Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwantatu Mbarak Khamis (5 total)

MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS Aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwainua Watu Wenye Ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya michezo na walimu ili waweze kushiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili kusimamia sekta ya maendeleo ya michezo kwa weledi, Serikali imetengeneza Mpango Mkakati wa Maendeleo ya Michezo wa Taifa ambao utazinduliwa rasmi mwezi Septemba 2021. Mpango mkakati huo una malengo ya kuendeleza michezo kwa ujumla wake ikiwa ni pamoja na michezo ya watu wenye ulemavu. Mpango huo unaainisha maeneo yote muhimu yakiwemo upatikanaji wa vifaa, ujenzi na ukarabati wa miundombinu, uendelezaji na upatikanaji wa wataalam na walimu wa michezo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na uendelezaji wa mpango huo, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imekuwa ikiwasaidia wana michezo wenye ulemavu kushiriki katika michezo mbalimbali kwa kuwapatia mahitaji muhimu ikiwa ni pamoja na vifaa vya michezo na wataalam wa mchezo husika. Mathalani mwaka huu wa 2021, Serikali imelipia usafiri, vifaa na posho kwa wachezaji na viongozi wanne kushiriki Michezo ya Paralimpiki inayofanyika nchini Japan – Tokyo kuanzia tarehe 24/08 - 04/ 09/2021. Zaidi ya milioni 15 zimetumika.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019, Serikali iligharamia timu yetu ya mchezo wa wheel Chair kushiriki mashindano ya Afrika Mashiriki Nairobi Kenya. Mwaka huo huo Serikali iligharamia Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa watu wenye ulemavu kushiriki mashindano ya Bara la Afrika (CANAF) yaliofanyika nchini Angola. Timu hiyo ilifuzu kushiriki mashindano ya Dunia ya mchezo huo yatakatofanyika mwaka 2022 nchini Uturuki.

Mheshimiwa Spika, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Michezo uliopo chini ya Baraza la Michezo la Taifa, ni matarajio yetu kuwa tutaendelea kuwasaidia wachezaji wenye ulemavu kwa mahitaji mbalimbali ili waweze kushiriki kikamilifu katika michezo ya Kitaifa na kimataifa kwa kuwapatia maandalizi na kuwa na vifaa mbalimbali pamoja na watalaam pale wanapohitaji msaada huo.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS aliuliza: -

Je, ni sababu gani iliyopelekea vituo vidogo vya Polisi Kidongo Chekundu, Jang’ombe na Beit El Ras visifunguliwe na kufanya kazi kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, Mbunge wa Kuteuliwa (Baraza la Wawakilishi), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya Polisi vya Kidongo Chekundu kilichojengwa mwaka 1993, Jang’ombe kilichojengwa mwaka 2018, na Beit El Ras kilichojengwa mwaka 1994 ni vituo vidogo vya polisi vilivyoko Wilaya ya Mjini Magharibi. Vituo hivi vilifungwa mwaka 2019 kutokana na upungufu wa askari. Kwa sasa Kituo cha Polisi Jang’ombe kimefunguliwa na kinafanya kazi saa 24 baada ya kupangiwa askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pindi askari walioko Shule ya Polisi Moshi watakapohitimu mafunzo ya awali, kipaumbele cha ugawaji wa polisi hao kitakuwa kwenye maeneo yenye upungufu wa askari ikiwemo Wilaya ya Mjini Magharibi ili kuwezesha vituo vilivyofungwa viweze kufunguliwa tena. Nashukuru.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuweka miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu katika vyombo vya usafiri ikiwemo mabasi ya mwendokasi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikisimamia upatikanaji wa huduma bora na salama kwa watumiaji wa usafiri kwa makundi yote ya jamii wakiwemo wenye ulemavu. Serikali imekuwa ikizingatia mahitaji ya makundi maalum hasa wenye ulemavu katika ujenzi wa miundombinu ya usafiri ikiwemo miundombinu ya mabasi ya mwendokasi.

Mheshimiwa Spika, miundombinu ya mabasi ya mwendokasi inayotumika sasa na inayoendelea kujengwa imezingatia watu wenye mahitaji maalumu. Aidha, mabasi yote ya mwendo kasi yamezingatia watu wenye mahitaji maalumu hususan wenye ulemavu, wazee na wajawazito. Ahsante.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS aliuliza: -

Je, vijana wenye ulemavu wamenufaika vipi na mafunzo na mikopo inayotolewa na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa mafunzo na mikopo kwa Vijana wenye Ulemavu inatekeleza mikakati na programu jumuishi mbalimbali inayolenga kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu, mafunzo na ujuzi kwa lengo la kuboresha hali zao za maisha na kukuza ushiriki wao katika shughuli za kijamii, kisiasa na kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi cha Mwaka 2022, kiasi cha mikopo ya shilingi bilioni 81.3 zilitolewa kwa watu 640,723 wenye ulemavu wakiwemo vijana wenye ulemavu. Mikopo hiyo imewezesha vijana wenye ulemavu kuanzisha au kuendeleza biashara zao na hivyo kupunguza utegemezi na kuwa na uwezo wa kuchangia kwa kiwango kikubwa katika mahitaji yao wenyewe na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, zaidi ya vijana wapatao 2000 wamenufaika na mafunzo yanayotolewa hapa nchini. Vijana hao wamepata mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali kupitia vyuo vya ufundi na marekebisho, vyuo vya VETA na kupitia programu ya ukuzaji ujuzi iliyopo nchini, ahsante.
MHE. MWANTATU MBARAK KHAMIS aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha huduma za marekebisho kwa watoto wenye ulemavu?
WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantatu Mbarak Khamis, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha huduma za marekebisho kwa watoto wenye ulemavu Serikali inatekeleza afua mbalimbali kupitia Wizara za Kisekta ikiwemo:-

(i) Kuweka moduli katika mtaala wa mafunzo ya walezi wa watoto ili kuwezesha kufanyika kwa utambuzi wa mapema wa watoto wenye ulemavu wanapokuwa katika vituo vya kulelea watoto wachanga na watoto wadogo mchana, kaya na familia.

(ii) Vilevile Serikali inawaunganisha watoto husika na huduma stahiki za kijamii zilizo kwenye Wizara za Kisekta kulingana na aina ya ulemavu mathalani; matibabu na vifaa saidizi, huduma za lishe na kufanya uchangamshi wa awali kupitia Maafisa Ustawi wa Jamii walio katika Hospitali, Wilaya na Kata ili kupunguza makali ya ulemavu kwa watoto.

(iii) Na hatua ya mwisho ni, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia Maafisa Maendeleo na Ustawi wa Jamii juu ya namna ya kuepuka ulemavu utotoni, elimu ya lishe bora kwa watoto na elimu kuhusu kuwapeleka watoto katika vituo vya kutolea huduma ili waweze kupewa huduma stahiki kulingana na aina ya ulemavu walionao.