Supplementary Questions from Hon. Abdul Yussuf Maalim (4 total)
MHE. ABDUL YUSUF MAALIM: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa kiasi gani TARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania Bara) na ZARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Zanzibar) zinashirikiana katika kutatua changamoto za kilimo kwa pamoja kupitia TEHAMA? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni tafiti za aina gani mpaka sasa zimefanyika katika teknolojia ya habari na mawasiliano ili kutoa matokeo chanya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nijibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia kuhusiana na matumizi ya TEHAMA na hasa ushirikiano wa taasisi zetu za utafiti kwenye kilimo kwa maana ya TARI kwa upande wa Tanzania Bara na ZARI kwa upande wa Zanzibar. Taasisi zetu, ikiwemo hizi zimekuwa zikishirikiana sana katika maeneo mbalimbali katika utafiti, kupeana na kujengana uwezo kati ya wataalamu kutoka ZARI na TARI.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali hayo kwa pamoja, hivi karibuni mwaka 2022 taasisi hizi zilifanya tafiti kwa ushirikiano katika mazao ya mihogo na mpunga ambapo moja kupitia Wakala wa Kimataifa wa Atomiki waone namna gani tunaweza kupunguza athari ya maradhi ya mihogo kwa maana ya michirizi kahawia ambayo inaathiri sana zao la muhogo ambalo linalimwa Tanzania Bara lakini pia na kule Visiwani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika mpunga (mchele) ambapo wameweza kufanya utafiti ili kuona namna gani ya kuongeza uzalishaji wa mpunga (mchele) ambao unalimwa kati ya Tanzania Bara na kule Visiwani ili kupunguza baadhi ya athari au kuboresha mavuno yanayotoka katika maeneo haya ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo moja, tunashirikiana sana kama Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa taasisi zote kama nilivyosema TARI na ZARI. Pili, tafiti zote ambazo zinatumia TEHEMA zimefanyika kwa kushirikiana na tutaendelea kuboresha ushirikiano huu kadiri muda unavyoendelea, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini Serikali itatatua changamoto za magari, pikipiki na vifaa vingine kwenye Kituo cha Polisi cha Ng’ambo – Unguja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, tayari tumeshagawa pikipiki 105 mpaka sasa na tunazigawa kwa awamu. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge pia kituo chako ulichokisema tutaweka kwenye mpango ili tuweze kupata polisi kwa ajili ya kutoa huduma katika eneo lako ulilotaja.
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Naomba kuuliza masuala madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa muktadha wa mabadiliko ya Katiba ya TFF hususan kipengele Na.2. Je, ni vipi ZFF itanufaika na mabadiliko ya Katiba hiyo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kiasi gani itasaidia kuinua viwango vya ubora wa waamuzi kutoka Zanzibar kuelekea kimataifa ukizingatia Zanzibar tuna upungufu wa waamuzi wa kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na mabadiliko ambayo Mheshimiwa Mbunge anayasema kwenye Katiba ya TFF, Zanzibar bado itakuwa inaendelea kunufaika na programu zote za maendeleo ya mpira wa miguu zinazofanywa na TFF, zikiwemo programu zinazoendeshwa kupitia CAF na FIFA kama ambavyo imekuwa ikitokea huko nyuma. Hakuna chochote ambacho kinakwenda kubadilika kwenye programu za maendeleo ya michezo na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Zanzibar itaendelea kunufaika.
Mheshimiwa Spika, hali kama hiyo pia inakwenda mpaka kwenye suala la waamuzi, kwa vile course zote za waamuzi ikiwemo mitihani ya kupata beji ya FIFA ambazo zinaendeshwa na TFF zinahusisha pia upande wa waamuzi kutoka Zanzibar. Kwa hiyo, fursa ya kufanya mitihani kwa ajili ya kupata beji ya FIFA bado itaendelea kuwepo kama ambavyo imekuwa ikitokea kama nyakati zote.
MHE. ABDUL YUSSUF MAALIM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza; je, Serikali inatumia njia gani kuelimisha wananchi juu ya athari ya mifuko hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Abdul kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, baada ya sheria hii kuwepo, kwa sababu sheria imeelekeza tuwe tunatoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali. Kwa hiyo, zipo njia mbalimbali za vyombo vya habari tunazotumia ikiwemo televisheni, redio, magazeti na namna nyingine. Pia, tumekuwa tunawakusanya wadau hasa wamiliki wa viwanda tunakutana nao kwa pamoja na kuwapa elimu namna ambavyo wanaweza wakapunguza, au ikiwezekana wakaondoa kabisa changamoto ya kuzalisha mifuko ya plastiki kwa sababu imekuwa inaleta athari kubwa kwa jamii. (Makofi)