Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Eng. Atashasta Justus Nditiye (8 total)

MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kuwadhibiti wakimbizi hasa maaskari ambao hutoroka kambini Nduta na kwenda kujumuika na wananchi, hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika, nchi yetu imekuwa ikipokea wakimbizi kwa miaka mingi na kuwahifadhi katika Kambi na Makazi. Kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi Na. 9 ya mwaka 1998 kifungu cha 16 na 17 kinaelekeza kuwa wakimbizi wote wanaishi katika maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili yao na hawaruhusiwi kutoka bila kibali maalum.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kudhibiti wakimbizi hasa maaskari kutoka nje ya kambi, Serikali imejiwekea mikakati ya makusudi ikiwemo kuwagundua wakimbizi/askari kwa kuwafanyia usaili wa awali na wale watakaobainika hupelekwa katika Kituo cha Utenganisho cha Mwisa kilichopo mkoani Kagera ambako huwekwa chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Serikali kujiridhisha na mienendo yao, hutakiwa kukana uaskari na kuomba hifadhi upya kwa masharti ya kutokujihusisha na harakati zozote za kisiasa na kijeshi zilizopo nchini. Hata hivyo Ofisi za Wakuu wa Kambi kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi hukusanya taarifa za kiintelejensia na kufanya doria na misako mara kwa mara kambini na nje ya kambi ili kubaini wakimbizi watoro na wanapobainika hushtakiwa na kuadhibiwa kwa mujibu wa Sheria ya Wakimbizi.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) aliuliza:-
Katika Jimbo la Muhambwe kuna Chuo cha Wauguzi (MCH) ambacho ni muhimu sana katika sekta ya afya, lakini hakiko katika hali nzuri.
Je, Serikali ina mpango gani wa kukiboresha chuo hicho na vingine vya aina hiyo ili viweze kujiendesha na kulipa wazabuni wengi ambao wanawadai?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Uuguzi na Ukunga Kibondo kilichopo Jimbo ka Muhambwe, ni kati ya vyuo sabini na saba ambavyo vinamilikiwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Vyuo hivi vilijengwa kwa nguvu ya Serikali na wadau wa maendeleo miaka michache baada ya uhuru, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa watumishi wa afya na kipaumbele ikiwa ni afya ya msingi kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Wizara kujikita katika kutekeleza Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) mwaka 2007, tumekuwa tukitenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kufanya ukarabati na upanuzi ili kukidhi ongezeko la udahili wa wanafunzi kwa lengo la kufikia udahili wa wanafunzi 10,000 kwa mwaka na pia kushirikisha sekta binafsi katika kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko hili la udahili limeongeza mahitaji ya kupanua miundombinu na pia kufanya ukarabati wa mara kwa mara kukidhi ongezeko hilo. Wizara imekuwa ikitenga fedha za ukarabati kupitia Mfuko wa Fadhili wa Pamoja yaani Basket Fund hadi mwaka 2006/2007. Kutokana na kusitishwa kwa fedha za basket mwaka 2006, majengo mengi ya Wizara hayakukamilishwa na kubakia magofu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali imejikita katika kutenga fedha zake za ndani kukamilisha majengo hayo kulingana na upatikanaji wa fedha. Kwa mwaka wa 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni nane kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Afya vya Serikali, ambapo Chuo cha Uuguzi na Ukunga Kibondo kimetengewa Sh. 630,000,000)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu madeni ya wazabuni, ni kweli Wizara inadaiwa na wazabuni mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa huduma za vyakula vibichi, vya kupikwa na huduma zinazoendana na ukamilishaji wa huduma hiyo, ambapo malimbikizo ya madeni kuanzia mwaka 2009 hadi 2015 yalifikia jumla ya sh. 6,859,299,159.05. Madeni yote hayo yamehakikiwa na yanasubiri upatikanaji wa fedha toka Serikalini ili yaweze kulipwa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kuanzia mwaka wa masomo 2015, huduma hii haigharamiwi na Serikali tena bali sekta binafsi imepewa fursa kutoa huduma kwa kuzingatia taratibu zilizopo.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Je, Shirika la UNHCR lina mpango wowote kwa usimamizi wa Serikali wa kujenga angalau wodi tatu za kulaza wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) naomba kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo ipo katika mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) kuomba msaada wa kujengewa wodi ya wanawake katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Maombi hayo yaliwasilishwa na Halmashauri kupitia barua ya tarehe 30 Machi, 2016 yenye Kumb. Na. HW/A/D.30/22/Vol.1/23 na mazungumzo yanaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo imetenga shilingi milioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa wodi moja katika hospitali hiyo ya Wilaya ya Kibondo.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Mwezi Septemba, 2015 Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aliwaahidi wananchi wa Kata za Busonzu, Busagara na Murungu ambao wamepakana na Hifadhi ya Taifa ya Muyowosi kwamba mpaka kati ya wananchi hao na hifadhi hiyo, utarekebishwa ili wananchi wapate eneo kwa ajili ya kilimo.
Je, utekelezaji wa ahadi hiyo utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu kupitia uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Kibondo inayo taarifa ya maombi kutoka kwa wananchi wa Kata za Busonzu, Busagara na Murungu kuongezewa maeneo kutoka Pori la Akiba la Moyowosi kwa matumizi ya shughuli za kibinadamu, ikiwa ni pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii katika vijiji vya kata hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu itayaorodhesha maombi haya katika orodha ya maeneo yanayopakana na hifadhi, yatakayoshughulikiwa kimkakati na Serikali; kwa kushirikisha wadau wote muhimu, zikiwemo Wizara za Maliasili na Utalii, Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI, Maji, Nishati na Madini na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, kwa nchi nzima. Utaratibu huu unaotarajiwa kuanza baada ya Mkutano wa Tatu wa Bunge la Kumi na Moja kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inaendelea kusisitiza kwamba utekelezaji wa azma ya Serikali ya kujibu kero za wananchi kuhusu changamoto za mahitaji ya ardhi, utazingatia uwepo wa sheria, kanuni na taratibu na pia kuweka mbele maslahi ya Taifa. Aidha Hifadhi ya Pori la Akiba la Moyowosi lilianzishwa kisheria, kwa Tangazo la Serikali namba moja, la mwaka 1981 baada ya kukidhi vigezo vyote, ikiwemo ushirikishwaji wa wananchi katika hatua za Vijiji, Kata, Mkoa hadi Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa kuhifadhi Pori la Akiba la Moyowosi Kitaifa, unazingatia bioanuwai katika mfumo wa ikolojia ya Moyowosi Malagarasi. Inayotoa mchango mkubwa wa viumbe mbali mbali wanaopatikana katika maeneo hayo, pamoja na utunzaji wa vyanzo vya maji kwa matumizi ya binadamu. Eneo hilli pia ni sehemu ya ardhi ya owevu, yenye hadhi ya kimataifa yaani Ramsar Site.
MHE. ENG.ATASHASTA J.NDITIYE aliuliza:-
Nchi yetu bado ina upungufu mkubwa sana wa sukari na kwa kuwa Wilayani Kibondo kuna ardhi oevu kwenye Bonde la Mto Malagarasi na Lupungu ipatayo ekari 52,000 na wananchi wako tayari kutoa ushirikiano kwa matumizi ya ardhi hiyo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafuta mwekezaji wa kiwanda cha sukari katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuwa katika Nchi yetu kuna upungufu wa sukari kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge. Viwanda vyetu vyote kwa pamoja vina uwezo wa kuzalisha tani 300,000 za sukari ya mezani na hakuna uzalishaji wa sukari ya viwandani ilihali mahitahi ya Sukari kwa matumizi ya nyumbani na viwandani ikikadiriwa kuwa tani 610,000 hivyo uhitaji wa uwekezaji katika sekta hiyo ya viwanda vya sukari ni mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuondoa upungufu huo, Serikali imeshatambua na inaendelea kuainisha maeneo yanayofaa kwa kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika Mikoa mbalimbali ikiwemo Morogoro, Mara, Pwani, Songwe na Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Bonde la Mto Malagarasi lililopita katika vijiji kumi vya Kasaya, Kibuye, Kigina, Kukinama, Kumsenga, Kumshwabure, Magarama, Nyakasanda, Nyalulanga na Nyarugusu ni moja ya maeneo ambayo Serikali imeyaainisha kwa ajili ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari. Tayari Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kwa kushirikiana na Wananchi na Kampuni ya Green Field Plantations imefanya vikao vya uhamasishaji katika vijiji vyote kumi na hivi karibuni wataanza taratibu za upimaji wa ardhi. Mradi huu utahusisha jumla ya hekta 25,000 sawa na ekari 61,776 ambapo Kampuni ya Green Field Plantations italima hekta 20,000 na itawasaidia wakulima wadogo pembejeo na teknolojia ili waweze kulima hekta 5,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimshukuru Mheshimiwa Mbunge na Mkuu wa Wilaya ya Kibongo kwani barua walizotuma Wizarani ziliongeza kasi hii, tuendelee kushirikiana.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Kwa muda wa zaidi ya miaka miwili, Hospitali ya Wilaya ya Kibondo haina mganga wa meno licha ya hospitali hiyo kuhudumia wagonjwa wengi kwa sasa ikiwemo wakimbizi kutoka nchini jirani ya Burundi:-
Je, ni lini Serikali itapeleka mtaalam wa meno katika hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Injinia Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekwishapeleka mtaalam wa meno (Daktari Msaidizi wa Meno) tangu tarehe 12/4/2016. Kwa sasa yupo katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo na anaendelea kutoa huduma kwa wagonjwa.
MHE. MHANDISI ATASHASTA J. NDITIYE aliuliza:-
Gereza la Wilaya ya Kibondo – Nyamisati limekuwa na ongezeko kubwa sana la wafungwa na mahabusu kwa sababu ya uwepo wa wakimbizi.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati unaofaa kupeleka mradi mkubwa wa maji kwenye gereza hilo ili kulinda afya za raia na askari walioko kwenye gereza hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Engineer Atashasta Nditiye, Mbunge wa Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kuna tatizo la upatikanaji wa maji katika Gereza la Kibondo. Mwaka 2010, Serikali kupitia Jeshi la Magereza lilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 20 kwa ajili ya kuchimba kisima kirefu na kazi hiyo ilifanywa na Wakala wa Uchimbaji Mabwawa na Visima iliyopo Ubungo Dar es Salaam. Uchimbaji wa kisima hicho ulikamilika tarehe 2 Oktoba 2010 na kilikuwa na uwezo wa kutoa lita 2,300 kwa saa ambayo ni sawa na lita 55,200 kwa siku. Kiasi hiki ni kidogo ukilinganisha na mahitaji halisi ya maji ya Gereza la Kibondo ambayo ni lita 94,870 kwa siku, hivyo kuwa na upungufu wa takriban lita 39,670 kwa siku.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2014 upembuzi yakinifu ulifanywa na wataalam wa Jeshi la Magereza kwa kushirikiana na Mhandisi wa Mamlaka ya Maji Wilaya ya Kibondo na kushauri kuwa ili gereza hilo liondokane na tatizo la maji, Jeshi la Magereza linapaswa kuvuta maji kutoka mtandao wa maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo hadi gerezani ambapo gharama zake ilikadiriwa kuwa ni shilingi 330,492,450. Hata hivyo, kutokana na ufinyu wa bajeti, mradi huo haujatekelezwa hadi sasa. Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha tatizo la maji Gereza la Kibondo linapata ufumbuzi wa kudumu.
MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE aliuza:-
Kwa muda mrefu sasa Mji wa Kibondo hauna maji baada ya chanzo cha maji kuharibiwa na shughuli za kibinadamu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mradi mwingine wa maji toka chanzo kingine (hasa Mto Malagarasi) ili Kata za Busunzu, Busagara, Lusohoko, Kitahana, Kumwambu, Kibondo Mjini na Miserezo zipate maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba la Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mhandisi Atashasta Justus Nditiye, Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango wa Maendeleo Sekta ya Maji awamu ya pili, Serikali imepanga kuboresha huduma ya Maji safi katika Mji wa Kibondo kwa kufanya usanifu wa kina na uandaaji wa vitabu vya zabuni ili kupata gharama ya ujenzi wa mradi mkubwa ambao utapita katika Kata saba zilizotajwa na Mheshimiwa Mbunge kwa kutumia chanzo cha Mto Malagarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mtaalam Mshauri anaendelea na usanifu wa kina pamoja na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni unaotarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2017. Vilevile taratibu za kumpata Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari za kimazingira na kijamii zinaendelea na anatarajiwa kupatikana mwezi Julai, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa Mji wa Kibondo. Taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi zinaendelea na ujenzi unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 21017/2018. Kazi zinazotarajiwa kufanyika ni pamoja na upanuzi wa mtandao umbali wa kilomita saba na ukarabati wa bomba la maji urefu wa kilomita nne, ununuzi dira 850 na ufungaji wa pampu na mota.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wananchi wa Wilayani Kibondo wanaendelea kupata huduma ya maji safi na salama, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imeitengea kiasi cha shilingi milioni 826.8 Halmashauri hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya vijijini.