Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 3 | Sitting 49 | Questions to Prime Minister | Maswali kwa Waziri Mkuu | 12 | 2016-06-23 |
Name
Venance Methusalah Mwamoto
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Primary Question
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa Serikali ya utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilitimiza malengo yake ya kusaidia kupigania uhuru nchi za Afrika na hivyo kupelekea nchi zote kupata uhuru; nchi hizo wakati zikiwa hapa zilijenga makambi ambayo yalitumika kwa ajili yao katika sehemu tofauti; na kwa kuwa makambi hayo yametumika baada ya kuondoka kama Vyuo na Sekondari na pia kufanya wao waendelee kukumbuka kwa yale ambayo tumeenzi:-
Ni lini Serikali sasa, itabadilisha makambi ya wapigania uhuru hawa ambayo yametumika kama Magereza na matumizi mengine yasiyofaa, ili waendelee kukumbuka sehemu ambazo walikaa kwa ajili ya kupigania uhuru wetu?
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la kwanza kabisa la Mheshimiwa Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba nchi yetu ilishiriki sana kuwakaribisha wapigania uhuru wa nchi mbalimbali, kuendesha harakati zao za kisiasa hapa nchini. Maeneo yote waliyokuwa wamekaa, waliweza kujenga miundombinu mbalimbali na yanatambulika kama makambi ya wapigania uhuru.
Katika kumbukumbu zangu, Morogoro kuna eneo linaitwa Dakawa ambalo sisi tunatumia kama Sekondari, lakini pia Mazimbu pale kwenye Compus ya SUA na maeneo mengine, nakumbuka kule Nachingwea kuna eneo la Matekwe na eneo lile lililotumika ni kama vile Pashule; na kuna eneo pale Msata, hapa jirani Chalinze pale ambako jeshi linatumia sana kama sehemu ya mazoezi. Pia kuna makambi mengine, nakumbuka nikiwa Naibu Waziri nilikuja kwako Kilolo, eneo moja kati ya maeneo ya makambi pale Kilolo ndiyo wanatumia kama Magereza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maeneo haya baada ya kuwa shughuli za wapigania uhuru kumaliza kazi zao, Serikali ilifanya maamuzi kutumia miundombinu ile kwa shughuli mbalimbali ikiwemo elimu. Eneo lingine kama hilo la Msata, Jeshi na pale Kilolo, Magereza. Maeneo hayo yote, kutokana na nature ya miundombinu iliyopo, maamuzi haya yalifanywa ili kutumia kwa umuhimu wa mahitaji ya nchi. Kwa hiyo basi, eneo kama Kilolo ambalo limetumika kama Magereza, suala la Magereza siyo suala la matumizi yasiyokuwa muhimu, ni muhimu pia kwa sababu ni sisi wenyewe ndio tunaenda kuishi pale na ni maeneo ya mafunzo, lakini pia ni eneo ambalo tunawahifadhi wale ambao wamepatikana na hatia kadhaa na kwenda kutunzwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pale ambako tumetumia miundombinu ile kwa shughuli nyingine nje ya elimu, basi napenda kutumia nafasi hii kuwasihi Halmashauri za Wilaya, pamoja na wananchi kujenga miundombinu mingine kwa ajili ya kutumia kwa matumizi ya elimu na haya maeneo mengine yanayotumika kwa elimu yataendelea kutumika kama ambavyo imepangwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumbukumbu hizi sasa ukiangalia kwa sehemu kubwa, makambi yale yote yaliyotumika, mengi sana yanatumika ni kwa matumizi ya elimu zaidi na maeneo machache ndiyo kama hayo mawili niliyoyataja, kule Msata na Kilolo ndipo ambako yanatumika kwa Jeshi pamoja na Magereza. Yote haya ni mambo muhimu kwetu sisi, ni lazima tutumie miundombinu ile ili pia badala ya kuwa tumeyaacha tu, bora yatumike ili huduma mbalimbali ziweze kutolewa katika maeneo hayo.
Name
Venance Methusalah Mwamoto
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Kilolo
Question 1
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa majibu mazuri, lakini nilikuwa naomba ile sehemu kwa umuhimu uliopo, kwa kuwa wenzetu wanaweza kuja siku moja pale, kwa ajili ya kutaka kujua walipoishi; kwa kuwa ni sehemu ambayo ina kumbukumbu muhimu na viongozi wengi wakubwa walikaa, basi angalau Serikali ifikirie kujenga kitu kingine mbadala kwa ajili ya kuwaenzi na kuwakumbuka wale wenzetu wa Afrika Kusini. Ahsante.
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge ametoa ombi kwamba kwa kuwa eneo hilo la Kilolo lina umuhimu wa kuwa na shule nyingi za sekondari, ifikiriwe kuwa eneo hilo libadilishwe badala ya Magereza liwe elimu. Ni wazo zuri na ni ombi, tunaweza kuangalia ndani ya Serikali, lakini bado nilipokuwa najibu swali la msingi, nilisema eneo hilo la Kilolo linahitaji kuwa na taasisi za shule nyingi kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bado Halmashauri na wananchi wanahitajika kuweka mikakati ya ujenzi wa shule nyingine, huku Serikali ikiangalia umuhimu na uwezekano wa kubadilisha hilo Gereza kuwa elimu; lakini bado Magereza ni eneo muhimu na ni jambo la msingi pia kuwa na Gereza kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadiri ambavyo Serikali tutafanya mapitio, tutawezakuwapa taarifa wananchi wote wa Kilolo.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved