Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hamza Saidi Johari (3 total)

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano, pamoja na Taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge kuhusu Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni kwenye Mkutano wa Kumi na Mbili na Mkutano wa Kumi na Tatu
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kukushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Taarifa hii nzuri. Pili, nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, Mheshimiwa Dkt. Jason Samson Rweikiza pamoja na Wajumbe wa Kamati wote kwa kazi kubwa na nzuri waliofanya na kwa hii taarifa nzuri ambayo inatupatia picha halisi ya changamoto ambazo tunazo katika uandaaji wa Sheria Ndogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuelezea kidogo hali ilivyo kwa sasa katika zile Sheria Ndogo ambazo zimefikishwa kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa ajili ya uhakiki ili baadaye ziweze kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa ya Kamati imeziainisha na ziko tatu. Pia, ingekuwa ni vema leo nikatoa hali halisi ilivyo sasa. Sheria Ndogo ya kwanza ilikuwa ni zile Kanuni za Shughuli za Uzalishaji, Upelekaji na Usambazaji wa Umeme za Mwaka 2023 ambazo zilifika kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uhakiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako kwamba, Kanuni hizi tayari zilishahakikiwa na zimeshatangazwa kwenye Gazeti la Serikali kwa matoleo mawili, Toleo la Kiingereza kupitia GN. No. 677 na lile Toleo la Kiswahili GN. No. 679) na Toleo hili lililotoka 9 Agosti, 2024.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna kanuni za The Accountants and Auditors Training and Examination Bylaws, 2023, naomba kulipa Bunge lako Tukufu kwamba, kazi hizi sasa ziko katika hatua za mwishoni, tumemaliza uhakiki na tunatarajia kutangaza siku ya tarehe 5 Septemba, 2024 kwenye Gazeti la Serikali kwa maana ya kesho Ijumaa. Kanuni zitakazosalia ni zile za ukusanyaji na uchakati wa taarifa binafsi ambazo ziko kwenye hatua za mwisho na nina imani kabisa kwamba, ndani ya muda uliowekwa na Kamati, kanuni hizi zitakuwa zimekwishatangazwa katika Gazeti la Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kusema tu kwamba, kimsingi Kamati hii imekuwa ikifanya kazi nzuri na kutokana na taarifa zao zimekuwa zikitusaidia kama Serikali katika kupunguza dosari na idadi ya Sheria Ndogo ambazo zimekuwa na matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kwamba, katika taarifa hii idadi ya Sheria Ndogo ambazo zinakinzana na masharti ya Katiba zimepungua kutoka 13 na sasa ziko mbili. Kwa hiyo, hiyo ni dalili nzuri kwamba tukiongeza bidii katika kuyafanyia kazi mapendekezo yanayotolewa na Kamati, idadi ya Sheria Ndogo zinazopingana na masharti ya Katiba zinaweza kupungua kabisa kutoka mbili na kuwa sifuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, idadi ya Sheria Ndogo zinazokinzana na Masharti ya Sheria Mama na zenyewe zimepungua. Zilikuwa 27 wakati huo mara ya mwisho na sasa tunazo 10 tu. Vilevile, Sheria Ndogo zenye masharti yasiyoakisi uhalisia hapo bado tunahitaji kuongeza bidiii kwa sababu zilikuwa sita wakati ule na sasa ziko 22. Kwa hiyo, tunahitaji kujiuliza kuwa kwa nini zinaongezeka? Pia, Sheria Ndogo zinazoakisi makosa ya kimsingi ya uandishi huko tumeendelea kufanya vizuri maana zilikuwa ziko 70 na sasa ziko 13 tu. Kwa hiyo, hiyo ni dalili kwamba tunafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Ndogo zinazoakisi suala zima la utengenezaji wa majedwali, kwa mujibu wa sheria hizi zimeongezeka kutoka saba kwenda 13. Kwa hiyo, tunahitaji kuongeza bidiii zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeandaa mkakati mahsusi. Kwanza, ni kutengeneza Mwongozo kwa Mawakili wote wa Serikali nchini ili uweze kuwasaidia wanapotengeneza hizi Sheria Ndogo. Vilevile, watakuwa na orodha au checklist ambayo itakuwa inaainisha hayo mambo ya msingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, ni kufanya mafunzo kwa Mawakili wote wa Serikali nchini, lakini na mafunzo kwa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali. Mafunzo Mahsusi kwa ngazi ya Diploma na ngazi ya Masters ili Mawakili wa Serikali waweze kuwa vizuri na tunaamini kwamba kwa kufanya hivyo, changamoto hizi tutazipunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nikushukuru tena kwa kunipa nafasi hii, ninakuahidi na niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba, mapendekezo yote tutayafanyia kazi kwa lengo la kuboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
The Fair Competition (Amendment) Bill, 2024.
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, ninaomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kufanya majumuisho ya mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) ya Mwaka 2024 (The Written Laws Miscellaneous Amendments (No.2) Bill, 2024).

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kwa kukushukuru wewe kwa uongozi wako mahiri wa kuongoza Bunge hili. Pia, nimshukuru Mheshimiwa Naibu Spika kwa uongozi wake wakati wa vikao vya asubuhi kabla hatujaahirisha mchana. Tumekuwa na mijadala mizuri ambayo imekuwa na lengo la kujenga katika muktadha wa Muswada huu ambao tunaujadili.

Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa nipende kuchukua nafasi hii kumshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Joseph Kizito Mhagama, kwa uongozi wake mzuri pamoja na wajumbe wote wa Kamati ambao waliwezesha wakati wa vikao vya Kamati kujadili Muswada huu vizuri katika mazingira haya ya ushirikishaji na kuridhiana. Pia, maeneo yote ambayo tulikuwa tunaona yanahitaji kuboresha tulikuwa tunakubaliana na matokeo yake. Tumekuwa na hoja chache sana tunapokuja kwenye Bunge lako Tukufu tunapohitimisha hoja hii.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema na kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati, ili tuweze kuandika sheria nzuri ambazo zitaakisi hali halisi iliyoko sokoni, ni vizuri tukashirikishana kwa kina na kuhakikisha kwamba changamoto zote ambazo tunazibaini tunazifanyia kazi kwa moyo mkunjufu kwa lengo la kuboresha.

Mheshimiwa Spika, napenda kukuarifu kwamba katika majadiliano haya tumekuwa na wachangiaji watatu ambao wote walijikita zaidi katika hoja inayohusu MSD. Nikianza na Mheshimiwa Salome Makamba, yeye alisema kwamba hakuna ombwe la kisheria, isipokuwa Serikali iipatie MSD mtaji ili kuiwezesha kufanya biashara. Aidha, Serikali ililipe deni la shilingi bilioni 135 inazodaiwa. Serikali imepokea ushauri wa Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, aidha, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imeanza kulipa madeni ya MSD ambapo kwa mwaka 2023/2024, Serikali imeshalipa shilingi bilioni 100. Aidha, jitihada za kumaliza deni zinaendelea kadri ya upatikanaji wa fedha unavyojitokeza.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Salome Makamba pia alikuwa na hoja kuhusu afisa uhamiaji kutokulazimika kuchukua ushahidi kwa kutumia picha jongefu, picha mnato na kurekodi kwa sauti. Naomba kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba kifungu hiki tayari kimeshafanyiwa maboresho kupitia kwenye jedwali la maboresho kwa kuweka sharti la lazima na tumeweka neno “shall” kwa afisa uhamiaji kuchukua ushahidi wa mtuhumiwa na mashahidi kwa kutumia picha jongefu, picha mnato au kwa kurekodi sauti kulingana na mazingira. Maana wakati mwingine wanaweza wakawa wako porini huko, sasa anaweza kutumia vitu vyote hivyo kulingana na mazingira. Akiwa mjini anaweza kutumia kulingana na mazingira yaliyopo. Kwa hiyo, nimtoe hofu Mheshimiwa Salome Makamba, kwamba suala hili tumeliweka vizuri kwenye jedwali la marekebisho.

Mheshimiwa Spika, pia Dkt. Kaijage yeye aliunga mkono zaidi suala la MSD kujiendesha kibiashara na ni kwa sababu ni mambo tuliyoyajadili wakati ule katika ngazi ya Kamati.

Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Wabunge pamoja na Kamati zako katika kuhakikisha kwamba Miswada inayopendekezwa inajadiliwa kwa spirit ile ile ya maridhiano na kukubaliana katika maeneo ambayo tunaamini kwamba, changamoto hizi tukizitatua kwa pamoja tutakuwa na Muswada ambao ni mzuri na ambao unaakisi hali halisi na siyo kuzua changamoto zaidi.

Mheshimiwa Spika, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba, hakukuwa na wachangiaji wa maandishi zaidi ya hao wachache kwa Muswada huu uliopo mezani. Pia, nichukue nafasi hii kuwashukuru wote kwa michango yenu mizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine tena nichukue nafasi hii kukushukuru tena kwa uongozi wako mzuri. Kwa namna ya kipekee pia niishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa mawazo yao mazuri hasa katika lile suala la diaspora na maoni yao waliyoyatoa kuhusiana na suala hili. Sisi kama Serikali tumeyachukua na tutayafanyia kazi na kuhakikisha kwamba tunaporudi mara ya pili tunarudi kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 2) Act, 2024