Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Question to Prime Minister

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2020-2025 Session 18 Sitting 8 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Maswali kwa Waziri Mkuu 4 2025-02-06

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Gender

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kumuuliza swali Waziri Mkuu. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kuwekuwa na baadhi ya mazao yanayopata bei nzuri, na yanasaidia wakulima kupata mahitaji wanayoyataka. Hata hivyo, kumekuwa na mwenendo mbaya sana wa baadhi ya mazao ambayo wawekezaji pamoja na wanunuzi, hawafanyi vizuri kwa wakulima, hasa yale mazao yanayoharibikia shambani.

Mheshimiwa Spika, ni nini mkakati wa Serikali, kusema na kutoa agizo kwa wawekezaji hao na wanunuzi hao kuhakikisha wananunua mazao hayo kwa wakati, ikiwa zao la parachichi na zao la chai? Kwa kuwa mazao hayo, ni mazao yanayokaribika na wao wanachelewa kuyanunua kwa makusudi ili bei iweze kushushwa na wakulima kuona sasa wana karibia kupata hasara? Ninaomba tamko la Serikali kutoka kwako. (Makofi)

Name

Kassim Majaliwa Majaliwa

Gender

Male

Party

CCM

Constituent

Ruangwa

Answer

WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza katika swali la awali linalohusu mazao, kwamba Serikali imejikita katika kusimamia kilimo nchini. Kilimo ambacho kinatoa mazao ya biashara na chakula, nadhani tumeona manufaa tunayoyapata hapa nchini. Kupitia usimamizi huu wa mazao ya kibiashara, tunatambua ziko changamoto kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwamba mazao mengine ni ya haraka sana kuharibika, hivyo, yanasababisha kuuzwa kwa bei ya chini.

Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali kwenye eneo hili ni kuhakikisha tu kwamba, mazao haya tunayawekea utaratibu ambao ndani ya Serikali tumeamua kuweka mamlaka au bodi: kuna Bodi ya Korosho, kuna Bodi ya Kahawa na kuna Bodi ya Chai. Hata hivyo, parachichi ipo kwenye Mamlaka ya Mazao ya Bustani, TAHA (Tanzania Horticultural Association), hawa wanafanya kazi ya uratibu kuanzia kilimo chake mpaka masoko yake.
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali ili kuokoa mazao haya yasipate hasara, kwanza tumehamasisha uwekezaji kwenye viwanda, ili tuweze kuchakata mazao haya na yasifikie hatua ya kuharibika. Kwa kuchakata tunapata bei nzuri kwa sababu unapata mazao mengi, mbali ya kula lakini tunaweza kupata mafuta na vitu vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utaratibu ambao sasa tunauweka ni wa kuhamasisha uwekezaji kwenye Sekta ya Kilimo kwa mazao mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maparachichi. Kwa bahati nzuri nami nimepata nafasi ya kutembelea wilayani kwako Tukuyu, pia nimeenda Busokelo.

Mheshimiwa Spika, nimetembelea kwenye kiwanda kimoja kikubwa ambacho wenyewe wamelima shamba na wanachakata mazao yao na pia wametoa nafasi kwa wananchi wa eneo lile kuuza mazao yao pale. Kwa hiyo, kwa kuwekeza kiwanda tumeona na mimi nimeshuhudia kwamba hakuna parachichi inaoza, hakuna parachichi inakosa soko kwa sababu yeye anakuwa mnunuzi nambari moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi tumeongeza viwanda, tumeruhusu uwekezaji. Tuna kiwanda Njombe, tuna kiwanda Mufindi na huenda kikajengwa kingine kule Kilolo, Iringa. Hizi ni jitihada za kuhakikisha kwamba tunayalinda haya mazao yasiwaharibikie wakulima pindi wanapovuna yaende viwandani.

Mheshimiwa Spika, ninajua juzi nilikuwa na Mbunge wa Njombe Kusini akilalamikia uwekezaji kwenye zao la chai. Ni kweli tunayo matatizo kwenye zao la chai. Nimeiagiza Wizara kumsimamia mwekezaji huyo ambaye amechukuwa viwanda karibu vyote vya chai na haviendelei ili wakulima wa zao la chai waweze kupata eneo la kuuzia na yeye kwa sababu amechukua viwanda tunataka tuone viwanda vile vikichakata zao la chai ili majani yasiweze kuharibika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tayari Wizara imechukua hiyo na Mheshimiwa Mbunge nilimwelekeza kuonana naye na wanaendelea kusimamia zao hilo na mwekezaji ambaye amechukua viwanda vingi. Kwa hiyo, bado nisisitize kwamba mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakaribisha uwekezaji mkubwa kwenye mazao haya ili mazao yaweze kwenda mahali pale kama eneo la soko lakini ukichakata na kuongeza thamani ya mazao haya, ahsante sana. (Makofi)

Additional Question(s) to Prime Minister