Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. AZIZA S. ALLY: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza katika Bunge hili, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wangu wa Chama Cha Mapinduzi, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuniteua na kunipitisha kuwa Mbunge wa Viti Maalum. Niipongeze na kuishukuru Kamati Kuu ya Chama changu Cha Mapinduzi kwa kuniteua. Pia, nichukue nafasi hii kuishukuru na kuipongeza UWT (Umoja wa kina Mama wa Chama Cha Mapinduzi) unaoongozwa na Mary Chatanda na Dada yangu Zainab Shomari. Pia, niwashukuru viongozi wa UWT kwa niaba ya Umoja wa Wanawake wa Mkoa wa Tabora, Mwenyekiti wetu Mwanne Mchemba na Rhoda ambaye ni Katibu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru sana kwa mapenzi yako na maelekezo yako juu yangu. Umekuwa ni mtu wa karibu sana kwangu katika kuniongoza katika Bunge hili nilipokuwa mgeni, nakushukuru sana na Mungu akubariki sana. Niipongeze ofisi yako kwa ushirikiano wote ambao wamenipa na wanaoendelea kunipa, ofisi yako inanipa ushirikiano mzuri kwa kupitia Katibu wetu wa Bunge, mdogo wangu Nenelwa ananipa ushirikiano wa kutosha na watendaji wote katika ofisi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru Wabunge wenzangu, Wabunge wenzangu wamekuwa ni chachu kwangu kwa ushirikiano, pia, Kamati yangu inayoongozwa na Mwenyekiti wetu Mhagama. Nimpongeze Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika nchi hii. Mama huyu amejitoa kwa mapenzi na kwa moyo kama tunavyofahamu mwanamke anapofanya kazi, anafanya kazi yake kwa jitihada na kwa moyo wake wote ili afanye vizuri na amefanya vizuri, ana haki ya kupongezwa kwa yale ambayo ameyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nipo kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria; katika maeneo ambayo tumeweza kuyatembelea moja wapo ni Sehemu ya Kwala. Ningemwomba sana Mheshimiwa Waziri atuletee hapa screen, bahati nzuri hizi ni nzima tuletee picha ya ile Sehemu ya Kwala ambayo tumeitembelea ili watu waone. Kusema na kuona ni vitu viwili tofauti, waone pale Kwala, waje waone na Ubungo ni sehemu ambazo huyu Mama amefanya kazi nzuri sana. Kila atakayeona kwa picha tu ambayo bado zoezi halijakwisha, lakini ataelewa ni nini ambacho kinataka kufanyika katika nchi hii na ni nini Mheshimiwa Rais anachotaka kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kutokana na yale mazuri ambayo ameyafanya Mheshimiwa Rais, nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wa Uturuki pamoja na Chuo Kikuu kwa kumpa tuzo Mama Samia Suluhu Hassan. Wameona kazi anayoifanya Mama Samia Suluhu Hassan na macho yao yameona ndiyo maana wameweza kumpa tuzo. Nawashukuru sana na naipongeza Serikali ya Uturuki kwa thamani kubwa waliyompa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nawapongeza pia washauri wa Mheshimiwa Rais, wote ambao wameweza kumshauri na kushirikiana naye na utendaji wote mkubwa ambao ameufanya, kwani wao ni chachu kwake ya kuweza kumwonesha na kumpa dira Mama yetu mpaka anafanya mazuri ambayo tumeyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niangalie kero ambazo wanapata wawekezaji. Wawekezaji wetu wana moyo, tumewatafuta, tumewaleta na tumewapa maeneo, lakini bado wanakumbana na kero ambazo zinawarudisha nyuma. Nina imani haya yanaweza yakamuumiza sana Mheshimiwa Rais kwa sababu alitoka kwenda nje kutafuta wawekezaji na akaleta wawekezaji, wawekezaji wanakuja. Kuna tatizo gani TIC? Kabla wawekezaji hawajaja waweke kwenye website vigezo vyao ambavyo wanahitajika kuwa navyo ili mwekezaji anapokuja kuwekeza hapa nchini, basi awekeze bila ya kuwekewa kikwazo chochote na wale ambao tayari wameshawekeza, basi tuangalie kama kulikuwa na makubaliano tuendeleze makubaliano yale yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, siyo mwekezaji amekuja na ameshaanza kuweka majengo yake anaanza kuleta wawekezaji wengine, leo unaanza kukataa kutoa vitu ambavyo tayari mmeshakubaliana. Hili ni miongoni mwa vitu vinavyorudisha nyuma maendeleo ya uwekezaji nchini kwetu. Tunachohitaji, ifikapo 2025 tuone uwekezaji umeamka kwa kiasi kikubwa sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nikufahamishe kama alivyoongea mwongeaji mwingine aliyemaliza, wawekezaji ni wengi ambao wanakuja katika nchi yetu, lakini kutokana na vigezo vinavyoweza kuwashawishi wawekezaji kuja hapa kwetu hawavipati, hivyo wanakwenda Uganda na wanapofika Uganda wanafungua viwanda, malighafi zinazotoka kule zinakuja hapa Tanzania. Sasa kuna sababu gani ya sisi kushindwa kuweka vile vigezo na kuwapa nafasi kidogo? Tunawakimbiza watu na muda ambao tunawakimbiza wawekezaji wanakwenda kuwekeza kule, sisi bado pale panasimama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna jambo lingine ambalo ni dogo au ni kubwa, wawekezaji wanaandika barua kwenda Wizara ya Fedha, GN mwekezaji hawezi kulipia chochote lazima itoke Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha barua inakaa zaidi ya miezi sita, wana tatizo gani? Wana kitu gani kinachoweza kuchelewesha barua isitoke? Wawajibu, kama wataweza kuwapunguzia kodi wawaambie tutaweza, hawawezi waache. Wanampa wakati mgumu hata huyu Mheshimiwa Waziri mwenyewe anayeshughulika na jambo hili, Waziri anapata unyonge kwa kufanya kazi kwa sababu ya wizara nyingine. Hiyo kwa kweli haiwezi kumpa nafasi Waziri akafanya kazi yake vizuri, wapeni nafasi Waziri afanye kazi yake vizuri. Wawajibu wawekezaji kwa wakati ili kazi iweze kuendelea na mambo yaweze kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, shida nyingine ni vivutio kwa wawekezaji. Tunaweka vivutio gani kwa wawekezaji? Mwekezaji anaweza akaamua kuja kuanzisha kilimo cha miwa, ambayo atawekeza kiwanda cha sukari. Muda anapofika tu, hajatulia Wizara ya Ardhi wameshakwenda, wakitoka Wizara ya Ardhi, wanaingia OSHA, OSHA wakitoka, NEMC inaingia. Sasa kuna tatizo gani hapa? Sisi tunategemea kama wanaweka utaratibu mmoja ambao utaweza kuwasaidia wawekezaji wetu watakaokuja bila ya kupata matatizo na wakawekeza kwa haraka. Hiyo inasaidia kuwapunguzia kero kwa kiasi kikubwa wawekezaji wetu kwani wao ni binadamu. Huwezi jua mwekezaji labda ameenda kukopa pesa ili aje kuwekeza hapa na aanze kuleta maendeleo yake. Aanze kuzalisha na kulipa kodi, lakini unapomchelewesha unachelewesha kwa kiwango kikubwa maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunawaomba wajipange vizuri ili kuweza kutoa kero hizi, kama ni vivutio waviweke na viwe ni vya kweli na hata watakapokuja basi wasiwe wenye kubadilika badilika. Wizara wawe na msimamo, wakiweka msimamo hata nchi yetu itaheshimika na kuthaminika kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipongeze sehemu nyingine ambazo tumeenda, mfano kwa kina Mzee Kamaka, ni mwekezaji wa Kitanzania lakini pamoja na kuwekeza, Idara ya Maji tu wanashindwa kumchukulia maji na kumsogezea pale. Yule amewekeza na akaweka miundombinu yeye mwenyewe, ni Mtanzania wa hapa hapa, lakini kumvutia maji tu kumwekea inakuwa shida. Wanamvunja moyo na wanawavunja moyo wawekezaji wa ndani ya nchi hii, wanakuwa hawana moyo tena wa kuwekeza, kwa sababu ya kitu kidogo. Je, wanahitaji kitu gani pale ili wamvutie na kumwekea maji kusudi shughuli zake ziweze kuendelea? Amewekeza pesa nyingi sana na ni mtu mzima lakini hakujali utu uzima wake kaamua kuwekeza katika nchi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni mapenzi makubwa ambayo ameyafanya. Mheshimiwa Waziri, tunaomba atuwekee, narudia tena Mheshimiwa Waziri naomba atuwekee zile picha za tulipotoka na tunapokwenda. Ubungo pale amefanya vizuri sana na kazi kubwa imefanyika. Kwa wale ambao tumeweza kutembeatembea kidogo tumeona pale Ubungo itakuwa ni sehemu ya kituo cha biashara kikubwa sana katika nchi hii na nchi Jirani zote maana viwanda vyote ambavyo vipo China vitakuja pale kufungua biashara zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wananchi wetu waliokuwa wanasafiri kwenda China wote watachukua bidhaa zao pale. Tanzania, Kenya, Uganda na nchi nyingine watafanya pale. Zoezi ni kubwa sana na soko litakuwa zuri sana, soko lenye maendeleo na nchi yetu itabadilika kwa kiasi kikubwa sana. Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hongera kwa kazi kubwa ambayo amefanya. Nchi yetu ameifanyia haki, anaitendea haki na ni mama mwenye mapenzi, maono na mwelekeo wa mbali sana na nchi hii. Tunajua anaumia kwa nchi yake, ana mapenzi na nchi yake, Mungu atamsaidia atafanya kazi zake kwa amani na baraka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)