Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Emmanuel Peter Cherehani (3 total)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kumekuwa na malalamiko makubwa sana hapa nchini kwa ndugu zetu wafugaji waliotaifishiwa na kuuziwa ng’ombe wao katika hifadhi zetu, na wakaenda Mahakamani wameshinda kesi na Mahakama ikaamuru Serikali iwarejeshee mifugo yao hawa wananchi, sasa Serikali imekaa kimya. Nini kauli ya Serikali juu ya suala hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Cherehani Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, natambua kuwepo kwa migogoro mingi kati ya wafugaji na wakulima, wafugaji na maeneo ya hifadhi. Wiki moja iliyopita siku ya Alhamisi nilikuja hapa mbele yako kutoa ufafanuzi wa kero hii ambayo inagusa maeneo yote kwa wafugaji, wakulima lakini pia maeneo yetu ya hifadhi, nilitolea kauli hapa, hili ni eneo moja kati ya maeneo ambayo nilitolea kauli. Tunatambua na tunajua kwamba tuna kesi nyingi ambazo wafugaji wameweza kupeleka Serikali Mahakamani au hifadhi imepeleka wafugaji Mahakamani. Kwa kuwa jambo hili ni la kisheria sana na lina sheria zake, pale ambapo imeamriwa ni lazima tutekeleze kwa sababu hakuna ambaye anaweza kupinga amri ya Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kama imetokea kuna mahali hukumu imetoka, Mahakama imeamua, halafu hakuna aliyetekeleza jambo hili tunaweza kupata taarifa ni wapi huko ili tuwaambie Serikali watekeleze mara moja kwa sababu ni hukumu na hatuwezi kupinga Mahakama. Lakini pia nitoe wito pale ambapo kuna migogoro ya aina hii Mahakama imetoa maamuzi yake uko utaratibu, kama eneo moja hilo iwe wafugaji au hifadhi hawajaridhika ni kukata rufaa badala ya kupinga moja kwa moja kutotekeleza amri hiyo.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo nitoe wito kwenye maeneo yote ambayo yana amri hii lazima tuheshimu mamlaka ya Mahakama na tutekeleze maamuzi ya Mahakama. Kwa kufanya hivyo tutajenga mshikamano zaidi kwenye mihimili yetu hii mitatu ambayo pia inafanyaka kazi kwa kuheshimiana na tunaenda vizuri. Kasoro kama hizo, tukipata mahali kuna tatizo hilo basi Mheshimiwa Mbunge atujulishe ili tuchukue hatu ili tuweze kuhakikisha kwamba kila mmoja anapata haki yake kupitia chombo kinachosimamia haki, ambayo ni Mahakama.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Waziri Mkuu kumekuwa na malalamiko makubwa sana hapa nchini kwa ndugu zetu, Watanzania wenzetu waliokuwa watumishi Serikalini walioondolewa kwa kigezo cha kutokuwa na cheti cha form four.

Sasa ni lini watalipwa stahiki zao halali za kiutumishi ambazo wanadai ili waweze kupeleka watoto wao shule na wengine waweze kujitibisha? Nini kauli ya Serikali? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ulipata taarifa wiki moja iliyopita agizo ambalo lilitolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan juu ya msamaha alioutoa kwa wale wote waliokuwa wameondolewa kwenye utumishi, waliokuwa wametambulika kama wameghushi vyeti vya kidato cha nne na wametumikia katika nchi hii kwamba sasa tufanye mapitio tuwatambue. Pia alitoa fursa la kuunda timu kutoka Wizara ya Utumishi na Utawala Bora kwa pamoja na TAMISEMI ili kuwatambua wale wote waliotumikia kwenye nchi hii na kutoa agizo kwamba walipwe asilimia tano ya pension walikuwa na mchango kwenye pension waliokuwa wanaichangia ili waweze kulipwa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Tume ile itakapokamilisha kazi tutayatambua haya yote, idadi yao, halafu pia wangapi, wale wote ambao wanastahili kupata hiyo asilimia tano ya mchango waliokuwa wanauchangia, lakini pia kuona makundi mengine na maelekezo yanayotolewa.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameunda Tume naomba nisitoe majibu juu ya hilo tuiache Tume ifanye kazi yake, halafu tutapata majibu sahihi. (Makofi)
MHE. EMMANUEL E. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi hii ya kuuliza swali kwa Waziri kwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu, hapa nchini Serikali imekuwa ikitoa 10% ya mikopo kwa walemavu, wanawake, lakini pia vijana ambao wako chini ya miaka 35, lakini kuna kundi hili ambalo linazidi miaka 35 ambalo ndio mhimili mkubwa wa familia na ndio walipa ada wakubwa kwa watoto na ndio wanaotibisha familia, lakini pia ndio kundi ambalo linalinda uchumi wa familia.

Sasa ni nini mkakati mkubwa wa Serikali wa kuweza kulikumbuka kundi hili katika masuala ya mikopo? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imetenga fungu maalum la mapato ya ndani katika kila halmashauri kutoa fursa za kuendeleza ujasiriamali kwa kutoa mikopo midogo midogo na ya kati kwa makundi ya wanawake 4%, walemavu 2% na vijana 4%. Sasa kundi hili la zaidi ya miaka 35 sio kwamba tumelisahau bali tunazo fursa nyingine za kupata mitaji kupitia mifuko mbalimbali, lakini pia kwenda kwenye taasisi za fedha kama vile mabenki na ile mifuko ambayo imepata vibali maalumu vya kukopesha.

Mheshimiwa Spika, haya makundi tunayoyazungumza kutokana na tathmini za ndani za Serikali ziko changamoto zinazokabili makundi haya ya vijana, lakini pia walemavu na wanawake. Mpango wetu ni kuhakikisha kwamba makundi haya nayo yanakuwa na eneo ambalo wanaweza kwenda kupata mikopo hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kuwapa faraja Watanzania kwamba Serikali imeendelea kuzungumza na benki kwa maana ya taasisi za fedha kufungua madirisha ya kutoa mikopo ya viwango mbalimbali kulingana na mahitaji ya mteja mwenyewe na huku ndiko ambako pia tunaruhusu hili kundi la watu kutoka miaka 35 na kuendelea ili kuweza kupata mikopo na kwa hiyo, kadiri Serikali itakapokuwa na uwezo itaendelea kufungua milango na kuanzisha mifuko mingine ili kutoa fursa kwa makundi mengi zaidi kupata mikopo kama mitaji kwa ajili ya shughuli zao za ujasiriamali.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)