Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Selemani Moshi Kakoso (1 total)

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, swali langu la nyongeza; kwa kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika mikoa hiyo ni nyingi na zimeharibu miundombinu. Serikali ina mpango upi wa dharura kuhakikisha mikoa hii inapata huduma ili katika kipindi inapojipanga waweze kupeleka huduma itakayosaidia kutatua matatizo ya barabara ambazo zimeharibika sana?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Kakoso, ni shahidi kwamba juzi tulipata taarifa kutoka Katavi, kwamba barabara zetu kule zimekatika kutokana na mvua nyingi. Hakuna mawasiliano sasa ya kutoka Mpanda, kwenda Tabora kupitia Sikonge, hakuna mawasiliano kutoka Mpanda kwenda Kigoma kupitia Uvinza, hata tuta la reli nalo limetetereka.
Mheshimiwa Spika, tulichofanya juzi tumechukua hatua za haraka na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amefanya kazi hiyo vizuri, amepeleka Wataalam, hapa ninapozungumza wataalam wapo pale wanaimarisha barabara ile, ili kuweza kurudisha mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuwa mvua zinaendelea tumeamua tutafute njia nzuri, ambayo itakuwa na uhakika wa kuunganisha mawasiliano kati ya Mpanda na mikoa ile pamoja na Tabora kwa kurudisha reli, njia ya treni kutoka Dodoma itakwenda Tabora - Kaliua ili iweze kwenda Mpanda. Ile sehemu ya tuta ambalo lilikuwa limeharibika tumeshakamilisha na tayari tumeliambia Shirika la Reli, wauze tiketi Dar es Salaam, abiria wote wanaokwenda Mpanda wapewe mabasi waletwe Dodoma kupanda treni inayokwenda Mpanda.
Mheshimiwa Spika, hiyo ndio njia ambayo tumeamua tuitumie sasa ili kuimarisha usafiri wa kwenda Mpanda; huku Tanroad wakiendelea na ukarabati wa barabara zote ambazo zimekatika na malengo yetu barabara hizo tuziimarishe ili ziweze kupitika wakati wote.