Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mohammed Said Issa (7 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adhimu kuweza kusimama leo katika Bunge lako Tukufu hili, ikiwa ni mara ya kwanza kwangu mimi kuweza kusimama na kuzungumza na mimi kutoa mchango wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ningependa kuanza na kutoa shukurani kwa sababu, mimi ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili. Ningependa kuwashukuru kwanza wapiga kura wangu wa Jimbo la Konde kwa kunichagua kwa kura nyingi sana, walinipa ushindi wa asilimia 72 katika uchaguzi ambao ulifanyika wa marudio nawashukuru sana. Pia ningependa kushukuru chama changu, Chama cha ACT-Wazalendo kwa kuniamini na kuni- support mpaka kufikia ushindi huo ambao leo nimepata heshima kubwa ya kuwa Mbunge katika Jimbo la Konde, nashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya yote mimi nimekaa hapa kwenye kiti baada ya msiba wa marehemu Kaka yangu Khatib Said Haji, Mwenyezi Mungu ailaze mahali pema roho yake peponi. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Amina.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru wewe pia kwamba ulikuwa unawasiliana na familia kwa ajili ya kusimamia matibabu ya Mheshimiwa Marehemu Khatib Said Haji. Yale mawasiliano uliyokuwa unafanya ulikuwa unafanya na mimi na niliziona juhudi zako. Kwa niaba ya familia tunakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru Serikali mbali ya juhudi ulizozifanya wewe, tulikuwa tukipata mawasiliano kupitia Serikali. Kwa ajili ya kuhakikisha mpendwa wetu yule maisha yake yanaokoka lakini kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu ilikuwa bahati mbaya Mwenyezi Mungu alimuhitaji zaidi. Kwa hiyo, kwa hali hiyo nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kuishukuru Serikali kwa kuendesha uchaguzi wa marudio wa Jimbo la Konde. Uchaguzi ambao ulikuwa ni mfano wa kuigwa, uchaguzi ambao ulionesha kwamba Tanzania tunaweza kufanya uchaguzi wa demokrasia, demokrasia ikashika nafasi yake na watu wote wakafurahia matunda ya demokrasia. Kwa kweli naipongeza sana Serikali kwa kufanya uchaguzi ule ambao hata kunguni hakuuliwa wala hakuguswa. Ahsanteni sana Serikali kwa kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ningependa kumshukuru pia Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na kumpongeza sana, katika hotuba yake ambayo alionesha dhahiri ana nia ya kusimamisha demokrasia katika nchi yetu pale alipokuwa kwenye kumbukizi ya maisha ya Marehemu Maalim Seif Shariff Hamad. Namshukuru sana na ninamuomba, aendelee na nia hiyo hiyo ya kusimamisha demokrasia ili Tanzania tusiwe ni wahanga wa demokrasia tuwe tunafurahia matunda ya demokrasia. Kwa hiyo, ningependa kushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo nije kwenye mpango. Mimi natoka Visiwa vya Zanzibar ni Mbunge kutoka visiwani. Ukisikia Visiwa ni kwamba tumezungukwa na bahari. Bahari sasa hivi imekuwa ikimeza visiwa kila uchao, visiwa vimekuwa vikimegwa kupitia bahari. Hili lipo katika sehemu ya mazingira. Ukija kwenye Jimbo langu la Konde nimezungukwa na bahari kupitia sehemu zangu za Msuka, Makangale, Tondooni, Mnarani kote ni bahari tupu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahari imeshakula karibu nusu kilomita ya eneo la ardhi katika Jimbo langu. Sasa, nikija kwenye mapendekezo ya mpango napendekeza kwamba, katika Jimbo langu kuna kilimo kikubwa sana cha mwani, kilimo hiki mwenzangu Mheshimiwa Omar alikizungumzia jana lakini mimi nitakizungumzia katika eneo tofauti. Nitazungumzia katika maeneo mawili. Eneo la kwanza ni kwamba, kilimo cha mwani ni kilimo ambacho kinalimwa baharini na unapolima kilimo cha mwani maana yake bahari unaifanya ikimbie katika eneo la ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiki kilimo ni kilimo ambacho Serikali inatakiwa kukiangalia sana na kukipa nguvu kubwa ili kuokoa ardhi kuliwa na bahari. Lakini lingine katika kilimo hiki unapolima kilimo hiki maana yake kunapatikana mazalia ya samaki, pia ni faida kubwa sana nimeona katika mpango, tunategemea kupata meli nane za uvuvi pia kama tutakuwa tuna mazalia wengi sana ya samaki, maana yake hizo meli za uvuvi ndio zitaweza kupata kazi. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba Mheshimiwa Waziri katika mpango wako uweke kipaumbele katika kilimo cha mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikihama katika sehemu hiyo nakuja katika kukuza mapato. Katika mpango umetueleza kwamba mapato yameendelea kukua kwa asilimia 7.2 ni kweli kwa data ulizonazo wewe ni hivyo, kama tunavyojua njia kuu ya mapato ya Serikali ni TRA, TRA ndiyo wanakusanya mapato kwa asilimia kubwa ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge lililopita TRA walilalamikiwa sana kwa kufanya makadirio ambayo yalisababisha wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao. Sasa hawa TRA wamekuwa kama vile sijui nisemeje mimi. Maana yake wakati ule walilalamikiwa kwa kutoa makadirio makubwa, kuwalazimisha wananchi kodi ambazo hazina msingi, sasa wamehama katika stage ile wamewachenga kidogo wafanyabiashara, sasa hivi wameleta e-filing. E-filing maana yake mfanyabiashara atapeleka ripoti zake kwa kutumia mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini e-filing tuelewe kwamba wafanyabiashara wengi hawana uelewa wa mambo ya mitandao. Wafanyabiashara wetu ni wale ambao wameshindwa na maisha wakaamua kujiingiza katika biashara. Sasa basi e-filing walivyoileta wameweka mambo ambayo ni ya ajabu ambayo hayamsaidii mfanyabiashara. Kwa sababu, kama walikuwa na shida ya kukusanya mapato kwa kutumia system hii ni sawa, lakini kwanza wangetoa elimu kwa wafanyabiashara hili halikufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili wameingiza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru Allah Subhanahu wa Ta’ala kwa leo kupata nafasi na mimi kuweza kuchangia katika Bunge hili tukufu katika Hotuba ya Waziri Mkuu. Lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ambayo ni kwa ruksa yako ndiyo naweza kuzungumza hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu kwanza utajikita katika biashara; na hii biashara ni katika nchi mbili hivi Zanzibar na Tanganyika, yaani Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Zanzibar na Tanzania Bara tumekuwa tukitegemeana katika mambo mengine ikiwemo biashara. Tunatumia bandari zetu ya Zanzibar na Dar es Salaam.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Waheshimiwa tumsikilize mchangiaji.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatumia bandari zetu ambazo zipo katika Zanzibar na Tanzania Bara katika kupitisha mizigo yetu, lakini mara nyingi biashara huwa inatokea Zanzibar kuja Dar es Salaam ama Tanzania Bara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye biashara ambayo tunafanya sisi Wazanzibar au wananchi wa Zanzibar tumekuwa tukikutana na changamoto nyingi sana ambazo kwa kiasi kikubwa imeonekana inakuwa ni tatizo linalosababishwa makusudi lakini si mipango ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango hii mara nyingi iko vizuri, lakini watendaji ndio wanaoiharibu. Nitoe mfano kidogo. Katika suala la declaration ya mizigo ambayo inasafiri kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara, mizigo ile mara nyingi meli yetu inakuwa ni za hapo kwa hapo siyo zile Meli ambazo tayari zina shadow. Kwa maana hiyo wafanyabiashara ambao wanaleta mizigo wanakuwa na mizigo ambayo ni ya kushtukizwa. Kwa mfano kama kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhan, mfanyabiashara ananunua mzigo leo anataka apakie mzigo kwenye meli lakini kwa bahati mbaya ni lazima awe ametuma ripoti mapema ili mzigo ule uweze kupakiwa na kufika kule, nje ya hapo mzigo ule ukifika meli inapigwa faini na mzigo unapigwa faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii ni changamoto ambayo wafanyabiashara wa Zanzibar wanakutana nalo. lakini si hilo tu, wafanyabiashara wa Zanzibar tumekuwa tukikutana na changamoto ya mizigo ambayo inafika pale Dar es Salaam. Tunakutana na bei kubwa ya wharfage ambayo inakuwa inachajiwa mizigo ambayo inatoka Zanzibar. Kwa hiyo tungeomba bei ile iendane na hali halisi, hasa ukizingatia ile sehemu ambayo inashushwa ni sehemu ambayo fedha zake za kujengea pale zilitoka kwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mheshimiwa Abeid Aman Karume, kwa ajili ya kuwasaidia Wanzazibar lakini leo imekuwa inawakwaza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, baada ya kuyasema hayo, ningependa kwenda kwenye hilohilo la TRA. Mizigo inapotoka bandarini kwenda madukani imekuwa ikisumbuliwa na TRA haohao ilhali imeshafanyiwa inspection na kulipiwa kodi kama kawaida lakini ikifika njiani ikifika tu, ikitoka nje ya geti kuna TRA wengine wanajitokeza na kuwasumbua wafanyabiasha hawa na kushindwa kufanya kazi zao vizuri. Kwa hiyo hili naomba lifanyiwe kazi ili kuendeleza Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie suala la Muungano. Katika ukurasa wa 72 Mheshimiwa Waziri Mkuu ameelezea kuudumisha, kuuenzi na kuulinda Muungano na mimi naipongeza Serikali yetu hilo ndiyo tunalolihitaji kwa sababu Muungano huu ni tunu ya taifa na sote tunaupenda. Lakini kubwa zaidi nilitaka nichangie hapa; hizi kero za Muungano ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi, mimi nakubaliana nazo, ni nzuri na zinasaidia kuondoa changamoto lakini bado tunatakiwa tufike kwa wananchi kujua ni changamoto gani hasa zinaweza kuulinda Muungano? Kwa sababu wananchi bado wanasema kwamba hizi changamoto ni zile zinazoikabili Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanzania, siyo zinazowakabili wananchi. Kwa hiyo, baada ya kutatua changamoto hizi 11 basi turudi kwa wananchi ili na wao waseme ni lipi hasa linaweza kuimarisha Muungano wetu huu na ukawa Muungano wa mfano kama ilivyosema Hotuba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hapo, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Awali ya yote, niwapongeze Mheshimiwa Waziri wa Nishati Mheshimiwa January Makamba pamoja na Naibu wake, lakini pamoja pia na watendaji wake katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli dira ambayo wameionesha ya kutuhakikishia Watanzania kupata umeme wa uhakika ni nzuri sana, mipango yao kwa kweli mimi binafsi naipongeza. Pia hii imeonesha, pale ambapo katika michango yetu ya leo Wabunge, baada ya kupata semina ambazo zimetupa uelewa mkubwa, nimeona pia Wabunge wengi sana wameelewa mipango ya Wizara. Kwa hiyo, hongera sana kwa Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu nitaanza kwa sehemu ya Umeme wa Joto Ardhi yaani geotherm. Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake hapa ameonesha kwamba tutapata umeme wa megawatt 195 ya Umeme wa joto ardhi, lakini mimi kama Mjumbe wa Kamati tulivyofuatilia tumeona kwamba bado Sheria ya JotoArdhi haijawa sawasawa, haijatekelezwa. Sasa najiuliza maswali, ni wapi hasa Waziri anaweza kuja kutekeleza kuzalisha umeme wa jotoardhi wakati bado haijatambulika kwamba bado ni sehemu ya madini ama ni sehemu ya nishati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Waziri anapokuja ku-windup atueleze tayari amefikia wapi kwanza sheria haijaletwa, lakini la pili hakuna miundombinu na la tatu pia bado fidia kwa wanaomiliki maeneo haya yenye jotoardhi haijafanyika. Kwa hiyo, tunakujaje kuzalisha umeme huu wakati haya mambo ya msingi bado. Tunaomba anapokuja ku-windup atufahamishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa REA, tunawapongeza sana mpango wao ni mzuri kwa kuhakikisha kila kijiji, kila kitongoji kinapata umeme unaostahiki, lakini kuna tatizo kidogo ambalo limejitokeza. Tulivyofanya ziara Kamati tuliona kwamba REA imepeleka umeme kijijini lakini nyumba zilizounganishwa ni mbili. Ina maana hapa hakuna maandalizi mazuri, watu hawakuandaliwa na pale tayari kuna mkandarasi tayari ameshalipwa, waliopata umeme ni watu wawili ama watatu, lakini zipo nyumba za jirani hazipata kwa sababu hawakuandaliwa. Nashauri kabla ya kufika pale wananchi waandaliwe, wafanye fitting ili wote wa-enjoy ule umeme wa REA unaokwenda pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine pia ni hili suala la ujazilizi; naona REA kwanza tulianza mita moja, halafu tukaenda mita mbili, halafu tunaenda ujazili, yaani tunakwenda mwisho tutafika hata majina mengine hatuyafahamu. Kwa hiyo, nashauri kwamba sisi lengo letu si mita moja, si ujazili lengo letu ni kuwapa umeme wa uhakika wananchi. Kwa maana hiyo tuhakikishe ile sehemu ambayo tuna deal nayo, basi wapate umeme wote sio tunarudia, hili jambo linatutia hasara kama Taifa, kesho tunarudia, kesho mkandarasi huyu, kesho mkandarasi huyu, linatutia hasara. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri alichukue hili pamoja na timu yake waliangalie ili kuondoa hasara kwa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niende kwenye suala la bei za umeme; hili suala la bei za umeme, nazungumzia umeme wa mijini, sizungumzii umeme wa vijijini ambao huo tumeshaujua ni Sh.27,000. Mheshimiwa Waziri watu wa mijini ambao tayari wana umeme, wale wenye uwezo tayari wameshaweka umeme kwa maana hiyo watu ambao hawajaweka umeme, hawana uwezo kwa nini sasa tumekwenda kuweka bei ya shilingi 320,000; shilingi 500,000 au shilingi 600,000 bila kuangalia hawa maskini ya Mungu, watu wanaishi mjini wanasaidiwa na watu wa vijijini. Kwa maana hiyo lazima hizi bei za umeme kwa sehemu za mijini bado tuziangalie, hii shilingi 320,000 ni kubwa mno, maskini ni wengi pale, tuna umaskini mkubwa katika nchi hii hata kama watu wanaishi mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba bei hii ya shilingi 320,000 ni kubwa sana, hata kama hawatalipa shilingi 27,000 lakini iangaliwe ilipwe ya nafuu ameshauri hapa Mbunge wa Manonga kwamba wao walikuwa wanalipa shilingi 170,000, hiyo kidogo ni affordable, lakini huwezi ukalipa 320,000 hata kazi huna na wewe unataka umeme, unataka kuuza ice-cream, unataka kuuza biashara ndogondogo, lakini hamna. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba aliangalie hili ili tupate bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pale ambapo mwananchi ameshalipa kuunganishia umeme, kunakuwa na muda mrefu anafuatilia muda mrefu, tunaomba Waziri aje na commitment hapa baada ya kulipa atachukua muda gani kuunganishiwa umeme kwa sababu watu wanachukua mpaka miezi miwili, mitatu, tayari wameshalipa lakini hawapati umeme. Kwa hiyo, Waziri atuambie muda halisi hasa baada ya kulipa ni shilingi ngapi na baada ya hapo nini kitafuata kama mwananchi hakupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa sikuona sehemu ambayo kutakuwa na ukarabati wa mabwawa kama vile Hale, Kidatu, Nyumba ya Mungu, Rusumo ambayo haya ni mabwawa yetu ambayo sasa hivi yanatuzalishia umeme, hakuna ukarabati, kwa maana hiyo anapokuja ku-windup atueleze kwamba haya mabwawa ambayo sasa hivi ndiyo tunafaidi keki yake, kuna mpango gani wa kuyaendeleza kwa sababu sasa hivi unapokwenda pale ukiangalia ile mitambo imechakaa. Kwa nini tusiipangie mipango ili ikawa nayo ni mazuri iendelee kutupa umeme wa uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye suala la mafuta; kwa kweli suala la mafuta napongeza bei ambazo zimetangazwa kwa sababu zimekuja kuleta unafuu mkubwa kwa Mtanzania. Kwa mfano, Dar es Salaam imepata ruzuku ya kila lita ya petrol Sh.306 lakini diesel Sh.320. Hii ni nafuu kubwa Mheshimiwa Rais anapaswa kupongezwa, lakini pia Wizara imefanya kazi nzuri, tunategemea kwamba huu mpango utakuwa ni endelevu na wananchi wapate nafuu waweze kufaidika na hii hali nzuri ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nataka kuzungumzia hii TPDC. Hii TPDC ina mchango mkubwa kwa Taifa, tuliiunda wenyewe na kwa ajili ya kufanya biashara ya mafuta, lakini cha kushangaza mtaji wake wote umemegwa na TANESCO na sababu ni nini? TANESCO wanauziwa umeme kwa kutumia gesi, lakini hawalipi, sasa leo unakuja kutuambia unaanzisha vituo vya TANOIL, yaani unaandaa nguo za mtoto lakini mama unampiga viboko atazaaje huyu mama… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. MOHAMMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye amenifanya leo hapa nikasimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuweza kupata nafasi hii ya kuchangia. Pia, nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia katika wasilisho letu hili la Wizara ya Elimu pamoja na Mihezo na Sanaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na elimu na nitachangia sehemu zote mbili. Mchango wangu, lolote lile nitakalolizungumza litaelekea kwenye bajeti ndogo lakini pia hata hiyo ndogo kutokufikia kwa wakati na wakati mwingine hata kutokufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Elimu pamoja na Michezo. Katika kuhudumu katika Kamati hii, nilikuwa kwenye Wizara nyingi. Nilianzia kwenye Nishati na Madini kule mambo ni safi, Wizara ya Biashara, Kilimo na Mifugo, kule bajeti zao zinakwenda vizuri. Huku kwenye Elimu, huku kwenye Michezo, kwa kweli hali ni mbaya. Kama Mheshimiwa Spika, alitaka nije kuangalia Wizara ambazo zinapokea fedha hizi na kuweza kuzifanyia kazi, basi huku kwa kweli fedha haiendi na hiyo inayokwenda ni ndogo mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuangalia hapa, naanzia kwa upande wa elimu ya watu wenye mahitaji maalum. Nimeona hapa sisi tunajikaza kupeleka mahitaji ya wanafunzi wote, mashuleni kote, vyuoni kote lakini kuna kundi muhimu la watu wenye mahitaji maalum, hili tumelisahau. Kundi hili ni muhimu sana kwa sababu tunataka twende nao kwa pamoja. Sasa jambo la kusikitisha, mambo yaliyoko huko kwa watu wenye mahitaji maalum, unaweza kulia wakati unapokea mawasilisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapungufu yaliyopo kwa upande wa vifaa vya kufundishia, vitabu hakuna walimu wanalalamika. Jana nilikuwa naangalia TBC hapa nikamuona mwalimu ambaye anafundisha watu wenye mahitaji maalum na yeye mwenyewe akiwa anahitaji hayo mahitaji maalum, analalamika kupata yale material ya kufundishia. Zile karatasi ambazo zinafaa kwa nukta nundu kufundishia, vitabu hamna, nikashangaa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati hii nikaona hii nayo ni point. Wanalalamika hawa hawana vitabu, hawana printer, hawapati yale mafunzo ya kitaalamu. Kwa hiyo, wao kama alikuja na utalaamu wake ndiyo wamebakia hivyo. Mimi natoa hayo lakini lengo langu Wizara iongezewe bajeti ili vitu hivi vipatikane. Kwa sababu tukiuliza Wizara wanasema bajeti ni ndogo na hiyo hiyo ndogo yenyewe bado haijafika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wanafunzi, kwanza hawa walimu, walimu hawa wenye mahitaji maalum naamini wana kazi kubwa. Tumchukulie mtu ambaye anafundisha mtu ambaye hasikii, hivi ni sawa na mtu ambaye anamfundisha anayesikia? Ana kazi kubwa huyu kubwa lazima tumhurumie leo tunauliza hapa, hana posho lakini ana mshahara sawa na yule anayefundisha mtu wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikirini kama unamfundisha mtu mwenye mahitaji maalumu, mtu asiyesikia, mtu asiyeona, kazi yake ikoje?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa namna anavyochangia lakini nilitaka nirekebishe kidogo maneno; haitwi mtu asiyesikia, anaitwa Kiziwi, mtu asiyesikia kwa tafsiri ya Kiswahili ni mtukutu au mjeuri.

Vilevile unaposema mtu mzima na huyu kwa tafsiri mtu mzima ana umri wa miaka 18 kwenda juu lakini kuna mtu aliyehai na aliyekufa, sasa, tafsiri hapa usiseme mtu mzima na huyu siyo, ni mtu asiye na ulemavu na huyu ni mtu mwenye ulemavu. Nashukuru. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mohammed Issa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MOHAMMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru mtoa taarifa kwa kunielimisha, sijabobea kwenye hizi lugha ambazo ni za kuficha ukakasi. Lengo langu ni kupeleka ujumbe, sasa nimepokea taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili hilo Serikali ilitakiwa ilizingatie kwa sababu hawa wanafundisha watu ambao wana mahitaji maalum. Kwa hiyo, ni lazima wawe na ziada kazi yao ni kubwa na ni tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini upande wa wale wanafunzi, mimi nilitamani wawe na vile vitu ambavyo vinasaidia. Tumeuliza hapa wheelchair tu hawana, zile fimbo za kutembelea hawana. Watafikaje shuleni? Pia, hawana wasaidizi wa kuwafikisha pale. Inachukua wiki haji shuleni, wiki anakuja, anasomaje huyu? Kwa nini hatuwapi nafasi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza bajeti yao hawa, walimu wapandishiwe mishahara ama posho lakini wale wanafunzi wapewe hivi vitu vya kusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa upande wa Wizara ya Michezo. Mimi nilibahatika kufika kule Ivory coast, lengo kubwa ni kwenda kuangalia miundombinu ili kuja kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko nyuma kwa asilimia karibu 80, wenzetu wamewekeza kwenye miundombinu hii. Sisi tunajiandaa kufanya hii AFCON 2027 lakini naona bado hatuko serious. Hatuko serious kabisa kwa sababu mpaka sasa hivi tunacho kiwanja kimoja tu ambacho tunakikarabati. Lakini viwanja viwili ambavyo tayari kule bajeti imetengwa havijaanza mpaka leo mwaka wa fedha unakwisha, sijui tuko serious kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nishauri juu ya yale ambayo nimeyaona kule. Wenzetu kule kwanza katika maandalizi yale wamejenga Kijiji cha Michezo ili kuepuka gharama za timu zile kuziweka kwenye mahoteli pamoja na Maafisa wale. Kwa hiyo kuna kijiji cha michezo maalum ambacho baada ya kumaliza michezo hii kitafanyiwa shughuli nyingine; pengine ni nyumba zitauzwa kwa watu binafsi ama kwa mashirika. Napendekeza ipatikane bajeti maalum kwa ajili ya kufanya miundombinu itumike kwa ajili ya kufanya mashindano yetu haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala hili la mapato, huu Mfuko wa Maendeleo ya Michezo tumekwenda kutenga five percent kwenye sport betting wakati hilo ilikuwa tupate sehemu zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nimalizie kwa sababu ni muhimu sana. Hii hata Mheshimiwa Rais anakuwa na ukakasi wa kutoa fedha huku kwa sababu fedha hizi zinakwenda kwenye miundombinu ya Serikali. Sheria zetu hazionyeshi kwamba tunapata vipi mapato, BMT hawa wanapata huku lakini ukija kwenye TFF hawapati. Kwa hiyo sheria hizi zote zingaliwe upya. TFF wachangie kule, michezo ile ya kukimbia wachangie kule na kila sehemu ili Mheshimiwa Rais awe na nguvu ya kutupa fedha. Tunamuona Mheshimiwa Rais ana nia ya dhati, ametoa bilioni 31 kwa kukarabati Uwanja wa Taifa na ninaamini atatoa nyingi zaidi ya hizo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii ya mpango. Kwa kuanzia, napenda niwapongeze Mawaziri wetu wote wawili kwa kazi nzuri ambayo wameifanya, kazi ambayo inakuja kuleta dira ya nchi yetu kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma vizuri hotuba zote mbili, nimeangalia sehemu za vipaumbele, kwa upande wa Wizara ya Fedha wameandika vipaumbele 12, Wizara ya Mipango wameandika vipaumbele nane, kidogo nilishituka, lakini nilipofanya uchunguzi wa kina nikaona vile vipaumbele vyote ni sawa. Huku wamechanganua, huku wameunganisha, lakini vyote ni sawa. Hii ni kuonesha kwamba Serikali iko katika single unit, yaani ni ya aina moja. Kwa hili, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utaanza sehemu ya biashara. Nimeona hapa wamesema kwamba katika mpango watasimamia One Stop Center. Kwanza napongeza. Hili jambo ni zuri ambalo linasababisha kufanya biashara vizuri na nchi ambazo zimetuzunguka. Hiki ni kilio cha Watanzania wengi, wanapofika kwenye mipaka yetu wanakwama sana na wakati mwingine wanatumia gharama kubwa kuweza kuvuka border nyingine, kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kuja na mpango huu. Napenda sana mpango huu usije ukakwama, tumalize mwaka huu na mwaka unaokuja tusizungumzie kabisa Mpango huu wa One Stop Center.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hili, nasisitiza Zanzibar nayo inahitaji kuwa na One Stop Center kwa sababu nayo ni border. Kwa hiyo, katika mpango huu nayo ije; Waziri akiwa ana-wind up, atuambie kwamba biashara kati ya Zanzibar na Tanzania Bara zimepewa kipaumbele gani? Kwa sababu gani nasema hivyo? Ni kwa sababu biashara inapotoka Zanzibar kuja Tanzania Bara, ama inapotoka Bara kwenda visiwani kunakuwa na stop nyingi. Kule kuna stop na huku kuna stop, kwa hiyo, hii One Stop Center, tunataka biashara inapoondoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ikifika kule iwe ni kulipa handling charge siyo jambo lingine, na vile vile ikija huku iwe ni kulipa handling charge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kasumba hapa inasemwa kwamba ushuru wa Zanzibar ni mdogo, jambo hili siyo kweli. Maana yake ushuru wa Zanzibar kweli uko chini, lakini ukiangalia gharama za Wazanzibar wanazolipa, ni zaidi ya ushuru unaotozwa Tanzania Bara. Nichukue mfano mmoja, freight charge kutoka nchi za nje, mfano kutoka Dubai kuja Zanzibar kontena moja ni dola 8,000 lakini kuja pale Dar es Salaam ni dola 2,600. Kwa hiyo, hii difference tu tayari inaleta gharama kubwa. Vile vile kutoa mzigo Zanzibar kuuleta Dar es Salaam kuna handling charge pia, kuna transport. Kwa hiyo, gharama ni za juu. Kumtoza mfanyabiashara differential tax, siyo halali. Jambo hili liondolewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumza, tumesema One Stop Center, hii ni kwa upande wa borders. Tunataka kujua, wakati Mheshimiwa Waziri unakuja ku-wind up hapa, Mheshimiwa Waziri wa Biashara, alisema kwamba leseni zote zitakuwa na mfumo wa aina moja. Maana yake, ukiomba leseni hii utakuwa umemaliza shughuli. Kwa hiyo, mara hii kwenye mpango tuje tuambiwe kwamba jambo hili limeanza katika mwaka unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la usafiri kwa upande wa nchi zetu hizi mbili, Zanzibar na Tanzania Bara. Usafiri siyo rafiki. Usafiri uliopo ni wa watu wenye uwezo. Wananchi hawana uwezo wa kulipa nauli ya shilingi 30,000 kwenda Zanzibar ama kurudi. Napenda hasa Serikali ichukue jukumu la kuleta public transport ambayo itakuja kuwa na gharama ya chini ili wananchi wetu hawa wasafiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano mmoja, Serikali haituambii hapa, lakini ndugu zetu wanaotoka Tanga kwenda Pemba ama wanaotoka Tanga kwenda Unguja pale, wengi sana wanakufa ndani ya Mitumbwi. Sasa Serikali hailioni hili? Naomba mpango huu utuelezee kupata public transport ili kuokoa maisha ya wananchi wetu. Tusiwe kila siku tunapuuzia jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye upatikanaji wa dola. Naipongeza Serikali kwa kutuambia kwamba wana dola za kutosha na benki zetu zinapata dola, lakini cha kushangaza wafanyabiashara wadogo wadogo hawapati hizo dola kule benki. Kwa hiyo, tunataka Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atueleze upatikanaji wa dola na wananchi watazipata vipi? Kwa sababu inawezekana benki zinafanya ulanguzi, sasa itueleze kwamba itafuatilia vipi? Pia kila mfanyabiashara au anayehitaji dola azipate vipi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mzuri, leo nilikuwa nahitaji dola mia tano kwa kumchangia jamaa yangu alikuwa anakwenda kupata matibabu, nimekosa. Mpaka nimekwenda kumuomba mtu ambaye anasafiri anipunguzie. Dola mia tano anakosa basi Benki? Basi hili naomba kama Serikali ilisimamie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumze suala la mkataba wa bandari ambao umezungumzwa hapa katika Mpango. Mkataba wa Bandari mimi binafsi naupongeza, ilikuwa ni mkataba mzuri na ninaipongeza TPA kwa kuingia huu mkataba wa utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa katika Mpango nimeona huu mkataba kutoka batch zero mpaka batch three, batch four mpaka batch seven. Naona kwamba, mkataba huu ni mzuri na unakuja kuleta tija. Mpango haujatueleza. Tuliambiwa hapa kwamba, kwa sasa bandari inakusanya asilimia 10 ya bajeti lakini tukishaingia mkataba huu tutakuja klukusanya asilimia 62. Sasa, Mpango utueleze, je, ni mwaka huu au mwaka unaokuja? Hili napenda kwenye mpango huu mje mtueleze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo ningependa kulichangia ni suala la Liganga na Mchuchuma. Suala hili ni suala ambalo tumeona Mheshimiwa Rais, kwanza tunapongeza sana kwa kuweza kulipa fidia kule kwa wenzetu ambako iko miradi hii. Hata hivyo, ningependa kujua sasa huu mpango umetaja jambo hili, tunakweda kwenye step gani? Kwa sababu tuliambiwa kuna Mkataba wa wale wenzetu wa kampuni ya kachina. Tunalipa hili ili kuwaokoa watanzania. Je, nataka kujua sasa status ya mkataba ule sasa utakuwa umekufa au tunakwenda kwenye mpango kwa kujisukuma ili baadaye tuje tushitakliwe ama tutakuwa kuwalipa share hawa wachina? Tunataka kujua katika Mpango huu tuje tuelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, nataka nimalizie suala la utawala bora. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind up hapa, aje aeleze huo utawala bora tunaoufuata ni wa aina gani? Kwa sababu bila utawala bora hata huo Mpango hautafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana, katika Jimbo langu, juzi watu wameshukiwa wanafanya Magendo ya Karafuu bila kukamatwa na bidhaa yoyote. Cha kushangaza wamekamatwa, wamepigwa mpaka mimi nikawajibika kwenda kuwaomba polisi kwenda kuwafanyia matibabu. Jambo hili haliwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana Wizara au Serikali itueleze kwa uyakini kwamba utawala bora umekaaje ili kusiwe kuna kunyanyasa wananchi. Nakushukuru.
The Finance Bill, 2022
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia hoja iliyopo mezani, Mmarekebisho ya Muswada wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2022.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanzia mchango wangu nitajielekeza kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato, Cap. 332. Hapa sheria ambayo inataka kubadilishwa inakuja kuleta kodi ya mfuto, kodi ambayo kwa upande wa Zanzibar na bara itakuwa ni sawa. Hii kodi pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakuwa ameshauriana na Waziri wa Fedha wa Zanzibar, lakini bado suala hili utekelezaji wake utakuwa ni mgumu na itawaletea shida kubwa sana Wazanzibar. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu hapa suala hili la mapato pia linakwenda kwenye mtambuka wa Wizara ya Biashara. Mikakati ya biashara ambayo ndiyo inapelekea mapato kwa pande zote mbili huwa ni suala la Wizara ya Biashara ambapo sasa Wizara ya Fedha kwa kutumia TRA wanakwenda kukusanya kodi.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa inavyoonekana ni kwamba kwa upande wa Zanzibar, sera za Zanzibar za biashara zinakuwa zipo tofauti, lakini hata hivyo wananchi wake asilimia kubwa sana wanakipato cha chini ukilinganisha uchumi wa Zanzibar na uchumi wa Tanzania Bara ni mbingu na ardhi, vitu hivi si sawa kabisa kwenda kuweka kodi sawasawa ni sawa na kuwasema Wazanzibar wawe katika hali duni zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka lifanyiwe uchunguzi suala hili kwamba hali ya maisha ya watu wa Zanzibar hasa wafanyabiashara ni ile kwamba hawana jinsi ya kufanya, lakini kwa kweli biashara wanafanya kwa kujilazimisha; mitaji hawana na asilimia kubwa ya wananchi wa Zanzibar wanategemea wale wafanyabiashara kidogo kuwasaidia ili kuendesha maisha yao. Kama si hivyo ningesema asilimia 80 ya Wazanzibar tungeingizwa kwenye mpango wa TASAF ili kusaidiwa kwenye kaya maskini. Sasa sheria hii naona ingefanyiwa mabadiliko viwango vikabakia kuwa tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili nakwenda kwenye Sura Na.438 kwamba Wizara ya Fedha ama TRA itatambua walipakodi waliosajaliwa Zanzibar sawa na walipakodi waliosajiriwa Tanzania bara. Suala hili pia ni sawa na lile ambalo limepita kwa sababu hii database ya TRA katika mfumo wa kupata TIN Zanzibar ipo kivyake na bara ipo kivyake. Hii inasaidia sana kwa maana ya kwamba sasa unapokwenda kuweka sasa ya aina moja maana yake ni nini? Itawafanya wafanyabiashara wale wa Zanzibar ambao kule kodi zake zinakuwa, kwa kweli kwanza uelewa wenyewe wa kutunza zile hesabu maana yake sisi kwa kweli kule kwetu biashara tunafanya kwa shida tu, hatufanyi kwa mitaji, hatufanyi kwa elimu, tunafanya kwa shida. Kwa maana hiyo, bado kwanza tunatakiwa sisi kama wafanyabiashara wa Zanzibar tubakie katika database yetu ile ile ya Zanzibar na database ya bara iwe vilevile na hakuna tatizo kwa sababu hata kwenye michango yetu ya bajeti hatukuchangia suala hili kwamba ni tatizo. Kwa maana hiyo mimi nashauri ibakie vilevile ili twende sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine pia katika sheria hii hii imesema kwamba ZRB itasaini makubaliano. Sasa haya makubaliano sasa mimi yananipa ukakasi kwasababu ZRB haina nafasi ya kufanya kazi Tanzania Bara, sasa makubaliano haya ndiyo yanatupa direction kwamba yanakwenda kuifanya TRA kule ifanye kazi zake lakini huku bara ZRB haina nafasi kabisa. Kwa maana hiyo bado nasema sura hii isiwe na mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea kwenye kifungu cha 32; kuzuia kodi ya mapato ya mlipakodi wa pango la nyumba. Hili suala limekuwa likifanyika na sijui ni kwa nini hii sheria imekuja au lilikuwa linafanyika bila sheria lakini ninachoweza kusema ni kwamba mwenye majengo anafahamika na mfanyabiashara anafahamika kwa maana hiyo mfanyabiashara alitakiwa aachwe kuwa na kodi yake inayomuhusu na yule mwenye kodi ya majengo yaani mwenye nyumba basi naye afuatwe kwa namna Serikali itakavyojua kuliko kumwongezea mzigo mfanyabiashara kwenda kulipa kule na mara nyingi wale wenye nyumba huwa hawataki kulipa ile capital gain tax ama ile kodi ya zuio. Kwa maana hiyo, nashauri kwamba bado kila mmoja aachiwe majukumu yake ya kulipa kodi.

Mheshimiwa Spika, pia nikija kwenye rufaa za kikodi kifungu cha 22 kimeelezea hivyo, kifungu hiki ni kifungu kandamizi, nakiita kifungu kandamizi kwa sababu hapa wanataka watoza kodi kusiwe na msuluhishi, maana yake mtoza kodi na mlipakodi wao kwa wao wamalizane. Sasa hakiwezekani kitu kama hiki, kwa maana ya kwamba huyu mlipa kodi kukiwa na fault yoyote hawezi kwenda popote kwenye chombo cha kisheria atamalizana na yule ambaye amemkosea. Sasa inakuwaje kwamba yule ambaye umemkosea, yeye ndiyo mkae pamoja na kusuluhisha hili haliwezekani, bado sheria hii nayo itakuwa haiwezekani kwa sababu bado sheria hata katiba inaruhusu chombo cha mwisho cha kutoa maamuzi ni mahakama, kwa maana hiyo bado iruhusu TRA kama kutakuwa na tatizo, basi mfanyabiashara anaweza kwenda mbele kutafuta haki yake.

Mheshimiwa Spika, mwisho nikimalizia ni katika Sura ya 394 kuhusu suala la Bima. Sura hii imeelezea kwamba kutoza Bima ya lazima kwa sehemu ya biashara, vivuko na mizigo inayotoka nje…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Spika, samahani, naomba nimalizie hii point.

Mheshimiwa Spika, ni kwamba mizigo inayotoka nje, tayari kule inakotoka ina insurance. Maana yake hata kodi zenu mnavyozifanya ni Cost Insurance and Freight (CIF). Sasa kwa nini leo unakuja kusema ikatiwe insurance hapa ya lazima? Ina maana itakuwa ni double insurance, ni kumwongezea mzigo mfanyabiashara. Nadhani suala hili pia halifai kwa sababu mzigo tayari umeshakuwa na insurance, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote wa Mwaka 2022
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi kuweza kuchangia katika Muswada huu, ambao kwa mimi binafsi naunga mkono kuletwa hapa Bungeni leo na kuweza kuujadili ili kwenda kumsaidia Mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Muswada huu kama walivyotangulia kusema wenzangu, ni Muswada ambao umekuja Bungeni mara nyingi lakini tukawa tunaurudisha kutokana na mapungufu mengi yaliyokuwepo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naipongeza Wizara pamoja na Kamati hii ya Afya na Masuala ya UKIMWI kwa kuweza kupitia Muswada huu vizuri na kuweza kuuleta sasa ukiwa walau una sura nzuri, ambao utakwenda kumkomboa mtanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nimefarijika sana kuja kwa Muswada huu kwa sababu sasa Watanzania watakwenda kupata huduma ya afya ambayo ni ya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kupongeza Muswada huu lakini mimi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Konde kuna mambo ningependa kushauri. Naona kuna baadhi ya sehemu hazijakaa sawa katika Muswada huu. Kwa mfano, katika ukurasa wa kumi pale namba 8(d) inayosema kwamba huduma za afya zitatolewa kulingana na michango; mimi ninaona suala hili la kusema kwamba zitatolewa kutokana na michango bado linaonekana kama kuna utofauti wa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba huduma hii ya afya inatakiwa iende kwa wananchi wote bila kuleta ubaguzi, kusiwe na kwamba mwenye kutoa mchango mkubwa ndiye atapata huduma hii na mchango mkubwa hivi. Huduma za afya tunajua kwamba kuna viwango tofauti, hii ni namna ya utoaji wa huduma lakini siyo zile huduma za afya zenyewe; huduma za afya zenyewe kwa magonjwa yote ziwe ni kwa yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, na huduma hii inapaswa kuwa siyo ya hiari, ni kwa wote, kwa sababu gani nasema hivyo? Ni kwa sababu, wananchi wote wanahitaji hii huduma. Sasa tukisema ni ya hiari itakuwa kwamba baadhi ya wananchi wanaweza kuamua wasiingie lakini wakakutana na hii shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napendekeza huduma hii ya kuingia kwenye bima ya afya iwe kwa wote na isiwe kwa hiari. Kwa nini nasema hivyo? Nasema kwa sababu ni jukumu la Serikali na Taifa kuweza kutoa huduma sahihi kwa wananchi wote kwa magonjwa yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kwa kweli nimeona hapa vyanzo vya kupata fedha kwa ajili ya kaya masikini. Kwa kweli, mimi bado haijaniingia vizuri, sijafahamu vizuri, naona kama jambo hili kweli wamejitahidi kufikiri lakini wamezungumza fedha ambazo zitasaidia kaya maskini ni zile zinazotokana na kodi ambazo zitatozwa kwenye vinywaji vikali, michezo ya kubahatisha (betting) n.k.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kwanza ni vya mapato vya nchi kwenye Bajeti yetu Kuu. sasa leo tunavipeleka moja kwa moja huku. Na tunapokuja na bajeti hapa huwa tunaona ndivyo vyanzo vya mapato. Kwa nini tunavipeleka kwenye mfuko huu? au tume-change gear sasa tunavipeleka moja kwa moja?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mapato haya hii ni njia moja ya kuwakataza watu wasifanye betting. Unapotoa kodi kubwa kwenye betting maana yake unazuia betting. Unapotoa kodi kubwa kwenye vinywaji vikali maana yake unazuia. Je watu wakiacha kunywa pombe kali, wakiacha kucheza hii michezo, fedha hizi za mfuko zitapatikana wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashauri Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iwe ni chanzo cha fedha hizi. Mimi nimefuatilia kwa makini suala hili, nachukulia mfano wenzetu nchi ya Uingereza, kule ni watu wote wanatibiwa kwa Mfuko wa Afya. Mwenye kazi na asiyekuwa na kazi lakini michango yao inakuja pale mwenye kipato officially kinakatwa moja kwa moja, yule ambaye hana michango, hana kipato, ambaye anapokea fedha za msaada wa Serikali yeye anatibiwa bure na anapata huduma zile zile za yule mtu aliyechangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nashauri bima hii iwe kwa wote, kwa lazima lakini vyanzo hivi viwe ni vya uhakika; ikiwemo kuingizwa katika bajeti kabisa bila kuangalia kwanza tunakwenda kupata vyanzo hivi vya michezo ya betting na nini. Hilo ni moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri hapa kabla ya kuja na huu Muswada aliwahi kusema kwamba Mfuko wetu wa Bima ya Afya, umechoka. Sasa leo hakuja kutueleza kwa nini sasa unakuja kupata msuli?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tulitakiwa tutafute kwanza tiba ya kwa nini huu mfuko ulichoka? Lakini hakuja kutueleza. Tuliangalia hapa Ripoti ya CAG ilisema kwamba fedha nyingi zimechukuliwa ndani ya mfuko huu kutokana na Hospitali za Binafsi. Fedha nyingi wamelipwa ambazo zimekuja kufanya mfuko huu kuwa dhaifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashauri Serikali isiogope kazi yake ichukue bima hii ya afya kwanza kufanya pilot kwenye Serikali yenyewe bila kuingiza kwenye private. Iende moja kwa moja kwa wananchi kwenye Shughuli za Serikali, halafu wakiona kwamba imefanikiwa ndipo viingie vituo vya private kwa sababu tunaogopa tunaweza kuja kukwama tena. Hili jambo ni zuri ni jambo jema, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kulileta kwa wananchi. Kwa kweli huo ni ushauri wangu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili.

MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.