Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Joshua Samwel Nassari (11 total)

MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nikushukuru sana kwa kunipa fursa na kwa sababu ni mara yangu ya kwanza nazungumza tangu nichaguliwe tena kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki na mimi niwashukuru Wanameru.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, unapoongelea suala la ukuaji wa viwanda huwezi ukaacha kuongelea habari ya viwanda ambayo vilikuwemo lakini leo hii havifanyi kazi. General Tyre Arusha kilikuwa ni kiwanda pekee cha kuzalisha matairi Afrika Mashariki. Mwaka juzi ndani ya Bunge hili nimejibiwa na Mama Nagu hapa kwamba in less than a year kiwanda kingerudi kifanye kazi, mwaka jana nimejibiwa ndani ya Bunge hili na Mheshimiwa Janeth Mbene kwamba kufikia mwezi wa 11 mwaka jana kiwanda cha General Tyre kingerudi kufanya kazi.
Sasa na mimi niiulize Serikali ya hapa kazi tu, kwamba ni lini kiwanda cha General Tyre kitarudi kufanya kazi kwa sababu tumechoshwa na ahadi za muda mrefu ndani ya Bunge hili na wananchi wa Mkoa wa Arusha ambao walikuwa wanapata ajira ndani ya viwanda vile leo wako nyumbani na matairi tunanunua Korea, India na Japan, lini General Tyre litaanza kufanya kazi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, General Tyre kinachoendelea General Tyre ni nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, General Tyre imeshatwaliwa aliyekuwa mbia mwenzetu mwenye asilimia 26 tumemlipa chake kiwanda ni chetu, kinachoendelea ni kurekebisha mitambo yote ya umeme. Lakini mitambo iliyokuwepo kwa ushindani wa sasa ni absolute zimepitwa na wakati. Tulikuwa tunatengeneza tyres zenye tube, sasa hivi soko linakula tubeless kwa hiyo, tunapaswa kuleta mitambo mingine. Lakini tunatafakari tuende vipi tutafute mbia mwingine au tutafute mtu wa kumwajiri afanye kazi. Kwa hiyo, sasa hivi kinachofanyika ikitoka Government Notice NDC itakwenda kupewa pesa bilioni 60 na itafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Catherine Magige amelifuatilia suala hili tumelizungumza sana, siyo suala la dakika moja naomba Mheshimiwa Mbunge uje au umuone Mheshimiwa Catherine Magige akueleze shule niliyompa masaa matatu kuhusu General Tyre. General Tyre is coming na iko kwenye score board yangu, nitapimwa kwa General Tyre. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi/Kicheko)
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu linafanana sana na swali la muuliza swali Mbunge wa Geita.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua jitihada ambazo zilifanywa na Serikali hapo nyuma kwa baadhi ya maeneo na vijiji kupata umeme kupitia Wakala wa Umeme vijijini kwa maana ya REA, lakini pia tunatambua mapungufu makubwa ambayo yameonekana kwenye miradi hii. Vipo baadhi ya vijiji ambavyo wananchi walipitiwa, ramani ikapitishwa, Serikali ikawaagiza wakakata mazao yao, wakakata kahawa…
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Wakachimba mashimo na mashimo yakachimbwa na Serikali kupitia Wakandarasi waliopewa kazi kwa ajili ya kuwapa umeme, lakini badala yake Wakandarasi wameondoka watu hawajapata umeme, mashimo yamebaki, mazao yao yameanguka, ng‟ombe wanaanguka kwenye mashimo. Sasa ningetaka kauli ya Serikali kwamba ni kwa nini unamnawisha mtu unamuweka mezani halafu kama huwezi kumpa chakula, kwa hivyo ni lini wananchi hawa ambao tayari ramani zimeshapita kwao na mashimo yakachimbwa halafu yakaachwa na mazao yao yakakatwa, ni lini wanakwenda kufungiwa umeme? Vijiji hivyo ikiwa ni pamoja na Mulala, Kilinga pamoja na baadhi ya maeneo mengine?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kuna maeneo mengine mkandarasi ameendelea kuchimba mashimo na kuweka nguzo.
Sasa ni lini maeneo haya yatapatiwa umeme, jibu la uhakika kabisa ambapo Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukiwaambia kwamba REA Awamu ya Tatu inakuja kusambaza umeme kwenye vijiji vyote, REA Awamu ya Tatu inaanza mwezi Julai baada ya bajeti yetu kupita mwaka huu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ni kuanzia mwezi Julai miezi inayofuata maeneo yenye mashimo yatapatiwa umeme kuanzia mwezi wa saba mwaka huu mara baada ya bajeti yetu kupita.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza. Migogoro ambayo imeendelea kuwepo baina ya vijiji ambavyo vinazunguka hifadhi haviko kwa Mheshimiwa Mchengerwa peke yake, pale Arumeru kuna Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Arusha National Park) na imekuwa na mgogoro wa siku nyingi sana hususani kijiji cha Momela, kitongoji cha Momela na hifadhi. Hifadhi ya Taifa ya Arusha ni miongoni
mwa hifadhi changa ambazo zimekuja kuanzishwa miaka ya juzi juzi tu.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri Makani ni kwamba ni lini basi atakuwa tayari tuende Arumeru ili tuweze kwenda kuhuisha mgogoro
ambao umekuwepo baina ya Kijiji cha Momela wananchi wa King’ori na wananchi wa Kiburuki na Hifadhi ya Taifa ya Arusha ili tuweze kurudisha mahusiano?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo amesema ni kweli kwamba masuala yanayohusiana na migogoro ya mipaka baina ya maeneo yaliyohifadhiwa na maeneo wanayoishi wananchi yapo maeneo mengi katika nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Arusha (Arusha National Park) ni mojawapo tu ya maeneo hayo, lakini nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba hivi tunavyozungumza ile Kamati ambayo tayari ilikwishaundwa inayoshirikishwa Wizara zaidi ya nne bado inaendelea na zoezi lake, watakapokuwa wamekamilisha kazi yao watakuwa wametoa ushauri Serikalini kuhusu namna bora zaidi ya kushughulikia migogoro hii ambayo tumekuwa tukiishughulikia kwa miaka mingi, lakini pengine tulikuwa hatujapata dawa ambayo ni sahihi. Sasa wakati tunasubiri kamati hii ikamilishe kazi yake pengine itakuwa si jambo
muhimu sana kwenda mahali ambapo pengine Kamati hii itakuwa imekwenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nafikiri itakuwa ni bora zaidi mimi na Mheshimiwa Nassari baada ya kuwa nimewauliza Kamati wamefikia wapi kama ni suala la kwenda kuona mimi na yeye tunaweza kwenda kama itasema kwamba bado haijakamilisha zoezi hili kwenye eneo analolizungumzia.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nami kwa kifupi tu ni kwamba, mwezi wa kwanza mwaka huu nilikuwa nchini Uswisi na kuna wadau nilizungumza nao na wakaonesha nia kwamba wako tayari kutujengea chuo cha ufundi pale kwenye Jimbo letu la Arumeru. Swali langu kwa Wizara; naomba commitment ya Serikali, kwamba wadau watakapokuja na watakapokuwa tayari kutujengea ninyi mtakuwa tayari kutusaidia utaalam na vifaa pale ambapo chuo kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Nassari na naomba niunganishe na maeneo yote ambayo wamejenga Vyuo vya VETA kwa kutumia taasisi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, katika kujenga vyuo vya ufundi kuna njia mbili za kuviendesha; kuna njia ya kwanza, watu wanajenga wenyewe na wanaendesha wenyewe katika sura zote za vifaa na Walimu. Njia ya pili, kujenga na kuikabidhi Serikali ili iweze kuviendesha. Sasa tatizo ninaloliona ni kwamba halmashauri zinashirikiana na wadau kujenga hivyo vyuo lakini baadaye wanakuwa hawawezi kufikia muafaka katika kupeleka Walimu pamoja na vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe tu
toka mwanzo, ni vema ushirikiano uanzie toka mwanzo ili tujue wadau watakaokuja kusaidia ujenzi wa chuo hicho wajibu wao utakuwa ni nini na upande wa Serikali wajibu wetu utakuwa ni nini ili suala hilo litekelezwe kwa ukamilifu kama inavyostahili.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Swali langu lilitaka kufanana kidogo na Mama Anne Kilango na nikichukulia mwenyewe kuwa mfano, lakini kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amekwishajibu labda nilisogeze mbele kidogo kwamba kama kweli lengo letu ni kuongeza idadi ya wanasayansi kwenye nchi hii na hususan walimu wa masomo ya sayansi kwenye shule zetu, ni kwa nini basi ile Programu ya Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ya Chama hiki cha Mapinduzi ambayo ilianzisha program maalum kwa ajili ya watoto, Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya kutengeneza walimu wengi wa sayansi kwenye nchi hii, ni kwa nini basi watoto wale walifukuzwa mwaka jana tena kwa polisi na mbwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TAKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi wale hawakufukuzwa kwa sababu wako kwenye vyuo kumi ambavyo wanaendelea na masomo yao na bado Serikali inaendelea kuwalipia. (Makofi)
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna watu ambao wanasaidia kazi za uongozi kwenye nchi hii nafikiri hata kuliko sisi Waheshimiwa Wabunge na wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu kwenye kutekeleza majukumu yetu kwenye majimbo na kwenye Halmashauri zetu ni viongozi wa Serikali za Mitaa kwa maana ya Wenyeviti wa Vijiji, lakini ambao wanafanya kazi kubwa zaidi ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu. Hata hivyo ukweli ni kwamba unapoangalia maslahi ambayo hawa watu wamekuwa wakiyapata ni madogo sana na mara nyingine Serikali inaamua ku-temper nayo kwa makusudi kabisa hata kuingilia ule utendaji wa ndani wa Halmashauri wa moja kwa moja inapokuja suala la matumizi ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kila wakati tumekuwa tukihoji kwenye Bunge hili kwamba ni lini Serikali inakwenda kuboresha maslahi ya Wenyeviti wa Vijiji pamoja na Madiwani ili nao waweze kuishi kama viongozi na waonekane kwamba kweli kazi wanayoifanya inathaminika kwenye Taifa? Kila siku Serikali inasema…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, Serikali naomba iji-commit kabisa kwamba ni lini watakwenda kuboresha kabisa haya maslahi ya wenyeviti wa vijiji pamoja na Madiwani na waache kusema tutaliangalia, tutaliangalia………..
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali tunatambua viongozi hawa wa ngazi za chini, Wenyeviti wa Mitaa, Wenyeviti wa Vijiji na Madiwani wanafanya kazi kubwa sana katika nchi hii, maendeleo yote yanasimamiwa na wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli pia kwamba maslahi ya watumishi mbalimbali wa umma pia watumishi wa kisiasa kila mmoja anasema hayatoshi, tuongeze. Hata Wabunge wanasema hivyo, walimu wanasema hivyo na wote wanasema tuongeze. Hili litawezekana endapo uchumi wa nchi utatengemaa. Katika mazingira ya sasa, kinachowezekana na ambacho sisi tunaona kinapaswa kufanywa na Serikali kwa ngazi hizi za chini ni ile asilimia 20 tunayoipeleka kwa ajili ya kuendesha ofisi, lakini pia huwa kuna posho ambayo inapatikana. Asilimia 20 ya kiasi cha shilingi bilioni moja au Halmashauri zingine zinakusanya makusanyo ya ndani mpaka shilingi bilioni 50 si hela kidogo zikigawanywa vizuri Kwa hiyo mimi niseme tu kwamba tunatambua mchango wa viongozi hawa wakati ambapo uchumi utatengemaa tunaweza tukaongeza lakini kwa sasa utaratibu ndiyo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgawanyo wake kama tulivyosema, 40% zitakwenda kwenye miradi wa maendeleo kwenye fedha ile ya own source, lakini 10% kwa mikopo kwa ajili ya wanawake na vijana na 20% itakwenda kwa ngazi za chini na hiyo 30% itatumika katika kuendesha Halmashauri. Hii ndiyo hesabu mpya ambayo tumeiweka baada ya bajeti yetu tuliyoisoma hivi karibuni.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, msingi wa swali langu unajikita kwenye suala la utafiti. Mataifa yote yaliyoendelea duniani ni yale ambayo yamefanya tafiti na kuzitumia tafiti hizi iwe ni kwenye masuala ya kielimu, teknolojia, kilimo au move ya viwanda kama ambavyo tumekuwa tunasema kwa sasa kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwa namna gani basi Serikali inatuhakikishia kwamba tafiti za kilimo zitafanyika na ziweze kutafsiriwa na kufika chini kwa wananchi kwa maana ya kwenda kwenye uhalisia ili hali kwenye bajeti ya Serikali tu ambayo tunamaliza sasa hivi peke yake, kwenye fedha za maendeleo Wizara ya Kilimo haijapata zaidi ya asilimia 30. Sasa ni kwa namna gani tunawahakikishia Watanzania tafiti na tafsiri yake na kufika chini ili ziende kwenye uhalisia kwenye kilimo?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti ambazo zinafanyika katika vituo vyetu 16 vya utafiti, kawaida huteremka moja kwa moja kwenda kwa wakulima kupitia huduma za ugani. Ndio maana kwa miaka ya karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa sana katika kilimo chetu, Serikali itaendelea kuongeza bajeti ya ugani ili tafiti zile ziweze kuwafikia wakulima na hatimaye kilimo chao kiweze kuwa kizuri zaidi.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIBU: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunashuhudia wanawake wengi wakati wanapojifungua wanapata maradhi ya fistula, je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha wanawake hawa wanaojifungua wanaepukana na maradhi haya ya fistula?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa swali zuri ambalo ameuliza Mheshimiwa Munira.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamke kupata fistula maana yake ni kwamba hakupata huduma nzuri wakati alipokuwa anakaribia kujifungua na hiyo ndiyo tafsiri yake kubwa ya msingi, kwa sababu fistula haipaswi kutokea kama mwanamke alipata uangalizi mzuri wakati anajifungua. Katika changamoto hiyo tumeiona, tunaendelea kuboresha utoaji wa huduma, kutoa elimu kwa watoa huduma wa afya, vilevile kuhakikisha kwamba tunazisogeza huduma za dharura za kumtoa mtoto tumboni karibu zaidi na wananchi ili hali ile ambayo inatokana na mwanamke kukaa labor kwa muda mrefu tuondokane nayo.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Tatizo kama hili la maji ya mvua ambayo yanapotea siyo tu kwamba liko huku Kilindi lakini hata kule kwetu Meru na siyo kupotea peke yake bali pia kusababisha maafa. Miaka ya 80 mwanzoni wakati Waziri Mkuu akiwa Marehemu Sokoine yalitokea maafa makubwa sana yaliyosababishwa na maji kwenye ukanda wa chini wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Iliundwa timu wakati ule ...

Mheshimiwa Mwenyekiti, najenga hoja tu ili waone umuhimu wa suala lenyewe tafadhali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba mwaka 2009, Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuja Meru na walitengeneza dossier kubwa sana ambayo ilitoa mapendekezo ya kukinga maji ili yatumike kwa kilimo cha umwagiliaji kwenye Kata za Mbuguni, Shambaraiburuka pamoja na Makiba. Mapendekezo hayo hayakufanyiwa kazi na mwaka huu wananchi wana maafa makubwa. Hivi tunavyoongea sasa hivi wameshindwa kutembea mpaka Wizara ya Afya imepeleka Mobile Services kwa ajili ya kusaidia watu wa eneo lile. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba ni lini watatumia ile ripoti ili kuweza kukinga maji na kuokoa watu wa Kata za Mbuguni, Shambaraiburuka na Makiba?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Nassari kwa namna anavyowatetea wananchi wake lakini kubwa sisi tumepokea hayo aliyoyaeleza. Mimi kama Naibu Waziri tutakaa na wataalam wetu tuyapitie mapendekezo hayo tujue namna ya kufanya. Ahsante sana.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, tatizo hili la wanawake wajawazito waliojifungua ku-share vitanda lipo pia kwenye Hospitali ya Wilaya ya Arumeru na mimi nikishirikiana na DMO aliyekuwepokwa sababu ya PR tulipata wafadhili ambao walikuwa tayari kutujengea maternity ward kubwa na nzuri na kisasa kabisa kwa kushirikiana na mimi na Dkt. Okiyoo ambaye alikuwa DMO wa kwetu. Unfortunately kwa sababu binafsi ambazo siko tayari kuzitaja hapa tumeshazijadili pia na Katibu Mkuu wa TAMISEMI, Mkurugenzi aliyekuwepo akafanya yake wakamhamisha DMO kumpeleka Lindi.
Baada ya kupitia na kwenda kupitia zile parameters hapo Wizarani TAMISEMI tukagundua kwamba aliondolewa kwa sababu binafsi na bahati ambaya wale wafadhili ambao walikuwa watujengee ile maternity ward ilitokana na mahusiano binafsi ambayo tulikuwepo sisi na wao na yule daktari. Kwa hiyo, baada ya yeye kuondoka ni kama wameingia mitini vile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuuliza tu Serikali iko tayari kumrudisha yule bwana ili ule mradi ukamilike halafu baada ya hapo wamhamishe? Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali si mtu, kama alikuwa DMO pale ame-coordinate pale kwamba maternity ijengwe pale suala la yeye kuhama haiwezi ikawa kigezo cha kwamba mchakato huo usiendelee ni vizuri akarithisha hiyo kazi nzuri ambayo aliyokuwa ameishainza ili DMO aliyepo sasa afanye kuhakikisha kwamba hilo linakamilika.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, kwanza ni-declare interest, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Bunge hili ya Ardhi, Maliasili na Utalii na unakumbuka ulikuja Meru wewe, siku mimi nimeoa wewe ulikuja Meru ukimwakilisha Mama Makinda, na kwenye harusi ulizungumza ukasema miongoni mwa vilio ambavyo Mbunge wenu Nassari amekuwa akipigia kelele kwenye Bunge ni suala la ardhi.
Mheshimiwa Spika, Kata ya Ngarenanyuki ambayo inapakana na Hifadhi ya Taifa ya Arusha, hususan Kitongoji cha Momela, wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana na Serikali na Wizara kwa sababu ya shamba namba 40 na shamba namba 41 yaliyoachwa na walowezi, walowezi ambao watu wa Meru hawa walichomewa nyumba miaka ya 1950, mwaka 1952 wakamtuma mtu UN, leo 2018 tumezungumza kwenye Bunge, aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Engineer Ramo Makani akakubali kuondoka hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiwa masomoni Uingereza Mheshimiwa Mzee Mbatia huyu wakazungumza na wakakubaliana kwenda Meru kuniwakilisha kunisaidia kumaliza mgogoro. Amefika Wilayani Arumeru kasimamishwa na Mkuu wa Wilaya kutokwenda kwenye mgogoro, Mheshimiwa Mzee Mbatia akarudishwa kutoka kijijini kule ameshatoka Moshi. Huyo Mkuu wa Wilaya ndio aliyekwenda kuweka vigingi bila kushirikisha wananchi na imagine Wizara ya Ardhi hii imetoa hati mwaka huu mwezi wa pili, mwezi wa tatu maaskari wamekwenda kupiga risasi ng’ombe wa wananchi kwenye shamba namba 40 na shamba namba 41. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati mimi nimetaka kulia, mwanaume nikajizuia, sasa swali langu, Naibu Waziri wewe uko tayari baada ya kikao hiki kuongozana na mimi twende ili tukauangalie mgogoro huu na ili tuweze kujenga mahusiano mema kati ya hifadhi na watu wa Momela? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mgogoro huu umedumu kwa muda mrefu na viongozi waliotangulia walishafika katika yale maeneo na wakaona hali halisi na mimi niko tayari kuongozana naye ili twende tukaangalie nijionee mwenyewe ili tuweze kufanya uamuzi unaostahili.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa kuongeza tu ni kwamba, kama tulivyosema, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya kubaini aina yoyote ya migogoro nchini na Kamati hiyo imeshamaliza kazi yake na imeleta mapendekezo Serikalini ambayo Wizara zinazohusika zinayafanyia kazi na kufikia uamuzi, tukishafikia uamuzi nina imani kabisa tatizo hili la Meru litakuwa nalo ni mojawapo ambalo litaisha kabisa.