Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 7 | Sitting 39 | Questions to Prime Minister | Maswali kwa Waziri Mkuu | 3 | 2017-06-01 |
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Primary Question
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Naomba kwanza kabla sijauliza swali langu niipongeze Serikali chini ya Dkt. John Pombe Magufuli kwa jinsi ilivyoshughulikia suala zima la vyeti fake pamoja na watumishi hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba niulize swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni Serikali ilifanya maamuzi ya kuzuia kusafirisha mchanga wa dhahabu nje ya nchi, katika kufanya hivyo Serikali itakuwa imepoteza dira katika demokrasia ya kiuchumi duniani, lakini si hivyo tu itakuwa pia imeleta mahusiano ambayo si mazuri na nchi mbalimbali duniani. Nini tamko la Serikali kuhusu jambo hili?
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sasa tuko kwenye matarajio ya kupata taarifa iliyo kamili kwenye sakata la mchanga na nataka nizungumzie eneo ambalo umehitaji zaidi la nini Serikali inatamka juu ya hili ili kuwaondolea hofu wawekezaji wetu wale waliowekeza kwenye maeneo ya madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni Watanzania wenyewe walionesha hofu kubwa kwa kipindi kirefu, hata Waheshimiwa Wabunge katika michango yenu mbalimbali kwa miaka iliyopita, hata pia katika kipindi hiki cha Serikali hii ya Awamu ya Tano mmeendelea kuitaka Serikali ichukue hatua thabiti na kutaka kufanya uchunguzi wa kina juu ya mchanga unaotoka nchini kupeleka nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli amelitekeleza hilo pale ambapo alinituma mimi mwenyewe kwenda Kahama, kwenda kuona zoezi la ufungashaji wamchanga na kuuona mchanga huo, lakini nilipomletea taarifa akaamua kuunda Tume na aliunda tume mbili, moja ya kwenda kuukagua mchanga wenyewe na kujua ndani kuna nini, lakini ya pili, ni ile Tume ambayo inahakiki, itatoa taarifa ya madhara ya kiuchumi, lakini pia madhara ya kisiasa kwa ujumla na mahusiano kwa ujumla wake. Mpaka sasa tumepata taarifa moja na bado tunasubiri taarifa ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nataka nitumie nafasi hii kuwasihi wawekezaji wote, kwanza wasiwe na mashaka kwa sababu, lengo la Serikali ni kujiridhisha tu kwamba, je, mchanga huu unaosafirishwa kwenda nje una nini? Na wala hatubughudhi uzalishaji wao. Baada ya kuwa tumepata taarifa ya kwanza, bado hatua kamili hazijachukuliwa, tunasubiri taarifa ya kamati ya pili, baada ya hapo sasa Serikali itakaa chini na kutafakari kwa kupata ushauri kutoka sekta mbalimbali za kisheria, za kiuchumi na maeneo mengine hatua gani tuchukue. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niendelee kuwatoa hofu wawekezaji wale walioko kwenye sekta ile ya madini wawe watulivu. Hatuna jambo ambalo tumelifanyia kazi dhidi ya hatua ambazo tumechukua ndani ya nchi kwa watu wetu ambao tunao ambao tuliwapa dhamana ya kusimamia hilo, lakini wawekezaji wote waendelee na shughuli zao za uwekezaji kama ambavyo tumekubaliana, wale ambao wako kwenye mchanga kwa sababu juzi wameambiwa watulie, watulie, hakuna jambo ambalo litafanywa ambalo halitatumia haki, ama litaenda nje ya haki au stahili ya mwekezaji huyo na kila kitu kitakuwa wazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia nitoe pia rai hata kwa Watanzania wawe watulivu. Tumeona watu wanatoa matamko wakidhani labda kuna uonevu, hapana! Watu watulie wasubiri majibu ya Serikali ambayo yatalinda haki ya kila mwekezaji, lakini na sisi pia Watanzania ambao tunaona tuna rasilimali zetu, hatuhitaji hizi rasilimali zipotee hovyo, lazima tuwe na uhakiki. Katika hili naomba mtuunge mkono Serikali kwa sababu kazi tunayoifanya ni kwa manufaa ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki huu ni kwa manufaa yetu Watanzania, ili tuwe na uhakika wa matumizi sahihi ya rasilimali zetu nchini. Kwa kufanya hilo tutakuwa tunajua tunapata nini na pia tujue tunaratibu matumizi yake na sisi Wabunge nadhani ndio hasa wahusika kama wawakilishi wa wananchi, twende tukawatulize wananchi waache kutoa matamko wasubiri Kamati zile. Pia tuzungumze na wawekezaji wetu ili nao pia wawe watulivu, bado Kamati ya pili haijatoa taarifa, baada ya hiyo maamuzi yatafanyika. Ahsante sana.
Name
Emmanuel Adamson Mwakasaka
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Tabora Mjini
Question 1
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Kwa kuwa tatizo hili la upimaji wa mchanga linaanzia kule ambako ndiko kuna machimbo yenyewe. Ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kule origin source kunawekwa mashine ambazo sasa tatizo hili halitajirudia tena?
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, moja kati ya mikakati ambayo tunayo ni kupokea wawekezaji na tumeanza kuona wawekezaji kadhaa wakija kuonesha nia ya kuwekeza kwenye eneo hili. Awali kulikuwa na usiri mkubwa wa namna ya kuwakaribisha wawekezaji hawa kuwekeza kujenga mitambo hii na ndio kwa sababu Serikali imeanza kuchukua hatua za awali kwa vile tunajua kwamba, kuna maeneo ambayo yalikuwa hayaoneshwi wazi ikiwemo na eneo la kuwakaribisha wawekezaji wa kujenga mitambo hii hapa nchini.
Baada ya muda mfupi kama ambavyo mambo yameanza kujitokeza tutaamua kuwekeza, kujenga mashine zetu hapa hapa nchini au kuwakaribisha wawekezaji au kuona uwezo wa Serikali kama tunaweza ili sasa tuweze kutatua tatizo ambalo linatukabili sasa la kupoteza mchanga ambao tunautoa hapa na kupeleka nje kwa ajili ya uyeyushaji na kupata aina mbalimbali za madini. Ahsante.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved