Primary Questions from Hon. Emmanuel Lekishon Shangai (9 total)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawapatia Vitambulisho vya Taifa na vyeti vya kuzaliwa wananchi wa Kata za Ololosokwan, Soitsambu na Enguserosambu Ngorongoro?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Shangai Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Agosti 2022 jumla ya wananchi 84,637 katika Wilaya ya Ngorongoro wametambuliwa na kusajiliwa. Namba za Utambulisho 61,237 ambayo ni sawa na asilimia 72.3 ya wananchi wote waliotambuliwa na kusajiliwa zimezalishwa na kugawiwa kwa wananchi. Aidha, jumla ya vitambulisho 46,997 ambayo ni sawa na asilimia 76.7 ya namba za utambulisho tajwa vimezalishwa pamoja na kugawiwa kwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, usajili na utambuzi wa wananchi na uzalishaji na ugawaji Vitambulisho vya Taifa ni kazi endelevu. Hivyo, Mamlaka itaendelea na usajili wa wananchi wanaokidhi vigezo kupitia ofisi za usajili wa wilaya pamoja na kuzalisha na kugawa Vitambulisho vya Taifa kwa wananchi kupitia katika kata zote.
Mheshimiwa Spika, usajili na utoaji wa vyeti vya kuzaliwa bila malipo unaendelea katika vituo vyote vinavyotoa huduma ya afya ya mama na mtoto pamoja na vituo vya kata.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Forodha katika mpaka wa Olaika Wilayani Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, TRA ilifanya utafiti katika maeneo yote nchini yenye uhitaji wa Ofisi za kudumu za usimamizi wa kodi ikiwemo mpaka wa Olaika Wilayani Ngorongoro na kubaini kuwa gharama za usimamizi wa shughuli za forodha katika mpaka wa Olaika zitakuwa kubwa ikilinganishwa na kiwango cha ushuru wa forodha unaotarajiwa kukusanywa. Kwa muktadha huo, TRA itaendelea kufuatilia mwenendo wa ukuaji wa shughuli za forodha katika mpaka huo ili kufungua kituo cha forodha cha kudumu. Aidha, TRA itaendelea kuimarisha mfumo wa sasa wa kuhudumia mpaka huo ili kuwawezesha wananchi kuendesha shughuli zao za kibiashara kwa ufanisi zaidi.
MHE. DANIEL A. TLEMAI K.n.y. MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, lini barabara ya Kibaoni – Endala – Endamarik hadi Endabash itajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Jimbo la Karatu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza matengenezo katika barabara ya Kibaoni – Endala - Endamariek hadi Endabash. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilipeleka shilingi milioni 599.97 kwa ajili ya ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 40 kwenye barabara hiyo, na ujenzi wake umekamilika. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 68 kwa ajili ya matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilomita tano katika barabara hiyo na utekelezaji wake unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali itatenga shilingi milioni 213.02 kwa ajili ya kujenga madaraja mawili katika matengenezo ya sehemu korofi yenye urefu wa kilometa 10 pamoja na matengenezo ya muda maalum yenye urefu wa kilomita mbili katika barabara hiyo.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza:-
Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya Mto Piyaya Kata ya Piyaya na Mto Juhe Kata ya Samunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Madaraja ya Mto Piyaya na Mto Juhe ambayo yana urefu wa zaidi ya mita 80. Aidha, ujenzi wa madaraja hayo unahitaji kuanza na kazi ya usanifu wa kina ikiwemo uchambuzi wa miamba, ili kupata gharama halisi ya ujenzi wake.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2024/2025, Serikali itafanya usanifu wa kina wa madaraja haya, ili kupata gharama halisi ya ujenzi. Vilevile, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya barabara za Jimbo la Ngorongoro ikiwemo ujenzi wa madaraja kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, lini Serikali itaondoa Kijiji cha Ngaresero kwenye eneo la Pori Tengefu la Pololeti baada ya kujumuishwa kimakosa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo: -
Mheshiwa Naibu Spika, Kijiji cha Ngaresero hakipo katika Pori la Akiba Pololeti ila kipo Kata ya Ngaresero, Tarafa ya Sale. Kijiji hicho ni mojawapo ya vijiji ambavyo vipo ndani ya Pori Tengefu Ziwa Natron. Kulingana na Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na marekebisho yake ya mwaka 2019, ardhi ya Pori Tengefu Ziwa Natron ipo kwenye kundi la ardhi ya hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori Tengefu Ziwa Natron ni moja kati ya maeneo yaliyotolewa maelekezo na Baraza la Mawaziri kuwa lipandishwe hadhi. Hivyo, wakati wa utekelezaji wa maelekezo hayo, wananchi wa kijiji cha Ngaresero watashirikishwa.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ilifanya tathmini na kubaini changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na imekwisha wapata watoa huduma watakaofikisha huduma za mawasiliano katika Kata za Alailelai, Alaitolei, Engaresero, Mundarara, Ngoile, Olbalbal na Ololosokwan. Aidha, Serikali itayaingiza maeneo mengine yaliyobaki yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika orodha ya miradi itakayotekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. EMANNUEL L. SHANGAI aliuliza:-
Je ni sheria ipi inawaruhusu Watumishi wa TANAPA, TAWA na NCAA kutoza mifugo shilingi 100,000 pindi iingiapo hifadhini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emannuel Lekshon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi za Uhifadhi za TANAPA, NCAA na TAWA zinaongozwa na Sheria mahususi za kusimamia rasilimali za wanyamapori. Mathalan, Sheria ya TANAPA Sura 282 Kifungu cha 28(1)(a) kama kilivyorekebishwa na Sheria ya Marekebisho Mbalimbali (Na. 11) ya mwaka 2003 ambayo imeongeza kifungu 20A cha Sheria hiyo kwa kuwapa mamlaka watumishi wa TANAPA kutoza faini isiyozidi shilingi 100,000 kwa kila kosa pale mkosaji anapokiri na kukubali kwa maandishi kulipa faini kwa kosa husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 116 cha Sheria ya Uhifadhi Wanyamapori, Sura ya 283 hutumika katika kutoza faini pindi mifugo inapoingizwa kinyume cha sheria, ndani ya mapori ya akiba. Kifungu hiki kimebainisha utaratibu wa kulipa faini ambapo mkosaji atalipa faini mara baada ya kukubali na kukiri kosa. Aidha, sheria imeelekeza kuwa kiwango cha faini hakitapungua shilingi 200,000 na hakitazidi shilingi 10,000,000. Mkosaji hukiri kosa kwa maandishi na kulipa faini hiyo, na endapo hatakuwa tayari kulipa faini, hufikishwa Mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Wananchi kwa ujumla kuwa Serikali itaendelea kuhifadhi na kusimamia rasilimali za wanyamapori kwa kushirikiana na jamii. Hivyo, tunawaomba wote watoe ushirikiano katika kufanikisha jukumu hilo na kuwasihi wazingatie sheria ili kuepusha migongano isiyo ya lazima baina yao na Wahifadhi.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza: -
Je, lini Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kumalizia Mradi wa Maji wa Mageri utakaohudumia vijiji nane Wilayani Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikitenga fedha za utekelezaji wa Mradi wa Maji Mageri utakaohudumia vijiji nane vya Tinaga, Oloirien, Ng’arwa, Yasi, Mdito, Mageri, Mugongo na Magaiduru, ambapo hadi sasa jumla ya shilingi 2,264,520,000 zimetolewa. Fedha hizo zimesaidia kukamilisha utekelezaji wa Banio la Chanzo cha Maji Orkanjor, ulazaji wa bomba kuu kutoka kwenye chanzo hadi kwenye tenki umbali wa kilometa tatu na ununuzi wa pampu mbili zenye uwezo wa kusukuma maji lita milioni 2.05 kwa Siku. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ujenzi wa matenki tisa yenye jumla ya ujazo wa lita 2,000,000 na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa kilometa 80. Aidha, utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 40 na unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2024. (Makofi)
Umaliziaji wa Kituo cha Afya Arash – Ngorongoro
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya umaliziaji wa Kituo cha Afya Arash?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Arash kilianza ujenzi mwaka 2018 ambapo Serikali kupitia Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ilipeleka shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD), jengo la wazazi na jengo la upasuaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje limekamilika na linatumika. Majengo ya maabara, wazazi na upasuaji yako katika hatua ya kupiga plasta.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepeleka shilingi milioni 30 kwa ajili ya kumalizia jengo la maabara ambalo liko hatua ya plasta. Aidha, Serikali kupitia TANAPA imejenga nyumba mbili za three in one ambazo ziko katika hatua za umaliziaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika Kituo cha Afya cha Arash, ahsante.