Primary Questions from Hon. Aziza Sleyum Ally (3 total)
MHE. SHALLY J. RAYMOND K.n.y. MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kuanzisha Kombe Maalum la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa anajitoa sana kwenye Sekta ya Michezo?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Watanzania wanatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya michezo nchini. Katika kuenzi mchango huo, tayari tumeelekeza vyama na mashirikisho ya michezo nchini kuona namna bora ya kuwa na kombe maalum la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ukubwa zaidi kwa michezo wanayoisimamia, lengo likiwa ni kuwa na mashindano makubwa ya Kitaifa yatakayohusisha michezo mbalimbali yatakayofahamika kama Samia Taifa Cup kuanzia ngazi za chini na tayari Wizara imegawa vifaa katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa wadau tofauti wameanzisha mashindano mbalimbali yanayotumia jina la Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo ni pamoja na Ligi ya Mama Samia Mshikamano Cup (Mbeya Mjini); Dr. Samia Katambi Cup (Shinyanga); Simiyu Samia Marathon; Dkt. Samia Cup (Same); Chato Samia Cup (Chato); na Samia Afya Cup ambayo ni mashindano yanayoandaliwa na Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) na kushirikiana na taasisi mbalimbali za umma na binafsi na mashindano mengine mengi.
MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza:-
Je, Vibali vya Ujenzi hutolewa baada ya muda gani tangu mwombaji aombe kupewa kibali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa vibali vya ujenzi unasimamiwa na Mwongozo wa Utoaji wa Vibali vya Ujenzi na Usimamizi wa Ujenzi wa Majengo wa Mwaka 2018. Mwongozo huo umeweka muda na taratibu za utoaji wa vibali kulingana na aina ya jengo linaloombewa kibali.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha Mfumo wa Kielektroniki wa Utoaji wa Vibali vya Ujenzi wa TAUSI na umeanza kutumika Julai, 2024 kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo halmashauri 47 tayari zinatumia katika kutoa vibali vya ujenzi na halmashauri nyingine zitaanza kutumia. Kupitia mfumo huo, muda wa kutoa vibali umepungua, ambapo kwa sasa kibali kinaweza kutolewa ndani ya siku moja.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE K.n.y. MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza:-
Je, nini mkakati wa Serikali wa kutafuta soko la asali?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa na mkakati wa kutafuta soko la asali ambao unajumuisha mafunzo ya uzalishaji bora katika mnyororo wa thamani wa asali. Ujenzi wa viwanda vya pamoja (common facilities) vya uchakataji bora wa asali, utangazaji wa bidhaa za asali zinazozalishwa nchini katika maonesho ya ndani, kikanda na kimataifa na kujumuisha fursa ya asali ya Tanzania katika majadiliano ya nchi na nchi, kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, hatua hizo zimewezesha kampuni ndogo (SMEs) 46 zinazozalisha asali kuuza tani 337.3 katika masoko ya nje, hususan soko la Ulaya, ambapo nchi zinazonunua kwa wingi ni Ujerumani, Uholanzi na Poland, ikifuatiwa na Soko la Afrika Mashariki (EAC); Kenya, Rwanda na Uganda na katika Soko la SADC, ikiwemo nchi ya Botswana. Jumla ya mauzo katika masoko hayo kwa mwaka 2023 yalikuwa na thamani ya shilingi bilioni 2.0.