Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 3 | Sitting 49 | Questions to Prime Minister | Maswali kwa Waziri Mkuu | 16 | 2016-06-23 |
Name
Mohamed Omary Mchengerwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Primary Question
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, Sera na Mifumo ya Kisheria tuliyonayo sasa inaruhusu kuwaenzi waasisi pamoja na viongozi wa n hi hii, lakini siku za hivi karibuni Mheshimiwa Waziri Mkuu, imejidhihirisha wazi kwamba baadhi ya viongozi wameingia katika dimbwi la wizi, ubadhirifu wa mali za Umma na ukiukwaji wa maadili:-
Je, ni lini Serikali itafanya mapitio ya Sera, Sheria na kubadilisha mifumo ili sasa wale wezi wote waweze kuchukuliwa hatua kali za Kisheria na watakaobainika hivyo dhidi ya ukiukwaji wa maadili ya nchi hii? Ahsante.
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kudhibiti vitendo vya wizi, kukosa uadilifu, kukosa uaminifu mahali pa kazi na Watumishi wa Sekta ya Umma. Serikali inafanya hilo bila kujali ngazi ya mtumishi huyo, awe ni kiongozi wa ngazi ya juu, wa kati, hata wale watumishi wa kawaida, ilimradi Serikali imetoa dhamana ya kuwatumikia Watanzania, tunatarajia kila mtumishi atakuwa mwadilifu, mwaminifu, lakini pia atakuwa mchapakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaokiuka, dhidi ya wale wote ambao hawatumii vizuri madaraka yao, dhidi ya wale wote wanaojihusisha na vitendo vya rushwa popote pale nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ametaka kuona ni hatua gani zinachukuliwa; kwanza, tunaendelea kutoa elimu kwa watumishi ya kwamba kila mtumishi anatakiwa kufuata maadili ya utumishi, ikiwemo na uaminifu, uadilifu na uchapakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali inaendelea kuboresha kwa kuunda; na tumeshaunda Taasisi ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Maadili ya Watumishi ambayo yenyewe inajiridhisha kwamba kila mtumishi anatangaza mali zake na kuendelea kufuatilia mara kwa mara mabadiliko ya mali hizo ili tuone kama mali hizo amezipata kwa utumishi wake huu alionao.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, Serikali imeendelea kuimarisha taasisi mbalimbali ikiwemo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo pia inafuatilia maeneo yote; kwa Watumishi wa Umma na hata raia wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunafanya mapitio ya lile jambo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelisema la Sera yetu na Sheria, Kanuni ili ziweze kuendana na mabadiliko ya wakati. Hii pia, ili kuisaidia Serikali kudhibiti tabia hii, sasa Serikali kupitia Bunge hili, siku mbili tatu zijazo mtapitisha Muswada wa kuanzisha Division ya Mahakama ya Mafisadi ili kuweza kupambana nao kwa lengo la kudhibiti vitendo vya Watumishi wa Umma wenye tabia ya kuiba fedha mahali pa kazi, lakini wale wenye vitendo vya ufisadi ili wote hao waweze kuchukuliwa hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa mbinu hizi, kwa njia hizi zote, tutaweza kuwa na Watumishi wa Umma wenye maadili mema na wenye kutumia madaraka yao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, malengo yetu Serikali ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanahudumiwa vizuri na Watanzania wawe na uhakika na Watumishi waliopo kwa kutekeleza wajibu wao kwa Watanzania wote bila kuwa na vitendo ambavyo vinaweza kuathiri utendaji wa kila siku.
Name
Mohamed Omary Mchengerwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Rufiji
Question 1
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru sana kwa majibu mazuri ambayo ninaamini yamekidhi kiu ya Watanzania wengi wanyonge, hususan Watanzania ambao wamekuwa wakikosa maendeleo, hususan wa Jimbo langu ya Rufiji. Ninaamini sasa Sheria hii itaweza kusaidia upatikanaji wa maendeleo kwa Jimbo langu la Rufiji, hususan ujenzi wa Barabara ya Nyamwage – Utete. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi tu kuhusiana na hilo, labda ni kama ombi tu kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu majibu ni mazuri, ni lini sasa Serikali itaamua mambo haya ya maadili yaingie katika Mitaala ya Shule za Sekondari na Shule za Msingi ili vijana wetu wawe na maadili? Msingi wa maadili uanzie Shule za Msingi na Sekondari.
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napokea ombi lako na ni ombi zuri kwamba, ili tujenge maadili mema tunatakiwa tuanze kutoka ngazi za chini, lakini njia ambayo tumeitumia ni kwamba, watumishi wetu hawa ambao pia wameapa kuwa watumishi wenye maadili mema, wakiwemo Walimu ambao wanafanya kazi yao kwa weledi mkubwa, ndio ngazi ya awali ambayo wanasimamia vizuri vijana wetu kutoka ngazi ya shule, wanawalea watoto wetu, wanawasimamia kuwa na nidhamu, kuwa waadilifu, lakini pia, wanadhibiti vitendo vya wizi miongozi mwao ni sehemu ya mafunzo tosha ikiwa ni sehemu ya malezi ambayo yanatolewa na ngazi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuimarisha mabadiliko ya mitaala yetu kwa kuingiza maeneo haya ya utumishi bora, maadili mema ili tupate Watanzania wengi wenye maadili na hatimaye huko mbele tuweze kujihakikishia na shughuli zote za maendeleo nchini tukiamini kwamba kila mmoja atakuwa amelelewa vizuri kwenye familia yake anapokwenda shuleni na pia hata kwenye utumishi kufuata pia Sheria na Kanuni ili kuleta matokeo mazuri. Ahsante sana.
Copyright © Bunge Polis 2024. All Rights Reserved