Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon Tamima Haji Abass (6 total)

MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, ni upi mkakati wa Serikali wa kutoa elimu kwa jamii dhidi ya udhalilishaji na ukatili wa watoto?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamima Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kupitia mpango kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na Watoto, Serikali imeunda Kamati za Ulinzi wa Watoto na kuandaa vijarida na vitini vya kutoa elimu katika jamii kuhusu madhara ya ukatili, vyombo mbalimbali vya habari vinatoa vipindi vya kitaalamu kuhusu haki na ulinzi wa mtoto pia elimu ya athari za ukatili; walimu wa malezi na unasihi wamepata mafunzo ya kutoa elimu ya ulinzi wa watoto kwa walimu wenzao na wanafunzi; pia kupitia viongozi wa kijamii walio sehemu ya kamati ya jamii kwa kushirikiana na maafisa maendeleo, ustawi na elimu wanatumika katika kubadili mitazamo na fikra hasi za jamii, ahsante.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, kuna utafiti uliofanywa na Serikali kujua sababu za uwepo wa Watoto wa mitaani?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wananwake na Makundi Maalum napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamima Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 ilifanya tafiti katika Mikoa ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Mbeya, Arusha na Iringa ili kubaini idadi na sababu za watoto kuishi na kufanya kazi mitaani ambapo walibainiwa jumla ya Watoto 6,393 (wavulana 4,865, wasichana 1,528). Vilevile, mwaka 2020/2021 Serikali ilirudia utafiti katika maeneo hayo na kubaini kuwa idadi ilipungua hadi watoto 4,383 (wavulana 3,508 wasichana 875).

Mheshimiwa Spika,miongoni mwa sababu zilizobainiwa ni pamoja na, malezi duni, yatima, migogoro kwenye familia, shinikizo la makundi rika, ukatili na unyanyasaji nyumbani, umasikini wa kipato katika familia na utumikishaji wa watoto mijini, ahsante.
MHE. TAMINA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kukarabati nyumba za makazi ya Askari Polisi Kaskazini Unguja?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tamina Haji Abass, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tathmini kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zote 14 za makazi ya askari polisi katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, imefanyika na kiasi cha shilingi 447,065,000 zinahitajika. Fedha hizo zinatarajiwa kutengwa kwenye Bajeti ya Serikali ya 2024/2025, ahsante.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza:-

Je, lini Serikali itatunga sheria mahsusi kwa makosa ya ukatili wa kijinsia?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuombe radhi, swali namba 589 ndilo nipo nalo hapa, bahati mbaya niruhusu nilipate jibu la swali hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sheria ya Ndoa, Sheria ya Mtoto, Sheria ya Makosa ya Mtandao na Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu zina vifungu vinavyozuia makosa ya ukatili wa kijinsia na vifungu vinavyohusika na makosa ya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, Wizara ya Katiba na Sheria kwa kushirikiana na Wizara nyingine na asasi za kiraia inafanya tathmini ili kubaini iwapo ipo haja ya kuwa na sheria mahususi ya ukatili wa kijinsia au tuboreshe sheria zilizopo. Tathmini hiyo ikikamilika, itasaidia Serikali kufanya uamuzi sahihi kuhusu suala la kutunga sheria mahususi kwa makosa ya ukatili wa kijinsia au kuboresha sheria zilizopo, ahsante.
MHE. TAMIMA HAJI ABASS aliuliza: -

Je, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini ukoje?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tamima Haji Abbas, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenendo wa utoaji wa elimu ya lishe nchini unaonesha maendeleo mazuri na umeendelea kuimarika kutokana na juhudi mbalimbali za Serikali pamoja na wadau na mwitikio mkubwa wa wananchi. Serikali imepanua wigo wa uelimishaji na uhamasishaji wa masuala ya lishe kwa kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo: -

(i) Matumizi ya vyombo vya habari kama vile redio, televisheni na mitandao ya kijamii kote nchini na katika mikusanyiko ya kijamii;

(ii) Uwepo wa mtaala wa elimu ambao umejumuisha masuala ya afya na lishe kwa ngazi ya msingi na sekondari unaotoa fursa kwa wanafunzi kupata uelewa wa elimu ya lishe;

(iii) Wizara imezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Chakula na Ulaji wenye lengo la kuhamasisha matumizi sahihi ya chakula mchanganyiko kwa kuzingatia vyakula vinavyopatikana hapa nchini;

(iv) Elimu ya lishe imeendelea kutolewa katika vituo vya kutoa huduma za afya kote nchini hususani wakati wa Kliniki za mama na mtoto; na

(v) Uhamasishaji kupitia Ujumbe wa Mbio za Mwenge mwaka 2024 ambao una kauli isemayo; “Lishe sio kujaza tumbo, zingatia unachokula.” (Makofi)