MHE. STELLA S. FIYAO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi yetu inaamini katika uongozi wa kisheria na utawala bora ili kujenga umoja, mshikamano na upendo baina ya wananchi na Serikali yao, lakini kumekuwa kuna changamoto kubwa kwa baadhi ya wateuliwa wa Mheshimiwa Rais, Wakuu wa Mikoa na baadhi ya Wakuu wa Wilaya kwa kutumia nguvu na mamlaka yao vibaya kukamata viongozi na wananchi na kuwatupa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kujua kwanza jambo hili moja, limetengeneza chuki kubwa baina ya wananchi na Serikali yao, lakini pili, linafifisha jitihada kubwa za Mheshimiwa Rais za kuhubiri 4R. Linatengeneza chuki kubwa, mwisho wa siku hili jambo linakuwa halileti mantiki. Nataka kujua kauli ya Serikali ni ipi katika kukemea jambo hili ambalo linatengeneza chuki kubwa baina ya Watanzania na Serikali yao. Je, ni ipi kauli ya Serikali kwa hawa watawala ambao wanatumia mamlaka yao vibaya kutesa na kuwanyanyasa wananchi?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali hili analoliuliza Mheshimiwa Mbunge ni lile ambalo jana Mheshimiwa Kunambi, Mbunge wa Ifakara eneo la Mlimba aliliuliza jana na Mheshimiwa Spika, alitupa kazi Serikali kulifanyia kazi. Tutakapokamilisha tutatoa majibu kwa Mheshimiwa Mbunge na naamini kwa majibu hayo pia tutamjibu na Mheshimiwa Fiyao.
Mheshimiwa Spika, kwa utangulizi ni kwamba ni kweli baadhi ya watawala kwenye maeneo yao wanazo sheria ambazo zinawaruhusu kuhakikisha kwamba hali ya utulivu na ulinzi wa usalama kwenye maeneo yao inaimarika na kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza kwamba baadhi ya wateuliwa.
Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie wale waliotamkwa jana, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ambao pia ipo sheria wanaitumia. Jana ulisimama ukafafanua vizuri na nataka kuungana na wewe kuuhakikishia umma wa Tanzania kwamba sheria ile inayomruhusu Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya kumkamata mwananchi au yeyote yule kumweka ndani haikulenga kama ambavyo baadhi wanaitumia. Lengo ni katika kuhakikisha kwamba mazingira hayo kusitokee uvunjifu wa amani mkubwa na kwa hiyo anaweza akatumia sheria hiyo kumhifadhi mahali ili hali itulie na baadaye aweze kutoka na kuendelea na majukumu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, anaweza kuwa tishio lipo kwa Mkuu wa Wilaya mwenyewe au Mkuu wa Mkoa mwenyewe anaweza kutumia nafasi hiyo ili kulinda, inaweza kuwa jambo hilo ni hatari kwa wananchi anaweza kuitumia nafasi hiyo kulinda usalama wa raia wale lakini pia hata huyo huyo mwananchi ambaye analeta hiyo hoja kulinda usalama wake, basi sheria inaweza kutumika kwa yeye kumwondoa eneo lile na kumhifadhi mahali.
Mheshimiwa Spika, jambo hili limeshazungumzwa mara kadhaa hapa Bungeni, jambo hili tumeshatoa ufafanuzi mara kadhaa hapa Bungeni na tulitaka tuchukue hatua. Nataka nikuhakikishie kwamba wiki mbili, tatu zilizopita Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa wote waliitwa hapa Mkoani Dodoma kwa semina katika maeneo mbalimbali. Eneo hili la sheria hii limezungumzwa sana na wameelimishwa sana na tunaamini sasa watakuwa wanaelewa namna ya kuitumia sheria ile bila kuleta madhara, bila kuleta chuki miongoni mwao na wananchi na bila kuleta mtafaruku katika jamii ili waweze kufanya kazi yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, hata kama anatumia sheria hii mashariti yake ni kwa masaa 24 ambayo baada ya masaa 24 anatakiwa kutoa taarifa ya kwa nini yule aliyepo ndani kawekwa na kuwezesha chombo husika kuchukua hatua. Kama hana jambo lolote anatakiwa baada ya masaa 24 yule aliyeingizwa polisi anatakiwa aondoke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jana tumefuatilia kule Kilombero tumeona wale watuhumiwa wote wameshapelekwa Mahakamani. Kwa hiyo jambo lile hatuwezi kulizungumza tena kwa sababu tayari hatua zimeshachukuliwa na sasa hivi wapo Mahakamani.
Mheshimiwa Spika, jambo hili tutaendelea pia kuelimisha wateule wote wenye sheria hizi ili waweze kuzitumia kwa weledi, lakini kwa uaminifu na uadilifu kuzingatia sheria na taratibu za nchi ili pia kuleta amani katika jamii bila kuleta msuguano, migongano isiyokuwa muhimu ili kuwezesha kufanya kazi yake.
Mheshimiwa Spika, hayo ndiyo maelezo ya msingi kwa awali. Tutakavyopata taarifa zilizokamili ya tukio hili lilikuwaje ili tuweze kuhusisha swali la Mheshimiwa, hoja ya Mheshimiwa Kunambi na Mheshimiwa Stella Fiyao, wote Waheshimiwa Wabunge tutawapa taarifa. Ahsante sana. (Makofi)