Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 18 Sitting 8 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Maswali kwa Waziri Mkuu 1 2025-02-06

Name

Kasalali Emmanuel Mageni

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Primary Question

MHE. KASALALI E. MAGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa mujibu wa Sera ya Kilimo ya nchi hii mazao ya choroko na dengu yamewekwa kwenye Mfumo wa Stakabadhi Ghalani. Hata hivyo, mazao haya ni chanzo cha chakula kama yalivyo maharage na mazao mengine. Sasa mazao haya yamekuwa chanzo cha akiba kwa wananchi wa maeneo ambayo mazao haya yanalimwa kwa wingi. Hata hivyo, kuyaweka kwenye Stakabadhi Ghalani kumesabaisha taharuki kubwa na usumbufu kwa wakulima. Ni nini kauli ya Serikali kuhusu jambo hili?

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ninajua kwenye Sekta ya Kilimo tuna mazao ya biashara na mazao ya chakula, lakini yapo mazao ya chakula yanayotumika pia kwa biashara. Muhimu hapa ni kwamba, Serikali yetu imeendelea kuimarisha masoko ya mazao mbalimbali hapa nchini na tunatumia mifumo mbalimbali kufanya biashara za mazao hayo. Choroko ni miongoni mwa mazao ambayo Wizara ya Kilimo imekuwa ikiratibu biashara yake pale ambapo mwananchi ameamua kuyatumia kama zao la biashara.
Mheshimiwa Spika, tuna mifumo hiyo ya mauzo, kama vile Mkulima kuuza moja kwa moja ndani ya nchi hata nje ya nchi kama anapata oda; pili, tuna mifumo ya kilimo cha mkataba, mnunuzi anafanya majadiliano na mkulima, wanakubaliana kwa maandishi kabisa kwamba zao hilo litakapoiva anaweza kulinunua; na tatu, tuna huu mfumo ambao sasa tunautumia kwa mazao mengi ya kibiashara wa minada. Minada hii ili iende vizuri tuliona tutumie Stakabadhi Ghalani ambayo Mheshimiwa umeisema.

Mheshimiwa Spika, Stakabadhi Ghalani ni mfumo ambao unawezesha wakulima kupata faida kubwa. Kwa sababu, wanunuzi wanakutana pamoja, wanaambiwa kwenye ghala letu tuna tani kadhaa za zao hili na anayetaka atuambie atanunua shilingi ngapi kwa kilo. Kwa hiyo, ule ushindani ulioko kwenye uwanda kwa njia ya mnada ndio unasababisha kupata bei kubwa.

Mheshimiwa Spika, lakini ninatambua, yako maeneo kadhaa yana migogoro ambayo inawafanya wakulima washindwe kuuamini mfumo huo, kwa sababu mfumo ule unamtaka mkulima kila alichokivuna akipeleke ghalani na wahusika wa ghala wanakusanya wakifikia kiwango cha kutosha wanatangaza mnada. Sasa kile kipindi cha kusubiri, kutoka siku unapoleta mzigo mpaka unafanya mnada wengi huwa hawawezi kuvumilia. Kwa maana hiyo Wizara ya Kilimo ilishaagiza kwa Warajisi Wasaidizi na Maafisa Kilimo kule kwenye halmashauri zetu na wilaya.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu unahitaji elimu kwa wananchi, waelewe, waridhie kile kipindi cha kuchelewa ili pale watakapohusisha mazao yao, kila mkulima ajue kwamba atakapopeleka hilo zao lake lenye kilo mbili, kilo tano, kilo kumi au zaidi, atakaa kwa kipindi ambacho wakulima wengine wataleta mazao hayo, yatangazwe mnada, yauzwe na kulipwa. Hivyo kutakuwa na kama siku mbili, tatu, nne za kusubiri malipo. Hapo ndipo panapokuwa na mgogoro.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naagiza Wizara ya Kilimo, iendelee kutoa elimu kwenye maeneo yote yanayotaka zao hilo liuzwe kwa Mfumo Stakabadhi Ghalani, ili kuondoa migogoro ambayo siyo muhimu, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, baada ya kuwa tulishaanza Stakabadhi Ghalani kwenye maeneo mengi, tumegundua kwamba, faida kubwa inapatikana. Kwa hiyo, muhimu ni wakulima kujua kwamba, mfumo huu unaweza kuwa na siku kadhaa za kusubiri. Hata hivyo, jitihada zetu pale ni kuhakikisha tu, tunapunguza zile siku na malipo yanapatikana kwa wakati ili wakulima waweze kupata stahiki yao. Ahsante sana. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister