Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kila jambo, pia aniwezeshe kutoa mchango wangu kwa ufasaha.
Mheshimiwa Spika, napenda kukushukuru wewe pamoja na kukupongeza kwa namna unavyoliongoza Bunge letu tukufu, hakika wewe ni Spika wa viwango, Mwengezi Mungu azidi kukumulikia mwanga wa mafanikio, wewe ni hazina kubwa ya nchi yetu. Hakika Mungu amekuibua kwa sababu, kwani Taifa linahitaji mtu kama wewe wakati huu. Pia nampongeza Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa namna wanavyoliongoza Bunge letu tukufu.
Mheshimiwa Spika, nikiendelea, nachukua fursa hii kwa dhati ya nafsi yangu kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia nampongeza kwa namna ambavyo anaiendesha nchi hii.
Mheshimiwa Spika, nampongeza Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa anavyotuongoza. Pia nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa uongozi wake na moyo wake wa kuwatumikia wananchi. Nampongeza Mheshimiwa Mwigulu Nchemba - Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara na viongozi wote wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kupata nafasi ya kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi kwenye hoja hii ya Bajeti Kuu ya Serikali. Naipongeza Serikali kwa bajeti nzuri ambayo inatoa faraja na matumaini mema kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, kwa kuendelea nauelekeza mchango wangu kwenye madawati ya jinsia; naipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuweka madawati ya jinsia nchini. Madawati haya lengo lake kubwa ni kuwasogezea huduma karibu wananchi wanaopata changamoto za kifamilia zikiwemo, udhalilishaji, ubakaji, ukatili, utelekezaji wa watoto pamoja na wanaokinzana na sheria.
Mheshimiwa Spika, madawati haya kama yalivyoundwa ipo haja ya kuyafanya yaweze kufanyakazi kama ikivyokusudiwa, kwani kinyume chake itakuwa ni kuzidisha changamoto badala ya kupunguza. Baadhi ya madawati haya yanakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi kama vile usafiri, kompyuta, karatasi, vifaa kwa ajili ya kuchezea na kutuliza akili za watoto wakati wa kuhojiwa na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa vitendea kazi hivyo vinachelewesha au kukwamisha kushughulikia mashauri yanayopelekwa na kupelekea wananchi kuona hakuna haja ya kwenda kwenye dawati, pia hupelekea wananchi kuchoka wakati mwingine wanakosa hata nauli pale inapotokea kuitwa mara nyingi.
Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kuweka mkakati maalum wa kuyawezesha madawati haya kwani ni mkombozi wa wananchi wanyonge wanaopata unyanyasaji hasa vijijini.
Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali kwa kazi kubwa inayofanya, pamoja na kazi kubwa inayofanywa wapo watu wanambeza na kumsema vibaya Rais wetu, hii sio sawa kabisa hasa kutumia ukabila, udini au anakotoka. Rais wetu hana ubaguzi kwa nini yeye abaguliwe. Naiomba sana Serikali kutunga sheria ya kumlinda Rais dhidi ya watakaomsema vibaya.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache naunga mkono hoja.
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. TAMIMA HAJI ABASS: Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi katika Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 iliyowasilishwa mbele ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa inayochukua katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Waziri wa Mipango na Uwekezaji kwa kuja na mpango wa maendeleo pamoja na Waziri wa Fedha kwa kuwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025, bajeti ambayo ni nzuri na mkombozi wa mwananchi.
Mheshimiwa Spika, pamoja na uzuri wa bajeti hiyo haitakuwa na thamani yoyote iwapo utekelezaji wake hautapewa umuhimu kwa maana ya watendaji ambao ndio watekelezaji wafanye kazi kwa bidii kuhakikisha wanakamilisha kazi walizopangiwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile Wizara ya Fedha ina wajibu wa kuzipatia fedha walioomba Wizara za Kisekta ili waweze kukamilisha shughuli walizozipanga, iwapo Wizara hazikupatiwa fedha zote na kwa wakati ni wazi kwamba malengo hayatoweza kufanikiwa.
Mheshimiwa Spika, naendelea na mchango wangu kwenye eneo la kuchangia pato la Serikali na nazungumzia eneo la mazingira. Serikali ijenge viwanda vikubwa vya kuchakata taka na kuzalisha mbolea ambayo tutatumia nchini pia tutauza nje na kupata fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunazalisha taka nyingi ambazo zimekuwa kero kwa kuchafua mazingira na kusababisha maradhi ya mllipuko, tukumbuke kuwa kila kiumbe nchini kinazalisha taka, hivyo changamoto hiyo tuigeuze kuwa fursa.
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu; kwanza, kupitia halmashauri zetu uwekwe mkakati maalumu wa kukusanya taka kwenye masoko yote; pili, kuwa na mkakati maalumu wa kukusanya taka majumbani; tatu, kuwa na mkakati maalumu wa kusafisha mitaro ya maji machafu; nne, kuwa na utaratibu maalumu wa kusafisha fukwe; tano, kitengo cha kukusanya taka kwenye halmashauri zetu kiimarishwe kwa kupatiwa vifaa vya kisasa na sita, wawepo wakaguzi wa kila siku kukagua usafi wa masoko. Hii itasaidia maeneo yetu kuwa safi, pia kupata malighafi ya kutengeneza mbolea.
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, naunga mkono hoja.