Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho (7 total)

MHE. CAPT. ABBAS ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zipo baadhi ya Taasisi za Serikali ambazo zinakidhi vigezo vya mkopo kutoka katika mabenki ya kibiashara. Je, taasisi ya aina hizo ni ruksa kukopa kwa lengo na madhumini ya kugharamia miradi yao bila kuingiliwa na Serikali?

Swali la pili, zile taasisi kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri, hazipeleki chochote na ni mzigo kwa vile ni tegemezi katika suala zima la ruzuku. Je, ni busara kuendelea na aina hiyo ya taasisi? Ahsante sana.(Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa alivyojibu swali la msingi, lakini pili, napenda kujibu swali la Captain Abbas Ali Mwinyi, Mbunge wa Fuoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba zipo taasisi ambazo zinakidhi vigezo vya kukopa Serikalini, lakini taasisi hizi zina mwenyewe ambaye ni Msajili wa Hazina. Kwa hiyo, japokuwa kazi hizi zinakidhi vigezo vya kukopa bado zinahitaji ruhusa ya Serikali kupitia kwa Msajili wa Hazina kabla ya kuweza kupata mikopo ili kuweza kuteleleza miradi yake ambayo nayo inabidi ipitiwe na kupitishwa na Wizara na kuingizwa kwenye bajeti kama ambavyo tumepanga hapa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu taasisi tegemezi, taasisi tegemezi tulizonazo ni zile ambazo zinatoa huduma ambazo zinategemea ruzuku ya Serikali. Kwa hiyo, ni muhimu ziendelee kuwepo kama Taasisi za Bodi za Usajili ambazo hazizalishi mapato bali zinatoa huduma kwa ajili ya udhibiti. Ahsante.
MHE. AGNESS M. MARWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, sambamba na hilo swali la Mheshimiwa Robert Maboto nauliza je, ni lini Serikali itakamilisha lami kutoka Kinesi yaani Wilaya ya Rorya inayounganisha kutoka Rorya mpaka Tarime ambayo pia ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa wetu Hayati Magufuli? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi za viongozi wetu wakuu tutaendelea kuzitekeleza kulingana na fedha itakavyopatikana ikiwa ni pamoja na hiyo barabara ya kutoka Rorya hadi Kinesi, ahsante.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza lakini pia namshukuru dada Grace kwa kuuliza swali ambalo tulikuwa tunajadiliana juu ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, aa ninacho…

SPIKA: Mheshimiwa Jackson kwa hiyo swali hili ulimtuma kumbe ee!

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, tunajadiliana, mimi na yeye tunafanya kazi kwa kushirikiana na kwa tunajadiliana; lakini amewahi kuuliza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la nyongeza ni kuhusu barabara inayotoka Kijiji cha Wenda kwenda Lupembelwasenga inatokea Mgama. Barabara hii kwa taarifa nilizonazo ilikuwa imetengewa fedha katika ule mpango wa European Union, na tayari nilishauliza RCC lakini sikupata majibu yanayoridhisha.

Je, Serikali inaweza kunipa majibu sasa, kwa kuwa barabara hii ni muhimu kwa sababu ya wakulima wanaotoka maeneo hayo na kuyawaisha kufika kwenye barabara hizi za lami ili awahi huku Dodoma? Ni lini sasa Serikali inaweza kututengenezea? Ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, barabara hiyo tumeichukua na tutaifanyia upembuzi ili tuone kama inakidhi vigezo vya kuhama ili tuihamishe iende TANROADS naomba kuwasilisha.
MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa suala hili limekuwa la muda mrefu sana, lina jumla ya miaka kama minne au mitano, wananchi wanaendelea kupata mateso ya kulipa 600 wakati wa kuingia na 600 wakati wa kutoka, wananchi hawa maskini. Mimi binafsi nimeshasumbuka sana suala hili nimezungumza na Mheshimiwa Kakoko, nimezungumza na Mheshimiwa Abood, nimezungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu amenijibu na barua ninayo hapa ya kwamba amewaagiza TPA washughulikie suala hili mara moja. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutoa tamko hapa kwamba tozo hizo zitapunguzwa mara moja ili wananchi waweze kuondoka kwenye mateso? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shigongo, Mbunge wa Buchosa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ilivyojibiwa katika swali la msingi tozo hizo zinatolewa kwa mujibu wa sheria na zinafuata tariff book ambayo ni ya TPA. kama ambavyo imejibiwa katika jibu la msingi, sasa hivi tunafanya majadiliano ili tuweze kupunguza tozo hizo kulingana na malalamiko ya wananchi ili tuweze kwenda kisheria. Hatuwezi kupunguza sasa hivi kwani ndiyo mambo haya haya ambayo yatazuka tena katika Ripoti ya CAG kwamba tumetoza kinyume na Tariff Book. Kwa hiyo, tunafanya marejeo hayo na tutakapoyakamilisha, tutawasiliana na vijiji vyote kama vilivyotajwa pale katika Visiwa vya Kasalazi, Yozu, Gembela watashirikishwa katika kikao cha wadau ili tuweze kupata tozo muafaka ambazo zitakubalika kwa wananchi wote. Ahsante. (Makofi)
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali hili limeulizwa mara mbili kwa mujibu wa Taarifa mbalimbali kutoka Bunge lako majibu yamekua ya kitolewa hayo hayo, sasa naomba kujua hata hizo bilioni 6 ambazo zimetengwa kwa ajili ya mwaka unaoishia mwenzi mmoja ujao hazijawahi kutumika mpaka leo. Naomba kujua lini sasa hizi bilioni 6 sasa zinaanza kufanya ujenzi kwenye barabara ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni nini commitment ya Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwasababu Mheshimiwa Rais alipokuja kwenye ziara ya kuomba kura aliahidi itajengwa kwa kiwango cha lami, naomba kujua…

NAIBU SPIKA: umeshauliza Mheshimiwa, ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumshukuru Mbunge kwa jinsi ambavyo ifuatilia barabara hii barabara ndefu na kweli ni kiunganishi cha mikoa tangu Singida hadi Tanga na imepangiwa katika bajeti bilioni 6.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuahidi Mbunge huyu kwamba kabla ya bajeti hii kwisha barabara hii itatangazwa katika kipande ambacho kimepangiwa kilomita 20. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana barabara hii tuna maslahi nayo kama alivyojibu swali Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa sababu barabara hii inaunganisha mikoa minne na barabara hii inahistoria katika nchi yetu imefika wakati sasa Serikali iamuwe kuijenga barabara hii kilometa 461 iishe kuliko kuanza kuwa na vipande vidogo vidogo.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina Wabunge wengi ambao wanaifuatilia sana na ninawashukuru sana kwa kuweza kuwa wanatukumbusha kila mara umuhimu wa barabara hii. Lakini kama alivyosema Mbunge barabara hii inaurefu wa kilometa 460 na tunaendelea kujenga kwa vipande kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu unaoendelea kama nilivyosema katika swali lilipita tutajenga kipande kimoja na katika bajeti hii ambayo tuna ijadili mwaka huu barabara hiyo vilevile imezingatiwa kwa hiyo napenda kuwaahidi wananchi tangu mikoa ya Singida hadi Tanga ambayo barabara hiyo inapita kwamba vipande vinaendelea kujengwa na barabara hiyo tutaizingatia kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nakuomba katika swali hili utupe msaada, maana sasa tunahitaji msaada wako.

Mheshimiwa Spika, mwezi wa pili mwaka huu 2021 tulikuwa na Waziri wa Ujenzi pale Butiama na Mkuu wa Wilaya ya Butiama alileta meseji ya Mama Maria kwamba anazunguka mno kutoka Musoma kuja kule mpaka apitie Kyabakari eneo lake limeshindwa kukamilika. Hii barabara Mkandarasi alipewa 2013 amalize 2015, miaka miwili hakumaliza;2015 -2017 hakumaliza; 2017-2019 hakumaliza; na 2019-2021 hajamaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi tulikuwa na Waziri wa Ujenzi nikamwambia huyu hatamaliza. Sasa hii miradi inayopita Butiama pale kuna shida gani? Katika mradi ambao unatia aibu katika Mkoa wa Mara ni mradi huu wa barabara. Tunaomba msaada wako, yule Mkandarasi hatamaliza ule mradi, hilo ni suala la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mkandarasi yule ameshindwa hata kwenda site mpaka sasa hivi. Toka tulipoongea na Waziri mwezi wa Pili, aliondoka mpaka leo. Barabara ya diversion ya kupita kwenye ile barabara haipitiki: Je, Waziri au Serikali ipo tayari kuwaambia TANROADS wa Mkoa wa Mara waende wakatengeneze diversion ya ile barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni mradi wa aibu, naomba msaada wako. (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba barabara hii ilipewa Mkandarasi huyu kwa muda mrefu uliopita na kama ilivyojibiwa katika jibu la msingi barabara hii ilipewa Wakandarasi hawa wazawa kama barabara ya kuwajengea uwezo. Tumekuwa tukiendelea kuwajengea uwezo hao lakini ilitokea changamoto mbalimbali ambazo tunaendelea kukabiliana nazo.

Mheshimiwa Spika, changamoto ambazo zilijitokeza ambazo zilikuwa ni ngumu kidogo kwa Wahandisi wapya wazawa ni baada ya kukutana na miamba ambayo ni dhaifu ambapo ilibidi wahangaike kutafuta miamba ambayo ni migumu kidogo. Kwa hiyo, tumekuwa tukishirikiana nao katika kuwajengea huo uwezo wa kutafuta miamba migumu ili kuweza kukabiliana na barabara hiyo.

Mheshimiwa Spika, nilichukua fursa hiyo ya kwenda mwenyewe kufanya ule ukaguzi na Mheshimiwa Mbunge tulikuwa naye na tukaahidiana kwamba tutaweza kulishughulikia jambo hilo kwa haraka ili usiwe ni mradi wa aibu.

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tunaendelea vizuri na tayari tumeshamwambia yule Mkandarasi na ameshatekeleza kupata kokoto mbadala kutoka sehemu ambayo inapatikana na tunaendelea kuwahimiza ili waweze kumaliza katika hii miezi minne ambayo tumewaongezea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, japokuwa ni kweli kwamba mradi huu umechelewa, tayari tumeshachukua hatua muhimu za kuhakikisha kwamba mradi huu utakamlika kwa wakati na usiwe mradi wa aibu na Wakandarasi wazawa tuendelee kuwajengea uwezo ili waendelee kuaminika katika miradi kama hii. Naomba kuwasilisha. (Makofi)