Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mohammed Said Issa (8 total)

MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wigo wa biashara baina ya Zanzibar na Tanzania Bara ili kuongeza mapato?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ina Mipango na Mikakati mbalimbali ili kuendelea kupanua wigo wa Biashara baina ya Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo: -

(i) Kuendelea kutoa elimu na kuongeza hamasa zaidi kwa makampuni ya Tanzania Bara na Zanzibar kushiriki katika Maonesho mbalimbali yanayofanyika ndani ya Tanzania Bara na Zanzibar;

(ii) Kufanya tathmini na kubaini vizuizi visivyo vya kikodi;

(iii) Kuzishirikisha Mamlaka mbalimbali ikiwemo Mamlaka za Mapato za Tanzania Bara (TRA) na Zanzibar (ZRA) kwenye majadiliano ya pamoja ili kupanua wigo wa Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Upanuzi wa ushirikiano wa kibiashara unazingatia na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu zilizopo. Ninakushukuru.
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati wa Kituo cha Polisi cha Konde katika Wilaya ya Micheweni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Saidi Issa, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi cha Konde ambacho jengo lake lilijengwa wakati wa ukoloni. Tathmini kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho imefanyika na kubaini kwamba kiasi cha fedha Sh.42,000,000/= kinahitajika ili kugharamia ubadilishaji paa, kubadilisha mfumo wa umeme, maji safi na maji taka, kuziba nyufa, kubadilisha dari na kupaka rangi. Ukarabati huo utafanyika kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Serikali inawahamasisha wadau walio tayari kushirikiana na Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya katika kuboresha vituo vya Polisi vilivyo kwenye maeneo yao.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA K.n.y. MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha TBS na ZBS zinafanya kazi kwa ushirikiano?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Jimbo la Konde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Taasisi ya Viwango Zanzibar (ZBS) wana hati ya makubaliano (Memorandum of Understanding) iliyosainiwa Mei, 2015 kwa kipindi cha miaka mitano na pia imehuishwa tena mwaka 2020.

Mheshimiwa Spika, katika makubaliano haya yanajikita katika maeneo yafuatayo: -

(i) Uandaaji wa viwango vya Kitaifa;
(ii) Udhibiti wa ubora na usalama wa bidhaa;
(iii) Huduma za metrolojia na upimaji;
(iv) Mafunzo ya kitaalam kwa maafisa wa ZBS; na
(v) Kutambua bidhaa zilizothibitishwa ubora baina ya mashirika haya mawili.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE.OMAR ALI OMAR K.n.y. MHE. MOHAMMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, ni vigezo gani Serikali inavitumia kusamehe kodi ya VAT kwa viwanda mbalimbali nchini ili kuleta usawa kwa wote?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Said Issa, Mbunge wa Konde kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu wa Msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani umewekwa kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148. Sheria imeelezea kwa kina vigezo vinavyotumika kutoa misamaha ya Kodi ya VAT. Vigezo vinavyotumika kusamehe VAT kwa sekta ya viwanda ni kama ifuatavyo: -

i. Uagizaji wa malighafi zinazotumika kutengenezea vyandarua;

ii. Uagizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa Serikali zitakazotumika kwenye miradi inayotekelezwa kwa fedha za Serikali, mikopo na misaada kutoka kwa Washirika wa Maendeleo;

iii. Uagizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa ajili ya unafuu wa majanga ya asili; na

iv. Uagizaji au usambazaji wa bidhaa au huduma kwa kampuni yenye makubaliano na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ahsante.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA K.n.y. MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani wa kuondoa tofauti ya Viwango vya Ufaulu kwa Mitihani ya Kidato cha Nne na Sita Kati ya Bara na Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Konde kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi wa jumla wa matokeo ya mitihani ya Kidato cha Nne na Sita uliofanywa na Baraza la Mitihani la Tanzania katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2022 ulibainisha kuwa Zanzibar ilikuwa na ufaulu wa juu zaidi kwa kidato cha nne na sita kuliko Tanzania Bara katika mwaka 2013, 2015 na 2016. Aidha, Tanzania Bara ilikuwa na ufaulu wa juu zaidi ya Zanzibar kwa mwaka 2014 na mwaka 2017 hadi 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi na uendeshaji wa elimu ya msingi (awali, msingi na sekondari) siyo suala la Muungano, ingawa kwa Kidato cha Nne na cha Sita wote wanafanya mtihani mmoja wa Baraza la Mitihani la Tanzania. Kwa msingi huo, kila upande wa Muungano una mikakati yake ya namna ya kuongeza kiwango cha ufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea na mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mitaala ya Elimu. Zoezi hili linafanyika kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunakuwa na Sera na Mitaala inayolenga kutoa ujuzi zaidi kwa wahitimu na pia tunaoanisha kwa kiwango kikubwa elimu inayotolewa Tanzania Bara na ile inakayotolewa Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliauliza: -

Je, hesabu zinazowasilishwa na CAG kila mwaka ni za mashaka au uhakika?
WAZIRI WA FEDHA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohammed Said Issa, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hesabu zinazowasilishwa na Maafisa Masuuli kwa CAG kila mwaka ni za uhakika kwa kuwa zinaandaliwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 30(2) cha Sheria ya Fedha za Umma, Sura 348, Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS), miongozo mbalimbali inayotolewa na Wizara ya Fedha na mifumo madhubuti ya kielektroniki ya usimamizi wa fedha ikijumuisha Mfumo wa Uhasibu Serikalini (MUSE).

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita (2019/2020 – 2021/2022), taarifa ya CAG imeonesha ongezeko la hati zinazoridhisha kutoka asilimia 92 mpaka 96 kwa Serikali Kuu, asilimia 70 mpaka 94 kwa Serikali za Mitaa na kupungua kutoka asilimia 97 mpaka 98 kwa Mashirika na Taasisi nyingine za Umma.
MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza kuhamasisha kilimo cha zao la Mwani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Said Issa, Mbunge wa Jimbo la Konde, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilishaanza kuhamasisha na kutoa elimu kuhusu zao la mwani na tayari jumla ya wakulima 4,569 wamepatiwa mafunzo ya uzalishaji, uhifadhi na kuongeza thamani katika zao la mwani. Ahsante sana.

MHE. MOHAMED SAID ISSA aliuliza:-

Je, Serikali inaisaidiaje Zanzibar kupata faida ambazo TFF inazipata katika kuendeleza soka la Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia TFF imeendelea kuhakikisha kuwa Zanzibar inanufaika na fedha za misaada kutoka FIFA ambapo hadi sasa miradi kadhaa ya kuendeleza soka imetekelezwa ikiwa ni pamoja na kusaidia timu za Taifa, mashindano ya ndani, mawasiliano na mafunzo kwa wadau wa michezo. Hata hivyo, Serikali inatambua changamoto zilizopo baina ya TFF na ZFF katika uendeshaji soka katika Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua changamoto hizi, Wizara yetu pamoja na Wizara ya Michezo na Vijana Zanzibar zimeitisha kikao maalumu baina ya ZFF na TFF kwa lengo la kutatua changamoto hizo.