Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Stergomena Lawrence Tax (29 total)
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
(a) Je, kwanini Serikali isihamishe Kambi za Jeshi la Wananchi (JWTZ) Zanzibar ambazo zipo katikati ya makazi ya watu kutokana na kasi ya maendeleo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza? na
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani za kumaliza mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati ya wakulima na JWTZ kambi ya Kisakasaka?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu. Kwa kuniteua kuwa Mbunge na hatimaye kuniteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Lakini pia na kwako kwa ushirikiano ambao nimekuwa nikiupata tangu niteuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, Makambi na Vikosi vya Ulinzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania yameundwa kwa Mamlaka ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa Na. 24 ya Mwaka 1966, ambayo imefanyiwa marekebisho na Sheria Na. 192 ya Mwaka 2002. Makambi haya na Vikosi yamejengwa kimkakati kukabiliana na tishio lolote dhidi ya Nchi yetu. Maeneo haya ni muhimu sana kwa ulinzi na usalama.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa migogoro baina ya Jeshi na wananchi wa Vijiji vya Sheha za Kisakasaka, Mwangani, Kombani, Fuoni na Kondemaji. Kwa nyakati tofauti serikali imefanya jitihada za kutatua mgogoro huu. Hivi sasa Wizara yangu inatekeleza Mkakati maalum wa miaka mitatu wa kupunguza au kumaliza kabisa migogoro ya ardhi baina ya Jeshi na wananchi.
Mheshimiwa Spika, kulingana na Mpango huu, Wizara imepanga kufanya upimaji na uthamini katika maeneo haya niliyoyataja katika robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2021/ 2022 ambayo ni robo hii. Wizara inawaomba wananchi kuendelea kuwa na subira wakati Wizara ikiendelelea na utekelezaji wa Mkakati huu wa upimaji na uthamini wa maeneo yote ya Jeshi.
(c) Mheshimiwa Spika, naomba pia nitoe rai kwa wananchi wanaoishi jirani na maeneo ya Jeshi, kuacha kuvamia maeneo hayo kwani ni hatari kwa usalama wao, na ni vigumu kwa Jeshi kuhamisha makambi kwa kuwa makambi hayo yamejengwa kimkakati. Nawasilisha. (Makofi)
MHE. LATIFA KHAMISI JUWAKALI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo ya Jeshi kama Chejuu na Dunga, Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA
K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Latifa Khamisi Juwakali, Mbunge wa Viti Maalum kupitia Kundi la Vijana kutoka Mkoa wa Kusini Unguja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, uthamini na upimaji wa maeneo ya Chejuu, na Dunga huko Zanzibar umekamilika, vitabu vya uthamini vipo Kamisheni ya Ardhi Zanzibar. Aidha, kukamilika kwa zoezi hili kunasubiri kukakamilika majadiliano yanayoendelea kati ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Mara majadiliano hayo yatakapokamilika, Wizara itawasilisha maombi ya fedha kwa ajili ya fidia kwa kutumia kiasi cha fedha kilichotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge, aendelee kuwaomba wananchi wa maeneo hayo ya Chejuu, Dunga na maeneo mengine waendelee kuwa na subira wakati tukikamilisha majadiliano hayo. Nakushukuru.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -
Je, ni fursa zipi anazopata Askari anayeoa au kuolewa na Askari mwenzake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kanuni, miongozo na taratibu za Majeshi ya Ulinzi, kila Afisa na Askari hupewa stahiki kulingana na cheo chake. Endapo Afisa au Askari ataoa au kuolewa na mwenzake, haitaathiri stahiki zake. Aidha, hakuna fursa za kipekee anazopata Afisa au Askari aliyeoa au kuolewa na mwenzake.
MHE. FELISTA D. NJAU aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha kifedha JKT ili iweze kutekeleza kwa ufanisi mradi mkubwa wa kilimo cha mpunga Chita JKT – Morogoro na Shamba la Mngeta?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Felista Deogratius Njau Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuliwezesha Jeshi la Kujenga Taifa kifedha kila mwaka ili liweze kutekeleza kwa ufanisi shughuli zake, ikiwa ni pamoja na miradi ya kilimo, ikiwemo mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika shamba la mpunga lililopo Chita mkoani Morogoro na Shamba la Mngeta. Katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali ilitoa Shilingi 4,000,000,000 ambazo zimetumika kununulia zana na vifaa vya kilimo kwa ajili ya shamba la Chita. Aidha, katika Mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi 4,000,000,000 katika bajeti ya maendeleo kwa ajili ya kumalizia awamu ya kwanza ya ujenzi wa skimu ya umwagiliaji wa ekari 2,500 huko Chita.
Mheshimiwa Spika, Katika kuliendeleza shamba la Mngeta lenye ekari 12,000, kiasi cha Shilingi 11.5 zinahitajika kwa ajili ya ununuzi wa zana, matengenezo na maboresho ya miundombinu ya uzalishaji, na gharama za uendeshaji. Wizara inaendelea kufanya mazungumzo na Wizara ya kilimo ili kuona uwezekano wa shamba hili la Mngeta, kuwa sehemu ya mpango wa skimu za umwagiliaji. Taratibu za ndani zinaendelea ili kuwasilisha maombi ya fedha Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza: -
Je, Serikali haioni haja ya kurejesha Kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Tunduru ili kuimarisha ulinzi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama iufatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuimarisha ulinzi katika mipaka ikiwa ni pamoja na mpaka wa Kambi ya Wananchi wa Jeshi la Tanzania Tunduru na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ipo katika mchakato wa kurejesha Kambi ya Jeshi la Wananchi Wilayani Tunduru. Tayari Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imekwishaomba fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kambi hiyo toka Wizara ya Fedha na Mipango.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali italipa wananchi wa Kijiji cha Usulo, Kata ya Mbungani Tabora Manispaa, ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inakiri kuwa walikuwepo wananchi watatu katika eneo hilo kabla halijachukuliwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Manispaa ya Tabora imekishafanya uthamini na vitabu vya uthamini viliwasilishwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Septemba mwaka 2021, Wizara imekwishawasilisha vitabu hivyo Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya uhakiki na uhakiki ulikamilika Disemba mwaka 2021.
Mheshimiwa Spika, fedha kwa ajili ya fidia zimejumuishwa katika bajeti ya Wizara ya Mwaka wa Fedha huu unaoendelea 2021/2022 na inatarajiwa kuwa wananchi husika watalipwa fedha hivi karibuni, mara baada ya Wizara kupokea fedha hizo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.
MHE. MWANAKHAMIS KASSIM SAID aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzana na Wakazi wa Kijiji cha Dunga – Zanzibar?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said Mbunge wa Magomeni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, eneo la Kambi ya Dunga 141KJ limejumuishwa katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Wizara wa Kutatua Migogoro ya Ardhi wa 2020/2021 – 2022/2023 unaoendelea kutekelezwa.
Mheshimiwa Spika, upimaji na uthamini katika eneo hili ulianza tarehe 19 Aprili, 2022 na umemalizika tarehe 25 Aprili, 2022. Hatua zinazofuata ni kuwasilisha kitabu cha uthamini kwa Mthamini Mkuu wa Zanzibar kwa ajili ya idhini na kisha kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa uhakiki na malipo ya fidia. Namwomba sana Mheshimiwa Mbunge avute subira, kwani mchakato umefikia hatua nzuri na Wizara imedhamiria kumaliza migogoro yote ya ardhi kati ya taasisi zake na wananchi.
MHE. BAHATI KHAMIS KOMBO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani na eneo lililoachwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania katika Shehia ya Kengeje – Pemba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y. NAIBU WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bahati Khamis Kombo, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo katika maeneo mengine, Serikali imeendelea kulitumia eneo lililotajwa la Shehia ya Kengeje, Kusini Pemba kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa Kisiwa cha Pemba upande wa Magharibi. Vilevile eneo hilo linatumika kufanyia mafunzo, ambayo ni muhimu katika kuliimarisha Jeshi.
Hadi sasa eneo hilo linakaliwa na kiteule cha Jeshi 14KJ. Nitoe rai kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kwa kutambua kuwa ulinzi wa nchi yetu pamoja na maeneo ya Jeshi ni jukumu la kila mwananchi. Ahsante.
MHE. AMEIR ABDALLAH AMEIR aliuliza: -
Je, Balozi za Tanzania zinatumia vipi fursa ya kukua kwa Kiswahili duniani kutafuta ajira kwa Watanzania?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdallah Ameir, Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Balozi zetu nje ya nchi zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali katika kukuza Kiswahili na kuchangia ongezeko la ajira kwa Watanzania ikiwemo kuanzisha programu za kufundisha, kutafsiri na kufanya ukalimani wa Kiswahili duniani, hatua ambayo inatoa ajira kwa Watanzania. Jumla ya Balozi 13 zimeweza kuanzisha madarasa, vituo na clubs za Kiswahili. Aidha, zaidi ya Watanzania 95 wamepata ajira katika maeneo hayo. Vilevile, vyuo na vituo binafsi zaidi ya 150 vinafundisha Kiswahili duniani. Kwa sasa, Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) limepewa kazi ya kufundisha walimu 10 wa Diaspora katika Ubalozi wetu wa Abu Dhabi ambapo ni uhitaji wa walimu kwenda kufundisha Kiswahili katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Balozi zetu zipo katika mazungumzo na vyuo vikuu kwenye maeneo yote ya uwakilishi ili Lugha ya Kiswahili iweze kujumuishwa katika mitaala ya vyuo hivyo ikiwa ni pamoja na kupata Wahadhiri wa Kiswahili kutoka Tanzania. Vyuo hivyo ni pamoja na Chuo Kikuu cha Kuwait, Chuo Kikuu cha Holon Institute of Technology nchini Israel na Chuo Kikuu cha Buraimi, nchini Oman, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Vijiji vya Msata, Kihangaiko na Pongwe Msungura kutokana na maeneo yao kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu tangu niteuliwe tena kuwa Waziri wa Ulinzi na na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake, lakini nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kuendelea kumsaidia katika nafasi hii. Niahidi kwamba nitaendelea kufanya kazi zangu kwa uwezo wangu wote, kwa uaminifu, kwa uadilifu na kwa kujituma.
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Vijiji vilivyotajwa yaani Msata, Kihangaiko, na Pongwe Msungura yapo katika Makambi mawili ya Jeshi ambayo ni RTS Kihangaiko na Msata Military Training Base katika Wilaya ya Chalinze. Serikali imeendelea na kutatua migogoro hii ya ardhi katika maeneo haya na katika mwaka 2021 ulifanyika uthamini wa awamu ya kwanza uliojumuisha Vijiji vya Msata, Pongwe Msungura na baadhi vitongoji katika Kijiji cha Kihangaiko. Uthamini awamu ya pili ulifanyika mwaka 2022 ukijumuisha vitongoji viiyosalia katika Kijiji cha Kihangaiko.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Uthamini uliofanyika mwaka 2021 iliwasilishwa katika Ofisi ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ili kukamilisha taratibu. Taratibu zitakapokamilishwa na Halmashauri ya Wilaya hii itawasilisha jedwali la malipo kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kuidhinishwa na hatimaye kufanyiwa uhakiki na malipo na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, katika uthamini uliofanywa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 2022, Wizara ya Fedha imekwishafanya uhakiki kwa Vitongoji vya Funta, Chokozeni na Kudikongo, vilivyopo katika Kijiji cha Kihangaiko kwa ajili ya kulipa fidia na malipo ya shilingi 330,788,467 yameshafanyika kwa wananchi katika Kitongoji cha Funta.
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, lakini pia na Halmashauri ya Chalinze ili kuhakikisha ulipaji wa fidia unakamilika.
MHE. SILVESTRY F. KOKA aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani kuhakikisha wazee waliopigana Vita ya Pili ya Dunia chini ya Chama cha TLC wananufaika na mali zao?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Silyvestry Francis Koka, Mbunge wa Kibaha kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mwezi Julai, 2022, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa iliunda Kamati maalum ya kuchambua na kutoa ushauri kuhusu hatma ya Askari waliopigana Vita Kuu ya Pili ya Dunia mwaka 1939 – 1945 na kuhusu mali za Chama cha Tanzania Legion & Clubs (TLC).
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini hiyo ilibaini kuwa Askari waliopigana Vita Kuu ya Dunia walikuwa 737, kati yao 57 wapo hai na 680 wamekwishafariki. Tathmini ilionesha pia kuwa TCL inazo mali zenye thamani ya Shilingi 37,366,323,048.000. Hata hivyo, baadhi ya mali hizo zina madeni na zingine zipo chini ya usimamizi au umiliki wa Taasisi nyingine na hivyo kusababisha mashaka kuhusu umiliki wake. Katika hali hii, mali zilizothibitishwa kuwa ni za TLC bila utata zina thamani ya Shilingi 15,952,574,800. Tathmini ilionesha pia kuwa, maveterani walio hai wanahitaji matunzo ikiwa ni pamoja na bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imetoa mapendekezo ya kuuza mali zisizo na utata ambazo nimezitaja za Shilingi 15,952,574,800 na kutoa fidia kwa Maveterani wote walio hai na warithi wa walio fariki. Pia kuwapatia bima ya afya Maveterani walio hai na kuwaenzi Maveterani wote kwa kujenga mnara wa kumbukumbu wa Askari wote waliopigana Vita Kuu ya Pili. Serikali inayafanyia kazi mapendekezo haya na tathmini kuhusu mali zenye utata inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, huu ndiyo mkakati wa Serikali wa kuwaenzi waliopigana Vita ya Pili ya Dunia na kuhakikisha wananufaika na mali zao.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa mpaka kati ya Kambi ya Jeshi 845 Itaka na Wananchi wa Vijiji vya Sesenga na Itewe?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Jeshi Itaka ilikuwa ni mashamba ya walowezi wa kikoloni (settlers), yaliyotwaliwa na Serikali kwa mujibu wa sheria. Mashamba hayo yaligawiwa kwa Jeshi kati ya mwaka 1980 na 1981. Mashamba hayo yalikuwa chini ya umiliki wa Jeshi la Kujenga Taifa Kambi ya Itende. Baada ya mafunzo ya JKT kusitishwa mwaka 1994, wananchi walianza kuvamia na kuendesha shughuli za kibinadamu, hususan kilimo na makazi.
Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Mwenisongole kwa kuendelea kulifuatilia suala hili kwa karibu. Kufuatia ufuatiliaji wake Wizara imeunda Timu ya Wataalam mbayo imepewa jukumu la kuangalia namna bora ya kutatua mgogoro huu. Timu hii ipo uwandani, ikishirikiana na viongozi, lakini pia pamoja na wananchi katika eneo husika. Nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge kwa heshima, awe na subira wakati tukisubiri timu hiyo ikamilishe kazi na mapendekezo yawasilishwe na timu hiyo ya wataalam. Ahsante.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Je, Serikali inatoa kauli gani kuhusu kuwasaidia wazee waliopata ulemavu wakati wa kupigana Vita ya Kagera mwaka 1979?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonesha kuwa wazee walemavu wa vita ya Kagera wapatao 272 wanalipwa pensheni ya ulemavu. Baada ya vita kumalizika Serikali iliwasaidia wapiganaji wote waliopigana vita. Wengi kati ya wapiganaji hao walipewa ajira katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza. Aidha, wapo walioshindwa kuajiriwa kutokana na sababu mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, wazee walemavu waliopigana vita ya Kagera wanaendelea kupata matibabu katika hospitali za Jeshi na wanalipwa pensheni za ulemavu kwa mujibu wa Kanuni za Pensheni na Viinua Mgongo za mwaka 1966. Wizara inaendelea kufuatilia hali halisi za wazee waliopigana vita ili kuchukua hatua stahiki. Endapo kuna wazee na walemavu waliopigana vita ya Kagera ambao hawanufaiki na huduma zinazotolewa inashauriwa wawasilishe taarifa zao kwa ajili ya uhakiki na hatimaye waweze kunufaika na huduma hizo, nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, utaratibu gani unaotumika kwa Kamandi mbalimbali nchini kuanzisha miradi ya kibiashara katika maeneo ya Kamandi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa miradi ya kibiashara Jeshini ulianzishwa kupitia Mess and Institutes ambayo ilikua na jukumu la kusimamia mabwalo (Mess) ambayo yalikuwa yanauza vinywaji na kuendesha maduka katika vikosi vya Jeshi. Baadaye utaratibu huo ulifanyiwa maboresho kadhaa yaliyopelekea kubuni na kuendesha miradi ya kibiashara Jeshini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa sasa Kamandi, Brigedi, Vikosi na Shule zinapaswa kubuni na kuandaa andiko la mradi au biashara na kuwasilisha Makao Makuu ya Jeshi kwa ajili ya kibali. Makao Makuu ya Jeshi huchambua maandiko yaliyowasilishwa kujiridhisha endapo mradi au biashara hizo, hazitaathiri majukumu ya msingi ya Jeshi. Aidha, miradi hiyo huzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira, taratibu za usajili BRELA na taratibu za Mamlaka ya Mapato Nchini.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-
Je, lini Jeshi la Wananchi litatimiza ahadi yake ya kujenga daraja la dharura katika Mto Mtitu Kata ya Ihimbo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA aljibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu ya kuendeleza na kusimamia barabara za vijijini na mijini ambayo awali yalikuwa yakitekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa yamekabidhiwa kwa Wakala wa Barabara za Vijijini Tanzania (TARURA). Hata hivyo, mwezi Julai, 2022 Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ilipokea maombi ya kujengewa daraja la dharura katika Mto Mtitu, Kata ya Ihimbo kutoka Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Kilolo Mkoani Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania ilipeleka kikundi cha Wahandisi wa Medani ambacho kilifanya uchambuzi wa madaraja ya chuma yaliyopo na kubaini kuwa lipo daraja la JWTZ la Bailey Bridge lililopo yadi za TARURA mkoani Mbeya ambalo lingefaa kujengwa katika eneo husika. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo inashauriwa kukamilisha ujenzi wa barabara ya vumbi yenye uwezo wa kupitisha magari ya tani 20 pamoja na uimarishaji wa eneo jipya la ujenzi wa daraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua changamoto ya kukosekana kwa mawasiliano baina ya wananchi wa Kata ya Ihimbo na maeneo mengine, Wizara inapendekeza kukutana na Mheshimiwa Mbunge pamoja na Ofisi ya TARURA Wilaya ya Kilolo ili kutatua changamoto hiyo.
MHE. MAIMUNA A. PATHAN aliuliza: -
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi waliopisha upanuzi wa maeneo ya Jeshi 843 KJ Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maimuna Ahmad Pathan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kikosi cha Jeshi cha 843 JKT Nachingwea, kilichopo Mkoani Lindi kilianzishwa mwaka 1964. Kumbukumbu zinaonesha eneo husika lilikuwa ni moja ya mashamba ya karanga yaliyokuwa yanamilikiwa na Mzungu aliefahamika kwa majina ya John Molam. Shamba hilo baadae lilitaifishwa na Serikali na kutumika kwa matumizi ya Kijeshi kwa ajili ya kuimarisha Ulinzi katika mipaka ya Kusini mwa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, mwaka 1964 wakati Jeshi wanakabidhiwa eneo hilo, upande wa mpaka wa Mashariki kikosi kilipakana na Kijiji cha Naipingo, baadaye eneo la Jeshi katika mpaka wa upande huo lilikatwa na kuanzishwa Kijiji cha Mkukwe ambacho kilisajiliwa Mwaka 1999. Kwa sasa kikosi kinapakana na Kijiji cha Mkukwe katika upande huo wa Mashariki. Upimaji mpya wa kurekebisha mipaka uliofanyika mwaka 2021 na Hatimiliki yake imetolewa 2023.
Mheshimiwa Spika, kwa mantiki hiyo hakuna upanuzi uliofanywa wa kuongeza eneo la kikosi, bali eneo la Jeshi ndilo lilipunguzwa na kuanzisha kijiji cha Mkukwe Mwaka 1999. Nashukuru.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, utaratibu gani unaotumika kwa Kamandi mbalimbali nchini kuanzisha miradi ya kibiashara katika maeneo ya Kamandi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Jumah Soud, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, uendeshaji wa miradi ya kibiashara Jeshini ulianzishwa kupitia Mess and Institutes ambayo ilikua na jukumu la kusimamia mabwalo (Mess) ambayo yalikuwa yanauza vinywaji na kuendesha maduka katika vikosi vya Jeshi. Baadaye utaratibu huo ulifanyiwa maboresho kadhaa yaliyopelekea kubuni na kuendesha miradi ya kibiashara Jeshini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu wa sasa Kamandi, Brigedi, Vikosi na Shule zinapaswa kubuni na kuandaa andiko la mradi au biashara na kuwasilisha Makao Makuu ya Jeshi kwa ajili ya kibali. Makao Makuu ya Jeshi huchambua maandiko yaliyowasilishwa kujiridhisha endapo mradi au biashara hizo, hazitaathiri majukumu ya msingi ya Jeshi. Aidha, miradi hiyo huzingatia taratibu za uhifadhi wa mazingira, taratibu za usajili BRELA na taratibu za Mamlaka ya Mapato Nchini.
MHE. ESHTER E. MALLEKO aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuhusisha Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika kulinda miradi mikubwa ya kimkakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alIjibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Edwin Malleko, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020. Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeendelea kulilinda Taifa letu pamoja na Miradi Mikubwa ya Kimkakati kwa maslahi mapana ya Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Makao Makuu ya Jeshi imekuwa ikitoa wataalam mbalimbali wanaoungana na wataalam wa vyombo vingine vya Usalama ili kuhakikisha miradi ya kimkakati inakuwa salama wakati wote, nashukuru.
MHE. MUSTAFA MWINYIKONDO RAJAB aliuliza:-
Je, lini Serikali itarejesha huduma za afya zilizokuwa zikitolewa kwa wananchi na zahanati ya jeshi, Kambi ya Jeshi Kisakasaka?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mustafa Mwinyikondo, Mbunge wa Dimani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Kisakasaka ni Kiteule cha 672 Rejimenti ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tazania ambayo ina kikundi kidogo cha Maafisa na Askari. Kiteule hiki hutoa huduma za matibabu za msingi zinazojumuisha madawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa Wanajeshi waliopo katika Kiteule hicho. Maafisa na Askari waliopo katika Kiteule hicho wanapozidiwa hupelekwa katika Zahanati ya Kikosi Mama iliyopo maeneo ya Welezo umbali wa kilometa 17.
Mheshimiwa Spika, hapo awali Kiteule hiki kilikuwa kinatoa huduma za afya kwa Wanajeshi na wananchi, Huduma kwa wananchi zilisitishwa mwaka 2010 kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za miundombinu kutokukidhi kutoa huduma kwa wananchi wengi na upungufu wa watalaam wa tiba.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika eneo la Kisakasaka kipo Kituo cha Afya cha Fuoni Kibondeni cha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kilichoanzishwa mwaka 2004, ninapenda kuwaomba wananchi waendelee kupata huduma kupitia kituo hicho wakati Wizara inatekeleza mkakati wa kuimarisha huduma za afya Jeshini, kwa kufanya maboresho katika hospitali za kanda, vituo vya afya na zahanati zilizopo katika vikosi chini ya kamandi mbalimbali nchini, zikiwemo zahanati za Jeshi zilizopo Zanzibar, ahsante.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Je, ni kwa kiasi gani Sheria ya Vijana kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria inatekelezwa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa ya Mwaka 1964 imeweka ulazima wa vijana wa Tanzania wanaomaliza kidato cha sita kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka mmoja kwa mujibu wa sheria. Mafunzo hayo huwajengea vijana uzalendo, ukakamavu na uhodari.
Mheshimiwa Spika, mafunzo hayo yalisitishwa mwaka 1964 kutokana na hali ngumu ya uchumi iliyoikumba Dunia. Kutokana na umuhimu wa mafunzo haya, Serikali iliyarejesha tena hapo mwaka 2013 na sasa hufanyika kwa miezi mitatu. Kwa mwaka jana au kwa mwaka huu mwaka 2023 vijana idadi 260,061 ambayo ni sawa na asilimia 59 wameweza kujiunga na mafunzo haya. Serikali inaendelea kuongeza miundombinu lengo ikiwa ni kuwachukua vijana wote wanaomaliza kidato cha sita kufikia mwaka 2025/2026.
MHE. COSATO D. CHUMI aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kuiongezea bajeti JKT ili kuiwezesha kuchukua wahitimu wote wa Kidato cha Nne na Sita wenye sifa za kujiunga na JKT?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cosato David Chumi, Mbunge wa Mafinga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kutoa mafunzo kwa wahitimu wote ambao wana sifa ya kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea na kwa mujibu wa sheria. Kwa sasa, vijana wote hawapati fursa ya kuhudhuria mafunzo hayo kutokana na ufinyu wa bajeti. Mpango uliopo ni kulijengea Jeshi la Kujenga Taifa uwezo ili liweze kuchukua vijana wengi zaidi wa kujitolea na wahitimu wote wa kidato cha sita, ambao wanastahili kujiunga na mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria, kwa kuongeza bajeti ili kuboresha mafunzo na kuongeza idadi ya makambi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, ili kuongeza miundombinu ya makambi na bajeti ya kuendesha mafunzo ya JKT kadri uwezo wa Serikali utakavyoruhusu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi baina ya Jeshi la Wananchi na Wananchi California Mtaa wa Mbae Mashariki, Mkoani Mtwara?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linalozungumziwa lipo katika Kikosi cha Jeshi cha 665 kilichopo Naliendele Mkoani Mtwara. Eneo hilo linalokizunguka Kikosi hicho lilivamiwa na wananchi na mwaka 2014 wananchi walifungua shauri Mahakamani wakidai kumiliki eneo hilo. Hukumu ya shauri hilo ilitolewa mwaka 2021 ambapo Mahakama ilitupilia mbali madai hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupitia Bunge lako Tukufu kuwaomba wananchi kuelewa umuhimu wa maeneo ya jeshi kwa maslahi mapana ya ulinzi na usalama wa Taifa na kutoa ushirikiano. Aidha, naomba wananchi walio ndani ya eneo hilo la jeshi waweze kuondoka kwa kuzingatia taratibu na sheria.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata ya Oldonyosambu ambao maeneo yao yalichukuliwa na Jeshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Eneo la Oldonyosambu kuna viteule viwili vya Jeshi ambavyo ni Kiteule cha Kikosi cha Oljoro na Kiteule cha Kikosi cha Rada. Katika maeneo hayo mawili, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hatujapokea taarifa ya kuwepo kwa maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa na Jeshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, endapo kuna malalamiko yoyote kuhusu maeneo ya wananchi kuchukuliwa na Jeshi, Wizara ipo tayari kupeleka wataalam katika eneo hili ili kushughulikia malalamiko hayo.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, kweli kuna wazee wanaodai haki zao kutokana na ushiriki wao kwenye Vita vya Dunia au Jeshi la KAR?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wapo wazee waliopigana Vita ya Pili ya Dunia (1939 - 1945) wakiwa askari wa Jeshi la KING’S AFRICAN RIFLES (KAR) lililokuwa chini ya Serikali ya Kikoloni ya Uingereza. Haki wanazodai zinahusiana na mali walizoachiwa na Serikali ya Uingereza mara baada ya utawala wao Tanganyika kukoma.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuongeza nafasi za ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara. Utaratibu wa kuandikisha Jeshi askari wapya umefafanuliwa kwenye Kanuni ya 5 ya Kanuni ya Majeshi ya Ulinzi Juzuu ya Kwanza (Utawala). Aidha, Serikali imeondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ongezeko la idadi ya ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne hutegemea bajeti inayotengwa kwa mwaka husika. Jeshi huandikisha askari wapya baada ya kupewa maelekezo na idadi ya nafasi kulingana na uwezo wa bajeti. Nafasi hizo hugawanywa kulingana na mahitaji ya kitaaluma na ujuzi.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kufanya mafunzo ya mgambo kuwa sehemu ya mafunzo kwa vijana wanaokosa nafasi ya kujiunga na JKT?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Nyasa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Akiba (Jeshi la Mgambo) lilianzishwa kwa Sheria ya Jeshi la Akiba Na.2 ya mwaka 1965 ili kuandaa nguvu ya akiba kwa ajili ya kusaidia Jeshi la Kudumu wakati wa vita, operesheni, majanga na kuuandaa umma wa Watanzania ili waweze kuelewa kuwa dhana ya ulinzi wa Taifa ni jukumu la kila Mtanzania. Vijana 600 kutoka kila Mkoa hupata mafunzo kila mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa kupitia Sheria ya Jeshi la Kujenga Taifa Na.2, Sura ya 193 ya mwaka 1964 ambayo ilirejewa mwaka 2002 kwa malengo ya ulinzi wa Taifa, kujenga uzalendo na mshikamano, uzalishaji mali na kutoa elimu ya kujitegemea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa vyombo hivyo kulilenga mahitaji tofauti. Kwa muktadha huo, hakuna mpango wa kuyafanya mafunzo ya Jeshi la Akiba kuwa sehemu ya mafunzo ya vijana wanaokosa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Aidha, vijana wenye sifa wanaruhusiwa kuomba kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Akiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha
MHE. MAIDA H. ABDALLAH aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja ya kuanzisha Mfumo wa Mafunzo yanayohusu uzalendo, ufundi, kilimo na ufugaji kwa vijana wanaoishi karibu na Kambi za Jeshi/ JKT?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa chini ya kifungu namba 3(2) cha Sheria Na. 16 ya Mwaka 1964 kwa lengo la kuwajengea vijana moyo wa uzalendo, misingi ya kujitegemea na malezi kwa vijana wa Kitanzania pamoja na kuwafundisha umoja, mshikamano, ukakamavu na kuwa tayari kulitumikia Taifa lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua uhitaji wa sasa wa vijana kupewa mafunzo ya ukakamavu na stadi za kazi imeamua kufanya tathmini ya kina juu ya uwezo wa makambi yetu kuchukua idadi kubwa ya vijana, imeundwa Kamati ya Tathmini ambayo imeanza kazi na itakamilisha tathmini yake Juni, 2025 ambapo hata hili la vijana wanaozunguka makambi litakuwa ni miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa kazi.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwaajiri vijana wa JKT walioshiriki ujenzi wa ukuta wa Mererani, Ikulu na maeneo mengine?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Kujenga Taifa lilianzishwa mwaka 1963 kwa lengo la kutoa mafunzo ya uzalendo, ulinzi na malezi kwa vijana wa Kitanzania. Mafunzo hayo, yanalenga kuwafundisha umoja na mshikamano, ukakamavu na kuwa tayari kulitumikia Taifa lao wakati wote. Katika mafunzo hayo, vijana hufundishwa pia stadi mbalimbali za kazi na maisha. Lengo ni kuwawezesha vijana hao kuwa na uwezo wa kujitegemea baada ya mafunzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara, kama ilivyofafanuliwa katika kanuni ya tano ya Kanuni za Majeshi ya Ulinzi, Juzuu ya Kwanza ya Utawala. Hivyo, vijana wote wanaojiunga na JKT huandikishwa kwa kufuata utaratibu. Hapa wanaojiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, wanaoandikishwa, huandikishwa kwa kufuata utaratibu huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2022, jumla vijana 5,744 waliokuwa na sifa ikiwa ni pamoja na wale walioshiriki katika ujenzi wa ukuta wa Mererani na Ikulu waliandikishwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kufuata utaratibu niliouelezea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA K.n.y. MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuongeza nafasi za ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cherehani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania huandikisha askari wapya kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo yanayotolewa mara kwa mara. Utaratibu wa kuandikisha Jeshi askari wapya umefafanuliwa kwenye Kanuni ya 5 ya Kanuni ya Majeshi ya Ulinzi Juzuu ya Kwanza (Utawala). Aidha, Serikali imeondoa utaratibu wa kuandikisha ajira kwa vijana wanaohitimu elimu ya darasa la saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ongezeko la idadi ya ajira na mafunzo jeshini kwa vijana wanaohitimu kidato cha nne hutegemea bajeti inayotengwa kwa mwaka husika. Jeshi huandikisha askari wapya baada ya kupewa maelekezo na idadi ya nafasi kulingana na uwezo wa bajeti. Nafasi hizo hugawanywa kulingana na mahitaji ya kitaaluma na ujuzi.