Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Term | Session | Sitting | Sector | Ministry | Qn No | Date |
---|---|---|---|---|---|---|
2020-2025 | Session 18 | Sitting 8 | Foreign Affairs and International Cooperation | Maswali kwa Waziri Mkuu | 2 | 2025-02-06 |
Name
George Ranwell Mwenisongole
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Mbozi
Primary Question
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali inajipanga vipi na mabadiliko ya Sera za Nje ya Nchi ya Marekani, ambapo tangu Rais Donald Trump aingie madarakani, amefanya mabadiliko makubwa kuhusu Sera ya Nje ya Nchi yake, ambayo inakwenda kuathiri utekelezaji wa Sera zetu kwenye Elimu, Afya na Kiuchumi especially miradi inayofadhiliwa na USAID, EP4R na programu ya kupunguza makali ya VVU? Ahsante.
Name
Kassim Majaliwa Majaliwa
Gender
Male
Party
CCM
Constituent
Ruangwa
Answer
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa George Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu, nchi yetu inaheshimu Sera za Mambo ya Nje na tunatekeleza mikataba kwa mujibu wa sera hizo kama ambavyo tumekubaliana na nchi husika, kwenye maeneo mbalimbali. Tumeanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa ikiwemo Marekani kubadilisha sera zao na mabadiliko yake yanaathiri baadhi ya nchi. Pia hata nchi yetu inaweza kupata athari, lakini kwetu sisi ni muhimu kuzingatia sera za nje kama ambavyo tumekubaliana.
Mheshimiwa Spika, ninaomba nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwamba ameendelea kuifanya nchi hii kuwa na mahusiano na nchi nyingi sana duniani, Marekani ni moja kati ya nchi hizo. Kwetu sisi, muhimu pamoja na upana huu wa mahusiano ambao tumeuweka ni kuhakikisha kwamba tunajiimarisha, tunakuwa na uwezo wa ndani wa kuhakikisha kwamba hatuendelei kuwa wategemezi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni lazima tujiimarishe kwenye mipango yetu, bajeti zetu ziweze kumudu kutekeleza maeneo yote muhimu ikiwemo na hiyo Sekta ya Afya, Elimu, Maji na maeneo mengine kadiri tulivyokubalina na nchi husika.
Mheshimiwa Spika, tuna uwezo, tuna maliasili na tuna rasilimali, kazi ambayo tunayo sasa Watanzania ni kushirikiana kuhakikisha kwamba, tunatumia maliasili na rasilimali tulizonazo kujenga uchumi wa ndani, kuwezesha mipango na bajeti yetu iweze kutekeleza haya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba, Marekani wameshatangaza na inawezekana pia nchi nyingine nayo ikatangaza kukawa na mabadiliko. Sisi tunaendelea kujiimarisha kuhakikisha tunakuza uchumi wetu kupitia vyanzo vya fedha na mapato, ambavyo tunaviweka pamoja na kuyaingiza hapa Bungeni ili yapangiwe mpango kazi na maeneo yaliyopungua pungua tuweze kujaziliza.
Mheshimiwa Spika, huo ndio mkakati ambao sasa tunatakiwa kuwa nao, na ndivyo ambavyo tunaweza kujipanga kutokana na mabadiliko ambayo sasa yanaendelea kwenye nchi zilizoendelea dhidi ya nchi ambazo zinaendelea kama Tanzania.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Copyright © Bunge Polis 2025. All Rights Reserved