Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ameir Abdalla Ameir (8 total)

MHE. BAKAR HAMAD BAKAR K.n.y. MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza: -

Je, Balozi za Tanzania zinatumia mikakati gani kutangaza bidhaa za Tanzania Kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sera ya Mambo ya Nje ya Mwaka 2001 inatoa msisitizo katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ambayo lengo kuu ni kujenga, kukuza na kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Kwa muktadha huo, balozi zetu nje ya nchi, zimeendelea kubuni mikakati mbalimbali katika kutekeleza vyema diplomasia ya uchumi kwa kutangaza bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ikiwa ni pamoja na masoko ya bidhaa na huduma hizo.

Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuratibu na kufanikisha upatikanaji wa vibali/ithibati kwa kampuni za Tanzania kuuza bidhaa zao katika masoko ya nje; kuratibu na kushiriki katika makongamano ya biashara, maonesho na mikutano ya kimataifa ndani na nje ya nchi; kuratibu na kufanikisha ziara za wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi; Kuratibu na kufanikisha ziara za kuutangaza utalii (road show), watu maarufu na mashuhuri, kampuni za kitalii na Kubidhaisha lugha ya Kiswahili na kuitangaza kimataifa, ahsante sana.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha utalii wa ndani unaimarika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utaii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika; katika kuhakikisha utalii wa ndani unaendelea kuimarika nchini, Wizara inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukuza utalii wa ndani ikiwemo: -

i. Kuwa na huduma bora zenye gharama nafuu kwenye vivutio zikiwemo malazi, chakula, usafiri na viingilio;

ii. Kuendelea kuhamasisha makundi mbalimbali ya kijamii ikiwa ni pamoja na wanafunzi, wajasiriamali, wafanyakazi na makundi maalum kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii na pia kufanya mikutano; na

iii. Kuendelea kutoa elimu kwa umma na kutumia chaneli maalum (Tanzania Safari Channel) ya kutangaza utalii kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio hivyo.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuongeza maeneo ya utalii, kuibua vivutio na mazao mapya ya utalii na kuendeleza miundombinu ya utalii katika kanda zote za utalii nchini.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza: -

Je, Balozi za Tanzania zinatumia vipi fursa ya kukua kwa Kiswahili duniani kutafuta ajira kwa Watanzania?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Balozi zetu nje ya nchi zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali katika kukuza Kiswahili na kuchangia ongezeko la ajira kwa Watanzania ikiwemo kuanzisha programu za kufundisha, kutafsiri na kufanya ukalimani wa Kiswahili duniani, hatua ambayo inatoa ajira kwa Watanzania. Jumla ya Balozi 13 zimeweza kuanzisha madarasa, vituo na clubs za Kiswahili. Aidha, zaidi ya Watanzania 95 wamepata ajira katika maeneo hayo. Vilevile, vyuo na vituo binafsi zaidi ya 150 vinafundisha Kiswahili duniani. Kwa sasa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limepewa kazi ya kufundisha walimu 10 wa Diaspora katika Ubalozi wetu wa Abu Dhabi ambapo ni uhitaji wa walimu kwenda kufundisha Kiswahili katika Umoja wa Falme za Kiarabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Balozi zetu zipo katika mazungumzo na vyuo vikuu kwenye maeneo yote ya uwakilishi ili Lugha ya Kiswahili iweze kujumuishwa katika mitaala ya vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kupata Wahadhiri wa Kiswahili kutoka Tanzania. Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kuwait, Chuo Kikuu cha Holon Institute of Technology nchini Israel na Chuo Kikuu cha Buraimi, nchini Oman, ahsante.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. AMEIR A. AMEIR aliuliza: -

Je, ni asilimia ngapi ya Wafanyabiashara hawajaingizwa katika Mfumo rasmi wa kodi na Serikali inachukua hatua gani kuwafikia?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kupanua wigo wa kodi. Hadi Juni 30, 2023 Mamlaka ya Mapato Tanzania ilikuwa imesajili jumla ya walipa kodi 4,696,999, sawa na asilimia 16 ya idadi ya nguvu kazi iliyopo nchini ambayo ni takribani milioni 33. Idadi ndogo ya usajili wa walipakodi, ikilinganishwa na fursa ya nguvu kazi iliyopo inatokana na sehemu kubwa ya shughuli za kiuchumi hapa nchini kuendeshwa na sekta isiyo rasmi inayokadiriwa kuajiri takribrani watu milioni 27.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kurasimisha sekta isiyo rasmi ni pamoja na kampeni ya mlango kwa mlango inayolenga kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wasiotambulika, kutenga na kujenga maeneo maalumu ya masoko kwa wafanyabiashara wadogo na kuendelea kutoa elimu na ufafanuzi wa kina kwa wananchi kuhusu masuala ya kodi ili kuhamasisha wananchi kurasimisha biashara na shughuli za kiuchumi kwa hiari, nakushukuru.
MHE. DENNIS L. LONDO K.n.y. MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza:-

Je, ubunifu una nafasi gani katika kuleta mageuzi ya kiuchumi?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ubunifu ni nyenzo na kichocheo cha kuongeza ufanisi katika sekta mbalimbali za uzalishaji na kutoa huduma nchini. Matumizi ya ubunifu yameongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma. Aidha, maeneo yaliyonufaika zaidi ni pamoja na: mawasiliano, huduma za fedha, utawala, masoko, afya, tafiti na usimamizi wa fedha za umma, mitambo inayojiendesha, kompyuta na roboti.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ubunifu wa teknolojia mpya ikiwemo mifumo ya TEHAMA katika undeshaji wa shughuli za Serikali (e-Government) na kukusanya mapato ya serikali kwa njia ya kielektroniki (GePG) kwa kiasi kikubwa zimechangia katika mageuzi ya kiuchumi tunayoshuhudia nchini. Mathalan ubunifu uliowezesha kutuma na kupokea fedha kupitia simu za mkononi, umeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi nchini hasa kwa wafanyabiashara na wananchi mijini na vijijini.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza: -

Je, kwa kiwango gani TEHAMA inatumika kuboresha sekta ya kilimo nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo ni mojawapo ya sekta zinazonufaika na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hapa nchini. Kwa kutumia TEHAMA sekta ya kilimo imeboresha maeneo mbalimbali ya huduma zinazotolewa na Wizara kwa wakulima, wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika sekta na umma kwa ujumla. Baadhi ya huduma zilizoboreshwa kwa kutumia TEHAMA ni pamoja na kutoa huduma za ugani kwa wakulima, masoko ya mazao ya wakulima, kutoa mbolea ya ruzuku, kupata vibali ama leseni za kufanya biashara za mazao ya mimea na vyeti vya afya ya mimea kwa mazao yanayosafirishwa nje ya nchi.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani BAKITA na BAKIZA zinaondoa changamoto za matumizi ya Lugha ya Kiswahili Kitaaluma na kijamii?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabaraza ya Kiswahili BAKITA na BAKIZA yameendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto za matumizi sahihi ya Kiswahili kitaaluma na kijamii zikiwemo, kuandaa semina za ukalimani; kusanifisha maneno mara tu yanapoibuka kutokana na maendeleo ya Sayansi na teknolojia na ongezeko la matumizi ya mitandao ya kijamii, kutoa elimu ya matumizi fasaha na sanifu ya Lugha kupitia vipindi vya redio na televisheni, kuandaa makongamano ya Idhaa za Kiswahili Duniani kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya Lugha, kupitia vitabu mbalimbali vilivyoandikwa kwa Kiswahili kwa lengo la kuhakiki usahihi wa Lugha na kutoa ithibati, kuwapiga msasa wataalam wa Kiswahili na kuwapatia mbinu za kufundisha Kiswahili kwa wageni na kusambaza msamiati wa Kiswahili kupitia mitandao ya kijamii.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza:-

Je, tafiti zipi ambazo Taasisi za Tiba Asili zimekamilisha na kuweza kuwa suluhisho la maradhi mbalimbali kama Tiba Mbadala?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2021 – 2024 zaidi ya tafiti 50 zimefanyika ndani ya nchi juu ya ubora na usalama wa dawa zinazotumika kwa tiba asilia kwa kupitia Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Mheshimiwa Spika, baadhi ya tafiti hizo ni pamoja na utafiti wa dawa ya Saratani ya NIMREGENIN, Dawa ya TANGHESHA inayotibu Selimundu, Dawa ya PERVIVIN inayotibu tezi dume, Dawa ya WARBUGISTAT inayotibu magonjwa nyemelezi na Dawa ya NIMRICAF inayosaidia mfumo wa upumuaji.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.