Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Suleiman Haroub Suleiman (3 total)

MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majawabu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja lenye kifungu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, timu ya Taifa Stars ni timu ya Tanzania na Tanzania ina ligi kuu mbili kwa maana ya kwamba Ligi Kuu ya Zanzibar na Ligi Kuu ya Tanzania Bara. Sasa je, kwenye kuchagua wachezaji kwenye kutafuta wachezaji kuunda timu ya Taifa hauoni haja au hauoni sababu kwamba sasa kocha wa timu ya Taifa kuweza kudhuru ligi zote mbili ili kupata wachezaji wazuri?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; zamani kulikuwa kuna ligi kuu ya Muungano kwa maana ya Super Cup ligi ile iliweza kutoa timu bora na timu nyingi ambazo zilishiriki ligi ile ilitoa wachezaji wa timu ya Taifa Stars. Sasa je, Serikali ina mkakati gani kuweza kurudisha kombe hili? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kunipa nafasi nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Suleiman kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Suleiman amependa kufahamu kwamba katika kuandaa timu za Taifa; je, si vyema timu hizi zikaandaliwa kwa kufatilia ligi zote mbili za TFF pamoja na ZFF.

Mheshimiwa Spika, hili ni dhahiri kwamba tunapochagua wachezaji wa timu ya Taifa kocha hakatazwi kwenda popote kwenye hizi ligi ndani ya Taifa letu na hili limekuwa likifanyika ndio maana wachezaji katika timu yetu ya Taifa wanatoka pia kwa upande wa Zanzibar pamoja na upande wa Bara. (Makofi)

Kwa hiyo hili tutaendelea kuimarisha tukishirikiana na ZFF pamoja na TFF ili kuhakikisha kwamba tunapata wachezaji wazuri na hata katika benchi la ufundi tumekuwa tukiwahusisha wenzetu wa Zanzibar kuhakikisha pia wanatoa mchango na wanakuwa sehemu ya ligi yetu na timu yetu ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili amependa kufahamu tulikuwa na ligi ya Muungano sasa anapenda kufahamu ni ligi hii itarudishwa? Nijibu hili kwamba jambo hili sisi kama Wizara pia tumeliona. Tumekuwa sasa na mazungumzo kati ya BMT, TFF pamoja na ZFF kuhakikisha kwamba ligi hii inarudishwa.

Mheshimiwa Spika, mwanzoni ilisitishwa kwa sababu Zanzibar ilipata associate membership kwa CAF wakawa wanapeleka timu zao mbili na huku Bara pia wakawa wanapeleka pia timu zao mbili. Lakini kwa afya ya Muungano wetu, kwa afya ya mashirikiano tuliyonayo kama Taifa tumekubaliana na kamati imeshaundwa ligi hii itarudishwa hivi karibuni tunaangalia tu tathmini na gharama kwamba gharama zitakuwaje, lakini itarudishwa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, pamoja na majawabu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ni lini miradi ambayo inahusiana na mabadiliko ya tabia nchi iliyopo Zanzibar SMT wataimaliza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Zanzibar inashirikishwa vipi kwenye mikutano ya Kimataifa hasa inayohusu masuala ya tabia ya nchi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suleiman, Mbunge Mwakilishi kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ipo miradi mingi ambayo inatekelezwa ama inasimamaiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na inatekelezwa Zanzibar. Kuna miradi ile ambayo inasimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais lakini kuna miradi inayosimiamiwa na NEMC. Kwa mfano, kuna Mradi wa Adaptation Fund ambayo ipo Zanzibar na imetekelezwa maeneo tofauti. Hii tayari imeshakamilika na wananchi wameshaanza kunufaika na miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, pia kuna miradi ya EBA ambayo hivi karibuni kama mnakumbuka tuliwahi kukabidhi boti za uvuvi Tumbatu na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar, lengo na madhumuni Serikali ya Jamhuri ya Tanzania inaunga mkono juhudi za Uchumi wa Bluu kwa upande wa Zanzibar na suala nzima la uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, vile vile kuna miradi ya LSDF. Hii ni miradi ambayo imekuja kwa ajili ya kukuza kilimo, kuboresha ardhi iliyoathirika na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Pia kuna miradi ambayo haijakamilika; hii tumeshatoa maelekezo kwamba ndani ya mwezi huu ianze. Ni mradi wa uchimbaji wa bwawa la maji uliopo Bumbwini Makoba. Tumesema ndani ya mwezi huu uanze na utaanza kwa ajili ya kunufaisha wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la piliā€¦

SPIKA: Kwa kifupi.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, Zanzibar inapata ushirikiano mkubwa kushirikishwa kutoka Serikali ya Jamhuri katika vikao vinavyohusina na mazingira katika mambo ya Kimataifa. Hivi karibuni tulikuwa tuna kikao cha COP27 Mkutano wa Kimataifa ambapo Zanzibar tulishiriki. Tanzania tulishiriki lakini Zanzibar walileta delegation yao, tulikuwa na Mkurugenzi wa Mazingira na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha kuonesha kwamba tunao ushirikiano wa karibu baina ya Serikali mbili hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. SULEIMAN HAROUB SULEIMAN: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kuna baadhi ya viongozi ambao walitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwemo Dkt. Salmini Amour Bin Jumaa, anaishi kwenye hali ngumu sasa hivi kwa maana kwamba nyumba yake inaendelea sasa hivi kupata erosion, ipo karibu na bahari. Je, Serikali ama Ofisi hii ipo tayari kushirikiana na Kamati ya Viongozi Wakuu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili kutatua changamoto hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kuna baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji kutunzwa, lakini mpaka hivi sasa maeneo hayo yanakuwa kwenye hali hatarishi ikiwemo shule aliyosoma Mzee Karume. Je, Serikali ina mpango gani kutunza maeneo kama hayo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Haroub. Naomba niseme Mheshimiwa Haroub ni mfuatiliaji sana na watu kule Baraza la Wawakilishi lazima wajue recognition yake ya kazi kubwa anayofanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tulikuwa na sheria yetu ambayo nimezungumza hapa, lakini hii ilikuwa inagusa maeneo mahususi, kwa sababu mimi ni Waziri wa Muungano haya mambo ambayo amezungumza, mengine tutayachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi kupitia taratibu zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mambo ya kumbukumbu ya maeneo hayo niseme, kwa sababu ofisi yangu inahusika na mambo mbalimbali na kwa sababu ofisi yangu inashirikiana vizuri na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, kule Zanzibar, tunalichukua jambo hili, tunali-discuss halafu tuone way forward, tunafanyaje kuboresha maeneo hayo. (Makofi)