Supplementary Questions from Hon. Emmanuel Peter Cherehani (48 total)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mwaka 2017/2018 Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa anazindua Siku ya Ushiriki wa Afya Duniani katika Jimbo la Ushetu katika Halmashauri ya Ushetu, Kata ya Ulowa, aliwaaahidi wananchi kuwajengea kituo cha afya, lakini hadi leo ni miaka mitano kituo hicho hakijaanza kujengwa.
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Kituo Cha Afya kwa wananchi wa Ulowa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ahadi zote za viongozi wetu wa Kitaifa ni kipaumbele katika utekelezaji, kikiwepo Kituo cha Afya katika Kata ya Ulowa. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba Serikali imechukua mahitaji na ahadi hii, na tunatafuta fedha, wakati wowote kupitia fedha za tozo tutaleta pale milioni 250 ili Kituo cha Afya cha Ulowa kianze kujengwa. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, hizi zimekuwa ni namba tu ambazo zikisomwa kila mwaka; lakini ukienda kwenye uhalisia kabisa huwezi kukuta mkulima mfano wa pamba ana kitambulisho cha usajili, hata kwenye korosho huwezi kukuta mkulima kwenye korosho ana kitambulisho cha usajili. Ukiangalia hata Chama chetu cha Mapinduzi juzi tu kimesajili wanachama wake, lakini tayari wamepewa kadi. Sasa mimi nataka nijue kauli ya Serikali ni lini sasa hawa wakulima wa mazao ya kimkakati watapewa kadi za usajili ambazo zitakuwa kama vitambulisho kwao?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; tumekuwa zikiagizwa pembejeo nyingi ambazo zinakuja kwa wakulima lakini madhara yake zinakuwa zinabaki kwa sababu uhalisia kamili wa wakulima waliosajiliwa bado haujajulikana. Nataka nipate majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Serikali tunaendelea na zoezi la usajili wa wakulima nchi nzima ambapo mfumo unaotumika hivi sasa ni mfumo ambao unampa kila mkulima utambulisho maalum kwa maana atakakuwa na namba yake maalum ambayo ndiyo utakuwa utambuzi wake. Zoezi hili linaendelea katika maeneo mengi kwa ukamilifu mzuri na uratibu unaendelea vizuri na tunaamini kabisa likikamilika litatibu changamoto zote ambazo wakulima wanazipata hasa katika utambuzi wao kwa sababu kila mkulima atapata namba yake maalum ya utambuzi; na tunaamini kupitia hapo sasa hata zile huduma muhimu watazipata kwa rahisi zaidi.
Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba zoezi hili linaendelea na linaendelea vizuri na mwisho wa siku tutakuwa na kanzidata ya wakulima wote nchini kila mtu kwa maeneo yake alipo pamoja na maeneo ambayo anayamiliki na mazao anayalima na yields anazipata.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, Serikali itapeleka lini mawasilino ya uhakika ya simu kwa wananchi wa Ushetu hasa katika Kata ya Ulewe, Igwamanoni, Igunda pamoja na Bukomela ambapo wananchi hao bado wanapanda juu ya mti na milimani kutafuta mawasiliano ambayo ni hatari sana kwenye maisha yao.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ambazo Mheshimiwa Cherehani amezitaja tayari katika bajeti ya Serikali ambayo ililetwa Bungeni hapa Kata hizo ziliwekwa katika bajeti. Bajeti hii ambayo inaunganisha minara 763 na kama ambavyo nimesema hapo mwanzoni tayari tumeshatangaza tenda tarehe 20 Oktoba na tarehe 2 Disemba itafunguliwa na baada ya hapo ujenzi wa minara hii utaanza mara moja. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa nini sasa Serikali isipeleke mbegu bure kabisa kwa wakulima wa alizeti ili waweze kuzalisha alizeti kwa wingi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya mafuta hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuona tunaongeza uzalishaji wa zao la alizeti, kila jambo linakwenda kwa hatua. Hatua ya kwanza tumeanza na ruzuku ya kuuza mbegu ya kilo moja kwa Sh.5,000 ambayo katika hali ya kawaida mkulima angepata kwa Sh.35,000 mpaka Sh.40,000. Kwa hiyo kwa hatua hii, ni hatua nzuri ambayo Serikali imeianza na huko mbeleni tutalifikiria ombi la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka 2020, wakati anafunga kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Ushetu, alipokea simu kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. Magufuli na akawaahidi maelefu ya wananchi pale kwamba atawajengea kilometa 54 za lami kutoka Kahama – Nyandekwa - Iboja mpaka Iyogo kilometa 54 za lami: je, ahadi hii itaanza kutekelezwa lini kwa wananchi wa Ushetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tumekuwa tukisema, ahadi zote za viongozi wa Kitaifa ni ahadi ambazo zinatekelezwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara zote ambazo zimeahidiwa tunazo lakini tunaendelea kuzitekeleza kadri ya upatikanaji wa fedha ikiwa ni pamoja na hii barabara ambayo Mheshimiwa Rais aliahidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii pia itajengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliagiza. Ahsante. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ahadi hii sasa ina miaka Sita na inaenda mwaka wa Saba, ahadi zote zinazotolewa na Viongozi wetu wa Kitaifa wanatoa kwa sababu ya hali ilivyo ngumu kwenye Majimbo yetu yaliyo mengi. Ninavyojua kwa Viongozi wa Kitaifa ni sehemu ya maelekezo ya Serikali, ahadi hii hata hayati marehemu John Kwandikwa aliifuatilia sana lakini utekelezaji wake mpaka leo haujafanyika.
Je, ni nini kauli ya Serikali juu ya ahadi hii na kwa nini Serikali isitafute fedha za ziada kuhakikisha kituo cha afya hiki kinajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, alichoeleza ni kwamba hii ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nieleze tu Bunge lako tukufu kwamba moja ya mpango mkubwa wa Serikali ambao ulikuwepo awali ni kuhakikisha kwamba zile Tarafa zote nchini ambazo hazikuwa na vituo vya afya tulikuwa tunapeleka vituo vya afya, ndiyo maana katika mwaka wa fedha huu unaokwenda kuisha Serikali imepeleka fedha za ujenzi wa vituo vya afya 233 ikiwemo katika Jimbo la Ushetu ambapo tumepeleka fedha awamu ya kwanza, fedha za tozo Milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya ambacho wao wamepeleka katika eneo lingine.
Meshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo katika eneo hili ambalo liko katika ahadi baada ya kumaliza huu mkakati ambao tumeuainisha kumaliza Tarafa zote nchini basi na eneo lako tutaliweka katika kipaumbele kuhakikisha kwamba hii ahadi haichukui muda mrefu ili kuwasaidia wananchi wa Kata ya Ulowa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwenye Bunge la Bajeti lililopita Mheshimiwa Naibu Waziri aliniahidi kupeleka fedha kwenye ujenzi wa Kituo cha Polisi kilichopo katika Halmashauri ya Ushetu; na wananchi wale walishajichanga pamoja na wadau mbalimbali wakajenga msingi. Sasa nataka nijue, ni lini Serikali inapeleka fedha hizi ili kuanza ujenzi wa Kituo cha Polisi katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu maeneo ya Wilaya mpya kama ilivyo ya Ushetu wanahitaji kuwa na vituo vya polisi ili kusogeza huduma za usalama wa raia karibu zaidi na wananchi. Ni ahadi yetu kwamba kwa vyovyote vile kwa sababu wananchi wameshajitokeza, wamechangia nguvu zao na jitihada wakafikia mpaka kiwango cha msingi, nimtie moyo Mheshimiwa Mbunge, kwamba pale ambapo tutapata fedha kwa ajili ya ujenzi, Wilaya ya Ushetu itazingatiwa pia. Nashukuru.
MHE: EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, Serikali itaanza lini ujenzi wa kilometa 30 kwa kiwango cha changarawe kutoka Uyogo kupita Iberansua, Mbika mpaka Urowa, ambapo barabara hii imekuwa kiungo kikubwa sana kwa wananchi na uchumi wa halmashauri wa Ushetu na mpaka tunavyoongea sa hizi magari yanadondoka ya wakulima wanaosafirisha mazao yao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Nyongeza la Mheshimwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii kama alivyosema inahitaji kujengwa kwa changarawe. Sehemu ya barabara hii ilikuwa chini ya barabara ya TARURA na sasa ndo imepangiwa bajeti. Nataka nimuhakikishie
Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka huu tutakwenda kuikarabati barabara hiyo. Nitumie nafasi hii kumuagiza Meneja wa Mkoa wa Shinyanga aende aitembelee hii barabara na kuifanyia ukarabati wa haraka ili kuokoa maisha na mali na hayo magari ya wananchi. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, hospitali ya Halmashauri ya Ushetu imekamilika ujenzi wake, lakini wananchi bado wanatembea zaidi ya kilometa 80 kwenda kupata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama.
Je, ni lini Serikali italeta vifaa tiba katika hospitali hiyo ili wananchi hawa waanze kupata matibu karibu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza priority ambayo Mheshimiwa Waziri wa Afya ameelekeza sasa hivi ni kuhakikisha hospitali zote zile ambazo zimeshajengwa vituo vya afya, zahanati na hospitali za Wilaya na majenzi yote, kuhakikisha sasa vifaa tiba vinaenda kununuliwa. Kama ambavyo nilisema jana sasa hivi shida siyo fedha kwa sababu Rais wetu kama nilivyosema tayari alishapeleka shilingi bilioni 333.8 na tayari kila mwezi kuna utaratibu wa kupeleka shilingi bilioni 15 MSD. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kwanza nitumie fursa hii kwa kushirikiana na wenzangu wa TAMISEMI kwamba RMO asimamie kwanza OPD kwenye hiyo hospitali ianze, kwa sababu inawezekana kuanza OPD mapema na kujipanga kwa ajili ya kuanza wakati tunangojea vifaa vya kuhakikisha hospitali hii inaenda kufanya kazi kama full flagged kama hospitali ya Wilaya. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kuondoka kwa kampuni ya TLTC hapa nchini kumechangia kudorora kwa soko la Tumbaku.
Je, ni lini Serikali itakamilisha mazungumzo na kampuni hii ili iweze kurudi Tanzania kununua Tumbaku za wakulima na kuongeza tija na ushindani? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu niwaambie wakulima wa Tumbaku na niwaambie Watanzania, kiwanda kilichokuwa cha TLTC na kampuni ya TLTC imenunuliwa na sasa hivi amepatikana mwekezaji mwingine na mwekezaji huyu yupo kwenye hatua za mwisho na mwaka huu kiwanda kile kitafunguliwa. Serikali tunawasaidia wawekezaji wapya kuweza kupata minimum quantity ya tumbaku ili kiwanda kile kifunguliwe, kwa hiyo nataka niwaambie tu wakulima wa tumbaku kilichokuwa kiwanda cha TLTC amerudi sokoni kupitia kampuni nyingine ambayo imeweza kununua kiwanda kile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie tu kwamba kiwanda kile kinafunguliwa na ninaamini msimu ujao wa 2022/2023 uzalishaji na makisio yataongezeka tofauti na tulivyokuwa sasa hivi. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nataka nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini Serikali itakuja kutatua mgogoro uliopo katika Halmashauri ya Ushetu pamoja na Kariwa ambao unazidi kuchukua sura mpya na sasa mpaka wananchi wangu zaidi ya 17 wamekamatwa na kuwekwa ndani bila sababu zozote za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampa pole Mheshimiwa Mbunge, na pia nawaomba wananchi wa Ushetu wawe na subira. Tulipanga kwenda kufanya mazungumzo na wananchi, lakini ratiba zikaingiliana. Nawaomba wananchi wa Ushetu wawe wavumilivu, baada ya Bunge hili, tutaondoka na Mbunge wao kwenda kuzungumza na kutatua changamoto hii, ahsante. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Zao la pamba ni kati ya mazao ya kimkakati hapa nchini lakini wakulima wake bado wanazalisha kilo 300 mpaka 400 kwa heka moja.
Je, ni nini mkakati wa Serikali sasa kwa wakulima hawa waweze kuzalisha kilo 500 mpaka 1,000 kwa heka moja?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, anachokizungumzia Mbunge hapa ni tija na sisi tumejipanga katika Wizara kuhakikisha wakulima wetu wanalima kwa tija. Kwanza, kabisa kuwasaidia kupata viuatilifu sahihi; pili, kuwasaidia kupata teknolojia za kisasa za kilimo cha pamba; na tatu, ni kuhakikisha kwamba wanajifunza kanuni bora za kilimo kama ambavyo hivi sasa tumeona kule kupitia TARI na Balozi wa Pamba juu ya mfumo mpya wa spacing ambao umesaidia sana kuongeza uzalishaji katika zao la pamba.
Kwa hiyo, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba, tunatambua changamoto hizo na tumejipanga kuhakikisha kwamba mkulima wa pamba anazalisha kwa tija.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimwulize Naibu Waziri wa Ardhi, Serikali inapeleka lini fedha za upimaji wa ardhi katika Halmashauri ya Ushetu hasa katika kata zinazokua kwa kasi; Kata ya Igwamanoni, Kata ya Idahina, Nyankende pamoja na Burungwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali lililoulizwa na Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli maombi ya wananchi wa Ushetu juu ya kupimiwa eneo lao yalishawalishwa kupitia Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa, tutakapokuwa tumeshapata fedha hizo, tutaleta fedha Ushetu ili sasa maeneo yale yaweze kupimwa, kupangwa na kumilikisha wananchi wetu ili maendeleo yaweze kupatikana kama ambavyo Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza.
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza napenda nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo ameyatoa kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka pengine nitoe ufafanuzi kuhusiana na hizi pesa ambazo halmashauri zinaomba kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha. Naomba watambue, fedha aliyotoa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, ile Shilingi bilioni 50 inakwenda kwenye Halmashauri kulingana na maandiko wanayotoa. Fedha ile inakwenda kusaidia kwenye Halmashauri ambazo ndiyo zenye mamlaka ya Upangaji. Kwa hiyo, tunategemea ile pesa isihesabike kama ndiyo fedha inayokwenda kukamilisha kazi, isipokuwa Halmashauri zinatakiwa kutenga fedha ya ndani kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya ardhi. Kwa hiyo ile isihesabiwe kama ndiyo fedha ambayo inategemewa sana katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Mamlaka za Upangaji, sisi tuna-support kuongeza kile ambacho ninyi mmetenga kwa ajili ya maendeleo ya Ardhi na siyo kwamba tunatoa bajeti kwa ajili ya ku-fulfill mpango mzima wa kupanga katika maeneo yenu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niwapongeze Wizara niwapongeze Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri wanazofanya. Kwa kuwa Manispaa ya Kahama ina chuo cha FDC ambacho kinafanya kazi kama ile ile ya Chuo cha VETA: Kwa nini sasa chuo hiki cha VETA kisijengwe katika Halmashauri ya Ushetu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili: Kwa kuwa uhitaji wa Chuo cha VETA kwa wananchi wa Ushetu mkubwa sana kulingana na ongezeko kubwa la vijana ambao wanamaliza vyuo vikuu lakini hawaendelei na masomo ya juu: Kwa nini sasa Serikali isione hili kwa umuhimu kulingana na umbali wa kilometea zaidi ya 113 kutoka Ushetu kuja Manispaa ya Kahama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kuwa Wizara haipangi maeneo ya kujenga vyuo hivi vya VETA, ni jukumu la Serikali za Mikoa pamoja na Wilaya kupanga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa vyuo hivi vya VETA. Naomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakuu wa Mikoa washirikishe Waheshimiwa Wabunge wa maeneo mbalimbali kuhakikisha kwamba wanakwenda kupanga maeneo sahihi ya kuweza kufanya ujenzi wa vyuo hivi vya VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lakwe la pili, tunajua umuhimu wa vyuo hivi na hivi sasa tumeanza katika ngazi ya Wilaya pamoja na Mikoa; baada ya kukamilika zoezi hili katika ngazi za wilaya pamoja na mikoa, tutafanya tathmini ya kina ili kuweza kuona namna gani tunaweza kuzifikia zile Halmashauri ambazo labda ziko mbali na maeneo ambayo yamejengwa katika VETA zile za Wilaya pamoja na Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wizara ya Mifugo imekuwa ikitoa ahadi kwa wananchi wa Ushetu kwa ajili ya kuwajengea majosho. Hata Mheshimiwa Mpina wakati akiwa Waziri alishafika Kaya za Nyankende, Ulewe na Ubagwe akaahidi lakini utekelezaji wake mpaka sasa hivi hakuna. Nataka nipate kauli ya Serikali.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Serikali imefanikiwa kupeleka jumla ya fedha shilingi milioni 540 kwa ajili ya ujenzi wa majosho katika halmashauri mbalimbali nchini, na bado kiasi cha shilingi takribani milioni 100 zipelekwe pia. Ninaamini Wilaya ya Ushetu ni miongoni mwa Wilaya ambazo ni wanufaika. Naomba mara baada ya hatua hii ya Bunge nikutane na Mheshimiwa Mbunge Cherehani aweze kunipatia orodha ya vile vijiji vyake ili niweze ku-cross check kwa ajili ya ufuatiliaji wa ujenzi wa majosho haya ya wananchi wa Ushetu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nikushukuru sana.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Ushetu lina changamoto kubwa sana ya umeme, hasa maeneo ya vijijini, maeneo ya shuleni, hospitalini na hata maeneo ambapo umeme upo unakatika katika sana.
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa uhakika kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/2023 Serikali imetenga takribani Shilingi Bilioni 400 ili kuboresha na kuimarisha gridi yetu ya Taifa na hivyo tunaamini baada ya kupata hizo pesa na mradi wa kuboresha gridi ya Taifa kutekelezwa, tatizo la kukatika katika kwa umeme litaendelea kupungua kwa sehemu kubwa.
Mheshimiwa Spika, pia katika eneo hilo umeme vijijini bado unaendelea kupelekwa kwa mikataba ambayo ipo na eneo la Shinyanga kwenye Jimbo lake ni eneo ambalo tayari lina Mkandarasi na anaendelea na kazi.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, changamoto ya maji katika Jimbo la Ushetu ni kubwa sana, lakini pia hata miradi iliyoanzishwa toka mwaka 2019 hasa katika Kata za Saba Sabini, Mkunze na Chambo haijakamilika.
Je, ni lini Serikali itaweza kukamilisha miradi hii ili wananchi hawa wa Ushetu waweze kupata maji safi na salama?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kaka yangu Cherehani kwa kweli ameingia muda mfupi, lakini amekuwa anawapigania watu wake na si mara moja ameshafika ofisini. Kubwa utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, tutatoa fedha kwa Jimbo la Ushetu kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na wananchi wa Ushetu waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tunatumia sasa maji ya Ziwa Victoria kuhakikisha wananchi wa Ushetu wanaenda kupata maji ya uhakika. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa vile utaratibu unaotumika sasa ni wa mkataba wa mwaka mmoja mmoja. Swali la kwanza; je, Serikali ina mkakati gani sasa ya kuwafanya wakulima hawa waweze kutambua ni kampuni ipi nzuri ili waweze kuingia nayo mkataba?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Bodi ya Tumbaku na ndiyo msimamizi mzuri wa zao hili, lakini haina fedha kabisa haina magari hata ya kwenda kwenye masoko, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuweza kuiopatia fedha Bodi ya Tumbaku ili iweze kusimamia vizuri masoko ya tumbaku hapa nchini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza kwa sababu Bodi ya Tumbaku ina ofisi katika mikoa yote ya tumbaku na Bodi ndiyo custodian wa taarifa zote za makampuni ya ununuzi wa tumbaku tumekuwa tukitumia nafasi hiyo kuendelea kuwapa taarifa sahihi wakulima kupitia ofisi zetu hizo ili watambue mnunuzi mzuri wa kuingia naye kwenye mkataba. Sambamba na hilo, pia tunayo taarifa za wanunuzi wote katika tovuti ya Bodi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili la bajeti kilifanyika kikao cha wadau wote wakakubaliana kwamba ili kuijengea Bodi uwezo kuanzia msimu unaokuja tutaanza kuchaja shilingi thelathini katika kila tumbaku mbichi kwa ajili ya kuiboresha Bodi yetu ya Tumbaku ili iweze kufanya ufatiliaji na kuendeleza zao hili la tumbaku.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Mgogoro kati ya Pori la Usumbwa Forest Reserve na Pori la Hifadhi ya Taifa Kigosi Moyowosi umedumu kwa muda mrefu sana. Sasa je, ni lini Serikali itaushughulikia mgogoro huu ili kuwapa nafasi wananchi wa Jimbo la Ushetu hasa wanaozunguka Kata za Idahina, Nyankende, Ulewe pamoja na Ubago waendelee na shughuli zao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote niendelee kuwaomba wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo haya waendelee kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kuangalia namna iliyo bora ya kutatua migogoro hii.
Mheshimiwa Spika, tuna Kamati ya Mawaziri Nane ambayo ina maelekezo kutoka kwa Mheshimiwa Rais kwamba tuzunguke nchi nzima kuhakikisha kwamba tunatatua migogoro hiyo. Sambamba na hilo tumezielekeza taasisi, endapo kuna migogoro mipya ambayo haimo ndani ya hii migogoro inayotatuliwa na Kamati ya Mawaziri Nane basi tuanze pia kuangalia mchakato mpya kuangalia namna iliyo bora ili tuweze kutatua migogoro hiyo. Kwa hiyo, niwaombe wananchi wote ambao wana migogoro mipya katika maeneo yao Serikali inaendelea kuyafanyia kazi ili tuone njia iliyo bora ya kutatua migogoro hiyo.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Serikali ina mkakati gani wa kuongeza Mkandarasi katika Wilaya ya Kahama yenye Halmashauri mbili Ushetu pamoja na Msalala kutokana na aliyepo kupeleka umeme kwa kusuasua sana?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi anaepeleka umeme katika Wilaya ya Kahama ni Mkandarasi anayeitwa Tontan ambaye tunakiri ana mapungufu na hasa katika kazi yake anayoifanya Tanga na tumewekeana masharti ya kutimiza, akishindwa kuyatimiza mwezi huu wa Nne hautaisha ataondoka site zetu ili tuweze kupata Mkandarasi mwingine wa kupeleka umeme katika maeneo hayo. Kwa hiyo wananchi wa Kahama ninawaahidi kabisa kwamba umeme katika maeneo yao utapelekwa na utakamilika kwa wakati kwa sababu ni jambo linalotakiwa kukamilika kwa wakati.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wakulima wa tumbaku wamekatwa makato makubwa sana ya upandaji wa miche ya miti ambapo ni zaidi ya shilingi 813 kwa kila mche mmoja.
Sasa kwa nini, Serikali isiondoe kabisa makato haya kwa wakulima wa tumbaku ili waweze kupanda miti kwa hiari yao bila makato yoyote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tumepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tuna kikao cha wadau ambacho tutajadili mambo haya na kuweza kukubaliana kwa pamoja. Kwa hiyo tumeuchukua ushauri wa Mheshimiwa Mbunge.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante; Barabara ya Mpunze-sabasabini ipo Nyagholo mpaka Igwamanoni imekatikakatika haipitiki kabisa na imepandishwa kutoka TARURA kwenda TANROADS. Ni nini mkakati wa Serikali kwa ajili ya kuijenga barabara hii angalau hata kujua maeneo yaliyokatika ili wananchi waweze kupita kwa urahisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara aliyoitaja ilikuwa inahudumiwa na wenzetu wa TARURA, na ndiyo kwanza imekuja sasa TANROADS. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa wa Ushetu pamoja na wananchi wa Ushetu, kwamba tumesikia, na ninamwagiza Meneja wa Mkoa wa Shinyanga, cha kwanza aende akahakikishe kwamba yale maeneo yote ambayo yamekatika anayarejesha ili kuwe na mawasiliano. Pia aweze kufanya tathmini ili maeneo yote yale korofi tuweze kuangalia namna ya kuyarakabati vizuri ili yaweze kupitika muda wote hata kipindi cha masika, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Wilaya ya Kahama ina mwingiliano mkubwa sana wa raia wa kigeni lakini Ofisi ya Immigration katika Wilaya ya Kahama haina gari kabisa na haina kabisa usafiri. Inafikia hatua mpaka viongozi wa uhamiaji wanakimbizana na raia wa kigeni kwa kutumia pikipiki ambayo ni hatari sana kwenye maisha yao. Je, Serikali itapeleka lini gari la Uhamiaji katika Wilaya ya Kahama?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali inaendelea kuimarisha kuviwezesha vyombo vyake vya usalama ili viweze kutekeleza majukumu yake vizuri. Bahati mbaya katika swali la msingi huwa tunauliza polisi na hili limekuja kwa Immigration. Tutafuatilia Idara ya Immigration kuona uwezekano wa kuwapatia watu wa Kahama gari kulingana na changamoto ya wageni na shughuli za kibiashara nyingi zilizopo katika Mji wa Kahama. Kwa hiyo tutawasiliana na Mheshimiwa Mbunge ili kuona namna ya kutanzua tatizo hilo, nashukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nawashukuru sana TAMISEMI kwa kazi wanazozifanya katika Jimbo la Ushetu. Tumepokea vifaa vya meno na x-ray, lakini hatuna wataalamu wa meno na mtaalamu wa mionzi: Je, katika ajira hizi 8,000 tutapatiwa hao wataalamu wa mionzi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Ushetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Nina Zahanati ya Bugomba A, Elias Kwandikwa, Bugera, Manungu pamoja na Makongoro, zina watumishi wawili wawili tu, inafika mahali Jumapili na Jumamosi wanafunga kwa ajili ya kupumzika. Katika watumishi hawa 8,000, na hizi zahanati zitapata watimishi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa
Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cherehani, swali lake la kwanza la wataalamu wa meno na mionzi, kwa sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ina timu ambayo inazunguka katika Halmashauri mbalimbali zilizopokea vifaa tiba kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wataalamu wetu kule kuweza kujua namna ya kutumia vifaa hivi vya kisasa vinavyokwenda. Kwa hawa wataalam wa meno na wa mionzi, tutahakikisha kwamba hospitali hii pia inapata wataalamu hawa kwenda kusaidia wananchi wa kule Ushetu.
Mheshimiwa Spika, nikijibu kwenye swali lake la pili, kama ambavyo nimesema kwenye majibu yangu ya msingi, hawa watumshi 8,070 ni katika upungufu uliopo nchi nzima, ikiwepo kule Ushetu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Ushetu nayo itapokea watumishi hawa wa afya.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ushetu haina jengo lolote la Kituo cha Polisi na wanaendelea kuishi kwenye majengo ya kupanga, hakuna nyumba za maaskari, lakini sioni mkakati wowote wa Serikali juu ya suala hili toka mwaka jana nalilalamikia. Je, ni nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunajua Ushetu ni wilaya mpya ilibebwa kutoka Kahama na ndio changamoto ya kuanzisha maeneo mapya ya makazi. Tunachokifanya katika Wizara ya Mambo ya Ndani, hususani Idara ya Jeshi la Polisi ni kuendelea na ujenzi wa maeneo haya hatua kwa hatua kadri tunavyopata bajeti. Nimuahidi Mheshimiwa Cherehani, nilishajibu hapa Ushetu ni eneo lenye kipaumbele kwa sababu ya shughuli za kiuchumi zilizoko huko. Wanahitaji kuwa na kituo cha polisi cha uhakika, kwa hiyo pale tutakapopata fedha kituo hiko kitajengwa, nashukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Wilaya ya Kahama ina Halmashauri tatu, lakini ina mwenyekiti mmoja tu wa Baraza la Ardhi. Sasa Serikali ina makakati gani wa kupeleka Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi kama nilivyolieleza katika jibu la msingi, tunaendelea na michakato ya kupata Wenyeviti katika kuziba pengo la karibu Wilaya 57, na tukishafanikisha, Ushetu nayo itapewa umuhimu wa pekee nao katika kufikishiwa Mwenyekiti wa Baraza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu, katika maeneo yote hapa nchini ambayo mabaraza hayajafika, Mamlaka za Miji husika, kama kuna majengo ambayo tayari yapo, ambayo tunaweza tukayatumia katika kipindi hiki, basi tuarifiane, na Waheshimiwa Wabunge kwenye maeneo yenu mtupe taarifa ili tuweze kuona uharaka wa kuwaleta wenyeviti wetu katika maeneo husika, ahsante sana.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa shirika hili limekuwa linajenga nyumba katika halmashauri mpya zilizoko mjini. Je, ni lini sasa shirika hili litaanza kujenga nyumba za watumishi katika halmashauri zilizoko vijijini hasa katika Halmashauri ya Ushetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Serikali inakuwa inapeleka fedha nyingi za ujenzi wa madarasa, zahanati na hospitalini lakini watumishi hawana nyumba kabisa. Ni lini mkakati wa Serikali kuwajengea nyumba watumishi hawa hasa walioko vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, Shirika la Nyumba la Taifa (National Housing) limeendelea kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Ushetu kwa kuwasemea watumishi wetu walioko katika maeneo na hasa Ushetu huko, kitu kikubwa kabisa ambacho tunaweza tukaahidi ni kwamba tunaendelea katika hatua mbalimbali za ujenzi na katika muda wowote ule tutafika huko Ushetu.
Mheshimiwa Spika, ombi letu sisi kama Wizara nikuomba halmashauri zote kutenga maeneo ambayo wangependekeza kujenga nyumba hizi zinazosimamiwa na mashirika kama hiyo National Housing na Watumishi Housing.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili; fedha nyingi zimepelekwa katika hizi mamlaka zetu za halmashauri kupitia TAMISEMI, na nimeona kwa sehemu kubwa sana fedha zinazopelekwa zinakuwa na kiambata cha nyumba za watumishi.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali la msingi kwa kupitia mashirika yetu haya taasisi zinazojenga nyumba zetu za watumishi. Sisi kama Wizara ya Ardhi tutaendelea kusimamia ujenzi wa nyumba hizo lakini niwahimize tu vilevile kwenye halmashauri wanapopata fedha zinazotoka Serikali kuu basi katika ile matumizi wajibane waweze kuweka na nyumba kiasi za watumishi wao katika maeneo wanapo pokea fedha zao. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Wananchi wa Ushetu wametenga hekta zaidi ya 5,000 ambazo ni nzuri na zina mtiririko wa maji kwa ajili ya umwagilijaji: Serikali inakuja lini kuwajengea skimu ya umwagiliaji wananchi wa Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Halmashauri kwa kutenga eneo kubwa hilo kwa ajili ya umwagiliaji. Maelekezo yangu ni kumwelekeza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kupeleka wataalam kwenda kuliangalia eneo hilo kama linafaa kwa ajili ya kuweka miundombinu basi, Serikali itahakikisha kwamba inaweka miundombinu katika eneo hilo. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka taa za barabani katika Mji wa Nyamilangano ambao tayari umewekewa kilometa tatu za lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, taa za barabarani katika maeneo ambayo ameyasema tumetenga kwenye bajeti ambayo imepitishwa na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo tutamuwekea katika eneo lake Mheshimiwa Mbunge.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, hali ya Daraja la Mto Ubagwe hali ni mbaya sana na Mheshimiwa Waziri ni shahidi alituma watu wa TANROADS.
Ni lini Serikali inaanza ujenzi wa daraja hili ili kuwanusuru wananchi na hali ya mvua?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafahamu na tumefanya mawasiliano makubwa, nimtoe shaka naamini daraja hilo ambalo ni muhimu sana kwa Wilaya ya Ushetu litaanza kujengwa kipindi hiki cha mwaka huu wa fedha, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, wananchi wa Ushetu wanaheshimu sana mipaka ya Serikali kwenye mapori yetu na ni walinzi wazuri sana, lakini idadi ya ng’ombe wa wananchi wa Ushetu inazidi kuongezeka. Mpaka sasa Wananchi wa Ushetu wana ng’ombe 176,000 na wanapakana na mapori haya hawana kabisa eneo la kuchungia.
Je, Serikali itamaliza lini hii tathmini ili wananchi hawa waweze kupata sehemu ya kulishia mifugo yao, badala ya kuendelea kugombana na watu wa maliasili?
Swali langu la pili, Halmashauri ya Ushetu ina mapori matatu. Inayo pori la Usumbwa Forest Reserve, Ubagwe Forest Reserve pamoja na Mpunze Saba Sabini, lakini Ubagwe Forest Reserve imekuwa na mgogoro mkubwa sana na Halmashauri ya Kaliua ambao umechukua sura mpya. Hata juzi wananchi wangu wamekamatwa wakawekwa ndani bila sababu za msingi, mbaya zaidi juzi kumekuwa na mgogoro kati ya maliasili wa TFS na Askari wa Maliasili wa Ushetu, Mheshimiwa Naibu Waziri huo mgogoro anaujua nilimtaarifu.
Nini kauli ya Serikali na Mheshimiwa Waziri ni lini tutaenda kutatua mgogoro huu kwa wananchi wangu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Katika eneo hili la kulishia mifugo, ninaendelea tu kumshauri Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Ushetu kwamba, kwa kuwa Wizara ya Maliasili imepewa dhamana ya kuyalinda na kuyasimamia maeneo haya, inapofika suala la mahitaji ya maeneo ya mifugo basi waendelee kuwasiliana na Wizara husika ili tukae Pamoja, tuone namna iliyo bora ya kutenga maeneo haya, tumepewa kazi ya kuyasimamia tu na kuyatunza maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, suala lingine hili la kuhusu mipaka na migogoro kati ya TFS na Pori la Usumbwa Forest Reserve tunaendelea kuangalia namna ya kuainisha mipaka na kwa kuwa sote ni Serikali moja kwa maana ya Halmashauri na TFS, hakuna haja ya kugombania mipaka isipokuwa ni masuala ya kiutawala tu kwamba hawa ni TFS na hawa ni Halmashauri ni kukaa pamoja tu ili sote tulinde haya mapori kwa pamoja.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa wananchi hawa walizoea kufanya shughuli zao za kibinadamu wakati pori hili halijaingizwa kwenye Hifadhi ya Taifa TANAPA; tathmini hii sasa itakamilika lini, kwa sababu nimekuwa nikiahidiwa kila mara, ili wananchi waweze kumegewa eneo lao waweze kuendelea kufanya shughuli za kibinadamu hasa katika Kata ya Ulewe, Kata ya Ubagwe na Kata ya Idahina? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kamishna wa Ardhi katika Mkoa wa Shinyanga kakamilisha tathmini katika Pori la Ubagwe Forest Reserve katika mpaka wa Kaliua ambapo sasa inahitajika gharama ya kwenda kuhakikisha wanaweka mipaka ili kuondoa mgogoro pia uliopo katika eneo hili. Serikali lini sasa itapeleka fedha ili mipaka hii iweze kuwekwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge. Ushetu nilifika na nilizungumza na wananchi wa pale na tuliwaahidi kwamba migogoro hii tunaishughulikia. Kwenye upande wa eneo hili ambalo wananchi wanadai, nataka tu niwaambie wananchi wa Ushetu kwamba wakati Usumbwa Forest Reserve ikiwa kwenye hadhi ya msitu kwa maana ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania wanalisimamia, pori hili lilikuwa linaruhusu shughuli za kibinadamu na hadhi yake tulikuwa tunaruhusu ufugaji wa nyuki na wananchi walikuwa wanarina asali katika maeneo hayo. Ndiyo maana leo hii wananchi wanaona ni kama walinyang’anywa, lakini hadhi ya pori ilibadilishwa kutoka kwenye forest reserve, ikapanda kuwa National Park. National Park inazuia shughuli za kibinadamu ndani yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa sasa hivi tunaangalia utaratibu wa kuyashusha hadhi baadhi ya maeneo ili wananchi waendelee kuanza kupata faida ya uhifadhi, na pia waendelee kufuga nyuki kwa ajili ya kurina asali. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi wananchi wa Ushetu, suala hili tunalishughulikia na Mbunge wao amekuwa akiliulizia mara kwa mara. Kwa hiyo, muda siyo mrefu tunatarajia kuleta azimio Bungeni. Nadhani kuna baadhi ya maeneo yatashushwa hadhi na wananchi wataanza kufaidika na urinaji wa asali. Kwenye suala hili la lini tutaweka mipaka, kwa kuwa tathmini tayari imeshakamilika ni wakati wowote tu kuanzia sasa. Kwa kuwa ni jukumu letu Wizara ya Maliasili na Utalii kuweka mipaka, basi tutaendelea kuainisha mipaka halisi, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Ushetu wamejichanga wakafanikiwa kujenga msingi wa Kituo cha Polisi lakini mpaka leo ni zaidi ya miaka mitatu Serikali haijafanya chochote. Sasa, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunafahamu Ushetu ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazijawa na Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na kwenye Kata mbalimbali. Pia tunatambua juhudi ambazo zimefanywa na wananchi kuanza ujenzi wa vituo hivi na Serikali inao wajibu wa kusaidia kukamilisha. Ninapenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kama nilivyokwishasema kwenye jibu la msingi kwamba kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo ambayo wananchi na wadau wameanza kujenga vituo hivyo ili kuvisaidia ujenzi huo uweze kukamilika. Nashukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wananchi wa Jimbo la Ushetu kwa kutumia nguvu zao wameweza kukamilisha zahanati saba; Zahanati ya Butibu, Zahanati ya Itumbo, Itebere, Makongoro, Manungu, Bugera na Misayo ambayo ni Zahanati tumeipa kwa jina la Eliasi Kwandikwa ambayo imejengwa kwa msaada wa Kampuni GTI na hiyo zahanati yenyewe tayari inavifaa tiba. Lakini sasa ni lini Serikali inatuletea vifaatiba na watumishi kwenye zahanati hizi ili wananchi waweze kupata matibabu yao maeneo ya karibu badala ya kuendelea kwenda zaidi ya kilometa 80 kupata matibabu.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwanza mimi na yeye ili tufanye mambo ambayo yanatekelezeka ametaja zahanati zenye tatizo cha kwanza awasiliane na Mganga Mkuu wa Wilaya yake kupitia Mkurugenzi ili walete mahitaji husika wa eneo hilo mimi na yeye tushughulikie hilo liweze kufanyika nanimuambie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na fedha ambayo Mheshimiwa Rais wetu ameshazipeleka MSD lakini kwenye manunuzi ya juzi ya fedha zile za UVIKO kununua vifaatiba kama X-Ray, CT Scan Serikali ime-save yaani imepata salio baada ya kununua kwa bei rahisi ime-save zaidi ya bilioni 17 na zote zinaelekezwa kwenye kununua vifaatiba na madawa kwaajili ya vituo vinavyoanzishwa.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, niendelee kumshukuru sana Rais na nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima hawa wa tumbaku wamekuwa wakipangiwa uzalishaji na makampuni na mwisho wa siku wanachozalisha kinakuwa kidogo tofauti na matarajio yao na hasa wakulima hawa wadogo; na wanachozalisha cha ziada mwisho wa siku kinashindwa kununuliwa na mwisho wake kinaitwa jina la makinikia; nini kauli ya Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili, kumekuwa na makato makubwa sana ya upandaji wa miti kwa wakulima hawa wa tumbaku. Fedha nyingi zinaishia kwa makampuni hayo na nyingine zinaishia benki na mkulima anaondoka bila fedha na mfano tu tosha mwaka jana wakulima hawa wa tumbaku wameweza kukatwa zaidi ya dola milioni tatu za miti ambapo ni zaidi ya bilioni sita. Nini kauli ya Serikali ili hao wakulima sasa tuwawekee mazingira mazuri waweze kuzalisha kwa wingi na weweze kupata faida kubwa na Serikali yetu iweze kupata fedha za kigeni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la kwanza ni kweli imekuwepo hiyo changamoto na ndiyo maana Serikali tumeendelea kuhakikisha kwamba tunafungua milango kuwaleta nchini wawekezaji wengi zaidi ili kupata soko la uhakika la tumbaku yetu. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba Serikali itaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kwamba zao hili la tumbaku linapata soko la uhakika na wakulima mwisho wa siku tumbaku yao inanunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la kuhusu makato, hii ni concern ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akiisema mara kwa mara na tumeshamuelekeza Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku, kukaa na wadau wote kuona namna bora ya uendeshaji wa shughuli ya biashara ya tumbaku ili mkulima anufaike na kila ambacho anakilima shambani.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hili tunalichukua kwa umakini mkubwa na tunaendelea kulifanyia kazi ili mwisho wa siku mkulima aweze kunufaika na tumbaku yake.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Jimbo la Ushetu wamejichanga wakafanikiwa kujenga msingi wa Kituo cha Polisi lakini mpaka leo ni zaidi ya miaka mitatu Serikali haijafanya chochote. Sasa, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Polisi kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunafahamu Ushetu ni moja ya Wilaya mpya ambazo hazijawa na Vituo vya Polisi ngazi ya Wilaya na kwenye Kata mbalimbali. Pia tunatambua juhudi ambazo zimefanywa na wananchi kuanza ujenzi wa vituo hivi na Serikali inao wajibu wa kusaidia kukamilisha. Ninapenda kumuahidi Mheshimiwa Mbunge kama nilivyokwishasema kwenye jibu la msingi kwamba kipaumbele kitawekwa kwenye maeneo ambayo wananchi na wadau wameanza kujenga vituo hivyo ili kuvisaidia ujenzi huo uweze kukamilika. Nashukuru.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri. Hali ya makali ya mgao wa umeme katika Wilaya ya Kahama pamoja na Halmashauri yake ni makali mno, hali ni ngumu, wafanyabiashara wanashinda wamekaa, umeme umekatika siku nzima. Sasa Mheshimiwa Waziri yupo tayari kufanya ziara katika Wilaya hii ya Kahama pamoja na Halmashauri zake ajionee hali ilivyo kwa wananchi hawa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuipa Mkoa wa ki-TANESCO Wilaya hii ya Kahama ambayo inakua kwa kasi kwa nchi hizi za maziwa makuu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Cherehani.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mgao wa umeme, kwa sababu sasa hivi tumetengamaa na tumepunguza kidogo ule upungufu ambao ulikuwepo, niwaelekeze TANESCO na kituo chetu cha pamoja cha gridi (Grid Control Center) wahakikishe maeneo yote yanaendelea kupata umeme kulingana na jinsi ambavyo tunaboresha upatikanaji huo wa umeme.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ziara, nitafika Ushetu Mheshimiwa Mbunge. Suala la pili kuhusiana na kuweka kituo cha kimkoa Ushetu, Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kuangalia tathmini kama Wilaya ya Kahama inafaa kuwekwa kama Mkoa wa ki-TANESCO kwa ngazi ya mkoa, na kama itafaa, basi tutafanya hivyo, lakini kama haifai, tutaendelea kuboresha huduma ili wananchi wa Ushetu waendelee kupata huduma bora na stahili za masuala ya umeme. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa kilometa 54 za lami kwa wananchi wa Ushetu ambapo Serikali iliahidi yenyewe, lakini hakuna dalili yoyote inayoendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli kwamba Serikali iliahidi kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami. Barabara zote zinazofanana na hiyo ya Ushetu, mpango wa Serikali ni kuzijenga kwa kiwango cha lami, lakini utakubaliana nami kwamba hapa ndio tunapopitisha bajeti, kwa hiyo bajeti ndio inayoamua. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba sisi tutaendelea kuweka kwenye mipango ile ahadi ya Serikali ambayo tuliahidi iweze kutimia kuijenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Niwashukuru sana TAMISEMI kwa kazi nzuri wanayoifanya, swali langu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara inayotoka Kata ya Burungwa – Kinamapula pamoja na Ngokolo mpaka Makao Makuu ya Halmashauri ya Ushetu pamoja na barabara ya kutoka Burungwa – Sabasabini – Ifunde inayounganisha Manispaa ya Ushetu na Manispaa ya Kahama; ni lini sasa zitafanyiwa marekebisho hizi barabara kwa sababu, mpaka sasa hazipitiki kabisa kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba bahati nzuei katika eneo lake la Halmashauri ya Ushetu tumeanza utekelezaji wa barabara kwa kiwango cha lami. Na sisi tutakachokifanya tu ni kuongeza fedha kwa maana ya bajeti katika eneo lake ili barabara alizozitaja ziweze kutekelezeka. Ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa maji pamoja na timu yake yote kwa kazi nzuri wanayoifanywa kwa miradi ya maji, lakini nina maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mkoa wa Shinyanga una Majimbo sita na Jimbo la Ushetu ni mojawapo lakini Majimbo matano yana miradi mikubwa ya maji ya Ziwa Victoria isipokuwa Jimbo la Ushetu ambalo ni kilometa kama 17 tu ilipo miradi mikubwa wa maji. Leo hii maji hayo yameenda Tabora, yameenda Shelui, Mkoani Singida. Sasa nataka nipate commitment ya Serikali ni lini sasa maji haya ya Ziwa Victoria yataanza kupelekwa kwa wananchi wa Jimbo la Ushetu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi kwenda kushuhudia adha wanayoipata wananchi wa Jimbo la Ushetu hasa katika Kata za Uyogo, Mapamba, Ushetu, Ulowa, Ubagwe na Ulewe ambako sasa wanauziwa ndoo ya maji kwa shilingi 1,500 hadi 2,000? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napokea shukrani za Mheshimiwa Cherehani. Naamini anafahamu wiki iliyopita tayari watendaji wetu kutoka Makao Makuu ya RUWASA walikuwa jimboni kwake na chanzo cha wale watendaji kufika pale ni kwa sababu tunaenda kuanza mradi huu ambao tutachukua maji ya Ziwa Victoria kuleta kwenye maeneo haya ambako miradi inahitajika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuongozana na Mheshimiwa Mbunge nilishamjibu kwamba baada ya watendaji wetu wataalam wakishamaliza eneo lao, nitakwenda kuongeza hamasa ya kuona miradi hii inatekelezwa ndani ya muda uliopangwa. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niwashukuru Wizara ya Kilimo kwa kazi nzuri wanazofanya. Wakulima wa pamba maeneo wanakolima pamba hasa katika Jimbo la Ushetu wamekuwa na changamoto kubwa sana ya maghala ya kuhifadhia pamba na madhara yake pamba hii inachafuka sana na kuhatarisha soko letu la ndani na la nje. Je, ni lini sasa Serikali itawajengea maghala ya kudumu wakulima wa pamba hapa nchini, hasa katika Jimbo la Ushetu ili waweze kuhifadhi pamba yao ili kulinda soko letu la ndani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja kati ya mikakati tuliyonayo ni kuhakikisha tunapunguza post harvest loss kutoka asilimia 35 ilivyo hivi sasa kurudi tarakimu moja. Mkakati uliopo ni ujenzi wa maghala ya kutosha, ndio maana kwenye bajeti yetu tuliyoisoma hapa Bungeni, bajeti ya ujenzi wa maghala imetoka Shilingi Bilioni mbili mpaka Shilingi Bilioni 25 lengo lake kubwa ni kuhakikisha kwamba tunakuwa na ujenzi wa maghala mengi zaidi. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunaangalia maeneo hayo yote hasa ya uzalishaji ili tuweze kuwa na maghala ya kutosha na tuweze kuhifadhi mazao yetu ya kilimo katika mfumo mzuri.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Maji wa Kata ya Igunda umekuwa wa kusuasua kwa muda mrefu. Ni nini kauli ya Serikali ili kuweza kukamilisha mradi huu ili kuondoa adha kwa wananchi wa Kata ya Igunda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba wilaya zilizoko katika Mkoa wa Shinyanga, zote zinapata maji kutoka Ziwa Victoria isipokuwa tu Ushetu. Tayari tumeshakaa na Mheshimiwa Mbunge na bahati nzuri jana tulijadili sana hili suala na hivyo vijiji tayari nimeshaviripoti kwa wataalamu wetu ili wakajiridhishe tuvute maji kutoka Kahama Mjini au tuvute maji kutoka Shinyanga ilimradi tu wananchi wa vijiji hivyo waweze kupata maji, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Halmashauri ya Ushetu tayari imekwishatenga eneo zaidi ya hekari 42 na lina hati na kila kitu, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa shule hii ya ufundi katika Halmashauri ya Ushetu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali dogo la Mheshimiwa Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Cherehani kwa kutenga eneo lile la Ushetu kwa ajili ya ujenzi wa shule zile za ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nilikuwa najibu swali hapa, azma ya Serikali ni kuhakikisha kwamba yale majimbo ambayo hatujajenga Chuo cha VETA tutakwenda kujenga shule ya ufundi. Kazi hii tunatarajia ianze mwaka ujao wa fedha wa 2024/2025. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Cherehani na wananchi wa Ushetu, Serikali ya Mama Samia iko kazini na mwezi Julai mwaka ujao wa fedha shule zile 100 za elimu ya amali tutakwenda kuanza ujenzi wake likiwemo na eneo la Ushetu.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Ushetu ina shule moja tu ya kidato cha tano na sita, lakini tuna Shule Kongwe ya Tarafa ya Mweli ambayo ina vigezo vyote. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuipandisha shule hii ili iweze kukidhi vigezo vya kidato cha tano na sita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, sawa, namwelekeza mkurugenzi atume watu waende wakafanye tathmini kwenye hiyo shule waone kama kuna miundombinu hitajika ili waweze kutuma maombi Wizara ya Elimu ili waweze kuja kuipandisha hadhi shule hiyo kama inakidhi vigezo. (Makofi)
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Wilaya ya Kahama imekuwa ndiyo kitovu cha kibiashara kwa Mkoa wa Shinyanga, lakini pia na Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Nchi hizi za Maziwa Makuu. Kwa nini Serikali isitenge japo fedha kidogo ili kuukarabati uwanja huu ambao ni wa kiwango cha moramu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Manispaa ya Kahama imekuwa ikikusanya fedha nyingi zaidi ya shilingi bilioni 13 mpaka shilingi bilioni 15 kwa mwaka. Kwa nini Serikali isitoe kibali sasa kwa Manispaa hii ya Kahama angalau uwanja huu uwekwe kwa kiwango cha lami pamoja na miundombinu yetu ili kuondoa adha wanayoipata wasafirishaji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Cherehani kwa ufuatiliaji wake wa karibu wa Uwanja wa Ndege wa Kahama lakini hata ule wa Shinyanga. Pili, napenda kumwarifu Mheshimiwa Cherehani pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kwamba katika kipindi ambacho Serikali imewahi kutenga fedha nyingi kuliko wakati mwingine wowote, ni sasa. Hivi ninavyozungumza, takribani Shilingi trilioni moja zinajenga viwanja vya ndege karibu vyote kwenye nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, moja, tumepokea ushauri wake mzuri kwa ajili ya kuweka moramu ili uwanja huu uendelee kutumika zaidi na ikizingatiwa ni jengo la ubia ambalo limejengwa na wenzetu wa Madini. Pili, namwomba pia awe na subira kidogo, tutakapokamilisha Uwanja wa Ndege wa Shinyanga, tutapima mahitaji makubwa yaliyopo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kahama halafu tuone ni hatua ipi ambayo inahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, izingatiwe kwamba, tunapozungumza hapa hata maeneo mengine kwenye viwanja vya mikoa, kuna mahitaji makubwa ya fidia pamoja na viwanja hivyo vifanyiwe maboresho. Kwa hiyo, watupe muda kidogo, baada ya hapo tutaona cha kufanya kama Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nampongeza kwa sababu amekuja na mawazo ya kimapinduzi. Anazungumza juu ya Halmashauri ya Kahama kwamba ni halmashauri kubwa ambayo inakusanya mabilioni ya pesa na anaomba kibali kwamba pengine waruhusiwe kufanya ukarabati. Kimsingi Serikali hii ya Awamu ya Sita inaunga mkono jitihada za halmashauri na Waheshimiwa Madiwani wa aina yake katika kuiunga mkono Serikali kusaidia maboresho mbalimbali ya viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu chini ya Mheshimiwa Waziri Mbarawa pamoja na Mamlaka yetu ya Viwanja vya Ndege haitakuwa kikwazo, bali itakuwa msaada katika kurahisisha azma yenu hiyo kutokana na umuhimu mkubwa ambao mmeuona endapo mtatenga fedha kwa ajili ya kufanya maboresho.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa Ndege wa Kahama unapokea watu zaidi ya 200 kwa siku. Je, Serikali ina mpango gani wa kuupanua na kuujenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Uwanja wa Kahama ni moja ya viwanja muhimu kwa Taifa letu na kwa kushirikiana na wadau tumeshajenga jengo la abiria zuri sana. Tuko kwenye hatua za tathmini ili kuhakikisha kwamba tunajenga njia kwa ajili ya kuruka na kutua ndege.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kahama ina mkandarasi mmoja tu wa kupeleka umeme wa REA vijijini pamoja na halmashauri zake tatu. Sasa ilhali amezidiwa na malalamiko ni makubwa sana kwa wananchi wetu, ni nini mkakati wa Serikali wa kupeleka kila halmashauri mkandarasi wake ili kuondoa malalamiko haya kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpa pole Mheshimiwa Cherehani kwa changamoto hii ya mkandarasi. Nataka nimhakikishie kuwa tunafahamu changamoto ya mkandarasi huyu wa Kahama na tayari tumeshachukua hatua ikiwemo kukaa naye na kuweza kujua ni namna gani tunamwongezea nguvu ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Mbunge, ndani ya hizi wiki mbili, tatu mimi na yeye tuongozane twende Kahama ili tuweze kuangalia utekelezaji wa miradi hii katika eneo hili kwa sababu ni kweli kuna changamoto, lakini sisi dhamira yetu ni kutatua changamoto hizi ili wananchi wapate umeme kwa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunafahamu changamoto za mkandarasi na tutaendelea kumsimamia kwa weledi mkubwa sana kuhakikisha anamaliza kazi ambayo alitakiwa kuimaliza kwa wakati, ahsante.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Spika, naomba kujua mkakati wa kuanza ujenzi wa Kituo cha Afya Ulowa, ahadi ambayo Mheshimiwa Waziri na wewe mlikuja kuwaahidi wananchi, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Kata ya Ulowa ni kata yenye wananchi wengi sana katika Jimbo la Ushetu. Tulishafanya ziara pale na kwa kweli mahitaji ya wananchi pale ni kituo cha afya. Nikuhakikishie tu kwamba, tumeshakiingiza kwenye Mpango wa Vituo vya Afya vya Benki ya Dunia na tunaamini fedha ikitoka mapema iwezekanavyo tutakwenda kuanza ujenzi katika Kata ya Ulowa. (Makofi)