Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Sebastian Simon Kapufi (43 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na neno la shukrani. Shukrani hizi nazielekeza katika maeneo matatu. Nimeanza na neno la shukrani nikizingatia na Mheshimiwa Rais wetu alianza na neno la shukrani, kwa maana kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, nikiamini yeye ndiye muweza pekee na nafahamu ndugu zangu kutoka kule Jimbo la Mpanda Mjini sikuyaweza kwa nguvu zangu, ni kwa uwezo wake yeye Mwenyezi Mungu, kupitia kwa waja wake ametusaidia leo kuwepo mahali hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme nikiungana mkono na Mheshimiwa Rais, nitawashukuru wananchi hawa, lakini namna ya pekee ya kuwashukuru ni kuwafanyia kazi na ndiyo maana hata Mheshimiwa alijikita katika hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani hizo naomba nizielekeze kwa wananchi wote kwa ujumla wao. Tutasema maneno mengi, lakini utulivu tuliouona wakati wa uchaguzi ni kwa sababu wananchi walikuwa tayari kushiriki uchaguzi ule na kutoa amani hiyo tunayoendelea kuiona hapa. Kwa hiyo, naomba na nikiamini mwananchi ndiye bosi wangu, ndiye Afisa wangu, hivyo, naendelea kuwashukuru wananchi hao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwashukuru viongozi mbalimbali wa dini, lakini naomba nivishukuru vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama. Katika hili naomba niwe muwazi, nimeushuhudia weledi hasa kule kwangu Katavi, Askari Polisi na vyombo vingine vingine vya
dola vimeshiriki kutufanya tushiriki uchaguzi salama. Kwa hiyo, nisipowashukuru nitakuwa siwatendei haki. Viongozi wa dini nafahamu kwa muda wote wamekuwa wakiliombea Taifa hili, nchi hii amani, kwa hiyo, nimesema ni vizuri nikiwashukuru hawa wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu, amejikita kwenye ahadi na kuna neno moja zuri ambalo nimelipenda katika rejea yake, ametuambia, anaomba atutoe wasiwasi, tulivyoahidi tumeahidi na anaahidi kwamba ahadi ni deni. Hili ametukumbusha sisi Wabunge,
lakini akawakumbusha wenzetu ambao ni Madiwani, tumeahidi na ahadi ni deni.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukimkuta kiongozi mkubwa kama huyu analizungumza hili na hakuna kitu kingine ambacho nimeendelea siku zote kukifuatilia na nikasema huyu mtu kweli Mwenyezi Mungu kamsimamia, pale ambapo muda wote anamtanguliza Mwenyezi Mungu na
anasema katika haya yote mema ya kuifanyia nchi hii tumuombee. Naamini, hakimu mwenye haki ni Mwenyezi Mungu, ndiye pakee atatusaidia kumlinda Mzee huyu ili atimize azma ya haya ambayo amekusudia kuwafanyia Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe ndugu zangu Wabunge, lakini niwakumbushe Madiwani tunayo kazi, tuna ahadi kwa watu wetu, wananchi kwa sasa hivi wameendelea kuonyesha utulivu. Nimekuwa nikisikiliza kupitia vyombo vya habari, ukipita katika makundi
mbalimbali, wanatushauri wanasema hata mkibahatika kuwepo hapo jengoni, hebu toeni nafasi ya utulivu kwa Mzee huyu ili tuone ataifikisha wapi nchi yetu. Kwa hiyo, niwaombe sote tuliopo hapa, tutoe nafasi, hata namna yetu ya kuchangia, kushiriki katika shughuli mbalimbali,
tutoe nafasi ili tuone wapi tutaipeleka nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo, naomba nijikite katika suala la amani na utulivu. Tuna wajibu wa kuilinda amani, ni wajibu wetu mkubwa kuilinda amani na nashukuru katika hotuba yake Mheshimiwa Rais amezungumzia hatokuwa na simile kwa wale atakaochezea amani na utulivu wa nchi hii. Kwa hiyo, ili tuweze kujikita kwenye suala la viwanda, ambayo ni azma kubwa ya kuitoa nchi hii kuifikisha kwenye uchumi wa viwanda, bila amani na utulivu hatuwezi tukafika huko. Nilikuwa najaribu kuangalia usemi mmoja wa Kichina, lakini tafsiri yake ni ya Kiswahili unasema hivi; nikisikia nasahau, nikiona nakumbuka, nikitenda naelewa au nafahamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tunasikia habari ya Mheshimiwa huyu kuhusu suala zima la kwamba hapa ni kazi tu, watu wakawa wanasahau, lakini baada ya kuona yale anayoyafanya sasa hivi kuhakikisha mapato ya nchi hii yanapatikana na maeneo mengine watu wamekumbuka, ahaa, kumbe yale tuliyokuwa tunasikia ni sahihi, lakini kwa hili ambalo tunaendelea kuliona elimu bure ambayo ni matendo yametendeka sasa hivi, ndio tunaendelea kufahamu kwamba Mzee huyu anamaanisha na anatembea kwenye yale aliyokuwa akiyasema.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la elimu, nishukuru kwa sababu zifuatazo:-
Tunapo zungumzia habari ya elimu bure changamoto haziwezi kukosekana, huu ni mwanzo, tumeanza na hilo na changamoto ni kitu cha kufanyia kazi. Siku zote ni muumini wa jambo moja, unapokuwa ni mtu wa kulalamika muda wote, wewe unakuwa ni sehemu ya tatizo, kwa hiyo naogopa kuwa sehemu ya tatizo, niwe sehemu ya kutatua tatizo. Kwa hiyo, changamoto tutakazoziona katika suala zima la elimu bure ambayo hiyo ni sehemu ya kuchangia hotuba ya baba huyu. Nasema kwamba tukiwa wawakilishi wa watu tutakuwa na wajibu wa kusema hapa, maana ukiwa na chai kama haina sukari utafanya zoezi la kuongeza sukari na kama sukari imezidi, unaweza ukaongeza hata maji, lakini tofauti na kutokuwa na chai kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la huduma ya afya, nishukuru na niseme kwamba, kule ninapotoka Katavi eneo hili la huduma ya afya ni jambo muhimu. Watu wetu akinamama na watoto, wazee tuendelee kama alivyozungumziwa Mheshimiwa Rais kuangalia makundi hayo,
kuangalia akinamama, watoto na wazee na ile sera yetu ya afya bure kwa makundi hayo tuendelee kuizingatia na naomba niendelee kumkumbusha Mzee huyu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la barabara, bila kuiunganisha nchi hii na ninashukuru hata kiongozi aliyepita aliongelea habari ya kuunganisha mikoa kwa mikoa, mikoa na maeneo mengine ya Wilaya kwa maana ya barabara kwa kiwango cha lami. Mimi ndugu yenu
ninayetoka Katavi, mkoa ambao leo hii tuna zaidi ya tani 3000 za mazao, natamani kuona mazao haya yakienda kwa Watanzania wengine waliopata uhaba wa chakula, lakini ili tuwafikishie ni kwa kuiunganisha eneo lile na barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hapo niseme Mheshimiwa kwa nia yake njema na nashukuru aliniambia ndugu yangu Kapufi ukibahatika kuwa Mbunge, kanikumbushe katika haya. Naendelea kusema alilolisema kuhusu barabara ni jambo jema, aliyoyasema kuhusu maji
ni mambo mema, aliyoyasema kuhusu afya ni mambo mema na wakati akiyafanya hayo akumbuke kule Katavi aliahidi suala hilo na ndio mkoa pekee uliobakia. Katavi, Kigoma na Tabora hatujaunganishwa kwa kiwango cha lami, tunatamani kuyaona maendeleo hayo na
kushiriki uchumi wa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusema, unapokuwa na sehemu nyingine anavunja barabara kwa sababu ni nyembamba ili aipanue, mwingine hata hiyo nyembamba hana, hapo ni eneo la kufanyia tafakari ya kina. Watu wa maeneo hayo wazalishaji wazuri eneo la
utalii wa nchi hii tuna maeneo mazuri ya kuweza kufanyia shughuli hizo za kitalii niendelee kumwomba Mzee huyu na kwa kuwa haya yote ameyaainisha katika hotuba yake kwamba, tutaangalia maeneo hayo ya utalii, tutaangalia masuala ya barabara na tutaangalia huduma za afya. Katika huduma za afya niendelee kumkumbusha Mzee huyu, tujikite katika vifaa tiba.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, najua kengele hiyo ni ya mwisho, nashukuru kwa kunisikiliza. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba na mimi nianze na pongezi. Naipongeza hotuba hii nzuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imesheheni mambo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya Mkoa wa Katavi naomba nianze na eneo la afya. Mkoa wetu ni mpya, najua zipo jitihada za maksudi za kuusaidia Mkoa ule kwa maana ya kupata hospitali ya Mkoa. Rai yangu ni kwamba kama kwa kila mwaka tunatengewa shilingi bilioni moja na mpango mzima unakusudia bilioni 27 maana yake kuna miaka 27 kuweza kuijenga hospitali hiyo. Ninaomba Serikali yangu sikivu tupaone hapo kwamba watu wale kwa namna yoyote ile wasaidiwe ili kuhakikisha hospitali ya Mkoa inapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la maji niendelee kuishukuru Serikali hii, tulikuwa na mradi wa Ikolongo sasa hivi tunakusudia kuwa na mradi wa Ikolongo II. Mipango yote ya kuhakikisha mradi huo wa Ikolongo Na. II inaendelea kukamilika. Naendelea kuiomba Serikali maji haya ni msaada kwa wananchi wetu, pamoja na kwamba siyo wote wanaofikiwa na maji haya naendelea kuamini, utakapokuja mradi huu wa Ikolongo Na. II uwezekano wa eneo kubwa la Mji wa Mpanda kupata maji utakuwa umekamilika pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo la barabara, mara ya mwisho tarehe 8 Aprili, kulikuwa na uzinduzi wa barabara Tabora – Koga - Mpanda kwa kiwango cha lami, mradi huo umeenda sambamba na watu wa Mbinga - Mbamba bay. Mimi nishukuru kwa jitihada hizo, lakini niendelee kuomba tena kwa maana ya barabara ya kutoka Sumbawanga - Mpanda na hiyo kama haitoshi kutoka Mpanda kwenda Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni muhimu mno kwa watu wetu, siku zote naendelea kusema sioni kama ni sahihi kuwaita wale watu ni watu wa wapembezoni maanake hata Dar es Salaam yenyewe iko pembezoni, lakini suala tu la kuwezesha miundombinu itapelekea kufanya maeneo yale yasisomeke kama ya pembezoni.
Mkuu wangu wa Mkoa nilimpenda siku moja, alisema badala ya kuita ni mikoa ya pembezoni ni bora ikaitwa mikoa ya mipakani maana yake pembezoni inafanya watu wajione kuwa wanyonge na hawana sababu ya kuwa wanyonge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la madini. Mkoa wetu una bahati ya kuwa na madini mengi. Kuna dhahabu, kuna shaba, kuna garena, ni rai yangu na bahati nzuri ndugu zangu wa madini wapo hapa, kwanza nitakuwa mtu wa ajabu nisiposhukuru jitihada za makusudi zinazofanywa hasa kuwawezesha wachimbaji wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiomba, kuna maeneo ya Ibindi, maeneo ya Kapanda, maeneo ya Dirifu, maeneo haya kwanza kuna vijiji kuna makazi lakini maeneo pia ambapo wachimbaji wadogo wamekuwa wakijipatia riziki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo maeneo mengine ya wachimbaji wadogo kutengewa maeneo, ninaomba Serikali hii sikivu iendelee kuyatenga maeneo hayo yawe rasmi kwa ajili ya wachimbaji wadogo, ili watu wao waendelee kukidhi shida zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la uvuvi, Mkoa wetu wa Katavi kwa ujumla wake upande mwingine tuna Ziwa Tanganyika. Tunapozungumzia uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kama ambavyo tumekuwa tukisaidia wananchi wetu kuwapa taarifa mbalimbali za hali ya hewa, kwamba kutakuwa na mvua kali, kutakuwa na mawingu, kutakuwa na nini.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba Serikali iende mbali zaidi, kama tutashindwa kuwa na vifaa vya uvuvi vya kisasa, walau basi iwepo na centre ya taarifa sahihi zinazogusa masuala ya kiuvuvi ili kuwasaidia wavuvi hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni nini? Kama kuna taarifa zilizotoka kwa wataalam wetu kwamba kama Jumatano, Alhamis, Ijumaa mtakusudia kwenda Ziwani kuvua, uelekeo wa samaki utakuwa eneo la Kaskazini, uelekeo wa samaki utakuwa eneo la Kusini, kwa hiyo, mvuvi badala ya kwenda Kaskazini akaachana na samaki wako Kusini, kwa taarifa hizi zitamfanya avue uvuvi wenye tija. Lakini zaidi ya hapo ni kuwa na vifaa vya uvuvi vya kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, naomba nizungumzie suala la bandari. Najua jitihada zinazofanywa na nchi hii na kwa kweli niombe sana, siyo dhambi kuwa hapa tulipo na kusomeka ni nchi ambayo inazungukwa na maji pande zote, tuitumie hii kama ni fursa. Sisi kule kwa maana ya Ziwa Tanganyika tuna bandari ya Kalema, ni bandari ambayo ikifanyiwa kazi vizuri itaendelea kuibua fursa mbalimbali za watu na mali zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoke hapo nije kwenye eneo la misitu. Mkoa wangu wa Katavi kwa sehemu kubwa una misitu mizito. Nilichokuwa naiomba Serikali hii sisi kuwa na misitu isiwe dhambi. Nimeona vyombo vingine vya Kimataifa vinatoa fedha kwa ajili ya watu kuendelea kupanda miti na vitu vingine vya namna hiyo ikisaidia dunia hii kama maeneo ya mapumulio na kuachana na suala la hewa ukaa. Kwa hiyo, sisi ambao kwa bahati nzuri tumeendelea kutunza misitu hii isiwe dhambi sisi kuwa kwenye maeneo ya misitu. Serikali iendelee kuona kwamba watu hawa kwa kutunza mazingira na kwa kuwa na misitu mikubwa wanaendelea kuwasadia watu wa maeneo mengine, kwa hiyo tule nafasi ya sisi kutunza maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo niende eneo la utalii. Tuna mbuga nzuri ya Katavi nilisema mahali pengine na nitarudia tena. Tabia ya watalii kama hana kitu kipya cha kuona hana sababu ya kuja. Kwa hiyo, kwa nchi hii kuna maeneo mengine ambapo watalii wamekuwa wakiyatembelea miaka nenda miaka rudi. Sasa tusiwapoteze watalii hao kwa ajili ya kwenda maeneo ambayo wamekwishaona kwa zaidi ya miaka 15, tuibue fursa nyingine ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, mtalii huyo badala ya kuikimbia Tanzania atakuja kwa kwenda eneo lingine, naomba sana tuinue eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kilimo najua kuna suala la pembejeo, lakini niombe sana habari ya matumizi ya mbegu ambazo hazina uhakika tutaendelea kuwafanya watu wetu wasitoke kwenye mduara wa umaskini. Kwa sababu kama anapanda halafu hana uhakika wa kuvuna huyu mkulima tunamtoaje hapo? Ataendelea kuzunguka kwenye mduara wa umaskini. Kwa hiyo, niombe sana, sambamba na pembejeo lakini tuendelee kuangalia suala hilo la mbegu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la uwanja wa ndege, sikatai maeneo mengine kujengwa viwanja vya ndege lakini kupanga ni kuchagua. Kama kuna viwanja vilikwishajengwa na vingine havikukamilika kwa nini tunakwenda kuanza na vitu vingine vipya? Uwanja wa ndege wa Katavi pale Mpanda ni mzuri, umebakiza mambo machache ili ukamilike na ndege ziweze kufika pale, leo siuoni ukizungumzwa popote pale. Kama tatizo ni route za ndege, Serikali yangu sikivu ifanye hilo kwa makusudi kuhakikisha kama ni shirika letu hili ambalo lengo lake ni kutoa huduma kwa watu wote wapangiwe route, wakienda mara moja wakiona idadi ya wateja inapatikana wao wenyewe ndiyo watajikita katika kuongeza idadi ya route za kwenda huko. Nalisema hilo kwa sababu wananchi wengi wa Katavi wakitamani huduma ya ndege ama wakaipandie Mbeya ama wakapandie Kigoma sometimes wakapandie Mwanza na uwanja uko pale. Nilikuwa naliomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli niendelee kushukuru lakini tukisema tafsiri ya reli ya kati ni kutoka Dar es Salaam kwenda mpaka Kigoma, hiyo inayokwenda Mwanza lakini bila kusahau matawi ya Kaliua, Mpanda na Kalema. Tukilifanya hili lina tija, si kwamba watu tunatamani kulisema hilo, hapana, ni kwa maana ya tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la vijana na mikopo niendelee kushukuru Serikali sikivu. Tukiendelea kuwawezesha vijana wao wenyewe ndiyo wataendelea kuibua miradi mbalimbali ya maendeleo. Kundi hili la vijana ambao wakati fulani wameonekana kama wamesahaulika tukiwajengea uwezo watatoka hapo walipo. Mimi nina mifano hai nikizungumzia kwa mfano wachimbaji wadogo wadogo ambao ni kundi la vijana, vijana hawa…
NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi kwa kuchangia naomba nianze na maneno yafuatayo; mtu mmoja aliwahi kusema hivi; “hata nikifa nisije nikatafutwa makaburini, nikasomeke kwa kazi nilizozifanya wakati wa uhai wangu na wale niliowatendea.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tafsiri yangu ni nini? Hapa tulipo katika jengo hili Tukufu watu wetu kule katika Majimbo yetu, kama kuna mambo mazuri tunayoendelea kuwatendea, umeonekana kwenye tv (television), haujaonekana lakini utasomeka kwenye nyoyo zao na yale uliowatendea. Ndiyo maana leo hii Baba wa Taifa ana muda mrefu amefariki, wengine hata kaburi lake hatujaliona kule Musoma lakini kwa uzalendo aliokuwa nao wa kulijengea Taifa hili amani na utulivu anaendelea kusomeka kwenye nyoyo za Watanzania. Mimi hilo ndilo ninaloliomba, nikasomeke kwenye nyoyo za watu wangu katika Jimbo langu.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la kilimo. Nafarijika kuna fedha za kilimo hapa nimeona hapa na kwa maana ya mkoa wangu wa Katavi kuna takribani shilingi milioni 46 lakini nataka kusema nini? Pamoja na fedha hiyo, kama mnavyofahamu Mkoa wa Katavi ni mzuri, unazalisha kwa kiwango cha hali ya juu, lakini maajabu ni kwamba kwa fedha hizi walizotengewa ni ndogo ukilinganisha na fedha za maeneo mengine. Leo nikiwaambieni kwa maana ya ziada Mkoa ule una zaidi ya tani 345,283 za mazao ya chakula. Kwa hiyo, tutakapokuwa tukitenga fedha hizi naombeni muangalie maeneo kama haya yenye uzalishaji mkubwa. Kuna maeneo ambayo leo hii watu wanazungumzia habari ya njaa, watu wana ukosefu wa chakula, sisi ambao tuna ziada angalia na fedha tuliyotengewa. Naomba hapo mpaangalie kwa umakini.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuzungumzia ni eneo la madeni. Ni kweli watu mbalimbali wanaozidai Halmashauri zetu wasipolipwa inawafifisha Moyo. Nilikuwa naendelea kuomba watu hao waendelee kufikiriwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni maeneo mapya ya utawala. Mkoa wangu ni kati ya mikoa mipya lakini leo hii hatuna jengo kwa maana jengo la mkoa. Ndugu zetu wa polisi wanafanya shughuli zao kwenye jengo ambalo lilikuwa ni la wilaya. Kwa misingi hiyo maana yake wanawazuia wenzetu ambao ni wa Polisi Wilaya kufanya shughuli zao kwa sababu wao hawana jengo. Naomba please watu hawa wa Polisi Mkoa waendelee kufikiriwa kwa maana wawe na jengo lao lakini vilevile kwa maana ya jengo la Mkuu wa Mkoa ili kuweza kupisha kwa sababu wanafanya kazi kwenye jengo ambalo ni la Manispaa ya Wilaya ya Mpanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoke hapo nije kwenye suala la ukusanyaji mapato. Pamoja na kusisitiza matumizi ya vifaa vya kielektroniki, lakini niendelee kusema kuwa tunapokuwa hatufanyi utafiti wa kutosha kuhusu vyanzo vya mapato inapelekea mapato mengi kupotea. Naomba tuendelee kufanya utafiti ili hata pale tunapokusanya tuwe na uhakika ni kitu gani tunachokusanya, hilo ni la muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nirudi kwenye hospitali yetu. Naendelea kuiomba sana Serikali hii kwa maana ya shilingi bilioni 27 ambazo ni makadirio ya ujenzi wa Hospitali hiyo ya Mkoa, kwa utoaji huu wa shilingi bilioni moja moja kwa mwaka, itatuchukua miaka 27 kuweza kumaliza hospitali ile. Naomba namna yoyote iweze kufanyika kuhakikisha tunapata fedha na hospitali ile ijengwe kwa wakati. Nalisema hilo kwa makusudi, jamani mtu kutoka Katavi aende Dar es Salaam, mtu kutoka Katavi aende Mbeya tutaendelea kupoteza watu wetu, kule ni mbali lakini ukombozi pekee ni kwa kuwepo kwa Hospitali ya Mkoa katika maeneo yale.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko wa Jimbo. Kwa maana ya Mfuko wa Jimbo fedha ambayo Mbunge aliyetangulia alikuwa anapewa alikuwa na kata tisa leo hii Jimbo lile limeongezeka kuna kata 15 lakini bado fedha inayotolewa ni ile ile. Naomba suala hili nalo liendelee kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la TASAF, suala hili ni jema, watu wetu wanaendelea kuwezeshwa na mimi nimeliona. Kuna kipindi niliwahi kwenda kutembea Makambako nilikuta kuna mkopo mpaka wa siku moja kwa maana mama anakopeshwa fedha ya kununua jogoo kwa siku moja, akipata fedha ile jamani mama yule kwa maana amekopeshwa shilingi elfu kumi…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sebastian Kapufi, muda wako umekwisha na tunaendelea.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu imara ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta nyingine zote. Naamini unapokuwepo mgawanyo sawa wa rasilimali za nchi, unapunguza ombwe la watu wengine kuilaumu Serikali. Napongeza ujenzi wa barabara ya Tabora - Koga - Mpanda kwa kiwango cha lami ambao utaanza hivi punde. Rai yangu ni mchakato huu wa ujenzi usichukue muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uwanja wa ndege Mpanda uendelee kuimarishwa kwani huduma ya ndege ni muhimu sana. Niiombe Wizara kutupatia huduma ya mafuta ya ndege, sambamba na route za ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati na matawi yake, ikiwemo Kaliua - Mpanda - Karema ni la msingi. Barabara ya Mpanda - Ugala - Kaliua ni muhimu mno, ukizingatia uwepo wa barabara moja bila kuwa na escaping route ni jambo la hatari, hasa pale barabara zinapojifunga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha na kuunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu changamoto ambazo ziko mbele yetu na kimsingi maendeleo ni matokeo ya mgongano wa mambo mbalimbali. Kwa hiyo, tunapozungumzia habari ya maendeleo tusiogope kukumbana na changamoto mbalimbali, la msingi ni tunafanyaje kwa maana ya kukabiliana na changamoto hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najaribu kufuatilia taarifa ya Kamati lakini hotuba ya Waziri na taarifa ya wenzetu kwa maana ya Kambi ya Upinzani, nimefarijika kuona kwamba wote wazo letu ni moja, ni namna ya kumsaidia Waziri tutoke hapo tulipo twende kwenye hatua nyingine. Kwa hiyo, naendelea kusema tusiziogope changamoto, la msingi ni kukabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, uboreshaji wa reli kwa maana ya miradi ya vielelezo. Nafahamu lengo zuri kwa maana ya uboreshaji wa reli ya kati kwa maana ya kuwa standard gauge ni jambo jema, lakini naomba twende mbali zaidi. Nitatoa mfano hai, leo hii pamoja na nia hiyo njema ya kuboresha reli lakini utakapoboresha reli mabehewa ikawa tatizo, suala zima la uboreshaji linakuwa limefanyika ndivyo sivyo. Nalisema hilo kwa sababu gani? Nitawapa mfano hai. Leo hii ukienda Mpanda, Katavi, treni zinakwenda kule kwa reli hiyo ambayo ipo kwa sasa hivi lakini shida kubwa ni suala la mabehewa. Wananchi katika maeneo yale wanakabiliana na changamoto kubwa ya mabehewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme shirika letu linatakiwa litoke hapo liende kwenye hatua nyingine ya mbele zaidi. Litoke kwenye mfumo ambao ulikuwa ukitumika toka enzi hizo za ukoloni liende kufanya kazi kibiashara zaidi. Nashangaa ukifika sehemu unaambiwa hapa tunahitaji abiria 40 tu, kama kuna abiria 100 wanasema idadi ya abiria wanaohitaji ni 40. Sasa wewe kama unafanya kazi kibiashara niliamini ungefurahia kupata abiria 100 badala ya ku-limit kuwa na abiria 40 kwamba abiria 40 ndiyo unaohitaji, 100 siku nyingine, wafanye kazi kibiashara. Nalisema hilo nikitolea mfano hai katika mazingira ya Mpanda, mabehewa ni machache, abiria ni wengi na kama shirika linataka kufanya kazi kibiashara ni kuongeza mabehewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la njaa kama fursa. Nilisikia wakizungumza kwamba nchi za jirani kuna maeneo mengine wenzetu kutokana na hali mbaya ya hewa suala la njaa linawakabili. Sisi Tanzania habari ya chakula Mungu katusaidia, je, tunafanyaje kutumia nafasi hii ya njaa kwa wenzetu kuwa ni fursa kwetu sisi ambao tuna chakula? Wanasema adui mwombee njaa. Kwa hiyo, naomba katika mazingira haya ambapo wengine wanakabiliwa na njaa kwetu sisi iwe ni fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoke hapo niende kwenye suala la ongezeko la watu. Nilikuwa nikijaribu kufuatilia data hapa, zinaonesha ongezeko la idadi ya watu kwa maana ya 2016 ni milioni 50.1 lakini itakapofika mwaka 2025 kutakuwa na watu milioni 63, namshukuru Mungu lakini ongezeko hili la watu linakwenda sambamba na mipango mingine ya maendeleo?
Naomba hilo tuliangalie. Tunazungumzia habari ya watu kuongezeka lakini vipi kuhusu mipango ya uzazi bora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani watu waongezeke lakini wakiongezeka katika mazingira ambapo mipango mingine iko nyuma ndiyo tunarudi kwenye matatizo haya ambayo tumeendelea kuyaona kama migogoro ya ardhi kwa maana watu wameongezeka lakini ardhi haiongezeki, migogoro kwenye maeneo ya hifadhi na maeneo mengine ya namna hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba wakati tutakapokuwa tukiliongelea Taifa kwenda kwenye ongezeko hilo la watu liende sambamba na mipango mingine hiyo kama suala zima hilo nililolisema la uzazi bora, lakini tuangalie na masuala mengine kwamba tumejipanga vipi kwa maana ya matumizi bora ya ardhi ili kuepuka migongano tunayoiona sasa hivi ya wakulima na wafugaji na mambo mengine ya namna hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya Serikali kuhamia Dodoma ni jambo jema, ni jambo la maendeleo, lakini naomba niendelee kushauri jambo moja na si kwa maana ya Dodoma tu ni kwa maana ya miji yote inayoendelea kukua Tanzania. Changamoto tulizoziona kwa Jiji la Dar es Salaam ni kwa kiwango gani changamoto hizo zimekuwa elimu kwetu kwa maana zisijirudie katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Dodoma, Arusha, Mwanza na kwingineko? Yale yote tuliyoyaona ya kuhusu watu kubanana barabarani, wanashindwa kufika makazini kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia tija, unapokuwa na watu wamechelewa kufika katika vituo vya kazi, muda mwingi wako barabarani tija utaipataje? Kwa hiyo, naomba wakati mpango mzuri huu wa Serikali kuhamia Dodoma ukifanyika tutoke hapo twende tukachukue yale yaliyojitokeza katika maeneo mengine na kwetu tusiyaogope, hayo yawe ni fursa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari kuhusu makusanyo katika majengo. Jambo hilo ni jema lakini ukifuatilia hata katika taarifa ya Kamati inasema hivi:-
“…kuhusu majengo ambayo hayajafanyiwa uthamini kukusanya viwango vya kodi vinavyofanana kwa majengo ya kila kundi. Vilevile katika ufanyaji tathmini, Serikali iangalie hali ya uchumi wa eneo husika, thamani ya ardhi na thamani ya nyumba yenyewe katika eneo husika”.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa sababu gani? Haki iende sambamba na wajibu, utakapotamani kupewa haki ya kodi na vitu vingine vya namna hiyo lakini ni kwa kiwango gani na wewe umetimiza wajibu wako? Kuna maeneo leo hii tunaweza tukatamani tupate kodi hiyo ya majengo lakini ni kwa kiwango gani Serikali hii imetimiza wajibu wake wa kuwapatia haki yao ya kimsingi wananchi wa maeneo husika kwa maana ya kuwapa hati husika za maeneo hayo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hilo kwa sababu gani? Kwa mfano, sehemu kubwa ya Mji wa Mpanda watu wanakaa katika majengo ambayo hayajafanyiwa uthamini na hivyo hawana hati za kumiliki maeneo hayo. Kwa hiyo, wakati tukiwa tunakusudia kwenda kuwaomba wananchi hawa watulipe kodi, basi Serikali iendelee kutimiza wajibu wao wa kimsingi wa kuhakikisha watu hawa wanapewa hati zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami niendelee kushauri, fursa alizotupa Mwenyezi Mungu, fursa ya kijiografia kwa maana ya bandari tusikosee na kama kuna sehemu tumekosea tujirekebishe, fursa hii ni adimu. Niliwahi kuzungumza siku za nyuma nikasema tumependelewa na Mwenyezi Mungu kwa maana kijiografia tumejikuta hapa tulipo. Sasa pamoja na zawadi ya jiografia aliyotupa Mwenyezi Mungu tunashindwa kuitumia! Naomba tuitumie fursa hii, changamoto zote zinazojitokeza kwa maana ya bandari tuzirekebishe na iwe ni fursa badala ya kuwa adha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu mapendekezo yakiendelea kujirudia mara kwa mara bila utekelezaji panakuwa na shida hapo. Naomba mapendekezo mbalimbali haya tunayoyatoa basi yaonekane katika taswira ya utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niongelee suala la vipaumbele. Tukiwa na vipaumbele vingi mwisho wa siku tutajikuta tuna vipaumbele ambavyo havijafanyiwa kazi. Tunaweza tusiweze yote kwa wakati mmoja pamoja na nia njema, basi twende kwenye vichache ambavyo tutavifanya kwa kiwango kinachostahili na watu wakaona hili na hili limefanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji, niendelee kuishauri Serikali yangu. Nafurahi kuona wananchi wa Kanda ile ya Ziwa tukitumia chanzo muhimu cha Ziwa Victoria, maji yanaendelea kuwafikia watu katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo, naomba tena, Ziwa Tanganyika ni chanzo muhimu ambacho ametupa Mwenyezi Mungu, tuna sababu gani ya kuendelea kuhangaika na visima virefu ambavyo vingine hata hupati maji wakati tuna ziwa na maji unayashangaa yale pale? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba mipango ile ambayo inaendelea katika ukanda ule na siyo huko tu tukiiangalia nchi yetu yote kwa ujumla wake, naomba mpango huu hata kama utakuwa ni wa muda mrefu tufike sehemu habari ya maji iwe ni historia. Kwa sisi ambao tuna water bodies zimetuzunguka, una Ziwa Victoria pale, Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, sijazungumzia mito mikubwa habari ya maji iwe ni historia. Kupanga ni kuchagua, kama tumechagua kwamba sasa tunakwenda kupambana na habari ya maji, tupambane! Ndiyo maana nimetangulia kusema tuwe na vipaumbele vichache ambavyo tunaweza tukavifanyia kazi kwa kiwango kinachostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ulindaji wa bidhaa za ndani na walaji pia, napata tabu sana. Siku za hivi karibuni kupitia vyombo vya habari nimeendelea kuona hata bidhaa kama dawa sehemu ambapo pameandikwa muda wa matumizi wa dawa hiyo watu wachache wasiowapenda Watanzania hawa wanakwenda kufuta ili bidhaa hiyo iendelee kuwepo sokoni. Hata kama tutakuwa na mipango mizuri wakati afya ya wananchi wetu iko mashakani hiyo mipango ni akina nani watakwenda kuifanyia kazi? Kama hatutahakikisha tunalinda afya ya watu wetu, kama hatutahakikisha chakula wanachokula watu wetu ni kile ambacho kinastahili, mipango yote hii itakuwa haina maana kwa sababu mwisho wa siku wale ambao walikuwa ni walengwa watakuwa wameshazikwa wote na wamekwenda kaburini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, nakuja eneo la changamoto, si kwamba Mheshimiwa Waziri haya yote tunayoyazungumza hayasikii au hayaoni, kuna sehemu nilifarijika kuona ameandika changamoto na namna ya kuzifanyia kazi. Kwa mfano, kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi, nimefarijika kuona Mheshimiwa Waziri kumbe anafahamu huko kwenye eneo la kodi kuna mwanya mkubwa na hata hizi mashine tunazozungumzia sasa hivi watu wengine wajanja wanaziharibu kwa makusudi. Ukiliacha hilo, kuna maeneo unaweza ukaenda mashine ipo lakini hupewi stakabadhi kutoka kwenye mashine unapewa ambayo imeandikwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani twende kwenye hatua moja zaidi, inawezekana hata tungekuwa na mashine nzuri namna gani, hata tungekuwa na mipango mizuri namna gani kuhusu suala zima la kodi, hebu turudi kwenye mioyo ya watu, turudi kwenye suala zima la elimu ikamfikie kila mmoja kuhusu umuhimu wa kodi. Kwa sababu leo tunapozungumza kuna sehemu fedha imekosekana, mtu ajue kabisa kwamba yeye ni sehemu ya kutukwamisha kufikia kule tulikokusudia kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, elimu hiyo ikiendelea kutolewa na watu wafike sehemu kama ni makanisani, mashuleni wawe pia na hofu ya Mungu. Kwa sababu mimi naamini hata hizo nchi nyingine ambazo tunaziona zimepiga hatua ni wakali katika suala zima linalogusa kodi. Kwa hiyo, nataka kusema hilo nalo la changamoto ambazo Mheshimiwa Waziri ameziona tuendelee kuzifanyia kazi kwa mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nafahamu unaweza ukawa na bilauri ina maji yamefika katikati itategemea mtu anakusudia kuleta picha gani. Mtu mwingine anaweza akakwambia ameiona bilauri maji yako nusu lakini mwingine akakuambia ameiona bilauri imejaa maji lakini imejaa maji nusu. Kwa hiyo, yupo atakayekuambia haina maji nusu lakini yupo atakayekuambia ina maji nusu. Kwa hiyo, ni namna ya mtazamo tu kila mmoja anakusudia kulitazama jambo kwa namna gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote, nami namshukuru Mwenyezi Mungu kuwepo mahali hapa wakati huu. Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Serikali za Mitaa, kwa misingi hiyo, mambo mengi tunayoongea haya tulipata nafasi ya kuyajadili katika ngazi ya Kamati.

Mheshimiwa Spika, niendelee kushukuru katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa maana ya fedha iliyotoa…

SPIKA: Nawaomba Wabunge ambao mmesimama upande huu, mnaopiga soga, kwanza mkae kwenye viti vyenu ili uchangiaji uweze kuendelea vizuri.

Mheshimiwa Kapufi, endelea.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali kwa maana ya lile zoezi la ukarabati wa shule kongwe. Zoezi hili limekwenda vizuri. Kote tulikopita; Jangwani, Azania, Kilakala, tumeona kazi nzuri iliyofanyika. Pamoja na kazi nzuri hiyo, changamoto hazikosekani, ni pamoja na eneo hilo la force account kama walivyozungumza Wajumbe wengine.

Mheshimiwa Spika, rai na ushauri wangu kwa Serikali, force account linaweza likawa ni jambo jema, lakini tusipojikita kwenye thamani ya fedha, suala la force account naliona lina matatizo pia. Tuliweza kupita kwenye shule moja, kama sikosei kama siyo Kilakala itakuwa ni Mzumbe; jengo la nyuma wataalam walishindwa kutindua cement. Walishindwa kutindua sakafu kwa sababu ya uimara wake, kiasi kwamba wakaamua kuiacha ilivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna baadhi ya majengo yanajengwa leo, kesho sakafu ni mbovu. Narudia kushauri suala la thamani. Tusipojikita hapo, tutajikuta tuna idadi kubwa ya vitu vilivyotengenezwa vyenye ubora hafifu. Naomba sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu na Maendeleo. Kwa nyakati tofauti tumekuwa tukikuita kushiriki katika semina zetu. Kama Mwenyekiti wa Chama hicho, nataka kusema nini kwenye Bunge hili? Idadi ya watu siyo tatizo, lakini ukiwa na idadi kubwa ya watu ambao ni tegemezi, tatizo linaanzia hapo. Tafsiri yangu ni nini? Leo tutaishia kutamani kujenga madarasa mengi, kuongeza madawati, lakini bila kwenda kuzingatia suala la idadi ya watu, kwa sababu kwa kupitia idadi ya watu ndiko huko ambako tunaweza tukapanga mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikilisema hilo namaanisha nini? Unapokuwa na kundi kubwa la watu ambao ni tegemezi na wachache ambao ni wazalishaji, hapo lipo tatizo; lakini kwa maana ya idadi ya watu na maendeleo, bado inaweza ikatumika vizuri ikawa ni chanzo cha maendeleo pia. Ikitumika vizuri! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikilisema hilo naendelea kumaanisha nini? Tukijikita kwenye kujua idadi ya watu, leo hatuna sababu ya kukimbizana na kufanya mambo kwa design ya zimamoto. Unajua kabisa tuna idadi hii ya watoto ndani ya muda huu watatakiwa kufika shuleni, ndani ya muda huu watahamia hapa, na hapa na watakwenda pale. Kwa hiyo, mipango yetu yote italiangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaendelea kushauri, katika hilo, tukiwa na idadi ya watu, bado mimi naweza nikasaidia kuishauri Serikali, tunafanya nini katika hili? Ni pamoja na kutoa elimu. Tusiache elimu kwa watoto wa kike. Mtoto wa kike tunapompa elimu maana yake ni nini? Kwanza ule muda atakaokaa shuleni na akapewa elimu nyingine ya kumsaidia kuepuka mimba za utotoni na ndoa za utotoni inatusaidia kuepuka kuwa na idadi ya watu wengi ambao baadaye wanakuja kuwa tegemezi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo. Wengi wameongelea habari ya TARURA. Namkumbuka Marehemu Baba wa Taifa, alisema hivi, “ukiwa kiongozi, ukapita mtaani, ukamwona mtu mmoja labda hana chakula, yule hana nguo, mwingine hajapata dawa hospitali, kiongozi unatakiwa kusema, huu ni mzigo au msalaba wangu.”

Mheshimiwa Spika, tafsiri yake ni nini? Leo ukienda kwa mfano Manispaa ya Mpanda, ule mji siyo tu kwamba barabara hazipo, lakini kwa mvua zinazoendelea kunyesha tumetengeneza mitaro. Kwa hiyo, TARURA wasipoongezewa fedha ile shida iliyokuwa inajitokeza ya mitaa ambayo barabara zake hazieleweki, tunakuja kwenye tatizo lingine, nyumba za wananchi wetu zimekuwa zikining’inia.

Mheshimiwa Spika, leo ukipita Mbunge, kama nilivyosema, Baba wa Taifa alikuwa anasema huu ni mzigo wangu, nami kama Mbunge, japo ule ni mzigo wangu, lakini nimetimiza haki yangu ya Kikatiba ya kulisemea suala hilo hapa Bungeni. Kwa hiyo, nisaidieni kunitua mzigo wataalam ninyi kwa sura ile iliyopo ya barabara pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili Mtendaji Mkuu wa TARURA ni mtu rahimu, lakini peke yake bila kumpa fedha atafanya nini? Kwa hiyo, naomba sana. Wakati wote tukipiga kelele TARURA iongezwe fedha, tunaishauri nini Serikali katika suala la kuongeza fedha eneo la TARURA? Wapo wanaozungumzia labda kwenye miamala ya simu tukiongeza kidogo hapo, sasa wataalam nendeni huko mkatusaidie kwamba chanzo gani kingine tunaweza tukakibuni kikatusaidia watu hao wakapata fedha ili wakati tunatafuta haki na wajibu uwepo pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa eneo la elimu; mimi kwangu Katavi ni bahati mbaya yale maeneo yanasomeka kama maeneo ya pembezoni. Kipindi cha nyuma wakati wa Awamu ya Nne ilikuwepo mikakati ya makusudi ili kuikomboa mikoa ya pembezoni. Leo maeneo yetu yale, kwa mfano, ukiacha tatizo la barabara, leo unaweza ukakuta hata kama mmeipatia fedha Halmashauri jirani ya Nsimbo kwa barabara moja, mfano barabara ya kutoka Mpanda kwenda Mtapenda, barabara ile ukiwa umeipa Halmashauri ya Nsimbo fedha, wakati yule mtu lengo lake aje mkoani nami wa Manispaa hujanipa fedha na daraja halipitiki, bado ile thamani ya fedha hutaiona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hayo mambo yanafanyika maeneo mengi. Tanganyika likewise; unakuta mwenzangu amepewa fedha lakini hawezi kuunganika kuja mjini. Barabara za kuja mjini hazipitiki. Kwa hiyo, naomba sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la elimu kama nilivyosema, kuna mazingira ambapo baadhi ya watendaji; walimu, mimi mwaka 2014 ndiyo mara ya mwisho kupata walimu wa Shule ya Msingi. Mpaka leo sijawahi kupata walimu wa Shule ya Msingi. Walimu wa Shule ya Sekondari unaweza ukaletewa wanne. Kwa sababu sisi ni mikoa ya pembezoni, inafika mahali wengine wanahama, kwa hiyo, kuna shida kubwa katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la afya, wengi wameongelea. Nami pale Manispaa ya Mpanda nina kituo kimoja tu cha afya. Sasa unapokuwa na kituo kimoja, hospitali ya mkoa haijaisha, mnafanya tunakuwa pembezoni zaidi. Tungeweza kupunguziwa upembezoni huo kwa kusogezewa huduma hizi karibu na maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafahamu eneo la miradi mingineyo, sisi leo tunakwenda karibia awamu ya pili upande wa barabara za lami. Sisi ni Manispaa. Manispaa nyingine wanabahatika kupewa kilometa chache za lami, lakini Mpanda sijui tumesahaulika katika nini? Naomba nalo hilo lijaribu kuangaliwa.

Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho tulipiga kelele, hata fedha tu za maendeleo kwa maana ya Mpanda Manispaa hatukuletewa. Ni baada ya kupiga kelele ndiyo tukaletewa fedha hiyo. Ni bahati mbaya, kuna kipindi fedha ikipelekwa ambayo leo ni Tanganyika, kipindi hicho ikiitwa Mpanda kama sisi; au ikipelekwa maeneo mengine, watu wa Manispaa tunaonekana tumeletewa fedha. Hilo tatizo limetuathiri sana. Mgao kwa maana ya Manispaa, tumeathirika sana katika eneo hilo. Kwa hiyo, naomba, kama nilivyosema upande wa walimu na mambo mengine ya namna hiyo, naomba sana tujaribu kuzingatiwa hapo.

Mheshimiwa Spika, nimalizie, kipindi cha nyuma walikuwa wanasema usiniletee biashara ya nyanya. Tafsiri yake ilikuwa nini? Maana yake katika ubovu wa barabara, unaweza usiifikishe nyanya sokoni. Leo hii katika mazingira ya barabara nzuri, hata nyanya bado ni biashara. Kuna maeneo mbalimbali, Ilula huko na kwingineko, miji imekua, biashara ya nyanya imesababisha maendeleo ya watu. Kwa hiyo, hata ile kauli iliyokuwa ya kubeza biashara ya nyanya imetoweka baada ya uwepo wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami nitajikita katika maeneo yafuatayo: Awali ya yote pamoja na kutoa pole kwa Watanzania wenzetu, lakini inanirudisha kwenye Mpango wa suala zima la usimamizi wa maafa. Kuna kifungu cha 35 cha Sheria ya Bajeti Sura ya 439, kuanzishwa kwa Mfuko wa Dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kuamini kwamba wenzetu katika suala zima la mipango ni kweli mengine yanakuja kwa mapenzi ya Mungu na vitu vingine vya namna hiyo. Hata hivyo ni vizuri tukajua kwamba maafa yapo na kwa misingi hiyo kama nchi tusipotengeneza mazingira maana yake inapofika sehemu Mtanzania anapoteza maisha kwa sababu tu hakuna gari ya kunyanyua kitu kizito anapata tabu. Kwa hiyo naendelea kuomba eneo hilo la usimamizi wa maafa tufike sehemu kama nchi mipango yetu tujielekeze huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa uchambuzi wa Kamati. Kamati imesema kwamba sekta zote zilizokua kwa kiasi kikubwa zimetokana na Serikali kuwekeza zaidi katika sekta hizo. Kwa mfano; Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Viwanda, Utalii na Uvuvi wa Bahari Kuu, lakini natamani kuongeza na madini. Hata hivyo, tumeambiwa Mfumuko wa bei, kupanda kwa bidhaa, mafuta ya kula, mbolea na petrol, UVIKO-19, Vita vya Urusi na Ukraine vimesababisha hilo. Hata hivyo, bado Kamati imetukumbusha kwamba haya tuyatumie kama fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napitia mtaalam mmoja wa Singapore, alikuwa anaeleza mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtaalam huyu alikuwa anasema nchi yao ya Singapore ni ndogo lakini wamewekeza katika size ya ngumi wakiutaja ubongo. Sehemu kubwa ya bajetii yao wameipeleka kwenye elimu kuhakikisha watu wanasoma. Baada ya kusoma kwa watu wao, wanaamini kwamba kwanza nchi ni ndogo, hawana eneo la kilimo, natural resources ni haba na kwa sura hiyo wameamua kuwekeza kwenye elimu ili sayansi na teknolojia yawe ni matunda na wamefika mahali ambapo umaskini wa nchi yao umegeuka kuwa ni utajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najiuliza nini? Kwa nchi kubwa kama Tanzania, hivi siku zote tunazungumza hapa na hata mimi nilishawahi kusema hapa, nchi kubwa kama hii mipango yetu hata tu uwepo wetu hapa tulipo, kijiografia, hivi mipango hiyo haituelekezi tuitumie kama ni fursa? Nchi zote zinazotuzunguka watu wanatutamani hapa tulipo, lakini niseme tu hata katika ardhi, yote yanayozungumzwa whether ni njaa ama ni nini bila matumizi bora ya ardhi hatutoacha kushuhudia ugomvi wa wakulima, wafugaji na watu wengine. Mipango yetu inasemaje katika maeneo hayo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kurudia kama siku nyingine unavyoniambia Mr. Kapufi declare wewe ni nani? Mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. Naomba nijikite katika eneo hilo la uchimbaji mdogo wa madini. Amezungumza Mheshimiwa mmoja hapa akitaja nchi kwa upana wake na idadi ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, labda sijui tunapata tabu, mtu mmoja aliniambia ukienda sehemu halafu ukamwagiwa vitu vingi, kwa wakati mmoja unashindwa kujua uchukue hiki au hiki au hiki. Sasa nchi nzuri Tanzania madini yapo ya kutosha na tumeambiwa idadi hiyo nyingine, nataka nijikite tu kwenye madini ya dhahabu. Leo mipango yetu niseme angalau kwenye kilimo Serikali inatoa ruzuku, vipi kwa wachimbaji hawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie hivi, amini usiamini dhahabu pekee inaweza ikafanya vitu vingine vikasubiri kwenye nchi hii. Pia achilia madini hayo mengine, nina mfano hai, kama kweli tumewawezesha vizuri watu wa GST, kwa maana ya tafiti zao, mtu unajua kabisa kwamba mashapo yaliyopo hapa, kwa maana kwamba, katika ekari moja pale chini ya ardhi labda huyu mtu ana kilo tatu, nne, tano au sita za dhahabu. Sasa utafiti utuelekeze tunaitoaje dhahabu hapo chini ili igeuke kuwa fedha? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sura hiyo hatutawafanya wachimbaji waonekana wanashiriki ushirikina, kwa sababu tafiti zinaonyesha kwamba hapa chini kuna madini kiasi hicho na labda ni three grams per ton or five grams per ton, tengeneza mazingira tani kadhaa ziweze kuzalisha kiasi kadhaa cha kilo za dhahabu. Kwa sura hiyo, kwa kufanya kisayansi kama hivyo, tunaitoa nchi hii na itafika mbali. Pia niendelee kusema, bado naamini hatujafanya vya kutosha na wenzetu wa fedha mipango yetu iende huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingine zao lao ni moja uvuvi tu na wako mbali. Sasa Tanzania ukija kwenye uvuvi tuko vizuri, kwenye madini tuko vizuri na leo sioni sababu ya nchi kulalamika kuhusu kilimo. Niliwahi kusema hapa na Mheshimiwa Kingu akaniunga mkono, nilisema je, tuna mpango wa mtandao wa maji wa nchi hii? Leo ukitengeneza mtandao wa maji hauzungumzii njaa, hauzungumzii sijui shida ya maji. Je, hatujikiti huko jamani? Nilizungumza ndani ya Bunge hili, nchi kubwa kama China unaunganishwa kwa mtandao wa maji kwa vyanzo vyao tu, labda kutoka kaskazini kwenda kusini, kutoka mashariki kwenda magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la maji tu, mipango ikijielekeza na kwa kutumia vyanzo vyetu tulivyonavyo, tuiweke kwenye mipango, hapa naomba pia twende mbali zaidi. Nimeona tumeambiwa kuhusu ununuzi wa vifaa vya kuchimba mabwawa na kuchimba visima. Bado Serikali wasiache kwenda kwenye tafiti. Sehemu nyingine duniani baadhi ya miji imeanza kuzama kutokana na uchimbaji wa maji haya ya visima. Kwa hiyo ningeweza kuishauri nchi yangu, sikatai, visima tuchimbe lakini tusisahau tafiti ili kuepuka hilo. Hata hivyo sehemu kubwa ya kuweza kupata maji ni kukinga maji ya mvua yanayopotea kwenda baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwa maana ya kufungamanisha fursa, leo unaweza ukakinga maji hayo na ukafanya shughuli zifuatazo: Utalima, kwa maana ya kumwagilia; Utafuga kwa maana ya samaki hapo; na Utafanya utalii kwa sababu ndani ya maji hayo hayo, watu wanaweza kufanya utalii ikiwemo man-made lakes and whatever, watu wanafanya mpaka utalii. Kwa hiyo tuyaangalie hayo…

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kumpa taarifa mzungumzaji kwamba hata nchi zinazoendelea wanatumia maji ya bahari, wanaya-purify na wanayarudisha kuyatumia. Kwa hiyo hata nchi yetu ianze kufikiri namna ambavyo tunaweza kwenda kwenye utaratibu wa kutumia maji ya bahari kwa sababu hata kina cha bahari kinaongezeka.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nusrat wana-purify au wanafanya desalination?

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu mimi ni Mswahili, naomba nitumie Kiswahili, wanayaondoa chumvi, wanayasafisha, wanayaondoa chumvi, yanatumika.

MWENYEKITI: Kwa hiyo ni desalination. Haya Mheshimiwa Kapufi.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepokea taarifa, lakini nimsaidie tu dada yangu hatujafika mahali pa kutumia maji ya bahari kwa vyanzo tulivyonavyo nchi hii. Maziwa yote tuliyonayo nenda Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, ziwa Nyasa, mito mikubwa mpaka tukaikute Bahari ya Hindi ni baadaye sana. Kwa hiyo sasa hivi nchi ijielekeze kwenye vyanzo vyote vikubwa tulivyonavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba, nafahamu kila mmoja anasema kilimo ni uti wa mgongo. Siamini sana kwa watu wengi kushiriki kilimo halafu ni kilimo kisicho na tija. Bora wachache wakafanye kilimo walishe wengine, wengine wakavue, wengine wakachimbe na kadhalika. Nchi za wenzetu percent kidogo ya watu wanaoshiriki kilimo wanalisha the rest of the world. Sasa sisi asilimia kubwa lakini hatujilishi hata wenyewe, kuna kitu cha kufanya hapo, lazima turudi tupaangalie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sio muumini wa nchi nzima kulima korosho au kulima sijui kama nini, mimi huko sipo. Tugawe kanda za kilimo, haiwezekani wote tukawe wakulima wa parachichi au korosho. Kwa hiyo mipango yetu nayo ijielekeze huko isije ikawa Mtwara walipata bei nzuri ya korosho, basi nchi nzima tunataka tulime korosho. Ikawa sijui Rungwe walipata bei nzuri ya parachichi, wote tunataka, hapana. Tugawane Kanda za kilimo, lakini kila watu wafanye kwa tafiti na mambo mengine ya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado narudia kusema, kwa kupitia madini peke yake, mipango ijielekeze huko na kama leo kwa mfano tunatoa ruzuku za kilimo, wachimbaji hawa wadogo wapewe ruzuku. Naamini kwa kufanya hivyo, Marehemu Rais John Magufuli alituita wachimbaji wote, akasema nataka mniambie mnafanyaje kuitoa nchi hapa ilipo kwa kupitia madini? Hata hivyo, watu waliuza mawazo yake, kwa hiyo hata kwa mipango yetu hebu tuwashirikishe hawa, kwa sababu kuna wakati ukisikia kuna gold rush, mfumuko wa dhahabu somewhere, ni kazi ya wachimbaji wadogo. Sasa kama mchimbaji mdogo ndiye anaweza kugundua dhahabu shambani, anagundua akiwa anachimba kisima, watafiti wetu wako wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, twende mbali zaidi, kwa kupitia taarifa zile, kwa mfano kama ni GST wangefanya vizuri, taarifa ya kitafiti isimame, ni fedha. Leo kuna watu wengine kwa kuuza tu taarifa za kitafiti wanasababisha watu wengine wawe matajiri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na niwashukuru ndugu zangu wa Wizara hii, lakini kwa ujumla wake nilifarijika niliposikia kwamba hawataacha kupeleka fedha katika maeneo yetu hata kama tutakuwa tumepata hati chafu. Jambo hili ni jema na yule aliyehusika kupelekea hati chafu ndiyo aadhibiwe, wananchi waendelee kupelekewa maendeleo, hilo ni jambo zuri na ni jambo lenye afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya kwanza kama si 2015 nilisimama hapa nikaendelea kuongelea habari za utalii, lakini habari za Ngorongoro. Bahati nzuri kipindi hicho nilikuwa ni Mjumbe wa Kamati hiyo wa mambo ya Maliasili na Utalii. Nilitembelea Ngorongoro, nilitembelea Loliondo, moja kubwa ambalo niliwahi kulisema wakati ule na nitalisema leo, bila utashi wa kisiasa hatuna Ngorongoro, bila utashi wa kisiasa hatuna Loliondo. Niseme, leo tunaiona hiyo Ngorongoro nzuri, Loliondo nzuri ni kwa sababu imehifadhiwa, bila uhifadhi hatuna maeneo hayo. Leo utatamani ni kwa sababu tumehifadhi, lakini tusipohifadhi ni eneo kama eneo lingine lolote, lakini kwa kupitia uhifadhi ndiyo panapata heshima hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na tusisahau hiyo kauli nimemsikia hata mwenzangu mwingine akiongea hapa, mazingira yaliyoharibiwa hayana huruma, yatakuadhibu tu hata kama ni miaka hamsini ijayo. Kwa hiyo, hilo Mheshimiwa kwa unyenyekevu mkubwa sana naomba tusilisahau. Katika eneo la utalii bosi wetu kafarijika kwa masuala ya Royal Tour na vitu vingine, lakini bosi wetu na naomba hapa tuelewane vizuri, atafanya yote, lakini katika eneo la utalii, bosi wetu ni mtalii na usipotii kiu yake haji, usipotii kiu ya mtalii haji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu anahangaika, anakusanya fedha zake kwa muda mrefu ili kuja kutembea Tanzania, kwa hiyo wewe usipotii kiu yake, usipotengeneza mazingira rafiki haji, ana uwezo wa kwenda sehemu nyingine yoyote. Hapa naomba tuendelee kuelewana vizuri, yawezekana sisi kama Tanzania, kama nchi, leo nafarijika, kuna baadhi ya maeneo huko duniani vyanzo vyao vya utalii labda ni jengo refu, kitu cha namna hiyo, sisi Mungu ametupa zawadi ya pekee, leo hii fanya ufanyavyo hata kama utaweza yasukume maji kama ambavyo wengine wamesukuma maji ya bahari ya hindi but thus not Ngorongoro, fanya ufanyavyo hata kama utatumia grader kupalilia viwanja kama 10 au 15 but that is not endless plains kwa maana ya Serengeti. Serengeti ina namna ya pekee, Ngorongoro ina namna ya pekee, hao wenzetu wengine vitu vyao ni artificial, vya kwetu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo, zawadi hii isiwe laana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tabia ya Mtalii nimesema usipotii kiu yake haji na naomba hapa tuelewe vizuri, kuna matabaka ya watalii. Wakati tumejipanga vizuri kabisa kwenda kuimarisha utalii wetu, kutangaza utalii wetu, vipi kuhusu sekta nyingine, naomba sana, kuna eneo hili, je, tumejipanga vizuri kwa maana ya trained personnel, watu ambao wapo well trained, kwa sababu kuna mtalii wa madaraja, achilia kuna mtalii wanamwita labda mtalii kishuka, mtalii ambaye tunabanana wote huku huku, mahindi ya kuchoma na vitu vingine vya namna hiyo, lakini kuna mtalii anakuja anauliza je, kama nime-fall sick, nimeugua napata wapi tiba? Je, kama nchi tumejiandaa kwa hilo? Nitatibiwa wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, isije kuwa tumetengeneza vizuri, tumeimarisha utalii wetu, lakini ikitokea amekuja mtalii wa kiwango hicho, unaanza kuzungumzia habari ya flying doctors labda tumsafirishe kumpeleka nchi ya Jirani, maana yake nini? Mmepambana kuinua utalii lakini inapokuja ni suala kama hilo kwamba you are finding flying doctors ili kumpeleka nchi za jirani. Kwa hiyo, maana yake tujipange kwenye maeneo mapana zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wanashindwa kuelewa jambo dogo kwa maana ya customer care. Leo hii kuna baadhi ya nchi ukifika tu uwanja wa ndege hata jinsi taxi drivers wanavyokupokea, inakupa nafasi ya kujua kwamba hapa napokelewa. Katika maeneo hayo wenzetu wa Wizara watengeneze mazingira, waandae watu wetu hata kama ni kwa kupitia semina tuwaandae watu hawa. Nimezungumzia habari ya well trained personnel, waiters and waitresses, watu hawa wakiwa well trained hata kama ni kwa semina, najua ni chanzo cha mapato kwa sababu mtalii huyo ambaye atakuwa amehudumiwa vizuri hawezi akaikimbia nchi hii, lakini hawa watu ambao ni well trained wana uwezo wa kuiuza nchi hata katika sekta nyingine. Unakutana na mtu anakwambia Tanzania hii tuna madini haya, tuna haya, lakini sio mtu unakutana naye, ndiyo kwanza anasema kama hutaki acha. Tunawaandaje watu wetu? Hili ni jambo la msingi sana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, naomba niende katika sekta nyingine ambao ni eneo la madini. Naomba ifahamike vizuri, madini ya Tanzania, utajiri tuliopewa na Mungu, hatuko peke yetu. Hata kama ni dhahabu, hatuko peke yetu. Kwa hiyo, unapokuja na tozo; kwa mfano, sasa hivi tuna asilimia mbili ya kodi ya zuio. Wachimbaji wadogo waliwahi kukaa na Mheshimiwa Marehemu Dkt. Magufuli, tukazungumzia habari ya kutoa tozo hizo, na hii ndiyo unaona sasa hizi makusanyao ya dhahabu ni makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri mkafahamu tunapozungumzia mchimbaji mdogo, tuelewe mchimbaji mdogo ni yupi? Tafsiri ya mchimbaji mdogo ni ipi? Kuna mchimbaji mdogo jamani, hata machinga ana nafuu. Sasa mtu huyu, kama ndio huyu kweli mnamlenga kwa maana ya kodi hiyo, maana yake katika maeneo hayo ya machimbo kuna mtu unakuta amekaa miezi sita hajapata hata gramu hata moja. Ni vizuri pia mkayasoma mazingira hayo. Kwa hiyo, katika mazingira hayo, kuna mtu huyu kama hujamtengenezea incentives, atatorosha madini yako. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba watu wa Wizara, Serikali imefanya kazi nzuri ya kutengeneza masoko, wachimbaji wanatoka katika maeneo yao, wanapeleka dhahabu sokoni. Bananeni na hawa wanunuzi wa pale; kama kuna utoroshaji hapo, mbanane hapo, lakini nje ya hapo nakuhakikishia… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kapufi!

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Naam Mheshimiwa Naibu Spika.

NAIBU SPIKA: Kaa chini kwanza.

Kanuni yetu ya 68 kutozungumza jambo ambalo lina maslahi binafsi ya kifedha. Wakati wa majadiliano Bungeni au kwenye Kamati yoyote ya Bunge, Mbunge hataruhusiwa kuzungumzia jambo lolote ambalo yeye mwenyewe ana maslahi nalo binafsi ya kifedha. Ina utaratibu mwingi sana. Kwa nini nakwambia hivyo? Kifungu kidogo cha (2) kinasema, “kwa madhumuni ya Kanuni hii, Mbunge au mwananchi yeyote anaweza kumwarifu Spika kwa maandishi akitoa na ushahidi kuwa Mbunge amezungumzia jambo ambalo ana maslahi nalo binafsi. Unatakaiwa u-declare interest.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, na-declare interest, pia mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. Kwa msingi huo, hili ninaloliongea ni kwa uzoefu mpana na lengo langu ni jema la kuisaidia nchi hii ili eneo la uchimbaji liwe na msaada kwa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kusisitiza, nawaomba sana kwa sababu lengo ni kufanya nchi iendelee kupata kipato kikubwa. Kwa hiyo, kwa sura hiyo nawaombeni sana wenzetu wa Wizara, katika eneo hilo nina uhakika tuna uwezo wa kuitoa nchi. Nafahamu tulikuwa na asilimia 6.7 mwaka 2020, lakini tukaenda asilimia 7.2 mwaka 2021. Kwa hiyo, tuna uwezo wa kwenda mbali zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa utoaji mikopo kwa wachimbaji, ni jambo jema, ni jambo la afya. Siyo kwa maana ya mwisho, lakini GST, kwa maana hawa watu ni wenzetu wa utafiti. Nchi hii ni kubwa, ina maeneo mengi, lakini hawa wenzetu wa GST tusipowazesha; leo karibia nchi kila sehemu utasikia leo kuna mfumuko wa madini, sasa wenzetu wa GST mko wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Bashe alipokuwa anazungumzia habari ya kuimarisha kilimo, lakini eneo la uchimbaji lina uwezo pia wa kuajiri Watanzania wengi especially vijana, lakini wenzetu watusaidie kitu kimoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema katika kilimo tutakuwa na extension officers waende kwa mkulima mmoja mmoja, vipi wenzetu wa madini? Mnasemaje Ma-geologist kwenda kwa wachimbaji huko kumsaidia mchimbaji? Kwa sababu hapa unaweza ukasema eneo hili labda akiba (reserve) ni kilo 20 za dhahabu. Maana yake kumbe tukifanya kitaalamu, tuna uwezo wa kuzipata kilo 20 za dhahabu, lakini watu wanachimba kwa design ile ile ya zamani ya kuganga njaa. Watusaidie kwenda mbali zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, nimalizie na suala la kilimo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Nakushukuru, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa the wind of change au kwa tafsiri yangu mwenyewe, upepo wa mabadiliko. Huko nyuma waliosoma zamani ilikuwa ukichaguliwa kwenda Shule ya Serikali unaona wewe ndio umefanya vizuri na watu hawakuwa tayari kwenda private schools, hilo ni jambo lilikuwa huko nyuma. Wote waliobahatika kwenda Shule za Serikali, walionekana wamefanya vizuri na wenzetu wachache walioenda shule za private walionekana kana kwamba hawakufanya vizuri. Liliendelea hilo kwa muda wote na watu waliziheshimu Shule za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa muda huu tujiulize, tumekosea wapi? Tujiulize tu swali hilo la msingi, tumekosea wapi? Tukishapata majibu, tutajua. Hata hii habari kwamba kuwe na ada elekezi au zisiwepo, ni suala tu la kujiuliza, tumekosea wapi ikiwa huko nyuma watu walipenda Shule za Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini katika haya yafutayo: kwa kuuliza wewe ni mjinga kwa dakika chache, kwa kutouliza, wewe unakuwa ni mjinga milele. Kwa hiyo, nakuomba Mheshimiwa Waziri, tujiulize ni wapi tumekosea ili tuweze kuwa werevu kwa muda wa kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye Mkoa wangu wa Katavi, tuna mkakati wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Katavi, naomba sana Halmashauri ya Manispaa ya Katavi kwa jitihada zake yenyewe imeanzisha mkakati huo wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Katavi pamoja na mazonge zonge mengi yanayoendelea, naomba Mheshimiwa Waziri watu hawa ambao wamekwishatenga eneo, kwanini na nyie kama Wizara msiwa-support wananchi hawa ambao wameonesha initiative?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu, nami naomba sana, ikiwa Mheshimiwa Rais Kikwete alitoa zawadi ya Chuo Kikuu cha Dodoma kwa Mkoa huu wa Dodoma na nchi kwa ujumla wake, namwomba na Rais wangu Mheshimiwa Dkt. Magufuli, auangalie Mkoa huu wa Katavi, ni mikoa ya pembezoni kwa ukweli. Nami niseme, uwepo wa Chuo Kikuu ni fursa. Maeneo ambayo yana vyuo, yanaibua mambo mengine! Watu wanaokwenda huko kwa ajili ya kusoma na kufanyaje, wanaibua fursa nyingine katika maeneo hayo. Kwa hiyo, naomba sana nikianzia na hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoke hapo niende kwenye Chuo chetu cha VETA, ni Chuo cha siku nyingi, lakini miundombinu imekuwa ni chakavu. Nakuomba Mheshimiwa Waziri tukiangalie, Chuo kile kimejengwa kwa siku nyingi, kinahitaji tu kuboreshewa miundombinu. Nikitoka hapo niende pia kwenye shule kongwe. Nalisema hili kwa sababu ukurasa wangu wa saba umesema ukarabati wa shule kongwe, umetaja shule saba. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, kuna shule ya watoto wa kike ya Mpanda Girls. Shule ile haina uzio, ni dada zetu na inapelekea watu wanaanza kuvamia maeneo ya shule. Ufumbuzi pekee ni kuwatengenezea fensi; na nikitoka hapo, ni kweli pamoja na huduma ya maji ili wale dada zetu waendelee kufanya vizuri.
Mhesimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo kwenye suala la Chuo Kikuu na Mpanda Girls, naomba nizungumzie kidogo suala la maslahi. Mimi naamini katika historia. Historia ni somo ambalo linatufunza wapi tumetoka, wapi tulipo na wapi tunakwenda. Kipindi cha nyuma ilikuwa ukiona mtu amevaa vizuri, anamiliki pikipiki au anamiliki baiskeli, ujue ni Mwalimu. Kipindi cha nyuma! Kwa hiyo, mtu ambaye alikuwa nadhifu, amekaa vizuri, ana maslahi mazuri, ni Mwalimu. Kama historia inatuambia tumetoka wapi? Tuko wapi na tunakwenda wapi? Kwanini tusirudi kwenye history, tukaangalia past ili ituangalie tuko wapi kwa maana ya sasa hivi na baadaye tunakwenda wapi? Tutapata ufumbuzi. Habari ya maslahi ya Walimu wakaaje, wafanywaje, tujifunze tu, huko nyuma tulikuwa tukifanyaje? (Makofi)
Vilevile Mheshimiwa Waziri, kwa maana ya elimu nilikuwa naomba nizungumzie habari ya maktaba ya Mkoa wa Katavi naomba sana eneo hilo. Kwa upande wa Chuo Kikuu, naomba nikizungumzie Chuo Kikuu Huria. Nimeona kuna mkakati wa makusudi wa kuviboresha Vyuo vya maeneo mengine lakini kwa eneo langu la Katavi niseme tena kuhusu habari ya Chuo Kikuu Huria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hatuna chuo chochote. Chuo pekee ambacho kiko kule kwa sasa hivi, ni Chuo Kikuu Huria. Kwa hiyo, nilikuwa naomba miundombinu hiyo ya Chuo Kikuu Huria tuweza kuiboresha ili watu hawa ambao kwa ukweli watoke pale kwenda katika maeneo mengine kwa ajili ya kufuata huduma za shule, waweze kuipata katika eneo ambalo liko jirani na wao. (Makofi)
Eneo la elimu bure, niseme kitu kimoja, naishukuru Serikali kwa hili. Jamani suala hili ni mchakato, nimewahi kusema huko nyuma. Ukiwa umepika chai, habari kwamba chai ina sukari nyingi, una uwezo wa kuongeza maji; au habari kwamba chai haina sukari, unaweza kutafuta sukari. Kwa hiyo, kwanza tumeanza na elimu bure, lakini kwa kutoka hapo tutaendelea kuboresha kwa kadiri mahitaji yanavyohitajika. La msingi ni kwamba tumeanza. It is a process, ni mchakato! Siyo suala la mara moja ukamaliza. Kwa hiyo, naipongeza Serikali, lakini na wazazi tusisahau wajibu wetu wa msingi, kuna maeneo ambayo wazazi wana nafasi yao ya kuendelea kuchangia, tusiiachie tu Serikali peke yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, naomba suala zima la study za kusoma kwa maana ya Kuandika Kuhesabu na Kusoma (KKK) lizingatiwe sana. Hilo litaendelea kutusaidia kuwafanya vijana hawa katika hatua ya awali. Ni aibu leo hii kuzungumza kwamba kuna mwanafunzi amepita shule, halafu hajui kusoma, hajui kuandika, hajui kuhesabu. Ili kukidhi mahitaji ya hilo, eneo la ukaguzi limekaaje jamani? Kwa sababu kama kuna eneo la ukaguzi, tutafikaje kusema huyu hajui kusoma? Au huyu hajui kufanyaje! Maana yake kuna sehemu tumekosea. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri tuboreshe maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba ku-declare interest, mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tunapomzungumzia mchimbaji mdogo haina tafsiri ya kuturudisha nyuma kwa mchimbaji aliyekuwa akitumia excel, akitumia Kinu na nyundo kuponda mawe. Bado mchimbaji mdogo anaweza akaja kwenye uchimbaji kwa kutumia crushers za sasa hivi akatumia tekonolojia ya sasa hivi. Kwa hiyo, tukimwongelea mchimbaji mdogo, naomba kwanza tupate sura hiyo, ili tupate picha ya huyu mchimbaji mdogo ni lazima awezeshwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchimbaji mdogo akiwezeshwa tutamtoa ambaye jabari analipasua pasua na kuligeuza unga kwa kutuma nyundo na nguvu zake „kwa kutumia muscles’ hao wengi kwa sasa hivi ninavyoongea na wengi walishapoteza maisha! Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri tuwaangalie hawa wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwawezesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kule Mpanda niwaelezeni tu, kuna maeneo ya Dirifu, Idindi, Katisunga, maeneo haya wanapatikana wachimbaji wadogo, lakini kuna leseni kubwa imewaatamia wachimbaji hawa! Nilichokuwa nakiomba kwake Mheshimiwa Waziri, kama alivyotenga katika maeneo mengine naomba na wachimbaji hawa wadogo wa eneo la Mpanda waweze kupatiwa leseni. Tukifanya hilo tutakuwa tumewasaidia watu hawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye gari kuna kitu kinaitwa shock absober. Wachimbaji wadogo tukiwapatia maeneo nao ni shock absober ya namna yake katika kupunguza suala la ajira. Katika eneo moja unaweza ukakuta kuna wananchi zaidi ya 500, mchimbaji mmoja mdogo tunapopiga kelele ya kwamba tunataka tuwainue bodaboda, machinga, mchimbaji mmoja mdogo aliyewezeshwa vizuri ana uwezo wa yeye pia kumiliki bodaboda, naye anaisaidia Serikali hii kwenye kufanya shughuli nyingine za namna hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, system ilivyokuwa huko nyuma tulikuwa tukiona wachimbaji wadogo wanashindana kwenye kunywa na kufanya vitu vingine, sasa hivi wamebadilika. Wachimbaji wadogo hawa wamekuwa wakijenga majumba mazuri, wachimbaji wadogo hawa wamekuwa wakiwekeza hata kwenye kilimo! Kwa hiyo, tukiweza kuwa-support maana yake tuna-support na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimweleze Mheshimiwa Waziri, ni kweli ule Mji kwa mfano, ukienda Johansburg ule mji umejengwa kwa dhahabu ya pale. Kwa hiyo, tukiwawezesha watu hawa wataijenga Mwanza, wataijenga Chunya, wataijenga Mpanda, naliomba sana hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mpanda ina shida nyingine ya umeme, tunazungumzia habari ya kupewa power plant, lakini eneo lile Mkandarasi ni mmoja ambaye tunaambiwa ana maeneo mengi ya kufanya kazi. Naomba namna yoyote ifanyike kuhakikisha eneo hilo linafanyiwa kazi mapema kwa sababu vinginevyo mji ule tutaendelea kupata umeme wa mgao.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru ndugu yangu mmoja, Mheshimiwa Ally Saleh, wakati akichangia aliongea kitu kimoja nilikipenda sana. Alisema, tunaweza tukafanya vizuri zaidi kwa sababu tuna utulivu wa kutosha, ile point niliisikia asubuhi aliongea hapa, nami niendelee kuamini kwa utulivu huu tulionao kama nchi, tuna nafasi kubwa ya kufanya mambo makubwa. Nimtie moyo tu Mheshimiwa Waziri kwamba sasa safari hiyo bado tunayo na ni nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nije kwenye eneo la tanzanite; Waheshimiwa Wabunge na Mheshimiwa Waziri, niseme kitu kimoja, tunaomba tujiulize, mtu mmoja aliniambia hivi; ukilifahamu swali ni sehemu ya kujibu mtihani. Kama hujajua swali linataka nini huo mtihani umefeli. Kwa nini tusijiulize hawa watu wanakwenda kuuza tanzanite nje kwa sababu gani, shida ni nini mpaka wakauze nje? Tukishajiuliza swali hilo tuna nafasi kubwa ya kurudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna siku nimekwenda South Africa, nakuta tanzanite, niliona tanzanite nikachekelea nikijua hapa naenda kusikiliza habari ya nchi yangu Tanzania, lakini wale watu katika kibao, anakwambia kutana na tanzanite ambayo Mama Afrika ameizawadia Afrika, haijatajwa Tanzania! Hivi tunafanyaje ku-promote mambo haya kwa sababu tunaweza tukawa tunalaumu tu tanzanite hazitoki, hazitoki! Je, eneo la promotion likoje? Pale South Africa mtu mwingine akifikiri tanzanite ni jina tu, lakini hajui kwamba kuna neno Tanzania pale. Tumefanyaje katika eneo hilo, naomba nalo hilo lizingatiwe sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuongelea suala la vinasaba, binafsi bila kushawishiwa na mtu yeyote, sababu za msingi zilizopelekea mpaka tukapata hii kitu, hizo hizo ziendelee kuimarishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa pongezi kwa wale wote waliopata bahati ya kujengewa barabara kwa kiwango cha lami katika maeneo yao nikiamini kwa kuwa wamepata wataunga mkono suala la kuhakikisha wale ambao hawajapata nao wanapata. Awamu ya Nne ililenga kufungua mikoa ya pembezoni, sambamba na kuiunganisha mikoa hiyo. Naamini wazo hilo bado ni la msingi kwa Awamu hii ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu Kitaifa unalenga kudhibiti uzito wa magari na matumizi sahihi ya mizani. Ushauri wangu, ili kulinda barabara zetu yawezakana adhabu ya fine imezoeleka, wakati umefika wa kuangalia adhabu yenye mguso kuepuka kujirudiarudia kwa suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la hifadhi ya barabara ni jambo la msingi. Suala hili liendelee kuangaliwa katika mipango ya muda mrefu ili kuepuka bomoabomoa na uwepo wa majengo yenye mandhari mbaya pembezoni mwa barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Mpanda – Ugalla – Kaliua – Ulyankulu - Kahama (kilomita 457), naomba iangaliwe kwa jicho la pekee kwani mara barabara hii itakapojengwa itakuwa kwanza ni njia ya mkato/fupi lakini itakuwa ni ufumbuzi wa ziada iwapo barabara ya Mpanda
– Inyonga – Koga - Tabora itapata shida ya kujifunga au vinginevyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kasi ya ujenzi wa barabara ya Ifukutwa - Vikonge (kilomita 35). Rai yangu ili ujenzi huu uwe na tija, tuone uwezekano wa upatikanaji wa fedha ili kipande kuelekea Uvinza kiweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Kavuu na barabara unganishi. Kilomita 10 za barabara unganishi naomba ziendelee kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia malalamiko ya wakazi waliopisha ujenzi na upanuzi wa Uwanja wa Ndege Mpanda kuhusu fidia yaendelee kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kasi ya ujenzi wa barabara ya Tabora – Ipole - Koga - Mpanda kilomita 373 iongezeke kama kweli fedha ya ujenzi huo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho pamoja na ujenzi wa reli ya kati, napongeza matengenezo yote yanayoendelea katika reli ya Mpanda. Niombe ratiba ya treni hiyo ya abiria iendeshwe kwa kufuata ratiba sambamba na uongezaji wa mabehewa likiwemo behewa la daraja la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kunga mkono hoja kwa asilimia mia.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mahali popote panapohitaji kupongeza isomeke kwamba nimepongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kulisema hilo, naomba nianze na suala zima la vyanzo vipya vya mapato. Nimeipitia hii taarifa ya Kamati ukurasa wa kwanza, nanukuu, imesema hivi, bado Kamati imebaini kuwa Serikali haijaonyesha utayari wa kupokea ushauri hususani eneo la ukusanyaji wa mapato kwa kutumia vyanzo vipya, ni taarifa ya Kamati.
Mheshimiwa Naibu Spika, habari ya bia na soda kabla sijazaliwa, nimezaliwa, nimekua, nimesoma ukisikiliza vyanzo vya mapato ni hivyo hivyo hatuwezi tukaja na vyanzo vipya, hatuwezi tukabuni vyanzo vipya! Nchi yetu nzuri ya Tanzania uwepo wake tu wa kijiografia ambao ametujaalia Mwenyezi Mungu hicho ni chanzo namba moja cha mapato. Uwepo wa hapo Tanzania ilipo nasema ni chanzo kikubwa cha mapato. Niwaombe wataalamu wetu katika eneo hilo waangalie suala hili tuna bandari, utalii, ukiniuliza nashangaa kwa nini soda na bia mpaka leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nchi nyingine utaambiwa chanzo chake cha mapato labda ni suala la maua tu, kuna nchi nyingine chanzo chake cha mapato ni fukwe na kuna nchi nyingine chanzo chake cha mapato ni madini. Sasa turudi kwa Tanzania yetu mbuga tunazo, wanyama tunao, maua tunayo, fukwe tunazo, bandari nzuri tunazo tumekosea wapi, tunashindwa wapi? Niseme tutakuwa tunamsingizia Mwenyezi Mungu kwamba labda Mungu hajatusaidia ametupa fursa zote hizo tunashindwa wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri wasomi wetu tunao, kwa nini tusitumie nafasi hii ya kijiografia? Ndiyo maana watu wengine walikuwa wanasema wangebahatika kuwa hapa Tanzania wangefanya maajabu. Kwa hiyo, niwaombe wataalamu ambao wamepewa dhamana na Watanzania hebu watusaidie kuitoa Tanzania hapo ilipo kwa maana ya kuibua vyanzo vipya vya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo la vyanzo vya mapato amani hii na utulivu ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia, hali nzuri ya hewa ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kwa nini tusivitumie kama fursa nzuri? Hayo tu tukiyafanyia kazi wala tusingekuwa na sababu hapa ya kuumizana vichwa kuhusu habari ya kiinua mgongo cha Wabunge na mambo mengine ya namna hiyo kwa sababu vyanzo vipo na ni vingi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa taarifa inatuonyesha kwamba Pato la Taifa limeongezeka kutoka 7.0 mpaka 7.2. Wananchi wetu wa kawaida ukiongelea habari ya ongezeko la pato wao wanatamani waone kwa macho na washike kwa mikono yao hilo ongezeko. Habari ya ongezeko la pato kwa kupitia maandishi kama hali ya mfuko wake ni korofi hawaipati sura hiyo. Tunasema kwamba nchi yetu tumepiga hatua kwa maana ya ongezeko ya Pato la Taifa basi uchumi usomeke kwenye mifuko ya watu, uchumi usomeke kwa yale wanayoweza wakayaona ndiyo tutakuwa na jambo la kuongea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji, napata tabu sana ukirudi hata katika ramani iwe ni ramani ya East Africa ama ya dunia Tanzania yetu imezungukwa na maji nchi nzima kuna Lake Tanganyika, Lake Victoria, Lake Nyasa lakini hata Bahari ya Hindi. Kuna nchi nyingine wanafanya kazi kubwa ya kuyabadilisha maji ya bahari kuwa maji ya kunywa Tanzania hatujafika hapo. Mimi nilikuwa natamani ule mtandao wa buibui jinsi ulivyo Tanzania hii ingeweza kuunganishwa kwa maji kwa sura hiyo. Maji yangeweza kuvutwa kutoka Lake Victoria yakafika upande mwingine, yakavutwa kutoka Lake Tanganyika yakafika upande mwingine na yakatoka Lake Rukwa yakafika upande mwingine. Leo kuendelea kuongelea habari ya maji kwa nchi ambayo imezungukwa na maji sipati picha, vipi hawa watu wengine ambao hawakupata baraka hii ya kuwa na maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitembelea nchi moja wale watu pamoja na kwamba wanapata mvua mara moja ndani ya miaka mitatu wameweza kutengeneza ziwa (man made lake). Huwezi kuamini ni kubwa linawasaidia kupata maji lakini kufanya utalii kwa sababu wanaenda watu pale kufanya utalii wanapata samaki lakini huku chini wanaweza kumwagilia pia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa Tanzania hii mimi narudi kwenye maandiko hivi ni nani ameturoga? Ukiangalia jiografia maeneo mengine jinsi milima ilivyokaa wala hauhitaji kufanya kazi kubwa ya kusema sijui utachimba bwawa ni suala la kukinga tu na wataalamu tunao. Ukishakinga hapo unatengeneza mazingira ya kuwa na maji ya kutosha, hatujafika mahali pa kulalamika suala la maji hebu tubadilike tuache kufanya kazi kwa mazoea. Tusiogope kuthubutu kuja na miradi mikubwa ambayo itakuwa ni ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, tusifanye kazi kwa mazoea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoke hapo nizungumzie kuhusu msamaha wa kodi kwa wanajeshi wetu. Jambo hili linaweza likawa jema lakini naomba niwakumbushe wapo wadau wengine kama askari wastaafu wale nao tunafanyaje ambao walikuwa ni wanufaika wa suala hili? Naomba wakati tukiliangalia hilo nao tusiwasahau. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la CAG halikwepeki, ni vizuri akaongezewa fedha. Nikirudi TAKUKURU kama ilivyo neno lenyewe ni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kwa hiyo, si muda wote wanapambana kuna wakati mwingine wanazuia. Kwa hiyo, katika suala la kuzuia wanahitaji fedha, naomba nao wafikiriwe. Lakini baada ya kutoka hapo, naomba nizungumzie suala moja. Nafahamu nafasi ya Watanzania walioko nchi za nje tunafanyaje kwa maana ya ndugu zetu hawa kurudisha mapato nyumbani? Naomba nalo hilo tuendelee kuliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati tukiwa tunaongelea mipango mipana niseme jambo moja, ukienda nchi za watu utakuta vijana wengi wa kutoka Kenya wanafanya kazi huko wanatumia hata nafasi ya Kiswahili kufanya mambo makubwa katika nchi nyingine. Sisi kama Watanzania nafasi ya Kiswahili tunaitumiaje? Kuna sehemu tumesema tufanye kwa makusudi kuhakikisha watu wanakwenda nje wakitumia nafasi hii ya Kiswahili na kwa kuwa huko nje wana uwezo wa kuzalisha na kurudisha fedha ndani, hilo tumejaribu kulifanya?
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza kabisa naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee pamoja na kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu na watendaji wote, nijikite katika kulifikisha hili mbele yenu kwa maana ya hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa ule wa kumi na moja na kwa afya ya kikao hiki naomba nipasome hapa. “Ili kuendelea kuboresha demokrasia hapa nchini, hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sharia, kanuni na taratibu za nchi pamoja na kuwa na uvumilivu wa kisiasa. Ninatoa rai kwa wadau wa siasa wote nchini kujenga utamaduni wa masikilizano na kuendesha siasa za maendeleo badala ya siasa za malumbano; siasa za kuunganisha watu watu wetu badala ya kuwagawa; na siasa za uwajibikaji badala ya siasa za mazoea. Serikali itaendelea kulinda na kuheshimu misingi ya siasa zinazolenga kuleta ustawi wa wananchi na zinazotanguliza maslahi ya nchi na wananchi”.
Mheshimiwa Spika, hili limebeba ujumbe wote ambao nilikuwa nakusudia kuusema. Pia nimejaribu kufuatilia hotuba ya Kambi ya Upinzani nikakutana na kauli moja na mimi niliiona sio mbaya, ambayo wanasema kwamba:-
“Wanazuoni wanasema kutofautiana kifikra ni afya ya akili na ili uvumbuzi utokee lazima kuwe na fikra mbadala.” Mheshimiwa Spika, mimi naona niende mbele zaidi na ili twende mbele tusipinge kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, eneo la kwangu kwa maana ya Katavi nikizingatia sekta ya utalii ambayo imeongelewa vizuri katika hotuba ya Waziri Mkuu, naiona sekta ya utalii na usafiri wa anga kama watoto pacha. Utakapoboresha usafiri wa anga unaboresha eneo la sekta ya utalii. Kwa misingi hiyo, hata nilipokutana na habari ya nchi kununua ndege, mara ya mwisho katika kutafuta habari nilikutana na nchi moja ya Ethiopia, uchumi wake mkuu umejikita katika maeneo yafuatayo, ukiacha kilimo, kuna suala la usafiri wa anga, wamekuwa wakifanya vizuri na kuibua fursa nyingine kwa kupitia usafiri wa anga. Leo tunapotamani hata kiongozi wa nchi atoke akaiangalie dunia anakwendaje huko kwingine? Ni lazima atakwenda kwa kutumia usafiri wa anga. Kwa hiyo, ninapoona nchi yangu inakwenda kuzungumzia habari za usafiri wa anga suala hilo naliunga mkono na kupanga ni kuchagua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mtu mmoja hakujenga nyumba, hakufanya kitu kingine, yeye alianza kwa kununua mziki. Kwa kupitia mziki ilimletea utulivu wa fikra akaweza kujipanga akaibua fursa mbalimbali na baadaye akajenga nyumba na vitu vingine vyote vikaendelea. Kwa hiyo, kupanga ni kuchagua. Kila mmoja anaweza akaamua anaanza na kitu gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikizungumzia suala hilo la utalii kwa maana ya Katavi, nimeshukuru katika hotuba ya Waziri Mkuu amezungumzia habari ya kupanua wigo. Eneo lile ni kweli tuna mbuga nzuri ya Katavi lakini pamoja na kuwa na uwanja mzuri, ukiuliza ni kwa nini uwanja ule wa Katavi haufanyi kazi tunaambiwa tatizo hakuna ndege zinazokwenda kule. Mimi niombe, kwa maana ya ndege hizi ambazo zipo, zianzishiwe safari ya kwenda Katavi ili kuibua fursa hiyo ya utalii. Kama kuna tatizo linalotokana na suala la mafuta au kutokuwepo kwa gari la zimamoto, naiomba Serikali yangu sikivu iangalie suala hilo kwa sababu upande ule tukifanya vizuri inakuwa sio kwa ajili ya wana Katavi tu ni
kwa ajili ya maslahi mapana ya nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo naomba nije upande wa sekta ya madini. Nilifarijika nilipokutana na habari ya kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo. Najua fursa hiyo ya uchimbaji madini na hasa tunapoelekeza kwa wachimbaji wadogo, baadaye watakuja kuchangia pato la Taifa. Kule kwangu kuna maeneo ya Dirif na Kapanda, niombe isiishie kwenye kuandika kwenye vitabu hivi kwamba maeneo hayo yatatengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo, twende kwenye hatua ya mbele zaidi ya kuhakikisha kweli maeneo hayo wanapatiwa hao wachimbaji wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuna suala zima la kuongeza thamani kwa maana ya madini lakini hata kama tutaongeza thamani naomba twende mbali zaidi na suala la masoko pia. Watu hawa tunaweza tukawahamasisha wakachimba, wakaongeza thamani lakini inapokuwa hakuna soko naona kama ni tatizo pia.
Mheshimiwa Spika, nikitoka kwenye sekta hiyo naomba niende kwenye sekta ya afya. Eneo la sekta ya afya nimeliona likizungumziwa humu kwa maana ya afya ya mama na mtoto mimi naomba niende mbali zaidi. Tunapozungumzia habari ya afya ya mama na mtoto naomba sana ilenge pia kwenye kupiga vita mimba za utotoni na hili naliona ni tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule kwangu Katavi taarifa zinatuambia 45% ya mimba za utotoni zinatoka kwetu Katavi, naliona hili ni tatizo. Kwa hiyo, naomba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, mazingira yaendelee kutengenezwa, namna ya kuirudisha jamii hii kulitambua hili kwamba ni tatizo, inapokuwa mama yeye mwenyewe ni mtoto halafu anakuwa na mtoto hata mipango mingine ya kitaifa hatutaifikia, kwa sababu mama mwenyewe anakuwa hajitambui na huyo mtoto atakuwa katika mazingira magumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kulisema hilo, naomba pia niende katika suala la elimu. Nafarijika kusikia habari ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu lakini naomba twende mbali zaidi. Katika eneo hili hili la elimu, fursa ambayo nimekuwa nikiiona na wakati huo Watanzania hatufanyii kazi fursa hii kwa maana ya lugha adimu ambayo ni Kiswahili, mimi napata tabu. Huko duniani watu wengine wanaajiriwa kwa kupitia Kiswahili tu. Kuna nchi moja watu wake wengi wanarudisha pato katika nchi yake kwa kupitia wasomi mbalimbali kwenda katika maeneo mbalimbali duniani wanakusanya fedha na kuzirudisha kwenye nchi yao.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Watanzania wenzangu katika eneo hili hili la elimu, Kiswahili tusikibeze. Kiswahili kitatoa ajira, kitatoa fursa kwa watu wetu, suala ni kujipanga vizuri. Tunapoambiwa kama ni wazungumzaji wazuri wa Kiswahili lakini unakuta nchi nyingine ndiyo
wanafanya kazi na wanakuwa mbele wakati Watanzania tuko nyuma mimi hapo nakuwa sijisikii vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa suala la michezo. Michezo ni afya lakini shida moja ambayo naiona kwa sisi Watanzania, muda umekuwa ni mrefu tunakuwa kama
kichwa cha mwendawazimu na sababu ni nini? Ni mipango yetu kuwa ya muda mfupi, mara nyingi tunakwenda na mipango ya zima moto. Naomba turudi kwenye mipango endelevu, tuwekeze katika eneo hili. Akina Bayi wa miaka hiyo wako wapi? Tunatamani kuwaona watu hao katika maeneo yote iwe ni riadha au mpira wa miguu. Nimefarijika kuona kwamba tutarudi kuendeleza michezo huko mashuleni na kwenye shule za msingi lakini tuendelee kuwekeza na ukitaka fedha, tumia fedha.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naendelea kusema naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na neno la shukrani. Nashukuru kwa maana ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, taarifa ya kamati nikiamini vyote vimesheheni mambo ambayo macho yanapenda kuona na masikio kusikia. Nikianza na nukuu kama ambavyo wenzetu wa kamati waliitoa ya Mahatma Gandhi, wao waliitoa kwa kingereza lakini mimi nitaitoa kwa tafsiri ya Kiswahili changu mwenyewe kwa maana ya afya ndio utajiri halisi na si vipande vya dhahabu na fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo nakwenda kuisemea Hospitali yetu ya Manispaa ya Mpanda. Hospitali ya Manispaa ya Mpanda ilianza mwaka 1957 ikiwa kituo cha afya. Leo hii inafanya kazi kama Hospitali ya Manispaa, na kwa misingi hiyo watu wote ndani ya mkoa wanaitegemea hospitali ile, na ndiyo maana sisiti kuishukuru Serikali yangu kwa sababu najua tuko mbioni kutengeneza hospitali ya mkoa na fedha zimekuwa zikitengwa na hivi karibuni tumetengewa shilingi bilioni moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini, Serikali itaendelea kutuangalia kwa jicho la huruma nikiamini sisi tuko pembezoni na tukikosa huduma muhimu za afya tunakuwa pembezoni zaidi. Kwa hiyo, hilo nilikuwa napenda kuliweka katika sura hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hospitali yetu hiyo hiyo, mara ya mwisho alikuja Naibu Waziri. Katika kuitembelea hospitali, alipokwenda kwenye chumba cha upasuaji, nasikitika kusema alikifananisha chumba kile na machinjio; yaani kwa maana kwamba vifaa vilivyomo mle havifanani na vifaa vya chumba cha upasuaji, kwa huduma zote, kama vile utoaji hewa na vinginevyo. Kwa hiyo, mahali ambapo tunakusudia tuokoe maisha ya watu ukifananisha na machinjio Mheshimiwa Waziri unaona kabisa kwamba watu wale wanatakiwa kuangaliwa kwa jicho la huruma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua pia kuna changamoto ya upungufu wa dawa. Ni kweli mara ya mwisho alikuja Mheshimiwa Waziri Mkuu akatusaidia tukaanzishiwa duka la MSD, hilo nashukuru maana usiposhukuru kwa kidogo hata kwa kikubwa unaweza usishukuru. Hata hivyo pamoja na uwepo wa duka hilo bado tuna tatizo kubwa la uhaba wa madawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakumbuka Mheshimiwa Waziri wetu mara ya mwisho aligusia habari ya kuiangalia mikoa ya pembezoni kwa maana ya kupeleka madaktari bingwa. Nilikuwa naomba wazo hilo muhimu, wazo hilo la uokoaji liendelee kuwa katika kichwa chako Mheshimiwa Waziri. Nafahamu tuna ukosefu wa magari na katika hili uungwana tu kama binadamu naomba niwapongeze wale wote waliobahatika kupata ambulance. Hata hivyo wakati nikiwapongeza hao Mheshimiwa Waziri maana yake na mimi natoa shukrani in advance kwa maana najua mgao unafuata na sisi tutafikiriwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Mkoa wangu wa Katavi napata aibu kuhusu suala la mimba za utotoni nikiwa mwakilishi wa wananchi. Tunapozungumzia habari za mimba za utotoni, na kwamba Mpanda ndio wa kwanza katika nchi hii sisi wawakilishi wa wananchi tunayo kazi nzuri kubwa ya kufanya. Nilikuwa naomba hiyo kazi kubwa ya kufanya, kwa maana ya kuwafikia vijana katika kuendelea kutoa elimu katika suala hili na tatizo la mimba za utotoni nahitaji msaada kutoka katika ofisi yako Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshazungumzia habari ya ujenzi wa hospitali ya mkoa ambayo inahitaji msisitizo na msukumo. Tunacho chuo cha afya, miundombinu yote ya kile chuo ambacho kilikuwa cha zamani imeshafufuliwa, kila kitu kipo katika hatua za mwisho. Rai yangu na ombi langu kwako, Serikali ifanye jitihada kuhakikisha chuo kile kinaanza. Najua ni chuo kwa ajili ya matabibu, lakini ningeomba tukibahatika pia katika chuo hicho hicho tukawa tunatoa na wauguzi tafsiri yake ni nini? Kwanza habari ya mahitaji ya wataalamu hawa itakuwa ni ndoto katika hospitali yetu, nilikuwa naomba hilo tusaidiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze, kwenye kitabu chako Mheshimiwa Waziri umeongelea habari ya huduma ya matabibu bingwa. Nafahamu kwa kupitia huduma ya matabibu bingwa kwa Taasisi ya Jakaya Kikwete na kwa MOI, huu ni mwarobaini wa kutusaidia Watanzania kwenda nje ya nchi, mimi hilo nalipongeza sana. Hata hivyo, pamoja na kulipongeza basi maeneo hayo yapewe fedha, na hapa si suala tu la kusema fedha zimetengwa ila ionekane fedha zikipelekwa, nilikuwa naomba kutoa rai hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niendelee tena kutoa pongezi kwa kupunguza rufaa nje ya nchi. Suala hili ni la msingi, najua ni kwa maana ya kupunguza rufaa ya nje ya nchi kama vile kwa masuala ya kupandikiza figo. Tumeona pale ukizungumzia nje ya nchi ni shilingi milioni 80 lakini kwa shughuli hiyo kufanywa ndani ya nchi inakuwa ni shilingi milioni 20, huu ni msaada mkubwa kwa wananchi wetu. Naamini nchi ya uchumi wa viwanda bila kuwekeza kwenye afya ya watu, rasilimali watu, nguvu kazi ndoto ya uchumi wa viwanda itakuwa mashakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niende kwenye ushauri, lakini wakati nikienda kwenye ushauri kuna suala la dharura...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante awali ya yote naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nje ya uhifadhi haya yote tunayoyazungumzia hayatakuwepo, tunayaona haya kwa ajili ya uhifadhi na sisi tukiwa binadamu mzigo tunamtwisha Waziri wetu Maghembe na watendaji mbalimbali, lakini nafasi ya uhifadhi ni ya kila mmoja na ndio maana hata kwa kupitia kitabu cha Mwenyezi Mungu kitabu cha Mwanzo binadamu alipewa wajibu wa kuja kuitawala dunia na viumbe vilivyopo hapo ikiwa ni misitu na vitu vingine vya namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba kuna kauli ambayo huwa naiongea mara zote nikipata nafasi, mazingira yaliyoharibiwa hayana huruma, yatatuadhibu tu hata kama ni miaka 50 ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo nitajikita zaidi kwenye utalii na uhifadhi. Nafahamu kwanza tunapoangalia matatizo tusiangalie kana kwamba hatujawahi kuwa na wakati tulivu tuyaangalie matatizo kwa namna ya kuyatatua, nikilisema hilo kwa kitabu cha wenzetu wa wanyamapori tunaambiwa kuhusu umuhimu wa maeneo yaliyohifadhiwa. Wanasema hivi; “Maeneo yaliyohifadhiwa yana umuhimu mkubwa nchini kiikolojia, kiuchumi na kijamii, aidha maeneo haya huchangia ustawi wa sekta nyingine kama vile mifugo, kilimo, nishati na maji,” hilo eneo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikilisema hilo nataka kumaanisha nini, leo hii tukihifadhi asili itatulinda na tunapewa nafasi ya kuamua ni lipi lifanyike na kwa wakati gani. Mfano, wapi tuchunge, wapi tulime, wapi tujenge na tusipohifadhi tutakimbizwa na matukio kwa mfano ukame wa kutisha, mafuriko, mimea vamizi na magonjwa pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna watu tunaweza tukaona ni kwa nini wataalamu wanatuambia ikiwezekana tusichanganye mifugo na wanyamapori, kuna magonjwa ya ajabu, magonjwa ambayo baadae binadamu huyu kumtibia ni kazi ya ziada kutokana na hiyo ya kuwachanganya hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wakati mwingine tuendelee kuheshimu maelekezo ya kitaalamu, na mimi naamini sisiwote lengo letu ni kuijenga nyumba moja, kwa hiyo tusigombee fito kama tatizo ni la mifugo turudi kwenye ufumbuzi. Je, tunasemaje mimi nafarijika sana, majuzi nikienda Dar es Salaam nilipita Kongwa pale kwenye ile ranchi nikabahatika kupata nyama nzuri kupelekea familia. Kwa maana ya ranchi tunasemaje kuwasaidia watu hawa wakati fulani kulikuwa na ajenda hiyo kwamba wakulima tuendelee kuangalia namna ya kuwasaidia kuwa na ranchi ndogo ndogo ili kuepukana na tatizo hilo. Kwa hiyo twende kwenye kutatua matatizo tusiwe walalamikaji twende kwenye kutatua matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikwenda Kilombero, nikafurahia uumbaji alioutenda Mwenyezi Mungu na katika hili niseme, bonde lile nilifurahi kusikia kwamba hata maji wanayokunywa Dar es Salaam kumbe ni kwa sababu kuna watu wengine wametunza mazingira yao, kwa hiyo, mmoja amefanya kazi kubwa ya kutunza lakini kwa msaada wa watu wengine kwa hiyo nilikuwa naendelea kuliomba hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiwa mjumbe wa Kamati hii majuzi nilikwenda Ngorongoro nikaenda Loliondo nilifurahishwa sana na ule usemi wa kiingereza unaosema seeing is believing, niliweza kuona na nikaamini maajabu ya uumbaji aliyoyafanya Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti,Ngorongoro na Loliondo ile tuamue tunataka nini kama kweli tunahitaji uhifadhi sheria na taratibu nyingine zizingatiwe, nje ya hapo kama hatulitaki hili tuamue jambo lingine. Sisi politicians kwa maana ya political will tuna nafasi kwamba sasa tunasema uhifadhi, utalii kwa ujumla wake ukae pembeni tutafanya mambo mengine, lakini ukirudi kwa maana ya vyanzo vya mapato fedha zinazoingizwa katika maeneo hayo ni habari isiyofichika kwa mfano ukiangalia ukurasa huu unasema kwamba katika mwaka wa fedha 2013/2014 utalii pekee ulichangia takribani17.2% ya Pato la taifa ikilinganishwa kwa mfano na michango kutoka GDP kwa mwaka huo ya mazao ya kilimo ilikuwa 17.8%, mifugo 8.4% na uvuvi 2.4% kwa miaka miwili mfululizo utaliona hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mi naendelea kusema tukiacha hilo la pato la Taifa kwa kupitia utalii mimi nina ushauri ufuatao, tusiwe kwamba tunafanyia kazi msaada wa Mwenyezi Mungu kwa kutuweka hapa tulipo. Tumechukua hatua gani sisi kama binadamu baada ya msaada wa Mwenyezi Mungu kwa maajabu haya ambayo ametupa kuwa na Ngorongoro nzuri, Mlima Kilimanjaro na mbuga nyingine, initiative sisi kama sisi tumefanyaje Mheshimiwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kuna watu wanaenda kufanya utalii kwa sababu binadamu amehangaika kujenga jengo refu, mnaenda kushangaa jengo refu lakini vipi sisi ambao Mwenyezi Mungu pekee ametupa maajabu haya why can’t we work on it? Kwa nini tusifanyie kazi?

Kwa hiyo, mimi naendelea kusisitiza ndugu zangu bila ya uhifadhi itabaki kuwa gumzo, na leo hii kuna mtu unatamani hata kwamba bora nimpeleke ng’ombe pale kwa sababu ni eneo limehifadhiwa ni eneo limetunzwa, turudi tu kama kuna tatizo ya usimamizi wa sheria tujikite hapo, tusimamie sheria, taratibu na kanuni, mimi ushauri wangu ni huo. Lakini eneo jingine tena nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri kwa maana…(Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nianze kwa kuunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo na mimi niungane na wazungumzaji wote wanaozungumzia habari ya Wizara kuongezewa fedha. Sambamba na hilo, wenzetu wa sheria wana usemi wao wanaosema; “Justice must not only be done, but must be seen to be done” ikiwa na tafsiri gani? Leo hii tunapozungumzia habari ya Wizara na fedha, inawezekana mwaka wa jana bajeti ile ilikuwa kubwa, safari hii tunapotamani tena kuwa na bajeti kubwa, tatizo ninaloliona mimi si ukubwa wa bajeti, ni utekelezaji kwa maana ya fedha zifike kwa walengwa, hilo ndilo tatizo ninaloliona. Kwa hiyo, kwa tafsiri hiyo, kama tuliweza kutekeleza kwa asilimia 19 vipi kama fedha ikienda hata kwa nusu ya bajeti ikiwafikia walengwa? Kila mmoja hapa atapunguza kupiga kelele, mimi ndiyo naliangalia kwa sura hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye mji wangu wa Mpanda nafahamu miundombinu ya maji katika mji ule imechakaa, sehemu kubwa ni mabomba ya chuma, nilikuwa naomba Wizara iliangalie suala hilo. Leo hii tuna maeneo ya Makanyagio, Majengo, Majengo A na B, zote hizo kwa kweli hazifikiwi na maji kutokana na uchakavu wa miundombinu. Nafahamu tunalo Bwawa la Milala, tuna changamoto ya uwepo wa viboko. Bwawa lile lilikuwa na uwezo mkubwa wa ku-supply maji, niendelee kuomba wahusika waliangalie hilo, ili kukidhi suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu tunao Mradi wa Ikorongo, ule mradi peke yake haukidhi mahitaji ya maji kwa Manispaa ya Mpanda. Tuna maeneo ya Mwamkuru, maeneo haya naendelea kuyaombea visima. Kuna wakazi wengi, lakini ukiangalia maeneo yale mpaka leo hii suala la visima ni tatizo. Eneo hilo hilo la Mwamkuru tuna skimu ya umwagiliaji ya Mwamkuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nasikitika kusema tunakwenda mwaka wa saba skimu ile haijafanya kazi. Ni tatizo, kwa hiyo nilikuwa naomba Waziri atakapokuja hapa aniambie tunafanya nini katika eneo hili, na ukizingatia watu wale kwa kupitia skimu za kwao wenyewe wamekuwa wakizalisha chakula cha kutosha. Leo hii mwarobaini ilikuwa ni skimu hii ambayo ingeweza kusaidia eneo lile likafunguka na chakula kikapatikana cha kutosha. Naomba niambiwe kwa nini tunakwenda mwaka was aba sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema yote hayo, nilikuwa naomba pia nielezee uelekeo pekee wa kusaidia mji wetu wa Mpanda kwa kweli ni kuyatoa maji kutoka Ziwa Tanganyika. Najua hii tunapozungumzia habari ya Ikorongo ni chanzo cha muda mfupi, tutapoteza muda mwingi kuzungumzia chanzo ambacho hatuna uhakika wakati chanzo cha uhakika kipo. Niombe na kwa wakati tofauti nimeshaongea na Mheshimiwa Naibu Waziri, aliangalie hili lianze kuingia kwenye mpango wa kuyatoa maji Ziwa Tanganyika na kuyaleta katika maeneo hayo, hata mikoa mingine ya jirani. Kwa kweli pale kilometa ni chache. Kilometa za kutoka Karema kuja Mpanda Mjini hazizidi mia au ni mia na kidogo, ni umbali mdogo huo. Nilikuwa naliomba hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kusisitiza, eneo la umwagiliaji ni ufumbuzi wa kutosha katika nchi hii. Mimi niombe, kwa maana ya umwagiliaji, leo hii tusilalamike; niliwahi kusema hapo mwanzo kwamba nchi hii tumebahatika kuwa na vyanzo vingi. Sizungumzii habari ya Bahari ya Hindi, nchi nyingine zinahangaika ku-treat maji ya bahari, sisi hatujafika huko…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kuipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani na majeshi yote. La msingi ni kuhakikisha fedha za maendeleo zinatolewa ili kuwezesha majeshi hayo kumaliza miradi kusudiwa katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi unalao tatizo kubwa la makazi ya askari sambamba na makao Makuu ya Mkoa (Jengo la Polisi la Mkoa). Suala hili limepelekea kutumika kwa yaliyo kuwa Makao Makuu ya Polisi Wilaya.

Mheshimiwa Spika, limekuwepo tatizo la msongamano wa wafungwa na mahabusu katika Gereza la Mpanda Mjini. Ombi langu ama ukarabati ufanyike katika gereza hilo au ujenzi wa magereza hasa katika Wilaya Mlele ili kufanya mahabusu toka Mlele wapatiwe huduma huko huko.

Mheshimiwa Spika, suala la mavazi/sare hasa za Askari Magereza na wafungwa naomba litazamwe kwa namna ya pekee maana vazi pia linaakisi kiwango cha utu na ubinadamu ambao ni haki ya msingi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Awali ya yote nami naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimejaribu kufuatilia vipaumbele vilivyotolewa na Mheshimiwa Waziri, kwa maana ya utekelezaji wa vipaumbele eneo la ujenzi wa miundombinu ya kiuchumi upande wa barabara, reli, usafiri wa anga, majini na umeme. Ukweli ni kwamba eneo hilo barabara, reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini na umeme vikifanyiwa kazi tutafika sehemu, kama hiyo haitoshi eneo lile la pili naambiwa

kwamba kipaumbele kingine ilikuwa ni kuhakikisha madini na maliasili zetu zinatumika kwa manufaa ya Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, mimi nina maslahi katika eneo la uchimbaji wa madini. Naomba nijikite kwenye Taarifa ya Kamati ukurasa wa 32, inaelezea kutoza kodi ya zuio ya asilimia tano ya bei ya kuuzia kwa wachimbaji wadogo ni hatua inayoongeza mapato stahiki ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa ule kwa maana ya Taarifa ya Kamati inasema hivi: “Kutoza kodi ya zuio ya asilimia tano ya bei ya kuuzia kwa wachimbaji wadogo ni hatua inayoongeza mapato stahiki ya Serikali, lakini inatafsiriwa kuwa wachimbaji wadogo watalipa mrabaha kwa asilimia tisa na inaweza kusababisha wachimbaji wadogo kufanya biashara haramu.”

Mheshimiwa Spika, lengo langu ni nini? Ikiwa tumekusudia kuwasaidia wachimbaji wadogo na ambacho nakiona sasa hivi, mkakati mkubwa wa Serikali kutoa ruzuku kwa ajili ya wachimbaji wadogo, lakini kwa kupitia vyombo vyake kama GST kufanya utafiti ili wachimbaji hawa waende kuchimba katika maeneo yenye tija. Sasa hayo yote ambayo ni nia njema ya Serikali kuyafanya, inapokuja suala la mrabaha kuwa kubwa kwa kiasi hicho, mimi napata tabu.

Mheshimiwa Spika, mchimbaji huyu mdogo na naomba Bunge lako lifahamu ningependa Waziri angeenda hata kwenye tafsiri, tunapozungumzia mchimbaji mdogo ni yupi? Maana mchimbaji mdogo ninayemfahamu mimi hana tofauti na Mmachinga mwingine wa kawaida. Mchimbaji mdogo ambaye anaweza akaenda porini ndani ya miezi mitatu hajapata hata gram moja ya dhahabu, huyo ndiye

mchimbaji mdogo ninayemfahamu. Mchimbaji mdogo anayetumia sururu na nyundo, labda kama tunamzungumzia mnunuaji wa madini, lakini kwa maana ya mchimbaji mdogo na Serikali hii imelenga kumsaidia mchimbaji huyo mdogo.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia habari ya mrabaha kwenda karibu asilimia tisa napata shida na ukizingatia leseni ya hekta moja ni 80,000, kama atakuwa na hekta kumi, maana yake ni laki nane ada ya leseni! Kwa hiyo eneo hilo naomba tuliangalie. Nalisema hilo kwa sababu gani?

Mheshimiwa Spika, jana nilikuwa nafuatilia taarifa ya mtaalam mmoja, ameitaja Botswana na uchimbaji wa diamonds kwa maana ya almasi. Botswana sasa hivi pato la Botswana linatushinda Tanzania lakini wamejikita kwenye uchimbaji wa almasi tu. Nchi yangu nzuri Tanzania, mikakati mikubwa na katika hili nimshukuru Mheshimiwa Rais jitihada anazozifanya katika maeneo yote hayo yanayogusa machimbo, lakini niendelee kusema; ili tukafanane na watu kama Botswana, jitihada hizi za makusudi ziendelee kulenga maeneo mengine yote.

Mheshimiwa Spika, tunapomzungumzia mchimbaji mdogo akiwezeshwa vizuri makandokando mengine yakakaa pembeni mimi ninachofahamu uwekezaji wake haufanyi nje ya nchi, ataufanya Tanzania hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukija kwangu Katavi, majengo mengi mazuri ni yale yaliyofanywa na wachimbaji wadogo. Biashara nyingi kubwa ni zile zinazofanywa na wachimbaji wadogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali yangu sikivu tuendelee kuliangalia eneo hilo kwa umakini wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kufungwa kwa biashara. Kutoka Julai, 2016 hadi Machi, 2017 kuna biashara 7,277 zilifungwa. Nafarijika kwa maana ya taarifa ya Waziri imejikita kwenye kutafuta kujua na jitihada zifanyike ni kwa nini biashara hizo zilifungwa ingawa upande wa pili ametuambia kuna zaidi ya biashara 224,738 ambazo ni mpya. Kubwa ambalo

ningependa kuendelea kushauri, ndugu zetu wa TRA na wafanyabiashara tuendelee kutengeneza mahusiano sio uadui. Katika hili, Mheshimiwa Waziri nashukuru pale aliposema wenzetu wa TRA waendelee kufanya mahusiano shirikishi na wenzetu wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la usambazaji maji vijijini na mijini. Naona Mheshimiwa Waziri ametenga bilioni 188.4. Katika eneo hili niendelee kusema, pamoja na jitihada za Serikali kule kwangu kwa maana ya suala la maji na kila mtu hapa ameongelea suala la maji. Naomba Mheshimiwa Waziri, ufumbuzi wa muda mrefu, tuwekeze fedha kwenye kuyatoa maji ziwa Tanganyika, hiki ni chanzo cha uhakika, watu watapata maji ya kutosha na kelele hizi zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni kuhusu dawa na vifaa tiba ambapo niliona pale inazungumziwa habari ya bilioni 156.1. Tuseme yote tutakayoweza kusema na nishukuru pamoja na kwamba tunakwenda kusaidia hospitali kwa maana ya Jakaya Kikwete na maeneo mengine hayo, lakini tusipowekeza kwenye hospitali zetu za mikoa kwa maana ya vifaa tiba na madawa kasi ya watu kutoka huku mikoani kwenda kuvamia huko kwenye hospitali hizo nyingine itakuwa kubwa.

Mheshimiwa Spika, naliona hilo kwa sababu gani? Kwa mfano, kule kwangu Katavi japo hospitali ile ya mkoa haijajengwa, utengaji wa fedha wa bilioni moja kwa kila mwaka kama lengo kweli tunataka tuhakikishe eneo hili la tiba watu wetu wanapata huko huko, maana yake hospitali ya mkoa ikiimarishwa, ikiwa na vifaa vyote, umerahisisha kazi, watu hawatakuja katika hizo hospitali nyingine kama Muhimbili na kwingineko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo, nami niungane mkono na wale wote kuhusu kusamehe kodi eneo la ufugaji pamoja na vyakula vya mifugo. Tutaiona tija katika eneo hilo, eneo la mifugo na kwa kweli tunasema ili mambo mengine yote yakae vizuri, tukiweza kukusanya mapato ya kutosha, maeneo mengine yote hayo yatakaa vizuri. Kwa hiyo, hapa tuliposamehe kodi katika eneo hilo la ufugaji pamoja na vyakula vya mifugo, naliona hilo limekaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ujenzi wa reli ya kati kwa maana ya kiwango cha standard gauge…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kama nilivyosema mwanzo, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote naomba niwatakie ndugu zangu Waislam mfungo mwema, ili waendelee kupata baraka za Mwenyezi Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nikikipitia kitabu cha Waziri na taarifa za Kamati, nikaanza na sehemu ambayo ilikuwa inazungumzia hoja mbalimbali na hatua ambazo Wizara imekusudia kuchukua kwa maana ya kukabili changamoto. Wanasema kuendelea kuwianisha mapato na matumizi kwa kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema jambo hili ni jema, lakini kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba, kuhakikisha kuwa mgawo wa fedha utaendana na upatikanaji wa mapato, fedha hizo zinazopatikana bila kuwafikia walengwa tabu ipo na ni tabu kubwa. Kwa hiyo, naomba ikiwa amesema hizo ni hatua za kukabili, kweli hilo jambo tulifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto nafahamu. Kuna changamoto kwa maana ya mashine za kielektroniki, niendelee kusema jambo hili ni jema, lakini waendelee kufuatilia suala la udanganyifu katika mashine hizo za kielektroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa kwa fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo inaendelea kutukumbusha kwamba, ni vizuri tukajenga uwezo wetu binafsi kwa sababu unapokuwa unatamani kusafiri, lakini kwa nauli ya kutoka kwa jirani, hiyo safari iko mashakani. Niendelee kuomba Mheshimiwa Waziri kwa maana ya kujenga uwezo wetu wa ndani, ili hata kama fedha za wadau wa maendeleo zitakuwa hazipatikani tutakuwa tuko sehemu salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba elimu kwa maana ya miradi ya ubia kwa wadau mbalimbali, wadau hao tusiwasahau Madiwani. Tutakapokuwa tukizungumzia elimu kwa miradi ya ubia Madiwani ni kiungo muhimu kwa sababu wanatufanyia kazi kubwa kule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mafanikio Mheshimiwa Waziri amezungumzia mafanikio kwa maana ya kupunguza malimbikizo ya madai ya Watumishi, Wazabuni na Wakandarasi yaliyohakikiwa hadi Machi, 2017, Serikali imelipa kiasi cha shilingi bilioni 796.3. Nasema kwa hatua hiyo ni jambo jema, lakini tuendelee, malalamiko huko ni mengi na kwa kweli eneo hili tukilifanyia kazi tunaamsha ari ya watu kufanya kazi, lakini na wale wengine kama ni Wazabuni au ni wadau muhimu wa maendeleo wanapokuwa wakilipwa, maana yake wanashiriki zaidi kwenye kufanya shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la upelekaji fedha za maendeleo. Mimi kule kwangu Katavi hivi ninavyoongea hawajapata OC, hawajapata fidia ya vyanzo vya mapato kwa maana ya General Purpose Grant, suala la National Water Supply Sanitation Program, hawa watu fedha zote katika maeneo hayo hawajapata. Kwa hiyo, tunapozungumzia suala zima la kupeleka mbele maendeleo naiona shida kubwa katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namna pekee ya kuenzi watumishi na hasa wale wastaafu, mafao ya wastaafu na mirathi ilipwe kwa wakati. Hapa nilikuwa naendelea kupongeza, najua kuna program wanasema mfumo wa TEHAMA unaoitwa Saperion mpaka Machi, 2017 inaonesha wastaafu 96,989 wamewekwa kwenye mfumo, hili ni jambo jema, lakini niendelee kusisitiza namna pekee ya kuwaenzi wastaafu ni kuwalipa kwa wakati ili watu hawa waone kwamba, nchi inawaheshimu kwa utumishi walioufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza suala la utoaji elimu kwa Maafisa Mipango. Hapa kuna Maafisa Mipango 183 kutoka Sekretarieti za Mikoa na 237 kutoka Halmashauri kwa maana ya kuwajengea uwezo wa kutafsiri vipaumbele vya Kitaifa. Ni vizuri kuwajengea uwezo kwa sababu, watu hawa tunao kule katika maeneo yetu, wanapokuwa wanafahamu nini tufanye, elimu hiyo wataishusha kwa watu wengine pale, kwa hiyo tutakuwa tunaimba wimbo mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu tunaambiwa kwamba, 2016/2017 kukua kwa Pato la Taifa ilitoka 7.2 kwenda 7.3 na kwa maana ya 2017 tunakusudia kukua kwenda 7.4 ni jambo jema, lakini ninachoomba Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wanatamani tunapozungumzia habari hii ya ukuaji huu wa uchumi walione bubujiko kwenye mifuko yao. Namna pekee ya kuweza kuimba ukuaji wa uchumi uende sambamba na hali halisi katika mifuko yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo yote, najua pia kwamba, mfumuko wa bei unabaki tarakimu moja na nakisi ya bajeti ya Serikali isiyozidi asilimia 4.5 ya Pato la Taifa yote hayo nasema ni mema. Eneo la sekta ya ujenzi, naona hapa tunaambiwa kwamba, imekua kwa asilimia 13. Sekta ya Ujenzi kwa mimi ninayetoka Katavi naona namna pekee tutakayoweza kufanya kwa sababu, leo ukiuzungumzia mfuko wa simenti katika maeneo ya kwetu, bei ya mfuko wa simenti wakati nikiona sekta hii inakua, natamani tuone namna ambapo mkazi wa Katavi anapokwenda kuununua mfuko 20,000/= anapokwenda kununua mfuko zaidi ya 20,000/= ni namna gani na yeye atakuwa sambamba na ukuaji wa sekta hii ya ujenzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, kwa upande wangu naomba niishie hapo. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Na mimi nianze kuchangia Mpango huu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni eneo la kilimo. Mimi eneo la kilimo naomba niliweke katika sura zaifuatazo. Namwomba Mheshimiwa Waziri mipango yetu na kama ambavyo mmeeleza hapo iendelee kujikita katika kuzingatia tafiti mbalimbali. Nalisema hilo kwa sababugani?

Leo hii isitokezee kwamba kwa sababu korosho ina bei kubwa basi kila mtu akatamani kulima korosho, twende kwa tafiti. Kwa misingi hiyo kama ambavyo nimeendelea kusema hapo kwa kupitia tafiti tunaweza tukafahamu ni kanda zipi zinafaa kitu gani na isitokezee tu kwamba kwa sababu leo pamba ina bei nzuri basi kila mmoja akataka kulima pamba, naomba mipango ituelekeze huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, eneo hilo hilo la kilimo upande wa mahindi ambao kila mmoja amezungumzia hapa, mimi nitatoa mfano na wanasema kama huna vielelezo, haujafanya utafiti usiongee, naomba niongee kwa vielelezo na kwa utafiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nililima maharage lakini baada ya kulima maharage nikafanya maoteo kwamba mahindi yatanipatia pesa nzuri, kwa hiyo, nikabilisha maharage kununua mahindi. Ni mkulima mimi niliyelima maharage, lakini nikanunua mahindi, nikayahifadhi kwa maana nipate fedha nzuri kwa maana ya maoteo. Leo hii nisipopewa nafasi ya kuuza mahindi yangu, sitokuwa na nafasi ya kulima tena hata maharage, nitakuwa nimekatwa miguu.

Kwa hiyo, naomba sana katika maeneo hayo, wale wote ambao wamelima mahindi wapewe nafasi vinginevyo tutakwenda kutengeneza mazingira ya watu hao kutoweza kusimama kwa miguu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba nusu ya 2017 kilimo kilichangia kutoka asilimia 2.7 mpaka 3.1, umuhimu wa kilimo uko pale pale. Nafahamu kwamba kwa kupitia kilimo ni sehemu kubwa ambayo inaajiri Watanzania walio wengi, lakini mipango iendelee kutusaidia. Kilimo hiki ambacho ni cha kijungujiko (hand to mouth) sort of economy, tunatakiwa tutoke huko. Haiwezekani ikawa Watanzania wengi wako kwenye kilimo lakini mwisho wa siku kilimo hiki kisifanye watu tujitegemee. Ni bora hata wachache wakalima lakini wakalima kilimo chenye tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa niongelee suala la afya. Nilishauri mara ya mwisho, ni kweli nimeona hospitali kama ya Muhimbili na Bugando tunaendelea kuzipa vifaa tiba na kuongeza vifaa mbalimbali. Ushauri wangu unabaki pale pale, tuna mipango ya kuboresha Hospitali za Mikoa, mimi binafsi natoka Mkoa wa Katavi, tukiboresha Hospitali za Mikoa tunapunguza msongamano wa watu kwenye Hospitali hizo za Bugando, Muhimbili na kwingineko. Kwa hiyo, niliombe sana hilo tuendelee kufanyia kazi kwa maana ya kuboresha maeneo haya ya chini. Ukiniboreshea mimi Katavi, ukimboreshea wa Kigoma na wa Tabora tutapunguza watu kutegemea maeneo hayo. Eneo la afya naomba nitoke kwa sura hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la maji. Itakuwa ni kichekesho, mara ya mwisho nilizungumza hapa pia nikasema nchi hii tuna uwezo wa kufanya muunganiko wa maji kuwa kama design ya buibui. Mtu wa Nyasa akiunganishwa kupitia Ziwa Nyasa na Viktoria wakiunganishwa kupitia Ziwa Viktoria, Tanganyika tukiunganishwa kwa kupitia Ziwa Tanganyika, nchi hii itakuwa na mtandao wa mabomba ya maji. Hatuna sababu ya kwenda kwenye vyanzo ambavyo siyo vya uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo hii katika Mkoa wa Katavi tunazungumzia habari ya Bwawa la Milala na chanzo kingine cha Ikorongo wakati Ziwa Tanganyika lipo kilometa 120 kufika Manispaa ya Mpanda. Miradi mingine tunayoiona ya kutoa maji VI-ictoria iwe ni dira kwenye maeneo mengine. Hatuna sababu, nimesema kwingineko duniani watu wanabadilisha mpaka maji ya bahari kuwa maji safi ya kunywa, sisi hatutakiwi kufika huko kwa sababu vyanzo vingine vya maji safi, baridi ya kutumia tunavyo, ni mipango tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la misitu, naomba eneo hili nilizungumze kwa kina. Leo tunazungumzia miradi mbalimbali, tukizungumzia hata suala la Stiegler’s Gorge na kwingineko. Nilifarijika sana mtaalam mmoja majuzi katika semina ile tulipokuwa tunazungumzia suala la Sera ya Taifa ya Misitu alipotuambia pasipo misitu hata suala la umeme tunaouhitaji hautokuwepo, habari ya Stiegler’s Gorge na kwingineko kwa sababu maji hayatapatikana. Hata tukizungumzia suala la utalii, lina uhusiano wa moja kwa moja na misitu kwa sababu kwa kupitia misitu kuna biodiversity ambayo hiyo moja kwa moja inakwenda na masuala ya ecosystem, tukikosea hapo iko shida kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri kwenye mipango yetu tuendelee kuboresha suala hilo la misitu. Leo mkizungumzia mipango yote, yawe ni mabwawa ama vitu vingine bila kujikita kwenye kuhifadhi misitu, tatizo ni kubwa, umeme hatutokuwa nao na wakati mwingine hata kilimo pia itakuwa shida na eneo hili naomba tuendelee kupewa elimu pana. Wakati mwingine ukiona miti imetunzwa sehemu, sio kwa sababu anatakiwa mnyama awe pale, ni kwa ajili ya kutengeneza biodiversity pamoja na ecosystem ambayo ina nafasi kubwa kwenye kumsaidia binadamu.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami nipongeze Kamati zote mbili lakini nitajikita kwenye Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na naomna nianze na suala la Ngorongoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali kuihuisha Sheria ile ya mwanzo ya mwaka 1959, Ordinance Na. 413 ya mwaka 1959, nasema imepitwa na wakati kwa sababu zifuatazo:-

Kwanza, tukumbuke kipindi kile cha mwanzo wenyeji katika eneo hilo walikuwa ni 8,000 lakini kwa sensa ya hivi karibuni wenyeji wamefikia 93,851. Kama haitoshi, kiwango cha kutojua kusoma ni zaidi ya asilimia 70 kwa maana ya takwimu za mwaka jana. Pale ndani kuna shule 21 za msingi na mbili za high school, hiki ni kigezo cha kuonyesha kwamba watu hawa wanakuwa masikini. Pamoja na kiwango hicho cha elimu kule ndani magonjwa yameongezeka na kuna ukame na kwa sababu hiyo naendelea kujenga hoja ya kwamba hii sheria imepitwa na wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, naomba nije kwenye suala zima la utalii. Kumuunga mkono Rais wetu ni kwa maana ya kuunganisha mawazo ya kuiletea nchi mapato, napenda kusema kwamba eneo hili la utalii ni sensitive, nikimuongelea mtalii kwa ujumla wake maana yeye anaweza asije Tanzania akaenda sehemu nyingine yoyote. Ndiyo maana eneo hili la utalii kwa lugha ya kigeni wanaita ni hospitality industry.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunatakiwa kuwa watu rahimu, tukicheza watalii hawa wanayo nafasi ya kwenda maeneo mengine, mbuga ziko maeneo mengine. Kwa hiyo, naomba sana na katika hili niendelee kumshauri Waziri husika tunatakiwa kuwa watulivu kwa maana hatuko peke yetu katika eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoke hapo, niende kwenye eneo la matangazo kwa maana ya TANAPA na TTB. Ndiyo maana kwa mfano wenzetu wa Coca Cola sehemu nyingine kubwa wameingiza fedha kwa maana ya matangazo. Nami niombe, kazi nzuri ambayo imeendelea kufanywa kwa maana ya matangazo waiendeleze ndugu zetu wa TANAPA na TTB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaunga mkono, najua mara ya mwisho kulikuwa na kitu kinaitwa SITE (Swahili International Tourism Expo) waliifanya mwaka jana na ilikuwa nzuri kwa sababu imeendelea kuwaita tour operators kutoka maeneo mbalimbali duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili la matangazo naendelea kuisihi Serikali yangu, inatia huruma kuona kwa mfano, majirani wana-take advantage ya vyanzo tulivyonavyo. Mtu aseme njoo sehemu fulani utauona Mlima Kenya, kwa nini na sisi Watanzania tusiendelee kuchangamkia fursa hii, kama vyanzo ni vya kwetu kwa nini watu wengine watumie nafasi ya vyanzo vyetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo la wazawa waendelee kusaidiwa kwa maana ya biashara nzima ya utalii na uwindaji lakini naomba kuboresha najua ukanda wa Kaskazini tunaendelealea kuboresha maeneo hayo lakini watalii kwa ujumla wake kulikoni tukawapoteza tuendelee kuwafanya waje nchini kwa kuboresha na kanda nyingine kama Kanda ya Magharibi na Kanda ya Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo ukisema Kanda ya Magharibi, Mbuga kama ya Katavi tunayo nafasi ya kutoka Ruanga na Burundi wakipita Kigoma, wakaja kushangaa mbuga yetu nzuri ya pale Katavi. Kwa hiyo, naomba ukanda huo uendelee kuboreshwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusijikite tu kwa maana ya suala la mbuga hizi, tufungue vyanzo vingine kama fukwe, masuala ya utamaduni na mapango. Tulikwenda kuyaona mapango ya Amboni pale Tanga. Watanzania kwa ujumla wake tuna vyanzo vingi ni suala tu la kupanga tunaanza na nini tunamaliza na nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Olduvai, naomba suala la maabara pamoja na maktaba ziendelee kufanywa za kisasa ili wanafunzi wetu waendelee kwenda pale kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mwisho kabisa, eneo la Saadani. Hii Mbuga ya Saadani kwanza wanasema unakwenda katika eneo ambalo nyika zinakutana na fukwe. Kwa hiyo, ina sura ya pekee sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule mgogoro wa kijiji kimoja kilichopo pale, naomba Serikali ifanyie kazi ili ile Mbuga ya Saadani iendelee kutoa mafao makubwa kwa maslahi mapana ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kwa maana ya Sera ya Taifa ya Misitu, naomba tuendelee kuiboresha hiyo kwa sababu pasipo kuwepo na misitu hata huu utalii wote tunaouzungumzia haupo. Vilevile pasipokuwa na misitu hata masuala mengine mipango mingine tunayoikusudia kuifanya kama ya umwagiliaji na mambo mengine itakuwa ni kizungumkuti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Awali ya yote naomba nipongeze kiteno cha Serikali kuwarjesha watumishi. Napongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo kwa maana ya ukurasa wa saba unaozungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano kuna eneo linalozungumzia kujenga ari ya uzalendo kwa kuilinda na kuisemea nchi yetu bila woga, kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Eneo hili bahati nzuri jana tulibahatika kupata semina ya Kamati inayoshughulikia masuala ya mauaji ya Kimbari kwa maana ya genocide. Tumeambiwa sisi kama Wabunge, tunayo nafasi kubwa ya kudumisha amani, lakini ni vitendo vidogo vidogo ambavyo vikiachiwa, vitendo hivyo vikiendelea bila ustaarabu vinazaa mauaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hiyo, kama haitoshi tunaambiwa tushughulikie mapema kwa maana ya conflict early warning system. Tukishughulikia mapema tutaendelea kutengeneza nchi yenye amani na utulivu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 54 na 56 unazungumzia suala la afya. Katika eneo hili la afya naomba nijikite kwa maana ya Hospitali ya Mkoa ya Katavi. Bajeti iliyotengwa takribani shilingi bilioni 11, kwa suala zima la utoaji wa fedha na nilikuwa naomba Waziri Mkuu anisaidie katika hili, leo asubuhi nilisikia taarifa nchi ikipongezwa kwa maana idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi wanaanza kupungua, ni jambo jema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukiipongeza nchi kwa hilo, kule Katavi unapoongelea ujenzi wa hospitali ya mkoa ambayo tunahitaji takribani shilingi bilioni 11 kwa kasi ya utoaji fedha, mara mmepewa shilingi milioni 500, mmebahatisha shilingi bilioni moja, maana yake tunakwenda miaka 11 ili kumaliza ujenzi wa hospitali hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana. Na ninaliomba hilo kwa sababu, unafahamu Jiografia, umbali kule tuliko na bila msaada wa hilo na kwa wakati huu hospitali ya Manispaa ya Mpanda ndio inabeba dhamana ya kuwa hospitali ya mkoa, imeleemewa sana, inahudumia takribani Wilaya tatu, Majimbo matano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana hata pale tunapozungumzia kuwezesha fedha, ili kupunguza mzigo nilikuwa naomba hilo tujaribu kuliangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kwa maana ya hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 31 mpaka 32 unazungumzia masuala ya umwagiliaji kwa ujumla wake kwa kupitia kilimo. Tunao mradi mkubwa wa Mwamkuro, mradi huu kwa maana ya bajeti ya mwaka 2013/2014 ulitengewa milioni 294 na fedha hizo zilikuwa zimelenga kukamilisha kilometa mbili, lakini umbali wa mradi mzima ni kilometa tatu. Eneo hilo ni ukanda mzuri ambao una uzalishaji mkubwa wa kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa nakiomba, ili thamani ya fedha iweze kuonekana kwa kiwango kile cha fedha kilichotengwa ambacho kimekwenda kukidhi kilometa mbili tu hatutaweza kuiona thamani ya fedha. Ni vizuri fedha ikatengwa ya kutosha ambayo itufikishe kwenye zile kilometa tatu zilizokusidiwa na ninalisema hilo makusudi kwa sababu kwa kupitia kilimo cha umwagiliaji na eneo lile ni zuri lina rutuba ya kutosha tutaweza kuzalisha mazao ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoke hapo, kwenye suala zima la nishati. Nafahamu jitihada za Serikali na kwa maana ya Mkoa wa Katavi tunazo mashine mbili pale zinasaidia japo umeme unakatikakatika, lakini muarobaini wa kutatua matatizo ya umeme…

(Hapa Kengele ililia kuashiria kuisha muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuanzia naomba niwapongeze Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa, Mheshimiwa Engineer Nditiye na Mheshimiwa Kwandikwa kwa kazi wanazoendelea kuzifanya na kwa ujumla wake chanda chema hivikwa pete. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mpanda – Koga – Tabora kwa maana ya kilometa 373 inayoendelea kutengenezwa, naendelea kuieleza Wizara, tunalo eneo korofi la Mto Koga. Eneo lile ni korofi muda wote, kwa mfano sasa hivi barabara ile haipitiki kutokana na ukorofi wa ule Mto Koga. Naomba hata haya matengenezo yanayoendelea tuzingatie maeneo yale ya daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana wakati tukiitengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami kwa ajili ya kukomboa maeneo yote ya Mkoa wa Katavi na Tabora kwa ujumla wake, tusisahau barabara ya Mpanda – Ugala – Kaliua – Ulyankulu - Kahama kwa maana ya kilometa 457.

Barabara hii hata kama ikitokea imepata tatizo tunakuwa na escaping route, hii barabara nyingine inatukomboa wakati ambapo barabara moja inakuwa na matatizo. Kwa hiyo, naomba barabara zote hizi ziende sambamba, lakini napongeza jitihada ya kutengeneza barabara ya Mpanda – Koga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la Kiwanja cha Ndege cha Mpanda. Mara ya mwisho niliuliza swali hapa, Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Nditiye alinihakikishia kupatikana kwa gari la zimamoto katika uwanja ule. Pamoja na kupatiwa gari la zimamoto na huduma nyingine tunaomba tupatiwe route sasa ya ndege kuja eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikizungumzia suala la route za ndege, vigezo vya kusema, je, tutapata wasafiri, hebu leteni ndege halafu muone kama mtapata wasafiri. Kuna maeneo mwanzoni walikuwa wanaona kama hawana wasafiri, nitatoa mfano wa Bukoba, leo hii wanatamani kuongeza route au Tabora, tunaomba mtuletee ndege halafu muone. Hii habari ya kusema tutapelekaje magari hakuna abiria lakii mkipeleka barabara mnashangaa magari yamejaa. Sasa hivi Sumbawanga kwenda Mbeya magari ni mengi lakini mwanzo walikuwa wanasema route ile haina magari. Kwa hiyo, naomba upande wa uwanja wa ndege tuleteeni route halafu muone. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo naomba nizungumzie suala la reli. Kipindi hiki naomba ziendelee kutengwa fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa reli kutoka Tabora - Mpanda, maeneo ni korofi. Sambamba na utengenezaji naomba kitu kingine, tuna mabehewa machache na nashangaa reli ile kwa muda mrefu hatujabahatika kupata behewa la daraja la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, najiuliza wananachi wako kule na si kwamba wanapanda bure, wanalipia, vipi tunashindwa kupatiwa behewa la daraja la kwanza? Naomba ufafanuzi wa suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niwasemee pia wananchi wa maeneo ya Msasani - Tambukareli. Kulikuwa na bomoabomoa, wataalam njooni muendelee kutusaidia, je, ni umbali upi hasa ambao watu wanatakiwa kupewa fidia? Njooni mtusaidie kuangalia kama wananchi wale wako katika maeneo husika na kama kweli wako katika maeneo husika wale ambao wamebomolewa suala la fidia lichukue mkondo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme jambo moja lenye sura ya kitaifa. Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ni jicho la nchi hii, ni kioo cha nchi hii na ni ubalozi unafanyika pale, wanapokuja watu kutoka nchi za nje inatia aibu. Naomba kasi ya ujenzi wa Terminal III iongezwe maana nimejaribu kuangalia hapa kwa kipindi hiki wametengewa shilingi milioni 179.82 kwa ajili ya ujenzi wake, tuujenge uwanja huo. Watalii wanapokuja, watu mbalimbali wanapokuja tunapata aibu na jambo dogo kama suala la air condition katika uwanja ule linatutia aibu.
Naomba tulifanye hilo kwa sababu mtu anapokuja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na Watendaji wote katika Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri nikaufahamisha umma kuwa mimi pia ni mmoja kati ya wachimbaji wadogo wa madini. Kwa sura hiyo, naona kabisa kwamba eneo hili likiendelea kutulea wachimbaji, mchango wetu kwa nchi hii utakuwa mkubwa. Mara ya mwisho niliwahi kuzungumza hapa, uzuri wa wachimbaji wadogo, fedha wanayopata hawaendi kuwekeza nje, wanakwenda kuwekeza ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, tukiwaendeleza wachimbaji wadogo kwa ujumla wake, maana yake tunakwenda kuboresha maendeleo ya miji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema hapa Johannesburg imejengwa kwa fedha ya pale pale. Kwa hiyo, naamini iwe ni Mwanza, Shinyanya, Chunya na Mpanda nakotoka, wachimbaji hawa wadogo wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiona kazi nzuri ya GST kwa maana ya suala zima la utafiti. Nina eneo moja la Kapanda pale kwangu ambapo kwa maana ya kitabu hiki inaelezea wakia 47,605 ziliweza kubainika pale Kapanda. Rai yangu, pamoja na tafiti hizo nzuri zinazofanywa na ndugu zetu wa GST, eneo lile la Kapanda wameshaelekeza kwamba kitajengwa kituo kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia wachimbaji, siioni kasi ya kufanya zoezi hilo. Kwa hiyo, naomba pamoja na tafiti hizo nzuri ambazo amezifanya, basi ile kasi ya kwenda kujenga kituo pale isomeke.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nami nizungumzie suala la leseni. Nafahamu utoaji wa leseni hapa katikati tulikuwa tunasubiria Tume. Nashukuru kwamba Tume imepatikana na kuna watendaji mahiri katika Tume hiyo basi nilichokuwa naomba tu-speed up suala la utoaji leseni. Niseme hivi, utoaji wa leseni ni chanzo kingine cha mapato. Kwa hiyo, tunapochelewa kutoa hizo leseni, pia tunachelewa katika suala la mapato. Tutakapokuwa tukitoa leseni hizo tusiwasahau wachimbaji wa eneo la Kapanda, Dilifu na kwa ujumla wake, maeneo yale ya Mpanda ambapo Serikali iliahidi kuwasaidia wachimbaji hawa wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona suala la migodi ya STAMICO pale ambapo inakuwa haifanyi vizuri, basi Serikali ione namna ya kuweza kuwapatia wachimbaji wa kati. Hilo nalo nami naendelea kuishauri Serikali, kama STAMICO itakuwa imeshindwa kufanya vizuri, basi mwone nafasi hiyo ya kuweza kuwapatia wachimbaji wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa smelter, nafahamu na hapa katika ukurasa wa 38 na 39 inaelezea. Kwa mfano, ukija maeneo ya Mpanda kwa maana tu ya tailings, hapa Kiswahili cha tailings wanasema visusu, ukija katika suala la tailings tu pale maeneo ya Mpanda kuna visusu vya kutosha katika eneo lile, tatizo lake ni teknolojia sahihi ya jinsi ya kuitoa dhahabu katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua jiolojia ya Mkoa wa Katavi ni tofauti na ilivyo Mwanza na Chunya, kwa hiyo, kila watu wachukuliwe kwa namna yake. Ndiyo maana leo unaweza ukakuta mchimbaji wa Mpanda pamoja na kuwa na visusu vya kutosha lakini hana uwezo wa kuipata ile dhahabu kwa sababu ya lack of technology. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ituangalie kwa jicho hilo la huruma watu wa kanda ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwa maana ya mwamba wa eneo lile, kuna madini mengi tu. Kwa wakati mmoja anaweza akapata dhahabu, copper, fedha na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, sasa namna ya ku-separate, it is an issue. Kwa hiyo, naomba sana hilo nalo liweze kuangaliwa kwa sura hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana naendelea kusisitiza, najua kwa maana ya thamani iongezewe hapa nchini, ujenzi wa smelter ni jambo la msingi, ingawa nafahamu uwezekano wa kujenga smelter inaweza isifanyike kwa usiku mmoja, ni suala la hatua. Kwa hiyo, wakati tukijipanga kwenda huko, tuendelee kuangalia tunafanyaje na wale ambao tayari wanaendelea na uchimbaji katika sura hiyo nyingine? Najua Mheshimiwa Waziri na Watendaji kwa ujumla wenu na Serikali yangu kwa ujumla wake kwa usikivu huu mtaliangalia suala hilo kwa jicho la pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ruzuku pia, kwa maana ya wachimbaji hawa tunapozungumzia kuwawezesha ni pamoja na kuwapatia ruzuku. Kama kulikuwa na upungufu huko nyuma, naomba tuzitoe zile tofauti lakini tusiache kutoa ruzuku kwa watu hawa. Ni kwa kufanya hivyo tutaongeza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, najua kuna suala la local content, kwa maana ya kuhakikisha wazawa wananufaika na suala zima la uchimbaji. Mimi naliangalia kwenye sura hii, tutakapojenga uwezo wa wachimbaji wadogo, fedha ambazo watapata watu hawa, mzunguko wake unarudi palepale. Mtu huyu kama akienda sokoni atanunua materials ambazo ni za hapa hapa nyumbani, atampeleka mtoto shule na maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama unamzungumzia mama lishe, fedha ikitoka mgodini itakuja huku, itamkuta mama lishe, fedha ikitoka mgodini ikija huku itamkuta mchuuzi mwingine sokoni. Kwa hiyo, kwa sura hiyo tunauona mtiririko wote wa suala la fedha kwa watu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la ujenzi wa Ofisi ya Kanda ile ya kule kwetu Mpanda. Mpaka leo suala hili la ujenzi wa ofisi sioni dalili. Kwa hiyo, naomba sana na Mheshimiwa Waziri wangu anasikia pale, sisi ni Kanda ya Magharibi, utashangaa Makao Makuu ya Kanda hata ofisi haipo. Kwa hiyo, naomba sana lile zoezi la ujenzi wa ofisi liendelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika maeneo tofauti tofauti upelekaji wa fedha katika Wizara inarudishwa kwa kiwango kidogo. Tutaipataje tija kama watu hawa hawapewi fedha za maendeleo? Naomba sana kwa ujumla wake kama ni Wizara ya Fedha tuendelee kuwaangalia watu hawa. Watu ambao wanachangia kwenye pato la Taifa unaposhindwa kuwarudishia fedha maana yake unakuwa umewakata miguu, hawataweza tena kutoka hapo walipo ili kuongeza mafanikio.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa ajili ya muda, nianze kwa kuunga mkono hoja. Naomba nianze na kipengele cha kwanza kinachogusia rasilimali fedha. Najua kwa kupitia Taarifa ya Kamati, ukurasa wa tatu na wa nne kwa ujumla wake naomba kipengele hiki muhimu tukione kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, katika ukurasa wa tatu ule, kipengele hiki kinagusa hilo suala la rasilimali fedha, anasema: “Baadhi ya mafungu ya Wizara yamepata fedha za kutosha na hivyo kutekeleza majukumu yake kikamilifu. Vile vile kuna mafungu ambayo hayakupewa fedha za kutosha, hivyo kuathiri utendaji kazi wake.” Hilo ni eneo la fedha.

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, tunaambiwa, kama Wizara ya Fedha na Mipango imeshindwa kuwezesha kwa baadhi ya vifungu vyake kupata fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake ya msingi, itawezaje kuhakikisha mafungu ya Wizara nyingine kupata fedha za kutosha?

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa rasilimali fedha, najua Wizara hii ni muhimu. Kama yenyewe tu inapata shida eneo la fedha, vipi kuhusu Wizara nyingine? Naomba hilo liangaliwe sana. Nalisema hilo kwa maana ya suala hilo hilo la rasilimali fedha, kuna huu mradi wa LGDG ambapo kwa nia njema kabisa, Serikali ilikuwa imekusudia kwa wakati mmoja kutoa fedha ili kumaliza miradi viporo, lilikuwa ni jambo jema sana. Kwa mfano, kule kwangu kwa kupitia ruzuku y a Serikali, kwa kupitia TAMISEMI of course, lakini Wizara ya Fedha iki-facilitate hilo jambo, kuna zaidi ya Sh.923,475,000. Fedha hizi zilikuwa zimelenga maeneo ya elimu na afya.

Mheshimiwa Spika, leo mashaka yangu ni kwamba tunakwenda karibu robo ya mwisho na bahati mbaya fedha hizi ambazo Serikali ilikuwa imekusudia kupeleka huko katika wilaya na maeneo mbalimbali, kwa bajeti hii inayokuja, hakuna sehemu fedha hii inasomeka. Kwa hiyo, nilichokuwa naomba kwa namna yoyote ile, tuhakikishe fedha hizi zimekwenda huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, kuhusu suala la rasilimali fedha, napongeza kwamba kwa kupitia Taarifa ya Kamati kuna maeneo mbalimbali yanazungumzia suala la Wizara kuendelea kufanya mazungumzo ili ama kupunguziwa au kusamehewa madeni. Najua hilo likifanyika, litaendelea kutoa nafasi ya fedha za ndani zinazopakana kugharamia bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua na nakubaliana na wale wote na Wizara tunaomba Mheshimiwa Waziri alielewe vizuri, nakubaliana na maelezo yaliyotoka kwenye Kamati kwamba ukitaka kukusanya mapato zaidi, ni lazima uwekeze zaidi, siyo kutegemea mapato bila kuwekeza. Kwa hiyo, naendelea kuomba namna yoyote ile ambayo itatusaidia kwenda kuongeza mapato.

Mheshimiwa Spika, katika hili niendelee kushauri, najua ndugu zetu wa TRA lengo ni kuhakikisha nchi inapata fedha kwa kupitia kodi. Bado nashauri namna rafiki, najua suala la kudai kodi siyo jambo jepesi, linataka kusukumana, lakini kwa kupitia namna rafiki, bado inaweza ikamfanya mtoaji wa kodi akaona umuhimu wa kutoa kodi ikienda sambamba na elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, eneo la mafao ya wastaafu na mirathi, naona hili katika Taarifa ya Wizara, ukienda ule ukurasa wa 39 na 40, najua kimetengwa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kulipia michango ya mwajiri kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hadi kufikia Aprili, 2018 kiasi cha shilingi bilioni 716.1 sawa na asilimia 71 kilikuwa kimetengwa.

Mheshimiwa Spika, nasema suala hilo ni jema Mheshimiwa kwa maana ya kujali mafao ya wastaafu na mirathi. Niendelee kusisitiza Mheshimiwa Waziri, wafanyakazi hawa, wastaafu hawa ni uti wa mgongo wa Taifa hili, ni watu ambao waliitumikia nchi hii kwa uzalendo mkubwa. Inapofika sehemu mtu kastaafu, ni wajibu wa Serikali kuendelea kumwangalia mtu huyu. Nashauri sana hilo liendelee kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo Mheshimiwa, kuna suala la uhakiki wa madeni ya watumishi na Wakandarasi na Wazabuni pia. Eneo hili la madeni najua mara ya mwisho Serikali ilitoa kiasi cha fedha kwenye kuonesha jitihada za kuanza kupunguza madeni ya wafanyakazi. Nafahamu kwa ujumla wake, katika eneo hili kule Mkoani kwangu Katavi, eneo tu la madeni ya watumishi kuna takribani Sh.501,918,296/= ambapo humo ndani pia tuna madeni yanayowagusa Wazabuni, kuna Watumishi wasiokuwa Walimu na kuna Walimu.

Mheshimiwa Spika, ninachoomba, ili kuondelea kutoa tija kwa watu wetu, eneo hili la madeni ya Watumishi na Wazabuni kama ambavyo imesomeka katika maeneo mbalimbali, nilikuwa naomba liendelee kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua kuna suala linazungumziwa kuhusu kupuangua kwa mfumuko wa bei. Kati ya vipengele vilivyoongelewa kuhusu suala la kupungua kwa mfumuko wa bei, limeongelewa suala la kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula kama baadhi ya vitu vilivyosaidia kupunguza mfumuko wa bei. Narudi kwenye point ile ile ya msingi, tunapofarijika na kuongezeka kwa uzalishaji wa chakula, mtu wa kawaida ambaye hana elimu ya uchumi, anatamani kuona kumbe kama hili linachangia kwenye kufanya mfumuko wa bei usiwepo lakini yeye aliyeshiriki kuzalisha chakula kwa namna gani anapata moja kwa moja mafao ya yeye kukizalisha chakula. Nikilisema hilo, tafsiri yangu tuendelee kuangalia namna ambapo huyu mzalishaji wa chakula na yeye anapata manufaa ya moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua lugha zote hizi zinazoongelewa hapo, tunaambiwa kwamba kutoka mwaka 2017 kwa maana ya mfumuko wa bei ilikuwa 5.3, napongeza hilo, lakini kwa maana ya 2018 umeshuka mpaka 3.8. Huu mfumuko wa bei na kushuka kwake ni jambo jema, lakini naendelea kuishauri Serikali yangu, namna pekee ya mtu wa kawaida kuliona hilo, usomeke kwenye mifuko yake. Ikisomeka kwenye mifuko, tunakuwa tunaimba wimbo mmoja, wananchi na Serikali yao.

Mheshimiwa Spika, najua kwa maana ya malengo ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/2019, umeandaliwa kwa kuangalia dira ya 2025, lakini kuna malengo endelevu ya 2030. Ukija katika ukurasa wa 85 kwa maana ya Hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwa maana hii ya malengo ya mpango wa bajeti, inasema hivi:

“Baadhi ya vitu ambavyo wamezingatia ni pamoja na masuala mtambuka kama vile jinsia, watu wenye ulemavu, mazingira, UKIMWI, makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi na masuala ya lishe kwa jamii pamoja na maelekezo na ahadi zilizotolewa Kitaifa.”

Mheshimiwa Spika, niendelee kushauri. Kama kumbe bajeti hii malengo na mipango yake inazingatia suala hilo; masuala ya walemavu, masuala yanayogusa UKIMWI, nilikuwa naomba suala hili liendelee kusomeka. Walengwa kwa maana ya walemavu wafike sehemu wakutane na kile ambacho mipango inaelekeza kwamba watu hawa wameguswa moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi, eneo la UKIMWI naomba niendelee kushauri, mara nyingi na watu wengine wamekuwa wakiliongelea hili. Wakati tukitenga fedha kwa ajili ya kusaidia masuala ya watu wenye maambukizo na vinginevyo, nashauri eneo la watu wazima kutumia sehemu kubwa ya fedha na walengwa wakawekwa pembeni, jambo hili naliona halina tija. Kwa hiyo, naomba niendelee kusisitiza, wakati tunazungumzia suala hilo tujaribu kuendelea kuangalia kwamba walengwa, fedha sehemu kubwa iende ikawaguse walengwa.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nami niendelee kupongeza kama nilivyosema mwanzo. Naunga mkono hoja. Nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza, nianze kwa kuunga mkono hoja. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote walioko katika ofisi hii, kitabu kimesheheni mambo mbalimbali na nitajikita katika maeneo machache, eneo la afya pia madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uhakika wa sera zisizoyumba, amani na utulivu, vitu hivi vikiwepo vinatengeneza ustawi wa uchumi. Kama hiyo haitoshi doplomasia ya kiuchumi ndiyo gari tunaloweza kusafiria na likatufikisha katika uchumi wa kati na uchumi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kitabu cha hotuba ya Waziri Mkuu katika sekta za uzalishaji kwa maana ya ukurasa wa 27, eneo la utalii ambao ni ukurasa wa 32, eneo linalogusia uendelezaji wa utalii Ukanda wa Kusini kwa maana ya REGROW nimeona linazungumziwa suala zima la uendelezaji wa viwanja vya ndege, ni jambo jema na lenye afya. Kwa kuwa Mkoa wangu wa Katavi uko katika Ukanda huo wa Kusini tunao Uwanja mzuri wa Ndege wa Katavi, bila kuufanya uwanja ule ukafanya kazi habari hii ya kuendeleza ukanda ule kiutalii itakuwa pia haijakaa vizuri. Nendelea kumkumbusha Waziri Mkuu Uwanja wa Katavi, Uwanja wa Mpanda ni mzuri, ni changamoto katika kuibua suala la utalii katika ukanda ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda kwenye eneo la madini natamani kwanza nigusie masuala yanayogusa afya, kwa maana ya kitabu cha Waziri Mkuu tutaikuta ukurasa wa 56, 57, 58, najielekeza katika suala la hospitali. Nafarijika sana nikija katika eneo hilo kwa maana ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Mloganzila.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili likitumika vizuri na kwa jinsi ambavyo nchi imejiwekeza kwenye kuimarisha sekta hiyo ya afya, tunakuja kwenye kitu kinachoitwa utalii wa tiba. Tukifanya vizuri, tukiendelea kuimarisha hospitali zetu hizo watu kutoka nchi za jirani iwe ni Malawi, Zambia au Kenya kama ambavyo Watanzania tumekuwa tukitoka hapa tukienda India, tutumie nafasi hii ya kuimarika kwa hospitali zetu kwenda kwenye eneo la utalii wa tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo siwezi nikashindwa kuzitaja hospitali zote za rufaa. Najua nchi kama nchi imejipanga vizuri na nafahamu mara ya mwisho tuna zaidi ya hospitali zile 67 kwa maana ya Halmashauri mbalimbali lakini kuna hospitali mbalimbali za rufaa ambapo nchi imejipanga kwenda kuzijenga, hospitali hizo ni pamoja na Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Rai yangu ni moja, kusema ahsante ni namna ya kuomba tena. Najua tumetengewa takribani shilingi bilioni 1 lakini kwa maana ya bajeti ya zaidi ya shilingi bilioni 9, naomba sana Serikali yangu sikivu uwezekano wowote wa kuona namna ya kupatikana kwa fedha ili badala ya kuwa na muda mrefu wa kujenga hospitali hizo tuwe na muda mfupi na tukamilishe zoezi hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikilisema hilo ninamaanisha nini? Niliwahi kusema katika Bunge lako hili Tukufu kwa sisi ambao tuko Mikoa hiyo kama Katavi, kumtoa mgonjwa kutoka Katavi kumpeleka Bugando au Dar es Salaam umbali huu unaweza ukamalizwa kwa kuwa na hospitali ya rufaa pale pale Katavi. Ndiyo maana naendelea kusisitiza ujenzi wa hospitali hizo za rufaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la madini na kama ilivyo ada mimi pia ni mchimbaji mdogomdogo wa madini, naomba hilo lifahamike mbele ya umma huu. Rai yangu katika eneo la madini, tumekuwa tukiongelea habari ya ajira. Nitoe ufafanuzi mdogo, eneo la madini katika muda mfupi na ukizunguka nchi hii ukaangalia eneo la machimbo ya madini ndiko ambako ni maeneo yamekusanya watu wengi. Kukiwa na kitu wanaita gold rush kwa wakati mmoja usishangae kukuta una watu hata 5,000 na zaidi ya hapo. Kwa hiyo, unaweza ukaona jinsi ambavyo eneo la madini limesheheni watu wengi na linatoa nafasi kubwa ya ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kazi nzuri ambayo inafanywa na Rais wetu, najua tarehe 22 Janauri, 2019 alihamasisha na Wizara ikawakusanya wadau wa madini, kazi aliyoifanya Mheshimiwa Rais ni kazi nzuri. Rai yangu naitoa upande wa Wizara ya Madini, wakati tukiendelea kuboresha, unapomboresha mchimbaji mdogo hatima yake atatoka hapo atakuwa mchimbaji wa kati na baadaye anaweza kuwa mchimbaji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunapomlenga huyu mchimbaji mdogo hatutarajii abaki kuwa mchimbaji mdogo, kesho atakuwa. Sasa rai yangu ni nini? Kama nchi tuendelee kuandaa watu hawa kwa maana ya elimu. Leo wachimbaji wengi wadogo ikifika sehemu anatakiwa aingie ubia labda na watu wa kutoka nchi za nje, je, kama nchi tumewaandaa vipi watu hawa kwa maana ya elimu ya mikataba, tunafahamu vipi watu hawa katika maeneo ambayo wanayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kinaitwa reserve, labda kwa kupitia GST wanaendeleaje kuwasaidia wachimbaji hawa wakajua hifadhi ya madini waliyonayo kwamba ile inaweza ikawa ni jambo jema la yeye kuingia mikataba? Anapoweza kuingia mkataba asilimia ambazo anaweza akazipata kutokana na eneo lake na hifadhi aliyonayo ya madini pale ni silaha tosha au ni ngao tosha ya kumpa kibali cha kuingia mkataba. Kama watu hawafahamu elimu ya mikataba, wanaishia kudhulumiwa. Naomba elimu hiyo ya mikataba iendelee kutolewa kwa wachimbaji wetu mbalimbali.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Awali ya yote nami nimshukuru Mheshimiwa Waziri na timu nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchangia naomba nianze eneo la elimu maalum kwa maana ya ukurasa wa128, nashauri jambo moja kwa maana ya wananchi tuendelee kuhamasisha mbali na kuhamasisha kuhakikisha hatuwafichi watu hawa wenye ulemavu, tunawaandikisha ili waweze kushiriki katika nafasi ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la upungufu wa elimu, eneo langu la Mkoa wangu wa Katavi, hasa kwa maana ya masomo ya physics na mathematics. Tatizo la Walimu kama tulivyoongea maeneo mengine na bahati mbaya, kuna Walimu wanapangwa kuja katika maeneo yetu, lakini hawafiki. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba hilo nalo alibaini. Kuna Walimu ambao wamekuwa wakijitolea kwa muda mrefu, labda tufike mahali tuone, hawa ambao wamekuwa wakijitolea labda ajira ziende kwa watu hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoka hapo, bahati nzuri, nimshukuru Mheshimiwa Waziri, aliweza kufika Mkoa wa Katavi, aliweza kutembelea Chuo cha VETA, aliweza kutembelea shule ya watoto wa kile pale Mpanda na kwa ujumla wake, nishukuru upande wa VETA, waliwezesha fedha kwa maana ya ukarabati, lakini kuna upungufu wa takribani milioni 100 kwa maana ya awamu ile ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ukarabati. Naomba hili Mheshimiwa Waziri alitilie maanani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kwa maana ya eneo lile la majengo, kwa maana ya shule za sekondari, Mheshimiwa Waziri, upande wa Mpanda, shule ya wasichana, ni kweli tumeongea hapo nyuma, naomba kwa maana kama maeneo mengine nayo ile ni shule kongwe, ameiona yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri, tuna tatizo la uzio na ukarabati wa shule kwa ujumla wake. Najua mazingira mazuri tunapojaribu kutafuta kujua mwanafunzi anasomaje, anawezaje ku-concentrate ni pamoja na mazingira mazuri, yana nafasi yake kubwa sana katika ufaulu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, nami katika elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi, naendelea kushukuru, wakati Serikali imejipanga, kwa mfano, kwa maana ya Arusha Tech, imejipanga kwa maana ya kununua vifaa vipya. Hili naliomba sana, dunia inakwenda kwa kasi, teknolojia zinabadilika, kwa hiyo, Wizara kwa kuliona hilo, kwamba ni vizuri basi, tukaja na vifaa vipya, hili jambo naliunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Wizara, kwa maana ya Mtaalam Elekezi, ule ukurasa wa 18, ambaye anakwenda kutengeneza capacity building, kwa maana ya labour market ya vitu vingine vya namna hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho mwaka jana, kati ya tarehe 19 na 20, nilishiriki katika mkutano mmoja mkubwa Astana, huko Kazakhstan, wenzetu, pamoja na kwamba ni nchi ambazo zimepiga hatua. Katika mkutano huo, ambao ulikuwa na kichwa cha habari Investing in Youth Living no One Behind. Watu hawa wamechambua mambo mengi, lakini katika hayo waliyochambua na hili nimeliona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri. Nimefarijika sana kwa hilo, kwamba wenzetu ambao tayari wamekwishaendelea, lakini wameona kwamba namna pekee ya kufanya, ni kufanya katika sura ifuatayo:-

Kwanza, ni kuamsha ufahamu kuhusu elimu, afya, ajira na masuala ya kijamii, lakini ufahamu huu, especially kwa those ambao ni disadvantaged. Tukitoka hapo, wameamua kwenda na jambo moja, uwezeshaji zaidi, elimu bora, kwa maana ya vocational training, inayokwenda na ushindani na mahitaji ya soko la ajira, uchumi wa dunia na maendeleo ya teknolojia. Haya yote ambayo wajumbe wamekuwa wakiongea, kama hatuendi kuangalia mahitaji ya soko, uchumi wa dunia, mabadiliko ya teknolojia, tutaendelea kupiga kelele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo kama halitoshi, kuna suala, wenzetu wamekuja na kitu wanasema, review and adjust the education system and vocational training in line with economic, social and entrepreneur realities. Kwa hiyo, haya yote nilikuwa nasema, wenzetu huko duniani wameendelea kuaona kwa sura hiyo. Kwa hiyo, niombe, katika mazingira haya, ambapo nilijaribu kusoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri, bahati nzuri, nilipokuwa nikitoka ukurasa mmoja nafikiria kwamba jambo hili linalogusa kuwawezesha watu kwa sayansi na teknolojia sasa hivi linapatikana wapi, nalikuta ukurasa wa pili, nikitoka ukurasa wa pili nalikuta ukurasa wa tatu. Kwa hiyo, katika hilo niendelee kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa kuheshimu muda, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote nami nianze kumshukuru Waziri Mheshimiwa Mbarawa, nafahamu aliweza kututembelea Mkoa wa Katavi na kwa pamoja tulikwenda kwenye chanzo cha Ikolongo lakini alifuatilia suala la Bwawa la Milala na akaona hali ya ugawaji maji katika Mji wetu wa Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu umuhimu wa maji kama walivyozungumza wazungumzaji wengine waliotangulia na kwa kuanzia nikiwa nimetangulia na kuunga mkono hoja, naomba niliweke katika sura zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kugawa fedha I mean ile Sh.50 tunayoiomba sina matatizo nayo, rai na ombi langu tunapokuwa na pipa lenye tundu wakati tunaendelea kujaza maji kwenye pipa hilo, ufumbuzi ni kwenda kuziba tundu, vinginevyo tutaendelea kuhakikisha pipa lile halijai maji. Kwa hiyo kupewa fedha, kuwaombea fedha sina tatizo nalo, lakini kudhibiti matumizi ya fedha hapo ndipo ilipo hoja ya msingi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, naomba, nafahamu kwa maana ya Jimbo langu la Mpanda Mjini tulipatiwa visima 15, uungwana unanituma kushukuru na visima vile vilishafanyiwa pumptaste, jambo linakwenda vzuri. Lililobaki Mheshimiwa Waziri na wananchi wale wamesharidhika na kazi nzuri ya Serikali kama tumefikia hatua hii ya pump taste limebaki jambo moja tu la kufunga pump. Kwa hiyo niiombe Wizara tukamilishe zoezi hilo la kufunga pump ili wananchi wale waendelee kuwa na imani na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukikamilisha suala hilo la ufungaji wa pump kwa visima 15, naomba nishukuru tena, nafahamu tumesaini kwa maana ya Ikolongo namba mbili na Mheshimiwa Waziri tulikwenda pamoja akakiona chanzo kile, Mji wetu wa Mpanda asilimia ya maji ambayo inagawanywa pale ni kati ya asilimia 30 ambayo ni kiwango kidogo na ukienda field inaweza ikawa chini ya asilimia 30, tuna maeneo ya Makanyagio, tuna maeneo ya Majengo kwa ujumla pale mjini kati mgawanyo wa maji ni tatizo na tunapata matatizo wakati vyanzo vimetuzunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba Serikali wametusaidia kwa maana ya kusaini na Wakandarasi wako site kwa maana ya Ikolongo namba mbili. Ninachokiombna fedha zile za awali zimetolewa lakini naomba basi ili tukiusukuma huo mradi wa Ikolongo namba mbili tatizo la maji kwenye eneo letu la Mji wa Mpanda itakuwa historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kupongeza zaidi, najua tunakwenda kuusubiri mradi mkubwa kuyatoa maji Ziwa Tanganyika kuyaleta maeneo ya Mpanda na kwingineko. Najua mradi huu utakuwa ni mwarobaini wa matatizo ya maji katika maeneo yetu. Wakati tukiishi kwa matumaini kwa mradi huo, nilichokuwa nakiomba sana Ikorongo Namba Mbili itakuwa ni ufumbuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua pia tuna mradi mmoja wa Manga – Kasokola, toka tumeleta certificate katika Wizara, ililetwa tarehe 12 Desemba, 2018 ya shilingi milioni 47 mpaka leo haijalipwa. Mradi ule kwa maana ya Manga na Kasokola, mkandarasi amefika sehemu ya kukata tamaa. Nachokiomba, tukipatiwa fedha hizi akalipwa mkandarasi sehemu ile ya Vijiji vya Manga na Kasokola tatizo la maji nalo litakuwa ni historia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona maeneo mengine wakizungumzia kuhusu vyanzo vya maji kwa maana ya mabwawa; sisi katika Mji wetu wa Mpanda tunalo Bwawa la Milala. Ni bwawa zuri lakini tatizo chanzo kile kama kimetelekezwa fulani hivi. Viboko wamezaliana, maji ni machafu, wakati wengine wanahangaika tutapata wapi maji sisi chanzo tunacho tatizo ni utunzaji na kuhakikisha tunaya-treat yale maji ili kuongeza mserereko wa maji pale Mpanda Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wanalalamika watapata wapi maji, sisi maji tunayo chanzo kipo cha Milala. Historia itatuhukumu kama watu walifanya kazi nzuri kuhakikisha chanzo kile kimekuwepo leo chanzo kipo tunakitelekeza kwa makusudi. Naomba Wizara ikiangalie chanzo hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana Bwawa la Milala limekuwa ni mazalio ya viboko limeanza kuwa ni hatari hata kwa wananchi wa Mpanda. Tuna Shule ya Mpanda Girls pale, viboko wale usiku na shule haina uzio ni hatari lakini wamekuwa wakitoka pale bwawani wanakuja mpaka Mjini Mpanda kuharibu mashamba ya watu lakini limekuwa pia ni tatizo kwa maana ya usalama wa wananchi wetu. Naomba hilo nalo mliangalie kwa namna ya pekee. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, awali ya yote, nami nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla na timu yake, lakini niwapongeeze watendaji wote kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma nilibahatika kutembelea Ngorongoro kama ambavyo sifa zimekwenda kwa ndugu yetu Manongi na naomba niendelee kusema uimara wa mhifadhi huyu unaendelea kutusaidia kulihifadhi eneo lile, najua hayupo peke yake pamoja na timu nzima. Vivyo hivyo kwa mzee Kijazi wa TANAPA na wengine wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, eneo la utaliii kwa ujumla wake ni tofauti na maeneo mengine. Tofauti yake inakuja hapa; unatakiwa utengeneze mazingira rafiki, mazingira ya kuweza kumshawishi mtalii ili kesho aweze kurejea nyumbani kwako. Utengeneze mazingira, kwa sababu fedha ni ya kwake yaani, huyo mtalii fedha ni ya kwake, yeye ndiyo ana hiyari aitumieje, kwa hiyo usipotii kiu yake haji, mazingira yasipokuwa mazuri hutomwona mtalii, huduma zikiwa za hovyo hovyo hutomwona mtalii. Kwa hiyo ninachoomba sana, pamoja na kujisifu kwamba tuko vizuri eneo la utalii, lakini tusipotii kiu, mahitaji ya Watalii itabaki kuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yasipokuwa mazuri hutomuona mtalii, huduma zikiwa za hovyo hovyo hutomuona mtalii. Kwa hiyo ninachoomba sana, pamoja na kujisifu kwamba tuko vizuri eneo la utalii, lakini tusipotii kiu, mahitaji ya watalii itabaki kuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa Sekta hii unaweza ukampata mtalii mmoja makini akakusaidia hata katika maeneo mengine. Sasa unakusudia kuwa na aina gani ya watalii hilo nalo ni jambo jingine. Kwenye fani kuna mpaka watalii wanaitwa watalii vishuka; mtalii ambaye mnaenda kugombania wote muhindi wa kuchoma na vitu vingine vya namna hiyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sehemu ya utalii, sikatai, lakini kuna mtalii ambaye akifika hapa kwanza anajiuliza je, mna huduma ya hoteli za kueleweka? Mna huduma ya tiba? Kwamba hata ikitokea afya yake imekorofisha atapata tiba kabla ya kurudi nyumbani kwake? Je, huduma za Viwanja vya Ndege zinaeleweka? Kwa hiyo ninapoenda kuzungumzia utalii kwa ujumla wake tuyaangalie maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru nchi kwa ujenzi ule mzuri wa Uwanja wa Ndege Terminal III, ni mlango wa kuingilia kwenye suala la utalii. Hata hivyo, ni aina gani ya watu wapo hapo? Kwa sababu kuwa na hoteli nzuri, kuwa na uwanja mzuri ni sawa lakini je, watendaji kazi wanaeleweka? Hilo nalo ni jambo linguine. Kwa hiyo naomba pia Wizara isiache kufikisha weledi kuwa na trained personnel hata katika masuala ya hoteli na maeneo mengine hayo. Kwa sababu a trained personnel yeye ni balozi wetu pia, anaanza kutuwakilisha pale, kuiuza nchi na Kuzungumzia masuala ya nchi. Pia tusiache masuala ya amani na utulivu, ni vigezo muhimu sana kwenye kuhakikisha masuala ya utalii yanachukua nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi natoka Mkoa wa Katavi, nakuomba Mheshimiwa Waziri; nakubali viboko, mamba ni muhimu. Hata hivyo tunalo bwawa la milala, huko wamejaa viboko, wamekuwa ni tishio kwa uhai wa watu wetu, ni hatari hata kwa wanafunzi, wanakula mazao ya wananchi wetu, naomba Mheshimiwa Waziri kwa kuwa dhamana hii iko mikononi mwako katusaidie kuokoa tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na wote kuhusu suala la Tanzania Safari Chanel, ni jambo jema. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri muda wote biashara ni matangazo. Haya mambo yote mazuri ya Ngorongoro, sijui wapi; bila kujikita kwenye matangazo, bila Bodi ya Utalii kuwezeshwa; na hapa narudi kwenye raslimali fedha; nimesikitika kidogo kwa kupitia taarifa ukizungumzia habari ya miradi yote ya maendeleo fedha hakuna, wakati hawa watu wanazalisha kwa kiwango kikubwa; tusipowarejeshea fedha tutakuwa tumewakata miguu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma niliwahi kusema hapa, tusipowarejeshea fedha, tutawakata miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na la mwisho, Mheshimiwa Waziri, mimi nilikuwa naendelea kuomba, nchi hii labda tunachanganyikiwa kwa sababu tuna vitu vingi; tuna fukwe nzuri, tuna mbuga nzuri; sasa tukishaona kila kitu tunacho, lakini tusipokuwa na vipaumbele, at the end of the day tutakuwa hatuna hata kimoja tulichokifanya kwa ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa naomba sana, Mheshimiwa Waziri tuamue, kama ni fukwe basi tuzifanye kwa ufasaha, kama ni Ngorongoro yetu iendelee kulindwa. Na mafanikio bila kuyajengea wigo, bila kuyalinda hatima yake itabaki kuwa historia pia, na tukumbuke tuko kwenye dunia ya ushindani. Mtalii kama hana kitu kipya cha kuona, anaweza akaona leo kwako, lakini kama ni twiga ni huyo huyo ataenda kumuona nchi nyingine za jirani. Kwa hiyo wewe usipomtengenezea mazingira rafiki atakukimbia tu. Kwa hiyo wakati tunajipanga, kutamani kuona tunapataje fedha kwenye maeneo haya tuendelee kutengeneza mazingira ya kuimarisha maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilizungumzie suala la uwindaji wa kienyeji. Mheshimiwa Waziri nimefarijika uliposema kwamba wananchi hawa pia tutawarejeshea uwindaji wa kienyeji. Mwananchi ambaye kwa muda wote amekuwa akiwaona wanyama, akishiriki kuwahifadhi, lakini yeye awe mshangaaji tu anapunguza mori au ile ari ya kuwa mlinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo tunapozungumzia habari ya uwindaji wa kienyeji itatusaidia sana pia kwenye kuhakikisha kwamba watu hawa wanakuwa ni sehemu ya ulinzi wa maliasili zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na kwa kuheshimu muda, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru, na mimi nimpongeze Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya.

Mheshimiwa Spika, na mimi pia nakumbuka hiyo tarehe 22 na 23 Januari nilikuwepo pale Dar es Salaam wakati akiwepo Mheshimiwa Rais akikaa na wachimbaji wadogo. Kati ya mambo aliyoyaongea Mheshimiwa Rais ilikuwa ni pamoja na haya yafuatayo; Aliwaomba watendaji akiwepo Waziri kwamba yeye kama amefunga mlango wao waangalie hata namna ya kufungua dirisha. Alipolisema hilo alikuwa anamaanisha haiwezekani yeye Mheshimiwa Rais akafanya mambo yote, kuna baadhi ya mambo wamsaidie, watendaji hawa.

Mheshimiwa Spika, nikilisema hilo namaanisha mimi ninafsi kwanza nikiri mbele yako ni moja kati ya wachimbaji wadogo wa madini, nchimba madini ya dhahabu. Limekuwepo tatizo moja la kitu wanaita makinikia. Naomba nikiri, katika mgodi wangu pale Mpanga tunayo makinikia ya kutosha ambapo naamini Serikali hii ilikuwa na uwezo wa kupata kiwango kikubwa cha fedha. Makinikia yale yamekuwepo kutokana na sheria ya zamani kabla ya sheri ampya kupitishwa hapa Bungeni. Sasa anapokuja kuadhibiwa mtu kwa sheria ya zamani ambayo ilimpa nafasi ya kufanyia hiyo kazi nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri utusaidie katika hili na najua Mheshimiwa Waziri nimekuwa nikipita kwako kwa muda mwingi nikikueleza kuhusiana na suala hili.

Mheshimiwa Spika, katika hili niseme, katika mgodi kwa mfano huu wa Katavi-Kapufi, kuna makinikia ya kutosha ambayo hayo, mbali ya makinikia hayo, kuna ajira za Watanzania wenzangu, zaidi ya Watanzania 400, wameajiriwa pale, lakini suala ambalo linatukabili sasa hivi ni hiyo kuzuia kuyasafirisha makinikia haya ambayo yalikuwepo kutokana na sheria ya zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hilo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, atusaidie na hata pale ambapo anaonyeshwa kwamba mchango wa dhahabu ni asilimia 86.07, bado mchango wa dhahabu ungeweza kuwa mkubwa zaidi. Nikilisema hili, niendelee kusema, kwa wale wote ambao hata wana makinikia ya kopa ya sheria ya zamani, ndiyo maana Mheshimiwa Rais alisema hivi, kiwepo kipindi cha mpito, wakati ambapo watu wanajipanga kwa ajili ya kuja na smelter na refinery. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo suala la mara moja, ni uwekezaji mwingine mkubwa, kwa hiyo, kama kuna watu wamefanya uwekezaji mkubwa, wengine wakishirikiana na watu wa nchi za nje, leo unapomwambia ashughulikie suala la smelter na refinery, hakuna mtu anakataa hilo, lakini siyo suala la usiku mmoja, it takes time, vipi watu hao wasipewe kipindi hiki cha mpito? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo, nije katika suala lingine, ni kweli tunazungumzia wachimbaji wadogo, lakini naomba sana jitihada ambazo zinaendelea kufanywa na Wizara, kuendeleza tafiti nyingine na kuhakikisha tunaendelea kujenga uchimbaji wa kati na uchimbaji mkubwa pia. Kwa sababu mchimbaji mdogo, ukimfanyia mazingira mazuri, atakua, akishakua anaweza kwenda kuwa mchimbaji wa kati na baadaye akaja kuwa mchimbaji mkubwa, kwa hiyo, maeneo yote hayo na bila kuacha tafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, madini yanakuwa na thamani ukiyatoa ardhini, lakini wakati yakiwa bado yako ardhini, ni mwamba kama mwamba mwingine wowote ule. Kwa hiyo, Watanzania kwa ujumla wake, Baba wa Taifa alifanya kazi nzuri ya kusema kwamba, hatuchimbi mpaka Watanzania watakapokuwa tayari. Wasiwasi wangu, tusipojitahidi tukachimba, kwa Baraka hizi alizotupa Mwenyezi Mungu, tutajisifu tuna dhahabu tuna nini, lakini kama bado iko chini ya ardhi, haina thamani, thamani yake ni pale itakapotoka ardhini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme, kwa nini tusi-take advantage ya madini haya tuliyonayo kuhakikisha yanachimbwa kwa kadri tutakavyoweza, halafu tunakwenda kwenye uwekezaji mwingine tofauti. Nchi zenye mafuta na gesi, wanahakikisha kwa sababu ina under go law of diminishing return, madini yanakwisha. Kwa hiyo, kabla ya hayajakwisha, tuhakikishe yametusaidia katika maeneo mengine, huo ndiyo ushauri wangu kwa Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, awali ya yote na mimi naomba nianze kwa kuunga mkono hoja. Nimshukuru Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote ndani ya wizara, lakini naomba naomba pia niseme mbele yako, mimi ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nyakati tofauti ndani ya mwaka huu, nilikuwepo katika miji ya Kigali, Rwanda; nilikuwepo Accra, Ghana na hivi majuzi nilikuwa Vancouver huko Canada. Dunia kwa ujumla wake inaongelea suala zima la akina mama na watoto wa kike, kwa maana ya idadi yao. Tunaambiwa kuna takribani bilioni 1.7 akina mama na wasichana ambao huwezi ukawaacha kwenye uchumi wa dunia. Tukicheza nje ya watu hawa kwa wingi wao, akina mama ambao pamoja na kuzungumzia suala la equality, lakini ndiyo watu ambao tunaambiwa tukija kwenye masuala yanayogusa uchumi, ni watu makini, ni watu ambao uchumi wao, katika eneo la kada ya familia, ukikuta kuna baba, kuna mama, mama anaimarisha uchumi wa familia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,kwa hiyo, mipango yetu na bajeti, bila kuwagusa hawa tunakuwa hatujawatendea haki. Kwa hiyo, nilikuwa naomba, duniani huko, wanawaangalia kwenye sura hiyo na huwezi ukakimbia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaambiwa na mtaalam mmoja wa IFAD, anakwambia kuijenga dunia bila njaa, huwezi ukaacha akina mama. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, na bado tunaambiwa wanakwenda kwa maana wanazalisha kati ya asilimia 20 mpaka 30, sasa nilitaka nianze kwa sura hiyo. Baada ya kulisema hilo, naomba pia Mheshimiwa Mpango, tunaambiwa hivi, tugusie standard gauge, tugusie mambo yote, bila kugusa afya ya msingi, kuna tatizo kubwa. Kwa hiyo, uwekezaji ambao hauendi kugusa afya, haya mengine yote hayana nafasi. Nalisema hilo kwa sababu walimu, wanafunzi, iwe ni askari, iwe watu wengine wote, nguvu kazi yenye afya ndiyo inaweza ikafanya mambo mengine yote. Kwa hiyo, naomba pia bajeti yetu ijikite pia katika universal health coverage, bila kusahau primary health care. Ni maeneo hayo ambayo tunaambiwa watu wetu wanakufa kwa sababu ya kukosa afya na pia tunakwenda kwenye umaskini mkubwa kwa sababu ya gharama kubwa za afya. Kwa hiyo, nilikuwa naomba hayo tuyaangalie kwa namna ya pekee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo naomba nigusie suala la reli, natoka Katavi, Mpanda, nilikuwa naomba na wazungumzaji wengine wameongea hapa, shirika hili bado linafanya mambo yake kizamani. Kwa mfano kule nyumbani, unaambiwa kwamba wateja ni wengi, mabehewa hayatoshi, hawaoni kwamba hilo ni soko, ni fursa ya kuchangamkia, kwamba kama wateja ni wengi, mabehewa machache, dawa ni kuongeza mabehewa, lakini utashangaa wamelalamika leo, wamelalamika kesho, watalalamika kesho kutwa, hatua hazichukuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama shirika linaona nivizuri kutofanya kwa, maana yake hata mashirika mengine, kwa mfano, mashirika ya ndege, hapa tumeona ikionekana wateja ni wengi Dodoma, wanaweza wakaongeza hata trip ya pili, zikaja hata ndege mbili kwa wakati mmoja. Sasa kwa nini hawa hawaangalii katika sura ya kibiashara? Nilikuwa naomba hilo waliangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, eneo la kilimo, ni kweli na nakubali, tuseme yote tutakayoweza, bila kilimo, liko tatizo, lakini kilimo pekee cha kutufuta machozi ni kilimo cha umwagiliaji. Uzuri wa kilimo cha umwagiliaji, kwanza, wewe unakuwa na nafasi ya kuki-control,maji kidogo, maji zaidi na mwanga unakuwepo, lakini hiki kilimo cha kutegemea mvua za Mwenyezi Mungu, mara mafuriko na vitu vingine vya namna hiyo. Kwa hiyo, tukijikita kwenye kilimo cha umwagiliaji, tukichanganya na hicho kingine cha kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu, tuna uwezo wa kuifanya nchi yetu ikawa ghala la chakula na kukasaidia watu wengine katika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, suala la diplomasia ya uchumi, ndiyo maana tuna mabalozi nje ya nchi, tuna watu wengine wa namna hiyo. Inasikitisha kusikia ukiliona chungwa zuri, kama ni parachichi zuri, ni kwamba lilizalishwa Tanzania, limekwenda huko, halafu likapewa label ya nchi nyingine, mabalozi wetu wako wapi! Suala zima la diplomasia ya uchumi iko wapi katika kuinusuru nchi katika mambo hayo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na inasikitisha pia, ni kweli, hata mimi mara ya mwisho nilivyokuwa huko Canada nilisikia mtu mmoja akizungumza kabisa, kwa maana ya Mlima Kilimanjaro uko nchini kwao. Hasa mimi niendelee kusema, haya yote, kama mwenzako anafanya hivyo kwa ku-take advantage ya wewe, si na sisi tuna nafasi ya kulifanya hilo pia! Kwa hiyo, eneo hilo nilikuwanaomba sana, naomba sana tuliangalie katika sura hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la umeme ni kweli, nashukuru kasi inayoendelea, lakini kwa maeneo mengine kwa mfano hata kule kwangu Katavi, kasi si ile, najua hili Mheshimiwa Waziri husika atasikia pia kwa kupitia wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, naomba niingie ene la madini, mara ya mwisho nilizungumza hapa, mimi ni mdau wa shughuli za uchimbaji madini, napata ugali wangu wa siku kwa kupitia uchimbaji wa madini. Nilikuwa naomba niishauri nchi yangu mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, pamoja na kuambiwa mchango wa uuzaji dhahabu nje ya nchi umeongezeka kwa asilimia 0.7, tuache maeneo mengine ya utalii, fukwe na mambo mengine ya namna hiyo. Mimi naomba nijikite kwenye madini tu, tuna uwezo wa kuitoa nchi hii hapo ilipo ikaenda mbali zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipokutana na Mheshimiwa Rais, kwanza chukulia niseme, kwa maana ya idadi ya wachimbaji, nichukulie hata kwa idadi kidogo ya 6,000, nitaje tu au milioni sita tufanye. Hebu chukulia kila huyo mmoja, akazalisha kilo moja tu ya dhahabu, ni grams ngapi, kilo ngapi za dhahabu zitapatikana katika nchi hii, lakini mambo ambayo tunatakiwa tuyafanye, mimi niseme nashukuru kwa hatua ambazo Serikali imeanza nazo, lakini tunatakiwa twende mbali zaidi! Tusifunge milango, tutoe nafasi, kwa mfano, kuna nchi hazina madini, lakini wazalishaji wazuri wa madini na wanauza nje ya nchi. Tujiulize wanafanyaje watu hawa! Kwa nini tusiige? Sisi kama nchi, kwanza madini tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme kwa mfano, leo pamoja na sheria hizi nyingine ambazo tunaziweka, bado wenzetu wa utafiti hawajafanya utafiti wa kutosha na ndiyo maana unaweza ukakuta ukilala, ukiamkia unasikia kuna gold rush somewhere, mtu alikuwa amekwenda tu kwa ajili ya kuchimba viazi, anaondoka na kipande cha dhahabu, mtu alikuwa ameenda kwa ajili ya kuchimba kisima, anaondoka na kipade cha dhahabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tutengeneze sheria rafiki ambapo, kwa mfano, mimi nimekwenda peke yangu porini, nikakutana na kipande cha dhahabu cha size ya kiatu, wewe haupo, polisi hayupo, mwingine hayupo, unategemea mimi nifanyeje!

MBUNGE FULANI: Naondoka nacho.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: ...ndiyo maana katika mazingira hayo, tukitengeneza mazingira rafiki, mtu huyu awe tayari ku...

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, kengele ya pili ilishagonga.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba moja kwa moja nijielekeze eneo la madini, niliwahi kuzungumza kwenye Bunge hili hapa eneo la madini pekee yake kwa maana ya nchi yetu ya Tanzania lina uwezo wa kuzibeba sekta nyingine. Nikilisema hili, niendelee kusema mbele ya Bunge lako mimi ni mchimbaji mdogo wa madini, kwa hiyo naomba nielezee kile kitu ninachokifahamu.

Mheshimiwa Spika, acha madini mengine, acha Tanzanite, acha madini ya vito zungumzia dhahabu peke yake. Kupitia dhahabu kwa kupitia wachimbaji wadogo nishukuru kwamba Serikali imeboresha maeneo hayo tozo mbalimbali zimepunguzwa, sheria zimerekebishwa, tunaweza kwenda mbali Zaidi. Nashukuru mara mwisho nimemsikia Rais wetu mpendwa akiongelea suala moja, leo unaweza ukawepo kwenye hifadhi, sikatai uhifadhi, lakini kwenye hifadhi kuna dhahabu, kuna almasi, kwa kupitia almasi hiyo, kwa kupitia dhahabu hiyo, tuna uwezo wa kufanya mambo mengine. Tembo hali dhahabu, kwa hiyo unaweza kwa kuitoa dhahabu tukajenga mahospitali, kwa kutoa dhahabu tukawaendeleza akinamama.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili pia naomba ulifahamu vizuri ninachokiomba sasa hivi, tafiti mbalimbali ambazo sekta imekuwa ikizifanya, tafiti hizo ziendee kwenda huko mbali. Kuna watu hapa wanatuangalia wachimbaji kama labda watu wa kupiga ramli hivi na mambo mengine ya namna hiyo, hapana. Tukiwa na tafiti kwa kupitia GST hakuna uchawi, ni suala tu la kujua kiwango cha mashapo, kujua dhahabu iko wapi, unachimbaje, kwa hiyo niombe na katika hili nafahamu kuna maeneo ambapo Wizara kwa kupitia Wizara ya Fedha, wameendelea kutoa ujenzi wa vituo mahiri. Niombe sana ili tuendelee kupata zao hasa kwa maana ya zao la dhahabu, bila tafiti, unaweza kushangaa leo umekaa hapa Dodoma dhahabu mtu anachimba choo kapata dhahabu, mtu amekwenda shamba analima kapata dhahabu maana yake kama ni kwa kupitia tafiti hatufanya kwa kubahatisha kwa kiwango hicho.

Mheshimiwa Spika, niseme, katika eneo hili leo sehemu ambayo inaisadia nchi katika eneo la ajira ni pamoja na uchimbaji. Nikilisema hili namaanisha, unaweza ukakuta sehemu ya mgodi mmoja idadi ya watu kama wale wangekuwa barabarani ni tatizo kwa nchi. Kwa hiyo ninapozungumzia habari ya kwenda kuimarisha huko namaahisha.

Mheshimiwa Spika, kubwa tuende kwenye jambo lingine. Leo kwa mfano, maeneo mengine kwa mfano kama Mkoa wa Katavi unaweza ukachimba ukapata dhahabu, ile dhahabu ni asilimia themanini tu, ukienda kuuza wanakuambia madini yako ni asilimia themanini, Serikali iende mbali Zaidi, tukisema themanini ina maana hii ishirini ni kitu gani, unakuta ni madini mengine yanaweza yakawa madini ya fedha, yanaweza yakawa madini ya shaba. Kwa hiyo Serikali itusaidie, watu wanajenga viwanda vikubwa, leo teknolojia iko wazi, maana yake huyu mtu mmoja anapoteza hayo madini mengine, lakini kama Serikali itakuja na utaratibu kwamba bwana nyie wachimbaji kadhaa mji-organize najua mipango hiyo ipo, lakini twende mbali zaidi kwa maana huyu mtu ukimsaidia hapahapa nchini katika kuchimba madini yake, hiyo dhahabu yake, baada ya kuiuza nje kama madini ghafi, tukilifanya hapa nchini mbali ya kuuza dhahabu tu anaweza akauza na madini mengine, yawe madini ya shaba au yawe madini ya fedha. Naomba sana Serikali yangu sikivu iweze kuliangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikizungumzia eneo hilo hilo la uchimbaji kwa maana ya teknolojia, leo niliseme hapa, zamani tulikuwa tukiwaona akinamama kama ni watu ambao hawawezi wakajikita katika eneo hilo la uchimbaji, wakifikiri kwamba ni kazi ilikuwa inahitaji nguvu zaidi na watu wenye misuli Zaidi. Serikali ina nafasi ya kufanya jambo moja, niwaombe turudi kwenye kuwapa ruzuku wachimbaji, nikisema hilo namaanisha kwa kupitia ruzuku, fedha iliyojificha huko itatoka na itaendeleza maeneo yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Nakushukuru sana na Mungu akubariki. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nianze kwa neno la shukrani kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake. Ni kweli Mheshimiwa Waziri ni mtu rahimu. Mimi niseme hadharani kwa zaidi ya mara mbili nilipokuwa na udhuru na yeye alipotembelea jimbo langu, alifikia hatua ya kupiga simu akaniunganisha na wananchi wangu. Huyu ni mtu muungwana, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba shukrani nyingine ziende kwako wewe. Bunge lililopita uliunda Kamati Teule ya Bunge ya kukushauri kuhusu suala la gesi na mimi nilikuwa mmoja kati ya Wajumbe uliowachagua. Rai yangu ni nini? Naomba Serikali iendelee kufanya rejea kwenye taarifa ile kubwa na kuona ni mambo gani tuliyoishauri Serikali. Nashauri sana katika hilo. Katika masuala yote ya gesi ujumbe mzima uko pale, kwa hiyo Serikali iendelee kufanya rejea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho Waziri alikuwa Uganda wakati Rais wetu na Rais wa Uganda walipokuwa wakitia saini moja ya mikataba. Nilijifunza mambo kama matatu na mambo hayo yalinifanya nipate wivu lakini wivu ambao ni chanya. Rais Museveni alisema mafuta ni jambo la kupita tu, linaweza likawa jambo la muda, lakini utajiri huo uwasaidie kwenda kufanya sekta nyingine kama kilimo, utalii na mambo mengine ya namna hiyo. Pia aliwasimamisha vijana akasema ugunduzi ule umefanywa na Waganda wenyewe, vijana ambao waliwapeleka shule wakasoma. Akasema pia eneo ambalo limechimbwa ni asilimia 40 bado asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi suala hili limenitia wivu wa maendeleo. Watanzania tunajifunza nini kutoka hapa? Je, tuna mpango gani wa makusudi wa kuhakikisha vijana wetu ama kupitia shule au na mambo mengine kwa sababu wao watakuwa na uzalendo kufanya kazi hizi? Mtu mwingine anaweza akaenda kufanya utafiti hapa na akakuta labda kuna mafuta na kwa sababu ya masuala ya kiuchumi asikupe taarifa sahihi lakini kwa wale ambao ni wazalendo, kama walivyofanya wale vijana wa Uganda hawatafanya hivyo. Naomba tuendelee kujifunza kutoka kwa wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua kuna maeneo kama Eyasi, Wembele ambapo jitihada zinaendelea lakini twende mbali zaidi. Sisi kule Tanganyika, kwa maana ya Mkoa wangu wa Katavi, utafiti umekuwa ukiendelea katika bonde lile. Ni vizuri basi tukaongeza kasi ya kuendelea kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo nirudi tena kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na sifa nilizokupa za kutembelea maeneo yangu, changamoto ambayo naipata mimi katika eneo langu, nasomeka niko Manispaa lakini umbali wa kijiji cha mwisho watu wa TANESCO wanasema wao ndiyo watashiriki na siyo suala la REA wakati huo wale watu wanasomeka wako kijijini. Kwa mfano, ukienda Kata ya Mwamkulu, japo inasomeka mitaa lakini ni vijijini; maeneo kama Mkwajuni, Kabwaga, Mkokwa, Nguvumali na Seso. Ninayo pia Kata ya Kasokola maeneo ya Kasolwa, Ivungwe na Isungamila.

Mheshimiwa Spika, mwisho ninalo eneo la Kakese, kuna eneo linaitwa Kamakuka. Mheshimiwa Waziri, ni shahidi, mara ya mwisho alikuja pale na akatusaidia kuhakikisha umeme unafika hata kwa maeneo yale yanayowagusa wachimbaji. Katika hilo mimi nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia tuliambiwa ongezeko la mapato lilikuwa ni pamoja na suala la LUKU. LUKU ilivyokuwa ikitumika vizuri ilifanya TANESCO wafanye vizuri. Tuliambiwa mara ya mwisho kulikuwa na shilingi bilioni 72 katika mwaka 2016 kwa mwezi, lakini mwaka 2021 ilikuja shilingi bilioni 160 kwa mwezi na hii yote ilikuwa asilimia 102. Sasa kama LUKU ilisababisha TANESCO wakapata matokeo mazuri na kipato kikapanda, hii juzi tumeona LUKU ikichezewa; wanataka kuleta ujumbe gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu waliofanikiwa duniani ni wenye jeuri ya kuthubutu. Nakuomba Mheshimiwa Waziri tusiache kuthubutu kuibua maeneo mengine mapya ya utalii kwa sababu waliofanikiwa duniani ni wenye jeuri ya kuthubutu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kwenye eneo la sheria tunasema kama huna vielelezo, haujafanya utafiti, usiongee. Mwaka 1996/1997 nilikuwa Mombasa, Kenya, sehemu moja inaitwa Mtwapa katika hoteli moja ya Serena. Nilikutana na mtalii mmoja akaniambia maneno yafuatayo: amekuwa akiitembelea Kenya na Mombasa for the last 15 years, hana kitu kipya cha kuona, anafikiria aende ama South Africa au kwingineko. Ujumbe anaouleta ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, aina hii ya watalii tunatakiwa ndani ya nchi yetu tusiwapoteze kwa kuibua maeneo mengine mapya. Kama this time around alikuwa Kaskazini, next time aende Magharibi, the other time around aende Mashariki, hivyo. Kwa hiyo, huyo tuna uwezo wa kumhifadhi ndani ya nchi yetu, lakini kwa kuboresha maeneo mengine. Nilikuwa naliomba hilo sana na hiyo ndiyo tabia. Naomba niwapitisheni, mtalii ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana, tutajikita kutengeneza hoteli nzuri, mbuga nzuri, lakini tusipomtambua mtalii na tabia yake, hizo hoteli Wazungu wanasema zitakuwa ni white elephant. Kwanza mkumbuke mtalii ndio bosi wetu. Kama bosi wetu, ana tabia zifuatazo; tusipotii kiu yake hana nafasi ya kuja kwetu. Kwa hiyo, nilichokuwa nawaomba Waheshimiwa, lazima tujikite kwenye kujua mahitaji ya mtalii. Ni mtalii gani tunayemlenga?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu ukiorodhesha, nikiacha watalii wa ndani ambao ni Watanzania wenyewe, lakini hata hao watalii kuna kundi la watalii huko kwenye kada, wengine wanasema watalii vishuka. Kuna mtalii ambaye tunaweza tukabanananaye mtaani, tunakula wote muhogo wa kuchoma, anatembea pekua na vitu vingine kama hivyo, hatukatai, naye tunamhitaji. Ila kuna mtalii mmoja anakuja kwenye nchi yako, mtalii huyu akiridhika na kazi zetu na huduma zetu; leo tunauliza habari ya kwenda kutangaza CNN na kwingineko, yeye mmoja ana uwezo wa kubeba dhamana hiyo akiridhika na huduma yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tunaambiwa kwenye Hotel Industry, kwenye utalii kwa ujumla wake ni Hospitality Industry. Kwa hiyo, tusipokuwa watu wa kutii kiu ya watalii, itabaki kuwa ni gumzo.

Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana. Sasa ili tukawapate watalii wa daraja hilo, je, tumejikita katika mahitaji yake ya kimsingi? Leo kwa mfano, tuna hoteli kweli za viwango vile? Tuna hoteli ambazo zinaweza leo ukisema mtalii mmoja makini wa kutoka Marekani amekuja hapa tunaweza tukam- accommodate? Hayo ni mambo tuendelee kuyaangalia. Mtu anayehitaji labda huduma, bima, anahitaji flying doctors, hayo yote kweli tunayo? Ni vitu vya kimsingi sana kuviangalia. Maana mwingine anasema, nakwenda Tanzania, nime-fall sick, nimeugua sasa hivi, huduma nazipata wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nashukuru Marais wote ambao wameendelea kuboresha huduma zetu hapa nchini hata kama ni kwa maana ya first aid ataipata nchini kabla hata hajaruka kwenda kwenye nchi yake, ni jambo la msingi sana. Naomba tena tuendelee kuelewa leo tuna trained personnel kweli kweli jamani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda baadhi ya nchi za watu, ile tu umefika kwenye nchi yao, even tax driver wamekaa kistratejia. Tax driver tu ukiwanaye kwenye gari anaiuza nchi yake. Umwache huyo, ukikuta kama ni air hostess wanauza nchi zao. Ukimkuta kama labda ni waiter au waitress, umekaa hotelin,i dakika mbili za kukaa pale yuko well trained, anajua kwamba nifanye nini katika kuiuza nchi yangu. Huko tuendelee kwenda kwenye namna hiyo ya kufanya shughuli zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba pia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Ooh! Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa nafasi. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo yafuatayo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa kuiruzuku nchi yetu kuwa hapo ilipo kwa maana ya jiografia. Nalisema hilo makusudi, kwani leo hii tukizungumzia habari ya ardhi, iwe ni ardhi nzuri; watu wanazungumzia habari ya kilimo, habari ya maziwa na vitu vingine vyote, mimi narudi kumpelekea shukrani Mwenyezi Mungu kwa kuturuzuku hayo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, point yangu moja ya msingi, kuna bahati moja mbaya unapokuwa na kila kitu, unaweza ukafika sehemu ukashindwa kujua uanze na kipi. Ndiyo maana nataka kuleta point ya kwamba pamoja na haya yote mengi mazuri, ni lazima tuwe na vipaumbele. Hatuwezi tukafanya kila kitu, lazima tuwe na vipaumbele. Nami niseme, kwa mfano, tukizungumzia habari hii niliyosema ya ardhi nzuri; ardhi nzuri ni jambo moja na matumizi bora ya ardhi ni jambo lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama tutafika sehemu tukijua tu tuna ardhi, ardhi, ardhi, tukaachana na matumizi bora ya ardhi, hautaacha kuona nchi hii ikiendelea kuwa kwenye migogoro ya ardhi, hautaacha kuona nchi hii ikiwa kwenye uzalisha duni. Kwa hiyo, naendelea kushauri na kusisitiza matumizi bora ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo, najua kwa ruzuku hiyo hiyo, tunazungumzia habari ya uwekezaji katika maziwa. Ni jambo jema, lina afya. Nami ukizungumzia kule kwangu Katavi, ndiyo maana tuna uwekezaji mkubwa wa Bandari ya Karema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, point ni nini? Leo hii tukifanya vizuri katika eneo hilo, changamoto tunazokutana nazo za kuhakikisha labda mizigo yetu inapita kupitia nchi nyingine, tutakwepa hilo. Tukiwekeza vizuri katika hizo bandari, nakuhakikishia tutakuwa na uchumi mkubwa. Kwa wale waliobahatika kufika DRC, uchumi wa maeneo yale ni mkubwa. Sasa tunafanyaje ili kuweza ku-take uchumi huo? Ni pamoja na uwekezaji huu katika Ziwa Tanganyika na maziwa mengineyo. Naomba nitoke hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilifurahishwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu kuhusu Sera za Mapato na Matumizi; lakini eneo hili kwa ujumla wake, kama kila kitu kikifanyika vile ilivyotakiwa, basi kelele zingekuwa ni chache. Nalisema hilo kwa sababu gani? Pale tunaambiwa kwa maana ya Sera za Mapato na Matumizi, tumeelekezwa kwamba usimamizi madhubuti wa fedha za Umma, lakini yawepo maeneo yenye tija bila kusahau ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiyasema hayo, tafsiri yake ni nini? Leo hii tunazungumzia habari ya uwezekaji na kwa maana nzima ya uwekezaji kuvutia wawekezaji. Pale tumeambiwa, kwa kuvutia uwekezaji, tunaweza tukazalisha ajira takribani 62,301. Nasema kuvutia wawekezaji, ni jambo moja, lakini tunasemaji kuhusu Watanzania hawa?

Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja, tukifurahi kuona wawekezaji wanakuja, nami hapa naomba ni-declare interest, mimi ni mchimbaji mdogo wa madini. Katika eneo hilo la uwekezaji nimeshiriki kwa kina na mafao nayapata katika eneo hilo. Kwa hiyo, hata mimi naweza nikatoa darasa kwa wenzangu.

Mheshimiwa Spika, kama nchi, wakati tunazungumzia habari ya uwekezaji, tunafanyaje kwa maana ya kumsaidia Mtanzania? Je, kama nchi, tumetengeneza mazingira ya kumwandaa Mtanzania na mikataba ya Kimataifa? Maana kuna wakati mtu anaingia kichwa kichwa katika masuala hayo. Tutafika mahali Watanzania wenzangu watabaki kuwa watazamaji. Kwa sababu wanakuja watu ambao kwanza wana-financial muscles. Wana msuli wa kifedha, wanamkuta Mtanzania ambaye kwa sababu hajaandaliwa kwa maana ya elimu ya mikataba na vitu vingine, unaweza ukamkuta yeye na ardhi yake ambayo Mwenyezi Mungu amemruzuku, akaona kama haina thamani, akafikiri thamani ni kwa huyu tu anayekuja. Kumbe yeye huyu mtu ni tajiri, lakini hajatengenezewa mazingira ya kujua kwamba ana utajiri wa kiasi hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa eneo la uchimbaji. Bahati nzuri niseme mikakati mizuri inayoendelea katika nchi yetu, mtu mmoja anaweza akafika sehemu akaingia mkataba, kwakuwa mtu mmoja ana mashine, ana fedha, na kadhalika, yeye kama hajatengenezewa mazingira ya kujua, kuelimishwa zaidi na kupewa elimu ya mikataba, ana ardhi yake ambayo labda kama ingekuwa imethaminishwa, kwamba bwana wewe hapa tulipo mashapo ya eneo lako ni kiasi hiki na hiki na hiki. Kwa hiyo, unapokwenda kwenye meza, nenda ukiwa kifua mbele, ukijua na wewe ni kama alivyo yeye. Haya yote, naiomba nchi yangu na Serikali iendelee kufanya jambo hilo jema la kuhakikisha tunawasaidia wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo kwenye eneo la elimu ya uwekezaji, kuna suala lingine la mwingiliano wa majukumu, taasisi za udhibiti na masuala mazima ya tozo. Kama hatutafika sehemu tukajaribu kuendelea kuona namna ambavyo kila taasisi inavyoingiliana na taasisi nyingine, masuala hayo ya tozo na vitu vingine vya namna hiyo, tunaweza tukakuta wakati mwingine tunarejesha nyuma ari ya watu kujituma katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la UVIKO na athari za UVIKO. Nafarijika kuona miradi mbalimbali ambayo imetengenezwa, lakini kama nchi, tumebaki na darasa lipi? Point yangu ya msingi ni hiyo. UVIKO kwa ujumla wake, angalia jinsi dunia ilivyosambaratika, angalia kila mtu alivyotamani kubaki kwake. Sasa katika mazingira haya ya kubaki kwetu, iwe ni somo. Kwa maana gani?

Mheshimiwa Spika, katika mazingira ambayo mtu wetu alikuwa anatakiwa labda akatibiwe India, Marekani au Uingereza, kwa somo lile la UVIKO unafika mahali unaona kumbe kama nchi, tuna kila sababu ya kuendeleza miundombinu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana naishukuru sana Serikali. Leo hii ukiichukulia Jakaya Kikwete pale, hata ukija tu Benjamin, shughuli zinazofanyika pale, uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali, hata kama ilikuwa UVIKO imetufikisha mahali ambapo tumefungiwa milango, kumbe unaweza ukafungiwa milango, lakini ukawa katika position ya baadhi ya mambo kujihudumia internally. Nilikuwa nasema, tukifurahia mambo mengine kwamba tumejenga madarasa, well and good; vituo vya afya, well and good, lakini somo pana tunalolipata ni lipi? Maana yake, tuendelee kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, nashukuru pia kwa kuwa mchangiaji wa mwanzo jioni hii.

Mheshimiwa Spika, mimi ni mjumbe kutoka Kamati ya USEMI, sehemu kubwa ya taarifa uliyoiona maana yake hata mimi mawazo yangu yako hapo. Nitakwenda kwenye maeneo machache kwa msisitizo.

Mheshimiwa Spika, eneo la TARURA kama tulivyoongea kwenye Kamati. Wenzetu wa TARURA kwa kweli wanafanya kazi kubwa na niseme kipindi hiki ambapo tuko kwenye majira ya mvua ukienda katika maeneo mbalimbali nchini barabara zimekatika. Kwa hiyo suala zima la Mfuko wa TARURA katika eneo la dharura, tukizungumzia kuongeza fedha ni kwa maana hiyo. Eneo la TARURA upande wa dharura.

Mheshimiwa Spika, kila sehemu, ukienda Katavi, huko kote mvua zinakonyesha hata maeneo mengine ambapo hakuna mvua. Kwa hiyo eneo la kuongeza fedha nilikuwa naomba sana.

Mheshimiwa Spika, eneo la TARURA pia nilikuwa naomba kuna baadhi ya maeneo kuna miradi mingine kwa kupitia TASAF unaweza ukakuta wananchi kwa maana ya kujipatia kipato wameelekezwa kwenye utengenezaji wa barabara. Wengine wamefikia hatua ya kuchimba mitaro. Point yangu ni nini? Ikiwa kazi nzuri imefanywa na wananchi kwa kupitia vyanzo vingine kama TASAF, au Mfuko wa Jimbo, kazi hii nzuri isipounganishwa na kazi za TARURA hautoiona thamani yake. Fedha nyingi inaweza ikapotea katika eneo hilo, lakini inapendeza barabara nzuri ikifunguliwa, mitaro ikichimbwa, basi na wenzetu wa TARURA wazipokee kazi hizo ili kuwe na uendelevu wa shughuli.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoke hapo. Eneo la pili ni kuhusu TAKUKURU rafiki. Nishukuru tumepitia kwa kupitia Kamati na tukaona mpango huu ni mwema, ni mpango mzuri, suala zima la TAKUKURU rafiki. Kwa maana siku zote tunaambiwa kama hujafanya utafiti hauna vielelezo usiongee. Wenzetu wa TAKUKURU rafiki wanatuambia 81.5% inazungumza kwamba rushwa ni tatizo nchini, lakini 92% wako tayari kwa mapambano dhidi ya rushwa na kuwapa ushirikiano Maafisa wa TAKUKURU. Point yangu ni nini? Mwelekeo wa dunia kwa sasa hivi au ulimwengu ni kuzuia rushwa kabla haijatokea na kwa kupitia TAKUKURU rafiki pia nao wamejikita huko kwa maana ya kuzuia zaidi.

Mheshimiwa Spika, wenzetu hawa kwa kupitia TAKUKURU rafiki na nimeeleza hivyo kwamba 92% wako tayari kutoa ushirikiano, lakini wenzetu wa TAKUKURU peke yao hawawezi, ni wachache, peke yao hawawezi, lazima wapewe ushirikiano. Niseme hivi, tutaishia kuwalaumu watu hawa, yaani mtu kama ni katika halmashauri, jiji au manispaa, usitimize wajibu wako, umemsainisha mtu ameingia kwenye kazi, mkataba haueleweki, baada ya hapo mtu huyo kapotea, amepotea kwa uzembe wa wewe kutomshirikisha kwenye mikataba, ikifika hapo unasema TAKUKURU njooni wakati wajibu wa kwanza ulikuwa ni wa kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachotaka kusema nje ya hapo tutabebesha watu lawama, lakini naomba turudi, ndiyo maana suala zima la TAKUKURU Rafiki inatuelekeza kwenye uwajibikaji wa pamoja. Mbali na uwajibikaji wa pamoja, juzi nilikutana na familia moja nikaambiwa na mzazi wake, ananiambia mwanangu hata ukimpa fedha kiasi gani, ni mtoto mdogo, ukimpa fedha sana sana ataileta kwa mama yake. Hakuna mahali atatumia atafanyaje. Nataka kujifunza nini? Yaani mtoto mdogo akiwa na umri mdogo anaanza kujengewa maadili, hili ndilo, hili hapana, hili ndilo, hili hapana. Kwa hiyo kwake yaani fedha, yule mtoto mdogo amefika mahali ambapo hata kama atakwenda kwa makuzi hayo, anajua hiki kinanihusu, hiki hakinihusu. Nikisema hivyo nataka kumaanisha nini pia?

Mheshimiwa Spika, bado ukiacha uwepo wa vyombo hivi, na vyombo hivi kwa utamaduni vina asili ya mabavu kidogo, lakini tutoke nje ya mabavu. Kila mmoja hapa ana dini yake, wapo Wakatoliki, wapo Waislam na wengine hawana dini, lakini bado siku zote, kwa mfano mimi ni Mkatoliki, ukienda kwenye amri pale kuna sehemu unaambiwa usiibe, usiseme uongo na vitu vingine vya namna hiyo. Kwa hiyo kwenye maadili yetu ya dini yatuelekeze kwenye kusema hili hapana.

Mheshimiwa Spika, nimesikia kengele ya kwanza hiyo. Kwa hiyo ninachotaka kusema, ushirikishwaji wa pamoja wenzetu peke yao pamoja na nia yao njema bila watu kuwasaidia, hawatoweza.

Mheshimiwa Spika, Sekretarieti ya ajira. Niwashukuru sana watu wa sekretarieti ya ajira na hasa kwa sababu kulikuwa na maombi, vijana wanasafiri umbali mrefu kwenda kufanya usaili, leo sekretarieti ya ajira kwa kupitia Mheshimiwa Jenista pale wamesikiliza kilio cha Wabunge. Sasa hivi usaili umepelekwa kwenye kanda na mimi niseme hili ni jambo jema. Wakati ule ilikuwa watu wanasafiri, atoke Katavi, atoke Mwanza, atoke wapi labda kuja Dodoma au Dar es Salaam. Wazazi vipato vidogo, lakini nitoke hapo.

Mheshimiwa Spika, tumekwenda kwenye kitu kingine ambacho nacho naomba kiendelee kufanyiwa kazi. Habari ya kupata ajira kwa kigezo cha kwamba umepitia JKT niombe, Kamati imeelekeza kwa sababu nafasi za JKT hazitoki kwa kila huyo. Ukituacha sisi, mimi ni namba Z2639 OP Kambarage ya kutoka tarehe 15 Juni, 1990 mpaka 14 Juni, 1991. Sasa sisi wa miaka hiyo ilikuwa ukisema mtu awe na sifa ya kupita JKT ni kwa sababu ilikuwa tunapita kwa mujibu wa sheria. Sasa hivi nafasi ni chache, ukija na kigezo kwamba mtoto lazima apite JKT wakati hakupewa nafasi ya kwenda JKT, tunawanyima nafasi. Kwa hiyo naomba kigezo cha kwamba lazima mtu apite JKT vinginevyo tutimize wajibu wetu kwa kuhakikisha wote tunawapeleka JKT halafu tuwahukumu baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuheshimu muda, naomba kuishia hapo. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mimi pia, kama ilivyo ada, naomba nimshukuru Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wengineo. Kwa ujumla wake Mheshimiwa Waziri wewe ni mtu rahimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo mimi nitajielekeza zaidi katika suala la uendelezaji wa rasilimali za maji na utafutaji wa vyanzo vipya. Eneo kubwa nita- concentrate hapo lakini niishukuru Wizara kwa ujumla wake. Najua sisi kwa maana ya Mpanda mahitaji ni lita 11,370,000 lakini tunapata lita 6,050,000. Tuna upungufu wa lita 5,320,000. Hiyo ndiyo sura ya suala la maji pale kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema nitakuwa si muungwana nisiposhukuru. Nafahamu kwamba kwa muda wote huu tuna Miradi ya Ikorongo Namba Moja na Ikorongo Namba Mbili. Vilevile kuna Mradi wa Manga ambao takribani shilingi bilioni 7.5 tumeletewa kutoka Serikalini. Lakini pia niishukuru kwa maana ya miradi mitatu. Tuna Mradi mmoja wa Mwamkulu ambayo hiyo Mwamkulu inakwenda Mkwajuni, Mlima Kipara na St. Maria. Tulipata fedha za UVIKO ambayo ilikuwa ni takribani shilingi milioni 476. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tuna mradi wa Kakese ambao ni Mfuko wa Maji wa Taifa, tulibahatika kupata shilingi milioni 951. Tunao mradi wa Milala kwenda Kampuni, tulibahatika kupata shilingi milioni 458. Hizo zote kwa ujumla wake nimshukuru Mheshimiwa Waziri. Isipokuwa, maombi yetu mapya kwako Mheshimiwa Waziri, tunaomba shilingi milioni 572 ili kuweza kumalizia mradi wa Kakese wenye thamani ya shilingi milioni 412 na Shilingi milioni 160 Mradi wa Milala kwenda Kampuni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo natamani nilete picha kwa hili jambo ambalo nilisema, ramani ya mtandao wa maji na masuala ya vyanzo vipya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuzungumza hapa. Bahati nzuri Waziri wa Fedha aliwahi kuleta taarifa akielezea wenzetu wa China. Ukiiangalia China pamoja na ukubwa wake lakini wametengeneza mtandao wa maji. Mtu wa Kaskazini ana uwezo wa ku-supply maji mpaka Kusini, mtu wa Kusini ana uwezo ku-supply maji mpaka Kaskazini, likewise Magharibi, Mashariki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini; nchi hii kwa ujumla wake ikiwa kuna miradi mikubwa; leo tunatoa bomba la mafuta kutoka Uganda linakwenda mpaka Tanga. Tuna bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam linakwenda mpaka Zambia. Ipate picha hiyo Mheshimiwa Waziri, na nikuombe, unayo nafasi ya kuacha kumbukumbu. Mzee wa Toronto pale Dodoma ameacha kumbukumbu ya miti. Unaouwezo wa kuacha kumbukumbu Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii visima sikatai, mabwawa sikatai. Lakini uwezekano wa kuiunganisha nchi kwa mtandao wa maji upo, tunachotakiwa ni kuthubutu. Bomba linaweza likatoka Dar es Salaam likafika Katavi. Bomba linaweza likatoka Bukoba likafika Mtwara. Inawezekana ni kuthubutu tu; na kupanga ni kuchagua. Lakini unaweza ukapanga kufeli, ukishindwa kupanga umepanga kufeli. Kwa hiyo, mimi niombe sana, na katika hili kuna nchi nyingine hatujafika huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kusema hapa ukienda kwa nchi za wenzetu wana-treat maji ya bahari, hatujafika huko, kwamba nchi hii tufike sehemu labda kama ni Bahari ya Hindi, tuyatoe maji ya Bahari ya Hindi kuyaleta huku, hatujafika hapo, vyanzo vinatosha. Chukua Ziwa Nyasa, chukua Ziwa Tanganyika, chukua Ziwa Rukwa inatosha. Habari ya visima sijataja Victoria na mimi kwa ajili ya uzalendo sioni tabu hata kama maji ya Ziwa Victoria yatamfikia mtu wa Dodoma sawa ni mipango ya ki-nchi. (Makofi)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Kingu Elibariki.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpa mchangiaji taarifa ya kwamba mambo mazito na ya muhimu anayoyazungumza ambayo kimsingi mimi naya-reflect kwamba ni long term plan ambazo Wizara yetu inaweza ikasaidia katika kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya maji lakini bahati mbaya sana Wizara ya Fedha nimejaribu kuangalia hapa simuoni Waziri, simuoni Naibu vitu kama hivi vingeweza kusaidia sana angalau kama mmoja anakuwa hayupo basi mmoja awepo kwa ajili ya kuchukua kumbukumbu ya kutengeneza mipango ya muda mrefu ya nchi. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kapufi, unapokea taarifa?

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi niseme pamoja na kuongelea mipango ya muda mrefu lakini watu waliofanikiwa duniani ni wenye jeuri ya kuthubutu. Mimi pale kwangu Mpanda tunalo Bwawa la Milala. Bwawa lile limechimbwa miaka ya 1950. Tuna chanzo cha Mto Ugala, Mkoloni kwa ajili ya kuyapeleka maji kwenye uchimbaji wa madini ameyatoa maji Ugala kuyaleta Mpanda Mjini, amechimba Bwawa la Milala uko miaka ya 1950. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama watu wa miaka ya 1950 walikuwa na mitazamo hiyo mipana, vipi kizazi cha sasa hivi? Kwa hiyo, naendelea kuomba hilo. Nishukuru kwa maana na miji 28 na Waziri mimi Mpanda pale najua kwa maana miji 28, mji wangu umeguswa. Nikikataa hicho kidogo nitakuwa mtu wa ajabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia habari ya kuendeleza Bwala la Milala, lakini chanzo cha uhakika ni Ziwa Tanganyika. Niombe sana; na nikilisema hilo liende sambamba kwa Mji wa Mpanda. Ukitumia maji safi inakwenda bila kujiuliza, utazalisha maji taka. Hatuna mfumo wa maji taka. Niombe sana wenzetu wa mipango miji; jamani maji taka bado ni bidhaa muhimu.

Leo mahali kama Dodoma kwa kupitia maji taka, ukizalisha maji masafi mfumo wa maji taka ndio unapendezesha miji. Ukienda miji ya watu wengine hawaangaiki kumwagilia maua na vitu vingine ni kutokana na maji taka. Uki-treat maji taka unapata uwezekano kwanza hamtobanana kwenye kutumia maji safi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuendelee kujipanga huko Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha habari ya maji taka isiwe ni tatizo iwe ni jambo la kuwekwa kwenye mipango yako pia. Miji inakua, Mji wangu wa Mpanda kasi yake ya kukua, na wewe Mheshimiwa Waziri umeshafika pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: … Kasi ya kukua ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami kama ilivyo ada nianze na neno la shukurani. Mimi ni Mjumbe kutoka TAMISEMI, kwa hiyo, kwa kiwango kikubwa, haya ambayo tumeyaona yanaakisi yale ambayo tulishiriki katika Kamati. Kwa hiyo, mchango wangu nitajielekeza katika maeneo machache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema naanza na shukurani. Awali ni kumshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Pia naomba kwa namna ya pekee, najua tunaye Waziri wetu na Manaibu Waziri; mkononi mwangu hapa ninayo barua ambayo Mheshimiwa Waziri ametupatia Wabunge wote ikiieleza taarifa za fedha za miradi ya maendeleo na matumizi mengineo kwa kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi, 2023. Mheshimiwa Waziri, jambo hili ni jema. Kwetu sisi, hiki ni kitendea kazi. Mimi mtu wa Mpanda Manispaa, kwa taarifa hii ya fedha ambayo umetuelekeza Wabunge, ikawe kitendea kazi. Takribani Shilingi bilioni 5.9 ikilenga maeneo mbalimbali. Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba, Wabunge tunafahamu, nami shukurani hizi nilizozitoa kwako naomba pia nizipeleke wa Waheshimiwa Wenyeviti wa Halmashauri, Mameya na Madiwani. Kwa sababu gani? Mabilioni haya peke yetu hatuwezi, ni lazima iwe kwa kupitia ushirikiano.

MBUNGE FULANI: Ndiyo!

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Kwa hiyo, ndiyo maana wapo Madiwani, wapo Wenyeviti, wapo Mameya, na kwa pamoja tunalisukuma hili gurudumu. Kwa hiyo, naomba huko Madiwani huko waliko, wapokee shukurani zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nijikite katika eneo la TARURA, najua kweli wanafanya kazi nzuri na siku zote hapa tumekuwa tukawasifia, bila kumsahau Engineer Seif. Nami nimesemaje? Siku zote yule ndugu yetu ni mtu rahimu. Ukimsifia mtu, unamtia moyo kwamba siku nyingine anajipanga vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba, najua kwa maana eneo letu la Katavi, Manispaa ya Mpanda, Mheshimiwa Waziri kipindi hiki cha mvua yapo maeneo katika nchi hii hayana mvua za kutosha. Sisi tumebahatika kupata mvua za kutosha. Sasa neema ile ya mvua imepelekea uharibifu mkubwa wa miundombinu. Nikiomba fedha Mheshimiwa kupitia TARURA lengo langu ni nini? Mazao mazuri yaliyozalishwa Katavi yaweze kukufikieni nyie ambao hamkubahatika kupata mvua. Kwa hiyo, nikiomba fedha, tafsiri yangu ni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwa maana ya matengenezo, tumetengewa Shilingi bilioni 1.1, ndiyo maana tulikuwa tunaomba watu wa TARURA waongezewe fedha. Kwa jinsi mvua ilivyoharibu miundombinu, ukija kwangu utanionea huruma. Nimesema wale watu wemelima vizuri, tunatamani mazao yatoke kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dada yangu Mheshimiwa Lupembe, yeye amebahatika kupata boost, wametengenea barabara ya lami mpaka kuisogeza kwenye mpaka na Manispaa. Nimeletewa kuchonganishwa na wananchi kule, wanasema, angalia mwenzake wa vijijini kapata lami, yeye wa mjini hana lami. Kwa hiyo, Waziri nafikiri ukilisikia hili, na wananchi kule wananisikia, kwamba jamani, mimi niliwasemeeni Bungeni. Ni kilometa chache tu Mheshimiwa Waziri. Ni kilometa kama nane hivi. Lengo ni nini? Lami nzuri iliyotengenezwa kule, isipounganika kuja mjini, inapoteza tafsiri. Jambo hilo nafikiri unaweza ukaliona na ukaona namna ya kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni MSD. Tumezunguka maeneo mbalimbali katika nchi hii, ni kweli najua nao wana changamoto kama Serikali, lakini naomba, kwa kuwa kuna fedha nyingi zimepelekwa huko, mimi tu kwa upande wa Katavi kuna zaidi ya shilingi bilioni tano kwa maana ya vifaa. Wanajitahidi kwa kiwango chake, lakini wafanye zaidi, kwa sababu kuna fedha imewekezwa huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni upungufu wa watumishi. Nina upungufu wa watumishi 969 katika maeneo yafuatayo: Walimu wa shule ya msingi 265, sekondari 148, watumishi afya 405, huo ni upungufu wa watumishi katika eneo letu la Katavi. Najua Serikali imefanya kazi nzuri kwa maana ya miundombinu, tumejengewa madarasa, vituo vya afya, lakini bila uwepo wa watumishi, kazi inakuwa ni ngumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kuna suala la upembuzi yakinifu kuhusiana na suala la miradi, Naomba sana wataalamu wetu, tumepita pale Mwanza tukaliona hilo, kama suala la upembuzi yakinifu ni jambo la kuanza nalo, nashangaa pale ambapo kazi imeshakwenda, inafika mwisho, mtu anawarudisha nyuma akisema kuna gharama moja, mbili, tatu. Hili jambo linatuchelewesha kama Serikali. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana katika eneo hilo tena Serikali ijitafakari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa maana ya SEQUIP; najua kuna Shilingi milioni 470. Kama walivyozungumza wazungumzaji wengine, naomba kwa maana ya thamani halisi ya fedha, Mheshimiwa Wizara yako iliangalie hili kwa jicho la pekee, ni kweli haiwezekani ikawa sare nchi zima, uwiano nchi nzima, na najua hilo kama Kamati tumelijadili na tukaomba mwangalie watu na jiografia za maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mtu anaweza akawa anapata mchanga sehemu ya karibu lakini akakosa cement. Kuna mtu anaweza akapata kokoto, lakini akakosa mchanga, hivyo; mabati na vitu vingine kwa upande wa vifaa hivyo vya ujenzi. Kwa hiyo hilo nalo ilikuwa ni vizuri tuliangalie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba eneo la Watendaji wa Kata, Vijiji kupata mafunzo kutoka Chuo cha Utumishi. Ni kwanini tunasema hili? Tunazungumzia Chuo cha Utumishi kwa sababu ndilo eneo ambalo watendaji wetu wanaweza wakapata ladha ya utumishi bora. Eneo la utumishi wa umma ni maeneo ambayo wanawaandaa watu wetu wajue Serikali inataka nini? Kwa hiyo, tukikuomba Mheshimiwa Waziri kwamba watu wetu hawa wapelekwe kwenye Chuo cha Utumishi wa Umma, tafsiri yake ni hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali, mpaka mwananchi akakukute wewe huko Wizarani, anaanza kucheza na Mtendaji wa Kata, Mtendaji wa Kijiji. Kwa hiyo, kule ndiko ambako taswira sahihi ya Serikali inajionesha. Kwa hiyo, tukiwa na mtu ambaye amefanya kazi vizuri katika ngazi ile, anamsaidia Mheshimiwa Rais, anakusaidia wewe na nchi inakuwa na ustawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, CSR, kama ilivyozungumzwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya muda, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nami kwanza nimshukuru Mheshimiwa hapa Ole-Sendeka amenisaidia kushukuru kwa niaba, kwa hiyo mimi nitaenda moja kwa moja kwenye point. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana ya Waziri nikushukuru, kule Mpanda tumepokea zaidi ya shilingi bilioni tatu kuboresha kilometa 38 lakini kuna mtandao wa kilometa 105 ambazo tunategemea kupata shilingi bilioni 4.7, lakini nishukuru sana Mheshimiwa Waziri tumepatiwa kwa maana Miji 28 tumepatiwa kilometa 42. Niseme ukilinganisha miji mingine yote naona Mji wa Mpanda jinsi ambavyo Mheshimiwa Waziri umeufikiria katika eneo hilo ili tuweze kuongeza mtandao wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu tuna miradi ya Kakese na Milala ambapo kuna fedha kutoka National Water Fund. Naomba fedha hizo zipelekwe kwa haraka Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo ya shukrani na mimi niendelee kusema nafahamu siku zote Waziri amekuwa akituambia hakuna mbadala wa maji, nakubaliana na wewe katika hilo na ukiongelea maji kwa maana maji ni usalama wa nchi ni usalama wa Taifa. Watafiti mbalimbali wanakwambia yawezekana vita vya tatu vya dunia vikatokana na tatizo hasa la maji katika maeneo mbalimbali duniani. Kwa hiyo, hayo yote yanaonyesha umuhimu wa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu najua tunaambiwa mpaka itakapofika mwaka 2025, kutakuwa na upungufu wa maji kwa maana ya 8,083 lakini mimi nataka kusema nini? Siku zote nikichangia hapa nimekuwa nikitoa mifano mpaka ya China, mito mbalimbali, vyanzo mbalimbali ambavyo vimekuwa ikiunganisha Kusini kuja Kaskazini, Mashariki kwenda Magharibi kwa maana ya Tanzania hii. Niombe sana sana sana, najua wakati nikiingia hapa uliniambia Kapufi mimi najua utakapoingia pale wazo lako ni moja tu kuhusu Gridi ya Taifa. Umeniambia pale, kwa hiyo maana yake suala hili wewe na Wizara yako mnalo akilini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie kwa maana ya nchi yetu hii njema, nafahamu umuhimu wa visima, nafahamu tumepeleka magari lakini twenda kushoto twende kulia, Waziri wa Kilimo juzi ameongelea namna ya kuigawa nchi hii kwenye kanda za kilimo. Nakuomba na wewe Mheshimiwa Waziri wa Maji igawe nchi hii kwenye kanda za maji. Kwa mfano, ukitumia tu Ziwa Victoria nilikuwa nikipiga mahesabu hapa kwa maana ya Mikoa yetu 26, Ziwa Victoria peke yake zaidi ya Mikoa 10 inakuwa covered. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Ziwa Victoria tu lime- cover zaidi ya Mikoa 10, Ziwa Tanganyika? Hebu chukulia Mikoa mingine mitano, Ziwa Nyasa Mikoa mingine mingapi? Ziwa Rukwa Mikoa mingine mingapi? Kwa hiyo, tukiigawa nchi hii katika Kanda hatuna sababu ya kuyatafuta maji kwa tochi. Kisima ambacho hauna uhakika nacho wakati maji yale pale unayaona kwa wingi wake. Iwe ni Ziwa Tanganyika, Ziwa Victoria, Ziwa Rukwa na ninajua Rais wa nchi hii ameongelea habari ya kutumia vyanzo hivyo. Kupanga ni kuchagua, naomba tuje na vipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu zilizopita tuliwahi kuambiwa tuna omba tuiunganishe nchi hii kwa barabara za lami na hili naliona likienda kuwa limetimia. Leo unaweza ukatoka Mtwara ukafika Bukoba kwa taxi au bajaji! Andika historia, Mheshimiwa Waziri aandike historia. Mimi niendelee kusema sibezi shughuli nyingine zote zinazofanyika, ununuzi wa magari, uchimbaji wa visima. Tugawe nchi hii, ukiigawa nchi hii nakuhakikishia kwa maji tu hayo tuliyonayo visima iwe ni ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hayo mabwawa tunayokusudia kukinga maji ni ziada. Maji tuliyonayo Victoria tu sisemi kwamba yamalize nchi nzima lakini hebu angalia kama Victoria imefanya miji 10, Tanganyika ikafanya mingine 10. Katika mikoa 26 tumebakiza mingapi? Najua Zanzibar watakuja na utaratibu mwingine kama ni visima tuseme sawa lakini bado ungeweza kuyavusha maji hata huko. Kwa hiyo mimi niendelee kusema naomba naomba, mimi sitaki kwenda mbali zaidi, katika hili hatuna sababu ya kulalamika, kupanga ni kuchagua na lazima tuje na vipaumbele. Tukisema tunakusudia kwenda kuiunganisha nchi kwa maji, kuwa na mtandao wa maji hilo linawezekana, hivi vyanzo vingine iwe ni ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeshukuru kama ambavyo tumesema hapo mwanzo ukizungumzia maji hata wenzako wengine wote awe ni mtu wa kilimo na wengineo, kwanza tuanze na maji. Ukizungumzia kilimo kwa maana ya umwagiliaji, so long as maji tumeyafanyia kazi, wewe ukienda ukaya-tap hata hayo maji mengine yanayotiririka ya mvua na mambo mengine ambayo yanapotelea baharini na kwingineko, sisi tuamue sasa kwamba haya maji mengine ndiyo yaende kwenye kilimo, haya ambayo ni mengine yaende kuwenye huduma za jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kwenda mbali zaidi ambako kuna nchi za wenzetu ukifungua tu maji ya bomba una uwezo wa kuyanywa. Sitaki kwenda huko kwa sababu kwanza tu ile mgawanyo wa maji hatujafika hapo lakini nilitamani pamoja na huduma hizi za maji tuendelee kuangalia ubora wa maji yenyewe. Nchi za watu huhitaji hata kwenda kununua maji dukani, unafungua tap yako unachota maji unakunywa. Kwa hiyo, mimi naamini tukianza kwanza na ufumbuzi huo wa kupatikana kwa maji hayo mengine yatafuatia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakubaliana na wengine wote kuhusu suala zima la majitaka. Nilisema hapa majitaka wala siyo maji ya kubeza. Unaweza ukapitia majitaka yakakusaidia kufanya majukumu mengine. Miji mingi duniani inapendezeshwa kwa kupitia majitaka. Kwa hiyo, kwa kuzalisha majitaka ukaya-purify, maji hayo yanarudi kufanya shughuli hizi nyinginezo kupendezesha Miji kama hivyo, badala watu kupita na kusema kwamba mji ni mchafu, wapite wakiuona mji umependeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo niombe kwa maana ya huduma ya majitaka kutolewa kwa mfumo wa magari na kama siyo magari tu hata kwa maana ya hayo mabwawa mengine ambayo ni ya kutibu maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la udhibiti wa uchimbaji holela wa visima ndiyo maana nakusudia ni bora tukaendelea kuangalia vyanzo hivyo tulivyonavyo tayari kwa sababu study zinasemaje? Hili nilikuwa naomba sana kwa maana ya muda mrefu haswa katika ile miji ya wenzetu tafiti zako zijielekeze pia. Unaweza ukafurahia kwa maana ya kuyachimba maji yaliyopo ardhini lakini ukazalisha tatizo jingine.

Kwa hiyo, naomba sana hilo likifanyika liende sambamba na tafiti. Sehemu nyinginezo duniani miji imekuwa ikizama kutokana na suala hilo hilo la uchimbaji visima bila kufanya tafiti. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri katika eneo hilo tuendelee kuyazingatia hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho lakini siyo kwa umuhimu kwa maana ya Chuo cha Maji kuzalisha wataalam. Haya yote tunayoyatamani naendelea kuomba tusiache kuboresha watu wetu katika fani hii ya maji ili waendelee kutoa huduma iliyotukuka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nakushukuru kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Na mimi, kama ilivyo ada, kuna usemi unaosema kwamba sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Nafahamu wengi wameongea kwa maana ya suala lililoko mbele yako lakini naamini kwa kuwa ni wengi wanalizungumza hilo tunarejea kwamba sauti yao ni sauti ya Mungu na mimi naikunja mikono yangu ikiamini Mwenyezi Mungu atatenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo nimshukuru ndugu yangu Mheshimiwa Januari, kwa maana ya Waziri, Naibu Waziri lakini na watendaji wote kwa kazi ambazo wanaendelea kufanya. Shukrani nyingine za ziada nizielekeze kwa Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa inayoendelea.

Mheshimiwa Spika, ulitutahadharisha tusitaje nchi moja moja kwa maana ya kuepuka migogoro ya kiitifaki na mambo mengine ya namna hiyo lakini mimi nikuombe…

SPIKA: Ngoja niiweke sawa. Ukiwa unataja kama mfano wa jambo zuri linalofanyika huko, ambalo sisi tunapaswa kujifunza ama kuiga ni sawa. Lakini kama wana changamoto yao hiyo ndiyo inayokuwa changamoto kwenye kuitaja nchi hapa ndani. Ahsante sana.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mimi nitaliweka kwenye sura kwamba haya yote mazuri tunayofanya ndani ya nchi basi changamoto zinazoifika nchi nyingine kwetu iwe ni somo. Nilikuwa naomba niliweke kwenye sura hiyo.

Mheshimiwa Spika, kwa maana ya utekelezaji wa vipaumbele vya mwaka 2022 na 2023 ni upelekaji wa mradi mkubwa wa kuimarisha grid ya Taifa kwa Mikoa ya Katavi, Kigoma na Kagera. Lakini hilo Mheshimiwa Waziri amelirudia tena, kwa maana pia ndio vipaumbele vya 2023/2024.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi kwa ujumla wake kuna wimbi kubwa la kuongezeka kwa miradi; na sisi pale Mpanda uzalishaji ambao tumekuwa tukiendelea nao ni uzalishaji kupitia majenereta haya ambayo yanatumia mafuta. Niishukuru Serikali kwa hilo, na najua tulikuwa na jenereta nne, kwa msaada wa Mheshimiwa Makamu wa Rais tukaongezewa jenereta moja, na watts ambazo tumekuwa tukipata kwa kipindi chote ilikuwa ni megawati 6.25 kwa majenereta matano. Lakini kwa maana ya ongezeko kubwa la miradi nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri, kuna mambo mawili, nikiamini kwa maana ya suala zima la grid ya Taifa njia ya msongo wa kv 132 kutoka Tabora Kwenda Katavi mpaka sasa hivi kwa mujibu wa taarifa za Mheshimiwa Waziri iko asilimia 26.7.

Mheshimiwa Spika, rai au ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri. Kasi ya maendeleo ya wananchi ni kubwa na yeyote akija Mpanda akija Katavi atakubaliana na mimi katika eneo hilo. Tumuombe Mheshimiwa Waziri, wakati tukisubiri huu umeme wa msongo mkubwa atusaidie, lengo ni kupeleka mbele maendeleo ya watu wetu. Nimuombe sana katika hilo. Waliweza kutusaiida jenereta, najua ni kipindi cha mpito kwa usikivu wake ndugu yangu Mheshimiwa Makamba tuliangalie hilo; wametusaidia hapo katikati. Na wakati wengine wakilalamika najua kuna suala la kukatika kwa umeme lakini mimi nishukuru walau kwa jitihada hizo zilizofanyika, maana unaposema ahsante hata ukiomba unafikiriwa kwa hiyo naomba mnifikirie katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo. Nimezungumzia habari ya mashine hizo na ongezeko la wawekezaji, na nimesema suluhu kwa kipindi hiki ni hiyo grid ya Taifa. Kuna mradi wa REA; mimi nimebakiwa na vijiji vitano. Vijiji hivyo ambavyo kwa mujibu wa taarifa wanasema mpaka ikifika mwezi Juni kwenda Agosti 2023 umeme utakuwa umewashwa katika maeneo hayo, vijiji hivyo ni vya Kamakuka, Mkokwa, Nguvu Mali, Nseso na Mkwajuni. Nimuombe Mheshimiwa, maeneo yote hayo ambayo nimeyazungumza kilimo kinafanyika, uzalishaji ni mkubwa na kuna viwanda vidogo vidogo vya ukoboaji wa mazao. Kwa hiyo tukiwapelekea umeme tunakwenda kuwasaidia na nikiamini upatikanaji huo wa umeme utasukuma mbele jitihada hizo za wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini nikitoka hapo, nimshukuru Mheshimiwa Waziri; tuna mradi mwingine tuna takribani milioni 260 ambazo tunakwenda kupeleka umeme kwa ajili ya kusukuma pump kwa ajili ya Vijiji vya Society na Kakese, lakini pia kwa maana ya Zahanati ya Mwamkulu na Kakese, tumepewa takribani milioni 260, nishukuru sana kwa suala hilo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo yote nishukuru pia kwa ajili ya mradi wa ujazilizaji mzunguko wa pili (b), tunaambiwa vitongoji 1,686 na Katavi ikiwemo vitanufaika. Kwa hiyo mimi nishukuru kwa hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya shukrani hizo maelezo yangu ya jumla natamani niione TANESCO, au shirika kwa ujumla wake ambalo kwa kiwango kikubwa Serikali imekuwa ikililea shirika hili, ikilipa nguvu shirika hili basi tufike sehemu tuone huyu mtu ambaye amaelelewa kwa kiwango kikubwa amefika sehemu anaweza kusimama.

Mheshimiwa Spika, nalisema hilo kwa sababu gani, kati ya maeneo ambapo huwezi ukalalamika uwepo wa wateja ni pamoja na eneo hili la TANESCO, wateja wapo tu ni wa kufikia. Labda nilichokuwa naomba au kushauri, tubadilishe mtazamo tuachane na ile biashara ya mazoea. Kama wateja ndio wanaolalamika tunaomba huduma, tunaomba huduma maana yake suala la soko siyo tatizo. Kwa hiyo tukiachana na biashara ya mazoea, TANESCO kwa jitihada wanazofanya, na wakabadilika; kuna taasisi nyingine mnaona kila kukicha inafanya mabadiliko; kawaangalie TANROADS na TARURA wanafanya mabadiliko kila kukicha. Na mimi natamani TANESCO waachane na biashara ya mazoea tunagalie sura hiyo kwamba ni soko la uhakika lakini kwa nini watu walalamike kila siku? Maana yake kuna kitu wanatakiwa wabadilike, na wakibadilika, mimi naamini haya yote ambayo yanazungumzwa, ukiangalia kwa maana ya nchi hii yenye fursa kibao, kwa maana ya kutekeleza miradi ya nishati jadilifu ikiwemo joto ardhi, tungamotaka, upepo na jua pamoja na matumizi bora ya nishati yanawezekana. Na nchi yetu njema, fursa zote zipo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naongea na jirani yangu hapa Mheshimiwa kuna sehemu moja kama unaenda Moshi, unaambiwa jihadhari upepo mkali, hiyo ni fursa. Kama tunaambiwa tunapita kwa magari kwamba jihadhari upepo mkali, hiyo ni fursa, na maeneo mengine yote ni fursa. Lakini moja kubwa haya yote hata kama tutatumia vyanzo vyote hivi kuviingiza kwenye grid ya Taifa, tusiache, kama nilivyozungumza pale mwanzo, kuchukua tahadhari. Sitamani siku moja tukaona migawo hii ikiendelea eti kwa sababu kuna jambo moja hatukufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa unyenyekevu mkubwa naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mchango wangu utakuwa katika maeneo machache, nikijielekeza katika pongezi, lakini sehemu kubwa itakuwa ni eneo la madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami kama ilivyo ada, nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake, lakini nafarijika sana, kuna huu mradi mkubwa wa TACTIC mara ya mwisho Serikali imetoa tangazo, naamini kwa maana ya Mji wa Mpanda, Manispaa ya Mpanda tunakwenda kunufaika na mradi huu wa TACTIC ambapo tangazo limetolewa. Tuko kwenye awamu ya pili, zaidi ya kilometa 15 za lami zinakwenda kutengenezwa katika Mji wa Mpanda, zaidi ya kilometa 30 kutoka Mwamkulu – Kakese - Misunkumilo, hili ni jambo jema. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kwenye msukumo wa kuzisukuma fedha hizi kwenda huko, usisite tafadhali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo kama haitoshi, naiongelee upande wa reli. Tunayo reli yetu kwa maana ya kutoka Kaliua kwenda Mpanda. Kuna zaidi ya Shilingi bilioni 379.3 zinapelekwa huko kuimarisha reli ile. Siyo hilo tu, wanakwenda kutujengea kituo cha kupumzikia abiria cha kisasa katika stesheni yetu ya Mpanda. Mheshimiwa Waziri, katika hili, utakapofika muda wa kuzisukuma fedha huko, naomba naomba sana. Ukanda huu wa kwetu, mkitusaidia kwenye maeneo hayo tutaendelea kujikita kwenye kusukuma kilimo mazao mbalimbali na kuyaleta kwa walaji huku. Tumebahatika, kwani maeneo yetu yana ardhi nzuri na rutuba nzuri, kwa hiyo, mnapotuletea miundombinu, nasi tunahangaika kuwaleteeni ninyi wenzetu huku ambapo wakati mwingine hali ya hewa ni mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo, nimeona kuna ununuzi wa kandarasi za ujenzi katika maeneo ya meli tatu ikiwa ni pamoja na Ziwa Tanganyika. Naomba sana, Ziwa Tanganyika kama chanzo cha mapato kinachotuunganisha na hizo nchi ikiwa ni Kongo, Burundi au Zambia, kandarasi hii ya ununuzi wa meli kwenye ziwa hilo ambayo Mheshimiwa Waziri ameisema, naomba sana fedha hizo zielekezwe huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema sehemu kubwa nitajielekeza kwenye suala la madini. Naomba sana, najua Serikali inatamani kupata mapato, huko nyuma wachimbaji tuliwahi kuwa na mkutano mkubwa, tukaiomba Serikali kwamba namna pekee ya kuisaidia Serikali, ipunguze utitiri wa tozo na kodi katika eneo la madini. Nami nikueleze Waziri wa Fedha, nakuomba sana, mimi bahati nzuri ni mchimbaji, kwa hiyo, nikiyaongea haya, naongea yale ambayo wakati mwingine tumekuwa tukiyafanya muda wote. Hakuna mtu anakimbia suala la kulipa kodi na vitu vingine vya namna hiyo, lakini nilichokuwa naomba sana, kwanza hebu ziangaliwe kanda tofauti za uchimbaji. Wako wenzetu wa kanda ya mwanza, Shinyanga, wako wenzetu wa Chunya huko, uko ukanda mwingine kama huku kwetu Mpanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukizungumzia kwa mfano dhahabu ya Mpanda, nilikuwa natamani sana, hapa kwenye taarifa yake amepongeza na kusema kuna suala zima la kuongeza thamani na kuthibiti utoroshaji wa rasilimali za madini. Naomba sana, refinery sikatai, ni jambo jema na ndipo hapo katika refinery amesema, “mtapunguza kutoka asilimia sita kwenda asilimia nne za mrabaha.” Ni jambo jema, lakini nilichokuwa naomba, eneo hili pia ikumbukwe kuna mchanga unasafirishwa kwenda nje, hiyo mnayoiita makinikia, lakini kule ndani Mheshimiwa Waziri tujiulize kama sehemu ya mchanga huo yapo madini ya dhahabu, yapo madini ya fedha, yapo madini ya shaba, Tanzania tunafeli wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa naomba sana, bado iko nafasi ya kuwa na viwanda vya uchanjuaji hapa hapa nchini, kama ambavyo tumesema refinery ile inayotengenezwa Mwanza; na hapa mimi nashukuru maana tunaambiwa hata dhahabu sasa hivi itaanza kununuliwa na Serikali, ni jambo jema, lakini nasema bado tuna nafasi ya kufanya uchenjuaji hapa hapa nchini. Kwa sababu kama unabebwa kama mchanga kwenye nje lakini ukumbuke huko ndani mmesema kuna shaba, kuna fedha, ni madini haya, ni chanzo cha mapato, hiki kitu ni vizuri kama kingeongezewa thamani hapa hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi tena kuuliza, lengo ni nini? Dhahabu hii nyingi iliyopo hapa nchini, naomba sana, leo katika maeneo ya uchimbaji yawezekana hawa watu wachimbaji kwa ujumla wake, tukiwapa motisha tukawapunguzia ongezeko hilo la tozo na kodi mbalimbali, kubwa ambao Mheshimiwa Waziri atakutananalo, wachimbaji hawa kwa ujumla wao, wakihangaika ikapatikana dhahabu, kodi mbalimbali atazipata kutokana na hawa watu kufanya manunuzi katika maeneo mbalimbali. Naomba aliangalie hilo, na bahati nzuri wachimbaji inapokuja kwenye matumizi ni watumiaji wazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huko ndiko ambako kama ni kwa maana ya kodi tuzipate huko. Ukumbuke dhahabu kama ilivyo, ikibaki ardhini huwezi ukaiona thamani yake. Utakuja kuiona thamani kama imetolewa ardhini ikawekwa hapa juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tujiulize, zipo nchi hawana hata shimo moja la madini, iwe ni dhahabu au vinginevyo, lakini wametengeneza refinery. Unajiuliza wanakusudia wapate dhahabu kutoka wapi? Kwa hiyo, maana yake sisi hapa nchini tulichotakiwa kwanza ni kufungua milango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikikupa mfano wa kule kwetu Mpanda, DRC Congo siyo mbali. Tukitengeneza mazingira rafiki hapa, ipo nafasi Mheshimiwa ya hata majirani zetu kuleta mali hapa nyumbani kwetu. Kwa hiyo ni wewe kufungua milango Mheshimiwa. Taabu iko wapi? Nimesema kuna nchi nyingine hawana hata shimo moja la kuchimba dhahabu, lakini wametengeneza viwanda vya kusafisha dhahabu. Unajiuliza, wanapata wapi dhahabu? Sasa kudhibiti utoroshaji, ushauri wangu, eneo hili la tozo mbalimbali wewe Mheshimiwa jipange vizuri. Watu hawa wakipewa motisha kila mmoja huko aliko, hata sisi tunaofanya uchimbaji wa kienyeji huwa tunatoa motisha kwa watu wetu nikiamini wakipata motisha hawa, wataongeza kasi ya kutafuta mali na mali ikipatikana upande wa pili wa Shilingi Serikali nayo inanufaika kwa sura hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba katika eneo hilo, ukumbuke wachimbaji hawa bado kuna tozo nyingine nyingi. Mfano mtu ana karasha ambalo ni kitendea kazi, anaambiwa alipie, maji alipie. Sasa tozo hizo mbalimbali ukizijumlisha, leo tunataka kwenda karibia zaidi ya asilimia kumi tozo mbalimbali zaidi ya kumi ambapo utashindwa kuiona thamani na mchango wa wachimbaji hawa ambapo naamini kwa kupitia madini ya dhahabu tuna uwezo mkubwa wa kuitoa nchi hapa ilipo ikapiga hatua mbele zaidi. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana tarehe 18 ya mwezi huu Rais wetu alifanya kitendo ambacho kwa sisi wana Katavi ilikuwa ni mkombozi, kwa maana ya Katavi, Tabora lakini na mikoa mingine ya uzinduzi wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kubwa ninalolikumbuka nikiacha kusema ahsante nitakuwa ni kiumbe wa ajabu, nashukuru sana kwa kitendo kile lakini bahati nzuri Waziri alikuwepo na Waziri anakumbuka sisi wana Katavi tulinufaika ile chenji itakayobaki kwenye ujenzi wa barabara ya Mpanda, Tabora imeombwa ielekezwe kwenye barabara ya kwenda Kigoma. Kwa hiyo, nilikuwa napenda nishukuru kwa suala hilo muhimu. Mkuu wa Nchi aliongea na yule kiongozi wa Benki ya Afrika kwamba chenji itakayotoka pale itusaidie wana Katavi kwa barabara ya kwenda Kigoma. Nashukuru sana kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutokana na hayo ya kwangu yatakuwa machache sehemu kubwa nikijikita kwenye kusema ahsante, lakini ahsante ni namna ya kistaarabu ya kuomba tena, ahsante kwa barabara ya Mpanda Tabora. Lakini tunayo barabara muhimu sana kwa maana ya Mpanda, Ugala, Kaliua, Ulyankulu kwenda Kahama. Barabara hii najua wataalamu wapo wanafanyia kazi suala hili lakini barabara ile na hii niliombe liwe katika sura ya nchi kwa ujumla wake kwa sababu zifuatazo;

Mheshimiwa Spika, inapotokezea mnabarabara moja tu ikipata dharura yoyote namna ya kutoka hapo inakuwa ngumu. Kwa hiyo, unapokuwa na barabara nyingine ambayo inaweza ikasaidia wakati wa dharura hilo jambo lisiwe tu kwa ajili ya Mkoa wa Katavi lipate sura ya kitaifa mnakuwa na barabara moja ikikatika matatizo uchumi unayumba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo kwa maana ya kufungamanisha fursa mbalimbali na suala zima la uchumi tumeongelea Ziwa Tanganyika. Tunayo meli moja ya Liemba labda kwa manufaa ya Bunge hili ile meli ilizinduliwa Februari 5, 1915 meli hiyo lakini ilianza kutengenezwa 1913 meli ya Liemba na ndiyo meli ambayo wanatuambia meli pekee duniani ambayo ilitumika katika vita vya kwanza vya dunia na inaendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, sasa tafsiri yake nini tunaweza tukafungamanisha hata wenzetu wa utalii kama meli hii kwa siku zote hizo na watu huko duniani wanaifahamu hivyo inaweza ikawa ni chanzo cha utalii pia lakini watanzania angalia tunavyokalia fursa. Mbali ya kufanya kazi katika Ziwa Tanganyika lakini ingeweza kuwasaidia na wenzetu wa utalii kufungamanisha fursa hizo. Kwa hiyo, nilikuwa naomba ukiachilia kwamba inaenda kuwasaidia wakazi wa ukanda ule lakini bado inaweza kusaidia kunyanyua mapato ya nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru juzi Mkoa wangu wa Katavi Shirika la Ndege wametuongezea safari nyingine ya nne tulikuwa na safari tatu katika wiki kwa maana Jumanne, Alhamisi na Jumamosi tumeongezwa na trip nyingine ya Jumatatu, kwa hiyo, tumekuwa na trip nne. Tafsiri yake ni nini? eneo lile linaendelea kufunguka. Kwa hiyo, niwashukuru katika hilo lakini na watu wengine muendelee kufahamu Katavi inafikika fursa hizo zipo, tumieni ndege, tumieni reli tumieni barabara.

Mheshimiwa Spika, upande wa fidia; kuna wananchi ambao wameendelea kusubiri maeneo ya Magamba, Misungumilo na Kawajense, hawa watu kwa muda mrefu wanasubiri fidia. Naomba sana tuwaangalie watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, reli; Mheshimiwa Waziri analo deni kwa maana ya kujenga kibanda cha kusubiria abiria katika stesheni yetu ya Mpanda. Namwomba sana sambamba na kuongezewa mabehewa, reli kwa ujumla wake, naomba wabadilike wasifanye kazi kizamani, wale watu wa Mpanda hawapandi bure, wanapanda kwa kulipa. Unapotafuta mabehewa yaliyochoka yaani sehemu nyingine zote mabehewa yaliyochoka ndiyo yanapelekwa kule Mpanda, wanatufanya tuonekane wa kizamani. Naomba tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa ujumla wake, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya TAMISEMI, kwa hiyo kwa kiwango kikubwa kazi unayoiona iliyoletwa mbele yako inaakisi yale ambayo na mimi kama Mjumbe nimeshiriki. Kwa hiyo, mchango wangu utajikita katika maeneo machache. Nitakwenda kwenye motisha, nitakwenda kwenye michezo na muda ukiruhusu nitakwenda kwenye TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo ya jumla, kabla sijaja Bungeni nilikuwa nikiangalia kipindi cha National Geographic. Kipindi kile niliona wenzetu na adha wanayoipata kutokana na matatizo kama barafu, baridi kali na vitu vingine vya namna hiyo. Nikawa najiuliza sisi kwa bahati nzuri hapa tulipo, msaada wa Mwenyezi Mungu eneo zuri la kijiografia tulipo na tunalalamika; tukipata mvua tunalalamika, tukikosa mvua tunalalamika, vipi kama tungepata na baridi kali na mabarafu kama yale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu huko duniani kwa kupitia mipango wanajua kuna kipindi cha baridi kali, kuna kipindi cha barafu, kuna kipindi cha mvua kwa hiyo mvua kwao si tatizo ni suala tu la kujua kwa mipango yetu tutakabiliana vipi na mvua na mambo mengine ya namna hiyo. Kwa hiyo nilichokuwa naomba kwanza tumshukuru Mungu kwa kuwa hapa tulipo kijiografia lakini huyu Mwenyezi Mungu tusimpelekee kila aina ya lawama, baadhi ya kazi ni za kufanya sisi wenyewe. Nilikuwa naomba nianze na hilo. Kwa hiyo jitihada zilizobaki ni zetu sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa watu wa mipango wanatusaidiaje? Ni kweli mimi pia nashiriki katika suala la Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu. Kwa ujumla wake sisi kule kwenye Chama cha Kibunge cha Idadi ya Watu tunasema hivi, kuwa na idadi kubwa ya watu ikitumika vizuri ni fursa lakini kuwa na idadi kubwa ya watu kama hutotumia vizuri ni changamoto. Kwa hiyo kwa sura yangu tafsiri yangu ni nini? Kila mwaka tunapozungumzia habari ya ujenzi wa vyoo, utengenezaji wa madawati, kila mwaka hicho pia ni kipimo cha umaskini. Tunatakiwa kwa kupitia watu wetu wa mipango watusaidie tutoke huko, kwa sababu suala la kujua una idadi gani ya watu, utafanya vipi, maoteo yakoje ni suala la kimipango. Kwa hiyo eneo hilo kwanza nilikuwa naomba sana tujaribu kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoka hapo, mmezungumzia suala la motisha, mimi eneo la motisha nishukuru kamati kwa maana ya ukurasa wa 21 imezungumzia wale waliofanya vizuri na katika hili nishukuru Mkoa wangu wa Katavi umefanya vizuri kwa ujenzi wa maboma; zaidi ya maboma 500 wanakusudia kuyajenga. Sasa nasemaje kwa maana ya motisha? Wale wanaofanya vizuri tuonyeshe kuwapongeza, kuwatia moyo na ikiwezekana kama kuna namna nyingine ya kuwaruzuku ili watu hawa waendelee kufanya kazi vizuri. Nikilisema hilo ukiacha hilo la kazi nzuri iliyofanywa na eneo hilo, tulipita Mbeya tukakuta kuna shule moja inaitwa Nsalanga, hii Nsalanga pale Mbeya jiji kuna mwalimu amefanya kazi nzuri kwa kwenye Mradi wa SEQUIP. Kazi nzuri kabisa, na kwa kiwango kile kile cha fedha ametengeneza kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa naomba motisha ya watu wanaofanya kazi; na huyu mwalimu kwa ajina anaitwa Mwalimu Pascal Lucas wa Nsalanga naona Mheshimiwa Spika amefurahi ni kweli kazi nzuri, shule nzuri wale watu wamejiongeza wamekuwa ni watundu wabunifu. Mahali pa shule wameweka mpaka badala ya tiles wameweka ile kitu wanaita tarazo wamejiongeza walikuwa watundu, wabunifu. Sasa watu kama hawa tuwatie moyo kuwapongeza katika maeneo mbalimbali ili na wengine waige. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo hilo la motisha mimi naomba, wenyeviti wa mitaa, wenyeviti wa vijiji, Madiwani wanafanya kazi nzuri tuwape motisha tuwatie moyo hilo ni eneo la motisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitoka hapo nije eneo la michezo. Tumesema kwa kupitia Kamati yetu. Ujenzi wa viwanja katika maeneo mbalimbali leo tusiwe watu wa kulalamika kwa nini wenzetu wa West Africa wanafanya vizuri ni uwekezaji. Leo ukikuta kila huyu mchezaji mzuri duniani anatoka huko haijaja kwa bahati mbaya, ni kutokana na uwekezaji. Kwa hiyo na mimi naomba eneo la ujenzi wa viwanja tusiache katika maeneo yetu mbalimbali. Niwapongeze Arusha tulipita pale tukakuta wenzetu wa TARURA ile chenji iliyobaki wamekwenda kujenga viwanja vizuri vya michezo. Nitoe shime kwa wadau mbalimbali wa michezo waturahisishie kazi hiyo nikiamini tukifanya vizuri eneo hilo la michezo huo ni uwekezaji kama uwekezaji mwingine. Tumeona wachezaji waliofanya vizuri huko duniani wanarudi katika nchi zao wanawekeza; iwe katika shule au katika hospitali. Kwa hiyo kwanza umeanza kwa kuwekeza kwenye michezo baadaye utaiona tija baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi katika eneo la TARURA kwa maana ya kumalizia. Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu, ukikuta watu wengi kwa nini wote tunazungumzia TARURA, TARURA, TARURA, niombe sana watu hawa kuwaongeza fedha mimi kwa suala la barabara na tatizo lilivyo naichukulia kama ilivyotokezea janga wenzetu hawa wa huku Hanang. Sura ile ilivyotokea na Serikali nzuri ikafanya kazi kwa uharaka ndivyo ilivyo. Kila sehemu ukienda ni tatizo, kila sehemu ukienda ni tatizo. Kwa hiyo hakuna namna zaidi ya kuwaongeza watu hawa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kwenda kwenye maeneo mengine ya kuboresha, kwa maana ya miradi mingine hiyo ya AGRI-CONNECT, TACTIC na RISE kwa maana tu huko kote tutafanya kazi ikiwa kwanza hii dharura iliyojitokeza tumei-address. Tulichukulie kama janga na watu hawa wapelekewe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda naunga mkono hoja. (Makofi)