Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Dr. Stergomena Lawrence Tax (5 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2022
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nashukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia hoja iliyo mbele yetu, nianze kwa kuzipongeza Kamati zote kwa taarifa nzuri walizowasilisha. Pia kipekee naomba nimpongeze Mheshimiwa Vita Kawawa, Mwenyekiti wa Kamati ya NUU na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa ushirikiano mkubwa wanaotupatia, ushauri wanaotupatia ambao unatuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea michango mingi kutoka kwenye Kamati na Wajumbe mbalimbali waliochangia. Naomba niwashukuru na niwahakikishie kwamba michango hii yote ni muhimu na tutaifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa umuhimu wa mambo yaliyojadiliwa na kwa uchache wa muda, nitajaribu kuongea machache na kwa ufupi sana. Mtanisamehe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu, napenda niweze kuongelea mengi kadiri nitakavyoweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo kubwa mojawapo lililoongelewa kwa umuhimu na kuchangiwa na watu wengi ni kuhusu diplomasia ya uchumi, kufunganishwa na uchumi, ushirikishwaji wa sekta, limekwenda mpaka Halmashauri na kupanua uelewa wa diplomasia ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kusema kwamba diplomasia ya uchumi ni kitu muhimu sana na imekuwa na mafanikio makubwa sana kibiashara, kiuwekezaji, kiutalii na hata miradi. Pengine Waheshimiwa Wabunge hamfahamu kwamba baadhi ya miradi mikubwa mnayoona ikitekelezwa hapa nchini imeibuliwa na Balozi zetu ikiwa ni sehmu ya utekelezaji wa diplomasia ya uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kipindi hiki au katika awamu hii ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, diplomasia ya uchumi imeshika kasi kubwa sana. Tumemwona yeye mwenyewe akitangaza fursa mbalimbali katika mataifa mbalimbali, tumemwona jinsi ambavyo amekuwa akitangaza utalii, tumemwona ambavyo amevutia wawekezaji mbalimbali, na hii yote imechangia katika kukuza diplomasia ya uchumi. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, diplomasia ya uchumi imekuwa na mafanikio makubwa, lakini hata hivyo siyo kwamba, hakuna changamoto. Tumefanya tathmini kama Wizara na kubaini kwamba zipo changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na masuala ambayo yameainishwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muktadha huo, tunaandaa Mpango wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutekeleza Diplomasia ya Uchumi. Madhumuni ni kuhakikisha kwamba tunaibua maeneo ya kimkakati, tunaainisha watekelezaji wote ikiwa ni pamoja na sekta binafsi na tunapanga utaratibu wa kutekeleza ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya umma kama ilivyoelezewa na kuwaleta wadau wote pamoja. Kama nilivyosema, matarajio yetu ni kwamba, tutakamilisha kazi hii mwezi Desemba mwaka huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na mchango kwamba pengine tuangalie kuajiri kutoka sekta binafsi. Katika kuandaa mkakati huu, tutaona kama kuna haja ya kuajiri au tunaweza kuishirikisha sekta binafsi kwa utaratibu mwingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, katika Taarifa ya Kamati, aya ya 3.2.1, sijui ni ibara au section (b) na (c), Kamati ilipendekeza tuandae mikakati miwili na mpango mmoja; Mkakati wa kuainisha fursa za kiuchumi, mkakati wa utekelezaji wa diplomasia ya uchumi, na mpango wa ushirikishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa ninaomba tuandae mkakati mmoja ambao tunaendelea kuuandaa na utajumuisha yote haya. Hii itakuwa na ufanisi zaidi. Kwa muktadha huo, naomba azimio hilo lisomeke namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nitapenda kuliongelea ni uratibu maalum wa kuwaandikisha diaspora. Hili ni jambo kubwa, na ni kweli, kama ilivyosemwa, limesimamiwa sana na Mheshimiwa Rais. Napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, siyo kweli kwamba hatuyajali maagizo ya Mheshimiwa Rais, la hasha, tunafanya kazi kubwa na tumefika pazuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaanza kuandaa mfumo wa kidijitali ambao mpaka sasa hivi umefika mbali na tunatarajia kufika mwezi Juni mwaka huu utakuwa umekamilika. Mpaka sasahivi prototype iko tayari, tumeshaandaa design na kilichobaki sasa ni kukamilisha mfumo huu. Kwa hiyo, hili limekwishakamilika, ni muda mchache tu mtaweza kuona matokeo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine muhimu ambacho kilijitokeza katika mazungumzo, mijadala au michango ni hadhi maalum kwa diaspora. Hapa ndipo tulipoambiwa tunamkwamisha Mheshimiwa Rais. La hasha, hatumkwamishi, na hatuwezi kufanya hivyo. Sisi ni jeshi lake, tuko nyuma yake, tunafanya kazi kuhakikisha yale yote aliyotuagiza kuyafanya, tunayatekeleza kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefika mbali sana. Mpaka sasa hivi tulishakusanya maoni ya wadau, tulishakusanya mapendekezo kutoka diaspora, tumeshayachambua, tumeshashirikisha wadau wote na tumeshaainisha maeneo ambayo tuna imani kwamba yanakwenda na matarajio na matakwa ya diaspora ambayo sasa mfumo umeshawekwa na utaratibu umeandaliwa, lakini kilichobaki sasa hivi tunapeleka kwenye Baraza la Mawaziri. Kitakachofuata baada ya hapo, kwa sababu yapo maeneo ya kisheria ambayo yatatakiwa kufanyiwa kazi, kwa hiyo, baada ya Baraza kupitisha waraka huu, tutaendelea na mabadiliko ya sheria ili hadhi hii maalum iweze kufanyiwa kazi. Tumefika mbali sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwa ruhusa yako, ni uendelezaji wa balozi na vitega uchumi, limeongelewa sana na ninawashukuru sana kwa kuliongelea hili. Hili ni jambo kubwa sana na ni kweli kabisa kwamba taswira ya nchi yetu inaonekana pia kupitia balozi zetu tulizonazo nchi mbalimbali, lakini ni suala kubwa linalohitaji rasilimali nyingi. Mjumbe mmoja ameeleza kwamba, kati ya majengo 110, majengo 67 yanahitaji aidha kujengwa upya, kukarabatiwa au kubomolewa kabisa na kujengwa upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua kwamba hatuwezi kufanya kazi hii peke yetu, na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tunafanya kazi hii kwa kushirikiana na sekta binafsi. Tayari nimeshaunda Kamati ya Kitaasisi inayojumuisha sekta binafsi na sisi wenyewe. Kwanza kuainisha nini tunaweza kufanya kwa haraka? Mahitaji tunayoyahitaji sasa hivi ni nini? Wizara ya Fedha inaweza ikatenga kiasi gani? Tuko katika mchakato wa bajeti ili iweze kuingia katika bajeti inayofuata, lakini sekta binafsi na yenyewe inaweza ikashiriki namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la sheria ambalo pia lilikuwa linatusumbua, lakini sasa hivi tayari PPP inafanyiwa maboresho na tuna imani kwamba sekta binafsi itaweza kushirikiana nasi na mtaona matokeo baada ya muda siyo mrefu. Ni kazi kubwa kwa sababu inahitaji uandae concept note, uwe na feasibility study, uwe na design; yote haya yanaandaliwa na Kamati ili hata pale tukapopata fedha tuweze sasa kwenda na kuanza kutekeleza kazi hii. Hata ukipata fedha sasa hivi Waheshimiwa Wabunge unaweza usifanye kazi hii kama haya maandalizi hayajawa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kama utaniruhusu, ni suala la kujitoa katika COMESA. Naomba tu kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, hatujapata hasara yoyote. Sisi tulikuwa wanachama wa jumuiya tatu, na tukiwa pekee wanachama wa jumuiya tatu. Tumebaki tukiwa Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC. Baada ya kuwa tumejitoa, tuliona kwamba hatuwezi kuwapoteza wale wachache ambao hatukonao ambao walibaki katika COMESA na nchi zote zilikuwa zikihangaika wakati huo, kwamba tuko katika configurations nyingi. Inatusumbua, tunalipa michango mingi, lakini pia kuna obligations ambazo zinapandana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukakubaliana kuanzisha utatu unaoleta pamoja COMESA, EAC na SADC na tunashirikiana katika mihimili yote mitatu; uendelezaji wa viwanda, uendelezaji wa miundombinu, na pia uendelezaji wa masoko na biashara. Pia ipo miradi ambayo tunatekeleza pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2016 ulizinduliwa ukanda huru wa biashara (FTA), kilichobaki sasa hivi ni kufanya ratification. Katika hii tripartite inatuwezesha sasa kufanya biashara kwa pamoja kama ambavyo tungefanya na COMESA peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ilikuja hoja kwamba, tunapoteza biashara kubwa na DRC. Kuna utoafauti kati ya ushirikiano wa kikanda na ushirikiano wa nchi na nchi. Vinapotokea vikwazo ambavyo ni baina ya nchi na nchi tunavitatua baina ya nchi na nchi. Tumeendelea kutatua vikwazo mbalimbali kama ilivyoelezewa kati ya Kenya na Tanzania na hata kati ya DRC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuthibitisha kwamba hatujapoteza biashara katika DRC, biashara hii imeendelea kukua mwaka hadi mwaka. Katika mwaka 2012 biashara yetu ilikuwa ni Shilingi bilioni 50.2 lakini miaka minane baadaye kufikia mwaka 2020 biashara yetu ilikua kufikia Shilingi bilioni 334 kutoka Shilingi bilioni 50. Kwa hiyo, biashara inaendelea na hatujapoteza kitu chochote na urari wetu kati ya DRC na Tanzania ni chanya. Hivyo hakuna tulichopoteza, bali tumenedelea kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua umenivumilia, umeniongezea muda. Nakushukuru sana, naomba niishie hapo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda nikushukuru kwa mara nyingine tena kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa ufafanuzi na kufanya majumuisho ya mjadala ambao umeendelea asubuhi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kukupongeza kwa kuongoza na kusimamia mjadala wa bajeti yetu kwa umakini na umahiri mkubwa. Aidha, naishukuru Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa ushauri na miongozo waliyotupa kufuatia hotuba niliyoiwasilisha. Nawashukuru sana pia Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu mizuri sana. Tumeipokea michango yote na yotwe tutaifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niwashukuru sana, sana kwa pongezi mahususi mlizozitoa kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya na yenye tija katika kuimarisha Uhusiano wa Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi na ambazo mmezitoa kwetu sisi wasaidizi wake. Napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu na Waheshimiwa Wabunge kuwa sisi wasaidizi wake katika Wizara tutaendelea kumsaidia ipasavyo na kutekeleza majukumu yetu kwa uaminifu, uadilifu na umahiri kadri ya uwezo wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwatambue na kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja niliyoitoa leo asubuhi na tumepokea maoni na ushauri na hoja kutoka kwa wajumbe 13 ambao wamechangia wote kwa kauli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya hoja hizo ambazo Waheshimiwa Wabunge na pia Kamati imezitoa zimejibiwa kwa ufasaha na Mheshimiwa Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk na kutokana na ufinyu wa muda, nitajitahidi kujibu baadhi ya hoja lakini tu niwahakikishie kwamba hoja zote zitajibiwa kwa maandishi. Wamechangia Waheshimiwa Wabunge 13 ikiwa ni pamoja na Kamati, lakini michango imekuwa mingi sana na mizuri, tunawashukuru, tutaijibu yote kimaandishi. Kwa hiyo, naomba sasa nijielekeze katika kutoa ufafanuzi katika baadhi ya hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja ya Mheshimiwa Kingu ambaye amesisitiza kwamba tuhakikishe tunaishirikisha Zanzibar kikamilifu. Naomba nikuhakikishie kwamba hili linafanyika na huu ndiyo msisitizo ambao tumepata muda wote kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wanaokumbuka wakati nikiapishwa, alisisitiza vitu vitatu na kimoja kilikuwa ni kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua pande zote mbili za Muungano. Kwa hiyo, sio mimi tu, Wizara kwa ujumla hili tunalifahamu na tunalitekeleza asilimia 100 ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika maeneo mbalimbali. Katika misafara yote tunahakikisha tunajumulisha pande zote mbili za Muungano, katika majadiliano yote tunahakikisha tunafanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimetoa ufafanuzi kwenye hoja hiyo hoja, nyingine ambayo imejadiliwa kwa hisia na kwa msisitizo mkubwa ni kuhusu utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi. Hii imeongelewa na Kamati na Waheshimiwa Wabunge wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Diplomasia ya Uchumi, nianze kusema tu kwamba ni kitu mtambuka. Watekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi ni sekta zote na ni katika Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Kwa hiyo, mpaka sasa mafanikio yamekuwepo makubwa kama nilivyosema kwenye hotuba yangu katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi. Pia tumebaini kama mlivyosema wenyewe kwamba uelewa kuhusu Diplomasia ya Uchumi bado ni mdogo. Tunakiri hilo. Kwa kulitambua hilo na kwa msisitizo mkubwa ambao umewekwa na Kamati yetu ya Bunge ya NUU, tumeanza maandalizi ya kutekeleza mpango mkakati wa utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi. Mpango huu utatoa tafsiri, nini Diplomasia ya Uchumi? Mpango huu utaainisha wadau wote katika utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema wadau wote ni katika sekta zote; Sekta ya Umma, Sekta Binafsi, lakini katika Sekta ya Umma ninatambua kwamba tunakwenda mpaka chini. Tunakwenda mpaka TAMISEMI, tunaihusisha mikoa na Wilaya, na utaainisha majukumu na pia tutaweka mpango wa ufuatiliaji kujua inatekelezwa namna gani? Kwa sababu kulikuwa na hoja, kwamba tuwawekee malengo Balozi zetu. Wao pia watakuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Diplomasia ya Uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuunge mkono tukamilishe kazi hii ambayo tumejipangia kuikamilisha mwishoni mwa mwaka huu kama ambavyo pia Kamati imesema tukamilishe mwisho wa mwaka wa fedha ujao, lakini sisi lengo letu ni kukamilisha kufikia Desemba mwaka huu 2023. Kwa hiyo, baada ya kuwa tumekamilisha hili, basi tutaweka bayana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba pia ieleweke kwamba sisi kama Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kazi yetu ni kuratibu, watekelezaji ni sekta zote. Nimesikia hoja kwamba tuweke dirisha Wizarani la kufuatilia utekelezaji. Tukishamaliza mpango huu, tutajua kila mmoja anajukumu gani na mmoja atatakiwa kutekeleza mahali pake. Kwa hiyo, sisi kama Wizara, kazi yetu itakuwa ni kufuatilia tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linakwenda pamoja na hoja kwamba tuweke wataalamu mahususi kwenye maeneo muhimu katika Balozi zetu. Tutaweza kulifanya hilo baada ya ya kukamilisha huu mkakati. Kwa sababu mkakati huu pia unalenga kujua katika nchi mbalimbali tunalenga nini? Tukishajua tunalenga nini kule, tutajua pia tunaweka wataalamu wa aina gani? Kwa hiyo, tuvute Subira, tutaendelea kufanya hivyo, lakini siyo kwamba hatupeleki wataalamu, tunapeleka wataalamu hata sasa ambao ni wataalam mahususi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imeongelewa kwa mkazo ni kuhusu Sera ya Mambo ya Nje kuikamilisha. Hili naomba tu niwahakikishie kwa kujiamini kabisa kwamba sera hii tunaikamilisha ndani ya mwaka huu wa fedha. Tuko mbali sana, tunajua umuhimu wake, Kamati imetusukuma kweli kweli na sisi tumesukumika, kwa hiyo, tunaahidi kwamba sera hii sasa itakuwa tayari. Imechukua muda kidogo kwa sababu mwanzo tulidhani kwamba tunaandaa sera mpya, lakini kadri tulivyoendelea tukabaini kwamba hatuna haja ya sera mpya. Iliyopo misingi yake inakidhi, tunachotakiwa sasa ni kuweka maeneo mapya ambayo yanapungua kama nilivyoyaainisha kwenye hotuba yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imejitokeza kwa sana ni suala la Hadhi Maalum na Uraia Pacha. Nashukuru wachangiaji na nimefurahi kwamba alichokisema Mheshimiwa Prof. Kabudi kimejitokeza hata kwenye mijadala yetu kwamba bado hili suala halijawa na muafaka wa pamoja, siyo nchini kwetu tu, lakini hata nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais kwa kutambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba Diaspora ambao wapo nje ya nchi ambao ni raia na wale wenye asili, tuna definitions mbili za Diaspora kama zilivyotolewa, wote wanapata haki, kwa hiyo, akatoa msisitizo kwamba tufanye mchakato wa kutoa Hadhi Maalum. Pamoja na kwamba Katiba yetu inasema nini, lakini msingi ni kuhakikisha kwamba wote wanapata fursa tunazoweza kuziandaa katika Hadhi Maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi nyingine, Mheshimiwa Prof. Kabudi ametoa takwimu kama ni nchi 49 tu zinazotoa Uraia Pacha. Sasa ukitoa Uraia Pacha kwa sasa hivi wakati hakujawa na muafaka kitaifa na kidunia, kuna wale watakaokosa fursa, kwa sababu kwenye nchi ambazo Diaspora zipo na zile nchi hazitambui Uraia Pacha, sisi tukitoa Uraia Pacha, wale hawatapata fursa ambazo tunatarajia kuzitoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuweza kutoa fursa kwa wote, Mheshimiwa Rais kwa busara yake akahimiza kwamba tutoe hii Hadhi Maalum, tena kwa haraka. Huu mchakato Waheshimiwa Wabunge umefika mbali sana, kufikia mwisho wa mwaka huu hii Hadhi Maalum itakuwa imetolewa. Inatoa fursa nyingi tu. Walileta mapendekezo kumi, mapendekezo yote hayo tumeyazingatia na yote yataingizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mchango wa Mheshimiwa Prof. Kitila, bahati mbaya katika yale mapendekezo hakukuwa na pendekezo la Haki ya Kimungu. Kwa hiyo, tutaenda kuliangalia hilo pendekezo la Haki ya Kimungu linaingia namna gani, lakini siyo miongoni mwa mapendekezo yaliyoletwa na Diaspora. Diaspora wanachotaka ni kuweza kuingia nchini, kumiliki ardhi, kupata huduma kwenye taasisi za fedha na kadhalika na yote hayo yamezingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kabla sijamalizia hoja hii, napenda sana kuzishukuru Taasisi zinazotusaidia. Tumepongezwa hapa kuhusu mfumo wa kuandikisha Diaspora wetu kidigitali. Tumefanya kazi hii na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na CRDB, NMB na NSSF. wanafanya hivyo kwa uzalendo wao, lakini kwa kujua kwamba na wenyewe ni wanufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fursa tunazoziongelea ni pamoja na huduma mbalimbali. Kwa hiyo, diaspora anapojiandikisha katika mfumo huu, watapata fursa za kiuchumi na kijamii, watapata fursa za ajira na pia watapata fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na hata Uhamiaji. Kwa hiyo, nihamasishe diaspora wetu waweze kujiandikisha na kutumia huu mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine iliyoongelewa ni suala la majengo kwamba Balozi zetu ziko katika hali mbaya. Ni kweli lakini hapa suala wala siyo kukosekana kwa fedha kutoka Hazina. Maana yake nisije nikarudi Hazina Mheshimiwa Mwigulu akaninyima pesa, akasema wewe umeenda kusema pesa hazitoki wakati na upungufu pia uko kwako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumebaini kwamba tulikuwa hatuko tayari. Ndiyo maana Kamati imesisitiza kwamba tuhakikishe taratibu zinakamilika mapema na maombi ya pesa yanapelekwa mapema. Hilo niwahakikishie Kamati tutalifanya, lakini pesa ya Serikali haitoshi. Ndiyo maana tumeandaa huu mpango ambao nimeueleza katika hotuba yangu kwamba tuna mpango wa kushirikisha sekta binafsi. Tumeshaainisha miradi yote ya kipaumbele, tumeshaainisha changamoto zote, tumeshaainisha mfumo tutakaotumia na tumeshaainisha jinsi ya kutatua hizo changamoto. Habari njema ni kwamba tayari miradi miwili tumeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hatua kubwa sana kwamba NSSF wanashirikiana na sisi katika kujenga kitega uchumi chetu na Ubalozi wetu Nairobi, na sasa tuko katika hatua za mwisho pia waanze kufanya Kinshasa, lakini wapo hata na wabia waliotoka nje ya nchi ambao tuko katika mazungumzo nao. Kwa hiyo, tuna imani kwamba hili sasa linaenda kufanyika. Naomba tu mtuunge mkono na mtutafutie hao wabia ambao wako tayari kuja kufanya kazi na sisi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona muda wangu umeisha. Kulikuwa na hoja ya kutotumia fursa zitokanazo na ushirikiano wa kikanda, tunalipokea tunalifanyia kazi na tumeendelea kulifanyia kazi. Misaada ya asasi kutoka sekta zisizo za kiserikali tuiangalie, tumeipokea; ajira nchi za nje, Mheshimiwa Naibu Waziri amelitolea maelezo; ajira katika Mashirika ya Kimataifa, tunafanya kazi, siyo kwamba halifanyiwi kazi, ila labda tuongeze juhudi, kwa sababu hapa kuna changamoto za ndani, za nje na kuna za uelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Neema kwa kusisitiza kwamba yako maeneo ambayo hata kama tunatoa Hadhi Maalum na Uraia Pacha ni maeneo mabayo lazima kama nchi tuyalinde. Nakushukuru sana kwa msisitizo huo. Chuo cha Diplomasia tumepokea. Kuhusu vikwazo kwa wafanyabiashara, kweli ni tatizo na tunavifanyia kazi. Hapa kulikuwa na tatizo kubwa ambapo wafanyabiashara wetu walikuwa wamenyimwa vibali ili watoe mahindi Zambia ambalo limechukua muda mrefu, lakini napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba sasa suala hili limetatuliwa na wafanyabiashara hawa wamepewa vibali siku ya leo. Kwa hiyo, tutaendelea. Haziwezi kwisha. Katika ushirikiano wa kimataifa na kikanda, vikwazo vinakuwepo. Kinachotakiwa ni kwamba muda wote kuwa macho na kushirikiana na wale wenzenu na kuhakikisha kwamba vikwazo hivyo vinatatuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuhitimisha, naomba niseme kwamba baadhi ya mambo ambayo yamesisitizwa hapa ni mambo ambayo yanafanyiwa kazi katika Kamati iliyoundwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, baada ya kuwa ameshazibaini changamoto mbalimbali zinazoikwaza Wizara yetu. Kamati hii isichukuliwe kwamba inapima utendaji wa Wizara kama utendaji wa Wizara kwa maana ya watumishi, inaangalia picha kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi haya mliyosema ya Diplomasia ya Uchumi, mambo mliyosema kwamba ni aina gani ya watumishi tuwe nao, mambo gani tujipange, tunajipanga namna gani, dunia ya sasa inakwenda namna gani? Twende namna gani? yote yataangaliwa katika kazi inayofanywa na hii Kamati. Kwa hiyo, ni matumaini yangu kwamba Kamati hii itakapomaliza kazi yake, basi tutakuwa tumepata suluhu ya mambo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nitoe hoja. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, muda mchache uliopita niliwasilisha katika Bunge lako tukufu hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu makadirio na mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2022/2023. Napenda kukushukuru kwa namna ulivyosimamia na kuongoza kwa umakini mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. (Makofi).

Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa kuzungumza, sina uhakika kama waliopo wamechangia kwa maandishi, lakini kama wapo hoja tutazipokea na tutazifanyia kazi, kwa hoja nzuri zitakazochangia katika kuimarisha utendaji na ufanisi wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie kuwa maoni na ushauri wenu tumeuchukua na tutaufanyia kazi ili kuendelea kuboresha utendaji wa Wizara yetu na kutatua changamoto ambazo mmeziainisha. Wizara inatambua na kuthamini michango iliyotolewa ambayo imetolewa kwa nia njema iliyotawala mjadala na msingi wake ni kuboresha shughuli za utendaji wa Wizara.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Vincent Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini na Wajumbe wote wa Kamati kwa maoni na ushauri waliotupatia. Ushauri tumeupokea tumeuzingatia, iliwasilishwa kwa muhtasari, lakini tumekwishaipata hiyo hotuba, kwa hiyo, tutafanyia kazi yale yote yaliyomo kwenye maoni mliyoyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upekee napenda niwapongeze watendaji wote wa Wizara na taasisi zake wakiongozwa na Katibu Mkuu, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe, kwa upande wa Wizara na Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kwa upande wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa weledi na kujituma na kuwezesha kufikia hatua hii ambapo tunaelekea kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara yetu. (Makofi)

Naomba kuwatambua Waheshimiwa Wabunge waliochangia hotuba ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa ujumla wao ambao katika mjadala wa asubuhi hii Waheshimiwa Wabunge 16 wameweza kuchangia. Asanteni sana Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na ufinyu wa muda napenda kuwahakikishia kuwa maelezo na majibu ya kina kuhusu hoja zote na michango yote iliyotolewa yataandaliwa kwa maandishi na kila hoja itajibiwa na tutawasilisha Ofisi ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi naomba nitoe ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge wakati wakichangia hotuba niliyoiwasilisha leo. Naomba nijikite katika hoja chache, kama nitaweza nitajibu zote ambazo kwa sehemu kubwa zimetawala mjadala wa hotuba ya Wizara yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze tu kwa kusema kwamba Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwake hapo tarehe 01 Septemba, 1964 limeendelea kukua na kuimarika kizana, kinyenzo, kiteknolojia na kiweledi kulingana na mahitaji ya wakati. Hali hii imeliwezesaha jeshi letu kutekeleza majukumu yake kwa umahiri mkubwa na kuiwezesha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendelea kuwa na amani na usalama hata pale ambapo pamekuwa na matishio, matishio hayo yamedhibitiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Spika, nalijibu hili kutokana na msisitizo mkubwa ambao mmeutoa Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati kwamba Jeshi letu na taasisi zake halina budi kuongezewa nyenzo, halina budi kuongezewa rasilimali fedha na niwahakikishie tu kwamba hii imekuwa ni dhamira ya Serikali na Serikali imeendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, pongezi nyingi zimetolewa kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Awamu ya Sita na Amiri Jeshi Mkuu, na ni kweli ametoa uzito mkubwa sana kuhakikisha kwamba Jeshi letu linawezeshwa na taasisi zote. Kwa hiyo, pongezi zote ambazo mmezitoa mafanikio yote ambayo yametolewa naomba pongezi hizo ziende kwa Amiri Jeshi wetu Mkuu ambaye ametoa uzito stahiki, Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu hoja iliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama na Waheshimiwa Wabunge wamechangia pia kuitaka Wizara kuhakikisha kuwa miundombinu ya kiulinzi mipaka kwenye Kamati wamesema pia mpaka katika mwambao wa bahari inaimarishwa napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tangu kuanzishwa kwake limeendelea kuwezeshwa kivifaa kama nilivyosema kizana na kiteknolojia kulingana na mabadiliko yanayotokana duniani. Ni dhamira ya Serikali kuendelea kuliwezesha Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania ipasavyo. Aidha, Wizara imeupokea ushauri huu muhimu na Serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika eneo hili mahsusi kwa ulinzi wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa maelezo mafupi kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Sera ya Ulinzi wa Taifa, hili pia limezungumzwa kwa nguvu sana na Mheshimiwa Saada nadhani naomba tu nitoe maelezo kwamba mchakato wa Sera ya Ulinzi wa Taifa ulianza mwaka 2008 ni kweli kama mlivyosema Waheshimiwa Wabunge kwamba mchakato huu ulianza muda mrefu sana. Hata hivyo sera hii ilichelewa kupata maoni kutoka kwa baadhi ya wadau muhimu, baada ya kupata maoni toka pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hii ilikuwa ni mwaka 2021 baada ya kupokea maoni hayo ilibainika pia kuwa yamekuwwepo maendeleo ya kitaifa na kimataifa katika sekta ya ulinzi yanayohitaji kuzingatiwa.

Mheshimiwa Spik,a mwaka 2008 na mwaka 2021 ni muda mrefu sana kwa hiyo ilibidi kuirejea hii sera upya. Kwa hiyo kazi hii imekwishafanyika na rasimu iko tayari kwa hiyo sasa hivi kinachoendelea ni kuhakikisha tunakamilisha sera hii na kwa umuhimu wake sera hii inakamilishwa kwa pamoja na Mkakati wa Usalama wa Taifa na Mkakati wa ulinzi wa Taifa letu. Kwa hiyo mpango tulionao tunatarajia kwamba katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 Sera hii itaweza kuwa imekamilika Wizara imetoa kipaumbele kikubwa sana kwa sera hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia kutoa ufafanuzi kuhusu umuhimu wa kuliwezesha Jeshi ikiwa ni pamoja na taasisi zake ikiwemo NYUMBU na ikiwemo Shirika la MZINGA kirasilimali fedha na watu. Kama ilivyo kwa taasisi nyingine Jeshi na taasisi zake zinahitaji rasilimali fedha na zinahitaji rasilimali watu ili kuweza kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuilinda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mipaka yake, kufanya tafiti na ubunifu, lakini pia kuzalisha mazao ya msingi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema wakati nikiwasilisha hotuba asubuhi hii nilieleza wazi kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan ambaye ni pia ni Amiri Jeshi Mkuu imetoa uzito sana katika sekta ya ulinzi na kwa muktadha huu katika bajeti ambayo nimeiwasilisha tumepata ongezeko la shilingi 53,754,747,000 ikiwa ni sawa na 15% kama ambavyo pia ilielezwa na Kamati ya Bunge wakati ikiwasilisha taarifa yake ambapo Wizara imepata ongezeko la 14%; Ngome imepata ongezeko la 16%; na JKT imepata ongezeko la 10%. Pia kuhusu rasilimaliwatu tayari tumekwishapata vibali vya kuandikisha askari na kuajiri watumishi wapya katika mwaka wa fedha 2023 kwa hiyo hii itatusaidia kuziba pengo ambalo mmelisisitiza Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mashirika ya NYUMBU, TATC na MZINGA pamoja na kutoa fedha kwa ajili ya kununua mitambo mashine na malighafi jitihada zinaendelea ili kuhakikisha kuwa mashirika haya yanawezeshwa kikamilfu ili kutimiza azma ya kuanzishwa kwake. Kwa kutambua umuhimu wa Shirika la TATC ambayo ni NYUMBU inavyoeleweka zaidi mpango wa maendeleo wa miaka 15 ambao ulirejewa wa kuliimarisha Shirika la NYUMBU utaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha huu 2022/2023 na kiasi cha shilingi 20,445,970,300 tayari kimeshatengwa. Kwa hiyo, hii inaonesha kwamba mawazo yenu, maoni yenu Kamati imesema kwamba imekuwa ikitoa maoni haya kwa muda mrefu yamezingatiwa na sasa mpango uliopitishwa unaenda kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa mpango huu utakuwa na manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uagizaji wa magari, zana, mitambo na vipuri na kukuza uwezo wa nchi katika utafiti na wa teknolojia za magari na mitambo jambo ambalo ni muhimu sana kwa Taifa lolote kuweza kujitegemea katika sekta hii.

Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa uzito lakini naomba ninukuu kauli yake katika hili ambapo amekuwa akisema kwamba; “yajayo yanafurahisha.” Kwa hiyo naomba tu tujipe muda tufanye huu utekelezaji na hayo yajayo yanayofurahisha mtayaona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine iliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge ni kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa miradi ya kilimo cha kimkakati hususan huko Chita na shamba la Mgeta, Mkoani Morogoro na msisitizo umewekwa katika kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Miradi hii ni muhimu sana kwa Taifa na kwa maono mapana kama ambavyo ilivyoelezwa unazo faida nyingi ikiwa ni pamoja na kuipunguzia Serikali gharama za kuwalisha vijana, kuchangia katika usalama wa chakula na moja ambalo halikusemwa na pia mradi huu miradi hii inatarajiwa kuchangia katika upatikanaji wa mbegu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri wa Kilimo jana alivyokuwa akitoa hotuba yake alisisitiza pia kwamba umuhimu wa mbegu ni kitu muhimu sana ili kuhakikisha kwamba unachangia katika upatikanaji wa chakula wa Taifa lakini na usalama wa chakula wa Taifa letu. Kwa hiyo, hili pia miradi hii itachangia katika hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu huu Serikali imeendelea kutenga fedha toka vyanzo vya ndani, lakini pia tunatafuta mikopo kwa ajili ya kuendeleza miradi hii na Mheshimiwa Waziri wa Fedha anatusaidia katika hilo. Kama nilivyosema utekelezaji wa miradi hii ya kimkakati utaliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kujitosheleza kwa chakula na hatimaye kuimarisha usalama wa chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la utatuzi wa migogoro ya ardhi limejitokeza kwa kiasi kikubwa katika mjadala; napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako tukufu kuwa Wizara imetoa kipaumbele kikubwa katika utatuzi wa migogoro ya ardhi baina ya Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania na wananchi na nina imani sote ni mashahidi tumeiona kazi kubwa inayoendelea. Hadi sasa utekelezaji wa mpango huo wa miaka mitatu unaendelea kwa ufanisi wa hali ya juu. Kazi hii ni sehemu ya timu za Wizara nane ambayo timu hii iliundwa na Mheshimiwa Rais lakini inasimamiwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kama alivyoeleza asubuhi ya leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango huo umejumuisha migogoro 87 na mpaka sasa migogoro 58, maeneo 58 yamekwishapimwa na kuwekewa mipaka kwa sababu suala la mipaka limesisitizwa sana na maeneo 17 yamefanyiwa uthamini na kati ya yaliyofanyiwa uthamini maeneo tisa yameshalipiwa fidia na asubuhi niliyataja sita, lakini tisa ni kwa ujumla wake tangu tumeanza kutekeleza. (Makofi)

Kwa hiyo yaliyosalia yanaendelea ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyoongelewa leo hapa na Mheshimiwa Haji Amour Haji na Mheshimiwa Saada Mansour na Mheshimiwa Kirumbe Ng’enda na Mheshimiwa Hawa Mchafu yote haya yamejumuishwa katika mpango huu katika yale ambayo yanaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Hawa Mchafu amenitaka nimpe taarifa ya task force hatua iliyofikiwa nimuombe tu kumuhakikishia Mheshimiwa Mchafu kwamba kazi hii tayari ripoti imeshawasilishwa nipatie tu muda niende niipitie ripoti hii na tutawasiliana tuone jinsi tutakavyo kamilisha zoezi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo napenda kuwashukuru viongozi wote na wananchi katika maeneo mbalimbali kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha Wizara kutatua changamoto hizo. Aidha, niwapongeze maafisa na watumishi wa Wizara wengine wametajwa humu kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kutatua migogoro hii.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za dhati za kutatua migogoro hii ambazo ni shirikishi nawaomba sana wananchi watambue umuhimu wa maeneo tunayohitaji kama Jeshi la Kujenga Taifa na pale ambalo tunahitaji kuchukua maeneo haya basi tushirikiane tuweze kupata maeneo haya, lakini pale ambapo maeneo yamekwishachukuliwa tuwaombe sana wasirudi kwenye maeneo haya. Kwa kufanya hivyo ni hatari kwao lakini pia ni kuzusha migogoro mipya. Kwa hiyo tushirikiane wote tuweze kwa kutoa elimu hii ili wote tuweze kutatua tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo limejitokeza ni uboreshaji na kuongeza makazi ya wanajeshi; hili ni suala muhimu sana na tunalipa uzito unaotakiwa naomba tu kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa Wizara inaendelea na utekelezaji wa mpango wa nyumba 10,000 kwa wanajeshi na hadi sasa nyumba 6,064 zimeshajengwa katika mikoa mbalimbali. Mpango uliopo ni kukamilisha hizo takribani 4000 zilizobaki na kuongeza zaidi pamoja na kwamba katika mwaka huu hatukuweza kutenga fedha, lakini bado tunaendelea kutafuta rasilimali ili kuhakikisha kwamba tunaongeza nyumba kwa ajili ya makazi ya wanajeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia kwa niaba ya watumishi wote kabla kulikuwa na hoja zingine chache ziizoletwa ambazo nyingine amenisaidia kuzijibu Naibu Waziri namshukuru sana kwa hilo, lakini nilipenda kuongelea suala la kuajiri vijana, alitoa hoja kwamba kuna vijana walifanya shughuli mbalimbali, lakini hawakuweza kuchukuliwa.

Nipende tu kuwafahamisha kwamba naimesemwa vizuri sana nafikiri na Mheshimiwa mmoja kwamba sababu kubwa ya kuwachukua vijana kwenda JKT ni kuwajengea stadi na hivyo ndivyo tunafanya na imeongezwa kwamba tuwajengee ufundi, hata hilo linafanyika. Kwa hiyo wanapokwenda JKT kinachotarajiwa pale ni kwamba wanajengewa stadi na baada ya pale waweze kwenda kujitegemea.

Kwa hiyo si rahisi kuweza kuwachukua vijana wote wanaokwenda JKT waende kuajiriwa kwa sababu kwanza hilo siyo lengo, lengo ni kuwapatia stadi lakini ushauri mzuri kabisa tumeupokea wa Mheshimiwa Asia Halamga na pia huu ulitolewa na Mheshimiwa Haji Amour kwamba pamoja na hayo tuweze kujaribu kuunganisha nguvu kama Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda kuona kwamba baada ya hapo tunawafanyia nini. Nipende tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hili tayari tunalifanyia kazi, tayari nimekwishaongea na Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na jana wakati akiwasilisha hoja yake moja ya eneo tuliloona tunaweza kulifanyia kazi mara moja ni kwenye upungufu wa sekta ya mafuta. Alieleza hapa kuna ukwasi mkubwa sana, kwa hiyo, tunataka tuone kwamba tunaweza kujumuisha nguvu zetu namna gani na kuwatumia hawa vijana wakaweza kushiriki katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia mazungumzo yanaendelea tuone kwamba na Wizara ya Viwanda tunaweza kushirikiana nao namna gani. Ushauri tumeuchukua lakini nipende kukuhakikishia kwamba tayari tunaufanyia kazi hata kabla ya hapo sisi tumekuwa tukijiuliza kwamba tukishawapa hizi taaluma basi waende kufanya nini, tuwawezeshe vipi, tunashukuru kwamba mmeongeza sauti katika hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mazingira; upandaji wa miti tunashukuru kwa pongezi hizo lakini ushauri kwamba tuongeze pia tumeuchukua, tutaufanyiakazi na ushauri wa kutoa elimu katika kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, uwekezaji usio na tija, naomba tu niseme kwamba uwekezaji unaofanywa na Jeshi umekuwa na tija kubwa sana rasilimali tunazozipata kutoka Serikalini ni kidogo na nikiwapa takwimu ni kwa kiasi gani uwekezaji huu umeweza hata kusaidia Jeshi la Ulinzi na Wananchi wa Tanzania kutekeleza majukumu yao ya msingi mtashangaa. Kwa hiyo, lakini kama yapo uwekezaji ambao unafikirika hauna madhara basi tutauangalia tuhakikishe kwamba madhara ya namna hiyo tunajikinga nayo lakini uwekezaji huu ni muhimu na umekuwa na tija sana.

Mheshimiwa Spika, mengine yalijibiwa; barabara limejibiwa lakini pia nipende tu kuwahakikishia kwamba barabara za doria na ulinzi ni kitu muhimu sana na hiki tayari nimekwishafanya mazungumzo na Mheshimiwa Waziri wa Uchukuzi na si barabara hiyo moja tu iliyoelezwa, ziko barabara nyingi na tayari baadhi zimeshaanza kufanyiwa kazi lakini baadhi tunaangalia jinsi gani ya kuziingiza katika mipango ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upandishaji vyeo wanawake; wanawake wanafanyakazi kama wanaume na hakuna ubaguzi katika upandishaji vyeo, vyeo vinapandishwa bila kujali jinsia kinachotakiwa katika Jeshi tu ni weledi, kwa hiyo, wanawake wanaendelezwa na wanapandishwa vyeo na wapo katika sehemu mbalimbali.

Kuhusu malimbikizo ya likizo hili limekwishafanyiwa kazi katika hotuba nimeeleza kwamba pamoja na mambo mengine Serikali imetoa kipaumbele kuhakikisha kwamba tunalipa madeni yote na hili limeshafanyiwa kazi kama wapo waliobaki basi hao wataendelea kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, michezo ni muhimu tumesikia na tutaendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, naomba pia kwa niaba ya watumishi wote wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na taasisi zake kupokea shukrani na pongezi kwa kazi nzuri inayofanywa ya kulinda mipaka yetu. Wengi mmetoa shukrani nazipokea kwa niaba ya Wizara na kudumisha amani na mmetoa maeneo mengi yanayofanyiwa kazi nzuri ikiwa ni pamoja na katika sekta ya afya, katika sekta ya elimu, lakini pia mmeeleza katika jinsi Jeshi lilivyosimama kuhakikisha kwamba nchi yetu imebaki salama wakati tumepata msiba wa Mheshimiwa wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na maeneo mengi. Kwa hiyo tunapongeza na pia kutoa mfano kwamba kwa kazi nzuri tumeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 65 katika ujenzi wa Kikombo, mifano ilikuwa mingi lakini napenda kushukuru na kuhakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa kazi zote zinazofanywa na Jeshi la Ulinzi na Wananchi wa Tanzania zinafanywa kwa weledi, umahiri na uzalendo wa hali ya juu na hii ndiyo misingi ya utendaji wa Jeshi letu na kazi nzuri zitaendelezwa daima. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri muda umeshaisha, lakini nakuongeza dakika tatu umalizie na Waheshimiwa Wabunge naongeza nusu saa tumalizie shughuli iliyo mbele yetu. (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante na kazi nzuri hizi zitaendelezwa kufanywa daima tu.

Mheshimiwa Spika, tumepokea pongezi ahsante baada ya ufafanuzi huu na kabla sijahitimisha hoja yangu naomba niwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii, waliofatilia hotuba na mijadala na naamini tutaendelea kushirikiana katika kudumisha ulinzi na amani na kuwaletea watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu katika kudumisha amani na kuwaletea wananchi maendeleo zinapaswa kuungwa mkono na sisi sote kama ambavyo mmeeleza ninyi wenyewe mmeshuhudia kwamba anafanyakazi kubwa kama Amiri Jeshi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inamshukuru kwa dhati kwa namna ambavyo amekuwa akisimamia ulinzi na usalama na kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zinazoikabili Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na taasisi zake tangu aingie madarakani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa pia mstari wa mbele kuidumisha diplomasia ya ulinzi na ameendelea kuiletea heshima nchi yetu kama Amiri Jeshi Mkuu mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie lugha hii ingawaje siyo rasmi kwamba ameupiga mwingi kwa kutusimamia kitaifa lakini pia kutupaisha kimataifa. Tuendelee kumuunga mkono Rais wetu mpendwa na napenda kusema kuwa wanawake wanaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na watanzania wote kuwa chini ya uongozi mahiri wa Amiri Jeshi Mkuu Mama Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Ulinzi na Taasisi zake zipo imara kuhakikisha kuwa nchi ipo imara na salama muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha naomba nitoe wito kwenu Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kuwa ulinzi wa Taifa letu ni jukumu la kila Mtanzania, ni jukumu la kila mmoja wetu na kila mmoja wetu anao wajibu wa kulitekeleza jukumu hilo. Wanajeshi wetu wanafanya kazi kubwa sana usiku na mchana kwa weledi, uhodari na uzalendo wa hali ya juu nawapongeza sana kwa moyo huo wa kujituma na kwa kazi kubwa wanayoifanya niwaombe sasa tuwaunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na baada ya maelezo hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tena kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuongoza katika mjadala huu wa uwasilisha wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Aidha, napenda niendelee kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa maono na miongozo yake katika kuiendeleza sekta hii ya ulinzi kama ambavyo wengi mmesema na kama ambavyo wengi mmempongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi ya leo katika Bunge lako Tukufu, niliwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na napenda kukushukuru sana kwa namna ambavyo umesimamia na kuongoza kwa umakini mkubwa sana mjadala huu wa bajeti ya Wizara ninayoiongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa. Najua leo ana majukumu mengine na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Mbunge wa Nkasi Kusini na Wajumbe wote wa Kamati kwa maoni na ushauri mliotupatia. Nawahakikishia kwamba ushauri huu tumeupokea kwa mikono miwili, tutaufanyia kazi na kuuzingatia kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote, ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza. Nilikuwa nafuatilia, lakini sijaambiwa kama tunao waliochangia kwa maandishi, lakini sijaona michango ya kimaandishi. Pia napenda kuwahakikishia kwamba tumezipokea hoja hizo na tuna imani kabisa zitaenda kuchangia katika kuimarisha utendaji na ufanishi wa Wizara. Maoni yenu tumeyachukua, tutayafanyia kazi katika kuboresha utendani na changamoto ambazo mmeziainisha pia tutazifanyia kazi. Wizara inatambua na kuthamini sana michango iliyotolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea hapa jumla ya Waheshimiwa Wabunge wanane wamechangia kwa mdomo, kwa hiyo, tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitajiribu kujibu baadhi ya hoja zilizowasilishwa katika michango hii ikiwa ni pamoja na hoja au ushauri ulioletwa kupitia katika Kamati ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuwepo hoja ya Bajeti, napenda kuwahakikishia, kuwathibitishia na kuwatoa hofu kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, imetoa uzito mkubwa sana kwenye sekta ya ulinzi ikiwa ni pamoja na katika Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na bajeti yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwathibitishia hili tu Waheshimiwa Wabunge, katika kipindi cha miaka mitatu tu tangu aingie madarakani, bajeti ya Wizara na taasisi zake imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka kutoka shilingi 2,358,694,986,000 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia shilingi 2,713,787,405,450 katika mwaka wa fedha 2022/2023 na hili lilikuwa ni ongezeko la 13%; na kufikia shilingi 2,989,967,122,000 katika mwaka wa fedha 2023/2024 ambao ni mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la 9.24%. Katika mwaka wa fedha huu ambao nimewasilisha bajeti ambayo nilikwishaitaja ya shilingi trilioni 3.3. Hili ni ongezeko la 9.4%. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza hizi zimeiwezesha Wizara na taasisi zake kutekeleza majukumu yake ipasavyo, lakini kama nilivyoeleza katika hotuba yangu, pia panapohitajika mahitaji mahususi fedha hizo zimeweza kutolewa na Serikali na kuiwezesha Wizara na taasisi zake ikiwa ni pamoja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kutekeleza majukumu yake bila kutetereka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mtiririko wa bajeti, mpaka sasa hivi tumekwisha pokea kiasi cha 80%. Kwa hiyo, hii inadhihirisha, na hizi figure au takwimu hii ni ya mpaka kufikia mwezi wa nne, bado kuna miezi miwili. Kwa hiyo, tuna imani kabisa mpaka kufikia mwisho wa mwaka wa fedha huu, fedha zote zitakuwa zimekwishatolewa kama ulivyokwishasema Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuwe na imani, Serikali iko makini, inatambua umuhimu wa Wizara na taasisi zake na tumeendelea kupata kinachotakiwa na kilichopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine lililojitokeza katika mjadala na kwa uzito sana kupitia Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ni kuhusu vifaa na mashine kwa ajili ya matumizi ya Jeshi kutozwa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili tumeendelea kulifanyia kazi kwa karibu sana kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha. Tumekwisha kuwa na mazungumzo ambayo yanapelekea kwamba tunaenda kulihitimisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizo ni pamoja na kuwasiliana na Wizara ya Fedha kama nilivyosema na kufanya mapitio ya kodi la ongezeko la thamani na Sheria ya Fedha. Hatua hii itaendeana na utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Ushuru wa Forodha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani The East African Community Customer and Management Act inayoelekeza kuwa vifaa vyote vinavyoingizwa nchini kwa matumizi ya jeshi visitozwe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muktadha huu, Wizara imewasilisha mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Kodi katika Tume ya Kurekebisha Sheria ili kutoa msamaha kwa vifaa vyote vinavyoingizwa nchini kwa matumizi ya jeshi. Ni imani yangu, nilidhani Mheshimiwa Waziri wa Fedha yupo hapa, ni imani yangu kabisa kwamba kwa hatua tuliyofikia suala hili linaenda kuhitimishwa mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo limesemwa kwa hisia sana na Kamati ya Bunge, lakini pia na Mheshimiwa Tendega, ni suala la uwepo wa madeni ya takribani shilingi bilioni 1.9 hususan kwa Taasisi ya Mzinga. Napenda kuwahakikishia kwamba suala hili pia tumelifanyia kazi kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, madeni ya kampuni hii Tanzu ya Mzinga Holding ya shilingi bilioni 1.9 yanatokana na miradi mbalimbali ya ujenzi iliyotekelezwa kama mnavyofahamu. Aidha, hadi sasa madeni haya kwa ujumla mmeonesha kwenye taasisi za Serikali, lakini kiujumla ukichanganya na yaliyopo katika taasisi za sekta binafsi ni shilingi 1,998,000,000 kwa maana ya shilingi bilioni 1.9 ni Serikalini na milioni 98 ni katika taasisi za umma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnavyofahamu hususan Waheshimiwa wa Kamati ya NUU, lakini sasa kwa kutoa taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge wote na Bunge lako Tukufu, madeni haya yalikuwa zaidi ya hapa. Tulikuwa na deni la shilingi 4,095,000,000. Kwa hiyo, kwa hatua tulizozichukua deni hili limeweza kupungua na kubakia deni hili la bilioni 1.998. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua tunazozichua ni imani yetu kabisa kwa sababu tumeshafanya mazungumzo na tumeshachukua hata hatua za kisheria, wale wanaohitajika kupelekwa mahakamani tumewapeleka. Kwa hiyo, kwa hatua hizi tunazoendelea nazo, tuna imani kabisa kwamba tutaweza kukamilisha haya madeni mengine ambayo hayajalipwa. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa msisitizo na kwa kuona kwamba hii ni changamoto na tunawahakikishia kwamba tunalitambua na tunaendelea kulifanyika kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ambayo imezungumzwa na Kamati na Mheshimiwa Salma Kikwete, Mbunge wa Lindi ameisisitiza, ni kuimarisha mipaka ili kudhibiti mianya na njia zisizo rasmi. Kamati imezungumza kwa njia mbalimbali, lakini pia Mama Kikwete ameongezea. Napenda tu kusema kwamba Wizara imeendelea kuimarisha ulinzi katika mipaka ya nchi yetu na nimesema katika hotuba yangu pia na kama nilivyoeleza hali ya mipaka yetu ni salama kabisa na ni shwari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto haziwezi kukosa, changamoto zitakuwepo hizi pia zinafanyiwa kazi inavyotakiwa kila zinapojitokeza. Aidha, Wizara imeendelea kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa zana na vifaa ili kutekeleza majukumu hayo ipasavyo. Naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Wizara inaendelea kuwekeza kwenye mifumo ya kisasa ili kuhakikisha kuwa inadhibiti mipaka yetu kikamilifu ikiwa ni pamoja na njia zisizorasmi mipakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wamesisitiza umuhimu wa teknolojia, wamesisitiza umuhimu wa kuwa na vifaa vinavyoendana na wakati na hiki ndiyo kinachofanyika, tunashukuru mmetukumbusha lakini niwahakikishie kwamba hili ndiyo tunaendelea kulifanya, ni suala endelevu linafanyika wakati wote kuhakikisha kwamba jeshi letu linavyo vifaa vya kisasa na katika ulinzi wa mipaka tunaweza kufanya kazi hiyo inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili kwa niaba ya Bunge lako Tukufu naomba sana kutoa shukurani zetu za dhati kwa Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu kwa uzito mkubwa anaoutoa kwa Jeshi letu katika kuhakikisha kwamba linawezeshwa kwa zana na vifaa vya kisasa katika kutekeleza jukumu lake la msingi la ulinzi wa mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyoeleza kuhusu ongezeko la bajeti, hiyo ni uthibitisho mmojawapo kwamba kweli Mheshimiwa Rais anatoa uzito unaotakiwa ili kuhakikisha kwamba Jeshi letu linaweza kuimarika, lakini yako mambo mengi makubwa yanayofanyika ambayo pia ni ya kukakikisha kwamba Jeshi letu linaimarika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeendelea kushirikiana na Wizara, liliongelewa suala la mipaka na Waheshimiwa Wabunge kadhaa na ulitolewa mfano, nafikiri alikuwa Mheshimiwa Mama Kikwete sasa nakumbuka kwamba kuna kati ya mpaka wetu na Kenya na Mpaka wetu na Malawi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kusema kwamba tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kuhakikisha kuwa barabara na alama za mipaka zinaendelea kuimarishwa. Hii ni kazi inafanyika, tumefanya kwa kiasi fulani katika mwaka huu wa fedha unaoendelea na tutaendelea kuifanya ili tuweze kuikamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mpaka wa Malawi, hilo linasimamiwa chini ya Wizara ya Mambo ya Nje lakini tunashirikiana nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Jeshi la Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa limeendelea kuimarisha viteule vilivyopo mipakani na kuviwezesha kufanya doria za mara kwa mara. Pia tunaendelea na kusimika mifumo ya ulinzi mipakani. Kwa hiyo, haya yote yanafanyika ili kuhakikisha kwamba kweli mipaka yetu iko imara na inaendelea kuwa imara kwa sababu ni imara, lakini tunaishi katika dunia ambayo ina matishio mbalimbali na wakati wote sisi tunatakiwa tuwe tumejipanga.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liliongelewa suala la umuhimu wa kuendeleza na kuboresha mashirika yetu ya Nyumbu na Mzinga na liliongelewa na Kamati na Mheshimiwa Tendega amelisisitiza sana. Napenda tu kusema kwamba Wizara inatambua umuhimu wa mashirika haya kwa maslahi mapana ya Taifa letu na jeshi na ulinzi kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu huu, Wizara imeendelea kutekeleza mpango wa miaka kumi wa kuimarisha Shirika la Mzinga. Nilieleza katika hotuba yangu kwamba tunao Mpango wa miaka kumi0 wa Kuliimarisha Shirika la Mzinga. Kwa hiyo, mpango huu utekelezaji wake unaendelea. Hela imeshatengwa, inaendelea kutolewa mwaka hadi mwaka na hatua za utekelezaji za kufanya masuala mbalimbali zinaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Shirika la Mzinga, Wizara ipo katika hatua ya awali ya kuanzisha Mzinga Two. Tunataka tuanzishe kiwanda kingine ambacho kitakuwa kinaongezea nguvu na kinaenda na mahitaji ya wakati wa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu rasilimali watu, Wizara kupitia jeshi na taasisi zake tumeendelea kuwawezesha na vilevile Ofisi ya Utumishi imeendelea kutupatia watumishi awamu kwa awamu. Hivyo, nawaahidi Waheshimiwa Wabunge kuwa tunaendelea kuyaimarisha mashirika yetu haya ili kutimiza azma ya kuanzishwa kwake. Hivyo nawaomba mtupitishie bajeti ambayo naileta hapa, imejumuisha bajeti ya mashirika haya ili yaweze kuendelea kufanya kazi zake na yaendelee kujiimarisha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liliongelewa suala la Sera ya ulinzi; hoja ya kukamilisha Sera ya Ulinzi, maandalizi ya sera yameendelea, yamefika mbali. Tumeshafanya tathmini ya hali ya ulinzi na usalama kwa sababu hiyo ndiyo inawezesha kuandaa hiyo sera. Tumeshafanya mazungumzo na upande wa pili na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na tumeshapata maoni yao, lakini suala hili limesimama kidogo kwa sababu kuu mbili; sababu ya kwanza, tuko katika mchakato wa kuandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2025 mpaka 2050 na wakati huo huo tunaendelea na maandalizi ya Sera ya Mambo ya Nje kama Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya yote yatakuwa yana uhusiano wa karibu na Sera ya Ulinzi. Kwa hiyo, tukienda haraka kukamilisha Sera ya Ulinzi sasa hivi, tunaweza tukajikuta tumeacha mambo ya msingi ambayo yanatokana na Dira ya Taifa na Sera ya Mambo ya Nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge, Sera ya Ulinzi ya Mambo ya Nje ya sasa ilivyo imejumuisha eneo ambalo linahusiana na mambo ya ulinzi na usalama. Kwa hiyo, baada ya hii michakato miwili kukamilika, nawahakikishia kwamba tutaweza kukamilisha sera hii kama itakavyokuwa imekubalika katika mijadala inayoendelea kwa sababu sasa hivi haya masuala yote mawili yanajumuisha wadau wote kitaifa ili kila eneo liweze kutoa mawazo yao. Pengine mnaweza mkaja mkasema hatuhitaji tena Sera ya Ulinzi. Sijui, kwamba kila kitu kimejumuishwa katika Sera ya Mambo ya Nje, sijui. Kwa hiyo, ndiyo maana tunajipa muda ili tuweze kuja na kitu ambacho kitakuwa ni sahihi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo pia maeneo mengine ambayo yaliongelewa sana ambayo niyajumuishe kwa ujumla wake; Mheshimiwa Nahodha, Mheshimiwa Ahmed Salum, Mheshimiwa Lugangira na hata Mheshimiwa Tendega, wameongea kwa njia tofauti, lakini hoja kubwa iliyokuwa inajitokeza ni kuhusu kuliimarisha jeshi letu kivifaa, kiteknolojia, kimafunzo na kiutaalamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda tu kusema kwamba jeshi letu liko vizuri sana lakini hatusemi kwamba kwa sababu tuko vizuri sana hatuna sababu ya kujifunza na kwenda na wakati. Ni kweli tuko katika karne ya 21, mahitaji yanabadilika na sisi wakati wote tunajitahidi kwenda na mahitaji ya wakati. Kwa hiyo, haya yote mliyoyasema tutayazingatia wakati wote, wakati wa utekelezaji na kwa kadiri tunavyoendelea kuliimarisha jeshi letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuko katika karne mpya, cyber security, technological warfare na food security inayoendana na usalama kwa ujumla wake ni lazima tuizingatie. Kwa hiyo, yote haya tumeyapokea, tutaendelea kuyafanyia kazi na hata katika kuliboresha jeshi letu kitaaluma na kiteknolojia, yote haya tunayazingatia. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge msiwe na wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umetolewa ushauri kuhusu kufanya ushirikiano na vyuo. Tunapokea na tunafanya hivyo na siyo vyuo tu, tunafanya ushirikiano na taasisi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilivyosikiliza huu mjadala kwa mapana yake, nimeona ni mjadala ambao hauihusu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa peke yake, ni mjadala unaoihusu Serikali kwa ujumla wake. Kwa hiyo, hapa sisi tutayachukua na tutaenda kukaa chini kama Serikali na tuone kwamba tunaweza kushirikiana kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ukisema Jeshi lisimamie uzalishaji wa mbegu bora, tunafanya lakini lazima tushirikiane na Wizara ya Kilimo. Tukisema twende kwenye masuala ya cyber security, tunafanya lakini lazima tushirikiane na Wizara ya Habari na Teknolojia na Wizara ya Mambo ya Ndani. Haya yote ni mengi ambayo mmeyasema, kwa hiyo, niwahakikishie tu kwamba tutaendelea kushirikiana kama Serikali na tunajua kabisa umuhimu na msisitizo mlioutoa, kwa hiyo, tutalifanyia kazi inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo yote haya ni mengi ambayo mmeyasema kwa hiyo niwahakikishie tu kwamba tutaendelea kushirikiana kama Serikali na tunajua kabisa umuhimu na msisitizo mlioutoa kwa hiyo tutalifanyia kazi inavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mwisho ambayo napenda kusemea ni ya Mheshimiwa Hawa ambayo yeye ameelezea kuhusu maeneo yaliyotwaliwa kwamba yanatakiwa kulipwa fidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijajibu hoja hii ya specific nipende tu kutoa shukrani sana kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mnaotupatia kwa sababu jeshi bila kupata maeneo utekelezaji wa baadhi ya majukumu utakuwa mgumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata katika utatuzi wa migogoro hii tumefanya pamoja nawashukuru sana. Tulikaa chini tulipohitaji maeneo ya ziada tumekaa pamoja mmeweza kutuelewa na tuendelee kufanya kazi pamoja katika eneo hili na ni kweli tumetoa maeneo mbalimbali kwenye hili hapa ambalo ukiangalia katika kitabu hiki maana yake amesema anataka kauli ulisema kweli Mheshimiwa mwaka jana na nilikuhaidi nitafanyia kazi na tumefanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia katika kitabu cha hotuba jedwali la pili na jedwali la kwanza, jedwali la pili linaonesha maeneo ambayo yalipimwa na kulipiwa fidia na hapo ukiangalia kwa mwaka 2022/2023 namba 14 tuna Tondorani, Pwani ambapo fidia ya shilingi 46,712,720 ililipwa Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Katika kitabu hiki hiki ukiangalia jedwali na kiambatanisho namba moja hicho nilichokuwa nimekirejea ni kiambatanisho namba mbili kuna maeneo ambayo hayajalipiwa fidia lakini tumeshayafanyia tathimini.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo namba moja katika jedwali hilo ni hiyo KJ191 ambayo umeirejea ambayo pia hii katika uthamini tunatarajia kuwalipa shilingi 2,520,249,865 kwa hiyo hii hapa uthamini umeshakamilika kilichosalia sasa hivi ni kwenda kulipa hiyo fidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nihitimishe kwa kuanza na kwa niaba ya watumishi wote wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa au Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na Taasisi zake kupokea shukrani na pongezi za dhati ambazo mmetupatia kwa kazi nzuri inayoendelea kufanyika ya kulinda mipaka yetu na kudumisha amani na aidha, napenda kuwahakikishia kuwa Wizara ya Ulinzi na taasisi zake ikiwemo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa weledi, umahiri na uzalendo na hii ndiyo misingi ya utendaji wetu wa kazi na tutaiendeleza daima.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafanya hivi tukitambua kwamba Amiri Jeshi Mkuu yupo nyuma yetu akitusimamia, akituangalia na akitaka kuhakikisha kwamba kweli tunafanya maukumu yetu kama inavyotakiwa na hatutakuwa tayari hata dakika moja kumuangusha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pongezi hizi ambazo mmezitoa kwa Wizara naomba nichukue kwamba ni pongezi ambazo zinatolewa kwetu, lakini zinatolewa kwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ndiyo msimamizi namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ufafanuzi huo na kabla sijahitimisha hoja yangu naomba niwashukuru tena kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii na hata waliosikiliza na waliofuatilia hotuba hii na mjadala, naamini tutaendelea kushirikiana katika kudumisha ulinzi na amani na kuwaletea Watanzania maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upekee napenda niwapongeze watendaji wote wa Wizara na taasisi zote wakiongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe kwa upande wa Wizara na Jenerali Jacob John Mkunda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi kwa upande wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kufanya kazi kwa weredi na kujituma na kuwezesha kufikia hatua hii ambapo tunaelekea kuhitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jitihada kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais na Amiri Jeshi Mkuu katika kudumisha amani na kuwaletea wananchi maendeleo zinapaswa kuungwa mkono na sisi sote. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inamshukuru kwa dhati kwa namna ambayo amekuwa akisimamia ulinzi na usalama na kuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto zinazoikabiri Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na taasisi zake tangu aingie madarakani, lakini changamoto zinazolikabili Taifa letu kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa pia mstari wa mbele kuimarisha diplomasia ya ulinzi na ameendelea kuiletea heshima nchi yetu, tuendelee kuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu mpendwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kuwa chini ya uongozi wa Amiri Jeshi Mkuu Wizara ya Ulinzi na taasisi zake ipo imara ili kuhakikisha kuwa nchi yetu ina amani, ipo shwari, ni imara wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuhitimisha naomba nitoe wito kwenu wote Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kuwa ulinzi wa Taifa letu ni jukumu la kila Mtanzania na kila mmoja wetu analo jukumu la kutekeleza wajibu huo. Wananjeshi wetu na watendaji wote wanafanya kazi kubwa sana usiku na mchana kwa weledi, uhodari na uzalendo wa hali ya juu. Nawapongeza sana kwa moyo huo wa kujituma na kwa kazi kubwa wanayoifanya niwaombe sote tuwaunge mkono na kutoa ushirikiano na tusiwakatishe tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya fedha; naomba sasa Bunge lako Tukufu liidhinishe kiasi cha shilingi 3,326,230,419,000 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kati fedha hizo shilingi 3,008,812,907,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 317,417,512,000 ni kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kukushukuru kwa kunipa fursa na mimi ya kuchangia katika taarifa ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Napenda kuanza kwa kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Vita Rashid kawawa, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Vincent Paul Mbogo, Wajumbe wote wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Pia nawashukuru Waheshimiwa Wabunge, kwa michango yote ambayo mmetupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Kamati kwa Miongozo Madhubuti ambayo wameendelea kutupatia, ushauri lakini pia na ushirikiano mkubwa ambao umetuwezesha kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi mkubwa ambao unatokana na michango ambayo wametupatia na miongozo ambayo wameendelea kutupatia. Nawaahidi tu Waheshimiwa Wabunge na Kamati kwa ujumla kwamba michango yote na ushauri wote ambao umetolewa, tutaendelea kuuzingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa na mimi kutoa ufafanuzi katika baadhi ya hoja ambazo zimejitokeza katika taarifa zilizowasilishwa lakini pia katika michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali. Nianze na hoja ambayo imejitokeza, imeongelewa na Kamati lakini pia imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge ambayo inahusiana na ufinyu wa bajeti. Katika Kamati imeonyeshwa kwamba, katika mwaka wa fedha tulitengewa kiasi cha shilingi bilioni 222, milioni 833 na laki 1 na 71 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya mwaka huu wa fedha. Katika kiasi hicho kwa ujumla wake tumepata asilimia 35.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kueleza kuwa, kiasi hiki ni cha mwaka mzima lakini katika kiasi hiki cha mwaka mzima, kwa nusu mwaka ambao umeripotiwa, tumekwishapata kiasi cha asilimia 65. Ni matumaini yetu kwamba kwa kiasi kichobakia, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha na kiasi hicho kitapatikana kama ilivyosisitizwa na Waheshimiwa Wabunge, na pia kama ilivyosisitizwa sana na Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kueleza kwamba, katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Amiri Jeshi wetu Mkuu, Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwa ni pamoja na Wizara, vimepewa uzito mkubwa sana. Kama mtakavyoona, mkifuatilia bajeti ambayo tumeendelea kupata imekuwa ikiongezeka tangu Mwaka 2021/2022. Katika mwaka 2021, bajeti tuliyokuwa tumetengewa kwa ujumla wake ilikuwa shilingi trilioni 2.4; lakini mwaka 2022/2023 bajeti hii iliongezeka na kufikia shilingi trilioni 2.7 ikiwa ni sawa la ongezeko la asilimia 13. Kwa Mwaka huu, bajeti tuliyotengewa ni kiasi cha shilingi trilioni 3 ikiwa ni sawa na asilimia tisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba hoja ya Kamati ilijikita zaidi katika Bajeti ya Maendeleo, lakini kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, huwezi kutenganisha Bajeti ya Maendeleo na Bajeti ya Matumizi Mengineyo kwa sababu vifaa vikinunuliwa lazima vitunzwe, vifaa vikinunuliwa, wanaoviendesha lazima wafanye mazoezi, vifaa vipashwe moto, ndege zirushwe, Marubani wapate nasaha, na kadhalika na kadhalika. Kwa hiyo hizi bajeti zote mbili ni muhimu sana kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwa muktadha huu, naomba kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais wetu na Amiri Jeshi wetu Mkuu kwa umuhimu mkubwa ambao ameutoa kwa Wizara yetu na kwa taasisi zake. Kazi inaendelea kufanywa kama ambavyo mmeona na mambo mengi yanaonekana, nchi yetu, mipaka yetu ipo salama, amani imetamalaki ndani ya Taifa letu kwa hiyo namshukuru sana Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kuwapongeza Makamanda wote, Maaskari wote na Maafisa wote kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Ulinzi ni jukumu letu sote kwa hiyo naomba pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa kushiriki katika kuhakikisha kwamba Taifa letu liko na amani na ulinzi uko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imeongelewa, ni suala la JKT kwamba vijana wengi wanatakiwa waende JKT lakini mpaka sasa hivi hatujaweza kuwapeleka vijana wote wanaomaliza Kidato cha Sita. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba vijana wote wanakwenda JKT kwa sababu Serikali inautambua umuhimu wa kuwapeleka vijana JKT ili waweze kuwa mahodari lakini pia kwa maslahi mapana ya Taifa letu. Kwa maana hiyo ndiyo maana Mwaka 2013 Serikali ilirejesha Mafunzo ya JKT ambayo yalikuwa yamesitishwa Mwaka 1994 ili kuwawezesha vijana wanaomaliza Kidato cha Sita waweze kwenda JKT.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwenda hatua kwa hatua, na imetolewa katika taarifa kwamba kwa mwaka jana tuliweza kuchukua asilimia 50 ya vijana waliokuwa wamemaliza form six. Matarajio yetu ilikuwa ni kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kufikia mwaka 2025/26.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyoelezwa, kutokana na changamoto za Miundombinu na kibajeti, inawezekana lengo hili tusilifikie lakini tumeupokea ushauri wa Kamati, tutaufanyia kazi ili kuona kwamba tunaweza kuwachukua vijana wote kama inavyotakiwa. Niunganishe hoja hii na hoja iliyokuwa imetolewa na Mheshimiwa Mbunge Ngassa, kwamba ili sharti lililowekwa la kwamba vijana wanaokwenda kuajiriwa katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama, lazima wawe na Mafunzo ya JKT nililitolea majibu nafikiri wiki iliyopita wakati nikijibu moja ya maswali na ni kwamba ni kweli tumekwishaona kwamba kuna changamoto hiyo. Katika Taarifa ya Tume ya Jinai ni Hoja ambayo imetolewa Mapendekezo na Serikali inalifanyia kazi. Tutaendea kulifanyia kazi kadri itakavyowezekana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Hoja nyingine ambayo imetolewa kuhusiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi kuwekeza katika Teknolojia. Hiki ni kitu muhimu sana na napenda tu kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Bunge lako Tukufu kwamba hatuko nyuma katika suala hili. Dhima ya Jeshi letu ni kuwa na Jeshi la kisasa. Si suala jipya, ni suala ambalo tunaendelea nalo na tumeendelea kuwekeza na kujipanga vizuri kiteknolojia. Najua Teknolojia inakua kwa haraka na sisi tunajitahidi hivyohivyo kwenda kwa haraka. Unaposema kuwekeza katika Teknolojia, si katika dhana na vifaa tu lakini pia ni katika utaalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote tunayafanya na kama waliosikiliza wakati Mheshimiwa Rais, Amiri Jeshi Mkuu akifungua Kikao cha Makamanda kilichofanyika Mwezi jana, Mwezi Januari, hili pia alilisitiza. Hii inaonyesha wazi kwamba, hata Amiri Jeshi Mkuu, anatambua hili na ameendelea kusisitiza kwamba lazima twende na Teknolojia. Hiyo ilikuwa ni hoja ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Lugangila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa na hoja ambayo ilitolewa na Mheshimiwa Fakharia kuhusiana na vifaa, kutenganishwa vifaa vya Jeshi. Tumeipokea hoja hii, tunaifanyia kazi na tutaendelea kuifanyia kazi. Hoja ya Mheshimiwa Grace Tendega kuhusu bajeti kwenda Mzinga, tumeliongelea sana, Kamati imesisitiza sana, tutaendelea kulifanyia kazi. Hoja ya Mheshimiwa Ngassa, nimeshaijibu, hoja za Mheshimiwa Zahor ilikuwa ya kiujumla kwa Serikali nzima, tutaendelea kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kurudia kwamba hoja zote tumezipokea na tutazifanyia kazi. Naomba kutoa hoja. (Makofi)