Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Stergomena Lawrence Tax (27 total)

MHE. USSI SALUM PONDEZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri swali moja la nyongeza kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, amenijibu kuwa Serikali ina mpango wa kufanya upimaji na kufanya tathmini. Je, wakati itakapofika kufanya tathmini na upimaji, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari na mimi niambatane naye kwenda kwenye zoezi hilo? (Makofi/Kicheko)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Mheshimiwa Mbunge ni mdau wetu na tutakuwa tayari kuongozana naye wakati zoezi hili likiendelea. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Wananchi wa Bugosi na Kenyambi kule Tarime Mjini walichukuliwa ardhi yao na Jeshi la Wananchi wa Tanzania tangu 2008, na jeshi hili au Serikali ilifanya tathmini mara ya kwanza 2013, 2017 wakafanya tathmini tena, 2019 na mara ya mwisho na ulitilia mkazo hapa Bungeni walikwenda kufanya uhakiki Juni, 2021 na wakatoa namba ya malipo na wakaahidi kwamba kufikia Agosti, 2021 watakuwa wamelipa lakini mpaka sasa hivi hawajawalipa wananchi hawa.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujua ni lini sasa wananchi hawa wa Kenyambi na Bugosi watalipwa fidia zao, ili wapishe Jeshi la Wananchi wa Tanzania waende sehemu zingine kufanya makazi na shughuli za kimaendeleo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa Esther Matiko kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika mkakati huo wa miaka mitatu tayari tumeshafanya tathmini na uhakiki katika maeneo yote isipokuwa maeneo ya Zanzibar ambayo ndiyo tutayafanyia quoter hii. Kinachoendelea sasa baada ya huu utathmini ni kufanya uhakiki na uhakiki unaendelea katika maeneo yote ambayo yamefanyiwa tathmini na uhakiki ili tukishakamilisha uhakiki taratibu nyingine zitafuata. (Makofi)
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni miaka mingi sasa toka ukoloni vijana wetu wanaoajiriwa na Jeshi la Kujenga Taifa wanapewa miaka Sita kabla ya kuolewa au kuoa. Kwa kuwa, magonjwa yamekuwa mengi na kwa kuwa stress za Askari wetu zimekuwa nyingi.

Je, ni lini Serikali itapunguza muda huu wa miaka Sita kuwa miaka Mitatu au Miwil?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni muda sasa tunapeleka vijana wetu JKT tunapeleka vijana 2,000 au 1,000 wanachukuliwa labda 50 wanaajiriwa wengine wanarudi nyumbani. Je, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango mkakati wa kuandaa vijana wanaorudi nyumbani kuwapa ufundi wa kutosha na saikolojia ili wasiwe panya road? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Getere kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaanza kwa kumpongeza kwa kuwa mdau wa karibu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na kuwatetea wapiganaji wetu. Swali lake la kwanza ambalo ni kuhusu umri, napenda kwanza nitoe ufafanuzi kwamba ni kweli kwamba Maafisa na Maaskari wenye elimu ya darasa la saba hadi kidato cha sita na wenye Stashahada wao ndiyo hukaa miaka Sita kabla ya kuolewa. Yapo makundi mengine kama wenye shahada ya kwanza wao hukaa kama makapera kwa miaka Minne na wenye Shahada ya Uzamili, wao hukaa kwa miaka mitatu na wenye Shahada ya Uzamivu wenyewe hawana muda wa kukaa kwenye ukapera na hii ni kutokana na aina ya majukumu ambayo maaskari hawa wanafanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Askari ambao nimewataja katika kundi la kwanza hao huwa ni vijana wadodo wanajiunga wakiwa na umri wa miaka 18 na kuendelea, kwa hiyo huhitaji kwanza kukomaa. Majukumu ya Jeshi ni majukumu mahususi lakini pia hawa ndiyo wanategemewa kama wapiganaji kwa hiyo huendelea na kozi mbalimbali na kuhakikisha kwamba wako imara wakati wote. Kwa hiyo, miaka hii Sita iliyowekwa imewekwa baada ya kufanya uchunguzi lakini pia kuzingatia vigezo mbalimbali. Kwa hiyo, kama tunaweza kubadilisha sidhani kama hilo linawezekana kwa sasa kwa sababu utafiti ulifanyika na lazima iwe hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii pia inatokana na aina ya majukumu ambayo wanafanya. Wengine wanapoajiriwa kama Madaktari huenda moja kwa moja kufanya hiyo kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ambalo linahusiana na vijana wanaokwenda JKT kwamba ni wengi lakini wanaoajiriwa ni wachache. Kwanza ninapenda kueleza kwamba madhumuni ya vijana kujiunga na JKT ni kuwajengea uzalendo, kuwajengea ukakamamu lakini kuwapa stadi mbalimbali ili baada ya hapo waende kujiajiri. Madhumuni siyo kutoa ajira kwa vijana hawa, hilo linafanyika vijana hawa wanafundishwa stadi mbalimbali ili baada ya hapo waweze kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tuna mpango gani, ni kweli nasi tumeona kwamba pamoja na kuwapa stadi mbalimbali bado kuna umuhimu kuwawezesha vijana hawa kujitegemea. Kwa hiyo, tumeanza kufanya kazi hii na tayari katika mpango wa block farming kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, tutaona jinsi gani tutaweza kuchukua baadhi ya vijana, lakini bado tunaendelea kulichakata suala hili tuweze kuja na program nzuri zaidi ambazo zitawawezesha vijana hawa kujiajiri baada ya kupata stadi ambazo tunawapatia. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali la kwanza; kwa kuwa, Waziri amesema tayari mipango ya kufufua Kambi ile inaendelea na sasa hivi hali ya usalama upande wa kusini hasa upande wa Msumbiji sio nzuri katika Vijiji vya Wenje, Lukala, Nasomba, Makandi na Kazamoyo watu hawa wanaishi kwa kutokuwa na amani. Je, haoni sasa ni muhimu kuweka angalau makambi ya temporary ili kurejesha amani ya wananchi wa vijiji hivyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa vijiji hivyo kwa sasa ulinzi umekabidhiwa kwa mgambo ambao wako 30 katika vijiji hivyo na wanapewa sh.50,000/= kwa mwezi na Halmashauri.

Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kuwalipa mshahara mgambo wale ili waweze kuendelea kulinda mipaka?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hali ilivyo katika mipaka yetu yote ikiwa ni pamoja na mpaka wa Kusini na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha ulinzi, hatukai tu tukisubiri kambi. Kambi itakuja lakini hatua za kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo zinaendelea na ulinzi umeimarishwa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu malipo, kwa mgambo kuwa na mishahara upo utaratibu unaotumika kulipa Jeshi la Mgambo na utaratibu huo utaendelea kutumika. Ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, suala hili la Usule limekuwa ni la muda mrefu sana na hii mambo ya uhakiki na hawa akina mama watatu watalipwa fedha zao imekuwa ni muda mrefu sasa. Hebu Serikali itoe majibu ya uhakika, lini hasa hawa wamama watapata fedha zao. (Makofi)

Swali langu la pili, katika Kijiji hiki cha Usule kuna ranch ya Kalunde ambayo Wanajeshi pia walichukuwa maeneo hayo kwenye kaya 14 zaidi ya miaka kumi sasa watu hawa wanaambiwa wamefanyiwa uhakiki lakini hawajalipwa fedha zao. Serikali itoe kauli ya hawa wananchi 14 pia katika ranch ya Kalunde ni lini mtawapa fedha zao ili waende kwenye maeneo mengine waweze kufanya shughuli zao za maendeleo. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, migogoro ya ardhi ina mchakato na kama unavyoona Mheshimiwa Mbunge mchakato umeshafika ukingoni, tumekwishafanya uhakiki vitabu vimeshaandaliwa na tayari imeshakubalika na fedha zimekwishatengwa. Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Mbunge na wananchi wavute subra kidogo ili waweze kulipwa, kwa sababu fedha tayari ziko katika bajeti ya mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili naomba nilijibu kwamba hii ni kero mpya, kwa hiyo tunaipokea na tutaifanyia kazi na kama itahitajika tutaingiza katika mpango wetu wa kutatua migogoro unaoendelea mpango wa miaka mitatu.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Madam Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la dogo nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hali iliyoko katika Kijiji cha Usule Mkoani Tabora inafanana kabisa na hali iliyoko Kjiji Tondoroni Wilaya ya Kisarawe, Kata ya Kiluvya Mkoani Pwani, sasa napenda kujua ni lini Serikali mtawalipa fidia wananchi wale au kurudisha yale maeneo ili waweze kuyaendeleza. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nitalijibu kwa ujumla nikianza kwa kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamekwisha niona kufuatilia migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

Mhesihimiwa Spika, niseme kwamba tunao mpango wa kusuluhisha hii migogoro baina ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania na wananchi ambao umejumuisha maeneo 152 yanayohusisha Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Mpaka sasa tumekwisha pima maeneo 86, tumekwisha fanya uthamini wa maeneo 13 na upimaji unaendelea katika maeneo 66, na mpango huu ni wa miaka Mitatu.

Mheshimiwa Spika, ninaomba baada ya kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, maana wengi sana wamekwisha nifuata kwa ajili ya migogoro katika maeneo yao, nawashukuru na kuwapongeza ila niwaombe tu wavute subira tuweze kukamilisha hii michakato inayoendelea. Ahsante.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mgogoro kama huo huko vilevile katika Jimbo la Kigamboni katika Kata ya Kimbiji eneo la Kijaka.

Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro huo.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika ahsante sana. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ndugulile kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana kwa kulifuatilia suala hili kwa karibu, kwa niaba ya wananchi wa Kigamboni na ninapenda kumfahamisha kwamba mgogoro huu tayari na wenyewe unashughulikiwa na upimaji ulishafanyika, kwa hiyo tunasubiri tupate hati na baada ya hapo hatua zinazofuata zitaendelea. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza mawali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niishukuru sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa kuonesha dhamira ya kushughulikia mgogoro huu ambao ulikuwa wa muda mrefu. Sasa kwa kuwa hatua ya kwanza ya kuanza kulipa malipo haya kwa Kitongoji cha Funta zaidi ya milioni 330 imeleta kama sintofahamu kwa wananchi wa Vitongoji vya Chokozeni na Kudikongo katika Kijiji cha Kihangaiko hicho hicho. Je, Serikali haioni ipo haja kwa vitongoji hivi viwili vya Kijiji kimoja cha Kihangaiko walipwe fidia yao kwa mwaka huu wa fedha unaoendelea?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa wapo baadhi ya wananchi waliotoa maeneo wa Vijiji vya Msata, Kihangaiko na Pongwe Msungura hawakupimiwa na kwa kuwa imeanza kulipa fidia. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wale wananchi ambao bado hawajapimiwa ili waweze kupata matumaini na waweze kuyaachia yale maeneo kuliko wanavyokwenda kufanya shughuli na wanakumbwa na matatizo makubwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa swali la kwanza ambalo ni kwamba kuna hawa ambao hawajalipwa, napenda tu kutoa rai kwa wenzetu ambao ni Halmashauri ya Chalinze kukamilisha taratibu na kuwasilisha jedwali ili taratibu ziendelee na ziweze kukamilika. Kama alivyosema ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba migogoro hii inakamilishwa na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wataona tulikuwa na migogoro 87 katika mpango wetu wa mwaka 2020 - 2023 na kati ya migogoro hiyo 87 migogoro 74 imekwishatatuliwa. Kwa hiyo hii 13 iliyosalia ni dhamira yetu kuhakikisha kwamba tunaikamilisha mwaka huu wa fedha kwani hata mpango tuliokuwa tumejiwekea kukamilisha mwaka 2023 umeshapita, tumeongeza mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, kwa hao wengine ambao wamejitokeza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kama hii migogoro mipya iko sehemu ya mpango wetu na kama haiko sehemu ya mpango wetu tutaona tunaiingiza namna gani. Jambo la kwanza ni muhimu tuende tukajiridhishe kwamba haya maeneo anayoyataja ni maeneo ambayo yapo katika maeneo ya vikosi vya Jeshi. Tutafanya hivyo Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wewe.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa vile changamoto iliyoko katika Halmashauri ya Chalinze inafanana na changamoto iliyoko katika Halmashauri ya Bagamoyo katika Kata ya Mapinga katika eneo la Kiharaka. Je, Serikali lina mpango gani kulipa wananchi wa eneo la Kiharaka katika Kata ya Mapinga? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema tunao mpango ambao umejumuisha migogoro mingi, kwa hiyo, kama hili eneo la Kiharaka ni sehemu ya mpango huu basi litakamilishwa katika mpango huu wa fedha, lakini kadri tulivyoendelea kutatua hii migogoro, migogoro mipya pia imekuwa ikijitokeza, kwa hiyo, kama huu ni mgogoro mpya tutaujumuisha katika mpango wetu baada ya kujiridhisha kwamba ni eneo ambalo lina mgogoro na Jeshi, ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, moja kati ya maeneo ambayo yanaleta changamoto ni eneo la Kata ya Tambukareli ambapo ni eneo la Jeshi na kuna makaburi ya wananchi ambayo yapo kwenye eneo la Jeshi.

Je, Serikali mna mpango gani wa kwenda kufanya mazungumzo na wananchi ambao wamezika ndugu zao kwenye maeneo yale ili waweze kuendelea kufanya Ibada kwa marehemu waliotangulia mbele ya haki? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia suala hili kwa karibu sana. Hata kabla, huko nyuma tulishazungumza kuhusu suala hili, hili ni miongoni mwa maeneo ambayo yanafanyiwa kazi. Kwa hiyo, nikuhakikishie tu kwamba tutaendelea kulifanyia kazi ili tuweze kupata suluhu yake, ahsante. (Makofi)
MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu hayo mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mali hizo zenye thamani ya takribani shilingi bilioni 37 ni mali ya Chama cha Wazee Waliopigana Vita ya Pili ya Dunia (TLC) ambazo wana haki nazo pamoja na watoto wao kwa mujibu wa katiba yao. Mali hizo zimekodishwa kwa muda mrefu na pesa zinakusanywa, mfano ni Upanga pamoja na kule Tarime, lakini fedha hizo hazijawafikia wale wazee ambao wanaishi kwa shida na wengine wanafariki hata kwa kukosa chakula: Je, ni lini Serikali itahakikisha fedha hizo zinawafikia wazee hao wafaidike nazo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kamati ya Serikali iliyokaa kwenye majadiliano mbalimbali haijawahusisha wazee hao wala watoto wao: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kupanga siku maalum ambayo atakutana na Kamati ya Wazee na Watoto hao ili washiriki kufikia maamuzi hayo ambayo Serikali imeyafikia?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa ku-declare kwamba baba yangu pia ni mmoja wa veteran waliopigana Vita ya Pili ya Dunia na sasa hivi ana miaka 103, ana akili timamu na anaulizia sana mali hizo.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tathmini imeshafanyika na sasa tuko kwenye hatua ya kuhakikisha kwamba tunawafidia wazee hawa. Kwa hiyo, hili linaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu tathmini ya kutowahusisha wazee waliopigana vita na watoto wao, tathmini hii ilikuwa pana na ilihusisha taasisi mbalimbali za Serikali. Bahati mbaya viongozi wa Chama cha TLC wote wamefariki, alikuwa amebaki mmoja wakati tathmini inaanza, lakini naye kwa sasa ameshafariki, hata hivyo tulihusisha baadhi ya familia ambazo tuliweza kuzifikia. Kwa hiyo, tathmini iliwahusisha wadau mbalimbali, nafikiri ikiwa nni pamoja na wewe Mheshimiwa Mbunge, tuliweza kupata mawazo yako kwa nyakati mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kuna wanajeshi wengi wastaafu waliopigana tokea baada ya uhuru, wamestaafu na mpaka leo wako hai, lakini pensheni zao za mwezi ni ndogo sana: Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwarekebishia ili waweze kukidhi maisha yao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli wapo watumishi wa umma ikiwa ni pamoja na wanajeshi wastaafu ambao wamekuwa wakilalamikia pensheni zao kuwa ndogo. Hili ni suala ambalo linafanyiwa kazi kwa pamoja na sekta nyingine zinazohusika na masuala ya pensheni. Kwa hiyo, tutaendelea kuliangalia na kuona ni jinsi gani linaweza kufanyiwa kazi kwa kuzingatia umuhimu wa kazi ambayo wanajeshi hao walifanya na pia kwa kuzingatia uhalisia wa bajeti ya Serikali yetu, ahsante.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri na niko tayari kuvuta subira kusubiri hiyo tume itakayotuletea majibu ila nilikuwa nina ombi moja kwa Mheshimiwa Waziri, je, tume hiyo itakapomaliza kazi, yuko tayari kwenda na mimi Mbozi kuzungumza na wananchi wa hivyo vijiji na kutoa majibu kwa wananchi hao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kama nilivyokwishamuahidi Mheshimiwa Mbunge, tumeshazungumza suala hili mara nyingi na nathibitisha tu kwamba, niko tayari kwenda kuongea na wananchi wake. (Makofi)
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na nimpongeze sana kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kama mnavyojua kwamba, baadhi ya Kamandi au Kambi kumekuwa na tabia ya ukataji wa miti na uondoaji wa misitu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu. Sasa, nilikuwa naomba tu kujua Mheshimiwa Waziri, wana mwongozo gani wa kushirikiana na Taasisi za Idara za Mazingira na Misitu hasa kule Zanzibar, ili kuona kwamba miradi hii ikiibuliwa na ikitekelezwa basi haiathiri mazingira?

Swali namba mbili, je, Kamandi au Wizara ina utaratibu gani wa kuwa na mwongozo wa mapato na matumizi kama vile walivyo wenzetu wa Jeshi la Polisi ule mpango wa Tuzo na Tozo, ili kuhakikisha kwamba, mapato yanayopatikana yanatumika katika njia ya ufanisi zaidi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, miradi hii huzingatia pia taratibu za uhifadhi wa mazingira. Kwa hiyo, tunafuata mwongozo wa Serikali kuhakikisha kwamba, taratibu za uhifadhi wa mazingira zinazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mwongozo wa mapato na matumizi; Miradi hii inaendeshwa kwa kuzingatia kwanza inachambuliwa na Makao Makuu ya Jeshi na umewekwa utaratibu ambao pesa zote zinazopatikana zinafuata Taratibu za Matumizi ya Fedha katika Taasisi za Umma. Kwa hiyo, hakuna wasiwasi kwamba, pesa hizi labda zinapotea na nipende kutoa pongezi kubwa sana kwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kwa kazi kubwa mabyo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi tulikuwa na ukwasi lakini miradi hii imesaidia katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Jeshi. Kwa hiyo, nawapongeza sana Jeshi letu na nikuhakikishie kwamba, taratibu na matumizi ya fedha haya yanafuata taratibu zote, hata audit huwa zinafanywa, ahsante sana.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na nimpongeze sana kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, kama mnavyojua kwamba, baadhi ya Kamandi au Kambi kumekuwa na tabia ya ukataji wa miti na uondoaji wa misitu ambayo imekuwepo kwa muda mrefu. Sasa, nilikuwa naomba tu kujua Mheshimiwa Waziri, wana mwongozo gani wa kushirikiana na Taasisi za Idara za Mazingira na Misitu hasa kule Zanzibar, ili kuona kwamba miradi hii ikiibuliwa na ikitekelezwa basi haiathiri mazingira?

Swali namba mbili, je, Kamandi au Wizara ina utaratibu gani wa kuwa na mwongozo wa mapato na matumizi kama vile walivyo wenzetu wa Jeshi la Polisi ule mpango wa Tuzo na Tozo, ili kuhakikisha kwamba, mapato yanayopatikana yanatumika katika njia ya ufanisi zaidi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, miradi hii huzingatia pia taratibu za uhifadhi wa mazingira. Kwa hiyo, tunafuata mwongozo wa Serikali kuhakikisha kwamba, taratibu za uhifadhi wa mazingira zinazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mwongozo wa mapato na matumizi; Miradi hii inaendeshwa kwa kuzingatia kwanza inachambuliwa na Makao Makuu ya Jeshi na umewekwa utaratibu ambao pesa zote zinazopatikana zinafuata Taratibu za Matumizi ya Fedha katika Taasisi za Umma. Kwa hiyo, hakuna wasiwasi kwamba, pesa hizi labda zinapotea na nipende kutoa pongezi kubwa sana kwa Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kwa kazi kubwa mabyo wameifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kipindi tulikuwa na ukwasi lakini miradi hii imesaidia katika kutekeleza majukumu ya msingi ya Jeshi. Kwa hiyo, nawapongeza sana Jeshi letu na nikuhakikishie kwamba, taratibu na matumizi ya fedha haya yanafuata taratibu zote, hata audit huwa zinafanywa, ahsante sana.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza ambalo linaendena na pongezi kwa Serikali kurejesha mafunzo hayo.

Mheshimiwa Spika, swali langu; je, kwa kuwa vijana wengi wamekuwa na mwitikio mkubwa sana wa kupenda kujiunga na mafunzo ya JKT lakini nafasi hazitoshi kwa wale wa kidato cha sita wanaomaliza na wale wa kidato cha nne ambao wana mafunzo ya ziada kama ya ufundi na kadhalika.

Je, ndani ya mifumo ya Serikali iko tayari kuongezea nguvu Jeshi la Kujenga Taifa ili kila kijana mwenye sifa aweze kupata nafasi hiyo kwa nia ile ile ya kumjengea ukakamavu na uhodari katika utendaji kazi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cosato David Chumi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mwitikio umekuwa mkubwa na Jeshi la Kujenga Taifa tumekwishaandaa mpango wa utekelezaji utakaowezesha kuwachukua vijana wengi zaidi. Utekelezaji wa mpango huu utatuwezesha kuwachukua vijana wengi lakini pia utategemea upatikanaji wa rasilimali. (Makofi)
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa condition hii ya kupita JKT na Serikali imekiri kwamba uwezo wa kuwachukua watu wote haupo lakini recently tumekuwa tunaona ajira nyingi zinazotangazwa zimeweka kigezo cha kwamba kijana awe amepita JKT. Kwa hiyo vijana wengi wanatamani waingie kwenye hizi ajira lakini kigezo cha kupitia JKT kinawanyima fursa na hawatendewi haki;

Je, hatuoni sasa ni wakati muafaka kwa Serikali kuondoa kigezo cha kupita JKT mpaka pale itakapokuwa tayari kuwahudumia watu wote ili ushindani uweze kuwa sawa?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba lalamiko hili limeshasikika, na kama tulifufatilia Taarifa ya Tume ya Jinai ni moja ya mapendekezo yaliyotolewa na ni pendekezo linalofanyiwa kazi na Serikali. (Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali kimsingi Jeshi la Kujenga Taifa wao wanapokea vijana kulingana na bajeti waliyotengewa. Kwa hiyo, swali langu kimsingi nilikuwa nimelielekeza Wizara ya Fedha, kuona kwa namna gani itawaongezea bajeti JKT ili ichukue vijana wengi kadri inavyowezekana. Kwa hivyo, sitakuwa na swali la msingi kwa Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, tunaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha ili kuongeza bajeti kwa ajili ya makambi pia uendeshaji wa Jeshi la Kujenga Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nilifahamishe Bunge lako Tukufu kwamba, tumekwishapokea maelekezo kutoka kwenye Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya kufanya tathmini, ili kuweza kujua ni kiasi gani kinahitajika, miundombinu kiasi gani inatakiwa ili tuweze kuwachukua vijana wote. Tathmini hii inaendelea, tumekwishatoa taarifa kwamba itakamilika Mwezi wa Sita mwaka huu na baada ya hapo, tutakuja na mpango mkakati ambao utaainisha mahitaji yote na haya tutayafanya kwa kushirikiana na Wizara ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tukikamilisha tutaleta taarifa kuonesha kwa ujumla wake ni kiasi gani kinahitajika, tumejipanga namna gani na tutaweza kuwachukua vijana hawa kwa utaratibu gani hatua kwa hatua. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri, kwa majibu mazuri. Nina swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo tajwa, lina wanajeshi zaidi ya 10 wapo kwenye maeneo hayo na wamejenga nyumba na wana hatimiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu, ni lini Serikali itakwenda kufuta hati zile, kwa sababu wanajeshi wale wanakuwa wanawapiga wananchi kwenye maeneo mengine na kuwavunjia nyumba ambazo zimejengwa na wanajeshi pale ambazo zina hati kwenye eneo la Jeshi, bado wanaendelea kukaa?



Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini Mheshimiwa Waziri tutaongozana kwenda kwenye eneo husika na wewe ukajionee hali halisi ili tuweze kutatua mgogoro huo kidiplomasia. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa vile Mheshimiwa Mbunge ameomba tuongozane nikaone hali halisi basi haya yote nitayaona tutakapotembelea eneo hilo na nakubaliana kuongozana naye. (Makofi)
MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuulizwa swali la nyongeza; je, ni lini Serikali itatatua migogoro iliyopo katika Wilaya ya Nachingwea kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania JKT pamoja na wananchi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyoeleza huko nyuma Wizara inayo mpango wa miaka mitatu ambayo inaendelea kuutekeleza na katika mpango huo tayari kulikuwa na maeneo yenye migogoro 87 tumekwishatatua migogoro 78. Kwa hiyo, kwa Eneo la Nachingwea bado tunaendelea kulishughulikia na tutaendelea kulishughulikia ili tuweze kukamilisha, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba migogoro hii yote inatatuliwa.
MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwenye Kata yangu ya Makoko pamoja na Buhare kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Jeshi la Wananchi pamoja na wale raia wa pale na Waziri aliyekuwepo Mheshimiwa Innocent Bashungwa aliahidi kwenda na mimi kwa ajili ya kwenda kutatua huo mgogoro.

Je, sasa ni lini Mheshimiwa Waziri uliyepo sasa utaandamana na mimi tukamalize huo mgogoro wa wananchi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri aliyenitangulia alikwishatembelea eneo hilo na amekwishanipa taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa. Kwa hiyo, tunaendelea hapo alipofikia na kama itahitajika twende tena basi tutafanya hivyo, lakini nafikiri tuna imani kwamba kwa ripoti aliyoitoa tutaweza kukamilisha tatizo hili na mgogoro huo, ahsante.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Serikali ambayo hayajaridhisha, nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Eneo la Oldonyosambu la wananchi limechukuliwa mwaka 1983 wakapewa Jeshi na Serikali ikawaahidi Wananchi wa Oldonyosambu kwamba watapewa maeneo katika Eneo la Oljoro ikiwemo pamoja na wananchi wa Kata ya Mlangarini ambao walitakiwa kulipwa fidia yao mwaka jana mpaka sasa hawakuweza kupewa fidia.

Je, nini kauli ya Serikali kuwapa wananchi haki yao kwa maana ya fidia ili kuondokana na migogoro na wananchi?

Swali la pili, kwa kuwa maelezo ya Mheshimiwa Waziri yanahitaji utafiti kwenye majibu yake. Je, yuko tayari baada ya Bunge hili kuambatana na mimi kuelekea Jimboni kwenda kuzungumza na wale wananchi ili waweze kupata majibu halisi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha migogoro yote ya ardhi inatatuliwa na ndiyo maana Serikali iliunda Kamati ya Mawaziri wa Wizara Nane ambayo imekuwa ikifanya kazi na taarifa ya kina ilitolewa pia jana kwa kiasi fulani na kwa upande wetu kama Jeshi tulikuwa na migogoro 87 tumeishaitatua migogoro asilimia 90.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili alilolieleza la Mlangarini ni moja ya maeneo ambayo tumekwishayafanyia kazi. Ni kweli tulishafanya uthamini, tulishafanya upimaji na Wizara ya Fedha ilishafanya uhakiki. Kwa hiyo, hatua iliyosalia ni kuwalipa wananchi hao fidia yao na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wao watalipwa fidia yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu eneo ambalo liko kwenye swali la msingi ambalo ni Oldonyosambu, kama alivyoomba na kama nilivyoeleza kwamba kwa vile suala hili linatufikia kwa mara ya kwanza, halimo hata katika mpango wetu wa migogoro, basi Wizara tutatuma wataalamu kama nilivyokwishasema, pia niko tayari kuambatana nae baada ya kupata hii taarifa ya wataalam ili tuone tunaumaliza namna gani mgogoro huu. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, shida kubwa sana katika Jeshi inayotokea na wananchi katika masuala ya ardhi ni Jeshi kutokuwa na hatimiliki kwa baadhi ya makambi. Ni lini Serikali mtajipanga kuwapatia Hati Majeshi haya ili kusudi wasigombane na wananchi? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli yalikuwepo maeneo ambayo hatukuwa na hatimiliki, tulikuwa na maeneo ambayo yalihitaji uhakiki wa mipaka, kwa hiyo zoezi hili kama nilivyosema katika ile migogoro 87 limekwishafanyika. Kwa hiyo, tumekwishapima, tumekwisha hakiki na baadhi ya maeneo tayari tumekwishawasilisha Wazira ya Ardhi ili tuweze kupata Hatimiliki, kwa hiyo, tuna imani hili linakwenda kuisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hii migogoro ni endelevu kila itakapotokea tutaendelea kuitatua kadri itakavyojitokeza. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao hivi karibuni katika Kata ya Mabama, Wilaya ya Uyui? (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata Mabama nafikiri huu ni mgogoro ambao unakuja kwa sasa hivi, kwa hiyo sisi tutakachokifanya ni kupata uhakika na baada ya kupata uhakika kama kweli wananchi eneo lao limevamiwa, basi taratibu zitafanywa za uhakiki na kama wanastahili fidia watalipwa fidia yao.
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mikumi tuna Kikosi cha Jeshi na moja ya mgogoro ambao wanao Wanakijiji wa Kijiji cha Vikweme na vitongoji ambavyo zinazunguka Vikweme pale Mikumi walitoa eneo lao kwa ajili ya mazoezi ya Jeshi, lakini Jeshi limechukua mpaka maeneo ya wananchi na taarifa hizo Serikali inayo. Je, ni nini kauli ya Serikali?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kwamba suala hili tumekuwa tukilishughulikia kwa pamoja, kwa hiyo tutaendelea kulishughulikia ili liweze kufikia hatma.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hili Jeshi la Akiba (mgambo) limeonekana kuwa na hadhi tofauti kidogo ikilinganishwa na Jeshi la Kujenga Taifa na tumeshuhudia kwa siku za hivi karibuni kabla ya marekebisho kwamba hata ajira zikitangazwa zilikuwa zinalenga zaidi Jeshi la Kujenga Taifa katika baadhi ya maeneo. Je, Serikali haioni kwamba iko haja sasa ya kuboresha haya mafunzo ya Jeshi la Mgambo ili kuwavutia vijana wengi zaidi waweze kwenda huko na kuwezesha uwiano na Jeshi la Kujenga Taifa ukizingatiwa kwamba Jeshi la Kujenga Taifa halina uwezo kwa sasa wa kuwachukua vijana wote wenye uhitaji wa kupitia huku. Ahsante sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa kuendelea kutoa umuhimu kwa Jeshi la Akiba ambalo ni jeshi muhimu sana, kama nilivyotoa majibu katika swali la msingi majeshi haya mawili yameanzishwa kwa madhumuni tofauti, lakini ushauri alioutoa ni ushauri mzuri, ukizingatia sasa hivi tunajaribu kuangalia ni jinsi gani tunaweza tukawachukua vijana wote wanaostahili kwenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa. Kwa hiyo pamoja na kwamba mahitaji hayo ya majeshi haya ni tofauti, tutauangalia huo ushauri tuone kama unaweza kufanyiwa kazi namna gani.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza ninauliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachukua nafasi hii kuishukuru sana Serikali yetu kwa kuendelea kuwajenga vijana katika misingi ya uzalendo, lakini katika misingi ya stadi za maisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza, kwa kuwa Serikali iliona kazi maalumu na kubwa ambayo imefanywa na vijana waliofanya kazi hiyo ya operation, waliojenga Ikulu pamoja na ukuta wa Mererani.

Je, Serikali haioni haja ya kuwachukua pia vijana waliojenga Chuo cha Mzumbe, Bwawa la Mwalimu Nyerere, nyumba za Ukonga pamoja na Msomela kwa sababu kazi za operation hazitokei kila mara, ni kazi ambazo zinatokea mara chache. Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwachukua na vijana hao waliojenga maeneo mengine? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, Serikali haioni kuwa kwa kuwa JWTZ itakuwa ina nafasi labda zisizokidhi vijana wote. Serikali haioni haja sasa kuungana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuwa na ile database ya vijana ambao wamefanya kazi maalumu, wakaweza kuwekwa kwenye majeshi mengine? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, swali la kwanza ambalo ameuliza, kuwachukua vijana wengine ambao wameshiriki katika operation mbalimbali alizozitaja, utaratibu wa kuwachukua vijana ni kama nilivyoeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ninafurahi na ninamshukuru kwamba katika swali lake la pili, ameeleza wazi nafasi za kuandikisha vijana jeshini ni chache. Kwa hiyo, tunawachukua vijana kulingana na mahitaji ya wakati huo, kulingana na taaluma walizonazo na vijana wote wanaopenda JKT hushiriki katika operation mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru sana vijana wetu kwa moyo huo wa kujitolea na kufanya kazi hizi wanazokuwa wamepangiwa kwa umahili wa hali ya juu. Kwa hiyo, kadiri nafasi zinavyopatikana na kadiri mahitaji ya wakati huo yalivyo vijana mbalimbali huchukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwa na database, database ipo na tunashirikiana na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama katika kuainisha vijana kuja kwetu. Kuainisha vijana ambao wana sifa kulingana na mahitaji yao. Kwa hiyo, tunafanya kazi pamoja na database ipo, lakini ikumbukwe tu kwamba Bunge hili lilitoa pia uhitaji au kigezo hicho. Kwa hiyo, pengine ni kulishauri Bunge likaangalia upya kigezo hicho ambacho kiliondolewa, ahsante. (Makofi)