Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Eng. Isack Aloyce Kamwelwe (6 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kuchangia hoja katika Bunge lako Tukufu, kabla sijafanya hivyo naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia amani nchi yetu na kutuwezesha sote kuwepo hapa kushiriki katika Mkutano huu ambao ni wa kwanza wa bajeti tangu kuingia madarakani kwa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Aidha napenda kutumia fursa hii kutoa pongezi zangu za dhati kwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kwa kupata ushindi wa kishindo katika chaguzi zilizopita. Ushindi huo ni ishara ya imani kubwa ya wananchi waliyonayo kwa Rais, Makamu wa Rais na kwa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa, Mbunge kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vilevile napenda kuwapongeza Mheshimiwa Spika na Naibu Spika kwa kuteuliwa kwao kuliongoza Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mhandisi Gerson Lwenge, Mbunge, kwa kuteuliwa kwake kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji na pia namshukuru kwa ushirikiano mkubwa anaonionesha katika kutekeleza majukumu yanayozikabili sekta za maji na umwagiliaji. Natoa shukurani zangu kwa Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Wizara inayomgusa kila mwananchi katika kurudisha imani hiyo kubwa ninaahidi kuwatumikia wananchi wa Tanzania kwa uadilifu haki bila upendeleo, nina ahidi kufanya hivyo kwa kadri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia na kwa ufupi niseme hapa..Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe shukrani kwa wananchi wa Jimbo la Katavi kwa imani yao waliyonipa kwa kunichagua kuwa Mbunge wao kwa kura nyingi za kishindo.
KUHUSU UTARATIBU...
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe shukurani kwa wananchi wa Jimbo la Katavi kwa imani yao waliyonipa kwa kunichagua kuwa Mbunge wao kwa kura nyingi za kishindo. Nawaahidi nitawatumikia wote, kwa nguvu zangu zote kadiri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwapongeze Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuchaguliwa kuliongoza Bunge letu Tukufu na pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwao kwa kuwawakilisha wananchi waliowachagua katika Bunge hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nichukue fursa hii kuishukuru familia yangu nikianzia na mke wangu kwa ushauri na ushirikiano mkubwa wanaonipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi, sasa naomba nichukue nafasi hii kuchangia hoja mbalimbali ambazo zimeibuliwa na Wabunge kupitia kwenye bajeti ambayo imewasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda niliopewa ni dakika 15, itabidi nipite kwenye maeneo machache ya ujumla, maeneo mengine yatahitimishwa na Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na suala la madeni. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia changamoto ya madeni kwamba ni kweli Wakandarasi ambao waliingia mikataba kwa ajili ya miradi ya maji, kumekuwepo na madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe taarifa ifuatayo:-
Miradi ya Maji Vijijini tuliingia mikataba ya shilingi 887,844,161,282. Hadi leo fedha ambazo zimeshalipwa ni shilingi 553,175,872,452 na kiasi kilichobaki ni shilingi 334,668,288,830. Hata hivyo, certificates tulizonazo mkononi ni za thamani ya shilingi 10,822,464,268. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha anaendelea kutupatia pesa na ameahidi kutupatia fedha hizi na zitakuwa zimelipwa kabla ya mwaka wa fedha huu tulionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Miradi ya Maji Mjini, tuliingia mikataba ya shilingi 1,379,471,322,665. Fedha iliyolipwa ni shilingi 1,266,610,684,020. Fedha tunayodaiwa ambayo tuna hati za madai mkononi ni shilingi 50,594,881,957.
Waheshimiwa Wabunge, kwa bahati nzuri kwa sababu hii miradi imekuwa inachangiwa na wafadhili, wadau wanaopenda kuchangia katika maendeleo yetu ya kuleta maji, Benki ya Maendeleo ya Ufaransa tayari wamekubali kwamba deni hili wao watalilipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari wameshaanza kutoa tayari fedha kwa ajili ya kulipa deni hili. Kwa hiyo, mpaka tunamaliza mwaka wa fedha huu tulionao, mwezi Juni tarehe 30, tutakuwa hatudaiwi katika miradi ya maji kwa maana ya hati ambazo zimeshawasilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wakandarasi wanaendelea na kazi, wanaweza wakaleta certificates nyingine na tutaendelea kwamba kila tukipata certificate tunapeleka Hazina ili tuweze kupewa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe maelekezo katika hili. Mamlaka zote kuanzia category A, B, na C; ambapo category C mara nyingi ziko upande wa Halmashauri; pale ambapo Wakandarasi wa miradi ya maji wana mkataba, wakishapata certificate, basi watutumie ili tuweze kuipeleka Hazina, tuweze kupata pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi hatuwezi kupeleka hela mahali ambapo hujaingia mkataba na ambapo hujazalisha. Tumegundua hilo tatizo kwamba watu wengi wanasema kwamba hela haijaja, kumbe unakuwa hujaleta certificate ili tuweze kuipeleka Hazina. Hazina haiwezi kutoa hela kama wewe hujaingia mikataba na kama wakandarasi hawajazalisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nitoe maagizo kwa Wakurugenzi wote ambao wanahusika na Miradi ya Maji, kwamba hatuwezi kuleta pesa mpaka walete hati za madai, kuhakikisha kwamba kazi hiyo imeshatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge pia katika michango walioneshwa kutokuridhishwa wakati mwingine na hali ya utekelezaji wa miradi. Wakati mwingine viwango vya utekelezaji vinakuwa viko chini. Certificates hizo tukizipokea, wakati mwingine tutalazimika kuunda timu katika Wizara na kwenda kukagua hiyo miradi kuangalia kama kweli kazi hiyo imetekelezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, Waheshimiwa Wabunge wamechangia kuhusiana na fidia kwenye maeneo oevu. Mpaka sasa hivi kwa upande wa Mkoa wa Kagera kwa ajili ya mradi wa kujenga mabwawa yale ya kutibu majitaka, tayari tumeshapeleka shilingi 1,800,000,000 kwa ajili ya kulipa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika Mkoa wa Singida tayari tumeshapeleka shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa fidia kwa chanzo cha Mwankonko na chanzo cha Irawo tunaendelea kufanya tathmini ili baada ya kukamilisha basi tuweze kupeleka hela kwa ajili ya fidia. Kwa hiyo, nako naagiza, maeneo yote ya vyanzo oevu, tathmini ikishafanyika tunaomba mtuletea hati za fidia ili tuweze kuzipeleka Hazina ili kutupatia pesa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge pia wamechangia kuhusu madeni ya maji ambayo yanatokana na Taasisi za Serikali ambazo hazijalipa bili zao. Mpaka hapa tunapozungumza, tuna deni la shilingi bilioni 31, ukikusanya kwa mamlaka zote nchini. Sasa hivi tunafanya mazungumzo na Hazina na tayari wameonesha mwelekeo kwamba madeni haya watayalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii ilichangiwa pia na Mbunge wa Viti Maalumu wa Tabora, Mama yangu Mheshimiwa Munde, ambaye alionesha kwamba Mamlaka ya Maji ya Mkoa wa Tabora inashindwa kujipanua kwa sababu inadai taasisi za Serikali. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Munde kwamba sasa hivi Serikali inafanya utaratibu wa kuhakikisha kwamba sasa hivi fedha hizi zinalipwa ili hizi Mamlaka za Maji ziweze kuendelea kupanua mitandao ya maji kwa ajili ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge pia walichangia kuhusu tatizo la upungufu wa wataalam wa Mamlaka za Maji. Ni kweli tuna upungufu mkubwa wa wataalam kwa Mamlaka zote za Maji nchini. Kwa upande wa Wahandisi tunahitaji Wahandisi 6,282. Kwa sasa waliopo ni Wahandisi 1,538. Upungufu huu ni mkubwa, ni upungufu wa zaidi ya Wahandisi 4,744. Vilevile tunahitaji Mafundi Sanifu na Mafundi Mchundo 4,005. Waliopo ni 752 na upungufu ni 3,253.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto hiyo, Wizara tayari imeshachukua hatua zifuatazo; tuliomba kibali cha kuajiri watumishi 475, kwa bahati nzuri kibali hicho kimetolewa kwa hiyo kwa mwaka huu wa fedha tunaomaliza, tayari tumeajiri wataalam 475 na wameshasambazwa kwenye Mamlaka mbalimbali za Halmashauri pamoja na Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto moja tunaipata tunapopeleka hawa wataalam; nitoe taarifa kwamba kuna baadhi ya Mikoa wamewakataa hawa wataalam, na Mikoa hiyo ni pamoja na RAS Dodoma, RAS Mbeya, RAS Arusha, RAS Dar es Salaam, Halmashauri za Manyara, Songea, Urambo na Geita. Hawana makosa kufanya hivyo kwa sababu na wao pia wanayo mamlaka ya kuajiri. Kwa hiyo, tunaona kwamba kama wamefanya hivyo, hao waliowarudisha tutawapeleka maeneo mengine ambayo wanahitajika. Kwa hiyo, tunaomba nao wachukue hatua ya kuajiri ili tusiwe na upungufu wa wataalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua muda wangu mdogo, nimeshapigiwa kengele, lakini niliona nisimalize bila kuzungumzia maombi ya Mheshimiwa Mchengerwa, ambaye ameomba tuanze kufikiria, kutengeneza mradi wa kuchukua maji kutoka Mto Rufiji na kuyaleta Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2005 mawazo hayo yalikuwepo na Serikali ilichukua hatua kutafuta vyanzo 26. Vyanzo hivyo vilitembelewa lakini ikaonekana kwa mahitaji ya maji ya Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo, vyanzo vilivyopatikana ambavyo viko karibu vina uwezo wa kulisha maji mpaka mwaka 2032. Kwa changamoto ambazo sasa hivi tunaanza kuzipata, tayari tunaanza kujipanga ili kuhakikisha kwamba tunaanza usanifu wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji ili tuweze kukidhi mahitaji ya maji ya Mji wa Dar es Salaam; na hasa baada ya kuwa na kiwanda cha kuchakata gesi kwa ajili ya kutengeneza umeme, ambacho miaka miwili ijayo kitakuwa kinahitaji lita milioni 100 kila siku kwa ajili ya kupooza ile mitambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mchengerwa kwamba hatujatenga fedha katika mwaka wa fedha unaokuja, lakini wazo hili tunalichukua na taratibu pengine mwaka kesho kutwa wa fedha tutaanza kuweka fedha kidogo, kwa ajili ya kuanza kufanya upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, nimalizie pia kwa kuzungumiza mradi wa maji wa kutoa Mto Ruvuma kuleta Mjini Mtwara Mikindani. Taratibu za kuongea na wafadhili zinaendelea vizuri na hivi ninavyoongea, wale Wachina, Wafadhili wenyewe wapo hapa Tanzania na mazungumzo yanaendelea vizuri. Kama hali itaendelea kama ilivyo, tunatarajia mpaka mwezi wa saba tunaweza tukawa tumesaini mikataba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nanyamba ana vijiji kwenye chanzo cha huu mradi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba vijiji vyako hivyo vitapewa maji pia kutoka katika huu mradi. Kwa bahati nzuri ni kwamba mtambo wa kutibu maji utajengwa kwenye chanzo. Kwa hiyo, wananchi wako watapata maji ambayo ni safi na salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nisingependa nipigiwe kengele. Basi kwa haya machache, naomba niishie hapo, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi uliyonipa. Kwanza naomba nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii nyeti kwa manufaa ya Watanzania kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia hotuba hii, kwa kweli inatoa mwelekeo mzuri wa kutufikisha mahali ambapo tutakuwa kwanza tuna chakula cha kutosha, lakini pia tutaendeleza uchumi wa viwanda ambapo sehemu kubwa itategemea kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikiliza Waheshimiwa Wabunge wengi wanavyochangia na wameishauri Serikali kwamba ni vizuri tuwe na mkakati wa kutosha wa kuinua kilimo cha umwagiliaji. Ni kweli nakubaliana nalo na ni kweli kwamba asilimia zaidi 75 ya kilimo chetu tunategemea mvua na kilimo cha mvua kwa kweli siyo endelevu, kama mvua hakuna maana yake hakuna kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa vyovyote vile lazima tuweke mkakati na ndiyo maana tayari tumeanzisha Tume ya Umwagiliaji ambayo ndiyo itakayosimamia eneo hili la umwagiliaji. Tumeona tuwe na Tume ili wawe na nguvu zaidi kuliko kufanya kama idara ya Serikali. Kwa hiyo, Tume tunayo na sasa hivi wanaandaa mpango kabambe wa umwagiliaji katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye bajeti yangu kwamba tuna hekta 29,000,000 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Bahati nzuri tumepata msaada kutoka shirika la JICA ambalo limetufadhili kuandaa mpango ule, sasa hivi tunafanya manunuzi ya kupata Mhandisi Mshauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu katika kuendeleza sekta ya kilimo tumekuwa na miradi midogo midogo ya kusaidia wakulima wadogo wadogo, kila Halmashauri imekuwa na miradi lakini kwa sehemu kubwa miradi hii haijawa endelevu. Kwa hiyo, sasa tunataka tufanye mkakati wa kuhakikisha kwamba miradi hii ya umwagiliaji ambayo iko kwenye Halmashauri zetu inakuwa endelevu kwa kuipa nguvu kupitia hii Tume ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi kubwa na ya muhimu kwanza maji kama ambavyo wanavyosema ni muhimu kwa binadamu lakini ni muhimu kwa mifugo yetu na ni muhimu kwa kilimo. Kwa hiyo, tutajenga mabwawa na mabwawa haya haya ndiyo tutakayoyatumia tupate maji
ya umwagiliaji ili tuweze kuinua kilimo chetu na tuwe na uhakika wa chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti,Kwa hiyo, hii ndiyo kazi kubwa ambayo tunakwenda kufanya, hatutaweza kuendeleza kilimo kwa kutegemea mvua. Kwa hali ya tabia ya nchi inavyoonekana sasa mvua imekuwa inapungua kila mwaka kwa hiyo tukitegemea mvua kilimo chetu kitakuwa si endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuijalia amani nchi yetu na kutuwezesha Wabunge wote kuwepo hapa kushiriki katika Mkutano huu muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais, Champion wa Maji kwa kuendelea kuniamini na kuamini wafanyakazi wa Wizara ya Maji ili tuweze kutatua tatizo la maji kwa wananchi wa Tanzania. Namshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu, Mheshimiwa Rais alimteua Mama na suala la maji ni la mama, kwa hiyo anatusimamia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuendelea kusimamia vizuri shughuli za Bunge na tunaendelea vizuri kwa amani kabisa bila fujo ya aina yoyote. Namshukuru Mheshimiwa Spika, nawe Mheshimiwa Naibu Spika na leo ndio umekalia kiti hicho kwa jinsi mnavyoliongoza Bunge kwa weledi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wenu, kwa miongozo yenu na kwa jinsi mnavyotuombea, lakini jinsi ambavyo mnaendelea kushirikiana nasi ili azma hii ya kuondoa tatizo la maji katika nchi yetu liweze kufikiwa bila tatizo lolote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole za dhati kwa wananchi wote nchini hususan wananchi wa Arusha, kwa msiba mkubwa wa ajali ya gari uliogharimu maisha ya wanafunzi, Walimu, dereva na shule, msiba uliotutokea mwezi huu, msiba mgumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikitika sana kwa sababu barabara ile nimeisimamia mwenyewe kutoka Makuyuni mpaka Ngorongoro. Tunaomba roho za vijana hawa na hawa watu wazima wote Mungu aziweke mahali pema peponi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Lwenge, amenipa ushirikiano mkubwa sana, ameniongoza ndiyo maana hata nimeweza kufahamu mambo mengi kwa muda mfupi. Namshukuru sana Mheshimiwa Lwenge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Katavi kwa ushirikiano wao mkubwa wanaonipa mimi Mbunge wao, unaosaidia kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo katika Jimbo letu, naendelea kuwaahidi kwamba nitawatumikia kwa kadiri Mwenyezi Mungu atakavyonijalia na kwa nguvu zangu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile naishukuru familia yangu sana kwa jinsi inavyonishauri na jinsi inavyonipa ushirikiano ikiongozwa na mke wangu ambaye ni Mwalimu Bora Jeremiah Ulaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda kuwa ni mdogo, nianze kuunga mkono hoja au shughuli yetu hii ya leo na niombe Waheshimiwa Wabunge mpitishe ili tukafanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea michango mingi sana kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge, michango ambayo kwa kweli inatutetea ili tuweze kuhakikisha kwamba tunatimiza kuwapatia wananchi wa Tanzania majisafi na salama lakini pia tuweze kuboresha kilimo cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza mchango wangu kwa kilimo cha umwagiliaji. Nchi yetu mwaka 1990 ilifanyika study ambayo ilibaini kwamba tuna hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, lakini ambazo zimeendelezwa ni hekta 461,000. Baada ya kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, nashukuru maeneo niliyofanya ziara; nimekwenda kuona jinsi gani hili eneo dogo ambalo limeendelezwa jinsi linavyofanya kazi na nimebaini upungufu uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea eneo la Mang’ola, nimekwenda kuona kilimo pale Wilaya ya Karatu, wanalima mara tatu. Hekta moja inatoa kuanzia tani tano mpaka tani kumi lakini hekta moja hiyo hiyo inalimwa mara tatu. Ni maeneo machache sana ambayo yameshafikia hatua hiyo ya kilimo kwamba hekta moja inaweza ikalimwa mara tatu. Maeneo mengi yanalimwa mara moja na ni kipindi cha mvua tu; kipindi cha kiangazi hatuwezi kulima kwa sababu hakuna maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Serikali kwa sasa imeweka Mhandisi Mshauri ambaye anapitia maeneo yote ili kubaini upungufu uliopo ni kwa nini hatuwezi kulima mara tatu ili tuweze kuondokana na tatizo la njaa katika nchi yetu. Upungufu huo ukishapatikana utaainishwa na malengo yetu ya kuhakikisha kwamba tunaandaa hekta nyingine millioni moja katika huu muda wa miaka mitano, nina hakika kwamba yatafikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu ni kuhakikisha tunalima mara mbili hadi mara tatu, kwa sababu hata hizo hekta chache ambazo nazo hazitumiwi kwa efficiency inayotakiwa, lakini bado zina uwezo wa kuchangia chakula kwa zaidi ya asilimia 25.

Mheshimiwa Naibu Spika, kilimo cha umwagiliaji ndiyo uti wa mgongo wetu na Ilani ya Chama cha Mapinduzi imeelekeza kwamba nchi yetu inakuwa ya viwanda na viwanda hivyo vitatumia rasilimali ya kutoka mashambani ili tuweze kunyanyua uchumi wa wananchi wetu twende kwenye uchumi wa kati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutahakikisha kawamba kilimo hiki cha umwagiliaji tunakisimamia ipasavyo. Kwa sababu Waheshimiwa Wabunge mlipitisha tume, katika huu muda mfupi ambao nimekaa nao, nimebaini upungufu uliopo. Upungufu uliopo, ni kweli kama mnavyolalamika Waheshimiwa Wabunge miradi mingi ambayo tulipata hela za wafadhili haijajengwa katika ile hali ambayo tulikuwa tunaitarajia. Kila ukiuliza, ukienda kwenye Halmashauri, Halmashauri wanakwambia ni matatizo ya Tume; ukiongea na watu wa Tume, wanakwambia ni matatizo ya Halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongea na Waziri wangu kwamba hiyo miradi iliyokuwa inaendelea iendelee, lakini miradi mipya yote itakayokuja, tunataka tuone mtu mmoja anaitekeleza na sio mwingine, itakuwa ni Tume ya Umwagiliaji, ili kama kuna upungufu katika ile tume, Waheshimiwa Wabunge tuweze kuurekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata michango mingi, Mheshimiwa Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini ameongea kitu cha msingi sana, kwamba Halmashauri yake ina matatizo ya Wahandisi, ina matatizo ya wataalam wa manunuzi. Ni kweli, lakini nashukuru bajeti ya mwaka 2016, mliagiza Wizara ya Maji na umwagiliaji kwamba mnataka tuunde Wakala wa Maji Vijijini. Mheshimiwa Waziri atalielezea vizuri, niwahakikishie kwamba tumeshaanza. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, hata mimi mwenyewe baada ya kuteuliwa katika Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kwa sababu nimetoka kwenye Wakala wa TANROAD niliona ili tuweze kwenda hakuna namna nyingine, ni lazima tuunde wakala ujitegemee, ufanye kazi kama ambavyo TANROAD imekuwa inafanya, ufanye kazi kama ambavyo REA inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mwalongo tatizo hilo alilonalo la wataalam wa manunuzi litakwisha baada ya sisi kuwa na Wakala wa Maji Vijijini. TANROAD imefanikiwa kwa sababu wataalam wa manunuzi ndani ya TANROAD ni Wahandisi hao hao wanaojenga barabara, ndiyo maana mambo yanakwenda vizuri; tunaelekea huko Waheshimiwa Wabunge. Sasa hivi inaandaliwa na tutakapoileta hapa, tutawaomba Waheshimiwa muipitie, mtushauri na muipitishe ili tuanze utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Musukuma katika mchango wake, nilikuwa nafikiri nami ataniuliza what is your weakness? Alisema kwamba miradi hii, bajeti hii hatuwezi kuitekeleza kwa mwaka mmoja.

Waheshimiwa Wabunge tumejipa miaka mitano, tumeanza na bajeti hii tumeitendea haki, tumeingia mikataba, tutatekeleza. Hebu tupimeni baada ya miaka mitano mtaona tutafanya nini? Huu mwaka mmoja tumejitahidi, tumeelewa tunatakiwa kufanya nini. Kwa hiyo, tupeni muda tuifanyie kazi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wako Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia uchimbaji wa visima vya Kimbiji na Mpera. Waheshimiwa Wabunge tayari visima 17 vimeshakamilika na niwaambie tu kwamba visima vitatu bado, lakini vinakamilika mwezi Juni, 2017 maana yake ni mwezi ujao. Visima hivi vikikamilika, visima vya maeneo ya Mpera vitahudumia wakazi wa maeneo ya Gongolamboto, Chanika, Luzando, Pugu, Mpera, Chamazi, Kidunda, Ukonga, Kinyerezi na Uwanja wa Ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, visima vya maeneo ya Kimbiji vitahudumia wakazi wa maeneo ya Temeke, Kisarawe, kibada, Kimbiji, Kigamboni, Tuangoma, Mkuranga, Kongowe, Mbagala, Kurasini, Mtoni, Tandika, Keko na Chang’ombe. Serikali inaendelea kutafuta fedha ili tuweze kuweka miundombinu ya usambazaji.

Waheshimiwa Wabunge, naomba mtuamini, tunaifanya hii kazi ili tuhakikishe wananchi wote wa Dar es Salaam na Pwani wanakuwa na majisafi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ignas Malocha, Mbunge wa Kwela. Amesema kwamba tumekuwa tukiomba pesa mfululizo kwa miaka mitano, hatujawahi kupewa. Tatizo ni nini? Anaelekeza kwenye miradi ya Maleza, Izia na Mfia. Mheshimiwa tutaweka fedha, tumeanza. Kama nilivyosema, utekelezaji wetu unakwenda miaka mitano, nimhakikishie wananchi wake watayaona sasa matokeo kwamba tunatekeleza maeneo yote haya aliyoyahitaji yakiwemo pamoja na maeneo ya umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe amesema mradi wa umwagiliaji wa Mwamapuri kwamba haujatengewa fedha katika bajeti ya mwaka huu; anaomba mradi huo utafutiwe fedha. Skimu ya umwagiliaji ya Mwamapuri ipo Halmashauri ya Mpimbwe, Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi. Skimu hii ina zaidi ya hekta 13,000 zinazofaa kwa umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Pudenciana Kikwembe, tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na tayari tumeshapata gharama, tunahitaji shilingi billioni 15 ili tuweze kuikamilisha hiyo skimu ikiwa ni pamoja na kujenga Bwawa la Ilalangulu ambalo litatunza maji ili tuhakikishe kwamba skimu hiyo inafanya kazi mwaka mzima isifanye kazi wakati wa mvua tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele ameuliza, katika nyakati hizi mbaya za mabadiliko ya tabianchi, licha ya kwamba sasa maeneo yetu bado ya misitu na miti kiasi, lakini suala la uharibifu wa mazingira litasababisha ukame utakaosababisha uhaba wa maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mpina ameeleza vizuri sana nini kinafanyika, sheria tunazo, lakini kikubwa Mheshimiwa Masele sisi ni Madiwani, lazima tukae na wananchi wetu, tuongee nao, tubadilishe tabia sisi wenyewe. Hatuwezi kuishi kwa sheria tu, lazima tuwe na tabia ya kufahamishana tuelewe kwamba misitu ni uhai na uhai ule siyo wa misitu wala siyo wa wanyama tu, ni pamoja na sisi binadamu. Tukielimishana, basi suala hili la mabadiliko ya tabianchi halitakuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, Wabunge wengi wamelalamika, miradi mingi ya maji tumetekeleza, lakini haifanyi kazi. Ukienda kuangalia, pamoja na matatizo yaliyokuwepo kwamba labda imejengwa vibaya, labda usanifu ulikuwa mbaya, lakini maeneo mengi ni kwamba vile vyanzo vilivyokuwa vimetarajiwa vimekauka. Sasa kama vimekauka, maji ya kuingiza kwenye bomba utayapata wapi? Haiwezekani. Tatizo hili sisi wenyewe, ndugu zangu tuhakikishe kwamba tunasimamia, tunaongea na wananchi wetu kuhakikisha kwamba tunadhibiti uharibifu wa misitu kwa sababu misitu ni uhai.

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia suala la kwamba mradi kutumia hela nyingi. Ukienda kuuliza, unaambiwa hii design iliharibiwa na Consultant. Mikataba iko wazi! Iko design liability ya Consultant. Kama Consultant ameharibu na ikathibitishwa kwamba ameharibu, lazima anailipia. Hizo fedha za kujenga huo mradi tutazipata kutoka kwenye insurance yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, iko michango mingi sana ya Waheshimiwa Wabunge ambayo hatuwezi kumaliza kuijibu yote, lakini tutahakikisha kwamba kwa muda mfupi michango yote hii tutaiandika na kuhakikisha kwamba tunawapatia Waheshimiwa Wabunge kabla ya kumaliza hili Bunge ili kila mtu awe na nakala na aone mchango wake na majibu ambayo tumeyapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Anna Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, maji yasiyotibiwa, malengo yetu na ndiyo Sera yetu kuhakikisha kwamba maji yote ya matumizi ya binadamu yanatibiwa ili mtu aweze kunywa maji yaliyo safi na salama. Concept hii tumeiona, Waheshimiwa Wabunge mmechangia, tukinywa maji yaliyo safi na salama tunapunguza hata kwenda hospitali na gharama za kununua madawa zitapungua. Hilo ndilo lengo letu. Sisi Wizara ya Maji hatupendi tuwe sababu ya kumaliza fedha za nchi hii kwa Serikali kununua madawa mengi kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Kapufi amezungumzia maji ya Ikorongo. Tayari tumeshasaini mkataba mmoja na wa pili utasainiwa ili tuhakikishe kwamba tunaongeza kiwango cha maji kufikia lita milioni
10.2 zinazohitajika katika Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Munde, Mbunge wa Tabora, tunakushukuru sana kwa pongezi. Tumesaini mikataba; mkataba ule ni wa zaidi ya shilingi bilioni 600, tunasimamia utekelezaji. Tumejipanga kuhakikisha kwamba unakamilika katika muda uliotarajiwa ili tuhakikishe tunamaliza yale matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa mama yangu Mheshimiwa Sitta amelalamikia kuhusu mradi tunaotoa maji Malagarasi kuleta Tabora kwamba utachukua muda mrefu. Tutahakikisha kwamba katika huo muda tunaosubiri ili tuweze kupata fedha kujenga huo mradi ambao utachukua miaka mingi, tutahakikisha kwamba tunafanya hatua za dharura ili wananchi wa Kaliua, Urambo waweze kupata maji yaliyo safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hapa nimeshapigiwa kengele tayari, nimalizie kwa kuunga mkono hoja, lakini nawaomba Waheshimiwa Wabunge, kila bajeti inapokamilika, tunawapatia vitabu. Katika mizunguko yangu ambayo nimekwenda huko kwenye Halmashauri, unakutana na Mkurugenzi anasema yeye haelewi kama ana bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Kabisa, kabisa mama yangu. nimeyaona haya na siyo Halmashauri moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Waheshimiwa Wabunge, baada ya leo, kesho mpigie Mkurugenzi wako, basi msomee hata kama hukumpa kitabu, kwamba Wizara ya Maji na Umwagiliaji una shilingi kadhaa ili waweze kujipanga. Zipo, lakini hawaangalii.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuungana na wenzangu kwa masikitiko makubwa sana kwa tukio ambalo limetokea mchana wa leo. Mimi nakaa Area ‘D’, nimesikia bunduki, lakini baadaye nakuja kupata taarifa kwamba ni Mbunge mwenzangu ambaye amejeruhiwa. Kwa kweli inasikitisha sana, kwa siku ya leo inaleta uwoga kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa shukrani kwa Kamati ya Bunge ambayo inashughulikia miundombinu ya maji kwa michango yao mizuri ambayo wametushauri kuanzia tulipoanzia michango hii kwenye Kamati. Pia nashukuru sana Maoni ya Kambi ya Upinzani ambao wameunga mkono moja kwa moja kwenye jambo hili. Nashukuru kusema kwamba kwenye masuala kama haya, kwa sababu tunajenga nchi kwa pamoja, sisi wote ni Watanzania, kwa hiyo, inabidi tuungane tuache suala la tofauti za itikadi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyoongea, tayari tuna Interim Secretariat na imeshafanya kazi kubwa sana. Hii Interim Secretariat Ofisi yake iko Kyela, nami nimeshatembelea pale. Ndani ya Watumishi; tuna Watumishi wa kutoka Malawi na Watumishi wa kutoka upande wa Tanzania. Makubaliano yaliyopo ni kwamba hata tutakapokuwa tumekamilisha hii Kamisheni, ikisharidhiwa ni kwamba Ofisi zitakuwa Kyela.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tangu Sekretarieti ilipoanza, Serikali ya Malawi na Serikali ya Tanzania wanachangia hela kuendesha ile Sekretarieti ya mpito; na imefanya kazi kubwa sana. Imeshakamilisha feasibility study, imeshakamilisha detailed design na imefanya semina mbalimbali na mikutano mbalimbali na Wafadhili na kutangaza kuhusu huu Mradi wa Bonde la Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari kuna indication kubwa kwamba Wafadhili wanasubiri tupitishe hili ili sasa mazungumzo ya mwisho yaweze kufanyika, tufanikiwe kutekeleza ule mradi. Kwa hiyo, suala kama hili Waheshimiwa Wabunge kwa kuliunga mkono, sisi kwa kweli kama Watanzania na kama Wabunge na Wizara ya Maji tunafarijika zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia juzi kulikuwa na Mkutano wa SADC, nami Mheshimiwa Waziri alinituma niende kule. Katika miradi miwili ambayo imepita; imepitishwa na SADC, ni pamoja na huu Mradi wa Songwe. Umepitishwa kwa sababu una components tatu ndani yake kama alivyokuwa amezungumza Mheshimiwa Mwakyembe. Tutazalisha umeme pale, tutatengeneza skimu za umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna hekta za mwanzo 6,200; na kati ya hekta hizo, hekta 3,150 ziko upande wa Tanzania na hekta 3,050 ziko upande wa Malawi. Kwa hiyo, wananchi wa maeneo ya Tanzania na huku watafaidika na umeme na bado watafaidika na kilimo cha umwagiliaji, kilimo chenye uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia maji yatachakatwa majisafi na salama. Kwa hiyo, sehemu ya maji yatakwenda upande wa Tanzania na sehemu ya maji watatumia watu wa Malawi. Kwa hiyo, sioni katika mpangilio kama huo ambao tuna-share umeme, tuna-share huduma ya maji safi na salama na tuna-share kilimo cha umwagiliaji, jamani undugu utazidi hapo. Unatarajia kuwe na ugomvi kweli hapo? Hata matatizo mengine yaliyopo kwenye lile Ziwa Nyasa, tuna imani kabisa kwamba utatuzi wake sasa utakuwa rahisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge katika michango yao wamezungumzia suala la ushirikishaji wa jamii. Tangu mwanzo hii Interim Secretariat ilivyoanza, imeshirikisha wananchi kutoka ngazi za Vitongoji, imekuja kwenye Vijiji, mpaka Kata, mpaka Wilaya. Wameshirikishwa na minutes zipo na taarifa hizi tumezitoa kwenye Kamati. Kwa hiyo, kila mwananchi yuko aware na suala hili na wanalisubiri kwa hamu kabisa kwamba Kamisheni hii ipitishwe na Bunge letu ili ianze kufanya kazi, wao wanasubiri kupata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, hebu tujaribu kuiangalia mipaka kwa wale ambao wanaishi kwenye mipaka. Kama maendeleo yakiwa upande mmoja kwingine kukawa hakuna maendeleo, maisha yanakuwaje katika hilo eneo? Kwa maana ya hii Kamisheni kwamba maendeleo yatakayopatikana yatakuwa shared upande wa Tanzania na upande wa Malawi. Kwa hiyo, tutazidi kuimarisha undugu wetu na ushirikiano utakuwa mkubwa. Migogoro mingine midogo midogo wakati mwingine unaitatua automatically kwa kuweka huo ushirikiano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, tunawashukuru sana na tunawaomba kwa kupitia kwenye michango ambayo wengi mlipata nafasi ya kuchangia, wengi mnaridhia na hili. Kwa hiyo, mwisho kabisa tunawaomba mridhie ili hatua nyingine ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, namalizia kwa kushukuru tena, ahsanteni sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ENG. ISACK A. KAMWELWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Katavi limepokea wafugaji wengi na mifugo yao na sasa maeneo hayatoshi kwa makazi, kilimo na malisho. Naomba eneo la hifadhi ya msitu wa Inyonga lipunguzwe na kuongezwa vijiji vya Mapili, Kamalampaka, Songambele, Imalauduki, Kafulu, Nzega, Kaulolo, Masigo, Nsemkwa na Ipwaga.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 3 wa Mwaka 2017
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kupewa nafasi hii, nimeambiwa dakika tatu lakini nilikuwa nina mengi, dakika tatu zinatosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe shukrani kwa kwa Kamati ya Sheria Ndogo, kwa bahati nzuri nimeshiriki. Pamekuwa na michango mizuri sana kuhusu uboreshaji wa hizi sheria ndogo za DAWASA.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitoe shukurani kwa Kambi ya Upinzani, kuanzia page ya tano mpaka page sita safari hii wameandika vizuri sana. Utakuta hata lugha ya vijembe iliyotumika inakubalika. Nimesoma hapa, kufanya usafi kila Jumamosi ni siasa nyepesi lakini pia kufunga biashara kila Jumamosi kwa ajili ya usafi wanasema ni siasa nyepesi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili linafanyika kwa sababu bahati nzuri mimi nimehudumia sana Jiji la Dar es Salaam. Kuna mifereji ya maji ya mvua mikubwa sana iko kule chini lakini Dar es Salaam population imeongezeka, wakati huo kilikuwa Kijiji, ikaja ikawa Mji, ikawa Jiji. Tusipozuia manailoni, karatasi na takataka zile ngumu zitakwenda kujaa kwenye mifereji ya chini ya ardhi kule, ndiyo maana sasa hivi tumeanzisha utaratibu kwamba tukusanye zile takataka ili zibebwe, zikatupwe, zichomwe mahali maalum, zisiendelee tena kuzuia mifereji iliyo huku chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu Wabunge wamechangia suala la DAWASA na DAWASCO, kubwa ni kwamba Mheshimiwa Mbunge Waitara amesema kwamba wakati tunafanya mabadiliko ya Sheria Ndogo DAWASCO kuna miradi mingi ambayo wameianzisha, hawajaikamilisha. Hatuvunji DAWASCO, DAWASCO, ipo na DAWASA ipo. Kwa hiyo, ule utekelezaji wa miradi iliyokuwa imeanzishwa utaendelea mpaka ikamilike na tunaendelea kuboresha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika hili suala la maji ya mvua, kwamba mvua ikinyesha barabara zinajaa maji, maeneo ya wananchi yanajaa maji. Ni kweli kabisa kwamba miundombinu ya maji ya mvua ni michache kwa sababu Jiji la Dar es Salaam, population imeongezeka, majengo yameongezeka. Kwa sasa hivi tumeanza kupata fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji taka na tayari Waziri wa Fedha amesaini mkataba, tumepata zaidi ya dola milioni 100 kutoka Korea na utekelezaji utaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Zuberi Mohamedi Kuchauka amezungumzia kwamba tatizo la maji taka si tatizo la DAWASCO wala la DAWASA, nakubaliana na yeye. Wakati ule Miji yetu ilikuwa kama Vijiji, hakukuwa na haja hiyo, ikaja ikawa Miji, haja haikuwa kubwa, ilipofikia kuwa miji ndiyo tukawa na mashirika ya majitaka, sasa hivi limekuwa Jiji. Kwa sasa ndiyo maana tumeanza, tunabadilisha sheria na kuweka hili jukumu liwe na ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo machache, naunga mkono hoja.