Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 7 Sitting 56 Questions to Prime Minister Maswali kwa Waziri Mkuu 4 2017-06-29

Name

Ritta Enespher Kabati

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni Serikali imetoa tamko la kutosafirisha chakula nje ya nchi, lakini kuna baadhi ya mikoa ambayo imezalisha chakula cha kutosha cha ziada kinachoweza kusafirishwa hata nje ya nchi. Je, Serikali inatoa ufafanuzi gani kuhusiana na utekelezaji wa tamko hilo?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Iringa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo hili nimelizungumza siku ya Idd Mosi nikiwa kwenye sherehe ya Idd kwenye Baraza la Idd kule Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Nilizungumza kwa msisitizo kwamba tumedhibiti na tumezuia usafirishaji wa chakula na hasa mahindi nje ya nchi kwa sababu historia yetu sisi kuanzia mwaka wa jana mwezi Novemba, 2016 mpaka Februari, 2017 nchi yetu ilikosa mvua za msimu unaotakiwa na tutapata usumbufu mkubwa ndani ya nchi kwa maeneo mengi kukosa chakula cha kutosha.

Mheshimiwa Spika, na chakula kikuu sasa nchi Tanzania naona utamaduni umebadilika, nilikuwa nazungumza pia na Mheshimiwa Mbatia hapa kwamba utamaduni umebadilika, Wachaga, Wahaya sasa badala ya kula ndizi wanakula ugali. Wamasai waliokuwa wanakula nyama tu pekee sasa wanakula ugali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utakuta mahindi yanatumika sana kuwa ni chakula kikuu nchini na kwa hiyo lazima tuweke udhibiti wa utokaji wa mahindi ili yaendelee kutusaidia kama chakula kikuu hapa nchini kwetu.

Kwa hiyo tumeweka zuio, na hasa baada ya kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Kilimanjaro ilitoa taarifa kwamba kuna utokaji wa mahindi mengi kwenda nchi za nje kwenye mipaka yetu. Na siku ile nilipokuwa Kilimanjaro malori kumi yalikamatwa yakiwa na mahindi yakivushwa kwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lazima tuweke utaratibu na ninyi wote ni mashahidi kwamba uzalishaji huu haukuwa wa uhakika sana kuanzia mwezi Machi mpaka mwezi Mei, kwa miezi mitatu. Maeneo machache yamezalisha sana kama ulivyosema Mheshimiwa Ritta Kabati lakini maeneo mengine hayana chakula. Juzi nilikuwa Mwanza nikiwa pale Usagara, Kigongo Ferry nilisimamishwa na wananchi, moja kati ya tatizo walilolieza ni upungufu wa chakula. Nimeona, hata Sengerema mahindi yote yamekauka, Geita mahindi yote yamelimwa yamekauka. Kwa hiyo, bado tuna tatizo la upungufu wa chakula. Pia bei za chakula chetu iko juu sana hatuna namna nyingine ni kudhibiti chakula chetu.

Mheshimiwa Spika, na nilieleza kwamba nchi nyingi za jirani hazina chakula. Sisi tuna barua hapa kutoka Congo, South Sudan tumepata kutoka Somalia na nchi za jirani wanaomba kupewa msaada wa chakula kutoka Tanzania wakati sisi wenyewe hatuna chakula cha kutosha. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa Serikali na wananchi mkatuunga mkono katika hili, kudhibiti utokaji wa chakula, na hasa mahindi yanayokwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwamba sisi tulichofanya ni kudhibiti kutoa mahindi nje bila kibali. Na kama kuna umuhimu wa kupeleka mahindi nje basi tunataka yasagwe ndani ili yapelekwe, kwa sababu ukisaga tunafaida zake, pumba tunazipata, tunazitumia kwa chakula cha mifugo lakini pia mashine zetu ambako tuna msizitizo wa viwanda vitafanya kazi ya kusaga, tutakuwa na ajira, lakini tunapotoa mahindi maana yake tunatoa kila kitu huku ndani tunakuacha tupu. Kwa hiyo, lazima tuwe na mpango ambao utasaidia sasa, sisi wenyewe Watanzania kunufaika kupitia zao hili.

Mheshimiwa Spika, bado msimamo ni ule ule kwamba tumezuia mahindi kutoka nje ya nchi na kama ni lazima basi aende Wizara ya Kilimo akaombe kibali kama ni lazima Wizara ikiona inafaa utapata kibali, lakini kibali hicho ni cha kutoa unga na si mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote ni mashahidi, jana tumepata taarifa malori zaidi ya 103 kwa siku nne kutoka siku ya Idd mpaka leo hii, malori 103. Je, kwa mwezi mzima tutakuta na mahindi hapa ndani?

Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa kupita Kamati za Ulinzi na Usalama kwamba wengi wanaofanya biashara kuja kuchukua mahindi Simanjiro, Kibaya kwa maana ya hapa katikati maeneo ya Kongwa ni watu kutoka nje ya nchi ndio wanaokuja kuchukua. Kwa hiyo hatuna faida sana hao kuingia zaidi ya kwamba wanatuachia fedha. Hivyo tunaitengeneza shida ambayo tutakuja kuanza kuuliza tutapateje chakula ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Watanzania kwa jambo hili naomba mtuunge mkono kwa sababu tunachofanya ni kwa maslahi ya nchi, hatimaye bei zitapanda tutashindwa kununua mahindi na wote mnajua angalau sasa mahindi yamepungua kwenye masoko

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuendelee na hali hiyo ili chakula kiwe cha kutosha baada ya kuwa tumefanya tathimini tukijiridhisha kwamba chakula cha ndani cha kutosha kipo na tuna akiba kutoka kwenye maeneo yanayozalisha sana basi vibali hivyo vinavyotolewa kwa utaratibu vitaendelea kutoka, na wale ambao wanataka kufanya biashara nje ya nchi wataendelea kupata fursa ya kufanya biashara nje ya nchi. Lakini kwa sasa tumezuia; na ninataka nimpongeze sana Mkuu wa Mkoa ya Kilimanjaro mama Anna Mghwira na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kusimamia.

Mheshimiwa Spika, tumeona malori yale agizo limebaki pale pale, mahindi yale ambayo yatakuwa yamaekamatwa; na tumejihisi kwamba yalikuwa yamekwenda nje ya nchi, yote yataingizwa kwenye hifadhi ya taifa, na hayo malori yanyofanya biashara hiyo yote yatabaki kituo cha polisi. Lakini pia kwa namna ambavyo wanaendelea na waendelee kwa utaratibu wote na maagizo yetu yatabaki vilevile ili tuweze kuwahudumia Watanzania ndani ya nchi.

Additional Question(s) to Prime Minister

Name

Martha Moses Mlata

Gender

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Question 1

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana kwa majibu ambayo hakika yameponya nyoyo za watu ambao walikuwa wanaguswa sana na suala hili la CDA. Lakini Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwa umesema mamlaka haya; na umeeleza vizuri Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma itakavyofanya kazi, naamini na Halmashauri nyingine nchi nzima zitafanya kazi kama ambavyo umetoa maelekezo.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo moja tu, kwamba wanapokwenda kuchukua ardhi kutoka kwa wamiliki au kwa watu ambao wanahodhi zile ardhi zao, wanalipa fidia kwa fedha ndogo sana, lakini wanapokuja kupima na kutaka kuviuza wanauza kwa bei ambayo ni tofauti na ile gharama ambayo walinunulia.

Je, Serikali hapa inaweza pia ikatoa maelekezo kwamba, angalau uwiano wake usipishane sana kwa ajili ya kuwanufaisha hata wale wahusika wa maeneo ambayo yanakuwa yamechukuliwa? Ahsante sana.

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mlata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ziko sheria ambazo zinaongoza fidia na ndizo ambazo tunazifuata. Fidia hizi kuna watu ambao wamepanda mazao kwenye ardhi, lakini wengine hawajapanda chochote. Kwa hiyo, mabadiliko ya bei ama tofauti ya bei inatokana na ambavyo mwenye ardhi alivyoweza kuwekeza kwenye eneo lile. Kama kuna mazao yoyote yanafanyiwa tathmini na tunalipa kwa mujibu wa bei na taratibu zilizopo kisheria.

Kwa hiyo, bado tutasisitiza mamlaka zote za halmashauri zote za Wilaya, Miji na Manispaa na Majiji kufuta sheria zile ambazo zimeelekezwa katika kufanya fidia. Na tumesemea ardhi ya mtu isichukuliwe bila fidia, kwa hiyo, bado hili litaende kuzingatiwa. Na agizo hili naomba wazingatie maeneo yote haya ambayo nachukua ardhi ya mtu, kwamba lazima alipwe kwanza ndipo uweze kuchukua, ili kuondoa migogoro ambayo siyo muhimu kwa sababu sheria ipo na inatuongoza kufanya hivyo, ahsante.