Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Emmanuel Lekishon Shangai (15 total)

MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ni moja ya halmashauri ambazo watumishi wanahama sana na kwa mwaka jana tu watumishi zaidi ya 93 wamehama. Pia watumishi waliohamia ni 14 tu. Kwenye ajira iliyofanyika mwezi Juni, 2021, watumishi 11 ambao waliajiriwa wakiwa na ajira nyingine baadaye Serikali iliwarudisha, lakini hakuna watumishi wengine walioletwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wengine ambao wanataka kuhamia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro hawapewi nafasi ya kuhamia kutoka kwenye halmashauri zao. Je, watumishi watapelekwa lini kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro ili waweze kuhudumia wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wanaopangiwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa wanapangiwa kulingana na taratibu na miongozo na kanuni za utumishi wa umma, lakini wanawajibika kufanya kazi katika maeneo yale isipokuwa wakiwa na sababu za msingi sana za kuomba uhamisho na sababu hizo mara nyingi ni zile za kiafya na baadhi ya sababu ambazo zinakubalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba watumishi wengi ambao wanapangiwa hasa maeneo ya vijijini hawahamishwi na hivi sasa uhamisho kutoka ngazi ya Halmashauri vijijini kwenda kwenye Manispaa na Majiji umesitishwa ili kuhakikisha kwamba watumishi wengi walioko katika maeneo hayo wanaendelea kubaki pale ili kutoa huduma kwa wananchi. Hii itatuwezesha kuondokana na wimbi la watumishi kuhama kutoka halmashauri za vijijini kwenda mijini kama ilivyo Ngorongoro. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba suala hilo lilishafanyiwa kazi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mkakati ni kwamba Halmashauri ya Ngorongoro ni moja ya halmashauri zenye upungufu wa watumishi na itapewa kipaumbele mara ajira zitakapopatikana ili kuweza kupunguza pengo la upungufu wa watumishi katika halmashauri hiyo. Ahsante.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwenye Kata nilizotaja za Oldonyosambu, Ololosokwan, Solosambu pamoja na Soitsambu ni kwamba kuna wananchi wengi ambao fomu zao zimezuiliwa kwenye Ofisi ya Uhamiaji.

Je, ni lini Serikali itamaliza uhakiki kwa haraka ili wananchi wapate Vitambulisho vya Taifa pamoja na vyeti vya kuzaliwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuna wananchi wengi Wilaya ya Ngorongoro hasa Kata ya Orgosorok Loliondo; wengi wao wazazi wao walizaliwa Tanganyika wamefanya kazi walikuwa watumishi na wengine wamestaafu lakini bado wanasumbuliwa hata kupata vitambulisho vya Taifa pamoja na vitambulisho vya kuzaliwa.

Je, Waziri yuko tayari kuongozana nami kwa ajili ya kutatua matatizo ya wananchi hao?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Shangai, Mbunge wa Ngorongoro kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nikianza na ombi lake la kutaka tuambatane pamoja kwenye jimbo lake kutatua changamoto hizi mbili; nimhakikishie Mheshimiwa Lekisho Shangai tutafanya hivyo. Naamini tutakapokuwa tumekwenda kwenye hiyo ziara jimboni kwake tutaweza kujua na kupata undani wa changamoto alizozungumza ili tuweze hatua stahiki ili wananchi hawa wanaostahiki haki yao ya msingi ya kupata vitambulisho waweze kupata; ikiwemo wale ambao amezungumza mara ya kwanza ambao fomu zao Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba zimezuiwa uhamiaji. Vile vile hata wale ambao amesema ni raia lakini bado wameshindwa kutambuliwa

Mheshimiwa Spikam, changamoto zote hizi mbili tutazishughulikia mimi na yeye kwa pamoja.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina uhakika kwamba tathmini ya mwisho kufanyika katika eneo hilo ni mwaka 2008.

Mheshimiwa Spika, basi naomba kumuomba Mheshimiwa Waziri kama inawezekana ili kuthibitisha yale anayoyasema tuongozane akaongee na wafanyabiashara wa Wilaya ya Ngorongoro ambao ndio wahitaji wa kituo cha forodha.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa
Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Shangai, Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote kabla ya kujibu swali hilo naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofuatilia na kufanyia kazi katika Jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungao wa Tanzania ni Serikali sikivu sana. Kwa hiyo, niko tayari kufuatana na yeye Mheshimiwa Mbunge kwenda katika eneo hilo na kuona uwezekano na kuongea na wananchi na wafanyabiashara kwa jumla. (Makofi)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali; kwamba kwenye kata za Swaiti Sambao, Lweipiri na Ololosopan, tembo wamekuwa wakiharibu mazao pamoja na kuumiza wananchi.

Je, Serikali ina mkakati upi wa kuhakikisha kwamba wananchi wale wanafidiwa?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Shangai Mbunge wa Ngorongoro kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu mwanzo, kwamba sasa tuna mpango wa kuangalia namna ya kuwa na askari wa kutosha ili kipindi kile ambacho ni cha migogoro kati ya binadamu ya wanyama wakali, basi hawa askari waweze kuelekea katika maeneo hayo na kudhibiti hawa wanyama wakali. Ahsante.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, kuhusiana na wanawake wanaoshiriki katika madini Mkoa wa Arusha lakini naomba kuuliza maswali mawili.

Swali la kwanza; wanawake wanapojishughulisha na shughuli za madini Mkoani Arusha wanakutana na changamoto nyingi sana; je, ni nini Mkakati wa Serikali wa kutatua changamoto zinazowakabili wanawake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Wilaya ya Ngorongoro yamegundulika madini mengi, lakini inaonekana kwamba wanawake hakuna mazingira yanayowawezesha kushiriki katika shughuli za madini. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba maeneo ya madini kwenye Wilaya ya Ngorongoro yanapimwa ili wanawake nao waweze kushiriki ipasavyo katika shughuli hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Ole–Shangai, Mbunge wa Ngorongoro, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa changamoto za wanawake Serikali imeendelea kutoa elimu, kuwahamasisha wajiunge na vikundi mbalimbali ambavyo nimevitaja kwenye swali la msingi ili waweze kusaidiwa kupata elimu juu ya sheria, kanuni na taratibu za madini pamoja na kufahamu fursa za biashara na uwekezaji kwenye sekta ikiwa ni pamoja na kuelekeza namna ya kupata mitaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili kuhusu Wilaya yake ya Ngorongoro, ni kweli kwanza nimpongeze Mbunge maana yake mwisho wa mwezi uliyopita aliniomba nifanye Wizara kwenye Jimbolake ili kwenda kubaini changamoto zinazowakabili wachimbaji wa madini. Tukagundua kwamba Ngorongoro ina madini mengi sana ya vito, lakini uendelezaji wa sekta uko chini sana hasa kwa upande wa wanawake. Nitumie fursa hii kumhakikishia kwamba baada ya ziara ile tuliagiza Taasisi yetu ya Jiolojia na Utafiti wa Madini pamoja na Tume ya Madini waende kule wakahamasishe ile jamii na wabainishe maeneo yenye madini ili wanawake nao wa Ngorongoro wajiunge waweze kufaidi fursa hii iliyopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatukuishia hapo, Wizara hii imeteua Mabalozi wa Madini, wanawake wanaongozwa na Dkt. Ritta Kabati ambao kazi yao ni kuwahamasisha wanawake wote wanaopenda kujiingiza katika biashara ya madini, wafahamu biashara ya madini na fursa zilizoko za wawekezaji, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha kwa ajili ya usanifu kwa madaraja yote mawili ya Mto Juhe na Piyaya kwa mwaka wa fedha 2023/2024?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; nini commitment ya Serikali pindi upembuzi utakapokamilika kutenga fedha haraka kwa sababu, madaraja haya yatakayojengwa yatasaidia kuokoa maisha ya watoto ambao wamekuwa wakichukuliwa na maji ya Mto Juhe pamoja na Mto Piyaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA – (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Emmanuel Shangai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimetoa majibu hapa kwenye majibu yangu ya msingi. Serikali itatenga fedha katika mwaka wa 2024/2025 ili kuhakikisha usanifu unafanyika katika madaraja haya ya Mto Piyaya na Mto Juhe.

Mheshimiwa Spika, lakini katika swali lake la pili; Serikali imeweka kipaumbele sana katika kuhakikisha inatengeneza barabara na madaraja katika Jimbo la Ngorongoro, lakini katika majimbo yote ya hapa nchini. Na tayari maelekezo yalikuwa yameshakwenda kwa mameneja wote wa TARURA wa Wilaya kuhakikisha wanatenga bajeti katika barabara hizi ambazo ni za kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, na ni imani yangu katika bajeti hii, barabara hii itakuwa nayo imetengewa fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu. Naomba kuwasilisha.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia Kituo cha Afya Samunge, Kata ya Samunge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutaangalia katika mwaka wa fedha unaofuata ili tuweze kutenga fedha hii ya kumalizia Kituo cha Afya cha Samunge.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, moja ya kata ulizotaja, kata ya Mundarara haipo Wilaya ya Ngorongoro, ipo wilaya ya Longido. Je, mpo tayari kubadilisha mnara ambao ulikuwa uende Kata ya Mundarara Kwenda moja kati ya wilaya za Ngorongoro?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, ni lini Serikali, itapeleka mawasiliano katika vijiji vya Kinaga, Loswashi, Nan pamoja na Osorosapia?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Emmanuel Shangai kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, napokea mabadiliko haya lakini itabidi tukutane ili tuweze kulifanyia uchunguzi wa kina ili tuweze kuona kwamba tunafanya nini. Tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tatizo hili linatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni kwamba katika kata ambazo amezitaja Serikali iko katika tathmini. Tathmini mpaka sasa tumeshafikisha vijiji 2,224 na tunaamini kwamba tathmini ikishakamilika na Mheshimiwa Rais tayari ameshapata fedha kwa ajili ya kujenga minara mingine 600. Kwa hiyo, tunaamini katika hizo kata zitaingizwa katika ya utekelezaji wa minara ambayo itakuja kwa awamu inayokuja, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; ni lini, Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais kujenga barabara ya lami kutoka kipande cha Ngaresero mpaka Engaruka kilomta 39?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Ole-Shangai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa amekuwa akifuatilia barabara hii na ahadi za Viongozi wetu ni maelekezo, tayari barabara hii tumeiweka kwenye kupaumbele. Kwa hiyo, nimhakikishie tutakapopata fedha barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. EMANNUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Nashukuru kwamba, ameshindwa kuthibitisha kwamba mifugo inatakiwa kutozwa shilingi 100,000 kwa kichwa cha ng’ombe wanapoingia hifadhini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wafugaji wengi Tanzania wamekuwa wakitozwa shilingi laki moja kwa kichwa cha ng’ombe wanapoingia hifadhini na kuna wananchi wametozwa mpaka shilingi milioni sabini kwa wakati mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza nini kauli ya Serikali kwa Watumishi wa TANAPA, TAWA pamoja na NCAA ambao wamekuwa wakitoza shilingi laki moja kwa kichwa cha ng’ombe?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili je, Serikali ipo tayari kurejesha fedha za wananchi ambazo wametozwa zaidi ya shilingi milioni kumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shangai kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeonyesha sheria inataka nini? Lakini sambamba na eneo hilo niseme tu kwamba, kosa la kuingiza mifugo kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Taifa lipo pia katika Kanuni Na. 7(1) ya Kanuni za Hifadhi ya Taifa GN Na. 255 ya mwaka 1970 kama ilivyorekebishwa ambavyo Kifungu kinazuia kuingiza mifugo Hifadhini na adhabu ya kosa kuingiza mifugo ni kwa kila mfugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nchi yetu, Serikali yetu ina heshimu Utawala wa Sheria na chombo ambacho kimekasimiwa kutafsiri sheria pale ambapo kuna changamoto ni Mahakama zetu. Nitoe rai kwamba wale wote wanaoona kwamba imepita hukumu ambayo wanaona haikuwatendea haki basi twende kwenye mfumo wa kisheria ili sheria iweze kutoa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hili la kurejesha bado narudi pale pale yeyote anayehisi kwamba hakutendewa haki tuzitumie Mahakama zetu ili haki iweze kutendeka. (Makofi)
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi; ni lini, Serikali itatekeleza ahadi ya Makamu wa Rais kujenga barabara ya lami kutoka kipande cha Ngaresero mpaka Engaruka kilomta 39?
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Ole-Shangai, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa amekuwa akifuatilia barabara hii na ahadi za Viongozi wetu ni maelekezo, tayari barabara hii tumeiweka kwenye kupaumbele. Kwa hiyo, nimhakikishie tutakapopata fedha barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, okay kwa kuwa sasa ujenzi wa shule umefikia 85%, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi huo pamoja na nyumba za watumishi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mbunge kwa swali hili zuri sana kwa maslahi ya watoto wote wa kike ambao watasoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha mwaka 2023/2024 Serikali itapeleka shilingi bilioni 1.1 katika shule zote zile 16 za wasichana ambazo zilipelekewa shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa kumi, lakini chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu na mabweni manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itapeleka fedha hii kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza kuzitumia.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali, lakini naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa Kituo hiki cha Arash kinategemewa na kata zaidi ya nne, ni lini sasa Serikali itatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kumalizia kituo hiki ambacho wananchi walichanga fedha zao? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Ole - Shangai kwa namna ambavyo anafuatilia sana miradi ya afya katika Jimbo lake la Ngorongoro na nimhakikishie kwamba Serikali ilishatambua Kata ya Arash kwamba ni kata ya kimkakati na ndio maana tumeanza kupeleka fedha hizi na nikuhakikishie tu kwamba tunatenga fedha kwenye bajeti zetu na tutatafuta pia wadau kwa ajili ya kupata fedha kukamilisha miundombinu inayobaki, ahsante.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, okay kwa kuwa sasa ujenzi wa shule umefikia 85%, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi huo pamoja na nyumba za watumishi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mbunge kwa swali hili zuri sana kwa maslahi ya watoto wote wa kike ambao watasoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha mwaka 2023/2024 Serikali itapeleka shilingi bilioni 1.1 katika shule zote zile 16 za wasichana ambazo zilipelekewa shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa kumi, lakini chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu na mabweni manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itapeleka fedha hii kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza kuzitumia.
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Serikali imeboresha miundombinu ya Bandari ya Tanga kiasi kwamba shehena zimeongezeka, lakini reli ya kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam na kutoka Tanga kwenda Arusha bado ni chakavu sana, je, kuna mpango wowote wa kuboresha reli hii ili sasa shehena hii iweze kutoka kwa urahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo na Katibu wa Bunge la CCM kwa swali lake kubwa na zuri la maslahi ya watu wa Tanzania na watu wa Kaskazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mpango mzuri na kabambe kwa sababu inatambua umuhimu wa upande wa Kaskazini kwanza kwenye utalii, kilimo pamoja na sekta nyingine, hivyo katika mwaka wa fedha 2023/2024 tumeshafanya kazi kubwa, tulishasaini mkataba wa kununua materials za kukarabati reli inayotoka Tanga kuelekea mpaka Arusha kilometa 533.

Kwa hiyo, mara baada ya kusaini mkataba huo katika mwaka wa fedha huu unaofuatia tunakwenda kuanza kutoa reli iliyokuwepo, tunataka tuweke reli nzito ambayo itakuwa na capacity ya ratilika 80 kwa yard, iliyokuwepo ilikuwa 45 kwa yard.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii reli iliyopo sasa hivi speed inayokwenda treni ni karibu speed ya 15 - 20 kwa saa moja, hivyo inawachukuwa muda mrefu sana kufika kwenye destination inayotakiwa. Tukifanya maboresho haya speed itaongezeka mpaka 75, kwa hiyo muda kama ilikuwa ni saa 12 tutakuwa tunatumia saa karibu nne. Kwa hiyo, habari njema hii kwa watu wa Kaskazini, Tanga na Watanzania kwa ujumla juu ya maboresho makubwa ya reli ya Kaskazini. (Makofi)