Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Selemani Moshi Kakoso (65 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Nawashukuru sana wananchi wa Jimbo la Mpanda Vijijini kwa kazi kubwa waliyoifanya ya kukichagua Chama cha Mapinduzi. Na mimi kama mwakilishi wao nawaahidi nitawafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kuchangia Mpango huu kwenye suala zima la miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya Serikali ni kuhakikisha mikoa yote inaunganishwa na barabara zote zinajengwa kwa kiwango cha lami. Bahati mbaya sana mikoa ya pembezoni imeachwa bila kuunganishwa ukiwemo mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora ni Mikoa ambayo ilisahaulika kimaendeleo. Katika Mpango huu ambao Serikali imeuleta, tunaomba rasilimali za nchi hii zigawanywe kwa uwiano ulio sawa. Inafanya wananchi wa maeneo mengine katika nchi yetu wanaonekana kama watumwa wakiwa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie kwa makini zaidi, tusielekeze kila siku Mikoa ya Kanda ya Kaskazini ndiko ambako wanaelekeza Serikali kupeleka huduma za kijamii. Tunahitaji maeneo ambayo yalisahaulika nayo yaangaliwe na kuwekwa kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali iharakishe kujenga miundombinu ya barabara. Barabara ya Sumbawanga kuja Mpanda ikamilike, barabara ya kwenda Kigoma kutoka Mpanda ikamilishwe na barabara ya kutoka Mpanda kwenda Tabora ikamilishwe. Vilevile bado barabara zile za Mkoa wa Tabora kwenda Kigoma nazo zikamilishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza leo hii, Mkoa wa Katavi umekaa kisiwani. Barabara ya kutoka Mpanda kwenda Tabora haipitiki. Nasikitika tu kwamba hata leo Serikali ilipokuwa inatoa kauli, uwezekano wa kupita barabara ile ya kutoka Sikonge kuja Wilaya ya Mlele, haupo. Bahati mbaya Serikali imesahau maeneo hayo. Naomba miundombinu iangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye suala la miundombinu ni ujenzi wa reli. Reli tunayoihitaji Watanzania ni reli ya kutoka Dar es Salaam kuja Tabora; reli ya kutoka Tabora kwenda Mwanza; reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma. Vilevile tawi la reli la kutoka Uvinza kwenda Msongati na tunahitaji reli ya kutoka Tabora kwenda Kaliua - Mpanda – Karema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo sababu za msingi ambazo tunaomba Serikali iangalie. Nchi ya Congo inajenga reli kutoka Lubumbashi kuja Kalemie kwa lengo la kutaka kuunganisha reli inayotoka Karema kwenda Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Wakongo wameona kuna umuhimu bidhaa zao zipitie kwenye nchi yetu, sisi ambao tuna umuhimu wa kutumia Bandari ya Karema na kuifanya Bandari ya Dar es Salaam ipokee mzigo mkubwa, ni kwanini tuwe na vikwazo vya kusuasua tusijenge reli hii na kutoa maamuzi? Naomba Serikali iliangalie hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la kilimo. Watanzania walio wengi wanafanya kazi na wengi wanajishughulisha na shughuli za kilimo. Naiomba Serikali, ni lazima ifike mahali iangalie umuhimu wa kuboresha kilimo. Ili kilimo kiweze kuwa na maboresho, kwanza iangalie gharama za pembejeo. Pembejeo nyingi zinazoletwa kwa ajili ya shughuli za kilimo ni za bei ya ghali. Tena inafikia mahali Jimboni kwangu, bei za pembejeo zenye ruzuku ya Serikali ni za ghali kuliko bei za soko.
Sasa inafanya kilimo hiki kisiweze kwenda. Naomba iangalie umuhimu wa kuboresha shughuli za masoko ili tuweze kusaidia mazao ya kibiashara. Ni lazima Serikali ifike mahali iwe na kitengo maalum cha kutafuta masoko ili kuyasaidia mazao ambayo yanalimwa na Watanzania walio wengi.
Jimboni kwangu kunalimwa zao la tumbaku. Tumbaku sasa hivi ni zao ambalo kwa wananchi ni kama utumwa, kwa sababu masoko yake ni ya shida. Naiomba Serikali iangalie umuhimu sasa wa kujenga kiwanda ambacho kitasindika mazao ya zao hili la tumbaku sambamba na mazao ya korosho, kahawa na mengineyo yale ya kibiashara ambayo yatakuza uchumi kwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine nilikuwa napenda kuishauri Serikali iwekeze kwenye shughuli nzima ya uvuvi na ufugaji. Ili wavuvi waweze kuwa na mazao mazuri yenye tija, ni lazima Serikali iangalie masoko na kuwapa huduma wavuvi ambao wanavua kwenye eneo la Ziwa Tanganyika ambako kunahitaji miundombinu ya umeme ili wananchi wanaofanya shughuli kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika waweze kunufaika na kuona umuhimu wa kuwekeza kwenye suala zima la uvuvi. Tunahitaji Serikali ijenge viwanda vidogo vidogo vitakavyowasadia wananchi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naiomba Serikali iangalie suala zima la huduma ya maji. Ili Watanzania waweze kufanya shughuli za kiuchumi vizuri, ni vyema Serikali ikasaidia kuwekeza miundombinu ya maji kwenye maeneo mengi, hasa vijijini. Naiomba Serikali, kwenye Jimbo langu tuna miradi ya maji ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ikamilishe haraka; na ipeleke kwenye maeneo mapya ambayo tuna Watanzania walio wengi ambao wapo kule maeneo ya Mishamo, hawana huduma ya maji. Tuna Kijiji cha Kamjela, Kijiji cha Kusi, Ipwaga, Ilangu na maeneo mengineyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mapya yanahitaji yapate huduma ya maji. Naomba Serikali iangalie maeneo yale kwani huko nyuma yalikuwa yanahudumiwa na UN, kwa sasa yapo mikononi mwa Serikali. Naomba Serikali pia iangalie eneo la migogoro ya ardhi. Tunayo maeneo mengi katika Jimbo la Mpanda Vijijini ambalo limezungukwa na mapori, ifike mahali Serikali imalize migogoro ya ardhi, hasa ile ya WMA kwenye vijiji vya Kabage, Sibwesa, Nkungwi, Kasekese na Kaseganyama. Lakini...
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa mwaka 2018
MHE. MOSHI S. KAKOSO - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuwasilisha na kupokea maoni ambayo wameyatoa Waheshimiwa Wabunge juu ya Kamati ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya hasa kwenye Sekta hii ya Miundombinu. Ametekeleza miradi mikubwa sana ambayo Serikali imeanza kuitekeleza na imeonekana kwenye jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ya usimamizi wa Serikali, nawapongeza Mawaziri, na Waziri mwenye dhamana ambaye anasimamia hii sekta, kwa kazi kubwa sana aliyoifanya kwa Kamati. Ushirikiano ambao ameuonyesha umetekeleza miradi ambayo ni mingi na ushauri wa Kamati umefanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kusukuma fedha kupeleka kwenye Sekta ya Miundombinu ambako kumeonekana miradi mingi ambayo imeanza kutekelezwa na zaidi kulipa fedha nyingi za Makandarasi waliokuwa wanadai, karibu ya zaidi shilingi trilioni tatu zimelipwa kwa kipindi cha miaka hii mitatu iliyokuwa na malimbikizo ya madeni huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge waliochangia ni 12. Kati ya hao, 11 wamechangia kwa kuzungumza na Mbunge mmoja amechangia kwa maandishi. Nawapongeza sana na kuwashukuru kwa kazi kubwa ambayo wameitoa na ushauri wao karibu asilimia kubwa umepitia mapendekezo ya Kamati. Mjumbe wa kwanza alikuwa ndugu yetu Mheshimiwa Musukuma, ametoa mapendekezo yake na kuishauri Kamati juu ya magari ambayo yanatumia super single.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ambayo ametoa Mheshimiwa Mbunge, Kamati ilishatoa mapendekezo na yalishaanza kufanyiwa kazi na Serikali. Kwa bahati nzuri, Waziri mwenye dhamana, Mheshimiwa Isaack Kamwelwe, amezungumza nia ya Serikali kuangalia upya sheria ambayo ipo, nasi kama Kamati tunasisitiza kwamba, ni vyema Serikali ikaliangalia hilo, kwani nchi yetu siyo kisiwa, tumekaa katika maeneo ambayo ni ya mzunguko, ambapo tunahitaji kuwa na mawasiliano na nchi za jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ambayo ameyatoa Mbunge Kamati ilishatoa mapendekezo na yalishaanza kufanyiwa kazi na Serikali kwa bahati nzuri, Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana Isack Kamwelwe amezungumza nia ya Serikali kuangalia upya sheria ambayo ipo na sisi kama Kamati tunasisitiza ni vyema Serikali ikaliangalia hilo kwani nchi yetu sisi sio kisiwa, tumekaa katika maeneo ambayo ni ya mzunguko ambayo tunahitaji kuwa na mawasiliano na nchi za jirani, kwani maeneo mengine ambapo tulitunga sheria hii hii, wapo wanaoitekeleza na wapo ambao hawaitekelezi. Kwa hiyo, ni vyema Serikali ikaliangalia upya na waweze kuliangalia kwa manufaa mapana ili liweze kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mjumbe mwingine aliyechangia Mheshimiwa Ally Saleh alizungumzia sana juu ya Shirika la Ndege ambalo mawazo yake makubwa alikuwa anashauri kwamba Shirika la Ndege lisiwe la kutoa huduma tu bali liwe la kibiashara na watendaji wajue shughuli ya kuliendesha hili shirika linahitaji ufanisi mkubwa. Kamati ilishatoa mapendekezo katika ukurasa wa 33 hadi 34, tumetoa mapendekezo juu ya kuliboresha shirika hili, lakini bado yapo mambo ya msingi ambayo ni vyema akayafahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, shirika lina mpango wa kuweka business plan ambayo shirika linalo. Plan yao ni ya kuanzia mwaka 2016 hadi 2017 na sasa wanayo plan ya 2017 hadi 2022 ambapo wamejipanga kuwa na Bombardier nne, Airbus tatu, Boeing mbili na pia wamepanga safari za nje na walishaanzisha Entebbe na sasa wanajipanga kwenda Harare, Lusaka, Guangzhou na baadaye wana mpango wa kwenda Kigali, Nairobi, Lubumbashi na London ili kuweza kushiriki kwa karibu sana kwenye biashara ya nje ambayo itatusaidia sana kukuza sekta ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hawa Mchafu ameipongeza Serikali kwa jitihada ambazo zimefanywa. Naamini kwa ambaye anaona, anaona juhudi kubwa sana za Serikali ambazo zimefanywa, miradi mingi imetekelezwa, lakini ushauri alioutoa ni juu ya kuzingatia umuhimu wa kutoa fedha kwa wakati. Kwa bahati nzuri sana Mheshimiwa Waziri amelitolea ufafanuzi na bado Waziri mwenye dhamana, Waziri wa Fedha kaeleza jinsi ya mikakati ambayo anaendelea kulipa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia amepongeza Serikali kwa ununuzi wa ndege na kuanzisha safari za nje. Vile vile amezungumzia masuala ya GN inayosababisha kuchelewa kwa miradi, kwa nini vifaa visipelekwe site mapema. Hili tumelishauri kama Kamati na tunaomba Serikali ilizingatie kwani linachelewesha sana miradi ya maendeleo hasa pale ambapo panahitajika kutoa msamaha wa kodi kwa vifaa vinavyohitaji kwenda kufanya kazi. Tunaomba Serikali ilifanyie kazi kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Mheshimiwa Daniel Nsanzugwanko, amezungumzia sana juu ya umuhimu wa ujenzi wa reli. Kama mnavyofahamu Serikali imeanza kutekeleza miradi ya reli kwa ujenzi wa kiwango cha standard gauge. Reli hiyo imeanza kujengwa Dar es Salaam mpaka Morogoro lakini kipo kipande cha kutoka Morogoro kuja Dodoma. Mipango ya baadaye ya Serikali ni kuhakikisha reli inajengwa kufika Tabora, Tawi la Mwanza na Tawi la Kigoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishauri Serikali kwamba mapendekezo yaliyopendekezwa na Kamati ni vyema yakaangaliwa upya kwani sisi tunaamini kwamba eneo la ukanda wa maziwa ndilo ambalo litakuwa na mzigo mkubwa sana. Kwa hiyo tunaamini Serikali wataangalia na karibu mapendekezo waliyoyatoa yapo kwenye ukurasa wa 31 na Kamati ilishatoa mapendekezo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kazungumzia juu ya ujenzi wa kuimarisha TAZARA. Reli ya TAZARA ni muhimu na kielelezo pekee cha cha urafiki kati ya nchi ya Tanzania na China na ndugu zetu wa Zambia. Tunaomba Serikali ilifanyie kazi kwa haraka sana ili kulinusuru shirika hili kwani bado lina nafasi ya kuweza kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Amon Saul amepongeza Serikali kwa ununuzi wa ndege na imesaidia sana kupunguza ajali za viongozi; tunashukuru na tunapokea pongezi zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa James Mbatia amezungumzia suala la bandari, umuhimu wa watu wetu kupata elimu, weledi katika mataifa mengine; bandari na reli lazima viende sambamba; suala la mizigo mikubwa reli ielekezwe huko ndiko msingi wa kiuchumi. Nami nimepitia na nimeeleza mapendekezo yaliyokuwa yameelezwa na Kamati. Karibu asilimia kubwa ya mapendekezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge mengi ni yaleyale ambayo tumeyatoa kwenye Kamati husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nuru Bafadhil amezungumzia juu ya kuimarisha barabara ya Chalinze kwenda Tanga hadi Kilimanjaro, hasa lile daraja la Mto Wami. Naamini Serikali ilishaanza kulifanyia kazi na tayari sio muda mrefu mkandarasi ataanza kulifanyia kazi eneo lile husika. Pia kashauri juu ya umuhimu wa kuweka taa kwenye Jiji la Dodoma; mapendekezo hayo tunayapokea na tutawaambia Serikali waweze kuyafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Genzabuke amezungumzia reli ya standard gauge, pia amezungumzia juu ya ujenzi wa barabara ya Kibondo mpaka Kakonko. Barabara hizi zipo kwenye mpango na tayari Serikali ilishaanza kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Amina Mollel ametoa pongezi kwa Serikali kufufua TTCL, shirika lijiendeshe kwa faida na wizara na taasisi zilipe madeni; viwanja vya ndege hasa Terminal III itasaidia kuleta wageni wengi toka nje, miundombinu kwa watu wenye ulemavu ni muhimu kuzingatiwa . Naamini Serikali kila inapojenga viwanja huwa inazingatia yale ambayo Mheshimiwa Amina Mollel ameyapendekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni ya ujumla; nitoe pongezi za dhati kwa Serikali kwa kuweza kukubali ushauri wa Wabunge kwa kiwango kikubwa sana. Ndio maana asilimia kubwa, Kamati yangu imepokea pongezi nyingi kwa sababu miradi mingi imetekelezwa. Tunaomba sana Serikali iweze kuzingatia kwenye maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni eneo la bandari. Ili bandari iweze kufanya kazi vizuri na ili bandari iweze kutoa msaada kwenye bandari zingine hasa za maziwa makubwa; Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa ni vyema tukaijengea uwezo. Tunapendekeza Serikali izingatie na kiasi cha asilimia 40 ya mapato yake kiweze kupelekwa bandarini ili iweze kusimamia miradi ambayo ina nafasi kubwa ya kusukuma shughuli za maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iangalie upya sheria hasa hii inayokataza magari ya single custom/ super single. Eneo hili ni vyema Serikali ikalitazama upya kwani tusipoliangalia tutawafanya wafanyabiashara wa nchi za nje wakashindwa kutumia barabara zetu na kukwepa kwenda kufanya shughuli sehemu zingine. Tunaomba hili Serikali tunajua ni sikivu, wataliangalia kwa makini ili waweze kulichunguza na kuufanyia kazi ushauri ambao Wabunge wameutoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali kwa jitihada ambazo wamezifanya na kupokea ushauri wa Wabunge. Mheshimiwa Waziri Mpango amezungumzia mambo ambayo kimsingi yalikuwa yanaleta tabu kidogo hasa kwenye utekelezaji wa miradi. Tunawahimiza ile misamaha ya kodi ambayo kimsingi inaweza ikachelewesha miradi, tunaomba sana waiangalie kwa kina wasipende kuchelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lijualikali amechangia kukwama kwa ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara. Kubwa zaidi ni kuchelewa kwa msamaha wa kodi; tunaomba wahusika wakae pamoja waweze kutekeleza kwa haraka kwani miradi inapochelewa inalifanya Taifa liingie gharama kubwa zisizokuwa stahiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishukuru tena Serikali na tunaahidi sisi kama Kamati kuendelea kuipa support na mawazo ya Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa Kamati tutayafanyia kazi na tutaendelea kuishauri Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naomba kutoa hoja.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MOSHI S. KAKOSO - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya kipekee kupokea michango ya Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia hoja. Wabunge waliochangia wako 16. Kati ya hao, ni Mheshimiwa Julius Kalanga, Mheshimiwa George Lubeleje, Mheshimiwa Bhagwanji Meisuria, Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mheshimiwa Vedastus Manyinyi, Mheshimiwa Deogratias Ngalawa, Mheshimiwa Mbaraka Dau, Mheshimiwa Boniphace Getere, Mheshimiwa Susan Kiwanga na wengineo ambao wanafika 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja za Wabunge waliochangia taarifa hii ni zinazohusu Sekta ya Ujenzi, Sekta ya Uchukuzi na Sekta ya Mawasiliano. Wengi wao wamejikita sana juu ya hoja ya uharibifu wa miundombinu kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imezingatia hili na kufanya majadiliano katika vikao vyake na Wakala wa Barabara (TANROADS) katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya dharura ni shilingi bilioni 8.2, wakati
gharama za kazi za dharura zimekadiriwa kuwa shilingi bilioni 15 na inaweza ikazidi karibu mara mbili ya kiasi kilichokuwa kimetengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeona kuwa fedha za dharura zinazotengwa ni kidogo ukilinganisha na uhitaji uliopo, hivyo kuona haja ya Serikali kufanya mapitio kwa ajili ya kuongeza fedha za dharura ili kusaidia kufanya matengenezo katika maeneo yaliyoathirika na mvua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hili hili la barabara, Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia wanachanganya barabara zinazomilikiwa na TARURA na zile ambazo zinamilikiwa na TANROADS. Hili ni vyema Waheshimiwa Wabunge wakaliangalia na tutakapokuwa tumekaa kwenye vikao vya Bajeti tukajielekeza zaidi kuitengea TARURA uwezo mkubwa ambao wanaweza wakajenga hizo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa barabara nchini umekasimiwa kwa TANROADS na TARURA. Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ina majukumu ya kupanga, kujenga, kukarabati na kutengeneza barabara kuu, barabara za mikoa za Tanzania Bara na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini. Hizi barabara zinazojengwa na TARURA ni kwa ajili ya kuhudumia barabara za mijini na vijijini ambazo haziko chini ya TANROADS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, niliona hili nilieze ili mwangalie zile barabara zinazotugusa ili tujue kwamba tunapochangia zipo barabara ambazo zinamilikiwa na TANROADS ambazo ziko chini yetu na zile ambazo zinamilikiwa na TARURA ambazo ziko Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Kamati imekuwa ikiishauri Serikali iendelee kusisitiza kuwa inaunganisha Miji yote Mikuu na Mikoa iliyosalia kama vile Mikoa ya Katavi - Kigoma, Katavi - Tabora, Kigoma – Kagera, Njombe – Makete, Morogoro, Lindi, Mbeya, Makete – Mbeya na barabara za lami ili kufungua fursa za maendeleo katika maeneo hayo. Aidha, Serikali kukarabati baadhi ya barabara za mikoa zilizo katika hali isiyoridhisha na kutokupitika hasa wakati wa mvua na kuathiri shughuli za kiuchumi na kijamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali kuendeleza ujenzi wa barabara za lami hasa maeneo yanayochochea uchumi wa Taifa letu kama vile maeneo yenye Miradi mikubwa, vivutio vya utalii, kilimo, viwanda na madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, wamezungumzia sana suala la Viwanja vya Ndege hasa Kiwanja cha Ndege ya Musoma ambacho Mheshimiwa Mbunge ameiomba Kamati kwenye mwezi wa Tatu wafike kwenye eneo la Mkoa wa Mara. Katika Bajeti ya mwaka huu 2019/2020 Serikali imetenga fedha za ndani kiasi cha shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya Kiwanja cha Ndege cha Musoma ambacho kitakuwa katika hali ya usanifu na TANROADS ndiyo watakaojenga na wako katika hatua ya kukamilisha maandalizi ya tender kwa ajili ya ukarabati wa kiwanja hicho. Kazi za ukarabati zinatarajiwa kuanza kufanyika mwaka ujao wa fedha wa 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia suala la kuchelewa kwa mizigo na meli kukaa kwa muda mrefu bandarini. Wabunge wengi wamelizungumzia hili. Hii ni kutokana na ucheleweshaji wa mzigo unaokuja kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Tumeshaishauri Serikali iangalie uwezekano wa kukaa na wadau ili waweze kutoa hili tatizo, kwani kutokufanya hivyo vipo viashiria vikubwa ambavyo vitakimbiza Wafanyabiashara waache kuitumia Bandari ya Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Tanzania ni nchi iliyobarikiwa, kwani kijografia hasa katika usafiri wa usafirishaji wa majini na nchi kavu kwani tumepakana na nchi takribani tisa ambazo zinategemea kupitisha mizigo na malighafi. Kamati imeendelea kuishauri Serikali mara kwa mara; pamoja na kuwa katika mazingira mazuri ya kijografia ni muhimu sana kupunguza urasimu na vikwazo mbalimbali ambavyo vinasababisha Wafanyabiashara kuhama kutumia Bandari yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo changamoto ambapo na Serikali wamezizungumzia kwamba zipo changamoto kiasi ambazo ni za mawasiliano hasa maeneo ya mipakani. Ni kweli kumekuwepo na changamoto za wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kukosa huduma ya mawasiliano au wakati mwingine kupata huduma ya mawasiliano toka nchi jirani, jambo ambalo siyo sawa na ni hatari kwa usalama wa nchi. Hivyo, Kamati imeendelea kutoa ushauri wa kuishauri Serikali kusimamia jambo hili liweze kufanyiwa maboresho ya maeneo ya mipakani na ikiwezekana kuweka minara yenye nguvu ambayo itawezesha kupata mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo michango ya Mbunge mmoja mmoja, siyo rahisi kuipitia yote, lakini kuna baadhi ya maeneo ambayo naweza nikagusa. Mheshimiwa Dau Mbaraka ametoa pongezi za ujenzi wa gati lakini ameelezea juu ya umuhimu wa kujenga boti mpya ya kisasa itakayotoa huduma kwenye eneo la bahari ya hindi kwenda eneo la Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishaanza kulifanyia kazi. Kwa sasa inaendelea na ujenzi wa boti ambayo itatoa huduma kwenye maeneo hayo, lakini amezungumzia suala la minara penye maeneo ya Mafia. Tunavyozungumza hivi, kesho kutakuwa na uzinduzi wa minara kwenye eneo la Mafia. Hivyo, Serikali ilishasikia ombi lake na sisi kama Kamati tumekuwa tukisimamia Mfuko huu ili uweze kutoa maboresho kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la maboresho ya Viwanja vya Ndege, Kamati imeendelea kutoa ushauri wa kuielekeza Serikali hasa kwenye Viwanja vya Ndege vya Mwanza, Mbeya, Songwe na Dodoma. Eneo hili ni muhimu sana ili kufanya maboresho ya viwanja hivi vya ndege. Viwanja hivi vinatumiwa na Watanzania walio wengi na Kiwanja cha Mwanza kinategemewa kuwa Kiwanja ambacho kitakuwa hub ya kutumika kwenye maeneo ya Afrika Mashariki. Hivyo, tunahitaji Kiwanja kile kifanyiwe ukarabati hasa kujenga Jengo la Abiria na kuweka wigo kwenye maeneo ambayo wananchi wanakatisha kwenye viwanja hivyo vya ndege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji mwingine amezungumzia juu ya umuhimu wa kuboresha reli ya TAZARA. Reli hii ni muhimu sana katika nchi yetu na ni ya kihistoria ambayo imeelekeza wazi kwamba ilikuwa ya uhusiano kati ya nchi mbili ya Zambia na Tanzania na rafiki wa karibu, nchi ya China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, reli hii ina changamoto, hivyo tumeishauri Serikali kuhakikisha wanakaa pamoja kati ya Serikali ya Zambia na Serikali ya Tanzania ili kupitia mapitio ya sheria ya kuweka mazingira mazuri yatakayoifanya reli hii iweze kutumika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye suala la Reli ya TAZARA ni umuhimu wa kulipa wafanyakazi waliokuwa wanaidai Serikali. Tunaipongeza Serikali, imelipa fedha nyingi kwa wafanyakazi na wanaendelea kulipa wafanyakazi mishahara, lakini bado kuna baadhi ya Watanzania wenzetu ambao wanadai Shirika hili. Hivyo, tunaomba Serikali ipitie na kuangalia umuhimu wa kuwalipa wale wafanyakazi ili kutoa motisha kwa wale wengine waliobaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wapo wachangiaji ambao Mheshimiwa Mwakajoka ameelezea kwa nini suala la miundombinu wanapewa fedha nyingi kwa ajili ya Bajeti? Ni ukweli usiopingika, miundombinu inapewa fedha nyingi kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano imetekeleza miradi mingi karibu kila mkoa, hakuna sehemu ambako hakujaonekana mradi ambao unafanyiwa kazi na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye maeneo tu ya Mkoa wa Songwe ipo barabara inayojengwa kutoka eneo la Mloo kwenda Kilyamatundu mpaka Mkoa wa Katavi. Hiyo barabara ni muhimu sana kwa maendeleo, lakini kuna ukarabati wa barabara ya kutoka Mbeya kwenda Tunduma, hizo ni kazi zinazofanywa na Serikali sambasamba na ujenzi ule wa Songwe ambao utawanufaisha sana wananchi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kusafirisha mizigo na kutoa fursa mpya ya usafirishaji wa zao la matunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mengi ambayo yametekelezwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ikiyafanya. Tunawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote walioipongeza Kamati, Serikali kwa kazi ambayo imefanyika na juhudi ambazo zimefanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Kamati hii na ninawashukuru sana Wabunge wote waliotoa mchango wao tunawaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha tunafanya maboresho. Tunawapongeza Manaibu Waziri ambao kimsingi wameungana na Kamati na kukubali yale ambayo tumeshauriana nao. Hivyo naamini tukiwa pamoja tutafanya kazi ambayo haitakuwa ngumu na itakuwa na manufaa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawashukuruni sana, naunga mkono hoja. (Makofi)

MWENYEKITI: Toa hoja Mheshimiwa.

MHE. MOSHI S. KAKOSO - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. MOSHI S. KAKOSO – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nawashukuru sana wachangiaji wote ambapo wamebahatika kuchangia hoja ya Kamati ya Bunge ya Miundombinu. Tumepata wachangiaji 16 wakiwemo na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Waziri, ambao wametoa hoja na ufafanuzi wa jinsi gani utekelezaji watakavyoufanya na ulivyotekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati inazingatia yale ambayo Serikali ilikuja ikayaleta mbele ya Kamati na wakati huohuo, ushauri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Mheshimiwa Anne Kilango amezungumzia suala la Miradi ya Maendeleo iliyoletwa na Serikali ya barabara na Miradi ya Maendeleo ya upanuzi wa bandari.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hii imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wamezungumzia juu ya tatizo la barabara. Kwenye eneo la barabara, TANROADS imezidiwa, uhalisia jisi ulivyo, ili barabara za kwetu ziweze kuimarika na ziweze kufanya kazi, TANROADS inahitaji ipatiwe na Serikali bajeti isiyopungua shilingi trilioni tatu kwa ajili ya kujenga Miundombinu na kuimarisha barabara ambazo zilishatangazwa kwa ajili ya kuendeleza miradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi ambao walikuwa na hamu kubwa ya kuangalia barabara zao zilizoahidiwa mbele ya Bunge Tukufu, asilimia kubwa hawajapata barabara zinazojengwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali kuhakikisha kile ambacho kilipitishwa na Bunge kinafanyiwa kazi; lakini tuna tatizo la Mfuko wa Barabara ambao hauna fedha za kukidhi mahitaji. Mfuko wa Barabara uwezo wake kwa sasa unakusanya shilingi bilioni 850, kati ya hizo fedha, zinazoenda moja kwa moja kwenye miradi ya matengenezo ya barabara ni shilingi bilioni 600 ndio zinazoenda kwenye upande wa TANROADS.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji halisi ya barabara zilizoharibika hapa nchini, zinahitaji matengenezo ya shilingi trilioni mbili. Kwa hiyo, kwa ujumla, Wizara ya Ujenzi ili tuweze kwenda vizuri, tuna uhitaji wa shilingi trilioni tano kwa ajili ya matengenezo ya miradi ya barabara mipya na iliyoanzishwa na Serikali na shilingi trilioni mbili ni kwa ajili ya matengenezo ya barabara ambazo zimeharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingi nchini zilishapitwa na wakati na mfano wametolea Waheshimiwa Wabunge, barabara ya kutoka Dodoma – Iringa, ile barabara ilishakwisha, barabara ya kutoka Morogoro – Dodoma, barabara hii nayo ilishapitwa na wakati, muda wake umeskwisha, hali kadhalika, Barabara ya kutoka Chalinze – Kilimanjaro, Kilimanjaro – Arusha, hizi zote zilishakwisha muda wake. Tunayo barabara ya kutoka eneo la Makambako – Songea, tuna barabara ya kutoka Dar es Salaam – Mtwara, hizi barabara zote zinahitaji matengenezo makubwa sana. Eneo hili, tunaishauri Serikali, kwenye Mpango wa Bajeti waje na Bajeti ambayo itahimili matengenezo ya barabara hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia kwa kina, ni suala la kushindwa kuwalipa wakandarasi kwa muda. Eneo hili, Serikali inapata hasara kubwa sana kwa sababu tunaweka Wakandarasi, wanashindwa kuwalipa kwa wakati na badala yake sasa kunaingia riba ambazo zinakuja kuwalipa Wakandarasi ambazo zinafanya gharama ya barabara kuwa kubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba Serikali kupitia Wizara, izingatie na waangalie hili kwamba ni suala muhimu sana ili tunapokuja kwenye mwaka wa fedha, tuje na bajeti ambayo itahimili kuweza kukamilisha hii miradi iliyotajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni fidia za barabara, kwenye Wizara ya Ujenzi nchi nzima Serikali imeweka alama za barabarani ambazo wananchi wanahitaji wapishe miradi. Bahati mbaya sana wapo watu ambao wamewekewa alama za kupisha miradi hiyo zaidi ya miaka kumi wana matumaini ya kuendelea kupata fidia. Kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge kwa ripoti za Wizara, zaidi ya shilingi trilioni saba zinahitaji kulipa fidia kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wa Kamati, tunaishairu Serikali maeneo ambayo wanayaona hawana uwezo wa kuweza kuwalipa fidia na miradi ile haitaweza kwenda kwa wakati, wawaruhusu wananchi waendeleze maeneo yao kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi kwa Wizara ya Ujenzi, tunaiomba izingatie mfumo wa Waheshimiwa Wabunge ambao wanaishauri Serikali. Ili tuweze kwenda vizuri wizara ijipange vizuri kwa ajili ya bajeti ijayo angalau ifikie hizo trilioni tano. Trilioni mbili kwa ajili ya matengenezo ya barabara na trilioni tatu kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunaipongeza Serikali kwa jitihada ni kwenye Taasisi ya TBA; TBA wameanza sasa kukusanya madeni yao, madeni ambayo asilimia kubwa wapangaji wamekuwa wakiishi kama nyumba za kwao binafsi ambazo haziitaji kulipa kodi. Walipoanza jitihada za kuwadai wananchi, zimekuwa na tija kidogo. kwa bahati mbaya taasisi za Serikali, watumishi wa Serikali ambao wanakaa kwenye nyumba za TBA bado hawajalipa hizo kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba ule mfano uliotolewa kwa sababu na Waheshimiwa Wabunge wametolewa kwenye hizo nyumba tunaomba na taasisi zile za Serikali wafanye kama walivyofanya kwa Waheshimiwa Wabunge. Hili litasaidia TBA iweze kukaa vizuri na ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa jitihada ambazo amezifanya. Tunaomba nguvu uliyoitumia kutoka kuwatoa Waheshimiwa Wabunge na wengineo kawaondoeni na watumishi wa Serikali ambao hawajalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu sekta ya uchukuzi; tunaipongeza Serikali, tunajua jitihada zipo kubwa sana zimefanywa na Serikali kwenye miradi ya maendeleo. Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia sana suala la kuiwezesha TPA ili iweze kuwa na nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, duniani kote wharfage wanalipwa mamlaka husika ya bandari. Sisi tunakusanya hela zote tunazipeleka Serikali Kuu, na wakati huo huo tunapoanza kujenga miradi ya maendeleo tunaenda kuomba. TPA ina uwezo wa kutengeneza fedha nyingi sana endapo kutakuwa na utashi. Tunaomba na kuishauri Serikali Mheshimiwa Waziri anapokuja mwakani kwenye bajeti yake, awaachie TPA waweze kujenga gati kwa kujitegemea wao. Wana nafasi, tumewasikiliza tumewaelewa na tumefananisha na nchi zingine ambavyo wanafanya. TPA wana nafasi ya kuweza kujenga gati kuanzia ile gati sifuri wakawa na gati tano ambazo wanaweza wakajenga kwa nguvu za kutumia nafasi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeishauri Serikali angalau mapato ya wharfage watoe kila mwezi waachie shilingi bilioni 35 ambazo zitawafanya waweze kujenga na watumie taasisi za fedha wajenge wao wenyewe; na zile fedha zitakuja kuleta return kubwa sana kwa Serikali kwa sababu gati moja ina nafasi ya kuweza kuzaisha bilioni 600. Kwa hiyo mkiwa na gati takriban tano zimejengwa Serikali itapata fedha nyingi sana kama mapato ya kodi pamoja na mapato ya ushuru wa gati yenyewe; kwa sababu tutakuwa tayari tumetengeneza mifumo sahihi. Naomba Serikali waliangalie hili kwa sababu ukitaka kumkamua ngombe aweze kuzalisha vizuri ni lazima umpe malisho ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la sekta ya uchukuzi, kuhusu Mradi wa SGR. Tunaipongeza Serikali, imejenga miradi mikubwa wa SGR kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma – Tabora – Isaka – Mwanza. Leo hii tena tumeanza mradi mkubwa wa kutoka Tabora – Kigoma na lile tawi la kutoka Msongati kwenda eneo la nchi ya Burundi. Tunaishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuanzisha miradi hii. Tunaiomba Wizara iweke usimamizi mkubwa wa miradi imechukua muda mrefu sana kukamilika. Mradi unapochelewa kuchukua muda wa kukamilika tuliokubaliana nao kati ya Serikali na wajenzi inaifanya Serikali kutumia gharama kubwa za ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hili mlifanyie kazi na Serikali kupitia Wizara husika iwasimamie wakandarasi na wapunguze tatizo lililopo, hasa kwenye kampuni inayojenga reli kutoka Dar es Salaam – Morogoro – Dodoma – Tabora wahakikishe haki za watanzania wanaofanya kazi walipwe na kusiwe na malalamiko ya mara kwa mara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya uwanja wa ndege. Viwanja vya ndege vinasimamiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kupitia Serikali. Tunaomba miradi hii iweze kusimamiwa ipasavyo na wakandarasi wale ambao wanadai waweze kulipwa haki na stahiki zao kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Kampuni ya Meli (MSCL). Kampuni hii imejenga meli, meli zile ambazo zinajengwa na Serikali; na tunaipongeza Serikali kwa jitihada ambazo zinafanywa za mara kwa mara za kuinusuru kampuni ambayo ilikuwa ilishakufa kabisa lakini Serikali tumeona nguvu yake iliyofanya; sasa tunaomba muwasimamie ile miradi ambayo imepitishwa na Serikali tuhakikishe inafanyiwa kazi ili kampuni ile iweze kusimama. Muda wote inategemea kupata ruzuku kutoka Serikalini. Tunaomba Serikali itoe fedha ya kutosha, wakamilishe ili ile kampuni iweze kusimama na ijitegemee yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa Ziwa Tanganyika tuna miradi ya maendeleo ya ujenzi wa meli mpya, ya ukarabati wa meli ya MV Liemba na MV Mwongozo. Tunaomba jitihada za Serikali zifanyike haraka kuhakikisha lile ziwa nalo linapata uhalali wa kutumika vizuri kama maziwa mengine yalivyopewa miradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, tunao Mradi wa Mkongo wa Taifa. Mkongo wa Taifa kwa sasa ni eneo ambalo Serikali wanaweza wakapata fedha za kiuchumi. Bahati mbaya sana, bado kuna maeneo ambayo hayajawekewa uzito mkubwa sana. Kamati imeshauri mradi wa kuunganisha Mkongo wa Taifa na nchi ya DRC Congo uharakishwe kwa sababu eneo hilo tukilishika tutakuwa tumetengezeza fedha ambazo Serikali itanufaika kama ambavyo sasa hivi Serikali wanapata fedha kupitia nchi ya Rwanda; wanalipwa kwa ajili ya uwekezaji wa Mkongo wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala la miradi ya minara ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi walifurahia sana kupata minara 758. Mpaka sasa minara iliyokamilika ni minara 15 tu. Kasi ya uendelezaji wa ujenzi wa minara ni ndogo. Tunaishauri Serikali ikasimamie kuhakikisha minara yote ambayo iliwekewa mpango mkakati kwa mwaka wa fedha unaoisha sasa iweze kukamilika, na tunapokuja kwenye bajeti ijayo Serikali iwe na majibu ya msingi ya kutueleza nini kimefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu TCRA tunaishauri TCRA kuhakikisha wawe wabunifu ili waweze kukabiliana na changamoto ambazo zipo kwenye teknolojia ya mitandao, kwani kila siku kuna mabadiliko na watu wanafanya ufundi wa kila siku kuhakikisha nchi wanaiweka katika mazingira ambayo ni tofauti. Tunawapongeza, wamefanya jitihada sana kupitia Serikali. Maeneo ambayo wengi wametetereka kwa ku-attack mitandao kwa Tanzania tumekuwa salama hasa kwenye mifumo ile ya kifedha. Tunaomba jitihada zile ziendelee kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kuna tatizo kati ya Serikali na TCRA na watu wanaomiliki mitandao wahakikishe yale ambayo ni maudhui ya Kitanzania yaweze kuwepo, na mfumo ule wa kupeleka vitu ambavyo vinaleta uchochezi na taharuki kwa nchi. Hivyo viweze kutolewa ili kuhakikisha nchi inakuwa salama.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze Mawaziri kwa majibu ambayo wameyatoa tunaomba wakaongeze kasi kuhakikisha miradi ile ambayo Watanzania wanaitegemea iweze kufanya kazi na Watanzania wote waweze kunufaika. Kuhusiana na miradi ya barabara, naleta msisitizo mkubwa sana kwamba huko ndiko kwenye siasa ya nchi yetu. Tunajua kwamba nchi inapita katika kipindi kigumu barabara zimekuwa mbovu kwa sababu ya hali ya hewa. Hata hivyo, kama Serikali mkisimama vizuri mkashirikiana na Waheshimiwa Wabunge na mkachukua mawazo ya Waheshimiwa Wabunge mnaweza kufika kabisa kwenye mazingira ambayo ni sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ninawashukuru sana Wabunge wote ambao wametoa mchango wao. Ninaamini mchango wenu utakuwa ni kumbukumbu sahihi na utakaotoa dira kwa Serikali kuweza kuyafanyia kazi mawazo ya Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.

MHE. INNOCENT E. KALOGERIS: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia Wizara hii. Awali ya yote, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo kaitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye suala la pembejeo. Pembejeo zenye ruzuku ya Serikali ni tatizo kubwa sana. Mkoa wa Katavi ulipokea pembejeo ambazo zilikuwa na gharama kubwa kuzidi hata zile zinazouzwa kwenye maduka binafsi. Ni jambo la kushangaza sana kwamba pembejeo zenye ruzuku ya Serikali zinakuwa na gharama kubwa kuliko hata zile zinazotolewa na Serikali. Naomba Mheshimiwa Waziri alifuatilie hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kwenye suala zima la masoko, tuna tatizo la masoko hasa ya mazao ya chakula kwa maana ya mahindi na mpunga. Mazao haya yanazalishwa kwa wingi sana kwenye maeneo ya Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.
Tulikuwa tunaiomba Serikali iandae mazingira ya kuwasaidia wakulima hawa wadogo wadogo ili waweze kupata nguvu ya uzalishaji mkubwa pale wanapokuwa na masoko mazuri ya mazao yao. Tunaiomba Serikali ifuatilie na iangalie mazingira ya kuaandaa viwanda vidogo vya usindikaji kwa ajili ya mazao ambayo yatasaidia sana kutengeneza mazingira ya kuwapa masoko wakulima wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni miradi ya umwagiliaji. Tuna miradi ya umwagiliaji ambayo ilianzishwa na Serikali; upo mradi wa scheme ya Karema ambapo Serikali imetoa fedha nyingi lakini imeshindwa kukamilisha huu mradi ambao sasa unaharibika kwa sababu umechukua muda mrefu na kusababisha hasara. Tunaomba miradi ile ambayo Serikali imeanzisha iweze kutekelezwa kwa haraka ili kusaidia wananchi hasa katika shughuli za uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huo wa Karema una fedha nyingi, lakini tunao mradi wa Mwamkulu na Iloba na miradi yote hii bado haijakamilika. Tunaomba Serikali iangalie na itume fedha ili hii miradi iweze kukamilika na isije ikachukuliwa kwamba kila mradi unaoshindikana kukamilika, wale ambao ni wasimamizi wanachukuliwa hatua; kumbe tatizo kubwa sana ni ukosefu wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la uvuvi. Mkoa wa Katavi tunalo eneo la uzalishaji hasa kwa wavuvi wetu wa Ziwa Tanganyika. Wavuvi hawa wanafanya uvuvi ambao ni wa kienyeji. Tunaiomba sana Serikali iweze kuangalia mazingira ya kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo. Serikali ilishatengeneza mazingira mazuri, ikajenga mwalo pale eneo la Ikola, lakini ule mwalo hautakuwa na thamani kama haujawezesha wale wavuvi wadogo wadogo. Nilikuwa naomba Serikali kupitia Wizara iwawezeshe wavuvi wadogo wadogo, wapatiwe mitaji na kuwapa zana za kisasa. Tutakapowasaidia wavuvi hawa tutakuwa tumesaidia mazingira ya kukuza uchumi kwenye maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna uvuvi haramu ambapo kuna nyavu zinazotoka nchi jirani ya Burundi, zile nyavu ni hatari sana kwa wavuvi na kwa usalama wa Ziwa Tanganyika.
Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie na iweke mikakati ya kuzuia nyavu haramu ambazo zikikatikia kwenye eneo la ziwa, zile nyavu zinaendelea kuua mazao yanayotokana na ziwa lile kwa sababu zile nyavu hazifai kwa matumizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la zao la tumbaku. Zao la hili lina changamoto kubwa sana. Naiomba Serikali itafute soko lenye uhakika la kuwasaidia wakulima wa zao la tumbaku nchini. Serikali imejitahidi kutafuta masoko, lakini bado kuna matatizo ambayo wanayafanya Serikali kama Serikali. Unapoenda kutafuta soko, ukayashirikisha makampuni ambayo yananunua hapa hapa nchini, hujafanya kitu chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itafute soko liwasaidie wakulima. Unapowabeba hawa wafanyabiashara ambao ndio wanaowanyonya wakulima, unaenda nao kutafuta soko, hujawasaidia, kwa sababu bado unatengeneza mazingira ya kubana lile soko ambalo linahitajika kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna eneo ambalo tunahitaji Serikali iingilie kati. Kuna utitiri wa fedha zinazotozwa mkulima. Tunaomba zile tozo ambazo zinamfanya mkulima akose bei nzuri ziangaliwe upya na ziweze kukokotolewa ili ziweze kuwasaidia. Ni pamoja na zile kodi za Halmashauri ya Wilaya, kuna asilimia tano ambayo sasa hivi inatozwa, tunaomba itozwe asilimia mbili na Halmashauri ibaki na asilimia tatu, nyingine ziwarudie wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la mabenki, mkulima anatwishwa mzigo mkubwa sana kwa sababu ya riba kubwa sana za mabenki. Naiomba Wizara iangalie kwa karibu sana kusaida kupunguza riba ili mkulima awe na mzigo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye zao la tumbaku tunahitaji mwangalie umuhimu wa kuajiri ma-classifier. Bila kuwa na classifier hatuwezi kuwasaidia wakulima wa zao la tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mifugo. Eneo langu lina wafugaji wengi sana na tunaomba sana muwasaidie wafugaji kwa kuwatengea maeneo. Tukitenga maeneo tutakuwa tumewasaidia wakulima/wafugaji na tunaepusha migogoro ambayo haina ulazima. Ipo haja ya kutenga maeneo na kuweza kuangalia umuhimu wa kuwapa wakulima wamiliki ardhi na wafugaji wawe na maeneo yao ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara kati ya wakulima na wafugaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuwajengee mazingira ya kuwakopesha hawa wafugaji ili na wao wafuge kisasa. Hiyo ni pamoja na kuwapelekea huduma zile za dawa, majosho na kadhalika ili viweze kuwasaidia na waache ufugaji wa kuhamahama. Wafugaji wanafuata malisho, ndiyo maana wanatembea kila eneo, lakini kama tutawajengea miundombinu kwenye maeneo yao, hawatakuwa na ufugaji wa kuhamahama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye suala la ushirika. Kwenye eneo la ushirika bado tumewasahau kwenye Idara hii. Kwanza Bunge lililopita tuliazimia kwamba watakuwa na Kamisheni ya Mfuko utakaokuwa unashughulikia suala zima la ushirika. Tunapouwezesha Ushirika ndiyo tunafanya sasa wapate kuwa na uwezo wa kukagua. Leo hii ukifika kwenye Idara ya Ushirika, hawana nafasi ya kufanya jambo lolote lile kwa sababu hawana fedha za kuendesha shughuli zao.
Tunaomba mpeleke fedha kwenye Idara ili zikaimarishe Mfuko wa Ukaguzi, ni pamoja na kusaidia Shirika la COASCO ambalo linakagua ukaguzi wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri mwenye dhamana aangalie maeneo haya ili aweze kusaidia shughuli za kilimo kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kunipa nafasi hii na mimi kuwa ni sehemu ya wachangiaji. Niwashukuru Mawaziri ambao wamewasilisha hotuba zao nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwenye suala zima la elimu. Eneo la elimu kwenye Jimbo la Mpanda Vijijini bado kuna changamoto kubwa sana. Zipo shule ambazo zimejengwa toka enzi za ukoloni, zimechakaa kwa kiwango kikubwa sana, tulikuwa tunahitaji katika bajeti hii Serikali iangalie mazingira ya kuziboresha zile shule ambazo zimechakaa kwa kiwango kikubwa sana.
Katika Tarafa ya Mwese kuna shule ya Lugonesi na Mwese, shule hizi zimejengwa toka kipindi cha wakimbizi wa Rwanda. Kwa hiyo, shule hizi zimechakaa, tulikuwa tunaomba Serikali iangalie jinsi ya kuzijenga upya ili ziweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi na watoto wetu waweze kupata elimu iliyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo shule ambazo zinahitaji kuboreshwa, shule hizo ni za sekondari. Tunazo shule za sekondari kwenye Jimbo la Mpanda Vijijini saba, bado zina uhitaji mkubwa sana wa walimu. Sambamba na kwenye shule za msingi ambako kunahitajika idadi ya kutosha ya walimu ili shule hizo zitoe elimu inayofanana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo maeneo mengine mapya ya kiutawala, tunalo eneo la Mishamo ambalo raia wapya wamepata uraia. Eneo hili lina changamoto kubwa sana kwani idadi ya watu ni wengi lakini bado tunahitaji huduma za kijamii hasa kwenye suala la elimu. Tunaomba Serikali iangalie kwa kina yale maeneo ambayo yalisahaulika kupata huduma za kimsingi ambazo huko nyuma zilikuwa zinatolewa na UN kwa sasa zinategemewa sana kutolewa na Serikali yetu. Naomba Waziri mwenye dhamana aelekeze nguvu, aende akaone mazingira ambayo vijana wanasoma, shule moja inachukua idadi ya wanafunzi karibu 1,800 na darasa moja unakuta lina wanafunzi zaidi ya watoto 100, tunaomba eneo hilo mliangalie sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni maji. Jimbo langu lina tatizo sana la maji kwenye vijiji vingi. Kipo kijiji cha Kamjelam ambacho kiko eneo la Mishamo, hakuna maji. Tunahitaji eneo hili kwa ujumla kwenye Kata za Bulamata, Mishamo, Ilangu na Ipwaga, wajaribu kufufua visima ambavyo vilikuwa vimechimbwa na UN kipindi hicho cha nyuma. Serikali ione umuhimu sasa wa kuangalia vile visima ili viweze kutoa maji na wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni barabara za vijijini. Maeneo ya Jimbo la Mpanda Vijijini yana vijiji vingi sana ambavyo havipitiki kwa sababu barabara zake si nzuri. Tulikuwa tunaomba Serikali iweze kuongeza bajeti hasa kwenye Wilaya ya Mpanda ambayo kimsingi ndio imezaa Halmashauri zote ambazo zimezaliwa katika Mkoa wa Katavi.
Kwa hiyo, tunaomba waelekeze nguvu kujenga miundombinu ambako kuna uzalishaji mkubwa sana wa mazao ya mahindi na mpunga, yanayotegemewa kuchukuliwa kutoka vijijini kuyaleta makao makuu ya Wilaya na mkoa na baadaye sehemu ya Mikoa ya Mwanza Shinyanga wanakuja kununua mazao hayo. Sasa ili kuweza kuboresha na wakulima waweze kunufaika, tulikuwa tunaiomba Serikali iboreshe barabara za kijiji cha Kabage kuja barabara kuu inayounganisha kutoka Kagwila - Karema. Iboreshe barabara za kutoka Kalilankurukuru kwenda kijiji cha Kamsanga na iboreshe barabara za kwenda kijiji cha Mnyagala ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mazao. Ili wananchi waweze kuzalisha na wapate bei nzuri lazima Serikali iboreshe barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara nyingine ambazo zinahitaji kufanyiwa urekebishwaji kwa kiwango kikubwa ni maeneo ya vijiji vya Mishamo ambako barabara nyingi zimeharibika. Tunaomba Serikali iweze kusaidia iweze kufanya kazi nzuri na iweze kutoa huduma nzuri kwa ajili ya kupita ili wananchi waweze kuzalisha mazao yao na yapate nafasi ya kupelekwa kwenye masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutaiachia tu Halmashauri ya Wilaya kwamba ndiyo itaweza kusaidia hizo barabara, itakuwa ni jambo gumu kwa sababu eneo la Wilaya ya Mpanda ni kubwa na ukubwa wa Jimbo umekuwa mkubwa sana tofauti kabisa na maeneo mengine. Jimbo la Mpanda Vijijini ni jimbo ambalo lina uwezo wa kuchukua Mkoa mzima wa Kilimanjaro, ukachukua na sehemu ya Zanzibar, ukiunganisha unapata Jimbo ambalo naliongoza mimi. Lina kilometa za mraba 16,900 kitu ambacho kuwafikia wananchi inakuwa ni taabu. Naomba Serikali iangalie ukubwa wa Jimbo hili ili liweze kugawanywa na wakati mwingine kutoa huduma zinazofanana ili tuweze kuwafikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwenye suala la afya. Eneo la afya Mheshimiwa Anna Lupembe amezungumzia sana na mimi nalitilia mkazo wa aina yake kwa sababu eneo hili ni muhimu sana. Kwanza, hatuna vifaa vya kuwafikia wananchi kwa maana vituo vya afya havina ambulance. Halmashauri hii ilipokuwa inatoa mgawanyo kwa Halmashauri zingine, kila Halmashauri iliyokuwa inazaliwa walikuwa wanatoa magari kutoka Halmashauri mama kuyapeleka kwenye maeneo ya Halmashauri zingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Halmashauri Mama kwa maana ya Wilaya ya Mpanda bado haina vitendea kazi kwa maana ya magaari. Ukienda kwenye sekta ya elimu hawana magari, sekta ya afya na vituo vya afya havina magari. Naiomba Serikali iangalie umuhimu wa kununua ambulance kwa ajili ya Halmashauri ya Mpanda ambayo itasaidia kutoa huduma kwenye vituo vya afya vya Mishamo, Mwese na Karema. Idadi ya wananchi walio wengi hasa akina mama wajawazito wanapoteza maisha yao kwa sababu ya umbali wa kufikia huduma ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho tunaomba Serikali iangalie kwenye sekta ya afya, itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kujenga Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Ni eneo pekee ambalo kiutawala halijakuwa na Hospitali ya Mkoa. Bado wanatumia Hospitali ya Halmashuri ya Wilaya ya Mpanda kama Hospitali ya Wilaya na Mkoa kwa ujumla. Kwa hiyo, tunaomba Serikali iangalie umuhimu wa kuweka mkakati wa kutoa fedha za kutosha ili kujenga Hospitali ya Mkoa itakayotoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, niishukuru Serikali kwa namna nyingine kwa kutupa Wilaya mpya ya Tanganyika. Bado Wilaya hii ya Tanganyika haijapata makao makuu yake. Niiombe Serikali iangalie mazingira ya kuweza kuharakisha mchakato wa kupeleka makao makuu hasa pale yalipokuwa yamelengwa na Waheshimiwa Madiwani walipokuwa wamependekeza. Ni vizuri Serikali itakapokuwa imepeleka huduma hiyo na mchakato wa Halmashauri kwa ujumla ukafanyika mapema utasaidia kupeleka maendeleo kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kunipa nafasi hii. Nianze mchango wangu kwa kuchangia kuhusu Shirika la Reli. Ili nchi iweze kuendelea inahitaji kuwa na miundombinu ya reli. Shirika letu la Reli linahitaji kufanyiwa mabadiliko hasa ya kisheria. Tayari Serikali ilileta mabadiliko ambapo RAHCO ilitenganishwa na TRL. Niiombe na kuishauri Serikali ni vizuri ikaleta sheria hapa Bungeni shirika hili liunganishwe liwe kitu kimoja ili liweze kuwa na ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto nyingi sana ambazo zimejitokeza kwenye Shirika la Reli. Ni vyema Serikali ikapata ushauri wa Wabunge ikaangalia umuhimu wa kuliunganisha ili liweze kufanya kazi vizuri. Litakapokuwa limeunganishwa litaisaidia nchi na wananchi walio wengi watanufaika na utekelezaji wa sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali wamekuja na mpango wa kujenga reli ya kati. Ujenzi wa reli ya kati tunahitaji Serikali ifanye mchakato haraka ili iweze kutengenezwa reli ambayo itawasaidia wananchi. Naomba Serikali iharakishe na iangalie kwenye maeneo ambayo yana umuhimu wa uwekezaji. Serikali itakapokuwa imejenga reli kuanzia Dar es Salaam - Tabora - Mwanza iangalie umuhimu sana wa kufikisha reli hii kutoka Tabora - Kigoma na tawi lake la kutoka Uvinza - Msongati. Pia tunahitaji reli hii itoke Kaliua - Mpanda - Karema kwa ajili ya uwekezaji. Ni vizuri Serikali ikaangalia umuhimu wa kuijenga hii reli kwa haraka ili iweze kutoa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine la pili ni suala la bandari. Bandari ndiyo lango kuu la uchumi wa nchi yetu. Bandari ya Dar es Salaam inahitaji kufanyiwa marekebisho kwenye maeneo hasa ya himaya ya pamoja ya forodha (single custom). Eneo hili ni muhimu sana kufanyiwa mabadiliko ya haraka kwani inalazimu kodi kwa mizigo ya nchi jirani kutozwa hapa nchini kabla ya mizigo hiyo haijatozwa nchini mwao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba na kuishauri Serikali iachane na mpango huu kwa sababu unawafukuza wafanyabiashara wa nchi jirani. Sheria hii inawafanya wafanyabiashara wakimbilie kupeleka mizingo kwenye bandari ya Mombasa, Durban na Msumbiji. Tunaiomba Serikali ifuate ushauri ili iweze kusaidia kutoa tatizo la kukimbia kwa wafanyabiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni warehouse rent ambayo inatozwa mara mbili, inatozwa na Bandari na TRA. Tunaomba Serikali iangalie suala hili na Mheshimiwa Waziri na timu yake tunaamini wana uelewa wa kutosha ili waweze kutoa hivi vitu ambavyo vinafanya kuwe na mgongano wa kimaslahi na kuwafanya wafanyabiashara wakimbie bandari yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba Serikali iboreshe bandari ambazo zipo mikoani, Mkoa wa Mwanza, Iringa kwa maana ya kule Njombe, maeneo ya Kyela, maeneo ya Ziwa Tanganyika kwa maana ya bandari ya Kigoma na Karema. Tunahitaji bandari hizi ziweze kuboreshwa ili ziweze kutoa huduma kwenye maziwa makuu, Ziwa Victoria na Tanganyika. Tukifanya ujenzi wa bandari na kuboresha hizo bandari, zitatoa uchumi mzuri kwenye maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na maboresho ya bandari kwenye Mikoa ya Mwanza, Kigoma, Katavi, Mbeya kwa upande wa Kyela na kule Njombe maeneo ya Ziwa Nyasa, bado tunahitaji kuunganisha Bandari na Marine kwani zikiunganishwa zitafanya kazi pamoja kuliko ilivyo sasa hivi. Marine service haina uwezo wa ku-operate meli ambazo zipo kwenye maeneo husika. Tunaomba Serikali iangalie maeneo haya ili kufanya maboresho yatakayosaidia kukuza uchumi na kutoa ufanisi kwa hivi vyombo viwili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizugumzie suala la barabara. Serikali ina dhamira ya dhati kuunganisha mikoa yote nchini kwa barabara za lami. Niiombe Serikali iangalie umuhimu sana wa kuunganisha barabara zote ambazo zilichelewa kupelekewa maendeleo hasa zile zilizo pembezoni. Mkoani kwangu nina barabara ya kutoka Mpanda - Kigoma haijaunganishwa kwa kiwango cha lami. Nashukuru Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 16. Niiombe Serikali iharakishe kusaini mkataba ili barabara ile iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini zipo barabara za kutoka mkoa wa Katavi kwenda mkoa wa Tabora, ni vyema Serikali ikaharakisha mchakato iliyonayo ili ziweze kukamilisha barabara hizi. Pia bado zipo barabara zinazounganisha mkoa wa Mbeya na mkoa mpya wa Njombe, mikoa ya kutoka Ruvuma kwenda Mtwara, lakini bado tunahitaji mkoa wa Kigoma kuunganishwa na Mkoa wa Kagera, tunahitaji barabara zote hizi ziunganishwe kwa kiwango cha lami ili nchi iweze kupitika vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na suala la mawasiliano. Kwenye suala la mawasiliano Serikali bado tunahitaji iendelee kukuza ule Mfuko wa UCSAF ili uweze kutoa mawasiliano kwa wote. Vipo vijiji jimboni kwangu ambavyo viliahidiwa na Serikali kupatiwa mawasiliano kama vijiji vya Kata za Sibwesa na Katuma, lakini bado kuna vijiji vya Igagala, Majalila na Rugufu eneo la Mishamo tunahitaji mawasiliano ya kudumu ili wananchi waweze kupata huduma hiyo muhimu. Tunaiomba Serikali ielekeze nguvu kwenye maeneo hayo ili watu wote wanufaike na mfuko ule ambao unafadhiliwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niishukuru Serikali na niombe ichukue ushauri ule na tunaunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi hii nichangie Wizara hii muhimu ya Nishati na Madini. Nianze juu ya umeme katika Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Katavi una umeme usio na uhakika. Nilikuwa naomba Wizara kupitia Waziri aangalie umuhimu wa kuboresha miundombinu ya umeme katika Mkoa wa Katavi. Mkoa huu umekuwa ni chaka la kupelekewa zana zile ambazo zimetumika katika baadhi ya maeneo zikichoka wanapeleka Mkoa wa Katavi. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atambue kwamba Mkoa wa Katavi ni sehemu ya Tanzania na wote wanastahili kupata stahili ya mgawanyo wa keki ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mradi wa Orion ambao ulikuwa unaunganisha Mkoa wa Katavi baada ya Wilaya ya Biharamulo na Ngara tunahitaji sana ule mradi upelekewe fedha ili uweze kutoa umeme wenye uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni umeme vijijini, eneo hili bado kuna ubaguzi ambao unatolewa katika baadhi ya maeneo. Mkoa wa Katavi ni baadhi ya maeneo ambayo yana vijiji vichache sana ambavyo vimepelekewa umeme, Jimboni kwangu sina hata kijiji kimoja ambacho kimepelekewa umeme vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa Phase II. Nilikuwa na kijiji cha Kabungu, Mchakamchaka, Ifukutwa, Igalula na Majalila, bahati mbaya mpaka Phase II inakwisha bado huo umeme haujafika. Kwenye eneo la Phase III limetengewa vijiji 49, ninaomba hivyo vijiji vipelekewe umeme ikiunganishwa na vile vijiji ambavyo havikupata awamu ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ya msingi ambayo yanahitaji kuboreshwa kupelekewa umeme vijijini, hasa maeneo ya Ukanda wa Ziwa. Eneo la Ukanda wa Ziwa lina vijiji vya Kapalamsenga, Itunya, Karema, Ikola, Kasangantongwe na vijiji ambavyo viko jirani vinahitaji kupata umeme kwa sababu kuna maeneo ya uzalishaji mali. Upo utafiti unaofanywa wa mafuta kwenye maeneo hayo lakini kuna shughuli za uvuvi zinazofanywa na wananchi katika kata hiyo na tarafa ya Karema kwa ujumla naomba vijiji hivi vipewe kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate majibu ya uhakika kwenye vile vijiji ambavyo vilikuwa vimelengwa kwa awamu ya kwanza na muunganisho wa vijiji vya tarafa ya Mishamo ambapo kuna vijiji 16 havina hata kijiji kimoja ambacho kimepata umeme vijijini, naomba vijiji vya Bulamata, Kusi, Kamjela, Ifumbula na vijiji vya eneo la Isubangala, Ilangu, tunahitaji vipewe umeme ambao ni muhimu uwasaidie wananchi katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi umeanzishwa ambao ungesaidia eneo zima la Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma, Mradi wa Umeme wa Malagarasi, ungekuwa suluhisho la umeme wa uhakika. Bahati mbaya sana eneo lile la Malagarasi kuna vitu ambavyo vinaelezwa huwa tunashindwa kuwaelewa, kinapozungumzwa unashindwa kuelewa kwamba Serikali ina maana gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna vyura, hawa vyura wamekuwa na thamani kubwa kuliko hata mahitaji ambayo yanaweza yakawasaidia wananchi. Umeme ule ambao ungefungwa mradi mkubwa ungesaidia Mkoa wa Kigoma na ungesaidia Mkoa wa Katavi kwa ujumla. Naomba Serikali ije na majibu ya msingi; je, mpaka sasa uwepo wa wale vyura kwenye maeneo yale umetoa tija kwa Taifa hili kwa kiasi gani? Tuambiwe kwamba kuna thamani ya fedha imetolewa kubwa ambayo inazidi kuleta ule mradi ambao ungetusaidia wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nizungumzie suala la utafiti wa mafuta kwenye Ziwa Tanganyika. Eneo la Karema ni eneo ambalo limekuwa likifanyiwa utafiti, lakini mpaka sasa hivi hatujajua kinachoendelea kwani baada ya tafiti na wale waliokuwa wanatafiti hawapo kwa sasa. Wananchi bado wanaangalia ni nini ambacho kitafanyika na walikuwa tayari kutoa baadhi ya maeneo kwa ajili ya kupata utafiti ule wa mafuta na gesi katika Ziwa Tanganyika. Sasa mpaka saa hizi hatujui ni kitu gani ambacho kimefanyika na kina tija ipi kwa wananchi wa maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la madini. Jimboni kwangu kuna miradi ya madini ya dhahabu kwenye Kata ya Katuma na kwenye Kata ya Kapalamsenga kuna machimbo ya shaba; nilikuwa naomba Serikali inawasaidia vipi hawa wachimbaji wadogo wadogo? Kwani wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa kama yatima ambao hawasaidiwi na Serikali kwa karibu ili waweze kupata manufaa ya machimbo yale ambayo yanafanywa ili yaweze kuwanufaisha wachimbaji. Naiomba Serikali iandae mazingira ya kuwasaidia hawa wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kunufaika na machimbo ambayo yapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijue kuhusu mradi wa shaba ambao uko Kata ya Kapalamsenga, naiomba Serikali ije na majibu mpaka sasa ule mradi unawanufaisha vipi wananchi? Wawekezaji wamekuja wamewekeza pale lakini hakuna mrahaba wowote unaopatikana kuwapa manufaa wananchi wanaozunguka kwenye maeneo yale na bado hata Halmashauri ya Mpanda hawajapata fedha za kuwanufaisha kutokana na madini yale yanayochimbwa. Niombe sana Serikali ije na majibu ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nasisitiza Wizara iangalie umuhimu wa kuweka uwiano ulio sawa kwenye Mikoa iliyosahaulika hasa Mikoa ya pembezoni. Miradi mingi hasa ya umeme vijijini bado imekuwa ikielekezwa kwenye maeneo ambayo wao wana miradi mingine, wanaongezewa mradi juu ya mradi. Tunaomba vijiji vya Wilaya ya Mpanda kwa ujumla vipewe miradi ya umeme ili iweze kuwasaidia na sehemu hizo zifunguke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii nichangie kwenye Wizara muhimu ya ardhi. Awali ya yote, nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ambaye amefanya kazi nzuri. Tunaamini kazi hii anayoifanya ni kwa manufaa ya Watanzania. Namwomba aongeze jitihada hasa aelekeze na maeneo ambayo yako pembezoni kama Mkoa wa Katavi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ipo migogoro ya ardhi kwenye Mkoa wa Katavi. Mkoa wa Katavi ni mkoa ambao asilimia kubwa sana umemilikiwa na hifadhi za misitu na hifadhi ya Taifa ya Katavi. Karibu vijiji vingi ambavyo vimezunguka mkoa huu viko kwenye migogoro ya ardhi, lakini ni mkoa ambao una ardhi kubwa sana. Namwomba Mheshimiwa Waziri ajaribu sana kuelekeza nguvu kwenye maeneo haya ili aje aangalie migogogro ambayo ipo. Ipo kwenye vijiji kadhaa ambavyo viko kwenye Jimbo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Kijiji cha Kabage na Kijiji cha Nkungwi. Vijiji hivi vina migogoro miwili. Moja, ni mgogoro wa mashamba kati ya wananchi waliomilikishwa ardhi kinyume na utaratibu. Wamechukua ardhi kubwa sana ambayo hawaiendelezi matokeo yake wananchi ndio wanaolima na wanabughudhiwa na wanauawa. Naomba aelekeze nguvu kwenye Kijiji cha Kabage. Yapo mauaji yamefanyika kwa matatizo ya ardhi; ayafuatilie kwa karibu ili tupate suluhisho la mgogoro huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo kwenye Kijiji cha Nkungwi. Kijiji hiki kina tatizo la mgogoro wa ardhi wa Mpairo. Mpairo ni ardhi ambayo imemilikwa na wananchi wachache. Ipo kwenye Serikali ya Kijiji na Serikali ya Wilaya ilishatoa maelekezo lakini bado mgogoro huu ni mkubwa sana. Naomba Serikali iweze kuingilia mgogoro huu ili tuweze kuwasaidia wananchi wa Kijiji cha Nkungwi. Vijiji hivi ambavyo viko kwenye Tarafa ya Mwese, vina tatizo sana la migogoro ya ardhi kati ya Serikali za Vijiji na WMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa nia njema iliweka hifadhi kwa manufaa ya Watanzania, lakini bado Serikali hii sikivu imeweka utaratibu wa kuangalia WMA kuwashirikisha Serikali za Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali hasa kupitia kwa Mheshimiwa Waziri, ajaribu kuja, afike Mpanda akamilishe tatizo la migogoro ya ardhi hasa inayosababishwa na WMA kuwa na kiburi bila kuwashirikisha wananchi wala kushirikisha Serikali, wanafanya wanavyotaka wao. Hili akilishughulikia atakuwa ametatua tatizo la Vijiji vya Mkabage, Mkungwi, Kasekese, Sibwesa, Kapalamsenga na Kaseganyama. Maeneo haya na mengineyo mengi kwenye Mkoa wa Katavi yana tatizo kubwa hili ambalo atakuwa amesaidia kutoa utatuzi kwenye eneo hili la migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lipo eneo la Vijiji vya Kapanga, Lugonesi na Lwega. Ni tatizo la migogoro ya ardhi ya mipaka ambayo kimsingi kama utatoa maelekezo kama Mheshimiwa Waziri, lina nafasi kubwa sana ya kuweza kutekelezwa kwa sababu ni usimamizi tu unaotakiwa ili kuweza kutoa tatizo hili kwenye vijiji hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa amefanya ziara kwenye Mkoa wa Katavi, ajitahidi sana kushirikisha Waheshimiwa Wabunge wamweleze migogoro ya ardhi ambayo ipo. Nikumbushe, wakati wa harakati za kuomba nafasi ya ridhaa ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, alikuja na Mheshimiwa Rais, yeye ni shahidi; alisimama eneo moja la Luhafu ambalo lina wakazi 25,000, mpaka sasa wananchi wanaendelea kukaa bila kuwa na amani kwa sababu Serikali imeshindwa kutoa utatuzi wa ardhi kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ajitahidi sana kutoa maelekezo ya Serikali yatakayowapa manufaa wananchi kwenye maeneo yale ambayo yeye mwenyewe ni shahidi, alifika na alisikia kilio cha wananchi na Mheshimiwa Rais alizungumza na akatoa ridhaa kwa wananchi, akatoa matumaini makubwa sana. Naomba hilo alifuatilie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni Shirika la Nyumba. Kwanza nampongeza Mkurugenzi wa Shirika hili kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kizalendo. Naomba sasa Shirika libadili mwelekeo wa kuelekeza ujenzi wa nyumba kwenye maeneo ya Miji Mikuu tu. Namwomba aelekeze kwenye mji ambao unakua sasa hivi, Mji wa Katavi. Tunajua Shirika lipo linafanya kazi vizuri, lakini tunaomba kulishauri shirika hili; kwanza, lijenge nyumba ambazo zitakuwa na thamani inayofanana na watu wanaojengewa nyumba, waweze kumudu gharama za upangishaji au gharama za manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika limekuwa likijenga nyumba kwa gharama kubwa sana kiasi kwamba sasa wanaojengewa nyumba hizi ni baadhi ya wale wachache tu ambao wanaweza wakamudu gharama hizo. Naomba Shirika liangalie mwelekeo mpya ili liweze kujenga nyumba ambazo wananchi wataweza kumudu kukaa na wataweza kuzinunua kwa gharama ambazo zinafanana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, kwenye eneo lingine kuna tatizo la uhaba wa wataalam wa ardhi. Kumekuwa na tatizo kubwa sana la uhaba wa wataalam. Eneo la kwetu Mkoa wa Katavi ni sehemu ambayo kuna tatizo kubwa sana la wataalam wanaohusika na suala zima la ardhi na ndiyo maana unakuta miji mingi inajengwa kwa uholela kwa sababu wataalam wanakuwa hawapo na hata kama wapo vitendea kazi vinakuwa havipo.
Naiomba Serikali ielekeze nguvu, itenge fedha za kutosha ili iweze kutoa tatizo la upimaji wa ardhi kwa manufaa ya wananchi wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie eneo la hatimiliki. Tunapotaka kuwasaidia wananchi na walio wengi wanaoishi vijijini, ni lazima Serikali ije na mkakati wa kuwezesha wananchi kumiliki ardhi ambayo itawasaidia kuweka masuala yao katika hali nzuri, hasa kwenye dhana ya kukopeshwa. Wananchi wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu ardhi walizonazo hazijamilikishwa kihalali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ije na mpango wa kuweza kuwasaidia wananchi wapate hatimiliki, hata zile za kimila ziharakishwe kutengenezewa mazingira ili wananchi waweze kumiliki ardhi yao. Maeneo mengi wananchi wanalima, wanafanya shughuli zao za uvuvi lakini hawana kitu ambacho kinaweza kikawasaidia kuwezeshwa na Serikali. Naomba eneo hili lipewe kipaumbele sana kwa sababu ni eneo ambalo linaweza likawasaidia na likawainua wananchi walio wengi, wanaokaa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa hotuba ya Waziri wa Ardhi na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi hii nianze mchango wangu kwa kuchangia juu ya Hifadhi ya Taifa ya Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi hii ipo Mkoa wa Katavi, ni hifadhi kubwa sana, lakini bahati mbaya sana Wizara husika haijaitangaza. Ili tuweze kutangaza utalii ni vema tukaelekeza mawazo kwa maeneo yote ya nchi yetu. Ukanda wa Kusini utalii haujatangazwa ndiyo maana Mbuga ya Ruaha, Mbuga ya Katavi, Mahale hazifanyikazi vizuri kwa sababu Serikali yenyewe imeweka mipaka; utalii unaotangazwa katika nchi yetu zaidi unatangazwa kwa Mikoa ya Kanda ya Kaskazini. Ninaiomba Serikali ielekeze nguvu kutangaza na maeneo mengine ili zile fursa wapate kuzitembelea, tuna imani watalii watakuwa wengi pindi watakapokuwa wamebadilisha na maeneo mengine wakaenda kuangalia fursa zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninazungumzia suala la Hifadhi ya Katavi kwa sababu Mbuga ya Katavi inayo uwezo wa kuunganisha watalii wa kutoka Katavi na wakaenda Mbunga ya Mahale ambayo iko Mkoa wa Kigoma ambao ni jirani, wanaweza wakitoka Mkoa wa Iringa katika Hifadhi ya Ruaha wakaja Mbuga ya Katavi na baadaye watalii hao wakaenda Mahale, wanaweza wakapata maeneo mengi ya kuangalia utalii wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mbuga ile ya Katavi tunaiomba Serikali iangalie uhifadhi wa hifadhi hiyo ya Katavi kwa sababu upo uwezekano hifadhi hii ikatoweka kwa sababu hakuna miundombinu mizuri. Ninaishauri Serikali tunao Mto wa Katuma ambao unaifanya Hifadhi ya Katavi iwepo, itunze na ihakikishe inaandaa mazingira mazuri ya kuhifadhi ili kuwe na utaratibu wa kuvuna maji, kuna maeneo wakati fulani inapofika kipindi cha mwezi wa Oktoba hifadhi hii huwa inakauka, hakuna maji na wanyama kama boko na mamba huwa wanakufa kwa wingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye hifadhi ya wanyama ya Katavi, bado wafanyakazi wanaofanyakazi kwenye hifadhi hii wanashida kubwa sana ikiwa ni pamoja na vitendea kazi hawana, ninaiomba Serikali kupitia Wizara husika iwapelekee vitendea kazi ili waweze kupambana na majangili wanaoenda kwenye mbuga hii sambamba na hifadhi ya Msitu wa Luwavi ambao ni jirani na kwa Mheshimiwa Keissy. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la migogoro kati ya vijiji ambavyo vinazungukwa na WMA. Kumekuwa na tatizo kubwa sana kati ya vijiji vya Kabage, Kungwi, Sibwesa, Kasekese, Kaseganyama na Kapalamsenga. Vijiji hivi kila mara wananchi wanasumbuliwa wanachomewa nyumba na Serikali kwa sababu wao wana migogoro na WMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, WMA ni ardhi ambayo wanavijiji walikubaliana, lakini bado wananchi hakuna walichonufaika na mpango mzima wa WMA. Ninaiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri, fanya ziara Mkoa wa Katavi utembelee kwenye vijiji hivyo, uje utatue tatizo la WMA ambayo inawalazimisha wananchi hawana faida nayo, ukitatua huu mgogoro utakuwa umesaidia sana wananchi kwenye maeneo hayo. Ni vizuri tukaangalia pande zote mbili, mimi naamini uhifadhi tunauhitaji sana kwa sababu unalinda mazingira na unawafanya wananchi waneemeke na fursa zilizoko. Yale maeneo ambayo yamekuwa na migogoro ni vizuri Serikali mkawa karibu ili mkawatendea haki wale wananchi, tutoe dhana ile ambayo ipo ya kila siku kusikiliza hii migogoro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ninapenda kuzungumzia ni hifadhi ya misitu. Mkoa wangu wa Katavi una hifadhi mkubwa sana ya misitu na tuna eneo la Hifadhi la Msitu wa Tongwe, ambapo kumekuwa na uvunaji holela wa magogo yanayochukuliwa na wasimamizi wakubwa sana ni TFS ambao wanasimamia misitu kwenye nchi yetu kwa ujumla. Ninaiomba Serikali tunahitaji sasa maeneo ambayo kunavunwa hiyo misitu, kuwe na kitu ambacho kinawanufaisha wananchi kwenye maeneo husika, vipo vijiji ambavyo vimepakana na hiyo misitu, wanatunza lakini hawanufaiki, unafika mahala hata watoto wanaosoma kwenye shule, hawapati madawati kwenye maeneo hayo. Ni vema Serikali ikaja na mpango wa kuangalia maeneo ambayo yanawanufaisha wananchi na wanatunza ile misitu kuwe na mrejesho ambao utawafanya wawe na nguvu ya kuhifadhi hiyo misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nazungumzia sana eneo lingine wakati ule wa Operesheni Tokomeza. Wananchi hasa wakulima walinyang‟anywa silaha ambazo zinawasaidia kufukuza wanyama waharibifu. Serikali ije na majibu kwa sababu wananchi hawa wanaolima, wanyama waharibifu wanakwenda kuharibu mazao yao na silaha zote walishazibeba. Tunaomba Serikali iwarudishie wananchi hawa....
MWENYEKITI: Ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kunipa nafasi hii.
Kwanza awali ya yote niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao
wamechangia, lakini ninanyongeza ya mambo ambayo tunahitaji kuishauri Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la fedha kwa Wizara husika ambayo imepewa
dhamana ya miundombinu bado ni ndogo, tunaomba sana Serikali ihakikishe inapeleka fedha
kwa wakati ili miundombinu iliyolengwa iweze kujengwa kwa wakati. Lakini tunaipongeza
Serikali kwa kufikia maamuzi ya ujenzi wa reli hasa reli ya kati ambayo kwa kuanzia Serikali
imesaini na Kampuni za Waturuki kuweza kujenga reli ambayo itakuwa na manufaa zaidi. Ombi
langu kwa Serikali ihakikishe inatengeneza mazingira mazuri ili kushawishi na makampuni
mengine yaweze kuomba tender ili iweze kujengwa reli ambayo itaenda kwa haraka,
ipambane na mazingira ambayo ni ya ushindani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kitendo cha kujenga reli ambayo itaanzia Dar es Salaam
kuishia Morogoro bado tuna kilometa nyingi ambazo zinahitaji kujengwa kwa wakati. Ni vyema
Serikali ikajipanga kuhakikisha maeneo hayo yanatengewa fedha ili tupate fedha zitakazojenga
reli kuanzia Morogoro kuja Dodoma, Dodoma - Tabora, Tabora - Kigoma, Kaliua - Mpanda hadi
kule Kalema.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kuna maeneo ya kuanzia Tabora kwenda Isaka
mpaka maeneo ya Kezya kule Rwanda ili yaweze kuendana na mazingira halisi ambayo
kimsingi tutakuwa tumeteka soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunahitaji kuishauri Serikali ni kufanya
maboresho ya ujenzi wa bandari hasa zile gati ambazo zinahitajika ziwe kwenye maeneo
ambayo yataenda kibiashara zaidi. Kwa sasa bandari bado haina uwezo mkubwa sana wa
kupokea meli nyingi, tunahitaji Serikali ielekeze nguvu kwenye maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado tunahitaji Serikali iboreshe bandari za mikoani hasa
kwenye maziwa makuu. Bandari zile zitachangia uchumi kwenye maeneo husika. Tunazo
bandari ambazo zimesemwa sana na Waheshimiwa Wabunge, Bandari ya Dar es Salaam
inahitaji maboresho, Bandari ya Tanga ambayo kimsingi itategemea kuchukua mzigo mkubwa
sana kutoka nchi ya Uganda inahitaji iboreshwe. Bandari ya Kigoma ikiboreshwa itasaidia sana
kukuza uchumi wa nchi hii kwa sababu iko jirani na DRC. Bandari ile ikitumika sambamba na
bandari ambayo inategemewa kujengwa Kalema itasaidia sana kukuza uchumi wa nchi na
sehemu kubwa na mzigo wa Congo ambao tunautarajia sana kutumika kwenye reli na Bandari
ya Dar es Salaam zitafanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzazji)
Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri kwamba barabara zitengewe fedha za kutosha kwa
ajili ya kuunganisha mikoa yote ya nchi yetu. Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niwe miongoni mwa wachangiaji kwenye hotuba ya bajeti. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo anaifanya pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wanafanya kazi ya kuwasaidia Watanzania hasa wale wenye kipato cha chini.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwenye eneo la mfumo wa bandari. Kwenye eneo la bandari yapo makubaliano ambayo yamekubaliana kati ya nchi yetu na nchi ya Kongo, Zambia na Malawi. Mfumo huu wa single customs territory ni mfumo ambao unadidimiza mapato ya nchi yetu. Ukusanyaji wa mapato unakuwa kidogo kwa sababu wale wafanyabiashara ambao walikuwa wanatumia bandari yetu wameihama, wamekimbilia kwenye bandari nyingine za nchi jirani. Bandari hizo ni bandari za Durban, Bandari ya Mombasa, Bandari ya Msumbiji ambazo ziko jirani, wanakwepa masharti ambayo kimsingi makubaliano yale hayainufaishi nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba Serikali iangalie mfumo huu, iurekebishe mapema ili tuweze kutoa wigo mkubwa sana wa ukusanyaji wa mapato kwa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo kodi nyingize ambazo zinawafanya wafanya biashara waweze kukimbia. Mfano nchi ya Zambia mizigo inayoletwa nchini wanatozwa gharama kubwa sana kiasi kwamba wale watu ambao wanatumia bandari yetu wanakimbia. Ni vyema Serikali ikaangalia ni sababu zipi zinazofanya mizigo ya kutoka Zambia iwe na gharama kubwa kuliko maeneo mengine ya watumiaji wa bandari hii?
Naomba Serikali iangalie kwa makini sana, tukiboresha kwenye maeneo haya, tutaisaidia nchi yetu iweze kupata mapato makubwa sana kwa sababu watumiaji wa bandari hii watakuwa wengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasisitiza hili kwa sababu siasa za sasa hivi ni uchumi. Wenzetu ambao wametuzunguka, wanatumia udhaifu tunaokuwa tumejiwekea sisi wenyewe. Mnakubaliana kwenye makubaliano halisi, lakini kwenye utekelezaji wao ndio wa kwanza kuvunja yale makubaliano, sisi tunabaki tumeng’ang’ania vitu ambavyo havitusaidii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, halikadhalika eneo la pili ni eneo la ukusanyaji wa mapato ambao Serikali imekuja na mpango wa kuongeza VAT juu ya utalii. Kwa hesabu za haraka haraka tu, tukitekeleza hili ambalo limeletwa na Serikali, watalii wanaokuja nchini watapungua kwa kiwango kikubwa sana na hii intatoa fursa kwa nchi jirani ya Kenya iweze kutumia udhaifu wa kwetu sisi kama nchi uweze kuwanufaisha wao Wakenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali iangalie na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana aone umuhimu wa hili jambo kwamba halitawasaidia Watanzania, linawasaidia jirani zetu ambao wanapakana na sisi na watumia udhaifu wetu, wanajua kabisa kwamba hiki kitu hakiwezi kuwasaidia Watanzania. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iangalie kwenye maeneo haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni mapato ya Halmashauri kukusanywa na TRA. Serikali imekuja na nia njema kutaka kusaidia mazingira ya uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato, lakini tunapata shaka sana; kama Serikali kipindi chote imekuwa ikikusanya mapato na kurudisha fedha kule kwenye Halmashauri, fedha hazifiki. Leo hii tunawapa jukumu la kukusanya wao, hata kile ambacho kimekuwa kikiwasaidia kitatoweka kabisa. Tunaangalia miaka hii mitatu, upelekaji wa fedha wa Serikali kwenda kwa walengwa ulikuwa hafifu sana, unakuta asilimia 40 mpaka asilimia 45. Sasa leo hii fedha zote zibaki zinamilikiwa na Serikali Kuu, tutakua tunaziua Halmashauri zetu. Naomba na hili mliangalie. Ni vyema tukatizama vitu ambavyo vitawasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kila kitu kama kitakusanywa na Serikali Kuu, huku chini mimi sina imani kwamba hizi fedha zitawafikia walengwa. Kwenye eneo la Halmashauri za Wilaya ndiko ambako kuna utekelezaji mkubwa wa fedha zinazopelekwa kule, kunakuwa na utekelezaji wa shughuli za maendeleo. Tunahitaji tupate huduma za maji, tunahitaji tuboreshe barabara vijijini na tunahitaji tupate huduma za afya zilizo bora. Kama Serikali haitakuwa imepeleka mazingira mazuri ya kuangalia fedha hizi, nawaambia tutakuja kulaumiana na Serikali itajuta kwa sababu sina imani itaweza kukusanya kadri wanavyokusanya sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali, kuna maeneo kwenye suala la uwiano wa fedha za miradi. Pamoja na kwamba Serikali ina nia njema ya kupeleka huduma zilizo sawa kwa wananchi, bahati mbaya sana Wizara husika ya Fedha bado haitumii uwiano ulio sawa wa kupeleka fedha kwenye Mikoa mbalimbali. Fedha nyingi zimekuwa zikipelekwa maeneo ambayo baadhi na sehemu nyingine hawapati kabisa hizo fedha. Naomba Serikali kwa sasa ibadili mfumo na iangalie uhalisia wa kusaidia hasa ile Mikoa ambayo ilisahaulika, ambayo iko nyuma kimaendeleo, wapelekewe fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana, ipo Mikoa mipya, Wilaya mpya ambazo zina changamoto nyingi mno. Tunaomba Serikali ipeleke fedha zikasaidie kutekeleza miradi ya shughuli za maendeleo kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo Wilaya nyingi sana ambazo ni mpya ikiwemo Wilaya mpya ya Tanganyika kule Jimboni kwangu Mkoa wa Katavi; lakini zipo Wilaya ambazo zinahitaji kusaidiwa kama Buhigwe, Chemba na Mlele. Zile Wilaya zinahitaji sana kupata fedha ambazo zitainua shughuli za maendeleo kwenye maeneo yao na kuna changamoto kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie eneo la kuziunganisha taasisi hizi za Kampuni ya TRL, RAHCO; TPA na Marine Service. Naomba Mheshimiwa Waziri, hizi kampuni ziunganisheni ziwe kitu kimoja ili ziweze kutoa huduma kwa wananchi. Kuongeza haya makampuni kila sehemu inafanya kazi zake, hakuna ufanisi wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, tumeangalia eneo hili kuna shida kubwa sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri muangalie sheria ile ambayo ilifanya kuwe na mgawanyo ije mwilete hapa Bungeni tuirekebeshe ili haya makampuni yaunganishwe na yafanywe kitu kimoja ambacho kitawasaidia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nami naungana na wenzangu kwenye suala la gratuity. Ni vyema Mheshimiwa Waziri ukatafakari, ukaangalia na ukaona umuhimu mkubwa kwamba Waheshimiwa Wabunge wanafanya kazi kubwa sana. Hawana pensheni; hiyo wanayopewa ni kama Honoraria tu, kwa sababu ndiyo malipo yao ya mwisho kwa kazi ambazo walizifanya. Nawaomba Mheshimiwa Waziri uangalie changamoto ambazo wanazifanya Waheshimiwa Wabunge. Naamini ungelikuwa umeshaonja nawe ukawa Mbunge wa Jimbo, ungeona adha yake ilivyo. Karibu misiba yote ni ya Mbunge, mahafali yote ni ya Mbunge, harusi zote za Mbunge, kila kitu kilichopo kwenye jamii kinamwandama Mbunge. Naomba katika hili uliangalie, siyo kwa Waheshimiwa Wabunge tu, lazima tuone kwenye maeneo yote yanayohusiana na mapendekeza yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, isije kengele ikanililia. Naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
MHE. MOSHI J. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nawapongeza sana Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Makamba kwa juhudi kubwa wanayoifanya hasa katika ziara zinazofanyika katika nchi yetu wakihamasisha suala la hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri alipokuja Mpanda na kutoa amri ya kuondoa mabanio ya Mto Katuma ambao ulikuwa unakaribia kutoweka. Ombi langu tunaomba Ofisi yako itoe fedha kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wanaotunza Mto wa Katuma wasaidiwe fedha za kuchimba mabwawa na malambo yatakayosaidia kuacha uharibifu wa mto huo ambao ni muhimu kwa ajili ya Hifadhi ya Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni hifadhi za misitu, ni vema suala la kuhifadhi misitu iliyopo Mpanda wasiachiwe watu wa maliasili pekee kwani suala hili ni muhimu sana katika kuhifadhi misitu ambayo inafyekwa kwa shughuli za kilimo, ufugaji na nishati ya kuni. Niiombe Serikali iangalie suala hili kwa uzito mkubwa kwani shughuli hizi za binadamu zinatumia sana misitu na kutengeneza uharibifu wa mazingira. Ushauri wangu ni;
(i) Serikali isimamie suala la kilimo cha kuhamahama;
(ii) Wafugaji wafuge ufugaji wa kisasa ili tupunguze wingi wa mifugo; na
(iii) Serikali iandae mpango wa kuwawezesha Watanzania wapate gesi kwa bei nafuu ili waachane na suala la kutegemea kuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa; Ziwa Tanganyika linaendelea kupungua siku hadi siku. Kama Serikali haitachukua hatua stahiki ziwa hili litapungua sana siku hadi siku. Serikali ichukue hatua ya kuweka banio nchini DRC Kongo, bila kufanya hivyo Ziwa Tanganyika litatoweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ziwa Tanganyika limejaa tope, Wizara nendeni na mpeleke wataalam waangalie uwezekano wa kutoa tope na kulifanya Ziwa hilo liwe hai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitoe shukrani kwa Serikali kwa kutenga fedha za ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi. Mheshimiwa Waziri Mkoa wa Katavi ni eneo linalokuwa siku hadi siku na una changamoto kubwa za afya. Ni vema Serikali ikaweka kipaumbele kikubwa kujenga Hospitali ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika haina Hospitali ya Wilaya, tunaomba Serikali kupitia Wizara ya Afya itupatie fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwani suala la huduma hiyo ni muhimu sana na ukizingatia jiografia ya Wilaya yangu ni ngumu sana na ndiyo Wilaya pekee yenye eneo kubwa sana kuliko Wilaya zote ambazo zipo Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika ina vituo vitatu tu japo ni Wilaya kubwa na ina idadi kubwa ya watu, bado ndiyo eneo ambalo lina vituo vichache sana. Naiomba Serikali itupatie vituo vipya vya afya ambavyo vitarahisisha kutoa huduma ndani ya Wilaya, na kupunguza mzigo mkubwa kwa Hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado niiombe Wizara katika vituo tulivyonavyo ndani ya Wilaya vituo hivyo bado huduma hizo ni duni sana. Naomba kituo cha Karema, Mwese na Mishamo viboreshwe na viwe na hadhi. Ni matumaini yangu Serikali italiangalia kwa jicho la huruma kwa kuboresha vituo hivyo kwa kuvifanyia ukarabati na kupeleka dawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ambulance, tunaomba ombi maalum la kupatiwa gari la wagonjwa, katika maeneo yenye uhitaji mkubwa ni Wilaya yangu ambayo ina taabu kubwa sana. Hivyo tunasisitiza ombi hili litiliwe mkazo mkubwa na muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na utalii wa ndani. Suala la utalii wa ndani halijawekewa umuhimu na Wizara. Ni vyema suala hili likapewa kipaumbele ili Watanzania wajenge tabia ya kutembelea vivutio vya maliasili ya nchi yetu. Na kwa kuanzia taasisi za Serikali, mashirika ya umma na shule zijenge mazingira ya kutembelea mbuga za wanyama, maporomoko, milima na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii wa Kanda ya Kaskazini na Kanda ya Magharibi; kumekuwa na tabia ya kutangaza utalii wa Kaskazini tu ikiwa yapo maeneo mengine ambayo kama yakitangazwa yatakuwa kivutio kikubwa kwa watalii. Kwa mfano Mbuga za Ruaha, Selous, Katavi, Mahare, Maporomoko ya Kalambo na fukwe nzuri ya Ziwa Tanganyika hazijatangazwa, ni vyema na maeneo hayo yakatangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la migogoro ya WMA; Jimboni kwangu kuna migogoro ya WMA wa vijiji vya Kaseganyama, Kapalamsenga, Simbwesa na Kabage. Naomba migogoro ya vijiji hivi imalizwe kwani ni muda mrefu suala hili halijapatiwa ufumbuzi. Naomba Waziri njoo jimboni kwangu umalize tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la misitu; Jimboni kwangu kuna misitu mikubwa ya Tongwe Mashariki na Tongwe Magharibi, maeneo haya ni makubwa sana na kuna wanyama vivutio kama sokwe na misitu minene ambayo inavunwa kwa wizi. Tunaomba Wizara yako itupatie magari ya doria ili tuweze kudhibiti uwindaji haramu na uvunaji haramu wa misitu. Ombi hili ni muhimu sana kwa Wilaya yangu ya Tanganyika kupatiwa magari kwa ajili ya uhifadhi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe sehemu ya mchangiaji kwenye Wizara hii. Awali ya yote nitoe pongezi kwa Serikali kwa kazi kubwa sana ambayo inafanyika hasa kwenye suala la miundombinu. Wapo watu ambao hawaoni kile ambacho kinafanywa na Serikali, lakini tunaipongeza Serikali kupitia kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo yamefanyika na yanaonekana ni mapinduzi makubwa ya haraka. Tuna upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa pale Dar es salaam. Kwa wale ambao hawajafika wanaona mabadiliko ambayo yapo, ni kazi ambayo inafanywa na Serikali. Kuna ununuzi wa ndege mpya ambazo zinatengeneza sura mpya na historia ya nchi yetu. Ndani ya kipindi kifupi tumepata ndege ambazo zimeanza kutoa huduma kwa wananchi, lakini baadhi ya watu hawaoni yale ambayo yanafanywa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yapo ambayo yamefanywa makubwa, ni ujenzi wa reli ya kati, tayari Mheshimiwa Rais alishaweka jiwe la msingi ambalo linaashiria kuanza kwa ujenzi ambao utatoa unafuu wa maisha ya Watanzania hasa wale ambao ni maskini wa kipato cha chini. Zipo jitihada ambazo Serikali imefanya kama ujenzi wa barabara ambapo karibu kila kona kuna ujenzi wa barabara. Hizi ni shughuli ambazo zimefanywa na Serikali, tuna haki ya kuipongeza.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze tu kutoa shukrani za dhati kwa Mkoa wetu wa Katavi japo yupo Mbunge mwenzangu ambaye amesema hakuna lolote lililofanywa, nasikitika sana. Tuna uwaja wa ndege ambao umejengwa, lengo la kujenga uwanja wa ndege pale Mpanda ni kuweza kukuza utalii ukanda wa Magharibi, kwa maana ya Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanapojenga ule uwanja wanahitaji sasa kui-promote mbuga ya Katavi pamoja Mbuga ya Mahale ambayo ipo Mkoa wa Kigoma; ndiyo malengo makubwa ya Serikali. Kwa taarifa tu, ni juzi juzi Watalii kutoka nchi ya Israel wamefika, wana interest kubwa sana ya kwenda Mkoa wa Katavi na kufanya utalii wa Ziwa Tanganyika. Sasa kwa wale ambao hawana uelewa hawajui. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza Serikali kwa kutengeneza miundombinu, tunayo barabara ya kutoka Sumbawanga kuja Mpanda tayari iliishaanza kujengwa. Tunachokiomba Serikalini ni kuimaliza ile barabara japo mwenzangu aliyetangulia amefika na kuponda na anasema
zile fedha zilizotengwa hajui kazi yake kwa sababu barabara imekamilika. Lakini kwa taarifa tu ni kwamba ile barabara inahitaji mifereji na vitu vingine ambayo vinahitajika kukamilika kwa barabara ndio maana asilimia 80 imekamilika lakini bado asilimia 20. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la bandari. Bandari ni nguzo kubwa sana ya kiuchumi na ni lango kuu la mapato ya Serikali kwa nchi yetu hasa Bandari ya Dar es Salaam. Tunaishauri Serikali ihakikishe inaandaa matengezo ya haraka kuhakikisha upanuzi wa ile bandari unafanywa kwa wakati. Bandari ile ikikamilika itaruhusu kuletwa kwa meli kubwa ambazo ni za kimataifa ambazo zinashindwa kwa sasa kufika kuweka gati pale Dar es Salaam kwa sababu bado miundombinu haijakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali ishughulikie ujenzi wa bandari sambamba na bandari zingine, Bandari ya Tanga, Bagamoyo na Mtwara ziweze kujengwa. Vilevile bado zipo bandari muhimu sana za Maziwa makuu. Tuna Bandari ya Mwanza inahitaji iboreshwe, tuna bandari ya Kigoma tunahitaji ifanyiwe maboresho makubwa, tuna bandari ya Karema ambayo Serikali iliazimia kwa nia njema kufungua mawasiliano kati ya nchi ya DRC na nchi yetu ili kuweza kujenga bandari ambayo itafanya shughuli za kibiashara kati ya bandari ya Kalemii na bandari ya Karema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali ielekeze nguvu, hii bandari ya Karema imekuwa kila Bunge linalopita inazungumzia ujenzi wa bandari, lakini leo hii tunaiomba sasa Serikali ipeleke nguvu ikamilishe ujenzi wa bandari hii ili iweze kutumika na kuwasaidia wananchi sambamba na ujenzi wa reli ule unaojengwa kutoka Mpanda kwenda Karema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie reli. Reli ni kiungo muhimu sana kwa wananchi, hasa ujenzi wa reli ya kati. Serikali imeazimia na tumeona dhamira kubwa ya Serikali ya kujenga miundombinu ya reli, lakini reli ya kati maana yake ni reli inayotoka Dar es Salaam kwenda Kigoma. Tunaomba sana Serikali ijielekeze kuhakikisha inakamilisha ujenzi kwa uelekeo wa kwenda Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na matawi yale ambayo yapo katikati kwa maana tawi la kutoka Tabora kwenda Mwanza, tawi la kutoka Kaliua kwenda Mpanda mpaka Karema na tawi jipya ambalo litajengwa kuanzia Uvinza kwenda Msongati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli hii malengo yake ni kuchukua mzigo wa nchi ya Congo kwa maana tuchukue mzigo wa Congo upande wa Kusini na upande wa Mashariki ni sambamba na uboreshaji wa bandari ya Kigoma ili iweze kutumika vizuri. Tunaomba sana Serikali iangalie route itakayoanza ianzie Tabora kwenda Kigoma, ianzie Kaliua kwenda Mpanda ili kuweza ku-cover kwenye maeneo ambayo kiuchumi ndiyo yana nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la barabara. Tunaishukuru Serikali, barabara sasa hivi zinaanza kujengwa, kutoka Mpanda kwenda Kigoma ilikuwa ni hadithi kwamba huwezi ukaona basi linalotoka Mkoa wa Kigoma likaenda Mpanda au Mbeya, lakini leo hii barabara zinapitika, tunaomba sasa zifanyiwe maboresho. Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mpanda kwenda Kigoma kwa kuanzia tuna kilometa 35.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sasa Serikali kama ilivyokuwa imeahidi iandae utaratibu wa barabara itakayoanzia Uvinza kuja Mishamo, na hii inayoanza kutoka Mpanda kwenda Mishamo iende sambamba na ujenzi ambao upo kwa sasa. Tukifanya hivi tutakuwa tumesaidia wanachi wa Mikoa hii ya Kanda ya Magharibi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado tuna barabara ya kutoka Mpanda kwenda Tabora, tunaomba sana Serikali ianze haraka ujenzi wa barabara hii. Kukamilika kwa barabara hii kutakuwa kumekamilisha mawasiliano ya Mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na Rukwa, hii ni Mikoa ambayo kimsingi ilisahaulika sana kwa kipindi kirefu, tunaomba barabara hizi ziwekewe kipaumbele kikubwa kama ahadi ya Mheshimiwa Rais alivyokuwa ameahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mawasiliano, yapo maeneo ambayo mawasiliano nchini bado ni duni hasa Mikoa yetu ya Ukanda wa Magharibi. Nizungumzie suala la Jimbo langu, kuna baadhi ya kata hazina mawasiliano. Tunaomba Serikali ipeleke mawasiliano kwenye kata ya Kabungu, Mpanda Ndogo, kata ya Tongwe ambako kuna makao makuu ya Wilaya ya Tanganyika pamoja baadhi ya maeneo ya Mkoa kama kata ya Ilunde; tunaomba mawasiliano yapelekwe ili wananchi waepuke adha ambayo ipo kwa kupata mawasiliano ambayo ni duni.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lipo jambo mahsusi ambalo kimsingi kwa Mbunge ambaye anaitakia mema nchi yetu amelizungumzia sana Mheshimiwa Zungu. Suala la kuipa nafasi TTCL iweze kumiliki na ikiwezekana Serikali inunue shares zile za Airtel ili imiliki yenyewe, iendeshe na kulisimamia hili Shirika, litaenda vizuri sana na litatoa tija na faida kubwa kwa nchi yetu; tukitengeneza mazingira haya tutakuwa tumewasaidia sana wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho nisisitize kwenye suala la reli Wilaya ya Mpanda na Mkoa wa Katavi kwa ujumla bado kuna wasafiri wengi. Tunamuomba Mkurugenzi mhusika wa Shirika hili aongeze mabehewa ili kuwasaidia wananchi wanaopata shida kubwa sana kwa ajili ya usafiri. Mabehewa yanayohitajika yaende yote, yale ya daraja la tatu, la pili na la kwanza yanahitajika. Kwa hiyo, tunaomba wananchi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji).

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa kunipa nafasi hii, kuchangia bajeti ya maji. Awali ya yote niishukuru sana Serikali kwa kuweza kukamilisha baadhi ya miradi ambayo ilianzishwa kwenye Halmashauri yangu ya Wilaya ya Mpanda, naipongeza sana Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja nashukrani za dhati ambazo Serikali imezifanya na kuonesha jitihada za maksudi za kutatua kero ya maji lakini bado Mkoa wa Katavi kwa ujumla tunatatizo kubwa sana la maji. Suluhisho la Mkoa huu katika kutatua tatizo la maji ili tuwe na uhakika wa kupata maji safi na salama ni vyema sasa Serikali ikajielekeza kupanga mipango mikakati ya kuleta maji kutoka ziwa Tanganyika mpaka Manispaa ya Mpanda sambamba na Halmashauri ya Nsimbo ili iweze kutekeleza mradi ambao kimsingi utatatua tatizo kubwa sana la maji. Mradi huu ukianza kwa kiwango kikubwa kwenye eneo la jimbo langu utasaidia sana kutatua tatizo la kero ya maji katika kijiji cha Itetemya, Kapalamsenga, Kaseganyama, Kasekese, Nkungwi, Sibwesa, Ikaka, Kabungu mpaka Mpanda Mjini. (Makofi)

Meheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba sana Serikali ielekeze nguvu kutatua tatizo la maji kwa kuyatoa maji Ziwa Tanganyika. Kama maji yanatoka Ziwa Victoria kuja Mkoa wa Tabora, zaidi ya kilometa mia 300 itashindwaje kuyaleta maji kutoka Ziwa Tanganyika mpaka Manispaa ya Mpanda Mjini ambapo ni kilometa 120 tu? Nilikuwa naomba sana hilo tulipe nguvu ili tutatue tatizo la maji ndani ya Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu miradi ya maji vijijni; maeneo haya vijijini kunashida kubwa sana ya maji. Nilikuwa naomba sana kwenye jimbo langu, kata ya Muhesi ni eneo ambalo kuna tatizo kubwa sana la maji, na kuna chanzo kizuri cha kutega maji tu ambacho kingetatua sana vijiji vyote vilivyopo kwenye kata ya Muhesi vikawa havina tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tuna maeneo kwenye kata za Mishamo ambako kimsingi Serikali haikuwekeza, ni eneo ambalo kuna Watanzania wapya, eneo hili bado tunatatizo kubwa sana la miundombinu ya maji. Nilikuwa naiomba Serikali ipeleke huduma kwenye vijiji vya kata ya Mishamo, kata ya Ilangu, kata ya Bulamata ili kuweza kutatua tatizo la maji kwenye maeneo ambayo kimsingi yalikuwa yakihudumiwa na UN sasa hivi yako mikononi mwa Serikali. Tunaomba sana Serikali iongeze huduma ya maji kwenye vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya umwagiliaji; tuna miradi ya umwagiliaji ambayo ilianzishwa na Serikali. Eneo langu tunamradi wa scheme ya Karema, Mwamkuru na Kabage. Hii miradi imechukua muda mrefu sana na imetumia fedha nyingi ambazo kimsingi zimechezewa tu na watu ambao walipewa dhamana ya kuisimamia. Miradi hii inaonekana ni mashamba ya fedha ambayo yanaliwa, lakini hayaleti tija ambayo imekusudiwa na Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii miradi imepewa fedha nyingi, lakini haisimamiwi vizuri, bahati mbaya sana hata Wizara yenyewe ambayo inatoa hizo fedha haina usimamizi, ni fedha ambazo zinachukuliwa tu kiana aina na zinaliwa bila kuwa na usimamizi wowote. Naomba Serikali iangalie kwenye maeneo haya na ninaomba Serikali ituhakikishie itakapokuwa inaleta majibu hii miradi itaikamilisha vipi ili iweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni usimamizi wa miradi. Serikali itakuwa inatoa fedha nyingi na kutoa ndani ya Bunge na Waheshimiwa Wabunge wakashangilia kwamba wamepata miradi, kama hakuna usimamizi mzuri hakuna kitu chochote kitakachokuwa kinafanyika. Kwa sababu fedha inatoka Serikalini inaenda kwenye Halmashauri ambapo hakuna usimamizi, halafu zile fedha ukizifuatilia zinarudi makao makuu. Tunaomba hili likomeshwe, tusidanganywe tuwe tunapewa changa la macho kwamba tumeletewa fedha baadae zinarudi kule ambako zilitoka. Tunaomba hii tabia ikomeshwe na tuhakikishe kwamba imefanyiwa kazi ili iweze kutekelezwa kama ilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo tungependa kuchangia ni uwiano wa miradi ambayo tunagawiwa. Sehemu hii ni vyema sasa Serikali na Wizara kwa ujumla ikaangalia, kwa sababu fedha nyingi zinazotolewa ukiangalia mgawanyo ambao unagawanywa kwenda kwenye maeneo husika tunatofauti kubwa sana. Sasa tunaomba tupewe vigezo ni vigezo vipi ambavyo vinafanya maeneo mengine yanapata fedha nyingi na maeneo mengine yanapata fedha kidogo. Ukiangalia pengine maeneo ambayo yana fedha kidogo yana idadi ya watu wengi kuliko maeneo ambako yanapelekwa fedha zingine. Tunaomba Serikali iangalie ili tuweze kwenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la bajeti; bajeti ya Wizara ya Maji mwaka huu imepungua lakini bado Watanzania walio wengi wanahitaji huduma ya maji. Mimi niiombe Serikali, ni vyema sasa tukajipanga kuhakikisha bajeti hii inaboreshwa na tusitoe fedha kwenye zile mradi wa REA hapana, naomba tukate kwenye simu, tunaweza tukapata fedha nyingi sana ili ziweze kuwasaidia wananchi kupata maji ambayo yatawasaida walio wengi. Vijijini kuna matatizo makubwa sana ya maji, hasa kwa akina mama, ni vyema Serikali sasa ikaangalia mfumo wa kupeleka huduma ya maji vijijini ambako ndiko Watanzania waliowengi wanaishi. Inavyoonekana ukiangalia vitabu hivi, karibu asilimia kubwa ya huduma ya maji inapelekwa maeneo ya mijini, lakini tunadanganyika, asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi vijijini na hawa ndio ambao wanahitaji huduma ili waweze kuzalisha na kuweza kulisha wananchi wanaoishi mijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono, lakini nitahitaji majibu ya Serikali ili tuweze kuangalia ile miradi ambayo imeletwa na Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niunge mkono hoja ya Wizara ya Elimu. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kufanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa sekondari. Tuna tatizo kubwa sana kwani maeneo mengi yana upungufu wa majengo ya shule za sekondari. Pamoja na juhudi kubwa inayofanywa na wananchi kwa kujitolea asilimia 20 bado Halmashauri zinashindwa kuwasaidia kumalizia majengo ya shule. Niiombe Wizara iangalie uwezekano wa kusaidia kuboresha majengo na kujenga shule mpya pale ambapo ni stahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwenye Wilaya mpya ya Tanganyika tupatiwe msaada wa fedha za kumalizia shule za sekondari za Tongwe, Bulamata sekondari, Ilangu sekondari na Mazwe sekondari. Shule hizi zinahitaji msaada wa Serikali wa kuzifanyia ukarabati na kuongeza madarasa na nyumba za walimu na kujenga maabara pamoja na vyoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa na matatizo ya uchakavu wa majengo na ukosefu wa vyumba vya madarasa kwenye shule zetu za msingi, bado tuna tatizo kubwa la ukosefu wa walimu. Tunaomba Serikali iangalie umuhimu wa kuongeza walimu wa kufundisha kwenye mashule hizi hii ikiwa ni pamoja na kuongeza marupurupu ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madai ya walimu, kuna malalamiko makubwa ya walimu kuidai Serikali stahili zao ikiwemo kutopandishwa vyeo, kutolipwa posho zao za likizo, nauli na posho za madaraka. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aje na majibu ya uhakika juu ya suala zima la madai ya walimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vingi vya ufundi vina hali mbaya sana kwa kukosa vitendea kazi hasa vya kufundishia jambo ambalo linasababisha vishindwe kukidhi malengo ya kuanzishwa vyuo hivi. Niombe Serikali iboreshe Chuo cha VETA Mpanda kwani hakina vitendea kazi pamoja na walimu. Chuo hiki kinategemewa sana na wananchi wa Mkoa wa Katavi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya pamoja na Waziri husika wa Ulinzi na Usalama pamoja na wanajeshi kwa ujumla. Niwapongeze kwa kazi nzuri wanayoifanya ya uzalendo kwa nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nizungumzie sana suala la ulinzi na usalama hasa kwenye mipaka yetu. Mheshimiwa Waziri alipokuwa anawasilisha amezungumzia mpaka mrefu wa Mashariki. Mimi niiombe tu Wizara hii ielekeze nguvu sana kwenye mpaka wa Mashariki hasa kwenye maeneo ya Mkoa wa Pwani, Lindi na Mtwara ili kuhakikisha mipaka hii inaimarishwa vizuri. Maeneo haya kwa sasa yameanza kuwa na dalili za ugaidi. Ni dalili ambayo Jeshi la ulinzi ni vema likajipanga vizuri kudhibiti yale yanayojitokeza ili kuokoa Watanzania wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni mpaka wa Magharibi, kwa maana ya Ziwa Tanganyika. Niipongeze sana Serikali kwa kutuletea kituo cha Jeshi la Ulinzi kwenye eneo la jimbo langu pale Kata ya Ikola. Kituo hiki ni kituo muhimu na kimesaidia vitu vingi sana hasa mali za raia ambao kipindi cha nyuma walianza kuwa na wasiwasi mkubwa baada ya Waasi wa Kongo wale waliokuwa wakizidiwa wanakimbilia nchini kwetu na kufanya uhalifu kiasi kwamba wananchi wa mwambao wa Ziwa waliishi bila amani lakini baada ya kuweka kile kituo, ukweli kimewasaidia sana wananchi na amani ipo ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali hasa kupitia Wizara hii, tunaomba kile kituo mkiangalie kwa makini sana vitendea kazi ambavyo wanafifanyia shughuli pale havitoshelezi. Wanajeshi ambao wako pale hawana gari zuri la kufanyia kazi, hawana boti za doria ambazo kimsingi ni vitendea kazi vinavyohitajika ili viweze kusaidia usalama wa nchi yetu. Mimi nilikuwa naomba eneo hili liangaliwe sana, sambamba na kuwawekea umeme kwenye kituo chao ambacho wanafanyia kazi. Hata hivyo, bado wanajeshi wanaofanyakazi kwenye maeneo haya ni wazalendo kweli kweli; hata zahanati hawana. Mimi nilikuwa naomba Wizara iangalie umuhimu wa kuweka angalau kituo kidogo pale ambacho kitasaidia afya za wanajeshi kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishukuru sana Serikali kupitia SUMA JKT ambao tumewapa maeneo makubwa sana kwenye Wilaya ya Mpanda kwa ajili ya uwekezaji. Kuwapa nafasi ya kutengeneza mazingira ya uwekezaji kwenye Wilaya yetu kutasaidia sana kutoa elimu kwa wananchi hasa wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapojipanga kuwekeza kupitia SUMA JKT, niombe yale maeneo ambayo watakuwa wamepewa wafanye kazi ya kuwasaidia wananchi wanaozunguka miradi ile ya maendeleo kwenye eneo hilo. Hii ni sambamba na kuwashirikisha, kuwapa elimu hasa kwenye suala zima la kilimo,ufugaji pamoja na kusaidia pembejeo kama watakuwa wanazo kwenye maeneo yale ili Jeshi liwe na dhamana ya kutengeneza mazingira ya kwao na kusaidia wananchi ambao kimsingi Halmashauri imetoa eneo bure bila kutoza gharama ya aina yoyote. Ninaomba sana katika hili Serikali kupitia JKT lisaidie kwenye maeneo hayo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, JKT wamepewa maeneo yale ni pamoja na kuomba msaada wa kusaidia suala zima la uhifadhi mazingira. Eneo hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa na uvamizi wa mazingira ambayo wananchi wanaingia kwenye misitu; sasa tunaamini ujio wa SUMA JKT utasaidia pamoja na kutatua tatizo lile la uharibifu wa mazingira ambayo kila mara unakuwa inajitokeza kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hali ya usalama, tuna misitu mikubwa sana ambayo ni pamoja na Msitu wa Tongwe Mashariki, Msitu wa Tongwe Magharibi. Kimsingi eneo hili linahitaji msaada sana ambao tutahitaji SUMA JKT watakapokuwa wanafanya shughuli zao za uzalishaji watusaidie na hali ya kutunza usalama kwenye maeneo yale na ikizingatiwa maeneo ambayo tayari tulikuwa ni maeneo yaliyokuwa na wakimbizi, kwa sasa hivi ni maeneo ambayo tayari wamekuwa Watanzania wapya. Hata hivyo wapo wachache ambao wanafikiria mazingira bado ni yale yale. Kwa hiyo, tutaiomba Serikali idhibiti wale wachache wenye malengo mabaya tofauti na Serikali ili waweze kutusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niombe sana ushirikiano na Serikali kwa ujumla, kwamba tunaomba sasa nafasi za kazi zitakapotoka wananchi wa maeneo yale wapewe kipaumbele ili waajiriwe na Jeshi la Kujenga Taifa kwa sababu ni nafasi pekee ambayo tumeipata itakayowasaidia Watanzania wote kwa ujumla na Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Nami nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa dhamira ya dhati ya kuleta viwanda nchi nzima. Sera ya Viwanda ni sera nzuri sana ambayo kimsingi, yeyote atakayeipinga ni yule ambaye hajui umuhimu wa viwanda katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sera hii imeoanisha mazingira mazuri kwamba kila mkoa ni lazima kuwe na viwanda ambayo vitawasaidia wananchi wetu kuweza kukuza uchumi ndani ya maeneo yao. Nzuri zaidi ni pale ambapo sera hii inaonesha maeneo ambayo yalisahaulika hasa pembezoni, yapewe kipaumbele ili yaweze kunufaika na mpango wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri tu Serikali kwamba, katika sera ambayo imewekwa, Sera ya Viwanda ni vyema wakaangalia mazingira ili tupeleke viwanda mahali ambapo uhitaji wa viwanda unafanana na mazingira yenyewe. Leo hii unapopeleka kiwanda cha kusindika ngozi kwenye maeneo ambayo hayana hata mifugo, hujawasaidia wananchi pale, hasa wale ambao wanatoka kwenye maeneo ya ufugaji. Ni vyema vile viwanda ambavyo vitakuwa vinahusiana na Sekta ya Mifugo, tukawapelekea kwenye maeneo husika ya uzalishaji ili viweze kutoa ajira kwenye maeneo ambayo wananchi wenyewe wanahusika na kulengwa moja kwa moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tulikuwa tunaomba kuangalia mazingira ya kuboresha Sekta ya Viwanda hasa viwanda vidogo vidogo. Kwenye maeneo haya ni vema Serikali sasa wakawa na mipango thabiti itakayokuwa inaunganisha nchi nzima na kwa kuwashirikisha Wakuu wa Mikoa ili waweze kutenga maeneo ambayo yatakuwa rafiki kuwasaidia wananchi ambao kimsingi tukiboresha kwenye Sekta ya Viwanda vidogo vidogo, tumewasaidia wananchi walio wengi. Huko ndiko ambako ajira zinatengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri, lazima aje na mpango mkakati wa kuwashirikisha Wakuu wa Mikoa ili kuhakikisha maeneo ya viwanda vidogo vidogo yanapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali itusaidie mikoa ya pembezoni; kule tunazalisha. Mkoa wangu ulishatenga maeneo ya uwekezaji. Nafikiri kila kitu kipo sawa, lakini tunaomba sasa ielekeze suala zima la kuwekeza kwenye mazao yanayozalishwa na wananchi hasa kwenye Sekta ya Kilimo. Tukielekeza huko, tutawasaidia sana wananchi ambao ni wengi. Mazao ya mafuta yanayozalishwa, tukiweka mipango mikakati mizuri, kwamba yale mazao ya mbegu za mafuta ambayo yanazalishwa, tukajenga viwanda vidogo vidogo huko, tutakuwa tumewasaidia sana wananchi ili waweze kujikwamua kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mazao ya chakula. Mkoani kwangu tunazalisha chakula kingi na tunauza mazao ambayo bado hayajasindikwa. Naiomba Serikali, pale ambapo tunafikiria mikoa ya pembezoni; Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Rukwa na Mkoa wa Kigoma ni vema sasa tukawa na viwanda ambavyo vitafanya kazi ya kuwasaidia wananchi kwenye maeneo hayo na eneo hilo likawa na ukuzaji wa kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuna mazao ya biashara; tuna zao la tumbaku kwenye Mikoa hiyo ya Tabora, Kigoma na Katavi. Hatujakuwa na kiwanda maalum ambacho kitasaidia kukuza zao hili. Ni vema sasa Serikali ikaja na mpango ambao utasaidia maeneo hayo ili kupata kiwanda ambacho kitasaidia kukuza uchumi ndani ya maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo mazuri ya kivutio cha uwekezaji. Lipo zao la miwa, kama Mkoa wa Kigoma wangepewa fursa, wana mabonde mazuri. Mfano, bonde la Mto Malagarasi; katika Mkoa wa Katavi, Rukwa vile vile; tunahitaji tupate Kiwanda cha Sukari kwenye maeneo haya ili tuweze kupunguza bei ya sukari kwenye maeneo ya pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado naiomba Serikali iandae mazingira ya kujenga Kiwanda cha Saruji kwenye maeneo haya; ni maeneo ambayo bei za saruji ni kubwa kweli kwa sababu viwanda vingi vimeelekezwa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkoa wa Pwani lakini maeneo ya pembezoni hakuna. Naiomba Serikali iweze kutengeneza mazingira mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie dhamira ya Serikali. Serikali imeonesha wawekezaji wengi kwa kushirikisha Mifuko ya Maendeleo ya Jamii; NSSF, PPF, PSPF na mengine, mashirika ambayo tukiweka ubia yana nafasi ya kuweza kusaidia kukuza uchumi. Ni dhamira nzuri ambayo Serikali imeweka; ni vizuri sasa tukawa na uwiano kwenye maeneo yote yasiwe yanaelekezwa kwenye maeneo maalum tu hasa Kanda ya Mashariki. Naomba Serikali iangalie mazingira haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nizungumzie eneo ambalo watu wengi wamekuja wanafananisha bei za chakula nchini Kenya na bei za kwetu hapa. Niwaambie wananchi tu kwamba, zipo propaganda ambazo zinaenezwa. Tukiangalia uhalisia, bado bei ya sukari kwa nchi yetu ipo chini kuliko bei ya sukari kwenye maeneo ya nchi ambazo ni jirani zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kenya leo hii bei ya sukari ni Sh.3,195/=, Uganda ni Sh.3,550/= mpaka Sh.4,000/=, Burundi ni Sh.3,700/= mpaka Sh.4,000/=. Tanzania bei ya sukari ipo kati ya Sh.2,700/= mpaka Sh.3,000/=. Bado maeneo mengine yote yanayotuzunguka yanahitaji kutoka kwetu kupata bidhaa muhimu kama hiyo. Ni vema sasa watu wakaacha kutumia propaganda ambazo kimsingi wenzetu sasa hivi wanazitumia kwa masuala ya kisiasa. (Makofi)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi ya kuchangia. Awali ya yote, niipongeze sana Serikali kwa kuja na mfumo mpya wa uagizaji mbolea. Eneo hili nawapongeza sana kwa sababu ndiyo eneo ambalo litawasaidia sana wakulima wa nchi hii ili kuepukana na mfumo uliokuwepo zamani uliokuwa unawanufaisha wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niiombe Serikali isirudi nyuma na nimwombe Waziri, najua anafanya kazi ambayo itakuwa ngumu sana, wapo watu ambao walikuwa wananufaika na biashara hii kwa hiyo ni vizuri wakajipanga wasirudi nyuma. Naamini kuleta mbolea kwa pamoja litapunguza gharama kubwa sana ya bei ya pembejeo na pale ambapo atakuwa amekwama zaidi tutahitaji sana kumsaidia ili tuweze kusonga mbele na kuwasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili nashauri, hata zile mbolea za NPK, KANI na SA zina uwezekano kabisa wa kuweza kuisimamia Serikali ikaweza kuagiza mbolea hizi, upo uwezekano. Naamini tu tukifanya jitihada za pamoja wakishirikisha na wadau wataweza kusaidia zoezi hili likakamilika na likawasaidia wananchi wote kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni suala la tozo ambalo limeletwa na Serikali. Tunaipongeza sana Serikali imetengeneza mazingira mazuri ya kuboresha mazao karibu yote kwa kupunguza zile tozo ambazo zilikuwa ni kero kwa wakulima wetu. Kuna maeneo ambayo zipo tozo zimeelekezwa hasa kwenye vyama vya ushirika, ni vyema wakaziangalia kwa undani zaidi tozo hizo kwani kuna baadhi ya maeneo wanaweza wakaviua vyama vya ushirika, vyama vya ushirika vinategemea sana tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa umahiri alionao Waziri atawashirikisha wadau kabla ya utekelezaji ili waangalie vile vyama visije vikafa kwa sababu ukiua vyama vya ushirika havina nafasi ya kuweza kushindana na makampuni. Vyama vya ushirika pekee ndivyo ambavyo vikiungana vina nafasi ya kuweza kutoa ushindani kwa haya makampuni ambayo yananufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zipo tozo ambazo zimeonesha wazi kwamba zinayasaidia makampuni ili yapunguze gharama sasa naomba Waziri aangalie tozo zile. Tunaweza tukatoa hizi tozo zikawasaidia makampuni moja kwa moja bila kwenda kwa mkulima. Ni vyema wakaangalia na wakachambua zile tozo mbalimbali ili zingine ziwarudie wananchi na kufanya zao liweze kuwa na bei nzuri kuliko tukitoa tu nafuu ni ya kuyabeba sana makampuni. Niombe sana hili waliangalie na naamini wataalam waliopo watasaidia kuchambua zile tozo ili ziweze kusaidia wananchi kama Serikali ilivyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye sekta ya uvuvi, kwangu kuna Ziwa Tanganyika ambalo kimsingi bado sekta hii haijafanya kazi vizuri sana. Tunaiomba Serikali iwasaidie wale wavuvi wa wadogo wadogo iwape mazingira ambayo yatawawezesha kufanya shughuli zao za uvuvi bila kupata shida. Ni vizuri tukaangalia vile vikundi vya wavuvi vikasaidiwa na Serikali ili viweze kutengeneza tija.
yangu ya Tanganyika tulileta maombi maalum ya kulima zao la pamba. Tayari wakulima walishafanya jitihada zao, wameonesha nia njema na nimshukuru alinipa ushirikiano na kuagiza wataalam wakaenda kuangalia jitihada ambazo zimefanywa kule. Kwa hiyo, nina imani eneo hilo tunahitaji kibali tu kwa msimu ujao ili wakulima wale waliojipanga waweze kulima lile zao liwasaidie na kuongeza kipato kwani watakaponufaika kwenye eneo hili litawasaidia sana kwa Serikali na wananchi kuongeza kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa bado kuna dakika moja, naomba niongelee sana miradi ya uwamgiliaji.
Nchi yetu ili iweze kwenda inahitaji sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Maji na Naibu Waziri na wasaidizi wake wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa miradi mikubwa inayotekelezwa jimboni kwangu. Nina mradi mkubwa wa kijiji cha Majalila na kijiji cha Igagala imetekelezwa na kutoa huduma kubwa sana kwa wananchi.

Naiomba Serikali kupitia Wizara juu ya miradi ya Mwese, Ilangu, Kamjela na Kabungu ambayo bado haijatekelezwa. Tunaomba Wizara isimamie kutekelezwa kwa miradi hiyo ambayo itawasaidia wananchi katika vijiji hivyo nilivyovitaja na ilitengewa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba ukarabati ufanyike katika visima katika vijiji vya Mishamo ambavyo vilichimbwa na Shirika la Wakimbizi la UNHCR mwaka 1978. Tunaomba vikarabatiwe ili viweze kutoa huduma ya maji kwenye vijij hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa ukarabati wa vijiji hivyo vya Ilangu, Bulamata, Kamjela, Ifumbula, Mazwe, Kapemba, Isenga Mazwe, Kusi Rugufu, Kabanga, Mgansa, Busongolala, Ipwaga na Mlibansi kunaweza kutatua tatizo la maji kwa gharama nafuu. Naomba sana vijiji hivi mvipatie fedha za kukarabati visima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Kijiji cha Ngomalusambo uliibiwa fedha, tunaomba wahusika wa mradi huu wachukuliwe hatua kwani mradi huu umesababisha hasara zaidi ya shilingi 280,000,000 ambazo zimetumika bila kutoa maji. Wahusika wapo na hakuna hatua iliyochukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na tatizo la ukosefu wa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo ya maji. Hivyo tunaomba Serikali iongeze tengo la fedha ili tuweze kutekeleza miradi na mahitaji ni makubwa sana kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali katika utekelezaji wa miradi iwe na udhibiti mkubwa ili iwe na tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Kamisheni ya Pamoja ya Bonde la Mto Songwe kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Malawi pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Amani na Usalama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kunipa nafasi hii kuchangia maazimio ambayo yamewasilishwa kwenye Bunge hili. Kwanza ninapongeze kwa uwasilishaji ambao wawasilishaji wote wameyaelezea kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la amani suala la msingi sana katika nchi yetu. Ili nchi iweze kufanya kazi vizuri ni sharti tuwe na amani ya kutosha, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri alipokuwa anawasilisha ni vema sasa kama Bunge tuli-support Azimio hili kwa ajili ya kulinda amani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi tunaoishi mipakani bado kuna shida kubwa sana ya Watanzania ambao wengine wanaishi bila kuwa na uhakika mzuri wa maisha yao, tunaiomba sana Serikali iimarishe suala zima la ulinzi na usalama hasa maeneo ya mipakani. Mimi natoka Mkoa wa Katavi ambao tumepakana na Ziwa Tanganyika pia nchi ya Congo tumepakana nayo. Wapo Watanzania ambao wanaishi mazingira ambayo siyo sahihi. Naomba sana Serikali iweze kuangalia mazingira hasa nchi zile zinazopakana na Maziwa kama ilivyo Mkoa wa Katavi, Rukwa na Kigoma maeneo haya tunahitaji sana kuweka ulinzi shirikishi katika nchi zote tunazopakana nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Watanzania ni watu wakarimu, tumeweza kuwapokea wananchi wa Mataifa mbalimbali kama Congo, Burundi lakini mazingira tunayoishi kule ni mazingira ambayo Serikali inahitaji kuweka ulinzi shirikishi ili kupunguza haya matatizo ambayo yanaweza yakajitokeza. Naipongeza Serikali kwa Azimio lililoletwa, naamini litakuwa suluhisho kwa nchi zote za Afrika Mashariki na zile ambazo ziko nje ya Afrika Mashariki kama DRC-Congo tuweze kuazimia yale ambayo yamewekwa ili yawe na tija kwa Taifa letu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni juu ya Bonde la Mto Songwe. Bonde la Mto Songwe, Azimio lililoletwa ni muafaka lakini lina mazingira ambayo yanafanana na maeneo mengine. Nizungumzie maeneo ya Mkoa wa Katavi.

Tunayo mabonde ambayo yametoka, tuna mito ambayo imetoka maeneo ya kwetu na imeenda mpaka nchi ya DRC- Congo, tuna Mto Lwegere ambao umevuka Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna madhara ya suala zima la mazingira. Upande wa Congo, Ziwa Tanganyika linapeleka maji ambayo yanaleta athari kwa nchi yetu, sasa ni vema tunapoweka mikataba hii tuangalie na maeneo mengine ambayo kimsingi yanaweza yakachangia suala zima la maendeleo na suala zima la mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, nje ya hapo tuna Mto Nile ambao unatoka Ziwa Victoria. Ni vema sasa tuangalie mazingira ambayo yatakuwa ni mazuri kwa nchi yetu, kuwatengenezea mazingira mazuri hasa Watanzania. Mfano, Mto Nile ni mto ambao unatoka kwenye maeneo yetu lakini Wamiliki wakubwa wa Mto Nile ni wenzetu watu wa Misri, ni vizuri tukaangalia maeneo haya, tukayapitia upya ili yawe na manufaa kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mazingira ni suala ambalo linahitaji sasa liwekewe kipaumbele na Wizara husika ili tuweze kulinda Mabonde na mito ambayo kimsingi inahama. Bonde la Mto Songwe linahama na ndiyo maana limeletwa hapa kwa sababu mipaka huwa inahama kutoka sehemu moja hadi sehemu nyingine, lakini bado kwenye maeneo yetu ya ndani, leo hii tunapozungumzia mabonde haya ambayo chanzo ni uharibifu wa mazingira, tuna Mto Katuma ambao unapeleka maji kwenye hifadhi ya Katavi na unapeleka maji mpaka kwenye Ziwa Rukwa, leo hii Ziwa Rukwa linapoteza thamani yake na upo uwezekano wa kutoweka kabisa, ni kwa sababu hakuna ulinzi mzuri wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Waziri mwenye dhamana aendelee na jitihada ambazo zitatengeneza mazingira mazuri ili kujenga mikakati ya kulinda suala zima la mazingira, lakini cha kufurahisha kwenye Azimio hili ni juu ya mpango wa uwezeshwaji wa kiuchumi kwenye maeneo yote. Tuwaombe sasa Wataalam waweze kushughulikia uhalisia wa kutengeneza mazingira ambayo yatalinda hadhi ya Watanzania waweze kuwezeshwa kiuchumi ili waweze kuendana na uhalisia wa mabonde haya ambayo wamezungukwa nayo kwenye maeneo ya mipakani.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado tuwaombe sana wataalam wetu watengeneze mazingira ya kisheria yatakayolinda nchi yetu ili Watanzania na wale ambao wanazunguka katika maeneo hayo wawe na faida na haya Maazimio tunayoyakubali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikupongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa unayoifanya ya kulinda maliasili ya nchi hii.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie juu ya utalii wa Ukanda wa Magharabi, Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma. Eneo hili la ukanda huu Serikali haijawekeza kabisa ambao una vivutio vingi vya utalii. Mkoa wa Rukwa kuna maporomoko ya Kalambo na Ziwa Rukwa na misitu mizuri ya kuvutia. Mkoa wa Katavi una mbuga nzuri ya Katavi National Park, mbuga ambayo ina wanyama wakubwa wenye afya njema na ndiyo mbuga pekee yenye twiga mweupe anayepatikana Katavi peke yake.

Mheshimiwa Spika, tunaomba mbuga hii muitangaze sambamba na kuweka miundombinu ya maji ili kunusuru wanyama wanokufa kwa kukosa maji wakati wa kiangazi Mto Katuma unapokauka.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma kuna mbuga ya Mahale jirani na Mkoa wa Katavi na Hifadhi ya Gombe. Mheshimiwa Waziri tunaomba ukanda huu utengwe kwa ajili ya utalii. Sambamba na hilo kuna fukwe nzuri ya Ziwa Tanganyika ambako watalii wengi wa kutoka nchi ya Israel wangependa sana kufanya utalii wa boti ndani ya Ziwa Tanganyika. Tatizo kubwa bado miundombinu ya kuvutia watalii haijawekwa. Tunaomba Wizara yako muweke mikakati ya kuwekeza katika kuweka miundombinu zikiwemo ununuzi wa boti ya kisasa na kushawishi wawekezaji wa kujenga hoteli za kisasa.

Mheshimiwa Spika, nitoe shukrani za dhati kwako wewe Mheshimiwa Waziri kwa kuidhinisha Pori la Tongwe Magharibi kumilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika. Mheshimiwa Waziri Wana Tanganyika wanakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuongoze vyema katika majukumu yako ya Wizara. Pia nakupongeza na kukushukuru sana kwa kutupatia gari ya doria Wilaya ya Tanganyika. Tunaahidi tutalifanyia kazi na kulitunza kwa ajili ya uhifadhi wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kunipa nafasi ya kuchangia bajeti hii. Awali ya yote niipongeze Serikali kwa kazi nzuri sana ya kuleta bajeti hii ili iweze kuwa ya mfano na kusaidia wananchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa sababu imekuja na mpango mzuri. Niwapongeze Kamati ya Bajeti kwa kuja na mapendekezo mazuri ya kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo nataka kuzungumzia ni suala zima la Serikali kuja na mpango wa kujenga au kuanza uchimbaji makaa ya mawe na chuma Mkoani Njombe. Eneo hili litakuza uchumi mkubwa sana kwa Serikali ya nchi yetu na itafanya maeneo haya ya ukanda wa kusini na Serikali kwa ujumla kuwa na kipato kizuri.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tunaishauri Serikali iwekeze kwa nguvu zote ni ujenzi wa reli ya kati. Ujenzi wa reli ya kati ni suluhisho kwa wananchi wa maeneo karibu yote ya nchi hii. Asilimia kubwa wananchi wa kada ya chini

wanatumia sana usafiri wa reli. Kwenye maendeleo, tukiboresha eneo la ujenzi wa reli ya kati tutakuwa tumesaidia sana wananchi wa maeneo ya nchi hii. Siyo tu kwa maeneo ya Dar es Salaam, lakini tutakuwa tumetengeneza uchumi wa Mikoa mingi kuanzia Dar es Salaam mpaka Mkoa wa Kigoma.

Mheshimiwa Spika, sambamba na tawi la reli la kutoka Tabora kwenda Mwanza, naamini uchumi kwenye maeneo hayo na maisha bora kwa kila Mtanzania yanaweza kupatikana kwa kiwango kikubwa sana. Niiombe sasa Serikali kwenye bajeti hii iwekeze nguvu kubwa sana kwa ajili ya kuimarisha ujenzi wa reli ya kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado kuna maboresho ambayo yamefanyika, maboresho ya Shirika la Ndege, ujenzi wa mitambo ya gesi, ni maendeleo ambayo yanategemewa sasa kwa Serikali yanaweza yakatoa suluhisho kubwa na kupata mapato makubwa ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, eneo ambalo ningependa kushauri Serikali ni kuachana na uwakala wa kukusanya kodi ya nchi ya Congo. Eneo hili tunapoteza mapato makubwa sana. Ni vema Serikali ikaangalia ule mkataba ambao tumewekeana na Congo, hauna manufaa kwetu sisi. Karibu wafanyabiashara wengi wa nchi ya DRC wamehama kutumia Bandari ya Dar es Salaam, kwa hiyo ni vizuri kwenye maeneo haya wakatazama upya ili kuweza kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, nina ushauri kwa Serikali. Ni vizuri sasa Serikali ikaangalia upya, nchi ya Zambia ni miongoni mwa nchi inayotegemea sana Bandari ya Dar es Salaam lakini bahati mbaya Zambia wanalipa ada tofauti na nchi zingine. Ni Vizuri Waziri wa Fedha akakaa na wenzetu wa Zambia wakaangalia zile tofauti ambazo zipo wakazitoa ili wenzetu waweze kutumia Bandari ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo ningependa kuzungumzia sana ni kwenye sekta ya kilimo, kwenye sekta ya kilimo, ni eneo pekee ambalo tukiwaboreshea wakulima wa nchi hii watakuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa sana wa pato la Taifa. Tunaomba sana Serikali iangalie kuweka mazingira mazuri yatakayowasaidia wananchi kupata pembejeo zenye bei nafuu. (Makofi(

Mheshimiwa Spika, tunapowawezesha wakulima, tumewawezesha wananchi karibu wote wa nchi yetu. Ni vema sasa Serikali ikaja na mkakati wa kusaidia hawa wakulima wadogo, wavuvi na wafugaji ili iweze kuwawekea mazingira ambayo yatakuwa rafiki kwenye uzalishaji kwa gharama nafuu na kuwawekea miundombinu ambayo itawasaidia sana katika kuboresha shughuli za kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ili nchi iweze kwenda vizuri Serikali sasa iangalie uwezekano wa kuweza kusaidia wakulima wakubwa. Ni vema tukaangalia hata Taasisi za Serikali tulizonazo, tukawekeza kwenye Jeshi la Magereza, Jeshi la JKT, tukawawezesha waweze kuzalisha kilimo kikubwa, wakalima mashamba makubwa ambayo kimsingi kwanza yatatatua tatizo la njaa, lakini bado watakuwa na ziada ya kuweza kuzalisha hata kuuza nchi za nje na kuleta pato la Taifa. Kwenye eneo hili tukifanya vizuri tutakuwa tumewasaidia sana Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine naishauri Serikali, dhamira ya Serikali ni kupeleka umeme vijijini. Naomba Serikali sasa ipeleke umeme vijijini na iangalie maeneo yote ya nchi. Tusije tukawa na maeneo ambayo mengine yananufaika na sehemu nyingine hakuna. Ni vizuri umeme vijijini ukapelekwa kwenye maeneo yote hasa kwenye mikoa ile ambayo iko pembezoni. Nafurahi Mheshimiwa Waziri wa Fedha na yeye ametoka kwenye maeneo ya pembezoni, anajua mazingira jinsi yalivyo. Naomba sana Serikali iweze kuangalia maeneo hayo ili iweze kuwasaidia wananchi.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara. Nchi yetu

ilikuwa na dhamira ya dhati kuhakikisha Mikoa yote inaunganishwa. Namwomba sana Waziri wa Fedha aangalie sasa uwezekano wa kuunganisha mikoa ambayo bado haijaunganishwa kwa barabara za lami. Mkoa wa Rukwa uunganishwe na Katavi, Mkoa wa Katavi na Kigoma, Mkoa wa Tabora na Kigoma, Mkoa wa Katavi na Tabora. Tunahitaji maeneo yote hayo yaweze kuunganishwa ili yaweze kutoa mchango mzuri kwa pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haya maeneo yalisahaulika. Kwenye bajeti hii tunaomba sasa dhamira ile ya Serikali iweze kuonekana. Mheshimiwa Waziri wa Fedha anajua mazingira yalivyo na anakotoka. Tayari Mkoa wa Kigoma hauna mawasiliano na Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Kigoma hauna barabara za lami na Mkoa wa Katavi; Mkoa wa Kigoma bado hauna mawasiliano na Mkoa wa Tabora sambamba na Katavi na Tabora. Tunaomba ile miradi iliyopangwa iweze kusimamiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nisisitize zaidi huduma ya maji vijijini. Tunaomba sana, fedha ambazo zinapatikana kwa michango ambayo tutaichangia hasa ile Sh.40/=, tuielekeze iende kutatua tatizo la maji. Katika maeneo haya tutakuwa tumewasaidia sana wananchi hasa akinamama walio wengi vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba na kuishauri Serikali iangalie mazingira haya kuyaboresha na tupeleke hii miradi iweze kwenda kuwasaidia wananchi kwenye maeneo hayo ili waweze kufanya shughuli za uzalishaji kwani bila kuwa na maji uwezekano wa kupata nafuu ya kuzalisha ni mdogo sana...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii. Awali niipongeze sana Wizara hii kwa jitihada za kazi wanazozifanya ndani ya Wizara hii. Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake pamoja na wasaidizi wake wamefanya kazi nzuri sana. Tunawapongeza hasa kwa kutatua migogoro mingi ambayo kimsingi ilikuwa inawagusa sana wananchi. Tunawapongeza na kuomba tuwaombee heri sana waendelee kutenda haki na misingi iliyowekwa ya kisheria juu ya kuwasaidia wananchi hasa walalahoi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuzungumzia tatizo la migogoro ya ardhi ya vijiji vya Kabage, Sibwesa, Mkungwi, Kagunga na Kapanga vilivyoko kwenye Wilaya ya Mpanda. Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ina mgogoro wa muda mrefu sana wa vijiji hivi, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri apange ziara aje amalize tatizo hili, akishirkiana na Wizara ya Maliasili. Wananchi wengi wanataabika hawana ardhi ya kufanyia kazi wakati ni vijiji halali ambavyo kimsingi kama vitasimamiwa tatizo hili tutakuwa tumelipunguza na kuwafanya wananchi waendelee kufanya shughuli zao. Naomba sana Waziri husika aje atatue matatizo ya Mkoa wa Katavi hasa Wilaya hii ya Tanganyika iliyoko kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni tatizo la kupata hati za kimila kwenye Wilaya ya Tanganyika. Karibu maeneo yote ya vijijini tuna tatizo kubwa sana la kukosa huduma ya kupata hati za kimila. Kuwasaidia wananchi hawa wanapopata hati za kimila tunawajengea uwezo wa kiuchumi, kwani watapima mashamba yao na watakuwa na nafasi ya kutumia dhamana ya hati miliki ili waweze kwenda kwenye taasisi za fedha, huduma hiyo kwetu sisi hatuna. Naomba Waziri aone kwamba ni wakati muafaka sasa kupeleka huduma hii kwenye maeneo yote ya nchi yetu hasa maeneo ya pembezoni kwenye Wilaya hasa zile ambazo ni changa. Tunahitaji huduma hii ili iweze kutatua matatizo yanayoikabili Wilaya kwa kukosa huduma ya hati miliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni uhaba wa wafanyakazi. Wataalam wa ardhi hasa Wilaya mpya, naamini na nchi nzima bado kuna tatizo kubwa sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri anapokuja aje na majibu sahihi yatakayosaidia kutoa
suluhisho hasa wataalam hawa ambao kimsingi wanahitajika ili waweze kufanya kazi ambazo zitawasaidia wananchi na kutatua migogoro mingi ambayo iko kwenye Halmashauri za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo tunahitaji kupata vitendea kazi, wataalam ambao wapo hata huko kwenye Wilaya hawana vitendea kazi vya shughuli ya upimaji ambavyo ni pamoja na magari. Unakuta Halmashauri haina gari, haina vifaa ambavyo vinahitaji kwa shughuli za kupima hivyo viwanja, matokeo yake wanaenda kwa miguu kitu ambacho hawawezi kutekeleza na kwenda na kasi ambayo ipo. Tunaomba sana hasa kwenye Wilaya yangu tupate wale ambao wana uwezo wa kufanya hiyo kazi ili tuwasaidie Watanzania. Kimsingi tukitekeleza hili tutakuwa tumetoa kero kubwa ambayo inawakabili wananchi kwa kukosa huduma. Tukipata hao watalaam nina imani kwamba eneo zima la suala la ardhi na migogoro ambayo tunaizungumzia itapungua kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya. Pili, nichukue nafasi ya kipekee kwa kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Selemani Jafo kwa kazi kubwa anayoifanya kwa kuwatumikia Watanzania wote bila ubaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza miradi ya Sekta ya Afya hasa katika kufanikisha kunipatia fedha za Vituo vya Afya vya Karema, Mwese na Mishamo; zaidi ya hayo, ni kutenga fedha za Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika. Pia nitoe shukrani kubwa kwa kunipatia gari ya ambulance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo naomba sana Serikali itusaidie, ni kutupatia magari ya Sekta za Elimu katika Wilaya ya Tanganyika, Ujenzi na Afya. Kuna tatizo kubwa kwani Halmashauri ya Mpanda DC haina magari kutokana na halmashauri hii kuwa mama wa halmashauri zote zilizopo Mpanda, hivyo kupelekea kila halmashauri iliyogawanywa kuchukua magari kutoka halmashauri mama na matokeo yake halmashauri hii haina magari ya kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uhaba wa Walimu; naomba tatizo hili liangaliwe sana hasa katika maeneo ya pembezoni ambako hakuna kabisa walimu hasa wa masomo ya sayansi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la barabara za vijijini ambazo zinahudumiwa na TARURA; tunaomba eneo la Mishamo lipewe budget ya kutosha, kwani eneo hili lina barabara kiasi cha kilometa 1008 ambazo TARURA pekee kwa bajeti inayotengwa haiwezi kutekeleza. Hivyo, tunaomba maombi maalum ya kutenga fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji, hasa katika shule na kwenye zahanati tunaomba iangaliwe na kusimamiwa ili iweze kuwasaidia wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nipate nafasi ya kuchangia Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa kuleta mpango mzuri na nishukuru sana Serikali kwa miradi ambayo imeanza kutekelezwa kwenye maeneo ya Jimbo langu na Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianzie na suala la kilimo. Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa, Rukwa, Katavi na Songwe ni mikoa ambayo inategemea sana kilimo cha mazao ya mahindi na mpunga, kwa ujumla ni wazalishaji wa nafaka ambao wanalisha sehemu ya nchi yetu kwa ujumla. Kwa bahati mbaya sana mikoa hii imepata balaa kwa sababu ya kuzalisha hizo nafaka ambazo kimsingi zinasaidia maeneo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo tunaona kwa mikoa hii tuna balaa ni kwamba Serikali ilipiga marufuku kuuza mazao ya aina ya nafaka kwa maana ya mahindi na mpunga kuuza nje ya nchi jambo ambalo kwa sasa linawatesa sana Watanzania wa mikoa hiyo. Ninaiomba sana Serikali ifike mahali sasa waangalie kwamba kuchagua zao la mahindi kulima si sehemu ya adhabu kwa wananchi wa mikoa hiyo, kwa sababu wananchi wanajitegemea, wanafanya shughuli za kilimo kwa kujituma sana, wamezalisha kwa kiwango cha juu mpaka wamepata ziada na matokeo yake eneo hilo mkulima hanufaiki na kitu chochote na inaonekana kwamba mkulima wa zao la mahindi hana thamani kubwa kwa sababu zao hilo halina soko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Serikali wasipochukua umuhimu wa aina yake wa kuangalia kutatua tatizo la ukosefu wa soko la mazao hayo wananchi hawatafanya shughuli za uzalishaji na mwakani kunaweza kukajitokeza njaa kubwa sana kwa sababu wanaona watalima kilimo cha kujikimu wao na familia zao tu. Ni vema Serikali lile katazo ambalo waliliweka wakaliondoa ili liweze kuwasaidia wananchi waweze kufanya shughuli zao. Sasa hivi wakulima watoto wao hawaendi shule, hawana uwezo wa kufanya shughuli za maendeleo kwa sababu mazao yako ndani, Serikali hakuna ilichowasaidia na ukizingatia mkulima huyu katumia nguvu zake zote kwake yeye binafsi na wala Serikali haikumsaidia kitu chochote. Kwa hiyo, naomba mliangalie hili na muone ni jinsi gani mnawasaidia wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zao la tumbaku. Mkoani kwangu wakulima wanazalisha zao la tumbaku, lakini si mkoa wa Katavi tu na mikoa jirani ya Tabora, Mbeya, Kigoma, Kahama kwa maana ya mkoa wa Shinyanga wanalima zao la tumbaku na Mikoa mingineyo. Wakulima walizalisha zao la tumbaku wakajituma, wamefanya shughuli njema wamezalisha lakini zao lile halina soko mpaka sasa na tumbaku yao iko ndani. Niombe sana Serikali wasiliangalie jambo hili kama ni jambo ambalo ni dogo, ifike mahali Serikali waangalie umuhimu wa kusimamia mazao mengine kama walivyosimamia korosho, walivyosimamia kahawa na mazao mengine kama pamba, walipe kipaumbele zao hili, kwa sababu ndiyo zao lililokuwa linaongoza kwa uzalishaji mkubwa na kuingiza kipato kwa Taifa letu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao hili limesaidia sehemu za Halmashauri ambazo wanazalisha zilikuwa na kipato kizuri kuliko ilivyo sasa, ni vema sasa Serikali ikaona umuhimu wa kulisimamia zao hili ili na wao waweze kunufaika kama mazao mengine yalivyosimamiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jitihada za Serikali zilizofanywa hasa kupeleka umeme vijijini. Niipongeze Serikali kwa juhudi ambazo zimefanyika lakini niombe sasa Serikali ielekeze nguvu sana kuhakikisha ile miradi ya umeme Phase III inafanyiwa kazi na inasambazwa kwenye maeneo husika. Jimboni kwangu nina vijiji 32 ambavyo vipo kwenye mpango. Mpaka sasa bado hata kijiji kimoja hakijafanyiwa kazi kwa sababu umeme uliokuwa umepangwa kuanza Phase III bado. Ulioanza kufanyiwa kazi ni ule ambao ulikuwa wa mpango wa Orion ambao vijiji vitano wamepata, tunaishukuru na kuipongeza Serikali. Pia tunaomba maeneo mengine ambayo yalibaki yaweze kufanyiwa haraka na kuweza kufanya shughuli za maendeleo yatakayowasaidia sana wananchi kwenye eneo la Jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo tetesi kuwa mradi huu umekwama kwa ajili ya kushindwa kuelewana kati ya wakandarasi, ninaiomba Serikali iingilie zoezi zima la kukamilisha utaratibu ambao ni wa kisheria ili waweze kuwaruhusu wakandarasi waweze kufanya kazi yao kwenye mikoa ambayo walikuwa wameelekezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la elimu. Niipongeze Serikali kwa jitihada ambazo zimefanywa kwa kupata idadi kubwa ya watoto ambao wanafaulu. Inaonesha Serikali imeangalia mfumo mzima na kuuthamini nzima hasa ya sekta ya elimu. Tunalo tatizo kubwa sana, tuna idadi ya wanafunzi ambao wamefaulu na wamekosa vyuo vya kwenda kusoma. Niombe sana Serikali iweke mazingira ya haraka kuhakikisha wale wanafunzi ambao wamefaulu wapewe nafasi kwenye vyuo ili waweze kuanza masomo ya kwao katika vyuo ambavyo wameomba. Na tuiombe Serikali, zile tofauti zinazojitokeza, zinazowafanya watoto washindwe kufika kwenye maeneo husika ya vyuo wazitoe ili waweze kuratibu haraka, watoto waanze kupata masomo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna maeneo kwenye suala hili la elimu hasa maeneo ya jimboni kwangu. Tunayo majengo mengi ambayo yameanzishwa, tunaomba sana Serikali ielekeze nguvu kusaidia yale majengo ambayo yameanzishwa na Halmashauri na Halmashauri zikawa hazina uwezo hasa yale yaliyoanzishwa na wananchi wenyewe kwa kujitolea. Serikali ielekeze nguvu kusaidia maeneo hayo ili kuweza kumudu ufaulu wa wanafunzi walio wengi kwenye maeneo husika ambayo ni kwenye eneo la shule za msingi, eneo la shule za sekondari, kote huko kunahitaji kukamilisha yale majengo ambayo yameanzishwa na wananchi kwa jitihada zao binafsi, lakini uwezo wa Halmashauri wa kuweza kuhudumia nguvu za wananchi ukweli bado hazijakuwa kubwa za kutosha. Kwa hiyo, tunaomba na maeneo haya Serikali ieleleze nguvu kuhakikisha miradi hii inasimamiwa na inafanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye eneo la afya. Tunaipongeza Serikali kwamba huduma za dawa kwa sasa zinapatikana, lakini bado tuna changamoto kubwa sana hasa pale sera ya Serikali ilipokuwa imezungumza kwamba kila kijiji kiwe na zahanati. Vijiji vingi vimejitokeza, wananchi wameweza kujenga majengo mengi na wameandaa utaratibu wa kuanzisha majengo ya zahanati lakini majengo yale bado hayajakamilika.

Kwa hiyo, tunaomba Serikali itenge fedha za kutosha kuhakikisha nguvu za wananchi ambazo wamejitolea waweze kupewa nafasi ya kukamilisha yale majengo. Naamini tukifanya hivyo tutakuwa tumewasaidia sana Watanzania hasa wa maeneo ya vijijini, ambako bado huduma za afya zinahitajika kwa karibu sana ili kuweza kuwasaidia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni sekta ya maji. Kwenye eneo la sekta ya maji Serikali inajitahidi kufanya kazi yake vizuri, lakini kwa ukubwa wa nchi yetu bado tunahitaji miradi ya maji kwa kiwango kikubwa sana. Niombe sana Mkoa wa Katavi ambao upo unategemea sana kupata maji kutoka kwenye chanzo cha Bwawa la Milala bado hautoshelezi. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba maji yapelekwe, hasa tunahitaji mradi mkubwa wa kutoka Ziwa Tanganyika ambao utapeleka maji kwenye Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi, lakini utasaidia kwenye maeneo mengine ya maeneo husika ya Jimbo la Mpanda Vijijini. Kwa hiyo, niiombe Serikali iharakishe kuweka mpango mkubwa wa maji ambao utasaidia kutoa kero ya maji ndani ya Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naiomba sana Serikali, Mkoa wa Katavi hauna hospitali ya Mkoa. Tunaomba Serikali iweze kutenga fedha za kutosha kujenga hospitali ya Mkoa sambamba na hospitali ya Wilaya mpya ya Tanganyika ambayo bado haijaanza kujengwa. Tunategemea sana Serikali itafanya hayo, ili kuweza kuwasaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana anayoifanya ya kutekeleza miradi mikubwa katika Taifa letu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapainduzi. Niwapongeze kwa dhati Mawaziri wale ambao wamefanya kazi kwa nia njema ya kulisaidia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza kwa sababu tuna miradi ambayo imeanza kutekelezwa kwenye maeneo ya Mkoa wetu. Tuna miradi ya maji ambayo imetekelezwa kwa kiwango kikubwa, miradi ya afya, miradi ya elimu, miradi ya umeme vijijini, miradi ya barabara kwenye maeneo ya Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Tabora. Pale Serikali inapofanya vizuri tuna haki ya kuipongeza na pale ambapo pana changamoto tutaishauri Serikali ili iweze kutusaidia kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilayani kwangu nina miradi ya maji ambayo imeshaanza kutekelezwa, miradi mikubwa ya Kijiji cha Majarida, Kijiji cha Igagala, wananchi wanapata maji, Kijiji cha Ikola wana miradi mikubwa ya maji ambayo imetekelezwa. Nampongeza sana Waziri mwenye dhamana kwa jitihada ambazo anazifanya kuwatendea haki wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ipo miradi ya maji ambayo inatekelezwa Vijiji vya Mwese, Kamjela, Kabungu, hiyo yote ni miradi ambayo inatekelezwa na tuna visima 20 ambavyo vinachimbwa kwa ajili ya kuwapa huduma ya maji. Kwa hiyo tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna miradi ya afya, tunavyo vituo vya afya cha Karema, Mwese, Mishamo, Serikali imetoa fedha kwenye vituo vya afya vya Mwese na Mishamo karibu zaidi ya shilingi milioni 800. Tuna matumaini makubwa sana kwamba Serikali itaendelea kusaidia kwenye sekta hii ili vituo hivi viweze kukamilika hasa kile kituo cha Mwese ambacho kinahitaji fedha kwa ajili ya kukamilisha ule mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi ya elimu ambayo inatekelezwa, kuna ujenzi wa shule za msingi, ujenzi wa shule za sekondari, karibu kila sehemu shule zinajengwa kwa kutegemea nguvu za wananchi na Serikali yenyewe pale ambapo panahitajika kutoa huduma hiyo. Tunawapongeza na tunaiomba Serikali kwenye miradi hiyo iweze kuongeza nguvu kuwasaidia wananchi kwa sababu wengi wamejitokeza kujenga shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa ya kipekee kwenye miradi, hasa ya elimu, nimpongeze sana Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika kwa jitihada anazofanya za kusimamia utekelezaji. Pia nimpongeze Mkuu wa Mkoa kwa kulinda amani na usimamizi mkubwa wa miradi mingi inayotekelezwa Mkoa wa Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo changamoto ambazo tunaiomba Serikali iweze kuzisimamia. Changamoto ya kwanza tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aingilie kati mgogoro wa Mradi wa Umeme Vijijini (REA) ambao unaunganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma. Kwa nini tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu, miradi ya REA imesimama kwenye Mikoa ya Kigoma na Katavi kwa sababu ya mgogoro ambao upo, watu walioomba tenda wamegombana na wakashtakiana wakapelekwa Mahakamani, kiasi kwamba sasa ule mradi umesimama, REA Awamu ya Tatu karibu sehemu nyingi nchini inatekelezwa, kwenye mikoa hii hakuna kilichotekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliingilie hili jambo ili wananchi wa mikoa hii miwili waweze kuepukana na mgogoro ambao kwao wao hauna manufaa, tunaomba Serikali iingilie ili tupate huduma ya umeme vijijini kwa vijiji vya mikoa hiyo miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Serikali iongeze fedha za Mfuko wa Barabara. Fedha za Mfuko huu zikiongezwa zitasaidia sana kuimarisha ujenzi wa barabara za vijijini na mijini. Mfuko wa sasa ambao upo una fedha kidogo sana na karibu wananchi wengi wa nchi nzima wanategemea sana fedha hizi ziweze kuwasaidia kuimarisha miundombinu ya barabara. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali iongeze fedha kwenye Mfuko wa Barabara ili barabara za vijijini, miradi ya barabara za mijini ziweze kuimarika na zifanye kazi vizuri kwa sababu huko ndiko kuna watu wengi wanaozalisha na wanahitaji huduma hii ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunaomba Serikali iongeze fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye miradi ya ujenzi hasa kwenye Wilaya ambazo ni mpya. Mkoa wa Katavi ni Mkoa mpya na una Wilaya mpya ya Tanganyika na bahati nzuri Mheshimiwa Waziri Mkuu alifika kwenye maeneo hayo, anajua changamoto zilizopo. Tunahitaji fedha zipelekwe zikajenge Makao Makuu ya Wilaya, nyumba za watumishi, hospitali ya Wilaya na Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Haya maeneo ni ya muhimu sana kwa ajili ya kuimarisha shughuli za kiutawala lakini vilevile kuimarisha shughuli za huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu katika jitihada za kufufua miradi ya kilimo, hasa kwenye mazao ya pamba na tumbaku. Ametoa msukumo mkubwa sana, tunampongeza, lakini yapo mambo ambayo yanahitajika kuyafanyia kazi ili kwenda sambamba na msukumo ambao kautoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tunaomba Serikali inapokuwa inasukuma mazao haya ihakikishe inatengeneza mfumo mzuri wa kupeleka pembejeo. Pembejeo mwaka huu wakulima hawakuzipata kwa wakati, kuna baadhi ya maeneo wamepata hasara kwa sababu hawakupata pembejeo ambazo zilihitaji kuzalisha kwa wakati. Kwa hiyo, tunaomba usimamizi kwenye eneo hili uwe mkubwa sana ili tuweze kupata mazao ambayo yatawasaidia wananchi, hasa wakulima na vilevile kusaidia kipato cha Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta hii ya kilimo bado suala zima la masoko linahitaji ufuatiliaji wa hali ya juu. Wananchi wamelima pamba kwa wingi, tunaiomba sana Serikali wanapolima wahakikishe wanunuzi wa mazao haya wanakuwa wamejengewa mazingira ambayo
yatawafikia wakulima kwa wakati. Naomba kwenye jambo hili tulifanyie umuhimu sana kwa sababu jitihada ambazo amezionesha Waziri Mkuu za kuhimiza mazao ya pamba, tumbaku na korosho zinaweza zikafikia mahali ambapo hazitakuwa na tija pale ambapo wakulima watakosa masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo ni kuhakikisha wanapata pembejeo za madawa ambayo yanahitaji kuhudumia mazao haya ambayo wananchi wamepewa fursa na wamehimizwa wayalime. Bila masoko tutalima mazao mbalimbali lakini hayatakwenda mahali popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwenye zao la tumbaku, mfumo wa zao la tumbaku uko tofauti sana na mazao mengine. Tunaiomba sana Serikali ihakikishe inawashirikisha wadau kwa ujumla ili wajue changamoto ya lile zao lakini tuhakikishe tunawajengea mazingira ya masoko yenye uhakika. Bila kutafuta masoko na bila kusaidia Serikali kuingilia kati, zao la tumbaku linaweza likapotea na linaweza lisitoe tija kwa wananchi, tunaomba sana Serikali iyafanye hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu miradi ya umwagiliaji. Kwenye eneo hili bado utekelezaji ni mdogo sana. Tunaiomba sana Serikali na tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu aangalie au aunde Tume itakayosaidia kuangalia miradi mingi ya umwagiliaji ambayo kimsingi haijafanya kazi na haijaonekana kabisa. Serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili ya miradi hii ambayo haijaonekana na ufanisi wake ni mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya hakuna mradi wa umwagiliaji ambao ulisimamiwa vizuri, hata Halmashauri zenyewe hawakushirikishwa, ni miradi ambayo ilikuwa inatoka huku juu inaenda moja kwa moja…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa kazi kubwa ya miradi mingi inayotekelezwa hapa nchini ikiwemo ya barabara, viwanja vya ndege, ununuzi wa meli, ununuzi wa ndege na ununuzi wa rada pamoja na miradi mingi ambayo ipo chini ya Wizara hii. Niwapongeze sana wafanyakazi wa Taasisi zote kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na Waziri na wasaidizi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda ni mfupi nilikuwa naomba nizungumzie maeneo ya msingi ambayo tunahitaji tuishauri Serikali; la kwanza tunahitaji suala la kurudishwa maduhuli ya fedha za taasisi zinazokusanya fedha kwenye maeneo hasa ya Bandari, TAA, TCRA, waweze kuwezeshwa. Maeneo haya ni ya msingi ili tuweze kuyawezesha yaweze kufanya kazi vizuri, tunapokusanya fedha na tukachukua zote zikaenda kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali tunazinyima hizi Taasisi ziweze kushindwa kufanya kazi.

Naomba sana Serikali iangalie umuhimu wa kuwawezesha bandari tunapoiwezesha bandari kuwarudishia fedha ziweze kufanya kazi wanaweza wakatengeneza mazingira ya kukuza bandari zingine nchini kwa maana Bandaria ya Mtwara, bandari ya Tanga na bandari za maziwa makuu kwa maana ya Mwanza na Kigoma. Tunaomba hili mliangalie kwa ukubwa wa aina yake ili muweze kuzisaidia taasisi hizi. Sambamba na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, sambamba na Mamlaka ya Anga ili waweze kuwezeshwa fedha hizi ziweze kufanya kazi za kuendeleza miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilikuwa naiomba Serikali iangalie tena ni jitihada ambazo zimefanywa kwa ajili ya kuliwezesha Shirika la MSL. MSL mmetoa fedha nyingi Serikali. Lakini tunaomba sana Serikali muwalipe mishahara wale wafanyakazi bila kuwawezesha au kuwalipa mishahara hamna kitu tutakachokuwa tumekifanya. Serikali inakarabati meli 14 lakini mpaka leo tunavyozungumza wafanyakazi hawajapata fedha na watakao operate hizo meli ni hawa hawa wafanyakazi. Tunaomba muwawezeshe ili waweze kufanya kazi na kulinda miundombinu ambayo tutakuwa tumewekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda ni mfupi naomba nijikite kwenye eneo la jimbo langu. Serikali imefanya kazi kubwa eneo la jimbo langu tuna ujenzi wa barabara ya kutoka Mpanda kwenda Kigoma eneo hili halijatengewa fedha nilikuwa naomba Serikali iangalie umuhimu wa kuweka fedha kiasi kwa ajili ya kuendeleza ile barabara. Tunashukuru Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mpanda kwenda Tabora naamni Serikali itafanya kazi kubwa kwa ajili yakuziunganisha hizi barabara, tunaomba eneo hili muliwezeshe na liweze kusimamiwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la reli; tunaomba reli ambayo imewekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ifanyiwe kazi kama ilivyotengewa. Kamati yetu imeshauri Serikali tunaunga mkono jitihada za Serikali na kazi kubwa ambazo wamezifanya. Reli ya kutoka Dar es Salaam - Morogoro, reli ya kutoka Morogoro kwenda Dodoma, reli ya kutoka Makutupora kwenda Tabora na Mwanza tunaunga mkono na tunaomba reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma muiwekee umuhimu wa aina yake sambamba na matawi ya kwake ya kutoka Uvinza kwenda Msongati sambamba na matawi ya kutoka Kaliua - Mpanda - Karema, tunaomba maeneo haya myafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi la mwisho kwa shirika TRC tunaomba eneo la Mkoa wa Katavi mlipelekee mabehewa ya kutosha kwa sababu barabara ya Mpanda - Tabora imefungwa tunaomba muwasaidie wananchi mpeleke behewa ili ziweze kuwasaidia kupata usafiri huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa muda ni mfupi naunga mkono hoja, ahsante
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi hii kuweza kuchangia hotuba ya Wizara ya Afya. Awali ya yote, niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo anayoifanya akisaidiana na wasidizi wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni muhimu imefanya kazi karibu maeneo yote ya nchi yetu. Mkoa wa Katavi hatuna Hospitali ya Mkoa. Mheshimiwa Waziri anafahamu na fedha ambazo zimetengwa na Wizara ni kidogo sana. Tulikuwa tunaomba Mheshimiwa Waziri aangalie mazingira ya Mkoa wa Katavi aongeze fedha ili tuweze kujenga Hospitali ya Mkoa ambayo itasaidia kutoa huduma ya afya kwenye maeneo ya mkoa na kutoa huduma za afya kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kutoa fedha za ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika, imepata shilingi bilioni moja na nusu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali Tanganyika. Hilo tunawapongeza sana Wizara kwa kazi kubwa na Mheshimiwa Waziri na timu ya wataalam ambao wametoa hizo fedha kwa ajili ya kutoa huduma. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aendelee kutusaidia kwenye Vituo vya Afya ambavyo viko kwenye maeneo husika. Nilishamwomba Kituo cha Afya cha Nyagala, naamini anakikumbuka, naomba sana hiki Kituo akiwekee kipaumbele kwa ajili ya kuwapa wananchi wa eneo hilo. Walishaanza hatua za awali, wamejitolea, wamejenga baadhi ya majengo, kwa hiyo tunategemea Mheshimiwa Waziri kwenye fedha atakazozipata, atusaidie kituo hicho ili tuweze kuwasaidia wananchi wa eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambasamba na hilo, tunaipongeza Serikali kwa kujenga Vituo vya Afya vya Mwese na Mishamo. Kwenye hivyo vituo viwili ambavyo vilitolewa fedha na Serikali upo upungufu ambao tunahitaji Wizara isaidie. Tunaomba vifaa tiba, kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mwese, tunaomba vifaa tiba kwa ajili ya Kituo cha Mishamo. Naamini tukipata hivyo vifaa tiba vitawasaidia kutoa huduma iliyo nzuri na wananchi wakanufaika na kile kilichoelekezwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri kwenye maeneo ambayo alifika Mheshimiwa Waziri, alifika eneo la Kituo cha Afya cha Karema, eneo lile tunahitaji watusaidie watupatie ambulance, yeye aliahidi na alifika akaona mazingira yalivyo, kwa hiyo tunaomba kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ahadi ambayo aliwapa Wanatanganyika, eneo lile la Karema aweze kukamilisha ili aweze kuwasaidia wananchi kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, tunaomba Madaktari na vituo vya afya, zahanati na hospitali inayojengwa sasa inahitaji wahudumu wa afya, Wilaya ya Tanganyika ina Daktari mmoja tu. Naomba kwenye bajeti hii, aangalie uwezekano wa kupeleka wataalam watakaotoa huduma kwenye vituo vya afya. Vituo vya afya hivyo vilivyojengwa ni vizuri, lakini vina tatizo la wahudumu ambao wanaweza wakatoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na naendelea kumpongeza kwa kazi nzuri ambazo anazifanya. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kupata nafasi ya kwanza kuwa mchangiaji wa Wizara hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Waziri kwa wasilisho la Wizara hii ya Kilimo lakini nimpongeze kwa jitihada ambazo alizifanya kwenye Mkoa wa Katavi, kuwaruhusu wananchi wa Mkoa ule waweze kulima zao la pamba. Tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye zao la tumbaku. Zao la tumbaku lilikuwa linachangia pato kubwa sana la Taifa na wakulima wa zao hilo kupata fedha nyingi ambazo zilisaidia jamii kwenye maeneo yanayozalisha zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo matatizo ambayo yamelikumba zao hili la tumbaku. Tatizo la kwanza ni mabadiliko yaliyosimamiwa na Serikali ya kubadilisha mfumo wa kuuza tumbaku badala ya kuuza kwa dola sasa inauzwa kwa shilingi ya Kitanzania. Maamuzi hayo tuliyoyatoa yamewapa umaskini wakulima wa zao la tumbaku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mjadala wa bei ulipokuwa unajadiliwa kilo moja ya tumbaku wastani wa dola ulikuwa Sh.2,246 leo hii dola moja ni sawa na Sh.2,289. Mkulima huyo atapoteza kwa kila kilo Sh.43 ukizidisha kwa kilo ambazo zitazalishwa kilo milioni 63, mkulima wa zao la tumbaku atapoteza karibu shilingi bilioni 4.77. Naamini ukifika mwisho wa msimu mkulima huyu anaweza akawa amepoteza shilingi bilioni 5. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, maamuzi mengine ambayo tunayafanya na Serikali tunayabariki, yanaleta umaskini kwa wakulima wa nchi hii. Ifike mahali Waziri ashuke chini akasikilize kilio cha wakulima wa zao la tumbaku, akaangalie mapato ambayo yanapotezwa kwa sababu ya maamuzi mabovu. Naomba hili mlifanyie kazi. Kima nilichowatajia cha shilingi bilioni 4 mpaka shilingi bilioni 5, tunakipoteza kwa sababu ya kushindwa kuwa na usimamizi mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye zao la tumbaku ni juu ya mfumo wa uagizaji wa pembejeo. Zao la tumbaku lina kalenda yake. Haiwezekani unaagiza pembejeo kwa kuchelewa ukitegemea kwamba utawasaidia wakulima hawa. Nia nzuri ya Serikali ya kuagiza kwa pamoja, mfumo huo kwa wakulima wa zao la tumbaku haukuwasaidia wakulima, ndiyo maana kila eneo wana bei yake tofauti na ilivyokuwa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ukienda Kahama mfuko mmoja unauzwa kwa Sh.74,00, Chunya Sh.96,000, Mpanda Sh.96,000, Tabora na maeneo mengine mpaka Sh.98,000 lakini walipokuwa na chombo kimoja, wakulima wa zao la tumbaku walikuwa wana uwezo wa kutumia bei moja kwa nchi nzima. Naomba Mheshimiwa Waziri, atakapokuwa ana-wind up hotuba ya Wizara hii, watafute majibu ya suluhu ya kuwatafutia chombo ambacho kitawasimamia wakulima wa zao la tumbaku ili waweze kusimamia zao lao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni zao la pamba. Serikali imefanya kazi nzuri ya kuhamasisha wakulima wa zao la pamba katika nchi yetu. Karibu maeneo yote wamelima na wameitikia wito wa Serikali. Niwaombe sana Serikali iangalie ni jinsi gani wakulima hawa wa zao la pamba watapata soko lao vizuri. Niwaombe sana mliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya yangu ya Tanganyika ambayo ndiyo imeanza kulima zao la pamba hawajajipanga vizuri juu ya kuweka msimamo wa kununua zao la pamba kupitia kwenye ushirika, watanunua vipi ile pamba? Naomba Waziri atupe majibu. Mfumo uliopo wamelima bila kupitia kwenye ushirika na ushirika haukuandaliwa, naomba na hili mlifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni zao la mahindi. Wakulima wa mahindi, mpunga, mbaazi na mazao mengine wamekuwa watumwa katika nchi yao. Mkulima wa mahindi ndiye pekee katika nchi hii anayeonewa, anapangiwa bei ya kuuza mazao yake hapewi nafasi ya kuyauza mazao mahali ambapo anahitaji kuyauza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba muwaonee huruma wakulima wa mazao ya tumbaku na mpunga. Hawa wakulima ndiyo wamekuwa watu ambao wanalinda mfumuko wa bei, kitu ambacho siyo sahihi. Mkulima wa zao la mahindi ama mpunga asipewe mzigo wa kulinda mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii sukari inauzwa Sh.3,000 mpaka Sh.2,800, kwa hiyo mkulima wa kijijini akitaka kununua sukari ya kilo 10 lazima abebe gunia mbili ndiyo anunue kilo 10. Haiwezekani! Fikeni mahali mbadili mfumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Waziri waimarishe Kitengo cha Ununuzi wa Mazao. Kwenye bajeti nimeangalia, mmetenga shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kununua mazao, ambapo uhalisia mnahitaji shilingi bilioni 86 kwa mujibu wa Kamati ya Kilimo. Niombe mfuate maelekezo ambayo Waheshimiwa Wabunge wanayatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani, mwananchi tajiri awe anapata unafuu kwa mwananchi kutoka kijijini. Mwananchi wa kati analishwa na mwananchi wa kijijini, mwananchi mzururaji wa nchi hii analishwa na mwanakijiji ambaye yuko kule kijijini, haiwezekani! Naomba Waziri aje na majibu ya msingi, wawaruhusu wakulima wauze mazao yao mahali popote wanapotaka. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mfumo wa pembejeo, Serikali ilikuja na nia njema lakini haijawasaidia wananchi. Pembejeo hazikufika kwa wakati na kulikuwa na urasimu mkubwa. Naomba Waziri aje na majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye ushirika. Serikali mmesema kwamba mtaanzisha Tume ya Ushirika, kwenye Tume ya Ushirika hamna kitu chochote kilichofanyika. Vyama vya Ushirika vinasimamiwa na Tume hii ya Ushirika, hampeleki fedha watajiendesha vipi? Katika wafanyakazi ambao wanashida nchi hii ni wanaushirika. Maafisa Ushirika wamebaki na jina tu kuitwa Maafisa Ushirika lakini uhalisia hakuna kitu chochote kinachofanyika. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kulinda amani ya nchi hii. Pia nimpongeze Waziri mwenye dhamana na Msaidizi wake kwa kufanya kazi kubwa ya kusimamia Wizara ambayo ni kubwa na ina majukumu mapana sana. Tuwapongeze Wakuu wa Vyombo vya Usalama, Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la Uhamiaji, Jeshi la Zimamoto. Wamefanya kazi kubwa, naamini kila mwananchi anashuhudia ile kazi ambayo imefanyika chini ya uzimamizi wa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wamefanya kazi kubwa sana, wamedhibiti mianya ya uingizaji wa madawa kulevya na kufuta kabisa nchi yetu iliyokuwa inaonekana kwamba ni eneo la uchochoro wa kupitisha madawa ya kulevya, hapa wamefanya kazi kubwa sana, tunawapongeza kwa dhati. Hata hivyo, wamedhibiti matukio ya ujambazi nchini ambayo yalikuwa yameshamiri kwa muda mrefu sana. Jeshi la Polisi wamefanya kazi ya kudhibiti hivyo vitendo na sasa hivi matukio yamepungua kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado katika eneo hilo la Jeshi la Polisi wamedhibiti vitendo vya kuhujumu uchumi wa nchi yetu. Tumeshuhudia Jeshi la Polisi likidhibiti utoroshwaji wa dhahabu ambao ulikuwa unafanywa na raia wasioitakia mema nchi yetu. Wamefanya kazi ambayo kimsingi Serikali imedhibiti vile vitendo ambavyo vilikuwa vinadhoofisha uchumi wetu. Pamoja na hayo Jeshi la Polisi pamoja na jitihada linalofanya na kazi inazolifanya ni kubwa, lakini bado kuna changamoto kubwa ambazo zinatakiwa zifanyiwe kazi, vitendea kazi hawana, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri tuangalie kwenye maeneo ya vitendea kazi. Jeshi la Polisi hawana magari ya kutosha, Jeshi la Polisi hawana nyumba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye eneo la jimbo langu, tumeshukuru Serikali wanajenga nyumba za askari zipo sita, lakini bado pamoja na kwamba wanajenga hizo nyumba, lakini hakuna Kituo cha Polisi cha Wilaya. Niombe sana Mheshimiwa Waziri alingalie hili na naamini ninachokiongea anakifahamu, alishafika kwenye maeneo husika, tunaomba kituo cha polisi. Zile nyumba anazojenga hazitakuwa na maana kama hakutakuwa na kituo cha polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vituo vya polisi ambavyo vipo mpakani, tuna Kituo cha Polisi Ikola na Kituo cha Polisi Karema, hivi vituo ni ambavyo havina hadhi inayofanana, tuombe sana Mheshimiwa Waziri ahakikishe hivi vituo wanavipelekea vitendea kazi. Hata hivyo, baadhi ya vituo vya polisi hata uwezo wa kupeleka silaha hakuna, askari polisi analinda kituo akiwa na rungu, kwa sababu hana nyumba ya kuweza kuhifadhi silaha. Naomba Mheshimiwa Waziri apeleke silaha kwenye maeneo ambayo ni mpakani ili yaweze kulindwa, na ajenge mazingira ambayo yatakuwa salama kwa ajili ya vile vituo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie Jeshi la Magereza, Jeshi la Magereza linafanya kazi kubwa na jimboni kwangu Wilaya ya Tanganyika tuna Gereza la Kilimo la Kalila Nkulukulu. Gereza hili ni la muda mrefu, ni chakavu, tunaomba likafanyiwe ukarabati sambamba na kujenga nyumba za watumishi hasa askari wanaofanya kazi kwenye gereza hili. Yapo maeneo mengine ukifika unawaonea huruma, hata hao watumishi unaowapeleka kwenye eneo hilo, unajua tu kwamba wanafanya kazi kwa sababu ni wito.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo Gereza la Kilimo la Kalila Nkulukulu lina eneo kubwa sana la uzalishaji. Kwa bahati mbaya sana vitendea kazi hawana. Tulikuwa tunaomba Waziri wanunulie treka Gereza la Kilimo la Kalila Nkulukulu ili liweze kuzalisha chakula cha ziada. Tuna matumaini makubwa sana wakiwapelekea vifaa na vitendea kazi watafanya kazi kubwa ambayo itawasaidia kuzalisha na kupata ziada ya chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu nina wakimbizi, lipo eneo la Mishamo lina wakimbizi zaidi 60,000, kati ya hao walio wengi walishakuwa raia na wengine hawajakubaliana na kuwa raia wa nchi hii. Sasa kuna vitu ambavyo vinakuwa tofauti kwenye eneo moja, kwa maana linakuwa na utawala wa aina mbili; utawala wa makazi unaosimamiwa na Afisa anayetambuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani lakini utawala mwingine ni ule ambao ni wa kawaida. Kwa hiyo kuna tawala mbili kwenye eneo moja, mkuu wa makazi analinda wale wakimbizi wachache waliobaki. Kwamba ni mali ya kwake, wanatambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe Serikali itoe maamuzi, wale wachache ambao hawakuchukua uraia wawahamishe wawapeleke kwenye maeneo mengine ambapo watakaa kwenye maeneo rasmi. Tukiwaacha hivyo tuna mashaka makubwa sana baadaye, tutaendelea kupokea wakimbizi kupitia hawa hawa ambao wapo kitu ambacho hatukitegemei tena. Si Mishamo tu, hata Katumba wapo. Kwa hiyo tunaomba hili walishungulikie na tunapata wakati mgumu kwenye Serikali za Mitaa katika uchaguzi ujao. Kuna hati hati ya kutokushiriki wananchi hao wa Mishamo, Katumba, Ulyankulu wanaweza wasishiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa sababu ya mwingiliano wa utawala. Naomba hili walishughulikie na walifanyie kazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kupata nafasi ya kuchangia kwenye bajeti muhimu ya Wizara ya Maji. Awali ya yote, niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa ambazo inazifanya hasa kwenye miradi ya maji. Jimboni kwangu ipo miradi ya maji ambayo ilishaanza kutekelezwa; nina mradi wa Kijiji cha Kabungu ambao una thamani ya shilingi milioni 600, mradi wa Kijiji cha Kamjela wenye thamani ya shilingi milioni 800 na mradi wa Kata ya Mwese wenye vijiji vitatu ambao una thamani ya shilingi bilioni moja na milioni mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi hii ikikamilika itawasaidia sana wananchi wa maeneo husika ambao wanategemea kutatua kero ya maji. Niiombe sana Serikali iharakishe kupeleka fedha kwa ajili ya kumalizia hii miradi. Fedha zitakapokuwa zimeenda, tunategemea kero ya maji ambayo ipo kwenye hivi vijiji itakuwa imetoweka na kuwafanya wananchi waweze kuzalisha na kufanya shughuli zao za maendeleo bila kuwa na wasiwasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vijiji 18 ambavyo vilichimbiwa visima. Vijiji hivi vinategemea mradi huo ambao ulikuwa na thamani ya shilingi milioni 400 uweze kutatua tatizo kubwa kwenye maeneo husika ya hivyo vijiji, mpaka sasa bado vijiji hivyo havijakamilishiwa hiyo miradi ya visima. Niombe sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana akisaidiwa na Naibu wake watoe msukumo mkubwa ili hivyo vijiji viweze kukamilika, miradi hii itawasaidia sana wananchi. Akinamama wengi kipindi cha kiangazi hawafanyi kazi nyingine, kazi kubwa ni ya kwenda kutafuta maji yalipo. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie uwezekano wa kusaidia kwenye maeneo haya ili vijiji hivi viweze kukamilisha na kazi ilishafanyika, wametumia fedha nyingi lakini bado kile kilichokuwa kimekusudiwa hakijatekelezwa ipasavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mmradi wa Kijiji cha Ngomalusambo. Mradi huu fedha zilizopelekwa zimeliwa, mradi ulikamilika lakini haujatoa hata tone la maji. Niombe sana Mheshimiwa Waziri afike kwenye eneo hili akajionee, aangalie tatizo lililopo kwenye eneo la Kijiji hiki cha Ngomalusambo. Mradi ulipokamilika wananchi walifurahi wakitegemea watapata maji ya kutosha, lakini toka ulipokuwa umekabidhiwa kwenye kijiji husika, mradi huu umebaki kuwa pambo, haujaonesha matunda yake. Naamini watendaji waliosimamia ule mradi hawakuutendea haki na ni vyema wakawafuatilia ili waangalie zile fedha zilizotumika zaidi ya milioni 200 hazikufanya kazi ya aina yoyote na tija haipo. Naomba hili Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mradi wa Kijiji cha Karema; Mradi wa Maji wa Karema ni mradi ambao tulitegemea kwamba ungekuwa umetatua kero ya wananchi kwenye eneo la Kata ya Karema. Kwa bahati mbaya sana mradi huu toka umekamilika umekuwa na shida kubwa sana ya kutoa huduma ya maji. Niombe sana Serikali iende ikachunguze ule mradi ili tuangalie ni kitu gani kinachosababisha mradi usitoe maji kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama chanzo cha maji kinaonekana hakifai, Mji wa Karema upo jirani sana na Ziwa Tanganyika; tutaona kitu cha ajabu sana kama maji hayatapatikana kwenye maeneo hayo. Niombe Mheshimiwa Waziri najua anaufahamu mradi huu, waufanyie uhakiki na watume wataalam waende wakafanye kazi ili tutoe tatizo lile la maji ambalo lipo kwenye eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utakapokuwa umefanyiwa ukarabati na ukakamilika, utakuwa umetatua kero kubwa sana. Wananchi wengi wa ukanda wa ziwa huwa wanapata mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa sababu ya kutumia maji ya ziwani. Kwa hiyo, tunaomba muufuatilie huu mradi ili uweze kutoa suluhisho la kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mradi mkubwa wa maji unaotarajiwa kufanywa na Serikali wa kutoa maji Ziwa Tanganyika kuyapeleka Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi, Mpanda Mjini. Mradi huu ni muhimu sana kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi na utasaidia karibu maeneo yote. Nauzungumzia mimi kwa sababu mradi huu upo Jimboni kwangu na utakapokuwa umekamilika, utawanufaisha wananchi wa vijiji takribani 10 ambao watapitiwa na ule mradi. Niombe sana Wizara iharakishe mchakato wa mpango wa kupeleka maji kwenye Mkoa wa Katavi, ule utakaotoa maji kutoka Ziwa Tanganyika ili uende kutatua kero ya Manispaa ya Mpanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Mpanda una matatizo makubwa sana ya maji, mji umekua lakini bado unahitaji sana huduma ya maji. Chanzo pekee cha maji kilichopo hakitoshelezi kupeleka maji kwenye maeneo husika. Kwa hiyo, tunaomba mradi huu ujengwe haraka na unapojengwa upewe kipaumbele kwenye maeneo ambayo yatapita kwenye mradi, Kijiji cha Kapalamsenga tunategemea kabisa nacho kitapata huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Itetemya, Kijiji cha Kasekese, Kijiji cha Kaseganyama, Kijiji cha Sibwesa, Kijiji cha Mkungwi, Kijiji cha Ikata, Kijiji cha Kabungu na vinginevyo ambavyo vitapitiwa kwenye Jimbo la Mheshimiwa Kapufi, Mpanda Mjini viweze kunufaika na mradi huu. Ni vyema Serikali ikausukuma huu mradi ili uweze kufanya kazi kwa wakati na tuna mategemeo sana na Waziri husika na msaidizi wake kwamba wataufanyia kazi wakishirikiana na timu yao ya wataalam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo Vijiji 16 kwenye Jimbo langu; Vijiji vya eneo la Mishamu. Vijiji hivi vilikuwa na visima vya maji, ni eneo lililokuwa la wakimbizi na UN ilichimba visima vingi kwenye maeneo hayo. Bahati mbaya, miradi hii ni ya muda mrefu na nimekuwa nikiiomba Wizara kila siku iweze kuwasaidia wananchi wa maeneo yale kuvifanyia ukarabati vile visima ili viweze kutoa huduma ya maji. Ni mategemeo yangu kwamba Wizara ni sikivu, mtaenda kuangalia changamoto zilizopo kwenye vijiji hivi vya Mishamo vipo 16 ili waweze kuwasaidia na waweze kutoa huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tunaipongeza Serikali kwa jitihada ambazo wamezifanya na zaidi tunawapongeza Mawaziri kwa kazi kubwa sana wanayoifanya. Naamini Waziri husika amefika kwenye miradi ambayo nimeitaja, tunaomba akaifanyie kazi, awape fedha wakandarasi waweze kukamilisha ile miradi ili iweze kutoa huduma husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Kilimo. Awali nimpongeze Mheshimiwa Waziri aliyepewa dhamana ya Wizara hii ameanza na mwanzo mzuri…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Naomba utulivu Bungeni.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ameanza na mwanzo mzuri, naamini akisaidiana na wasaidizi wake watafanya kazi vizuri ya kuisimamia Serikali na Wizara kwa ujumla. Nianze kwa ushauri, Mkoa wa Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma hii ni mikoa ambayo inazalisha chakula kwa wingi sana. Kazi ya Serikali ni kuwawezesha hawa wakulima wasikate tamaa. Mwaka jana wakulima wa mazao ya mahindi na mpunga wamekula hasara sana kutokana na Serikali kufunga mipaka na kuwazuia wakulima wasiuze mazao yao kwenye masoko ya nje. Nashauri hili kosa tulilolifanya tusije tukalirudia tena, wakulima wanazalisha mazao yao kwa nguvu zao binafsi na hawasaidiwi kitu chochote, muda unapofika mazao yao kuyauza Serikali inaleta vikwazo, tunawaletea umaskini sana. Tunalo soko la kongo, Rwanda na Burundi, sasa hivi maeneo yote hayo yana uhitaji wa kuhitaji mahindi na nafaka nyinginezo. Kwa hiyo nashauri kosa la kuzuia mazao haya lisifanyike tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba waweke mazingira wezeshi ili kusaidia mazao ambayo yanazalishwa kwa wingi hasa Nyanda za Juu Kusini yapate dirisha la kutokea eneo la Sumbawanga kwenye Bandari ya Kasanga ili yaweze kwenda nchi ya Congo. Nchi ya Congo mazao haya yanahitajika muda wote, wenzetu kule hawalimi kwa sababu ya vita vinavyotokea mara kwa mara. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi eneo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninaloshauri kwa Serikali ni kupeleka pembejeo kwa wakati. Mwaka huu uzalishaji wa mazao ya mahindi si mkubwa sana kwa sababu Serikali ilishindwa kupeleka pembejeo kwa wakati. Nimwombe Mheshimiwa Waziri aendelee kufanya utafiti na wawaachie Vyama vya Ushirika viweze kupeleka na kusambaza pembejeo kwa wakulima wake ili waweze kuzalisha kwa wakati. Kuingilia hizi pembejeo kwa Serikali tunaona tunafanya makosa makubwa, tunapeleka kipindi ambacho si cha uzalishaji. Niombe eneo hili wakalifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mazao ya biashara. Jimboni kwangu tunazalisha, tumbaku, kahawa na pamba. Haya mazao ya biashara Serikali inatakiwa kwanza ikae na makampuni ili waweze kuangalia mazingira rafiki yatakayowezesha kusaidia ununuzi wa mazao haya. Zao la pamba ambalo limezalishwa Mpanda hasa katika Wilaya ya Tanganyika ni zao ambalo limepokelewa vizuri kwa wananchi na niipongeze Wizara ya Kilimo kupitia Bodi ya Pamba, wamewasaidia sana wakulima na takribani tuna matarajio ya kuzalisha karibu kilo milioni 16.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana bado hatujakuwa na uhakika wa soko la zao hili. Makampuni yanayonunua zao hili ni makampuni manne tu kiasi kwamba yanatia wasiwasi kwamba pamba iliyozalishwa Mkoa wa Katavi upo uwezekano ikakosa soko la uhakika. Tunaomba Waziri alifanyie kazi, asukume makampuni mengine yaweze kwenda kununua pamba katika eneo hilo na pamba inayozalishwa kule ni nzuri na walionunua kwa awamu ya kwanza wamesema ni pamba ya grade one ambayo imepatikana kwenye mnada wa kwanza uliofanyika kwenye eneo la Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zao la tumbaku, zao hili ndilo lilikuwa linaongoza hapa nchini kwa kuleta fedha nyingi za kigeni na tulikuwa tuna uzalishaji mkubwa wa zaidi ya kilo milioni mia moja. Ni zao ambalo lilikuwa linaongoza kwa nchi yetu kuleta fedha nyingi za kigeni, lakini kwa sasa linaporomoka siku hadi siku, kutoka uzalishaji wa kilo milioni mia moja kwa sasa uzalishaji ni wa kilo milioni hamsini. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kunusuru hili zao. Kwanza wakae na makampuni ambayo yananunua zao la tumbaku, sasa hivi kuna tetesi kwamba kampuni la TLTC ambalo linanunua kwa kiwango kikubwa linaondoka hapa nchini kwa sababu ya mazingira kutokuwa rafiki kwao. Niishauri Serikali yangu wakae na haya makampuni zao la tumbaku ni zao ambalo linalimwa kwenye mikoa mingi katika nchi yetu, watafanya mdololo wa kiuchumi wasipofanya shughuli ya kufuatilia hili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi ya umwagiliaji, miradi mingi ya umwagiliaji Serikali imeitelekeza na karibu ambao waliopewa dhamana ya kuisimamia wameshindwa kabisa na wengi waliipiga hii miradi, niombe Serikali wafuatilie hii miradi. Ninao Mradi wa Skimu ya Karema, kunaMmradi wa Skim ya Mpailo na Mradi wa Skimu ya Kabage, bado hiyo miradi yote haijakamilika. Niombe Serikali hebu watumeni wataalam waangalie kifo cha fedha zilizotengwa na Serikali ambazo kimsingi mpaka sasa hazionekani kwamba zimefanya shughuli gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa suala la pembejeo, naomba utaratibu wa pembejeo ubadilike na tunaomba sana hasa kwenye suala la tumbaku, utaratibu uliozoeleka huko nyuma hebu waviachie Vyama vya Ushirika viweze kufanya kazi yake ili viweze kupeleka kwa wakati na ni jambo jema kwao wao. Serikali wanapowaachia vyombo vingine vinapofanya kazi hata wakifanya makosa Serikali itakuwa na nafasi ya kuelekeza mkono wake kwamba chombo hiki wakisimamie...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wanaochangia Mpango. Awali ya yote naishukuru sana Serikali, namshukuru Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake kwa kuleta Mpango mzuri ambao unaonyesha dira ya maendeleo yetu. Katika mpango huu yapo ambayo yametekelezwa na Serikali, kimsingi tunaipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa jitihada kubwa sana ambazo amezifanya za kuboresha vitu vingi ambavyo amevileta katika nchi yetu. Kwenye Mpango amezungumzia suala la miundombinu. Tumeshuhudia Serikali ikiboresha eneo la miundombinu kwa ujenzi wa barabara karibu nchi nzima. Haya ni maendeleo makubwa sana na unapotaka maendeleo, kwanza rahisisha shughuli za kuwafikia wananchi, lakini bado Serikali tumeona ikitekeleza miradi mikubwa, wameboresha viwanja vya ndege karibu 11 ambavyo tunategemea vitarahisha sana shughuli ya uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, Serikali imenunua ndege ili ziweze kukuza Sekta ya Utalii, lakini kutoa huduma kwa wananchi. Serikali bado imeendelea kuwaona wananchi hasa wale wa chini, imekuja na Mpango wa kununua au kujenga meli mpya kwenye maziwa makuu; Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa. Haya ni maendeleo makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Ziwa Victoria kuna ujenzi wa meli mpya itakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na karibu tani 400 za mizigo. Eneo hili watakuwa wamewasaidia sana wananchi wa kanda ya ziwa, ambao kwa kipindi kirefu walikuwa wana shida kubwa ya usafiri wa majini. Vile vile kuna ukarabati wa meli ya MV. Victoria, haya ni maendeleo makubwa sana katika kipindi kifupi. Tunaona mipango ambayo iliwasilishwa na Serikali ikitekelezwa kwa haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, bado kwenye hiyo hiyo Sekta ya Uchukuzi, Serikali imeamua kusaidia au kupanua ujenzi wa bandari pale Dar es Salaam. Bandari yetu ilikuwa na uwezo mdogo, leo hii tunashuhudia maendeleo makubwa sana ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na tumeshuhudia nchi yetu ikipokea sasa meli kubwa ambazo zinatua kwenye bandari yetu na kupakua mizigo ambayo haikutegemewa huko nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tuna Bandari ya kule Mtwara, imepanuliwa. Tunaamini eneo lile la Kusini nalo litakuwa katika huduma kubwa ya maendeleo katika nchi yetu. Bado kuna upanuzi wa Bandari ya Tanga, ambayo nayo ipo katika Mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la Kanda ya Ziwa Victoria, kuna ujenzi wa kivuko kikubwa karibu kilomita tatu kutoka Busisi ambacho kitatoa huduma kubwa sana kwa wananchi. Maeneo haya ni Serikali inatekeleza kwa ajili ya kusaidia wananchi kukuza uchumi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza sana Serikali, lakini tumeona mapinduzi makubwa sana katika nchi yetu. Ili uweze kuendelea, tunahitaji miundombinu na nishati ya umeme. Mheshimiwa Rais kwa nia nzuri ameamua kujenga bwawa kubwa la umeme katika Mto Rufiji; bwawa lile maarufu kwa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere. Hili litakuwa ni eneo ambalo litawasaidia wananchi wote katika nchi yetu. Ninaomba hizi jitihada tuziunge mkono na tuangalie maeneo mengine ambayo yalisahaulika yaweze kupelekewa miradi ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kilimo. Tukitaka kuwasaidia wananchi walio wengi, baada ya Serikali kuweka miundombinu, karibu maeneo yote, sasa Mheshimiwa Dkt. Mpango elekeza mawazo yako ukuze Sekta ya Kilimo ambayo inawaguza wananchi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili natoa ushauri, kwanza Serikali ianze kufikiria kutoa ruzuku kwenye mazao ya korosho, pamba, chai, tumbaku na yale mazao makubwa ambayo yanatuletea fedha za kigeni kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yeyote ile iliyoendelea inawasaidia sana wananchi hasa wakulima kuweza kushindana kwenye ushindani. Pale mazao yanapokuwa yameanguka, lazima Serikali iweze kuwasaidia hawa wananchi wapate nguvu, lakini wasiposaidiwa watakuwa na maeneo mabaya ambayo yatawafikisha kutokufanya kazi na kuachana na hayo mazao ambayo yalikuwa yakiwaingizia kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie zao la pamba ambalo linazalishwa wilayani kwangu. Zao la pamba wananchi walilichukulia kwamba ni zao ambalo ni sasa lingewatoa kwenye umasikini na wamezalisha kwa kiwango kikubwa na pamba nzuri, kuzidi hata ile iliyokuwa inazalishwa ambako imetoka mbegu zake maeneo ya ukanda wa ziwa, lakini mpaka sasa wakulima bado hawajauza pamba, iko majumbani kwao. Naomba eneo hili mkalifanyie kazi, mboreshe ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao lingine ni tumbaku. Nchi yetu ilikuwa inapata fedha nyingi kupitia zao la tumbaku. Kwa bahati mbaya sana mwaka huu yapo makampuni ambayo yalikuwa yananunua tumbaku kwenye nchi yetu kampuni kama TLC lakini imeacha kununua zao hili. Tuna mikoa zaidi ya 12 inayozalisha zao la Tumbaku ukiwemo na Mkoa wa Kigoma ambapo Mheshimiwa Waziri ametoka wananchi hawana mahali ambapo watauza tumbaku walizokuwa wanazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri sasa Serikali iangalie eneo la Kitengo cha Masoko, kwenye masoko bado hamjapaangalia. Tunahamasisha kilimo lakini kuwatafutia wakulima masoko bado Serikali haiajawekeza kwa kiasi cha kutosha. Niombe eneo hili nendeni mkalifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na kuboresha eneo la masoko pia ni muhimu kuboresha mazao ya chakula ambapo mkiwasaidia hawa wakulima na mkawawekea mazingira mazuri ya masoko kilimo ni eneo ambalo litaajiri wananchi wengi na Serikali itakuwa inanufaika kupitia huduma mbalimbali na kodi zitakazokuwa zinatokana na upatikanaji wa fedha. Tunaomba sana hapa Serikali mkapafanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo tunapenda kushauri Serikali ni kwenye …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Muda umekwisha, ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa utendaji uliotukuka kwa kipindi cha miaka minne ya Uongozi wake
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi hii nami niunge mkono hatua ambayo imeletwa mbele ya Bunge lako Tukufu ya kumpongeza Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amefanya mambo makubwa sana, hata wale ambao wanapinga wanapinga tu kwa sababu wanajua ukweli. Mheshimiwa Rais ameamua kutengeneza nchi yetu yote bila kuwa na ubaguzi; katengeneza mundombinu ya barabara kila sehemu, tumeshuhudia miradi mingi ya barabara ambayo imejengwa bila kuangalia ukanda, kila sehemu amepeleka miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, amejenga madaraja ambayo yalikuwa hayawezekani kujengwa katika kipindi hicho, jumla ya barabara zipatazo 77 kubwa zimejengwa katika nchi na mikoa mbalimbali. Amejenga na kuboresha viwanja vya ndege; tumeshuhudia Uwanja wa Terminal III ambao ni mkubwa na ni kivutio sasa hivi kwa nchi yetu, lakini ameboresha Viwanja vya Songwe, Viwanja vya Mwanza, Viwanja vya Chato; huu ni uthibitisho mkubwa kwamba sasa hivi nchi yetu inaweza sasa kupokea hata ndege zile kubwa za kimataifa katika eneo letu.

Mheshimiwa Spika, amenunua ndege, zaidi ya trilioni moja zimetumika kununua ndege. Wakati ndege zinanunuliwa watu wengi walibeza na kupinga, lakini cha ajabu ndege ziliponunuliwa wa kwanza kuzipanda hizo ndege ni wale ambao walikuwa wanapinga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia ujenzi na upanuzi wa bandari. Bandari yetu ya Dar es Salaam sasa hivi inapanuliwa na imepokea meli kubwa kwa mara ya kwanza katika nchi yetu hatukuwahi kuona meli kubwa ambazo zinakuja kupakua mzigo. Sambamba na hayo, amepanua Bandari ya kule Mtwara, amepanua anaendelea kujenga Bandari ya kule Tanga; haya ni mapinduzi makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, amejenga Reli ya Standard Gauge ambayo tunaishuhudia, kitu ambacho kilikuwa kama ndoto, leo hii tunaangalia jinsi miundombinu ilivyo na wenzetu wanashuhudia kuona kama kitu cha utalii ambacho kinafanyika katika nchi yetu.

SPIKA: Malizia Mheshimiwa.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, tunaunga mkono hoja, na ninaamini wewe ni shabiki wa Simba, hata siku moja huwezi ukaungwa mkono na mshabiki wa Yanga; ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kupata nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote niipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya ya kupeleka huduma ya Nishati hasa kwenye miradi ya REA ambayo kila eneo katika nchi yetu imeweza kufanyika. Nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri kwa jitihada kubwa na juhudi ambazo amezifanya kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo Jimbo la kwangu amefika zaidi ya mara tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri ameenda kijiji cha Kasekese, alipata mapokezi mazuri, makubwa lakini amefanya jitihada za makusudi kusukuma umeme kwenye vijiji vya Majalila, Kijiji cha Ifukutwa, Kijiji cha Kabungu na kwenye eneo la Gereza la Kilimo Kalilangurukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi letu sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi, Kigoma na Rukwa hatuna umeme wa grid ya taifa, umeme huu ndiyo umeme ambao utakuwa suluhisho la kudumu kwenye maeneo mbalimbali ya mikoa hii mitatu na mr adi wa grid ya taifa ni wa muda mrefu toka mwaka 2010 ulianza kuzungumzwa kwenye vitabu mbalimbali vya Wizara. Niwaombe sasa kuwe na jitihada za maksudi ule umeme wa kilovolt 400 ambao tunategemea utoke Tunduma hadi Nyakanazi Mkoa wa Kigoma. Uwekwe kwenye mpango ambao na msukumo mkubwa ili uweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme huu utawasaidia wananchi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma. Tuombe sana Serikali ipeleke fedha kwa ajili ya kuanza mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, umeme wa REA phase III. Tunapongeza jitihada za Serikali zilizofanyika lakini kasi ya wakandarasi waliopewa nafasi ya kuandaa miundombinu ya umeme wa REA III bado si ya kuridhisha. Pamoja na jitihada nzuri zinazofanywa na Wizara lakini bado uhitaji wa miradi hii kutekelezwa kwa wakati ni mkubwa sana. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, umeenda pale Kijiji cha Mchakamchaka umezindua umeme, lakini baada ya kuondoka jitihada zile ambazo zilikuwa zinahitajika kusukuma ili miradi iweze kwenda kwa haraka bado hazijafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri alipofika eneo la Kasekese na alipofika Ifukutwa aliwaahidi wananchi wa Wilaya ya Tanganyika kwamba vijiji vyote vitapata umeme wa REA phase III. Niombe sana eneo la Mishamo na vijiji vyote vilivyoko kwenye eneo hilo naomba upeleke umeme na mkandarasi umuagize ahakikishe vile vijiji vinapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko eneo la ukanda wa ziwa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, kengele imeshagonga, ahsante sana.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
MHE. SELEMANI M. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi kuwa miongoni mwa wachangiaji wa hotuba ya Mheshimiwa Rais. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa ambayo amefanya ndani ya nchi hii. Katika hotuba aliyoitoa yapo mambo ya msingi ambayo aliyasisitiza ambayo na sisi tunahitaji yafanyiwe kazi hasa kwenye maeneo ya watendaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya vitu vingi na vikubwa katika nchi hii, lakini bado kuna eneo moja la kilimo halijawekewa msukumo mkubwa sana. Hili ni eneo ambalo linawashika Watanzania walio wengi na karibu asilimia kubwa ya ajira za wananchi ziko kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hotuba ya Mheshimiwa Rais, ameelezea zaidi kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji. Miradi mingi ya umwagiliaji haijatendewa haki katika nchi hii na ili tuweze kuwa na uzalishaji mkubwa lazima tuwekeze uwekezaji mkubwa kwenye eneo hili. Nchi hii ina mabonde mengi ambayo hayafanyiwi kazi. Tunaweza tukawa wazalishaji wakubwa na tuchukulie mfano tu Mkoa huu wa Dodoma. Mkoa wa Dodoma ndiyo mkoa ambao una ardhi nzuri yenye rutuba sana, kwa bahati mbaya sana mkoa huu mvua zake ni za shida. Sasa kama tungekuwa tumewekeza kwenye eneo la umwagiliaji karibu kila sehemu ya mkoa wa nchi hii ungekuwa na uzalishaji mkubwa sana. Tunaishauri Serikali…

SPIKA: Mheshimiwa Kakoso, watu wengi hawafahamu hilo kwamba Mkoa wa Dodoma of course that means and Singida and a little bit of Shinyanga ni mkoa wenye ardhi yenye rutuba sana, ni mvua tu! Mvua ikinyesha ukiona hayo mahindi yalivyokaa vizuri utafikiri yamewekewa mbolea ya aina gani.Endelea tu Mheshimiwa Kakoso.

MHE. SELEMANI M. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunaishauri Serikali iwekeze fedha nyingi za kutosha kwenye eneo la Sekta ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, la pili, hata kama wananchi wengi watawekeza kwenye kilimo na kikawa kinalipa, kama hakuna masoko ya msingi, Serikali haijajikita kutafuta masoko ni kazi bure. Mkulima anapozalisha hawezi kusukumwa, kinachomsukuma ni soko, ndiyo maana mnaona mwaka huu watajikita kwenye kilimo cha mpunga, baadaye watahama wataenda kwenye kilimo cha mahindi, ni kubahatisha kutafuta soko.

Tunaiomba Serikali iwekeze kwenye kitengo cha masoko ilikile kinachozalishwa na wakulima kiweze kuwa na uhakika wa kupata masoko yaliyo mazuri.

Mheshimiwa Spika, tunayo mazao makubwa nchini yanayoingiza fedha nyingi za kigeni. Kwa bahati mbaya sana bado Serikali haijawekeza sana. Tukitaka uzalishaji wa tumbaku, mkonge, pamba ni lazima tuwe na uwekezaji mkubwa na ifike mahali Serikali iwekeze na kuweka ruzuku ya kutosha kwenye mazao haya. Naamini tukifanya hivi, Serikali itakuwa inanufaika kwa kiwango kikubwa, mzunguko wa fedha utakuwa mkubwa na wananchi watanufaika sana, ukata hautakuwepo kwa sababu ni eneo ambalo limeshika walio wengi.

Mheshimiwa Spika, nichangie kwenye eneo la miundombinu. Serikali imewekeza fedha nyingi sana kwenye eneo la miundombinu, lakini ushauri wangu naomba nijikite sana kwenye eneo la TARURA.

Mheshimiwa Spika, tulianzisha TARURA lakini haina bajeti. TARURA inategemea fedha za Mfuko wa Barabara ambazo zinakusanywa asilimia 100. Kati ya asilimia 100, asilimia 30 ndizo zinazoenda kwenye eneo la TARURA na asilimia 70 zinaenda kwenye Mfuko wa Barabara kwa ajili ya matengenezo ya TANROADS. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaweza tukawa kituko pale ambapo tulianzisha kitu ambacho hakiwi supported. Tunaomba Serikali kuu itenge fedha za kutosha, nchi yetu imekuwa kubwa, tuna maendeleo ya kila aina, kila sehemu panahitaji miundombinu ya barabara. Hata hayo mazao tunayozalisha yanategemea barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuna bajeti ya TARURA. Kama nilivyozungumza hapa naelewa mfuko ule unaotumika kwenye bajeti ya TARURA ni Mfuko wa Barabara tu ambao chanzo chake tumekiweka kwenye eneo la mafuta. Sasa niombe Serikali ifanye kama inavyofanya kwenye eneo la barabara kuu zinazohudumiwa na TANROADS ifikie mahali itenge fedha za kutosha ili ziweze kuhudumia barabara. Maeneo haya ni muhimu sana kwa hiyo Serikali iangalie ili tuweze kupata kile ambacho Mheshimiwa Rais anakitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni mindombinu ya umeme. Serikali imejikita kupeleka umeme vijijini. Tuna mategemeo makubwa na Serikali kwamba itapeleka miundombinu hiyo.

Naomba Serikali ihakikishe kama Mheshimiwa Rais alivyosema tuhakikishe maeneo yote vijijini yanapata umeme. Tukifanya hivyo tutakuwa tunakuza uchumi kwa kiwango kikubwa ambacho kitawasaidia wananchi. Maeneo mengi bado kwenye vijiji hawajapata umeme ambapo malengo ni kusukuma na kuleta mapinduzi ya kiuchumi. Tunaomba eneo hili liangaliwe sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nichangie kwenye eneo la sekta ya afya. Hapa bado tuko nyuma sana kwenye bima ya afya. Niiombe sana Serikali katika kipindi hiki cha miaka mitano tuhakikishe Watanzania wote wanapata bima ili waweze kunufaika na Serikali ambayo imefanya mambo makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali, tunampongeza Mheshimiwa Rais, nami naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafsi nami nichangie Mpango wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nijikite katika eneo moja ambalo litatusaidia sana Waheshimiwa Wabunge tujue nini cha kufanya. Asilimia kubwa ya Wabunge wanalalamikia sana miundombinu na TARURA. Yalikuwepo mawazo kufikia hatua ya kutaka kufanya mgawanyo wa fedha za Mfuko wa Barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kuwaelimisha ili wajue. La kwanza Mfuko wa Barabara umeundwa kwa sheria ambayo ilipitishwa na Bunge. Malengo yake yalikuwa kuhakikisha barabara zilizojengwa na TANROADS zinakuwa imara na zinapitika katika kipindi chote. Fedha za Mfuko wa Barabara si nyingi, ni karibia bilioni 900 kwa mwaka. Asimilia 70 ya fedha hizo zinaenda TANROADS kwa ajili ya maintenance barabara zetu, 30% ndizo ambazo zinaenda kuhudumia barabara za vijijini na mijini. Sasa hapa ndipo ambapo mnaweza mkaona kwamba tuna eneo ambalo Serikali inatakiwa ilifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa Barabara ambao una 100%, 70% zinachukuliwa na TANROADS na ..

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, anayechangia ndiye Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Miundombinu. Kwa hiyo, tumsikilize vizuri mawazo yake kuhusu hii hoja ambayo Wabunge tumekuwa tukiisemea sana ya TANROADS na TARURA. Endelea Mheshimiwa. (Makofi)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hizo 30% hazina uwezo wa kutengeneza kitu chochote. Kwa mwaka 2015/2016 Mfuko wa Barabara; TANROADS walipata shilingi bilioni 541 na TARURA zilienda shilingi bilioni 257. Mwaka 2016/2017 TANROADS zilienda shilingi bilioni 519 na TARURA zilienda shilingi billioni 247. Mwaka 2018 TANROADS zilienda shilingi bilioni 573 na TARURA zilienda shilingi bilioni 246. Mwaka 2020 TANROADS zimeenda shilingi bilioni 524 na TARURA zimeenda shilingi 224. Mwaka 2021 TANROADS zitaenda shilingi bilioni 572 na TARURA zitaenda shilingi bilioni 245. Barabara za TARURA zina zaidi ya kilometa 130,000 kitu ambacho haziwezi kutengenezwa kwa hizi fedha zinazotengwa. Ni miujiza ambayo itatokea kama tutaweza kutatua tatizo la TARURA. TANROADS wanaweza kwa sababu Serikali Kuu wanatoa bajeti ya kujenga barabara na hata hizi zinazotengwa kwa 70% hazitoshi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina ushauri Waheshimiwa Wabunge, tunapokuwa tunajenga hoja ili barabara zetu ziweze kutengenezwa tuna maeneo ambayo tunaweza tukaishauri Serikali. La kwanza Serikali itenge fedha iwape TAMISEMI wawe na bajeti kwa ajili ya kujenga barabara zetu za vijijini. La pili linahitaji maamuzi sisi wenyewe kama Wabunge. Mimi naangalia chanzo kipya ambacho tunaweza tukakiangalia kikaja kutatua tatizo la ujenzi wa barabara za mijini na vijijini kupitia TARURA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele ambacho nataka niwashawishi Wabunge wenzangu kama tutafika mahali tukakubaliana, tukaishauri Serikali na Serikali ikachukua mawazo yetu, tuna eneo la mawasiliano. Kwenye sekta ya mawasiliano kwa siku tuna uwezo wa kutumia simu milioni 30, hizo zinafanya kazi ndani ya nchi yetu, tuna idadi ya simu karibia milioni 50. Kwa hiyo, milioni 30 zina uwezekano wa kupata chanzo kipya cha fedha na huko ni eneo ambalo ni luxury tu asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza tutenge shilingi kumi kila mtumiaji wa simu ajue kwamba leo ninapopiga simu nachangia shilingi kumi kwa ajili ya mfuko wa barabara, zitakazokuja kujenga barabara za miji na vijijini. Milioni 30 mara kumi utapata milioni 300 mara saa moja, mara mwezi, mara mwaka, tuna uwezo wa kupata trilioni 1.296 ambazo zitakuja kutoa tatizo la barabara, hapo tunakuwa na chanzo ambacho ni kizuri na ambacho hakitakuwa na tatizo kwa wananchi wote na watu watakuwa wanajua kwamba mimi kama mtumiaji wa simu ninayetumia siku ya leo nimechangia barabara za miji na vijijini, tatizo hili litakuwa limeondoka kabisa. Naomba eneo tulifanyie kazi na wenzetu wa Kamati ya Bajeti waendee wakajaribu kuangalia haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni kwenye eneo hilo hilo la mawasiliano, sisi tunafanya miamala ya simu kwa siku kwa mwezi tunafanya miamala yenye thamani ya shilingi milioni 300, kila mwezi ambayo iko kwenye mzunguko na Serikali wanapata fedha kupitia mzunguko huo huo karibu kwa mwezi mmoja kunakuwa mzunguko wa fedha wa trilioni 18 zinazozunguka kwenye sekta ya mawasiliano. Kwa hiyo, hata huko nako tukiangalia kwamba pana uwezekano naamini tunaweza tukafikia karibu trilioni moja na nusu tukapata fedha hizi zikaja kujenga mazingira ambayo yatawasaidia Watanzania, hata hiki kilimo tunachokisema kama hatuna barabara zinazounganisha huko vijijini ni sawa na hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni eneo ambalo nililiona ni la muhimu sana, na ile dhana ambayo mnafikiri Waheshimiwa Wabunge kwamba tuzigawanye zile fedha tunakosea. Tusije tukarogwa kuja kupotosha kabisa kuuhamisha ule Mfuko wa TANROAD, tukihamisha matokeo yake barabara nyingi zilizojengwa na Serikali zitakufa, tukajifunze Zambia, Zambia walifanya kosa kama hili walijenga barabara hawakutenga fedha za maintenance matokeo yake barabara zote asilimia kubwa zilikuwa mashimo mashimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nchini ipo barabara ambayo ni ya mfano ilijengwa kwa mfumo huo, haikutengewa fedha za maintenance, barabara ya kutoka Arusha, Minjingu iliisha ndani ya kipindi kifupi sana. Naomba hili tulifanyie kazi na naomba Serikali ipokee mawazo ili yaweze kusaidia kutatua tatizo la barabara za miji na vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hili ndilo nililochagua kuchangia kwenye mpango ili liweze kutusaidia na wananchi wote wajue na Waheshimiwa Wabunge waelewe kwamba mfuko tunaouchangia ni mfuko ambao fedha zake sio nyingi sana na tukiumega una athari kubwa sana ambazo zitaleta kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Nami niungane na wenzangu waliotoa pole kwa kuondokewa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ngumu sana kusahau yale ambayo yamefanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa Watanzania wote bado wana kumbukumbu ya urithi ambao ametuachia kwa miradi mikubwa ambayo ameitekeleza hapa nchini. Naamini karibu kila Mtanzania ameguswa kwa sababu Dkt. John Pombe Magufuli alifanya kazi ya kujitoa kuwatumikia Watanzania kwa nia moja na kupeleka miradi karibu kila sehemu. Hakuna asiyejua dhamira ya Mheshimiwa Rais aliyokuwa nayo. Amejenga barabara, karibu kila mkoa kuna alama alizoziacha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika,Hayati amejenga Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo litawanufaisha Watanzania wote kwa kupata umeme ambao utakuwa na gharama nafuu. Bado amejenga meli kwenye maziwa makuu, ziwa Victoria kuna ujenzi wa meli mpya na amekarabati meli ya MV Victoria na MV Butiama. Ziwa Nyasa kuna meli mbili ambazo zimejengwa, Ziwa Tanganyika kuna mpango wa kukarabati meli ya MV Lihemba na kuna ujenzi mpya wa meli ndani ya Ziwa Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, amejenga bandari na kukarabati bandari; Bandari ya Mtwara, Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga, haya yote yamefanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Amenunua ndege ambazo kimsingi zinaonekana na zimepata alama ya Taifa letu, huko nyuma tulikuwa na ndege moja tu, ameacha ndege nane na ndege tatu zilishanunuliwa japo kuna maneno mengi ambayo wananchi wanazungumzia ambayo hawafahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Ndege lilianza kuwekezwa upya na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa hiyo ustawi wa shirika hili hauwezi kustawi kwa muda mfupi kwani uwekezaji wake umetumia gharama kubwa na hasara ambazo zinasomeka kwa sasa ni za kawaida kwa mashirika ya ndege. Jirani yetu Shirika la Kenya Airways wamepata hasara ya zaidi ya shilingi bilioni 600 katika kipindi hiki ambacho tulikuwa na matatizo ya Covid. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sana ujenzi wa reli. Wapo ambao wanapotosha ukweli, mimi na Kamati yangu kwa ujumla tumeshuhudia mradi wa reli ambao umejengwa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro ulishakamilika. Hatua ambayo imefikiwa kwa sasa ushauri wangu kwa Serikali naomba katika kipindi wanakamilisha zile asilimia 97 ambazo zimefikia kwa sasa, tunaishauri Serikali wajipange kwa wakati ili wanunue vichwa vya treni, wanunue mabehewa ili treni ile ianze kufanya kazi. Pengine yale maneno yanazoyungumzwa yatakuwa yamekatika kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipo kipande cha reli cha kutoka Morogoro – Makutupora nacho kimejengwa kwa sasa karibu asilimia 60. Maendeleo ni mazuri sana, naishauri Serikali kwamba pamoja na jitihada ambazo zinajenga reli kipande cha kutoka Mwanza – Isaka, tunaomba Serikali sasa ijipange haraka kuhakikisha kipande cha kutoka Makutupora – Tabora kinajengwa ili reli iweze kukamilika. Tunafahamu mipango ya reli kipande kingine ni kukitoa toka Tabora kwenda Kigoma na kutoka Kaliua kwenda Mpanda na Mpanda hadi Karema ambako kunajengwa bandari. Niiombe sana Serikali iweke mahusiano na nchi jirani ya DR Congo kuhakikisha wanatengeza mahusiano ya kibiashara ili tuweze kuitumia vizuri fursa ya bandari. Naamini Serikali iliratibu vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo naomba Serikali iangalie ni mradi wa maji wa kutoka Ziwa Tanganyika kuleta maji Mkoa wa Katavi. Huu ni mradi ambao utawasaidia sana wananchi wa Mkoa wa Katavi na mikoa jirani. Mradi huu ukikamilika utatoa fursa kubwa sana. Mradi mwingine ambao tunautegemea sana Mkoa wa Katavi ni Hospitali ya Mkoa wa Katavi. Tayari Serikali imetoa fedha, lakini tunaomba kasi ya utoaji wa fedha iongezeke ili tuweze kupata huduma ile ya kimsingi inayohitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo. Huwezi kuzungumzia maendeleo ya nchi hii kama hujazungumzia kilimo. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kusimamia mazao makuu ya pamba, tumbaku, kahawa, korosho, mkonge na mazao mchanganyiko. Mazao haya yanahitaji usimamizi mkubwa sana na Serikali inahitaji iwekeze ipasavyo ili kuweza kukuza uchumi. Unapokuza uchumi kwa mkulima utakuwa umetengeneza uchumi kwenye maeneo yote ambayo yatazaa viwanda kutokana na rasilimali iliyopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la kilimo kunahitajika sana kitengo cha masoko kiweze kuimarishwa ipasavyo kwani eneo kubwa ambalo kuna shida kubwa sana kwenye mazao pindi yanapozalishwa ni uhaba wa masoko. Niiombe Serikali ihakikishe inafuatilia masoko hasa ya nje kwenye mazao haya ambao ni ya kimkakati hasa yale ambayo sio ya chakula ambayo yanahitaji mfumo mzuri wa mawasiliano ya nchi na nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tukihitaji kutengeneza uchumi wa nchi hii ni kuwasaidia wafugaji na wavuvi. Kwenye maeneo haya bado Serikali haijawekeza fedha za kutosha kwani tukiwekeza kwenye maeneo haya ya ufugaji tutawasaidia sana wananchi. Maeneo ambayo tunahitaji Serikali ipeleke fedha za kutosha tuboreshe ranch, ranch za Taifa zitakapokuwa zimeboreshwa zitawafanya sasa ranch waweze kununua mazao kutoka kwa wananchi wale wa chini wafugaji na vile vile tukiimarisha viwanda kwa ajili ya kuchakata samaki vitasaidia kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa kunipa nafasi, niishukuru Wizara kupitia kwa Waziri kwa kazi nzuri sana ambayo imefanyika ndani ya kipindi cha miaka mitano. Tumeshuhudia ongezeko la vituo vya afya, shule nyingi zimejengwa na fedha zilikuwa zikienda, na mimi jimboni kwangu nilipata hizo sehemu ya huduma za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita zaidi kwenye eneo ambalo Wabunge wengi wamezungumzia, suala la TARURA. TARURA kwa bajeti ambayo ipo haitakuwa na uwezo wa kufanya kitu chochote kile, na Waziri nikuhakikishie dada yangu, kama utakuwa na bajeti uliyonayo ni ngumu sana kutekeleza miradi ya maendeleo. Tuna kilometa zaidi ya 100,000 za barabara za mijini na vijijini. Pamoja na ongezeko uliloleta la shilingi bilioni 124 kwenye bajeti hiyo, haiwezi kufanya kitu chochote kile kwani mahitaji ni makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, sasa ninawaomba tutoke na maazimio ya kuishauri Serikali na maamuzi magumu ambayo tukiyafaya tutapata suluhisho la kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kwenye Bunge hili, Bunge hilo ndilo lililotoa maamuzi tukapata fedha za kujenga barabara Mfuko wa TANROADS, zilipatikana kupitia Bunge. Mfuko wa REA, Wabunge hapahapa ndio tuliopitisha tukapata fedha za kuendeleza miradi ya umeme vijijini. Bado tumekuwa na mawazo ya kujenga uwezo juu ya Mfuko wa Maji. Ni sisi hawahawa Wabunge ambao ndio tunahitaji kutoa mawazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mapendekezo ambayo yataisaidia Serikali kutoka mahali tulipo. Naomba Waheshimiwa Wabunge turidhie, tutenge shilingi 100 – haya ni mawazo ambayo ataweza kuangalia sasa Waziri wapi watakwenda – tuna maeneo matatu ya mapendekezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la kwanza alilitoa Mheshimiwa Zungu; shilingi 50 tuitenge kwa ajili ya sekta ya mawasiliano, kila mtu anapopiga simu kwa siku tuwe tunachangia shilingi 50, na tuweke wazi kwamba shilingi 50 tunatenga kwa ajili ya kujenga barabara za mijini na vijijini. Itatusababisha kupata shilingi bilioni 540.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutaona shilingi 50 haitoshi, tukitenga shilingi 100 kwa siku, kila mtumiaji wa simu akitumia shilingi 100, tutapata shilingi trilioni moja na bilioni 80 ambayo ni fedha zitakazoweza kwenda kujenga miundombinu ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda mbali zaidi kama tunaweza tukatenga shilingi 200, kila siku mtumiaji wa simu akawa anatenga shilingi 200 Watanzania tukawaambia ukweli, na sisi Wabunge twende tukawaeleze ukweli wananchi wananchi kwamba shilingi 200 tunaitenga kwa ajili ya kuhudumia barabara za mijini na vijijini; tutapata trilioni mbili na bilioni 160. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa miaka mitano tutakuwa na miundombinu bora sana kwenye nchi yetu. Na zile fedha ambazo zimetengwa kwa sasa tulizonazo zitasaidia kwenda kuimarisha miundombinu ya zahanati, vituo vya afya na hospitali, mtajenga na majengo mengine kwa hii bajeti uliyonayo. Kwasababu tutakuwa tumepata chanzo kikubwa ambacho kitatoa fedha za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vinginevyo tutakuwa tunasema maneno ambayo yatajirudia. Kila mtu atakuja atasemea juu ya TARURA, TARURA haina fedha ya kutosha. Naomba hili Waheshimiwa Wabunge tuungane kwa pamoja, tuwe na maamuzi ambayo yatatusaidia kupata mahali pa kutoka kupata fedha za kutosha za kuhudumia maeneo ya huduma za simu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie fedha za Mfuko wa Jimbo; kumekuwa na uwiano usiokuwa sawa kwenye majimbo mbalimbali ambayo yanatofautiana. Bado Mfuko wa Jimbo ni uleule, tena ambao haujapitia tathmini ya kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, mnakuta mtu ambaye ana kata tatu, tano au sita mnapewa sawa na wale ambao wana kata zaidi ya kumi mpaka ishirini, naomba hili mkalifanyie kazi, mfanyie review ya majimbo yote, muangalie ukubwa wa majimbo ili tuweze kupata uhalisia mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ninapenda kuiomba Serikali; zipo halmahsauri kama ya kwanga ambayo mimi nimetoka, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda, ndiyo iliyozaa halmashauri zote ambazo zipo Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kila halmashauri iliyokuwa inazaliwa walikuwa wanatoa magari kwenye halmashauri mama, matokeo yake halmashauri mama ilikosa vyombo vya usafiri. Tumetoa kupeleka manispaa, tumepeleka Mlele, Mpimbwe na Nsimbo, matokeo yake hii halmashauri haina vyombo. Ninaomba kupitia kwa Waziri, aiangalie halmashauri hii aipatie vyombo vya usafiri ili viweze kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tunayo majengo yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi, ni karibu sehemu zote. Naamini kama mapendekezo tuliyotoa yakifanyiwa kazi zile fedha zitakazobaki hapo tuzipeleke ziende zikaimarishe kujenga majengo ambayo wananchi wamejitolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni karibu nchi nzima kila sehemu wanajitolea, wanajenga kwa nguvu zao, bahati mbaya yale majengo yanachukua muda mrefu na wakati fulani yanaanguka kuwavunja nguvu wananchi. Tunaomba sehemu ambako wamejenga majengo ya zahanati, vituo vya afya, shule za msingi na sekondari, Serikali muwaunge mkono mpeleke fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ni kauli ya kwenu ninyi Serikali ambayo mnaitoa kwamba asilimia 20 ikifanywa na wananchi na asilimia 80 Serikali itakuja kuwa-support sasa matokeo yake wananchi wako fasta kuliko Serikali inavyopeleka huduma hiyo ya msingi. Naomba hili mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba muangalie sana posho za wenyeviti wa Serikali za vijiji, posho za Waheshimiwa Madiwani, ambao wanafanya kazi kubwa sana. Kila jambo linalotekelezwa na Serikali linashuka huku chini. Wanaofanya hiyo kazi ya hamasa ni hawa wenyeviti wa Serikali, wenyeviti wa vitongoji na Madiwani ndio wasimamizi wakubwa. Kwa hiyo tunaomba eneo hili mliangalie ili waweze kufanya kazi kwa tija na kwa ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kunipa nafasi. Awali ya yote niishukuru sana Serikali kupitia kwa Waziri kwa kuleta miradi mikubwa na mingi kwenye jimbo langu, ninakushukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kuzungumzia tunahitaji Mradi wa Ziwa Tanganyika. Kati ya maeneo ambako hatujatendewa haki na karibu Mikoa ya Kigoma, Katavi na Mkoa wa Rukwa hatujapata huduma ya maji safi na salama, lakini tukiwa tumeyaangalia. Ziwa Tanganyika ndio ziwa ambalo lina maji mengi, tena maji safi, kwa bahati mbaya sana wananchi wa mikoa hiyo hawajapata huduma ya maji kutokana na hilo ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuombe sana Mheshimiwa Waziri, nimeona kwenye kitabu tuna bilioni karibu 600 ndani ya mikoa hiyo mitatu. Niombe sasa Serikali ije na mpango mkakati kuhakikisha mikoa ambayo inazungukwa na hilo ziwa iweze kunufaika kupata mradi wa maji ya kutokana na ziwa Tanganyika. Mradi huu ukiyatoa maji Ziwa Tanganyika jimboni kwangu utanufaisha karibu vijiji kumi, Vijiji vya Ikola, Kapalamsenga, Karema, Kasangantongwe, Sibwesa, Kasekese, Ikaka, watanufaika na huu mradi, lakini utakuja kuwanufaisha sana wananchi wa Mkoa wa Katavi, Makao Makuu ya Mkoa pale Mpanda Mjini. Niombe Mheshimiwa Waziri hili ukalifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo jingine ambalo nina ombi ni mradi wa ukarabati wa visima kwenye eneo la Mishamo. Eneo hili lilikuwa ni eneo lilikuwa linahudumiwa na shirika la wakimbizi. Karibu miradi mingi iliyochimbwa visima vilivyokuwa vimechimbwa kwenye maeno hayo vilihudumiwa kwa muda mrefu na shirika hilo la wakimbizi na baadaye visima hivyo vikawa vimeharibika. Nimeona kwenye bajeti upo mpango mkakati wa kuvikarabati. Niiombe sana Serikali kupitia kwako Mheshimiwa Waziri tunahitaji sana ufufuaji wa hivyo visima viwasaidie wananchi. Karibu wananchi 60,000 wanaoishi kule huduma yao ya maji si nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini upo mradi wa maji ambao tulishaiomba Serikali Kijiji cha Ifumbula, Kijiji cha Kapemba, Kijiji cha Mwazwe na Kijiji cha Rugufu. Tunaomba huu mradi muupelekee fedha ili uweze kuwanufaisha wananchi kwenye maeneo haya. Ni imani yangu Mheshimiwa Waziri kama mtapeleka huu mradi utasaidia sana kutatua kero ya maji kwenye eneo la Mishamo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho tunaomba Mheshimiwa Waziri, tunajua jitihada ambazo unazifanya ni kubwa sana wewe na wataalamu wako na wasaidizi wako kwa ujumla. Miradi ya maji ina gharama kubwa sana ni vyema sasa Mheshimiwa Waziri uende ukaangalie, tuna miradi ambayo inaidhinishwa na Serikali ukiungalia fedha zinazotolewa na mradi unaokuwa umetekelezwa haviendani sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri hili uweze kulisimamia tunakuamini kwamba, umefanya kazi nzuri na ulishafika jimboni kwangu umefanya mikutano na umezindua miradi ya maji ambayo ilishatekelezwa. Lakini ni vizuri sasa mkaangalia mfumo wa utekelezaji kwa ajili ya miradi hii ambayo inachukua fedha nyingi. Mkiibana mnaweza mkapata nafasi ya kuweza kupunguza gharama na tukatekeleza miradi mikubwa mingi itakayowanufaisha wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kukushukuru Mheshimiwa Waziri. Yupo Engineer ambaye anafanya kazi kwenye halmashauri yangu amefanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)
Hoja Kuhusu Bei ya Kuuza na Kununulia Mahindi
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nikushukuru kwa kunipa nafasi. Maelezo aliyoyatoa Mheshimiwa Bashe jana kwenye Bunge hili ni vitu viwili tofauti na uhalisia uliopo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Rukwa na mikoa yote ambayo inazalisha zao la mahindi, bei ilikuwa nzuri sana katika kipindi ambacho soko lilikuwa huria. Mkoa wangu gunia la kilo 100 lilikuwa likiuzwa shilingi 90,000 mpaka shilingi 95000. Hali halisi baada ya maelezo ya Mheshimiwa Waziri, leo hii Mkoa wa Katavi mahindi ni shilingi 50,000, shilingi 60,000. Kwa hiyo, ni anguko kubwa sana kwa wwakulima.

Mheshimiwa Spika, maelezo ambayo yanazungumzwa na wenzangu na maelezo ya Mheshimiwa Musukuma ambaye amesimama hapa, asilimia kubwa ya maelezo hayo ni wale ambao ni madalali, walanguzi ndio wanaokwenda watachangia hoja hii, lakini uhalisia kwa mwananchi mkulima ambaye anazalisha ana masikitiko makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, NFRA hawana uwezo wa kununua mahindi kwa sasa na masharti yao ni magumu mno. Hata hivyo, namba mbili, mfumo uliozungumzwa na Mheshimiwa Waziri haujafunguka mpaka sasa, ni vitu viwili tofauti vinavyozungumzwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri asisahau, alisimama kwenye Bunge hili akauthibitishia umma kwamba hakuna mkulima yeyote atakayezuiliwa kuuza mahindi mahali popote pale. Alishasahau? Ni jambo ambalo linafanywa tofauti kabisa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wazo kwa mikoa ambayo tunazalisha zao la biashara ambalo sasa hivi tumeambiwa na Serikali na wao wenyewe wakatuhamasisha, zao la mahindi ni zao la biashara na ni zao la chakula…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa kengele imegonga.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, kazi ya Serikali ni kununua mazao. Kama hawana uwezo wa kununua, waaachie wakulima wauze mahali popote pale wanapotaka. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kunipa nafasi hii na niwashukuru sana Waziri mwenye dhamana, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara hasa kwa kushughulikia kero za wavuvi kwenye eneo la Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nitajikita zaidi kwenye eneo la uvuvi. Uvuvi ni eneo ambalo linaweza likalipatia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa sana. Lakini kwa bahati mbaya sana Ziwa Tanganyika ni ziwa ambalo halijawekezwa kitu chochote ambacho kinaweza kikatoa tija kwenye sekta ya uvuvi. (Makofi)

Niombe sana Mheshimiwa Waziri sisi Watanzania tunatamani keki iliyo ndogo iweze kuwanufaisha sehemu zote, kwa bahati mbaya sana Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa ni mikoa ambayo inapakana na Ziwa Tanganyika na tunapakana na nchi jirani ya Zambia, Kongo na Burundi.

Mheshimwia Spika, mazao yanayozalishwa ndani ya maeneo hayo wanufaikaji wakubwa ni nchi jirani kuliko sisi ambao tuna eneo kubwa sana eneo la ziwa na hiyo ni kwa sababu Serikali haijawekeza kitu chochote ziwa Tanganyika lina kina kirefu na bahati mbaya asilimia kubwa ya mazao yanayotoka kwenye ziwa hili mengi yanapatikana kwa uvuvi ule wa kubahatisha. Tunaiomba Serikali sasa ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais ya kujenga kiwanda kwenye eneo hilo na kuhakikisha wanapeleka zana za kisasa liweze kutekelezwa, kinyume na hapo tutakuwa tuna shuhudia samaki ambao wanakufa ndio unawajua kwamba kwenye ziwa hili kuna samaki wakubwa kama hawa.

Mheshimiwa Spika, niombe Mheshimiwa Waziri aje na maelezo ya kutueleza uwekezaji mkubwa utakaowekwa kwenye Ziwa Tanganyika, tumeshuhudia kila mradi unaokuja kwenye Wizara unaelekezwa ukanda wa Pwani, unaelekezwa ukanda wa Ziwa Victoria na pengine Naibu Waziri anatoka ukanda wa Pwani na Waziri anatoka ukanda wa Ziwa Victoria. (Makofi)

Sasa tunataka watuthibitishie katika Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Rukwa ni mradi upi ambao watakuja kuwekeza kwenye ziwa Tanganyika. Nilikuwa naomba maelezo yatoke ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo hilo hilo bado tuna mialo ambayo inahitaji kujengwa kwenye ukanda wa ziwa, kwa bahati mbaya sana mialo iliyopo kwenye eneo hilo ni kidogo mno. Nilikuwa naomba maelezo ya Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja yake ni lini ataleta mwalo kwenye Kijiji cha Karema, Tarafa ya Karema ambako kuna wavuvi wapo na wanahitaji huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna eneo la mifugo; sisi tuna mifugo mingi sana ambayo imetoka Ukanda wa Ziwa iko kwenye Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa; tuna idadi ya mifugo mingi sana, lakini hakuna uwekezaji wa aina yoyote ile. Tulikuwa tunaomba atueleze Mheshimiwa Waziri sisi tutakuwa tunapokea tu idadi ya mifugo, lakini miradi ya maendeleo hakuna. Hakuna cha kiwanda chochote hata cha maziwa kilichoko kwenye maeneo hata kidogo, lakini bado wafugaji wanaishi kwenye mazingira ya kuhamahama kwa sababu hawana malisho ya kutosha. Tulikuwa tunaomba atueleze ni lini atatujengea mabwawa; atajenga mabwawa ambayo yatawasaidia wavuvi na wakulima na wafugaji ambao wapo kwenye maeneo hayo ili yaweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunahitaji sana mipango ya masoko ya zao la ng’ombe tuna ng’ombe ambao ukweli wanauzwa kwa bei ya chini mno ni kwasababu hatuna masoko mazuri. Kwa hiyo, tunaomba sana atuhakikishie Mheshimiwa Waziri ana mikakati ipi ya kuimarisha masoko kwenye maeneo ya minada. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Selemani Moshi Kakoso.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa jitihada wanazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ninalozungumzia zaidi ni eneo la Ziwa Tanganyika hasa kwenye Sekta ya Uvuvi. Ziwa Tanganyika ni ziwa ambalo lina kina kirefu na wavuvi ambao wanavua kwenye eneo la Ziwa Tanganyika wanavua uvuvi wa kubahatisha. Naiomba sana Serikali ielekeze nguvu kuwasaidia hawa wavuvi kwa kuwapelekea zana za kisasa ili waweze kujikwamua katika shughuli zao za kiuchumi, bila hivyo hawawezi kabisa kujikwamua. Kwa sababu eneo la Ziwa Tanganyika ni eneo ambalo mvuvi anaweza akakaa hata mwezi mzima asipate mazao ya uvuvi kutokana na kina kirefu kilichopo Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kuiomba Serikali, punguzeni tozo kwa wavuvi. Eneo hili linawakwamisha sana wavuvi. Unakuta mvuvi mmoja analipia leseni ya mtumbwi, analipia leseni yake kama mvuvi, analipia leseni ya wavu na analipia leseni ya umiliki wa chombo. Kwa hiyo, mtu mmoja analipa leseni karibu nne. Naiomba sana Serikali ikae iangalie jinsi gani ya kuwasaidia hawa wavuvi kupunguza zile kero ili wavuvi waweze kujikwamua katika shughuli zao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alifanya ziara kwenye eneo la Jimbo langu. Amefika eneo la Ikola; ule mwalo ulishamezwa, nilimwomba awajengee mwalo kwenye Kata ya Karema ili wavuvi hawa wanaovua kwenye Ziwa Tanganyika, eneo la Kata ya Karema wapate sehemu ya kuhifadhi mazao yao. Naomba sana hili alifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine kwenye Sekta ya Uvuvi ni eneo la mazalia ya samaki. Eneo hili ni muhimu sana kwa Wizara ili itenge maeneo muhimu ndani ya Ziwa Tanganyika ambayo yatasaidia sana kuwa na mazalia ya samaki ambayo yatakuwa endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni uthibiti wa nyavu haramu zinatokea nchi jirani ya Burundi. Zile nyavu za filamu ni mbaya sana ambazo kipande cha nyavu kikakatikia kwenye ziwa kinaendelea kuua samaki na vizalia vyote vilivyoko kwenye ziwa. Naomba hili mlifanyie kazi ili wavuvi wawe na uvuvi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie Sekta ya Mifugo. Tunamwomba Waziri aje na mpango mkakati wa kuboresha ranchi za Taifa ili ziweze kuwasaidia wafugaji wakubwa na wadogo. Pia tunamwomba aje kutujengea majosho kama alivyokuwa ameahidi alipokuwa amekuja kwenye ziara kwenye Jimbo langu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa hizo dakika tano…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa kwanza asubuhi hii.

Mheshimiwa Spika, kwanza, niipongeze sana Serikali kupitia kwa Waziri mwenye dhamana kwa kazi nzuri ambazo wanazifanya, hasa kwenye mradi mkubwa wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambapo naamini mradi huu ukikamilika utatua tatizo la umeme kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Spika, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa ajili ya Mradi wa Standard Gauge. Sisi kama Kamati ya Miundombinu tumeikagua reli, tumeshuhudia jinsi Serikali ilivyoanza kujenga vituo vya kupozeshea umeme kupitia Shirika la TANESCO ambalo naamini kabisa ndiyo tunategemea huo umeme uweze kuendesha Shirika hilo la Reli kupitia reli ya mwendokasi. Tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie sana mradi wa Grid ya Taifa, hasa kwa Mkoa wa Katavi. Mkoa wa Katavi unakua, una mahitaji makubwa lakini kwa bahati mbaya sana tunatumia umeme wa ma-generator ambao kimsingi haukidhi mahitaji ya watumiaji. Namuomba sana Mheshimiwa Waziri afanye mikakati ya haraka kuhakikisha Mradi wa Umeme wa Grid ya Taifa kutoka Mkoa wa Tabora kupitia Wilaya ya Sikonge uweze kukamilika haraka na ule mradi ambao unatokea Mkoa wa Mbeya, Songwe, Sumbawanga kuja Katavi nao ukamilike. Pia naomba ule Mradi wa Malagarasi, sisi Mkoa wa Kigoma ni jirani naamini ukikamilika utasaidia sana wananchi.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie Mradi wa REA. Tunaishukuru sana Serikali imeleta Mradi wa REA kwenye maeneo ya Jimbo langu, Wilaya ya Tanganyika lakini vipo vijiji vingi ambavyo bado havijapata umeme. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aweze kukamilisha miradi kwenye Kata ya Mishamo, Kata ya Bulamata, Ipwaga na Ilangu ambapo kwa ujumla vijiji vilivyobaki vipo 26 kwenye Jimbo la Wilaya ya Tanganyika. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na kutuletea mkandarasi ni vyema akawa na usimamizi wa karibu sana ili kuhakikisha miradi hii inakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na kuleta wakandarasi, vipo viko vijiji ambavyo kwenye Mradi wa REA II vilisahaulika, hasa kwenye Tarafa ya Karema, kipo Kijiji cha Kasangantongwe. Naomba Mheshimiwa Waziri watakapokuwa wanakuja kukamilisha kwa sasa na vile vijiji vilivyokuwa vimesahaulika viwekwe kwenye mpango ili viweze kuwasaidia wananchi.

Mheshimiwa Spika, vipo vijiji ambavyo vilishapelekewa umeme. Kwa bahati mbaya sana vimepelekewa umeme lakini kwenye maeneo ya mitaa na vijiji, vitongoji vimekuwa havipati umeme wa kutosha. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kukamilisha taratibu za kupeleka umeme kwenye vitongoji kwani tunapopeleka umeme kwenye vijiji, tusipeleke tu pale kijijini, tunahitaji uwafikie wananchi kwenye mitaa mbalimbali. Naomba suala hili alishughulikie, naamini Mheshimiwa Waziri ni msikivu, ni Waziri pekee ambaye anawasikiliza sana Wabunge na anaenda kila sehemu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, amefanya ziara kwenye jimbo langu, naamini vijiji vingi ambavyo naviongelea yeye anavifahamu. Amefika pale Kasekese, Mchakamchaka, Ifukutwa, sehemu zote hizo amezindua miradi ya maendeleo ya REA Phase III. Kwa hiyo, naomba hivyo vijiji vilivyobaki avifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa jioni hii. Awali ya yote, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu ya Wataalamu wote kwa jitihada kubwa ambazo wanazifanya za kuboresha utalii na kutunza Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwenye eneo la Mbuga ya Katavi. Mkoa wa Katavi una Mbuga ya Katavi na jirani Mkoa wa Kigoma tuna Mbuga ya Gombe na Yamahale ambazo ziko Jirani. Eneo hili halijawekewa mazingira mazuri ya kutangaza utalii kwenye ukanda huu. Naomba sana Serikali iangalie ukanda wa Magharibi kwamba kuna vivutio vingi na vizuri ambavyo vinaweza vikashawishi watalii wakaja kwenye maeneo ya kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalo Ziwa Tanganyika; ni utalii ambao unaweza kabisa ukawavutia wawekezaji na watalii wakaja kuangalia madhali nzuri ya kule. Sasa karibu asilimia kubwa, utalii unaotangazwa ni wa upande mmoja tu wa mikoa ya Kaskazini. Naiomba sana Wizara ielekeze nguvu kama walivyokuwa wameagiza kwamba sasa watawekeza kwenye ukanda wa kusini na nyanda za juu, halikadhalika kwetu kule magharibi wapeleke nguvu kuutangaza utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo la game reserve ya Lwafi. Game reserve ya Lwafi inapakana na msitu wa Nkamba Forest ambao unamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika. Kwa bahati mbaya sana, Pori la Akiba la Lwafi linatoa leseni ya uwindaji; na karibu sehemu kubwa wanapoenda kuwinda wanaenda kwenye pori la msitu wa Nkamba. Sasa msitu huo tunaishia tu kuuhifadhi lakini hatuna manufaa ya aina yoyoye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, pale ambapo wawindaji wanapotokea kwenye Pori la Lwafi, wanakuja msitu wa Nkamba Reserve, fedha zinazoitajika pale tuzipate kupitia Halmshauri ya Tanganyika. Ni eneo muhimu ambalo hatunufaiki nalo. Naamini wahusika watalifuatilia ili wajue ukweli ukoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo hifadhi ya misitu inayomilikiwa na TFS ya Pori la Msaginya, Mpanda North East na Msitu wa Kabungu. Maeneo haya yalishapoteza sifa ya kuwa na uhifadhi kwenye hii misitu. Mheshimiwa Rais alipokuja akiambatana na timu ya Mawaziri, walitokea ufafanunzi kwenye maeneo haya ambayo hayana uendelezwaji. Msitu wa Msaginya umejaa wafugaji humo ndani, kuna miji ya watu, kwa hiyo, sifa ile haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu wa Mpanda North East kwanza kuna makazi ya Katumba ambayo yana watu wengi. Katika msitu huu, sifa iliyokuwa imewekwa katika kipindi hicho, haipo. Nilikuwa naomba mshungulikie ile migogoro ambapo tunacho Kijiji cha Ngomalusambo, Kijiji cha Vikonge, Kijiji cha Majalila na vijiji vinginevyo ambavyo viko kwenye Jimbo la Mheshimiwa Anna Lupembe muweze kuvishughulikia tutoe ile migogoro ambayo haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya haya tutakuwa kwanza tumemuenzi Mheshimiwa Rais ambaye alitoa maelekezo na ninaamini Katibu Mkuu wa sasa ana kumbukumbu, pale tulipofanya ziara tukapitia kwenye Mbuga ya Hifadhi ya Katavi, tukaandaliwa chakula; karibu wanyama wa aina zote walipatikana pale. Kwa hiyo, naomba eneo hili mlishungulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao Msitu wa Tongwe Mashariki na Msitu wa Tongwe Magharibi ambapo tunapakana na eneo la Mbuga ya Mahale na pia tuna Msitu wa Nkamba. Misitu yote hii mitatu inamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika na tumefaulu kuilinda vizuri, kwa sababu tunadhamini kile ambacho kinafanywa; na wananchi sasa hivi walishaanza kuelimika, wametunza ile misitu wakiamini inawasaidia. Tayari tumeanza kunufaika, tunavuna hewa ya ukaa na vijiji sasa hivi vinapata fedha kupitia utunzaji wa misitu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri, najua yupo Meneja wa Kanda ya Magharibi wa TFS. Huyu amekuwa akijihusisha kuhujumu misitu kwenye maeneo ya kwetu. Huyu Meneja anashirikiana na wavunaji haramu wa misitu na kuwanyanyasa wafugaji wa nyuki wapatao 12,000 ambao wamo kwenye ile misitu. Sasa naomba huyu mumshungulikie ipasavyo. Kinyume na hapo, mtaleta matatizo na watu watakaa bila kuwa na imani. Pia ameenda mbali sana, badala ya kulinda huo msitu, anafikiria kugawa vitalu vya wafugaji. Nashangaa sana kwamba bado mko naye mpaka sasa hivi. Naomba hili mkalishughulikie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi, naomba Serikali ishungulikie migogoro ya vijiji nilivyovitaja hapo. Ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji wa siku ya leo. Awali ya yote niipongeze sana Serikali kwa kuleta bajeti ambayo ina matumaini makubwa sana kwa Watanzania. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada anazozifanya za kuijenga nchi yetu kwa vitendo, tumeshuhudia miradi mingi mikubwa ambayo anaizindua ikiwa ni muendelezo wa yale ambayo aliahidi kuwatumikia Watanzania hasa pale alipoahidi kwamba ataendeleza kazi zilizoachwa na mtangulizi wake, tunampongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ambayo imekuja ni bajeti ambayo inaweza ikatusaidia sana Watanzania. Hata hivyo tuna ushauri kwenye bajeti, yapo mambo ya msingi ambayo Serikali kupitia Wizara ya Fedha ni vyema ikayafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi sana wamezungumzia suala la kilimo. Watanzania wengi wanajihusisha sana na shughuli za kilimo ambazo ndizo zinawapatia kipato. Watanzania wengi wanajihusisha na shughuli za uvuvi na ufugaji. Sasa ukitaka kuutengeneza uchumi wa nchi lazima kwenye maeneo hayo ambayo yamewashika wananchi walio wengi mtenge fedha na muwezeshe kwa kiwango kikubwa. Na unapotenga fedha kwenye sehemu ya kilimo umewasaidia Watanzania wote. Kilimo kina mahitaji mengi kwanza kinahitaji uwezeshaji wa zana za kilimo, lakini pili kinahitaji mbegu za kisasa ambazo mkizisambaza wananchi watazalisha kwa tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado, lingine ambalo Serikali halifanyi kwenye sekta ya kilimo ni kutokutafuta masoko. Mazao yanapozalishwa wananchi wengi wanakosa masoko; na wanapokosa soko tunawajengea uwezo duni wakulima. Niiombe sana Serikali, katika mwaka huu wa fedha Wizara ijitahidi sana kuhakikisha mazao yale ya biashara na mazao ya chakula mnatenga fedha kwa ajili ya kutafuta masoko ambayo yatawasaidia wakulima wa nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kwenye kilimo hasa cha zao la mahindi jirani zetu wa Kenya ndio wanaozalisha mbegu wanatuletea sisi. Ni kitu cha ajabu, kwamba jirani anakuzalishia mbegu, unanunua na baadaye unaenda kumuuzia malighafi kutoka kwako. Ni vyema sasa Serikali itenge fedha kwa ajili ya kukuza vituo vya utafiti, na wale wanaozalisha mbegu tuwapate kwa wingi kwenye maeneo haya ili yaweze kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo linguine ambalo hatujalifanyia kazi zaidi ni kwenye sekta ya uvuvi. Mwenyezi Mungu alitujalia tukawa na Bahari ya Hindi yenye eneo kubwa sana la uvuvi. Tunaipongeza Serikali kwamba ina dhamira sasa ya kununua meli za uvuvi kwa ajili ya bahari ya hindi. Sasa tunaomba na kwenye Maeneo ya Maziwa Makuu Ziwa, Tanganyika pamoja na Ziwa Victoria tupeleke meli ambazo zitaanza shughuli za uvuvi sambamba na kutafuta mazao ya uvuvi ambayo masoko yake yatakuwa na uhakika. Hili litasaidia sana kuongeza tija kwa wananchi na wavuvi wa kwenye maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaipongeza Serikali kwa kuja na hoja ya kuongeza tozo ya simu na kuongeza fedha kiasi kwa ajili ya mafuta ili ziweze kuja kutatua kero ya Watanzania walio wengi, hasa wenye barabara za vijijini na barabara za mijini. Wakala wa TARURA ilipoanzishwa Serikali iliianzisha huu wakala tulikuwa hatujakuwa na maandalizi mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA ilipoanza haikuwa na fedha iliyotengwa kutoka Hazina, ilitegemea Mfuko Mkuu wa Barabara ambao wao walikuwa wanapewa asilimia 30 na asilimia 70 wanapewa TANROADS; na kazi yake kubwa ilikuwa ni kufanya matengenezo ya barabara kwa zile barabara zilizojengwa. Kwa bahati mbaya sana TARURA ina kilometa zaidi ya 100,000 ambazo zinahitaji kuhudumiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwa amekuja na pendekezo, na tumeangalia kwenye kitabu chake; Waheshimiwa Wabunge wengi walileta mapendekezo, niombe sasa fedha itakayotokana na ukusanyaji wa hiyo tozo tunaomba uziwekee mfuko maalumu kwa ajili ya kujenga barabara za mijini na vijijini, kuliko ilivyo sasa fedha hizo ambazo mmezitenga hazikuoneshwa kwamba zitalindwa vipi, huo mfuko.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini kero ya Watanzania walio wengi wanaoishi mijini na vijijini ni barabara. Na Watanzania wakishajua kwamba hizi fedha tunazochangia zinaenda kutatua barabara za mijini na vijijini hata kulalamika hakutakuwepo. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri zitenge hizi fedha ili ziwe na mfuko maalum kama ulivyo Mfuko wa Barabara; itatusaidia sana kuwa na uhakika wa kutengeneza miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nilikuwa napenda kuishauri Serikali ni kwenye sekta ya maliasili. Nchi yoyote ile ambayo ina watalii wengi iliwekeza fedha nyingi za kutangaza utalii. Zipo kampuni nyingi za wakala ya utalii ambazo ziko nje ya nchi. Sasa kwa nchi yetu bado hatujawekeza kwa kiwango kikubwa. Ninaomba sana Mheshimiwa Waziri tutenge fedha za kutosha ili tuwezeshe mawakala wa kutangaza vituo vya utalii nje ya nchi. Hii itatusaidia sana kuwa na idadi kubwa ya watalii kuliko ilivyo sasa. Nchi yetu ina vivutio vingi lakini idadi ya watalii wanaokuja hapa nchini ni wachache sana. Naomba hili tukawekeze kwa kiwango cha juu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala linguine, kwenye sekta hiyo ya maliasili, Serikali inapata mapato madogo sana kupitia misitu. Nchi nyingine kwa sasa zinanufaika sana kupitia misitu kuliko ilivyo sisi, tunategemea sana kuvuna misitu na kwenda kuuza magogo. Nikuombe Waziri mwenye dhamana mkishirikiana na Waziri wa Fedha, kipo chanzo ambacho mnaweza mkapata fedha nyingi sana wekeni mikataba na mashirika ya kimataifa kwa ajili ya kuvuna hewa ya ukaa. Eneo hili linatoa fedha nyingi mno. Mkisimamia uvunaji wa hewa ukaa sisi tuna misitu mingi ambayo inaweza ikatoa fedha itawanufaisha wanavijiji wanaolinda hiyo misitu, itanufaisha halmashauri na itanufaisha Serikali Kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninao mfano, kwenye halmashauri yangu tumejipanga. Halmashauri ya Tanganyika miaka ijayo tunaweza tusitegemee kabisa Serikali Kuu kwa sababu tunaweza tukapata mapato kwa mwaka kati ya bilioni 30 kwa ajili ya utunzaji wa misitu. Sasa eneo hili halijafanyiwa kazi kwa kina. Serikali imejielekeza zaidi kuvuna ile misitu, na mahala ambapo panavunwa misitu huwezi ukalipwa fedha kwa ajili ya hewa ya ukaa na mashirika ya kimataifa. Naomba hili mkae mliangalie kwa kina.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunaishauri Serikali ni kuwekeza kwenye teknolojia, hasa za mawasiliano. Ninaamini Serikali ikiwekeza hapo tunaweza tukapata ajira kwa vijana na tukapata mafundi vijana ambao watakuja kufanya shughuli nyingi katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana na ninaunga mkono hoja, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa Taifa. Sisi tunatokea kwenye maeneo yanayozalisha kilimo. Katika eneo hili, kila Mbunge atawajibika kuelezea yale ambayo ni ya msingi kwa ajili ya wananchi ambao wanategemea sekta hii ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeuangalia Mpango, haujawa na suluhisho la kudumu na kutatua kero ya wakulima hapa nchini. Kilimo kinahitaji mambo ya msingi; la kwanza ni suala la umwagiliaji. Mungu alitujalia kwenye maeneo yetu, karibu kila sehemu ya nchi yetu inapata mvua za kutosha na tunapata maji mengi yanayoishia kwenda baharini bila kuwa na mfumo sahihi wa kuyavuna yale maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuwa na maendeleo ya sekta ya kilimo kama hatujawa na mipango thabiti ya umwagiliaji. Umwagiliaji pekee ndiyo utakaofanya kilimo kiweze kukua hapa nchini. Kwenye Mpango hatujaona mipango ambayo ipo ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni suala la ruzuku ya mbolea. Bila ya kuweka ruzuku ya mbolea hatutawasaidia wananchi. Bei za pembejeo ni kubwa kiasi kwamba uwezo wa kumudu kununua hizo pembejeo hawatakuwa nao. Tunaishauri Serikali iangalie umuhimu sasa wa kutenga fedha kwa ajili ya kuweka ruzuku ya mbolea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zinazofanywa na wakulima binafsi, bado wana kero nyingine kubwa sana ya ukosefu wa masoko. Eneo hili lazima Serikali waongeze fedha hasa za kununua mazao ya wakulima. Tunaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwawezesha wananchi waweze kulifikia soko la nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wa Mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa, Katavi na Kigoma ni maeneo ambayo yana eneo kubwa sana la mwambao la Ziwa Tanganyika, na wanaweza wakapata soko kupitia nchi ya DRC Congo. Serikali haijatafuta soko hili vizuri na kuwawezesha wananchi wakapata nafasi ya kulitumia hili soko. Tunaishukuru Serikali imejenga bandari kule eneo la Karema, bandari ya Kasanga na kule Kigoma, lakini bado tunahitaji barabara ambazo zitaunganisha maeneo haya yaliyo na bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru Serikali imejenga barabara eneo la Kasanga kutoka Sumbawanga kwenda Kasanga, lakini tuna barabara ya kutoka Mpanda Mjini kwenda eneo la Karema ambako kunajengwa bandari. Eneo hili ni muhimu sana, ni vyema ijengwe barabara ambayo itasaidia kujenga mazingira ya soko lililoko nchi ya DRC Congo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia nchi jirani ya Zambia ina vikwazo vikubwa sana kwenye maeneo ya usafirishaji. Kwa hiyo, tukitengeneza maeneo ambayo yanaweza yakawasaidia wananchi kwenye maeneo hayo, yatasaidia sana masoko kuwa mazuri na yatavutia na kuhakikisha soko la DRC Congo tunalishika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie maeneo mengine na kuongeza fedha za NFRA kwa ajili ya kununua mazao ya wakulima. Eneo hili ni muhimu sana ili tuweze kuwasaidia wakulima wawe na uhakika wa masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta nyengine ambayo tunahitaji kuishauri Serikali ni sekta ya uvuvi. Kwenye eneo la uvuvi bado Serikali haijapeleka fedha wala kuwasaidia wananchi. Tukiwasaidia wakulima, wavuvi na wafugaji, ni maeneo ambayo yanaweza yakasaidia kukua kwa uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashauri kwenye uvuvi hasa nizungumzie Ziwa Tanganyika. Sisi wa Ziwa Tanganyika tunapakana na nchi ya Burundi, Kongo na Zambia. Wanufaikaji wakubwa wa hili ziwa ni nchi ya Congo DRC, Burundi na Zambia. Sisi ambao tuna eneo kubwa la Ziwa Tanganyika, sheria tulizoziweka sisi wenyewe, siyo rafiki kwa wavuvi wa wetu. Nichukulie mfano tu kwamba mvuvi wa Tanzania haruhusiwi kuvua mazao yake mchana, lakini nchi zinazotuzunguka wao wanavua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia, karibu mazao yote ya Ziwa Tanganyika, asilimia kubwa wasafirishaji wa mazao hayo ni nchi jirani ya DRC Congo ndiyo wanaouza au Zambia. Kwa hiyo, naomba zile sheria ambazo zinawabana hasa wavuvi wanaokatazwa kuvuna mazao kwenye kipindi cha mchana, waruhusiwe wawe wanavua mazao hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo lingine ambalo ni katika kulisaidia Shirika la Ndege la ATCL. Shirika hili kama Serikali hawataweka dhamira ya kulisaidia, halitasimama. Shirika hili lina madeni makubwa, linadaiwa karibu shilingi bilioni 215 ambazo ni fedha zinazodaiwa za kipindi hicho cha nyuma shirika lilipokuwa limekufa. Mzigo huu bado shirika hili linao. Kwa hiyo, tunaomba Serikali ichukue hili deni ili tuweze kulisaidia hili shirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utapanda ndege kutoka hapa Dodoma kwenda Dar es Salaam, nauli ya ndege kutoka hapa kwenda Dar es Salaam ni sawa na ya kwenda Dubai, kitu ambacho ni kigumu kwa Mtanzania wa kawaida kuweza kumudu kusafiri. Naomba hili Serikali waliangalie…

MWENYEKITI: Una maana gani Mheshimiwa Mwenyekiti?

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nauli ya ndege kutoka Dodoma, ukipanda ndege ya Shirika la Ndege la ATCL kwenda Dar es Salaam, nauli yake ni kati ya shilingi 500,000 mpaka shilingi 600,000 na mpaka wakati fulani inafika shilingi 700,000. Nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dubai ni shilingi 500,000 mpaka shilingi 600,000. Sasa haiwezekani kwamba shirika hili utaweza kulibeba; na linakuwa na…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana. Naona ni kengele ya pili.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Ndiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Naomba Serikali ilisaidie shirika hili kulipunguzia madeni makubwa ambayo yapo ambayo kimsingi tukilipunguzia litaweza kumudu kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. MOSHI S. KAKOSO – MWENYEKITI KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote niwashukuru sana wote waliounga mkono hoja ya kamati ya Bunge ya Miundombinu, kwa bahati nzuri kati ya wachangiaji wote hakuna aliyepina hoja ya kamati yetu tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo mambo mengi ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa wabunge, nimepata hoja za wachangiaji wapatao 10 wakiwemo mawaziri Mheshimiwa Prof. Mbarawa na Mheshimiwa Nape ambao wamekuja kutoa ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazungumzaji ambao wamechangia kuunga mkono hoja ya kamati yetu wamesisitiza juu ya umuhimu hasa wa kuunganisha barabara kati ya mkoa na mkoa ambazo zimetolewa hoja kutoka kwa waheshimiwa wabunge naamini haya yote yaliyokuwa yakichangiwa yalikuwa yakiunga mkono hoja ya kamati yetu, na msisitizo wetu bado tunaishauri Serikali kuweka mipango thabiti ya kuimarisha na kuunganisha miundombinu ya barabara hasa kwenye mikoa ile bado haijaunganishwa ikiwemo mkoa wa Morogoro dhidi ya mkoa wa Lindi, Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma na Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Njombe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ipo mikoa mengine ambao inahitaji kuunganishwa ikiwemo Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Mara na Mkoa wa Arusha na Mkoa wa simiu, hiyo ni mipango ambayo tunaisistiza Serikali kuhakikisha wanaunganisha hiyo mikoa. Lakini wachangiaji wengine wamezungumzia juu ya ucheleweshaji wa GN ni mambo ambayo tumekuwa tukiishauri Serikali na hilo naamini wao kama Wizara husika watakuwa na mahusiano au kuwa na ukaribu na Wizara ya Fedha kuhakikisha wanalimaliza hili tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawapongeza sana waheshimiwa mawaziri kwa ufafanuzi ambao wameutoa. Mheshimiwa Profesa Makame Mbarawa amezungumzia suala la ujenzi wa reli. Lakini amezungumzia juu ya ushauri ambao umetolewa na kamati kwenye eneo la ushauri uliotolewa juu ya umuhimu sasa wa Serikali kuwachia viwanja vya ndege ambavyo vimekuwa vikijengwa na TANROADS sasa vianze kujengwa na mamlaka husika, ametoa ufafanuzi na amekubali maelekezo ya kamati, tunashukuru sana na tunawapongeza kwa uamuzi huo ambao kimsingi utakuja kuleta tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nape amezungumzia juu ya maalalamiko ya wananchi ambao wamekuwa wakilalamikia zaidi juu ya vifurushi ambavyo wanavitumia kabla havijakamilika wakiwa wamenunua vinakuwa vinatumika kinyume na matarajio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia jinsi utaratibu unavyotumika kwenye hizo bando zinavyotumika lakini kuna malalamiko yale ambayo wamekuwa wakilalamika wananchi juu ya makosa ya kimtandao ambayo kamati imeendelea kuishauri Wizara kuhakikisha wanawahusisha Wizara ya Mambo ya Ndani kwa maana ya Jeshi la Polisi ili waweze kutoa ushirikiano wa karibu kwa ajili ya kumaliza tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaamini sekta ya mawasiliano imefanya mapinduzi makubwa kupitia TCRA, ni kweli kabisa kwamba matatizo mengi ambayo yanajitokeza kwenye mitandao mengi yanaiangukia Wizara ya Mambo ya Ndani kushindwa kutoa ushirikiano kwa maana ya Jeshi la Polisi wanapobaini wanashindwa kutoa ushikiano wa karibu. Naamini Mheshimiwa Waziri wakikaa pamoja kama Serikali tatizo lile ambalo linajitokeza mara kwa mara linaweza likatoweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo ambayo tumeyapata kutoka kwa Waheshimiwa wabunge sisi kama kamati tutaendelea kuishauri Serikali na tunawapongeza kwa mchango wao wa mawazo makubwa, nirudie kuwashikuru sana wajumbe wa kamati ya Bunge ya Miundombinu kwa kazi kubwa ambayo mmeifanya naamini mchango wao umeonekana kwa kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kupata nafasi hii. Kwanza, niipongeze Serikali kwa jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Serikali yetu kwa kupeleka huduma muhimu za elimu, afya na maji na miundombinu kwa ujumla. Nataka nijikite kwenye eneo la Mradi wa Bandari ambao umewekezwa kwenye Wilaya ya Tanganyika, Mradi wa Bandari ya Kalema. Serikali imejenga Mradi wa Bandari ambao ni mkubwa na kimsingi tunayo fursa kubwa sana ambayo Serikali inaweza ikaipata pale ambapo tutafanya maboresho makubwa. Nchi ya DRC Kongo imejiunga na Umoja wa Afrika Mashariki, malengo ni kutaka kuitumia fursa ya soko la Afrika Mashariki. Sasa sisi kama Nchi ni vyema tukawa na uwekezaji mkubwa ili fursa iliyopo sasa, iweze kuwanufaisha wananchi wa Tanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ile bandari hautakuwa na faida kama hatutakuwa na uwekezaji mkubwa na fursa ile itatumiwa na nchi jirani ambao wataichukua kama fursa muhimu. Niiombe sana Serikali ujenzi wa Bandari ya Kalema uende sambamba na uwekezaji wa ujenzi wa reli na uimarishaji wa reli ya kutoka Kaliua, Mpanda hadi Kalema. Sambamba na hilo ni lazima kuwe na mpango mkakati wa ujenzi wa barabara ya Kabungu hadi Kalema. Kwani, ile bandari itakapokuwa imekamilika kama hakutakuwa na miundombinu shirikishi ujenzi ule utakuwa hauna maana yoyote. Kwa hiyo, naomba na naishauri Serikali tuwekeze mradi ule uwe na matawi yake ya ujenzi wa reli na ujenzi wa barabara. Ni muhimu sana katika kuimarisha ushirikiano wa East Africa tufanye mipango na mikakati ambayo Serikali itaisimamia kuhakikisha Nchi ya Congo inatumia Bandari ile ya Kalema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kongo ni Nchi kubwa na ina madini na ina mzigo mkubwa sana ambao tukiutumia kwa Bandari ya Kalema na Bandari ya Kigoma tutakuwa na fursa kubwa sana ya Bandari ya Dar es Salaam ikapata mzigo wa maana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala la kilimo. Nchi yoyote ile inaendelea kwa kuwekeza kwenye kilimo, bila uwekezaji mkubwa wa Serikali kwenye kilimo hatutafanya kitu chochote cha maana. Naomba sana lazima Serikali ije na mpango mkakati wa uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji kitawasaidia watanzania wote na kitaimarisha uchumi kwa nchi yetu. Niiombe sana Serikali iwekeze kwenye kilimo cha kisasa tuwe na mabadiliko ambayo, yataanza kuepuka sasa kilimo cha kutegemea jembe la mkono. Sambamba na hilo ni muhimu kwa Serikali kuwekeza kwenye mbegu, tuwekeze kwa wataalam, lakini kubwa zaidi ni kuimarisha Vyama vya Ushirika. Kwenye Vyama vya Ushirika ndivyo vinavyoweza kumkomboa mkulima mdogo mdogo ambaye anaweza sasa kuwa kiunganishi na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji Serikali iangalie umuhimu wa kusogeza huduma za pembejeo. Bei za pembejeo ni kubwa sana kiasi kwamba Watanzania wanashindwa kumudu hizo bei. Niombe Serikali yetu iimarishe Mfumo wa kuleta pembejeo na kujenga viwanda vya pembejeo ambavyo vitasaidia kupunguza gharama. Sambamba na hilo ni kuimarisha masoko, mazao mengi ambayo yanalimwa masoko yake ni ya shida. Tutoe ukiritimba wa Serikali ambao mkulima akilima kwa jasho lake, wakati fulani huwa anaanza kupangiwa bei na kuzuiliwa mazao yake kutokupelekwa nje ya nchi. Hili tunaomba Serikali ilifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna ushauri kwa Serikali kwenye eneo la uvunaji wa hewa ya ukaa. Nchi yetu ina misitu mingi ambayo haijatumika vizuri, wenzetu wa nchi zingine wanatumia fursa ambayo ipo kwenye maeneo yao. Serikali ni vyema sasa ikaangalia Mfumo wa uwekezaji na kuwasogeza wawekezaji wanaokuja kuwekeza kwenye uvunaji wa hewa ya ukaa. Mataifa mengi duniani yanaharibu mazingira sisi tuna misitu ambayo inamilikiwa na Serikali za vijiji, tuna misitu ambayo inamilikiwa na Halmashauri na misitu inayomilikiwa na Serikali Kuu. Katika maeneo haya ni vyema Waziri mwenye dhamana, akaja na mpango wa kubadili Sheria itakayonufaisha maeneo hayo yote yaweze kuvuna hewa ya ukaa. Kuna fedha nyingi sana ambazo tunazipoteza kama Taifa, eneo ambalo tuna Hifadhi za Serikali hawaruhusiwi kuvuna hewa ya ukaa. Sasa tukija na mabadiliko ya Sheria yatasaidia katika maeneo yote yaweze kuvuna hewa ya ukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kwenye eneo hili ninaiomba Wizara ya Maliasili, mgogoro uliopo Wilaya ya Tanganyika kati ya TAWA na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika waushughulikie ili wananchi waweze kunufaika kwani tayari tulishafanya mpango mkakati ambao utawawezesha wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika wapate fedha karibu zaidi ya Shilingi Bilioni Tano ambazo zitawanufaisha kwenye huduma zile za kimsingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie suala la barabara. Barabara inayotoka Mpanda kwenda Uvinza inayounganisha Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma, tunaomba Serikali iishughulikie na kuijenga ili iweze kuwa kiunganishi kwani ni barabara ambayo inaunganisha nchi na nchi, lakini kwenye maeneo haya tutakapokuwa tumejenga hii barabara Watanzania na nchi jirani watanufaika kwa sababu, miundombinu ndiyo inayoleta mazingira mazuri ya kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba na kuishauri Serikali mradi wetu wa maji wa Mkoa wa Katavi kutoa maji Ziwa Tanganyika kuja Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi, tunaomba sana mradi huu ufanyiwe kazi ndani ya kipindi hiki kwani miradi mingi midogomidogo imekuwa haina tija na kwenye Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ndiyo mikoa ambayo haijanufaika, wanayaangalia maji ambayo yapo kwenye Ziwa Tanganyika bila kunufaika nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kunipa nafasi. Awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada za kuleta maendeleo katika nchi yetu. Pia nimpongeze Waziri mwenye dhamana kwa kuwasilisha mpango ambao kama utafuatwa utakuwa na manufaa ya siku za baadaye. Niipongeze Kamati ya Bajeti kwa mawazo yao mazuri sana ambayo wameishauri Serikali. Mimi naamini mawazo yaliyowasilishwa na Kamati ya Bajeti mengi ni yale ambayo Wabunge wengi wamekuwa wakiishauri Serikali lakini kwa bahati mbaya huwa hayatekelezwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze mchango wangu kwenye sekta ya kilimo. Sekta ya kilimo ni sekta ambayo inawagusa wananchi wengi hapa nchini. Na Serikali kama inadhamira ya dhati kuwasaidia kundi kubwa la wakulima watakuwa na maendeleo makubwa sana na nchi itanufaika. Lakini kilimo ambacho tunakishauri kwa Serikali ni uwekezaji mkubwa ambao lazima Serikali iwe na dhamira ya dhati kuhakikisha wanatoka kwenye kilimo cha kubahatisha tuingie kwenye kilimo ambacho kina uhakika, cha umwagiliaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina maeneo mapana ambayo tuna maziwa na mito mikubwa ambayo haitumiki vizuri. Maeneo mengi yanafaa kwenye shughuli za kilimo lakini kwa bahati mbaya nchi yetu ilishakuwa na mabadiliko ya tabia nchi. Sasa kwa kuwa kuna mabadiliko ya tabia nchi, lazima Serikali ije na mkakati wa kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima ili waweze kulima kilimo ambacho kina uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matajiri wote duniani wanatengenezwa na Serikali. Kama Serikali haijawatengeneza matajiri, huwezi kuwapata. Matajiri hao ni hao hao Watanzania ambao wapo. Wanachohitaji ni uwezeshwaji. Rasilimali ya kwanza waliyonayo ni ardhi ambayo haijatumika vizuri kwa sababu taasisi nyingi za fedha hazitoi mikopo kwa wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali kupitia Wizara ya Fedha, tuache mipango ile ambayo haitekelezeki. Tumeanzisha Benki ya Kilimo ambayo kimsingi haijamkaribia sana mkulima. Taasisi zile za fedha tunaomba ziandae mpango mkakati ambao utakuwa chini ya Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha wanawawezesha wakulima ambao wanaweza wakatoa tija kwa kiwango kikubwa sana. Naomba hili mlifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine kwenye Sekta ya Kilimo ni kuwawezesha wakulima watoke kwenye kilimo cha jembe la mkono. Wakulima wengi wanalima kilimo cha kujikimu, wawezesheni wapewe zana za kisasa, sambamba na kuwawezesha kuwapa eneo la masoko, itawafanya wakulima wawe na manufaa na watu wengi watakimbilia kwenye Sekta ya Kilimo. Naomba hili Serikali ilifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo maeneo ambayo Serikali ikiwawezesha katika eneo la masoko, kwenye sekta ya kilimo kutakuwa na ukuaji mkubwa sana, Tumezungukwa na nchi ambazo uzalishaji wake ni mdogo...

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba pamoja na wakulima kutumia jembe la mkono, lakini wakulima hao hao kwenye korosho mwaka huu wamepata shilingi bilioni 300, kwenye tumbaku shilingi bilioni 600, kwenye pamba shilingi bilioni 275, lakini hawana matrekta. Pia mabenki hayo hayo yametangaza riba kutoka 15% mpaka 9% lakini kwa wakulima bado masharti ni makubwa sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Moshi Kakoso.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hiyo ambayo ameitoa Mheshimiwa Cherehani, ingawa bado pamoja na hiyo taarifa tunayopata, tija ni ndogo. Kipato wanachokipata wakulima bado hakitoshelezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wetu kwa Serikali, tuwekeze kwa kiwango kikubwa kwenye sekta ya Kilimo. Pamoja na kwamba mwaka huu Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kutoa ruzuku ya pembejeo, lakini kwenye maeneo ya kilimo cha umwagiliaji na uwezeshaji mkubwa kwenye sekta hiyo ya kilimo kutoka kwenye jembe la mkono kwenda kwenye kilimo cha kisasa ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nashauri Serikali ni miradi inayowekezwa na Serikali kwenye sekta ya ujenzi. Nakubaliana na wachangiaji wenzangu ambao wamechangia kwamba Serikali iachane na mpango wa kuanzisha miradi midogo midogo hasa ya ujenzi wa barabara. Ujenzi huu utaifanya Serikali iwe inatumia gharama kubwa lakini tija yake inakuwa ndogo. Mwaka huu tulipitisha bajeti na mpango uliopita wa mwaka jana 2021, walionesha kila eneo kwamba wanaweza kupeleka Kilometa 25, kitu ambacho hakiwezekani. Ni lazima Serikali iwe na mpangilio wa maeneo ya kipaumbele cha kujenga miradi ya maendeleo. Tukifanya hivyo tutakuwa tumeisaidia sana Serikali kuliko kama ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shabiby ameishauri Serikali kujenga miradi ya maendeleo ya ushirikishaji wa PPP na ile ambayo imekuja Wizara ya Fedha ya EPC iliyopendekezwa. Tunaafikiana nayo, lakini hoja yetu hap ani kwamba iharakishe mpango mkakati kuliko iliyopo tu kwenye mipango ya kwenye makaratasi. Tunaishauri Serikali iharakishe mpango huu, utasaidia kufanya maboresho makubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo Serikali ni vyema ikapeleka miradi ya maendeleo ni kwenye maeneo ambayo yatakuwa yana return ya urejeshaji wa fedha zilizowekezwa kwa kiwango kikubwa. Tunajenga reli. Reli ambayo ina manufaa makubwa ni reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma; reli ya Kaliuwa - Mpanda – Karema. Hizo ndizo reli ambazo zina uwezo mkubwa kuweza kutoa manufaa makubwa sana. Serikali imewekeza uwekezaji mkubwa wa Bandari ya Karema.

Mheshimiwa Mwenekiti, sasa hivi wafanyabiashara wa DRC Congo walishaanza kusafirisha shaba kwa njia ya mashua ambayo inatuharakisha sisi tupokee kwamba ni fursa iliyopo, tuweze kuitumia vizuri. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali mchango mkubwa wa uwekezaji wa reli uwekezwe kwenye reli ya kutoka Tabora kwenda Kigoma na kile kipande cha kutoka Uvinza kwenda Msongati hadi Burundi. Hata hivyo, reli ya Kaliuwa - Mpanda hadi Karema ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miradi ya maji. Tuna miradi ya maji mingi midogo midogo ambayo haiwasaidii Watanzania. Tukichukulie mfano wa Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, ni mikoa ambayo imezungukwa na maziwa. Kwa bahati mbaya, hakuna mradi mkubwa wowote unaounganisha miradi hii ya maji. Naomba tutumie fursa tulizonazo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, nizungumzie suala la uvunaji wa hewa ya ukaa. Tanzania ina misitu mingi na Wizara tumeishauri mara kwa mara na kwa bahati mbaya hawajaitumia hii fursa vizuri. Wenzetu Kenya wanaitumia fursa ya uwekezaji mkubwa kwenye uvunaji wa hewa ya ukaa. Kwa nchi yetu sasa hivi tuna maeneo kama matatu; Mkoa wa Katavi, Kiteto, eneo la Mkoa wa Manyara na Ruvuma, wameanza uvunaji lakini kwa kiwango kidogo sana. Tunaomba sasa Serikali ije na sheria mpya ambayo itafanya mabadilko hata kwenye maeneo ya hifadhi za Taifa, tuweze kuvuna hewa ya ukaa kama wenzetu Kenya wanavyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumekuwa tukitoa mawazo haya na kwa bahati mbaya sana Serikali haifanyii kazi. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, itumie nafasi hiyo ili muweze kupata fedha nyingi ambazo wenzenu jirani Kenya wanazipata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye sekta ya utalii. Utalii ulielekezwa ukanda wa Kaskazini, lakini nchi yetu ina maeneo mengi ambayo yana vivutio vya utalii na kwa bahati mbaya havijatumika vizuri. Naomba na maeneo hayo yafanyiwe kazi. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru sana kupata nafasi ya kuchangia. Nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwakutoa fedha ambazo zimetekeleza miradi mingi ya maendeleo ndani ya wilaya yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Waziri ni miongoni mwa Mawaziri ambao ni wasikivu wanasikiliza Wabunge na wasikiliza wananchi kwa ujumla. Kazi anayoifanya pamoja na wasaidizi wake ni mfano mzuri wa kuigwa kwani anawatendea haki Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nimuombe sana Mheshimiwa Waziri; Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Rukwa wote tuna kilio cha aina moja. Sisi tuna chanzo cha uhakika cha maji cha Ziwa Tanganyika, ziwa ambalo linakina kirefu na ziwa ambalo lina maji safi ambayo ni mengi na yanaweza kutumika kwa mikoa yote na mpaka kutoa ziada kwenye maeneo mengine. Tunachoomba ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kile chanzo kianze kupeleka maji kwenye mikoa hiyo mitatu ikiwemo Mkoa wa Katavi ambao mimi ni sehemu ya jimbo na Mheshimiwa Waziri alishafika mpaka kwenye eneo ambako chanjo kinachopendekezwa kutoa maji kuyatoa eneo la Karema kuyapeleka Makao Makuu ya Mkoa pale Katavi, Mpanda Mjini inaweza ikasaidia sana kupeleka huduma ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi bila kupata chanzo cha maji cha kutoka Ziwa Tanganyika tutaendelea kupata miradi midogo midogo ambayo haitasaidia sana. Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali kutupatia fedha kwaajili ya miradi midogo midogo lakini mwarubaini wa suluhisho la maji kwenye Mkoa wa Katavi ni kuyatoa maji Ziwa Tanganyika na kupeleka eneo la Makao Makuu ya Mkoa Mpanda Mjini. Niombe sana Mheshimiwa Waziri ninachokizungumza wewe mwenyewe ni shuhuda na unajua, na nikupongeze sana. Umefika kwenye eneo la chanzo cha maji na umetoa ushirikiano mkubwa sana kwa watendaji na niwapongeze Watendaji wa Mkoa kwa ujumla wa Katavi na meneja wa MRUASA wa Wilaya ya Tanganyika kwa ubunifu ambao na wewe mwenyewe ulishuhudia mpaka ukafika ukaona umuhimu wa yule meneja ukatoa fedha za kwako kumpa kama zawadi ambayo ni motisha kwa ufanyaji kazi mzuri.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni wakandarasi ambao wanateuliwa na Serikali kwaajili ya kujenga ile miradi ya maendeleo. Tunaye mkandarasi ambaye alipewa kazi ya kujenga Mradi wa Katuma mkandarasi huyu Hema-Tec anamuda mrefu toka amesaini mkataba ambao ulitakiwa kuwa amekamilisha huu mradi ifikapo tarehe 21 mwezi wa sita. Wenzie ambao walisaini pamoja huu mkataba walishatekeleza miradi yao na imekamilika na maji yameanza kutoka; lakini huyu tangu aliposaini huo mkataba hata kwenda kwenye site hajafika na alishasaini huo mkataba.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naomba sana Mheshimiwa Waziri aingilie kati mkataba wa Hema-Tec usimamishwe ili tutafute mkandarasi ambaye anauwezo anayeweza kwenda kufanyakazi kuliko kuwarundikia kazi ambao hawana uwezo wa kufanya kazi. Eneo hili ni muhimu na naamini si Mpanda tu peke yake au Katavi kwa ujumla; wapo wakandarasi wabovu ambao wanapewa miradi ya Serikali wanashindwa kuitekeleza kwa wakati. Niombe muwapime na muangalie vigezo ambavyo mnapowapa kazi wahakikishe wanaenda kutekeleza kazi ambayo inaweze ikawasaidia wanananchi kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lipo eneo lingine ambalo Serikali ilifanya kwa nia njema tulipoanzisha jumuiya za watumia maji. Jumuiya hizi zinafanya kazi nzuri, lakini kwa bahati mbaya sana kuna waraka ulitoka wa Serikali uliokuwa unataka kila jumuiya za watumia maji wawe angalau wana elimu ya kuanzia kidato cha nne, na huko nyuma Serikali iliwapa elimu ya mwanzo waliokuwa wanasimamia ile miradi huko nyuma, ambao walikuwa ni vijana wazalendo wa kutoka kwenye maeneo husika ya miradi husika. Kwa bahati mbaya sana tangu mlipotoa ule waraka mkaleta vijana wengine wapya ukweli usimamizi umekuwa si mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe muwarejeshe wale ambao mliwapa elimu, mliwasaidia mkawapa elimu na wakajitolea wamefanya kazi na ilikuwa na ufanisi. Na ukichunguza waliokuwa huko nyuma walisimamia miradi vizuri na mapato ya jumuiya za maji yalikuwa yakijiendesha vizuri. Sasa hivi mmeongeza gharama kwa kuwajaza hao vijana ambao ukweli miradi mingi imeshindwa kufanya kazi ile iliyokusudiwa ni eneo hilo ambalo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa sekunde 30 malizia.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: ...ni eneo hilo ambalo tunashukuru, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada kubwa ambazo anazifanya za kuleta fedha za maendeleo kwenye maeneo yote ya nchi yetu. Miongoni mwa walionufaika ni sehemu ya Mkoa wa Katavi, Wilaya ya Tanganyika tumepata fedha nyingi za maendeleo, kwenye sekta ya elimu, maji, miundombinu na kwenye afya tumeletewa fedha nyingi za maendeleo ambazo zinaonesha kabisa jitihada za Serikali zilizofanywa na Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza Watendaji wa Serikali wakisimamiwa na Mawaziri kwa jitihada zao ambazo wamezifanya kusimamia miradi ile ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie mradi wa bandari. Serikali imewekeza mradi mkubwa wa bandari eneo la Kalema ambao una thamani ya Shilingi Bilioni 48. Mradi huu ni mradi mkubwa na una manufaa kwa nchi yetu, kitu ambacho tunaiombe Serikali ni kuhakikisha sasa mradi huu ili uweze kufanya kazi ni lazima Serikali ijenge barabara yenye kilometa 110 kutoka Kagwira kwenda Karema ili ile bandari iweze kufanya kazi kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa DRC Congo wanaitumia fursa hii ya kupatikana kwa bandari ili waweze kuleta mizigo ipitie Bandari ya Karema na hatimaye kufika kwenye Bandari ya Dar es Salaam. Ninaiomba Serikali iharakishe mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo ili iweze kusaidia shughuli za kiuchumi kwenye maeneo hayo, vilevile kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuondoa msongamano uliopo pale eneo la Tunduma pindi utakapokuwa umekamilika mradi huu wa barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo tunaishukuru Serikali ni miradi ya umeme wa REA ambao mimi kwenye Jimbo langu tuna vijiji 26, kwa bahati nzuri Serikali ilitoa fedha na ikapata Mkandarasi lakini kumekuwa na changamoto kubwa sana Mkandarasi aliyepewa dhamana ya kupeleka umeme vijijini kwa Mkoa wa Katavi ameshindwa kutekeleza mradi ule kwa wakati. Ninaiomba Serikali Wakandarasi wanapopewa kazi wasimamiwe vizuri ili waweze kukamilisha miradi ambayo wameiweka kwa ajili ya kuwafikia wananchi.

Mheshimiwa Spika, ninavyo vijiji 26 ambavyo alipewa huyu mkandarasi lakini mpaka sasa bado hajakamilisha na kila mwaka wanamwongezea muda ili aweze kukamlisha. Ninaomba kwenye eneo hilo Serikali ilifanyie kazi ili mradi huu uweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana mkandarasi aliyepewa dhamana ya kupeleka umeme vijijini kwa Mkoa wa Katavi ameshindwa kutekeleza mradi ule kwa wakati. Niombe Serikali wakandarasi wanapopewa kazi wasimamiwe vizuri ili waweze kukamilisha miradi ambayo wameiweka kwa ajili ya kuwafikia wananchi. Nina vijiji 26 ambavyo alipewa huyu mkandarasi lakini mpaka sasa bado hajakamilisha na kila mwaka wanamwongezea muda ili aweze kukamilisha. Ninaomba kwenye eneo hilo Serikali ilifanyie kazi ili mradi huu uweze kukamilika.

Mheshimiwa Spika, eneo jingine ni miradi ya maji. Tunaishukuru Serikali Halmashauri yangu imepata Shilingi Bilioni 8.9 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali na Serikali imejitahidi kupeleka miradi, iko iliyokamilika na mingine bado ambayo haijakamilika ukiwemo mradi wa eneo la Mishamo wenye thamani ya shilingi bilioni1.3. Shida kubwa ambayo ipo katika eneo hilo ni Mkandarasi aliyepewa hana uwezo wa kwenda kufanya kazi na asilimia kubwa anatafuta fedha apewe fedha kabla hajafanya kazi wala kwenda kwenye eneo la site.

Mheshimiwa Spika, ninaomba Serikali iweze kutoa Mkandarasi mwingine kuliko yule ambaye walimpa na hana uwezo. Mkandarasi huyo anaitwa Hamwa, kazi anayoifanya ni kwenda kufanya lobbying na kutisha watendaji wa Serikali waidhinishe kumpa fedha wakati uwezo wa kufanya kazi haupo.

Mheshimiwa Spika, ipo miradi mingine ya maji katika Vijiji vya Kapalamsenga wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3 inaenda vizuri lakini tunaomba Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo aweze kuisimamia ikamilike kwa wakati. Kubwa zaidi ambalo tunalihitaji wananchi wa Wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi kwa ujumla kwenye mradi wa maji tuliishauri Serikali kuhakikisha mradi ambao unaweza ukabeba matumaini ya wananchi wa Wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi ni mradi ule mkubwa wa maji kuyatoa Ziwa Tanganyika kuyapeleka Makao Makuu ya Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, najua jitihada za Serikali zimefanywa hatua za awali, tunaomba kwenye bajeti hii waangalie umuhimu wa kuanza ujenzi wa mradi huu mkubwa wa maji ambao utatatua kero ya maji Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo tulikuwa tunaishauri Serikali ni ujenzi wa meli wa Ziwa Tanganyika. Tumejenga Bandari lakini bado vitendeakazi havipo. Ili bandari zilizopo Mkoa wa Kigoma, Katavi na Mkoa wa Rukwa ziweze kufanya kazi tunahitaji kuwa na meli. Meli ambazo zitafanya kazi kwenye Ziwa Tanganyika na ni kitendo cha aibu kwamba katikati ya nchi zilizozunguka Ziwa Tanganyika eneo la nchi yetu tu ndiyo ambayo haina vyombo vya usafiri. Niombe Serikali iweze kufanya mchakato wa haraka ule ambao wameuanzisha wa kuanza kujenga meli kwenye Ziwa Tanganyika tupate meli za mizigo na abiria kwa ajili ya kuwasaidia wananchi. Bila kufanya hivi hata uwekezaji tuliouwekeza kule utakuwa ni sawa na hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo hili ni muhimu kiuchumi na wenzetu nchi za Burundi, Congo wanaitumia kama fursa na sisi hii fursa tuitumie ambayo itatusaidia sisi na kwa nchi kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ya mchango wangu ni kwenye eneo la kilimo. Tunaishukuru Serikali ilileta mbolea zenye ruzuku ya Serikali kwenye eneo hili. Tunaipongeza sana, lipo jambo ambalo tulikuwa tunaomba na kuishauri Serikali iweze kulifanyia mchakato kwa kiwango kikubwa. Mbolea za ruzuku za Serikali zilizotolewa zimebagua baadhi ya maeneo hawakupewa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu. Wakulima ambao wanatoka Mikoa inayozalisha zao la tumbaku hawajanufaika na ruzuku iliyotolewa na Serikali. Ninaomba kwenye mchakato huu na wao waangaliwe kwa sababu na wao ni sehemu ambayo wananufaika na wana mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

Mheshimiwa Spika, mfuko mmoja unauzwa kati ya shilingi 170,000 na hawa wakulima faida yao inakuwa ndogo sana kwa sababu gharama ya uzalishaji inakuwa kubwa sana. Ninaomba Serikali ilichukue hili na ilifanyie kazi ili iwasaidie wananchi kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili kwenye eneo la kilimo juu ya mbolea hizo, tunaomba utaratibu ambao ulifanyika mwaka huu mwakani ufanyiwe maboresho kwa kiwango kikubwa ili iwafikie walaji waliowengi kuliko ilivyokuwa sasa walionufaika ni wachache na pengine unawanufaisha watu wengine ambao ni wafanyabiashara middleman ambao wanatumia hizo huduma zilizotolewa na Serikali kuliko wale walengwa ambao ni wakulima halisi.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuishukuru Serikali kwenye miradi ya afya. Tumeletewa miradi mingi ya afya kwenye Mkoa wa Katavi lakini tatizo kubwa tulilonalo ni watumishi ambao wanahitaji kutoa huduma za afya. Kwenye zahanati, vituo vya afya, hospitali ya Wilaya bado uhitaji mkubwa wa watumishi ni mkubwa kwenye maeneo haya. Mimi binafsi tu kwenye Wilaya yangu nina vituo vya afya ambavyo vimejengwa zaidi ya vitano lakini watumishi tulionao ni wachache, tuna hospitali ya Wilaya ambayo inahitaji huduma kutolewa kwa wananchi, bahati mbaya sana hata vitendeakazi havipo! Kwa hiyo, tunaomba uwekezaji uliowekezwa na Serikali kwenye eneo hili ni vizuri sasa na ni muhimu wakatoa fedha kwa ajili ya kutoa ajira kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji kwenye hotuba ya Waziri. Awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada kubwa sana ambayo anaifanya pamoja na Naibu wake na Wasaidizi wake kwenye Ofisi, wanafanya kazi nzuri lakini yapo ambayo tunahitaji kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, nianze kwenye eneo la mifugo. Kwenye eneo la mifugo, Serikali ina wajibu wa kuimarisha Ranch ambazo zitasaidia wakulima au wafugaji wadogo wadogo waweze kupeleka mifugo kwenye hizo Ranch na Ranch hizo zitumike kwa ajili ya kuwa kama soko ambalo litakusanya mifugo ya wafugaji wadogo wadogo ili mifugo ikinenepeshwa wao wanaiuza kwenye masoko ya nje. Hili litasaidia sana kukuza sekta hii ya ufugaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ufugaji wetu asilimia kubwa wamekuwa wachungaji kwa sababu ya kukosa huduma zile za msingi. Hawana malisho ya kutosha, hawana malambo na majosho. Kwa hiyo, wafugaji wanalazimika kutafuta malisho na kutafuta huduma zile ambazo zinaweza zikasaidia mifugo iweze kuishi. Kwa hiyo, niombe Serikali iimarishe eneo hili ili kuwasaidia hawa wafugaji wetu ambao maisha yao kweli ni ya kuhamahama kwa sababu wanahitaji kupeleka mifugo ili iweze kupata huduma.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine nizungumzie suala la uvuvi. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia sana hoja au mapendekezo ya Serikali juu ya kufunga Ziwa Tanganyika. Mimi ni miongoni mwa Wabunge ambao wapigakura wetu wapo kwenye eneo hilo la Ziwa Tanganyika. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, endapo kama zoezi hili litakuwa limekubalika na likatekelezwa, ukanda mzima wa Ziwa Tanganyika kuanzia Kasanga hadi Kigoma tutatengeneza wezi wengi na majambazi wengi, kwa sababu maisha yote ya wananchi wa ukanda wa mwambao wa Ziwa Tanganyika, yanategemea suala zima la uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuwaeleze tu ule ukweli, Serikali haijafanya utafiti mzuri. Ziwa Tanganyika ni Ziwa ambalo linajifunga lenyewe kulingana na jiografia ilivyo. Ziwa Tanganyika, muda mchache sana wanatumia wavuvi kufanya shughuli za uvuvi kwenye Ziwa hilo. Tunayo miezi ambayo Ziwa Tanganyika haliwezi kutoa hata samaki wa mboga, kwa sababu Ziwa lile lina kina kirefu na ndio Ziwa kubwa ambalo lina kina kirefu karibu mita 1500 ambazo kina chake kinaenda chini. Kwa hiyo, kuna kipindi samaki wanakwenda chini wanakimbia ubaridi wa huku juu. Kipindi hicho wavuvi huwa hawapati kitu chochote. Sasa sioni sababu Serikali inapokuja na mawazo ya kulifunga hili Ziwa kwa sababu jiografia na uhalisia ulivyo Ziwa huwa linajifunga lenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie jambo lingine la pili kwenye eneo hili la uvuvi wa Ziwa Tanganyika. Uvuvi haramu ndio chanzo cha mawazo ya kufikiria kwamba Ziwa lifungwe, lakini kuna mambo ambayo yanafanywa Serikali wanashindwa kusimamia wao wenyewe. Uvuvi haramu chanzo chake ni kuleta nyavu zile ambazo zimekatazwa na Serikali. Pia inanisikitisha sana kama nchi ya Zambia, Congo na Burundi waliafikiana kulifunga hili Ziwa wakati wao wanaruhusu nyavu hizo haramu zinauzwa bila kuwa na shida yoyote. Mfano halisi, nenda pale mpakani Tunduma, ukivuka tu upande wa pili unakuta zile nyavu zipo zinauzwa wala hazina shida ya aina yoyote, marufuku iko huku huku nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wavuvi wanaovua na nyavu hizo haramu wanatoka Nchi za DRC Congo, Burundi na Zambia. Mvuvi wa Tanzania hawezi kwenda kuvua kwenye eneo la Ziwa linalomilikiwa na Zambia wala Congo wala Burundi. Asilimia kubwa ya wavuvi wanaoendesha shughuli za uvuvi haramu ni wenzetu wa kutoka nchi za jirani. Kwa hiyo, naomba hili Mheshimiwa Waziri alielewe. Mbaya zaidi Maafisa wetu wa Serikali ambao ndio wenye jukumu la kulinda rasilimali za kwetu, wao ndio wamekuwa wahusika wakubwa wa kuwalinda na kuwahifadhi hao wanaovua kwa njia ya haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutamsaidia Mheshimiwa Waziri, akituhitaji na bahati nzuri tumeona kuna mwaliko ambao amewaalika Wabunge wote wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma. Tutamweleza uhalisia jinsi ulivyo. Maafisa wao wanatumika. Mfano, tunapopakana Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Kigoma, kuna eneo ambalo wavuvi wa nchi zote hizo nilizokutajia hasa DRC Congo na Burundi wapo pale katikati na Maafisa wao wanakwenda kuchukua michango ambayo inawaruhusu waweze kuendeleza shughuli za uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zipo zile nyavu haramu ambazo ni hatarishi kwa maisha ya viumbe hai kwenye maeneo ya Ziwa. Hizo nyavu zinatumika na Maafisa wa Wizara wanazikuta na hawachukui hatua ya aina yoyote. Kwa hiyo, sioni sababu ya Mheshimiwa Waziri kuungana na tamko ambalo wamekubaliana kwamba tulifunge hili Ziwa, kwa sababu uzembe upo Serikalini. Kwa hiyo, naomba hili Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri hawezi kufunga Ziwa hajaweka vitendea kazi. Uvuvi ule wa kisasa ambao ungepelekwa kwenye eneo la Ziwa Tanganyika hajawapelekea, dhana zote wamepeleka Ziwa Victoria. Kwa sababu, kule kama ni tamko la kufunga Ziwa wangepeleka kule kwa sababu walishaandaa utaratibu. Kwa Ziwa Tanganyika hawajapeleka kitu chochote kile. Kwa hiyo, naomba hili wasiende wakafanya maamuzi ambayo yatawaumiza wananchi na baadaye wakaumiza Serikali na Chama cha Mapinduzi kwa ujumla. Niombe hili walifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, yapo ambayo tutaishauri Serikali, kama dhana ni kulinda rasilimali, kitu cha kwanza ambacho tunahitaji kukifanyia kazi waende wakaisimamie sheria ambayo itaondoa tatizo la uvuvi haramu. Wakaimarishe doria, wakatafute watu ambao watawasaidia ili waweze kulinda rasilimali.

Mheshimiwa Spika, la pili, ni kulinda baadhi ya maeneo ambayo yatatenga mazalia ya samaki ambayo yatakuwa yamehifadhiwa na walianzisha vizuri na kuna dalili ambayo walianza, wakaweka mpaka maboya kwenye maeneo ambayo wanaonesha kwamba maeneo haya yatakuwa ya matunzo na mazalia ya samaki. Ile ndio njia sahihi ambayo wanaweza wakasaidia hawa wavuvi. Wawapelekee sasa uvuvi na ufugaji wa samaki wa kisasa ambao wamepeleka Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika wawapelekee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine, wapeleke zana za kisasa ambazo zinaweza zikavuna kwenye eneo la Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika ndilo Ziwa pekee ambalo wapo samaki ambao kumwona mpaka aweze kufa yeye mwenyewe ndio anapanda huku juu, kwa sababu hakuna zana za kuweza kuwavuna. Naomba hili wakalifanyie kazi kuliko yale ambayo wanaweza tu wakifika wanakubaliana mikataba ambayo itakuja kuwaumiza Watanzania na mkataba huo asilimia kubwa watakaonufaika ni nchi jirani kuliko sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu asilimia kubwa ya wavuvi wanaokuja kuvua eneo letu ni Nchi ya Congo, Nchi ya Burundi na upande ule wa Kusini ni Zambia wanavua kwenye maeneo ya kwetu. Ukiangalia maeneo haya yote uvuvi wa kwao na maeneo wanayoyamiliki ni kidogo sana lakini ndiyo wanaovua kwa kiwango kikubwa kuzidi kwenye maeneo ya kwetu. Zambia wamewekeza, wamepeleka vifaa ambavyo vinaweza kuwasaidia wavuvi lakini kwenye maeneo mengine kama DRC Congo, Burundi wameruhusu nyavu hizo ambazo ni hatari kwetu na kwa maendeleo ya sekta ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunayazungumza haya ili kuepusha tafrani ambayo inaweza ikajitokeza endapo Serikali itaenda kwa mawazo ambayo wakakubaliana kitu ambacho hakitakuwa na tija kwa wananchi wetu. Mimi naamini Serikali mkijipanga vizuri mkasikiliza mawazo ya Wabunge, mnaweza mkatatua tatizo ambalo kimsingi litaleta furaha kwa wananchi ambao tunawasimamia.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kakoso, kengele ya pili ilishagonga.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, naomba Mheshimiwa Waziri ayafanyie kazi. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote, naipongeza Wizara kwa kuleta bajeti ambayo inamatumaini kwa Watanzania, lakini yapo maeneo ambayo nataka niishauri Serikali. Nianze kwenye eneo la miradi ya umwagiliaji. Ili nchi iweze kwenda mbele, ni lazima tuwekeze kwenye miradi ya umwagiliaji. Jimboni kwangu mimi ipo miradi ya umwagiliaji ambayo mpaka sasa bado haijakamilika. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri aangalie ule mradi wa umwagiliaji wa skimu ya Karema uweze kukamilika, kwani kila bajeti inayokuja huwa tunaambiwa kwamba inakwenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili, ahadi zilizotolewa na Mawaziri ni nyingi kwenye mradi ule wa skimu ya Karema, sambamba na ile skimu nyingine ya Kabage ambayo ilianzishwa na Serikali. Kwa hiyo, tunaomba mkakamilishe ile miradi. Yapo maeneo mengine nchini kama tutawekeza kwenye miradi ya umwagiliaji, nchi itakuwa na usalama wa chakula, tutakuwa na uhakika wa uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo napenda kuchangia ni suala la mbolea ya ruzuku ya Serikali. Kwenye eneo hili, Serikali ilitoa fedha na tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuongeza fedha za ruzuku ambazo zimeenda kuwasaidia wananchi, lakini zipo kasoro kubwa sana ambazo zilijitokeza. Mwaka huu kuna baadhi ya wakulima ambao wamekula hasara kwa sababu mbolea zilizopelekwa zile ambazo tulikuwa tunakusudia kwamba zingeenda kuwafanyia kazi wananchi hazikuwa na ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, mbolea zile ambazo zilikuwa na mashaka, tunaomba sana mziangalie, msije mkafanya makosa makubwa kama yaliyojitokeza, kupeleka mbolea mbazo hazina ubora uliokusudiwa. Hili ni jambo la kufanyiwa kazi na wataalam wafanye kazi ambayo inaweza kupambanua mbolea ambazo zinaweza zikawa na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kilimo cha tumbaku. Nampongeza Mheshimiwa Waziri, kwanza kwa ushawishi wa kuleta makampuni ya ununuzi wa tumbaku. Amefanya jambo jema, wananchi wengi sasa wanaanza kupata manufaa makubwa. Hata hivyo, kuna kasoro ambayo tunamwomba Mheshimiwa Waziri akalifanyie kazi. Mbolea za ruzuku zililoletwa hazijawagusa wakulima wa zao la tumbaku. Hawa wanatumia mbolea za CAN, UREA, SA na hizo ni miongoni mwa mbolea ambazo zilitolewa ruzuku na Serikali, lakini hawajanufaika na kitu chochote. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi. Ahakikishe mbolea hizi zimewafikia, tena kwenye msimu huu huu ambao wamelima, ziwanufaishe na wao. Ni muhimu sana kwenye eneo hili mlifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uweze kufanya maboresho makubwa kwenye zao la tumbaku, ni vyema Mheshimiwa Waziri mkaweka fedha ambazo zitakuwa zinafanya maboresho ya kuongeza idadi ya ma-classifier wanaoteua zao la tumbaku kupitia Bodi ya Tumbaku. Eneo hili linachelewesha masoko sana. Leo hii Mkoa wa Katavi una classifier watatu tu. Mahitaji ni zaidi ya classifier sita ambao wana kazi ya uteuzi wa tumbaku. Sasa nazungumzia mkoa mmoja tu, lakini hata ambao natoka, Mkoa wa Tabora, una uhitaji mkubwa, Mkoa wa Shinyanga una uhitaji mkubwa, Mkoa wa Ruvuma na pengine mikoa yote inayolima zao la tumbaku.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aelekeze mawazo ya kuboresha Bodi ya Tumbaku kwa eneo ambalo wanateua wateuzi ambao ni wa Serikali. Hili tunaomba Mheshimiwa Waziri akalifanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tuweke mkakati wa mazao yale ya kibiashara. Mazao ya kibiashara ndiyo yanayoleta fedha za kigeni hapa nchini, lakini kwa ujumla bado Serikali haijawekeza kwa kiwango kikubwa sana. Mazao haya ni kama yako yatima, yanajiendesha yenyewe bila nguvu ya Serikali. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri aje na mkakati wa kufanya maboresho ili mazao haya ya kimakakati yaweze kutoa tija kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye Wizara hii. Niishukuru sana Serikali kupitia Mheshimiwa Rais kwa kutoa fedha za miradi ya maendeleo ya maji. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri na wasaidizi wake kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwatendea kazi Watanzania.

Mheshimiwa Spika, nianze na Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika. Wananchi wa Mikoa ya Kigoma, Katavi, Rukwa, kilio chao kikubwa ni Mradi wa Maji kuyatoa Ziwa Tanganyika, ili yaje tatatue kero ya maji kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Waziri amekuja Mpanda na kwa uungwana alionao aliwashirikisha Wabunge na alibadilisha mfumo wa ziara yake ambayo alikuwa amepangiwa na watendaji. Tukaenda naye kwenye chanzo cha maji Ziwa Tanganyika na yeye aliona umuhimu kabisa. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri mradi ule ndiyo utakaowasaidia wananchi wa mikoa hiyo, tunaomba akautekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mji wa Mpanda umekua, una mahitaji makubwa sana ya maji na tatizo la maji kwa Mkoa wa Katavi litatatuliwa kwa Mradi wa Maji wa kuyatoa Ziwa Tanganyika. Niombe sana hili alishughulikie Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao napenda kuuzungumzia ni Mradi wa Mishamo. Mheshimiwa Waziri amenipa miradi mingi ya maendeleo kwenye Wilaya ya Tanganyika, tunayo miradi yenye zaidi ya shilingi bilioni nne ambayo ameitoa na inatusaidia japo ni miradi midogo midogo, lakini ikikamilika tutakuwa na asilimia karibu 80 ya upatikanaji wa maji safi na salama, lakini shida ambayo ipo tuna wakandarasi wabovu wanaotuletea.

Mheshimiwa Spika, tuna Mkandarasi wa Mradi wa Mishamo, HAMWA; mradi huu una thamani ya shilingi milioni 886, toka alipokuja akasaini huo mradi na akapewa fedha za awali shilingi milioni 100 hajafanya uendelezaji wa aina yoyote. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wamsimamie huyu mkandarasi ili aweze kukamilisha huu mradi ambao utahudumia Vijiji vya Mishamo, eneo la Ifumbula, Kapemba na Kijiji cha Isenga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao Mheshimiwa Waziri tunaomba akasimamie ni Madi wa Kata ya Katuma. Mradi huu ni mradi wa muda mrefu na Naibu Waziri aliambatana na Makamu wa Rais pale Katuma na Makamu wa Rais alitoa maelekezo ya kuhakikisha Mkandarasi
HERMATEC anakamilisha ule mradi kwa muda uliokuwa umepangwa. Mpaka sasa tunavyoongea, bado huo mradi haujakamilika na inashangaza Makamu wa Rais anatoa amri, lakini mtekelezaji mpaka muda huu hajafanya hivyo. Sasa sijui atamsikiliza nani? Kama Makamu wa Rais anatoa maagizo na hayatekelezwi?

Mheshimiwa Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri, najua kazi anayoifanya na jitihada anazofanya ni kubwa. Sisi Wabunge asilimia kubwa tunamwamini anachapa kazi nzuri, wakamsimamie ili akamilishe huo mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni tatizo la vitendeakazi. Halmashauri yangu ya Wilaya ya Tanganyika Mheshimiwa Waziri anaijua, ametembea, tumeenda kule ukanda wa ziwa na ametembea hadi kwenye eneo tunalopakana na Mkoa wa Kigoma. Hakuna magari ambayo yanaweza yakawasaidia kufanya shughuli za maendeleo na wakati huu tuna miradi mingi ambayo inasimamiwa na hao watendaji wa MURUWASA. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti hii tunahitaji atoe msukumo ili tupate gari ambalo litasaidia utekelezaji wa miradi ambayo inaenda kwenye maeneo ya kwetu. Mheshimiwa Waziri, akiyafanya haya yatatusaidia sana katika utekelezaji wa miradi ile ambayo anaisukuma ili iweze kuwafanyia kazi wananchi.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo napenda nitoe ushauri, ni kuunganishwa kwa Jumuiya za Watumiaji Maji. Ni wazo zuri ambalo wanakuja kuunganisha mfumo wa kuunganisha jumuiya zile za watumiaji maji, lakini kuna kasoro ambazo zinajitokeza. Unaunganisha eneo ambalo wengine wanataka kupewa huduma na wengine ndio wanaotoa gharama za maji. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, tusije tukawalazimisha mahali ambapo mifuko inaweza ikajitegemea, tuwaache wafanye hivyo kwa ajili ya ustawi wa miradi endelevu. Kuna maeneo mengine mifuko hiyo imekufa na huduma inakuwa ya shida kwa sababu tunawalazimisha kuwaunganisha ili waweze kubebana wakati wapi wengine uwezo wa kubebana haupo.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, niendelee kumshukuru Mheshimiwa Waziri na watendaji. Naamini yale ambayo ni ya msingi kwetu sisi Mkoa wa Katavi tunahitaji Mradi wa Maji wa Ziwa Tanganyika ambao naamini atatusaidia katika utekelezaji. Mradi ule ukikamilika kuna nafasi ya kuwa zaidi ya asilimia 100 tutakuwa na upatikanaji wa maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Awali ya yote nishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa jitihada kubwa sana ya kuleta fedha za maendeleo ambazo zimekuja kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika. Naishukuru sana Serikali kupitia Mheshimiwa Rais kwa kuleta fedha nyingi za maendeleo. Tumejengewa Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika, tunavyo vituo vya afya visivyopungua saba, na vipo vingine viwili vinajengwa. Hayo ni mafanikio makubwa sana kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika. Tunaipongeza Serikali, na tunawapongeza Mheshimiwa Waziri, na Naibu Waziri. Wote walishafika kwenye maeneo ya Wilaya hiyo ya Tanganyika na kwenye hospitali ya wilaya na baadhi ya vituo vya afya. Tunawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie sana uhaba wa watumishi. Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika ni miongoni mwa Wilaya ambayo imejengewa hospitali nzuri ya kisasa, lakini kwa bahati mbaya hospitali hii haina watumishi kabisa. Ina watumishi wachache na huduma ambazo zinatolewa kwa sasa ni kama vile hadhi ya zahanati. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Mheshimiwa Waziri atuletee watumishi ambao watakuja kufanya kazi ili hadhi ya majengo yaliyojengwa, na Mheshimiwa Waziri ni shahidi, amefika kwenye eneo lile. Mheshimiwa Rais alimsifia kwa kujenga hospitali nzuri na ya kisasa, na mandhari yenyewe ilikuwa ya kuvutia sana. Sasa zile sifa ambazo ulipewa Mheshimiwa Waziri, kazifanyie kazi ulete watumishi. Vile vile Naibu Waziri amefika hapo, ameleta fedha za vitendea kazi na aliwaahidi wananchi kwenye eneo lile ili kufanya maboresho makubwa kwenye Hospitali ya Wilaya. Naomba sana, Mheshimiwa Waziri nendeni mkalete wafanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika ina watumishi 20 tu. Kwa hiyo mkija kuangalia hadhi ya hospitali iliyojengwa ni tofauti na vitendea kazi kwa maana ya rasilimali watu. Namwomba Mheshimiwa Waziri, pelekeni watumishi kwenye vituo vya afya ambavyo vimejengwa. Tunavyo vituo vya afya vya Karema, Mheshimiwa Waziri umefika pale. Tunavyo vituo vya afya vya Kasekese, Kituo cha afya cha Mwese, Kituo cha Afya cha Mishamo, tunavyo Vituo vya Afya Nyagala, hivyo vyote havina watumishi. Naomba sana kwenye eneo hili mlifanyie kazi na mtusaidie ili wananchi waangalie huduma iliyoletwa na Serikali iendane na mazingira halisia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Hospitali ya Wilaya tumeletewa x-ray ya kisasa kabisa, nzuri, lakini kwa bahati mbaya hata kutuletea wataalam wa mionzi imeshindikana. Kwa hiyo, huduma hiyo haipo. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri alikuja, aliona hali halisi, lakini vifaa tiba vilivyoletwa, kuna upungufu, wale wataalam wa Tume ya Mionzi wameshindwa kufika kwenye eneo hilo. Naomba Wizara ishughulikie ili wananchi waweze kupata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliahidiwa na Mheshimiwa Naibu Waziri vifaa tiba, alileta vyenye thamani ya shilingi milioni 270, zikabaki kama shilingi milioni 230 ili hospitali ile iweze kufanya kazi, mpaka sasa bado vifaa hivyo havijakamilika. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba mtuletee hivyo vifaa tiba, sambamba na watumishi ili wataalam wetu waweze kutoa huduma. Tunao watumishi wachache ambao wanajitahidi sana kufanya kazi nzuri ya kuwatumikia wananchi. Kwa bahati mbaya idadi ya wanaohitaji huduma ni kubwa. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba Serikali iangalie tatizo lililopo kwenye Wilaya ya Tanganyika na ukiangalia ni mazingira ambayo ni Wilaya iliyoko pembezoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilijenga kwa nguvu za wananchi hospitali teule eneo la Ikola kule Tarafa ya Karema na ilijengwa mahususi kwa sababu katika ukanda wa ziwa kuna mlipuko wa magonjwa ya dharura ambayo huwa yanajitokeza, na ukiangalia tumepakana na nchi jirani ya DRC ambapo kuna milipuko ya mara kwa mara ya magonjwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa bahati mbaya pamoja na jitihada ambazo zilizofanywa na Serikali kupitia halmashauri ya wilaya, bado hatuna hata mtumishi mmoja na kuifanya hospitali ile iliyojengwa kuwa kama eneo ambalo ni mazalia ya popo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri utakapopata fursa ya kuja Mkoa wa Katavi, tembelea kwenye eneo hilo uangalie jitihada ambazo zimefanywa na nguvu za wananchi namkaona jinsi walivyojipanga. Tusiangalie tu pale ambapo magonjwa yanapokuja kwenye mlipuko ndio tunakuja kuangalia jitihada za kutatua wakati wenzetu walishafanya jitihada za awali. Niombe na niishauri Serikali wafanye jitihada za dharura kuja kuwasaidia wananchi wa Wilaya ya Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo ahadi za viongozi ambazo zimetolewa kwenye Wilaya ya Tanganyika. Mheshimiwa Waziri, alifika kwenye eneo la Kata ya Katuma alituahidi kumalizia Kituo cha Afya cha Katuma. Niombe Mheshimiwa Waziri, ahadi yako uikamilishe na wananchi walishatumia nguvu zao na wametumia fedha za mfuko wa hewa ya ukaa kama chanzo cha awali cha kujenga kituo chao cha afya. Kwa hiyo, kilichobaki sasa tunasubiri fedha zile ambazo ziliahidiwa na Serikali ziweze kwenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na ahadi nyingine zilizotolewa na ukiangalia mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilivyo ni ambulance ambazo ziliahidiwa mbele ya Makamu wa Rais. Tunaomba ahadi ile iweze kutolewa. Ukiangalia jiografia ilivyo tumetembea na Mheshimiwa Waziri anaijua vizuri Wilaya ya Tanganyika jinsi ilivyo. Kwa hiyo, tulikuwa tunaomba ambulance kama tatu hivi kwa ajili ya vituo vya afya cha Kalema, Kituo cha Afya cha Mishamo, Kituo cha Afya cha Mwese. Sambamba na ambulance ambazo zitahitajika kwenye hospitali ya wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie eneo la Bima ya Afya, Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, wamepata fedha za hewa ya ukaa ambazo waliziingiza kwenye vijiji nane ili wapate huduma ya bima ya afya. Kwa bahati mbaya na masikitiko makubwa sana, pamoja na kuweka fedha nyingi na Mheshimiwa Waziri ndiye aliyekuja kuzindua kwenye eneo hilo, bado huduma ile iliyokusudiwa haipo kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nikuombe ufuatilie jambo hili uone ni kitu gani ambacho nakizungumzia kwa sababu ninaelewa ninachokisema wewe unakifahamu tulishiriki wote lile zoezi. Huduma haipo, wananchi wamelipa fedha na huduma ya afya haipo kabisa kiasi kwamba sisi wawakilishi tunaonekana kama tumeshirikiana na Serikali kuwaibia wananchi kwa sababu hawapati hiyo huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, naamini haya yote ambayo tumeyazungumzia kama Wabunge, Serikali ikiyachukua ikayafanyia kazi itawasaidia sana wananchi wa eneo la Wilaya ya Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nizungumzie hospitali ya Mkoa, hospitali yetu ya mkoa…

NAIBU SPIKA: Ahsante na ndio mwisho wako huo.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana. Ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho. Awali niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya hasa ya kupeleka miradi ya maendeleo, hasa kwenye miradi mikubwa ambayo imeanza kutekelezwa na inaonekana mbele ya nchi yetu. Miradi hiyo hiyo mikubwa ni kama ujenzi wa reli, barabara, miradi ya umeme, miradi ya maji, miradi ya elimu ambayo kimsingi imekuja kuwa na mafanikio makubwa sana mbele ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninalo eneo moja ambalo ningependa kulichangia kwa kina kuishauri Serikali. Bahati mbaya tu leo hata wasaidizi wa Waziri ambao wanaweza wakachukua mawazo ya Wabunge hawapo kabisa, yupo Waziri na Naibu Waziri, lakini yapo mambo ya msingi ambayo tunaweza tukalisaidia Taifa letu ili liweze kuepukana na kodi tunazozichukua kwa wananchi za kila mwaka kwenye eneo la mafuta na eneo la bia na kwenye maeneo mengine madogo madogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana niliishauri Serikali, lipo eneo ambalo hatujawekeza kabisa na kuna fedha nyingi na wenzetu wananufaika sana. Nchi yetu imebahatika kuwa na misitu mingi na sasa hivi tunapata fedha nyingi kwa sababu dunia nzima wanahamasa kubwa ya uvunaji wa hewa ya ukaa, kwa sababu mataifa ya nje yameharibu hali ya hewa huko duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa fursa tuliyonayo sisi Watanzania hatujaitumia vizuri kabisa. Ninao mfano, Nchi jirani ya Kenya, wenzetu wanavuna hewa ya ukaa kwa mwaka wanapata dola bilioni moja ambazo wanazivuna kupitia kwenye hifadhi zao. Sisi nchi yetu Tanzania ina maeneo makubwa mno karibu kila sehemu tuna Hifadhi za Taifa, tuna misitu inayomilikiwa na TFS, tuna misitu inayomilikiwa na vijiji, nchi yetu tu tunao uwezo wa kuvuna karibu tani zinazoweza kutoa shilingi trilioni 6.9 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungepata hizi fedha zingeweza kutusaidia kuepukana kuwakamua wananchi kupitia kwenye mafuta, lakini bahati mbaya Wizara hawajatoka ofisini na hatujazitumia Balozi zetu zilizoko huko nje. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, eneo hili lina fedha nyingi na inawezekana mkawa mnaona kama hadithi. Nchi ya Brazil inavuna hewa ya ukaa na asilimia kubwa wanatumia hizo fedha kwa ajili ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimetolea mfano Nchi jirani ya Kenya, wao wanavuna hewa ya ukaa karibu dola bilioni moja. Sisi tuna nafasi ya kufika dola bilioni tatu ambazo zinaweza kutupelekea shilingi trilioni 6.9. Tunao mfano ambao kwa nchi yetu tayari walishaanza kuvuna hewa ya ukaa. Katika Jimbo langu wanavuna hewa ya ukaa kupitia misitu ambayo ipo, kati ya shilingi bilioni nne na wanaweza kufika mpaka bilioni 30 na kuachana na utegemezi wa kutegemea Serikali Kuu. Eneo hili ni eneo muhimu, waendeni wakajifunze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pakistan baada ya kupata tatizo la mafuriko, yale maeneo ambayo walihama wananchi wao saa hizi wanayatumia kwa ajili ya uvunaji wa hewa ya ukaa. Mheshimiwa Waziri aende akalifanyie kazi eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo aina tatu za uvunaji wa hewa ya ukaa na inawezekana hata kwenye Wizara yake Mheshimiwa Waziri hajui hivi vyanzo. Kuna soil carbon ambayo inazalisha organic kwenye eneo la agriculture, wanaweza kupata fedha huko. Kuna eneo lingine ambalo ni kwenye blue carbon inayopatikana kwenye Maziwa Makuu na ufukwe wa Bahari, katika maeneo hayo yote wanaweza wakapata fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunayo green carbon ambayo inaweza ikazalisha fedha nyingi kupitia misitu tuliyonayo. Maeneo haya Serikali haijawahi kuyafanyia kazi, tunakaa tu kwa ajili ya kuhakikisha wanyama wanaongezeka na wakiongezeka ndiyo wanaoenda kuleta shida kwa wananchi, kula mazao ya wananchi. Eneo hili Waziri aende kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua wana mipango mizuri ambayo Serikali wanategemea kupeleka fedha. Mimi kwenye eneo langu Jimbo la Mpanda Vijijini, tunayo Barabara ya kutoka Kabungu kwenda Kalema, Serikali wamewekeza ujenzi mkubwa sana wa bandari karibu shilingi bilioni 48. Zile fedha ni kama wameenda kuzi-dump, muhimu ni kujenga ile barabara ili waweze kuunganisha na nchi jirani ya DRC, Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo wenzangu wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma wamezungumzia umuhimu wa kuwepo kwa meli itakayofanya shughuli za maendeleo kwenye Ziwa Tanganyika. Ziwa Tanganyika ndiyo pekee ambalo halina usafiri wa aina yoyote na kwenye maeneo ambayo yana mzigo mkubwa sana ni Ziwa Tanganyika, tunayo Bandari ya Kasanga ambayo ikitumika vizuri itaunganisha na eneo la Lubumbashi upande wa Congo, Bandari ya Kalema yatakayounganishwa na Mji wa Kalemie, lakini tunayo Bandari ile ya Kigoma itakayounganisha na nchi ya Burundi na Kongo ya Mashariki kwa maana ya Miji ya Uvila na Goma wanaweza wakatumia hiyo na tukatengeneza uchumi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali tujenge barabara ya haraka na ya dharura ili iweze kuunganisha na ile bandari ambayo tumeijenga kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo tunaomba kwa Mheshimiwa Waziri, tunaomba fedha za dharura za Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Katavi kwa sasa hauna umeme. Tunaishukuru Serikali ilileta jenereta, lakini kadri ya idadi ya watu na shughuli za maendeleo zinavyokuwa tayari Mkoa wa Katavi una shida kubwa sana ya upatikanaji wa umeme. Nimwombe Mheshimiwa Waziri kwenye hii bajeti wapeleke jenereta mpya ambayo inaweza kwenda kusaidia na kutatua kero ya wananchi. Wakati tunasubiri ule mradi mkubwa wa Gridi ya Taifa bado kuna haja ya kupeleka umeme wa dharura kwenye eneo hilo ambalo litasaidia ukuaji wa kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuiomba Serikali kujenga mradi mkubwa wa maji. Nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Fedha ampe Waziri wa Maji ajenge Mradi mkubwa wa Maji kutoka Ziwa Tanganyika kuleta Makao Makuu ya Mkoa pale Mpanda Mjini. Watakuwa wamewasadia wananchi na hilo linawezekana, kama maji wanayatoa Ziwa Victoria na wana mpango wa kuyafikisha mpaka Dodoma ambako ni eneo la kilometa nyingi zaidi ya kutoka pale, kutoka Mji wa Kalema hadi Mpanda ambao ni kama kilometa 100. Nina imani Serikali ikiwa na dhamira ya dhati wanaweza wakawasaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi na wao wakanufaika na keki ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana, lakini narudia kuisisitiza Serikali, wapate mawazo kutoka kwa watu wa chini, wana uwezo kabisa wa kuweza kupata mbadala wa fedha. Mawazo ya Wabunge tunapoishauri Serikali kwamba iache kukamua watu hapa, kuna eneo lingine walifanyie kazi, huko ndiko ambako tunaishauri Serikali. Naamini na nina uhakika, chanzo hiki cha mapato wakikitumia vizuri Serikali watapata fedha nyingi na wana uwezo mkubwa sana wa kukusanya mapato na nchi ikanufaika, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuwa miongoni mwa wachangiaji. Awali ya yote nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada kubwa sana anayoifanya kuwatumikia Watanzania na kupeleka huduma mbalimbali ambazo kila eneo zimewafikia Watanzania. Hata hivyo, yapo ya msingi ambayo kayafanya, amewaongezea mishahara watumishi wa Serikali, ni jambo kubwa sana na bado kwenye sekta ya elimu ametoa elimu bure mpaka kidato cha sita. Kwenye bajeti hii aliyoleta Mheshimiwa Waziri, hili ni jambo la faraja kwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na ushauri kwa Serikali hasa kupitia Wizara ya Fedha kwenye maeneo ya mapendekezo waliyoyaleta juu ya kuhamisha vifungu vya kisheria ambavyo kwenye sekta ya mawasiliano wanainyang’anya Mamlaka ya Mawasiliano TCRA wanapeleka kwenye TBS ambayo hawatakuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo inayokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hili Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi na ni vizuri Serikalini wanapokuwa wanaleta mapendekezo wawashirikishe wadau wote kuliko wakijifungia tu wanaleta ya kwao ambayo hayatafanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hilo tu kwenye eneo la sekta ya ujenzi na LATRA wameleta mapendekezo ya kuhamisha baadhi ya mambo ambayo wanapeleka TBS, jambo ambalo si zuri na ni vizuri wakawashirikisha. Hata kwenye Wizara ya Kilimo nako kuna mapendekezo ambayo wameyaleta, wanahamisha shughuli zilizokuwa zinafanywa na mamlaka ya pamba, wanapeleka kwenye TBS. TBS kazi yake ni kutunza ubora na kuhakiki ubora ule ambao umefanywa kwenye eneo la viwanda. Hili naomba Waziri mwenye dhamana aliangalie na a-review kabisa hivi haya mapendekezo ambayo ameyaleta ambayo ukweli kimsingi ukiyafuatilia hayawezi kufanya kazi kama walivyokusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kusisitiza kwenye eneo hilo hilo, ni kumkumbusha Mheshimiwa Waziri TBS kupitia Bunge hili hili tuliwapa mamlaka ya kuhakiki mitambo ya magari na Serikali ikagharamia mtambo karibu wa shilingi bilioni 10 ambao uliletwa na umeshindwa kufanya kazi kwa sababu ya kung’ang’ania shughuli ambazo hawajazifanyia uhakiki ule unaokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijikite kwenye sekta ya kilimo, kwenye sekta ya kilimo ni sekta ambayo ndiyo inayoweza kukuza uchumi na tuangalie nyakati zinavyokwenda. Sasa hivi dunia nzima ina njaa na tutakuwa na njaa kubwa na sisi kama nchi yetu ni nchi ambayo ina maeneo ambayo tungeyapanga vizuri Serikali ikajikita, tungetatua baadhi ya maeneo na kuwafanya Watanzania wenzetu wakawa na kipato kikubwa sana na nchi ikawa na fedha ambazo zingesaidia kufanya shughuli zingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna tatizo la ukosefu wa ngano tunajua Ukraine, Rusia kuna vita, Wazungu hawatakuja kuwasaidia Waafrika, ngano yote itabaki kule kule iweze kufanya shughuli za kuwasaidia wenzao. Niombe sasa Serikali ijikite katika kipindi hiki cha mwaka huu wa fedha wahakikishe kwenye maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa na unaofanana na hali ya hewa kama Mkoa wa Njombe, Mkoa wa Mbeya, Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Arusha na hata kwetu Katavi kwenye eneo la Tarafa ya Mwese ni maeneo ambayo yanaweza yakazalisha ngano. Sasa wafanye utafiti wahakikishe wanawawezesha Watanzania kwenye maeneo haya wazalishe ngano ambayo itauzwa hapa hapa nchini na kupunguza fedha zile ambazo tunatafuta za kigeni kwenda kununua ngano nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni la muhimu sambamba na kukuza mazao ya mafuta. Tunayo mikoa ambayo tunazalisha mafuta ya michikichi kwa upande wa Mkoa wa Kigoma na Mikoa ya jirani kama vile Katavi, Tabora hadi Kagera wana uwezo wa kuzalisha michikichi, Wizara ihakikishe inawawezesha hawa wakulima wazalishe ili kuwe na uwezekano wa kuweza kuzalisha mafuta ndani ya nchi yetu. Kwenye zao la alizeti karibu kila mkoa alizeti inastawi mahali pote, wahakikishe wanaandaa mbegu, wanawapa mbegu bora ili wazalishe mazao hayo ambayo yatapunguza kupoteza fedha za kigeni ambazo tunazitumia kwa ajili ya matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tunaishauri Serikali ni kwenye sekta ya maliasili. Kwenye eneo la maliasili hatujafanya vizuri pamoja na jitihada ambazo zinafanywa na Serikali kuhakikisha tunatangaza utalii kwa nguvu zote na Mheshimiwa Rais amefanya hili vizuri sana, lakini kuna eneo ambalo hawajalifanyia kazi kama Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Nchi za Magharibi au zilizoendelea kwa ujumla zina uchafuzi wa mazingira kupitia viwanda. Sasa maeneo haya sisi kama Taifa hatujatumia fursa aliyopo, viwanda vyote duniani ambavyo vinazalisha na kuchafua mazingira vinatakiwa kulipa gharama za kutunza mazingira. Wenzetu Nchi jirani ya Kenya wanapata fedha karibu dola bilioni mbili kwa mwaka kupitia uvunaji wa hewa ya ukaa ambayo wanaifanya na sisi ambao tupo kwenye maeneo mengi ya misitu hatujanufaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri amefanya kazi kwenye Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira, analijua ninalolizungumzia. Tanzania wilaya chache tu ndizo ambazo zinavuna hewa ya ukaa. Wilaya ya Tanganyika nilikotoka mimi nina ushuhuda, vijiji karibu 10 vinanufaika, wanapata karibu kila kijiji kwa kipato cha mwaka huu tu wamepata bilioni tatu vijiji na tunategemea wanaweza wakapata karibu bilioni 10. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tukitoa sheria ambazo tumeziweka zinazoziba mazingira ya kuweza kukusanya fedha hizi kwenye National Park kama Wakenya wanavyofanya, kwenye misitu ambayo ni tengefu, naomba hili walifanyie kazi. Naamini Mheshimiwa Naibu Waziri analifahamu, tukieleza nguvu kwenye hii sekta ya misitu, Tanzania tuna uwezo wa kupata fedha zaidi ya bilioni 400 kwenye misitu tunayoimiliki. Naomba hili walifanyie kazi sambamba na kuchungulia ni mahali gani ambako tunafanya nao biashara, kwa sasa tunafanya na watu wa kati, middle man ambao wapo katikati, hatujawafikia wale ambao wanatoa hizo fedha. Naomba hili Wizara ilifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie eneo la sekta ya miundombinu. Tunapojenga miundombinu hasa barabara nashukuru Wizara ya Ujenzi imekuja na mpango wa kushirikisha sekta binafsi ili waweze kujenga barabara ambazo wata-design, watajenga na watakuwa financier wao, ni jambo lililo zuri. Sasa tuangalie ni barabara zipi tunazoenda kuzijenga, tujenge barabara ambazo zitakuwa na uchumi na zitakazorudisha return ya fedha tulizowekeza. Mfano, tunayo barabara ya kutoka Ifakara kwenda Madete hadi Njombe – Ludewa ambako kuna machimbo ya mkaa na sasa hivi kupitia vurugu ya dunia, mkaa unahitajika karibu kila sehemu. Naomba hili walifanyie kazi, tujenge barabara ambazo zina faida. Barabara nyingine ni ile ambayo inatoka Wilaya ya Mpanda, Mkoa wa Katavi kwenda eneo la Karema ambako Serikali imejenga bandari. Hii barabara waijenge haraka ili washike soko la Kongo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuchangia Hotuba ya Waziri ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Naipongeza Serikali kwa jitihada ambazo zinafanywa ambazo zimekuwa za kuleta mafanikio makubwa sana hasa kwenye Sekta ya Utalii; tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumzia mazingira ya migogoro kati ya Pori la Msitu wa Tongwe Mashariki na Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ambao ndio wamiliki wa huo msitu. Mheshimiwa Waziri unaujua vizuri mgogoro huu na tulikuwa tunategemea kabisa kwamba ungekuwa umefanya jitihada za karibu kumaliza huu mgogoro ili wananchi wa Wilaya ya Tanganyika waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuchelewa kwa kutokutoa maamuzi ya haraka, kumefanya eneo hilo ambalo lina mgogoro kuingia hasara karibu ya thamani ya shilingi 30,000,000,000 tumezipoteza kwa sababu ya mgogoro uliopo. Kama unavyofahamu Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Tanganyika inavuna carbon credit na imekuwa wilaya ambayo ni ya mfano katika nchi yetu. Wewe mwenyewe unafahamu, karibu halmashauri 50 zimekuja kujifunza huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Mazingira, juzi alikuwepo, ameshuhudia maendeleo makubwa sana ambayo yapo kwenye vijiji vile nane ambavyo vinapata carbon credit. Nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, uje na majibu ili tuweze kumaliza mgogoro huu ambao kimsingi ukiumaliza, utakuwa umewasaidia wananchi karibu vijiji 32 watanufaika kwenye misitu inayozunguka maeneo hayo karibu na vijiji hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni ushauri kwa Serikali. Mheshimiwa Waziri, tumejielekeza sana kwenye Sekta ya Utalii, jambo ambalo ni jema. Nawaomba sana, ili tuweze kukuza utalii, matangazo ni muhimu sana katika nchi yetu. Utalii mahali popote pale ambapo umetangazwa kwa kina, umetoa faida kubwa na tija kubwa kwa nchi zilizofanya hivyo. Kwa hiyo elekezeni nguvu kuweka matangazo ya Kimataifa ambayo yatatangaza hifadhi tulizonazo na zitaleta fedha za kifgeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri, nawaomba Wizara muelekeze nguvu sasa kuitumia rasilimali tuliyonayo hasa misitu tunayomiliki, tuweze kuvuna carbon credit. Mheshimiwa Waziri, tuna misitu yenye hekta 48,000,000 kwa nchi nzima. Hii misitu haijafanya kazi ya aina yoyote ambayo tungeweza kupata faida kama nchi. Mimi naamini, kama Serikali itakuwa ina nia ya dhati, hata kodi tunazokuwa tunaongeza kwenye vinywaji, tusingekuwa tunaelekea huko kwenda kudai kodi hizo kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna rasilimali ambazo naamini tukiwekeza kwa kiwango kikubwa sana, tuna nafasi ya kupata kati ya shilingi 10,000,000,000,000 au zaidi kupitia kwenye misitu kwa idadi ya misitu tuliyonayo. Inawezekana Waheshimiwa Wabunge wasilielewe hili na wakaona kama miujiza, lakini huo ndiyo ukweli. Zipo nchi ambazo zinanufaika kupitia uvunaji wa carbon credit, wao wamenufaika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba na kuishauri Serikali, iwekeze kwenye eneo hili, tuweze kubadilisha Sheria ambazo ni vikwazo vinavyoweza vikatufanya tukakosa kupata hizo fedha. Ni matumaini yangu ushauri huu mtaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine, namuomba sana Mheshimiwa Waziri aje atusaidie. Tuna mgogoro kati ya wawekezaji ambao wanafanya shughuli za uwindaji kwenye Msitu wa Nkamba. Sisi Msitu wa Nkamba tumepakana na Msitu Msitu wa Luwafi. Muwekezaji yule anaenda kulipa mapato kwenye Msitu wa Luwafi ambao uko Mkoa wa Rukwa, lakini uvunaji anafanya kwenye eneo la Wilaya ya Tanganyika. Naomba hili, mtupatie mapato yetu ambayo ni stahiki ya Wilaya ya Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, kwenye mkoa wetu sisi, tuna Hifadhi ya Katavi. Hifadhi ya Katavi haijatangazwa ipasavyo. Tuna wanyama wakubwa pengine kuzidi wale ambao tunawaona kwenye Hifadhi ile ya Mikumi. Mfano tembo, tunao mpaka tembo ambao ni wakubwa sana na tuna twiga mweupe yupo kule Katavi. Sasa, hawajaweza kuitangaza hii hifadhi na matokeo yake inatumia rasilimali kubwa kutoka kwenye hifadhi nyingine ili kuendesha ile hifadhi. Naomba hili muweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja na naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha, aje na majibu sahihi juu ya mgogoro wa Msitu wa Tongwe Mashariki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu. Nianze kuipongeza Serikali kwanza kwa kuongeza bajeti ambayo inakuja kutekeleza miradi mingi hasa kwenye Sekta ya Uvuvi, lakini niende moja kwa moja kuchangia mchango wangu juu ya kufungwa kwa Ziwa Tanganyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Serikali imefunga Ziwa Tanganyika kuanzia mwezi Mei, lakini zipo changamoto kubwa sana kwenye eneo la mkoa wangu na eneo la Jimbo la Mpanda Vijijini. Ninavyo Vijiji saba vya Karema, Ikola, Itetemya, Shukula, Isengule na Kasangantongwe ambavyo maisha yote ya wananchi wa vijiji hivyo yanategemea shughuli za uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa bahati mbaya sana mwaka huu tumepata mafuriko karibu vijiji vyote. Hali ya maisha yao ni duni na shughuli ambazo wanazitegemea ni shughuli za uvuvi. Sasa naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-wind up atueleze njia mbadala za kuwasaidia wale wananchi ambao maisha yao yote wanategemea shughuli za uvuvi katika kipindi cha miezi hii mitatu itakayokuwa haiwaruhusu kuvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha kuweka angalizo na katazo la kutokuvua kwenye Ziwa Tanganyika ni uvuvi haramu. Asilimia kubwa ya uvuvi haramu upo kwenye nchi jirani, Nchi ya DR Congo na Nchi ya Burundi ndiyo wanaovua sana uvuvi haramu ambao upo kwenye Ziwa Tanganyika. Kwa bahati mbaya Serikali wameshindwa kudhibiti uvuvi haramu hata kama wale walipewa dhamana ya kusimamia uvuvi haramu kwenye maeneo hayo ambao ni watu wa Serikali wanashindwa na wanashirikiana na hao hao ambao wanavua uvuvi haramu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana Mheshimiwa Waziri waliangalie hili jambo kwa kina na mapana na marefu ili tuone tunatokaje kwenye hili jambo. Mimi binafsi sikatai kwa wazo la protocol iliyosainiwa ya Nchi ya Zambia DR Congo, Tanzania na Burundi, lakini tutafute mfumo sahihi ambao tutalinda rasilimali zilizopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mkoa wa Katavi hatujapata vizimba, tunavyo vizimba viwili tu ndani ya mkoa kwenye eneo la vijiji saba. Nimwombe Mheshimiwa Waziri anapokuja ku-wind up hotuba yake atueleze watu wa Mkoa wa Katavi, wavuvi wale watanufaika vipi na atapeleka vizimba kiasi gani kwenye maeneo hayo. Halikadhalika boti, wananchi wengi ili waweze kunufaika tunahitaji boti za kisasa za uvuvi. Amepeleka kwenye maeneo mengine tofauti kabisa kwenye eneo la Mkoa wa Katavi kuna boti moja tu. Tunaomba kundi la wavuvi wawapelekee boti za kutosha ambazo zitawasaidia kuvua uvuvi wa kisasa. Sambamba na hilo tunaomba boti za doria ili ziweze kusaidia kulinda rasilimali na wale wafanyakazi walionao waweze kufanya kazi sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo napenda kuchangia ni suala la wafugaji. Mkoa wa Katavi una ng’ombe wengi, mbuzi na mifugo mingineyo. Kwa bahati mbaya sana bado Serikali haijapeleka vitendea kazi kwa maana ya kuwachimbia mabwawa, malambo, majosho. Kwa hiyo, naomba maeneo haya wayafanyie kazi ili waweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania wa Mwaka 2018
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho kuchangia Miswada miwili ambayo imewasilishwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali tu, tuipongeze sana Serikali kwa kuleta hii Miswada miwili ambayo kimsingi ni muhimu na inakuja kwa wakati muafaka kwa ajili ya kuleta ufanisi kwenye utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali, kwa asilimia kubwa sana imechukua maoni ya Kamati, imesikiliza na imeweza kuyafanyia kazi. Yapo marekebisho mengi sana ambayo tumeafikiana na Serikali ambayo yamefanywa kwa pamoja kati ya Kamati na Serikali kwa ujumla. Tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu na Wajumbe wengine waliofika kwenye Kamati hii wametoa mchango mkubwa sana. Naamini mtaona mabadiliko ambayo yamefanywa na Kamati yamezingatiwa na kuchukuliwa na Serikali. Hii ni kuonesha kwamba wote waliofanya kazi hii walifanya kwa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sana kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa. Kipo kifungu Na. 32 ambacho
Kamati iliishauri Serikali kwamba pale ambapo Serikali inaweza kwenda kuweka mitambo kwenye maeneo yanayomilikiwa na wananchi, ni umuhimu wa wananchi kupewa fidia. Eneo hili ni la muhimu kwa sababu linagusa wananchi kwa karibu. Tunaomba sana Serikali izingatie yale maoni. Pamoja na kwamba wameyaona na kuyachukua, ili kuleta ufanisi na kufanya mamlaka iweze kufanya kazi na kulinda mali zitakazowekwa, ni vyema Serikali ikawa imewalipa fidia wananchi ambao kimsingi ndio wanaoguswa na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili lilizungumzwa sana kwenye Kamati na Serikali waliona jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge walivyoona hiki kifungu kilivyokuwa hakijakaa vizuri. Tunaipongeza Serikali kwa kuchukua sehemu ya maoni ya Kamati husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kifungu cha 22 juu ya taasisi ambazo zitatumia data zinazotolewa na Mamlaka. Hapa tumeishauri Serikali kwamba siyo kila taasisi ni lazima iweze kufuata kipengele kile ambacho kinamhitaji aweze kutumia data za Mamlaka. Tumeangalia kwa upana kwa sababu zipo taasisi nyingine ambazo zinafanya shughuli zake na zitachelewa kupeleka huduma na taarifa kwa wahusika. Kwa hiyo, tunaomba eneo hili Serikali waliangalie vizuri ili wasiweze kufunga zile taasisi nyingine ambazo zinaweza zikatumia data zinazotokana na Mamlaka husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya LATRA, tunapongeza sana Serikali kwa kuleta Muswada unaoendana na kuongeza ufanisi na ubora kwa wakati. Pia tunaipongeza Serikali kwa kuweza kudhibiti ajali nyingi ambazo kwa sasa zimeanza kupungua kupitia Sheria zinazodhibitiwa na LATRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kuishauri Serikali katika maeneo haya pamoja na kukubali maoni mengi yaliyotolewa na Kamati ya Miundombinu, bado tunaomba waangalie kifungu 42(1) na 42(2); Kamati ilishauri kifungu hiki kipunguzwe adhabu ambayo imependekezwa na Serikali, katika kifungu hiki 42(1) Kamati ilikuwa imependekeza angalau mtu atozwe shilingi laki tano na kifungu 42(2) Kamati tulipendekeza tozo za faini angalau zifikie bilioni mbili kuliko ilivyo kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya ni vyema Serikali ikayaangalia ili kuweza kuendana na hii Sheria tunayoitunga kwa sababu tungependa sana Sheria hii tunayoitunga iwe ya kudumu na ichukue muda mrefu sana na itaonekana Bunge limeshiriki kwa karibu sana na imeangalia umbali juu ya maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kifungu cha 35(3) Serikali tunaipongeza kwa kuweza kukubali mawazo ya Waheshimiwa Wabunge na Kamati kwa ujumla juu ya kupunguza annual levy iliyokuwepo ya asilimia 1. 5 na kufika asilimia moja. Hili ni eneo ambalo Wabunge waliliangalia kwa makini sana na tunaomba sana Serikali tuweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Kamati yangu ya Miundombinu imepitia vifungu kwa vifungu na karibu maeneo mengi Serikali iliweza kuchukua sehemu ya mawazo ya Kamati na kuyafanyia marekebisho. Hatukuwa na mvutano mkubwa tunawapongeza sana Waziri na timu yake, lakini tunawapongeza Wanasheria wa Serikali kupitia Bunge wametoa msaada mkubwa sana na tunaamini kwamba Sheria iliyopendekezwa kwa sasa itakuwa nzuri na vile vipengele ambavyo tumeshauri, tunaomba vifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini wa Mwaka 2018
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho kuchangia Miswada miwili ambayo imewasilishwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali tu, tuipongeze sana Serikali kwa kuleta hii Miswada miwili ambayo kimsingi ni muhimu na inakuja kwa wakati muafaka kwa ajili ya kuleta ufanisi kwenye utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali, kwa asilimia kubwa sana imechukua maoni ya Kamati, imesikiliza na imeweza kuyafanyia kazi. Yapo marekebisho mengi sana ambayo tumeafikiana na Serikali ambayo yamefanywa kwa pamoja kati ya Kamati na Serikali kwa ujumla. Tunawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Wajumbe wa Kamati ya Miundombinu na Wajumbe wengine waliofika kwenye Kamati hii wametoa mchango mkubwa sana. Naamini mtaona mabadiliko ambayo yamefanywa na Kamati yamezingatiwa na kuchukuliwa na Serikali. Hii ni kuonesha kwamba wote waliofanya kazi hii walifanya kwa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie sana kwenye Mamlaka ya Hali ya Hewa. Kipo kifungu Na. 32 ambacho Kamati iliishauri Serikali kwamba pale ambapo Serikali inaweza kwenda kuweka mitambo kwenye maeneo yanayomilikiwa na wananchi, ni umuhimu wa wananchi kupewa fidia. Eneo hili ni la muhimu kwa sababu linagusa wananchi kwa karibu. Tunaomba sana Serikali izingatie yale maoni. Pamoja na kwamba wameyaona na kuyachukua, ili kuleta ufanisi na kufanya mamlaka iweze kufanya kazi na kulinda mali zitakazowekwa, ni vyema Serikali ikawa imewalipa fidia wananchi ambao kimsingi ndio wanaoguswa na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili lilizungumzwa sana kwenye Kamati na Serikali waliona jinsi ambavyo Waheshimiwa Wabunge walivyoona hiki kifungu kilivyokuwa hakijakaa vizuri. Tunaipongeza Serikali kwa kuchukua sehemu ya maoni ya Kamati husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kifungu cha 22 juu ya taasisi ambazo zitatumia data zinazotolewa na Mamlaka. Hapa tumeishauri Serikali kwamba siyo kila taasisi ni lazima iweze kufuata kipengele kile ambacho kinamhitaji aweze kutumia data za Mamlaka. Tumeangalia kwa upana kwa sababu zipo taasisi nyingine ambazo zinafanya shughuli zake na zitachelewa kupeleka huduma na taarifa kwa wahusika. Kwa hiyo, tunaomba eneo hili Serikali waliangalie vizuri ili wasiweze kufunga zile taasisi nyingine ambazo zinaweza zikatumia data zinazotokana na Mamlaka husika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya LATRA, tunapongeza sana Serikali kwa kuleta Muswada unaoendana na kuongeza ufanisi na ubora kwa wakati. Pia tunaipongeza Serikali kwa kuweza kudhibiti ajali nyingi ambazo kwa sasa zimeanza kupungua kupitia Sheria zinazodhibitiwa na LATRA.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapenda kuishauri Serikali katika maeneo haya pamoja na kukubali maoni mengi yaliyotolewa na Kamati ya Miundombinu, bado tunaomba waangalie kifungu 42(1) na 42(2); Kamati ilishauri kifungu hiki kipunguzwe adhabu ambayo imependekezwa na Serikali, katika kifungu hiki 42(1) Kamati ilikuwa imependekeza angalau mtu atozwe shilingi laki tano na kifungu 42(2) Kamati tulipendekeza tozo za faini angalau zifikie bilioni mbili kuliko ilivyo kwa sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo haya ni vyema Serikali ikayaangalia ili kuweza kuendana na hii Sheria tunayoitunga kwa sababu tungependa sana Sheria hii tunayoitunga iwe ya kudumu na ichukue muda mrefu sana na itaonekana Bunge limeshiriki kwa karibu sana na imeangalia umbali juu ya maeneo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kifungu cha 35(3) Serikali tunaipongeza kwa kuweza kukubali mawazo ya Waheshimiwa Wabunge na Kamati kwa ujumla juu ya kupunguza annual levy iliyokuwepo ya asilimia 1. 5 na kufika asilimia moja. Hili ni eneo ambalo Wabunge waliliangalia kwa makini sana na tunaomba sana Serikali tuweze kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Kamati yangu ya Miundombinu imepitia vifungu kwa vifungu na karibu maeneo mengi Serikali iliweza kuchukua sehemu ya mawazo ya Kamati na kuyafanyia marekebisho. Hatukuwa na mvutano mkubwa tunawapongeza sana Waziri na timu yake, lakini tunawapongeza Wanasheria wa Serikali kupitia Bunge wametoa msaada mkubwa sana na tunaamini kwamba Sheria iliyopendekezwa kwa sasa itakuwa nzuri na vile vipengele ambavyo tumeshauri, tunaomba vifanyiwe kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)