Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 2 | sitting 3 | Questions to Prime Minister | Maswali kwa Waziri Mkuu | 1 | 2016-01-28 |
Name
Freeman Aikaeli Mbowe
Gender
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Hai
Primary Question
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kumuuliza Waziri Mkuu swali.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, wewe ukiwa kama Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni na wewe ukiwa kama mwanasiasa mzoefu, nina hakika unatambua kwamba ujenzi wa demokrasia ni gharama na ni mchakato wa muda mrefu. Nina hakika utakuwa utajua vilevile kwamba nchi yetu imepiga hatua kubwa katika kujenga jamii inayoheshimu demokrasia, inayoheshimu Sheria na inayoheshimu Katiba ya nchi. Katika muda mfupi tangu Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, yapo mambo matano makubwa yaliyotokea ambayo yanaashiria, aidha Serikali hiyo haiheshimu kukua kwa demokrasia katika Taifa ama pengine ina dhamira ya kuondoa lengo kubwa hilo lililowekwa na Katiba ya Taifa.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, mambo hayo ni pamoja na baada tu ya uchaguzi wa mwaka 2015, Jeshi la Polisi limeweka makatazo nchi nzima kwa Vyama vya Siasa kufanya kutokufanya kazi zake za kisiasa, haki ambayo ni haki ya kikatiba.
Leo tayari ni miezi mitatu na siku tatu katazo hilo linaendelea na katazo hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu uliliunga mkono na kulisisitiza katika mkutano wako uliofanywa katika Jimbo lako la Ruangwa, kwamba wenye haki ya kufanya ni wale walioshinda, lakini Vyama vya Siasa haviendelei kuruhusiwa kufanya kazi hiyo ya siasa. (Makofi)
Swali langu sehemu (a) ni kama ifuatavyo; Mheshimiwa Waziri Mkuu unataka kuithibitishia Bunge hili, nchi hii na dunia hii, kwamba wewe kama Kiongozi Mkuu wa Serikali una kusudio la kuendelea kuzuia Vyama vya Siasa kufanya kazi zake za kisiasa ambayo ni haki yao ya Kikatiba? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu, tukiendelea hapo hapo unatambua vilevile kwamba urushaji wa matangazo ya moja kwa moja ni haki ya Kikatiba ya wananchi kupata taarifa na Shirika la Habari la Taifa ni shirika la umma, lakini ndani ya Bunge kuna taarifa zilizo rasmi kabisa kwamba Serikali yako imetoa kauli hapa kuzuia urushaji huo wa matangazo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na uzuiaji wa urushaji huo wa matangazo kumeendelea kuwepo matumizi makubwa ya majeshi yetu kuanzia Zanzibar hadi hapa na Zanzibar katika kupinga matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar ambao ulikuwa ni uamuzi wa wananchi?
Mheshimiwa Waziri Mkuu unaiambia nini dunia kwamba Awamu yako ya Tano sasa imekubali kuwa na utawala wa kijeshi kwa mgongo wa utawala wa kidemokrasia? (Makofi)
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme namshukuru sana Kiongozi wa Kambi ya Upinzani kwa maswali yake mawili ambayo yanahitaji ufafanuzi na Watanzania waweze kujua, kwamba uongozi huu wa Awamu ya Tano ni uongozi ambao unaongoza kwa kufuata demokrasia, kanuni, sheria na taratibu kadri ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yapo mambo yanajitokeza na tunapojaribu kutoa maelekezo ya kimsingi ya kuweza kufuatilia na kwa sababu ya utaratibu wa mazoea tu yanaweza kutafasiriwa vinginevyo. Suala lako la makatazo ya Vyama vya Siasa kufanya mikutano, ni jambo ambalo naweza kusema msemaji wa kwanza kabisa hakutumia nafasi yake ya uandishi kuandika kwa mfululizo kwa sababu ni mimi ndiye ambaye nilikuwa nimefanya ziara kwenye Jimbo langu kusalimia wapiga kura wangu.
Mimi ni Mbunge kama nyie na ninapokuwa Ruangwa sivai koti la Waziri Mkuu bali nakuwa Mbunge nazungumza na watu wangu. Nimekuwa na vikao mbalimbali vya makundi mbalimbali nikiwashukuru binafsi kwenye Jimbo langu ambako najua tuna utamaduni wetu. Nimepita pia kwenye Kata ambazo pia Madiwani wetu ni wa Vyama vya Upinzani, lakini tumeweka msimamo wa vyama vyote katika Jimbo lile kwamba lazima sasa tufanye kazi za maendeleo kwenye Jimbo letu.
Mheshimiwa Spika, kama mwandishi yule angeweza kuweka mtiririko wa ziara zangu na matamko yetu ndani ya Wilaya yangu kwa Jimbo langu, angeweza kunitendea haki, kwa sababu nilichotamka mimi kilifuatiwa na kauli zilizotamkwa na Madiwani kwenye Kata ambako nimetembela wakiwemo wa upinzani, ambao walisisitiza na kutoa msimamo kwamba sasa Jimbo hili tunataka tufanye kazi suala la siasa tunaliweka pembeni na tunaondoa tofauti zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya yanazungumzwa na Madiwani wenzangu wa vyama vingine. Kwa hiyo, ni jambo jema wanapolitamka kwa wananchi kwa maana ya kuweka msimamo wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mtiririko ule tulizungumza pia na Baraza la Madiwani, nimezungumza na wafanyakazi wa Halmshauri, nimezungumza na Baraza la Wazee, nimezungumza na akinamama na pia nikazungumza na Jeshi la Polisi, wale ni sehemu ya raia walioko kwenye Jimbo langu. Mimi nimefanya kazi nyingi kwao na wao wamefanya kazi nyingi sana kwangu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kauli yangu ilikuwa inatokana na mazingira yale, kama mwandishi angeamua kufanya kazi yake vizuri kwa kueleza shughuli zangu hata nilipotamka kwamba kuanzia sasa sisi tumeamua tufanye kazi, bila kuzingatia itikadi za vyama vyetu na kwamba sasa mambo ya siasa tuache pembeni. Wale wote ambao sasa wangetakiwa kupita kwenye maeneo ya walioshinda ni wale tu ambao wameshinda kwenye maeneo yao. Kwa hiyo jambo lile kama lingekuwa limeelezwa, limeripotiwa kwa mtiririko ule wala lisingeweza kuleta tafsiri ambayo imekuja kutolewa.
Mheshimiwa Spika, najua utawala wa sheria, najua Vyama vya Siasa vina haki yake, najua nchi inatambua kwamba chama cha siasa kinaweza kufanya mkutano. Pia kama msingi ule wa kauli ya Wanajimbo wa Ruangwa unaweza kufuatwa na watu wengine unaweza kuwaletea tija pia.
Mheshimiwa Spika, kwa hayo niliyosema, niseme tu kwamba, jambo lile lilitokana na mazingira ninamoishi na sikulitamka kama Waziri Mkuu, nilitamka kama Mbunge wa Jimbo na lilitokana na matamko ya sisi wawakilishi wa Vyama vya Siasa kutoka kwenye Jimbo lile Mheshimiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ni lile ambalo Mheshimiwa ametaka kujua suala la kauli ya Serikali juu ya TBC kuacha kutangaza siku nzima na badala yake watatangaza vipindi vya maswali na majibu, lakini baada ya hapo wataendelea na shughuli zao na huku waki-record ili waweze kututangazia baadaye.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amelifafanua vizuri sana jana kwenye kipindi maalum na naamini Watanzania wametuelewa. TBC haijaacha kutangaza, walichofanya ni kubadilisha ratiba. Matangazo ya Bunge yataendelea kutangazwa, lakini tumebadilisha muda, badala ya muda ule ambao wao wangeweza kufanya matangazo ya kibiashara na matangazo mengine, suala la Bunge waandishi wao wako, TBC ina wawakilishi Dodoma, watafanya recording, halafu baadaye watatafuta muda mzuri ambao pia tunaamini Watanzania wengi watapata muda mzuri wa kuweza kuyasikiliza matangazo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huo ni mpango wa Taasisi yenyewe wa ndani, unaotokana na kazi wanazozifanya, wanajua matatizo na faida wanazozipata ndani ya Taasisi. Kwa hiyo, wanapoishauri Wizara, wanapoieleza Wizara na kwa kuwa walishaanza kutekeleza na Watanzania waliona mkatiko wa matangazo, lakini pia kulikuwa na mwongozo ulitolewa hapa. Kwa hiyo, tukasema jambo hili ni lazima sasa tulieleze kesho yaani lazima kuwe na kauli ya Serikali kwa Watanzania kwa sababu Mwongozo ulitolewa na mmoja kati ya Wabunge wetu anataka kujua kwa nini kuna mkatiko wa matangazo. Kwa hiyo, ndivyo ilivyokuwa na huo nadhani ni msimamo wa TBC na ndiyo msimamo wa Serikali.
SPIKA: Tunaendelea na Mheshimiwa Kiongozi wa Upinzani swali la nyongeza!
MBUNGE FULANI: La majeshi bado.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa ametaka pia kujua matumizi ya Majeshi. Majeshi yetu yapo kwa malengo kwamba lengo kuu ni kutunza amani na utulivu ndani ya nchi. Wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba watu kwa maana ya Watanzania kwa Majeshi ya Tanzania, wajibu wake ni kuhakikisha kwamba watu wetu wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na wako nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jukumu lao ni kumlinda Mtanzania popote alipo bila ya kukiuka misingi ya jambo ambalo anatakiwa kulifanya wakati huo. Wapo Zanzibar, wapo pia Tanzania Bara na wote hao kazi yao na jukumu lao ni lilelile. Sasa wanaweza kulazimika kutumia nguvu pale ambapo wanaona utaratibu uliowekwa eneo hilo unakiukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo kazi ya Jeshi la Polisi, kwamba wataendelea kutunza amani ili Watanzania waliokuwa kwenye eneo hilo kila mmoja afanye shughuli yake. Kila mahali kuna utaratibu wake na kila mahali kuna msingi wake na tunatarajia katika eneo, wote walio kwenye hapo, wanaofanya jambo hilo, wafanye jambo hilo kwa msingi unaofanana, usiokiuka taratibu za eneo hilo.
Kwa hiyo, Jeshi la Polisi lipo na litaendelea kufanya kazi yake kwa uaminifu, kwa uadilifu na naomba sana tuwasaidie Jeshi la Polisi kufanya kaziWAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa ametaka pia kujua matumizi ya Majeshi. Majeshi yetu yapo kwa malengo kwamba lengo kuu ni kutunza amani na utulivu ndani ya nchi. Wajibu wao mkubwa ni kuhakikisha kwamba watu kwa maana ya Watanzania kwa Majeshi ya Tanzania, wajibu wake ni kuhakikisha kwamba watu wetu wanafanya shughuli zao kwa amani na utulivu na wako nchi nzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jukumu lao ni kumlinda Mtanzania popote alipo bila ya kukiuka misingi ya jambo ambalo anatakiwa kulifanya wakati huo. Wapo Zanzibar, wapo pia Tanzania Bara na wote hao kazi yao na jukumu lao ni lilelile. Sasa wanaweza kulazimika kutumia nguvu pale ambapo wanaona utaratibu uliowekwa eneo hilo unakiukwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo kazi ya Jeshi la Polisi, kwamba wataendelea kutunza amani ili Watanzania waliokuwa kwenye eneo hilo kila mmoja afanye shughuli yake. Kila mahali kuna utaratibu wake na kila mahali kuna msingi wake na tunatarajia katika eneo, wote walio kwenye hapo, wanaofanya jambo hilo, wafanye jambo hilo kwa msingi unaofanana, usiokiuka taratibu za eneo hilo.
Kwa hiyo, Jeshi la Polisi lipo na litaendelea kufanya kazi yake kwa uaminifu, kwa uadilifu na naomba sana tuwasaidie Jeshi la Polisi kufanya kazi yao bila ya usumbufu ili wasionekane wanafanya kazi nje ya utaratibu wao. Hilo ndiyo jibu la msingi. (Makofi)
Name
Freeman Aikaeli Mbowe
Gender
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Hai
Question 1
MHE. FREEMAN A. MBOWE: Nakushukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu yako, lakini ningependa kuuliza maswali ya ziada kama ifuatavyo:-
Kauli yako Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba katika Jimbo lako la uchaguzi mmekubaliana muache siasa mfanye kazi, niliomba tu utambue kwamba siasa vilevile ni kazi. Vilevile kwa sababu kauli ya Waziri Mkuu ni agizo bila kujali umeitolea Jimboni kwako ama nyumbani kwako Mheshimiwa Waziri Mkuu, kauli yako unapoitoa mahali popote kama Kiongozi Mkuu ni agizo. Sasa kwa sababu Mahakama Kuu Mwanza wakati ikisikiliza kesi ya Alphonce Mawazo ilitoa hukumu kwamba Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kisheria ya kuzuia mikutano ya Vyama vya Siasa yakiwemo maandamano kwa kisingizio cha...
Mheshimiwa Spika, narudia hapo kwa kisingizio cha wana taarifa za kiintelijensia na Mahakama Kuu ikaagiza Jeshi la Polisi kama mna taarifa za kiintelijensia ina maana mna msingi mzuri wa kulinda usalama. (Makofi)
Kwa hiyo solution siyo katazo, solution ni Jeshi la Polisi kuwasiliana na wahusika ili waweze kuwalinda vizuri kwa sababu tayari wana taarifa za uvunjifu wa amani.
Sasa Mheshimiwa Waziri Mkuu uko tayari sasa kutoa tamko kwa Taifa na kwa kupitia Bunge hili, kwamba lile katazo la mikutano ya siasa ya vyama vya siasa, sasa unalisitisha rasmi?
La pili hapo hapo, je, kwa kutoa tamko lile vilevile uko tayari tena kulieleza Jeshi la Polisi, liheshimu mhimili wa tatu ambao ni Mahakama ambayo ime-declare kwamba hawana mamlaka ya kutoa katazo wakati wanapopata taarifa za kiintelijensia?
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa maswali mawili ya nyongeza ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Mheshimiwa Mbowe. Kama ambavyo nimeeleza awali kwamba Katiba inaeleza, lakini Sheria ndiyo inayoongoza nchi hii kuweka miongozo ya utaratibu. Siasa nchi hii haijaanza leo, upo utaratibu na zipo taratibu za kimsingi, kama chama kinahitaji kufanya mikutano lazima wafuate utaratibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la Mahakama kuzuia Jeshi la Polisi kufanya kazi, hii ni mihimili miwili tofauti, Mahakama siwezi kuzungumzia habari za mhimili mwingine na kuutolea kauli.