MHE. AZIZA S. ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu Kiwanda cha Nyuzi Tabora ambacho kwa muda mrefu kimefungwa hakifanyi kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, tunajua tulikuwa tunazungumzia suala la mbolea na Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusu Kiwanda cha Nyuzi na sisi Wizara ya Kilimo pamoja na Viwanda na Biashara, jambo hili tunalifahamu. Tunafahamu changamoto ambazo zipo katika viwanda vingi vya nyuzi na moja ya mkakati wa Wizara ya Kilimo ambao tuko nao sasa hivi, ni kuhakikisha tunafufua viwanda vingi ili pamba yote inayozalishwa hapa nchini iweze kutumika na hivi viwanda viweze kufanya kazi. Kwa hiyo, mpango tulionao ni huo kwa sasa na tuko serious katika eneo hili, ahsante sana. (Makofi)
MHE. AZIZA S. ALLY: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mkakati gani wa kuinusuru Barabara ya Itigi – Tabora ambayo imejengwa kwa muda mfupi na imeshaanza kuharibika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokifahamu ni kwamba Barabara ya Itigi – Tabora imejengwa yote kwa kiwango cha lami na kama kuna uharibifu ambao siyo wa kawaida na najua ni barabara ambayo siyo ya muda mrefu, namwomba Mheshimiwa Mbunge aweze kutusaidia ama niwaagize Mameneja wa Mkoa wa Singida na Tabora waweze kupita katika barabara hiyo ili waweze kujiridhizisha.