Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2015-2020 | Session 2 | sitting 3 | Finance and Planning | Maswali kwa Waziri Mkuu | 3 | 2016-01-28 |
Name
Mussa Azzan Zungu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ilala
Primary Question
MHE. MUSSA A. ZUNGU: Mheshimiwa Waziri Mkuu, nami nichukue nafasi hii kukupongeza wewe na Serikali yako kwa kazi nzuri mnayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri Mkuu, viwango vya VAT sasa hivi Tanzania ni 18% na viwango hivi havitofautishi biashara, kati ya katikati, kubwa na za chini. Je, Serikali haioni sasa ikipunguza viwango vya VAT kwa biashara za chini, compliance ya watu wa biashara za chini, wengi wataweza kulipa VAT hii kwa kiwango cha chini na kuiongezea mapato Serikali kwa kiwango kikubwa sana. Naomba kujua kama Serikali inaweza ikapokea ushauri huu na kulifanyia kazi na kuhakikisha kila mtu alipe VAT kwa kiwango cha shughuli ya biashara anayofanya.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukienda Super Market sasa hivi ukinunua chochote, unalipa 18%. Kwa hiyo, inaongezea mzigo kwa wale wachache ambao wanalipa kodi hii, lakini kodi hii ikishushwa kwa viwango, 18, 14, 10 na labda na tano itafanya compliance ya wananchi wote ambao wanafanya biashara waweze kulipa kodi hii na Serikali kujiongezea mapato. Naomba majibu yako Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azzan Zungu, Mbunge wa Ilala, kama ifuatavyo:-
Swali hili, pia nimewahi kupata bahati ya kukaa na wafanyabiashara wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuwatia moyo wa kufanya biashara zao zaidi.
Moja kati ya mambo ambayo yalijitokeza kwenye vikao vile ni mjadala ambao leo umeuliza swali linalofanana sana kama ambavyo walikuwa wameomba. Pia tuliweza kuwaeleza wafanyabiashara na naomba nijibu swali lako kama ambavyo tuliweza kujibu, kwamba, VAT ya 18% mara nyingi huwa inatozwa kwa wafanyabiashara wanaofanya biashara kuanzia milioni arobani na kuendelea kwa mwaka au wanaopata pato la milioni kumi ndani ya miezi mitatu na miezi minne. Chini ya hapo hawausiki na VAT.
Mbili, kuruhusu biashara zote za aina zote zile kutoza 18%, kuna matatizo mengi. Moja, ni ngumu sana kumwacha Afisa wetu wa TRA kwenda kutoza VAT kulingana na biashara aliyonayo hasa kwa sababu ni ngumu pia kiutawala katika kutambua thamani ya jambo hilo, halafu pia, menejimenti yake inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, pia unaweza kutengeneza mianya ya rushwa ya wale watendaji wetu wanapofanyakazi ya kufanya tathimini ya biashara hizi za aina mbalimbali, lakini unapoweka 18%, wewe unaangalia tu pato lake la jumla kwa mwaka au kwa miezi mitatu, unafanya calculation ya 18%, kuliko kuanza kupitia biashara yenyewe ukubwa wake, unapata shilingi ngapi kwa mwezi, inakuwa ngumu sana.
Kwa hiyo, tumefanya study maeneo mengi na nchi mbalimbali tumegundua kwamba, njia nzuri ni ya kuweka flat rate, kwa biashara hasa kuanzia ile milioni arobaini kwa mwaka na milioni kumi kwa miezi mitatu, minne; inakuwa rahisi zaidi, hata menejimenti yake pia inakuwa ni nzuri.
Kwa hiyo, tumegundua kwamba jambo hili linaweza likasumbua hata wafanyabiashara, linaweza likawasumbua pia hata watendaji wetu wa TRA. Kwa hiyo, tunaendelea kukutana na wafanyabiashara, kupeana mawazo zaidi, lakini jambo hili sasa linahitaji utafiti wa kina, tutakapokuja kufanikiwa, tunaweza pia tukalitambulisha, lakini kwa kuwa tumejifunza pia na nchi za jirani jambo hili lina matatizo haya ambayo nimeyaeleza.
Name
Mussa Azzan Zungu
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ilala
Question 1
Mheshimiwa Waziri Mkuu nakushukuru kwa jibu lako, lakini bado niko hapo hapo.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, nchi jirani moja hapa katika hizi za Afrika Mashariki, informal sector watu hawa wa madaladala, vinyozi, welders na kazi za kawaida ambazo siyo rasmi, wamewekwa katika viwango hivyo na wameweza kuchangia kwenye pato la Serikali trilioni nane mwaka 2009.
Hoja yangu ni kwamba, najua changamoto ambazo zipo kwenye Idara za TRA na zingine, basi Serikali ijaribu tu kulipitia na kutazama kwa sababu trilioni nane, kwa informal sector ni sawasawa na kiwango ambacho TRA ndiyo ilikuwa inakusanya miaka minne, mitano iliyopita.
Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Waziri Mkuu, mlitazame na mlifikirie kwa siku zinazokuja kama Serikali itaona upo umuhimu wa kuongeza mapato yake, informal sector nayo iweze kulipa VAT na Serikali ipate mapato yake. Nakushukuru.
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Azzan Zungu Mbunge wa Ilala, kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa ametoa ombi na kwenye jibu langu la msingi nimesema, bado tunaendelea kukaa pamoja na wadau wetu; ambao ni wafanyabiashara wakiwemo na hao wa informal sector. Kwa hiyo, kadri tutakavyokuwa tunakutana, tunabadilishana mawazo, tunaweza pia kuboresha mfumo mzuri wa ukusanyaji wa mapato, tukitambua pia kwamba, sekta hiyo nayo ina mchango mkubwa sana kwenye pato la Serikali.
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved