Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Emmanuel Peter Cherehani (16 total)

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa wakulima wote nchini hasa wa mazao ya kimkakati ikiwemo pamba, korosho, kahawa, chai na michikichi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikisajili wakulima kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo Bodi za Mazao, Sensa ya Kilimo na Vyama vya Ushirika. Hadi Agosti, 2022 jumla ya wakulima 1,499,989 wa mazao ya kimkakati ya chai wakulima 31,093, pamba wakulima 556,384, kahawa 305,261, korosho 483,034, miwa 6,746, mkonge 2,369, pareto 10,846, tumbaku 53,758 na mazao mengine 50,498, wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Usajili wa Wakulima (Farmers Registration System) na vyama vitatu vya ushirika wa michikichi wamesajiliwa. Serikali imeanza kupitia upya mifumo ya usajili wa wakulima kwa lengo la kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha usajili wa wakulima wa mazao yote nchini ili kurahisisha upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani na masoko.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Waziri Mkuu aliyoitoa mwaka 2017/2018 ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa katika Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza ahadi mbalimbali zinazotolewa na viongozi wa Kitaifa kote nchini ikiwemo ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika jimbo la Ushetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 inaendelea na mpango wa kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati yenye uhitaji mkubwa nchini kote ikiwemo Kituo cha Afya cha Ulowa.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika kila Mkoa na Wilaya nchini. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 100 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa vyuo vya VETA katika Wilaya 63 ambazo hazina vyuo hivyo. Kiasi hiki pia kitatumika katika ujenzi wa chuo cha VETA cha Mkoa wa Songwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kahama ni miongoni mwa Wilaya zitakazojengewa Vyuo vya VETA ambapo kwa sasa Serikali ipo katika hatua za maandalizi ya ujenzi. Hivyo wananchi wa Jimbo la Ushetu watanufaika na Chuo cha VETA cha Wilaya ya Kahama.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaruhusu kampuni zinazonunua tumbaku kwenda kwenye AMCOS kujinadi ili kuongeza ushindani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hapo awali Serikali iliruhusu kampuni za ununuzi wa tumbaku kujinadi kwa wakulima na kuingia mikataba kwa misimu mitatu ya kilimo. Kilimo cha mikataba kwa misimu mitatu kiliathiri bei ya Tumbaku kwa mkulima kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji kampuni na uzalishaji. Jambo hilo lilisababisha Serikali kubadili mfumo huo na kwenda mfumo wa msimu mmoja ili kuongeza ushindani na ufanisi.

Mheshimiwa Spika, Kilimo cha mkataba kwa msimu ni mbadala mzuri kwa wakulima na kampuni kwasababu kinapunguza gharama zinazotokana na kampuni kujinadi. Vilevile, kilimo hicho kinatoa fursa kwa pande zote mbili kujitathmini kabla ya kuingia mkataba kwa msimu unaofuata.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka Watumishi pamoja na Vifaa Tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa kada za afya. Katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 na 2021/2022, watumishi wa kada hiyo 10,462 waliajiriwa kote nchini. Katika ajira hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ilipangiwa watumishi 55 na watumishi 25 walipelekwa kwenye Hospitali ya Halmashuri ya Wilaya ya Ushetu. Aidha, Aprili, 2023, Serikali imetangaza nafasi 8,070 za ajira kwa kada za afya ambapo baadhi ya watumishi hao watapelekwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Hospitali ya Wilaya ya Ushetu ilipelekewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na tayari MSD wameanza kusambaza vifaa tiba kwenye Hospitali za Halmashauri 67 ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Ushetu. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Hospitali hiyo imepokea shilingi milioni 100 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya macho na meno. Vilevile, Hospitali hii imepokea vifaa tiba kwa ajili ya jengo la Kutolea Huduma za Dharura (EMD).
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa nyumba za Watumishi nchini hasa katika Halmashauri mpya?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2012 hadi 2014, Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa ilijenga nyumba za gharama nafuu 1,189 katika halmashauri 31 kwa ajili ya kuziuza kwa watumishi waliopo katika Halmashauri hizo. Aidha, kuanzia mwaka 2013 hadi sasa, jumla ya nyumba 983 zimejengwa na taasisi ya Watumishi Housing Company katika mikoa 19 na kuuzwa kwa watumishi wa umma na wanachama wa mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Serikali kupitia taasisi zake ikiwemo Shirika la Nyumba la Taifa na Watumishi Housing itaendelea kujenga nyumba bora kwa ajili ya watumishi wa umma ili kuwaongezea tija katika utendaji kazi.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itatenga maeneo ya malisho ya mifugo katika Pori la Usumbwa Forest Reserve?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua mahitaji ya Wananchi wa Ushetu na inaendelea kufanya tathmini ya eneo la Msitu wa Usumbwa Forest Reserve ili kujiridhisha kama unastahili kumegwa kwa ajili ya kutengwa eneo la kuchungia. Pindi tathmini itakapokamilika wananchi watajulishwa. Wakati Serikali inaendelea na tathmini hiyo wananchi wanashauriwa kuendelea kuheshimu maeneo hayo ili kuhifadhi msitu huo.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Pori la Usumbwa Forest Reserve na Hifadhi ya Pori la Kigosi Moyowosi – Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Pori la Usumbwa Forest Reserve ambalo kwa sasa ni Hifadhi ya Taifa Kigosi, haina mgogoro wowote wa mpaka na wananchi wa Ushetu. Kwa sasa kilichopo, wananchi wa Ushetu waliwasilisha maombi ya kumegewa eneo ambapo Serikali inaendelea na tathmini na pindi itakapokamilika, wananchi watajulishwa, nakushukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka wa Pori la Usumbwa Forest Reserve na Hifadhi ya Pori la Kigosi Moyowosi - Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pori la Usumbwa Forest Reserve ambalo kwa sasa ni hifadhi ya Taifa Kigosi haina mgogoro wowote wa mpaka na wananchi wa Ushetu. Kwa sasa kilichopo ni wananchi wa Ushetu waliwasilisha maombi ya kumegewa eneo, ambapo Serikali inaendelea na tathmini na pindi litakapokamilika, wananchi watajulishwa. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha majadiliano na Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco ili iweze kurudi nchini kuendelea kununua tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu na wakulima wa tumbaku nchini kuwa mwekezaji mpya ambaye ni mzawa Kampuni ya Amy Holdings Limited imekamilisha taratibu za kuchukua shughuli zilizokuwa zinafanywa na Kampuni ya TLTC na ameshapewa leseni. Aidha, Kampuni ya Amy Holdings Limited imeanza kununua tumbaku ambapo inatarajiwa kununua tani 10,000 za tumbaku katika msimu wa mwaka 2022/2023 ambazo itazichakata katika kiwanda kilichopo Morogoro ifikapo mwezi Julai, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wakulima wote nchini, ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua milango ya wawekezaji ambayo matokeo yake ni pamoja na kupatikana kwa mwekezaji huyu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali wa kupeleka umeme wa uhakika katika Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ili kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwenye Halmashauri za Ushetu, Msalala na Kahama, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa muda mfupi wa kujenga kituo kidogo cha umeme (Switching Station) kwenye eneo la Nyamirangano lililopo kwenye Halmashauri ya Ushetu. Kupitia kituo hicho kidogo, TANESCO itaongeza njia nyingine za umeme kutokea kwenye kituo hicho kwenda Ushetu, Msalala na Kahama ambazo zitasaidia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme. Mradi huu unategemewa kukamilika 2024 na unagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.2, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imekamilisha ujenzi wa Miradi ya Maji katika Vijiji vya Kisuke, Igunda na Nyankende. Vilevile utekelezaji wa Miradi ya Maji katika Vijiji vya Mpunze, Sabasabini, Iponyanholo, Itumbili, Mitonga na Ididi inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2022. Kukamilika kwa miradi hii kutaboresha huduma ya upatikanaji wa maji toka asilimia 58 hadi asilimia 62. Aidha, mpango wa muda mrefu ni kutekeleza mradi utakaotumia chanzo cha maji cha Ziwa Victoria ambapo usanifu utafanyika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuongeza nafasi za ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara. Utaratibu wa kuandikisha Jeshi askari wapya umefafanuliwa kwenye Kanuni ya 5 ya Kanuni ya Majeshi ya Ulinzi Juzuu ya Kwanza (Utawala). Aidha, Serikali imeondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ongezeko la idadi ya ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne hutegemea bajeti inayotengwa kwa mwaka husika. Jeshi huandikisha askari wapya baada ya kupewa maelekezo na idadi ya nafasi kulingana na uwezo wa bajeti. Nafasi hizo hugawanywa kulingana na mahitaji ya kitaaluma na ujuzi.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa upanuzi wa uwanja wa Ndege uliopo Wilaya ya Kahama ili uwe na hadhi ya kutua ndege kubwa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo, Benki ya Uwekezaji ya Watu wa Ulaya imeendelea na ukarabati pamoja na upanuzi wa miundombinu yote katika Kiwanja cha Ndege Shinyanga ili kiwanja hicho kiweze kutumika wakati wa usiku na mchana. Utekelezaji umefikia 66.8%. Pia Serikali kwa kushirikiana na kampuni binafsi iliyokuwa ikichimba madini Mjini Kahama, imefanya maboresho katika Kiwanja cha Ndege cha Kahama kwa kujenga jengo jipya ya abiria na kuendelea kufanya maboresho ya miundombinu mingine ili kuendelea kutoa huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa kuzingatia mahitaji ya sasa, Serikali itakamilisha kwanza Mradi wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga na endapo mahitaji ya mkoa yataongezeka, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Kahama.
MHE. MOSHI S. KAKOSO K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imejipanga kujenga ghala katika Halmashauri za Wilaya nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkoa wa Shinyanga.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuongeza nafasi za ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara. Utaratibu wa kuandikisha Jeshi askari wapya umefafanuliwa kwenye Kanuni ya 5 ya Kanuni ya Majeshi ya Ulinzi Juzuu ya Kwanza (Utawala). Aidha, Serikali imeondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ongezeko la idadi ya ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne hutegemea bajeti inayotengwa kwa mwaka husika. Jeshi huandikisha askari wapya baada ya kupewa maelekezo na idadi ya nafasi kulingana na uwezo wa bajeti. Nafasi hizo hugawanywa kulingana na mahitaji ya kitaaluma na ujuzi.