Contributions by Hon. Kavejuru Eliadory Felix (17 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na namshukuru Mungu kwa mara ya kwanza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitumie nafasi ya pekee kwanza kuwashukuru wananchi wapiga kura wote walionipigia kura nyingi kule kwenye Jimbo la Buhigwe. Ninawashukuru sana na ninawaahidi sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi ya pekee kutoka kwenye moyo wangu wa shukrani kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliotoka humu wakaja kunipambania. Ushindi wangu nilioupata ni wa sisi sote, ni wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi/Vigelegele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Chama changu Cha Mapinduzi, Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi iliyoniteua na hatimaye nikapeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi na leo niko hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo, ninaomba sasa niende kwenye hoja mama. Kwenye wilaya yangu naenda kujikita kwenye suala la minada ya mifugo. Wizara ya Mifugo tunashukuru sana imetengeneza, imekarabati, imejenga mnada ambao unasimamiwa na wizara. Lakini huo mnada mpaka sasa hivi una zaidi ya miezi saba ulikwishakamilika, mkandarasi amekwishawaomba ili awakabidhi Wizara nao hawajafika. Ninaomba Wizara ije ifungue ili huo mnada ufanye kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wilaya ninayotoka iko mpakani, tunayo changamoto inayotokana na tozo ambalo inaonekana ni kubwa kwa wafanyabiashara wa mifugo. Ng’ombe mmoja anayesafirishwa nje na ni wafanyabiashara wadogo wadogo tu, tozo yake, ada yake ni 25,000. Hiyo imesababisha wafanyabiashara wa nchi jirani ambayo ni Burundi pale, hawaji kwenye minada yetu. Naomba Wizara ipunguze tozo hiyo ili waweze kuvuka na wanunue mifugo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mnada wa halmashauri ambao uko mbali kwenye Tarafa ya Myama. Kwenye Tarafa ya Manyovu tuna ng’ombe wengi sana. Mifugo hio wanaenda kiholela, wanatoroshwa, hatuna mnada. Ninaomba tufungue mnada mwingine wa Halmashauri katika Kata ya Kibande ambayo ni karibu kabisa na iko mpakani mwa Burundi, ili Warundi waweze kuvuka wenyewe na wakishavuka wanunue wale ng’ombe na biashara nyingine zitaamka pale pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi hapo hapo kwenye Idara ya Mifugo ninayo Tarafa ya Myama, ina kata saba. Kuna kata moja inaitwa Kata ya Kajana, ina mifugo wengi; hatuna josho. Naomba josho lijengwe pale. Nikirudi kwenye minada, tulikuwa na Afisa Minada mmoja lakini mpaka ninaposimama na kuzungumza hapa mbele ya Bunge lako Tukufu amekwishahamishiwa Pugu. Naomba mtuletee Afisa Minada ili aendeshe huo mnada ambao mmetujengea ulete tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea kuchangia hapo kwenye mifugo, tuna matatizo na tuna upungufu wa Maafisa Ugani. Hata wale waliopo hawana vitendea kazi. Tunaomba Wizara yako iwaone.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara ya kwanza, naamini Wabunge wenzangu mtaendelea kunilea. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza nianze kumpongeza Waziri wa Nishati na Naibu wake na viongozi wote wanaoshirikiana kwa utumishi wao uliotukuka, Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nikushukuru wewe binafsi kwa kuniona lile la vinasaba kurudi kwenye TBS na Wabunge wote wakaamua litungiwe sheria. Hili ni jambo jema na la ukombozi kwa uchumi wa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda ni mchache, naomba niende moja kwa moja kwenye changamoto za umeme katika Mkoa wa Kigoma. Umeme ndiyo ufunguo wa maendeleo ya viwanda na ni uhai wa maendeleo ya jamii. Mkoa wetu mpaka sasa haujaungwa na Gridi ya Taifa na katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati amesema hapa kwamba ifikapo 2023, Mkoa wetu utakuwa umeungwa na Gridi ya Taifa na hilo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu. Kuna vituo viwili vya kupozea umeme, Kituo cha Nguruka na Kidahwe. Nilikuwa nawasiliana mchana huu, je, ile site ambayo ilipendekezwa kijengwe kituo cha kupozea umeme kuna shughuli yoyote inayofanyika, jawabu ni kwamba hakuna chochote kinachoendelea na muda unaendelea kusonga mbele. Watu wa Kigoma tumekaa kwenye giza kwa muda mrefu, watu wa Kigoma wanaasili ya kufanya kazi sana, tuna mazao ya kimkakati ya michikichi ambapo mwaka kesho tunahitaji tuwe na viwanda, tunaomba tuungwe kwenye Gridi ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye Jimbo langu la Buhingwe, namshukuru Waziri na mkandarasi ambaye alitupa amesonga mbele, lakini naomba kasi iendelee kwa kuweka umeme kwenye Vijiji vya Janda, Murungu, Changwe, Kilelema na vingine vyote vilivyobaki ili na sisi pale pafunguke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri ustawi wa Taifa lolote ule utategemea maendeleo yaliyopo lakini ukiwa unaongezwa na kukuzwa na tafiti. Nimshauri Waziri wa Nishati awekeze kwenye utafiti kwa kuwa kule Uganda pamekwishagunduliwa mafuta kwenye Ziwa Albert na wataalam wa miamba wanasema kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu ambapo sisi Tanzania ni matajiri yawezekana tuna hazina kubwa ya mafuta na gesi basi utafiti uendelezwe na kuwepo mtaji wa kuweka kwenye tafiti ili tafiti ziendelee na tuendelee kubaini utajiri ambao Mwenyezi Mungu ametujalia.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naunga mkono hoja kwa asilimia 100, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii adhimu kwanza kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia kwa kutuletea bajeti nzuri. Nampongeza na Makamu wake Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Nampongeza Waziri wa Fedha, Naibu wake, Katibu na watumishi wote wa Wizara ya Fedha. Bajeti waliyoiandaa hakika inatibu kiu ya Watanzania. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru kwa namna ya pekee Waziri Mkuu kwa Mkoa wetu wa Kigoma jinsi anavyosimamia zao la kimkakati la Mchikichi, Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye hoja ya bajeti. Nimeipitia bajeti, nikaangalia Tanzania sasa hivi inakadiriwa kuwa na idadi ya watu milioni 60. Katika milioni 60, ni 5% tu ndio ambao ni direct tax payer, wanaolipa kodi moja kwa moja. Asilimia tano katika milioni 60 ni sawa na milioni tatu. Ukitoa kwenye milioni 60 unabakiza milioni 57 ambao sio walipaji wa kodi wa moja kwa moja. Nikajiuliza swali: Je, upo uwezekano wa watu milioni tatu kulipa kodi ambazo zitatosheleza Serikali itoe huduma kwa watu milioni 57? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri wa Fedha anisikilize kwa makini tuna kila haja ya kutafuta na kuangalia ni kwa namna gani tunaweza tukapanua wigo wa kodi. Wigo wa kodi ni lazima utokane na kupanua wingi wa shughuli za kiuchumi ndani ya nchi yetu, naomba nishauri, Tanzania tumejaliwa vyanzo vingi. Mungu ametujalia, lakini hatujavifanyia kazi. Mathalani Mkoa wetu wa Kigoma, Mungu ametupa ardhi nzuri, inastawi kila aina ya mazao, lakini ndani ya ardhi hiyo Mungu ametupa madini ya Dolomite ambayo ndiyo malighafi haswa ya mbolea ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atambue kwamba katika Mkoa wa Kigoma tuna madini ya Dolomite ambayo mimi mwenyewe niliwahi kuhusika kwenye kampuni iliyokuwa ya Kimarekani wakapita wa Anglo American walikuwa kwenye utafiti wa madini, walisema maeneo yafuatayo; Ilagara, Kazuramimba, Basanza, Makere na Kitagata ni maeneo ambayo yana malighafi ya kutengeneza mbolea ya kusaidia nchi hii na tunaweza tukafanya mapinduzi ya kilimo kwa kupata mbolea ambayo inaweza ikatengenezwa ndani ya nchi yetu. Naomba Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa jicho la pekee. Wakati wale wa Ngara wanasaidiwa kile kiwanda cha Nikeli na Liganga tuangalie uwezekano wa kuwa na kiwanda cha kutengeneza mbolea katika Mkoa wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikijiuliza, kwa nini tunaagiza chumvi kutoka nje wakati sisi kwenye ukanda wa ziwa wa bahari tuna vyanzo vingi vya kutengeneza chumvi? Ukienda kule kwenye Ziwa Eyasi upande Meatu Mkoa wa Simiyu, tuna deposit kubwa ya chumvi. Ukija Kigoma, ile miamba yote ya Uvinza ni chumvi. Kwa nini tusiweke uwekezaji mkubwa na tukazalisha ya kutosheleza na ile fedha ambayo tunaagiza bidhaa ya chumvi nje tukaitumia kwa mahitaji mengine na badala yake tukauza sisi wenyewe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuangalie mahali hapo kama sehemu mpya ambapo itakuwa ni chanzo cha mapato ya fedha ya Serikali na chanzo cha ajira kwa waliokosa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuendelea, ni lazima tufunge mkanda kwa kufanya mapinduzi katika kilimo chetu. Hata Ulaya waliendelea baada ya kufanya mapinduzi katika kilimo. Tunahitaji sekta ya umwagiliaji ipewe fedha. Zaidi ya hapo kwenye tafiti papewe kipaumbele. Hatuwezi tukasonga mbele kama hatuna tafiti. Tunaomba tafiti kwenye kilimo zipewe kipaumbele, kwenye madini zipewe kipaumbele na kwenye uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwenye uvuvi nayo ni sehemu ambapo tunaweza tukapata fedha.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri, mengine unaweza ukamwandikia Waziri, umechangia vizuri sana.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Azimio la Bunge la kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa upekee kabisa kwa kupata nafasi hii ili niweze kuchangia hoja kwenye Azimio la uanzishwaji wa Soko Huru katika Bara la Afrika.
Mheshimiwa Naibu Spika, azimio hili ni azimio zuri sana, linafaida nyingi sana, ningeomba kila Mbunge aweze kuridhia mkataba huu, una faida nyingi sana. Kwanza ukiangalia nchi yetu kijiografia Tanzania mahali ilipo tumebahatika kuwa sehemu nzuri kijiografia, tuna maliasili, tuna ardhi nzuri. Kwa hiyo ni suala tu la kujipanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuridhia mkataba huu utafungua masoko mapya kwa mazao yetu ya kilimo. Tunachangamoto ya mazao kama tulivyoona kwenye mahindi, lakini litafungua masoko mapya kwa mazao mengine madogo madogo kama alizeti na choroko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mkataba huu utaimarisha mnyororo wa thamani utakuwepo na nini na ushindani, ushindani wa uzalishaji ambao tunaenda kushindana katika soko hilo huru utaboresha ubora wa mazao yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo mimi ninashauri sana, ninashauri Serikali ijipange kwa kuelimisha kwa kutoa elimu kwa mapana na kwa marefu kwa wazalishaji wetu. Kama ni kilimo sasa twende kwenye kilimo cha biashara, tulime kilimo cha kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile taasisi za kifedha zijipange kupunguza riba na ziwe tayari kusaidia wazalishaji kwa maana ya wakulima na wajasiriamali wapate mitaji ili tuweze kusogea kwenda kwenye masoko ya mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takwimu ambazo zipo sasa hivi nchi ambayo ina uchumi mzuri kwenye hili soko ambalo tunaenda kwenye wale wanachama ambao wamekwisha saini ambao ni 42. Nchi ambayo ina uchumi mzuri sasa hivi ni Nigeria ikifuatiwa na Egypt, ikifuatiwa na Afrika Kusini, sisi hatupo mbali sana tupo kama namba 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sisi tuna nafasi nzuri kama Serikali ikijipanga ikahakikisha, ikaboresha miundo mbinu ili wakulima wetu huko wanako zalisha barabara zikafika, kukawepo na gharama ndogo za usafirishaji wa mazao yetu tutafaidika zaidi, zaidi na zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo azimio hili ni zuri, litatusogeza mbele, litaenda kuzalisha mabilionea wengi katika Tanzania yetu na litaenda kuleta mabadiliko makubwa sana katika sekta mbalimbali; sekta ya kilimo na biashara pia kutokana na ushindani utakaotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kuunga hoja Azimio hili la Mkataba wa Uundwaji wa Soko Huru la Afrika. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu ili niweze kutoa ushauri kwenye Mpango huu wa Maendeleo. Ushauri wangu utajikita katika maeneo matatu: Kwanza, ni kwenye zao la chikichi; pili, ni zao la kahawa; na kama muda utatosheleza basi nitakuwa na ushauri kwenye shughuli ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu idadi kubwa ya watu wamejiajiri kwenye kilimo. Asilimia 65 ambayo ukipiga hesabu kwa sasa hivi ambayo tumepata idadi ya milioni 61 ya Watanzania, kama asilimia 65 ndio inayoshughulika na kilimo, basi ukipiga hesabu kwa harakaharaka utakuta kwamba kilimo kimeajiri zaidi ya milioni 39.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu za mwaka jana 2021, Sekta hii ya Kilimo ilichangia kwenye pato la Taifa asilimia 26.1, ukilinganisha idadi ya wanaoshughulika na kilimo na kiwango kinachochangiwa kwenye pato la Taifa haviwiani kabisa. Hapa kuna gap, tunatakiwa tuangalie ni kitu gani kinachokosekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo ya jumla ambayo bado tunatakiwa tuyafanyie kazi. Kwa kuwa idadi kubwa ya Watanzania wamejiajiri kwenye shughuli ya kilimo, basi Serikali inahitaji kuwa na jicho pevu la kuwekeza hasa hasa kwenye shughuli za kilimo na hasa kwa kuboresha miundombinu ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na zao la chikichi; nchi yetu kwa mwaka imetumia zaidi ya bilioni 500 kuagiza mafuta. Mafuta mengine ambayo yanatokana na zao la chikichi ambalo tayari Mwenyezi Mungu amekwishatupa lipo Kigoma. Kigoma ina ardhi inayofaa kwa chikichi pamoja na Katavi. Nchi ya Malaysia ambapo tunaagiza mafuta walipata mbegu ya mchikichi kutoka Kigoma. Tunatumia zaidi ya bilioni 500 kuagiza mafuta ambayo tayari tungeweza kuzalisha Kigoma na hizo hela zingine zikatumika kwenye maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri, kwanza kabla ya kutoa ushauri nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ambayo ameifanya kwa Mkoa wetu wa Kigoma. Amehamasisha wakulima wapanue mashamba, walime na kweli wamehamasika na wamelima zao la chikichi mashamba sasa ni makubwa. Kituo cha TARI kimezalisha mbegu na miche mizuri wamehamasika. Changamoto ambayo Serikali inatakiwa ikafanyie kazi ili tuokoe hayo mabilioni ni kuleta viwanda vya kati vitakavyoweza kuchakata zao hili la michikichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda tulivyonavyo Kigoma ni vidogovidogo, kutokana na zao la chikichi, unapata mafuta haya ambayo ni ya kula tunayatumia kila siku, unapata chakula cha mifugo bado unapata malighafi ya kutengeneza samani za nyumbani na bidhaa nyinginyingi. Naomba kwenye Mpango huu wa Serikali, Wizara ya Kilimo ishirikiane na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kutafuta wawekezaji wa ndani na nje ili wajenge viwanda vya kuchakata mafuta katika Mkoa wetu wa Kigoma. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeokoa fedha nyingi na nchi itakuwa na uwezo wa kupata mafuta yenyewe ya kuzalisha mafuta na kutosheleza mahitaji ya ndani na ziada tutapeleka kwenye nchi zingine, tutauza kama biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, ni kwenye zao la kahawa. Kahawa ni zao la biashara ambalo linatuingizia fedha za kigeni. Katika nchi yetu ya Tanzania zaidi ya mikoa 16 inalima zao la kahawa. Tunashukuru kwa juhudi kubwa na tunamshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ruzuku ambayo ameiweka kwenye mbolea. Watu tunaolima kahawa ametugusa, tunasema mama ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili bado halijapewa kipaumbele na ndiyo mwarobaini ambalo linaweza likatuingizia fedha za kigeni. Ukilinganisha na nchi zingine ambazo wanazalisha lakini kwa maeneo madogo, bado miche inayozalishwa na TARI na TaCRI bado ni midogo ukilinganisha na nchi jirani. Uganda kwa mwaka wanazalisha miche ya kisasa bora zadi ya milioni 61. Ethiopia ambayo ndio wazalishaji wa kwanza wanazalisha miche kwa mwaka zaidi ya milioni 121, lakini sisi Tanzania kwa mwaka huu ndio tumeongeza tumezalisha miche milioni 21. Hiki ni kiwango kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tunayo maeneo makubwa na wananchi wamehamasika na tuna vijana wengi ambao wako mitaani, kama zao hili likiboresha, likawekewa pembejeo zote asilimia mia, sawa na korosho nina uhakika kwamba mapato yatakayotokana na kahawa yataongezeka na hela za kigeni zitaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mambo yafuatayo yafanyike, bado kwenye kilimo hicho hicho cha kahawa, tunahitaji kuwekeza kwenye tafiti. Naomba Mpango huu uoneshe ni namna gani ambavyo itawekeza kwenye tafiti za kupata miche bora na usambazaji wa matokeo yake ya utafiti na kwa kuwa kilimo ndio uti wa mgongo, basi Mpango unaokuja ni lazima, bora, vyema uoneshe namna gani ambavyo wakulima wataweza kupewa mafunzo pamoja na Maafisa Ugani ili uzalishaji uweze kuongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la kahawa, watu wamehamasika wanalima kahawa lakini soko lake limekuwa likipanda na kushuka. Mkulima amekuwa akilima lakini bila kuwa na uhakika wa masoko. Tunaomba Mpango wa Serikali katika bajeti ijayo ituwekee masoko, ituonyeshe masoko ili wakulima wawe wanalima wakijua kwamba masoko ya zao hilo la kahawa ni wapi na wapi. Tukifanya hivyo, basi Taifa litaweza kuingiza fedha nyingi za kigeni na uchumi wetu utaongezeka, utakua ili tuweze kufikia asilimia nane kama ilivyoelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu ni kwenye uvuvi. Tanzania katika Bara la Afrika ndio nchi iliyopendelewa na Mwenyezi Mungu tukapewa maziwa yote makuu, matano yako Tanzania, tuna Ziwa Tanganyika, Victoria, Rukwa, Manyara, Eyasi na maziwa mengine madogo madogo. Hata hivyo, mchango unaotokana na shughuli za uvuvi bado ni mdogo. Mwaka 1954 na mwaka 1957, Serikali ya Kikoloni ya Uingereza ilikuwa na Kituo chake cha Utafiti, walifanya majaribio wakachukua samaki aina ya sangara kutoka katika Ziwa Tanganyika ambalo halikuwepo katika Ziwa Victoria, wakaenda kufanya majaribio wakapata katika Ziwa Victoria kwa mwaka 1954 na 1957. Leo tunashuhudia sasa sangara inatuingizia fedha nyingi sana kutoka kwenye Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye upande wa uvuvi tuna vituo vile vya TAFIRI, viwezeshwe wafanye tafiti kutokana na haya maziwa madogo madogo ambayo tunayo. Wafanye tafiti ikiwezekana kama sangara anaweza bado akaenda kupandwa kwenye maziwa mengine madogomadogo au migebuka, au samaki wengine ziende kupandikizwa kwenye maziwa mengine madogo madogo ambayo sasa hivi mchango wake wa kiuchumi kwenye upande wa uvuvi ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ya nne ni kwenye biashara. Mkoa wetu wa Kigoma uko mpakani ile ni gateway ya biashara ambapo pale tunapakana na Wakongo ambao zaidi ya nusu ya watu wa Kongo wako kwenye ukanda wa mashariki. Tungeomba kwenye mkakati ujao Wizara ya Uchukuzi iwezeshe kutengeneza zile bandari za nchi kavu ile ya Katosho na kuhakikisha ukamilishaji wa meli katika Ziwa Tanganyika, zikamilike mapema ili mzunguko wa kibiashara ukamilike na uende vizuri ili ile SGR itakapokamilika tayari ile Kongo ya Kati kuanzia Kalemii, Bukavu, Bujimai, kuja mpaka huku Kindu wawe wamekwishazoea wote kuja kufanya biashara na Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye hoja ya Waziri wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimpongeze Mheshimiwa Daktari Philipo Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nimpongeze Mheshimiwa Kassim Majaliwa Waziri Mkuu wa Serikali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa iliyotukuka ya kutuletea maendeleo endelevu katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wana Buhigwe tunawashukuru sana kwa miradi mingi ambayo Mama ameleta. Tumejenga madarasa 53 kutoka kwenye fedha ya UVIKO, tumepata fedha za vituo viwili, tunashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi nyingine ya pekee kumpongeza na kumshukuru Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, lakini nimpongeze tena David Ernest Silinde Naibu Waziri wa TAMISEMI na Daktari Festo John Dugange kwa kazi kubwa wanazozifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze kwenye uchangiaji wa hoja. Nimesoma Hotuba yako mwanzo hadi mwisho, ninashukuru hotuba iko vizuri na mimi ninaiunga mkono. Ukurasa wa 46 kwenye miradi ya kimkakati Buhigwe ni Wilaya mpya ni Wilaya changa, bado tuna mapungufu makubwa sana. Mapato yetu ya ndani ni madogo sana, hatuna stendi ya Wilaya kwa ajili ya mabasi, hatuna stendi ya malori, hatuna soko la Makao Makuu la Wilaya. Ninamuomba sana Waziri wa TAMISEMI atukumbuke katika mpango wake, katika bajeti yake ya 2022/2023 kutupa mradi wa kimkakati utakaoweza kutuongezea mapato ikiwa ni pamoja na stendi ya mabasi, stendi ya malori na soko la Wilaya la kimkakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 66 na ukurasa wa 105, nimeona pale kwenye upande wa TARURA kwenye bajeti yako umeeleza kinagaubaga kwamba kwa mwaka 2022/2023 madaraja na vivuko 322 vinaenda kujengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Buhigwe tuna matatizo makubwa sana ya kimawasiliano, tunalo daraja ambalo ni muhimu sana la kuunga Wilaya ya Buhigwe na Wilaya Kigoma Kaskazini, ukitokea daraja hilo lijengwe ukitokea kwenye Kijiji cha Kigogwe kwenda kwenye Gereza la Kwitanga. Kwenye bonde la mto huo kuna vijiji takribani Nane ambavyo vinalima sana zao la tangawizi na vimeitikia mwito wa zao la chikichi ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelisimamia kweli. Vijiji hivi ni Kigogwe, Mrungu, Kishanga, Munzenze, vyote hivi vinahitaji viunganishwe, daraja hili ni kubwa nalo ni la mto Ruiche. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambasamba na hilo nichukue nafasi ya pekee kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Shilingi Milioni 500 alizotupatia, ninaomba tena kwa bajeti ijayo atupatie Milioni 500 kwa Majimbo ili tuweze kutengeneza tena barabara zetu huko Majimboni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu wananchi wamefanya jitihada kubwa sana. Kuna maboma makubwa ya Zahanati, maboma hayo ya Zahanati yapo katika Kijiji cha Kitambuka, Msagala, Ndoha, Mulungu, Kimara, Mbanga, Chagwe, ninaomba na Waziri wa TAMISEMI ananisikia kwa dhati kabisa Wanabuhigwe wamenituma haya maboma ya Zahanati yana zaidi ya miaka saba yanahitaji kupauliwa tu, Milioni 50 zinatosha tungeomba utusaidie katika bajeti ijayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na maboma ya zahanati ni kwenye Elimu. Buhigwe kuna Kata ambazo zimefanya jitihada zimejenga zenyewe zinasubiri msaada wa kupaua, maboma yako tayari kwa ujenzi wa shule za sekondari nayo yamejengwa katika vijiji vifuatavyo, Kilelema, Mbanga, Chagwe, Kirungu na Songambele, tunahitaji katika bajeti ya mwaka ujao na Wizara hiyo ilione.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii ya pekee kuungana na Wabunge wenzangu kwa kutambua kazi kubwa wanayoifanya Madiwani, posho na mshahara wanaoupata hauwatoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo awali posho za Madiwani zilikuwa ikilipwa na Halmashauri, posho zao zilikuwa zikilipwa na Wakurugenzi, ninaomba ikiwezekana uelekeze sasa viwango vile vilivyokuwa vikilipwa na Halmashauri vikawaendee Wenyeviti wa Serikali za Mitaa, Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wanafanya kazi kubwa sambamba na Watendaji wa Vijiji lakini Serikali imewasahau wanaacha shughuli zao usiku na mchana wanafanya kazi za kusimamia miradi yetu, Serikali iwakumbuke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo machache ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii ambayo umenipa. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mheshimiwa Bashe Waziri wa Wizara ya Kilimo na watendaji wakuu wote wa Wizara ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisoma hotuba hii ya kilimo ukurasa ule wa 83, nimejiuliza, na umezua manung’uniko makubwa sana kwa sisi wakulima wa kahawa. Mazao ya korosho, pamba na tumbaku ni mazao ya kimkakati sambamba na zao la kahawa. Haya matatu yana ruzuku, lakini zao la kahawa halina ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia katika mauzo ya nchi, zao la kahawa kwa muhula uliopita limetuingizia Tanzania Dola za Kimarekani milioni 142, tumbaku milioni 90. Tumbaku ina ruzuku, lakini zao la kahawa ambalo linatuingizia fedha nyingi za kigeni halina ruzuku. Ninaleta kwako manung’uniko makubwa sana ya wakulima wa kahawa kutoka katika Mkoa wa Kagera, Ruvuma, Songea, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha, Kigoma, Mara, Tanga, Njombe, Iringa, Manyara, Katavi, Morogoro, Mwanza, wanaomba ruzuku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii Serikali inatakiwa iwe na will. Haiwezekani kabisa tukalia miaka yote. Ukilinganisha na nchi zinazolima zao hili la kahawa, ukiangalia Uganda ambayo kila mwaka inauza tani 389,000 na Ethiopia ambayo inauza zaidi ya 457,000 uzalishaji wao unaongezeka, lakini sisi unadorora, sababu kubwa ni kuwepo kwa manung’uniko kutoka kwa wakulima wa kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nitoe mapendekezo yangu ili hakika kabisa kuwepo na mapinduzi makubwa katika uzalishaji wenye tija wa kahawa nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja. Serikali iweke mipango madhubuti ya kuendeleza zao la kahawa. Mpaka sasa hivi hakuna mipango chanya yoyote ile ya kuendeleza zao hili la kahawa ambayo inaonekana licha ya kutupatia fedha nyingi za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili. Kipaumbele kiwekwe kwenye uzalishaji wa mbegu bora na miche bora. Sisi Tanzania kwa takwimu iliyopo kila mwaka tunazalisha miche bora milioni 20, wenzetu wa Uganda kila mwaka milioni 124, tuongeze ruzuku hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele imeshagonga.
MHE. KAVENJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninaomba angalao hata dakika mbili. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Mheshimiwa umemaliza muda. Sentensi yako ya mwisho imeeleweka, nimeikatiza kwenye sehemu inayostahiki.
MHE. KAVENJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi ninaunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii, kwanza nichukue nafasi ya pekee kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye mchango wangu nataka kuzungumzia juu ya upungufu wa mafuta ya kula. Kwanza nimpongeze Waziri Mkuu wa hamasa kubwa ambayo ameitoa katika Mkoa wa Kigoma hasa kwenye kilimo cha michikichi. Michikichi sasa hivi inalimwa katika Wilaya za Kakonko, Kibondo, Kasulu, Buhigwe, Kigoma na Uvinza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wameitikia kilimo hiki kinaenda kuondoa uhaba wa mafuta ya kula nchini, kinachohitajika kwa Wizara hii ya Viwanda na Biashara ni kusaidia hawa wakulima kuhakikisha kwa haraka sana kwasababu wameitikia na wamelima mashamba makubwa sana kuhakikisha wanatengeneza mazingira mazuri ya kuleta viwanda vya kuchakata mawese Kigoma. Wakileta viwanda vikubwa ambavyo vitakamua mawese pamoja na bidhaa nyingine zinazotokana na michikichi uchumi wa Kigoma utabadilika na uchumi wa nchi nao utabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze SIDO wanao mchango kwa wakulima wa michikichi, wanatoa mashine ndogo ndogo za kukamua mawese, wanatoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali wanaojishughulisha na ukamuaji wa mawese, lakini shida ni moja tu riba ambayo wanaitoa kwa vikundi hivyo vya wajasiriamali ni kubwa. Mikopo hiyo ina riba ya zaidi ya asilimia 18 hadi 21; riba hiyo ni kubwa kwa wakulima, haiwezi kuleta tija kwenye makundi ya wajasiriamali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali kwa dhati kabisa ili kuharakisha na kuondoa upungufu wa mafuta ya kula nchini cha kwanza Kigoma tuhakikishe vinaletwa viwanda vitakavyokamua michikichi ili tupate mafuta ya kula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili Kigoma ina mazao mbalimbali, tuna zao lingine ambalo tumelishahau ni zao la mihogo ambayo inalimwa katika Wilaya zote za Kigoma, wakulima wa Kigoma wanavuna mihogo haina soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa Kigoma wanaiomba Wizara ya Viwanda kupitia TANTRADE mtuhakikishie, mfanye jitihada za kututafutia soko la mihogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zao lingine ambalo tunahitaji msaada mkubwa sana kwa TANTRADE kututafutia soko ni tangawizi, takribani sasa Wilaya yote ya Buhigwe inalima tangawizi. Zao hili ni zao ambalo nalo ikiwezekana likawekwe kuwa zao la kimkakati. Tunaomba TANTRADE na Wizara ya Viwanda ihakikishe, itusaidie watu wa Kigoma kutuletea kiwanda cha kuchakata tangawizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine naenda kuchangia ni kwenye biashara. Miaka ya nyuma Mkoa wa Kigoma ulikuwa ni mashuhuri sana kwenye biashara, lakini sasa hivi biashara zimedumaa. Hii imetokea ni baada ya meli ambazo tulikuwa tunazitegemea katika Ziwa Tanganyika ambazo zilikuwa zikisafirisha bidhaa na wafanyabiashara kwenda Congo, kwenda Burundi, kwenda Zambia, meli hizi ni Liemba na Mwongozo zilikwishaharibika ziko grounded. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali meli hizi zitengenezwe ili kuwepo kwa biashara na majirani. Mkoa wetu wa Kigoma ndio mkoa ambao unapakana na nchi karibu tatu ambazo Mashariki yake kuna idadi kubwa ya watu lile ni soko, tunaomba Wizara ya Viwanda itengeneze mazingira na kuhakikisha inaleta wawekezaji waweke viwanda katika Mkoa wetu wa Kigoma ili uchumi wetu uinuke sambamba na wa nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii ya kuwa mtu wa kwanza katika kuchangia hotuba ya TAMISEMI kwa jioni ya leo ya tarehe 14 mwenzi wa nne mwaka huu wa 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza wananchi wa Buhigwe wamenituma nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Tanzania kwa fedha nyingi sana ambazo amepeleka katika Wilaya ya Buhigwe. Amefungua wilaya yetu na ameendelea kufungua mkoa wetu. Amefanya nini katika Wilaya yetu ya Buhigwe? Amegusa Maisha ya wananchi ya kila siku katika yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 tulipata shilingi 3,336,624,000,901 ambazo zilikuja kwenye ukamilishaji wa maboma ya shule za msingi, ukarabati wa shule kongwe, ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi, ukamilishaji wa zahanati, ununuzi wa vifaa tiba kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati. Wananchi wa Buhigwe wanasema ahsante sana. Wanatoa shukrani za dhati kwa Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki pamoja na Manaibu wake Mawaziri akiwepo Mheshimiwa Festo pamoja na Mheshimiwa Ndejembi kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi ya pekee kwa kuwashukuru kwa utaratibu mzuri ambao mwaka huu tumeuona. Walituita wakiwa na kikosi kazi cha TAMISEMI, tukakaa nao sisi kama Wabunge wa kila mkoa na wakatupa nafasi ya kutoa vipaumbele vyetu na changamoto. Katika nafasi hiyo, kuna methali Waswahili wanasema, “kiu isiyoweza kuishia kwenye mto, hiyo ni kifo.” Basi tuliweza kutoa changamoto zetu, tukatoa vipaumbele vyetu na tumeona kwa uhakika waliyapeleka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ameyajibu kwa matendo. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika upande wa afya, tumeona kazi kubwa sana kwa wilaya ambayo ni changa. Tumepata vituo vitatu vya afya. Kituo cha Kajana, tulipata shilingi milioni 500, Mayaya shilingi milioni 500 na Lusaba shilingi milioni 500. Tunategemea mwezi wa Saba vitaanza kutoa huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo tumepata fedha za kumalizia maboma ya zahanati katika vijiji sita, tulipata shilingi milioni 300. Wananchi wa Buhigwe pamoja na viongozi wote wa vyama vyote na wa madhehebu yote wamenituma nije nitoe shukrani kwa Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye TARURA, katika miaka hii miwili ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametusaidia pakubwa. Japokuwa mahitaji yetu ni makubwa, lakini tulipata shilingi bilioni 5.9 ambazo zimeweza kutujengea kilometa tano za lami Makao Makuu ya Wilaya na tukajengewa kilometa 1.2 ya lami na kilometa moja. Mpaka sasa hivi tunao mradi mwingine ambao tumeupata, na tumepatiwa fedha. Mradi huo unatoka katika Kata ya Muyama kupitia Kasumo kwenda Kasulu kilometa 12, ambazo zitagharimu fedha ya Kitanzania shilingi bilioni 15.6, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utawala bora, Mheshimiwa Rais ametusaidia parefu na pakubwa sana. Kwa miaka mingi tulikuwa hatuna Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, alitoa fedha na mwaka 2022 tarehe 16 Mwezi wa Kumi yeye mwenyewe amekuja kuizindua. Sambamba na hilo, ujenzi wa Mahakama ya Wilaya umeshakamilika na huduma zinaendelea kutolewa. Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Buhigwe umeanza kujengwa. Tunamshukuru sana, tunampongeza sana na Mungu ambariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na shukrani, bado tunazo changamoto nyingi. Moja, tunao upungufu mkubwa kwenye kada ya watumishi wa afya. Mahitaji yetu kwenye afya ni wafanyakazi 819, waliopo ni 210 pungufu ni 609. Tuna upungufu wa asilimia 75. Tunaomba ajira mpya mtupe kipaumbele mlete watumishi. Kwenye upande wa elimu, mahitaji ni walimu 1,487; waliopo ni 692, pungufu ni 794, sawa na asilimia 55. Kwenye ajira hizi mpya tunaomba Serikali ituangalie kwa jicho la huruma na kwa upendo mkubwa mwaelekeze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi maalumu kwa vijana wanaojitolea wa tasnia ya elimu. Kuna vijana wengi ambao wamejitolea baada ya kumaliza vyuo vyao, wapo kwenye shule zetu za kata, wapo kwenye shule zetu za Serikali, hao ndio wahimili, ndio wazalishaji, na wameshatoa mchango mkubwa. Naomba sana, katika hizi ajira mpya ambazo zimetolewa kwa moyo wa dhati na kwa huruma ya Mungu, hawa wapewe kipaumbele. Wapewe kipaumbele katika ajira hizi zilizotangazwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la pili, pamoja na kwamba tumepata vituo vya afya, bado tuna kata ambazo zina idadi kubwa ya watu, na uzuri watu wa kule Buhigwe wameshajipanga kwa ajili ya kuchangia kwenye shughuli za maendeleo. Kata ya Muhinda na Kata ya Mubanga wameshachagua sehemu ambayo wakipata fedha ya kujenga kituo cha afya ambacho kitasaidia wananchi zaidi ya 45, wameshaanza na mchakato wa kufyatua tofali. Tunaomba kituo cha afya kijengwe katikati ya Kata ya Muhinda na Mubanga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi lingine ni kituo cha afya tena ambacho kitasaidia tena kata mbili na ni mpakani mwa Burundi kabisa kuna watu wengi, zaidi ya 44,000, nayo ni Kata ya Mkatanga na Kata ya Kibwigwa. Kituo hicho kije kijengwe katikati ya Kata ya Kibwigwa na Mkatanga, nao wameshachagua sehemu yao ambayo inaitwa Muharuro hapo ni center nzuri sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo marefu, nakushukuru sana, naishukuru Serikali, najua imesikia na itatekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi ya pekee kukushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya Waziri wa Kilimo. Awali ya yote nimpongeze kwa kazi kubwa na nzuri ambayo yeye mwenyewe Mheshimiwa Bashe na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde wanaifanya, hongereni sana.
Mheshimiwa Spika, Baada ya kutoa pongezi, kwa kuwa muda ni mfupi naomba niende moja kwa moja kutoa mchango wangu kwenye hotuba yako hasa kwenye mazao ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimeipitia hotuba ya Waziri wa Kilimo. Nimeenda kwenye jedwali kwenye mazao ya biashara. Yapo mazao saba yanayotuingizia fedha nyingi za kigeni nayo ni tumbaku, kahawa, chai, korosho, pamba, pareto na mkonge.
Katika mazao haya saba kwa msimu huu wa kilimo wa 2022/2023 zao ambalo limeingiza fedha nyingi za kigeni ni zao la kahawa, limetuingizia fedha USD 204,670,147 likifuatiwa na tumbaku ambayo imetuingizia USD 154,084,169 likifuatiwa na pamba ambayo imetuingizia USD 147,135,803 na zao ambalo ni la mwisho na limetuingizia kiwango kidogo ni pareto ambalo limetuingizia USD milioni 5,484,927. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo nchi ambazo uchumi wake umekua kutokana na mchango wa kahawa. Brazil ndio nchi ulimwenguni ambayo kabisa ni mkulima na mzalishaji mkubwa na imetajirika kwa sababu ya zao la kahawa. Katika Afrika tunazo nchi, ipo Uganda imetutangulia mbele, lakini ipo Ethiopia. Ukienda kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025 inasema hivi; “Ifikapo mwaka 2025 zao hili la kahawa kwa mwaka tuwe tuna uwezo wa kuzalisha tani 161,000,” lakini mpaka sasa hivi ndiyo tumefikia tani 80,000 na ndizo hizi zimetuletea hizi fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe ushauri mkubwa kabisa kwa kulinganisha na majirani zetu. Ukiangalia tukijilinganisha na Nchi jirani ya Uganda ambayo sisi katika nchi yetu kahawa inalimwa katika mikoa 16 ukitafuta arable land, ardhi inayofaa kwa zao hili ni zaidi ya mara tatu ya ardhi ambayo inalimwa kahawa Uganda, lakini wao wenyewe kwa mwaka huu, kwa msimu huu wameingiza USD milioni 800, kiwango hicho ni kikubwa tukijilinganisha.
Mheshimiwa Spika, zipo jitihada ambazo bado kama nchi tunatakiwa tufanyie kazi. Ni zao pekee hili la kahawa ambalo linaweza likawa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Bado kuna nafasi kubwa ya juhudi ambazo zinatakiwa zifanyike, nchi inatakiwa iwekeze, pamoja na kwamba, imekwishaandikwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ukiangalia kwenye uzalishaji kwa miaka hii miwili, mitatu, tukianzia na msimu ule wa 2019 na 20 tulizalisha tani 73,000, mwaka uliofuatia tani 70,000, msimu uliofuatia 66,000 tulishuka, lakini sasa tumepanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inatakiwa ichukue hatua madhubuti kwanza ili tuweze kuwa na malengo makubwa. Tuwe na malengo makubwa ya kuhakikisha kiwango cha uzalishaji wa kahawa ambayo ndio zao namba moja ambalo limetuingizia fedha za kigeni ni lazima Serikali iwekeze. Sehemu za kuwekeza kwanza ni lazima uwe na uwezo wa kuzalisha mbegu bora katika mikoa yote ambayo inalima kahawa kwa kuitumia TACRI. Uganda kwa mwaka huu wenyewe wanaenda kuzalisha miche bora milioni 171, Ethiopia wanaenda kuzalisha miche bora ya kahawa milioni 362, sisi milioni 20, kiwango hicho ni kidogo, hakiwezi kuleta mapinduzi ya kilimo cha kahawa na kikachangia kwenye uchumi wetu. Kwa hiyo, zinahitajika jitihada. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lazima tuwe na malengo makubwa tutoke kwenye milioni 20 twende hata kwenye milioni 200 halafu tuigawe hiyo miche, tupanue mashamba, tuwawezeshe wananchi ambao tayari wanajishughulisha na kilimo hiki cha kahawa, tuwawezeshe vijana kufungua mashamba mapya na tuwape mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ya pili, naomba nichangie tena kwenye zao la chikichi. Kwanza nampongeza Waziri na sisi watu wa Kigoma tunamshukuru sana kwa sababu, kwenye bajeti hii tumeona chikichi kwa mara ya kwanza imeenda kupata ruzuku, inaenda kuwa mkombozi. Itaenda kuokoa bilioni 470 ambazo Serikali inatumia kwa ajili ya kununua mafuta ya kupikia na kuyaleta humu nchini. Yafuatayo yanatakiwa yafanyike ili kuhakikisha uzalishaji wa chikichi unaongezeka.
Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Kandege ambavyo amekwishazungumza ukitoka Kigoma, Katavi mpaka Rukwa ule ukanda wote ni wa hali ya hewa ambao unaweza ukakuza zao la chikichi, ule mpango wa Waziri sasa wa BBT wa zile block farms ndio wakati wake sasa. Serikali ije kuyafungua mashamba hayo, iwatayarishe vijana na iwape mashamba hayo wayasimamie, itachukua muda mfupi tu tutaweza kujitegemea kwa mafuta na tutakuwa tumeokoa fedha hizi za kigeni ambazo tunazitumia katika kuingiza mafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zao la tatu ni tangawizi, nalo linalimwa katika Jimbo langu la Buhigwe. Tunavyo vijiji zaidi ya kumi ambavyo sasa hivi vinashughulika na kilimo cha tangawizi. Tangawizi ni mojawapo ya viungo muhimu sana, kwa hiyo, tunaomba katika bajeti hii Waziri ajitahidi na aoneshe namna gani Serikali inaweza kuboresha miundombinu ili kuongeza kipato cha wakulima wa tangawizi na hasa kwa kuwaletea viwanda vya kuchakata zao la tangawizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa fursa hii na mimi kuchangia kwenye hoja ya Maliasili na Utalii. Awali ya yote nichukue nafasi ya pekee kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwa mhifadhi namba moja na mtangazaji wa vivutio vya utalii namba moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili ninampongeza Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango kwa juhudi kubwa na kazi kubwa anayoifanya ya kuhifadhi mazingira hapa nchini. Kipekee nishuke kwa Mheshimiwa Waziri nimpongeze rafiki yangu Mchengerwa mtu kazi pamoja na Dada Mheshimiwa Mary Masanja, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi Said, Naibu Katibu Mkuu Anderson Mutatembwa kwa kazi kubwa wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja waliyoiandaa ambayo sasa tunaijadili kuna mikakati mikubwa sana. Katika mchango wangu nitachangia mambo mawili tu. Moja ni maombi kwenye sehemu mbili ambazo zina migogoro kule Mkoani Kigoma. Mgogoro wa kwanza lipo eneo ambalo lina itwa Kagerankanda iko Kasulu, eneo hilo ni tegemeo kwa kilimo cha mahindi na maharage kwa Wilaya karibu tatu za Kasulu, Buhigwe na Kigoma Kaskazini. Uko mgogoro ambao umedumu kwa muda mrefu kati ya TFS na wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mgogoro huu chanzo chake ni TFS. Mvua zinapoanza kunyesha wakulima huruhusiwa kwa sababu hawajui mipaka na mipaka haijajulikana, TFS wanawaacha wanalima, wanapalilia, wanaweka mbolea ikifika wakati wa kuvuna kiangazi kama hiki, wanawazuia kuvuna mazao yao au wakienda kwa kujificha wanawanyang’anya mazao yao, hiyo ni dhuluma! Ninakuomba Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mchengerwa mtu kazi ushuke pale ndani ya Wilaya ya Kasulu uwasikilize wakulima utatue mgogoro huo na mipaka iwekwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa pili ni wa Kijiji cha Karirani kiko katika Wilaya ya Uvinza, kinapakana na Hifadhi ya Milima ya Mahale. Kijiji hiki kilisajiliwa mwaka 1995 na kina barua ya usajili ya tarehe 5 Juni, 1995 na kina usajili wa Namba 244. Kuna taharuki kubwa sasa hivi katika kijiji kile. Tarehe 13 Machi mliwapelekea barua kuwaonesha katika vitongoji vinne kati ya vitongoji vinne katika Kijiji cha Karirani vitongoji viwili mnasema viko kwenye sehemu ya hifadhi. Vitongoji hivyo ni Mahasa na Kabukuyungu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vitongoji hivi vina kaya 479 zenye idadi ya watu 1,721. Kuna taharuki kubwa, hawa ni Watanzania, wamekaa pale zaidi ya miaka 28. Eneo hilo ambalo mnarudisha kwenye hifadhi ya Milima ya Mahale lina Shule ya Msingi, lina makanisa sita, lina misikiti miwili na taasisi zingine za Kiserikali wana nyumba za kudumu. Mmepeleka barua mwezi wa Tatu tarehe 30 mnatuma Kamati ya Ulinzi na Usalama kuwajazisha fomu waondoke bila kuongea nao. Hiyo siyo halali, haikubaliki! (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haiwezekani hifadhi yoyote ile conservation is for human development ni kwa ajili ya maendeleo ya watu. Ni lazima mshuke muwashirikishe wananchi. Hatukatai, tunajua mnayo programu ya kuhakikisha kwamba zile shoroba ambazo zilijengwa sasa ziwe wazi lakini muende kwa utaratibu wa kiutu. Tunataka fedha lakini hatutaki migogoro. Hatutaki kuona kila mwaka kwenye taarifa au kwenye ripoti kwamba askari wangapi wameuawa, au wananchi wangapi wameuawa. Hatutaki fedha tutakazozipata kutoka kwenye Wizara hii zingine ziwe zimeambatana na damu ya watu. Itakuwa ni dhuluma, hatuwezi kubarikiwa kama Taifa na hatuwezi kupata baraka. Ninakuomba sana ushuke pale Karirani uwasikilize wananchi wako, ni Watanzania uwasikilize muyaweke mambo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ni ya ushauri. Nimesoma bajeti yako ukurasa ule wa 27 kuna biashara ya hewa ya ukaa, nami ninaenda kuungana na Mheshimiwa Reuben kwamba makusanyo yanayokusanywa na Wizara yako bado ni madogo. Sasa hivi kuna biashara ya hewa ya ukaa na nimeona mmeingia mkataba na kampuni mbili. Ipo Kampuni hii moja ya Singapore ambayo inaonekana tayari mmekwisha ingia mkataba na mmelipwa shilingi bilioni 8.4. Je, mmeshindanisha? Bado mmeingia tayari kwenye mkataba na Falme za Kiarabu kuna Kampuni hapo inaitwa Carbon Cop; je, mmeshindanisha? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika nchi hii kwenye maliasili kwenye misitu tunayo misitu ambayo ni natural forest zaidi ya 452 na tunayo misitu ambayo iko chini ya Halmashauri ambayo inamilikiwa na Halmashauri 46 lakini inatia aibu mpaka sasa hivi katika nchi nyingi wenzetu majirani wa Kenya wanavuna fedha nyingi kutokana na biashara hii ya ukaa, sisi bado tuna misitu hii miwili. Je, mmekwisha fanya tathmini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hii ya hewa ya ukaa imezungumzwa kwenye Wizara ya Mazingira na ninyi mmeizungumza. Je, fedha ambayo sasa mmepanga au kwenye mkataba huu ni Wizara ipi itakayohusika na makusanyo hayo? Ninaomba utakapokuja ku-finalize mtuelekeze ni Wizara gani hasa itakayohusika kwa sababu Wizara ya Mazingira ndiyo imetoa mwongozo namna gani hiyo biashara inaweza ikafanyika lakini tunaona tayari kwenye mikataba tayari iko ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na tunaomba hawa TFS ambao wanatumia nguvu kubwa kupitia Askari Wanyamapori ambao wanatumia nguvu kubwa ya kuonea wananchi waumize kichwa sasa hivi wasaidie namna ya kuwashirikisha wananchi kwa sababu wananchi ndiyo wahifadhi namba moja. Hakuna usalama bila kushirikisha wananchi. Hao ndiyo wahifadhi namba moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo mimi ninakushukuru sana, ninaunga mkono hoja na ninakuombea sana kwenye lile jambo lako ambalo umeomba tunakuombea ushindi wako itakuwa ni heshima kwetu. Uthubutu wako ni heshima kwetu na Mungu akutangulie na akubariki sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi niweze kuchangia kwenye hii Bajeti Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba kwa niaba ya wananchi wa Buhigwe na wananchi wa Mkoa wote wa Kigoma nitoe pongezi za dhati kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kazi kubwa sana ambayo anaifanya kwa kufungua Mkoa wetu akishauriwa na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdory Mpango. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana Mkoa wetu wa Kigoma umeendelea kufunguliwa katika Awamu hii ya Sita kupitia miundombinu ya Barabara, sasa Mkoa wa Kigoma tunaenda kuunganishwa rasmi na Mkoa wa Tabora. Tunayo barabara ambayo Mheshimiwa Rais ametoa fedha kulikuwa kumebakia na kipande kidogo cha kutoka Kazilambwa mpaka Magu mpaka Chabu pale Nguruka kilometa 36 Mkandarasi yuko site. Kulikuwa tumebakia kipande cha kilometa 51.1 cha kutoka Malagarasi hadi Uvinza Mkandarasi yuko site tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaenda sasa kuunganishwa na Mkoa wa Kagera kuanzia Kakonko kuja Kibondo sasa ni lami, tuna kipande kingine ambacho sasa ni cha Mvugwe – Nduta kilometa 59 Mkandarasi yuko site, tuna Mvugwe – Kanyani kilometa 70.5 Mkandarasi yuko site, na tuna Kasulu Manyovu kilometa 68 Mkandarasi yuko site, tunashukuru sana. Miradi hii inaenda kugharimu zaidi ya bilioni 560 katika mradi huu mkuu wa kutuunganisha na Mkoa wa Kagera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na barabara hii ndani yake kulikuwa na miradi ya bakshishi inaitwa complimentary projects. Miradi hii ilitakiwa kwa kadri inavyotekelezwa tuliomba na inatakiwa kwenye mujibu wa mkataba na inatakiwa miradi ile ambayo ni bakshishi ya mradi huu nayo iwe imetekelezwa. Ndani ya hizi bilioni zaidi ya 560 zipo bilioni 23 kwa ajili ya kutengeneza shule ya Sekondari ya kisasa Buhigwe. Tunaomba Serikali sasa iandae utaratibu ili hii miradi ambayo ni complimentary projects ya mradi huu mama nayo ianze kutekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo ujenzi wa kituo cha mabasi kule Manyovu na ujenzi wa kituo cha forodha tuongeomba navyo utekelezaji wake uende sambamba. Upo ujenzi wa kituo cha afya Makere nao tungeomba ujenzi huo uanze mara moja. Pia upo ukarabati wa stendi ya Kibondo pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Kibondo, tungeomba navyo viende sambamba. Tunashukuru sana Mheshimiwa Rais, sambamba na hilo tunamshukuru na Waziri wa Fedha Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya, endeleeni kutoa fedha kwenye miradi inayounganisha na inayoenda kuufungua Mkoa wetu wa Kigoma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kushukuru ni kuomba, tunaomba tena sisi tupo mpakani mwa Burundi na Congo, bado tunazo barabara muhimu ambazo hizo zikitengenezwa kwa kiwango cha lami zitaleta tija, zitaongeza mapato katika nchi yetu lakini zitachagamsha biashara kati ya nchi ya Tanzania na Burundi na Congo. Barabara hizi nazo zimekwishafanyiwa usanifu ningeomba kwenye bajeti hii ya 2023/2024 nazo zitengenezwe kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hiyo ni ya Kalela – Muzenze – Janda kilometa 57 na barabara ya Buhigwe – Muyama – Kilelema – Kitundu kilometa 120 na barabara ya Kakonko – Muhange kilomita 38. Hizo barabara zote zinakwenda kutuunganisha na nchi ya Burundi na Congo ambapo sasa tunaenda kufanya bishara nao. Tukifanya nao biashara, kama Kigoma itafanywa kuwa Mkoa wa kiuchumi, ikafanyika kuwa ndiyo hub ya uchumi, Tunaamini nchi hii itaenda kukuza uchumi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo ombi lingine ambalo ni malalmiko ya muda mrefu ya wafanyabiashara. Wafanyabiashara wana mangung’uniko wana malalamiko kwenye mfumo wa ETS, ningeomba sana Serikali pamoja na Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo ya ETS pamoja na wafanyabiashara, wakae pamoja waangalie namna gani ambavyo wanaweza wakaondoa malalamiko au minong’ono au manung’uniko ya wafanyabiashara ili bei iweze kushushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kuchangia tena kuhusu kilimo. Sisi kwenye Jimbo letu la Buhigwe tuna kituo cha TaCRI ambacho kinazalisha mbegu na miche bora ya kahawa. Kwa mwaka 2022/2023 tumeona zao la kahawa ndiyo zao ambalo limeongoza kuipatia nchi zaidi ya bilioni 248 fedha ya kigeni. Ninaishauri Serikali ili iweze kupata fedha nyingi za kigeni ni lazima kuwepo na mkakati wa dhati wa kuhakikisha maeneo na mashamba yanayolimwa kahawa yanaongezeka, pia kuwepo na kusudi madhubuti kabisa la Serikali kusaidia Wizara ya Kilimo, iweze kuzalisha miche ya kahawa kutoka milioni 20 ambayo inazalishwa sasa ifike zaidi ya milioni 200. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia wenzetu wa Uganda kwa mwaka wanazalisha miche milioni 161, ukenda Ethiopia wanzalisha miche zaidi ya milioni 360. Kwa nini sisi ambao tuna eneo kubwa kabisa linalofaa kwa kulima kahawa, zaidi ya Mikoa 16 sasa hivi inalima kahawa, kwa nini tuzalishe miche 20,000 kwa mwaka? Haitoshi! Hili zao lenyewe ndiyo linalotuingizia fedha nyingi za kigeni, ningeomba muangalie wakulima wa zao la kahawa, mtafute namna gani ambavyo mnaweza Serikali ikaongeza nguvu pale miche iongezeke na ikiwezekana zao hili la kimkakati nalo liangaliwe ni namna gani ambavyo hawa wakulima wanaweza kupewa ruzuku, kwa sababu ni sehemu ambayo Serikali inapata fedha nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa pili niende kwenye biashara. Mkoa wetu wa Kigoma umepakana na nchi ya DR Congo, Burundi na Zambia. Katika Ziwa letu Tanganyika, bado hatujapata meli. Meli zote zilisimama, tunahitaji meli ili biashara zilizokuwa zikifanyika siku za nyuma kwenda Zambia kwenda Moba, kwenda Kalemi, kwenda Ubwari, kwenda Uvira, kwenda Goma kwenda Gbadolite. Palikuwa pamechangamka na Mkoa ulikuwa umechangamka zirudi. Tunaomba bajeti hii ambayo imeelekeza na imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya nazo zitengenezwe ili kupunguza changamoto hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kuunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa fursa hii. Kigoma tuna kilio cha umeme tangu nchi yetu ipate uhuru miaka 60 iliyopita, Kigoma na Katavi hatujaunganishwa kwenye grid ya Taifa. Viongozi wa Taifa wa ngazi za Kitaifa wamekuwa wakifanya ziara mbalimbali katika Mikoa ya Katavi na Kigoma na kutoa ahadi ya kuunganisha mikoa hiyo katika grid ya Taifa kwa muda mrefu, lakini mpaka sasa hivi miradi hiyo haijakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri mwaka 2019 tarehe 25 Machi, 2019, Serikali iliahidi ifikapo mwezi Aprili, 2020 Kigoma itakuwa imeungwa na umeme wa grid ya Taifa na ilisema tayari bilioni 87 zipo tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, leo tuko mwaka 2022 mradi huo haujakamilika, hizo bilioni 87 zilienda wapi? Haitoshi tu, mwaka jana tarehe 26 Novemba, 2021, Serikali ilitangaza kwamba itaunganisha umeme wa grid ya Taifa kwa Mikoa ya Katavi na Kigoma kwa mwaka 2022, wananchi wa Kigoma na Katavi wanasubiria kwamba je, ni kweli ifikapo Desemba 31 mwaka huu mikoa hiyo itakuwa imepata umeme wa grid ya Taifa? Tuna kilio cha muda mrefu, umeme ndiyo kila kitu, huwezi kupata uchumi wa viwanda bila umeme, umaskini wa Mkoa wa Kigoma na Katavi umesababishwa na ukosefu wa miundombinu ikiwa ni pamoja na umeme. Mikoa hii inazalisha sana, lakini imekosa umeme, kwa hiyo haiwezi kuvutia wawekezaji wa viwanda pasipo na umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Waziri kwenye vipaumbele vyake 12 ambavyo amevileta hapa Bungeni, amesema kipaumbele namba moja ni kutekeleza miradi mbalimbali ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme ikiwepo kupeleka umeme wa grid ya Taifa kwenye Mikoa ya Katavi na Kigoma. Najiuliza nimeona vyanzo vya Kigoma kuunganishwa na umeme wa grid wa Taifa ni kutoka Nyakanazi kuja Kigoma, kutoka Urambo kuja Kigoma, kutoka Sumbawanga kwenda Kigoma na maporomoko ya Mto Malagarasi. Inanichanganya kwamba hivi vyanzo vyote vinatokea kwa wakati mmoja? Naomba Waziri atakapokuja kutoa hitimisho lake awaeleze wananchi wa Kigoma, katika hizo njia zote nne ni njia ipi hasa ambayo ameipa kipaumbele cha haraka sana ifikapo Desemba tuwe tumepata umeme wa grid ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taifa tunatakiwa tujiulize gharama ya kuendesha umeme ule wa generator Kigoma kila mwezi, Shirika linapata hasara ya zaidi ya milioni 700, ukizidisha kwa mwaka Shirika la TANESCO linapata hasara zaidi ya bilioni 8.4, kwa miaka kumi ni bilioni 84 kulikoni? Ukiangalia gharama ya kuunganisha umeme wa grid ya Taifa kutoka kituo cha Urambo kwenda Kigoma ni bilioni 69, kwa nini huu mradi hautekelezeki wakati Taifa linaendelea kupata hasara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna haja ya kuangalia, kutakuwepo na watu wanaofaidika na ununuzi wa mafuta, kutakuwepo na maslahi ya supplier anaye-supply mafuta ya kuendesha hii mitambo ya generator. Tunaomba sana wananchi wa Kigoma na Katavi wanalalamika, wana maombi makubwa sana, wana imani kubwa sana na Mheshimiwa Waziri, ana muda mfupi tu lakini ameweka kipaumbele kwa mikoa yetu. Nilikuwa nimejiandaa kukamata shilingi ya Waziri, tunasubiri, endapo itafika mwaka kesho, mikoa yetu haijaunganishwa na grid ya Taifa tutakuja kukamata shilingi ya Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leo, ninaunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii nami nichangie kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kwa mwaka 2022/2023. Kwanza nianze kwa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuijenga nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi ya pekee kuwapongeza Waziri wa Wizara ya Fedha, Naibu wake na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kutuletea bajeti ambayo kabisa inaonesha nia ya dhati ya kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu unaenda kujikita kwenye uchumi wa bluu kama sehemu mojawapo ambapo bajeti hii imeweka kipaumbele katika sekta za uzalishaji. Uchumi wa bluu unamaanisha mazao, uchumi unaotokana na uvunaji kutoka kwenye maji ya bahari, maziwa, mito, mabwawa na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Uvuvi inakua kwa asilimia 2.5 na inachangia pato la Taifa kwa asilimia 1.8 na inaajiri zaidi ya Watanzania milioni 4.5. Kiwango cha pato kinachochangiwa na sekta hii muhimu ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuwa na maziwa makubwa katika Bara la Afrika ambayo yanapatikana Tanzania ambayo ni Victoria, Tanganyika, Rukwa, Nyasa na ukanda mkubwa wa bahari na maziwa mengine madogomadogo ambayo ni Eyasi, Natron, Manyara. Kwa maliasili yote hiyo ambayo Mwenyezi Mungu ametupa na ukalinganisha na mchango unaochangiwa na maliasili hii ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite kwenye Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika kabla ya uhuru ndiyo ziwa ambalo lililokuwa likichangia pato kubwa kwenye uchumi wa mkoloni. Tunapozungumza Ziwa Tanganyika, tulichozawadia dhahabu ya kwanza ya Ziwa Tanganyika ni dagaa, kwa jina maarufu dagaa wa Kigoma. Zawadi nyingine ya pili inayopatikana katika Ziwa Tanganyika ambayo tulipewa inaitwa ni almasi ambayo ni migebuka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ziwa Tanganyika lina aina za samaki zaidi ya 224 lakini samaki ambao ni wa kibiashara (commercial fish species) ziko mbili tu na sana ukiongeza ya tatu ni moja. Ya kwanza ni dagaa, ya pili ni migebuka na ya tatu ni sangara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2000 ziwa hili limedoroka katika mapato yake. Wavuvi wamekuwa wakihangaika, hawana miundombinu, lakini kitu kikubwa zaidi tunachoweza kukiangalia ni kipi. Naomba niende kwenye chimbuko lenyewe la uzalishaji la mapato ya Ziwa Tanganyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika miaka ya 1990 hadi 2000, uvuvi katika Ziwa Tanganyika, wastani wa mapato ilikuwa ni metric tons 200,000 na mwaka 2000 hadi 2013 uvuvi ulishuka hadi tukawa tunavuna kwa wastani wa metric tons 120. Kwa 2013 mpaka sasa inasemekana kiwango tunachokipata ni metric tons 80. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kushuka kwa mapato ya uvuvi yanatufikirisha sana. mwaka 1953 wakati wa utawala wa wakoloni, Mwingereza alipoona Ziwa la Victoria halina mapato makubwa yeye alichukua sangara kutoka katika Ziwa Tanganyika na kupeleka Kamati ya Utafiti ya Uvuvi ya Kikoloni ilichukua sangara kutoka katika Ziwa Tanganyika na kuipeleka kupanda katika Ziwa Victoria. Uchumi tunaoshangilia sasa hivi wa sangara umetokana na kazi nzuri iliyofanywa na mkoloni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tujiulize, tafiti zetu za uvuvi (TAFIRI) je, hawana mpango au wana upungufu wa fedha hawawezi wakafanya utafiti kuangalia namna gani ambavyo wanaweza wakachukua sangara wakaweka kwenye maziwa haya mengine ambayo siyo productive kama Ziwa Rukwa na Eyasi? Nashauri sana Idara ya Utafiri ya Uvuvi (TAFIRI) waongezewe fedha ili waweze kufanya utafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kushuka kwa mapato katika Ziwa Tanganyika, sasa hivi kuna zoezi linaloendeshwa na Serikali yetu ya fish stock assessment ambayo inafanyika upande wa Tanzania. Samaki walioko katika Ziwa Tanganyika ni pelagic ni migrant wana-move. Ili zoezi hili liwe na tija, basi ni vema nchi yetu ishirikiane na nchi zile ambazo zote zina-share Ziwa Tanganyika ambazo ni Burundi, Congo na Zambia. Hilo zoezi lifanyike kwa pamoja, zoezi hilo litaleta tija. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihamie kwenye nishati kwa maana ya kuleta msisimko wa kuleta viwanda nchini Tanzania. Nimepita nikiangalia nchi zilizoendelea, nchi zilizoendelea nyingi zilifanya utafiti na kuhakikisha kwamba zina nishati ya kutosha. Kwa mfano, Afrika Kusini ina megawati 80,000, Uturuki ina megawati 60,000. Sisi tukiangalia vyanzo vyetu pamoja na umeme uliopo vyote kama tutakuwa tumeviendeleza, tutaweza kupata megawati 5,579.8. Umeme ndiyo moyo wa viwanda…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Felix kwa mchango mzuri na hongereni kwa dagaa wazuri.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia kwenye taarifa hasa ya Kamati ya Maji na Mazingira. Kabla sijaanza kuchangia kwanza niwapongeze Wenyeviti wote wa Kamati hizo mbili, Mheshimiwa Vita Kawawa na comrade kaka yangu Mheshimiwa Kiswaga kwa kazi kubwa wanayoifanya na kwa jinsi wanavyotuongoza. Ninawashukuru sana na kuwapongeza Mawaziri wa Wizara mbili ambazo kwao wanatupa ushirikiano, kwanza Wizara ya Maji Comrade Mheshimiwa Jumaa Aweso, tunakushukuru sana kwa kazi kubwa na nikupongeze tena Mheshimiwa Selemani Jafo kwa kazi kubwa unayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utakuwa katika sehemu mbili kama muda utatosheleza nitaanza na biashara ya carbon (carbon trade). Biashara hii ni biashara mpya wengi hawajaielewa ningependa nianze kuielezea kwamba hii biashara ya hewa ya ukaa ni biashara ya namna gani na ningeomba nitoe tafsiri angalau kwa lugha ya kigeni. Carbon trade is a commerce meant to lower carbon emissions and capture atmospheric carbon dioxide by protecting forest as a leading captor. Sasa ni biashara ya kupunguza emission za hewa ya ukaa kwenda angani lakini na kushusha kiwango cha carbon dioxide ambayo iko angani, hewa ambayo iko kwenye atmosphere ili kwenda kwenye viwango vya chini na ni kitu gani kinachoshusha hasa cha kisayansi ni misitu kwa sababu yenyewe ina vidakio tunavyoviita captors hii ndiyo carbon trade. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni fursa mpya katika ulimwengu wa sasa, biashara hii inafanyika na inalipa katika nchi za ulimwengu wa tatu ambazo zinatoa hewa chache zinazotoka kwenye viwanda ni chache ukilinganisha na nchi zilizoendelea kwa maana kwamba carbon emission to the atmosphere is very much lower compared to the developed industrialized countries. Kwa hiyo hiki ndicho kiini hasa hasa cha biashara hiyo kwamba zile nchi ambazo hazichafui hali ya hewa zikiwa na captors kama msitu basi zinaweza zikafaidika na biashara hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara hiyo inafanywa na watu gani? Biashara hiyo inaweza ikafanywa na mtu binafsi, inaweza ikafanywa na makampuni yaliyosajiriwa na inaweza ikafanywa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni eneo jipya, biashara hii kwa hapa kwetu nchini imeanza mwaka 2018 na Waziri juzi alituambia mpaka 2022 kwa miaka takribani mitatu minne, Tanzania ilikuwa imepata bilioni 32 lakini kwa mipango ambayo sasa Wizara ya Mazingira inayoongozwa na Comrade Selemani Jafo anasema wamejipanga kila mwaka watakuwa na uwezo wa kupata trilioni 2.4 za Kitanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii biashara inaenda kuitajirisha nchi yetu endapo mambo yafuatayo tukiyafanya, inaonekana ni nyepesi kuzipata hizo lakini ni kazi ngumu.
Moja, nchi yetu ina misitu ya kupandwa na ile ya asili jumla ya misitu tuliyonayo ni 589. Misitu yote hii inafaa kwa biashara ya carbon, kwa maana kwamba yote hii ni leading captors wa atmospheric carbon dioxide ina uwezo wa capture. Kwa hiyo, hii ndiyo bidhaa ambayo tunayo ambayo inaweza ikatuingizia fedha hizi za Kitanzania trilioni 2.4 tunazipataje? Sasa hivi sisi hatujafaidika, nimpongeze Mheshimiwa Jafo Waziri wa Mazingira kwa juhudi ambayo amekwishaifanya, tayari wamekwisha tengeneza mwongozo lakini huo muongozo sijajua ni kwa upande gani lakini bado haijafika mpaka kwenye ngazi ya chini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashauri yafuatayo yafanyike ili Tanzania iweze kufaidika na biashara hiyo. Kwanza ni capacity building, ni lazima Serikali ijipange kujenga uwezo kwa watumishi wote wanaohusika na Wizara za Maliasili na Utalii na zile za Mazingira na wadau wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili, ni lazima utengenezwe uelewa wa pamoja kwa wananchi, creation of awareness to the community ili wananchi waelewe hii biashara inaendeshwa namna gani? Wote tukishajenga uelewa wa pamoja basi wananchi naamini watashiriki kimalifu katika kutunza mazingira, hususani ni misitu na tutafaidika na biashara hizi za carbon. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu kuna uvunaji unaoendelea wa miti asili ambao unafanywa na TFS, huwa wanauza vipande vya misitu kwa ajili ya wananchi wale ambao wamesajili biashara ya mkaa na kuni ili kufanya biashara. Ni kweli sasa hivi hatuna njia mbadala ya nishati ambayo inaweza ikatumika kwa watu ambao ni maskini, ningeomba fedha hizi ambazo zitatokana na biashara hii ya ukaa ziende kwenye tafiti ikiwa ni pamoja na tafiti za kutafuta nishati mbadala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nihame hapo lakini niende tena hapohapo kwenye Wizara ya Mazingira. Tunayo Sheria ya Mazingira ni ya muda mrefu sana, Sheria ya Mazingira Namba 191 inatakiwa ihuishwe, na ni vema sasa Serikali vilevile iharakishe mchakato wa kulifanya Balaza la Mazingira kuwa Mamlaka Kamili ambayo sasa Balaza la Mazingira ambayo ni NEMC ibadilike iwe authority, iwe ni National Environmental Management Authority ili kuipa nguvu na iweze kufanya kazi kikamilifu, itakuwa na meno lakini itakuwa na soko kwenye taasisi za kidunia zinazotoa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niende kwenye Wizara ya Maji harakaharaka…
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umekwisha malizia sekunde kumi.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri wa Maji kwa juhudi kubwa ambayo ameifanya inaonekana ni chanya kabisa na atakuwa ni mkombozi hata kwa Mkoa wa Tabora. Ipo juhudi kubwa anapeleka miradi kwenda kutatua changamoto ya maji na siyo kwa Tabora tu hata kwenye Mikoa mingine, tunampongeza na hongera sana kazi yake inaonekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii niweze kutoa mchango wangu kwenye Bajeti ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali, namshukuru Mwenyezi Mungu Muumba wa Mbingu na Nchi kwa zawadi ya uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi ya pekee kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa hasa hasa nikianza na hiyo ambayo ametoa shilingi bilioni 15.4 kwa ajili ya kuwapa wananchi wanaopisha mradi ule wa Liganga na Mchuchuma, hongera sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na Naibu wako kwa Hotuba nzuri sana ambayo imeeleza mambo mengi sana, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Wizara hii ya Viwanda na Biashara, maendeleo ni hatua, tunaiona hatua, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye maeneo matatu; moja, ni eneo la biashara za mpakani, ni Mbunge ninayetoka Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Kigoma unapakana na nchi karibu tatu; tuna Burundi, Congo DRC na kusini, siyo mbali sana, unaiona Zambia iko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara zetu zinategemea usafirishaji, miaka 10 ya nyuma iliyopita, biashara iliyokuwa ikifanyika katika Mkoa wa Kigoma na Wakongo ilikuwa ni kubwa ukilinganisha na sasa. Kwa nini imepungua? Ni kwa sababu chombo kilichokuwa kinatuunganisha na kilichokuwa kikisaidia usafirishaji wa bidhaa na wafanyabiashara ni meli, hamna kabisa mpaka sasa hivi ni miaka nane katika Ziwa Tanganyika hatuna meli inayo-operate. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko karibu sana na biashara ili iweze kufanyika ni lazima kuwepo na maboresho ya miundombinu. Ujenzi wa barabara zetu nikianza na kilometa 51 ambayo inaanzia Malagarasi kwenda Uvinza, ambayo sasa inaenda kutuunganisha iweze kutusaidia na kuchochea biashara ya kwenda upande wa Congo kuja Kigoma na hatimaye twende Congo, bado haijakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba ili tuweze kufanya biashara hiyo nzuri na Congo na tuweze kufaidika kama nchi, ni lazima miundombinu ya usafirishaji iboreshwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu mazao yetu, bado tunasafirisha nje ya nchi yakiwa ni malighafi. Nianze na zao la kahawa, wakulima kwa miaka mingi wakilalamika na hadi sasa wanalalamika, bei ya zao la kahawa bado ni ndogo. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Wizara yako ndiyo credo na taa ya kusaidia wakulima kutatua changamoto hii, tuna TANTRADE haijawajibika ipasavyo ili kuweza kutafuta masoko ya uhakika kwa zao hili la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri kwa Serikali kwamba kwa kuwa miaka yote tumekuwa tukisafirisha malighafi, ninashauri sasa Wizara yako ihangaike usiku na mchana kutafuta masoko ya uhakika na kuzishawishi zile nchi ambazo wananunua zao hili la kahawa, ambazo ni Ujerumani, Japani, China, Marekani na Afrika Kusini; mwalete wajenge viwanda kwenye maeneo ambapo kahawa inazalishwa ili tusafirishe kahawa ambayo tayari imeshaongezewa thamani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vijengwe kwenye mikoa ile ambayo inazalisha kahawa. Kwa mfano, ukijenga kiwanda cha kahawa Kigoma, utachukua malighafi ya Mkoa wote wa Kigoma na Katavi. Ukijenga kiwanda cha kuchakata kahawa Moshi, utachukua kahawa yote inayozalishwa Tanga, Manyara, Kilimanjaro na Mara. Ukijenga kiwanda cha kuchakata kahawa katika Mkoa wa Mbeya, utachukua kahawa yote inayozalishwa Mkoa wa Songwe, Rukwa na Ruvuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, kwanza tutakuwa tumeongeza na tumetengeneza ajira nyingi ndani ya nchi na viwanda hivyo vitatumia umeme huu ambao sasa unaenda kuzalishwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya tatu, ni kuhusu gap au upungufu wa mafuta ya kula, Kigoma tuna zao la chikichi na tuna zao la alizeti ambalo linalimwa nchi nzima, kwa nini hatuoni uchungu? Bado tunaagiza mafuta ya kula nje ya nchi. Tunatumia zaidi ya shilingi bilioni 400 ya fedha za kigeni ambazo tungeweza kutumia kununua mahitaji mengine kama madawa. Bado tunaenda kununua kitu ambacho tunaweza tukazalisha ndani ya nchi. Bado Serikali inahitaji iweke mkakati wa ndani wa kusaidia kuhakikisha uzalishaji wa chikichi na alizeti unaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuta haya ambayo yanazalishwa, yazalishwe ndani ya kutosheleza na hakuna haja ya kuendelea kununua kutoka nje ya nchi. Tujenge mazingira yaliyo mazuri kwa wawekezaji wa ndani na kwa SIDO ili iweze kuandaa mitambo midogo midogo ambayo inaweza ikachakata mazao haya. Tuwajengee uwezo Serikali ijenge uwezo kwa TEMDO, CAMARTEC, VETA ili hizi taasisi zote ziweze kusaidia katika ujenzi wa viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaweza kusaidia kuchakata mazao ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne ni mazingira ya uwekezaji. Bado mazingira ya uwekezaji katika nchi yetu siyo mazuri sana. Ukiongea na wawekezaji wa ndani na hata wa nje watakwambia barrier mojawapo ya uwekezaji katika viwanda, hususan ujenzi wake, ni kodi. Mtu ili awekeze kwenye viwanda kikwazo cha kwanza anachokutananacho ni utitiri wa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta kuna mamlaka nyingi ambazo zote zinamwendea mwekezaji mmoja kumlipisha kodi pamoja na kumtoza tozo mbalimbali. Ninashauri iundwe mamlaka moja ambayo tayari tunayo TRA, iwe ni dirisha moja, mwekezaji akifika, basi malipo yote yafanyike pale, yatengenezwe mazingira ambayo ni mazuri. Tukifanya hivyo, itawezesha wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza kwenye viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwepo na biashara nzuri na uwekezaji mzuri wa viwanda ni lazima tuhakikishe miundombinu yetu imeboreshwa. Barabara zetu kutoka vijijini sehemu ambako bidhaa mbalimbali, hususan za kilimo, zinazalishwa ziboreshwe na reli zitengenezwe. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumewezesha usafirishaji wa bidhaa na huduma kutoka kwenye maeneo ambapo zinazalishwa kwenda kwenye masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu mpango wa kuboresha mazingira mazuri ya biashara Tanzania. Serikali ilikuja na mpango wa blue print, ninashauri mpango huo wa Serikali uendelee kusimamia ili kuweza kuweka mazingira bora ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, napendekeza yawepo Mabaraza ya Biashara ngazi ya Wilaya. Kwa sisi tuliopo kule mipakani, wafanyabiashara wadogo wadogo ambao wanafanya biashara na nchi tunazopakananazo kuna shida kubwa sana. Naomba Wenyeviti wa Mabaraza ya Biashara ambao mara nyingi ni Wakuu wa Wilaya wawezeshe kutengeneza mazingira mazuri ili zile biashara za mpakani ziende vizuri bila kuwa na tozo zisizokuwa na idadi. Tukifanya hivyo, basi uchumi wetu utaongezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, ni Wizara hii, ili iweze kuleta mapinduzi ya viwanda inahitaji fedha nyingi. Hizi shilingi bilioni 110 ambazo tunaenda kuzipitisha hivi punde ni ndogo. Kwa hiyo, bado jitihada na uhitaji wa fedha nyingi unahitajika, ili tuweze kuleta mapinduzi ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nitoe mchango wangu kwenye Bajeti Kuu. Niwapongeze watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Wizara ya Mipango kwa kazi kubwa na njema wanayoifanya. Niishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miradi mingi ambayo inatekelezwa Mkoani kwetu Kigoma na katika Wilaya yangu ya Buhigwe ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali. Nasema ahsante na hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mchango wangu katika Bajeti hii Kuu utajikita kwanza kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ambayo ni alizeti ambayo inalimwa sana sana katika Mkoa wa Singida, Simiyu, Shinyanga na Dodoma. Zao la pili ni chikichi ambayo Mungu alituzawadia Kigoma, makao makuu na sehemu ambayo ni ukombozi kwa kilimo cha chikichi ni Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazao haya ni mazao ya kimkakati. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa miaka miwili mitatu nimeshuhudia kwa macho juhudi kubwa ambavyo amehamasisha kilimo cha chikichi Kigoma na kilimo cha alizeti Singida. Amezindua na amewatembelea wakulima. Mazao haya ni ukombozi kwa Taifa letu yanaweza yakaokoa fedha nyingi za kigeni ambazo tunazitumia kwenda kununua mafuta ya kula. Mazao haya (alizeti na chikichi) yakiwekewa msisimko, yakawekewa ruzuku, yakawekewa nguvu kubwa ya kisekta na Wizara ya Kilimo ikahamasisha, mazao haya yanaweza yakaokoa fedha nyingi tunazozitumia kuagiza mafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mzuri unajionesha kwenye Taarifa ya Wizara ya Fedha. Mwaka 2019 uzalishaji wa zao la alizeti kwa mwaka ilikuwa ni tani laki 561,297 lakini baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhamashisha kwa mwaka jana 2023 alizeti iliyozalishwa hapa nchini ilikuwa ni tani 1,103,298. Kwa zao la chikichi kwa mwaka 2019 chikichi iliyokuwa ikizalishwa ilikuwa ni tani 42,176 baada ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuhamasisha na kuja mara kwa mara katika Mkoa wetu wa Kigoma uzalishaji umeongezeka kutoka tani 42,000 hadi kufikia tani 62,125 kwa mwaka jana (2023).
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuzunguma ni nini? Hatuna sababu yoyote ile ya kutumia fedha za kigeni ambazo zinaendelea kuwa chache kuagiza mafuta nje ya nchi wakati sisi Mungu ametupa ardhi nzuri, yenye rotuba na uwezo wa kuzalisha mazao haya. Tunaweza tukazalisha na hiyo gap ya mafuta ikafutika. Kinachohitajika ni juhudi, tunahitaji huduma bora za kilimo ziongezwe katika mikoa hiyo inayozalisha alizeti na chikichi na mazao haya yapewe ruzuku maalumu kwa ajili ya kuongeza uzalishaji bora. Zaidi tafiti ziendelee zaidi kupata mbegu bora ambazo zinaweza zikazalisha mafuta mengi ili kuokoa fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili mazao ya biashara kahawa na chai. Tuna mikoa 16 inayolima kahawa na mikoa ambayo inalima kahawa vilevile inalima na chai. Mazao haya ni muhimu kwa nchi yetu kwa sababu ndiyo yanayotupatia mchango mkubwa, ndiyo yanayotupatia na kutuingizia fedha nyingi za kigeni lakini mazao haya mawili uzalishaji wake unashuka. Ukiangalia kwa mwaka 2019 kahawa iliyozalishwa nchini na kuuzwa nje ya nchi ilikuwa ni tani 68,147 lakini kwa mwaka jana (2023) tani zilizozalishwa na kuuzwa nchi za nje ni tani 62,917.
Mheshimiwa Naibu Spika, chai kwa mwaka 2019 chai iliyozalishwa na kuuzwa nje ya nchi ilikuwa ni tani 37,193 lakini kwa mwaka jana (2023) ni tani 23,775. Mazao haya ya biashara uzalishaji wake unashuka kwa nini? Ni kwa sababu Serikali haijachukua maamuzi ya dhati kwenda kutatua changamoto zinazowakabili wakulima wa chai na kahawa. Tunaomba bajeti hii ikatatue matatizo ya wakulima wa kahawa na chai ili uzalishaji uongezeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ahsante, kengele ya pili hiyo.
MHE. KAVEJURU E. FELIX: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaunga mkono hoja.