wa ulipaji wa posho kwa hawa Wenyeviti wa Mitaa, Vitongoji na Vijiji na wamejitengenezea utaratibu wa kujipatia fedha kupitia mihuri yao na uuzaji wa viwanja kitu ambacho kinaleta migogoro mingi sana kwenye jamii na kaadhia kubwa kwenye jamii na urasimu mkubwa.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwa na utaratibu maalum wa kuwa na posho ya madaraka kwa viongozi hawa wa ngazi ya mitaa, vijiji na vitongoji? (Makofi)

Swali la pili, Wenyeviti hawa wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji pamoja na Madiwani wamekuwa na dhamana kubwa sana ya usimamizi wa miradi ya Serikali kwenye maeneo yao, lakini mpaka leo hawana posho ya usimamizi wa miradi.

Je, nini kauli ya Serikali kuhakikisha kunakuwa na posho ya usimamizi wa miradi kwenye maeneo yao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwandabila.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza la Serikali haina utaratibu maalum na ni nini kauli ya Serikali kuweka utaratibu huo. Kama nilivyokwishasema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba kwa mujibu wa Sheria ile ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura Namba 290, posho hizi zinatakiwa zilipwe kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri husika na ndiyo maana Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuziimarisha hizi Halmashauri zetu kwa kuwapa miradi ya kimkakati kuwajengea vyanzo vya mapato mbalimbali ambavyo vitaongezea nguvu kuweza kulipa posho hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikienda kwenye swali lake la pili ya usimamizi wa miradi. Ni kweli Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji, Mitaa wanafanya kazi nzuri katika kusimamia miradi, hasa miradi mingi ambayo kwa sasa tumeona Taifa letu Mheshimiwa Rais amemwaga miradi katika Sekta mbalimbali. Nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kulileta hili hapa na tunalichukua kama Serikali kwa sababu lina budget implication na pale ambapo tutaona Serikali ina uwezo wa kuweka kwenye bajeti zake tutaweka lakini kwa sasa bado tutaendelea na utaratibu ule kama sheria inavyotaka ile ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura Namba 290.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na ucheleweshaji wa ukamilishaji wa miradi mingi ya kimkakati ambayo inakuwa imeandaliwa na Serikali. Swali la kwanza; nataka kufahamu ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha miradi hii ya kimkakati inaisha kwa wakati? Mfano mzuri ni Mradi wa Chumvi, Momba, mpaka leo haupelekewi fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nataka pia, kufahamu, kwa kuwa, kumekuwa na miradi mingi ambayo inaibuliwa ambayo inatumia fedha nyingi za Serikali na haiishi kwa wakati na mingine imekuwa na poor designing na allocation ya miradi kwa hiyo, pesa nyingi zinaenda zinakuwa hazileti tija kwa wakati. Ni nini mkakati wa Serikali wa kupunguza hasara inayotokana na miradi hiyo ambayo inakuwa imebuniwa chini ya kiwango? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Miradi mingi inayotekelezwa na Serikali ni kweli mingine inaweza kuwa na changamoto katika utekelezaji wake kutokana na sababu mbalimbali, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, miradi ambayo imeshawekewa mikakati maalum na ikatengewa fedha kwa wakati husika, tunatekeleza kwa wakati. Pale kunapokuwa na changamoto basi zinakuwa ni zile ambazo ziko nje ya uwezo ambao tumeupanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mbunge ametoa mfano wa Mradi wa Chumvi, Momba ni kwamba, huu ulibuniwa na Halmashauri, lakini na sisi kama Serikali Kuu tutaweka fedha hapo kama tulivyosema hapo awali, ili waweze kutekeleza mradi huo, lakini kwenye miradi mingine ambayo inatekelezwa kwa muda mrefu, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeshatoa maelekezo kwamba, miradi ambayo imewekwa kwenye mipango lazima tuikamilishe kulingana na wakati na fedha nyingi zitatolewa kadiri ambavyo Serikali inapata, ili kuhakikisha tunaondokana na ucheleweshaji katika miradi husika, nakushukuru.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ujenzi wa hostel unahitaji miundombinu ya maji na shule nyingi hazina maji, kwa mfano Shule ya Ndugu iliyopo Mbozi. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha maji yanakuwepo kwenye shule zote za hostel? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, ni mkakati wa Serikali kuhakikisha shule zote zinazojengwa ambazo ni za bweni zinakuwa na maji. Ndiyo maana tunasisitiza coordination kati ya taasisi zote za Serikali katika maeneo husika. Pale ambapo shule inajengwa, Mkurugenzi wa Halmashauri afanye kazi kwa karibu na wenzetu wa RUWASA kwa ajili ya kuhakikisha miundombinu ya maji inafika karibu.

Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya alikotaja Mheshimiwa Neema Mwandabila kuhakikisha kwamba anawasiliana na wenzetu wa RUWASA kuvuta maji katika shule hii ambayo maji bado hayajafika.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu ya Serikali ni mazuri na imeonesha kwamba sheria ipo, lakini ukweli ni kwamba utekelezaji wa sheria hii umekuwa ni hafifu sana. Pia kama hivyo ndivyo, Watanzania wengi wamekuwa wakiathirika na utekelezaji huu hafifu wa hii sheria, kitu ambacho kinawafanya waathirike kisaikolojia, kijamii na hata kiuchumi. Vilevile wanapotoka na kuja mtaani baadaye watu hawa wanakua wamepoteza uelekeo sana lakini tunajua utekelezaji huu hafifu wa hii Sheria umeipa mzigo mkubwa sana Serikali kwa kuwahudumia watu ambao wanakaa muda mrefu rumande. Kitu ambacho tulivyofanya ziara mbalimbali tumeona kabisa kuna watuhumiwa wengi…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Neema, uliza swali.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi wengi wako gerezani kwa zaidi ya miaka 15. Swali la kwanza; je, Serikali ina mkakati gani wa kuwalipa fidia watuhumiwa wote waliokaa mahabusu muda mrefu na kushinda kesi hizo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nataka kufahamu ni nini kauli ya Serikali katika kufuta kesi zote za watuhumiwa waliokaa zaidi ya miaka mitano mahabusu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Naomba sasa nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Neema Gerald, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sio kweli kwamba haya tunayoongea hapa hayatekelezeki, ndio maana ukiangalia kwenye takwimu zetu za masijala za mahakama hadi jana tarehe 29/5/2023 mashauri ni 1,863 lakini backlogs ambazo hazijafanyiwa kazi ni asilimia nne tu. Hapa maana yake ni nini? Maana yake Mahakama imekuwa ikizisikiliza kesi hizi na zimekuwa zikihukumiwa na kuondoka na sasa katika mahakama zetu hakuna kesi ambayo mtuhumiwa yuko mahabusu mpaka sasa zaidi ya miaka mitano hajahudumiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumshukuru Mheshimiwa Rais, amekuwa akiboresha mahakama zetu, amekuwa akiteua Majaji, amekuwa akitoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama Kuu na mwaka huu wa fedha tunakwenda kujenga Mahakama za Mikoa zaidi ya 14 ili Majaji hawa wakasikilize kesi hizi. Kwa hiyo, naomba nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba kwenye Mahakama kesi hizi zinasikilizwa na kasi imeongezeka ndio maana backlogs zimebaki asilimia nne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, anataka kufahamu kama watu hawa waliokaa zaidi ya miaka mitano wanaweza wakafidiwa. Taratibu za kisheria na principles za kesi kwamba pale ambapo unaona kwamba mashtaka haya yamekamilika na unaona ulibambikiziwa kesi na imechukua muda mrefu unaweza kurudi Mahakamai kufungua kesi ya madai.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nilitaka tu kusema kwamba, pamoja na kuchimba miamba hiyo, barabara hiyo bado magari hayawezi kupanda. Kwa hiyo, pamoja na kufanya jitihada zote hizo wanapaswa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha magari yanapanda katika ule mlima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali yangu mawili ya nyongeza ambayo nilitaka Mheshimiwa Waziri aweze kunijibu. Kuna Barabara ya Kanga – Ifwekenya haijalimwa muda mrefu. Nilitaka kufahamu ni lini Serikali itailima barabara hii na kuiweka kuwa kwenye kiwango cha kokoto?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Barabara ya Mlowo – NAFCO – Magamba ambayo inaunganisha Wilaya ya Songwe na Makao Makuu ya Mkoa. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha barabara hii inaweza kupitika muda wote na kutengenezwa kiwango cha lami ili iweze kuunganisha Mkoa wa Songwe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwandabila, la kwanza juu ya hii Barabara ya Kanga hadi Ifwekenya. Barabara hii ina urefu wa kilometa 20.4 na tayari Serikali kutoka mwaka wa fedha 2021/2022 ilianza kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa maeneo korofi ya barabara hii. Mwaka wa fedha huo nilioutaja, Serikali ilitenga Shilingi milioni 250 kwa ajili ya ukarabati na hivi sasa kuna fedha nyingine katika mwaka wa fedha tunaomaliza, ilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa kilometa saba kwa barabara hii ya Kanga kwenda Ifwekenya. Mwaka wa fedha tunaoenda kuanza Julai mosi 2023/2025 kuna Shilingi milioni 60 ambayo imetengwa kwa ajili ya ukarabati wa barabara hii. Serikali itaendelea kukarabati barabara hii kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha kuhakikisha kwamba huduma kwa wananchi zinapatikana muda wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili kuhusu barabara hii ya Mlowo – NAFCO, nikiri kwamba ni barabara muhimu sana ambayo inaunganisha Wilaya ya Songwe na Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe pale Mlowo. Barabara hii imetengewa fedha katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida. Kwa sababu barabara hii pia na yenyewe haipo katika kiwango cha changarawe, kwa hiyo, katika mwaka wa fedha unaoanza wataanza ukarabati katika maeneo korofi kuweka changarawe badala tu ya kuwa wameilima na greda, wataanza kuweka kifusi katika maeneo korofi na tutaendelea kuitengea fedha kadiri ya miaka ya fedha inavyokwenda na upatikanaji wake.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba fedha za wafanyakazi zinaweka uwekezaji ambao unaendelea, yaani unafanyika uwekezaji mfano kujenga majengo ambayo yanaongeza kipato kwenye Vyama vya Wafanyakazi. Ninatamani kufahamu.

Ni lini Serikali itakuja na sheria ambayo inampa haki mwanachama yule kuweza kupata gawio kwa fedha zinazopatikanika kwa uwekezaji huo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Nataka kufahamu, kumekuwa na malalamiko mengi ya walimu kuhusiana na kulazimishwa kuingia kwenye vyama viwili viwili vya wafanyakazi: Ni nini kauli ya Serikali kuhakikisha kwamba kujiunga na uanachama wa Vyama vya Wafanyakazi ni hiari ili kusikuwepo na huko kulazimishana kuingia kwenye vyama viwili viwili hususan kwa walimu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, napenda nimjibu Mheshimiwa Neema Gelard Mwandabila na nimpongeze kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini kwenye eneo hili la uwekezaji nimefafanua vizuri na sheria ipo ambayo inaviruhusu vyama hivi vya wafanyakazi, pia zipo kanuni ambazo zinawaongoza katika vyama vya kwa misingi ya katiba walizojiwekea. Kwa hiyo, nichukue tu kama maoni katika eneo hili, nitaonana naye baada ya hapa ili tuweze kuzungumza zaidi kuona nini hasa alimaanisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile amesema kwamba wanachama wanalazimishwa kujiunga. Niseme kwamba vyama hivi ni vya hiari, lakini Katiba zao ndiyo ambazo zinawabana kwamba pengine ujiunge au ukijiunga atanufaika na nini na kipi? Kwa hiyo, siyo kwamba ni lazima kwamba lazima sasa ujiunge kwenye chama hiki. Hapana, lakini pia nitakutana naye tufahamiane zaidi ili tuone namna ya kuliweka vizuri, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ningependa niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tunafahamu katika shule zetu nyingi za msingi miundombinu muhimu kama maji na umeme haipo. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha miundombinu hii inapewa kipaumbele katika shule zetu hizi hususan katika Mkoa wangu wa Songwe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; natamani kufahamu, huko kwetu shule nyingi za msingi zimekuwa hazina vyoo, hususan kwa Mkoa wangu wa Songwe na hasa zaidi katika Wilaya yangu ya Momba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Gerald Mwandabila, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baadhi ya miundombinu ya maji pamoja na umeme ambayo tunayo ina changamoto kubwa. Moja ya Sera ya Serikali ni kuhakikisha sasa hivi kwenye taasisi zote hizo za kielimu zinapatiwa umeme pamoja na maji. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hilo lipo katika mpango wa Serikali na ndio maana sasa hivi unaona katika usambazaji wa umeme wa REA, wamekuwa wakiwapa vipaumbele taasisi hizo ambazo nimeziainisha hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kuhusiana na maeneo mengi kukosa vyoo hususan shule zetu, katika bajeti ya mwaka huu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyoo. Miongoni mwa vyoo tutakavyojenga ni katika Mkoa wa Songwe ambao yeye Mheshimiwa Mbunge ni Mbunge ambaye tunawakilisha pamoja. Ahsante sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna Gereza la Ngwala ambalo liko Wilaya ya Songwe, Mkoani Songwe, ambalo ni gereza kongwe na kwa sasa limechakaa sana. Nilifanya ziara pale nikagundua kwamba idadi ya askari walioko pale ni wengi kuliko maelezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini mkakati wa Wizara kuhakikisha Gereza lile kwanza linapokea wafungwa wengi na kukarabatiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokwishasema kwenye jibu la msingi ni kipaumbele cha Serikali kukarabati magereza yote yaliyochoka kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa kuwa mwaka huu gereza hili halimo hili la Mkoa wa Songwe basi tutalipa kipaumbele katika ukarabati katika miaka ijayo ya bajeti, nashukuru.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Katika Wilaya ya Songwe, ujenzi wa Mahakama umeshaanza tangu mwaka jana, je, lini Serikali itamaliza ujenzi katika Wilaya hii? Hilo ni swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini changamoto za Mahakama katika Wilaya ya Ileje ni nyingi sana katika Tarafa zote mbili Mbundali na Ulambia, sasa nilitamani kufahamu ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha katika tarafa hizi zote kutakuwa na majengo ya Mahakama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katibu na Sheria, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, umaliziaji wa jengo la Songwe kimsingi upo mwishoni kabisa, ni matarajio yetu katika muda mfupi ujao jengo lile litaweza kukamilika na kwa sababu lilikuwa kwenye mpango huu unaoishia mwezi wa sita na baada ya kikao hiki cha Bunge tutakwenda kuliangalia ili tujue wapi wamekwamia kwa sababu ilikuwa limalizike haraka.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu Mahakama za Ileje, mpango wa Serikali hadi kufikia mwaka 2025 makao makuu yote ya tarafa nchini tutakuwa tumejenga Mahakama ambazo zitakuwa ni bora na nzuri kabisa. Kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mwandabila baada ya kikao hiki cha Bunge tuwasiliane ili nimpe detail ya mpango kazi ambao tumeuweka kwenye suala la ujenzi wa Mahakama zetu, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kulingana na majibu ambayo yametolewa na Waziri, nataka kufahamu, ni upi mkakati maalum na wa haraka wa Serikali kuuingiza Mkoa wa Songwe kiujumla wake katika mpango wa uwekezaji wa kimkakati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka kufahamu: Je, Serikali imeshafanya vitu gani katika kuongeza biashara na uwekezaji katika Mkoa wa Songwe katika maeneo yafuatayo: eneo la madini, dhahabu na makaa ya mawe, kilimo cha mpunga, uvunaji wa chumvi na mazao mengine ya kibiashara yanayoendelea katika Mkoa wa Songwe? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, maswali ya nyongeza yanahusu fursa za uwekezaji katika Mkoa wa Songwe na ametaja maeneo specific; madini, chumvi na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, ninahitaji kumwandalia taarifa hizi kwa kina ili nisije nikatoa majibu ambayo ni ya kurukaruka. Kwa hiyo, naomba tupate nafasi kwa sababu kwa kweli ni swali ambalo ni jipya kidogo, ahsante.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Ninataka kuuliza kwamba, hasara zinazosababishwa na watumishi wa Serikali ambao wanagawa viwanja mara mbili mbili au kama hivyo wamekosea designing na kwenda kwenye maeneo ambayo kibioanuwai hayakubaliki; zinafidiwa na nani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hasara yoyote ambayo inasababishwa na watumishi wa Serikali, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali dhidi ya hawa wanaosababisha hasara hizi. Kumekuwepo na hatua mbalimbali za kuchukua tahadhari lakini kuwafidia wale waathirika; kwa sababu katika mazingira ya kawaida, watu waliopewa kiwanja kimoja katika eneo moja, tunaona uwezekano wa jinsi ya kuwafidia kwa sababu tumeelekeza halmashauri zote nchini kuwa na akiba ya ardhi ili kutatua migogoro hii kwa kuwapa viwanja vingine mbadala wale wote watakaobainika kuwa wamepewa double allocation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua kali zimechukuliwa. Kwa mfano hapa Dodoma kuna idadi kubwa tu ya watumishi tumewapeleka kwenye vyombo kuangaliwa utendaji kazi wao mbovu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu, ni lini Wizara itapeleka X-Ray katika Kituo cha Kamsamba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba baada ya hivi vituo vya afya kukamilika na kujengewa majengo maalum ya X-ray vinatafutiwa fedha na kupelekewa vifaa vya X-ray kwa maana ya mashine za X-ray kwa ajili ya huduma hizo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya kukamilisha jengo la X-ray tutahakikisha tunatafuta fedha kwa ajili ya kupeleka mashine ya X-ray, ahsante sana.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Spika, kupitia huu Mradi wa REGROW natamani kufahamu wana mkakati gani wa kuwekeza kwenye hoteli kwenye maeneo ambayo wanakuwa wamejenga vituo vya utalii, mfano ile Ngorongoro Reservation ambayo iko pale Ndolezi, Mkoa wa Songe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, msingi wa REGROW ni kujenga mfumo ambao utawezesha kutangaza utalii kwenye maeneo haya. Sasa yapo maeneo ambayo mradi kama mradi unafanya wenyewe, lakini yapo maeneo ambayo tunafanya kutoa chachu kwa sekta binafsi ione umuhimu wa kuja kuwekeza kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, natoa rai kwa sekta binafsi iliyoko kwenye maeneo haya iweze kujiingiza kwenye utekelezaji wa miradi hii na hata yale maeneo ya hoteli ambayo tunaanzisha bado tutahitaji sekta binafsi ije ishirikiane na sisi kuendeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuko tayari kupokea mawazo yake na baada ya hapa tukae pamoja tuone jinsi gani kuweza ku-accommodate mawazo aliyonayo.
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Awali ya yote kwanza niwapongeze kwa sababu zao la kahawa kipindi hiki lipo juu sana kwa bei yake sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa sasa zao la kahawa limeonekana ni fursa ya kiuchumi, je, wana mkakati gani wa kuongeza idadi kubwa ya wanawake watakaoshiriki katika hiki kilimo cha kahawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kuwa benki ya KCBL imekuwa Benki ya Taifa ya Ushirika, je, benki hii ina mkakati gani wa kupeleka huduma katika vituo vya kuuzia kahawa Mkoani Songwe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja ya mkakati wa Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha wanawake wanajihusisha na kilimo cha kahawa kwa kiwango kikubwa na huo ndiyo mkakati ambao tupo nao na ndio maana kati ya mashamba ya mfano kwa maana ya block farms, tumekuwa tukiwa-engage wanawake. Moja ya mfano wa shamba zuri lipo kule Mkoani Kagera katika Wilaya ya Muleba ambapo vijana na akinamama wamehusishwa kwenye kilimo cha kahawa. Kwa hiyo, ni sehemu ya mkakati wetu na tutaendelea kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Benki ya Ushirika ambayo tumeizindua hivi karibuni ni kwamba kwa sasa itakuwa na matawi makubwa matatu kwa maana ya katika eneo la Dodoma itakuwa ndiyo makao makuu, Kilimanjaro pamoja na Tandahimba ambako ndipo ilipoanzia. Baada ya hapo tumekubaliana kwamba watafungua matawi ikiwemo katika Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, hili lipo katika mpango mkakati wa benki hiyo ambayo sisi kama Wizara tunaisimamia, ahsante.